Simulizi : Massacre (Mauaji Ya Halaiki)
Sehemu Ya Tatu (3)
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Tukio la kuuawa kwa mzee Matimya ndani la pori la Pande lilionekana kuwashtua polisi. Hawakuweza kufikiria hata siku moja kama kuna siku pori lile lingetumika kama sehemu ya kufanyia mauaji. Ulinzi mkali ukaanza kuwekwa ndani ya pori lile ili kuzuia kufanyika kwa mauaji mengine zaidi. Kila siku polisi walikuwa na kazi ya kupiga doria ndani ya pori hilo hasa kuanzia nyakati za usiku.
Doria liliendelea kila siku. Hakukuwa na siku za mapumziko kwa polisi ambao walikuwa wamepewa jukumu la kuhakikisha wanaweka ulinzi ndani ya pori hilo. Bunduki zilizokuwa na risasi za kutosha zilikuwa mikononi mwa kila porisi ambaye alikuwa na jukumu la kulilinda pori lile. Huku polisi wakiendelea kuwa katika doria ndani ya pori hilo, ghafla wakashtuka baada ya kuliona gari dogo aina ya Baluni likiingia katika pori hilo.
Hawakutaka kupuuzia kitu chochote kile, walichokifanya ni kuanza kupiga hatua kulifuata gari lile ambalo lilikuwa likienda kwa mwendo wa taratibu. Waliendelea kulifuata zaidi na zaidi huku wakiziweka bunduki zao tayari. Baada ya kufika umbali fulani, gari lile likasimamishwa na vijana watatu kuteremka pamoja na msichana ambaye walimweka chini ya ulinzi wao.
Polisi wote wakaanza kuisikia sauti ya msichana yule ikianza kuomba msamaha. Ghafla kijana mmoja akaonekana akichomoa bunduki yake na kumuelekezea msichana yule ambaye alikuwa akiendelea kulia. Kitendo kile cha kumuelekezea bunduki Judith kilionekana kuwashtua polisi wote.
“Wanataka kumuua…wapige risasi” Polisi mmoja alisema.
“ Kwa haraka sana bila kuchelewa, polisi wawili wakachukua bunduki zao na kuanza kuwamiminia risasi vijana wale. Damu zikatapakaa katika eneo lote, Judith alikuwa akilia huku mikono yake ikiwa kichwani. Milio ya risasi ambayo alikuwa ameisikia ilimfanya kujua kwamba ilikuwa imepenya kichwani mwake kama ambavyo ilitakiwa ifanyike.
Judith akafumbua macho yake, mshangao mkubwa ukawa umempata mara baada ya kuwaona vijana wale wakiwa chini huku damu zikiendelea kuwatoka. Huku akionekana kufikiria juu ya kilichotokea mahali pale, ghafla akashtuka baada ya kuwaona wanaume watatu wakitoka vichakani huku wakiwa na bunduki mikononi mwao. Judith akaingiwa na hofu, akaanza kulia tena.
“Nisameeeeeniiii….sijaf……” Judith aliendelea kulia huku akiomba msamaha.
“Usilie binti. Upo katika mikono salama” Polisi mmoja alimwambia Judith.
Kila Mtanzania alionekana kushtuka kutokana na taarifa za kuchomwa moto kwa kanisa katika usiku uliopita. Vifo vya watu zaidi ya mia mbili na hamsini ndivyo ambavyo vilionekana kuwashtua zaidi. Vyombo vya habari viliandika na kutangaza mambo mengi ambayo yalikuwa yametokea katika kanisa lile. Nchi nzima ya Tanzania ikagubikwa na majonzi, msiba mkubwa ukaonekana kuupata nchi ya Tanzania.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Watu hawakuamini mara baada ya kuiona picha ya kijana ambaye alikuwa amehusika katika kulichoma moto kanisa na kuua idadi kubwa ya watu. Benedict akaonekana kuwa kijana mdogo ambaye hasingethubutu kufanya kitendo kama kile kilichoigusa mioyo ya Watanzania. Watu wakaanza kutoa laana mbalimbali juu ya maisha ya Benedict ambaye alionekana kuwa kama gaidi mwenye roho ya chuma.
Furaha yote ya kuingia mwaka mpaya ikaonekana kuingia doa katika mioyo ya Watanzania. Badala ya watu kufurahia siku hiyo, wakaanza kuhuzunika. Watu wakaanza kukusanyika tena katika eneo la kanisa hilo, ni gofu tu ndilo ambalo lilikuwa limebakia. Hakukuonekana kuwa na dalili ya kunusurika kwa mtu yeyote yule. Mafuta ya binadamu bado yalikuwa yakionekana katika sakafu ya kanisa lile ambalo lilikuwa limebakia kuwa gofu tu.
Kila mtu ambaye alikuwa akiliangalia gofu lile alibaki akitokwa na machozi tu kwani picha ambayo ilikuwa ikionekana ilikuwa ikimuumiza kila mtu. Hasira zao zikaongezeka zaidi na zaidi hasa mara baada ya kuziona picha za Benedict. Ahadi ya shilingi milioni tano kwa mtu yeyote ambaye angefanikisha kukamatwa kwa Benedict ambaye alikuwa ameiumiza mioyo ya Watanzania.
“Ni lazima akamatwe na kufikishwa mbele ya sheria” Mzee mmoja aliyeonekana kuwa na hasira aliwaambia watu waliokuwa wamemzunguka.
Benedict akawa kama lulu katika macho ya Watanzania. Ahadi ya shilingi milioni tano ambazo zilitolewa na serikali kwa yeyote ambaye angefanikisha kukamatwa kwa Benedict kilionekana kuwa kiasi kikubwa cha fedha. Kila Mtanzania akawa makini barabarani. Watu ambao walionekana kufanana na Benedict walikamatwa na kupelekwa katika vituo vya polisi, walipoonekana kuwa si Benedict, waliachiwa huru.
Wapelelezi walikuwa wamekwishasambazwa katika kila kona ndani ya jiji la Dar es Salaam kuhakikisha kwamba Benedict anakamatwa na kufikishwa mbele ya sheria. Kila gari ambalo lilikuwa likiekea nje ya jiji la Dar es Salaam lilikuwa likipekuliwa, hakukuwa na dalili zozote za Benedict kuweza kukimbilia nje ya jiji la Dar es Salaam.
Kadri muda ulivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo dau lililovyozidi kuongezwa mpaka kufikia milioni ishirini kitu ambacho kiliwafanya Watanzania waishio Dar es Salaam wamtafute Benedict kwa nguvu zote. Watanzania wengi walikuwa wakifikiria biashara ambazo wangetakiwa kuzifanya mara tu watakapofanikisha kukamatwa kwa Benedict.
Mlango wa choo ulionekana kuwa mgumu kuvunjika. Walijaribu kuuvunja zaidi na zaidi lakini bado mlango ule haukuweza kuvunjika. Wakabaki wakishauriana ni kwa njia gani ambayo wangeitumia kuuvunja mlango ule. Kwa haraka bila kupoteza muda msimamizi wa vyoo vile akaanza kupiga hatua kuelekea nje, alitumia dakika kadhaa, akarudi akiwa na nyundo.
“Hapa tumemuweza. Ni lazima tumkamate” Kijana mmoja aliwaambia wenzake huku tabasamu likianza kuonekana usoni mwake.
Kazi ya kuuvunja mlango ikaendelea, wakakipiga kitasa kwa nguvu zao zote, kitasa kikavunjika. Hawakutaka kupoteza muda, kijana mmoja akaupiga mlango teke, mlango ukafunguka. Kila mmoja akaonekana kushtuka, ndani hakukuwa na mtu. Wakayapeleka macho yao katika kidirisha kidogo kilichokuwa chooni hapo, nyavu pamoja na nondo havikuwepo.
“Mungu wangu! Amekimbia kupit…..” Msimamizi wa vyoo vile alisema lakini hata kabla hajamalizia sentensi yake vijana wale wakachomoka na kuanza kuelekea nje ya choo kile upande wa dirishani. Alama za viatu zilikuwa zikionekana kuelekea nyuma ya mabanda ya wauzaji wa redio kitu ambacho kila mmoja alibaki akiwa na mshangao mkubwa kwani hawakutegemea kama Benedict angewaacha kwa urahisi namna ile.
Benedict alipiga hatua za haraka haraka kuelekea chooni. Hakutaka kupoteza muda wowote ule, vijana ambao walikuwa wakimfuatilia tayari walikuwa wamekwishamtia wasiwasi. Mara baada ya kuufikia mlango wa choo kile, akaufungia na kuingia ndani. Macho yake yakaanza kuangalia kila kona ndani ya choo kile, akabahatika kukiona kidirisha kidogo kilichokuwa kwa juu huku kikiwa na nondo moja kuu kuu pamoja na nyavu iliyoonekana kuchoka.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Benedict hakutaka kuchelewa, akaichukua ndoo ambayo ilikuwa imejaa maji, akayamwaga, akaigeuza na kisha kuipanda kwa juu. Dirisha lilikuwa usawa na uso wake kitu kilichompelekea kuanza kuisukuma nondo ile. Kazi haikuwa rahisi hata kidogo, japokuwa nondo ile ilikuwa imechoka kupita kiasi lakini ilionekana kuwa ngumu kutoka katika mbao iliyokuwa imeishilia.
Akapigwa na mshtuko mara baada ya kusikia sauti za watu zikiongea nje ya choo kile. Alichokifanya ni kuipeleka mikono yake katika nondo ile na kuanza kuivuta kwa mara nyingine tena. Nondo haikung’oka. Moyo ukamripuka kwa hofu mara baada ya kusikia kitasa cha mlango ule kikianza kutekenywa.Nguvu mpya zikampata Benedict, akaishika vizuri nondo ile. Akaivuta kwa nguvu zote, mbao zile zilizochoka ambazo zilikuwa zimeshikilia nondo ile zikaanza kuiachia. Hakutaka kuacha, aliendelea zaidi na zaidi, nondo ikaanza kutoka kwenye zile mbao zilizochoka. Nguvu alizokuwa nazo zikaongezeka zaidi, hakutaka kujiona akikamtwa kirahisi namna ile, alikuwa radhi kuisumbua serikali na vyombo vya dola na hatimae kukamatwa lakini si kwa kukamatwa kirahisi namna ile.
Mbao ambazo zilikuwa zimeshikiria nondo ile zikachomoka pamoja na nondo ile, Benedict akautoa wavu ambao ulikuwa umeshika dirisha lile na kwa haraka haraka pasipo kupoteza muda akaanza kuuparamia ukuta ule na kutoka nje ya choo kile. Benedict hakutaka kukimbia kwa kuogopa kushtukiwa, akaanza kutembea kwa mwendo wa haraka haraka.
Bado macho yake hayakuwa yakiamini kama alifanikiwa kutoka salama ndani ya choo kile, mara kwa mara moyo wake ulikuwa ukimshukuru Mungu. Uso wake bado ulikuwa ukiangalia chini, hakutaka kumwangalia mtu yeyote usoni. Alitembea katika hali hiyo kwa takribani mwendo wa dakika thelathini, akaamua kusimama mara baada ya kumuona muuza kofia.
“Hiyo kofia shilingi ngapi?”
“Ipi?”
“Hiyo kama ya Malboro”
“Elfu saba” Muuzaji alimjibu.
Benedict hakutaka kupoteza muda kwa kutaka kupunguziwa bei, akauingiza mkono katika mfuko wake na kutoa noti ya shilingi elfu kumi na kumgawia muuzaji. Mara baada ya kugaiwa kiasi kilichobakia, akaendelea na safari yake ya kuelekea Sinza Makaburini. Wala hakukaa sana kituoni, akapanda daladala huku lengo lake likiwa ni kwenda kwa rafiki yake, Hamidu ambaye alikuwa akikaa Tandale.
Kila mtu ndani ya gari alikuwa akilielezea tukio lile la kuchomwa kwa kanisa usiku uliopita pasipo kujua kwamba mchomaji wa kanisa lile alikuwa ndani ya gari lile. Benedict hakuongea kitu chochote kile, alitulia tuli huku kofia ikiwa kichwani mwake jambo ambalo lilimfanya kutokugundulika na mtu yeyote yule. Mara baada ya kufika katika kituo cha Mtogole, akateremka na kuanza kupiga hatua kuelekea katika sehemu iliyokuwa nyumba alikuwa akiishi Hamidu.
Benedict akaanza kupita katika vichochoro tofauti tofauti huku akionekana kutokuwa na wasiwasi kutokana na kofia aliyokuwa ameivaa kumpa ulinzi wa kutosha. Alitumia muda wa dakika tano kupita katika vichochoro, alifika katika nyumba ambayo ilikuwa imezungushiwa ukuta. Benedict akaanza kupiga hodi getini. Wala hazikupita sekunde nyingi, geti likafunguliwa.
“Nikusaidie nini?” Mlinzi wa nyumba hiyo aliuliza.
“Nahitaji kumuona Hamidu”
“Nikamwambie anaitwa na nani?” Mlinzi aliuliza.
Benedict hakutoa jibu lolote lile kwa haraka, akatulia kwa muda huku akianza kujifikiria jibu la swali ambalo alikuwa ameulizwa na mlinzi yule. Hakuwa tayari kulitaja jina lake kwa mtu yeyote ambaye hakumfahamu kwani alijua kwamba alikuwa akitafutwa kwa udi na uvumba.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Mwambie rafiki yake, Matimya” Benedict alijibu.
Moja kwa moja mlinzi akaondoka mahali hapo kuelekea ndani ya nyumba hiyo. Alikaa kwa takribani dakika moja , aliporudi, akamruhusu Benedict kuingia. Benedict akaanza kupiga hatua kuelekea ndani ya nyumba hiyo, alipoufikia mlango wa kuingia sebuleni, akaufungua na kuingia. Akaanza kuyafuata makochi yaliyokuwepo mahali pale na kutulia.
Wala hazikupita sekunde nyingi, Hamidu akatokea mahali hapo. Kila mmoja akaonekana kuwa na furaha mara baada ya kuonana kwa mara nyingine tena. Benedict akainuka kutoka pale kochini, akamfuata Hamidu na kisha kukumbatiana. Wakaanza kuongea kwa furaha, tabasamu pana yalikuwa yakionekana katika nyuso zao. Walipoongea kwa kipindi kirefu, Hamidu akaandaa chai, wakanywa na kutulia tena.
“Hivi ni kweli ulilichoma moto kanisa?” Hamidu alimuuliza Benedict.
“Ndio. Nililichoma kwa sababu nililazimishwa kufanya hivyo” Benedict alijibu.
“Ulilazimishwa! Na nani?”
“Wao wenyewe”
“Wao! Wakina nani?”
“Walioteketea kanisani” Benedict alijibu.
Hamidu akapigwa na mshangao zaidi na zaidi, akamwangalia Benedict mara mbili mbili huku akionekana kutokuelewa kile ambacho kiliongelewa. Akachukua glasi ya maji na kupiga pafu moja na kisha kuyarudisha macho yake usoni kwa Benedict. Jibu ambalo alikuwa amepewa ndilo ambalo lilionekana kumchanganya zaidi.
“Unanichanganya Ben”
“Huo ndio ukweli”
“Walikulazimisha kivipi?”
“Walianzisha chuki kwa familia yetu, hawakutupenda hata kidogo. Mbaya zaidi nafikiri walihusika katika kifo cha baba yangu, mzee Matimya” Benedict alijibu.
“Pole sana” Hamidu alimwambia Benedict.
Hamidu hakuwa na jinsi, akamruhusu Benedict kukaa ndani ya nyumba hiyo na kuahidi kumpa kila kitu kama kumhakikishia ulinzi wake. Benedict hakumtilia shaka Hamidu kwani moyo wake ulimuamini kupita kiasi. Mara kwa mara picha yake ilikuwa ikionekana katika vituo mbalimbali vya televisheni. Moyoni alikuwa akicheka tu, aliamini kwamba hakukuwa na mtu yeyote ambaye angeweza kufahamu kama alikuwepo ndani ya nyumba hiyo.
Watu mitaani bado walikuwa na shauku ya kumpata Benedict. Dau ambalo liliongezwa mpaka kufikia milioni ishirini lilionekana kumchanganya kila mtu. Benedict alitafutwa kwa udi na uvumba lakini hakupatikana sehemu yoyote ile. Picha zake ziliendelea kusambazwa zaidi na zaidi hali iliyopelekea watu wengi kumfahamu Benedict.
Muda ulizidi kwenda mbele, macho ya Benedict yakaanza kujawa na usingizi kutokana na kutokulala usiku uliopita. Akainuka na kuelekea chumbani ambako akajitupa kitandani. Wala hazikupita dakika nyingi, usingizi mzito ukampitia.
Alikuja kushtuka mara baada ya masaa manne kupita. Akaiangalia saa yake ya mkononi na kugundua kwamba ilikuwa imetimia saa kumi alasiri. Huku akionekana kuwa na uchovu, Benedict akaamka na kuanza kuelekea sebuleni. Nyumba nzima ilikuwa kimya, Benedict akaanza kuliita jina la Hamidu lakini wala hakuitikiwa.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Benedict akaanza kuzunguka zunguka ndani ya nyumba hiyo tena katika kila chumba lakini wala Hamidu hakuonekana. Benedict hakutaka kuwa na wasiwasi wowote ule, akaanza kurudi sebuleni na kutulia kochini. Ghafla akainuka na kuanza kuufuata mlango wapae sebuleni, akakishika kitasa na kujaribu kukitekenya, mlango ulikuwa umefungwa kwa ufunguo. Hali ile ikaanza kumtia wasiwasi Benedict, akaanza kueleka sebuleni, napo hali ilikuwa ile ile, mlango ulikuwa umefungwa kwa ufunguo.
“Ni lazima nifanye kitu” Benedict alisema na hapo hapo kuufuata mlango wa kuingilia darini, alipouona, akaufungua na kuingia kwa lengo la kujificha.
Taarifa bado zilikuwa zikiendelea kutolewa katika vyomba mbalimbali vya habari juu ya kutafutwa kwa Benedict. Kiasi cha shilingi milioni ishirini ambacho kilikuwa kimetolewa kilionekana kutokutosha kabisa hali iliyofanywa kuongezwa hadi milioni ishirini. Benedict akaonekana kuwa mtaji hali iliyowafanya watu kuzidi kumtafuta zaidi na zaidi.
Benedict akaonekana kuchoka kukaa sebuleni pale kutokana na macho yake kuwa mazito.Hapo hapo Benedict akainuka na kuelekea chumbani kulala. Hamidu alibaki peke yake pale sebuleni akiangalia televisheni. Moyo wala haukutulia, mvutano mkubwa ukaanza kuvutana ndani ya moyo wake. Upande mmoja ulimtaka aelekee katika kituo cha polisi na kutoa taarifa juu ya uwepo wa Benedict ndani ya nyumba ile lakini upande mwingine ulimkataza kufanya hivyo.
Hamidu hakujua afanye nini, alibaki kimya sebuleni pale huku macho yake yakiendelea kuangalia televisheni. Hamidu hakuendelea kubaki katika hali ile, nae akainuka na kuanza kuelekea chumbani kulala.
“Siwezi kuusaliti urafiki kwa milioni ishirini” Hamidu alijisemea huku akijitupa kitandani na kulala, hakuchukua muda mrefu, usingizi ukampitia.
Hamidu aliamka mara baada ya masaa matatu kupita. Moja kwa moja akayapeleka macho yake katika saa kubwa ya ukutani, tayari ilikuwa imetimia saa tisa alasiri. Hamidu hakutaka kuendelea kubaki sebuleni pale hali ambayo ilimfanya kuelekea sebuleni huku akimwacha Benedict kitandani.
Hamidu akaiwasaha televisheni, macho yake yakatua katika picha ya Benedict ambayo ilikuwa ikionyeshwa mara kwa mara katika televisheni tofauti tofauti. Kiasi kile cha shilingi milioni ishirini kikatangazwa tena kuwa kama zawadi kwa mtu yeyote ambaye angefanikisha kukamatwa kwa Benedict. Matatizo mbalimbali ya kifedha yakaanza kumiminika kichwani mwake.
Alimkumbuka mama yake ambaye alikuwa akiugua ugonjwa wa moyo, zilihitajika fedha kwa ajili ya matibabu. Mawazo ya matatizo yake hayakuishia hapo, akaanza kumkumbuka mpenzi wake, Salama ambaye alikuwa mjauzito. Salama alikuwa akihitaji matunzo na aliamini kama angekuwa na kiasi kie cha fedha basi mambo yangekuwa rahisi zaidi. Kila kitu katika kipindi hicho ambacho alikuwa akikifikiria kilikuwa kikihitaji fedha.
Hadi kufikia hatua hiyo, moyo wake haukutaka kufikiria urafiki tena, kwa haraka haraka akainuka kochini na kuanza kuelekea chumbani kwake. Akafungua droo ya kitanda na kutoa funguo zote za milango ya nyumba ile. Akatoka chumbani mule na kuanza kufuata mlango wa jikoni na kisha kuufunga. Hakuishia hapo, pia akaufuata mlango wa sebuleni na kisha kuufunga.
Akaanza kupiga hatua za haraka haraka kuelekea getini. Akili yake haikuwa ikifikiria kitu chochote zaidi ya fedha, tena kiasi ambacho kingemaliza matatizo yote ambayo alikuwa nayo. Hakutaka kumwambia mlinzi kitu chochote kile ka kuhofia kwamba nae angehitaji kiasi fulani cha fedha.
“Mbona unaonekana una haraka namna hiyo?” Mlinzi alimuuliza Hamidu.
“Narudi saa hivi”
“Unaelekea wapi?”
“Narudi sasa hivi” Hamidu alilirudia jibu lake.
Mlinzi akabaki kutokuelewa kitu chochote ambacho kilikuwa kinaendelea. Alitamani kuuliza swali jingine lakini hakupata nafasi hiyo kwani tayari Hamidu akawa amekwishapotea machoni mwake.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hatua zake zilikuwa za haraka haraka, kijasho chembamba kilikuwa kikimtoka hali iliyomfanya kuchukua kitambaa chake na kuanza kujifuta. Katika kipindi hicho alikuwa akipiga hatua kuelekea katika kituo cha polisi cha Tandale huku kichwa chake kikiwa kinafikiria fedha kiasi cha shilingi milioni ishirini. Moyo wake ulikuwana furaha kwani hakuamini kama katika kipindi kichache kijacho angekuwa na kiasi kikubwa cha fedha. Moyo wake ulikuwana furaha kwani hakuamini kama katika kipindi kichache kijacho angekuwa na kiasi kikubwa cha fedha.
Ingawa alikuwa akitembea kwa hatua za haraka haraka lakini bado alijiona akitembea kwa mwendo wa taratibu. Moyoni alitamani apate mbawa katika kipindi hicho ili apae na kutua katika kituo cha polisi cha Tandale. Akili yake wala haikuukumbuka urafiki kati yake na Benedict, kitu ambacho alikuwa akikikumbuka ni milioni ishirini ambazo aliziona zikiwa mlangoni.
Hamidu akaanza kukimbia, kila mtu njiani alibaki akimshangaa lakini hilo wala hakuonekana kujali chochote kile. Kadri alivyozidi kupiga hatua kuelekea mbele na ndivyo ambavyo furaha ndani ya moyo wake ilivyozidi kuongezeka zaidi. Mara baada ya kutumia dakika kadhaa, akafika katika kituo cha polisi cha hapo Tandale.
“Vipi kijana?” Polisi mmoja alimuuliza Hamidu.
“Yu…po..nyu..mban..i” Hamidu alijibu huku akihema.
“Yupo nyumbani? Nani?”
“Benedi…ct…” Hamidu alijibu.
Kila polisi akaonekana kushtuka, jina ambalo alilitaja Hamidu ndilo ambalo lilionekana kuwashtua. Wote wakaanza kumwangalia Hamidu huku wakionekana kutokuamini kile ambacho kilitoka mdomoni mwa Hamidu.
“Unasemaje?”
“Benedict”
“Yupo wapi?”
“Nyumbani” Hamidu alijibu.
Kila polisi akaonekana kuchanganyikiwa kwa furaha, gari aina ya Defender likasogezwa karibu, polisi watano waliokuwa na bunduki mikononi mwao wakaingia pamoja na Hamidu. Gari likaanza kuendeshwa kwa mwendo wa kasi. Kila polisi akashikilia vizuri bunduki aliyokuwa nayo mkononi. Wananchi wakabaki wakishangaa, mwendo wa kasi wa gari lile uliwafanya kujua kwamba kuna kitu ambacho kilikuwa kimetokea.
“Una uhakika kijana kwamba mtu huyo ni Benedict?” Polisi mmoja alimuuliza Hamidu.
“Asilimia mia tatu” Hamidu alijibu.
Gari likafunga breki katika eneo la Mafyoso Camp. Wahuni wote ambao walikuwa wakipita njia karibu na eneo la Camp hiyo wakaanza kukimbia. Polisi wote wakaruka chini kama makomandoo, wakaanza kupiga hatua kuelekea katika vichochoro huku wakimfuata Hamidu. Wananchi hawakuelewa kitu chochote ambacho kilikuwa kinaendelea mahali hapo, kila kitu kilichokuwa kikitokea kilionekana kuwa kama filamu.
Mlinzi akabaki kuwa na mshtuko mara baada ya kuwaona polisi waliokuwa na bunduki wakifika katika eneo hilo huku wakiwa na bunduki mikononi mwao. Moja kwa moja wakaingia ndani ya eneo la nyumba hiyo, polisi watatu wakaanza kuzungu zunguka katika eneo hilo huku polisi wawili wakiingia ndani pamoja na Hamidu.
Moja kwa moja wakaanza kupiga hatua kuelekea chumbani. Mikono yao ilishikilia vizuri bunduki zao. Mara baada ya kuufikia mlango wa chumba kile, wakaufungua na kuingia ndani. Kitanda kilionekana kuwa kitupu, hakukuwa na mtu yeyote yule. Wakaanza kuangalia uvunguni mwa kitanda, kabatini na kila sehemu chumbani mule lakini hakukuwa na mtu yeyote.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wakatoka chumbani na kuanza kuangalia katika kila sehemu ndani ya nyumba ile lakini napo hakukuwa na mtu yeyote yule. Kila mmoja akabaki kimya akimwangalia mwenzake. Hamidu alibaki akishagaa tu, hakuamini macho yake kama Benedict hakuwepo ndani ya nyumba hiyo na wakati milango ilikuwa imefungwa na funguo alikuwa nazo yeye mwenyewe.
“Vipi?” Polisi mmoja aliyeonekana kuwa kiongozi aliuliza.
“Hayupo”
“Mmeangalia vizuri?”
“Ndio mkuu”
“Hadi stoo na chooni?”
“Kila sehemu. Hakuna mtu”
Kila mmoja akakaa kimya huku wakimwangalia Hamidu ambaye alionekana kama kujifikira kitu. Hamidu akakaa katika hali hiyo kwa sekunde kadhaa, akaanza kupiga hatua kuelekea katika korido ndani ya nyumba hiyo. Moja kwa moja akayapeleka macho yake katika mlango wa kuingilia darini, mlango ulionekana kukaa upande tofauti na siku nyingine hali iliyoonyesha kuwa kuna mtu alikuwa ameufungua.
“Benedict….” Hamidu alisema kwa sauti ya chini huku macho yake yakiangalia mlango ule wa dari.
“Unasemaje?” Polisi mmoja aliuliza.
“Nafikiri atakuwa darini” Hamidu alijibu.
Hakukuwa na muda wa kupoteza, hapo hapo polisi mmoja akaanza kupanda darini kwa msaada wa polisi wengine. Darini kulikuwa na giza kitu ambacho kilimfanya yule polisi kutokuona kitu chochote kile. Akaomba tochi, kwa haraka haraka Hamidu akaelekea chumbani kuleta tochi.
“Kuna dalili za kuwepo huko?” Polisi mmoja aliuliza.
“Ndio. Nasikia harufu ya pafyum huku” Polisi yule aliyekuwa darini alijibu. Hamidu wala hakuchelewa kurudi, ni ndani ya sekunde kadhaa akarudi mahali pale na kumgawia tochi polisi aliyekuwa darini.
Bado msako wa kumtafuta Benedict ulikuwa ukiendelea kama kawaida mitaani. Kila polisi alionekana kuchanganyikiwa kutokana na kutokupatikana kwa Benedict. Kamanda mkuu wa polisi, Bwana Idrisa alionekana kuchanganyikiwa zaidi. Ofisini hakukukalika kabisa, akili yake ilikuwa ikimfikiria Benedict tu. Kila alipokuwa akiziangalia picha za Benedict ofisini pale, alikuwa akipiga meza kwa hasira.
Kamanda Idrisa akaunyanua mkonga wa simu na kupiga namba fulani ambapo baada ya muda simu ikapokelewa na kuanza kuongea na mtu wa upande wa pili. Aliongea nae kwa takribani dakika tano, akakata simu. Bwana Idrisa alionekana kuwa na mawazo, hakuamini kama kweli mpaka muda huo Benedict hakuwa amepatikana japokuwa walikuwa wametangaza kutoa kiasi kikubwa cha fedha kwa mtu yeyote ambaye angefanikisha kukamatwa kwa Benedict.
Alikaa katika hali hiyo ya mawazo kwa takribani dakika thelathini, mara akashtushwa na sauti ya mlango ambao ulikuwa ukigongwa. Akatoa kauli ya kumtaka mgongaji kuingia ndani. Vijana watatu, wavulana wawili na msichana mmoja wakaingia ndani ya ofisi ile na kutoa salamu kwa kupiga saluti na kisha kukaa katika viti vilivyokuwa ndani ya ofisi hiyo.
Kamanda Idrisa hakuongea kitu chochote kile, alibaki kimya kwa muda huku akiwaangalia vijana wale ambao walikuwa mule ofisini mwake. Kwa kuwaangalia tu, vijana wale walionekana kuwa shupavu sana kutokana na miili yao kujengeka vizuri kutokana na mazoezi ambayo walikuwa wakiyafanya. Aliporidhika, akachukua moja ya faili ambalo lilikuwa pale mezani, akalifungua na kutoa picha za Benedict na kuziweka mezani.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Mnamuona huyu?” Kamanda Idrisa aliwauliza.
“Ndio” Wote waliitikia kwa pamoja mara baada ya kuziangalia picha zile.
“Masaa kumi na moja yamepita tangu aiumize mioyo ya Watanzania” Kamanda Idrisa alisema na kuendelea.
“Kwa masaa hayo yote wananchi wameshindwa kumkamata kabisa na sidhani kama wataweza kumkamata. Kazi hii nawaachieni ninyi, fanyeni kazi hii kwa nguvu zote, tunamhitaji mtu huyu” Kamanda Idrisa aliwaambia vijana wale ambao walikuwa wapelelezi.
“Martin, Moody na Sabrina, tunamtaka mtu huyu ndani ya masaa sabini na mbili” Kamanda Idrisa aliwaambia.
“Usihofu mkuu. Ndani ya masaa hayo tutakuwa tumefanikisha zoezi hilo” Moody alimwambia kamanda Idrisa.
Mara baada ya kupewa maelekezo yote, wapelelezi wale wakatoka ndani ya ofisi ile huku wakiwa na picha tatu za Benedict. Wakalifuata gari lao ambalo walikuwa wamelipaki katika eneo la ofisi ile ya makao makuu ya polisi na kisha kuondoka mahali hapo.
Kila mmoja ndani ya gari alikuwa akifikiria lake, kazi ambayo ilikuwa mbele yao ilikuwa ngumu lakini kutokana na uzoefu mkubwa waliokuwa nao kazi ile ikaanza kuonekana kuwa nyepesi tofauti na kazi mbalimbali ambazo walikuwa wamezifanya kabla. Mafanikio makubwa ya kipelelezi ambayo walikuwa wameyapata katika kazi nyingi zilizopita ziliwapa nguvu za kuona kwamba walikuwa na uhakika wa asilimia mia moja kufanikisha kile ambacho kilikuwa mbele yao.
“Hii ni kazi ndogo sana, yaani ni kama kumsukuma mlevi mlimani” Marini aliwaambia wenzake.
“Tuliwapata watu ambao waliisumbua serikali kwa kipindi kirefu sana, huyu hawezi kutusumbua hata mara moja” Moody alichangia.
“Nafikiri masaa tuliyopewa ni mengi sana, yaani naona tungepewa masaa matano tu” Sabrina alisema maneno ambayo yaliwafanya wote kuanza kucheka kwa uhakika wa kufanikisha kumkamata Benedict.
Mara baada ya kukabidhiwa tochi moja kwa moja polisi yule akaanza kumulika mule darini. Alimulika katika kila sehemu ndani ya dari lile lakini hakukuwa na mtu yeyote yule ni mabomba ya nyaya za umeme pamoja na mbao ndivyo ambavyo vilikuwa vikionekana mbele yake. Kadri ambavyo polisi yule alivyozidi kumilika darini mule na ndivyo ambavyo jasho lilivyozidi kumtoka kutokana na joto kali ambalo lilikuwa mule darini.
“Vipi tena? Mbona hausemi chochote?”
“Hakuna mtu. Mungu wangu!”
“Kuna nini tena?”
“Siamini!”
“Huamini nini?”
“Njooni muone” Polisi yule alisema.
“Acha hizo. Tuambie kuna nini?”
“Ametoroka. Bati limeachia, nafikiri alitoa baadhi ya misumali”
“Lakini si umesema kuna harufu ya pafyumu?”
“Harufu bado ipo ila yeye hayupo” Polisi yule alijibu.
Jibu lile lilionekana kumchanganya kila mtu aliyelisikia. Hawakuonekana kuamini kama kile walichokisikia kilikuwa sahihi au walikuwa wamesikia vibaya. Polisi yule akateremka, Mwili wake ulikuwa umejaa jasho huku shati lake likionekana kuchafuka. Hawakutaka kuendelea kubaki ndani ya nyumba ile, wote wakaanza kutoka nje na kumfuata mlinzi ili kutaka kufahamu mahali alipokuwa Benedict.
“Mgeni wangu yupo wapi?” Hamidu alimuuliza mlinzi ambaye alionekana kutetemeka.
“Sijui yupo wapi”
“Hakutoka hapa?”
“Hakuna aliyeingia wala kutoka” Mlinzi alijibu.
Kila mmoja akaonekana kuchoka. Walimwangalia mlinzi mara mbili mbili huku wakionekana kutokuamini kile ambacho alikuwa akiwaambia. Milioni ishirini zilizokuwa kichwani mwa Hamidu zikaanza kupotea, matatizo ambayo alikuwa nayo aliyaona kuendelea kama jinsi ambavyo yalivyokuwa. Machozi yakaanza kumlenga kwani hakuamini kama Benedict angeweza kutoroka ndani ya nyumba ile na kumfanya kukosa kiasi cha shilingi milioni ishirini ambacho kilitangazwa kuwa kama zawadi kwa yeyote ambaye angefanikisha kukamatwa kwake.
Joto lilikuwa kali darini kutokana na jua ambalo lilikuwa likiendelea kumulika na kulifanya bati la nyumba ile kupata joto. Darini kulikuwa na giza kitu ambacho kilimfanya kutokuona kitu chochote kile. Benedict hakutaka kufanya kitu chochote kile, alitulia kwa muda huku akiyapa nafasi macho yake kulizoea giza lililokuwa kule darini. Ni ndani ya dakika mbili tu, macho yake yakaanza kuona kila kitu.
Ni mbao zilizoshikilia bati na mabomba yaliyokuwa na nyaya za umeme ndivyo vitu ambavyo vilikuwa vikionekana mule darini. Benedict akaingia ndani zaidi, jasho likaanza kumtoka huku kadri muda ulivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo joto lilivyozidi kuongezeka. Hakukuonekana kuwa na njia yoyote ile ambayo ingemfanya kutoka salama ndani ya nyumba ile.
Kitu alichokifanya ni kuanza kutembea chini chini hadi kufika katika sehemu ambayo ilikuwa karibu na nje. Akajilaza chali juu ya kenchi na kisha miguu kuipeleka kwenye bati. Kwa kutumia nguvu zote ambazo alikuwa nazo, akaanza kulisukuma bati lile kwa juu huku wakati mwingine akiligongagonga. Akaendelea kupiga zaidi na zaidi tena kwa nguvu zote, mara bati likaanza kwenda juu huku misumali ile ambayo iliishikilia bati lile ikianza kuachia.
Nguvu alizokuwa nazo zikaongezeka zaidi kwani alitumaini kwamba kazi ile wala haikuwa ngumu kama alivyofikiria kabla, aliendelea zaidi na zaidi. Nguo zake zote ambazo alikuwa amezivaa zilikuwa zimeloana kana kwamba alikuwa amemwamgiwa ndoo ya maji. Kadri alivyokuwa akifikiria jinsi alivyokuwa akitafutwa na polisi na ndivyo ambavyo alipta nguvu zaidi ya kufanya kile ambacho alikuwa akikifanya kwa wakati ule. Akili yake haikutaka kukubali kabisa kama Hamidu alikuwa ameelekea sehemu nyingine zaidi ya kituo cha polisi.
Taratibu misumali ikapanda zaidi hadi kuachia mbao. Benedict akalisogeza bati kwa nguvu zote na kuliinua upande ule aliokuwa na kisha kuanza kupitisha kichwa. Hali ilionekana kuwa ngumu sana kwake lakini aling’ang’ania mpaka akafanikiwa huku akiwa amejichuna vya kutosha. Akafanikiwa kutoka, akajirusha mpaka chini, akaangalia katika kila upande, hakumuona mtu yeyote yule.
Sauti za watu zikaanza kusikika masikioni mwake, akajisogeza pembezoni mwa ukuta na kuanza kuchungulia kule kulipokuwa na geti. Akapigwa na mshtuko mara baada ya kumuona Hamidu akiwa na polisi watano huku wakiingia ndani ya eneo la nyumba ile. Hakutaka kubaki mahali hapo ili kuona ni kitu gani ambacho kingeendelea, alichokifanya ni kuuparamia ukuta na kutokea upande wa pili na kuondoka zake huku akimshukuru Mungu kwa kumtoa salama ndani ya nyumba ile.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wapelelezi, Martin, Moody na Sabrina hawakutaka kupoteza muda. Moja kwa moja wakajiweka tayari na kuanza kazi ya kumtafuta Benedict kwa masaa sabini na mbili tu. Kitu walichokifanya ni kuanza kuelekea Mwenge alipokuwa akiishi Benedict huku lengo lao likiwa ni kutaka kupata kila kitu walichokihitaji kuhusu Benedict.
Mara baada ya kufika nje ya geti, dereva akaanza kupiga honi ambako baada ya muda mchache, Angelina akafika getini na kufungua geti. Gari likaingizwa ndani hadi katika sehemu ya maegesho. Wapelelezi wakateremka, wakaongea kidogo na Angelina na kisha kuanza kuelekea ndani huku dhumuni lao likiwa kutaka kuongea na Bi Meriana.
Wakajiweka kochini, Angelina akaondoka mahali hapo kuelekea chumbani na baada ya muda akarudi sebuleni hapo akiongozana na mama yake, Bi Meriana. Uso wa Bi Meriana ulionekana kuwa na majonzi, macho yake yalikuwa mekundu hali iliyoonyesha kwamba katika kipindi kichache kilichopita alikuwa akilia. Huku akionekana kuwa na uchovu, akajiweka kochini na kuanza kuangaliana na wapelelezi wale.
Wakabaki wakiangaliana kwa muda fulani. Kitu walichokifanya wapelelezi wale ni kutoa vitambulisho vyao na kumgawia Bi Meriana ambaye akaanza kuviangalia. Aliviangalia kwa sekunde kadhaa, aliporidhika, akawarudishia.
“Tunahitaji kufahamu baadhi ya vitu kuhusu Benedict” Martin alimwambia Bi Meriana.
“Vitu gani?”
“Vitu vyote ambavyo tutaviulizia” Martin alijibu.
Wote wakaanza kutoa karatasi pamoja na kalamu walizokuwa nazo tayari kwa kuandika maelezo ambayo walitarajia kuyapata kutoka kwa Bi Meriana na Angelina. Ukimya ukatawala mahali hapo kwa dakika kadhaa na baada ya muda maongezi yakaendelea.
“Hupendelea kwenda sehemu gani baada ya mapumziko ya muda mrefu nyumbani?” Martin aliuliza huku mkono wake ukijiandaa kuandika.
“Kwa marafiki zake mbalimbali” Angelina alijibu.
“Marafiki hao wanaishi maeneo gani”
“Maeneo tofauti tofauti, Magomeni, Ilala, Tandale, Mbag…….”
“Na vipi kuhusu kumbi za starehe?” Moody alidakia kwa kuuliza swali.
“Shindwa. Mwanangu ni Mkristo safi hawezi kwenda sehemu kama hizo” Bi Meriana alijibu huku akionekana kukasirishwa na swali lile.
“Samahani. Vipi kuhusu ufukweni?”
“Ni mara chache sana huenda huko”
“Nyakati gani?”
“Jioni” Angelina alijibu.
Maswali hayakuendelea tena, wakaweka makaratasi yao ndani ya vitabu vyao, wakainuka, wakaaga na kuondoka mahali hapo. Vichwa vyao tayari vikaanza kupata picha fulani, kutokana na ujuzi mkubwa waliokuwa nao katika kazi ile, tayari walionekana kufahamu baadhi yavitu ambavyo waliviona vingewasaidia. Wakaingia ndani ya gari lao, nyuso zao zilikuwa zikionyesha tabasamu ya mafanikio. Gari likawashwa na kuondoshwa ndani ya eneo la nyumba hiyo.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Umepata picha gani?” Sabrina aliuliza.
“Kuna asilimia kubwa atakuwa ufukweni” Martin alijibu.
“Kwa nini?”
“Hawezi kwenda sehemu nyingine tofauti na hiyo kwani anajua kwamba anatafutwa”
“Ok! Unafikiri fukwe gani? Coco au?”
“Haiwezekani kuwa huko”
“Kwa nini?”
“Kwa sababu ya idadi kubwa ya watu” Martin alijibu.
Benedict hakutaka kuendelea kupoteza muda katika upande wa pili wa nyumba ile ambayo ilikuwa ikikaliwa na Hamidu. Akaanza kukimbia huku akipita katika vichochoro tofauti. Sauti kubwa ya muziki wa taarabu ikaanza kusikika masikioni mwake, Benedict akapunguza kasi, akaanza kutembea kwa mwendo wa kawaida kuelekea kule ilipokuwa ikitokea muziki wa taarabu.
Benedict akaiweka vizuri kofia yake kwa kuishusha zaidi ili kuuziba uso wake. Akaendelea mbele zaidi hadi alipokimaliza kichochoro kile. Akatokea katika sehemu iliyokuwa na eneo kubwa. Idadi kubwa ya watu wasiopungua sabini walikuwa katika eneo hilo, maspika makubwa zaidi ya matano yalikuwepo katika eneo hilo.
Benedict hakutaka kupoteza muda mahali hapo, akaanza kutembea kuelekea katika upande mwingine kwa kupita katikati ya watu waliokuwa wakicheza muziki ule wa taarabu. Hakukuwa na mtu yeyote abaye alikuwa akifahamu kwamba mtu yule ambaye alikuwa akipita katikati yao alikuwa Benedict, muuaji ambaye alikuwa akitafutwa na Watanzania katika kipindi hicho.
Mara baada ya kutoka katika eneo lile lililokuwa na ‘rusha roho’ moja kwa moja Benedict akaendelea na safari yake. Maswali kibao bado yalikuwa yakiendelea kumiminika kichwani mwake juu ya usaliti ambao aliufanya rafiki yake, Hamidu dhidi yake. Moyo wake haukuamini hata kidogo kama Hamidu angeweza kufanya kile alichokifanya cha kumletea polisi ili wamkamate.
Hakutaka kumuamini mtu mwingine yeyote, Hamidu alionekana kumpa picha halisi juu ya marafiki zake wengine ambao alikuwa nao. Mara baada ya kufika katika barabara ya vumbi, akaanza kunyoosha moja kwa moja huku lengo lake likiwa ni kutaka kufika katika kituo cha mabasi cha Argentina kwa kupitia katika soko kuu la Tandale.
Alitumia dakika kumi mpaka kufika katika kituo cha daladala cha Argentina, akapanda daladala iendayo Kariakoo. Stori kuhusu yeye ndizo ambazo zilikuwa zimetawala ndani ya daladala ile. Benedict hakuonekana kushtuka, akabaki katika hali ile ile ya kawaida. Gari lilipofika katika kituo cha Usalama, Magomeni, akateremka na kuanza kutembea kwa miguu kuelekea katika kituo cha Magomeni Hospitali.
Picha zake zilikuwa zimezagaa katika kila sehemu alizokuwa akipita. Kofia yake bado ilikuwa kichwani mwake, uso wake alikuwa ameuinamisha chini kwa kuhofia kujulikana na watu ambao alikuwa akipishana nao. Kutoka Usalama hadi Magomeni Hospitalini alitumia dakika tano tu akawa amekwishafika katika katika kituo hicho ambapo akachukua daladala iliyokuwa ikielekea Kawe.
“Yaani siku ya pili hii, hata dalili za kukamatwa kwake hazijajionyesha” Mzee mmoja aliongea kwa sauti huku mkononi akiwa na gazeti la Ze Utamu. Kila abiria aliyekuwa ndani ya daladala ile akageuka na kumwangalia mzee yule.
“Yaani hata tetesi kuwa alionekana Mwenge” Kijana mmoja alimwambia mzee yule.
“Kama alionekana kwa nini sasa wasimkamate? Huo ni uongo” Mzee yule alisema.
Benedict akazidi kuuficha uso wake vizuri kwa kutumia kofia ile kwani hali ilivyoonekana ndani ya daladala ile, ni lazima angepigwa hata kabla ya kupelekwa polisi kama tu angegundulika. Safari bado iliendelea mbele, abiria wengine walikuwa wakiteremka na kupanda lakini hakukuwa na mtu yeyote ambaye aligundua kama Benedict alikuwepo ndani ya daladala ile.
Mara baada ya kufika katika kituo cha Sanaa, Benedict akateremka, akavuka barabara na kuanza kupiga hatua kuelekea ufukweni. Benedict hakuonekana kujiamini, mara kwa mara macho yake yalikuwa yakiangalia nyuma kuona kama kulikuwa na mtu aliyekuwa akimfuatilia. Alitumia mwendo wa dakika kumi hadi kufika ufukweni. Benedict akaendelea kupiga hatua hadi katika sehemu ambayo ilionekana kufaa machoni mwake.
Macho yake yalikuwa yakiangalia jinsi ambavyo mawimbi yalikuwa yakipiga nchi kavu. Furaha ya kulichoma kanisa na kuua watu zaidi ya mia mbili na hamsini bado iliendelea kuwepo ndani ya moyo wake. Aliporidhika kuangalia mawimbi yale, akayapeleka macho yake katika kioo cha saa yake na kugundua kuwa ni saa kumi na mbili na nusu jioni.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Benedict akayaamisha macho yake kutoka katika kioo cha saa yake na kuyapeleka pembeni. Benedict akapigwa na mshtuko mkubwa mara baada ya kuyagonganisha macho yake na ya mwanamke ambaye alikuwa amekaa mchangani. Msichana yule akashtuka kupita kiasi, akamwangalia vizuri Benedict huku akionekana kuamini kile ambacho alikuwa akikiona mbele yake.
Kwa mbali msichana yule akaanza kutetemeka kwa woga, kwa haraka haraka akainuka kutoka pale alipokuwa na kuanza kuondoka huku akianza kugeuka geuka nyuma kumwangalia Benedict. Mara baada ya msichana yule kupotea machoni mwake, hapo hapo akainuka na kuanza kuelekea sehemu nyingine ambapo kulikuwa na mawe mengi. Wala hazikupita dakika nyingi, mara akamuona yule msichana akirudi pale ufukweni akiongozana na polisi aliyeonekana mlinzi ambaye alikuwa na bunduki mkononi.
Safari ya kuelekea katika ufukwe wa Msasani bado ilikuwa ikiendelea. Mara baada ya kufika Sanaa, Moody akalikata gari kona ya upande wa kulia na kuanza kuelekea katika ufukwe huo. Njia nzima, wapelelezi walikuwa makini kuwaangalia watu ambao walikuwa wakipishana nao. Walichukua dakika tatu wakafika katika ufukwe huo ambako kulikuwa na idadi ndogo ya watu.
Hakukuwa na mtu yeyote ambaye aliteremka garini, walibaki humo huku wakiyapeleka macho yao katika kila kona ufukweni hapo. Dalili za uwepo wa Benedict hazikuwepo kabisa ufukweni hapo. Huku Moody akianza kuingiza gia tayari kwa kuliondosha gari ufukweni hapo, ghafla macho yake yakatua kwa msichana ambaye alikuwa akitembea kwa mwendo wa haraka haraka huku akiangalia nyuma.
“Nafikiri kuna kitu kinaendelea” Moody aliwaambia wapelelezi wenzake.
“Sabrina, mfuatilie msichana yule” Moody alimwambia Sabrina.
Kwa haraka sana pasipo kupoteza muda, Sabrina akateremka garini na kuanza kumfuatilia msichana yule. Yule msichana hakuonekana kujiamini, muda wote alikuwa akiangalia angalia nyuma. Sabrina hakutaka kumuacha msichana yule mbali, alimuacha umbali wa hatua kumi tu. Safari ya msichana yule iliishia mbele ya geti kubwa ambako kulikuwa na mlinzi mmoja aliyekuwa na bunduki kubwa.
“Yupo kuleeee….” Yule msichana alimwambia mlinzi yule.
“Nani?”
“Benedict…..Benedict Matimya” Msichana yule alijibu.
Mlinzi yule akaonekana kushtuka, alimwangalia msichana yule mara mbili mbili huku akioenekana kutokuamini kile ambacho alikuwa amekisikia kutoka kinywani mwake. Akaishika vizuri bunduki ile na kuanza kuondoka na msichana yule kuelekea kule ufukweni. Kichwa cha mlinzi yule kikaanza kufikiria fedha, milioni ishirini ambazo kila siku zilikuwa zikitangazwa zikaonekana kumchanganya na kujiona akiwa tajiri.
Sabrina akaanza kupiga hatua kuelekea kule ambako alikuwa amewaacha wenzake ndani ya gari. Macho yake hayakuacha kumwangalia mwanamke yule na askari yule ambao walikuwa wakizidi kuondoka kuelekea ufukweni. Mara baada ya kulifikia gari lile, akaufungua mlango na kuingia ndani.
“Vipi?” Martin aliuliza
“Endesha gari kuelekea kule, wafuate wale. Yupo kule” Sabrina alimwambia Moody.
Hakukuwa na cha kuuliza tena, Moody akawasha gari na kuanza kuelekea kule walipokuwa wakielekea askari yule na mwanamke yule. Waliendelea mbele kwa mwendo fulani, Moody akasimamisha gari na wote kuteremka. Wakaanza kutembea kwa mwendo wa haraka haraka kule ambapo mwanamke yule na askari walipokwa wakielekea. Wakaziandaa bunduki zao vilivyo kwani kila mmoja alikuwa na uhakika kwamba Benedict alikuwa kule.
“Yuko wapi sasa?” Waliisikia sauti ya askari yule ikiuliza.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Alikuwa hapa. Nilimwacha hapa. Alikuwa amevaa kofia kubwa” Mwanamke yule alijibu.
Martin na wapelelezi wenzake wakajifanya kutokujishughulisha na kitu chochote kile, wakaanza kuyapeleka macho yao katika kila kona ufukweni pale. Hakukuwa na uwepo wa Benedict mahali pale. Waliendelea kuangalia angalia katika kila kona mahali pale huku giza likiendelea kuingia lakini wala Benedict hakuonekana ufukweni pale hali iliyowafanya kuanza kukata tamaa.
“Martin……Moody…” Sabrina aliwaaita. Kwa haraka haraka Martin na Moody wakaanza kumfuata Sabrina ambaye alikuwa amesimama karibu na ukuta uliozunguka hoteli ya Casanova.
“Angalieni ukuta huu” Sabrina aliwaambia.
“Mbona sijakupata. Unamaanisha nini?” Moody aliuliza.
“Hauoni alama za viatu? Atakuwa ameruka kuingia katika eneo la hoteli hii” Sabrina aliwaambia.
Hawakutaka kuendelea kubaki mahali hapo, walichokifanya ni kuanza kuelekea katika sehemu walipokuwa wamelipaki gari lao, wakaingia ndani na kuanza kuelekea mbele ya hoteli ile. Ndani ya gari, kila mmoja alikuwa kimya huku bunduki zao zikiwa viunoni mwao, kila mmoja aliona kwamba Benedict atakuwa amechukua chumba ndani ya hoteli ile. Hawakuchukua muda mrefu wakawa wamekishafika ndani ya eneo la geti lile na kuteremka garini.
“Kuna mtu yeyote aliyetoka?” Martin alimuuliza mlinzi mara baada ya kumuonyeshea vitambulisho vyao.
“Muda gani?”
“Ndani ya dakika tano zilizopita”
“Hapana”
Hawakutaka kupoteza muda, walichokifanya ni kuanza kupiga hatua kuelekea katika sehemu ya mapokezi hotelini hapo. Mara baada ya kufika mapokezini pale, wakatoa vitambulisho vyao na kumuonyeshea dada yule aliyekuwepo pale mapokezini. Macho yao wala hayakutulia, walikuwa wakiangalia katika kila kona mahali pale ili Benedict asiweze kuwatoroka tena.
Wapelelezi wakapewa ruhusa ya kumtafuta Benedict katika maeneo ya hoteli ile. Walimtafuta katika kila kona ndani ya maeneo ya hoteli ile lakini hawakuweza kumpata. Kila mmoja akaonekana kuchanganyikiwa, hawakuelewa sehemu ambayo Benedict alipokuwa amejificha. Wapelelezi hawakutaka kuridhika, moja kwa moja wakarudi mapokezini na kuomba ruhusa ya kumtafuta Benedict katika vyumba ndani ya hoteli ile.
“Hawezi kuwa huko jamani. Hawezi kuwa huko” Dada wa mapokezi aliwaambia.
“Kwa nini isiwezekane?”
“Ataingia chumba gani? Atatumia funguo zipi?”
Hakukuwa na mtu ambaye aliyajibu maswali yale ambayo yalikuwa yameulizwa na dada yule, walibaki wakiangaliana tu. Ingawa dada yule wa mapokezi alikuwa amewaambia kwamba Benedict hakuwa kaika chumba chochote ndani ya hoteli ile lakini wakaonekana kabisa kutokukubaliana nae.
“Acha tufanye upekuzi tu. Bado hatujaridhika” Martin alimwambia dada yule.
Dada wa mapokezi hakutaka kuendelea kuweka mgomo, alichokifanya kwa wakati huo ni kumpigia simu mmiliki wa hoteli ile, Bwana Matemba. Zilipita dakika kumi, gari moja la kifahari likaanza kuingia ndani ya hoteli ile na kisha mzee mmoja ambaye alikuwa na ndevu zilizojaa mvi kuteremka na kuanza kuelekea mapokezini.
“Kuna nini Shannia?”
“Kuna watu kutoka katika makao makuu ya polisi” Shannia alijibu.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wapelelezi wakatoa vitambulisho vyao na kisha kumgawia mzee Matemba ambaye alivichukua na kuanza kuviangalia. Aliviangalia kwa sekunde kadhaa, aliporidhika, akawarudishia.
“Na vipi kibali cha kufanya upekuzi?” Bwana Matemba aliwauliza
“Hicho hatuna kwa sababu kitu chenyewe kimetokea ghafla” Martin alijibu.
Mzee Matemba hakuwa na kipingamizi, akawaruhusu wapelelezi waanze kufanya msako ndani ya vyumba vilivyokuwa katika hoteli ile ingawa vyumba vingine vilikuwa na wageni. Msako ukaanza kufanyika kutoka katika chumba kimoja hadi kingine. Kila mmoja alikuwa makini, walimtafuta katika kila vyumba, bafu na vyoo lakini Benedict hakuwepo huko hali iliyoonekana kuwachanganya.
“Vipi?” Mzee Matemba aliwauliza.
“Hayupo” Moody alijibu.
Wapelelezi hawakutaka kubaki mahal hapo, walichokifanya ni kuanza kutoka nje. Wakaangalia saa zao, ilikuwa imekwishaingia saa moja na dakika kumi usiku huku sauti ya muziki ikisikika kutoka katika ukumbi ambao ulikuwa jirani na hoteli ile. Wakaingia katika gari lao lakini hata kabla hawajaondoka, Martin akateremka hali iliyowafanya Moody na Sabrina kushtuka.
“Nina machale. Nisubirini” Martin aliwaambia.
Martin akaanza kupiga hatua za haraka haraka kumfuata mlinzi, alipomfikia, akaanza kuongea nae maongezi ambayo yalichukua dakika moja tu. Hapo hapo Martin akaanza kupiga hatua kuelekea nyuma ya hoteli ile huku akiongozana na mlinzi yule. Walipofika nyuma ya hoteli ile, Martin akauparamia ukuta.
“Huku kuna nini?”
“Ukumbi wa starehe. Kuna bendi ya Twanga Pepeta itapiga hapo usiku wa leo baadae” Mlinzi alijibu.
Martin akaendelea kuchungulia zaidi na zaidi ndani ya ukumbi ule. Baadhi ya watu wachache walikuwa wametulia vitini huku wengine wakilishughulikia jukwaa ambalo lilitarajiwa kutumika katika usiku huo. Macho ya Martin yakaendelea zaidi na zaidi kuchungulia. Mara moyo wake ukamlipuka kupita kawaida mara alipomuona mtu ambaye alikuwa na uhakika kwamba alikuwa Benedict japokuwa alikuwa amevalia kofia kubwa.
“Benedict….Benedict…” Martin alikuwa akijisemea huku macho yake yakimwangalia mwanaume yule ambaye aligeuka nyuma na kuyafanya macho yao kugongana.
“Ndiye yeye. Ndiye yeye” Martin alisema kwa mshtuko huku akionekana kutokuamini.
Mara baada ya Benedict kuuparamia ukuta ule akafanikiwa kuingia katika eneo la hoteli ya Casanova. Benedict akaanza kupiga hatua kuelekea katika upande uliokuwa na geti la kutokea hotelini pale. Hata kabla hajafika, akapigwa na mshtuko mara baada ya kuliona gari moja likiingia ndani ya hoteli ile jambo ambalo likaonekana kumtia wasiwasi.
Akajificha, vijana watatu wakateremka na kuanza kuongea na mlinzi. Tayari Benedict alikuwa ameshikwa na wasiwasi zaidi, alichokifanya ni kuyapeleka macho yake katika ukuta ambao ulikuwa umetenganisha ukumbi mmoja wa muziki na hoteli ile na kisha kuuparamia.
Akayapeleka macho yake upande wa pili, akawaona watu zaidi ya ishirini wakiwa wamekaa katika viti ukumbini pale huku wakiwa wamempa mgongo na wengine wakiandaa jukwaa. Benedict hakuonekana kujali uwepo wa seng’enge zilizokuwa na ncha kali, akajipenyeza na kisha kushukia upande wa pili huku mwili wake ukiwa umetobolewa na seng’enge zile.
Benedict akaanza kupiga hatua kukifuata kiti kimoja kilichokuwa mahali pale ndani ya ukumbi ule na kisha kutulia huku kofia yake aina ya Malboro ikiwa vizuri kichwani mwake. Benedict hakutaka kuondoka mahali pale kwani kulionekana kuwa na ulinzi mkubwa kwake, Muda uliendelea kusonga mbele, mara baada ya nusu saa kupita, akayageuza macho yake na kuangalia pale ukutani aliporukia.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Benedict akapigwa na mshtuko mara baada ya macho yake kugongana na macho ya mtu ambaye alionekana kumtilia mashaka. Walahazikupita hata sekunde tano, yule mtu akaacha kuchungulia. Wasiwasi ukaanza kumshika Benedict. Akajiona kuwa karibu kukamatwa.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment