Search This Blog

Sunday, July 10, 2022

ULINIUA GLORIA - 3

 





    Simulizi: Uliniua Gloria

    Sehemu Ya Tatu (3)



    Vijana wa kundi la Kunta Kinte walionekana kuwa makini kwa kila kazi ambayo walipewa malipo makubwa kwa ajili ya kuifanya, kitu ambacho mara nyingi walikuwa wakitaka kukifanya kwa uaminifu mkubwa basi kilikuwa ni kufanya mauaji kwa watu ambao walitakiwa kuitwa marehemu ndani ya siku chache.

    Katika miaka yao yote ya kazi, walikuwa wakizifanya kazi kwa moyo wa dhati, hakukuwa na siku ambayo walikuwa wakizembea au hata kuingiwa na huruma mioyoni mwao. Hata kama ulikuwa mrembo, hata kama ulikuwa mtoto, kitu ambacho walikuwa wakikitaka ni kutekeleza maagizo ambayo walikuwa wametumwa na kulipwa kiasi kikubwa cha fedha.

    Kuua bila kuona huruma ndio ilikuwa kauli mbiu ya kundi lao ambalo lilikuwa likiogopewa sana nchini Zambia. Bado kazi zao zilikuwa zikiendelea kama kawaida na walikuwa wakifanikiwa katika kila kazi ambayo walikuwa wakiifanya. Baada ya kipindi kirefu, hapo ndipo walipopewa kazi na tajiri, Bwana Stewart kwa ajili ya kumuua Kaposhoo.

    Hawakutaka kuchelewa, hawakutaka kujali kama wakati mwingine mzee Mbwana alikuwa akiwapa fedha kwa ajili ya kumfanyia kazi ya kuwaua watu wengine, kitu ambacho walikuwa wakikitaka ni kukamilisha kazi, hawakujali kama mtu ambaye walitakiwa kumuua alikuwa mtoto wa mtu ambaye mara nyingi anakuwa mteja wao.

    Wakapanga mishemishe zao, zilipokamilika, wakafanikiwa kumteka Kaposhoo na kumpeleka katika pori dogo la Maipompo. Katika pori hilo ndipo ambapo walipofanikiwa kumpeleka Kaposhoo na kisha mkubwa wao kumnyooshea bunduki. Kila mmoja katika kipindi hicho alikuwa akitaka kaposhoo afe kama kukamilisha kazi ambayo kwao haikuwa kubwa.

    Kaposhoo alikuwa akilia huku akiomba msamaha lakini hakukuwa na mtu ambaye alionekana kujali, kiungozi yule akammiminia Kaposhoo risasi tatu. Giza lililokuwepo mahali pale lilionekana kumsaidia Kaposhoo, risasi moja ikapenya katika ubavu wake wa kulia karibu na kifua, nyingine ikapenya kiunoni karibu na kitovu na nyingine kupenya karibu kabisa na bega lake.

    Vijana wa Kunta Kinte wakaondoka mahali hapo, kwa jinsi Kaposhoo alivyokuwa ameanguka baada ya kupiga uyowe mkubwa na kukaa kimya, kila mmoja akajua kwamba kazi ilikuwa imefanyika, hawakuwa na muda wa kumchunguza kuona kama alikuwa amekufa au la, wakaondoka zao huku kila mmoja akiwa na uhakika kwamba Kaposhoo alikuwa marehemu.

    Alionekana kuwa kama mfu mahali pale, risasi zilikuwa zimepenya mwilini mwake, mpigaji wa risasi yule hakuonekana kuwa makini katika upigaji wake, yaani kwa hali jinsi ilivyokuwa ilionyesha kabisa kwamba Mungu alikuwa upande wa Kaposhoo. Maumivu yalikuwa makali, damu zilikuwa zikimtoka kupita kawaida, akabaki pale chini huku akianza kugalagala kwa maumivu makali.

    Alitamani kusimama, akashindwa, alitamani kupiga magoti, napo akashindwa, baadhi ya viungo vyake vikaonekana kutokufanya kazi kabisa. Aliendelea kulia kwa maumivu makali lakini kwa sauti ya chini kwani akili yake ilijua vilivyo kwamba endapo watu wale wangesikia sauti yake, wangeweza kurudi na kisha kumuua.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Usiku sana, hakukuonekana kuwa na msaada mahali pale, hapo ndipo alipoona kwamba alitakiwa kufanya kitu, si kusimama na kukimbia au kutembea, alitakiwa kuanza kutambaa kama nyoka. Hivyo ndoivyo alivyofanya, japokuwa alikuwa akisikia maumivu sehemu kubwa ya mwili wake, akaanza kutambaa.

    Hiyo haikuwa kazi ndogo, ilikuwa kazi kubwa kwake kwa sababu alikuwa kwenye maumivu makali mno. Majeraha yake yalikuwa yakigusa ardhini, ardhi ambayo ilikuwa imejaza vijikokoto pamoja na vipande vya miti. Maumivu yaliendelea kuwa makali zaidi, alikuwa akilia sana lakini hakutaka kuacha kwani alijua fika kwamba hapo porini hakukuwa na mtu yeyote yule.

    Japokuwa kilikuwa ni kipori kidogo, Kaposhoo alitumia masaa mawili mpaka kukimaliza na ndipo alipoingia katika barabara ya vumbi. Kaposhoo akashindwa kuendelea zaidi ya hapo, akajikuta akilala, hakujua ni kitu gani kingeendelea, jitihada zote ambazo alikuwa amezifanya, hapo zilifikia tamati. Akaanza kuona giza mbele yake, baada ya dakika chache, hakujua ni kitu gani kiliendelea.

    *****

    Kaposhoo alikuja kupatwa na fahamu ilipofika saa mbili asubuhi. Kwanza akayafumbua macho yake na kisha kuanza kuiangalia sehemu ambayo alikuwepo kwa wakati huo. Sehemu ile ikaonekana kuwa ngeni, akataka kuinuka, akauhisi mwili wote kuwa na maumivu makali.

    Hapo ndipo ambapo kichwa chake kikaanza kukumbuka kila kitu ambacho kilikuwa kimetokea usiku uliopita, alipoziangalia zile sehemu zilizokuwa na majeraha, alikuwa amefungwa bandeji. Kaposhoo akashtuka, hakujua ni sehemu gani alipokuwa katika kipindi hicho, hakujua ni nani ambaye alikuwa amemchukua na kumleta mahali pale. Mshipa wake mkononi ulikuwa umechomwa na sindano ambayo ilikuwa ikiingiza maji kutoka kwenye dripu ambayo ilikuwa ikining’inia.

    Huku akiwa kwenye mawazo lukuki, mlango ukafunguliwa na mzee mmoja kuingia huku akiwa ameshika kikombe cha chai ya moto. Alipomfikia Kaposhoo, hakuongea kitu chochote kile, akaanza kumwangalia mzee yule ambaye usoni mwake alionekana kuwa mgeni kabisa.

    “Afadhali umefumbua macho” Mzee yule alimwambia Kaposhoo.

    “Hapa ni wapi na wewe ni nani?” Kaposhoo aliuliza kwa sauti ya chini ambayo ilionyesha kabisa hakuwa kwenye hali ya kawaida.

    “Mimi ninaitwa Desdeus, ila ninajulikana zaidi kama Des” Mzee yule alimjibu Kaposhoo.

    “Na hapa ni wapi?” Kaposhoo alimuuliza mzee des.

    “Nyumbani kwangu”

    “Sawa. Najua. Ila ni sehemu gani?”

    “Hapa ni Kabwe” Mzee Deus alimwambia Kaposhoo.

    Kaposhoo hakuongea kitu chochote, bado mwili wake ulikuwa kwenye maumivu makali mno. Pembeni yake, kulikuwa na chombo ambacho kilikuwa kama sahani huku kukiwa na risasi tatu ambazo zilionekana kutolewa kutoka mwilini mwake. Kaposhoo akaona hiyo ilitosha sana kumhakikisha kwamba alikuwa salama kabisa.

    Hapo kitandani, dripu moja ya maji ilikuwa ikiendelea kuingia ndani ya mishipa yake kwa kuonekana kwamba mwili wake ulikuwa na kiwango kidogo cha maji. Kaposhoo akakirudisha kichwa chake na kuyafumba macho yake. Hapo ndipo kumbukumbu za kile kilichokuwa kimetokea kuanza kumrudia tena kichwani mwake.

    Akaanza kukumbuka maneno ambayo mwanaume mmoja aliongea kwamba walikuwa wametumwa na bosi wao, Bwana Stewart kwa ajili ya kumuua huku kisa kikiwa ni msichana Gloria. Moyo wa Kaposhoo uliumia sana, akagundua kwamba kumbe katika kipindi hicho msichana Gloria alikuwa akitembea na Bwana Stewart ambaye alitaka kummaliza.

    “Nitawaua” Kaposhoo alijisemea huku akionekana kuwa na hasira.

    Kila siku akawa akipokea tiba ndani ya nyumba hiyo, mzee Des alikuwa akimhudumia kwa madawa mbalimbali tena ya gharama ya juu hali ambayo ilionekana kumshangaza sana Kaposhoo kwani mzee Des hakuonekana kuwa mtu mwenye uwezo mkubwa sana.

    “Ila wewe ni nani hasa?” Kaposhoo alimuuliza mzee Des mara baada ya siku nne kupita akiwa ndani ya nyumba hiyo akipokea matibabu.

    “Ninaitwa Desdeus”

    “Unafanya kazi gani? Wewe ni daktari au?” Kaposhoo alimuuliza mzee Des.

    “Ndio. Mimi ni daktari wa jeshi la hapa Zambia” Mzee Des alimwambia Kaposhoo.

    “Nimekuelewa. Hivi ilikuwaje mpaka kunileta hapa?” Kaposhoo alimuuliza.

    “Nilikukuta usiku wa manane ukiwa umelala pembeni ya barabara katika kipindi ambacho nilikuwa natoka Lusaka kuja hapa Kabwe na gari langu. Nilihofia kwamba inawezekana ulikuwa jambazi lakini kwa ujasiri mkubwa nikateremka huku nikiwa na bunduki yangu kiunoni, nilipofika pale ulipokuwa, ulikuwa umepoteza fahamu huku ukiwa na majeraha. Nikaamua kukubeba na kuja nawe nyumbani” Mzee Des alimwambia Kaposhoo.

    “Asante sana” Kaposhoo alimwambia mzee Des.

    “Usijali kijana wangu. Nimetumia madawa mengi sana na ujuzi wangu wa juu ambao huwa tunatumia kuwatibu wanajeshi wanapotoka vitani na ndio maana hali yako inaonekana kuwa salama kwani bila hivyo, ungekuwa marehemu kwa sasa” mzee Des alimwambia Kaposhoo.

    “Asante sana”

    “Usijali. Ila nini kilitokea mpaka wewe kuwa pale huku ukiwa katika hali hii?” Mzee Des aliuliza.

    “Nilitekwa na watu wasiojulikana” Kaposhoo alijibu.

    “Kisa nini?”

    “Sijui. Wala sijui kisa nini”

    “Ikawaje?”

    “Wakanipeleka katika lile pori dogo la Maipompo ambapo wakataka kuniua. Walinipiga risasi tatu, wakajua nimekufa, wakaondoka zao” Kaposhoo alimwambia mzee Des.

    “Pole sana”

    “Asante. Umewaambia polisi kuhusu mimi?”

    “Kuwaambia polisi! Toka lini ukamuona mwanajeshi akimwambia polisi kitu kama hiki?” Mzee Des aliuliza.

    “Ili waache kunitafuta, baba ajue nipo hai”

    “Hapana. Sijamwambia mtu yeyote yule” Mzee Des alimjibu Kaposhoo.

    “Na kila siku nakuona ukiwa peke yako, hauna mtu mwingine ndani ya nyumba hii?” Kaposhoo alimuuliza mzee des.

    “Nipo peke yangu. Mke wangu pamoja na watoto wangu waliuawa mwaka jana katika mapigano ya jeshi la serikali na waasi” Mzee Des alimjibu Kaposhoo.

    “Pole sana”

    “Asante sana. Ila namshukuru Mungu kwani naendelea vizuri kwa sasa. Sina mawazo kabisa, maisha yanaendelea” Mzee Des alimwambia Kaposhoo.

    Kaposhoo aliendelea kukaa katika nyumba ile kwa zaidi na zaidi huku akipatiwa matibabu makubwa. Majeraha yake yote yalikuwa yamewekewa damu. Kila wakati ni dripu ndizo ambazo zilikuwa zikipokezana. Mara dripu za maji na wakati mwingine dripu za damu kutokana na kupoteza damu nyingi mwilini mwake.

    Hali yake haikuwa nzuri sana, bado aliendelea kuugulia maumivu kitandani pale. Hasira zake zilikuwa juu ya Bwana Stewart, mzee ambaye alikuwa amesababisha yeye kuwepo mahali pale kwa wakati huo. Kwanza akaumia sana moyoni, hakuamini kama Gloria angeweza kumsaliti kwa mzee huyo ambaye alikuwa na umri mkubwa sana.

    Akajikuta akimchukia Gloria, akajikuta akimchukia Bwana Stewart, pamoja na hayo yote, moyo wake ukaingiza kisasi, akatamani kuwaua hao wote. Hakuona kama kulikuwa na sababu ya watu hao kuendelea kuvuta pumzi ya dunia hii na wakati walitaka kumuua, alijua fika kwamba watu ambao walikuwa wametumwa kwa ajili ya kuifanya kazi ile hawakuwa watu wenye masihala hata kidogo, walikuwa wamekuja kwa ajili ya kumuua tu.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nitawaua wote” Kaposhoo alijikuta akisema kwa sauti yenye hasira.

    “Umesemaje?”

    “Nitawaua wote ambao wamenifanya niwe hapa” Kaposhoo alimwambia mzee Des.

    “Hao majambazi?”

    “Hapana. Watu waliowatuma hao majambazi” Kaposhoo alijibu.

    “Unawajua?”

    “Ndio”

    “Umewajuaje?”

    “Waliniambia”

    “Wakina nani?”

    “Majambazi wenyewe”

    “Eeh! Majambazi walikuambia? Kivipi?”

    “Walijua kwamba ningekufa, hivyo walitaka kuniona nikifa huku nikimjua aliyesababisha kifo changu” Kaposhoo alijibu.

    “Ni wakina nani hao?”

    “Mzee Stewart”

    “Huyu bilionea?”

    “Ndio”

    “Ulimfanya nini? Na wewe nani?”

    “Mimi ni Kaposhoo. Mtoto wa mzee Mbwana” kaposhoo alijibu.

    “Kumbe mtoto wa mzee Mbwana?”

    “Ndio”

    “Bila shaka ugomvi ni wa kibiashara huu”

    “Hapana. Ugomvi wa kimapenzi”

    “Ugomvi wa kimapenzi! Mbona unanichanganya. Ulimchukulia mkewe?” Mzee Des aliuliza huku akionekana kushtuka.

    “Hapana. Amenichukulia msichana wangu na kutaka kuniua”

    “Pole sana Kaposhoo”

    “Asante sana”

    Siku ziliendelea kukatika mahali hapo, bado Kaposhoo alikuwa na hasira kali na Bwana Stewart pamoja na msichana Gloria. Kila alipokuwa akiendelea kupatiwa tiba na kuwa katika hali nzuri na ndivyo ambavyo hamu ya kutaka kutoka ndani ya nyumba hiyo ilivyozidi kumshika zaidi na zaidi ili aende akakamilishe kile ambacho alikuwa amekipanga.

    Mwezi wa kwanza ukakatika, mwezi wa pili ukaingia, bado alikuwa na hamu kubwa ya kutaka kutoka mahali hapo. Kichwa chake hakikuwa kikifikiria kitu kingine, kitu ambacho alikuwa akikitaka ni kuwaua wabaya wake kama njia moja ya kulipiza kisasi.



    Pori dogo la Maipompo bado lilikuwa likihofiwa na kila mtu ambaye alikuwa akiishi nchini Zambia kutokana na mambo ya kishirikina ambayo yalikuwa yakiaminika sana kuwepo ndani ya pori hilo. Wakinamama walikuwa wakikatazwa kuingia ndani ya pori hilo kwa ajili ya kukata kuni, vijana wadogo nao walikuwa wakikatazwa kuingia sehemu hiyo kwa ajili ya kuwinda ndege na mambo mengine.

    Pori hilo likaonekana kutengwa japokuwa kulikuwa na watu ambao walikuwa wakijifanya vichwa ngumu ambao walikuwa wakiingia ndani ya pori hilo. Hiyo ndio ilikuwa imani yao, kila mtu alikuwa akiuhofia uchawi na kuna wengine waliamini kwamba pori lile lililetwa ndani ya nchi ya Zambia kwa sababu tu watu wengi walikuwa washirikina.

    Wananchi waliitaka serikali kuikata miti yote ya pori hilo lakini serikali haikutaka kufanya hivyo. Haikuamini katika uchawi, wao, pori lile lilichukuliwa kama sehemu moja ambayo mtu anaweza kuingia na kufanya mambo mengine kama katika mapori mengine.

    Miaka iliendelea kukatika, watu waliendelea kujawa na hofu juu ya pori lile ambalo lilikuwa likijulikana sana nchini Zambia hata zaidi ya jinsi alivyokuwa akijulikana rais wa nchi hiyo. Watu wengi ambao walikuwa wakiuawa humo, kila mmoja alikuwa akifikiri kwamba ni mashetani na majini ndio ambayo yalikuwa yamefanya mauaji hayo.

    “Umesikia mlio wa bunduki?” Kijana mmoja alimuuliza mwenzake huku ikiwa ni saa tatu usiku.

    “Nimeusikia. Wapi hiyo?” Kijana yule alimuuliza mwenzake huku milio mingine ikiendelea kusikika.

    “Kama kule porini”

    “Kule porini sidhani. Inawezekana kuna majambazi sehemu fulani” Kijana yule aliyemshtua mwenzake alimwambia.

    “Kwa nini isiwezekane?”

    “Hakuna wanaoingia kule. Mimi mwenyewe napaogopa”

    “Hahaha! Wewe si uliniambia umeokoka! Sasa unaogopea nini uchawi, au hauamini kama Mungu anakulinda?”

    “Sio kwamba siamini, naamini ananilinda ila maisha yenyewe yamejaa dhambi. Hebu jifikirie, jana tu nimetoka kuzini na Janeth, halafu nikiingia kule unadhani Mungu atanilinda? Unadhani Mungu anamlinda muovu? Lazima niogope kaka”Kijana yule alimwambia mwenzake.

    Kila mtu alikuwa akihofia kuingia ndani ya pori lile, mauaji bado yalikuwa yakiendelea kutokea kila siku lakini hakukuwa na hatua ambazo zilichukuliwa. Serikali haikuwa ikiogopa uchawi na wala haikuwa ikiamini kwenye uchawi lakini hito serikali ilipokuwa ikigawanyika na kuwa mtu mmoja mmoja, kila mtu alikuwa akihofia.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mauaji mengi ambayo yalikuwa yametokea yakaonekana kuwatisha watu, polisi hawakuonekana kufuatilia kitu chochote kile. Mara kwa mara milio ya risasi ilikuwa ikiendelea kusikika mpaka katika siku hiyo ambayo milio hiyo iliposikika ndipo watu wakawapigia simu polisi kwa mara nyingine tena.

    Kama kawaida yao, polisi waliposikia kwamba walikuwa wakihitajika katika mtaa wa Maipompo wakaonekana kuhisi kitu, wakajua dhahiri kwamba kulikuwa na kitu kimetokea katika msitu ule. Wote walikuwa na woga mioyoni mwao, imani za kishirikina ziliendelea kuwa mioyoni mwao.

    Toka simu ipigwe, yalipita masaa matatu, hakukuwa na polisi ambaye alifika mahali pale, polisi wengi walikuwa wakihofia mara baada ya kuambiwa kwamba kama kawaida milio ya risasi ilikuwa imesikika kutoka katika pori la Maipompo.

    Mara kwa mara simu ilikuwa ikiita katika kituo kikuu cha polisi cha Mansansa, kila polisi ambaye alikuwa akiipokea simu hizo, zilikuwa zile zile za kuwataka kufika katika mtaa wa Maipompo ndani ya pori dogo ambalo kulikuwa na risasi kadhaa ambazo zilikuwa zikisikika.

    “Hivi hawa wananchi wanafikiria nini?” Polisi mmoja aliuliza huku akiwa na bunduki mkononi, usoni, hakuonekana kuwa na ujasiri.

    “Kwa nini?”

    “Muda wote wameng’ang’ania kupiga simu kutaka sisi twende kwenye pori hilo. Hivi wanalichukuliaje pori lile?” Polisi huyo alisema na kuuliza swali. Alipoona kila mmoja alikuwa kimya, akaendelea.

    “Lile pori si mchezo, yaani utafikiri hawalijui. Tunaweza kuingia kule tukaanza kupigana risasi wenyewe kwa wenyewe bila kujua wala kupenda” Polisi yule aliwaambia wenzake.

    Serikali haikuamini katika uchawi lakini polisi mmoja mmoja alikuwa akiamini katika uchawi. Hofu zilikuwa kuu mioyoni mwao, walikuwa radhi kwenda kupambana na majambazi kwa risasi lakini hawakuwa radhi kuingia ndani ya pori lile. Masaa yalizidi kusogea mpaka kufika kipindi ambacho mzee Mbwana alipofika mahali hapo, yalikuwa yamepita masaa kadhaa.

    Mzee Mbwana hakuonekana kuwa kwenye hali ya kawaida, japokuwa alikuwa ametumia gari lakini kijasho chembamba kikaanza kuonekana pajini mwa uso wake. Alipoingia ndani ya kituo kile, akaanza kutoa taarifa juu ya utekaji wa mtoto wake huku Peter akiwa pembeni yake.

    Hapo ndipo polisi walipoanza kuhisi kitu kwa kuona kwamba inawezekana kabisa milio ya risasi ambayo walikuwa wameisikia basi ilikuwa ikimhusisha Kaposhoo, walichokifanya mara baada ya mzee Mbwana kuondoka mahali hapo na Peter, wakaingia ndani ya gari lao na kisha kuanza kuelekea katika pori lile.

    Kila mmoja ndani ya gari alikuwa na bunduki yake, kila mmoja alionekana kujitia ujasiri mkubwa usoni mwake japokuwa mioyoni mwao walionekana kuwa tofauti sana na ujasiri ule. Dereva wao alikuwa akiendesha gari kwa kasi ya ajabu, kila mmoja alikuwa akihisi kijibaridi mwilini mwao, walikuwa wakiliona gari lile likiendeshwa kwa mwendo mkubwa ambao uliwafanya kuwahi.

    “Mmmh! Hii isingekuwa amri...nisingekubali kwenda” Polisi mmoja alimwambia mwenzake kwa sauti ya chini.

    “Wewe ni kama mimi. Yaani bila mkuu kusema kwenda huko ni lazima, nisingekubali. Kwanza sijui kilitokea kitu gani mpaka nikabaki kituoni” Polisi mwingine alisema.

    Mtoto wa tajiri mkubwa nchini Zambia alikuwa ametekwa na hakujulikana ni mahali gani alipokuwa kwa wakati huo. Mkuu wa kituo hakuonekana kujali, hakutaka kuziendekeza hofu za vijana wake, alichowaamuru ni kwenda ndani ya pori hilo huku yeye akibaki kituoni.

    “Tushafika” Polisi mmoja aliyekuwa amekaa kiti cha mbele na dereva aliwaambia polisi wale.

    “Nani akae mbele?” Polisi mmoja aliuliza.

    “Kwanza mwananchi aliyetupigia simu yupo wapi?”

    “Unafikiri tutaweza kumpata, cha msingi tuingieni. Si walisema kwamba milio ya risasi ilisikika kutoka katika pori hili?”

    “Ndio”

    “Basi tuingieni”

    “Sawa mkuu”

    “Nani mkuu? Mimi sio mkuu. Hakuna mkuu hapa. Unaniita mkuu ili niwe mtu wa mbele kuingia. Tuingieni pamoja, hakuna mkuu hapa” Polisi yule aliwaambia wenzake huku usoni mwake akionekana kuwa na hofu.

    “Ngoja nifuate tochi kituoni wakati nyie mnaingia ndani ya pori hili”

    “Tochi za nini?”

    “Za kumulika. Kuna giza sana”

    “Kwa hiyo unataka tochi?”

    “Ndio. Na ndio maana nimesema nizifuate kituoni”

    “Kuhusu tochi hakuna tatizo. Zipo garini, ngoja nichukue moja na kukupa” Polisi yule alimwambia mwenzake, akaelekea garini, akachukua tochi na kumgawia.

    “Twendeni sasa” Polisi yule alisema huku akiwa ameshika tochi.

    “Mwenye tochi ndiye wa kutangulia”

    Polisi wote walikutana waoga, hakukuwa na mtu ambaye alikuwa radhi kutangulia kuingia ndani ya msitu ule, kila mmoja alikuwa akiyahofia maisha yake. Walikaa kwa kujibizana mpaka pale walipoamua kuingia pamoja, yaani huyu akiwa mkono wa kushoto na huyu akiwa mkono wa kulia.

    Wote wakaingia ndani ya msitu ule, wote waliokuwa mahali pale walikuwa wageni ndani ya msitu ule. Japokuwa walikuwa na bunduki mikononi mwao lakini wote walionekana kuwa waoga kupita kawaida, imani za kishirikina ndizo ambazo zilikuwa zimetawala mioyoni mwao. Walipiga hatua huku mwenye tochi akimulika huku na kule.

    Walizunguka katika pori zima, hakukuwa na mtu yeyote yule, hawakuweza kubahatika kuona kitu chochote kile jambo ambalo lilionekana kuwakasirisha kupita kawaida. Walitumia dakika zaidi ya arobaini, wakapanga kwamba ilitakiwa waondoke ndani ya posiri hilo ingawa walikuwa wamekwishaanza kulizoea na kuliona la kawaida sana.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kumbe hili pori la kawaida sana, tulikuwa tunaogopa bure”

    “Unaliona la kawaida kwa sababu tupo wote. Ungekuwa peke yako ndio uwe na ujasiri wa kusema hivyo”

    Waliendelea zaidi na zaidi mpaka pale ambapo mwanga wa tochi ukatua katika sehemu ambayo ilikuwa na nyasi zilizolala kuliko sehemu yoyote ile, kwa mwendo wa haraka haraka wakaanza kusogea mahali pale, bunduki zao zilikuwa tayari, walipofika mahali pale, wakaanza kuangalia vizuri.

    Michirizi ya damu ndio ambayo ilikuwa ikionekana katika nyasi zile, michirizi ile ilionekana kuelekea barabarani, walichokifanya ni kuanza kuifuata huku wengine wakiwa makini kuangalia huku na kule. Baada ya dakika fulani, mkusanyiko mkubwa kiasi wa damu ukaonekana sehemu fulani pembezoni kidogo mwa barabara, wote wakasimama na kisha kuanza kuangalia huku na kule.

    “Ina maana huyu mtu aliuawa na kisha kuanza kuburuzwa?” Polisi mmoja aliuliza.

    “Hatujui. Sijui ilikuwaje”

    Walichokifanya ni kupiga simu kutuoni na kutoa taarifa juu ya kile ambacho walikuwa wamekutana nacho katika pori lile. Ilionekana kuwa habari ya kushtua sana masikioni mwa kiongozi wao lakini hakuonekana kuwa na jinsi.

    “Kwa hiyo ameuawa?” Sauti ya mkuu wa polisi kituo cha Mansansa ilisikika ikiuliza swali.

    “Hatujui. Tumekutana na damu tu”

    “Au wamemtoa kafara?”

    “Bado hatujajua mkuu. Hali inaonekana kuwa si ya kawaida kabisa” Polisi huyo alisema.

    “Ok! Cha msingi njooni kisha tupange ili tujue nini cha kufanya” Mkuu wa kituo aliwaambia.

    “Hakuna tatizo mkuu”

    Polisi wote wakaelekea katika upande ambao ulikuwa na gari lao na kisha kuingia. Kila mmoja alionekana kuwa na amani, wakaonekana kutokuwa na hofu hata kidogo, kila mmoja alionekana kuuzoea msitu ule, imani zao juu ya ushirikina ambao ulikuwa umetawala ndani ya pori lile zikaonekana kutoweka moyoni mwao.

    Walipofika kituoni, mkuu wa kituo akaanza kuwagawia majukumu upya. Wengine walitakiwa kufanya upelelezi kwa kuulizia huku na kule na huku wengine wakitakiwa kuhakikisha kuanzisha ulinzi mkali katika msitu ule.

    “Mkimuona mtu yeyote anaingia ndani ya pori hili nyakati za usiku, piga risasi tu” Mkuu wa kituo aliwaambia vijana wake.

    “Sawa mkuu” Vijana hao wanne waliitikia huku wakipiga saluti. Kilichoendelea ni kwenda kwenye pori hilo na kisha kuanza kuweka ulinzi mchana na usiku.

    “Jibu la kutoa endapo mzee Mbwana atauliza kuhusu mtoto wake, bado tunaendelea na uchunguzi. Mmesikia?”

    “Sawa mkuu”



    Hali ambayo ilitokea katika pori dogo la Maipompo ikaonekana kuwachanganya polisi na kugundua kwamba ndani ya pori hilo kulikuwa na michezo mingine hatari ambayo ilikuwa ikiendelea kufanyika. Bila kuchelewa, ulinzi ukatakiwa kuwekwa ndani ya pori hilo kwa kuona kwamba endapo wasingefanya hivyo basi kungeweza kutokea mambo mengine zaidi, mambo mabaya ambayo yangewagharimu wao wote.

    Polisi sita wakawekwa tayari na kisha kuanza ulinzi ndani ya pori hilo huku wote wakiwa na bunduki mikononi mwao. Polisi wakaonekana kuchoka, matukio ya mauaji ambayo mara kwa mara yalikuwa yakitokea ndani ya msitu huo yakaonekana kuwashtua kutoka katika usingizi wa woga.

    Hofu ambayo walikuwa nayo juu ya pori hilo ikawatoka mara baada ya kuona kwamba kulikuwa na mambo mengi ambayo yalikuwa yakiendelea. Ulinzi ukaimarishwa, hakukutakiwa mtu yeyote kuingia ndani ya pori lile kwani waliona kama wangeruhusu basi kungekuwa na mambo mengine zaidi ambayo yangeweza kutokea.

    “Unasemaje?” Polisi mmoja aliyekuwa akivuta sigara kwa madaha alimuuliza mwenzake.

    “Umewaona watu walioingia ndani ya pori lile?” Polisi yule alimuuliza mwenzake.

    “Hapana”

    “Kuna watu wameingia”

    “Mmmh! Mimi mbona sijawaona?”

    “Hujawaona kabisa?”

    “Sijamuona hata mmoja”

    “Hebu twende”

    “Peke yetu?”

    “Sasa tutakwenda na nani?”

    “Wenzetu”

    “Yaani mpaka tuwaite kutoka upande wa pili. Hapana bwana, twende wasije wakaondoka” Polisi yule alimwambia mwenzake ambaye alionekana kutokuwaona watu ambao aliwambiwa na wenzake kwamba walikuwa wameingia ndani ya pori lile.

    Hawakutaka kuendelea kukaa mahali hapo, walichokifanya ni kuondoka kuelekea kule ambapo polisi mmoja alikuwa amewaona watu wakiingia ndani ya pori lile. Kila mmoja alikuwa na bunduki mkononi mwake, walijiandaa kwa kila kitu ambacho kingetokea mahali hapo, hata kama ingewabidi kutumia bunduki, wangefanya hivyo.

    Waliendelea kwenda mbele zaidi, kila mmoja alikuwa na bunduki mkononi mwake, hawakutaka kuwashtua wenzao ambao walikuwa katika pande nyingine kwa kuhofia kwamba endapo wangewashtua basi wale watu ambao waliingia ndani ya pori lile wangeweza kukimbia.

    Walizidi kusogea na kuingia ndani ya pori lile, japokuwa kulikuwa na giza lakini wakaonekana kuhimili mwanga hafifu sana wa mbalamwezi ambao ulikuwa ukiendelea kumulika angani. Wakaendelea kupiga hatua kuelekea mbele zaidi huku wakijaribu kuangalia huku na kule,

    Waliendelea kusogea mbele zaidi, hakukuwa na mtu ambaye aliweza kuonekana mbele yao jambo ambalo likaonekana kuwashangaza sana, Hawakukata tamaa, waliendelea kusogea mbele zaidi na zaidi lakini napo hali iliendelea kuwa vile vile, hakukuonekana kuwa na mtu yeyote ndani ya pori lile.

    “Au ulijichanganya na kuona maluweluwe?”

    “Hapana bwana. Niliwaona watu wakiingia humu”

    “Walikuwa wangapi?”

    “Sikumbuki, ila ni zaidi ya watatu”

    Hawakutaka kukata tamaa, bado waliendelea kusonga mbele mpaka pale ambapo wakaanza kusikia sauti za watu kwa mbali. Hapo ndipo wakaziandaa bunduki zao na kisha kuendelea kusonga mbele hadi katika sehemu ambayo waliweza kuwaona vizuri watu wale ambao walikuwa wamesimama katika sehemu iliyokuwa imejificha kidogo.

    Waliweza kusikia vilivyo kila kitu kilichokuwa kikiongelewa mahali pale, walichokifanya ni kuchukua bunduki zao na kulenga kule tayari kwa kufyatua risasi. Katika kipindi ambacho walisikia sauti ya mwanaume mmoja ikiomba msamaha huku mtu mwingine akiwa ameshika bunduki kumuelekezea, hapo hapo wakafyatua risasi kwa pamoja.

    Japokuwa wote walikuwa wamefyatua risasi, hakukuwa hata na risasi moja ambayo ilikuwa imewapata watu wale ambao kwa kasi ya ajabu wakaanza kukimbia ovyo mahali pale kuelekea katika upande mwingine. Polisi wale hawakutaka kubaki, walichokifanya na wao, wakaanza kuwakimbiza huku wakiwafyatulia risasi ambazo zilikuwa zikigonga kwenye miti tu.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Pori likatawaliwa na milio ya risasi, milio ile ndio ambayo ikaonekana kuwashtua polisi wengine ambao walikuwa katika pande nyingine mbili na wao kuanza kuingia porini. Siku hiyo ikaonekana kuwa kama siku ya mapigano ya waasi na majeshi ya serikali, milio ya risasi ilikuwa imetawala katika kila kona porini hapo.

    Polisi wale waliendelea kuwakimbiza mpaka pale ambapo walikaribia na nje ya pori lile, wakawakuta wenzao wakiwa wamekwishafanya kazi ambayo walikuwa wakitaka kuifanya, miili ya vijana wa Kunta Kinte ilikuwa chini huku damu zikiwatoka, walikuwa wamepigwa risasi na kupoteza maisha.

    “Hawa ni wakina nani?” Polisi mmoja ambaye alionekana kutokuelewa vizuri aliwauliza wenzake ambao walikuja mahali hapo.

    “Niliwaona wakiingia porini”

    “Kufanya nini?”

    “Sijui. Ila waliingia porini”

    “Peke yao?”

    “Umenikumbusha. Twendeni huku” Polisi yule aliwaambia wenzake na kisha kuanza kuondoka mahali hapo huku wakiwaacha polisi wengine wawili wakiwa mahali pale.

    Safari yao katika kipindi hicho ilikuwa ni kwenda kule alipokuwa amelazwa Peter kwa ajili ya kufyatuliwa risasi, wala hawakuchukua muda mrefu, wakafika mahali hapo, Peter alikuwa chini huku akiwa amefungwa kamba mikononi kwa nyuma. Kitu cha kwanza walichokifanya ni kumfungua kamba zile na kumuacha huru.

    “Kuna nini?”

    “Walitaka kuniua” Peter alijibu huku akiwa haamini kama alikuwa amenusuruka kuuawa.

    “Wakina nani?”

    “Sijui ni wakina nani”

    “Unawafahamu?”

    “Hapana. Ila si mara ya kwanza kuwaona” Peter alijibu huku akionekana kuwa na wasiwasi.

    “Ushawahi kuwaona wapi?”

    “Niliwahi kuwaona juzi. Walikuwa wamekuja kumteka Kaposhoo” Peter alijibu huku akionekana kutokuwa huru mahali hapo.

    “Kumbe wale ndio waliomteka Kaposhoo?” Polisi mmoja aliuliza huku akionekana kushtuka.

    “Ndio”

    “Sasa kwa nini walikuteka na wewe pia?”

    “Walitaka kuniua”

    “Kwa sababu gani?”

    “Sijui kwa sababu gani”

    “Wamekujeruhi popote pale?”

    “Hapana”

    “Na Kaposhoo yupo wapi?”

    “Sijui chochote kile” Peter alijibu mfululizo.

    Hakukuwa na haja ya kupoteza muda mahali hapo, tayari waliona kwamba Peter angeweza kuwasaidia katika kile ambacho wangekuwa wakikihitaji kukifahamu kuhusiana na Kaposhoo, walichokifanya ni kumchukua Peter na kisha kuondoka nae mahali hapo kuelekea katika kituo cha polisi cha Mansansa.

    Njia nzima Peter alikuwa akimshukuru Mungu, hakuamini kama alikuwa amenusurika kuuawa porini. Muda wote lawama zake zilikuwa kwa Gloria, Peter alijua fika kwamba Gloria ndiye alikuwa chanzo cha kila kitu ambacho kilikuwa kikiendelea mahali hapo. Moyoni aliumia sana, hakuamini kama kitendo chake cha kumleta Gloria nchini Zambia ndio kingesababisha mambo yote hayo.

    “Ila kwa nini Gloria ameamua kufanya mambo yote haya kwangu? Yaani mapenzi yote ambayo nilimuonyeshea haya ndio yamekuwa malipo yake? Hakika ninamchukia Gloria, kama yeye ndiye anasababisha mpaka mimi kutaka kuuawa, ni lazima nimuue yeye na bwana aliye nyuma ya kila kitu” Peter alijisemea katika kipindi ambacho gari lilikuwa likiendelea kuelekea kituoni huku miili ya vijana wa Kunta Kinte ikiwa ndani ya gari lile.

    Walichukua zaidi ya dakika kumi na ndipo walipoingia ndani ya eneo la kituo cha polisi cha Mansansa ambapo wakateremka na kisha kuishusha miili ile chini huku tayari ikiwa imetimia saa sita usiku. Walichokifanya, wakaanza kumhoji Peter maswali kadhaa na kisha kumtaka kuondoka kuelekea nyumbani kwa ajili ya kupumzika na kesho kuitwa tena mahali hapo.

    “Hapana. Siwezi kwenda nyumbani” Peter aliwaambia polisi.

    “Kwa nini?”

    “Wale watu wataniua. Wataniua wale” Peter aliwaambia.

    “Ila si tumekwishawaua?”

    “Mtandao wao inaonekana kuwa mkubwa. Wanaweza kuniua hawa” Peter aliwaambia huku akionekana kugoma kwa asilimia mia moja kuelekea nyumbani.

    Hakukuwa na jinsi, kwa sababu Peter alikataa kuelekea nyumbani, akatakiwa kubaki hapo hapo kituoni. Akaingizwa katika chumba kimoja ambacho kilionekana kuwa kama ofisi na kuambiwa kutulia huko huku televisheni ikiwa imewashwa.

    Usingizi haukupatikana kwa Peter, usiku mzima alikuwa akimfikiria Gloria, bado kila kilichokuwa kimetokea kilionekana kumuumiza kupita kawaida, aliona kwamba kufanyiwa kitendo kile na binadamu kilikuwa ni cha kawaida lakini kwa mtu kama Gloria, hakuona kama kitendo kile kilikuwa cha kawaida.

    Kadri dakika zilivyokuwa zikizidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo hasira zake zilikuwa zikiongezeka juu ya Gloria, alikuwa akimchukia sana, alikuwa akichukia kila kitu ambacho alikuwa amefanya pamoja na Gloria.

    “Nitamuua tu” Peter alijiseme huku akionekana kuwa na hasira zaidi na zaidi.

    Mawazo yake hayakuishia hapo, bado alikuwa akiendelea kumkumbuka mpenzi wake ambaye katika kipindi hicho hakuwa mikononi mwake tena, alikuwa amechukuliwa na mtu mwenye fedha, mtu ambaye hakuwahi kumtambua japokuwa alikuwa amemuona mara kadhaa, Bwana Stewart.

    Asubuhi ikafika, usiku mzima alikuwa amekesha kama popo ndani ya chumba kile huku akiendelea kuangalia televisheni. Muda ulizidi kwenda mbele zaidi na zaidi mpaka katika kipindi ambacho akaona kwamba alitakiwa kuondoka kuelekea nyumbani ambapo huko angechukua kila kilichokuwa chake na kuondoka mahali hapo.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ngoja kwani nikae kae mpaka saa tatu ndio niondoke” Peter alijisema huku macho yake yakiendelea kuangalia televisheni, ilikuwa saa 2:11 asubuhi.

    ****

    Taarifa zilikuwa zimekwishatolewa katika vyombo vya habari kwamba kijana wa kitanzania, Peter alikuwa akitafutwa na polisi kutokana na mauaji ambayo alikuwa ameyafanya siku mbili zilizopita. Kila mtu ambaye alizipata taarifa zile alionekana kushtuka, hakukuonekana kuwa na mtu ambaye aliamini kwamba mtoto wa mzee Mbwana, Kaposhoo alikuwa ametekwa na kuuawa na kijana kutoka nchini Tanzania.

    Wanachuo wa chuo cha St’ Victor wakaonekana kutokuamini kile ambacho walikuwa wamekisikia, walimfahamu Peter vilivyo kutokana na upole wake ambao alikuwa nao na vile vile waliufahamu ukaribu ambao alikuwa nao kwa Kaposhoo, hawakuonekana kuamini kama kijana yule angeweza kufanya kile ambacho alikuwa amekifanya.

    Vyombo vya habari asubuhi hiyo vikaanza kutangaza taarifa hiyo huku televisheni zikianza kuweka picha zake huku kiasi cha kwacha milioni kumi zikiwa zimeandaliwa kwa mtu yeyote ambaye angeweza kufanikisha kukamatwa kwa mtu huyo, mtanzania ambaye alidiriki kufanya mauaji nchini Zambia.

    Peter akaonekana kuwa lulu mitaani, watu wakaonekana kuwa makini, kiasi cha fedha ambacho kilikuwa kimetangazwa kilionekana kuwa kiasi kikubwa ambacho kila mtu alitamani kuwa nacho mfukoni mwake. Japokuwa watu walikuwa wakiendelea na shughuli zao kama kawaida, kila mtu kichwa chake kilikuwa kikimfikiria Peter tu.

    Saa 2:50 asubuhi, gari aina ya difenda ya polisi ilikuwa ikisimama katika kituo cha polisi cha Mansansa na kisha polisi wawili kuteremka huku wakiwa wameshika karatasi ambazo zilikuwa na picha za Peter, walipoteremka, wakaanza kuelekea ndani ya kituo hicho na kusimama kaunta, wakaziweka zile picha juu ya kaunta ile.

    Polisi ambao walikuwepo mahali pale, wakasalimia kwa kupiga saluti na kisha kuchukua picha zile na kuanza kuziangalia. Kila mmoja alikuwa makini kuziangalia picha zile, maneno makubwa yaliyosomeka MOST WANTED yalikuwa yakionekana vizuri katika kila karatasi iliyokuwa na picha ya Peter.

    “Hizi ni karatasi kutoka makao makuu. Huyu mtu anatafutwa” Mmoja wa polisi ambaye alizileta karatasi zile aliwaambia polisi ambao walikuta pale kaunta.

    “Anatafutwa?” Polisi mmoja aliuliza kwa mshtuko.

    “Ndio”

    “Amefanya nini?”

    “Anatafutwa kwa kujibu kesi ya mauaji”

    “Mauaji gani?”

    “Ya kumuua mtoto wa mzee Mbwana, Kaposhoo” Polisi yule alijibu.

    “Mmmh! Inawezekana vipi?”

    “Kwa nini?”

    “Mbona nae alitaka kuuawa jana usiku”

    “Hiyo wala hatujui. Kitu tunachokifahamu ni kwamba anatafutwa na vyombo vyote vya dola hapa Zambia” Polisi yule aliwaambia.

    “Kama ni muuaji, hakuna haja ya kumtafuta. Yupo hapa” Polisi aliyekuwa pale kaunta aliwaambia polisi wale waliotoka makao makuu.

    “Yupo hapa?”

    “Ndio. Yupo ndani ya chumba hiki. Ngoja tumlete. Yaani tulikuwa hatujui kama yeye ndiye aliyefanya mauaji haya. Ngoja tumchukue na kumpeleka makao makuu” Polisi yule aliwaambia wenzake, wote wakaziandaa bunduki zao kwa kuona kwamba Peter alikuwa muuaji mkubwa. Polisi yule akaingia ndani ya chumba kile tayari kwa kumleta Peter ambaye alikuwa chumbani.





    “Kama ni muuaji, hakuna haja ya kumtafuta. Yupo hapa” Polisi aliyekuwa pale kaunta aliwaambia polisi wale waliotoka makao makuu.

    “Yupo hapa?”

    “Ndio. Yupo ndani ya chumba hiki. Ngoja tumlete. Yaani tulikuwa hatujui kama yeye ndiye aliyefanya mauaji haya. Ngoja tumchukue na kumpeleka makao makuu” Polisi yule aliwaambia wenzake, wote wakaziandaa bunduki zao kwa kuona kwamba Peter alikuwa muuaji mkubwa. Polisi yule akaingia ndani ya chumba kile tayari kwa kumleta Peter ambaye alikuwa chumbani.

    ****

    Peter alikuwa amekaa ndani ya chumba kile katika kituo cha polisi cha Mansansa. Muda wote macho yake yalikuwa yakiangalia televisheni tu. Hakuonekana kuwa na raha hata mara moja, kichwa chake kilikuwa kikimfikiria mpenzi wake ambaye katika kipindi hicho hakuwa nae tena, Gloria.

    Bado hakuonekana kuamini juu ya kila kitu ambacho kilikuwa kimetokea, kwake, Gloria alionekana kuwa mwanamke tofauti sana, mwanamke ambaye alibadilika kwa asilimia mia moja kwa kumtaka auawe muda wowote ule kwa sababu alikuwa amepata mwanaume ambaye alikuwa na fedha kuliko yeye.

    Peter alikuwa amepanga kukaa ndani ya kituo hicho mpaka saa tatu asubuhi muda ambao angeondoka na kuelekea nyumbani ambapo huko angechukua kila kilicho chake na kisha kuondoka zake kurudi Tanzania. Ilipofika saa 2:35, Peter akaonekana kushtuka mara baada ya kuangalia taarifa ya habari na kuona picha yake huku taarifa ikitangazwa kwamba alikuwa akitafutwa nchini Zambia na yeyote ambaye angefanikisha kupatikana kwake angepewa zawadi nono ya fedha taslimu, kwacha milioni kumi.

    Peter hakuonekana kuamini kile alichokuwa akikiona kwenye televisheni, hakuamini kama taarifa zilikuwa zimeanza kuzagaa kwamba alikuwa amehusika katika mauaji ya Kaposhoo jambo ambalo hakuwahi kulifanya au kulifikiria hata siku moja. Tayari akaona kwamba mahali hapo hakukuwa sehemu sahihi ya kuendelea kukaa kwani endapo asingefanya harakati za kuondoka mahali hapo, angeweza kutiwa katika mikono ya sheria.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Lazima niondoke” Peter alijisemea.

    Hakutaka kuendelea kubaki mahali hapo, aliiona hatari kubwa ambayo ilikuwa mbele yake, alijua fika kwamba endapo asingefanya jitihada za kuondoka mahali hapo basi kungeweza kutokea hatari zaidi.

    Peter akasimama na kisha kuufuata mlango, akaufungua na kisha kuanza kuondoka mahali hapo. Kaunta hakukuwa na mtu yeyote yule jambo ambalo lilimfanya kutoka kwa kujiamini sana. Nje ya kituo kile, kulikuwa na polisi ambao walikuwa wamekaa wakipiga stori lakini hakukuonekana na polisi yeyote ambaye alimuona Peter wakati anatoka ndani ya kituo kile kitu ambacho kilimfanya Peter kukata kona kulia, akaelekea nyuma ya kituo kile na kisha kuondoka mahali hapo huku akikimbia.

    “Gloria....Gloria....Gloria....” Peter alijisemea katika kipindi ambacho alikuwa akikimbia kuelekea nyumbani.

    Peter alikuwa akikimbia kwa kasi kuelekea nyumbani. Bado kichwa chake kilikuwa kikimfikiria Gloria ambaye alimuona kwamba alimuingiza katika matatizo ambayo alikumbana nayo katika kipindi hicho. Jambo ambalo lilimshangaza na kumstua Peter, picha zake zilikuwa zimebandikwa katika kila sehemu katika jiji lote la Lusaka.

    Mzee Mbwana alionekana kuwa na hasira na Peter, kwa sababu alikuwa na fedha nyingi, aliamua kuchapisha picha nyingi za Peter na kisha kuzibandika katika sehemu nyingi nchini Zambia kwa kutaka kila mtu aweze kuziona na kumkamata popote pale ambapo angeweza kuonekana.

    Peter hakuchukua muda mrefu, akafika nyumbani, akaanza kuligonga geti lakini hakukuwa na mtu yeyote ambaye alikuja kulifungua. Peter hakuonekana kukata tamaa, akaendelea kuligonga geti lile, baada ya muda kidogo, mlinzi akafika mahali hapo, akamfungulia geti.

    “Peter...vipi tena rafiki yangu?” Mlinzi alimuuliza Peter ambaye alionekana kuchanganyikiwa.

    “Hapa sipo sawa Mbwiza” Peter alimwambia mlinzi.

    “Kwa nini?”

    “Nimesingiziwa kuua”

    “Nimeona picha zako zimebandikwa kila kona. Sasa kwa nini uliamua kumuua Kaposhoo?” Mlinzi alimuuliza Peter.

    “Hapana. Sikumuua. Siwezi kumuua kaposhoo. Kaposhoo alitekwa na watu ambao walikuja kuniteka na mimi pia” Peter alimwambia Mbwiza.

    “Mbona baba yake aliniambia kwamba wewe ndiye uliyemuua Kaposhoo” Mbwiza alimwambia Peter.

    “Baba yake ndiye kasema hivyo?”

    “Ndio”

    “Hapana. Sikumuua kaposhoo. Sikumuua Kaposhoo Mbwiza, naomba uelewe hilo, sikumuua Kaposhoo” Peter alimwambia Mbwiza huku akianza kutokwa na machozi.

    “Sasa ni nani aliyemuua?”

    “Watakuwa wale watu waliomteka kwani hata mimi waliponiteka walitaka kuniua pia” Peter alimjibu Mbwiza.

    “Sawa. Nimekuelewa. Kwa hiyo umerudi kufanya nini hapa?” Mbwiza alimuuliza Peter.

    “Mimi si mkaaji mahali hapa Mbwiza. Nimekuja kuchukua baadhi ya vitu vyangu ili niondoke” Peter alimwambia Mbwiza.

    “Uondoke uelekee wapi?”

    “Nyumbani”

    “Tanzania?”

    “Ndio”

    “Leo hii hii?”

    “Ndio”

    “Hapana Peter. Umekwishachelewa, hakuna gari linaloondoka kuelekea nje ya nchi kwa sasa, labda ingekuwa alfajili” Mbwiza alimwambia peter.

    “Najua Mbwiza, ila napo kukaa hapa ni hatari sana. Nchi nzima inanitafuta, imekwishatangazwa kwamba nimeua, nisipofanya hivyo nitakamatwa na hata kupewa hukumu ya mauaji” Peter alimwambia Mbwiza.

    Peter hakutaka kuendelea kubaki mahali hapo kuongea na mlinzi, alijiona akichelewa sana kitu ambacho kikamfanya kupiga hatua kuufuata mlango wa kuingia sebuleni. Kichwa chake kilikuwa kimechanganyikiwa, kila kitu ambacho kilikuwa kikimtokea hakuamini kama kilikuwa kikimtokea katika kipindi hicho. Msichana wake, Gloria alionekana kusababisha mambo hayo yote, japokuwa alimuonyeshea mapenzi ya dhati lakini yeye aliamua kuyajibu tofauti na alivyotegemea.

    Mara baada ya kufika ndani, akaifuata simu yake na kisha kuichukua, akaanza kubonyeza vitufe na baada ya muda simu ikapokelewa. Sauti ya mama yake, Bi Stella ikaanza kusikika simuni. Hata kabla Peter hajaongea kitu chochote kile, akajikuta akianza kulia.

    “Hallo Peter” Sauti ya Bi Stella ilisikika upande wa pili.

    “Mama....” Peter aliita huku akilia.

    “Kuna nini Peter?”

    “Gloria mama”

    “Amefanya nini tena?”

    “Amenifanyia mambo mabaya sana”

    “Kuna mengine yametokea tena?” Sauti ya Bi Stella ilisikika ikiuliza.

    “Nimesingiziwa kesi ya mauaji mama. Nimesingiziwa kumuua kaposhoo mama” Peter alimwambia mama yake.

    “Kesi ya mauaji?” Bi Stella aliuliza kwa mshtuko.

    “Ndio mama. Nimesingiziwa kumuua Kaposhoo” Peter alimwambia mama yake huku akilia.

    “Kwa hali hiyo, naomba urudi nyumbani Peter” Mama yake, Bi Stella alimwambia Peter.

    “Nitakuja mama. Ila alichonifanyia Gloria, milele sitoweza kukisahau” Peter alimwambia mama yake.

    Peter hakutaka kuongea zaidi, alichokifanya ni kukata simu ile na kisha kukaa kitandani. Bado alionekana kuwa mwenye majonzi mengi, hakuonekana kuamini kama katika kipindi hicho alikuwa akipitia hali hiyo, lawama zake zote alikuwa akimbebesha Gloria kwani alijua kwamba nae alihusika katika kuwataarifu polisi kwamba yeye ndiye alikuwa amemuua Kaposhoo.

    “Hapa ni kutafutana tu. Ni lazima nimuue Gloria. Nisipomuua mimi, ataniua yeye” Peter alijisemea na kisha kuchukua baadhi ya vitu vyake ambavyo ni rahisi kubebeka na kisha kutoka nje.

    “Mungu wangu!!”

    Peter hakuonekana kuamini kile ambacho alikuwa akikiona mbele ya macho yake, vijana watatu ambao walikuwa na mapanga mikononi walikuwa wamesimama getini huku wakimuangalia yeye, tayari alikwishajua kwamba mahali hapo kulikuwa na hatari ambayo ilitaka kutokea kwa kuona kwamba vijana wale walikuwa miongoni mwa vijana ambao walikuwa wamemteka.

    Peter akabaki akiwa amesimama tu, kichwa chake kikaanza kujifikiria ni kitu gani ambacho alitakiwa kufanya mahali hapo. Huku akiwa hajui nini cha kufanya, mlinzi, Mbwiza akatokea na kisha kuungana na vijana wale, Peter akaonekana kuhisi kitu.

    “Kila mtu anataka kuwa tajiri Peter. Wewe twende tu tukupeleke kituo cha polisi” Mbwiza alisema kwa sauti huku akimwangalia Peter.

    Hapo ndipo ambapo Peter akaonekana kugundua kwamba vijana wale walikuwa wamekuja mahali pale kwa lengo moja tu, kumkamata na kisha kumfikisha kituo cha polisi. Kitita kikubwa cha kwacha milioni kumi ambacho kingetolewa kwa mtu yeyote ambaye angefanikisha kumkamata Peter.

    Hapo ndipo ambapo Peter akaona kwamba hata Mbwiza mwenyewe hakuwa mtu mzuri, alikuwa miongoni mwa watu ambao walikuwa wakikihitaji kiasi hicho cha fedha na ndio maana alikuwa amewaita vijana kwa ajili ya kushirikiana kumkamata na kumpeleka katika kituo cha polisi.

    “Hebu tumchukueni” Mbwiza alisema na hapo hapo vijana wale kuanza kupiga hatua kumfuata Peter, mikononi walikuwa na mapanga, mapanga hayo yalikuwa na lengo la kumjeruhi tu kama kumchosha endapo angeleta usumbufu.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Walijua kabisa kwamba hata kama ungemkata Peter mguu na kumpeleka kituo cha polisi, hilo lisingeonekana kuwa tatizo, mtu aliyekuwa akihitajika alikuwa peter, haijalishi awe kilema au vyovyote vile, alikuwa akihitajika akiwa hai tu. Peter akabaki akitetemeka tu huku hajui ni kitu gani ambacho alitakiwa kukifanya mahali hapo ambapo vijana walikuwa wamebakisha hatua kumi kabla ya kumfikia.

    *****

    Polisi yule aliyekuwa kaunta akaingia ndani ya chumba kile, kichwani alikuwa na uhakika wa asilimia mia moja kwamba Peter alikuwepo ndani ya chumba hicho na hivyo hawakutakiwa kuwa na wasiwasi wowote ule, akaufungua mlango na kisha kuingia ndani, Peter hakuonekana ndani ya chumba hicho.

    “Hayupo” Polisi yule alisema kwa mshangao.

    “Wewe si umesema yupo?”

    “Ndio. Alikuwepo muda mchache uliopita”

    “Sasa atakuwa amekwenda wapi?”

    “Sijui kwani kama ametoka, hatukuweza kumuona” Polisi yule alijibu.

    Kila mmoja alikuwa na uhakika kwamba endapo Peter alikuwa ameondoka basi hakuwa amefika mbali na kituoni hapo, walichokifanya, baadhi ya polisi ni kuanza kuelekea nyumbani kwa Kaposhoo ambapo alikuwa akiishi peter. Njiani, walikuwa wakitembea kwa mwendo wa haraka haraka, mikononi walikuwa na bunduki, walijua fika kwamba katika kipindi hicho Peter alionekana kuwa mtu hatari sana, mtu ambaye hakutakiwa kuletewa masihala hata kidogo.

    “Kama tukifika hapo nyumbani, kwanza ni kumpiga kwa usumbufu na kisha kuondoka nae” Polsi mmoja aliwaambia wenzake.

    “Kuhusu kupiga, odnoa shaka au labda kama kuna jingine” Polisi mwingine alimwambia.

    Bado walikuwa wakielekea kwa mwendo wa kasi kueleke nyumbani kwa Kaposhoo, wala hawakuchukua muda mrefu sana, wakafika mahali hapo, geti lilikuwa wazi, wakaingia ndani, mlinzi hakuonekana katika kijumba chake. Walichokifanya ni kuusogelea mlango wa kuingilia sebuleni, walipojaribu kuufungua, mlango ulionekana kufungwa kwa ndani. Hata kabla hawajajua kipi cha kufanya, vijana watatu pamoja na mlinzi wakatokea mahali hapo huku wakiwa na mapanga, walipowaona polisi, wakaonekana kushtuka.

    “Vipi tena?” Polisi mmoja aliuliza huku wote wakiwanyooshea bunduki. Hakukuwa na kijana yeyote aliyejibu chochote kile.

    “Peter yupo wapi?” Polisi mmoja aliuliza.

    “Yule jamaa ninja aiseee” Kijana mmoja alijibu huku wote wakionekana kuchoka.



    Mlinzi Mbwiza akaonekana kuchanganyikiwa, hakuamini kwamba kitendo cha kufanikisha kukamatwa na Peter kingeweza kumfanya kupata kiasi cha kwacha milioni kumi, kiasi ambacho kingemfanya kuwa na fedha nyingi na kufungua biashara zake ambazo zingemfanya kuingiza fedha kila siku.

    Katika kipindi ambacho alikuwa amezipata taarifa zile, Peter hakuwepo nyumbani jambo ambalo lilimfanya kuwa na hamu kumuona tena na hivyo kufanikisha kile ambacho alikuwa amekifikiria. Suala la kumkamata Peter na kumpeleka kituo cha polisi lilionekana kuwa suala gumu sana, alijua fika kwamba kamwe asingeweza kulifanya peke yake, hivyo alitakiwa kuwa na watu wengine ambao angeweza kusaidiana nao.

    Hapo ndipo ambapo Mbwiza akaondoka nyumbani hapo na kuwafuata vijana ambao walikuwa katika mtaa huo kwa ajili ya kuwaomba kusaidiana kumtia nguvuni Peter na hivyo kumpeleka katika kituo cha polisi.

    “Ndio maana nilipomuona kwenye televisheni nikaanza kujiuliza huyu jamaa nilimuona wapi vile, kumbe nilimuona kwenu aisee” Jamaa mmoja ambaye alipewa taarifa na Mbwiza alimwambia Mbwiza.

    “Kwa hiyo ndio hivyo” Mbwiza alimwambia.

    “Hakuna tatizo. Huo tayari ni utajiri. Hata kama tutapata milioni tano kila mmoja, bado ni fedha nyingi sana” Jamaa huyo, jackson alimwambia Peter.

    “Unafikiri sisi wawili tutaweza kumtia nguvuni?” Mbwiza aliuliza.

    “Mmmh! Sidhani. Anaweza kutuzidi nguvu huyu”

    “Sasa tufanye nini?”

    “Kama vipi tuongeze japo watu wawili”

    “Sasa tumchukue nani na nani?”

    “Ngoja kwanza” Jackson alisema na kisha kuondoka mahali hapo.

    Mbwiza alibaki akisubiri, kichwani mwake kwa wakati huo alikuwa akifikiria fedha tu, alijua kwamba endapo wangefanikisha kumtia nguvuni Peter basi lingekuwa jambo la maana sana ambalo lingewafanya kupata fedha za haraka haraka. Walihitaji kuongeza nguvu zaidi, walihitaji kupata watu wengine ambao wangeweza kuwasaidia katika kukamilisha mpango wao.

    Mbwiza alikaa mahali hapo mpaka katika kipindi ambacho Jackson alirudi huku akiwa na vijana wengine wawili. Hapo ndipo walipoanza kusuka mipango yao, japokuwa ilikuwa saa saba usiku lakini hakukuwa na mtu ambaye alikuwa na usingizi, kwanza walikuwa wakipanga mipango yao juu ya namna ya kumtia Peter nguvuni na kisha kujichukulia kiasi hicho cha fedha.

    “Kwa hiyo mpaka sasa hivi bado hajarudi?” Kijana mmoja aliuliza.

    “Bado” Mbwiza alijibu.

    “Ila atarudi kweli?” Jackson aliuliza.

    “Kurudi atarudi tu, hapa si ndio nyumbani kwake bwana, atarudi tu” Mbwiza alijibu.

    “Au nae amekwishajua kwamba anatafutwa?”

    “Kujua! Mmh! Sidhani. Nadhani bado hajajua. Hata kama amejua, kurudi lazima arudi” Mbwiza alijibu.

    “Sasa sisi tutampataje?” Kijana mwingine aliuliza.

    “Hilo ni swali la maana sana. Ila hapa ndio tupange sasa” Mbwiza aliwaambia.

    “Ila kumpata ni lazima tutumie silaha, hivi hivi hata sisi wanne anaweza kutushinda” Jackson aliwaambia.

    “Silaha gani unapendekeza tutumie?”

    “Mapanga”

    “Kwa hiyo unamaanisha tumjeruhi?”

    “Ikiwezekana. Mapanga yanakuwa tayari kama tutaona analeta usumbufu mkubwa, tunaweza kuyatumia” Jackson aliwaambia.

    “Sawa. Hapo hakuna tatizo, cha msingi ngoja nikamsikilizie nyumbani tuone itakuwaje” Mbwiza aliwaambia.

    “Poa. Akifika usisahau kutuambia, maisha magumu, kila mtu anahitaji fedha” Jackson alimwambia Mbwiza ambaye akaondoka mahali hapo.

    Mbwiza bado hakuonekana kuwa na raha, kichwa chake bado kilikuwa kikifikiria fedha tu, aliona kwamba endapo wangefanikisha kumkamata Peter basi wangeweza kupata kiasi kikubwa cha fedha ambacho kingewafanya kugawana na kila mtu kuondoka na chake.

    Mbwiza akaanza kumsubiria Peter, muda wote alikuwa macho kama kawaida yake, akilini mwake alikuwa akimfikiria Peter tu, alikuwa akitaka kumuona Peter akiingia mahali hapo na kisha kuwaambia wenzake na hivyo kufika mahali hapo na kumkamata. Usiku uliendelea kukatika, mpaka alfajiri inaingia, bado Peter hakuweza kutokea mahali hapo jambo ambalo lilimfanya Mbwiza kuona kwamba Peter alikuwa ameshtukia mchezo na hivyo asingeweza kurudi mahali hapo.

    “Bado hajafika, sijui ameshtukia mchezo” Mbwiza alimwambia jackson simuni.

    “Vuta subira tu. Subiri mpaka saa sita mchana, kama hajatokea basi atakuwa ameshtukia mchezo” Sauti ya Jackson ilisikika simuni.

    “Poa”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mbwiza aliendelea kusubiria mahali hapo. Muda ulizidi kusonga mbele kama kawaida, ilipofika saa tatu na robo asubuhi, geti likaanza kugongwa, alipolifungua, alikuwa peter.

    Mbwiza akaonekana kufurahi moyoni kiasi ambacho alitamani kumkumbatia Peter kwa furaha. Mbele yake, hakumuona Peter bali alikuwa akiziona fedha kiasi cha kwacha milioni kumi zikiwa zimesimama. Alichokifanya ni kumkaribisha, akaongea nae kidogo na Peter kuelekea ndani.

    Mbwiza hakutaka kusubiri mahali hapo, tayari alikuwa na uhakika kwamba Peter alikuwa amerudi mahali hapo kwa kuwa alikuja kuchukua baadhi ya vitu vyake kama alivyomwambia na hivyo angeweza kuondoka mahali hapo, alichokifanya ni kuwafuata marafiki zake kwa ajili ya kuwaambia juu ya ujio wa Peter nyumbani hapo.

    Hiyo ikaonekana kuwa taarifa nzuri, walichokifanya wakachukua mapanga yao na kisha kuanza kuelekea nyumbani hapo. Kitu ambacho walikuwa wamekipanga mahali hapo kilikuwa ni kumjeruhi peter endapo tu angeweza kuleta ushindani wowote kwao. Wala hawakuchukua muda mrefu, wakafika nyumbani hapo.

    “Yupo wapi?” Jackson aliuliza huku akionekana kuwa na uchu wa fedha.

    “Yupo ndani”

    “Hajaondoka huyu?”

    “Hakuna. Nilifunga geti. Hajatoka” Mbwiza alimwambia Jackson.

    Waliendelea kusubiri zaidi na zaidi getini hapo lakini bado peter hakuwa ametoka ndani. Kila mmoja hakutaka kukata tamaa, kila mtu alikuwa na uhakika kwamba Peter alikuwa ndani ya nyumba ile. Baada ya dakika kumi, Peter akatoka ndani ya nyumba ile, alipofika nje, akasimama, akaangalia mbele, vijana watatu, wa nne akiwa Mbwiza walikuwa wamesimama huku wameshika mapanga, peter akaonekana kuhofia kupita kawaida, alijua kwamba vijana wale hawakuwa mahali pale kiamani, walikuwa kivita zaidi.

    *****

    Peter alibaki akiwa amesimama, hakujua ni kitu gani ambacho alitakiwa kukifanya mahali hapo, vijana wale walikuwa wamesimama huku wakiwa na mapanga mikononi mwao, Peter hakujua ni kitu gani ambacho alitakiwa kukifanya mahali hapo, aliona kwamba endapo angebaki mahali hapo basi vijana wale wangeweza kumkamata na hivyo kumfikisha katika kituo cha polisi.

    Katika kipindi ambacho vijana wale walikuwa wakipiga hatua kumfuata, Peter akaona kwamba hakukuwa na kitu kingine ambacho alitakiwa kukifanya mahali hapo zaidi ya kukimbia tu. Kwa kasi ya ajabu akageuka nyuma, akaufungua mlango na kisha kuingia ndani huku akiwa ameufunga.

    Mbwiza na wenzake wakaufikia mlango na kisha kuanza kuupiga huku lengo lao likiwa ni kuuvunja na kisha kuingia ndani kwa lengo la kumkamata Peter ambaye kwao alionekana kuwa njia ya mkato kuwapa kiasi kikubwa cha fedha.

    Peter akaanza kuelekea chumbani, tayari aliona kwamba alikuwa kwenye hatari kubwa ambapo kama asingeweza kufanya jambo fulani basi angeweza kukamatwa na hivyo kufikishwa katika vyombo vya sheria. Alichokifanya mule ndani ni kuanza kuufuata mlango wa nyumba, jikoni na kisha kuufungua.

    Alipoona kwamba mlango umefunguka, akaufuata ukuta uliozunguka nyumba ile kwa lengo la kuuparamia. Vijana wale ambao walikuwa pamoja na Mbwiza walipoona kwamba mlango ulikuwa umefungwa, kwa haraka sana wakaanza kuelekea nyuma ya nyumba ile kwani walijua kwamba mlango wa nyuma ulikuwa wazi hivyo peter angeweza kuwatoroka.

    Walipofika nyumba ya nyumba ile, kila mmoja akapigwa na mshtuko, peter alikuwa akionekana mbele yao huku akiwa ameuparamia ukuta na alibakisha hatua ndogo sana ili aweze kurukia upande wa pili. Walichokifanya vijana wale huku wakionekana kuwa kwenye mshtuko mkubwa, wakaanza kumrushia mapanga ambayo yalipiga ukuta na kunguka chini, peter akawa amerukia upande wa pili na kutokomea kusipojulikana.

    “Tumemkosa” Jackson aliwaambia wenzake.

    “Tuzungukeni upande wa nyuma” Kijana mwingine aliwaambia.

    “Tutamkosa tu. Mpaka ufike upande wa nyuma tutachukua muda mrefu sana kwani hapo kati kuna nyumba nyingi sana ambazo zimejengwa” Mbwiza aliwaambia wenzake.

    Mategemeo ya kupata fedha ambayo yalikuwa ndani ya vichwa vyao yakaonekana kupotea, mtu ambaye alionekana kuwa njia ya mkato kuwapatia fedha alikuwa amewatoroka na kuelekea katika sehemu ambayo hawakuweza kuifahamu. Walichokifanya ni kuchukua mapanga yao, walipoondoka kuelekea mbele ya nyumba ile, midomo ya bunduki ilikuwa ikiwaangalia.

    “Peter yupo wapi?” Polisi mmoja aliuliza huku akiwa amekunja ndita.

    “Yule jamaa ninja aiseeee” jackson aliwajibu.

    “Peter yupo wapi?” Polisi yule alilirudia swali lake huku akionekana kuwa na hasira.

    “Amekimbia. Ameruka ukuta kutokea upande wa pili. Tulitaka kumkamata kama nyie mnavyotaka kumkamata” Mbwiza aliwaambia polisi wale.

    Polisi hawakuonekana kuamini maneno yale, walichokifanya ni kuufuata mlango wa kuingilia sebuleni na kisha kuanza kuufungua. Mlango ukaonekana kufungwa kwa ndani, walichokifanya ni kuzunguka upande wa nyuma ambapo wakaufungua mlango wa jikoni na kisha kuingia ndani.

    Wakaanza kumtafuta peter katika kila kona, hawakuonekana kuyaamini maneno ya vijana wale, kwao, vijana wale waliuonekana kama kumficha Peter na hivyo hawakutaka aonekane. Walimtafuta kwa zaidi ya nusu saa tena katika vyumba vyote lakini Peter hakuweza kuonekana machoni mwao.

    “Kwa hiyo mlisema alikimbia?” Polisi mmoja aliwauliza.

    “ndio. Aliparamia ukuta. Nyie si mnaona hapa tuna mapanga” jackson aliwaambia.

    “Sasa hayo mapanga ya nini?”

    “Ya kumjeruhi endapo angejifanya mbishi” jackson aliwajibu.

    “Huyu atakuwa mitaani, ni lazima atafutwe mitaani” Poilisi mmoja alisema na kisha wote kutoka mahali hapo, kitu ambacho walikuwa wakikijua, peter hakuwa amefika mbali na eneo lile, hivyo walitakiwa kumtafuta mpaka kumpata.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mzee Mbwana alionekana kuwa kwenye hali mbaya, hakujua ni kitu gani ambacho alitakiwa kukifanya. Moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali, hakuamini kama kijana Peter angeweza kufanya kile ambacho alikuwa amekifanya. Alimpenda Peter kama mtoto wake, alikuwa akimpa vitu vingi pamoja na kumkubalia Kaposhoo kuishi na huyo rafiki yake katika nyumba ya kifahari ambayo alikuwa amemjengea mtoto wake, Kaposhoo.

    Leo hii, huyo huyo Peter ndiye ambaye alichukua uamuzi wa kumuua mtoto wake pekee ambaye alikuwa akimpenda sana, Kaposhoo. Kama kujeruhiwa, tayari moyo wake ulikuwa umejeruhiwa vibaya sana na ulikuwa katika maumivu makali mno. Alimchukia Peter, alimchukia kutokana na kile kitendo ambacho alikuwa amekifanya, kumuua mtoto wake ambaye alikuwa akimpenda sana.

    Alijua fika kwamba alikuwa ametoa taarifa katika kituo cha polisi na hivyo Peter angeanza kutafutwa muda wowote ule lakini bado hakuonekana kuridhika. Kitu ambacho alikuwa akikihitaji katika kipindi hicho ni kusikia kwamba Peter alikuwa amekufa, hiyo ndio ilikuwa taarifa ambayo alikuwa akitamani sana kuisikia kutoka masikioni mwake.

    “Nitamuua tu, kama polisi hawajampata, nitamuua tu” Mzee Mbwana alisema huku akionekana kuwa na hasira.

    Alichokifanya ni kuwaita vijana wake wa kazi ambao alikuwa akiwaaminia sana, vijana ambao walikuwa wakimfanyia kazi kwa uaminifu mkubwa na kisha kuwapa jukumu moja ambalo kwake lilionekana kuwa jukumu jepesi sana kwao, jukumu la kumuua Peter na kisha kumletea mwili wake tu ambapo kwa mkono wake angeweza kuuchoma moto na kubaki majivu tu.

    Hilo wala halikuonekana kuwa tatizo kwa vijana wake, kitu ambacho bosi wao alikuwa akikitaka kutoka kwao kingeweza kufanya tena ndani ya siku chache tu kila kitu kingekuwa tayari. Walichokifanya ni kuchukua bunduki zao na kisha kuanza kazi huku wakienda sambamba na polisi.

    “Utafurahi mwenyewe bosi” Kijana mmoja, Revocatus alimwambia mzee Mbwana.

    “Ndio nataka nyie muikamilishe furaha yangu, isiwe furaha ya kuongea tu” Mzee Mbwana alimwambia revocatus,

    “Cha msingi tuachie sisi tu, hii kazi ni nyepesi sana”

    “Nawaamini”

    Kitu alichokifanya mzee Mbwana ni kuwapa kiasi cha fedha cha kwacha milioni mbili kwa ajili ya matumizi yao ya hapa na pale na kisha kuwaambia kuingia kazini. Kwao, kwa sababu walikuwa wakifahamiana na watu wengi ndani ya nchi ya Zambia hilo wala halikuonekana kuwa tatizo kabisa, waliona kwamba wangeweza kufanikisha kila kitu tena kwa haraka mno.

    “Tuna siku ngapi?” Pius aliwauliza wenzake.

    “Wiki moja”

    “Basi hakuna tatizo, tukamilisheni kila kitu”

    Walichokifanya mahali hapo ni kuanza kuwasiliana na askari wa mipakani ambao walikuwa maswahiba zao na kutaka kupewa taarifa juu ya kila kitu ambacho kingeendelea endapo wangefanikiwa kumuona Peter ambaye alikuwa akitafutwa sana nchini Zambia.

    Askari hao hawakuwa na tatizo, kwa sababu nao walikuwa sehemu ya kila mchongo ambao alikuwa akiutoa mzee Mbwana, wakawakubalia na mambo mengine kuendelea kama kawaida.

    Kitu ambacho walikuwa wakikifahamu kwa wakati huo ni kwamba kulikuwa na uwezekano mkubwa wa Peter kuondoka nchini Zambia na kurudi nyumbani kwao nchini Tanzania na hivyo hali ingekuwa ngumu sana kwa wao kumpata na kuufikisha mwili wake kwa mzee Mbwana.

    “Kwa hiyo tuanzie mpakani?” Pius aliwauliza wenzake wawili.

    “Kama itawezekana”

    “Mpaka upi sasa?”

    “Mpaka wa Zambia na Tanzania” Revocatus aliwaambia wenzake.

    “Kwa nini tusielekee katika mipaka mingine?”

    “Sikilizeni. Watanzania ni waoga sana, hakuna mtanzania anayeweza kwenda kwenye mipaka ya Kongo, wengi wanawahofia wakongo kutokana na ukatili wao” Revocatus aliwaambia wenzake.

    “Kwa hiyo hapa twende kwenye mpaka wa Zambia na Tanzania?”

    “Hicho ndicho nilichomaanisha. Huyu mtu hatokuwa na lengo la kwenda Kongo, moja kwa moja atataka kwenda nyumbani kwao” Revocatus aliwaambia.

    Hakukuwa na cha kupoteza, walichokifanya ni kuondoka mahali hapo huku kila mmoja akiwa na lengo la kwenda katika mpaka wa nchi ya Zambia na Tanzania.

    Wakatoka ndani ya chumba walichokuwa na moja kwa moja kulifuata gari lao kwa lengo la kuelekea mpakani. Kutoka Lusaka mpaka mpakani kulikuwa na umbali mkubwa sana kwa zaidi ya kilometa elfu moja. Walipolifikia gari lao, wakaingia ndani na kisha safari ya kuelekea mpakani kuanza huku kila mmoja akionekana kuwa hasira na Peter, kijana ambaye wala hawakuwahi kumuona zaidi ya kuwa na picha zake tu.

    ****

    Mapenzi yakaonekana kuingia doa, kila mmoja katika kipindi hicho alikuwa na wasiwasi na Peter tu ambaye alikuwa akiendelea kuvuta pumzi ya dunia hii. Uwepo wa Peter duniani ungekuwa na maana kubwa sana, maana ya kwanza ungewafanya kutokuwapa uhuru mkubwa wa kutanua huku wakijua kwamba muda wowote ule kijana yule angeweza kufanya kitu chochote kibaya katika maisha yao.

    Peter alihitajika kuuawa ili kila kitu kiwe kama kilivyopangwa. Hawakuonekana kuwa na wasiwasi na Kaposhoo, tayari Bwana Stewart alikuwa amekamilisha kila kitu kwa kuwatuma vijana wa kundi la Kunta Kinte ambalo lilikuwa limekamilisha kila kitu pasipo kugundua kwamba kijana huyo alikuwa hai.

    Peter ndiye ambaye alikuwa akiviumiza vichwa vyao kwa wakati huo, hawakutaka kumuona kijana huyo akiendelea kuvuta pumzi ya dunia hii, kwa haraka sana walihitaji kuona kijana huyo akiuawa kama ilivyokuwa kwa Kaposhoo. Vijana wa kundi la Kunta Kinte ndio ambao walitakiwa kukamilisha kila kitu.

    “Mmmh! Yaani sina hata raha baby” Gloria alimwambia mpenzi wake ambaye alikuwa na umri sawa na wa baba yake, Bwana Stewart.

    “Kwa nini?”

    “Uwepo wa Peter. Yaani mtu huyu akiendelea kuwa hai, kila kitu kinaweza kuharibika” Gloria alimwambia Bwana Stewart.

    “Usiwe na wasiwasi, kama alivyokufa Kaposhoo, na huyu nguchiro nae atakufa tu” Bwana Stewart alimwambia Gloria.

    “Waambie wafanye haraka hata kabla wazazi hawajajua kinachoendelea” Gloria alimsisitiza Bwana Stewart.

    “Hilo si tatizo, kila kitu kitakwenda sawa, ni ishu ya muda tu ndio iliyobakia” Bwana Stewart alimwambia mpenzi wake, Bwana Stewart.

    “Naamini litawezekana tu, mtu mmoja hawezi kusumbua maelfu, na hawezi kusumbua watu wenye fedha na mahandsome kama wewe” Gloria alimwambia Bwana Stewart ambaye akaachia tabasamu pana, tabasamu lilionyesha hasira kwa mbali, hasira juu ya Mungu ambaye alikuwa amempa mvi kichwani mwake.

    “Niamini. Nakupenda mpenzi”

    “Nakupenda pia”

    Japokuwa walionekana kuwa kwenye mapenzi ya dhati lakini bado kila mmoja alionekana kuwa na wasiwasi, hakukuwa na mtu ambaye alikuwa akitaka Peter aendelee kuvuta pumzi ya dunia hii, tayari Peter akaonekana kuwa tatizo kubwa katika mahusiano yao na walitaka kumpoteza kwa haraka sana hata kabla mambo hayajaharibika.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kwa Bwana Stewart, bado alikuwa akiwaamini sana vijana wa kundi la Kunta Kinte ambao walikuwa mstari wa mbele kukamilisha kazi zake. Mpaka katika kipindi hicho hakujua kwamba vijana wale ambao alikuwa akiwaamini sana walikuwa wameshindwa kutekeleza kazi zote mbili ambazo alikuwa amewapa, hawakuweza kumuua Kaposhoo kama alivyoagiza na wala hawakuweza kumuua Peter kama alivyowaagiza.

    Wote wawili wakaanza kusubiri taarifa kutoka kwa vijana wa kundi la Kunta Kinte ili kujua kwamba kama ishu ilikuwa imekwishafanyika kama alivyoagiza au haikuwezekana kufanyika. Muda ukaanza kwenda, ukaenda zaidi na zaidi, dakika zikazidi kusogea mbele lakini hali ikaonekana kuwa kimya.

    Hawakujua ni kitu gani ambacho kilikuwa kimetokea mpaka hali kuwa vile, simuni hawakuweza kupatikana, yaani simu zilikuwa zikiita tu lakini hakukuwa na mtu yeyote ambaye alipokea simu yake. Hali ile ikaanza kuwatia hofu kwamba kulikuwa na kitu ambacho kilikuwa kimetokea na hivyo walishindwa kukamilisha kazi ile.

    Bwana Stewart akajipa uvumilivu, kitu ambacho alikuwa akikiamini ni kwamba vijana wale walikuwa wamekamilisha kila kitu na ni matanuzi tu ndio ambayo walikuwa wakiyafanya kwa wakati huo.

    “Nina wasiwasi baby” Gloria alimwambia Bwana Stewart.

    “Wasiwasi wa nini tena?”

    “Watu wako wananitia wasiwasi sana”

    “Kwa nini?”

    “Mbona wapo kimya sana?”

    “Hilo si tatizo. Kila kitu kitakuwa kimefanyika, hautakiwi kuhofia chochote mpenzi” Bwana Stewart alimwambia Gloria ambaye dhahiri alionekana kuwa na wasiwasi.

    “Sasa kama kazi wameifanya, kwa nini wasipige simu na kutoa taarifa?” Gloria aliuliza.

    “Bado sijajua kwa nini. Unajua fedha nilizowapa ni nyingi mno, inawezekana zimewatia wazimu na kuwafanya kutanua bila kufanya kazi niliyowaambia waifanye” Bwana Stewart alimwambia Gloria.

    “Mmmh! Kama unawaamini, sawa, ila kwani naona nishaanza kuingiwa na wasiwasi” Gloria alimwambia Bwana Stewart.

    Wasiwasi haukumtoka Gloria kwa kuona kwamba bado Peter alikuwa hai. Moyoni mwake hakuwa na amani hata kidogo, alijua fika kwamba endapo Peter angekuwa hai basi mtu huyo angeweza hata kumuua kutokana na kile ambacho alikuwa amemfanyia. Kila alipokuwa akimwambia Bwana Stewart juu ya wasiwasi ambao alikuwa nao, Bwana Stewart alimtoa hofu kwani moyoni mwake alikuwa na uhakika kwamba vijana wake walikuwa wameifanya kazi ile.

    Muda ulizidi kusogea, hakukuwa na simu yoyote iliyoingia kutoka kwa vijana wale. Muda wote masikio yao yalikuwa yakisikilizia simu kutoka kwa vijana hao lakini hakukuwa na simu yoyote ile. Kuanzia hapo hata Bwana Stewart akaonekana kuwa na wasiwasi, mpaka inatimia saa saba usiku, hali ilikuwa kimya kabisa.

    “Kuna kitu kinaendelea” Gloria alimwambia Bwana Stewart.

    “Unahisi kitu gani?”

    “Wameshindwa kumuua Peter” Gloria alimwambia Bwana Stewart.

    “Haiwezekani. Labda sio Kunta Kinte. Hawana rekodi ya kushindwa kabisa” Bwana Stewart alimwambia Gloria.

    “Sasa kama wamemuua, kwa nini wasipige simu kutoa taarifa mpaka wanatuacha tunakaa roho juu juu?” Gloria aliuliza.

    “Hata mimi nashangaa. Hebu tusbiri kwanza” Bwana Stewart alimwambia Gloria na kuendelea kusubiri zaidi.

    Hali haikuonekana kubadilika hata kidogo, bado ilikuwa vile vile. Hakukukuwa na simu iliyoingia kutoka kwa vijana wa kundi lile, mpaka wanalala saa nane usiku, bado hali ilikuwa vile vile.

    Usingizi wao ulikuwa wa mang’amung’amu, hakukuwa na mtu ambaye alilala usingizi wa amani, bado walikuwa na wasiwasi mno. Ilipofika saa moja asubuhi, wakaanza kupiga simu za vijana wale, leo hazikuwa zikipatikana kabisa jambo ambalo liliwachanganya kupita kiasi.

    “Na mimi nimeanza kuhisi, kutakuwa na kitu” Bwana Stewart alimwambia Gloria.

    “Wewe umehisi nini?”

    “Simu zao zitakuwa zimekwisha chaji” Bwana Stewart alimwambia Gloria.

    “Simu zao zimekwisha chaji?” Gloria aliuliza huku akionekana kumshangaa Bwana Stewart ambaye alionekana ‘serious’ na jibu lake.

    “Yeah! Jana usiku zilikuwa zikiita tu, leo hazipatikani, unahisi nini hapo?” Bwana Stewart aliuliza.

    “Watakuwa wameshindwa kumuua Peter”

    “Hiyo ngumu”

    “Niamini mpenzi”

    “Ngoja nijaribu kitu kimoja”

    “Kitu gani?”

    “Nimpigie simu Mbwana”

    “Umwambie nini sasa?”

    “Na yeye si anataka kumuua Peter, ngoja nisikie ataniambia nini?” Bwana Stewart alimwambia Gloria.

    “Hakuna tatizo” Gloria alisema na kisha Bwana Stewart kuanza kumpigia simu mzee Bwana na kutaka kusikia kuhusu Peter, kijana ambaye alikuwa akitafutwa na polisi, wananchi, vijana wa mzee Mbwana.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Je nini kitaendelea?

    je Peter atauawa na vijana wa mzee Mbwana?

    Je Peter atakamatwa na polisi au wananchi?



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog