Simulizi : Usilie Nadia
Sehemu Ya Tatu (3)
Huyu avae ya huyu mara huyu avae ya huyu. Hapakuwa na moja, huenda hicho kitu ndio kilisababisha hata tukashindwa kuelewana, mtu mmoja akavaa nguo yangu nilipomshika akanitukana akidai mimi ni kichaa.
Umoja ukajengeka, wakamuunga mkono kuwa mimi ni kichaa na sijui ninachokiongea, wengine wakaenda mbali zaidi na kusema kuwa ni mimi nimewazulia balaa lile la aina yake.
Mara nikatengwa maneno yakawa maneno!! Mara nisukumwe mara nitukanwe!!
Ile nguo aliyoing’ang’ania yule dada ndio nguo ambayo ilikuwa ndani yake nimeishonea ile pesa yangu niliyomuibia bosi Mwanza….na niliamini kuwa lazima itakuwemo, nilishona kwa ustadi mkubwa sana.
Ni heri ningekaa kimya tu nisijibizane na umati…..ni heri ningekubaliana na usemi wa mwenye nguvu ndo mwsenye haki.
Nilikosea sana kuthubutu kuongea….nilikosea sana kuidai haki yangu……”
Nadia alivuta pumzi kidogo kisha akanitazama….
“Mwandishi, hivi wanadamu wana roho za aina gani? Yaani watendwe na watu wengine halafu hasira zao wamalizie kwangu….ama hakika walipata pa kupoozea hasira zao. Alianza kijana mmoja kulaumu kuwa mimi ndiye nilikuwa chanzo cha mikosi. Mara mwingine akaunga mkono. Wakaanza kunizonga zonga hapo nikiwa sina walau nguo moja mwilini. Nikajaribu kujihami, hapo nikiwa nawaza kitu kimoja tu kuipata nguo yangu, hasahasa ile blauzi yenye pesa zangu ambazo nilipanga kuzitumia katika mchakato mzima wa hapo Musoma mjini nilipokuwa naelekea.
Nilijaribu kumkaba yule msichana aweze kunipatia blauzi yangu, kweli nilifanikiwa kumwangusha chini, sasa nikawa juu yake nikifanya jitihada za kuiondoa nguo.
Mara nikasikia sauti moja ikidai kuwa mimi ni kichaa na nikiachwa naweza kumuua yule binti, hapo sasa kundi la watu shupavu likanivamia. Nilipojifanya mkomavu sana nikaanza kupokea kichapo huku nikiwa uchi wa mnyama. Nilijaribu kujitetea lakini sauti yangu moja haikuwa chochote kwenye umati ule. Nikasukumiwa kichakani, huko napo kipigo kikaendelea, hatimaye sauti haikutoka tena, nikabaki kutazama tu jinsi walimwengu walivyoamua kuikatisha safari yangu hapa duniani katika namna ya kipekee.
Ninakufa nikiwa sijapata haki yangu!!
Iliniuma sana!!
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilichoweza kukiona kwa uhakika wakati jicho langu likiwa na uhai bado ni mwanaume akija mbio huku akiwa amenyanyua kitu mfano wa jiwe juu juu. Nilifanikiwa kupiga kelele lakini sijui kama ile kelele niliisikia mimi peke yangu ama kila mmoja aliweza kuiskia. Na kama waliisikia mbona wasinisaidie.
Nilipofumba macho kukwepa kumtazama yule mtu, sikuyafumbua tena hadi nilipojikuta mikononi mwa mzee mwenye ndevu nyingi anayezungumza Kiswahili kwa shida sana.
Watoto wake hawakuweza kabisa kuzungumza Kiswahili.
Kitu cha kwanza baada ya fahamu kunirejea ni kuutazama mguu wangu, mguu ambao niliusikia ukiwa mzito sana na sikuweza kuunyanyua.
“Porepore..porepore mona wane.” Aliyasema maneno haya katika lafudhi ambayo nilikuwa naifahamu, lafudhi ya kikurya.
Nilipojitazama, mguu ulikuwa umeunganishwa na vifaa visivyokuwa vya kitaalamu sana. Na hogo lililofungwa lilikuwa limechafuka sana.
“Mama Marwaa uuuuuuh!!” aliita yule mzee, akaitikiwa na sauti ya kike kutoka mbali kiasi fulani. Kisha baada ya sekunde kadhaa akafika mwanamke imara kabisa mbele yangu.
Wakaanza kuongea kikabila!!
Sikujua nini wana maanisha!!
Lakini baadaye mzee yule aliyejitambulisha kwangu kama Marwa kwa kulazimisha Kiswahili alinisimulia jinsi nilivyookotwa hali yangu ikiwa mbaya sana wakidhani nimekufa.
Katika kusimuliwa ndipo nikaikumbuka taswira niliyoiona mara ya mwisho kabla ya kuzimia. Kumbe yule mtu aliniponda na jiwe katika ugoko wa mguu wangu na hapo nikapoteza fahamu huku nikiuacha mguu ukivunjika.
Mzee Marwa katika kuchunga mifugo yake ndipo akakutana na mwili wangu ukiwa katika hali mbaya, lakini akabaini kuwa bado nilikuwa napumua. Hakuweza kujua nilikaa pale kwa siku ngapi nami pia sikujua lolote kwa sababu sikumbuki ilikuwa siku gani niliyozimia.
Nikayaanza maisha mapya katika familia ya mzee Marwa.
Mwandishi kuna watu wana maisha magumu sana. Wanaishi bila kuijua kesho yao lakini bado wanapata nafasi ya kuonyesha upendo wao wa dhati.
Sijui kwa nini familia ya akina Desmund haikupewa mioyo ya aina ile maana ni kama walilaaniwa wale binadamu. Mwanzoni nilidhani labda ni kila mtu katika kabila lao alikuwa na tabia kama zile lakini sasa nilikuwa nayapata majibu kuwa sikuwa sahihi hata kidogo. Tabia ya mtu hutegemea na mtu mwenyewe na wala sio kabila lake.
Mwandishi, nikikuambia kuwa zamani nilikuwa nakula sana basi huu ulikuwa mwisho, asubuhi tulitazamana tu na kama ikitokea bahati tunapata uji usiokuwa na sukari nilisikia wakiuita ‘litaghata’, mchana tulikula ugali wa mtama, na usiku tulikula ama usiku ulipita hivyo hivyo, nilihangaika sana kuizoea hali ile lakini sikuwa na pa kulalamika, mguu wangu ulikuwa mbovu.
Niliishi pale kwa miezi mine ya mateso, lakini afadhali mateso yale nilikuwa nimeyazoea, baada ya muda fulani nikiwa ninatembea vyema japo nilichechemea kidogo alikuja mtoto wa mzee Marwa, alikuwa ametokea mjini Musoma ambapo alikuwa anasoma. Nilimtambua kwa jina la Mwita japo alipenda sana kujiita ama kuitwa David. Aliichukia asili yake na hakupenda kuzungumza kabila lake, mara zote alipoongeleshwa kikabila alijibu Kiswahili. Elimu yake ilikuwa imemfanya mtumwa wa mambo ya kizungu. Kuingia kwa Mwita kukaanza kunikosesha amani kutokana na tabia zake za kupenda kunitazama kwa macho fulani yaliyoonyesha matamanio, na mara nyingine alikuwa akinikonyeza. Nilimkanya kuwa sitaki hicho anachokitaka lakini hakutaka kujirekebisha, nilitamani kumshtaki kwa baba na mama yake lakini niliona kuwa haina haja mimi ni wa kupita tu pale.
Wakati huo nilikuwa naweza kuhudhuria shambani na kulima kwa bidii. Iliniwia ngumu sana kuamini kuwa Desmund na penzi lake haramu wameniharibia maisha yangu kiasi kile.
Lakini yote sikutaka yaendelee kujikita katika kichwa change nikaacha maisha yaendelee.
Ulipotokea msiba, mzee Marwa na mkewe wakahudhuria ni hapa nilipoianza safari nyingine ya kuhaha kuitafuta amani bila kusahau haki yangu.
Nyumbani tulibaki mimi, Mwita na watoto wengine wawili wadogo. Majira ya saa tatu usiku Mwita anayejiita David alinifuata katika nyumba ya majani ambayo nilikuwa naishi kwa wakati huo.
Hapakuwa na umeme katika mji ule wala majirani hivyo kiza kilikuwa kimetanda haswa.
Mwita alikuwa peke yake mwanzoni. Alianza kunieleza mambo ambayo ninayaita ya kipuuzi, alilalamika kuwa kulikuwa na baridi sana, sikumjibu niliendelea na shughuli yangu ya kushona nguo yangu iliyokuwa imechanika.
Aliongea mengi lakini nilimweleza kuwa sipo tayari kwa jambo lolote lilena iwapo akiendelea kunilazimisha nitamshitaki kwa baba yake.
Huenda jibu hili lilimkera sana Mwita, akaondoka na kisha baada ya nusu saa hivi akarejea akiwa na kikundi cha wanaume wanne wote walikuwa wanaongea kikabila na sikuweza kuwaelewa walichomaanisha.
“We demu unajifanya mjanja sio.” Alinikoromea kijana mmoja, lafudhi yake ikifanana kabisa na ile ya Desmund kabla hajajanjaruka.
Niliwatazama sikusema neno, wakasemezana kikabila tena. Mara mmoja wao akanishika mkono nakutaka kuninyanyua. Mwandishi wale watu wana nguvu balaa!! Nilijaribu kujitoa lakini haikuwezekana, wakaanza kunivuta kuelekea walipojua wao. Giza lilikuwa limetanda haswa. Niliendelea kupambana lakini hali haikuwa shwari. Hatari mbele yangu.
“Mwita nipo katika siku zangu!!!” nilimlilia yeye ambaye nilikuwa nikimfahamu kwa jina, lakini hakutaka kunisikiliza alikuwa amekasirika.
“Acha ujanja wa kizamani we demu, mbona hukusema mapema.” Alinikaripia kijana mwingine.
Sasa tulikuwa tumekifikia kichaka fulani, wakanisukuma huku na kule, wakafanikiwa kuitoa kanga yangu.
Nikaiona dalili ya kubakwa. Sikuwa tayari kwa jambo lile. Nikafurukuta hukuna kule lakini ushindi ulikuwa upande wao.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Haya nimekubali naomba nilale mimi mwenyewe.” Niliwasihi, wakanielewa. Nikajilaza chali, wakaitoa nguo yangu ya mwisho.
Hakika nilikuwa katika siku zangu na ndio kwanza nilikuwa nimeanza, lakini wale vijana walionekana mshipa unaosaidia kuona kinyaa kwao haukuwepo. Hawakujali ile damu!!!
Mwita akajiteua kuwa wa kwanza. Mimi nilikuwa nikiombea wafanye kosa lolote niweze kutimua mbio. Lakini wakati huo huo nikajiuliza iwapo nitakimbia ni wapi naelekea sasa, kulikuwa na giza nene sana.
Mwita akaondoa nguo zake na kunivamia pale chini tayari kwa kuniingilia kimwili.
Wakafanya kosa!!
Kosa ambalo walipaswa kujutiana hawakuupata muda huo wa kujutia.
Kijana mmoja aliyekuwa ameshika panga kali kabisa alilichomeka chini. Akaanza naye kuvua nguo zake ili zamu yake ikifika imkute akiwa tayari tayari.
Hilo likawa kosa ambalo nililisubiri bila kujua kama litatokea.
Mwita alikuwa amejiweka kimjini mjini na hakuwa shupavu kama wenzake. Hata mimi kukaa kwangu kijijini kwa muda mfupi niliweza kumuhimili. Alipokuwa juu ya kifua changu akitaka kunibaka, nilimuhesabia mara tano tu kuwa atakuwa katika ulimwengu mwingine.
Kweli nikahesabu kisha kwa nguvu zangu na kujitetea kwangu kwa mara ya mwisho, chuki ikinitawala juu ya wanaume, nilimrusha mbali nami, kisha upesi nikasimama na kukimbilia lile panga, nikalitia mkononi.
Nikashukuru kwa sababu nilikuwa mzoefu tayari katika kukata kuni kila kukicha hivyo nililimudu panga.
Nikaanza na yule aliyekuwa uchi nikamfyeka mgongoni akaangukia pembeni huku akipiga yowe kikabila, nikamrukia Mwita, sikutarajia kama nitamkata shingoni lakini panga lile kali lilitua shingoni.
Mwita hakupiga kelele, kijana mmoja aliyebakia akawahi kutimua mbio. nami nikatimua mbio baada ya kuikwapua kanga yangu , panga mkononi, mbio kuelekea popote penye njia.
Kwa sababu nilikuwa nakuja kukata kuni mara kwa mara nilijikuta naizoea njia!!!
Nilijua tayari nimezua balaa na sitakiwi tena hapo kijijini.
Nikaendelea kukimbia hadi nilipoifikia barabara ya lami…..
Lami ya kuelekea Musoma!!!
Musoma kwa akina Desmund.
Nilikuwa na panga langu bado kwa ajili ya kukabiliana na hatari yoyote usiku ule.
Mvua kali ilinikuta barabarani!! Nikiwa sijui lolote la kufanya kujiepusha na balaa ambalo lilikuwa linanikabili.
Mvua ilinipiga, nikaanza kujiuliza kuwa mimi nanyeshewa, Desmund aliyenidhulumu mali zangu na kisha kuupondaponda moyo wangu alikuwa amelala ndani, amemkumbatia mkewe na wamejifunika blangeti….tena bila shaka walikuwa wameahidiana kuamshana asubuhi wawahi kazini.
Kazi ambayo ni jasho langu mimi Nadia, nikapandwa na hasira kisha hapo nikaikumbuka simulizi marehemu Jadida baada ya kuja Musoma katika kunisaidia kudai haki yangu!!!
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nikakumbuka jinsi Jadida alivyoyumbishwa na kuambiwa kuwa mimi nilikuwa msichana wao wa kazi na waliniokota nikiwa chokoraa mjini Mwanza familia yangu ikiwa ina maisha magumu sana. Hapo tu alipoelezea kuwa alikuwa ni dada yangu na alikuja kudai mali zangu walau nusu tu!!
Jadida akajazwa mneno kuwa nilipokuwa msichana wao wa kazi nilipata mimba na nilipojaribu kuitoa nikapata kichaa cha mimba!! Wazimu wangu ukazua utata baada ya kuanza kuwapiga watoto mtaani. Nikawa nusu siku nakuwa mzima na nusu nyingine nakuwa na wazimu!! Polisi walipotaka kuniweka ndani ndipo wakanirudisha nyumbani kwetu Mwanza. Huko wakaikuta familia yangu yote ikiwa imetekete kwa ugonjwa hatari wa kipindupindu. Kabla hawajajua nini cha kufanya nikapandwa na wazimu na kuanza kufanya vurugu kisha nikakimbia na kutoweka. Kama hiyo haitoshi wakamueleza Jadida kuwa yeye sio wa kwanza kudanganywa na mimi juu ya mali zile kuwa nahusika nazo.
Mwandishi!! Kwa maelezo yale Jadida akaanza kuamini kuwa huenda kuna ukweli kwani mwanamke aliyemkuta hapo nyumbani alikuwa mama haswaa mwenye heshima zake. Na alipokuaja Desmund mwenyewe ambaye ni baba mwenye nyumba ndipo Jadida alizidi kunywea, Desmund hakuonekana kuwa mwanaume wa ajabu kama nilivyomzungumzia mimi kwa Jadida hapo kabla, Jadida akabakiza imani kidogo sana kwangu na kuamini kuwa huenda nilikuwa na wazimu kweli.
Lakini alipokutana na kimbembe cha kukamatwa ghafla na polisi wakati akitaka kutoka katika nyumba ya Desmund ndipo akili yake ikafunguka kuwa maneno aliyoambiwa yote ni uongo na kuna kila dalili ya dhuluma imefanywa na Desmund na mkewe. Jadida akawekwa mahabusu kwa siku tano kwa kosa la kutaka kufanya utapeli, baadaye akaachiwa huru.
Jadida akatumia ujanja wa mjini kuwaweka sawa makondakta wakampakia katika gari kuja jijini Mwanza. Jadida alikuwa na hasira sana, huenda hata ni hasira hizi zilimuua, Jadida akaamua kujiingiza katika umalaya uliokubuhu kuliko ule w awali ilimradi aweze kuzisaka pesa nyingi kisha aandamane nami mjini Musoma katika kudai haki yangu. Lakini haikuwa kama tulivyopanga!! Jadida akabakwa na kuuwawa katika nyumba ya kulala wageni!!!
Nilichoamini hadi dakika ile ni kwamba Jadida aliniachia kitu kimoja kikuu na muhimu. Jadida aliniachia roho yake!! Nilibadilika na kuwa jasiri sana!! Hakuna nilichokuwa nahofia.
Sasa ni kiza kinene na nilikuwa nipo peke yangu katika eneo tata, panga langu mkononi. Mvua kali ikiwa imenipiga na kunifanya nitetemeke haswa.
Kuendelea kunyeshewa nikiwa nimekaa sehemu moja niliona si jambo sahihi, nikikumbuka kuwa nimefanya balaa kwa kutumia panga huko nilipotoka. Nikaanza kutembea kuelekea nisipopajua lakini nikiifuata lami, nilitembea bila kuchoka, mvua nayo iliendelea kunimwagikia. Kadri nilivyojihakikishia kuwa ile sio ndoto bali nipo katika maisha halisi nikazidi kumwona Desmund kama mnyama hatari asiyestahili kuishi tena.
Nilitembea sana hadi nikafikia sehemu nikakutana na vibao vinavyoelezea juu ya njia ya kwenda Tarime, Sirari ….na kibao kingine kilionyesha mahali nilipokuwa napahitaji. Musoma!!!
Hii sehemu niliikumbuka vyema kabisa, ni huku alikuwa akiishi mama yake Desmund!!
Walipaita Makutano, haswaa nilikuwa sijakosea hata kidogo.
Wazo la kwenda Musoma likaishia pale kwa muda kwa sababu hata ningeendelea bado nilikuwa sijaweka mikakati yangu vizuri. Nikaamua kufanya kitu ambacho roho ilikuwa imenituma!!!
Nikachepuka katika njia ambayo niliikumbuka vizuri panga langu sasa nilikuwa nimelichomeka kiunoni. Nikaruka matuta katika shamba la mihogo. Hatimaye usiku huo huo nikaifikia nyumba ambayo ilikuwa ngeni sana machoni mwangu!! Lakini mti mkubwa wa mwembe ulinikumbusha kuwa sijapotea.
Sikujali kama ule ulikuwa ni usiku ama la!! Nikajikongoja hadi mlangoni kisha nikagonga hodi!! Niligonga hodi bila kupata majibu yoyote…lakini mara nilisikia hatua za mtu akisogea pale mlangoni, nguvu zikaanza kuniishia mwilini lakini nikajikaza. Akauliza kikabila kuwa mimi ni nani? Nikamjibu kwa kumtajia jina la Wankuru!! Akafungua mlango huku akionekana kuwa na wasiwasi.
Akafanya kosa moja tu kuacha mkon wake nje, mara moja nikamvuta!! Akapiga yowe moja lakini nikawa nimemkamata tayari. Hakuna nilichokuwa naogopa.
“Wewe ni nani?” nilimuuliza nikiwa nimemshikia panga.”
“Bhooke!” alijibu.
“Desmund ni nani yako?”
“Mjomba wangu!!”
Alipojibu hivyo tu, nikaamua kumtumia huyu kama sadaka.
Na damu yao yote ilikuwa halali yangu!!! Ni neno aliwahi kusema Jadida kabla hajafa. Nami nikaona lipo sahihi sana.
“Kama alinitukania familia yangu!! Kama aliudhalilisha utu wangu, kwa nini nimuonee huruma YEYE na kizazi chake.” Nilijiuliza. Kisha nikamfyeka yule mtoto na panga begani, akapiga yowe moja, nikamfyeka tena mkono. Kisha kama ifanyavyo kuku, nikamkanyaga asirukeruke. Nikahakikisha kuwa anatulia tuli.
Nikaitimiza azma yangu ya ghafla kuwa ili nimpate Desmund vizuri lazima niweke huruma yangu kando!!! Nimpe adabu kimya kimya kisha nikumbane naye….nikaanza na huyo mjomba wake.
Nilitarajia litatokea nililokuwa nahitaji!!
Desmund alikuja kuhudhuria msiba ule. Nami sikulaza damu siku ya kuaga mwili nikiwa naishi maisha ya kula msibani hapo kwa kubangaiza na kulala palepale msibani. Msiba ambao nilikuwa nahusika nao kwa asilimia zote! Sasa niliamua kumkabili Desmund.
Nilisubiri amalize kumwaga mchanga katika kaburi la mjomba wake niliyemuondoa maksudi. Sasa nilihitaji kuzungumza naye kistaarabu.
Baada ya maziko macho yangu yakiwa makini kabisa kumtazama hatimaye nilimuona kwa uzuri kabisa.
Mwandishi, Desmund alikuwa amebadilika sana. Alikuwa na afya nzuri sana na alikuwa ameng’aa haswa.
Hatua kwa hatua nikapiga moyo konde, bila viatu miguuni nikajikongoja kwenda kukutana na yule. Litakalokuwa na liwe….
Mwandishi, nilikutana na Desmund. Nikaziba njia nikasimama mbele yake. Macho yetu yakatazamana ana kwa ana. Desmund alikosa neno la kusema kwa ghafla ile. Nami sikusema kitu niliendelea kumtazama tu. Jinsi alivyong’aa na jinsi mimi nilivyopauka!!
“Ni pete yako hii kidoleni mwangu Desmund!! Pete uliyonivika mbele ya wanafunzi wenzangu, ni jeraha hili Desmund ulilonipa kwa kupigania penzi langu. Sijaivua pete yako mpaka leo na sitaivua hata mpaka unieleze tu nilikukosea nini mimi hadi ukanitenda hivi. Hongera kwa kufunga ndoa naona pete yangu ulishaitupa mbali. Desmund sina hadhi ya kuzungumza na wewe nadhani hata watu wanatushangaa. Naomba unipe changu niendelee na maisha yangu. Nipe walau nusu tu ya mali zangu nijiondokee zangu. Nahitaji kuishi kwa amani. Desmund ni mazito umenifanyia, nadhani unajua ni kiasi gani nimeishi maisha yasiyokuwa na tofauti na jehnamu kama kweli jehanamu ipo kama wanavyosema wenyewe. Unajua umeniharibia kiasi gani. Ok kwa kifupi Desmund, kama ni njaa nimelala njaa, kama ni kutukanwa nimetukanwa, familia imenitenga, uchangudoa nimefanya sana tu…nimebakwa sana, nimelawitiwa mimi sana tu!!. Desmund huoni kama yanatosha yaliyonitokea. Halafu by the way, yule dada yangu uliyemwambia kuwa mimi ni mwendawazimu amekufa tayari. Sina pa kuegemea. Desmund nipatie walau nusu nasema nusu tu!! Nikayamalizie maisha yangu nikiwa na amani.NAKUOMBA!!” Nilimweleza Desmund kwa kirefu kabisa. Bado tukiwa tunatazamana na wapita njia wasijue lolote linaloendelea. Zaidi ya kutushangaa
“Wewe ni nani binti?” hatimaye aliniuliza swali la ajabu sana ambalo lilinishangaza. Desmund anajifanya hanijui mimi!! Desmund hanijui wakati amesababisha niwe katika hali ile.Hapo ndipo ulizuka utata… utata juu ya utata.”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Desmund alinishangaa sana hadi nami nikaanza kujishangaa kuwa huenda ni kweli nimemfananisha. Nikaanza kugwaya na kumsikililiza kwa makini kila neno alilokuwa anasema.
Lakini kutokana na kuduwaa kule niliishia kuona tu mdomo wake ukichezacheza bila kusikia ni kitu gani alikuwa akisema. Pia macho yangu yaliishuhudia hasira kali kutoka machoni mwake. Macho yalikuwa mekundu na alinyesha chuki ya waziwazi, sijui kwanini niliendelea kuamini yule ni Desmund na wala sijamfananisha, japo nilikuwa naelekea kukata tamaa sikufikia hatua ya kumkwepa niliendelea kumkabiri.
Ile hali ya kuamini kuwa yule aliyepo mbele yangu ni Deus ilinifanya nishikwe na donge zito kooni, donge ambalo lilinikera na kunifanya nisipumue vizuri. Nilipojaribu kumeza mate ili kulilainisha, uso wangu ukachafuka kwa machozi.
Macho yakaikosa nuru na nikashindwa kabisa kuona mbele kulikoni. Nikawa naona kama ukungu na mara badala ya kuwa kiwiliwili kimoja cha Desmund, sasa vikaongezeka na kuwa viwili. Sikujua kile kingine ni cha nani.
Kile kiwiliwili kipya kikaanza kunisogelea huku kikiwa katika mavazi ya kanga. Kabla sijakitambua kikanibamiza na kitu kizito usoni.
Maumivu niliyoyapata hayasimuliki, nikapangusa machozi na mara nikakutana ana kwa ana na yule mke wa Desmund. Mwanamke aliyejifanya ni dada yake Desmund, nikamheshimu na kumtunza vyema jijini Mwanza lakini baadaye nakuja kugundua ni mke wa mume wangu!!
Desmund!!
Mshtuko nilioupata ukanifanya damu ichemke sana na mara nikahisi mchuruziko puani, nilipojishika na kutazama nilikuwa natokwa damu. Yule mwanamke alivyonibamiza na kitu kizito usoni, kisha nikakumbwa na mshtuko.
Sasa nilikuwa natokwa damu!! Yule mwanamke kuna maneno aliyokuwa anaongea kwa kikabila, baadhi niliyatambua kuwa ni matusi, kwa sasa hayana haja ya kukweleza maana nitakuwa kama nakutukana mwandishi katika kabila usiyoijua.
Niliyavumilia yote lakini akavuka mipaka akanitukania na mama yangu wa kunizaa, yule mama aliyezikwa tayari huku akiniachia laana kuwa hanipendi. Sasa watu waliosababisha niuone uchungu wa laana wanamtukana marehemu mama yangu.
Mwandishi!! Kama nilivyokueleza awali kuwa huenda Jadida aliniachia roho yake ya ujasiri na ukatili. Nilimvamia yule mama mwenye mwili kunipita mimi, hakutarajia ujio ule, nilimshika nywele zake ndefu, nikazivuta. Alipiga yowe kubwa. Nadhani unafahamu maumivu yanayopatikana ukivutwa nywele. Desmund akanivamia pale na kuanza kunipiga ngumi mgongoni lakini sikumwachia mkewe yule, nikazidi kuongeza nguvu.
Naam! Nikaridhika hatimaye, nywele zikakatika!!
Nikawa nimemnyoa bila kutumia mkasi. Nikamwachia akaanguka chini kama mzigo.
Mwandishi, nikiwa sijui hili wala lile, mara niliona kundi la watu lililokuwa likishuhudia ugomvi ule likitawanyika. Mara nikamwona mbwa mkubwa aklielekezwa kunishambulia. Si mbwa aliyenifadhaisha la! Ni mtu aliyekuwa anamwelekeza kufanya vile.
Ni mama yake Desmund!! Yule mama aliyeugua sana Desmund akakata tamaa kuwa lazima mama yake atakufa, nikachukua ada yangu ya chuo kwa penzi langu kwa Desmund na familia yake nikaamua kumuhudumia mama hadi akapona. Desmund na mama yake wakasema mimi ni Mungu wao, nikakataa wasiniite hivyo. Mama yule akadai kuwa hatanisahau kamwe katika maisha yake, nikafurahi kuwa nimepata mama mkwe anayenipenda kwa dhati, kisha akaongezea kwa kumkanya Desmund akimwambia kuwa ‘ole wake aje kuniacha siku moja’. Sasa yule mama ambaye nilishatambua kuwa alikuwa mnafiki mkubwa alikuwa ameshikilia mbwa na akiielekeza kuja kwangu. Anaielekeza kuja kunifanyia shambulizi mimi Nadia Mungu wake katika shida iliyomkumba. Sasa ni adui yake nikiwa mimi nina shida.
Mwanadamu!! Usimtendee mtu wema ukatarajia atakulipa wema vilevile, moyo wa mwanadamu una siri nzito. Mdomo wake unadanganya na sura yake inashawishi na anaweza kutokwa machozi, sauti yake ya upole ikikulaghai kuwa ana uchungu sana nawe ukasema huyu ndiye sahihi!! Kumbe ule moyo usioonekana unakukejeli na kukutukana matusi mazito!! Eeh! Mwenyezi Mungu ungenionyesha muujiza.
Hapo nikajikuta nimefanya kosa kubwa kupindukia, nilisimama na kujaribu kukimbia. Yule mama aliyekuwa na uso wenye hasira kali alimuachia yule mbwa!!
Mbwa akatii amri ya bosi wake!!
Desmund badala ya kumzuia yule mbwa yeye akamsisistiza, yaani Desmund akafurahia mimi kukimbizwa na mbwa! Desmund akatoa tabasamu kali mimi kudhalilika katika kijiji nisichokijua.
Sijui kwanini Mungu aliniruhusu kugeuka na kumtazama Desmund jinsi alivyokuwa ananicheka!! Maana nilizidisha chuki dhidi yake, badala ya kumkimbia mbwa nikataka kumkimbilia Desmund! Kabla sijamfikia yeye mara mbwa akanirukia na kunitupa chini.
Neno la mwisho kulisikia tena kwa sauti ya Desmund!!!
“Huyu Chokoraa sijui katoka wapi maskini wee!!”
Desmund akaniita mimi chokoraa na hatambui wapi nilipotoka!!
Huenda alikuwa sahihi kabisa, kama marafiki zangu niliosoma nao hawakunikubali tena wakadai nina majini, familia yangu ilinikataa na mama akanilaani.
Naam!! Hakik nilikuwa chokoraa, lakini kuwa chokoraa mbele ya Desmund ni uongo uliotukuka. Sikuwa chokoraa, alijua kabisa maovu aliyonifanyia.
Mara yule mbwa akakutanisha meno yake makali katika paja langu!! Na hapo ndipo kiza kikatanda, kabla nuru haijatoweka nililiona tabasamu la dharau kutoka kwa Desmund!!
Kilio cha mbwa nacho kikasikika, bila shaka alikuwa anafurahia paja!
Kisha kimya!! Sikujua nilipoteza fahamu kwa muda gani.
Nilipozinduka nilikuwa nina pingu mkononi. Kila mmoja alikuwa ananizomea, lazima kuna kitu walikuwa wameambiwa aidha na Desmund ama mama mkwe wangu yule mnafiki. Walinizomea huku wakicheka haswa!!
Wakati huu nilikuwa katika mkeka, mtu pekee ambaye nilimwona kuwa mkarimu alikuwa ni nesi, ambaye bila shaka ndiye aliyenifunga bandeji katika kovu langu pajani.
Kovu la kung’atwa na mbwa!!
“Samahani dada nahitaji kuondoka hapa.” Nilimweleza yule nesi.
“Oooh!! Huwezi kuondoka dada wanadai hapo kabla umewahi kuwa na kichaa cha mbwa ni vyema twende hospitali kwanza, halafu na hawa polisi wanahitaji kuzungumza na wewe.” Aliniambia kwa upole sana.
“Nesi, sijawahi kuugua ugonjwa wa hivyo mimi.”
“Usijali dada utakuwa salama muda si mrefu!!”
“Na mbona wananizomea viumbe hawa sasa.”
“Eti ulivua nguo zako ndipo wakakushikishia mbwa maana ulitaka kuleta hatari msibani, ulitaka kufukua kaburi. Yawezekana ukichaa ulipanda, lakini usijali mrembo kila kitu kitakuwa sawa mama eeh!” nesi aliendelea kunieleza vitu ambavyo vilikuwa kama simulizi tu maana nilikuwa na akili zangu timamu na nilikuwa najua chanzo cha yote yaliyotokea.
“Nesi mimi ni mzima tafadhali niamini!!”
“Hapana binti, usingeweza kumng’oa yule mama nywele zake kwa kutumia mikono. Na kama hiyo haitoshi yule mbwa usingeweza kumvunja miguu yake kwa nguvu za kawaida.
Alipoongelea mambo haya nikakumbuka kile kilio cha mbwa kabla sijapoteza fahamu, kumbe hakuwa akilia bure. Katika tapatapa yangu nilimkamata miguu yake, hatimaye nikaivunja. Lakini eti haya yote ni kwa ukichaa wangu.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mimi Nadia baada ya kuzushiwa kuwa nina majini, sasa Napata kesi kuwa nina ukichaa wa mbwa!!
Baada ya muda likafika gari la wagonjwa, nikakimbizwa Musoma mjini hospitali.
Kama utani vile, ile hospitali ambayo ilishindwa kumtibu Desmund alipovunjika miguu nami nikaingizwa humo.
Baada ya juma moja la matibabu. Nikahamishiwa katika jengo jingine la serikali.
Rumande!!
Nikashikiliwa kwa kosa la kufanya vurugu msibani kisha nikajeruhi na baadaye kutishia kuua. Aliyelalamika kutishiwa kuuwawa alienda kwa jina la Desmund!!
Maajabu!! Huyu Desmund aliyenikataa kuwa hanijui, akachekelea niking’atwa na mbwa sasa anadai tena mimi nimetishia kumuua!! Desmund!! Sikutaka kuamini kama familia yao ilikuwa na roho za kawaida, kila baya wananirushia mimi!!
Kila nilipotaka kuilaani familia yao nikakumbuka kuwa laana ya mama ilikuwa inaishi. Laana ya mama ikanifanya niishi kama kivuli, kivuli kisichopata muda wa kupumzika. Kila dakika kila sekunde nikawa mtu wa majanga!!
Nilipokelewa rumande majira ya saa moja usiku, tangu nesi anipatie chakula ile asubuhi nilikuwa sijapata chakula tena. Nikapokelewa katika selo ya wanawake, nikakutana na wababe. Usiku ule nikalazwa mbele ya mlango wa choo. Choo kichafu na kinachonuka, kumbuka ile bandeji ilikuwa haijatolewa na nilikuwa na maumivu bado lakini yote haya hakuna aliyejali. Nikaingizwa kule, katika siku nilizohisi kuwa dunia nzima imenilalia ni hiyo!! Nilijaribu kutoa machozi yanifariji lakini hata yenyewe hayakutoka.
Kidonda, njaa, kisha nalazwa chooni!!
Mungu msamehe Desmund! Msamehe mama yake, lakini Mungu usisahau kukilaani kizazi chake, ishushe laana yako Mungu! Ni wewe ulisema tusihukumu lakini hebu nipe nafasi ya upendeleo, nihukumie kizazi hiki..kiteseke kisha kimlaani Desmund, mama yake na yule mwanaharamu mkewe!!”….hapa Nadia akasita kidogo kusimulia, akajifuta machozi, alikuwa anatetemeka haswa, bila shaka ni hasira. Maana kwa simulizi yake hii hata mimi nilijikuta namchukia mtu nisiyemjua hata sura yake. Desmund!! Hakika nilimchukia mwanaume huyo, kisha nikajilaani kwa sababu hata mimi nilikuwa mwanaume!!.
Nadia alipomaliza kujifuta machozi na kupenga kamasi akaendelea kusimulia.
“Nikabaki rumande nikiingoja siku yangu ya kusomewa mashtaka. Hakuna mtu aliyeniletea chakula, nilikuwa mtu wa kudowea vya wenzangu kila leo. Majira ya saa tisa nakula ugali na maharage mabovu!!
Mwandishi!! Hakuna kitu kama uhuru, ni heri uwe na mateso mtaani lakini usifungwe mahali kama nilipokuwa uukose uhuru. Mbaya zaidi sikuwa na kosa lolote sasa. Lakini nani atanitetea, sina ndugu wala rafiki!!
Ukimya wangu nikaona hauna maana hata kidogo. Katika kusoma kwangu niliwahi kusikia kuhusu haki za mahabusu. Nikaamua kunyanyua mdomo wangu na kuanza kumuita kila afande anayepita.
Nilipoona sisikilizwi nikaanza kupiga kelele kila sekunde!! Nilitaka kuijua hatma yangu.
Hatimaye kelele zangu zikasikiwa na askari mpelelezi aitwaye Daniel ama walivyozoea kumuita kwa jina la afande Dany.” Nadia akakaa kimya kwa muda kisha akasema neno lililoniacha njia panda na kugundua kuwa binti huyu amepitia mengi,
“Mungu amsamehe Dany kwa maovu yake, ampe kibali kwa mema aliyotenda na kama itabidi basi alazwe pema peponi!!......Dany maskini yaani alikuwa bado hata hajapata mtoto jamani, dah!! Sijui mama yake alijisikiaje baada ya kifo chake, yaani haya maisha haya. Mwandishi naomba nilale siwezi kusema zaidi kwa wakati huu.” Nadia akanyamaza na hakuendelea kuzungumza.
Nikabaki kujiuliza maswali magumu.
MOJA. Kama Nadia alikamatwa kwa kesi ile, ilikuwaje akatoka?
MBILI: DANNY ni nani na mbona Nadi anadai kuwa ni marehemu tayari..
TATU: Harakati za Nadia kudai haki yake ziliishia wapi??
Nadia alilala hatimaye, nikamsaidia kuviondoa viatu vyake miguuni nikamfunika shuka kisha nikaishusha na neti ili asisumbuliwe na wadudu warukao iwapo watatokea. Nilimtazama binti yule aliyekuwa amefumba macho, uso wake ukiwa mwekundu na machozi yaliyomtoka muda mfupi uliopita yakiacha michirizi.
Nilitikisa kichwa huku mengi yakipita katika kichwa changu!! Ni kipi kilimfanya hadi kila hatua anayopita akutane na mikasa mizito kiasi hiki.
Japo mimi nilikuwa sijwahi kutokewa na msala kama huu lakini nilikiri kuwa kama ningevaa viatu vya Nadia na kuwa yeye. Kwa haya magumu aliyopitia bila shaka ningekuwa nilishajikatia tamaa kitambo kirefu na labda hata ningekuwa nilishajifia huko kwa kujiua.
Lakini Nadia alikuwa anaishi na alikuwa akiusimulia mkasa huo ambao ulimweka katika nafasi ambayo alikuwa sasa. Nafasi ya mjutaji!!
Hakika alikuwa mwanamke wa aina yake binti huyu!!
Nilitafakari sana na usingizi ulinipitia baadaye sana usiku!!
Majira ya saa tatu na nusu asubuhi nilikuwa katika chumba cha Nadia tena, siku hii nilimkuta akiwa amemaliza kujiandaa, tulikuwa na safari ya kwenda katika hifadhi ndogo ya ‘SAA NANE’ iliyopo jijini Mwanza.
Tulitaka tuwahi kwenda ili tuwahi kurudi.
“Leo umejitahidi kuwahi!” alinambia.
“Aah! Leo nimeota ndoto mbaya nilikuwa nakimbizwa, sasa nikajikwaa, ile nainuka nikimbie tena nd’o nainuka kitandani.” Nilimtania tu lakini akastajabu…
“Eheee…umenikumbusha umenikumbusha…” alisema huku akijilazimisha kukumbuka jambo fulani…hapo nikatambua kuna maelezo marefu yanataka kutoka katika kinywa chake, nikabofya kifaa changu cha kurekodia kilichokuwa mfukoni.
“Nini tena Nadia au na wewe umeota unakimbizwa…” nilidadisi.
“Hapana kaka huenda kweli ni Desmund alimuua jamani!! Desmund atakuwa alimuua..”
“Nani tena Nadia….” Nilimuuliza swali kimakosa, sikutakiwa kumuuliza, lakini haikuleta madhara yoyote kwani huenda hata hakunisikia.
“Ujue jana nimegundua kitu ambacho nilijiuliza siku nyingi sana, huenda yeye Desmund aligoma kabisa kukiri lakini nilibaki na imani hiyo kuwa ni yeye alimuua Danny yule askari mpelelezi. Maskini Danny, sawa alikuwa na mabaya yake lakini kwa nini Desmund alimuua kwa kuniibia siri kidogo tu isiyokuwa na mantiki?
Jana nilikwambia nilivyokuwa nimewekwa rumande bila kutolewa kwa ajili ya mahojiano, nilikwambia jina kama Danny hivi. Yah! Danny!! Bila yeye nadhani ningeweza kuishia kuhamishwa rumande na kiha kutupwa gerezani bila kosa lolote, Danny alinitoa rumande na kuamua kunihoji, alinihoji kama mtu anayejua kitu fulani, alinihoji maswali mengi sana, nami kwa kuwa sikuwa na njia nyingine bali kusema ukweli nikamweleza juu ya hila ninayofanyiwa na Desmund na familia yake kwa ujumla. Danny alinisikiliza huku kila baada ya dakika kadhaa akiandika nukuu anazozijua yeye.
Baada ya mahojiano aliniambia kauli nzito. “Binti, kwanini usijiweke mbali na Desmund. Jiweke mbali naye yule atakusumbua sana, kila mtu mweupe anayejaribu kumgusa kwa sasa anaishia pabaya. Desmund hapendi wahindi, hapendi waarabu na anayo haki ya kuwachukia. Wewe jiweke mbali naye tu!!
“Lakini alikuwa mume wangu!!” niliingilia kati.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kuwa mume wako ama bwana yako kwa sasa haina maana, tuachie sisi tunaomjua Desmund na historia yake, cha muhimu kwa sasa jiweke mbali naye. Kulingana na maelezo yako, umenijeruhi sana kama ni mateso yametosha na hautakiwi kutumikia kifungo kisichokuwa na jina wala hukumu. Mimi nitakusaidia, lakini ukitoka hapa potea mbali kabisa. Maana Desmund hakupendi hata kidogo na nina kuhakikishia kuwa ukifa hataumia hata kidogo. Hawapendi waarabu kwa sababu zake za miaka mingi ambazo yeye anaziita sababu za msingi!! Tumejaribu kumshauri lakini hataki kubadili msimamo.” Maelezo ya askari yule yalinichanganya sana, nikabaki kuduwaa. Desmund na umasikini wote ule niliomkuta nao ana kisa gani na wahindi na waarabu. Kumbe tangu siku ya kwanza alikuwa ananichukia!! Nilibaki kuduwaa.
Nikataka kuuliza swali lakini afande Danny akanikata kidomodomo kuwa ule haukuwa wakati wa maswali!
Akanirudisha rumande bila kunieleza jambop jingine la ziada. Baada ya dakika kadhaa nikaletewa chai nzito ya maziwa, nikawagawia rafiki zangu wa wakati ule ndani ya selo. Mimi sikuweza kunywa chochote.
Usiku ambao sikufahamu ni saa ngapi mlango wa mahabusu ukafunguliwa, nikaitwa jina nikaitika. Nikatolewa nje ya ile mahabusu!! Safari hii hakuwa Danny bali askari mwingine tu ambaye sikuwahi kumjua jina lake.
Aliponifikisha nje nikiwa pekupeku vilevile nilikutana na gari ndogo ikinisubiri. Mlango ukafunguliwa nikaingia mle ndani. Gari ikaondolewa!! Taa ya ndani ilipowashwa nikagundua kuwa dereva ni Danny.
Moja kwa moja tukafika mtaa uitwao ‘Kariakoo’ hukohuko Musoma. Hapa ndipo Danny aliongea mara ya kwanza akiniambia chanzo cha mtaa ule kuitwa Kariakoo.
Baada ya dakika chache nyingine tukafika nyumbani kwa Danny.
Vilikuwa ni vyumba viwili vilivyoungana, choo na bafu vilikuwa nje.
Kitu cha kwanza baada ya kufika kwa askari huyu nilitakiwa kuoga, lakini bado sikutakiwa kwenda nje. Aliniletea maji katika ndoo na beseni kubwa akaniambia niogee ndani ya beseni, japo nilikuwa naona aibu nilioga.
“Safisha masikio hayo vizuri binti!!” Danny alinisisitiza kutokea chumba cha pili.
Baada ya chakula, nikamsihi Danny anieleze chanzo kidogo tu kwanini Desmund alikuwa akiwachukia watu weupe. Nilitamani sana kujua ili niamini kuwa Desmund yu sahihi ama la!!
“Umechoka sana binti! Kesho siingii kazini, nitakusimulia asubuhi sawa!!” alinijibu huku akipiga mwayo!! Sikuwa na kipingamizi, nikamkubalia. Akanipa gogoro tukapangua viti nikalitandaza chini. Akaniletea mashuka.
“Unajua bila kumshirikisha mama yangu walaah nisingeweza kukutoa kule, mama yangu amelizwa na historia yako Ameumizwa na machungu yote uliyopitia na mwisho amenipa kibali cha kukusaidia, mama yangu ni kila kitu kwangu na mimi ni kila kitu kwake. Mimi mtoto wa ngama.” Alinambia huku akitabasamu.
“Mtoto wa ngama nd’o nini?”
“Mimi ni mtoto pekee na yeye nd’o mama pekee.” Alinijibu tena.
Moyo wangu ulikuwa wa baridi sana katika namna ya utulivu, nilitamani sana kumuona mama huyo awezaye kuumizwa na maisha ya mtu ambaye hajawahi kumuona kamwe. Hakika ilishangaza hali hiyo. Danny akaniambia tutaongea mengi asubuhi. Lakini alipoona sijaridhika akachukua simu yake, akabonyeza namba kadhaa, alivyozungumza kwa kudeka nikajua anaongea na mama yake. Akanipa nami nikamsalimia, sauti ya mama yule ilikuwa ya ukarimu sana. Nikatamani kumuona siku moja.
Sasa niliridhika na nikatabasamu!!!
Nikajitupa katika godoro na baada ya muda kidogo nikasinzia!!
Baadaye nikahisi kama ndoto, kuna kitu kilikuwa kinanipapasa matakoni. Nikawa nahisi ni ndoto nami napuuzia, nikazidi kupapaswa, safari hii nikaunyanyua mkono na kupeleka mahali nilipohisi ule mpapaso!!
Nikakutana na mkono ukinipapasa. Nikataka kupiga kelele nikakutana mara nikazibwa mdomo wangu, nilijua kuwa Danny anataka kunibaka, Danny alikuwa naye anataka kunitendea unyama ambao kama ni kweli basi mama yake mzazi alikuwa anaulaani. Nikajaribu kufurukuta lakini haikuwezekana.
Hakika alikuwa Danny, mara akanisogelea masikioni.
Wanaume!! Wanaume na tamaa!! nililalamika kimya kimya huku nikimtazama.
Kumbe nd’o maana alikuwa anasisitiza nioshe masikio vizuri…shenzi kabisa!!
Ajabu!! Mawazo yangu yalikuwa batili. Danny hakuingiza ulimi wake masikioni mwangu. Badala yake aliongea kwa sauti ya kunong’ona.
“Kuna watu nje…….simama njoo huku.” Sauti yake ilimaanisha. Sasa nikawa kimya, nikajiziba mdomo mwenyewe.
Danny akanipakata hadi katika chumba alichokuwa amelala. Akaniamuru kwa vitendo niingie uvunguni!!
Nikatii!!!
Nikiwa uvunguni nikasikia mlango unagongwa!! Danny akaondoka kuelekea kule mlango ulipogongwa.
“Msichana yupo wapi kijana!!” sauti nzito iliuliza.
“Mi sijui msichana gani kwani?” sauti ya Danny ikajibu.
Hapo halikuulizwa swali kwa muda nikasikia kukurukakara, na mara Danny akasikika analia. Bila shaka alikuwa anatembezewa kipigo kikali.
Walimpiga huku wakianza tena kumuuliza kuhusu msichana ambaye bila shaka ni mimi, lakini ajabu Danny hakuwaambia. Nilikuwa natetemeka, mikojo ikizidi kulowanisha chupi yangu nikiwa chini ya kitanda uvunguni. Nilijua kuwa lazima Danny akizidiwa atanitaja na safari hii nadhani nd’o nilikuwa naenda kufa.
“Nasema nasema….” Nilimsikia Danny akisema huku sauti ikimkwamakwama.
“Yupo wapi msichana sema upesi.”
“Nimemsafirisha kwenda kwao…” alidanganya. Nami uvunguni hali ikiwa tete!!
“Unataka mama yako acute kichwa chako mlangoni kwake” sauti ilimuuliza.
“Haki ya Mungu nawaambia….nimemsafirisha kwenda Mwanza.” Alisisitiza Danny.
“Kijana yaani umemtoa usiku huu halafu unasema umempeleka Mwanza….unatutania sivyo. Ayubu hebu na wewe mtanie.”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hapo nikasikia kilio kikuu kutoka kwa Danny kisha kimya kikatanda baada ya kishindo.
“Mpumbavu huyu atakuwa amemuhifadhi kwa mama yake. Watoto wengine kujitafutia vifo maksudi tu!!” kauli hiyo ikanipagawisha. Ina maana Danny amekufa kwa sababu yangu!! Danny amekufa akinitetea, kwanini hakusema tu waniue…Danny alikuwa anategemewa na taifa na mbaya zaidi hakuwa hata na mtoto..niliumia sana. Mara nikawa kimya tena baada ya watu wale kuingia mle chumbani, sijui walichukua nini lakini niliwasikia wakivuruga vitu huku na kule. Kisha wakatoweka!!
Niliendelea kudumu uvunguni kwa nusu saa nyingine kisha nikatoka nikiwa natetemeka sana. Niliamini kuwa nimemuua Danny iwapo nitamkuta akiwa mfu!!!
Haswaa!! Haikuhitaji elimu ya utabibu kutambua kuwa Danny ni mfu, inanilazimu kukueleza mwandishi ili upate picha alivyokuwa lakini vinginevyo sitaki kukumbuka picha ile. Danny alikuwa amepasuliwa kichwa chake bila shaka kwa panga nililolikuta pale chini, nondo ilipenya katika tumbo lake na utumbo ulikuwa nje. Mwandishi niliumia kumtazama Danny niliumia sana, yaani wakamkata na mikono yote miwili…..aaaah!! Danny!! Kwanini sasa ulinisaidia mimi nisiyekuwa na umuhimu!! Na ni akina nani sasa waliokuja kukuua Danny!!....sasa kama laana mama alinipa mimi mbona wapate majanga na hawa wengine eeh!! Mama niambie hivi ulinilaani mimi ama uliwalaani hata wanaohitaji kunisaidia, mama ongea nami sasa eeh!! Sema nami…nife sasa kama ni hivyo…niue nije huko unieleze!!” Hapa Nadia akaanza kuomboleza kwa sauti ya juu. Nikamkabili nikauzungusha mkono wangu begani mwake na kuanza kumbembeleza
“Nadia haya mambo hutokea, binadamu hatufanani licha tu ya kutokamilika ambayo ni kwetu sote lakini kumbuka kila mtu ana roho yake, USILIE NADIA hayo yametokea tayari na yamepita, USILIE NADIA..tena kuhusu mama acha kukufuru, mwache apumzike….” niliendelea kumsihi.
Sasa akatulia kidogo kisha akiwa anabubujikwa machozi bado akaweza kumalizia maelezo yake.
“Kabla ya kulala Danny aliweka simu yake katika chaji kisha akaitia katika mfuko wa suruali yake. Akaitundika palepale sebuleni nilipokuwa nimelala.
Akili yangu ikafanya kazi upesi, nikaamini kuwa wauaji walikuwa wakimtambua Danny vizuri na hata mama yake walikuwa wanamtambua. Sasa kama walikuwa wanamtambua mama yake pia. Bila shaka walikuwa wameenda kumuuliza pia na yeye kama hana jibu wanamua vilevile.
Nilichukua simu ya Danny,nikabofya kitufe cha kupigia.
“La Mujer De Mi Vida” nikajikuta natabasamu mwenyewe, kwa sababu nilikuwa mtazamaji mzuri sana wa tamthilia hivyo nikaelewa maana kuwa alimaanisha ‘Mwanamke wa maisha yangu!’….nikapiga namba hiyo.
Iliita kwa muda mrefu sana kisha ikapokelewa.
“We Danny nawe…nini sasa..” alilalamika mama.
“Mama ni mimi Nadia, kuna tatizo mama jihadhari huko usiwe peke yako kuna watu wabaya mama wanakuja huko..” nilimweleza.
“Unasema?” aliuliza sasa akiwa makini.
Nikataka kumweleza tena simu ikaishiwa salio.
Nikasubiri anipigie!! Hakupiga!!
Nikatazama saa ya ukutani ilikuwa saa nane na nusu usiku!! Nikayacha maiti ya Danny ndani, nikapekua pesa nikazipata kiasi kidogo. Nikaondoka na simu yake.
Majira ya saa tisa usiku nilikuwa nazagaa huku na kule ndani ya mji wa Musoma bila kuelewa ni kitu gani natakiwa kufanya…
Hapa nikakiri kuwa hakika Nadia mimi nilikuwa nimelaaniwa
Mji ukazidi kuwa mchungu!!!........nilifanikiwa kupata salio baadaye kabisa lakini mama hakuwa akipatikana tena…chozi la uchungu likanitoka, nayapigania maisha yangu, naipigania haki yangu, mali zangu za halali, mali nilizozivuna na Desmund kwa sababu tu ya mapenzi yangu kwake!! Leo hii nachukiwa kila pande, nimetengwa na sasa nasababisha vifo, Danny amekufa akinitetea, sijui kuhusu mama mwenye upendo uliopitiliza mama aliyenipenda hata bila kuniona!!...Desmund, Desmund mapenzi yangu yooote niliyokupa umenitenda hivi Desmund….kweli umeamua kunifanya niwe mkimbizi kiasi hiki Desmund ambaye sijawahi hata kukutukana sijawahi kukulaumu Desmund, Des niliyekunyenyekea licha ya kuwa nakuzidi kwa kila kitu…leo unaniita Chokoraa na nisiyefaa katyika jamii, unawatuma watu waniue mimi Desmund!!” kikafuata kilio kikuu huenda kupita vyote, Nadia alilia sana, alilia akiomboleza juu ya kifo cha Danny na kuhusu mama asiyejua kama alikufa ama la!! Lakini Nadia aliamini kuwa walimuua. Nadia alilia kinyakyusa!! Alilia huku akilaani katika namna ya kuimba!!
“Nadia, mimi nipo upende wako na sitakusaliti, ni mimi na wewe tunajua wapi tulipokutana amini kuwa …”
“Shhhhhhh!!!! Wote ninyi ni wale wale..” alinikaripia. Nikatambua kuwa hii ni hasira iliyopitiliza. Nikaamua kumuacha Nadia alie akimaliza apumzike na huenda anaweza kusema nami tena, maana kwa hali aliyokuwanayo angeweza kunipiga hata makofi!!
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
**saa tisa usiku NADIA mtaani, Danny amekufa…je vipi kuhusu mama Danny!! Alikufa ama alipona….
**Nadia amekuwa mkali sasa amenigeuzia kibao na mimi mwandishi..nimeamua kumwacha apumzike akitulia tutaendelea!!!
TOA MAONI YAKO TAFADHALI!!!
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment