Search This Blog

Sunday, July 10, 2022

SITOISAHAU MBEYA - 3

 





    Simulizi : Sitoisahau Mbeya

    Sehemu Ya Tatu (3)



    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Evelyne Gando wiki ya pili sasa. Nilikuwa nakonda kila mshale wa sekunde wa saa ulivyokuwa unasogea kuelekea upande wa kulia. Siku moja wakati tunakula, baba na mama waliniuliza kwanini nilikuwa napungua sana, lakini sikuwa na jibu la maana la kuwapa. Nitawaambiaje wazazi kwamba nilikuwa nakondeshwa na mapenzi? Nilijiumauma tu, na kusingizia nakondeshwa na masomo. Wote waliniangalia kwa jicho la huruma sana, huku wakinipa pole ya masomo.



    Wahenga walisema, mtu atakunyima vyote lakini si rahisi kukunyima maneno. Victor Anyimike ndiye aliyekuja kunithibitishia ukweli wa msemo huo wa wahenga. Victor alininyima vyote wakati tunasoma pamoja pale shuleni Sangu, lakini tulivyokutana pale Mwanjelwa hakuninyima neno. Alinambia habari iliyopasuapasua moyo wangu vibaya sana, eti kwamba kwasasa Evelyne Gando na Richard Chali walikuwa na uhusiano wa kimapenzi huko shuleni Sangu. Ilikuwa ni taarifa mbaya sana kwangu, taarifa iliyosafiri katika mishipa ya damu ya mwili wangu na kwenda kutua katika moyo wangu. Na kuanza kuupasuapasua moyo wangu na kuumiza vibaya sana. Hisia za WIVU zikanitawala moyoni mwangu. Nilipatwa na wivu wa ajabu sana wakati mimi sikuwahi kumueleza hata siku moja Evelyne Gando kuwa nilikuwa nampenda. Chozi la uchungu lilinidondoka hadharani na kupotelea



    katika ardhi yenye vumbi ya Mwanjelwa. Sikumbuki hata kama tuliagana na Victor Anyimike.



    Nilirudi nyumbani na kujifungia chumbani kwangu na kuanza kulia. Sasa uadui wangu dhidi ya Richard Chali ukakomaa, niwe mkweli tu nilimchukia sana Richard Chali kuliko hata shetani!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Evelyne Gando hivi ni kweli unanisaliti, Richard Chali hivi ni kweli unanisaliti!" Hayo ndiyo maneno pekee niliyothubutu kusema huku nikiwa natokwa na machozi kitandani.



    Nakumbuka nililia sana siku ile. Nilijiona kuwa nimempoteza Evelyne Gando kirahisi sana. Nikiwa nimejilaza pale kitandani nakumbuka mdogo wangu wa kike, Christina aliingia ndani kwangu bila hodi, sijui alifata nini, lakini alichokifata hakukifanya. Alipigwa na butwaa alipogundua kwamba nilikuwa nalia. Kwa mwendo wa taratibu alinifata pale kitandani, alinishika mkono na kwa sauti ya huruma mdogo wangu aliniuliza ni kitu gani kilikuwa kinaniliza lakini nilishindwa kumwambia. Utamwambia vipi ndugu yako wa kike eti unalia kwakuwa umesalitiwa, tena umesalitiwa na mwanamke, mwanamke ambaye hujawahi kumwambia kuwa unampenda.



    AIBU ilioje hii.





    Niliamua kumdanganya ndugu yangu kuwa nilikuwa naumwa kichwa. Christina aliondoka huku akiwa kichwa chini. Aliamini kweli nilikuwa naumwa, na ugonjwa wangu ulimtia simanzi sana Christina. Nilikuwa mtu mcheshi sana, niliyependa kufurahi muda wote na familia yangu. Lakini leo hii Evelyne Gando na Richard Chali walikuwa wameondoka na furaha yangu. Nililia sana siku ile mwishowe nilinyamaza, niliona kulia hakunisaidii kitu. Nilikaa kitandani na kutafakari kipi cha kufanya. Mawazo mengi yalipita katika kichwa changu. Yalitathminiwa na wazo moja lilikubaliwa kati ya mengi yaliyopita katika kichwa changu. Nikaamua kulifanyia kazi. Niliamua lazima nikutane na Evelyne Gando mahala popote pale ili nimueleze hisia zangu. Nimueleze kuwa nampenda sana. Nataka awe mpenzi wangu. Kisha aje kuwa mke wangu. Mke wangu wa ndoa.



    Niliamua siku ya jumapili nikakae pale nje ya geti la shule ya Sekondari Sangu. Ili nisubiri muda wa wanafunzi wa hosteli kwenda kanisani ukifika. Nimfate Evelyne Gando na kumueleza kiasi gani alikuwa ananitesa, kiasi gani alikuwa anautesa moyo wangu, kiasi gani nilikuwa nampenda. Nampenda sana.



    Wahenga walisema siku hazigandi.



    Pamoja na kuona kwamba siku zinasuasua na kuchelewa sana lakini siku ya jumapili ilifika. Siku ya kwenda kupasua jipu, kwa kueleza hisia za kweli zilizokuwa ndani ya moyo wangu. Nakumbuka jumapili hiyo nilivaa suruali yangu nyeusi ya kitambaa na shati jeupe lenye madoa madoa meusi. Huku chini nikivaa viatu vyeusi vilivyochongoka, maarufu kama mkuki moyoni. Ukweli kwamba nilikuwa nimependeza sana siku hiyo kuliko siku zote.



    Tangu saa kumi na moja alfajiri nilikuwa nimekaa nje ya geti la shule ya Sekondari Sangu kumsubiri Evelyne Gando. Mwanamke nikiyemhusudu sana. Saa mbili kamili asubuhi geti lilifunguliwa, na hatimaye nilimuona Evelyne Gando nae akitoka kwa mwendo wa madaha. Evelyne Gando alikuwa amependeza sana siku hiyo.

    Alikuwa amevaa suti nzuri za kike za rangi nyeusi, na viatu vyeusi vyenye kisigino kirefu ambavyo vilileta ladha tamu kila Evelyne alivyokuwa akiikanyaga ardhi. Kwa bahati nzuri Evelyne Gando alitoka nje akiwa peke yake, hiyo ilikuwa ni habari njema sana kwangu. Kwa mwendo wa taratibu aliongoza katika barabara ambayo ilikuwa inaelekea njiapanda ya Mafiat, nami nilimfata kwa nyuma huku nia yangu nimsimamishe endapo akifika katika usawa shule ya Msingi Meta ama shule ya Sekondari ya wasichana ya St Francis. Cha ajabu moyo ulikuwa unanidunda sana!

     CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Ilikuwa mithili namfatilia Simba!



    Nilifata taratibu huku nikijificha kwenye miti pale nilipoona Evelyne Gando alikuwa anataka kugeuka nyuma. Alipofika pale katika usawa wa shule ya msingi Meta ambako ndipo palikuwa moja ya shabaha yangu kumsimamisha Evelyne Gando. Evelyne alisimama chini ya kivuli cha mti mrefu, nilimshukuru Mungu kwa kuitikia dua yangu nami nikijibanza nyuma ya mti wa mwarobaini.

    Ghafla! Nilimuona yule mshenzi!

    Richard Chali, akiwa kavaa jeans ya bluu na t-shirt nyeupe, huku kichwa akiwa amevaa kofia ya kapelo. Richard Chali alifika pale aliposimana Evelyne Gando, huku akiwa anabonyazabonyaza simu yake. Alipomkaribia kabisa Evelyne alimkumbatia kwa nguvu huku akimpiga busu zisizo na idadi katika mashavu yake. Niliyashuhudia yote hayo nikiwa pale nyuma ya Mwarobaini. Nilishikwa na hasira yenye mchanganyiko na wivu. Nilitamani nifumbe macho ili nisishuhudie kinachoendelea lakini sikufumba. Ubongo ulikuwa unataka lakini macho yenyewe yalikuwa hayataki.



    Baada ya kuongea kwa muda kama wa dakika tano walishikana mikono na kuifuata njia ileile iliyokuwa inaelekea njiapanda ya Mafiat.



    Nilichoka sana.

    Sura yangu ilisawajika kwa huzuni pamoja na hasira, nilikuwa nataka kulia lakini nilikuwa najizuia kwa nguvu huku nikijiambia kimoyomoyo kuwa

    'Sasa kulia kwa ajili ya mapenzi imetosha'

    Sikuwa na jinsi kabisa, Evelyne Gando na Richard Chali walinifanyia vitu vibaya sana nikiwa nashuhudia kwa macho yangu yote mawili. Nilirudi nyumbani siku ile nikiwa na hasira nyingi sana. Hasira ambayo sasa ilianza kugeuka taratibu na kuwa CHUKI!

    Chuki kwenda kwa Evelyne Gando na baradhuli la kiume Richard Chali.



    Nilifika nyumbani nikiwa hoi, nilipitiliza hadi chumbani kwangu na kujitupia kitandani, nililala kifudifudi, huku kichwa changu kikiwa kimelala juu ya mto, nikapitiwa na usingizi, usingizi ambao nilishangaa kwanini ulikuja haraka vile, kwa jinsi nilivyokuwa najisikia sikutegemea kabisa kama nitalala siku ile.

    Cha ajabu nililala sana siku ile, nilala saa tatu asubuhi pindi niliporudi kumfatilia Evelyne Gando na kuamka saa tisa jioni. Bahati nzuri wazazi wangu na mdogo wangu Christina hawakuwepo nyumbani siku ile, walienda kukutana na dalali huko Nzovwe, baba alikuwa anataka kununua kiwanja ili nasi tujenge Mbeya.



    Saa tisa jioni. Niliamka na kutoka nje, kutafuta kibanda wanachouza chipsi, maana njaa ilikuwa inaniuma sana. Nilikipata, nilikula chipsi nyama na kushushia na soda ya baridi aina ya sprite. Kisha nilirejea nyumbani. Nikaenda tena kitandani kwangu na kujilaza chali, sasa nikaanza kutafakari tukio lilikonitokea asubuhi kule shule ya Msingi Meta.

    Niliwaza



    "Hivi kwanini nalia bila sababu ya msingi. Nalia wakati ninayemlilia hana habari na mimi. Haniwazi. Hajui kama naumia kiasi hiki. Nalia wakati ninayemlilia sijui kama ananipenda ama hanipendi. Pia hajui kama nampenda. Kwanini najitesa kwa kumpenda msichana mmoja tu, Evelyne Gando ilihali wasichana wako wengi sana hapa duniani. Wasichana wazuri pengine zaidi ya Evelyne Gando. Nasema, hii ni mara ya mwisho kulia kwa sababu ya mapenzi, siyo kwa Evelyne Gando tu, ninaapa sitalia tena kwa sababu ya mwanamke yeyote yule duniani!'

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Maneno hayo ya mwisho niliyoyatamka kwa sauti ndogo nikiwa nimelala chali pale kitandani. Yalipata baraka katika moyo wangu. Niliamua kwa moyo wangu wote tokea siku ile kuwa sitolia kwa ajili ya mapenzi. Na ilikuwa hivyo, tokea siku hiyo nilimtoa kabisa Evelyne Gando katika kichwa changu!



    Naam nilimsahau kabisa Evelyne Gando moyoni. Na nikasahau pia mambo ya wanawake hapa duniani. Sasa nikawa nakumbuka masomo. Nawaza masomo. Nayapenda masomo. Masomo ndio yakawa Evelyne Gamdo wangu. Nilibadilika kabisa, nikawa najibidiisha katika masomo. Sasa masomo yaliuteka moyo wangu kama alivyokuwa ameuteka Evelyne Gando hapo awali. Furaha yangu moyoni ilirejea kwa kasi kubwa sana. Sasa nikawa na furaha kama zamani, kama zile siku za mwanzo zilivyokuwa shuleni Sangu. Nilisahau kila kitu kuhusu rafiki yangu ambaye kwa sasa aligeuka na kuwa adui kwangu, Richard Chali. Nilisahau kila kitu kuhusu mwanaharam yule wa kike, ambaye mwandishi anamwita Evelyne Gando lakini mimi naweza kumwita shetani wa kike.



    Ulipita mwezi nikiwa nimesahau hadithi ile mbaya iliyoanza ndani ya basi. Sasa nikawa 'bize' na masomo. Furaha yangu ilirejea kwa kasi kubwa sana. Tofauti kabisa na nilivyofikiria, na afya yangu ilitengamaa, nikaanza kunenepa tena.



    *****



    Nakumbuka siku moja ya jumatatu jioni nilienda kujisomea katika maktaba ya mkoa Mbeya iliyokuwa kule mjini, Uhindini. Sasa nilikuwa napenda kusoma kuliko kitu chochote kile katika maisha yangu na



    nilikuwa naenda maktaba kila mwisho wa wiki kwa ajili ya kujisomea.



    Niliingia maktaba, baada ya kumaliza taratibu zote za pale mapokezi ikiwa na pamoja kuonesha kitambulisho changu kilichokuwa kinaniruhusu kuitumia ile maktaba, niliingia ndani ya maktaba. Nikatafuta shelvu ya  vitabu vya historia iliyokuwa upande wa kushoto wa maktaba ile na kuanza kutafuta kitabu nilichokuwa nakihitaji. Baada ya muda mfupi nilikiona kitabu nilichokuwa nakitafuta. Kilikuwa kinaitwa" How Europe underdelop Africa' kitabu kizuri kilichoandikwa na mwandishi mahiri Walter Rodney. Nikakiona, nikatafuta sehemu nzuri ya kukaa ili nikisome kitabu hiko kizuri cha historia, nilipata sehemu sahihi nikatulia kwenye kiti na kuanza kukisoma.



    Baada ya kama dakika saba ya kusoma kitabu kile, bila kutarajia Ilitokea tu nikacha kusoma kitabu na kuanza kuangalia watu ambao walikuwa wanaingia kwa muda mle maktaba. Niliwaona vijana wawili wakiingia kwa muda ule, mmoja kati ya vijana hao wawili nilimtambua vizuri sana, alikuwa ni Richard Chali! Hasimu wangu mkubwa sana hapa ulimwenguni! Adui yangu wa kweli. Shetani wa kiume. Msaliti mkubwa. Binadamu asiye na urafiki wa kweli. Kiumbe mwenye tabia za mbwa koko...



    Nilimuona.



    Richard Chali aliingia maktaba na kuelekea upande uleule ambao nilikuwa nimekaa mimi nikijisomea. Wakati yule mwenzie akienda katika upande mwengine kabisa. Richard Chali akitembea kwa mwendo wa kibabe alikuja kukaa siti ya pili toka pale nilipokuwa nimekaa. Bila shaka alikuwa ashaniona. Nami nilimuona vizuri sana lakini sikujishughulisha nae kabisa, sikutaka kumsalimia, na wala sikuwa na haja na salamu yake. Nilijiinamia katika ile meza yangu, kwa umakini mkubwa nikiendelea kusoma kitabu cha Walter Rodney, how Europe underdevelop Africa.

    Nilijifanya kama sijamuona kabisa Richard Chali.



    Baada ya kama dakika tano kupita, tangu Richard Chali aje kukaa karibu yangu, niliiona mkono ukisogea taratibu pale katika meza yangu, mkono ukatua mezani na kuacha kikaratasi kidogo cheupe, na mkono ule kurejea ulikokuwa awali. Mkono ule ulikuwa mkono wa Richard Chali. Nilikiacha kile kikarasi kikiwa kimekaa pale juu ya meza kwa muda, nilikuwa natafakari nikichukue ama la, nikiache palepale au. Baadae niliamua kukichukua kikaratasi kile, ili nijue kimeandikwa nini na baradhuli yule, rafiki msaliti, Richard Chali.

     CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nilikifunua taratibu kile kikaratasi, kikaratasi toka kwa Richard Chali. Nikayasoma maneno yaliyoandikwa katika kile kikaratasi kimyakimya. Kiliandikwa maneno matatu tu.

    ' Hujambo Domo zege'.

    Maneno hayo niliyasoma taratibu huku nikitetemeka midomo yangu yote miwili. Yaliniumiza sana. Yalinipandisha hasira toka huko zilizokuwa, na kuzileta pale maktaba. Maneno yale yalinikumbusha kila kitu kuhusu ugomvi wetu mimi, Evelyne Gando pamoja na Richard Chali. Kila nilivyokuwa nakumbuka walivyonifanyia wanyama hawa wawili huko nyuma ndipo hasira zangu zilizidi kututumka katika moyo wangu!



    Bila kutegemea wala kufikiria mara mbili, nilinyanyuka pale katika kiti changu nilipokuwa nimekaa na kusogelea katika kiti alichokuwa amekaa baradhuli, Richard Chali, nikiwa nimefura kwa hasira na jazba juujuu!

    Niligeuka mbogo!

    Nilikuwa naongozwa na hasira. Na mbaya zaidi niliamua ile inaitwa liwalo na liwe. Sikuwa na uwoga hata chembe. Sikuwa na hofu! Nilidhamiria kumfanya kitu kibaya sana Richard Chali! Nilisogea pale katika kiti alipokuwa amekaa baradhuli yule wa kiume. Richard alikuwa amejiinamia katika meza yake akiandika, bila shaka akiandika kikaratasi kingine cha



    kunikejeri, labda alimaliza kukiandika, lakini hakufanikiwa kunitumia tena ujinga wake!

    Nilimkaribia pale alipokuwa na kumkaba kwa nguvu sana kutokea nyuma kwa kutumia mkono wangu wa kulia! Richard alijaribu kufurukuta lakini hakufanikiwa kuitoa kabali ile, kwa kutumia mkono wangu wa kushoto nilikuwa namshindia migumi ya nguvu ya mbavu! Richard alijitahidi sana kuitoa kabali kimyakimya, thubutu yake! Hakufanikiwa hata chembe. Mkono wangu uling'ang'ania shingo yake mithili ya ruba! Baada ya kama dakika moja ya msuguano huo wa kimyakimya, yule baradhuli akajiona atakufa bure.

    Ghafla! alipiga kelele kwa nguvu za kuomba msaada. Huku akinitukana matusi ya nguoni. Mimi nilikuwa kimya, nikitekeleza jukumu langu kwa umakini mkubwa sana. Makelele yake pamoja na matusi yaliyokuwa katika mtindo wa mkoromo yakawafikia wahudumu wa maktaba ile, na nusu ya watu waliokuwa maktaba. Walikuja kwa kasi huku nao wakipiga makelele, ilikuwa tafrani ndani ya maktaba.



    Walifika pale tulipokuwa tumeshikana na Richard Chali na kufanikiwa kutuachanisha. Nilikuwa nimevimba sura kwa hasira karibu ya kupasuka! Wahudumu wa maktaba wakatupeleka katika chumba chao. Bila kutusikiliza utetezi wetu walituambia wanatupeleka kituo cha Polisi. Niliogopa sana. Sikuwa



    nimewahi kupelekwa polisi kwa kosa lolote lile. Richard Chali nae alikuwa mwoga wa Polisi pia. Baada ya kuomba sana radhi uongozi wa maktaba walitupa zuio la kuingia maktaba ile ya mkoa wa Mbeya katika maisha yetu yote. Huku wakitupa vitisho vya kutupeleka Polisi endapo tusipotii agizo hilo.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Niliondoka ndani ya maktaba nikiwa na hasira kubwa sana. Sasa nilimchukia Richard Chali kuliko hata nilivyokuwa namchukia shetani. Inawezekana kweli nilikuwa na domo zege lakini sikuwa napenda hata kidogo kuitwa jina hilo. Hata Richard Chali alijua chuki zangu juu ya jina hilo.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog