Simulizi : Ulikuwa Wapi
Sehemu Ya Nne (4)
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kipindi fulani alitokea kaka mmoja tuliyesali naye kanisa moja, akaonesha kunipenda sana, na kutaka kuwa karibu na mimi sana. Ni mtu wa kwanza kumpa nafasi ya kunizoea kidogo, lakini baada ya miezi michache tu alisafiri na kwenda nchi za Ughaibuni. Siku ananiaga ndipo aliniambia kuwa ananipenda na angependa niwe mke wake, lakini amepata nafasi ya kwenda kusoma na itamchukua miaka miwili kurudi. Alinipa ahadi ya kwamba tutaendelea kuwasiliana kwani hana mpango wa kuwa na mwanamke mwingine zaidi yangu. Sikutilia maanani sana maneno yake kwani kutoa ahadi ya kumuona binti ambaye hata hajakukubalia na hauko naye kwenye mahusiano, na unasafiri kwa muda mrefu, ni kitu ambacho niliona hakina uhalisia. Ni kweli alisafiri na kuwa akinitumia baruapepe mara kwa mara, na hata kupiga simu. Nilimchukulia kama rafiki tu, nisiweke matarajio yoyote ya urafiki wetu. Na kama nafsi yangu ilijua, baada ya miezi nane alianza kupunguza mawasiliano sana. Miezi mingine sita ilipita, siku moja nikiwa naangalia mtandaoni facebook, niliona picha zake akiwa na msichana. Ingawa hawakuwa wamekaa namna ya kuonesha ni wapenzi, lakini mimi nilijua kuwa ni watu walio kwenye mahusiano. Kiukweli nafsini niliumia, na hapo ndipo nikajua kuwa huyu kijana kwa kiasi fulani alishaanza kuingia moyoni mwangu. Nilijipongeza kwa kutomkubalia, kwani ningeumia sana kama ningechukulia ahadi zake kama mtu anayemaanisha na kisha kuja kuona ana mahusiano mengine. Haikupita muda, alinitumia baruapepe kuniomba msamaha na kusema kuwa yeye tayari yuko kwenye mahusiano mengine. Sikumjibu mpaka hii leo, na wala hakurudi baada ya hiyo miaka miwili aliyosema, bali mpaka leo yupo huko nje, ana familia tayari.
Uzoefu wa yule kijana ndio ulinifanya kabisa nisitamani kuwa na mahusiano yoyote. Nilihisi kuwa nikimpa mtu nafasi, atanidanganya na kuniumiza. Kuna wakati nilitamani kaka Bahati angepata mke mwingine akaoa, lakini naye nilimuogopea sana, kuliko mimi mwenyewe. Kila nilipofikiri juu ya ndoa yake ya kwanza ilivyomtesa, sikutamani wala sikuamini mwanamke mwingine yeyote kwa ajili yake. Nadhani ningechanganyikiwa kama kaka angeoa na kuteswa na mwanamke tena, na kufanyiwa mambo kama aliyofanyiwa na Ketty awali, kwani niliamini Ketty alimfanyia uchawi ili kumuuguza na kumnyang’anya mali zake.
Baada ya kukutana na Ketty, niliisubiria simu yake, nikipanga nini cha kumwambia kumuonesha jinsi gani hatumuhitaji tena kwenye maisha yetu. Siku moja, wiki kama mbili zimepita baada ya kukutana naye, alinipigia simu, akiniomba sana tukutane. Nilimjibu kuwa nina mambo mengi, lakini alinibembeleza akidai kuwa angenifuata popote kwa wakati wowote. Nilimwambia kuwa ningemjulisha kama ningepata muda. Baada ya kukata simu yake, alinitumia ujumbe mfupi wa simu. “Zawadi, najua sistahili hata kuwa na namba yako ya simu au kupokelewwa simu yangu na wewe. Lakini naomba nafasi moja tafadhali, ya kuonana na wewe. Nina shida nyingi mno, sina tegemeo wala mtu hata mmoja wa kunisaidia. Tafadhali nipe tu nafasi ya kunisikiliza, hata usiponisaidia, lakini unisikilize tu angalau mara moja.” Niliamua kuwa nitamtafuta nimpe nafasi ya kumsikiliza, ingawa huo ujumbe sikuujibu kwa wakati huo. Kesho yake mchana nilimtumia ujumbe mfupi kumwambie tukutane sehemu fulani, mjini posta, katika mgahawa wa kawaida wa chakula pale mjini, kwani pia haikuwa mbali na ofisini kwangu. Sikutaka kabisa ajue ofisi zetu zilipo hivyo sikumuita ofisini ingawa tungepata nafasi nzuri zaidi kama angekuja ofisini. Tulikutana muda niliopanga, nikakuta ameshafika, ananisubiri kwa nje nadhani akihofia kuwa akikaa ndani watamlazimisha kuagiza walau kinywaji. Tulikaa meza ya peke yetu, nikamtaka aagize chakula kwani ulikuwa muda wa chakula cha mchana. Tukiwa tunasubiria chakula chake (mimi sikutaka kula hapo), nilimtaka aanze kusema kile alichoniitia.
“Sijui nianzie wapi zawadi, na sijui kama utanielewa. Hata usiponielewa sitakulaumu, lakini tangu siku ile tumeonana, nimetamani nikutafute nikuombe msamaha walau ufikishe msamaha wangu kwa kaka yako Bahati kwani sina kabisa ujasiri wa kuonana naye. Sikuweza kukutafuta, niliogopa sana, nikahisi hungetaka kabisa kuonana namimi tena. Yaani hata kitendo cha kunipa namba yako ya simu siku ile kilinishangaza kwani najua sistahili hata kuzungumza nawewe. Kilichonifanya nikutafute ni maji kunifika shingoni Bahati. Miaka yote nimetamani kujua kama huenda Bahati bado anaishi, nikapata ahueni sana siku ile umekuja sokoni. Sidhani kama unakumbuka, lakini kabla ya kuanza kununua nyanya, ulichukua simu na kuzungumza na mtu, nadhani dereva, ukimwambia kuwa kaka Bahati anahitaji kufuatwa kazini mapema kwani kuna sehemu anaenda. Sikutaka hata kukuonesha kama nimekukumbuka na nakufahamu vizuri, lakini mimi nilikutambua mapema sana na kwangu ile simu ilikuwa ya muhimu sana kunijulisha kuwa Bahati ni mzima. Kabla hujaanza kuongea na simu, nilikuita kwa juhudi uje uniunge nyanya, nisijue kama ni wewe, lakini nilitamani nikimbie au niyeyuke baada ya kutambua nakutana na wewe kwa mara nyingine.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Niliolewa na mwanaume mwingine baada ya kuondoka kwa kaka yako Bahati. Huyu mwanaume kusema kweli nilikuwa na mahusiano naye kabla ya Bahati, na sikuwahi kuacha kumpenda hata baada ya kuolewa. Nilimkubali Bahati kwa kuwa huyo kijana hakuwa na maisha mazuri, nikamuahidi kwamba mahusiano yetu yangeendelea hata baada ya mimi kuolewa. Ni kweli tuliendelea, baadaye akanipa wazo la kumuua mume wangu na kuchukua mali zake. Sielewi ni shetani gani aliniingia, nikakubaliana na wazo lake, kwani mwanzoni niliogopa sana na kumkatalia kwa juhudi zote. Sikuwahi kufikiri kama naweza kuwa muuaji, sikuwahi kutamani kukatili maisha ya mtu. Nilimuangalia Bahati aliyenipenda kwa moyo wake wote, nikamuhurumia na kulaani wazo la kumuua au kumdhuru kwa hali yoyote, lakini miezi ilivyosogea, mapenzi yakazidi kushamiri kati yangu na huyo kijana, taratibu wazo lake lilianza kuchukua nafasi akilini mwangu.
Nilimtaka anishauri ni namna gani nitamuua kwa taratibu bila kujulikana, akaniahidi kushughulikia hilo suala yeye mwenyewe. Baada ya muda alinipa dawa, akanitaka nimpe katika chakula na haitaonesha kwamba amepewa sumu bali ataanza kuumwa ugonjwa ambao utamuua. Nilifanya hivyo, Bahati akaanza kuumwa, hapo ndipo nikajiaminisha kuwa ni mtu wa kufa na mali zake zote ni zangu. Nimemtesa Bahati, kana kwamba nina moyo wa mnyama. Sijui nilirogwa au ni nini, lakini sikuwa na huruma kabisa na Bahati hata kidogo. Nilipoona anakawia kufa, nilihisi anachelewesha maendeleo yangu, nikazidi kumtesa kwa kutomjali. Sikutaka apate msaada kutoka kwa rafiki yake yeyote hivyo niliwaaminisha rafiki zake vitu vingi vya uwongo. Nilijifanya mimi ndiye niliyempenda na kumjali Bahati kuliko yeye alivyonipenda, na kwa kuwa rafiki zake walifahamu kuhusu mahusiano yake ya nyuma, waliniamini.”
Wakati anajieleza, nilihisi kutetemeka kwa hasira na uchungu. Ni kweli nilihisi kuwa Ketty ndiye muhusika wa tatizo la kaka Bahati, lakini nadhani sikuwa tayari kuhakikishiwa hilo, tena na yeye mwenyewe. Yaani adui yangu mkubwa zaidi maishani, mtu aliyewahi kuniumiza na kunitesa zaidi, mtu aliyewahi kunisababishia kupoteza tumaini kabisa la maisha, alikuwa anakiri alichokifanya mbele yangu. Ni kweli baba zangu wadogo walinitesa baada ya baba na mama kufariki, lakini wao sio walioua wazazi wangu, hata kama walihusika kwa kiasi. Niliwaza kwamba endapo kaka angefariki, leo hii sidhani kama ningeweza hata kukaa meza moja na Ketty. Nilijihisi kumchukia zaidi, nikatamani asiendelee kuongea na nisionane naye tena kamwe, lakini nilijikaza na kuishawishi nafsi yangu kuendelea kumsikiliza. Aliendelea kuongea, “Baada ya kuona muda unapita na kile nilichotarajia hakifanikiwi, nilimtapeli Bahati mali nilizoweza kuchukua, nikaondoka na kuanza maisha na huyo mwanaume. Tumeishi kwa mapenzi tele kati yetu, tukifurahia maisha na mali za kaka yako, huku mwanaume akinirubuni bila mimi kujua na kumfanya mmiliki wa kila kitu. Nilipata mtoto wa kwanza, lakini akiwa na mwaka mmoja alifariki. Nikaanza kuhisi kuwa Mungu ameanza kunilipa, lakini tukafarijiana na kutiana moyo na mume wangu, maisha yakaendelea. Tulifanya taratibu za kufunga ndoa ya kidini, hapo nikawa na uhuru zaidi wa kummilikisha mwanaume kila kitu aliyedai kuwa yeye ndiye anatakiwa kuwa msimamizi wa kila kitu kwani ni mwanaume na ana elimu kidogo zaidi yangu. Kwa mapenzi aliyokuwa akinipa, sikuona shida kumpa chochote alichohitaji. Alinipenda na kunipa mahaba yasiyo ya kawaida, yaani sikuwa najua kupika, kufua, kufanya chochote, mpaka kuoga aliniogesha mara nyingi tu. Aliniambia maneno matamu mno na hakuchoka kunihubiria kiasi anachonipenda kila siku iliyoitwa leo. Nilijiona nimefika, nikasahau kabisa kama kuna mtu anateseka kwa ajili yangu, tena si yeye peke yake, bali na wale waanomtegemea.
Nilipata mimba ya pili, ikaharibika, mume wangu Peter akanifariji tu akiniahidii tutapata mwingine. Maisha yaliendelea, nikaanza kujaribu kupata ujauzito, bila mafanikio. Mwaka wa kwanza ulipita, wa pili na wa tatu, nikafanikiwa kupata ujauzito, nikajifungua mtoto mwingine wa kike, lakini naye akiwa na miezi sita, akafariki. Hapo sasa nikahisi kuna kitu si cha kawaida, nikalia sana. Mume wangu ambaye ndiye alikuwa faraja yangu kubwa, safari hii alionekana kuwa na mawazo mengi sana kiasi cha kushindwa kunipa faraja. Maisha yaliendelea baada ya msiba, huku Peter akionekana kushuhwa moyo sana na kitendo cha mtoto kufariki mara hii tena. Ndoa ilianza kuingia doa kidogo, amani kati yetu ikapungua kwani Peter alikuwa na mawazo mengi mara kwa mara. Nilimvumilia, nikajaribu kuwa mchangamfu zaidi kwake, nikimfariji kwamba tutapata mtoto mwingine.
Baada ya miezi kadhaa nilimshauri twende kwa mganga atusaidie kutafuta mtoto. Kweli, tulienda kwa waganga kadhaa, nikafanikiwa kubeba mimba na kupewa masharti mengi sana, nikiambiwa endapo nitayavunja mimba itatoka au mtoto atakayezaliwa atafariki. Nilikaa na mimba hiyo kwa miezi tisa, lakiini siku ya kujifungua, mtoto wangu wa kiume alizaliwa akiwa amefariki. Peter alilia sana, asikubali kufarijiwa. Aliongeza kuwa mtu wa mawazo, na maisha baada ya mtoto huyo kufariki yalikuwa sio kama awali hata kidogo. Peter alianza mawazo kiasi cha kuchanganyikiwa. Alianza kuwa mtu wa kunywa pombe, akashindwa kabisa kuendelea kuwa mtafutaji au kwa namna yoyote kuendeleza mali nilizomkabidhi. Nilijitahidi kuongea naye, lakini alikuwa mkali kama pilipili. Hakuendelea kuonesha mapenzi aliyoonesha awali kwangu, hakunijali tena na kadiri siku zilivyoenda, alianza kunitamkia maneno ya kunilaumu kuhusu watoto wanaokufa. Alifanya hivyo mara nyingi akiwa amelewa, nikawa nikimsamehe bure huku nikiona ni pombe ndiyo inayomuondoa akili. Nilimsubiria akiwa sawa, nikawa nikimbembeleza aache pombe, nikimueleza jinsi gani ananitesa, akaniahidi kuacha mara kwa mara lakini hakufanya hivyo badala yake alizidisha sana kulewa. Akiwa amelewa sana, alinizungumzia maneno ya kuniumia, akidai ataacha pimbe siku nitakapompatia mtoto na asife.
Maisha yalizidi kuwa machungu kwangu, Peter akaanza kuwa akinipiga akilewa, akawa akirudi nyumbani usiku, akinitukana na hakuwa tena Yule mpenzi wangu wa zamani aliyenifanya niisaliti ndoa yangu. Nilianza kwenda tena kwa waganga, kutafuta msaada sio tena wa mtoto, bali wa ndoa yangu. Nilipewa dawa, nikamuwekea, akawa anaanza kuwa sawa tena, kupunguza pombe na kuanza kunipenda kwa upya, nikajua maisha nimeyawezea tena. Lakini baada ya miezi kadhaa, siku moja kwa bahati mbaya aliona dawa niliyoiweka chumbani, akawa mkali sana. Alinipiga sana siku hiyo huku akidai siku zote za maisha yake nimemroga. Nilimuomba msamaha lakini hakunielewa, akaanza kwa upya vituko, pombe na safari hii akaanzisha na mahusiano ya mapenzi na wanawake wengine, kitendo ambacho hakuwahi kufanya kabla. Aliniumiza sana, mapenzi yakawa machungu zaidi ya shubiri, akawa akilala na mimi kwa lazima kila akitoka kunywa pombe, akaniletea wanawake hadi ndani, na hakunijali tena. Nilivumilia, nikijua kuna siku atabadilika. Mali zilianza kupungua na kupungua mpaka kuisha kabisa, maisha yakawa magumu mno huku nikijaribu kujishughulisha na biashara za hapa na pale.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kipindi fulani nadhani kwa ajili ya pombe nyingi, mume wangu alipata ugonjwa wa akili, akachanganyikiwa kabisa, akawa mtu wa kufungwa kamba. Nilihangaika naye sana baada ya kupata ugonjwa huo, nikijaribu kwa waganga mbalimbali bila mafanikio. Lakini wakati anapata tatizo hilo nilikuwa nimepata ujauzito, hivyo nikawa nikimuuguza na kuhudumia mimba yangu wakati huo huo. Niliangaika na waganga, nikakata tamaa, nikaona nijaribu hospitali. Nilianza kupata matumaini hospitali, hali yake ikaanza kuwa nzuri, na mpaka kupona kabisa, nikiwa tayari na mtoto wa mwaka na nusu. Baada ya kupona, ametulia na hanywi tena pombe, lakini kiukweli mahusiano yetu yamebadilika sana. Peter kuna wakati anadai kuwa tabia yangu ya kupenda waganga ndiyo iliyomfanya achanganyikiwe, na hata ugumu wa maisha tulionao ananilaumu mimi. Nimekuwa mtu wa kulia kila siku, na kuhangaika na maisha kuipatia familia yangu hela ya chakula na hata kodi ya nyumba. Nimefanikiwa kuanza biashara ya nyanya, na ninapata nyanya nzuri sana, lakini pesa haitutoshi kabisa. Peter hukaa tu nyumbani, akidai kuwa hatakiwi kujiangaisha na chochote kwani mimi ndio chanzo cha maisha yetu kuwa vile alivyo. Hunisaidia kulea mtoto kwani anampenda sana mtoto wake, lakini majukumu mengine yote ni juu yangu. kuna wakati tunalala njaa, isipokuwa mtoto ambaye huwa najitahidi asikose angalau muhogo wa kulalia. Tunaishi nje ya mji ambapo maisha ni rahisi, kama kijijini, lakini nyumba tunayoishi ya tope, bado sio ya kwetu, ni ya kupanga. Kilichonifanya nishindwe kuvumilia na kukutafuta ni mtoto wangu. Juzi ameanza kuumwa, ameshikwa na homa kali mno na usiku kucha alikuwa akilia. Peter ana hofu kubwa kwamba mtoto anakwenda kufa, kwani dalili anazoonyesha ni sawa kabisa na wale wawili waliofariki walivyoumwa. Tumempeleka hospitali, inaonekana ameshikwa na malaria kali, lakini pia ana degedege iliyojificha na wamesema tukifanya uzembe tutampoteza. Matibabu yake siyo ya gharama kubwa lakini hapa ninapokwambia, nimeshatafuta watu wanikopeshe bila mafanikio. Nina shida kubwa, ingawa watoto umri wake hutibiwa bure serikalini, lakini kuna gharama nyingi za dawa ambazo hazitolewi bure, na pia kuna vipimo ambavyo serikalini havipo imebidi niandikiwe kwenda hospitali binafsi. Ninavyokwambia, hata nauli kwangu sasa ni shida kubwa. Sijui nitafanya nini nikimpoteza mwanangu mara hii tena Zawadi, tafadhali naomba unisaidie.”
“Zawadi, kuna mkutano wa wafanyabiashara tumetumiwa barua, sijui kama umeiona?” Aliniuliza kaka Bahati jioni wakati wa chakula. “Nimeiona, kiingilio ni kikubwa kidogo, sijui watakuwa na lipi jipya!” Nilimjibu, nikiashiria kutotaka kushiriki kwa kuona gharama ni kubwa kidogo. Kuishi maisha ya shida sana nadhani kulinifanya niwe mtu fulani ninayefuatilia sana gharama. Kwa wakati huo, mpaka sasa, kutoa dola mia moja au laki mbili, mbili na nusu za ki-Tanzania, haikuwa pesa nyingi, lakini niliona wamefanya gharama kubwa sana nikawa naona ubahili kuilipa. Lakini kaka alisisitiza kuwa kama si sote basi mmoja kati yetu angetakiwa kuhudhuria. Tulishahudhuria mara kadhaa mikutano ya namna hiyo, ila mingi iligharimu shilingi laki moja. Nilipanga ratiba zangu, nikalipia na kuchukua kadi kwa ajili ya huo mkutano. Ulitakiwa kufanyika hoteli moja ya nyota tano, iliyoko maeeneo ya Posta jijini Dar es Salaam, inaitwa Kilimanjaro, zamani Kempiski.
Tangu nianze kujikita katika biashara na kuanza kupata fursa ya kuikuza biashara yetu, nimejifunza tabia fulani za kisasa kidogo. Ninaamini katika mtazamo ambao watu hutoa kutokana na muonekano. Kuna wakati huwa tunaonana na wateja wakubwa, wengine viongozi serikalini au viongozi wa makampuni mbalimbali. Nimejifunza kuvaa kitanashati sana, na kuendana na matukio, na pia kujiamini ninapozungumza na watu hasa wateja. Nadhani elimu kubwa nimeipata katika ufanyaji wa biashara ndani ya muda mfupi tangu nianze biashara. Mara nyingi tukiwa na miadi na wateja wakubwa, huonana nao hoteli za kifahari, hivyo kuniongezea uzoefu au exposure kwa lugha ya wenzetu. Siku ya mkutano nilivaa sketi fupi, ya kiofisi, viatu virefu kiasi vya kufunika na shati ya kike ya kuchomekea, nikahakikisha nimetoka kiofisi na kimaridadi kabisa. Katika huo mkutano, kuna wafanyabiashara maarufu kutoka nchi za Kenya na Uganda, na Afrika Kusini walishiriki, waliokuwa kati ya wawezeshaji.
Mkutano ulianza, wakawa wakiongea watu wenye uzoefu mkubwa, wa ndani na nje ya nchi. Tukiendelea na mkutano, nilielewa ni kwa nini gharama ya kushiriki ilikuwa juu, kwani waliozungumza ni watu wenye uzoefu sana na biashara. Tulitumia muda mrefu, karibu siku nzima, ukiacha dakika tulizotumia kwa ajili ya chai na chakula cha mchana, ila muda mwingine wote ukitumika kufundishwa na kuuliza na kujibiwa maswali. Nikiwa ndio namalizia kuchukua chakula, kijana mmoja mzungu aliyekuwa nyuma yangu alinigusa bega, nikageuka, akanipa kitambaa changu nilichokuwa nimekidondosha bila kujua. Wakati nachukua chakula, niliweka pochi yangu ndogo, pamoja na kitambaa kwenye kwapa, bila kuhisi kuwa niliangusha kitambaa cha jasho yaani handkachif. Nilimshukuru, nikaichukua na kuelekea sehemu maalumu tuliyokaa wakati wa kula. Nilikaa meza yenye viti viwili, yule mzungu akanifuata kwa nyuma, akaja kukaa pamoja nami. Tulikaa tumetazamana, akaniangalia na kutabasamu, nami nikampa tabasamu, tukaendelea kula. Kuna wakati nikataka kufungua maji ya kunywa ninywe, akafanya haraka akafungua na kunisaidia kumimina, nikamshukuru. Baada ya hapo, alianza kuniuliza maswali kadhaa kuhusu biashara ninayofanya, nikamueleza, akanieleza pia kuhusu yeye na taaluma yake. Nilimuona ni kijana mdogo, lakini inaonekana hakuwa mdogo katika biashara. Nilitumia fursa hiyo kutaka kujua vitu vingi kuhusu biashara kutokana na uzoefu wake, akanieleza mambo kadha wa kadha.
Tulimaliza kula, tukasimama kurudi ndani, nilipotembea kama hatua mbili, alinisifia, “You look very elegant, I like your dressing code” akimaanisha kuwa nimependeza sana na amependa nilivyovaa. Nilimshukuru kwa tabasamu, tukaendelea kwenda. Tuliingia tena sehemu ya mkutano, akakaribishwa msemaji mwingine, akazungumza kwa muda, baada ya huyo akakaribishwa mnenaji wa mwisho, nikashangaa kuona yule kijana tuliyekaa naye wakati wa chakula akisimama. Alisimama na kutoa utambulisho wake kwa kirefu zaidi ya alivyojitambulisha kwangu, nikagundua ni mmiliki wa kampuni kubwa sana nchini Afrika Kusini, inayosambaza bidhaa zake sio tu nchini kwake, bali Afrika Mashariki yote na nchi nyingine. Niligundua yeye ndiye alikuwa mkubwa zaidi kati ya wafanyabiashara wakubwa waliokuwepo, na ni kama mkutano huu uliandaliwa hasa kwa ajili yake. Katika maelezo ya barua tuliyoletewa, ilisema kutakuwa na wafanyabiashara wakubwa sana lakini sikufuatilia ni nani hasa wangekuepo. Bidhaa za kampuni yake ni maarufu sana nchini, na kama ningefahamu mmiliki wa kampuni hiyo atakuwepo basi ningetamani sana kuwepo katika huo mkutano bila kujali gharama.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Naitwa bwana Jones Lincoln, ingawa wengi hunifahamu kwa majina ya kampuni yangu mama ya the great pioneer, ambayo nina hakika wengi wenu mliopo hapa ni watumiaji wa bidhaa zake. Kwangu hiyo si muhimu sana, wala si sababu kubwa ya mimi kuwa msemaji mkuu siku ya leo. Nitakuonesha nini ni sababu ya mimi kupata fursa hii siku ya leo.” Utambulisho wake huo ulinifanya nitake kujua mambo mengi zaidi kuhusu huyu kijana, tajiri mdogo. Nilivutiwa na namna alivyojitambulisha, lakini pia nilivutiwa sana kuona katika umri wake kuwa mmiliki wa kampuni kubwa kama ile. Akiendelea kuongea, niligundua hiyo si kampuni pekee anayoiendesha. Ana kampuni nyingine kubwa nchini Canada, ambayo ndiyo nchi ya mama yake, na inafanya vizuri katika nchi za Canada na za jirani. “Kitu kikubwa ninachojivunia ni namna nilivyoweza kusimama kila mara nilipoanguka na kushindwa. Kuna wakati nilipoteza mtaji niliokopa wa kiasi cha zaidi ya dola elfu 20 za ki-Marekani, ikanilazimu kushuka chini kabisa na kuanza upya. Nililia kwa usiku mmoja, lakini kesho yake nikainuka nikiwa na nguvu mpya, nikapuuza kunyang’anywa mali zangu nilizoweka dhamana na kutafuta namna gani nitasimama tena. Nimepoteza binti niliyempenda sana, tuliyekuwa kwenye mahusiano kwa miaka sita, baada ya kuanguka mara nyingine tena. Sizungumzii kuanguka kidogo, sizungumzii kupoteza pesa chache, nazungumzia kushuka chini kabisa. Najua nini maana ya kupoteza, najua nini maana ya hasara, na sio kwamba nilianguka na kupata hasara kwa uzembe.
Katika umri mdogo nilipata fursa ya kusoma na kuwa na elimu nzuri tu, lakini shauku yangu tangu utoto ilikuwa kufanya biashara. Baada ya kumaliza shahada ya pili, ya biashara na masoko, sikutaka kuajiriwa bali nilitafuta namna nitakayoanza biashara. Nilipata upinzani mkubwa toka kwa wazazi na familia waliotegemea niajiriwe. Nilionekana sijitambui kwani nilipata fursa za kuajiriwa katika kampuni kadhaa mashuhuri lakini sikuzikubali. Katika uchanga wangu katika uzoefu wa biashara, nimekutana na changamoto nyingi sana. Lakini nilijigundua mimi ni mtu mwenye nguvu nyingi. Sio kwamba sipotezi, lakini sikubali kuishi katika manung’uniko ya kupoteza kwa muda wa zaidi ya siku moja. Sio kwamba siumii ninaposhindwa au nikipata hasara, lakini hudharau maumivu yangu kwa haraka sana. Natumia usiku mmoja tu, kulia, kuumia na kuudhika, lakini kesho yake huinuka na nguvu mpya na kuanza kutafuta njia mpya.
Nimewahi kupata maanguko makubwa mara nne, yaliyonipa hasara kubwa sana, sio tu ya pesa na mali, bali hata ya mahusiano. Ilinigharimu kutengwa na familia, nikisimamia ndoto zangu. Lakini leo hii, mimi ndiye naiweka familia pamoja. Sijabahatika kupata mpenzi tena, pengine nitapata hapa leo (ha ha ha ha). Lakini hiki ndicho ninachovunia zaidi, kwamba nina nguvu nyingi, na uwezo mkubwa wa kusimama tena. Hicho pekee ndicho kimenifanya niwe msemaji mkuu siku ya leo. Na hicho kinaweza kukufikisha wewe kama mfanyabiashara, popote unapotaka kufika.”
Nilimtizama akizungumza, kijana huyu ambaye nina hakika hakufikisha miaka 35. Niliguswa sana na kila alichokisema kuhusiana na uzoefu wake wa biashara. Wengi tunatamani kuwa wakubwa katika biashara, au katika mafanikio mbalimbali ya kimaisha, lakini tunaogopa sana kushindwa au kupoteza. Wengi walianza biashara kwa nguvu nyingi sana, lakini walipopoteza mara moja, waliogopa na kukata tamaa. Wengine wamekatia tamaa ndoto zao za kitaaluma, za kiuongozi au mambo mbalimbali ambayo kama wangedharau changamoto na kujiongezea nguvu, leo hii wangekuwa watu tunaosikia habari zao. Huyu mnenaji, Jones, aliifungua akili yangu katika namna ya tofauti sana, akanipa changamoto katika jitihada zangu za kufika pale ninapotamani kufika kiuchumi.
Tukiwa tunatoka, kulikuwa na chai ya jioni, ambayo tungepata kabla ya kuondoka. Walisisitiza tusikose kwani pia ingetupa fursa ya kujichanganya vizuri na kubadilishana namba. Nilichukua kikombe cha kahawa, nikawa nikinywa huku nimesimama, nikisalimiana na watu wawili watatu. Nilitizama upande na kumuona bwana Jones amezungukwa na watu, akiendelea kuzungumza na kusikilizwa. Kuna waliouliza maswali, kwani muda wa maswali haukutosha wakati wa mkutano. Nilitamani ningemfuata, lakini sikuona kama muda ungetutosha hata kama ningepata fursa ya kuongea naye tukiwa pale. Nilipuuza, nikaendelea na waliokuwa karibu yangu, tukiulizana maswali ya hapa na pale, huku nikimalizia kikombe changu cha kahawa ili niondoke. Niliweka kikombe mezani, baada ya kumaliza kahawa, nikaanza kuondoka. Ukumbi tuliofanyia mkutano ni mkubwa, hivyo kuna hatua kadhaa kutoka nyuma nilipokuwa mpaka mlangoni, nikaanza kutembea taratibu kuelekea mlangoni .
“Zawadi!” Nilisikia naitwa na mtu ambaye ni kama alipata shida kutamka jina langu kwa ajili ya lugha. Nikageuka, nikashangaa sana kuona ni bwana Jones, aliyekuwa akijaribu kunikimbilia aniwahi kabla sijatoka. Nilisimama huku nikimtizama na kujaribu kuficha mshangao usoni pangu. “Nitaendelea kuwepo Tanzania kwa muda usiopungua wiki tatu, nitakuwa na mambo mengi sana lakini ningependa tukae pamoja kwa chakula cha jioni siku moja.” Alisema, akimaanisha kuniomba muda wa faragha. Kuombwa nafasi kama hiyo na kijana huyu mkubwa sana kubiashara, kwangu ilikuwa fursa kubwa. Sikuwaza kwa haraka alihitaji nini kutoka kwangu, lakini kama ningeweza kumuomba kuonana naye kabla yake, nadhani ningefanya hivyo. Nilihisi huenda alijaribu kutafuta mwenyeji au kampani kwa kipindi atakapokuwa nchini, ila hakutaka tuonane mapema, hivyo inamaana alikuwa na wenyeji na ratiba zilizopangwa. Tulibadilishana namba, nikaondoka.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilimuhadithia kaka kuhusu mkutano huo ambao binafsi niliona ulikuwa na faida kubwa kwa ajili ya biashara zetu. Kaka akijua jinsi gani matukio ya namna hiyo yalivyo na umuhimu, alisema, “Nlijua, siku zote kuna vitu ambavyo ni muhimu sana kuliko thamani ya pesa. Kusikiliza watu wenye uzoefu ni moja ya nguzo za msingi sana katika mafanikio ya biashara. Makosa ambayo wengine wamefanya si lazima na wewe uyafanye, kama unapata fursa ya kujifunza kutoka kwao.”
Sikuwa nimemwambia kaka kuhusu kuonana kwangu na Ketty kwa mara nyingine. Sikutaka kabisa ajue chochote kuhusu mazungumzo yetu, kwani nilihisi kila kitu kingemuumiza. Lakini pia sikutaka kabisa kuendelea na mawasiliano na Ketty. Kukubali kumsaidia, haikumaanisha kwamba moyo wangu umefunguka dhidi yake, au uhusiano kati yetu ni mzuri. Siku moja, kama mwezi baada ya kuonana naye na kumsaidia, alipiga tena simu. Hakuwa na simu, lakini alikuwa na namba ya simu ambayo aliitumia alipotaka kuwasiliana. Kuona namba yake, nilishikwa na hasira. Ilikuwa siku ya Jumamosi saa nne asubuhi, tukiwa uani, baada ya chai. Mara nyingi siku za Jumamosi mimi huenda kazini mchana, nikijipa muda wa kufanya baadhi ya mambo yangu binafsi nyumbani. Lakini kaka huwa namtaka apumzike siku za mwisho wa wiki, hivyo yeye haendi kazini kabisa. Nilichukia kuona namba yake, sio tu kwa kutotaka mawasiliano naye, bali pia kwakuwa sikutaka kaka ashtukie kama tumewahi kuwasiliana kabla. Huwa sina kawaida ya kupokea simu pembeni, kama niko na kaka, kwani kati yetu hakuna siri. Niliwaza kwamba nikiipokea mbele yake atajua, na nikiondoka na kwenda pembeni, atahisi kitu. Niliiweka kimya, nikaipuuza, lakini napo aliuliza, nikamzuga tu. Sikutaka simu ya Ketty iite tena nikiwa na kaka hivyo nilijifanya nina haraka ya kwenda kazini, nikaenda kujiandaa, nikaondoka.
Nikiwa njiani Ketty alipiga tena, nikaipokea, nikaitikia ‘halo’ ya kikauzu kabisa. Ketty alianza kuongea, akilia, “Zawadi, samahani sana kwa kukupigia tena, lakini mwanangu amegundulika na tatizo kubwa sana, sidhani kama hata wiki mbili zitafika kabla hajafa Zawadi. Anatakiwa apelekwe India au Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu, lakini haitawezekana kwa ajili ya gharama, hivyo tumerudi nyumbani tu kusubiria kitakachotokea.” Alizungumza, kisha akakata simu kama mtu ambaye alipiga kwa lengo la kutoa tu taarifa na sio zaidi. Nilijikuta nimepaki gari pembeni na kuanza kuwaza. Ni kama niliingiwa na huruma na huzuni ya ghafla sana, nikasahau kwamba mtoto ninayemsikitikia ni wa adui yangu. Niliwaza tatizo ni nini haswa na matibabu yake ni yapi. Nilinyanyua simu tena na kupiga lakini hakupokea, ikaita mpaka ikakata. Sikuwa na cha kumwambia bado zaidi ya kumfariji tu, ila nilipoona hapokei nikaanza tena kufikiri ninaweza kumsaidia vipi mtoto apone. Niliwaza pengine kufuatilia bima ya matibabu itakayoweza kugharimia hata matibabu ya nje ya nchi, lakini nikawa na wasiwasi kwamba muda hautaruhusu kwani mtoto ameshaanza kuumwa na yuko katika hali mbaya.
Nilipofika kazini nilipiga tena simu, nikiwa na lengo la kumtaka Ketty tuonane kwa ajili ya kujadili nini cha kufanya. Alisema wako nyumbani tu na hawezi kutoka, hivyo nikafikiri kwenda kwake. Ni kama akili yangu ilisahau kwa muda yote aliyotufanyia Ketty, wakati haya yote yanaendelea. Kichwani sikuwa tena na hasira naye wala chuki, bali niliwaza maisha ya mtoto wake kana kwamba tuna undugu naye. Nafahamu vizuri uchungu wa kufiwa, na ingawa Ketty aliniumiza sana, lakini sikutaka apitie uchungu huo kwa mara nyingine tena, kwani tayari alishapoteza watoto kabla. Nilipanga kwamba kesho yake ambayo ingekuwa Jumapili, ningeenda kumuona, baada ya kutoka kanisani. Siku hiyo niliporudi nyumbani, kaka Bahati alijua kuwa nina tatizo, akajaribu kuniuliza, lakini sikumwambia nini shida. Sikutaka ajue kabisa habari yangu na Ketty, lakini pia sikuweza kuficha yaliyoendelea akilini mwangu usoni pangu. Niliwaza sana nitamsaidiaje mtoto huyo asiyekuwa na hatia. Matibabu ya India au Afrika Kusini yangegharimu pesa nyingi sana, na nisingeweza kutoa kiasi hicho cha pesa kwenye biashara. Kukata bima pia haingewezekana, na kuchangia kiasi nayo haingesaidia kwani Ketty hakuwa na watu wengine wa kumchangia gharama hizo.
Jumapilii baada ya kutoka kanisani nilienda moja kwa moja njia ya Bagamoyo, nikawa nikiwasiliana na Ketty mpaka nikafika. Kaka Bahati nilimwambia tu kuwa kuna sehemu nitakwenda, lakini sikumwambia wapi, kwani hata hivyo amekuwa akinichukulia kama mtu mzima tayari, nisiyehitaji kuaga kila wakati nitokapo nyumbani. Nilifika kwa Ketty, kilomita kadhaa kutoka mwisho wa Dar es Salaam, kuelekea Bagamoyo, maeneo ya ndani kidogo, mandhari ya kijijini kabisa. Nilishangaa muonekano wa lile eneo ni kama tuko mkoa mwingine kabisa, kijijini, na sio jirani na jiji la Dar es Salaam. Hata hivyo, akili yangu haikuelekea katika kushangaa mazingira ya kijijini na hali ya kimasikini sana ya pale nyumbani kwa Ketty, ingawa kama ningekuwa nimeenda kukiwa na shwari, ningeshangaa sana. Sijui nifananishe na nini, ila kama ulishawahi kutembelea vijijini ndani, kwa watu ambao wanaweza kukaa siku tatu bila kuona shilingi elfu mbili, ndivyo ulivyokuwa muonekano wa pale kwake.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilikaribishwa na kuingia ndani, nikapewa kiti cha mbao na kukaa, Ketty akakaa kwenye mkeka, na mtoto alikuwa amebebwa na baba yake aliyekaa kwenye kigoda. Kulikuwa na hali ya huzuni sana, nikaanza kuwauliza nini hasa kinamsumbua mtoto. “Ni saratani ya damu, lakini imesambaa mpaka kufika kwenye ubongo, hivyo hawezi kutibiwa hapa Tanzania, Ocean road (oshenirodi) tena, balada yake inabidi apelekwe nje kufanyiwa upasuaji. Kuna nafasi ndogo ya kupona kulingana na daktari, lakini amesema anaweza kupona endapo atapata matibabu hayo.” Alisema Ketty huku akilia. Niliomba kumshika mtoto, nikamtazama kwa karibu, akiwa na muonekano wa kuugua sana. Nilizuia machozi baada ya kumuona mtoto huyo aliyeteswa sana na magonjwa katika umri mdogo. Alikaa mkononi mwangu akiwa amepooza, huku akitoa sauti fulani ya kulalamika kana kwamba anasikia maumivu aliyoitoa mfululizo. Baada ya muda alianza kulia kwa uchungu sana, nikastuka, nikidhani kuna kitu kimemuumiza. Mama yake alimchukua na kutoka naye nje, baba yake akanieleza huku machozi yakimlenga, “Ni kawaida, huwa muda mwingi analalamika na kulia. Tumeambiwa kuwa ana maumivu makali ambayo hutulia akinywa dawa zake za maumivu kwa muda mfupi na kisha huanza tena kwa ghafla. Hapo anaweza akalia hata saa mbili mfululizo namna hiyo, bila kunyamaza.”
Sikuweza tena kuvumilia, niliona nikiendelea kukaa nitalia tu namimi, na kuwakatisha tamaa zaidi. Niliwaomba niwaachie kiasi kadhaa cha pesa ambacho nilijua kisingewatosha kwa matibabu lakini walau kwa chakula kingewafaa, hasa chakula cha mtoto. Niliacha shilingi laki nane, nikaaga na kuondoka, nikiwaahidi kuendelea kuwasiliana nione tunafanyaje. Kiukweli niliondoka pale nisijue nitafanya nini kuwasaidia zaidi, ila pia niliondoka na huzuni sana na huruma juu ya yule mtoto. Ghafla nikakumbuka kuwa ugonjwa unaomsumbua ungemuhitaji kufanyiwa upasuaji mithili ya ule aliofanyiwa kaka Bahati, nikajikuta nimesema kwa nguvu, “Mungu wangu!” Ni kweli watu husema kila jema au baya utendalo, utalipwa hilo, lakini sikuwa nimewaza kwamba hii ni namna Ketty na mume wake wanalipwa kwa kile walichomfanyia kaka Bahati kwa namna hii. Nilipowaza hivyo, niliona kama Mungu hatendi haki, kwani mtoto yule ni kama malaika asiye na hatia, lakini wakati huo huo nikafikiri kuwa wao pia walifanya hivyo kwa mtu ambaye hakuwa na hatia yoyote, na zaidi labda hakuna namna nyingine ambayo wangehisi maumivu waliyosababisha, kama isingelikuwa hilo jambo kumpata mtoto wao. Hata hivyo moyo wangu haukuweza kuhimili huruma niliyopata juu ya yule kiumbe, nikajikuta nikisema, “Mungu, naomba umuhurumie huyo mtoto, umsaidie. Naomba usikumbuke maovu ya wazazi wake tena, usimuadhibu kiumbe huyu asiyekuwa na kosa lolote.” Niliendelea kuendesha gari mpaka nyumbani, siku hiyo nikaamua kuwa ningemwambia kaka juu ya Ketty na yote yanayoendelea kwenye maisha yake.
“Nimetoka kwa Ketty leo,” nilimwambia kaka Bahati hiyo sentensi baada tu ya kumsalimia tulipoonana. “Unanitania!” Alijibu kwa mshangao. “Ni kweli, sikutanii, nimetoka kwake huwezi kuamini.”
Kaka aliniangalia kwa mshangao, maswali mengi yakiendelea kichwani mwake. Hakutegemea kama kuna siku ingetokea nikapanga kukutana na mwanamke huyo ambaye alijua kuwa nilimchukia kuliko mtu yeyote duniani. Sasa haikuwa tu kuonana naye, bali nilikwenda nyumbani kwake. Najua hii haikuingia akilini mwake, lakini alijua ninachosema ni kweli. Hapo ikabidi nianze kumuelezea mkanda mzima, kuanzia siku ile alipopiga simu na kuomba kuonana na mimi, nilivyompatia kiasi cha pesa awali kwa ajili ya matibabu ya mtoto wake, na jana yake alipopiga simu tukiwa pamoja mpaka nilivyoenda kwake na hali ya mtoto kwa wakati huo pamoja na mambo mabaya yote yaliyompata baada ya kuachana naye na kuolewa na mwanaume wake. Sikusita kumueleza pia kuhusu ubaya wote aliomfanyia, ingawa nilijua ukweli huo ungeweza usiwe mzuri kusikia. “Ndio sababu jana hukuweza kupokea ile simu na wala hukutaka kuizungumzia! Mie nilidhani shemeji yangu ambaye hujataka kumzungumzia bado?” Alinitania. “Wewe unajua sina cha kukuficha kabisa, yaani shemeji yako siku ya kwanza tu akitokea wewe ndiye utakuwa wa kwanza kumjua. Lazima nimlete apitishwe katika viwango vyako kwanza.”
Simulizi la Ketty na maisha yake lilimshangaza mno kaka, kiasi cha kukosa maneno sahihi ya kusema. Nilielewa kuwa alipata hisia mchanganyiko. Katika hali ya kawaida, hata kama alikuwa na chuki kiasi kikubwa namna gani, haingekuwa rahisi kutohisi huruma juu ya mtoto aliyekuwa akiteswa na ugonjwa unaomsababishia mateso makali. Alibaki ameniangalia usoni muda wote namuelezea, akishangaa kana kwamba naelezea hadithi fulani ya kufikirika. Baada ya kunisikiliza, na kukaa kimya sekunde za kutosha, kaka Bahati alisema, “Kweli hivyo ndivyo Mungu ameamua kutulipia kisasi? Akili yangu haiwezi kuamini! Namuhurumia huyo mtoto maskini, hana kosa.”
Baada ya kuzungumzia kuhusu Ketty kwa muda mrefu, hasa hali ya mtoto, kaka alionekana kutamani kumsaidia mtoto pia, lakini kugharimia kiasi kikubwa namna ile cha pesa kutokana na pesa za biashara kwa wakati huo, haingewezekana, ingerudisha nyuma biashara kwa kiasi kikubwa. Tuliacha kuongelea habari za Ketty kama saa tano usiku siku hiyo, baada ya kujadili kila kilichomtokea, lakini hatukufanya maamuzi yoyote juu ya namna ya kumsaidia mtoto wake. Kama ambavyo suala hilo lilikuwa akilini mwangu, lilikaa akilini mwa kaka Bahati pia baada ya kujua, kwani kesho yake tulipoonana wakati wa chai aliniuliza kama nimewasiliana na Ketty kujua hali ya mtoto. Nilikuwa nimempigia asubuhi mara tu nilipoamka, nikitaka kujua kama kuna lolote wamefanya, akasema wanaanza kujaribu kuchangisha watu, na pia wana mpango wa kwenda kituo cha televisheni kuzungumza nao kama watapewa fursa ya kuomba michango.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nikiwa njiani kuelekea kazini naendesha, siku hiyo hiyo ya Jumatatu, Ketty alinipigia simu akilia. Mtoto wake alikuwa amefariki. Ni kweli kabisa sikuwa na mahusiano yoyote ya ukaribu naye, lakini nafsi yangu ilimuhurumia sana. Nilihisi ni uchungu kiasi gani aliupata kwa kupoteza mtoto kwa mara nyingine tena. Hata kaka nilipomwambia, alisikitika sana. Tulienda kwenye msiba kesho yake, tukachangia kiasi cha pesa tulichoona kinafaa kwa ajili ya shughuli za msiba na kuwafariji. Baada ya msiba Ketty aliniomba sana nimuombee kwa kaka waonane, ili apate nafasi ya kumuomba msamaha, nikafanikiwa kumshawishi, wakaonana. Kulingana na maelezo ya kaka Bahati, kuna maneno ambayo aliyasema Ketty kuonesha ni kiasi gani anajutia mateso aliyomsababishia. “Najua ni kiasi gani nimekuwa mchawi wa maisha yangu mwenyewe Bahati. Sihitaji kuambiwa kuwa yote yaliyotokea na yanayotokea kwenye maisha yangu ni malipo ya kile nilichokufanyia. Siwezi kuendelea kuishi na laana hii maishani mwangu, ndiyo sababu nimekutafuta nikuombe msamaha. Naomba ujaribu kuushawishi moyo wako unisamehe na kuniachilia, ili unifungue na laana zinazonipata tafadhali. Naomba uuruhusu moyo wako kusahau niliyokutenda, na kuamini tena katika mapenzi, umpe nafasi mwanamke mwingine ya kumpenda. Sio wanawake wote wako kama mimi Bahati, kuna wanaothamini penzi la wawapendao. Naomba unisamehe tafadhali, hata kama moyo wako unakataa, nahitaji sana msamaha wako. Nimepoteza vitu vingi mno kwenye maisha, ukiwemo wewe mwanaume uliyenipenda kwa dhati, watoto na mimba kadhaa. Kwa sasa sihitaji chochote kutoka kwako zaidi ya msamaha tu, ili maisha yangu yaendelee salama na kwa amani.”
“Nimeamua kumsamehe kabisa Zawadi. Sina haja ya kuendeleza chuki kwa mtu ambaye Mungu ameshamuadhibu vya kutosha. Hata ningekuwa kwenye nafasi ya kumlipa kisasi, nisingelipa kwa ukubwa ambao Mungu amenilipia. Hivyo haina maana kuendelea kumchukia au kuwa na hasira naye. Nimemwambia namtakia maisha mema, na Mungu amjalie kupata mtoto mwingine na kuinuka upya kwa uchumi wao,” Alisema kaka.
Ketty alinipigia kunishukuru kwa kumpa fursa ya kuomba msamaha, na kunitaarifu kuwa wameona wahamie kijijini, yeye na mume wake, wakajaribu kujishughulisha na kilimo. Imepita miaka kadhaa tangu waondoke, na hatukuendelea kuwasiliana.
Alinipigia Jones, yule mfanyabiashara mkubwa sana mzungu, akaniomba tuonane, wiki kama nne baada ya ule mkutano. Alidai kwamba amekaribia kuondoka hivyo angependa tuonane mapema iwezekanavyo, nikapanga ratiba zangu, tukaonana kama tulivyopanga. Maongezi yetu yalikuwa ya kawaida sana, isipokuwa mwishoni ambapo alisema angetaka kufanya biashara namimi endapo mradi aliokuwa akipanga kufanya ungekubali. Baada ya kuniuliza maswali kadhaa kuhusu biashara na kampuni yetu, bwana Jones alisema,“Siku ile tulipozungumza kifupi wakati wa chakula cha mchana, niligundua unaweza ukawa mtu sahihi wa kufanya naye mradi mpya ninaotaka kuanzisha kwa Afrika Mashariki. Utahusiana kwa ukaribu na mambo ya IT yaani mawasiliano ya teknolojia. Napenda zaidi kuanzisha biashara na watu ambao si wakongwe sana kibiashara, endapo ninaanzisha na mtu, kwani hutumia fursa hiyo pia kujifunza mambo mapya toka kwa watu ambao pengine hawajapata fursa kuonesha walichonacho. Nitawashika mkono na kuwafundisha vitu kadha wa kadha kuhusiana na hiyo biashara, na biashara kwa ujumla, na ninaamini endapo tu mtaruhusu, tutafanikiwa bila shaka.” Sikuelewa sana kwanini alichagua kufanya kazi namimi, au na kampuni yetu. Sijui kama unaweza kuelewa nilivyohisi, lakini niliona ni bahati na fursa ya kipekee sana mfanyabiashara huyu mkubwa kutaka kufanya kazi nasi. Sikuweza kumkubalia mara moja, kwani mbali na kuona ni fursa, niliona pia ni changamoto kubwa anatupa, na pia nilihitaji kujadili suala hilo na kaka Bahati. “Utanipa anuani yako ya baruapepe nikutumie dokumenti kadhaa za muhimu zinazoeleza kwa kirefu kuhusu hii biashara, na nini hasa nitahitaji kutoka kwako. Tutawasiliana kwa kirefu, nitakuongoza kila hatua, na kama ukitaka nikae na kaka yako, ambaye umesema ndiye mwenza wako kibiashara, ningependa ndani ya siku mbili au tatu tukae naye tuzungumze kwa kirefu,” alinieleza baada ya kumuuliza maswali yangu ya msingi.
Tuliagana, nafsi yangu ikiwa imeridhika sana, ingawa bado nilikuwa na maswali kadhaa. Hapo pia bado akili yangu haikuamini kuwa kati ya wafanyabiashara zaidi ya mia moja walioshiriki mkutano ule, mimi ndiye nilipata fursa hii ya kipekee. Jones alidai kwamba sababu nyingine iliyomfanya atake kushirikiana nami katika biashara yake mpya, mbali na kuwa alihitaji mtu aliye tayari kwenye biashara za kompyuta, ni vile tulivyozungumza siku ile wakati wa chakula. Aliniambia, “Nimeona hauna uzoefu wa miaka mingi katika biashara lakini una uelewa mkubwa. Nimebahatika kujua kiasi kuhusu saikolojia, na kwa muda mfupi tuliozungumza nimegundua ulivyo na akili yenye uwezo mkubwa sana kibiashara. Kwa hizi siku ambazo nimekuwa hapa, nimejaribu kuangalia kama naweza kukuweka kwenye mzani na wafanyabiasha wengine, lakini hakuna ambaye nimefanikiwa kumpata wa kumlinganisha na wewe. Kitu kingine ni uwezo wako mkubwa wa kujiamini, nadhani kuliko mabinti wengi wa umri wako, unaonesha jinsi gani una uwezo wa kukabili hata biashara zenye changamoto kubwa.” Kiukweli maelezo yake yalinifanya nijione maalumu sana, nikamuahidi kumtafuta kwa ajili ya kukaa na kaka, tujadili kwa pamoja kuhusiana na huo mradi, tuone namna ya kufanya.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Usiku wake alinitumia hizo nakala alizoahidi kunitumia, nikatumia muda wa asubuhi sana baada tu ya kufika ofisini, nikazisoma karibu zote, nikaelewa vizuri nini hasa huo mradi unahitaji. Tulionana naye siku iliyofuata, na kaka, tukazungumza kirefu sana. Katika mazungumzo, niligundua kuwa uzoefu wa kaka wa biashara ulikuwa muhimu sana kwa maongezi yetu na bwana Jones. Kaka Bahati alimpa changamoto ya maswali kadhaa, na kuibua mijadala iliyokuwa ya muhimu sana, ikamfanya aeleze kwa undani zaidi kuhusiana na huo mradi ila pia ikamfanya afikiri zaidi juu ya mradi huo hasa upande wa changamoto anazoweza kukutana nazo kwa hapa nchini. Tulijadili zaidi ya saa nne, kisha tukakubaliana kupeana muongozo wa kila kinachotakiwa kufanyika pindi Jones atakaporudi nchini kwake.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment