Simulizi : Massacre (Mauaji Ya Halaiki)
Sehemu Ya Pili (2)
Maturubai zaidi ya matano yalikuwa yamefungwa katika eneo la nyumba ya mzee Matimya. Idadi ya watu ambao walikuwa wamehudhuria msibani hapo wala haikuwa kubwa kama jinsi ambavyo ilitarajiwa. Ingawa wachungaji mbalimbali kutoka katika makanisa tofauti tofauti walikuwa wamehudhuria msiba huo lakini wala hakukuwa na zaidi ya washirika watano kutoka katika kanisa la Praise And Worship la Mwenge.
Watu wengi ambao walikuwa wamehudhuria msibani pale walikuwa watu ambao wala hawakutoka mbali na eneo lile pamoja na waandishi wa habari. Kanisa likaonekana kupunguza ukaribu, kitendo cha waumini watano kuhudhuria katika msiba ule kilidhihirisha wazi kwamba mapenzi makubwa juu ya mzee Matimya hayakuwepo tena katika mioyo ya waumini wa kanisa lile.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Vilio vya ndugu wa marehemu vilikuwa vikisikika kutoka kila kona msibani hapo. Sehemu kubwa ya mikeka iliyokuwa mahali hapo ilikuwa wazi jambo ambalo lilionekana kumshangaza kila mtu.
“Mbona washirika wa kanisa la Praise and Worship hawaonekani hapa msibani?” Mchungaji Melek aliuliza kwa mshangao huku akiangalia katika kila kona msibani hapo kana kwamba alikuwa akimtafuta mtu fulani.
“Wote walikasirishwa na kitendo kilichotokea. Mapenzi yao yakapotea. Mbaya zaidi, mzee Matimya alijinyonga” Kijana mmoja alimjibu mchungaji Melek.
“Mungu wangu! Kumbe alijinyonga?”
“Ndio. Nafikiri alijiona kuwa mkosaji mbele za Mungu wake” kijana yule alijibu.
Benedict alikuwa ametulia pembeni kidogo mwa mchungaji Melek. Maneno yote aliyoyaongea mchungaji Melek na yule kijana yalionekana kumuumiza kupita kiasi. Hapo hapo akanyanyuka na kuanza kuelekea ndani ya nyumba yao.
Idadi kubwa ya wanawake ilikuwa ndani ya nyumba hiyo. Benedict hakutaka kuongea chochote kile, kitu alichokifanya ni kupiga hatua kuelekea chumbani kwake.
Akajilaza kitandani huku macho yake yakiangalia juu, machozi yakaanza kumtoka. Benedict akazidi kushikwa na hasira juu ya washirika wa kanisa la Praise and Worship lililokuwa Mwenge. Kadri ambavyo alivyokuwa akilikumbuka kanisa hilo na ndivyo ambavyo hasira zake zilivyozidi kuongezeka zaidi.
Huku Benedict akiwa katika hali hiyo chumbani, mara mlango ukafunguliwa na Angelina kuingia. Macho ya Angelina yalikuwa mekundu huku mashavuni akiwa na alama za michirizi ya machozi hali iliyoonyesha kwamba kipindi fulani kilichopita alikuwa akilia. Angelina akaanza kupiga hatua mpaka pale kitandani alipokuwa amejilaza Benedict.
“Najiona kama tumetengwa” Angelina alimwambia Benedict kwa sauti ya chini iliyojaa majonzi.
“Mapenzi yao yamepotea kabisa. Ukaribu wao hauonekani, ni lazima nifanye kitu juu ya kanisa hili” Benedict alimwambia Angelina huku akionekana kuwa na hasira.
“Kitu gani?”
“Niwaue. Ni lazima niwaue washirika wote wa kanisa lile. Hasa Judith” Benedict alisema.
“Usifanye hivyo Benedict”
“Haina jinsi, nataka kurudisha furaha yangu iiyopotea” Benedict alisema huku akichukua kitambaa chake cha mkononi na kujifuta machozi yaliyokuwa yakimtoka.
Ukimya mrefu ukatawala mahali hapo huku kila mtu akionekana kufikiria lake. Kadri muda ulivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo hasira za Benedict zilivyozidi kumkamata. Hakulipenda kanisa la Praise And Worship lililokuwa Mwenge, hakumpenda mshirika yeyote ndani ya kanisa lile, kila mtu alionekana kuwa adui namba moja katika maisha yake.
Huku kila mmoja akifikiria lake, mara simu ya mkononi ya Benedict ikaanza kuita, akaitoa kutoka mfukoni. Kabla hajapokea, akayapeleka macho yake katika kioo cha simu ile, macho yake yakatua katika namba ambayo ilikuwa ngeni machoni mwake. Akabonyeza kitufe cha kijani na kisha kuipeleka sikioni.
“Upo wapi Benedict? Mbona sikuoni hapa nje?” Sauti ya upande wa pili ilisikika ikiuliza.
“Wewe nani?” Benedict aliuliza.
“Mkuu wa polisi kitengo cha upelelezi”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Benedict hakutaka kuongea kitu chochote kile, akakata simu, akainuka kitandani na kuanza kuelekea nje. Alipofika nje, akaanza kuangalia katika kila upande. Macho yake yakatua katika uso wa mwanaume mmoja aliyekuwa na ndevu nyingi ambaye alimuonyeshea ishara ya kumuita. Benedict akaanza kupiga hatua kumfuata mwaname yule.
“Hebu tusogee pembeni kidogo” Mwanaume yule alimwambia Benedict na kuanza kusogea pembeni. Hata kabla mzee yule hakuongea chochote, akatoa kitambulisho chake na kumuonyeshea Benedict.
“Uchunguzi wenu umeishia wapi?” Benedict aliuliza.
“Kwamba baba yako hakujinyonga”
“Unasemaje?”
“Huo ndio ukweli. Hakujinyonga bali alinyongwa”
“Umejuaje?”
“Tulipima alama za vidole katika kamba ile, na vile vile tulikuta alama za kiganja katika shavu lake hali iliyoonyesha kwamba alipigwa kibao kabla ya kunyongwa”
“Sawa. Kwa hiyo mmeamua nini?”
“Kumtafuta muuaji. Jambo hilo libaki kuwa lako tu, usimpe taarifa dada yako wala mama yako katika kipindi hiki. Wape taarifa baada ya mwezi mzima kupita” Mkuu yule wa polisi alimwambia.
Benedict akaonekana kuchanganyikiwa, maneno ambayo aliongea mzee yule ndio ambayo yalionekana kumchanganya zaidi. Alimwangalia mzee yule mara mbili mbili huku akionekana kutokuamini kile ambacho alikuwa ameambiwa. Hasira zikazidi kumpanda zaidi juu ya kanisa la Praise And Worship kwa kuona kwamba kanisa lile pia lilikuwa limehusika katika mauaji ya baba yake.
Unyonge ukaongezeka zaidi moyoni mwake, kiu ya kumtafuta muuaji ikaonekana kumkamata. Maswali mengi juu ya muuaji huyo yakaanza kumiminika kichwani mwake, mbele yake akaona giza, tumaini ndani ya moyo wake likaonekana kupotea.
“Ni kanisa. Kanisa linamjua muuaji” Benedict alijisemea kwa hasira.
Mchungaji Mwakipesile hakuonekana kuridhika japokuwa mchungaji Matimya alikuwa amevuliwa cheo cha uchungaji na kusimamishwa kazi ya Utumishi wa Mungu. Hakutaka mzee Matimya abaki ndani ya dunia hii kwani kama angemuacha basi ni lazima ingetokea siku ambayo angekuja kufahamu njama zote alizozifanya na hivyo kumuingiza katika matatizo.
Mchungaji Mwakipesile hakutaka kutulia, akaiweka pembeni kazi yake ya Utumishi wa Mungu aliyokuwa nayo na kujiingiza katika mambo ambayo yalikuwa kinyume na kazi yake. Akaamua kuwafuata vijana ambao akaamini kwamba wangeweza kumfanyia kazi yake kama alivyotaka kufanyiwa. Mchungaji Mwakipesile hakutaka kuendelea kubaki Morogoro, kitu alichokifanya ni kuanza safari ya kuelekea Dar es Salaam kwa kutumia gari lake.
“Unahitaji nini mzee?” Kijana mmoja aliyejazia mwili alimuuliza mchungaji Mwakipesile.
“Nahitaji kuonana na kiongozi wenu”
“Unamfahamu au?”
“Hapana” Mchungaji Mwakipesile alijibu.
Hapo hapo akaambiwa ateremke kutoka ndani ya gari lake. Vijana watatu wakatokea mahali hapo kutoka katika sehemu ambayo hakuifahamu na kuanza kumpekua. Walitumia dakika tano kumpekua yeye pamoja na gari lake, walipomaliza wakaanza kumwangalia usoni.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Wewe ni polisi?” Kijana mmoja aliuliza.
“Hapana”
“Unahitaji nini?”
“Nataka kuonana na mkuu wenu” Mchungaji Mwakipesile aliwaambia.
Hapo hapo akafungwa kitambaa usoni na kisha kupakizwa ndani ya gari nyingine na safari ya kuelekea asipopafahamu kuanza. Muda wote mchungaji Mwakipesile alikuwa akitetemeka kwa woga. Imani aliyokuwa nayo juu ya vijana wale ikaanza kupotea, kitu alichokifanya katika kipindi hicho ni kutulia ili kuona ni mahali gani ambapo angefikishwa.
Safari ilitumia dakika kumi huku kitamba kikiendelea kuwa usoni mwa Mchungaji Mwakipesile. Mara baada ya dakika chache gari likasimama nje ya jengo moja ambapo geti likafunguliwa na gari kuingizwa ndani. Mchungaji Mwakipesile akateremshwa na moja kwa moja kupelekwa ndani ya nyumba hiyo. Kitambaa kile alichokuwa amefungwa usoni kikafunguliwa na kuamrishwa kukaa kochini.
Macho ya mchungaji Mwakipesile hayakutulia sehemu moja, yalikuwa yakiangalia kila kona sebuleni pale ambapo alikuwa ameachwa peke yake. Wala hazikupita dakika nyingi, mzee mmoja mnene akafika mahali hapo na kutulia katika kochi jingine huku mkoni akiwa na chupa ya kinywaji cha Heineken.
“Nasikia unanihitaji” Mzee yule alimwambia mchungaji Mwakipesile.
“Ndio”
“Una shida gani?”
Mchungaji Matimya akaanza kuelezea shida zake huku mzee yule akiwa kimya kumsikiliza. Mchungaji alitumia dakika tano kuelekezea kila kitu ambacho alitaka kifayike kwa wakati huo. Mara baada ya kumaliza maelezo yake, mzee yule akachukua kinywaji chake kile na kupiga funda moja.
“Una kiasi gani?” Mzee yule alimuuliza.
“Milioni mbili” Mchungaji alijibu lililomfanya mzee yule kuanza kucheka.
“Unataka tumuue mtu au kuku?” Mzee yule aliuliza.
Tayari muonekano wa mzee yule ukaonekana kuwa tofauti na jinsi alivyokuwa kabla, ndita zikaanza kuonekana usoni mwake hali ambayo ilimuongezea wasiwasi mchungaji. Mchungaji Mwakipesile akashindwa kutoa jibu, alibaki akimwangalia usoni mzee yule kana kwamba hakulisikia lile swali aliloulizwa.
“Acha utani na kazi yetu” Mzee yule alimwambia.
“Milioni tatu” Mchungaji Mwakipesile alimwambia.
“Nimekwambia acha utani”
“Milioni nne. Naomba unisaidie”
“Utani wako umezidi”
“Milioni tano. Please, naomba unisaidie”
“Sawa. Nitafanya hivyo kwa kiasi hicho kwa sababu tu umeniomba” Mzee yule alimwambia Mchungaji Mwakipesile.
Mchungaji akaanza kutoa maelekezo kama njia ambazo zingewezesha kupatikana kwa mzee Matimya. Akatoa picha yake na yule mzee kuanza kuiangalia kwa makini. Alieleza kila kitu ambacho kilionekana kuwa muhimu kuhitajika na watu hao.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Utafurahia kifo gani?” Mzee yule alimuuliza.
“Chochote kile ili mladi aonekane amejiua” Mchungaji Mwakipesile alijibu.
Kadri muda ulivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo idadi ya watu ilivyozidi kuongezeka karibu na eneo la kanisa lile. Simu zikapigwa katika kitengo cha Zimamoto. Kadri ambavyo watu walivyokuwa wakiliona kanisa lile lilivyokuwa likiteketezwa na moto na ndivyo ambavyo machozi yalivyozidi kujaa machoni mwao.
Tukio lile la kuteketezwa kwa moto lilikuwa likimhuzunisha kila mtu ambaye alikuwa akiliangalia. Furaha ambayo walikuwa nayo ya kuingia mwaka mpya ikatoweka kabisa mioyoni mwao. Hakukuwa na sauti ya mtu yeyote ambayo ilisikika kutoka kanisani, ni sauti ya muungurumo wa moto tu ndio ambao ulikuwa ukisikika.
Zilipita dakika kumi na tano, magari mawili ya kitengo cha Zimamoto yakafika katika eneo hilo. Kazi kubwa ya kuuzima moto ule ikaanza huku idadi ya watu ikizidi kuongezeka mpaka kufikia watu elfu tatu. Hadi kufikia kipindi hicho, hakukuwa na mtu yeyote ambaye alikuwa akifahamu sababu zilizopelekea kuwaka kwa moto ule ambao ulikuwa umeliteketeza kanisa.
“Au umeme ulilipuka kanisani?”
“Hapana bwana. Nafikiri kuna mtu alilichoma moto”
“Umejuaje?”
“Hausikii harufu kali ya mafuta ya Petroli?”
“Mhh! Inawezekana”
Magari matatu ya polisi yakafika katika eneo hilo. Kwa haraka haraka, polisi ambao walikuwa na bunduki mikononi mwao wakateremka na kuanza kuelekea katika eneo lile la kanisa. Joto kali la mvuke wa moto ule bado lilikuwa likitawala mahali hapo. Walisubiri mpaka joto lile kuisha na ndipo wakaanza kwenda lilipokuwa gofu la kanisa lile. Wakaupiga teke mlango, ulipovunjika, wakaingia ndani.
Picha ambayo ilionekana dani ya kanisa lile ilionekana kumuogopesha kila aliyeiangalia. Miili ya watu ambayo iliteketezwa na moto ule ilikuwa ikionekana vizuri machoni mwao, wakinamama ambao walikuwa wamewabeba watoto wao walikuwa wameteketezwa na moto pamoja na watoto wao. Mafuta ya binadamu yalikuwa yametapakaa sakafuni, hakukuwa na kitu ambacho kilikuwa kimesalia, kila kitu kilikuwa kimeteketezwa kwa moto.
“Hali inatisha sana” Mkuu wa kituo cha polisi cha pale Mwenge, Bwana Marwa alisema huku akitoka nje ya kanisa.
Bwana Marwa alionekana kuchanganyikiwa, akili yake bado ilikuwa ikijiuliza juu ya chanzo ambacho kilisababisha moto ule. Akaanza kuwaangalia wananchi ambao walikuwa wamesimama karibu na eneo lile, machozi yalikuwa yakijikusanya machoni mwake. Kwa mwendo wa taratibu akaanza kuwasogelea wananchi katika eneo ambao waliambiwa watulie kule hadi kila kitu kitakapokuwa sawa.
“Kitu gani kilitokea?” Bwana Marwa aliuliza huku akionekana dhahiri kuchanganyikiwa.
“Labda naweza kuhisi kitu” Mmoja wa wananchi alisema na hapo hapo kuitwa.
“Unahisi nini?”
“Kuna mtu amehusika”
“Umejuaje?” Bwana Marwa aliuliza.
“Nafikiri mnatakiwa mfanye kitu fulani ili hisia zangu ziwe na uhakika” Kijana yule alijibu.
“Kitu gani?”
“Mkamwangalie mtu fulani ambaye inawezekana amehusika na tukio hili”
“Mtu gani?”
“Benedict Matimya. Mtoto wa marehemu mchungaji Matimya” Kijana yue alisema.
Hawakutaka kupoteza muda, kwa haraka haraka Bwana Marwa, polisi watano wenye bunduki pamoja na yule kijana wakaingia garini na kuanza kuelekea nyumbani kwa mzee Matimya. Kijana yule bado alikuwa akilia, moyoni alioekana kuumizwa kupita kawaida huku muda wote akisisitiza kwamba Benedict ndiye ambaye alikuwa akihusika katika mauaji yale.
“Tukifika, hakuna kuuliza,tunamuweka chini ya ulinzi. Mmesikia?” Bwana Marwa alisema huku akionekana kukasirika.
“Ndio mkuu” Polisi waliokuwa ndani ya gari lile waliitikia huku wakikoki bunduki zao.
Safari ilichukua dakika tano, dereva akasimamisha gari nje ya geti la nyumba ya mzee Matimya. Honi zikaanza kupigwa na baada ya sekunde kadhaa, Angeline akafika mahali hapo na kufungua geti. Gari likaingizwa ndani na polisi wote kuteremka. Angelina hakujua ni kitu gani ambacho kilikuwa kikiendelea kwa wakati huo, alibaki akitetemeka tu.
“Benedict Matimya yupo?” Sauti ya Bwana Marwa ilisikika ikimuuliza Angelina.
“Ndio…”
“Alitoka siku ya leo?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ndio. Alienda kanisani kwenye mkesha. Amerudi dakika tano zilizopita” Angelina alijibu.
Bi Meriana akatokea mahali hapo, polisi hawakutaka kuongea kitu chochote kile, kitu walichokifanya ni kuanza kuelekea katika chumba cha Benedict huku wakiongozwa na Angelina.
“Jamani! Kuna nini tena?” Bi Meriana aliuliza huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Usihofu mama”
“Lazima nihofu. Bunduki zinanikosesha amani”
“Usijali mama” Bwana Marwa alisema huku wakiwa wamekwishafika katika mlango wa kuingilia chumbani kwa Benedict.
Mara baada ya Benedict kulifikia gari lake akaufungua mlango na kuingia. Hakutaka kubaki mahali hapo, hivyo akaliwasha gari lake na kuondoka huku akiliacha kanisa likizidi kuteketezwa kwa moto ambao aliuwasha.
Njia nzima Benedict alikuwa na furaha, kitendo alichokifanya cha kulichoma moto kanisa alikiona kuwa kitendo sahihi ambacho kilikuwa kimemletea furaha kwa wakati huo. Hakuonekana kuwaonea huruma watoto wadogo ambao walikuwa wakiteketezwa kwa moto kanisani mule, kila mtu ambaye aliteketezwa kwa moto ndani ya kanisa lile, kwake alimuona kuhusika katika mauaji ya baba yake.
“Ni Biblia tu ndizo hazikustahili kuchomwa moto” Benedict alijisemea.
Mara baada ya kufika katika geti la nyumbani kwao, akateremka, akalifuata akafungua na kuingiza gari katika eneo la nyumba yao. Alipoliegesha, akateremka, akaufuata mlango akaufungua na kuingia ndani.
“Kwa nini ulitufungia mlango?” Bi Meriana alimuuliza Benedict huku akionekana dhahiri kukasirika.
“Sikutaka muangamie. Bado ninawapenda na kuwahitaji” Benedict alijibu.
Bi Meriana na Angelina wakabaki wakishangaa, jibu ambalo alilitoa Benedict lilionekana kumshtua kila mtu. Wakabaki wakimwangalia Benedict mara mbili mbili kana kwamba hawakukisikia kile ambacho kiliongelewa mdomoni mwake. Bi Meriana alitamani kuuliza swali jingine lakini Benedict akaelekea chumbani kwake.
Moyo wa Benedict ulikuwa umetawaliwa na furaha, akajitupa kitandani huku macho yake yakiangalia darini. Moyo wake uliridhika na kila kitu ambacho kilikuwa kimetokea. Kitendo cha kulichoma kanisa na kuua zaidi ya watu mia mbili hamsini kilikuwa ni kitendo ambacho kilimfurahisha kuliko kitu chochote katika maisha yake katika mwaka uliopita.
Kwa kasi ya ajabu Benedict akainuka kutoka kitandani. Muungurumo wa gari kutoka nje ulionekana kumtia wasiwasi kupita kawaida. Kwa haraka haraka akaelekea dirishani, akalifungua kidogo pazia na kuanza kuchungulia nje. Macho yake yakatua katika gari aina ya Defender ambalo ubavuni liliandikwa ‘Polisi’ huku mbele kukiwa na polisi waliokuwa na bunduki mikononi.
“Benedict Matimya yupo?” Sauti ya mwanaume mmoja ilisikika.
Benedict hakutaka kusikia jibu la swali lile kutoka kwa Angelina. Kitu alichokifanya katika wakati huo ni kufungua droo ya kitanda chake, akachukua kadi ya benki na kisha kutoka nje ya chumba kile. Hakutaka kuelekea sebueni, kitu alichokifanya ni kuanza kuelekea jikoni ambako akafungua mlango na kutoka nje.
Japokuwa nyumba ilikuwa imezungushiwa ukuta mkubwa, Benedict akauparamia na kushukia upande wa pili nje ya eneo la nyumba yao. Hakutaka kuendelea kusubiri kuona ni kitu gani ambacho kingeendelea, kitu alichokifanya ni kuanza kukimbia kuelekea gizani zaidi.
Wala hawakutaka kupiga hodi, moja kwa moja Bwana Marwa akaufungua mlango ule ambao haukuwa umefungwa kwa ufunguo na wote kuingia ndani ya chumba kile. Chumba kilikuwa kitupu, hakukuwa na mtu yeyote yule. Hakuna aliyeonekana kukubaliana na hali ile, wakaanza kumtafuta Benedict katika kila sehemu ndani ya chumba kile.
Wakaufungua mlango wa kabati la nguo, wakapekua katika kila sehemu ndani ya kabati lile lakini wala Benedict hakuonekana. Hawakuonekana kuridhika, wakaanza kuchungulia katika uvungu wa kitanda lakini bado Benedict hakuwa huko. Kila mmoja akaonekana kuchanganyikiwa, kutokuwepo kwa Benedict ndani ya chumba kile kuliwafanya kuchanganyikiwa kupita kawaida.
“Mbona hayupo?” Bwana Marwa aliuliza huku akionekana dhahiri kuchanganyikiwa.
“Sijui, ila alikuwepo ndani ya chumba hiki” Angelina alijibu.
Kwa haraka haraka polisi wakatoka ndani ya chumba kile na kuanza kumtafuta katika sehemu nyingine ndani ya nyumba ile. Kila chumba kilikuwa kitupu. Kila mmoja alionekana kuchoka, wakaanza kupiga hatua kuelekea sebuleni. Bwana Marwa akatulia kochini, hakuelewa ni kitu gani ambacho walitakiwa kufanya kwa wakati huo.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Bi Meriana na Angelina bado walikuwa wakishangaa, hawakuelewa ni kitu gani kilikuwa kimetokea mpaka Benedict kuanza kutafutwa na polisi waliokuwa na bunduki mikononi. Bi Meriana akayapeleka macho yake katika uso wa Bwana Marwa, ndita za waziwazi zilikuwa zikionekana.
“Kuna nini jamani? Mbona hamtaki kutuambia?” Bi Meriana aliuliza huku akiwaangalia polisi wale kwa zamu.
“Mwanao ni muuaji. Tena muuaji wa halaiki” Bwana Marwa alijibu.
Bi Meriana na Angelina wakashtuka, jibu ambalo lilitoka mdomoni mwa Bwana Marwa lilionekana kuwashtua kupita kawaida. Bi Meriana akalifuata kochi na kutulia huku macho yake yakimwangalia Bwana Marwa. Maneno ambayo aliyaongea Bwana Marwa yalionekana kuanza kujirudia rudia kichwani mwake.
Alimfahamu sana mwanae, muda wote alikuwa akionekana kuwa mpole, hakuwahi kugombana na mtu yeyote kuanzia nyumbani mpaka kanisani. Kila alipokuwa akijiuliza juu ya mauaji, Bi Meriana alikosa jibu. Alitulia kwa muda, uso wake ulionyesha dhahiri kutokukubaliana na maneno ambayo alikuwa akiyaongea Bwana Marwa.
“Haiwezekani. Benedict hawezi kuwa muuaji” Bi Meriana alisema.
“Kwa nini isiwezekane?”
“Kwanza ni mpole sana. Pia ni mcha Mungu” Bi Meriana aijibu.
Jibu alilolitoa Bi Meriana lilionekana kuwakasirisha polisi waliokuwa mahali pale. Bwana Marwa akaagiza kijana yule aliyekuwa ndani ya gari aletwe mahali pale. Bi Meriana na Angelina wakaonekana kushtuka, kijana ambaye aliitwa mahali pale walikuwa wakimfahamu kama Shemasi mmoja ndani ya kanisa lile.
“Kwa nini umesema kwamba Benedict atakuwa amehusika katika mauaji haya?” Bwana Marwa alimuuliza shemasi Mjuni.
“Mimi ni mmoja wa mashemasi kanisani pale na katika siku ya leo nilikuwa zamu na shemasi John pamoja na shemasi Anania” Shemasi Mjuni akasema na kuendelea.
“Baada ya mchungaji kusema kwamba kila mtu aliyekuwa nje ya kanisa alikuwa akihitajika ndani ya kanisa, nikaamua kutoka nje na kuwaita washirika. Nilimfuata hata Benedict ambaye alikuwa ndani ya gari lake” Mjuni alielezea. Machozi yakaanza kuyaloanisha machozi yake.
“Nilimwambia kwamba kila mtu alikuwa akihitajika. Alipofungua kioo cha gari lake, harufu kali ya harufu ya petroli ikaingia puani mwangu. Nilipoangalia katika viti vyake vya nyuma, nikayaona madumu matatu ya lita ishirini yaliyokuwa na petroli” Mjuni alielezea huku kila mtu akiweka umakini kumsikiliza.
“Nini kiliendelea?” Bwana Marwa aliuliza.
“Sikutilia sana mashaka. Sikurudi kanisani bali nilikwenda chooni kujisaidia haja kubwa. Nilitoka mara baada ya kusikia kelele za kuomba msaada huku kanisa likiteketea. Nilijaribu kuangalia huku na kule, nikamuona Benedict akielekea katika gari lake kwa mwendo wa haraka haraka, akaingia garini na kuondoka katika eneo la kanisa kwa mwendo wa kasi” Mjuni alimalizia.
Bi Meriana na Angelina wakapigwa na mshtuko. Habari aliyoielezea Mjuni iliwashtua kupita kiasi. Hapo hapo wakapata majibu ya sababu iliyomfanya Benedict kuwafungia milango katika kipindi ambacho alielekea kanisani. Hawakuishia kupata jibu hilo tu, walilikumbuka jibu lililotoka kinywani mwa Benedict mara baada ya kuingia ndani ya nyumba hiyo.
“Sikutaka muangamie. Bado ninawapenda na kuwahitaji” Jibu la Benedict lilijirudia kichwani mwa Bi Meriana.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Moyo wa mchungaji Mwakipesile ulikuwa na furaha mara baada ya kuona kazi ambayo aliitaka ifanyike ilifanyika kwa haraka sana. Kila wakati mchungaji Mwakipesile alikuwa akifurahia huku tabasamu mara kwa mara likionekana usoni mwake. Mara kwa mara moyo wake ulikuwa ukishangilia, kifo cha mzee Matimya kilikuwa kimemfurahisha kuliko kitu chochote kile katika maisha yake.
Moja kwa moja akaanza safari ya kuelekea Dar es Salaam huku lengo lake likiwa ni kutaka kuhudhuria mazishi ya mzee Matimya. Moyo wake ulikuwa ukimshukuru Mungu wake kwa kile ambacho kilikuwa kimetokea. Furaha yake iliongezeka maradufu mara baada ya kufika katika eneo la nyumba ya mzee Matimya. Maturubai ambayo yalikuwa yamezunguka katika eneo la nyumba ile ndio ambayo yalikuwa yamempa furaha zaidi.
Akayapeleka macho yake katika eneo la nyumba ile, idadi ndogo sana ya washirika kutoka katika kanisa la Praise and Worship la pale Mwenge walikuwa wakionekana mahali pale. Mara baada ya kuwasalimia wachugaji ambao walikuwepo mahali pale, moja kwa moja akaanza kupiga hatua kuwafuata wafiwa kuwasalimia na kisha kurudi mkekani na kutulia.
Aliutengeneza uso wake kuwa katika majonzi huku akijaribu kuyatengeneza machozi ya uongo ndani ya macho yake. Ingawa uso wake ulikuwa ukionyesha majonzi makubwa lakini moyo ake ulikuwa tofauti kabisa. Moyo wake ulitawaliwa na furaha, kila kitu ambacho kilikuwa mbele yake kilionekana kufanikiwa siku za usoni.
Huku akiwa mkekani, ghafla akashtuka katika mshtuko ambao ulionyesha kwamba alikumbuka kufanya kitu fulani. Jina la Judith likamjia kichwani. Jina hilo likaonekana kuwa hatari kwake katika siku za baadae. Hakutaka kuuacha moyo wake kumwamini mwanamke, hasa Judith. Kwake, mwanamke alionekana kuwa kiumbe dhaifu, moyo wa mwanamke haukuonekana kuvumilia kutuza siri kwa muda mrefu, angekaa na siri kwa muda fulani na kisha baadae kuitoa.
Alijiona kutakiwa kufanya kitu fulani, hasa kumuua Juliet. Alihitaji kuishi kwa amani, hakutaka kitu chochote cha hatari kitokee katika maisha yake. Muda kwake ukaonekana kwenda taratibu tofauti na siku nyingine, mara kwa mara alikuwa akiyapeleka macho yake katika kioo cha saa yake. Muda ulikuwa ukizidi kusonga mbele huku muda wa mazishi ukizidi kusogea.
Mara baada ya kuuaga sura ya mwisho mwili wa mzee Matimya, magari yakaanza kuelekea katika makaburi ya Kinondoni.Vilio bado vilikuwa vikiendelea kusikika kutoka kwa wafiwa pamoja na watu wa karibu. . Mara baada ya jeneza kuingizwa kaburini, mchanga ukaanza kutumbukizwa ndani ya kaburi lile. Baada ya kila kitu kukamilika, watu wakaanza kutawanyika katika eneo lile.
Mchungaji Mwakipesile akaanza kulifuata gari lake na kisha kuanza safari ya kuelekea Mbagala. Ndani ya gari, mawazo ya mchungaji Mwakipesile yalikuwa yakimfikiria Judith. Kiu ya kutaka kumuondoa Judith duniani ilikuwa imemkaba kupita kiasi.
“Vipi?” Kijana mmoja alimuuliza mchungaji Mwakipesile mara baada ya kufika sehemu husika.
“Nahitaji kuonana na mzee” Mchungaji Mwakipesile alijibu.
Mchungaji Mwakipesile na yule kijana wakaanza kulifuata gari moja lililoonekana kuwa la kifahari na kuingia ndani. Safari ya kuelekea katika jumba la kundi hilo ikaanza mara moja. Ndani ya gari kila mtu alikuwa kimya.
“Ni lazima nimmalize” Mchungaji Mwakipesile alijisemea moyoni.
Walichukua dakika kumi hadi kufika katika jumba hilo la kifahari, wakateremka na kisha kuanza kuelekea ndani ya jengo hilo. Wakaingia ndani huku eneo la jumba hilo likionekana kuwa na ulinzi mkubwa na kisha kuanza kuelekea ndani ya jumba hilo. Wakajiweka kochini na baada ya dakika chache, mzee yule akatokea mahali hapo.
“Kuna mwingine?” Mzee yule aliuliza swali hata kabla ya salamu.
“Ndio. Ila huyu ni msichana, yule niliyeshirikiana nae”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Iache picha yake pamoja na nusu ya malipo” Mzee yule alimwambia Mchungaji Mwakipesile.
Mara baada ya kujiandaa, moja kwa moja Judith akaanza safari yake ya kuelekea kanisani kwa ajili ya mkesha wa kuukaribisha mwaka 2008. Maisha yake yalikuwa ya upweke yaliyojaa wasiwasi, mara kwa mara alikosa amani, nafsi ilikuwa ikimhukumu kutokana na kile ambacho alikuwa amekifanya. Moyo wake ulijuta, mara kwa mara alikuwa akisali sala ya kuomba msamaha.
Furaha ilipotea moyoni mwake, kila wakati picha ya mzee Matimya ilipokuwa ikimjia kichwani, amani ilitoweka zaidi. Judith aliendelea kupiga hatua kuelekea kanisani huku kitabu Kitakatifu cha Biblia akiwa amekikumbatia kifuani mwake. Mwendo wake ulikuwa wa taratibu huku akionekana kuwa katika lindi la mawazo.
Dakika thelathini ndizo ambazo zilikuwa zimebakia kabla ya kuingia mwaka mpya wa 2008. Judith aliendelea kupiga hatua kulifuata kanisa. Huku akiwa amebakiza hatua mia tatu kabla ya kulifia geti kubwa la kanisa lile, akashtukia gari likija na kusimama mbele yake. Judith alitulia huku akiliangalia gari lile dogo a Baloon.
Kioo cha gari kikateremshwa, sura ya kijana mmoja ikatokeza na kumwangalia Judith usoni. Kijana yule hakuongea kitu chochote kile, walibaki wakiangaliana kwa muda kadhaa, tabasamu pana likaanza kuonekana usoni mwake. Mlango ukafunguliwa na kumtaka Judith aingie ndani ya gari lie, Judith akagoma na kuendelea na safari yake.
“Judith…. Judith Simon. Binti mrembo aliyedanganya kubakwa” Kijana yule alisema.
Judith akasimama, akageuka nyuma na kumwangalia kijana yule usoni. Maneno ambayo alitamka kijana yule yalikuwa yamemshtua kupita kawaida. Akajikuta akianza kupiga hatua kulifuata gari lile.
“Binti umejiaribia. Zile milioni ulizopewa na mchungaji Mwakipesile si kitu” Sauti ya kijana yule ilisikika.
Judith akapigwa na mshtuko, maneno ambayo aliyasikia kutoka kwa kijana yule yalionekana kumshtua. Damu yake ikaanza kuzunguka kwa kasi ya ajabu hali iliyoufanya hata moyo wake kudundwa mara themanini kwa dakika, kijasho chembamba kikaanza kumtoka.
Hakumfahamu mvulana yule na wala hakuwa na uhakika kama alikwishawahi kumuona sehemu yoyote ile katika maisha yake. Kichwa chake kilichanganyikiwa, hakujua sehemu ambayo kijana yule aliyapata yale yote ambayo alikuwa akimwambia kwa wakati ule. Siri ambayo alikuwa amejitahidi kuitunza moyoni mwake akaiona ikianza kuvuja.
“Ni lazima tuitoe habari hii katika magazeti yetu wiki hii” Kijana yule alimwambia Judith.
Moyo wa Judith ukashtuka zaidi. Akaanza kumuona kijana yule kufahamu kila kitu kilichotokea katika tukio lile wiki mbili zilizopita. Mwili wake ukazidi kutetemeka huku kijasho kikizidi kumtoka. Hakukumbuka tena kama alikuwa na safari ya kuelekea kanisa, akabaki akimwangalia kijana yule.
“Kwa heri. Tutaonana……” Kijana yule alimwambia Judith huku akiwasha gari lake.
“Sub..ir..ii..” Judith alimwambia kijana yule.
“Kuna nini tena?”
Judith hakujibu kitu, alibaki kimya huku akimwangalia kijana yule ambaye dhahiri alionekana kufahamu kila kitu. Judith akalisogelea dirisha la gari lile, akaliegemea huku macho yake yakiendelea kumwangalia kijana yule.
“Unanitisha!” Judith alimwambia kijana yule.
“Ukweli ndio huo. Nafahamu kila kitu”
“Nisaidie kaka yangu. Sitaki watu wafahamu”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kuficha jambo hili litanikosesha fedha nyingi sana”
“Kivipi?”
“Mimi ni mwandishi wa habari Judith. Habari hii ina fedha nyingi sana”
“Nisaidie kaka yangu. Nakuomba nisaidie” Judith alimwambia kijana yule huku machozi yakikaribia kumtoka.
Yule kijana akaanza kumwangalia Judith kwa macho yaliyojaa huruma. Judith akabaki kimya, machozi yakaanza kuonekana machoni mwake na baada ya muda fulani yakaanza kutiririka mashavuni mwake. Judith akaambiwa kuingia garini na bila ubishi akafanya hivyo.
Kijana yule akaingiza gia na kisha kulindoa gari mahali pale huku Judith akiwa katika kiti cha nyuma. Muda wote uso wa kijana yule ulikuwa ukionyesha tabasamu pana, Judith alikuwa na wasiwasi, hakuonekana kumuamini kijana yule, lakini kwa sababu alikuwa katika matatizo, hakuwa na jinsi, alijitolea kumuamini kwa kumsaidia.
Safari kuelekea mahali asipopafahamu bado ilikuwa ikiendelea, mara baada ya kufika kijiweni, gari likasimamishwa na vijana wawili kuingia garini. Judith akapigwa na mshtuko, akatamani kuufungua mlango na kutoka, akashindwa kufanya hivyo kwa kuwa vijana wale walikuwa katika pande zote mbili, yeye alikuwa katikati.
“Wapi sasa?” The Killer aliuliza.
“Kama kawa” Zolaya alijibu huku akiitoa bunduki yake.
Judith alibaki akitetemeka, bunduki ambayo alikuwa akiiona kwa Zolaya ilikuwa ikimuogopesha kupita kawaida. Mapigo yake ya moyo yalikuwa yakizidi kumdunda zaidi na zaidi. Hakujua ni kitu gani ambacho kilikuwa kikiendelea mahali hapo. Mbele yake alikiona kifo, machozi yakaanza kumtoka zaidi. Akaanza kuomba msamaha pasipo kulifahamu kosa lake.
Walitumia dakika arobaini tayari wakawa wamekiwishafika katika msitu wa Pande. Giza lilikuwa kubwa msituni mule kutokana na idadi kubwa ya miti mirefu na mikubwa pamoja na nyasi ndefu. Gari likaanza kupita katika nyasi kubwa, wala hakukuwa na mtu yeyote ambaye alikuwa akiongea kitu chochote kwa wakati huo.
Mara baada ya umbali fulani, gari likasimamishwa, Zolaya na The Killer wakamteremsha Judith kinguvu kutoka garini. Judith akaanza kupiga kelele za kuomba msaada, hakukuwa na mtu yeyote aliyeonekana kujali, wakamlaza chini, Judith alizidi kulia huku akiendelea kuomba msamaha.
“Nimuue kwa risasi ngapi?” Zinja aliuliza huku akiikoki bunduki yake.
“Fanya tatu. Mbili kichwani na moja kifuani” Zolaya alijibu.
Mara baada ya kuikoki bunduki yake, Zinja akamuelekezea Judith bunduki ile kichwani. Kelele za kuomba msamaha bado zilikuwa zikiendelea kusikika kutoka kwa Judith. Zinja wala hakuonekana kuzisikia kelele zile, akajiweka tayari kwa ajili ya kumfyatulia risasi Judith.
“Moja….mbili….tatu…” Zinja alihesabu.
Milio ya risasi ikasikika mahali hapo, kelele za Judith ambazo zilikuwa zikisikika kipindi kichache kilichopita zikapotea. Milio mingine zaidi ikasikika, eneo zima likatapakaa damu huku ukimya mkubwa ukiwa umetawala mahali hapo.
Mara baada ya kuondoka nyumbani kwao, moja kwa moja Benedict akaanza kuelekea Sinza. Moyo wake bado ulikuwa na furaha kubwa mara baada ya kuona amefanikiwa kuwaua watu ambao hakuwapenda hata kidogo katika maisha yake, washirika wa Praise And Woship lililokuwa Mwenge. Moyo wake wala haukujuta, kitu alichokifanya alikiona kuwa sahihi kufanywa kwa mkono wake.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mara baada ya kufika maeneo ya Sinza kwa Remmy, akapanda daladala huku lengo lake likiwa ni kuelekea nyumbani kwa mjomba wake, Joseph ambaye alikuwa akiishi Magomeni Mapipa. Benedict hakutaka kuongea na mtu yeyote, muda wote alikuwa kimya huku akiangalia nje kupitia dirishani. Baada ya dakika ishirini, daladala ikafika Magomeni Hospitalini ambako akateremka na kuanza kupiga hatua kuelekea Mapipa kwa kupitia Magomeni Garden.
Idadi ya watu bado ilikuwa kubwa barabarani. Vijana bado walikuwa wakipiga ngoma barabarani kusherehekea mwaka ambao walikuwa wamefanikiwa kuuona huku wakitembea kwa makundi makundi kama watu waliokuwa katika maandamano. Mafataki mbalimbali yalikuwa yakirushwa hewani huku mabati na ngoma mbalimbali zikiendelea kusikika.
Benedict alitumia muda wa dakika kumi kutoka kituoni mpaka katka nyumba ya mjomba wake, mzee Joseph. Hakukuwa na mtu yeyote nje ya nyumba ile kitu ambacho kilimfanya Benedict kuusogelea mlango na kuanza kuugonga. Alitulia kwa sekunde kadhaa, shangazi yake, Bi Stella akaufungua mlango huo na Benedict kuingia ndani. Kila mmoja akaonekana kushangaa, ujio wa Benedict ndani ya nyumba ile tena kwa muda kama ule ndio ambao ulikuwa ukiwashangaza.
“Vipi tena Benedict? Mbona usiku hivyo?” Mzee Joseph alimuuliza Benedict ambaye alitulia kochini.
“Ni habari ndefu sana, ninahitaji kukaa mahali hapa na kesho nitaendelea na safari yangu” Benedict aliwaambia.
“Mbona unatutisha Benedict! Safari ya kwenda wapi tena?” Mzee Joseph aliuliza huku akimwangalia Benedict usoni.
“Safari ya mbali ambayo hata mimi sihifahamu. Ila msihofu, nitarudi salama” Benedict aliwaambia.
“Bado hatujakuelewa Benedict”
“Msihofu. Nitakapoanza safari kesho, mtanielewa tu” Benedict aliwaambia.
Hakukuwa na kilichoendelea, Benedict akaonyeshwa chumba cha kulala na kuelekea huko. Mzee Joseph na mkewe walionekana kuwa na wasiwasi, maneno ambayo aliyaongea Benedict yaliwaongezea wasiwasi zaidi. Walitamani kufahamu ni kitu gani ambacho kilikuwa kinaendelea, walitamani kupiga simu nyumbani kwao na kuuliza, ila kila walipotaka kufanya hivyo, walisita.
Benedict hakupata usingizi, usiku kucha macho yake yalikuwa wazi. Katika kipindi hicho hakutaka kumuamini mtu yeyote yule, kila mtu alionekana kuwa kama polisi katika maisha yake. Mpaka inaingia saa kumi na mbili asubuhi, macho ya Benedict yalikuwa wazi. Kwa haraka haraka akasimama kutoka pale kitandani tayari kwa ajili ya kuanza safari yake ya kuelekea kule asipopafahamu.
Mara baada ya kumaliza kujiandaa, Benedict akatoka ndani ya chumba kile na kuelekea sebuleni. Hakutaka tena kuendelea kubaki mahali hapo. Kitu alichokifanya ni kuanza kuondoka ndani ya nyumba hiyo bila kuaga. Benedict hakuonekana kuwa na wasiwasi kabisa, alitembea kwa kujiamini hadi kituoni.
Benedict akashtuka kupita kawaida mara baada ya kuiona sura yake ikiwa katika ukurasa wa mbele wa kila gazeti ambalo alikuwa akiliangalia kituoni pale. Maneno makubwa yaliyosomeka ‘ANATAFUTWA NA POLISI’ yalikuwa yakionekana vizuri katika kila gazeti ambalo lilikuwa na picha yake.
Benedict hakuamini kama picha zake zilikuwa zimechapishwa kwa haraka sana toka afanye tukio lile, magazeti yale yalikuwa na picha zake ambazo zilikuwa zimetolewa na mama yake kwa polisi ambao walikuwa wamekwenda kumtafuta.
Kitu alichokifanya Benedict ni kuingia ndani ya daladala moja na kukaa katika kiti cha nyuma huku kichwa chake akiwa amekiinamisha chini. Sala ya kimoyo moyo ilikuwa ikiendelea, hakutaka kukamatwa katika kipindi hicho, alitamani aendelee kuishi zaidi na zaidi ili apate muda wa kuendelea kusherehekea ushindi mkubwa ambao alikuwa ameupata.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alitulia ndani ya gari, hakutaka kumwangalia mtu yeyote usoni kwa kuogopa kugundulika. Safari ya kuelekea Mwenge bado ilikuwa ikiendelea, wasiwasi ukamshika zaidi mara baada ya kusikia abiria ndani ya gari lile wakianza kulizungumzia tukio lile alilolifanya la kulichoma moto kanisa. Kila abiria ambaye aliliongelea tukio lile, aliliongelea kwa hasira kiasi ambacho wasiwasi aliokuwa nao Benedict moyoni ukaongezeka zaidi.
“Huyu kijana anastahili adhabu zaidi ya kifo” Mzee mmoja alisema huku akionekana kukasirika.
“Tena kabla ya kifo chake, inampasa kupokea mateso makali” Mwanaume mwingine alisema.
Furaha yote aliyokuwa nayo moyoni ikatoweka. Hofu ya kukamatwa ndani ya daladala ikaanza kumkamata. Ingawa alijua fika kwamba alikuwa amefanya dhambi ya uuaji mbele za Mungu lakini bado sala yake iliendelea kusikika moyoni mwake kwa kutaka Mungu amuokoe kutoka katika daladala ile bila kugundulika.
Mara baada ya kufika katika kituo cha Mwenge, Benedict akamlipa konda nauli yake. Benedict akaanza kupiga hatua kuelekea katika sehemu ambayo ilikuwa na magari yaendayo Bagamoyo. Hofu ikaongezeka maradufu mara baada ya kuziona picha zake kubwa za rangi zikiwa zimebandikwa katika kila kona kituoni pale.
Hata kabla hajayafikia magari yale, akageuka nyuma. Nyuma yake walionekana vijana watatu ambao walikuwa wakimfuata huku mikononi mwao wakiwa na picha zake. Hofu ikaongezeka zaidi na zaidi, akalipinga wazo lake la kuyasogelea magari yale, alichokifanya ni kukata kona na kuanza kuvifuata vyoo vya kulipia ambavyo vilikuwa katika eneo la kituo kile.
Vijana wale bado walikuwa wakiendelea kumfuata huku makaratasi ya picha zake zikiwa mikononi mwao. Walimuona Benedict akimfuata kijana ambaye alisimama nje ya choo kile ambaye kazi yake kubwa ilikuwa ni kupokea fedha za kila mtu aliyekuwa akitaka huduma ya choo au bafu. Akamlipa kijana yule kiasi cha fedha kilichohitajika na kisha kuingia ndani.
“Tukamuingilieni mule mule” Kijana mmoja aliwaambia wenzake.
“Tukamuelezee kwanza muhusika wa vyoo vile” Kijana mwingine akashauri.
Ushauri ule ukaonekana kukubalika, wakaanza kupiga hatua za haraka haraka kumfuata muhusika wa vyoo vile. Wakaanza kumuelezea kila kitu ambacho kilikuwa kinaendelea kwa wakati huo. Mhusika yule wa vyoo vile akaonekana kupigwa na mshtuko mara baada ya kuambiwa juu ya mtu yule ambaye alikuwa ameingia chooni kwa wakati ule. Kwa furaha, nae akainuka na wote kuanza kuelekea ndani ya vyoo vile.
“Kwani haukumtambua hadi ukapokea fedha yake?”
“Nilikuwa namfananisha. Niliona kwamba kama nilikwishawahi kumuona sehemu fulani” Msimamizi wa vyoo alijibu.
“Ulikwishawahi kumuona wapi?”
“Kumbe kwenye gazeti ambalo nilikuwa nalo mahali pale”
Mara baada ya kuingia ndani ya jengo la vyoo vile, wakaanza kugonga katika kila mlango wa choo. Kila mtu aliyekuwa akifungua mlango, hakuwa Benedict. Milango tisa ilikuwa wazi, mlango wa choo kimoja tu ndio ambao haukuwa umefunguliwa. Walijaribu kupiga hodi zaidi na zaidi lakini wala mlango haukufunguliwa.
“Kwa hiyo tufanye nini?”
“Tuuvunjeni tu”
“Hebu acheni utani huko. Mkiuvunja mtaulipa?” Msimamizi wa vyoo vile aliuliza.
“Sikiliza bro. Tukimkamata huyu Benedict kuna milioni tano kutoka polisi. Acha tuuvunje tu, tumkamate halafu fedha zako utalipwa na mlango utatengenezwa” Kijana mwingine alimwambia msimamizi wa vyoo vile.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Sawa” Msimamizi wa vyoo alijibu na kazi ya kuuvunja mlango ikaanza huku Benedict akiwa ndani ya choo kile.-
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment