IMEANDIKWA NA : JUMA HIZA
*********************************************************************************
Sehemu Ya Kwanza (1)
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Utangulizi;
“Nimeshindwa kabisa kukusahau katika maisha yangu, nimeshindwa kukufuta katika kumbukumbu zangu. Kitabu cha mapenzi tulichokiandika moyoni bado kinanitesa. Naishi na jina lako, kila siku nimekuwa ni mtu wa kumwagika machozi na hakuna wa kunifuta machozi. Ni wewe tu ni wewe uliyesalia ambaye unaweza kunirudisha nikawa katika hali yangu ya kawaida. Bado nakupenda tafadhali usiendelee kunipa adhabu hii ninayoipata kwako,” aliyasema maneno haya huku machozi yakiendelea kumbubujika mashavuni mwake.
Je, ni nani huyo ambaye aliyatamka maneno haya na kwanini simulizi hii imeitwa NIMESHINDWA KUKUSAHAU? Tafadhali ungana nami katika simulizi hii ili upate kujifunza kitu katika maisha yako.
****
Andrew alikuwa ni mwanafunzi mwenye akili nyingi sana darasani, alikuwa akiongoza katika mitihani mbalimbali iliyokuwa ikifanyika pale shuleni. Mbali na uhodari wake katika kuongoza kimasomo alikuwa akiwaogopa sana wasichana, kila siku shuleni alionekana kujitenga na kujiepusha mbali na kuwa na ukaribu dhidi ya wasichana aliyokuwa akisoma nao, hata pale baadhi ya walipomfuata na kuhitaji kuanzisha mahusiano naye alikuwa akiwakimbia na hata wakati mwingine aliweza kuwatukana. Hakuwa na muonekano mbaya sana kwa kumtazama angalau katika macho ya harakaharaka alionekana kuwa ‘Handsome Boy’.
Wanafunzi wenzake walimdharau sana na kumuona kuwa alikuwa na mapungufu katika mwili wake. Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa ugomvi baina yake na baadhi ya wanafunzi aliyokuwa akisoma nao kidato cha pili katika shule ya sekondari Wazalendo iliyokuwepo katika wilaya ya Moshi mjini mkoani Kilimanjaro.
“Adrew atakuwa ni shoga siyo bure,” alisema mwanafunzi mmoja wa kike akimwambia mwanafunzi mwenzake, walikuwa wakimsema Andrew kwa wakati huo.
“Mmh! Yani yupoyupo tu hata haeleweki,” alisema yule mwanafunzi mwingine.
“Atakuwa na homoni za kike.”
“Au kalogwa?”
“Alogwe wapi yule ni shoga.”
“Ananiudhi yani mtu hata kwenye kesi za kuwa msichana shuleni hayupo.”
“Hunishindi mimi yani kama angekuwa kaka yangu ningeshamtoa kafara.”
“Na kweli,” walimaliza kumteta kisha wakagongeana kuyasaili mazungumzo yao.
Kila siku Andrew alikuwa akiingia katika mgogoro na wanafunzi wenzake huku sababu kubwa ikiwa ni wasichana.
Walimu walikuwa na kazi kubwa ya kuwasuluhisha kila siku, kuna kipindi baadhi ya wanafunzi walikuwa wakipewa adhabu kali kutokana na ukorofi wao waliyokuwa wakiuonyesha kama utovu wa nidhamu pale shuleni hasa ya kumkorofisha Andrew ambaye alionekana kuwa kijana mpole sana na vilevile alikuwa akitegemewa na walimu kutokana na umahiri wake wa kufanya vizuri katika mitihani.
“Hivi wewe domo zege utakuwa mjanja lini?” aliuliza mwanafunzi mmoja huku akimtazama Andrew kwa madharau, huyu alijulikana kwa jina la Selestine, mmoja kati ya wanafunzi ambao walikuwa watukutu sana pale shuleni, mbali utukutu wake aliyokuwa nao lakini pia alikuwa akipenda sana wasichana, alikuwa akitembea na wasichana lukuki hata wale waliyokuwa wamemzidi darasa.
“Tafadhali Sele naomba uniache,” alijibu Andrew huku akionyesha msisitizo wa kauli yake.
“Nikuache nini wewe unatudhalilisha wewe,” alisema Selestine huku akijitunisha kifua chake kilichoonekana kuwa na afya hafifu kabisa.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Naomba uniache tafadhali sitaki ugomvi na wewe,” alisema Andrew huku akijaribu kuondoka eneo lile ambalo tayari baadhi ya wanafunzi wapambe walikwishaanza kutawala.
Aliamua kuondoka kuepusha ugomvi kwa wakati ule, wanafunzi wenzake wakaanza kumcheka, walifahamu fika kuwa alikuwa akiwaogopa wasichana, kiumbe kinachoitwa msichana kwake ilikuwa ni vigumu kukizoea.
****
Maisha yaliendelea huku Andrew akizidi kujiweka mbali na wasichana pale shuleni, si kwamba alikuwa akiwachukia lahasha! isipokuwa alikuwa akiwaogopa, alihisi mdomo wake ukikosa kitu cha kuzungumza hivyo aliamua kujiweka mbali.
Baada ya miaka miwili kupita hatimaye akawa amefika kidato cha nne, tabia yake ya kuwaogopa wasichana aliendelea kuwa nayo. Wanafunzi wenzake walikuwa wakimtania kwa kumuita majina mabaya yaliyozidi kumuweka katika wakati wa maumivu makali sana, kila siku alikuwa akiumia maumivu ya ndani kwa ndani na hakukuwa na mwanafunzi aliyeweza kuyatambua maumivu hayo.
Siku moja aliweza kuhamia mwanafunzi wa kike darasani kwao, alikuwa ni msichana mrembo sana, alivutia kila kitu kutazama katika mwili wake. Alikuwa na uzuri wa kipekee kuanzia macho yake legevu, kifua kilichobarikia chuchu zilizochongoka mithili ya kifuu, umbo matata pamoja na rangi yake nyeupe iliyosisimua kutazama.
Kila mtu aliyemtazama aliweza kukiri hilo na ni hapa ambapo wale wavulana waliyokuwa wakipenda wasichana walianza kumtamani ghafla!. Kimoyomoyo kila mtu akatamani kuwa naye.
Miongoni mwa wavulana waliyomtamani msichana huyo, Andrew alikuwa ni miongoni mwao, alijikuta moyo wake ukimpenda msichana huyo mgeni ambaye ilikuwa ni mara yake ya kwanza kumuona.
Historia yake hakuwahi kumpenda msichana wala kuwa katika mahusiano na msichana yoyote yule, Ilikuwa ni mara yake ya kwanza kupenda.
Moyo wake ulizidi kuteseka sana, alikuwa akiteswa na mapenzi kwa wakati huo. Kila alipokuwa akimuangalia msichana yule mgeni moyo wake ulikuwa ukienda mbio kana kwamba alikuwa amefanya kosa kubwa na alikuwa katika mchakato wa kutafutwa.
Hakujua ni wapi alitakiwa aanzie ili aweze kumpata msichana huyo ambaye alijaaliwa uzuri wa kipekee. Aliishia kumtazama tu! darasani asiwe na la kusema.
Kuna kipindi alikuwa akijikuta anashindwa kusoma kwa kumfikiria msichana ambaye mpaka kufikia wakati ule hakuwa amemueleza lolote juu ya hisia zake.
“Unaitwa nani?” ilisikika sauti ya Selestine akimuuliza yule mwanafunzi mgeni. Wakati huo walikuwa darasani kila mmoja alionekana kuwa bize kujisomea kwani ni siku chache zilikuwa zimepita tangu walipotangaziwa kufanya Test siku ya ijumaa ya wiki hiyo, siku hiyo ilikuwa ni Jumanne.
“Naitwa Herieth,” alijibu Herieth kwa sauti ya chini iliyogubikwa na kila aina ya aibu.
Selestine hakutaka kuishia kumfahamu msichana huyo, alichoamua kukifanya ni kujitambulisha na kisha kuzidi kujitapa kwa kuuonyesha uhodari wake hasa katika masomo jambo ambalo halikuwa la kweli, kila siku alikuwa ni mtu wa kushika mkia darasani, mtu aliyekuwa akiwaongoza alikuwa ni Andrew.
Wakati yote yale yakiendelea Andrew alikuwa akiyashuhudia, moyoni alizidi kuumia sana kwa kuona msichana aliyetokea kumpenda alikuwa ameshaanza kufuatwa na wavulana wenye tabia mbaya. Hakuwa akimpenda Selestine kutokana na ugomvi wao wa kila siku uliyokuwa ukitokea.
Alihisi kumchukia sana na ndiyo sababu iliyomfanya abaki kuwa kimya hata pale Selestine alipoanza kuwatambulisha baadhi ya marafiki zake pale darasani.
“Hao wote ndiyo marafiki zangu yani tunashirikiana kwa kila kitu kama ndugu,” alisema Selestine mara baada ya kuwatambulisha baadhi ya marafiki zake wakiume kasoro Andrew.
Utambulisho huo ulimshangaza sana Herieth, alipotazama mule darasani alimuona Andrew akiwa amekaa peke yake huku akionekana kuwa mwenye mawazo sana.
“Mbona yule umemuacha?” aliuliza Herieth huku akimnyooshea kidole Andrew.
Lilikuwa ni swali lililofanya darasa zima liangue kicheko, kila mtu alikuwa akicheka huku wengine wakicheka vicheko vyenye kukejeli ndani yake.
Vicheko hivyo vilizidi kumshangaza sana Herieth, hakujua ni nini kilichokuwa kimetokea mpaka kusababisha darasa zima lianze kucheka. Katika hali ya kushangaza na yeye akajikuta akianza kucheka kwa kufuata mkumbo wa vicheko vya wanafunzi wengine.
“Yani mimi nikajua utaniuliza swali la maana,” alisema Selestine huku akijifanya kuchukizwa na swali lile.
“Kwani kuna nini?” aliuliza Herieth huku macho yake yakiweweseka katika kumtazama Selestine na Andrew, hakujua ni nini kilichokuwa kikiendelea.
“Niulize kuhusu wavulana wenzangu lakini siyo huyo kibisa,” alijibu Selestine jibu lililofanya darasa zima lianze kumzomea Andrew.
Hakukuwa na mwanafunzi aliyekuwa akimpenda, kila mwanafunzi alikuwa akimchukia kutokana na tabia yake ya kutojihusisha na masuala ya wasichana, maisha yake yote ya pale shuleni alikuwa akiishi bila kuwa na mpenzi. Hilo ndilo lilikuwa kosa kubwa alilokuwa amelifanya katika maisha yake. Wanafunzi wenzake walianza kumuhisi kuwa hakuwa ridhiki huku baadhi yao wakisikika wakisema kuwa katika uumbwaji wake alichanganyika na homoni za kike hivyo alikuwa ni shoga.
Jibu la Selestine pamoja na sauti za kumzomea Andrew za wanafunzi zilizidi kumfanya Herieth asielewe ni nini walichokuwa wakikimaanisha. Baada ya kukaa dakika kadhaa katika kulitafakari lile jibu la Selestine ndipo alipoweza kung’amua jibu la haraka la swali lililokuwa likimuumiza kichwa kwa wakati ule ambapo sauti za kuzomeza Andrew ziliendelea kusikika.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ni shoga?” aliuliza Herieth huku akimtazama Selestine ambaye alikuwa akijifanya yupo makini kusikiliza.
“Unanijibu au?” aliuliza Selestine swali ambalo lilikuwa na kejeli ndani yake, alikuwa amedhamiria kumchafua Andrew, aliamini ile ndiyo ilikuwa nafasi yake ya kuuonyesha uanaume wake hasa kwa msichana Herieth ambaye alikuwa ni mwanafunzi mgeni kabisa.
Andrew hakutaka kuendelea kuyavumilia maumivu aliyokuwa akiyapata kwa wakati ule pale darasani, kila kitu kilichokuwa kikiendelea aliamua kubaki kimya, hakutaka kujibu lolote lile hata pale lilipokuja suala la wanafunzi wenzake kuanza kumcheka kwa sababu za kuitwa shoga aliamua kubaki kimya.
Aliamini katika ukimya wake ungeweza kumsaidia kuepukana na ugomvi ambao ungeweza kutokea muda ule ambapo Selestine alikuwa akimchafua kwa kumpa sifa ambazo hazikuwa zake, hakustahili kuambiwa vile.
Aliamua kuondoka darasani kwa ghadhabu huku nyuma akiwaacha wanafunzi wenzake wakiendelea kumcheka. Alijaribu kuyavumilia maumivu aliyokuwa akiyapitia katika moyo wake lakini kuna muda uvumilivu ulimshinda mwisho machozi yakashika hatamu yake, alikuwa akilia kwa uchungu.
Machozi yaliendelea kumdondoka, alikuwa akihisi maumivu makali mno katika moyo wake, kitendo cha kuambiwa na Selestine kuwa alikuwa ni shoga tena mbele ya Herieth msichana ambaye alikuwa ni mgeni pale darasani hakika kilimuumiza sana, alijisikia vibaya mno.
Kwa wakati ule alipoamua kutoka darasani, aliongoza moja kwa moja mpaka ilipokuwa ofisi ya mwalimu wa nidhamu, alikuwa amedhamiria kumshtaki Selestine kwa kitendo kile cha kumdhalilisha darasani kwa kumuita shoga jambo ambalo halikuwa na ukweli ndani yake. Alipofika alibisha hodi kisha akaruhusiwa kuingia, machozi yalikuwa yakiendelea kumbubujika kwa wakati huo.
“Kuna nini mbona unalia?” aliuliza mwalimu huyo wa nidhamu ambaye alijulikana kwa jina moja la Mr. Mwasha.
“Mwalimu…..” aliita Andrew kisha akanyamaza kwa muda, alikuwa akiyafuta machozi yaliyokuwa yakimbubujika kwa wakati huo.
“Niambie kuna nini?” aliuliza Mr. Mwasha.
“Selestine sijui ananitakia nini Mwalimu, kila siku ananitafuta najaribu kuwa mkimya lakini bado anazidi kuniandama,” alisema Andrew.
“Amekufanyaje tena?” aliuliza Mr. Mwasha.
“Ananiita mimi shoga,” alijibu Andrew jibu ambalo lilimshtua sana Mr. Mwasha, alibaki akiwa amekiacha kinywa chake wazi, hakuwa akiamini kile alichokuwa akikisikia kwa wakati huo.
“Ati nini?” aliuliza kana kwamba hakuwa amesikia vizuri na ni hapa ambapo sura yake ilibadilika ghafla! aliingiwa na hasira.
“Ananiita mimi shoga Mwalimu,” alijibu Andrew jibu ambalo lilizidi kumpandisha hasira Mr. Mwasha.
Alikuwa ni Mwalimu wa nidhamu katika shule ile ya sekondari ya Wazalendo lakini mbali na kuwa Mwalimu wa nidhamu pia alikuwa ni Mwalimu wa somo la History (Historia). Alikuwa ni miongoni mwa Walimu ambao walisifika sana kwa kuwa na haiba ya ukali shuleni pale. Wanafunzi wengi sana walikuwa wakimuogopa kutokana na ukali wake huo aliyokuwa nao.
Baada ya Mr. Mwasha kupokea malalamiko yale kutoka kwa Andrew hakutaka kuyafumbia macho hata kidogo, kitu alichoamua kukifanya kwa wakati huo ni kumuita Selestine katika ofisi yake na alipoweza kufika aliamua kumuuliza kuwa kama kweli yale aliyokuwa akiyasikia kutoka kwa Andrew yalikuwa na ukweli wowote. Selestine hakuweza kujibu lolote alibaki kimya ukimya uliyokuwa ukiashiria kukubali yale aliyokuwa akiambiwa kwa wakati ule.
“Nakuuliza wewe Selestine haya aliyoniambia Andrew ni ya kweli?” aliuliza Mr. Mwasha kwa sauti iliyochanganyika na ukali.
“Hapana Mwalimu mimi nilikuwa namtania,” alijitetea Selestine huku sura yake ikionekana kudanganya kabisa. Wakati huo Andrew alikuwa kimya.
“Utani! Utani ndiyo umuite mwenzako shoga?” aliuliza tena Mr. Mwasha huku akiwa ameyatoa macho yake makali.
“Mwali….” alisema Selestine lakini kabla hajamaliza kuzungumza sentensi yake Ghafla! akajikuta akipokea kibao kikali kutoka kwa Mr. Mwasha, kilikuwa ni kabao chakushtukiza.
“Naona unataka kuifanya hii shule ni ya Baba yako mzazi, sasa ngoja nikakuadhibu mbele ya Wanafunzi wenzako halafu ndiyo iwe fundisho kwa wengine,” alisema Mr. Mwasha kisha akaagiza kengele igongwe na Wanafunzi wote wakusanyike mahali pamoja (Assemble).
Hatimaye kengele iliweza kugongwa na Wanafunzi wote wakaweza kukusanyika. Kila Mwanafunzi alionekana kushtushwa na kengele ile ya ghafla! ambayo ilionekana kuwa na tatizo fulani.
Kila Mwanafunzi alitamani kufahamu ni nini ambacho kilikuwa kimetokea kwa wakati huo kwani ndiyo kwanza ilikuwa ni majira ya saa tano za asubuhi. Baadhi ya Wanafunzi wa kidato cha nne walikwisha fahamu nia na madhumuni ya kengele ile, waliamua kubaki kuwa watazamaji wa kile ambacho kilikuwa kinakwenda kutokea muda mfupi. Miongoni mwa hao Wanafunzi wa kidato cha nne, Herieth pia alikuwa ni mmoja wao. Macho yake hayakutulia sehemu moja, alikuwa akitazama huku na kule, alionekana kuwa mgeni wa kila kitu katika mazingira yale.
“Kuna nini jamani?” ilisikika sauti ya Mwanafunzi mmoja wa kike ikiuliza, alionekana kutofahamu lolote lile.
“Hata mimi sijui kuna nini,” alijibu Mwanafunzi mwingine na kusababisha minong’ono kwa wakati huo, kila Mwanafunzi alionekana akisema lake.
****CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya kupita dakika kadhaa, walionekana baadhi ya Walimu wakianza kufika eneo lile walipokuwa wamekusanyika Wanafunzi, kati ya hao Walimu alikuwepo Mwalimu wa nidhamu Mr. Mwasha ambaye mikononi mwake alikuwa ameshikilia viboko huku nyuma yake akifuatwa na wanafunzi wawili.
Zile sauti za minong’ono iliyokuwa ikiendelea kusikika kutoka kwa Wanafunzi Ghafla! zilinyamaza.
Ukimya wa ghafla! ukatawala eneo lile.
Kila Mwanafunzi alionekana kuingiwa na hofu baada ya kumuona Mr. Mwasha huku akifuatwa na Wanafunzi wawili ambapo alikuwa ni Andrew pamoja na Selestine, walifahamu ni kitu gani kilichokuwa kinakwenda kutokea.
Walipofika mbele ya Wanafunzi kama ilivyokuwa kawaida wakapewa heshima na baada ya hapo Mr. Mwasha alianza kuzungumza, wakati huo Andrew na Selestine walikuwa nyuma yake huku wakifuatiwa na baadhi ya walimu wengine.
“Wanafunzi tumewaiteni hapa kutokana na dharura iliyoweza kujitokeza muda huu,” alisema Mr. Mwasha kisha akanyamaza halafu akawa kama anayejaribisha maumivu ya bakora kwa kujichapa mwenyewe katika kiganja chake, haikuchukua muda akaendelea kuzungumza.
“Kati yenu hapa wapo baadhi ya Wanafunzi ambao wanaonekana kuwa wapole sana kwa kuwatazama, wana busara na heshima ambazo huwa napenda sana tena natamani kumuona kila mwanafunzi akiwa hivyo. Miongoni kati ya hao wanafunzi kwa kweli huwezi kuacha kumtaja Andrew. Andrew ni mwanafunzi mtaratibu sana nadhani nyie wenyewe mtakuwa ni mashahidi katika hilo,” alisema Mr. Mwasha maneno yaliyofanya baadhi ya Wanafunzi watokwe na minong’ono ya chinichini.
Aligeuka nyuma na kumtazama Andrew kisha akamuita. Andrew akaanza kuzihesabu hatua zake kumfuata pale alipokuwa amesimama kwa wakati ule. Wanafunzi wote wakamtupia macho na kumtazama, kila mmoja alikuwa akimtazama katika namna yake.
“Mmemuona Andrew?” aliuliza Mr. Mwasha huku akiwa ameuweka mkono wake katika bega la kushoto la Andrew.
“Ndiyoooooo tumemuonaaaaaa,” walijibu Wanafunzi wote kwa pamoja huku sauti za vicheko vikisindiza jibu lao, kila mmoja alikuwa akicheka baada ya kulisikia jina la Andrew.
“Mnacheka nini?” aliuliza Mr. Mwasha huku sura yake ikiwa imebadilika, kitendo hicho kilifanya ukimya mwingine wa ghafla! utawale eneo lile.
“Huwa sipendi kuona Wanafunzi wanaosoma pamoja au hata kama sio kusoma pamoja maadamu nyie ni wanafunzi wa shule hii basi hamna budi kuishi kwa upendo kwani nyie wote ni kitu kimoja. Wote mliyokuwepo hapa mmefuata elimu na hilo ndiyo lengo letu na si vinginevyo. Hakuna ambaye yupo hapa kwa ajili ya kucheza au yupo hapa kwa ajili ya kukua na kama unajijua kuwa upo hapa kwa ajili ya kukua au umekuja kucheza basi jua hapa sio sehemu yako sahihi, utakuwa umekosea njia,” alisema kisha akamtazama Andrew ambaye kwa wakati huo alikuwa ametazama chini kwa kuona aibu ya kuwatazama Wanafunzi wenzake.
“Kuna Mwanafunzi mmoja ambaye anaonekana kuwa tofauti na vitu vyote hivyo ambavyo nimetoka kuvizungumza, anaonekana kuwa mkaindi wa kila kitu, nahisi atakuwa anahitaji sisi Walimu tuweze kumfunza jinsi anavyotakiwa kuishi hapa shuleni na kama Mwalimu wa nidhamu nitahakikisha nalishughulikia hilo mbele yenu ili na wengine wenye tabia kama hizi waziache mara moja,” alisema kisha akamuita Selestine, alipomkaribia alimwambia apige magoti chini.
“Nimesema piga magoti hapo,” alisema kwa ukali kisha Selestine akanya kama alivyoambiwa, alionekana kuwa na hasira za waziwazi.
“Huyu ni miongoni kati ya wale Wanafunzi wenye nidhamu mbovu,” alisema Mr. Mwasha kisha hakutaka kuishia hapo, alianza kusema kosa alilokuwa amelifanya Selestine la kumuita Andrew shoga mpaka kufikia hatua ya kuwakusanya Wanafunzi wote kwa lengo la kutaka kumuadhibu mbele yao ili iwe ni funzo kwa Wanafunzi wengine.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kama ilivyokuwa kawaida yake, hakutaka kuacha maongezi yachukue nafasi kubwa, baada ya kumaliza kulisema kosa alilokuwa amelifanya Selestine adhabu ya viboko vya kwenye makalio kwa kila Mwalimu ilichukua hatamu yake, kila mwalimu aliyekuwepo pale alitakiwa kumuadhibu viboko vitatu vitatu.
Ilikuwa ni moja kati ya adhabu kali sana iliyoweza kumpa maumivu makali Selestine ambaye uvumilivu ulimshinda kwa wakati huo, alikuwa akilia kama mtoto mdogo, machozi yaliyokuwa yakimdondoka yaliweza kuthibitisha maumivu aliyokuwa akiyapata kwa wakati huo.
Lilikuwa ni tukio la dakika kadhaa na baada ya kuadhibiwa alipewa adhabu nyingine ya mwisho. Alipewa adhabu ya kuchimba shimo la taka huku akitakiwa kumuomba msamaha Andrew kwa kosa alilokuwa amemfanyia la kumuita shoga.
Selestine alifanya kama alivyoambiwa, aliamua kumuomba msamaha Andrew na kuahidi kutorudia wakati huo machozi yalikuwa yakimbubujika. Andrew aliweza kumsamehe na baada ya hapo Wanafunzi waliruhusiwa kurudi katika madarasa yao.
****
Aliianza adhabu yake ya kuchimba shimo la taka kama alivyoambiwa, adhabu ambayo hakuipenda hata kidogo, alihisi kuonewa. Moyo wake ulikuwa umehifadhi chuki kwa wakati huo, alikuwa akimchukia Andrew kupita kawaida.
“Yani huyu shoga amefanya mpaka nimepewa adhabu ya kuchimba shimo la taka na ngoja nitamuonyesha,” alisema Selestine wakati alipokuwa ameanza kuchimba shimo la taka, alionekana kuwa mwenye hasira kali mno. Hakutaka maumivu yale aliyokuwa ameyapata yabaki kuwa yake peke yake, alipanga kumlipitizia Andrew mmoja kati ya Wanafunzi wenzake aliyokuwa akiwachukia sana.
Alichokuwa akikifikiria kwa wakati huo ni kulipiza maumivu aliyokuwa ameyapata, hakutaka kesi ile iishie katika kuchimba shimo la taka kama adhabu aliyopewa na na Mwalimu wa nidhamu. Alipanga kumlipizia Andrew maumivu aliyokuwa ameyapata.
“Hivi kweli mimi ni wa kuchimba shimo la taka?” alijiuliza swali lililomfanya atokwe na tusilililomlenga Andrew.
Aliwakumbuka wale wasichana aliyokuwa akitembea nao pale shuleni, alihisi kudhalilishwa sana hasa kwa kitendo cha kuadhibiwa mbele ya umati wa Wanafunzi na kisha kupewa adhabu ya kuchimba shimo la taka.
“Dah! Aisee huyu shoga amekuweza kweli yani…,” ilisikika sauti ya mwanafunzi mmoja wa kiume ikisema ambaye aliamua kumfuata Selestine pale alipokuwa akiitumikia adhabu yake, alionekana kuwa mbeya kwa kumtazama lakini kabla hajamaliza kutamka sentensi yake mara Selestine aliweza kumkata kauli.
“We ngedere embu toka hapa nisije nikakuchimba sasa hivi,” alisema Selestine huku akitokwa na tusi la nguoni.
Yule mwanafunzi aliamua kuondoka mahali pale, alimfahamu vizuri Selestine pamoja na utukutu wake, aliamua kuepusha shari.
****
Baada ya kupita wiki moja tangu Andrew na Selestine walipoweza kuingia katika mgogoro. Andrew aliamua kusamehe kila kitu kilichokuwa kimetokea, hakutaka moyo wake uendelee kuifadhi chuki kwa Selestine, alimchukulia kuwa kama rafiki yake na ni katika kipindi hicho ambapo waliweza kufanya test katika masomo yao.
Mitihani iliporudishwa Andrew aliweza kuongoza kama ilivyokuwa kawaida yake, alikuwa amefanya vizuri katika masomo yake Sayansi.
“Mambo Andrew,” alisema Herieth huku akimtazama Andrew ambaye alionekana kutetemeka, alikuwa akiogopa kuzungumza. Wakati huo ulikuwa ni muda wa mapumziko.
“Poa tu,” alijibu Andrew.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hongera, kumbe unaakili nyingi kiasi hicho?” aliuliza Herieth.
“Hapana mbona kawaida.”
“Mmmh! Mimi mwenzako nilikimbia sayansi maana naiona ni ngumu sana bora masomo yangu ya biashara hayatumii akili nyingi.”
“Asante,” alijibu Andrew huku akiweweseka, hakujua ni neno gani lingine alitakiwa kulisema kwa wakati ule, alikuwa akimpenda sana katika moyo wake japo hakuwahi kumwambia, alibaki na siri yake moyoni.
Kitendo cha Herieth kumfuata na kuzungumza naye tena kwa mara ya kwanza hakutaka kuamini kabisa, alihisi wenda alikuwa katika usingizi wa ndoto na muda wowote angeweza kuamka.
Aliikumbuka ile siku ambayo aliitwa shoga darasani tena mbele ya Herieth. Kumbukumbu hiyo hakika ilimtesa sana, hakujua msichana huyo alimchukulia vipi.
Katika mawazo yake akahisi Herieth tayari ameshakuwa mpenzi wake, akatengeneza tukio wakiwa wanazungumza.
“Andrew kwanini wanakuita Shoga?” aliuliza Herieth huku uso wake ukiachia tabasamu mwanana.
“Sijui kwanini ila nadhani watakuwa wananionea wivu kwa sababu kila siku naongoza darasani,” aljibu Andrew.
“Sipendi wanavyokuita.”
“Usijali kuna siku hutowasikia tena wakiniita hivyo.”
“Siku gani?”
“Siku tutakapomaliza shule.”
“Nakupenda Andrew.”
“Nakupenda pia Herieth,” alijibu Andrew kisha akamsogelea Herieth kwa lengo la kutaka kumkumbatia Herieth lakini ghafla! kwa mbali akaisikia sauti ya mtu akiwa anamuita huku akimgusa begani.
“We boya muda wa darasani huu au huisikii kengele?” sauti ya mwanafunzi mmoja wa kiume ndiyo iliyoweza kumtoa katika dimbwi la mawazo, wakati huo alikuwa akitaka kuukumbatia mti. Alipotazama hakumuona Herieth, alikuwa ameshaondoka kuelekea darasani.
****
“Huyu shoga nahisi hanijui vizuri akili zangu, nitamuonyesha,” alisema Selestine.
“Achana naye bana,” alisema Derick rafiki mkubwa wa Selestine pale shuleni.
“Siwezi kufanya huo ujinga hata mara moja.”
“Sasa unahisi utamfanya nini wakati kama kuchapwa umechapwa na adhabu umepewa.”
“Nitajua nitakachomfanya.”
“Halafu leo nilimuona akiongea na Herieth.”
“Saa ngapi?”
“Saa nne muda ule wa mapumziko.”
“Unasemaje?”
“Nimeona akiongea na Herieth sasa sijui walikuwa wakiongea nini ila kuna muda nilimuona Herieth akiwa anacheka.
“Kweli?”
“Sasa mimi nikutanie ili iwaje?”
“Haiwezekani.”
“Haiwezekani nini sasa.”
“Yule ni demu wangu mimi.”
“Demu wako?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ndiyo yule ni demu wangu sasa anataka kuniharibia shoga huyu,” alisema Selestine kwa ukali.
Hakutaka kuamini kile alichokuwa akiambiwa na Derick kwa wakati ule, alizidi kuchanganyikiwa hasa pale aliambiwa kuwa Herieth alikuwa akicheka na Andrew.
Moyo wake uliingiwa na wivu mno, alikuwa akimpenda Herieth, aliamini kwa vyovyote vile lazima angeweza kumpata msichana huyo kutokana na muonekano wake aliyokuwa nao, kila siku wasichana hawakuisha kujigonga kwake, aliutumia muonekano wake pamoja na utukutu wake katika kutembea na wasichana tofautitofauti pale shuleni.
Mpaka kufikia wakati huo Andrew alikuwa amemzidi vitu viwili ambavyo yeye hakuwa navyo. Kitu cha kwanza ilikuwa matokeo ya test walizofanya ambapo yeye aliweza kufeli kwa kupata alama za chini kabisa na kitu cha pili ni ukaribu uliyoanza ghafla! kati ya Andrew na Herieth. Hakutaka kuamini kama kweli shoga angeweza kuwa na hisia za kimapenzi kwa mwanamke, hilo lilizidi kumshangaza sana.
“No, haiwezekani,” alisema Selestine.
Andrew moyo wake ulizidi kumuuma sana, kila alipokuwa akimfikiria Herieth alihisi kumpenda kupita kawaida. Alichokuwa akiamini kwa wakati huo ni mapenzi ya dhati aliyokuwa nayo kwa msichana huyo ambaye hakuwahi kumwambia ukweli wowote kuhusu hisia hizo. Zilibaki kuwa hisia zilizokuwa zikimuumiza tu! hakujua ni kwa namna gani alitakiwa kuwasilisha hisia zake kwa msichana huyo.
Mawazo kutwa kucha yalikuwa kwa Herieth mpaka ikafikia kipindi akawa hapati usingizi, kila alipojaribu kufanya hivyo alijikuta akiambulia usingizi wa maruweruwe, taswira ya Herieth ilikuwa inamjia kila wakati. Aliamua kwenda sebuleni kwa lengo la kujisomea usiku huo lakini kila alipojaribu kujisomea kwa umakini hakuweza kuambulia lolote, mawazo bado yalikuwa kwa Herieth.
“Andrew mwanangu mbona mpaka sasa hivi bado hujalala?” aliuliza Mama yake baada ya kumkuta sebuleni akiwa na vitabu vyake.
“Mamaa najisomea tu!” alijibu Andrew huku akijifanya kuwa bize na vitabu vyake.
“Hapana hata kama ni kujisomea kuna muda wake embu nenda kalale mwanangu sawa,” alisema Mama yake kisha Andrew akafanya kama alivyoambiwa.
Alipoingia chumbani kwake na kuanza kuutafuta usingizi kwa mara nyingine bado taswira ya Herieth ilizidi kumjia, alikuwa akitabasamu kila wakati alipokuwa akimkumbuka.
“Nakupenda Herieth,” alijisemea kimoyomoyo huku tabasamu likizidi kushika hatamu katika uso wake. Hatimaye usingizi uliweza kumpitia.
****
Siku iliyofuata aliweza kuamka kama ilivyokuwa kawaida yake, alijiandaa, akanywa chai kisha akaanza kuelekea shuleni. Barabarani aliendelea kumfikiria Herieth, kuna kipindi alipokuwa akipishana na baadhi ya wasichana aliwafananisha na Herieth lakini hayo yote yalibaki kuwa mawazo tena mawazo yasiyowezekana kutokea katika maisha ya kawaida.
“Kwanini moyo wangu unakupenda hivi?” alijiuliza alipokuwa kwenye daladala lakini hakuweza kupata jibu lolote lile.
Kwa umri wake wa miaka kumi na nane alihisi tayari ameshakuwa mtu mzima ambaye alitakiwa kuwa na uhuru katika kufanya maamuzi hasa katika suala zima la kimahusiano lakini alihisi kushindwa kufanya hivyo kutokana na maumivu aliyokuwa akiyapata kutoka kwa msichana huyo ambaye bado hakuzungumza naye lolote.
“Wewe dogo embu simama vizuri hapo unasimama kama mjamzito bhana,” sauti ya kondakta ilisikika ikisema huku akionekana kuwa kama mwenye hasira lakini Andrew hakutaka kujali lolote, alichoamua kufanya ni kusimama vizuri kama alivyoambiwa.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kwanini unanipenda?” alihisi kuulizwa swali na Herieth lakini yalikuwa ni mawazo, hakukuwa na ukweli katika hilo.
****
Selestine bado aliendelea kuhifadhi chuki kwa Andrew, alikuwa akimchukia sana. Kila alipokuwa akimfikiria alikuwa akiona mabaya ambayo alitakiwa kumfanyia.
Aliwaza kumchafua kwa kumtangaza kuwa alikuwa ni shoga shule nzima lakini alihisi kufanikiwa katika hilo, kuna kipindi alipanga kumpiga mpaka amjeruhi sehemu yoyote ya mwili wake ili aache kumuingilia katika anga zake, hilo aliweza kukubaliana nalo kabisa. Alichokuwa amepanga kufanya kwa wakati huo ni kuhakikisha anampiga Andrew mpaka anamjeruwi sehemu moja wapo ya kiungo cha mwili wake, alikuwa amedhamiria.
“Lazima nimuonyeshe kuwa hapa ndiyo mjini,” alisema Selestine huku akionekana kujisifia kumpata Herieth.
“Sasa utamfanya nini?” aliuliza Derick.
“Dawa yake ni kumipiga mpaka namtoa alama kwenye mwili wake ili aache kuwa karibu na Herieth kwanza yule sio levo yake,” alisema Selestine huku akionekana mapenzi yakiwa yanamuendesha.
Alikuwa akimpenda Herieth japo alikuwa akijaribu kutumia ubabe lakini kwa mtazamo wa haraka haraka alionekana kumpenda msichana huyo. Ilikuwa ni kazi rahisi kumfuata Herieth na kumwambia ukweli kuwa alikuwa akimpenda lakini kwa upande mwingine ilikuwa ni ngumu kwani msichana huyo alionekana kuwa mrembo sana. Uzuri aliyojaaliwa Herieth ulizidi kumchanganya kila kukicha. Alianza kuwapiga chini baadhi wasichana aliyokuwa akitembea nao pale shuleni, hakutaka tena kuwa katika mahusiano nao.
“Kwani kuna nini nimekukosea?” aliuliza Magreth mwanafunzi wa kidato cha tatu aliyekuwa na mahusiano na Selestine.
“Hakuna kitu ila nimeamua huu ndiyo uwe mwisho wetu,” alisema Selestine huku akionekana kumaanisha kila neno alilokuwa akilitamka.
“Au umepata msichana mwingine ndiyo maana unaamua kuniacha?”aliuliza Magreth.
“Kwanini hutaki kunielewa nimesema naomba tuachane.”
“Baby kumbuka lakini nakupenda.”
“Yes! I know so?” (Ndiyo najua kwahiyo?)
“Usiniache basi mimi bado nakupenda sana.”
“Natumia lugha ya Kiswahili lakini nimesema naomba tuachane sikutaki,” alisema Selestine kwa sauti ya ukali.
“Sawa nashukuru,” alijibu Magreth kwa unyonge kisha akaondoka.
Huo ndiyo ulikuwa mwanzo na mwisho wa mapenzi yao, Selestine hakutaka kuona anakuwa na mahusiano na msichana mwingine shuleni zaidi ya Herieth, alihisi kumpenda mpaka akawa hajielewi. Mapenzi yalikuwa yakimuendesha kupita kawaida.
Baada ya kufanikiwa kuwaacha wasichana wake wote aliyokuwa akitembea nao sasa kazi kubwa iliyokuwa imebakia ni kuhakikisha anafanikiwa kumpata Herieth.
Kila alichokuwa akikifanya alihisi yupo sahihi kukifanya wala hakuhitaji muda wa kutaka kufikiri lolote kabla ya kuchukua maamuzi. Hata lilipokuja suala la kuwaacha wasichana aliyokuwa akitembea nao pale shuleni hakujali lolote, aliamini yupo sahihi kufanya hivyo wala hakujali maumivu aliyowaacha nayo.
“Umemfanya nini Magreth mbona analia?” aliuliza Derick.
“Achana nae mpumbavu huyo,” alijibu Selestine.
“Kwanini kuna nini kimetokea?”
“Nimemzingua.”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kisa nini?”
“Basi tu.”
“Hivi una akili wewe.”
“Ndiyo ninazo.”
“Sasa mtoto wa watu amekufanya nini?”
“Demu mwenyewe hata sio mzuri hata kidogo yupoyupo tu.”
“Sasa hiyo ndiyo sababu mpaka umzingue?”
“Embu tuache hiyo mada.”
“Kwahiyo hana umuhimu tena.”
“Nimesema tuache hiyo mada,” alisema Selestine.
Hakutaka tena kusikia habari kuhusu Magreth wala msichana mwingine yoyote pale shuleni zaidi ya Herieth. Alijikuta akizidi kuongeza mapenzi kila siku kwa msichana huyo ambaye alikuwa mrembo sana.
Alichoamua kukifanya ni kumfuata Herieth na kumueleza ukweli kuwa alikuwa akimpenda sana na hivyo alitaka wawe wapenzi. Lilikuwa ni jambo gumu mno hasa kumfuata msichana mrembo kama Herieth na kumueleza ukweli wa maneno hayo ambayo aliamini kwa asilimia zote angeweza kukubaliwa.
“Unasemaje?” aliuliza Herieth baada ya Selestine kumwambia kila kitu kuhusu hisia za moyo wake.
“Nakupenda sana Herieth naomba unielewe,” alisema Selestine huku akionekana kama anayelazimisha kitu.
“Umenipendea nini?”
“Jinsi ulivyo tu! nataka kuwa mpenzi wako naomba unikubalie.”
“Hivi unadhani itawezekana kirahisi hivyo?”
“Kwanini?”
“Siwezi kukuamini nitajuaje kama unanidanganya.”
“Wewe nikubalie utajua kama nakutania au lah!”
“Nyie wanaume ni waongo sana.”
“Kumbuka lakini hapa huzungumzi na wanaume bali unazungumza na mimi peke yangu.”
“Hata kama lakini nyie waongo sana.”
“Naomba uniamini basi nakupenda sana, umetokea kuziteka hisia zangu.”
“Mmh!”
“Nini?”
“Naomba unipe muda nifikirie.”
“Nikupe muda mpaka lini Herieth.”
“Wewe nipe muda tu!” alisema Herieth.
Selestine hakutaka maongezi yaishie pale, aliamua pia kuitumia nafasi ile katika kumchafua Andrew, hakutaka kumuona akiwa karibu na msichana huyo ambaye tayari alikuwa ameshampenda hivyo kila maneno aliyokuwa akiyazungumza alikuwa akizungumza mabaya kuhusu Andrew.
“Mimi nakushangaa sana unavyojipendekeza kwa mtu kama yule kwanza shule nzima hii kila mwanafunzi anamfahamu kuwa ni shoga,” alisema Selestine huku akijaribu kutilia mkazo sentensi yake ambayo haikuwa na ukweli wowote ule.
“Mbona anaonekana kuwa sawa lakini?” aliuliza Herieth huku akionekana kama kutoamini kile alichokuwa akiambiwa.
“Sisi ndiyo tunamfahamu, wewe umehamia juzi tu huwezikufahamu lolote kuhusu yeye embu tuulize sisi tunaomfahamu.”
“Wewe unamfahamu?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kila siku anaonekana anakwenda kulala na wanaume gesti, sasa hapo unataka niseme nini, jamaa jogoo hapandi mtungi yule,” alisema Selestine maneno yaliyozidi kumpigilia msumari wa kumuaminisha Herieth.
Kuna muda Herieth hakutaka kuamini kile alichokuwa akiambiwa, maneno ya Selestine yalizidi kumuingia vilivyo na sasa akaanza kuamini kuwa Andrew alikuwa ni shoga. Hilo alianza kuliamini kabisa na sasa hata ule ukaribu ambao alikuwa tayari ameuanza kuuonyesha kwa Andrew alianza kuupunguza, alihisi kumchukia sana Andrew hasa kutokana na tabia zake na ushoga ambazo alikuwa akiambiwa, hakupenda kuwa karibu na mwanaume wa aina hiyo hivyo kitendo cha kumuona Andrew kila mara darasani hakika kilimtesa sana.
****
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment