Search This Blog

Friday, July 15, 2022

ULIKUWA WAPI - 5

 







    Simulizi : Ulikuwa Wapi

    Sehemu Ya Tano (5)



    Muda umeshapita tangu tuanze biashara na Jones, na kwangu umekuwa uzoefu ulionipatia changamoto kadhaa lakini wenye mafanikio makubwa sana kiuchumi na katika taaluma yangu ya biashara. Nisingependa kuzungumzia sana upande huo, lakini kwa kutoa picha ya haraka tu, mwaka jana tumezawadiwa kati ya wawekezaji hamsini bora wa nchini Tanzania, na katika masuala ya kompyuta na teknolojia ya mawasiliano, tumeshika nafasi ya pili. Tumesambaa nchi nzima, na Afrika Mashariki, na kwa sasa tunataraji kupanua mipaka yetu nje ya Afrika Mashariki. Tuna waajiriwa zaidi ya 200, asilimia 95 ikiwa nii watanzania, jambo ambalo linanifanya nijivunie sana kwa kuwapa fursa watanzania wenzangu wengi. Maisha yangu kwa sasa ni mapya kabisa, na ukilinganisha hali ya uchumi ya kaka Bahati kwa sasa, na kabla hajaugua, ni kama mara tano au zaidi. Kila nikitafakari nasema kweli Mungu hafanyi makosa. Miaka yote tuliyoteseka, kaka Bahati kuugua sana na kupotelewa mali, imepita kama maji, na sasa imebaki historia tu isiyo na maumivu yoyote tuikumbukapo.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mara ya kwanza kwenda Afrika Kusini nilienda kibiashara. Wenzetu wameendelea kidogo zaidi ya nchi nyingi za Afrika, na hata kiteknolojia wako mbele kwa kiasi kikubwa zaidi yetu. Jones alinialika katika mafunzo fulani kwa ajili ya kupanua ufahamu wangu kibiashara hasa katika masuala ya teknolojia, na baada ya hapo nimeshahudhuria mafunzo kadhaa ya namna hiyo kwa nchi za Afrika Kusini, Canada na Ujerumani. Tumekuwa na mazoea sana mimi na Jones, lakini haijawahi kuwa nje ya biashara, mpaka mwaka juzi ambapo alinialika kwa mwaliko binafsi nchini Canada, nyumbani kwake. Siku moja tukiwa tunaongea kwa skype, nilihisi mazungumzo yamebadilika kidogo, na kuwa zaidi ya vile nilivyozoea, akaanza kuniuliza maswali kadhaa kuhusu mambo binafsi, na akazungumza na mimi kwa utani mwingi. Namfahamu kama mtu mchangamfu na mwenye utani kiasi, ambaye mara zote hapendi kuweka akilini jambo linalompa msongo wa mawazo, lakini kwa kiasi kikubwa uhusiano wetu umekuwa wa kibiashara zaidi, hata kama kuna utani na ucheshi basi ni kwa kiasi na zaidi kuhusiana na kazi. Hakuwahi kuniuliza kuhusiana na undani wa maisha yangu, mpaka siku hiyo tukizungumza mida ya usiku wa saa nne au tano hivi. Kwanza ilinishangaza kupiga simu muda ukiwa umesogea tofauti na muda ambao huwa anapiga, kwani mara nyingi huwa hapigi simu baada ya saa nne usiku. Tulipoanza kuzungumza siku hiyo nilishangaa zaidi kwamba licha ya kupiga mida hiyo ambayo niliiona kama mida ya dharura, hakuzungumza mambo ya dharura wala hata mambo ya kazi kama nilivyotegemea, badala yake aliongea vitu ambavyo havihusiani na kazi kwa muda mrefu tu.



    “Nataka nikualike makazi yangu ya Canada, uone ninapoishi na ufahamiane na familia yangu pia. Kipindi kile umekuja nilitamani ningekuwepo, lakini nadhani huu ni wakati sahihi zaidi.” Aliniuliza, baada ya kuwa tumeongea kama nusu saa hivi; nikabaki kimya kwa muda nikifikiria cha kumjibu. Sikutaka kabisa uhusiano wangu na Jones ubadilike na kuleta maana nyingine yoyote nje ya kazi zetu. Alikuwa rafiki ndiyo, lakini misingi ya urafiki wetu ilikuwa ni biashara iliyotuunganisha. “Naweza kukupa muda wowote ufikiri kama itawezekana au la, ila ukikubali hata kesho nishughulikie tiketi uje, vinginevyo uwe huru sababu hii ni safari binafsi zaidi, na sio ya kibiashara.” Aliongeza kuniambia baada ya kuona nimekaa kimya kwa muda. Nilihisi kumaanisha alichokisema, baada ya kutoa hayo maelezo ya pili, nikamkatiza maongezi nikidai anipe muda nifikiri kidogo kisha ningemjibu kesho yake. Sikutaka tena kuendelea na maongezi naye kwa usiku huo, badala yake nilisingizia usingizi, tukaagana.



    Nilipata mawazo kidogo usiku huo, kutokana na namna maongezi yetu na Jones yalivyokuwa. “Huyu mtu leo amewaza nini kuongea na mimi namna hiyo? Kwanini amenipigia usiku wote huu, bila cha maana cha kuongea kuhusiana na kazi? Nini kinaendelea kichwani mwake, mpaka kunialika kwake, nikutane na familia yake?” Niliwaza na kujiuliza hayo maswali, nikajitahidi kuyapuuza na kusinzia. Nimekuwaa na uzoefu mkubwa na wanaume wengi ambao mara nyingi tumekuwa na ukaribu wa kibiashara na kisha baadaye kunitaka kimapenzi. Akili iliwaza kidogo kuwa huenda na Jones ndicho anachotaka, nikahisi moyo wangu kushuka sana. Haingekuwa kosa kabisa kufanya hivyo, lakini nilihisi italeta doa katika uhusiano wetu. Kwanza sikuwa na wazo wala mpango wa kuwa na mwanaume mzungu katika maisha yangu, sio tu kuolewa naye, bali hata kuwa na mahusiano naye ya muda mfupi ya kimapenzi. Kama unakumbuka niliwahi kupewa kisa cha ndoa ya binti wa mzee Magessa, na vituko vya mume wake mzungu. Lakini pia nimekuwa na mtazamo mbovu sana kuhusu hawa watu, kutokana na baadhi ya mambo au vijitabia nilivyowahi kusikia na hata kushuhudia. Sikutamani kuwa na ndoa ambayo haina uhakika wa umilele, ndoa ambayo nitahofia kuna siku mtu anaweza akahisi tabia yangu fulani haiwezi, akaamua tuachane. Na hata akilini mwangu, sikuwahi kuvutiwa na muonekano wowote wa ngozi nyeupe, yaani wazungu. Niliwaza endapo Jones atanitaka kimapenzi na nikamkatalia, hatutaendelea kuwa na urafiki tuliokuwa nao awali.



    Siku kadhaa zilipita, tukiendelea na mawasiliano ya kibiashara bila kumpa jibu kama nilivyoahidi, lakini niligundua Jones amekuwa rafiki zaidi kwangu na uchangamfu wake umeongezeka. Baada ya wiki na siku chache, nilianza kuzoea simu zake za kila siku, jambo ambalo awali halikuwa hivyo. Nilijaribu kutotia akilini, na pia kujisahaulisha kuhusu mualiko wake wa kwenda Canada, mpaka siku aliyoniuliza, nikamjibu kirahisi tu kuwa bado nafikiria. Kesho yake tukiwa tunakula chakula cha jioni na kaka Bahati mezani, nilishangaa kaka akiniuliza, “Wazo la Jones kukualika Canada unalichukuliaje?” Kidogo nipaliwe na chakula kilichokuwa mdomoni, kwani sikutegemea kuwa angeongea chochote kwa kaka kuhusiana na mualiko wake. “Sijui kwakweli, sidhani kama niko tayari kukubali ila pia sitaki kuwa hasi sana. Nahisi kuna kitu anataka, labda kuanzisha mahusiano ya kimapenzi, jambo ambalo kwa kiasi kikubwa linanipa mawazo sana. Sioni kama hiyo safari itakuwa na tija sana kwangu zaidi ya kuharibu kabisa mahusiano mazuri kati yetu. We unaonaje?” Nilimjibu kaka na kutaka kujua mtazamo wake, nikijua huyu ni mtu mwenye nia njema zaidi na mimi kuliko mtu yeyote pengine, na zaidi ya kuwa kaka kwangu alikuwa rafiki na mshauri. Labda hapo nilikuwa tayari kuamua kulingana na maamuzi ya kaka Bahati kuhusiana na safari hiyo.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

     “Ni kweli, huenda akawa na wazo la kukutaka kwa mahusiano ya mapenzi, lakini huenda siyo. Huhitaji kuchukulia kwamba safari yako ndiyo itasababisha apate fursa ya kutaka uhusiano na wewe, au ukikataa kwenda utaondoa wazo hilo kichwani mwake kama lipo, unachotakiwa kufanya ni kuamua wewe binafsi, bila msukumo wa sababu yoyote ya nje. Mimi nachukulia hivi, pengine kwa muda ambao mmefahamiana kama wafanyabiashara wenza, Jones anataka mpige hatua zaidi, na kujenga urafiki zaidi kati yenu. Nadhani marafiki waliokomaa kiakili, huweza kufanya kazi vizuri zaidi. Haina haja ya kukwepa ukaribu naye zaidi, kwani hiyo haitasababisha kumbadili nia endapo moyo wake umekupenda. Kuwa chanya, na kama nafsi yako ikikuruhusu, kubali mualiko, huku ukiiaminisha akili yako kwamba mnautoa uhusiano wenu katika hatua ya wafanyabiashara wenza kwenda hatua ya marafiki wa karibu, na sio zaidi, mengine yakitokea, utajua namna sahihi ya kukabiliana nayo.”



    Hapo sikuwa na la kuongeza, kwani alichosema ni kweli kabisa. Niligundua nimekuwa muoga sana kuruhusu ukaribu na mwanaume yeyote, na hiyo imenifanya hata kuwafikiria vibaya vijana ambao pengine walikuwa na nia njema kabisa ya kujenga urafiki na mimi. Niliwaza usiku huo, kesho yake nikaamka na jibu la kukubali mualiko wa Jones.



    “Nadhani ni sawa, nitakuja, subiri nipange ratiba zangu vizuri,” Nilimjibu Jones tukiongea kwenye simu siku iliyofuata. “Hapana, siamini unachokisema, tafadhali usiseme unanitania,” Aliongea kwa msisimko sana kiasi cha kunifanya nihisi kama namuona. Ni kama hakuwa anategemea hilo jibu kabisa. Nilifanya maandalizi na kuweka mambo ya ofisini sawa, nikasafiri. Nchi ya Canada ni nzuri, yenye hali ya hewa ya baridi kali kwa baadhi ya majira ya mwaka, yenye wa-Afrika wachache sana. Mara ya kwanza kufika, sikuweza kuzunguka maeneo mbalimbali kwani sikuwa na mwenyeji maalumu na muda wa kutosha, lakini safari hii, nilijihisi nimeenda mapumziko haswa. Jones alinitembeza kwenye hifadhi za taifa, na maeneo mengi maarufu nchini Canada kama mto Niagara, mnara wa Toronto na maeneo mengi mno mazuri. Kuna sehemu tulitembelea zenye michezo namna ya ile ya Fun city ya jijini Dar es Salaam, lakini yenyewe mikubwa mno na iliyoendelea. Yaani ukubwa wa eneo ni kama unaingia kwenye kijiji, na kuna michezo ya kila aina ya kufurahisha, ya kusisimua na ya kuogopesha. Alinipeleka kwa wazazi wake siku tatu baada ya kufika, wakanifurahia sana, tofauti na nilivyotegemea kwani nilihisi wangeweza kuwa na ubaguzi wa rangi. Nilikaa Canada kwa wiki mbili, ambazo naweza kusema katika maisha yangu haikuwahi kutokea kuwa na wakati wa kufurahi na kupumzika kama huo kuwahi kutokea kabla. Mbali na hisia zangu za awali, Jones alinijali kama rafiki wa karibu anayemthamini na si vinginevyo. Lakini pia kipindi chote hicho ni kama tulikuwa mbali kabisa na masuala ya kazi, au kama sote tulikuwa likizo. Akili zetu tulizisahaulisha mambo ya biashara yetu kwa muda, ikawa ni wakati wa mapumziko ya kimwili na kiakili.



    Siku moja kabla ya safari ya kurudi Tanzania, tukiwa mgahawa mmoja mzuri sana mida ya jioni, baada ya kutoka kuwaaga wazazi na familia yake, Jones aliniambia maneno kadhaa ambayo kiukweli yalinitia moyo sana. “Nia ya kukutaka uje kunitembelea ni kukufanya upumzike na kazi nyingi ambazo umekuwa ukifanya. Nilitamani kipindi hiki usahau kabisa masuala ya kazi, uone kuna maisha mazuri nje ya majukumu yako ya kila siku na ufurahie mambo kadhaa ya kuvutia ya nchi yetu. Lakini pia nilitaka kutumia fursa hii kukushukuru kwa uchapakazi, uhodari na kila jitihada unayoionesha katika kazi. Wewe ni kati ya mabinti wachapakazi sana, na najivunia kuwa na wewe kama mwenza katika biashara. Kufanya kazi na ninyi kumenifanya kupiga hatua kubwa mno ndani ya muda mfupi, na ingawa nilishawahi kujaribu kufanya biashara na muafrika, ikashindwa kwa sababu ya uzembe wake, ninyi mmenipa sababu tena ya kujenga imani na waafrika.” Nilijua alimaanisha alichokisema, ingawa mwanzo sikuwa najua kuwa ndivyo ananichukulia. Nilijisikia vizuri kuona kuwa jitihada ninazoweka, zinaonekana, na zaidi zimejenga imani sio tu juu yangu bali hata kwa watanzania wenzangu.



    Nilinunua zawadi kadhaa za kaka, na watu wengine kama wafanyakazi wetu, zawadi kama chokoleti, mapambo madogo madogo, na mashati na manukato ya kaka Bahati, pamoja na vitu vingine nilivyohitaji kununua. Mimi hutumia fursa za kusafiri nje ya nchi kununua vitu kama manukato, baadhi ya nguo au mikoba, na hata vitu vidogo kama chokoleti, ambavyo kwa ndani ya nchi vingepatikana kwa bei ghali, lakini kwa wenzetu huuzwa kwa bei nafuu na ubora pia mara nyingi huwa juu zaidi. Baada ya kurudi nchini, nilipumzika kwa siku mbili, nikaanza kwenda kazini. Siku ile nimerudi, usiku tulikaa nje na kaka nikaanza kumuhadithia mambo mengi kuhusu safari yangu, ila nikiendelea na masimulizi yangu, kuna wakati ni kama kaka alinikatiza, na kuniuliza, “Unamfahamu Nuru wa benki ya BOA?” “Ndio namfahamu, si nilishawahi kukwambia kuna dada mmoja mchangamfu na ana huduma nzuri sana kwa wateja, huwa nampenda, kwani ana nini.” Nilimjibu, nikamtaka anieleze kama huenda kuna kilichompata. “Hajapatwa na kitu, nilitaka tu kujua kama unamfahamu, kumbe ndio huyo.” Siku zote mimi ndiye hupeleka pesa benki au kutoa, au meneja wa fedha, na sio kaka Bahati, ingawa naye ni kati ya wasainiji wa kampuni. Kipindi nimesafiri, kaka alilazimika kwenda mwenyewe benki mara mbili, meneja akiwa anaumwa. BOA ni kati ya benki tunazotumia, ambayo kaka Bahati hana akaunti yake binafsi huko, hivyo nadhani hakuwahi kwenda kabla. Aliponiuliza kuhusu Nuru, nilihisi kuna kitu, lakini nikaona hakutaka kuniambia, nikaamua kupotezea. Siku niliyoenda ofisini, nilitakiwa kwenda benki asubuhi, kaka akijua kuwa siku hiyo nitaenda benki, akanipigia simu mapema nikiwa ofisini, “Fanya juu chini uchukue namba ya Nuru wa BOA.” Nilicheka, nikamtania kuwa huyo Nuru lazima kuna kitu, akanibishia, akidai kuna vitu anataka kumuuliza.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wiki kama mbili baada ya kumpa namba ya Nuru, nilianza kuhisi kaka amekuwa na hekaheka fulani ambazo sikuzizoea. Alianza kuwa anatoka mara kwa mara jioni, au chakula cha mchana haendi kula mgahawa wa jirani ambao nilizoea ndio huenda mara zote, badala yake akawa akienda mbali kidogo na akichukulia kana kwamba ni maalumu sana. Kuna mara nyingi ambazo awali kaka hakutoka kwa chakula cha mchana na badala yake kuomba aletewe chakula, lakini sasa kila siku alienda nje ya ofisi kwa ajili ya chakula cha mchana. Jioni alianza kuchelewa kurudi nyumbani kidogo, na kuonekana akiwa mtu bize kiasi na simu yake. Niligundua kuwa kuna mtu ameanza kuchukua nafasi tena kwenye maisha ya kaka Bahati, nikapata hisia mchanganyiko ndani yangu. Kwanza nilifarijika kuwa hatimaye anaanza kupenda tena, lakini pia niliogopa sana, nikihofia endapo huyo mwanamke hatakuwa mwema kwake, atamtenda kama alivyomtenda Ketty. Nikiwa katika mawazo hayo, siku moja kaka alianza mwenyewe kuniambia kuhusiana na huyo mtu niliyemuhisi ni Nuru, “Nadhani Nuru anafaa kuwa mke Zawadi, kama akinipa nafasi.”



    Nilikuwa nikitegemea ataniambia, kwani mimi na kaka tu huru sana kwa kila kitu, lakini hata hivyo niliona kama ni mapema sana kwake kuamua kuwa anaweza kuwa mke. Sikutaka kumkatisha tamaa au kumuonesha kwamba nimestuka, ila sikusema neno, zaidi ya kuendelea tu kumsikiliza. “Najua unashangaa kwamba ndio kwanza nimeanza kuwasiliana naye, hata miezi mitatu haijaisha, lakini kuna vitu vya msingi sana nimeangalia. Nuru amenipa nafasi ya kuwa karibu naye kama rafiki, na bado sijamwambia kama nampenda, wala sijamwambia mambo mengi kuhusu mimi, ila kwa muda huu mfupi nimeona tabia kadhaa ndani yake ambazo zimenifanya nihisi ni mwanamke anayefaa. Kwanza ni mkarimu mno, na ana huruma sana. Ila pia ni muwazi na yuko huru sana, kiasi cha kunifanya nijisikie huru kwake. Ameniambia ukweli fulani kuhusu maisha yake, kwamba ana mtoto, lakini baba wa mtoto alimkimbia siku ya mahari, akamuacha na mimba. Yeye ni mtu ambaye haoni haya kuzungumzia makosa aliyowahi kuyafanya kabla, na ni muwazi sana. Ninachohisi, ana imani ndogo sana na wanaume, kiasi kwamba hata maongezi yake, yananifanya nipate hofu kama anaweza kuniamini endapo nitamwambia nampenda na nataka awe mke wangu. Pia inaonekana mimi si mtu pekee ninayetaka mahusiano naye, kwani kuna mara mbili amekuwa akitoka jioni na mwanaume mwingine aliyedai ni rafiki tu kama mimi. Sijui kwanini, ila kwa muda mfupi niliomfahamu, nahisi moyo wangu umetokea kumuamini kuliko mwanamke mwingine yeyote kabla.”



    Ni kweli, mambo aliyoongea kaka yalionekana ya msingi kwa mwanamke sahihi wa kumuoa, lakini bado nilipata hofu sana. Nilimshauri tu aendelee kumchunguza kabla hajamwambia kuwa anampenda kwani wengine huweza kuonekana tofauti na walivyo. Ni kama kaka hakufurahia sana mpokeo wangu wa habari ya Nuru, pengine alitegemea ningefurahia sana au kumtia moyo. Hiyo ilifanya maongezi yetu kama yakatizwe na kutokuwa na mwisho mzuri sana siku hiyo. Nilihisi vibaya sana, kwani hali kama hiyo haikuwahi kutokea kabla. Niliwaza kuwa ni kama amekuja kumpa habari njema rafiki yake halafu rafiki huyo hakuifurahia, badala yake amempa angalizo tu. Usiku huo nilitumia muda mwingi sana kufikiria juu ya Nuru, na kila kitu kaka alichosema, na hofu niliyokuwa nayo juu ya kaka kuanzisha mahusiano mapya. Kesho yake, niliona kaka si mchangamfu kama ambavyo huwa, lakini nami pia sikuwa mchangamfu, na nilikuwa mchovu kwa ajili ya kulala saa chache. Baadaye ni kama sote wawili tulipotezea lile jambo, mambo mengine yakaendelea, lakini nikaona kama kaka amepunguza kidogo kuwa bize na Nuru au na zile ratiba alizokuwa ameanza. Akilini mwangu vitu viwili vilipingana, kwamba Je niko sahihi kutoshabikia wazo lake la kuanzisha mahusiano kwa haraka, au nimemvunja moyo na pengine kumfanya apoteze mwanamke wa maisha yake?



    Siku moja nilienda benki, nikahudumiwa na Nuru, ambaye pia hakuonekana mchangamfu kama nilivyokuwa nimemzoea. Baada ya kunihudumia nilimuuliza kwanini leo haonekani na uchangamfu wake, akadai yuko sawa, lakini akaniomba kama nitakuwa na nafasi tuonane siku hiyo jioni. Nilikuwa na uhakika kuwa Nuru hajui uhusiano wetu na kaka Bahati, nikastuka kidogo aliponiomba tuonane, kwani nilihisi huenda kaka amemwambia kuhusu mimi, jambo ambalo sikutamani iwe kweli. Tulionana siku hiyo, nikiwa na shauku na hofu pia, kutaka kujua nini anataka kuzungumza na mimi. “Kuna kaka mnafanya naye kazi Zawadi, anaitwa Bahati, nadhani unamfahamu,” aliniuliza, nikamkubalia huku nikipumua kwa kupata uhakika kuwa hakuwa anajua kwamba ni kaka yangu. “Unamfahamu kwa ukaribu?” Aliuliza tena, nikajifanya namfahamu tu kama mfanyakazi wa kampuni yetu na sio zaidi. “Nimehisi wewe ni mtu sahihi wa kuongea naye, japo sijakuzoea sana, lakini nimefikiria nikaona unaonekana muelewa, nikaamua tuongee tu. Kwa sasa mimi sina mahusiano yoyote, ingawa kuna wanaume wawili ni kama wako kwenye mzani wangu, mmoja akiwa huyo kaka mnayefanya naye kazi. Lakini nyuma nimewahi kuwa na mahusiano kadhaa, na uhusiano wangu wa mwisho ndio ulinifanya niogope sana wanaume. Kuna mwanaume nilimpenda sana, tukakaa katika uhusiano kwa miaka mitano, kwani alikwenda kusoma nje ya nchi akaniacha huku kwa miaka miwili, tukiwa kwenye uhusiano mzuri kabisa. Akiwa nje tuliwasiliana na upendo kati yetu haukupungua. Baada ya kurudi alipata changamoto ya kupata kazi kwa miezi sita, hivyo kuchelewesha taratibu nyingine. Baada ya kupata kazi, tuliendelea kuwa kwenye uhusiano kwa mwaka mmoja, tukianza kupanga mipango ya harusi yetu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Huyo mwanaume alinizidi miaka mitano, hivyo akili yake niliamini imekomaa kiasi, na ndivyo alivyokuwa. Alionesha kunielewa na kunipenda sana, yaani sikuwahi kumtoa kasoro, na ni mtu aliyenifanya nisahau mara kadhaa nilizoumizwa na mapenzi. Nyumbani kwao walinifahamu na yeye alifahamika kwetu. Tulifanya utambulisho rasmi, akaleta barua ya posa, kukawa na kisherehe kidogo cha familia nyumbani. Miezi miwili badae tulipanga alete mahari, wakaja nyumbani, wakapangiwa mahari na siku ya kuleta. Nakumbuka siku ya mahari, asubuhi niliamka nampigia simu, akapokea akionekana yuko sehemu yenye kelele, nikashangaa kidogo, akadai anashughulikia vitu vya mahari. Tuliongea kwa muda mfupi, akaniaga akisema hanisikii vizuri, na baada ya hapo sikumpata tena. Muda ulifika ambao walitakiwa wawe wamefika au walau wawe njiani kuja, lakini hakuwa anapatikana. Nilianza kupata wasiwasi, muda ukizidi kusogea, saa moja ikapita, masaa mawili hadi matatu. Nilishikwa na tumbo la kuhara, nikaenda uani, nikajikuta badala ya kuharisha, natapika. Nilitapika sana, kuliko nilivyowahi kutapika wakati mwingine kabla. Alipigiwa mshenga hakupokea simu, wala mtu yeyote wa nyumbani kwao. Nikiwa nimechanganyikiwa, ndugu waliokusanyika wameshaondoka, mida ya saa sita usiku, niko tu kitandani nalia huku mama yangu akinibembeleza, ujumbe mfupi wa simu uliingia wa huyo mwanaume. “Nisamehe kwa nilichokutenda Nuru, ila nilikutana na mwanamke wa maisha yangu nikiwa masomoni, na muda huu wote nilijaribu kutafuta namna ya kukuacha nikashindwa. Nimeona nisijiingize kwenye kifungo cha kukulipia mahari ilhali najua sitakuoa, kwani ukweli ni kwamba mapenzi na wewe sina tena.”



    Sijui kama unaweza kuelewa ule mkuki uliochoma moyoni nikisoma huo ujumbe Zawadi. Nilijikuta nimelia kwa sauti, mama yangu akiwa na mimi, ikabidi anizibe mdomo sauti isisikiwe na wengine nje ya chumba. Niliumia mno, sikuwahi kuumia hivyo kabla na hata baada. Nimeishi na maumivu hayo, nikaja kujigundua ni mjamzito, nikaamua akilini mwangu kwamba mtoto wangu ndiye atakuwa faraja yangu na hivyo sitaolewa kamwe. Sikuwa tayari kuamini mwanaume mwingine kamwe kwenye maisha yangu, na mpaka sasa hajatokea mwanaume ambaye nimekubali kumuamini, kwani nafsi inagoma kabisa.



    Kilichonifanya nitake kuongea nawewe leo ni kuhusiana na Bahati. Amekuwa akijenga ukaribu na mimi, na kama mwanamke, nimeshajua nia yake kuwa ananipenda. Sikuwaza kama ananivutia, yeye na huyo mwanaume mwingine anayenifuatilia, nilikuwa nikiwachukulia sawa kabisa. Lakini siku chache zilizopita nimeanza kuona kama Bahati anarudi nyuma kidogo. Nahisi ananipenda, tena sana, lakini nimeshindwa kuelewa nini kinamtia hofu. Kurudi kwake nyuma kumenifanya nigundue kuwa moyoni mwangu alishaanza kupata nafasi, na sivyo kama nilivyokuwa nikimdhania awali. Hapa sijielewi, sijui kama ni mwanaume sahihi au la, ila ndani ya nafsi yangu naona kama huenda akawa mtu sahihi kwangu. Naogopa, sijielewi, siju kama niko tayari kupenda tena, ila pia nahisi sitaki kumpoteza huyo kaka. Labda kama unamfahamu kiundani, unieleze kama ni kweli anaweza akawa ananifaa, ukizingatia historia niliyokupa kuhusiana na maisha yangu ya mahusiano.”



    Nilijikuta nimekuwa mpole na mdogo kama piritoni, nikimsikiliza Nuru. Nilihisi kama Mungu ameamua kunionesha kuwa huyu ni mwanamke sahihi kwa kaka yangu, na mimi ndiye natakiwa kuwaunganisha tena. Niliona aibu kwa kuwa chanzo cha kaka kuogopa kuanzisha uhusiano na Nuru, lakini nilifurahi kuwa nitakuwa na amani kwamba kwa kiasi kikubwa nimemfahamu huyo mwanamke ambaye ataanzisha uhusiano na kaka yangu. Nuru alijiweka wazi kwangu bila kujua kwa kiasi nina nafasi ya kuamua kuhusu hatima ya mahusiano yao na huyo Bahati, ambaye hakujua kuwa ni kaka yangu. Inaonesha kaka hakuwa amemwambia kiundani kuhusu mahusiano yake yaliyopita, ila ilinifariji kwamba nafsini Nuru alikuwa na imani isiyo na sababu kwa kaka. Niliamini kila alichosema kwani hakuzungumza namimi kama mtu ambaye anaweza kuwa na mchango wowote kati yake na Bahati, zaidi tu ya kunitaka ushauri. Sikutaka kumueleza Nuru ukweli kuhusu mimi na kaka Bahati hata baada ya maelezo yake marefu, badala yake nilimshauri tu kama msichana mwenzie, au kama rafiki na mtu ninayemfahamu Bahati, nikampa sifa nzuri kumuhusu kaka kiasi ili asistukie kama ni mtu wangu wa karibu.



    “Nadhani nina habari njema leo, inaweza kuwa habari nzuri ya kukupa usiku mzuri leo,” nilimwambia kaka mara tu nilipoonana naye, kabla hata ya salamu. “Unajua kwa sasa habari njema zinahusu sana, nimekuwa na mambo mengi yananisumbua kichwani, hivyo nahisi kusikia jambo zuri kutanipunguzia mawazo. Vipi, umetoka kuonana na mteja usiku huu nini?” Alijibu akitegemea habari hiyo itakuwa inahusu biashara. “Hapana, nimetoka kuonana na Nuru. Huenda hiyo ikawa habari njema kuliko kuonana na mteja.” Kaka hakuamini kama nilimaanisha ninachosema, alikaa kwenye kochi, akajibu kwa mshangao, “Unasema? Anasemaje? Imekuwaje?” Nilianza kumuelezea kila kitu kama tulivyozungumza na Nuru, maisha ya Nuru kwa undani na kwanini aliamua kuongea na mimi. Naweza kusema ni kiasi gani nilihisi furaha aliyoihisi kaka Bahati baada ya kusikia habari za Nuru kutoka kwangu. Hakusema maneno mengi, zaidi ya kusema tu, “Umenipa habari njema kweli mdogo wangu. Hii ni fursa ya kipekee kwangu. Yaani nakuhakikishia, ndani ya miezi miwili, nitamleta hapa wifi yako.”



    Miezi miwili au mitatu badae, kaka na Nuru walianza mahusiano, kaka kama alivyoahidi, akamleta Nuru nyumbani. Wakati huo wote hatukumjulisha Nuru kama sisi ni ndugu, japo nilishawahi kuonana naye mara nyingine tena, tukazungumza, na hata alipomkubali kaka alinijulisha. Siku aliyofahamu ukweli ni siku aliyoalikwa nyumbani, akatukasirikia kidogo, lakini nikajitetea kuwa sikutaka kwa namna yoyote nisimame kati yao wawili, au nipunguze uhuru wa yeye kuniambia kuhusiana na hisia zake kwa kaka. “Unajua kama ungejua mapema kuwa mimi ni wifi yako, kuna vitu nisingevijua, na ingepunguza uhuru uliokuwa nao kwangu. Hata hivyo huoni kwamba ni vyema, unagundua mimi ni wifi yako wakati tayari tu marafiki?” Kwa wakati huo alikuwa tayari amekuwa rafiki kwangu, kwani tulizoeana kwa kiasi kikubwa na tulizungumza mambo kadhaa. Kaka na Nuru walikaa kwenye mahusiano kwa muda wa mwaka mmoja tu na kisha wakaoana. Ni kweli Nuru amekuwa rafiki yangu na ninampenda, lakini simsifii, ni mwanamke mwenye tabia za kipekee, mwenye mapenzi ya dhati sana kwa kaka yangu. Ana moyo wa huruma, dhamira safi na ni mchangamfu, asiye na hasira za haraka. Kwa sasa wanaishi pamoja na mtoto wa Nuru, ambaye kaka ameshughulikia taratibu za kisheria kumfanya awe mwanae, na anampenda kama mwanae wa kumzaa. Nuru amenifanya niwe na amani kuwa kaka yuko kwenye mikono salama, na ingawa si muda mrefu sana nimemfahamu, lakini nina amani zote kuwa ni mtu sahihi kabisa kwa kaka Bahati.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kuna vitu katika maisha hutokea ambavyo hukuwahi kuvitegemea, kiasi kwamba unaweza ukadhani unaota. Nimeanza kuandika simulizi hili la maisha yangu baada ya kukutana na baba yangu mdogo Musa kwa mara ya kwanza tangu nitoroke nyumbani. Kipindi fulani tukiwa nchini na Jones, tulisafiri kwenda kuzungukia baadhi ya mbuga za wanyama nchini, tukaenda ngorongoro na mikumi. Siku moja tukiwa Ngorongoro, kwenye hoteli moja ya kitalii maeneo ya huko, nilipiga simu kuomba mtu aje anisaidie mizigo ili tuondoke. Nikasikia mlango ukigongwa, nikafungua na kumuona mzee amesimama, akanisalimu, nikamjibu na kumuamkia. Nikamtazama tena na kugundua ni mtu tunayefahamiana naye, lakini yeye hakunitambua. Ni mtu mzima kiasi, na amechakaa sana. Namuuliza kwa mshangao, “Baba mdogo Musa, nini kimekutokea?” Anavuta kumbukumbu na kunitambua, kisha anaanza kulia. Anapiga magoti mbele yangu na kushika mikono yangu. Anaomba msamaha kwa uchungu na machozi, akiniita ‘mwanangu, binti yangu.’ Namtazama kwa muda, nisijue kabisa nini cha kufanya. Natamani nimfukuze, au nisimjibu kitu, au nianze kumsema sana. Nafsi yangu inakataa kupokea msamaha wake, hivyo najikuta naanza kulia. Nimekumbuka nyuma sana ghafla, kiasi cha kutamani nisingeonana naye kabisa. Nakumbuka maumivu yote aliyowahi kunisababishia, lakini naumia sana nikimkumbuka mama yangu aliyenifia mkononi.



    Najikuta namjibu neno moja tu, “Laiti ungekuwepo na kujali, mama yangu asingekufa.” Sina tena cha kusema, bali narudi chumbani nikiwa nalia. Jones ambaye ni mume wangu kwa sasa ananiuliza nini kinaniliza, na ninaposhindwa kumuelezea, anatoka nje kuangalia ni nani nilikuwa naye. Anaona sura asiyoifahamu ya mtu mzima akiwa amepiga magoti na kulia mbele ya mlango. Anachanganyikiwa na kurudi tena ndani, ili anibembeleze. Kipindi hicho nilikuwa mjamzito, na kwa kiasi mimba ilinisumbua. Nilitamani sana mama angekuwa hai, anishauri na anielezee kuwa hiki na hiki ni kawaida na kitapita. Mume wangu ni mtu anayejali kupita maelezo, mwenye upendo mwingi mno kwangu, lakini bado nahisi nafasi ya mama yangu kukosekana kwenye maisha yangu, hasa kwa wakati huu.



    Nirudi nyuma kidogo, nikuelezee kuhusiana na mahusiano yangu na Jones. Sikuwahi kuwaza wala kuota kuolewa na mzungu, na sikuwa nataka kabisa wala hawakuwahi kunivutia, lakini baada ya kuanza kuwa karibu na Jones hasa baada ya safari yangu ya Canada, najikuta namzoea na anakuwa mwanaume wa pili kuwa rafiki kwangu, ukiacha kaka Bahati. Tunaendelea na uhusiano wa kibiashara, lakini sasa ni kama umepiga hatua nyingine, na naona inaniongezea ufanisi katika biashara, kwani nakuwa huru zaidi kwa Jones na kujifunza vitu vingi zaidi toka kwake. Jones anafungua milango yote ya kunifanya rafiki wa karibu, asiseme lolote kuhusiana na hisia zake kwangu, ambazo siku aliyonitamkia, ndipo niligundua kuwa alikuwa nazo kwa muda mrefu sana. Mimi nilichukulia ni kawaida tu ya wazungu kuonesha kujali sana wanapokuwa na urafiki na mtu, hivyo wala sikumdhani kuwa ana lake. Tulijenga urafiki wetu kwa muda mrefu, nikajikuta nimemzoea sana, tukawa tukitumia muda wetu wa mapumziko kuwa pamoja na kwenda sehemu mbalimbali. Safari za Jones za Tanzania zikaongezeka sana, na ukaribu wetu unaongezeka kiasi cha kunifanya nianze kuona ni mtu wa karibu zaidi ya hata marafiki zangu wa kike. Nilianza kuhisi huenda namzoea kupita kiasi, nikawa nikijiogopea, lakini hakunipa nafasi ya kuwa mbali naye. Alijihusisha na kila kinachonihusu, alipenda kunisikiliza sana na ndani ya muda mfupi alijua mambo karibu yote kuhusiana na maisha yangu.



    Siku niliyomwambia kuwa nilibakwa ndipo kidogo iliingia akilini kuwa huenda Jones akawa na hisia za mapenzi juu yangu. nikiongea naye, alianza kutokwa na machozi, kisha akatania, “Huyu mtu alithubutu kugusa mali yangu bila idhini yako, nikimuona nitamuua.” Tulizoea sana kutaniana na tulikuwa huru, lakini hata siku moja hakuwahi kuongea utani wa namna hiyo. Nilijikuta nimekatiza maongezi na kumtazama kwa kushangaa, lakini kabla sijasema chochote, aliniwahi, “Natania.” Nilipotezea tu, ila nikaweka hilo neno moyoni. Nikaanza kuangalia kila alichokuwa akinifanyia, sasa akili ikaanza kufunguka kuwa huenda huyu mtu ananipenda, ila nikajishawishi siyo na kupuuza.



    Siku aliyonitamkia, sikuweza kukataa kumpa jibu siku hiyo hiyo. Tofauti na nilivyotegemea kwa mzungu, Jones alikataa kabisa kunipa muda wa kufikiri. “Umekuwa na mimi siku zote kama rafiki wa karibu sana na wa pekee wa kiume, najua unanijua vizuri. Akilini unafahamu kama mimi ni mwanaume sahihi kwako au la. Najua una jibu nafsini mwako, na hilo ndilo jibu halisi. Ukienda kufikiri, utakuja na jibu lisilo halisi. Niangalie machoni, useme nini unahisi ndani mwako Zawadi.” Alisema maneno hayo baada ya kujieleza sana kuhusiana na hisia zake juu yangu. Tumewahi kutembelea maeneo kadhaa na Jones, lakini sehemu aliyonipeleka siku hiyo sikuwahi kujua kama kuna sehemu kama hiyo Tanzania. Ni hoteli nzuri yenye mazingira ya kimahaba sana kuliko zote nilizowahi kutembelea kwa hapa nchini kabla. Haiko ufukweni ila imetengenezewa kama kijito kikubwa cha maji, kuna miti mizuri, maji yanayotiririka, mwanga hafifu na mzuri mno kwa mida ya jioni, na muonekano wa kila kitu wa kuvutia ikiwa ni pamoja na viti vilivyotengenezwa kwa ubunifu wa hali ya juu. Nilijikuta nikisema ndio usiku ule ule baada ya Jones kunishawishi sana nimpe jibu. Ni kweli, nafsini hakukuwa na mwanaume mwingine zaidi yake, lakini hata kama ningekuwa na marafiki kadhaa wa karibu wa kiume, bado huyu kijana angekuwa chaguo langu. Jones amenipa mtazamo tofauti kabisa na niliokuwa nao kuhusiana na wazungu, kwani amenifanya nihisi jinsi gani amekuja kwangu kwa umilele. Sitasema mengi kuhusiana na mahusiano yetu, lakini mume wangu ni zaidi ya rafiki wa karibu kwangu, mpenzi wa dhati, asiyechoka kunihudumia, na hunifanya niishi kama malkia.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alipoona nalia, baada ya kurudi tena ndani, akawa akinibembeleza nami kwa ajili ya uchungu ndani yangu, nikiendelea kulia, alikasirika na kutaka kutoka ampige yule mwanaume aliyekuwa mlangoni. Kipindi natoka kufungua mlango, Jones alikuwa anamalizia kuoga, kwani kwa ajili ya hali yangu alikuwa akiniogesha kwanza. Nilipoona akiinuka kwa hasira, ilibidi nijizuie kuendelea kulia, nimkalishe chini na kumwambia kuwa huyo mwanaume ni baba mdogo Musa. Mume wangu ananikumbatia sana na kunituliza, mpaka kuhakikisha uchungu na hasira ndani yangu vimepungua, kisha tunatoka naye nje na kumkuta mzee Musa yuko vile vile utadhani tumemuacha hapo kwa dakika tano au kumi, na kumbe ni karibu saa nzima imeshapita. Nikiwa na ujasiri na nguvu tena, naanza kumuuliza, “Ulikuwa wapi wakati mama yangu anafariki? Ulikuwa wapi nikiomboleza kwa ajili ya baba yangu? ulikuwa wapi nafukuzwa shule kwa ajili ya ada? Ulikuwa wapi nilipoanza kuzurura mtaani? Ulikuwa wapi nauza bikira yangu kwa ajili ya maisha ya mdogo wangu? Ulikuwa wapi miaka yote 22 ya maisha yangu bila wazazi na bila msaada? Nawezaje kuona thamani yako?” Nashindwa kujizuia tena na kuanza kulia, huku Jones akiniweka kifuani pake na kunibembeleza, halafu ananirudisha ndani, kisha kutoka tena nje na kumuomba baba mdogo aondoke, akichukua namba yake ya simu na kumuahidi kumtafuta siku nyingine.



    Kilichotokea siku hiyo kilitufanya tuahirishe kuondoka hotelini hapo siku hiyo, na badala yake kuongeza muda wa kukaa Ngorongoro. Muda huo, mume wangu ilibidi aanze kuzungumza nami kwa taratibu kabisa akinisaidia kusamehe niliyotendewa. Kiukweli, awali nilidhani nimewasamehe wote walionikosea, hasa baada ya kumsamehe Ketty. Sikujua kuwa nafsini mwangu kulikuwa na maumivu yaliyofichika, yaliyosubiri nione walioyasababisha. Jones alijaribu kuongea na mimi, akinikumbusha jinsi nilivyo na moyo mzuri wa huruma na uwezo wangu wa kuachilia. “Zawadi, sina mashaka na uwezo wako wa kusamehe mke wangu, na najua tayari ulishasamehe, lakini bado uchungu haujatoka nafsini mwako.” Alisema hayo mara kadhaa akiwa amenikumbatia, na kunifariji. Maneno yake ya faraja yalianza kufanya uchungu uliokuwa ndani yangu upungue. Nilipokuwa tayari, alimtafuta tena baba yangu mdogo, tukakaa naye sehemu ya hoteli hiyo kwa nje. Siku tumekaa naye, baba mdogo, kwa upole na unyenyekevu mwingi mno, alianza kuzungumza. Vitu alivyosema, nilihisi kama naota au ni vya kutunga, kwani sikuamini kama Mungu anaweza kulipa kisasi kikubwa namna hiyo. Nilidhani ule usemi wa malipo ni hapa hapa duniani ni maneno ya kujifariji tu, lakini kwa kile kilichotokea kwa anti Ketty, na halafu nikashuhudia tena kilichotokea kwa baba mdogo, nilimuogopa Mungu.



    “Zawadi, unastahili kunichukia na kutonisamehe maisha yako yote, kwani mimi ndio chanzo cha mambo yote yaliyotokea na kukuumiza maishani. Lakini naomba nikwambie sababu moja tu kwanini ninastahili msamaha wako, ni kwamba Mungu ameshaniadhibu, adhabu ambazo hata wewe ungepewa nafasi ya Mungu pengine usingenifanyia hivyo, ungenihurumia kidogo. Kwa kifupi, hapa nilipo ndio nafanya kazi, baada ya kuhangaika sana na maisha, na nilipata miaka miwili baada ya kutoka gerezani. Niliishi na mke wangu Selina baada ya nyie kuondoka, bila hofu wala wasiwasi kuwa mtakuwa mmeenda wapi. Niliona mmeamua kunitua mzigo wa kuwalea, na wala sikutaka kuhangaika kuwatafuta, ila kukwepa lawama, nilijaribu kutoa taarifa polisi, nikahonga honga ili wasifuatilie, tukaendelea kutumbua maisha. Miaka miwili baadaye, mdogo wangu Naise, ambaye tangu kipindi kile muondoke hakuwa amerudi nyumbani zaidi tu ya kunipigia simu mara kadhaa akinihakikishia ni mzima, alirudi tena akiwa na muonekano uliobadilika sana. Siku moja tulimuacha nyumbani, na mtoto wetu aliyezaliwa miezi kadhaa baada ya nyie kuondoka, pamoja na msichana wa kazi tuliyekuwa naye, lakini tulirudi na kukuta nyumba imesombwa karibu kila kitu, huku dada amefungwa na mtoto ameachwa peke yake akilia. Tangu siku hiyo sikumuona tena Naise, ila miaka minne baadaye, tulimuona kwenye taarifa ya habari akiwa amekamatwa na polisi kwa ujambazi. Naise alifungwa, lakini tulipata taarifa kuwa imegundulika amewekewa sumu akiwa gerezani na kufa. Sielewi ni uzembe gani ulifanyika, kwani vyakula vya wafungwa huwa vinajaribiwa kabla ya kuliwa. Tulifuatilia, askari kadhaa wakafukuzwa kazi, lakini tayari Naise alishapoteza maisha. Nilisikia ni kati ya majambazi aliokuwa akifanya nao kazi, wenye majina, walimuua ili asiwataje, au kuua ushahidi wake.



    Lakini tuliendelea na maisha, na mke na mtoto wetu mmoja. Mke wangu alikuwa ni mtu wa kupata ujauzito kwa shida, na mimba humsumbua sana. Alipata ujauzito wa pili, akaumwa kuanzia siku ya kwanza mpaka ya mwisho, lakini siku ya kujifungua, alimwaga damu nyingi na kufa, akaniachia watoto wawili, mmoja akiwa na miaka sita na kichanga aliyemuacha wakati wa kujifungua. Nilijikusanya nguvu, nikaanza kulea watoto, nikisaidiwa na msichana wetu, ila badae nilipata mwanamke nikataka kumuoa. Sikujua kuwa yule binti wa kazi alishaweka akilini kuwa huenda nikamuoa yeye, na labda ndio sababu aliwalea watoto kwa mapenzi tele. Alipoona nimeoa mwanamke mwingine, hakuonesha sana chuki na hasira aliyopata, akajaribu kuwa mnafiki, ili afanye alichotaka kufanya. Tukiwa na mwaka mmoja wa ndoa yetu, aliaga na kuondoka, lakini kama miezi miwili baadaye alikuja na kumkuta mke wangu na nadhani alimlangai na kumsaidia kazi. Akawa akifanya hivyo mara kadhaa, yaani akija na kufanya shughuli za nyumbani na kuondoka. Sasa aliichota akili ya mke wangu na kuanza kumwambia mambo ya uwongo. Alidai kuwa mimi nimekuwa nikimtaka kimapenzi tangu mke wangu wa awali bado anaishi, na tulianzisha uhusiano. Alidai nilimuahidi kumuoa na ndio sababu hakuweza kustahimili nilipooa mwanamke mwingine. Binti yule tangu tukiishi naye, ni mtu ambaye ilikuwa ni rahisi sana kujenga imani naye na kumuhurumia. Mke wangu alimpenda sana na hata siku anaondoka alimbembeleza mpaka kulia. Aliiteka akili yake na kufanikiwa kumshawishi kile alichosema ni kweli.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mke wangu alinificha ukweli kuhusiana na yule binti alichokuwa akidai juu yangu kwani alihisi nisingekubali, badala yake walijenga ukaribu naye zaidi. Kwangu alisema tu kuwa fulani huja mara kwa mara kumsaidia kazi. Niliona mke wangu akinibadilikia kwa kiasi kikubwa, ila nilijitahidi kuvumiliana naye. Mke wangu hakujua kuwa huyu binti alikuwa mtoto wa mjini, mjanja na aliyekuwa na mkakati maalumu wa kuniharibia maisha na ndoa. Wakati huo hali yangu ya kiuchumi ilikuwa imeimarika sana kutokana na mali za baba yenu, hivyo nilikuwa tajiri mkubwa na mwenye pesa nyingi sana zisizowiana na kazi yangu.



    Siku moja ya Jumapili, tukiwa mapumziko nyumbani na mke wangu na watoto, nilishangaa kuona polisi wakija na kudai kuwa wanataka wanikague kwani wamegundua kuwa nauza madawa ya kulevya. Niliwajibu kwa kujiamini kuwa sijawahi wala sina mpango, na kuwaruhusu wakague. Tuliingia nao ndani, wakaanza kukagua sana, maeneo yaliyofichika, mimi nikishangaa kwanini wamenihisi hivyo. Baada ya muda walifanikiwa kupata kitu kimefungwa, wakahakikisha ni dawa za kulevya, wakanichukua na kunipeleka kituoni, nikafungwa na baada ya kesi kusikilizwa nilihukumiwa kifungo cha miaka mitano. Nimetoka, nakuta mke wangu ameshaolewa na mwanaume mwingine, ambaye amewamilikisha watoto wangu kisheria. Mke wangu alikuwa anawapenda wanangu kama wake, hivyo hata nilipowataka tena, watoto wenyewe hawakukubali ikabidi niache kwanza kwani pia hali ya maisha haikuwa inaniruhusu. Nimehangaika mtaani baada ya kutoka gerezani, nimepoteza kila kitu, mke, kazi, watoto na hata marafiki. Sikuwa na pesa kabisa, kwani pia kesi ikiendelea nilijaribu kuhonga lakini rushwa yangu ilisaidia tu nisifungwe muda mrefu zaidi. Na pia baada ya kufungwa mke wangu alipata uhalali wa kuchukua kila kitu, kwani ndiye alikuwa mlezi wa wanangu.



    Nilikuja kupata kazi hapa hotelini baada ya kuhangaika sana, na kwa sasa nafanya kama mtu wa usafi na mesenja. Kila nikikumbuka niliyokutenda wewe na mdogo wako Zita, naumia kupita kiasi. Nilimuona Zita kwenye luninga, jinsi alivyokuwa maarufu, nikatamani kurudisha siku nyuma nioneshe upendo kwenu. Mungu ameniadhibu Zawadi mwanangu, kiasi cha kutosha. Naishi maisha ya majuto na ya kimasikini kana kwamba sikuwahi kuwa tajiri. Ukiwa mtu mzima halafu unafanya kazi za vijana, unanyanyasika sana. Ni kama kila mtu anakutegemea ufanye zaidi ya matarajio. Wakubwa zangu kikazi ambao wengi wao nimewazidi umri hunigombeza na kuninyanyasa, na hata wafanyakazi mwenzangu ambao karibu wote pia nimewazidi umri, hunidharau na kunionea bila sababu. Mshahara hautoshi, siwezi kufanya maendeleo yoyote kwani naishia kula tu, na nikijaribu kuomba kuongezewa naambiwa sio lazima niendelee na kazi hapa. Sina tena thamani Zawadi, sina chochote katika maisha haya. Maisha ya gerezani yamenitesa mno, watu hawana huruma wala heshima. Nimefanyiwa vitendo vibaya mara kadhaa, nimefanyishwa kazi nisizostahili na sikuwa tena meneja wa benki kule, na mbaya zaidi wafungwa wale wahuni wakikuona ulikuwa mtu mkubwa kidogo, hutumia nafasi hiyo kukunyanyasa sana.”



    Baba mdogo alisema hayo huku akilia na kuniomba msamaha, nikaamua nitamsamehe bure na kumsaidia tu. Ni kweli, nilijiona hata mimi ningekuwa Mungu nisingemuadhibu kwa yote hayo, kwani akiendelea kunielezea, nilihisi kumuhurumia. Yeye alisababisha nibakwe na mdogo wake, lakini malipo aliyopata ni kubakwa na wanaume wenzie. Alisababisha nimpoteze mama, lakini Mungu akamuondolea mke wake wa kwanza, na wa pili akanyang’anywa. Alifanya niishi maisha ya mateso mtaani, yeye akaishi maisha ya mateso gerezani. Alisingiziwa na kupoteza mali zote, na tayari alipoteza ndugu yake mmoja aliyekuwa amebaki, hivyo maisha kumuacha mpweke kabisa. Maisha aliyoringia awali hakuwa nayo tena, na hata watoto waliokuwa halali yake hakuwa na mamlaka wala ujasiri nao tena. Nilimsaidia kumuinua tena, na sasa angalau hupata kiasi cha pesa cha kumfanya kukidhi mahitaji yake kwani nilimsaidia kupata kazi sehemu bora zaidi.



    Mungu hana upendeleo, Mungu hana kuwahi wala kuchelewa, Yeye hatazami kama wanadamu tunavyotazama, na binafsi nimehakikisha hayo kwenye maisha yangu. Nilipoumizwa sana nilimuhisi Mungu kama mwenye upendeleo kwa baadhi ya watu kama baba zangu wadogo, nilimtazama kama asiyejali hisia zangu na labda hayupo kabisa. Mungu aliona mateso yangu, na hata hali ilipokuwa ngumu sana, alinisaidia kuendelea mbele. Leo hii ninaandika kuhusu maisha yangu, ni mwanamke mwenye familia ya furaha mno. Nimesahau mateso yangu kwa kiasi kikubwa, machozi yangu yamefutwa na kuna wengi ninawasaidia kusimama na kutoka kwenye mateso ambayo maisha huwapitisha. Nina mume mzuri, mcha Mungu na mwenye mapenzi ya dhati, asiye na ubaguzi wowote wa rangi. Nina familia ya mume wangu yenye upendo sana na mimi, ambao kwa kiasi kikubwa wamenifanya kuhisi wazazi wangu wamerudi tena. Mdogo wangu ana maisha mazuri, ana ndoa na familia yenye furaha na upendo mwingi. Na kaka yangu Bahati pia ana ndoa yenye amani na upendo, na hali yake ya uchumi ni bora kuliko kabla hajaugua. Lakini hata wafanyakazi wetu kaka Abdalah na dada Shanisa, ambao tuliishi nao kama ndugu, wamekuwa na maisha bora ya kiuchumi na kifamilia. Mimi na mume wangu tuna makazi ya kudumu Afrika ya Kusini ambako ndiko kuna biashara zetu kubwa, ila pia tuna nyumba Tanzania na Canada. Lakini kwa Tanzania, msimamizi mkuu na mwendeshaji wa biashara zetu ni kaka Bahati na mkewe.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Natumai umejifunza mengi toka katika historia yangu, katika upande wa mateso na katika upande wa mafanikio pia. Ningependa kutabaruku (dedicate) simulizi hili la maisha yangu kwa yatima wote, walioachwa na wazazi katika umri mdogo au mkubwa lakini wakiwa bado wanawategemea. Ninaomba jamii ione jukumu la kuwalea na kuwapenda, ili walau kwa kiasi kusimama nafasi ambayo wazazi weo wangesimama. Hakuna aliye na hakika mzazi wake ataondoka lini, hakuna anayepanga kifo cha baba au mama yake, na tena hakuna anayefahamu watoto wake atawaacha katika hali gani. Ni vema kujali wa wenzio ili Mungu akupe neema ya kulea wakwako, au hata ukiondoka, wabaki mikono salama. Ila pia nawatia moyo yatima kwamba Mungu ni Baba na Mama yenu, na ninaamini anawapenda. Usiruhusu kuyakatia maisha tamaa na kujikinai kwa uyatima wako au kwa mateso unayopitia, usiruhusu kuingia katika tabia za ajabu zitakazoathiri maisha yako, na usifikie uamuzi wa kujiua. Kuna siku moja Mungu atayafuta machozi yako na kukupa hatima bora, na hayo ndio maombi yangu kwa Mungu.



    M W I S H O



    Andika Maoni au Ushauri wako hapo chini:



0 comments:

Post a Comment

Blog