Search This Blog

Friday, July 15, 2022

SITASAHAU - 2

 







    Simulizi : Sitasahau

    Sehemu Ya Pili (2)



    Miezi miwili baadae nikapokea simu ya mdada mmoja huku akihitaji kuzungumza na Richard, bila shaka niliipokea simu ile na kuzungumza nae kwa umakini mkubwa, ndipo alipojitambulisha anaitwa Aisha ni Katibu Muktasari wa kampuni ya Tanzania Transport company, akinipa taarifa ya kuitwa kwenye usaili siku ya jumamosi ofisini kwao kutokana na maombi ya nafasi ya kazi niliyoomba miezi michache iliyopita. Hakika ilikuwa tukio lenye kuleta furaha sana kwa upande wangu. Nikaazimia kushinda usaili huo.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Jumamosi kwa upande wa Dar es salaam mara nyingi nyakati za asubuhi huwa hakuna shida ya usafiri, lakini mimi saa moja kamili ilinikuta nimeshafika Msasani mahali ilipo ofisi za Kampuni ile, nakiri kabisa sikuweza kupata usingizi usiku wa kuamkia siku yangu ya usaili. Hata hivyo niliwahi sana maana ofisi ile ilikuwa inafunguliwa saa mbili na nusu asubuhi na usaili ulipangwa kufanyika saa nne asubuhi, sikujali sana umbali wa muda huo. Nikasubiri kwa hamu kubwa.



    Baada ya kuvumilia sana huku nimekaa na watu nisio wafahamu malengo yao, tukaja kuitwa wale wote waliotakiwa kufanyiwa usaili siku hiyo, ndipo nikatambua sikuwa peke yangu, tulikuwa kama watu sita hivi. Nikasogea na kukaa kwenye chumba ambacho kilitengwa maalumu kwa shughuli hiyo. Tukakaa kwenye benchi ya kisasa lililopo pembeni ya chumba kwa ajili ya kusubiriwa kuitwa. Muda Ukawadia na nikapigwa na bumbuwazi.

    Nilikuwa mtu wa kwanza kuingia chumba cha usaili, ikiwa ni mara yangu ya kwanza kufanyiwa usaili tangu nilipoanza kutafuta kazi, hivyo suala la hofu sikuweza kuepukana nalo. Hofu ikanitawala. Ni wakati ambako nilisikia sauti kwenye masikio yangu ikiniambia "Richard ondoa hofu uliokuwa nayo, jiamini kwa sababu hii ni nafasi muhimu ambayo umeipata, shinda hofu hii" Kauli hiyo ilisambaa kwa kasi ya ajabu masikio mwangu, haraka nikashusha pumzi kwa nguvu zote. Wakati huo tayari nipo ndani ya chumba kizuri ajabu.



    Chumba chenye kunakshiwa na rangi nzuri na vitu vya thamani kubwa. Chini ya chumba kile kulitandikwa zulia zuri jekundu, pembeni ya ukuta kulikuwa na tv nzuri ya kisasa iliyokaa vyema ukutani pale. Macho yangu kwa kasi ile ile yakaendelea kusawiri chumba kile. Hakika ni chumba kilichokuwa kinavutia sana kwa harufu nzuri iliyosambaa chumbani mle ,huku hali ya kiubaridi ikitawala eneo lile. Wakati ukawadia.

    Wakati nikiendelea kustaajabu uzuri wa chumba kile ghafla sauti ya kike ikasikika " Naitwa Tayana Masenga ni Afisa Uajiri wa kampuni hii na nipo hapa na Afisa habari Mr Salim Mhando, karibu sana ndugu" Wakati huo nilimuona yule dada akivua mawani yake kwa utulivu husio kifani. Ni wakati huo huo macho yangu yalipokimbia maili nyingi kwa kasi ya ajabu na kutua usoni mwa msichana yule. Nikashtuka! Sikuamini macho yangu kwa wakati ule.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Haraka kumbukumbu zangu zikarejea kwa kasi ya ajabu, nikajiuliza wapi nilimuona binti huyu? wakati huo huo mapigo ya moyo wangu yakawa yameongezeka kwa kasi isiyo ya kawaida. Ni wakati ambapo moyo wangu ukahisi hali ile ile, hali ambayo niliwahi kuhisi kipindi fulani uko nyuma. Naaam! haraka nikamkumbuka..."Ndiye huyu! ndiye yeye hasa" Nikajiambia...



    .Ni binti yule yule ambaye nilikutana nae Posta na kumgonga kwa bahati mbaya tu kama nilivyohisi kwa upande wangu , ni binti huyu ambaye alinifanya nipewe maneno ya kashfa na konda. Ni binti huyu ambaye alinifanya nipoteze simu yangu ya thamani wakati wa tukio lile, kumbe anaitwa Tayana? nikajijibu. Badala ya kuanza kumchukia nikajikuta nabakia kutabasamu..tabasamu la uongo. Tabasamu la kihisia! nikajikuta najitambulisha..."Naitwa Richard Kamba na nipo mahali hapa kwa ajili ya usaili" Wakati najitambulisha macho yangu yalikuwa yanamtazama binti yule ambaye naweza kusema kwa wakati huo ni adui yangu. Hata hivyo sikuona chochote kilichobadilika usoni kutoka kwa binti yule mrembo. alionesha sura ile ile yenye kuvutia. Ajabu ilioje?



    ***************

    Nilianza usaili ule kwa kujibu kila swali kwa umakini mkubwa na uwerevu wa hali ya juu, majibu yangu yalionekana kumfurahisha sana Afisa habari wa kampuni ile, wakati wote kila nilivyokuwa nikijibu kwa umahiri mkubwa alikuwa akibakia akitabasamu na huku akiandika kitu nisichokifahamu kwenye 'Note Book' yake. Ndipo binti yule mrembo aliponiuliza swali ambalo lilionekana kama la mwisho kwa upande wangu. Aliniuliza: " Unataka ulipwe mshahara kiasi gani?" Hakika lilikuwa swali gumu kulijibu na kuna sauti nikaisikia masikioni mwangu ikinisisitiza nilijibu swali hilo kwa uangalifu wa hali ya juu.



    Nikajibu: " Napaswa kulipwa kutokana na kiwango ambacho kampuni hii imekitenga kwa ajili ya nafasi ninayoiomba. Napaswa kulipwa kutokana na utendaji wangu na kiwango cha faida nitakachokiletea kampuni. Pia napaswa kulipwa kutokana na kiwango cha elimu yangu" Nikamaliza kulijibu swali lile. Na kuwatazama wale watu wote wawili walio mbele yangu. Nilimuona yule afisa habari akitabasamu na kumuangalia binti yule kwa furaha hata hivyo sura ya binti yule ikabakia vile vile katu haikujibu tabasamu la afisa habari yule. Nikafadhaika!CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya usaili niliruhusiwa kuondoka mahali pale huku yule afisa habari akinipa pongezi za kipekee na kunipa matumaini makubwa juu yangu ya kupewa ajira katika kampuni ile.Tofauti na yule binti mrembo yeye aliguna tu. kisha akafunga kitabu chake na kuvaa miwani yake ambayo ilionekana wazi ni ya matatizo ya macho. Nilitoka ndani mle nikiwa nusu nina furaha na nusu nikiwa na huzuni, hasa nikikumbuka kuwa binti yule mrembo alikuwa ni kama ufunguo wa ajira yangu, ni yeye ndie atakayeamua nafasi yangu. Nikasali! nikasali! nikasali kwa Mungu wangu nishinde usaili ule.



    **************

    Wiki zikapita, hadi miezi ikapita, sikuwahi itwa na kampuni ile kwa ajiri ya ajira. Hakika nilikata tamaa kabisa ya kuajiriwa na nikatamani kujiajiri mwenyewe hata hivyo nilikosa mtaji wa kuanzisha biashara. Mjini nikapaona pachungu huku manyanyaso yakizidi toka kwa walezi wangu. Maisha yalikuwa magumu sana kwa upande wangu. Mwanaume mimi nilikosa hata pesa ya vocha. Wakati mwingine nilitegemea chenji zinazotokana na mahitaji madogo madogo ninayotumwa kwenda kununua na kiasi kidogo kinachobakia ndio hutumia kununua vocha. Nilikata tamaa ya maisha. Nikazidi kuchukia muda wangu niliyoupoteza kuitafuta elimu. Wakati ukawadia.

    Ni siku chache baadae nikaliona tangazo kwenye gazeti la serikali kuhusu nafasi za ajira kutoka shirika la Ethiopian Airline, ambalo limefungua tawi hapa nchini. Niliandika maombi yangu na kuambatanisha CV yangu yenye nyaraka kivuli za kuthibitisha kile nilichokiandika kwenye wasifu wangu na bila kuchelewa nikatuma. Wiki moja baadae niliitwa kwenye usaili.



    Baada ya wiki moja kupita nilipokea simu ya kuhitajiwa ofisini kwa kupeleka nyaraka zangu halisi ni baada ya kuelezwa kushinda usaili niliyofanya. Kila kitu kilienda kama simulizi nzuri ya kuvutia ni kama kusoma vitabu vya Robson Kruso. Hatimaye nikaajiriwa rasmi kama Afisa wa IT yaani 'Information Technology' katika shirika hilo. Kumbuka nina shahada ya kwanza ya IT kutoka chuo kikuu cha Dar es Salaam. Maisha yakaanza kwa upande wangu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nilianza kazi kwa juhudi kubwa na kujituma kusiko kwa kawaida huku nikiazimia kufidia muda wangu nilioupoteza kwa kipindi chote. Miezi minne baadae niliomba kuhama na kuanza maisha ya kujitegemea. Ilikuwa jambo gumu kwa walezi wangu kunielewa hawakupenda kuhama kwangu kwa haraka kwa kipindi hicho. Nilijaribu kuwashawishi na mwishowe wakakubaliana na uamuzi wangu. Wakati huo huo nikaanza kujiuliza inakuwaje sasa wananipenda, wananililia nikae pale ilhali kipindi sina kazi walikuwa wananinyanyasa? Huku wakinishinikiza nirejee kijijini ....Nikagundua kuwa ni kwa sababu ya kazi yangu, nikasema kwa sababu ya pesa. Hakika pesa ni kila kitu "Nikawaza".

    Nilipanga chumba na sebule eneo la Mbezi Kimara, mbali na mahali walipo walezi wangu. Sikutaka kukaa karibu nao. Nilitaka kuwa huru zaidi katika eneo jipya. Miezi michache baadae nilibahatika kupata mkopo ambao niliutumia kununua vitu vya ndani kama Tv, fenicha za kisasa na vingine vingi. Sasa chumba changu kikaanza kuwa na mwonekano mzuri na wenye kuvutia, chumba anachostahili kuishi mvulana wa kisasa. Pia ukumbuke kwa kipindi hicho sikuwa na msichana hata mmoja, hakika niliwachukia wanawake . Kila siku inayokwenda , nilimuomba Mungu anioneshe mke wangu kwa sababu wakati huo sikuwa nawaamini wanawake tena pamoja na kukutana na vishawishi vingi kwa wakati huo.



    ******************************

    Mwaka mmoja baadae kupitia akiba niliyokuwa nikijiwekea nilifanikiwa kununua kiwanja maeneo ya Kigamboni. Nilianza kufurahia maisha na hata mwonekano wangu ulianza kubadilika. Nilikuwa mvulana mtanashati sana, kila mmoja aliyepata kuniona kabla ya kuajiriwa alibaki akipigwa na bumbuwazi mara tu alipopata bahati ya kukutana nami kwa wakati huu. Nilikuwa mwaminifu na mtiifu sana kazini.



    Uwezo wangu wa kufanya kazi bila kuchoka, ushirikiano wangu na wafanyakazi wenzangu uliwavutia wakuu wangu wa kazi. Hivyo nikajikuta nakuwa mwakilishi mzuri wa shirika sehemu mbali mbali ndani na nje ya nchi kwa muda mfupi. Kote huko nilipopitia shirika lilikuwa likipata sifa kubwa kupitia mimi. Nikafarijika sana na kuendelea kufanya kazi kwa bidii zaidi. Jambo nisilotegemea likatokea!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ni miaka miwili baadae yaani miaka miwili na miezi sita tangu niajiriwe kwenye shirika hili. Tukapata msiba mzito wa kuondokewa na Meneja wa shirika kwa upande wa Tanzania. Kifo cha meneja huyu kilikuja baada ya kupata ajali ya gari maeneo ya Tazara wakati huo akielekea nyumbani kwake Tuangoma -Mbagara. Ilikuwa pigo na huzuni kubwa kwa shirika na wafanyakazi ofisini hapo. Nakiri kwa muda mchache niliyomfahamu meneja huyu nilijifunza mambo mengi hasa ukarimu na busara zake bila kusahau ucha Mungu wake. Baada ya kumalizika shughuli nzima ya mazishi ya meneja wetu maana niliteuliwa na shirika kusimamia msiba huo. Wiki moja baadae nikaripoti kazini.



    Niliwasili jumatatu ya asubuhi kama kawaida yangu na baada ya kuwasalimia wafanyakazi wenzangu nilielekea ofisini kwangu. Hata hivyo nilijikuta nikiwa na maswali mengi baada ya secretary wa ofisi ya meneja kunichangamkia kusiko kawaida huku akinitizama kwa tabasamu fulani lenye kumaanisha kuna jambo muhimu angependa kuniambia. Wakati huo bado miguu yangu na akili yangu nilishavielekeza kuelekea ofisini mwangu.

    Niliingia ofisini mle kama ilivyo kawaida, macho yangu yakatua vema juu ya meza ya ofisi yangu na kuiona bahasha ikiwa imeandikwa jina langu, bahasha hisiyo ya kawaida kimuonekano. Nilikuwa napokea bahasha nyingi lakini hii ilikuwa tofauti, muonekano wake ulinisisimua . Nilishtuka sana, na kwa kasi ya ajabu haraka niliifungua barua ile na kuisoma kwa muda ule ule huku ningali nimesimama. "Mungu wangu!" Nilijikuta natoa sauti hafifu huku nimepigwa na butwaa. Mle ndani ya barua ile ambayo nimeisoma ilieleza imetoka makao makuu ya shirika likitoa taarifa ya kuteuliwa kwangu kuwa meneja mpya wa shirika la ndege la Ethiopia Airline. Kila kitu kilikuwa kama tamthilliya fulani ya kifilipino, nikajihisi kama nipo ndotoni. Nilifumba macho na kufumbua tena bado macho na akili yangu iliniambia kuwa sio ndoto. Ni ukweli halisi. Nikapagawa!

    Uteuzi wangu ulienda sambamba na kupewa likizo yenye malipo ya wiki moja, kujiandaa na nafasi mpya ya umeneja ofisini hapo. Likizo yangu iliandikwa inaanza siku hiyo hiyo. Nikajikuta natoka nje kama mwehu. Kila mmoja miongoni mwa wafanyakazi wenzangu walikuwa wakinipa hongera kwa uteuzi wangu. Bado nilihisi nimo ndotoni.Ndoto nisiyotarajia. Nikajikuta najikana mwenyewe kusiko tarajiwa. Hapana sio mimi Richard. Nikarejea kuisoma upya bado jina lililomo kwenye barua hiyo lilikuwa langu. Bila shaka ni mimi niliyekusudiwa.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nilianza kujiuliza kama nastahili cheo hiki?, wakati wapo wafanyakazi wa muda mrefu kuliko mimi. Kitu gani uongozi wamekiona toka kwangu hadi kufikia kustahili kupewa nafasi hii kubwa kabisa katika shirika? Maswali yangu kwa wakati huo hayakuwa na majibu katika kichwa changu. Nikaazimia kufanya kazi ambayo itawashangaza hata wakuu wangu. Kazi itakayokuwa na faida kubwa kwa shirika hili. Moyoni nikakubali uteuzi huo.



    *************

    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog