Simulizi : Sitasahau
Sehemu Ya Tatu (3)
Ni baada ya kupata kazi ndipo nilichukua jukumu la kulea wazazi wangu, ulikuwa mzigo ambao katu sikuweza kuepa. Nikabeba majukumu. Majukumu niliyostahili kuyabeba. Haraka nilimsimamisha Baba na Mama yangu kulima kwa kutumia jembe la mkono, kisha nikawa naweka vibarua huku wao wakibakia kuwa wasimamizi tu. Pia nililazimika kuwawekea msichana ambaye muda mwingi atakuwa anawasaidia kwa kazi za pale nyumbani. Kila mwezi nilituma kiasi fulani cha pesa kwa ajili ya kununulia mahitaji ya hapo nyumbani. Wazazi wangu walifurahi sana na kila mara walikuwa hawachoki kuniombea mimi mtoto wao.
Pengine, ushirikiano wangu na upendo wangu kwa kila mtu pale kazini uliwavutia sana wakuu wangu,nilijiambia. Hata pia utendaji wangu kazini ulikuwa wa hali ya juu na hata kufikia kupata tuzo ya mfanyakazi bora wa shirika kwa miaka miwili mfululizo. Karibu wafanyakazi wengi pale ofisini walikuwa wakinipenda na kuwa karibu nami. Na hata aliyekuwa Meneja mkuu hayati mzee Johnson Ndeluma alikuwa ananipenda sana na siku zote alikuwa anapeleka ripoti kuhusu mimi makao makuu. Hapo ndipo maswali yangu ya kuteuliwa kwangu kuwa meneja mkuu wa shirika kwa upande wa Tanzania yalipopata majibu katika wakati sahihi. Nikatabasamu!
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya kumaliza kila kitu na kukabidhi ofisi kwa mtu atakayekaimu nafasi yangu mpaka pale nitakapomaliza likizo yangu kisha kukabishi nyaraka za kitengo nilichokuwa mwanzo kwa msaidizi wangu wa kazi kama barua ile ilivyoeleza. Msaidizi wangu moja kwa moja anaenda kuwa ofisa wa IT ofisini hapo. Kila kitu nilikifanya kwa haraka kisha niliwasha gari yangu na kuelekea katika ufukwe wa Coco ulioko katikati ya jiji la Dar Es salaam ili angalau nipunge upepo na kufurahia kuwaona watoto waliotoka katika maisha ya tofauti wakijimwaga kwenye ufukwe huo.
Ufukwe wa Coco nilitokea kuupenda sana kwa sababu nilihisi ni sehemu sahihi kwa mtu mwenye msongo wa mawazo kufika hapo. Maana kila makundi ya watu hufika hapo tofauti na fukwe zingine ambazo huwezi kuingia mpaka ulipe kiingilio. Ufukwe huu ni bure na watu wa kila aina wanapatikana hapo.
Niliwasili katika ufukwe huo mida ya mchana, sikumbuki ilikuwa saa ngapi bali ilikuwa kati ya saa saba hadi saa nane mchana. Nikakijongea kiti cha plastic na kukaa hapo nje ya mgahawa na kuagiza kinywaji huku nikiwatizama vijana kwa watoto wakiogelea. Nilijisikia raha sana na kukumbuka nyakati nyingi zilizopita.
Wakati huo nilipokuwa mwanafunzi kule Tukuyu na kipindi fulani tulikuwa tunakwenda Matema beach kujivinjari. Kumbuka mpaka wakati huo sikuwa na mahusiano na msichana yoyote. Hata wale wafanyakazi wa kike waliokuwa wakijigonga ofisini waliishia njiani. Ilifikia hadi kupewa kashfa kuwa mie Jogoo halipandi mtungi. Binafsi sikujali kwa sababu niliufahamu ukweli.
Vile vile sikuwa mnywaji wa kilevi chochote na sikuwa mvutaji pia. Kinywaji changu pekee ni juice na soda tu. Baadhi ya marafiki zangu walikuwa wananidhihaki kwa kuniambia mie bado mshamba tu kwa sababu situmii kilevi kama wao. Nalo pia sikujali sana kwa upande wangu Kwa sababu kitu kimoja nilichokuwa nacho ni kusimamia kile ninachokiamini. Hicho ndicho kilichokuwa kinanisaidia.
Wakati nipo hapo Coco beach nikawaza sana na kisha nikajiambia likizo hii ya wiki moja yanipasa niende kuitumia Tukuyu pamoja na wazazi wangu ambako toka nilipohitimu chuo kikuu sikuwahi kwenda au niende sehemu nyingine nje ya Dar es Salaam?. Nikawaza sana. Wakati naendelea kuwaza jina la Zanzibari likapita kichwani mwangu. Ni hapo sauti mbili zikaanza kushindana na akili yangu katika maamuzi.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Upande mmoja ukaniambia ukienda Tukuyu ni sehemu sahihi zaidi kwako kwa sababu Baba na mama yako wana hamu kubwa ya kukuona. Na upande mwingine sauti ikanitaka nipuuze kwenda Tukuyu, na ikinitaka kuwa niende katika kisiwa cha Unguja kilichopo Zanzibari. Huko nitafurahia sana wakati wangu alafu pia kwenda Tukuyu ni vizuri niende na mchumba kumtambulisha. Sauti hizi mbili zikanifanya nibakie njia panda nisijue wapi ni sahihi zaidi. Mwishowe niliazimia kwenda Tukuyu mkoani Mbeya kuwaona wazazi wangu.
Baada ya kutosheka mahali hapo nikawasha gari na kurejea nyumbani kwangu Mbezi ya Kimara mahali ambako ndipo nilipopanga. Usiku huo kwangu ulikuwa mgumu sana, bado sauti ya kunishawishi nibatilishe uamuzi wangu wa kwenda Tukuyu na kisha niende Zanzibar haukukoma. Kila muda ulivyokuwa unakwenda ndivyo nikajikuta naanza kushindwa kuutetea uamuzi wangu nilioufanya kabla...Uamuzi wa kwenda Tukuyu. Sasa akili ikatawaliwa na kwenda Zanzibari.
Bila kutambua nikajikuta nawasha Laptop yangu ndogo na kuitafuta Zanzibar. Nikaanza kuona uzuri na mambo mengi yakaanza kunivutia.Simulizi za marafiki zangu ningali chuoni hasa kwa vijana wale watokao huko visiwani vikanifanya niufikirie mara mbili uamuzi wa kwenda Tukuyu haukuwa uamuzi sahihi. Bila ajizi nikabadili safari ya Tukuyu huku nikikubali ushauri wa kuwa nitaenda huko nikipata mchumba ili wazazi wangu wafurahi. Nikaamua niende Zanzibar. Ni Zanzibari ndipo historia yangu ikabadilika.
Baada ya kufikia makubaliano na akili yangu, na kuazimia kwenda Zanzibari. Usiku huo huo nikajikuta nikivutiwa na Hoteli ya MELIA iliyopo Zanzibar tena ni baada ya kusoma tangazo lao kwenye Gazeti siku chache zilizopita na usiku huo nikajikuta naitafuta hoteli hiyo kwenye mtandao. Ilionekana ni Hoteli nzuri kwa upande wangu. Nikachukua mawasiliano yao na kuongea nao usiku huo huo.
Hakika niliongea na muhudumu na kunifanyia Booking ya chumba cha stahiki yangu. Baada ya yote hayo nikajiuliza ni usafiri gani ambao ningeutumia kwenda huko kati ya Ndege au Boat. Hapo nilikuwa na uamuzi wa haraka sana. Sikuwahi safiri na chombo chochote cha majini nikaona hii ni fursa ya kipekee kutimiza ndoto hizo. Usafiri wa Boti ukawa chaguo lisilo na upinzani.
Bila kuchelewa, asubuhi ya saa kumi na mbili nilikuwa barabarani naelekea bandarini kwa ajili ya safari hiyo. Kutokana na foleni kubwa ya Dar Es salaam nikajikuta nakosa usafiri wa saa moja. Hivyo nikapata usafiri wa saa tatu na nusu asubuhi. Ni baada ya kupata tiketi kutoka ofisi za Azam Merine zilizoko hapo hapo Bandarini.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Saa tatu na nusu tayari nimo ndani ya Boti ya Kilimanjaro nikielekea Zanzibari. Hakika ilikuwa safari nzuri sana kwangu ukizingatia ilikuwa mara yangu ya kwanza kutumia usafiri wa majini. Pia sikuweza kukaa ndani kutokana na hofu ya kutapika. Basi nikakaa juu kabisa ambako kuna hewa na upepo unapatikana kwa wingi. Upepo ambao ulinisaidia nisitapike.
Masaa mawili baadae nilikuwa nateremka bandarini Unguja, kila abiria alikuwa mwenye furaha kubwa ya kufika salama. Nje ya geti nikaiona gari yenye maandishi ya Hoteli ya Melia na pembeni yake kuna mwanaume ameshika bango lenye jina langu kuwa yeye ndiye atakayenipokea. Nikamuendea na kujitambulisha kwake huku nikitoa kitambulisho na kumkabidhi mtu yule. Haraka alichukua begi langu dogo na kuweka mlango wa nyuma ya gari lake kisha akanifungulia mlango wa mbele pembeni yake. Kitabia huwa sipendi kukaa mbele katika chombo cha moto labda mimi niwe ndie Dereva. Huwa navutiwa kukaa nyuma zaidi kwa imani kuwa inapotokea ajali ni nadra mtu wa nyuma kupata tatizo na hata akipata huwa bahati sana kufa. Imani niliyokuwa naishikilia kwa muda mrefu sasa.
Siku hiyo nilipenda kukaa pembeni ya dereva. Ni uamuzi huo uliokuja kunipa furaha kubwa maana niliweza kuyasawiri maeneo mengi ya Zanzibar. Huku nikistaajabu na hali ya ukimya niliokuwa naushuhudia barabarani. "Hakika Zanzibar ni mji wenye kuvutia sana" Nilijisemea. Wakati naendelea kuangalia mandhari ya mji wa Zanzibar nilikuja kushtukia tunafunguliwa Geti la Hoteli ya kisasa ya Melia. Kwa nje ilionekana hoteli nzuri sana kwa jinsi ilivyopambwa kwa namna ya kipekee kabisa. Jambo hilo likanifanya niwe na shauku ya kuingia ndani humo.
Ni baada ya dakika chache ya kufanya malipo, ndipo nilipokabidhiwa chumba cha kisasa kabisa ambacho kilinifanya niupongeze uamuzi wangu wa kuichagua Hoteli hii kwa ajili ya likizo yangu fupi. Nikajitoma Chumbani. Siku hiyo sikutoka nje ya Hoteli hiyo. Muda mwingi niliutumia kusoma na kutazama Tv. Siku zikasonga, muda ukatimia na majibu ya maswali yangu yakapata majibu.
Baada ya siku tatu tangu niwasili hapa Zanzibar na siku mbili nilizitumia kutembelea maeneo ya kihistoria. Nilianza kupapenda Zanzibari. Ilikuwa ni siku ya nne nyakati za asubuhi sana kama kawaida. Niliamka na kutoka nje ya Chumba changu kwa ajili ya kufanya mazoezi. Sikumbuki ilikuwa muda gani ila bado nakumbuka kila kitu. Ilikuwa kati ya saa moja asubuhi na saa mbili.
Nikiwa nimevalia mavazi ya kimazoezi baada ya kukimbia pembezoni mwa bahari na kuchoka sana. Ndipo nilipokuwa narejea taratibu kwa mwendo wa uchovu kutoka pwani ya Bahari mwa hoteli ya Melia. Macho yangu yakanasa kiumbe kilichokuwa kimejilaza kwenye kiti cha uvivu ambacho wazee wengi wa maeneo ya Pwani hupenda sana kuvitumia viti hivyo...viti vya kulala ambavyo mara nyingi vinakuwepo maeneo ya beach zile kubwa na za gharama. Msisimko wa ajabu ukatawala mwili wangu ,nikajikuta nashikwa na bumbuwazi!.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Na kwa mara ya kwanza moyo wangu ukavutiwa na kiumbe kilicholala kama mita arobaini kutoka nilipo. Sijui kwa namna gani macho haya yaliweza kunasa kiumbe hicho. Ni wakati ambapo nikaanza kupoteza kujiamini kwangu. Nikajikuta hisia za uwoga zikianza kutambaa mwilini mwangu kama vile kitu fulani kibaya nimekiona. Nikajikuta moyo na macho yangu yakihitaji kuendelea kumtazama kiumbe huyo. Huku akili haikuweza kuhama kwenda sehemu nyingine kutokana na hofu ya kukipoteza kiumbe kinachoonekana mbeleni mwangu. Kila kiungo changu kikawa kinafanya kazi kwa namna ya ushirikiano wa ajabu. Kiumbe kikaonekana.
Hatua za miguu yangu zikaongezeka atimaye nikakaribia kumfikia kiumbe hicho. Hata hivyo sikuweza kufika mwisho kabisa ya lengo langu kabla ya kupigwa na butwaa. Nikasita. Mungu wangu! nikashtuka!. Ulikuwa mshtuko mkubwa sana kwangu. Hapo hapo nikajikuta sina namna nyingine niende mbele au nibadili mwelekeo wangu. Hata hivyo sauti ndani yangu ikaniambia " wewe ni mwanaume, na siku zote mwanaume husifiwa kwa ujasiri. Onesha uanaume wako" Nikatii sauti hiyo. Nikasogea na macho yakatua kwenye mwili wa binti mrembo. Akiwa amejilaza mahali hapo huku macho yake yakiwa yamefichwa na miwani mikubwa ya urembo ambayo siku hizi vijana wengi wanapenda kuyatumia. Bado nywele zake zikawa kama zinakaribia kugusa ardhi. Ardhi hisiyo na huruma, ardhi iliyomeza miili ya binadamu wengi. Ndipo nilipomtambua.
Nikamtambua kiumbe huyo na haraka nikaanza kurudisha kumbukumbu zangu nyuma. Ndio! Ni binti yule ambaye niliwahi kumgonga kule Posta. Duh! . Ni wakati huo huo binti nae akivua miwani yake na kubakia akinishangaa. Sikuwa nafahamu kwanini alikuwa ananishangaa? Nikaanza kujiuliza amenionaje mimi, ni kwamba sistahili kuwa hapa au ameshtushwa uwepo wangu mahali hapa?. Mwisho nikajiona mpuuzi kuwaza vitu ambavyo sikuwa na uhakika navyo. Nikajikuta namsalimia kiumbe huyo. Jibu lake lilikuwa tofauti na nilivyofikiria.
Nilifikiri hasingeweza kupokea salamu yangu. Alinijibu kwa upole na huku akinisindikiza na tabasamu zuri lililonifanya nibabaike kidogo. Niliomba kujumika nae mahali hapo kama hatajali. Jibu lake lilinishangaza pia, hakika hakuwa na hiana hata kidogo alinikaribisha kwa uchangamfu wa aina yake. Nilivuta kiti ambacho hakikuwa mbali na eneo hilo. Tukazungumza.
Tulizungumza mambo mengi sana. Ni wakati wa mazungumzo hayo ndipo nilipouona uzuri maradufu wa binti huyo ambaye alinikumbusha jina lake kuwa anaitwa Tayana, Tayana Masenga. Hakika siku zote nilitambua ya wazi ni msichana mrembo. Hata hivyo sasa ndio nagundua ni msichana mrembo zaidi kuliko nilivyofikiri, zaidi nilivyomuona mbali kwa mara ya kwanza. Ni mrembo hasa. Alikuwa msichana anayeonekana ana akili nyingi huku akiwa ni mwanamke mwenye kujiamini. Nikagundua pia ni mwanamke anayejua nini anachokifanya. Tukaendelea kuzungumza.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ni katika mazungumzo hayo ndipo alipoonekana kushtushwa na mabadiliko makubwa niliyonayo. Kiukweli tangu niajiriwe nilibadilika sana. Hata mwili ulianza kujiachia. Huwezi kuniweka kwenye kundi la wanene na pia huwezi kuniweka kwenye kundi la watu wembamba. Nilikuwa mtu mwenye mwili wa wastani. Hakika hakutegemea kunikuta mahali hapo ila kwa kauli yake aliamini kuwa siku moja tutaonana. Nilimuuliza kwanini yupo pale? Alinijibu kuwa yupo pale kwa ajili ya likizo yake ambayo kampuni ilimpa kwa ajili ya kupunguza mawazo. Ni hapo ndipo nilijawa na udadisi wa kujua kipi kilimsibu mpaka apewe likizo ya kuondoa "stress'' Maana si kazi rahisi hata kidogo.
******************
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment