Search This Blog

Friday, July 15, 2022

SITASAHAU - 4

 







    Simulizi : Sitasahau

    Sehemu Ya Nne (4)





    Hakuniambia, akanijibu si wakati wake, ila siku moja ataniambia. Hakika siku hiyo tuliongea mengi zaidi na baada ya muda tukajikuta tumekuwa marafiki. Baada ya chuki faraja nikatambua. Hata hivyo kuhusu kazi yangu sikumwambia ukweli. Aliponiuliza kuhusu ninafanya shughuli gani kwa sasa? Nilimjibu kuwa nafanya kazi shirika la ndege la Ethiopian nikiwa mfanyakazi ninayehusika na mifumo wa mawasiliano ofisini hapo. Baada ya kutumia masaa machache hapo, sote kwa pamoja tukarejea hotelini.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Urafiki wetu ukadumu na kuimarika sana, kila mahali tulikuwa pamoja. Sasa nikahisi nimepata mwenyeji, mwenyeji binti mrembo. Kwa siku tatu hata wahudumu wa hoteli hiyo walikuwa wanatutania kuwa tumependeza sana kama mtu na mke wake. Maneno hayo yalikuwa yakituingia moja kwa moja ila sote tuliishia tukitabasamu kwa furaha, Tabasamu lenye kumaanisha jambo. Mpaka hapo tulikuwa marafiki tu.

    Likizo ilipokuwa inafikia tamati. Likizo ya wiki moja ambayo nilipewa na shirika baada ya kupandishwa cheo kazini na nitakaporejea nirejee katika majukumu mapya. Makubwa zaidi niliyokuwa nayafanya mwanzo. Nilimweleza kila kitu Tayana kuhusu kuisha kwa likizo yangu hivyo nitawajibika kurejea Dar es salaam kuendelea na majukumu yangu ya kikazi.

    Uamuzi wangu ulionekana kuwa wa ghafla sana kwake. Nikauona uso wake ukipoteza ile nuru ya furaha niliyoizoea siku zote huku akiachia tabasamu hafifu machoni pake. Nikahisi hakutegemea uamuzi wangu kwa kipindi kile. Kipindi ambacho alianza kusahau kila kitu kuhusu matukio ya maisha yake ya nyuma yaliyopelekea apoteze sio tu furaha yake hata amani ndani ya moyo wake.



    Tayana akawaza sana kisha akanijibu kuwa kwa kipindi tulichokuwa pamoja ametambua wazi mimi nina umuhimu mkubwa kwake....ni mimi ndiye niliyemsahulisha na mawazo mengi yaliyopelekea kutaka kufupisha uhai wake hivyo katu hataweza kubaki peke yake yu radhi naye kufupisha likizo yake na kuongozana nami kurejea Dar es salaam kama tu nitakuwa radhi kuongozana naye. Machozi yalionekana yakimtiririka kwenye mashavu yake, nikashtuka! Nikajikuta namuuliza kwanini analia?





    Ndipo aliponieleza kuwa alipewa likizo na kampuni kwa ajili ya kupunguza mfadhaiko uliomkumba baada ya kuachana na mwanaume aliyempenda sana. Mwanaume ambaye siku zote aliamini kuwa ndiye atakayejenga nae familia siku za usoni. Mwanaume ambaye siku zote alimuamini na kumpenda. Mwanaume ambaye alimfanya ajisikie mwenye furaha kila wanapokuwa pamoja. lakini kila kitu kilikuja kubadilika ndani ya usiku mmoja tu. Pale mwanaume huyo ambaye alimwambia kuwa kila kitu kati yetu kifikie tamati leo. Tayana hakuwa na namna tena, alilia na kuuliza sababu lakini mwanaume huyo akamjibu hana sababu. Maumivu ya moyoni yakamtawala kwa wakati huo. Mapenzi yakamuumiza Tayana .

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Siku mbili baadaye tulikuwa sote mimi na Tayana tulikuwa ndani ya Boti ya Kilimanjaro kurejea nyumbani huku nyuso zetu zikitawaliwa na tabasamu lenye kuvutia sana. mazungumzo yetu yalitawaliwa na vicheko vya hapa na pale. Ni kama tunakutana kwa mara ya kwanza huku kila mmoja akimuhitaji mwenzake, kwa upande wangu halikuwa jambo nililowazia kwa wakati huo. Nikasahau kama tupo safarini. Tena juu ya maji....Safari ikawa fupi ajabu.

    Masaa mawili kasoro baadae tuliwasili salama bandarini Dar es salaam. Baada ya kumaliza hatua zote muhimu tuliagana mimi na Tayana. Tukikubaliana kuendelea kuwasiliana kwa kadiri iwezekanavyo. Wakati anapoelekea kupanda gari iliyokuja kumchukua eneo hilo huku macho yangu yakimsindikiza binti huyo ghafla bila kutegemea, Tayana aligeuka nyuma mita chache niliposimama na mita chache iliposimama gari ikimsubiri. Tukatazamana! Macho yetu yakagongana ...macho yakatoa ishara , ishara ya kihisia. Nikatabasamu naye akanijibu kwa tabasamu. Tabasamu lake likanifanya nicheke naye akacheka. Nikampungia mkono kama ishara ya kumuaga kwa mara nyingine tena naye akapokea ishara yangu na kuingia garini.

    Nami nilielekea kwenye gari iliyokuja kunichukua na kunipeleka nyumbani kwangu. Mawasiliano yangu na Tayana yaliendelea kuimarika kila siku. Ikafikia hatua siwezi kulala bila kusikia sauti ya Tayana naye pia hivyo hivyo hawezi kulala bila kusikia sauti yangu. Tukaendelea kuwa karibu zaidi huku kila wikiendi tulikuwa tukikutana sehemu mbalimbali.Mpaka kufikia kipindi cha miezi miwili hakuwa anapajua nyumbani kwangu, kila wakati aliniletea ombi la kuhitaji kunitembelea nyumbani kwangu kila mara nilitoa visingizio vingi. Sikutaka apajue nyumbani kwangu kwa wakati huo. Maana nilikuwa naendelea kumalizia ujenzi wa nyumba yangu kisha nihamie hapo na ndipo ningeweza kumkaribisha kwangu. Ndivyo nilivyopanga siku zote. Mpaka kufikia hapo hakuna aliyepata ujasiri wa kumueleza mwenzake hisia zake. Sote tukaacha matendo pekee yazungumze.





    Miezi mitatu baadaye tangu kumfahamu na kujenga ukaribu kati yangu na Tayana. Nilikuwa mimehamia nyumbani kwangu. Nyumba yangu haikuwa imekamilika kila kitu kama nilivyotaka ila kwa kiwango ilipofikia haikunizuia kutohamia hapo. Hapo ndipo ndoto yangu ya kwanza ya kumiliki nyumba nzuri ya kisasa ikatimia.Nikasahau matatizo yote ya nyuma. Wakati mwingine nilipokuwa nayakumbuka maisha yangu ya nyuma nilijisikia kuumia sana. "Katu husiyakumbuke ya nyuma maana yanaumiza sana" Nilisikia sauti ikiniambia masikioni mwangu. Kumbuka mpaka kufikia hapo nilishaenda zaidi ya mara moja nyumbani kwa Tayana. Hakika Tayana alikuwa msichana wa kisasa, mwenye kumiliki nyumba ya kisasa katika umri wake ilikuwa jambo gumu kuamini. Zaidi ya hapo nilipigwa na butwaa baada ya kuyaona magari matatu ya kifahari yaliyopaki ndani ya uzio wa nyumba yake. Magari ya ndoto yangu, nilijisemea. Tukio la ajabu likatokea.........

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wiki moja sasa tangu nihamie nyumbani kwangu. Siku hiyo nilikuwa ofisini wakati nilipotembelewa na mgeni bila kutarajia. Nakumbuka ilikuwa mida ya saa tano asubuhi wakati katibu muhtasi wangu alipoingia na kuniambia nina mgeni anayehitaji kuniona nami... je amruhusu kuingia? Kwa sababu siku hiyo nilimwambia katibu muhtasari nahitaji muda mwingi wa kuwa busy na kazi hivyo hasimruhusu mgeni yoyote hasiye wa kampuni kuniona. Nina hakika kwa siku hiyo alitelekeza hilo lakini ilionekana mgeni huyu alikuwa mbishi sana kukubali kuondoka bila kuonana nami. Alisisitiza lazima aonane nami hata pale alipoulizwa je ana miadi ya kuonana na mimi? Mgeni yule alikataa na alihitaji kuonana na mimi kwa dharura.

    Bila shaka niliruhusu katibu wangu amruhusu mgeni huyo kuingia ofisini. Ni wakati huo macho yangu yalikuwa yameukazia mlango huku nikijawa na shauku ya kumfahamu mgeni huyo mkorofi hasiyeheshimu kanuni za ofisi. Nilitaka kumuona kwa hamu kubwa macho yangu yakaendelea kuuelekea mlango kwa umakini mkubwa. Ndipo niliposhikwa na butwaa kwa kutoamini ninachokiona mbele yangu. Alikuwa Tayana akiwa ndani ya gauni zuri yenye rangi ya pink iliyomkaa vema mwilini.



    Bila kutarajia macho ya Tayana yalitembea maili nyingi na kusambaa kwa kasi ya ajabu na niliyashuhudia yakitua kwenye kibao kilicho mbele ya meza yangu. Kibao kilinitambulisha "Manager Richard Kamba" Ni wakati ambapo macho ya Tayana yakionesha mshangao mkubwa kama mtu hasiye amini kitu anachokiona mbele yake . Nikamuachia tabasamu mwanana na kumkaribisha ofisini kwangu. Ni wakati alipokaa ndipo nilipogundua amepoteza hali ya kujiamini mbele yangu ni kama amepigwa na bumbuwazi . Haraka nilitambua kwanini yupo katika hali ile? Siku zote alinifahamu kama mfanyakazi wa kawaida tu katika shirika hili mpaka muda mchache uliopita ndipo alipotambua hilo hivyo kuja kwake ghafla ofisini na kunikuta mimi ndio meneja wa shirika hili ilibidi ajiulize maswali mengi zaidi bila kupata jibu.



    Baada ya maongezi madogo alinieleza wazi hakupanga kuja hapa lakini ilitokea dharura kuja eneo la ofisi yetu akaonelea ni vizuri kunifanyia "suprise" kuja ofisini kwangu na alipata shida sana kufika hapa kwa sababu naliniulizia kama mfanyakazi wa kawaida lakini wote walisema hakuna mfanyakazi mwenye jina hilo zaidi ya meneja wa shirika. "Nikajikuta nafadhaika lakini nafsi yangu ilikuwa ngumu kukubali kushindwa ndipo nilipohitaji kumuona meneja huyo mwenye jina la mtu aliyeniambia anafanya kazi hapa. Nilipokuona wewe ndio meneja wa ofisi hii hakika nilipigwa na butwaa ni kama nisiyeamini kitu".

    Maelezo ya Tayana yalinifanya nitabasamu kisha kwa mara ya kwanza nilimuomba nimpe mwaliko wa kunitembelea nyumbani kwangu wikiendi inayokuja. Nilimwambia hapo ofisini si mahali sahihi kuzungumza mambo mengi kati yetu ambayo si ya ofisi. Alinielewa huku akinisindikiza na tabasamu....tabasamu la kihisia! Tabasamu lenye kutuma ujumbe fulani mahususi....Nikang'amua anachomaanisha. Nilimuomba tukutane siku tatu baadae nyumbani kwangu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    =============================================================

    Kwa muda wa zaidi ya miezi mitatu tangu nilipoanza kumfahamu Tayana niligundua vitu gani anavipenda na mambo yapi hayapendi hata kwenye vyakula pia niligundua vyakula anavyovipenda. Siku hiyo ya jumapili nilitayarisha chakula anachokipenda Tayana, chakula hicho nilikiandaa kwa mikono yangu mwenyewe. Binafsi mimi ni mpishi hodari sana jikoni na siku zote nilipenda kupika mwenyewe. Saa sita kamili mchana Tayana aliwasili nyumbani kwangu baada ya kumuelekeza .

    Alikuja na gari yake mwenyewe moja kati ya magari yake ya kifahari niliyowahi kuyakuta nyumbani kwake. Alishuka garini taratibu kama malaika fulani hivi ....hakika nakiri Tayana alipendeza sana siku hiyo...uzuri wake uliongezeka maradufu ndani ya gauni fupi lenye rangi nyekundu...Gauni la kisasa ambalo lilivaliwa ndani ya mwili wa msichana mrembo wa kisasa. Sikujali sana. Nilipenda alivyovaa alikuwa "amazing". Kwa mara ya kwanza mimi na Tayana alikuwa ananitembelea nyumbani kwangu, tukasalimiana kisha nikamkaribisha ndani mwangu. Ndani ya nyumba iliyopuliziwa marashi yenye harufu nzuri ya kunukia.Marashi anayoyapenda Tayana siku zote kuyatumia. Niliifanya siku hiyo kuwa maalumu kwa Tayana. Ndivyo nilivyotegemea.

    Tulizungumza mengi na Tayana siku hiyo. Aliniuliza mahusiano yangu ya kimapenzi yalivyo. Tangu tulipoanza kuwa karibu hakuwahi nigusia jambo lolote linalohusiana na mapenzi lakini siku hiyo aliniuliza. Jambo hilo katu sikushtuka kwa sababu nililitegemea. Nilimueleza wazi kutokuwa na mahusiano ya kimapenzi kwa sasa hasa chuki yangu kwa wanawake. Alinishangaa sana kwa kutoamini ninachomueleza. Aliniuliza kwa nini nawachukia wanawake? Ilinilazimu nimueleze Tayana bila kuficha ili apate kunielewa...Nikamueleza....



    "Nilikuwa na mwanamke niliyempenda sana wakati ningali chuoni ni baada ya kuwa marafiki tulijikuta tukianzisha uhusiano wa kimapenzi, kila mara alikuwa akiniambia ananipenda sana. Na mapenzi yangu kwake niliyaamini. Na Nilimuamini zaidi aliponiambia anahitaji kujenga familia na mimi. Siku zote nilijenga matumaini makubwa juu yake. Miaka yote mitatu chuoni ilikuwa ya kusisimua sana kati yangu mimi na yeye, marafiki na wanafunzi wenzetu walituchukulia kama mfano mzuri wa mahusiano yao.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nikajikuta nawekeza pendo langu ndani yake. Ni baada ya kuhitimu masomo yetu, haraka yeye alipata bahati ya kuajiriwa mapema nami ikanibidi nisote kutafuta kazi kwa muda mrefu...ni kipindi ambacho mpenzi wangu alipobadilika sana kitabia hasa baada ya kupata kazi akaanza dharau juu yangu. Miezi miwili baadaye alinitumia ujumbe kwenye simu yangu kuwa mahusiano yangu mimi na yeye yafikie tamati, aliniomba msamaha kwa kunipotezea muda wangu mwingi pia alinieleza wazi sikuwa mwanaume wa ndoto yake. Kwangu mimi alikuwa nami ili kupoteza muda na sasa amepata mwanaume wa ndoto yake. Alinieleza anatamani kubadilisha historia kati yangu mimi na yeye....anajutia uamuzi wake wa kuwa nami kimapenzi. Maneno yake yakaniumiza sana siku hiyo ilikuwa ghafla bila kutarajia...Mvulana mimi nikachanganyikiwa"

    Jambo moja ambalo nililiamini.....Kila jambo hutokea kwa sababu, hili pia lilikuwa sababu. Sikutaka kupigania pendo langu kwake kwa sababu aliniambia ukweli..ukweli wenye kuumiza. Tangu wakati huo nilianza kuwachukia wanawake sikuwa na hamu tena ya viumbe hao. Niliyapigania maisha yangu kwanza.Lakini pia sikuweza kumsahau msichana huyo.Kwa ufupi nilimaliza kumuelezea Tayana mahusiano yangu yaliyopita.Muda wote Tayana alikuwa kimya akinisikiliza huku akiniangalia usoni kutambua ukweli wangu.Bila kutarajia....Nilimuona akinifuata mahali nilipo...nami nikasimama.....ujasiri umemuingia wakati huo Tayana.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog