Simulizi : Sitoisahau Mbeya
Sehemu Ya Nne (4)
Nilifika nyumbani nikiwa na hasira vilevile nikisahau hata kuwasalimia wazazi wangu niliowakuta wamekaa pale sebuleni. Nilifika ndani na kujibwaga kitandani kwangu. Nillianza kulia huku nikiwa nimebanwa na kwikwi. Kwa mara nyingine tena Richard Chali alikuwa ananiliza, kwa mara nyingine tena mapenzi yalikuwa yananiliza! Yananitoa machozi! Baada ya muda mfupi wa kulala pale kitandani, nilihisi napapaswa mgongoni, ishara kuwa kulikuwa na mtu chumbani kwangu ananiamsha, niligeuka nyuma taratibu huku sura yangu ikiwa imetapakaa machozi. Nilikuwa natazamana na mama yangu mzazi!
"Vipi mwanangu mbona unalia" Mama aliniuliza kwa sauti yake ya upole.
"Najisikia homa mama" Nilidanganya tena huku nikiangalia darini.
"Homa nd'o inakufanya usisalimie hata wazazi wako?" Aliniuliza tena mama.
"Samahani mama nilipitiwa tu, kichwa kinaniuma sana" Nilidanganya tena.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Umekunywa dawa sasa" Aliniuliza.
"Nimemeza panadol" "Sawa pumzika, usilie ukilia homa inazidi, umenielewa?"
"Sawa mama"
Mama aliondoka na kuniacha chumbani peke yangu. Nililala pale kitandani bila kupata hata lepe la usingizi. Usingizi utakuja vipi katika hali kama niliyokuwa nayo mimi? Baada ya kuhangaika kitandani kwa muda mfupi, niliinuka na kukaa kitako katika ncha ya kitanda changu. Sasa nami niliamua kupanga mashambulizi yangu kwenda kwa Richard Chali na Evelyne Gando. Niliwaza na kuwazua niwafanye nini watu wale, lakini sikupata jibu la kuuridhisha moyo
wangu. Mwishowe nikaamua niache kuwaza kuhusu wao, na kulala usingizi.
Siku iliyofuata nilienda shule kama kawaida. Niliwakuta wanafunzi shuleni wamechangamka sana, tofauti kabisa na kawaida, wanafunzi walikuwa na furaha isiyo na kifani. Niliulizia sababu ya furaha yao, nilipata jibu, wanafunzi wenzangu walinambia.
'Wanafunzi wa shule ya Sangu watakuja wiki ijayo. Kutakuwa na mashindano ya mpira wa miguu na mpira wa pete, kati yetu na wanafunzi wa Sangu, tangazo liko katika mbao ya matangazo'
Nilihemewa sana!
Taarifa hiyo kwangu ilimaanisha kwamba rafiki baradhuli, Richard Chali na mwanamke msaliti, Evelyne Gando walikuwa njiani kuja shuleni kwetu!
Wanafunzi wote wa shule ya Sekondari Meta walikuwa wanafurahia ujio wa wanafunzi wa shule ya Sekondari Sangu. Kwa maana, Shule ya Sekondari Meta na Shule ya Sekondari Sangu zilikuwa ni shule pinzani sana kuanzia kitaaluma hadi katika michezo. Lakini kwa upande wangu sikujua kama natakiwa kushangilia ama natakiwa kuchukia. Shule ya Sekondari Sangu ndio shule ambayo alikuwa anasoma Evelyne Gando. Shule ya Sekondari Sangu ndio shule ambayo alikuwa anasoma Richard Chali. Shule ya sekondari Sangu ndio
shule ambayo mkuu wake wa shule alikuwa mwalimu Bukuku. Mkuu wa shule ninayemchukia zaidi hapa duniani. Ama hakika sikujua kabisa kama natakiwa nifurahia ujio wa shule ya Sekondari Sangu pale shuleni kwetu? Shule hasimu katika maisha yangu.
Nililala pale kitandani bila kupata hata lepe la usingizi. Usingizi utakuja vipi katika hali kama niliyokuwa nayo mimi? Baada ya kuhangaika kitandani kwa muda mfupi, niliinuka na kukaa kitako katika ncha ya kitanda changu. Sasa nami niliamua kupanga mashambulizi yangu kwenda kwa Richard Chali na Evelyne Gando. Niliwaza na kuwazua niwafanye nini watu wale, lakini sikupata jibu la kuuridhisha moyo wangu. Mwishowe nikaamua niache kuwaza kuhusu wao, na kulala usingizi.
*****
Hatimaye siku ya siku ikafika. Siku ambayo wanafunzi wa shule ya Sekondari Sangu walikuwa wanakuja kwa ajili ya michezo katika shule yetu, shule ya Sekondari Meta.
Pamoja na wanafunzi wenzangu wengi kuwa na furaha isiyo na kifani siku hiyo kutokana na ujio wa shule hiyo lakini mimi sikuwa na furaha hata chembe. Nilitamani nisiende uwanjani kabisa, lakini nilipiga moyo konde, niliamua kwenda uwanjani, na kweli.. nilienda. Nia na
madhumuni ya kwenda uwanjani siku ile sio kwenda kuangalia mpira kati ya shule hizo mbili.
Nia yangu ilikuwa ni kwenda kuangalia ujio wa 'marafiki zangu' wawili, Richard Chali na Evelyne Gando.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wakati mpira wa miguu siku hiyo ulikuwa unaanza saa kumi kamili ya jioni, mimi saa nane mchana nilikuwa nimeshawasili uwanjani. Nilikaa katika upande wa kaskazini mwa uwanja. Upande ambao watu wengi walikuwa hawapendi kukaa, kwakuwa kulikuwa na nyasi nyingi. Nilijilaza kwenye nyasi nyingi nikiwa sina raha kabisa. Nilitegemea kuja kupigwa pigo kubwa sana na wanaharamu wale, lakini sikuogopa sana, nilijiandaa vyema.
Nakumbuka saa nane na nusu mchana nilisikia muungurumo wa gari. Nikanyanyuka pale nyasini nilipokuwa nimelala na kukaa kitako. Uwanja wa shule ya Sekondari Meta haukuwa na uzio, hivyo ulikuwa unaruhusu gari aina yoyote kuweza kuingia hadi uwanjani. Nililitazama kwa makini sana gari lile, nililitambua!
Lilikuwa gari la la baba yake mzazi, rafiki yangu aliyenisaliti Richard Chali. Nilikuwa nimeshawahi kuliona gari lile mara nyingi sana nilizoenda kumtembelea Richard Chali nyumbani kwao. Nilikaa
vizuri, huku umakini wangu ukiongezeka maradufu. Lengo ni kutaka kujua, ni nani atakayeshuka katika gari lile. Haikuwa mbali sana pale nilipokuwa nimekaa na lilipokuwa limesimama gari lile. Niliweza kushuhudia kila kitu kwa umbali niliokuwepo.
Ndio maana, nilishuhudia kiatu cheusi cha kiume aina ya mkuki moyoni kikitangulia kukanyaga ardhi ya uwanja. Nilinyanyua sura yangu kutoka katika kiatu na kumwangalia mmiliki wa kiatu kile, nilimtambua vizuri sana. Alikuwa ni Mzee Chali. Baba mzazi wa hasimu wangu, Richard Chali !
Baadae kidogo mlango wa kushoto wa mbele wa gari lile ulifunguliwa. Safari hii kilitangulia kiatu cha kike chekundu kugusa ardhi. Naam, kilikuwa chekundu, mchuchumio. Viatu hivyo vilimilikiwa na msichana aliyekuwa amevaa gauni jekundu. Alishuka kwa madaha ya kike huku akitembea kama anaogopa kuikanyaga ardhi. Alilizunguka lile gari la Mzee Chali, na kumfikia Mzee Chali bila ajizi wala uwoga wowote ule. Mzee Chali nae hakuzabaa, alimdaka kwa umahiri mkubwa sana binti yule, binti aliyekuwa na umri sawa na mwanae ambaye kwa sasa alikuwa hasimu wangu, Richard Chali. Walikumbatiana kwa muda mfupi, wakaachiana. Wakapigana mabusu tele kila mahali walipojisikia. Mabusu mashavuni. Mabusu usoni. Mabusu mdomoni. Ilikuwa ni mabusu mabusu mabusu huku mikono ya Mzee Chali ikiwa imekishika vizuri
kiuno cha binti yule. Na yule binti akiwa ameshika mabega ya Mzee Chali. Ilikuwa picha nzuri sana kuitazama. Maana waigizaji walimaliza ufundi wao wakijua wako peke yao. Hakuna jicho lililokuwa linawaona. Kwa bahati nzuri nilipokuwa nimekaa mimi ilikuwa ngumu sana kwa wao kuniona.
Baadae kidogo yule binti aliyevaa gauni jekundu aliingia tena ndani ya gari. Huku Mzee Chali akiwa ameegemea boneti ya gari yake akichezea simu yake ya mkononi. Ilichukua takribani dakika tano yule msichana alitoka tena, sasa hakuwa amevaa lile gauni jekundu. Alikuwa amevaa blauzi jeupe lenye mtindo wa kipekee kiunoni, pamoja na sketi nyeusi. Kitu pekee kilichonifanya nimtambue yule binti kuwa ndiye yuleyule aliyeingia ndani ya gari na gauni jekundu muda mfupi uliopita ni vile viatu vyekundu ambavyo bado vilikuwa miguuni mwake. Nilimwangalia kwa makini sana, usoni, na sasa nilimtambua. Alikuwa ni Evelyne Gando akiwa amevalia sare zake safi za shule ya Sekondari Sangu. Niliziba midomo yangu kwa mikono yangu yote miwili, kutokea pale nilipokuwa. Nikiwa siamini kabisa macho yangu!
Ndio, niliamini macho yangu yananiongopea. Nilimuona Evelyne Gando nae akienda pale mbele ya boneti ya gari, mahali alipokuwa kasimama Mzee Chali, baba mzazi wa hasimu wangu Richard Chali. Alimbusu pajini yule baba ambaye nilikuwa
namuheshimu sana katika maisha yangu huku mikono ya Evelyne Gando ikiwa imekishika vizuri kiuno cha Mzee Chali, wakati mikono ya Mzee Chali nayo ikiwa imekishika vizuri mno kiuno laini cha Evelyne Gando. Nilijisikia hasira sana, safari hii hasira zangu zilikuwa tofauti na nikizozipata mwanzo wa sakata hili, hasira za safari hii zikiwa hazina hata chembe ya wivu. Zilikuwa hasira halisi. Hasira kwa vitendo walivyokuwa wanavifanya Evelyne Gando na Mzee Chali. Niliwaza kimoyomoyo "Inamaana Evelyne Gando anawachanganya mtu na baba yake? kwanini lakini mwanamke huyu amekuwa mnyama namna hii. Hivi ni kweli Richard Chali anajua uchafu huu unaofanywa na Evelyne Gando, msichana anayemwita mpenzi wake? Hivi anajua kweli, kama baba yake mzazi anatembea na mpenzi wake?" Nilijiuliza maswali ambayo sikuwa kabisa na majibu yake.
Nilijiinamia chini kwa huzuni huku nikimuonea huruma sana Richard Chali. Nikimuonea huruma pia mama yake Richard Chali. Sikuweza kabisa kuvumilia chozi la huruma lilinidondoka na kupotelea nyasini.
Niliponyanyua tena sura yangu na kuwaangalia tena wanaharam wale, niliwashuhudia wakiagana na Mzee Chali kuingia katika gari lake na kuondoka, na kumuacha mwanamke yule shetani akiwa kasimama katikati ya uwanja.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya kama dakika kumi, Richard Chali aliwasili pale uwanjani. Evelyne Gando na Richard Chali walionana wote kwa pamoja. Walikimbiliana kwa furaha kubwa sana na kukumbatiana kwa nguvu.
Nilimuona Richard Chali akisogeza mdomo wake usoni kwa mwanamke yule msaliti kuwahi kutokea hapa duniani na kumpiga busu mahali palepale nilipomshuhudia akipabusu baba yake mzazi muda mfupi uliopita.
Pale nyuma ya goli nilipokuwa nilikuwa natetemeka kwa hasira, sasa nikiwa nimekinaishwa na uchafu uliokuwa unafanywa na msichana huyu, Evelyne Gando. Lakini niliamua kusubiri palepale. Sikutaka kabisa kupelekeshwa na hasira. Nilitulia tuli. Kwa muda ule nilikuwa naangalia picha mbaya sana katika maisha yangu. Na mbaya zaidi nilikuwa shahidi pekee katika jambo zito sana kama lile.
Ndio! Nilikuwa shahidi pekee wa kushuhudia uchafu ule. Baba na mwana wakiwa katika mahusiano ya kimapenzi na mwanamke mmoja. Kwa bahati mbaya zaidi nilikuwa shahidi lakini adui!
Shahidi adui!
Nilikuwa sipatani na Evelyne Gando, nilikuwa sielewani na Richard Chali. Wote walikuwa maadui
wakubwa kwangu. Ni nani angeukubali ushuhuda wangu? Kwanza ningemwambia nani habari ile mbaya kabisa. Ama hakika ulikuwa mtihani mkubwa sana kwangu. Kuwa na siri nzito inayowahusu maadui zangu.
Baada ya lile busu kutoka katika mdomo wa Richard Chali kwenda katika shavu laini la Evelyne Gando waliachiana. Kisha wakatazamana kwa muda mfupi. Pale nilipokuwa niliona midomo yao ikichezacheza, bila shaka walikuwa wakijadiliana jambo. Umbali niliokuwepo haukuruhusu kusikia kitu walichokuwa wanaongea. Baada ya maongezi hayo ambayo nilikuwa sijasikii yaliyochukua kama dakika tatu walikumbatiana tena.
Wakabusiana tena.
Nikiwa pale nilipokuwa nilitamani nitoke pale nyasini niende mahali pale. Ili kumueleza uchafu uliokuwa unafanywa na mwanamke yule mbaya kabisa, Evelyne Gando mahali palepale, lakini nani angenielewa. Mimi na Richard Chali sasa tulikuwa maadui wakubwa sana, asingeweza kunielewa kabisa!
Baada ya muda mfupi wa kuongea walitoka pale katikati ya uwanja na kwenda pembeni mwa uwanja.
Walikaa chini.
Wakiendelea na maongezi yao. Kutoka pale nilipokuwa nimekaa nilisikia mlio wa gari, gari la wanafunzi wa shule ya Sekondari Sangu likiingia pale uwanjani. Waliingia kwa shangwe na kelele nyingi sana, huku wakisindikizwa na nyimbo, nyimbo ambazo nazo zilikuwa katika mfumo wa kelele. Muda huohuo wanafunzi wa shule ya Sekondari Meta nao walikuwa wanakuja uwanjani makundi kwa makundi huku wakiwazomea wanafunzi wa shule ya Sekondari Sangu. Waliokuwa wanaingia na gari yao.
Ilikuwa tafrani.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilitumia kama dakika tatu kuyashuhudia na kuyasikia yote hayo. Dakika ya nne niligeuka pale walipokuwa wamekaa Evelyne Gando na Richard Chali.
Evelyne Gando hakuwepo!
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment