Simulizi : Ulikuwa Wapi
Sehemu Ya Tatu (3)
Usiku huo sikulala kabisa, kesho yake asubuhi mapema nikaenda kugonga chumbani kwa kina kaka na mzee. Nilikuta siku hiyo kaka anatakiwa kuhamia wodini kwa ajili ya maandalizi ya upasuaji, hivyo mzee alianza kuweka vitu tayari kwa ajili ya kuhama. Nilipoingia, sijui aliona hofu niliyokuwa nayo usoni au aliamua tu kusema. “Una wasiwasi? Usiogope, tutamuomba Mungu siku ya leo, naamini kila kitu atasimamia Yeye.” Aliniambia maneno hayo, yakanipa ahueni kidogo. Tulipanga vitu ambavyo havikuchukua muda, tukaweka tayari kila kitu, tukaenda kunywa chai. Ilitakiwa tuhame mida ya saa tano au sita asubuhi, lakini ilikuwa lazima aje mtu wa kutuhamisha, muhudumu wa hapo hospitali.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kitu nilichopenda kwenye hospitali ile, au niseme kwa wenzetu, ni namna ambavyo wanamjali sana mgonjwa na wateja wao. Kabla ya kwenda kwenye vipimo, muhudumu alitangulia kuweka miadi, ili mgonjwa akija asikae kwenye foleni, lakini pia licha ya kuwa na ndugu wa kumuuguza, hakuna sehemu ambayo mgonjwa alipelekwa bila muhudumu. Wao ndio waliohusika kumsukuma kwenye kiti maalumu cha kusukumia wagonjwa (wheel chair), na kumpeleka kwa wakati eneo husika. Sisi tulifuatana naye kama watu tunaotakiwa kujua kila kinachoendelea, lakini wahudumu walitoa msaada mkubwa.
Baada ya chai, mida ya saa tatu asubuhi, tulirudi chumbani, baba mzee Magessa akasema inabidi tuwe na muda wa kusali kabla ya kuhamia wodini. Alifungua maandiko matakatifu, akasoma vifungu viwili vinavyohusu nguvu za Mungu na uponyaji, akatoa maelezo kidogo kwamba madaktari hufanya kazi yao kulingana na utaalamu na ujuzi wao, lakini Mungu ndiye anayeponya. Kwa lugha nyingine, daktari hutibu, Mungu huponya. Yeye aliamini jambo moja tu, kwamba kama Bahati angekuwa wa kufa, asingeishi miaka yote hiyo. Mungu aliyemlinda miaka yote, akampa na watu wa kumuhudumia, ndiye atakayemponya. Baada ya maelezo yake kwa ufupi, tulishikana mikono sote, na kusali, baba akituongoza. Binafsi sikuwa najua namna ya kuomba, zaidi ya kulia tu, nikisema neno moja, “Mungu mponye kaka.” Akili yangu niliishawishi kwamba Mungu yupo, na anasikia maombi ya watu, ingawa ilikuwa ngumu kuamini hilo kwani kitendo cha kaka kuumwa miaka yote hiyo, na kukimbiwa na mkewe, kilinifanya nione Mungu hayupo au hajali.
Kwa upande wake, mzee Magessa, alisali kama mtu anayemaanisha kuongea na Mungu. Katika umri niliokuwa nao, sikuwahi kukutana na mtu anayesali namna hii, kwa kumaanisha na kwa utulivu kabisa kana kwamba anazungumza na mtu wanayeonana na wanaye heshimiana sana. Nilijisemea moyoni kwamba, labda Mungu atasikia na kujibu maombi ya mzee huyu, hata kama hupuuza yangu. Kwa jinsi alivyosali, nilihisi ni mtu ambaye Mungu ameshamtendea mema mengi mno, kiasi kwamba hana sababu hata moja ya kutompenda na kutomuamini Mungu, tofauti na mimi ambaye maisha yangu yamejaa machungu na mateso makubwa.
Tulimaliza kusali, tukakaa kusubiri, akaja muhudumu mida ya saa tano, tukahamishiwa wodini, lakini mimi niliwasindikiza tu, nikawa nikienda kushinda huko lakini narudi kulala hotelini. Ilipofika jioni, kaka alichukuliwa kwenda kuandaliwa kwa ajili ya upasuaji. Wakamrudisha, akaambiwa asile kitu chochote kuanzia saa nne usiku. Usiku huo, tukiwa tumekaa mule wodini, chumba cha pekeyetu, alikuja muhudumu kumuita baba. Waliondoka kwenye saa mbili na nusu usiku, akakaa kama saa nzima, akarudi. Hakutaka kutuambia walichozungumza kwa undani ila alisema alikwenda kuongea na daktari. Akinirudisha hotelini kwenye saa tano usiku, nilimuuliza tena daktari alimuitia nini muda ule, akasema ni maelekezo ya msingi tu kuhusu matibabu, huku akionesha hakuna cha maana sana.
Alikuja kuniambia ukweli baadaye kabisa, tukiwa tumesharudi nyumbani, nikaelewa kwanini alituficha. “Upasuaji utachukua saa nane au zaidi, lakini hilo si tatizo, hata ukiwa ni wa saa 20, kwani lengo ni mgonjwa apone tu. Ila kuna hatari ya kupona au kufa karibu kwa asilimia sawa. Akitoka salama katika upasuaji, kuna asilimia 70 ya kupona kabisa, na kurudi hali yake ya awali, lakini inaweza kuchukua kati ya mwaka mmoja hadi mitatu. Lakini pia kuna asilimia 30 za kupoteza baadhi ya viungo vyake vya fahamu, au kubaki hivyo alivyo kwa maisha yake yote. Hivyo kama unakubaliana na hayo maelezo, na uko tayari tufanye upasuaji, inabidi utie sahihi.” Baba aliniambia daktari alimpa hayo maelezo, wakiwa na wenzake watatu, huku wakimchukua video, ili ikitokea lolote asije akawashitaki. Siku ananiambia hivyo, nilisisimka, sikujua kama angeniambia hayo maelezo siku ile ile, ningefanyaje.
Hatimaye siku ya upasuaji iliwadia, nikadamka alfajiri sana kwenda wodini, nikakuta tayari wameamka. Alikuwepo muhudumu akikata kucha za miguu za kaka, kisha wakahakikisha ameoga vizuri. Wakati huo kichwani alinyoa kipara kabisa, akapakwa dawa maalumu kichwani ya kuua wadudu, akavalishwa kikofia na nguo ambayo ndiyo aliingia nayo thieta, wakamchukua huku tukimsindikiza. Baba aliendelea kumpa matumaini mpaka anaingia chumba cha upasuaji, mimi nikijizuia kulia mbele yake.
Saa mbili asubuhi tulitaarifiwa kuwa ameanza kupasuliwa, tukawa tukisubiri nje. Siku hiyo nilijiahidi kuwa sitakula wala kunywa chochote, mpaka kaka yangu atoke mule ndani akiwa mzima. Nilimwambia baba kuwa nitafunga, nione kama nikimuomba Mungu kwa kufunga atanisikia. Sote hatukujua habari za chakula, muda wote kaka akiwa kwenye upasuaji. Kuna mara kadhaa nilishikwa tumbo la kuhara, kuna wakati nilihisi kama naishiwa nguvu, wakati mwingine nilikimbia chumbani kwangu mara moja na kulia sana, yaani siku nzima ilikuwa na hekaheka kwangu. Baada ya saa nne kupita, daktari mmoja alitoka na kutuambia kuwa wanaendelea na upasuaji, wamelifikia tatizo, watatujuza tena baada ya muda. Hapo ndipo nilichanganyikiwa zaidi. Muda niliona hausogei kabisa, nilitamani arudi kutuambia kama wameondoa tatizo bila kaka kufa.
Sijui kama unaweza kuelewa hali niliyokuwa nayo siku hiyo. Kumbuka huyu ni mtu pekee ambaye amenionesha nini sababu ya mimi kuendelea kuishi, kwa kunishika mkono wakati ambapo maisha yalinikatisha tamaa kabisa. Kumbuka pia huyu ndiye baba na mama, kwangu na kwa mdogo wangu Zita. Ukiacha Zita, hakukuwa na mtu wa muhimu kwangu zaidi ya kaka Bahati, naye ndiye alinifanya nipate watu wengine kama mzee Magessa, dada na kaka Abdalah.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Muda zaidi ulipita, tukingoja nje, sehemu maalumu ya kusubiria wagonjwa walio thieta. Alitoka tena yule daktari, nikatamani nimkimbilie kumuuliza nini kinaendelea. Alikuja tulipokuwa, akasema wamefanikiwa kuondoa tatizo na sasa wako katika harakati za kurudishia kila kitu na kumshona. Nilianza kujaribu kufikiri kama daktari, yaani nikaanza kuona kichwani kwangu namna kaka Bahati amepasuliwa kichwa, kikachokonolewa sana kwa masaa kadhaa na sasa kinashonwa. Nilijikuta nimetaka kupiga kelele kwa nguvu, nikaweka mkono na kitambaa kinywani, nikaanza kulia. Mzee Magessa alinishika bega na kunibembeleza, akinihakikishia kuwa inavyoonekana kazi imeshaenda vizuri. Tuliendelea kukaa tukisubiri, nikitaraji daktari atarudi baada ya saa moja au mawili, kwani zilikuwa zimeisha saa saba tayari.
Tulikaa zaidi ya saa tatu tukisubiri, daktari hakutokea. Wasiwasi ulinizidi sana, nikiwaza huenda wakati wa kurudishia kaka amefariki. Sikuweza tena kuzuia machozi muda wote, huku nikimpa mzee Magessa kazi ya kunibembeleza na kunitia moyo. Katika siku mbaya nimewahi kukutana nazo kwenye maisha, ukiacha wakati wa kufiwa na wazazi na bibi, hii ilikuwa siku mbaya mno kwangu. Nilijikuta nikikumbuka maisha tuliyoishi kabla kaka Bahati hajaoa, nikailaani hadi siku ya harusi yake. Nilitamani nimpate anti Ketty na kummwagia mafuta ya moto usoni. Hakukuwa na mtu niliyemchukia zaidi ya huyo mwanamke, na hata kama ningesikia amekufa, ningeona bado anastahili adhabu zaidi.
Baada ya saa 11 tangu aingie kwenye chumba cha upasuaji, daktari alitoka tena, akatufuata. Nilimtazama usoni, nikitaka kujua sura anayoonesha ni ya huzuni au ya matumaini, lakini hawa watu wenye taaluma zao za udaktari, muda wote sura yake inakua sawa tu, huwezi ukasema inaonesha habari mbaya au nzuri. Sitasahau hizia nilizohisi daktari akitupa habari kwamba upasuaji umekamilika na Bahati ametoka salama. Nilijikuta nimemkumbatia baba kwa furaha kubwa mno, nisitake kujua maelezo zaidi ya daktari huyo. Alituruhusu twende kumuona, lakini alisema huenda akachukua saa kati ya 12 hadi 20 kuamka, na kwa sasa hajitambui. Alisema matokeo ya upasuaji tutayajua baada ya mgonjwa kuamka, lakini kwa asilimia kubwa, kazi imefanyika vizuri.
Tuliingia kumuona kaka Bahati, akiwa amelala, hajitambui, chumba cha wangonjwa wa uangalizi maalumu yaani ICU. Nilijisikia kumuhurumia sana, na kuogopa. Sikuwahi kuingia ICU kabla, sikuwahi kumuona mgonjwa katika hali kama ile, yaani mipira puani, mdomoni, kifuani kuna vitu kama vimipira vimeweka, mashine zimemzunguka. Dah, nilihisi kama walivyosema ataamka ni uongo. Sikuamini kama ile hali aliyoonekana nayo, na mamipira yote yale, angeweza kuamka tena. Nilisogea karibu na kumuangalia, akiwa amelala na kukoroma kwa ugonjwa. Nilijitia moyo tu kwa maneno aliyosema daktari, nikawa nikisubiri muda upite, nione ataamka akiwa na hali gani.
Niliendelea kukaa wodini na mzee Magessa, baada ya kutoka kumuona kaka. Mzee ikabidi atafute namna ya kunichangamsha kwa hadithi za hapa na pale. Alinisimulia kisa kilichomchelewesha kipindi kile anataka kuja Tanzania kwa mara ya kwanza, yaani sababu iliyomfanya ahairishe safari. “Nina binti yangu, ndiye binti wa pekee, ana miaka 24 sasa. Mwaka juzi akiwa na miaka 21, alipata rafiki wa kiume, akatutambulisha, mtu wa huko Poland tunapoishi. Mimi huwa siwekei sana watoto mipaka ya nani wa kuoa au kuolewa naye, naamini katika maamuzi binafsi, lakini nafsi yangu wala ya mama yake, hazikuwa na amani sana na yule kijana. Nilijipa moyo kwamba wataishia kwenye urafiki tu, wasioane, lakini cha kushangaza, baada tu ya miezi sita, walikuja kutuambia wanataka kuoana. Unajua kwa nchi zilizoendelea, ndoa ni changamoto sana. Kwao kuoana ni suala tu la hisia, na kuachana vilevile. Wengi wao hawana nguvu ya lile agano la ndoa, bali huchukulia kwamba siku hisia za mapenzi zikiondoka kati yetu, tunaachana.
Sikuwa na namna ya kumzuia msichana ambaye huenda moyo wake ndio umependa kwa mara ya kwanza, kuolewa. Lakini umri wake haukuwa mkubwa, hivyo nilitamani asubiri kidogo, nikiamini kuwa katika kusubiri atagundua kuwa uamuzi anaofanya si sahihi, abadilishe. Lakini binti hakuwa anazuilika. Mama yake alijaribu kuongea naye, na hata mimi, lakini hakutuelewa kabisa. Alidai kwamba tukimkatalia atakuwa mzinifu tu, hivyo ni bora akaolewe. Hatukuwa na namna, tukakubali akaolewa, kwa sherehe ya kawaida, maisha yao yakaanza. Nadhani tangu waoane, huu mwaka wa tatu sasa, ni miezi sita ya kwanza pekee ndipo hatukusikia kesi. Alianza akimwambia mama yake kuhusu vituko vya huyo mwanaume, baadaye familia nzima tukawa tukijua.
Yaani wazungu wana mambo ya ajabu mwanangu, siku nimepanga safari yangu kuondoka, tukiwa tumeshasuluhisha migogoro yao mingi sana, walikuja nyumbani pamoja na watoto wao wawili. Yule mwanaume alikuja akidai amechoka na majukumu ya mke na watoto nyumbani kwake, hivyo anahitaji mapumziko ya muda. Alisema kwamba ameileta familia yake kwa wazazi wa mkewe wamsaidie, na hata pale walipokuwa wakikaa alisema angehama ili ahamie nyumba ya kibachela kwa muda. Alisisitiza kuwa yeye na mkewe hawataachana, ila anachukua likizo ya muda mfupi tu, kupumzika na majukumu ya ndoa na familia.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Akili yangu haikuelewa kabisa kile kitu, nikahisi kama kijana amechanganyikiwa. Binti yangu Joyce ana elimu ya chuo kikuu, na alikuwa kwenye nafasi ya kupata kazi nzuri baada tu ya kumaliza chuo. Lakini hakutaka kazi kabisa, akidai kwamba anahitaji aishi mwaka au miaka miwili ya ndoa yake, wakila fungate kwanza, ndipo atafute kazi. Alipoingia tu kwenye ndoa, hakuchukua muda, akabeba mimba. Na unajua kule ni vigumu sana kuajiri msichana wa kazi, hivyo baada ya kuwa na watoto, tena waliofatana sana, ilimlazimu kubaki kuwa mama wa nyumbani. Mwanzo alidanganyika na yale mapenzi ya kuahidiana ahadi za uongo, akiamini kuwa mume wake kwa kuwa ana kazi, maisha yao yataendelea vizuri. Lakini mwanaume pia hakuwa amejipanga kimajukumu nadhani, alihisi maisha yataendelea kuwa sawa kiuchumi wakati kipato hakijaongezeka ilhali familia inakua.
Mpaka nakaribia kuondoka, Joyce alikuwa nyumbani huku mwanaume amekaa kimya kabisa. Wiki moja kabla ya safari, mumewe alikuja, akimuomba msamaha na kumuahidi hatafanya hivyo tena. Sasa hapo tulimuacha Joyce mwenyewe aamue kama anamsamehe au la, mwanaume akabembeleza sana, kama siku tano mfululizo, akija na zawadi, maua, anaongea mpaka analia. Niliacha wamesameheana na wamerudi kwao, ametafuta nyumba nyingine, wamehamia. Ila nilimshauri Joyce atafute kazi haraka iwezekanavyo. Ni bora hata watoto wawe wanawaleta nyumbani, yeye anaenda kazini, na nadhani mpaka sasa ameshaitwa kwenye usahili.”
Hiyo habari ya Joyce ilinisahaulisha kidogo kuhusu kile kilichokuwa kinaendeelea kwa kaka Bahati. Nilichekeshwa sana na yule mzungu kuomba likizo ya ndoa na familia, nikaiaminisha akili yangu kuwa hawa si watu sahihi wa kuolewa nao. Kuanzia siku hiyo nilisema hata ikitokea mzungu anioneshe ananipenda kiasi gani, kamwe sitajitumbukiza kwenye ndoa naye, na wala sitaruhusu Zita aolewe na mzungu.
Tuliendelea na maongezi na mzee Magessa, mpaka ikafika usiku kabisa, huku kila mmoja hana dalili ya usingizi. Lakini baba akanishauri niende nikalale kwani ana hakika jana yake nilikesha. Alinipeleka hotelini chumbani kwangu, nikaoga na kukaa pale kitandani, nikiwaza maisha. Umri wangu kwa sasa ulikuwa umezidi kidogo miaka ishirini, yaani kijana mbichi, lakini uzoefu wangu wa maisha ni kama wa mtu wa miaka arobaini. Nilishapitia hali ninazofananisha na milima na mabonde yenye wanyama wakali mno, bila msaada, lakini nikavuka salama. Pia nilishaambiwa maneno ambayo nayafananisha na mikuki ya moto kifuani, lakini nayo pia nilivuka salama. Katika umri mdogo, nimekuwa mama na baba kwa mdogo wangu Zita. Katika umri huo pia, nimekuwa mtu ninayetegemewa kufanya maamuzi yote yahusuyo afya ya kaka yetu, hasa kabla baba Magessa hajaja. Nimekutana na watu mbalimbali, walioonekana usoni kuwa na sura za binadamu, lakini mioyoni ni mbwa mwitu hatari. Nakumbuka kaka Bahati akiwa mzima, kuna rafiki zake kadhaa waliokuwa wakimchekea na kuongea naye vizuri, lakini alipoumwa, hakukuwa na wa kusimama upande wake kuhakikisha uzima wake. Wengi walionekana miezi ya mwanzo tu, na kwa urubuni wa anti Ketty, ndivyo alivyopotea mmoja baada ya mwingine.
Asibuhi niliamka, nikaenda wodini mapema, nikamkuta baba anajiandaa kwenda ICU. Mwili wangu ulikuwa dhaifu kiasi, kwa ajili ya kutokula muda mrefu, lakini kusema kweli sikuhitaji chakula kabisa, mpaka nihakikishe kaka ameamka. Tuliingia ICU na kukuta hali ile ile kwa kaka Bahati, madaktari wakitupa moyo kuwa anaendelea vizuri na ataamka muda si mrefu. Tulikaa, kisha tukatoka nje, sehemu ya kusubiri wagonjwa, tukawa tumekaa hapo kwa muda, tukingoja ahudumiwe kwa muda. Baada ya kama nusu saa hivi, alitoka daktari, akatuambia kuna habari njema, tunaweza kuingia. Nilikuwa wa kwanza kuingia, nikasogea karibu kabisa na usawa wa kichwa cha kaka Bahati, pembeni akiwepo daktari mwingine. Nilimuangalia usoni kaka, nikisubiri daktari atuambie hiyo habari njema, lakini kabla hata ya sekunde kumi, nilimuona kaka akifumbua macho na kunitazama. Nilipata msisimko, mkubwa mno wa furaha, nikashindwa kumkumbatia wala hata kumshika mkono kwani alikuwa na sindano za dripu na mirija kila sehemu. Alinitizama nikitoka machozi ya furaha, nikamgeukia mzee Magessa na kumkumbatia tena kwa furaha, nikaona tabasamu la mbali mno kwenye macho ya kaka, nilipomtizama tena. Nimemfahamu kaka Bahati katika hali ya ugonjwa kwa miaka mingi, hivyo ilikuwa rahisi sana kwangu kujua akionesha uso wa huzuni au wa furaha, kabla mtu yeyote hajatambua.
Baadaye, daktari alituambia hali yake inaleta matumaini sana, kwani alipotuona aliulizwa kama anatukumbuka, akaonekana kutukumbuka sote. Kwa madaktari wapasuaji wa vichwa, kitu cha kwanza na cha muhimu kwa mgonjwa baada ya upasuaji, ni kujua kama kumbukumbu zake ziko sawa. Siku hiyo kusema kweli ilikuwa siku nzuri kwangu, nikaanza kuamini kwamba huenda kweli Mungu yupo na anajibu maombi. Nafsi yangu ilichangamka, tukawa tukingoja kwa hamu kujua ni namna gani afya yake itakuwa baada ya kutoka hospitali. Kaka alikaa na mashine ya kupumulia kwa siku mbili, kisha wakaitoa, wakatuhakikishia kwamba maendeleo yake ni mazuri. Hakuwa anaweza bado kuongea, lakini tulipewa matumaini kuwa kuna nafasi kubwa ya kupona kabisa, endapo atafuata masharti kwa muda wa kutosha. Baada ya siku nane, alitolewa ICU na kuhamishiwa wodi ya kawaida, akaendelea kuhudumiwa hapo kwa wiki mbili zaidi.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Tuliruhusiwa kutoka hospitali, baada ya kukaa siku kama 23 jumla, tukahamia hotelini, huku tukiendelea kupata matibabu ya nje. Kila siku muuguzi alikuja kumuangalia, alihakikisha amekunywa dawa zake kwa wakati na kumpeleka endapo alitakiwa kuonana na daktari. Kaka alianzishiwa mazoezi pia, ya kumsaidia viungo vyake kurudi katika utendaji wake. Katika mazoezi aliyoanzishiwa, kuna mazoezi yalikuwa ya kumsaidia kuanza kusimama na hatimaye kutembea, mazoezi ya kushika vitu kwa mikono yake, na mazoezi ya kutoa sauti na kuongea, na mengine.
Wiki mbili baadaye, tulipata ruhusa ya kusafiri, tukapewa vibali maalumu na madaktari vya kuturuhusu kusafiri na mgonjwa, ili iwe rahisi kwenye ndege tunayosafiria. Tuliondoka Uturuki na vifurushi vya dawa, kama za aina saba au nane. Maelekezo ya kutumia hizo dawa ilibidi tuandike, na tuweke alamu kwenye simu za kukumbusha, kwani alitakiwa kunywa dawa zote kwa wakati. Sikutaka nifanye kosa la kupitiliza hata dakika mbili za muda wake wa dawa. Tuliambiwa pia tumtafute daktari mtaalamu wa mazoezi ya viungo, atakayeweza kumsaidia katika mazoezi. Lakini walitutaka turudi kwa ajili ya uangalizi wa hali yake baada ya miezi mitatu.
Mara baada ya kurudi Tanzania, ilibidi baba asafiri kurudi nchini kwake kuweka mambo sawa halafu arudi tena baada ya miezi mitatu. Kwa kipindi tulicho kuwa naye, alijua mimi ni mtu wa aina gani, ikamjengea imani juu ya uangalizi wa kaka Bahati. Mimi nina kawaida ya kujali kupita kiasi, nadhani kuachwa na wazazi na kuachiwa mdogo nikiwa bado mtoto, kulinijengea akili ya kuwajibika. Nina uwezo mkubwa mno wa kukumbuka kitu chochote kuhusu mtu ninayemjali. Tangu kaka Bahati aanze kuumwa, sijawahi kusahau kuhusu dawa zake na muda wa dawa, muda wa chakula (kuna wakati alitakiwa ale kwa wakati kabisa), au chochote kinachomuhusu.
Pia kwa kiasi kikubwa, nimepata msaada wa hawa ninaowaita sasa ndugu zangu, kaka Abdalah na dada Shanisa ambao tumeishi nao nyumbani kipindi chote, kabla na baada ya kaka kuugua, na hata baada ya upasuaji. Wenyewe wamenichukulia kama dada yao, licha ya kuwa umri wangu ni mdogo kwao. Hatukuwahi kupishana kwa maneno, kipindi chote tulichoishi pamoja, na wameifanya kazi yangu ya kumuuguza kaka kuwa nyepesi sana. Wameshirikiana na mimi kwa kila hatua, kwa mfano, kaka Abdalah ndiye aliyekuwa akilala na kaka Bahati baada ya kutoka Uturuki na baada ya baba kuondoka, na kuna dawa za asubuhi sana alitakiwa kumpa, hakuwahi kufanya uzembe kusahau hata siku moja.
Tuliporudi nchini, baba, mzee Magessa alitafuta madaktari wote wanaohitajika kwa ajili ya kaka. Aliacha ametukatia bima ya matibabu, hasa kwa ajili ya kaka lakini alitukatia sote. Tuliishi, tukifanya kila kitu kinachotakiwa kwa ajili ya kaka Bahati, taratibu nikaanza kuona mabadiliko kwenye afya na mwili wake. Baba alipiga simu karibu kila siku, akiulizia hali ya mgonjwa. Alituma pesa pia kwa ajili ya vyakula vya mgonjwa, kila mwezi mara mbili, kwani tulitakiwa kumnunulia maziwa fulani ya lishe, yanauzwa maduka makubwa ya dawa na yana bei sana. Pia alitakiwa kula matunda kwa wingi sana, kula almondi, zabibu kavu, mboga za majani kwa wingi, mayai ya kienyeji, samaki wabichi na vyakula kadhaa kwa ajili ya kumsaidia kupona kwa haraka.
Baada ya miezi mitatu, baba alikuja tena, tukafanya taratibu za kurudi tena Uturuki, lakini safari hii bima ya afya ililipia gharama zote za safari yetu, kasoro tiketi ya mtu mmoja tu, kwani mgonjwa alitakiwa kwenda na mwangalizi mmoja na si wawili kama tulivyoenda. Tulienda, madaktari wakashangaa sana maendeleo ya kaka, wakisema hii ni zaidi ya walivyotegemea. Kaka alikuwa ameanza kusimama na kutembea kwa kushikiliwa, japo hatua kadhaa, lakini pia alianza kutoa maneno ingawa kwa sauti kama ya mtoto. Ilinitia moyo sana kuona mpaka madaktari wanashangaa, nikaamini kweli mkono wa Mungu ndio uliofanya haya. Walimpima, wakatuhakikishia kwamba hakuna tena tatizo kwenye ubongo wake, na kwa jinsi anavyoendelea, inaweza chukua muda mfupi zaidi ya waliosema awali, kaka kupona kabisa.
Nakumbuka siku tumepata hiyo taarifa ya daktari, usiku wake nikiwa chumbani nilianza kuwaza kwamba japo nimekuwa mtu nisiyeamini utendaji na upendo wa Mungu, lakini sasa naona Mungu ameamua kunionesha kwamba yupo, ananipenda na amekusudia kunitendea mema. Nilihisi kama ni ndoto tu, kaka kuwa mzima tena, lakini sasa madaktari wenyewe walithibitisha kwamba ndoto hiyo itakuwa kweli. Akilini nilianza kumuona kaka Bahati akiwa mzima tena, akiwa anatembea, anaongea, anafanya kazi zake na ni mtu mwenye furaha.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Siku hiyo kwa mara ya kwanza kabisa, nilipiga magoti kitandani kwangu, na kuzungumza na Mungu kwa staili za mzee Magessa, nikasema, “Mungu, najua sijawa mtoto mzuri kwako, na nimejihesabia haki kuliko wewe. Suala la kaka Bahati nimelifanya kama kipimio kama kweli upo au la, na kama unatupenda, ili nikushutumu kwamba Wewe si mwenye haki, lakini sasa najiona mjinga. Umenionesha kwamba unanipenda, na tena unaweza kunitendea yale nikuombayo. Naamini kaka yangu atakuwa mzima tena, kama ambavyo madaktari wamesema, na ninajua sio kwa uwezo wao, kwani hata wenyewe wameshangaa hali ya kaka. Nashukuru sana kwa upendo wako, naomba unisaidie nisikulaumu tena.”
Sikuwa mtu wa kusali wala wa ibada kabisa wakati huo, na wala sikuwa najua namna ya kusali, lakini siku hiyo nilipangilia maneno kama mzoefu wa sala. Hapo nikaamini kwamba shida hufundisha, lakini mafunzo zaidi ni pale ambapo tunauona upendo wa Mungu katikati ya shida zetu. Katika kipindi kaka alichoanza kuumwa, nilianza kuwa nasali kama kujaribisha, ila si kwa kumaanisha, huku nikikumbuka kuwa nimesikia watu wakisema Mungu huponya. Lakini miaka ilivyozidi kwenda, nilikata tamaa kabisa na sikuwa naona umuhimu wa maombi hata kidogo, nikajiaminisha mambo mengi mabaya kuhusu Mungu. Lakini sasa, nilielewa kuwa nimeishi katika ujinga kwa miaka mingi. Pengine kuna mateso ambayo nisingepata kabla kama ningegundua umuhimu wa Mungu kwenye maisha yangu mapema.
Tuliporudi nyumbani safari ya pili, nilianza kuwa balozi mzuri kwa ndugu zangu pale nyumbani, kuhusu nafasi ya Mungu kwenye maisha yetu. Niliwaeleza vizuri kuhusu mtazamo wa madaktari wa kaka, mambo waliyosema kuhusu maendeleo yake, nikiwahakikishia kwamba hiyo ni nguvu ya Mungu. Kuanzia wakati huo, hata baba alipoondoka tena, tulianza kuwa na wakati wa kuomba na kumshukuru Mungu kama familia, kwa pamoja kila siku. Sasa nikaanza kuona kweli kuna mabadiliko ya waziwazi yanayotokana na maombi, kwani kaka Bahati alianza kuimarika afya yake kwa kasi sana. Tulishangaa kuona uwezo wake wa kuzungumza unaongezeka kwa kasi sana, akaanza kutamka maneno ya kueleweka. Pia alianza kutembea kwa kujitegemea, bila kushikiliwa, ingawa alitembea kama roboti, lakini hiyo ilikuwa hatua kubwa mno.
Maisha yalianza kuonesha nuru, na mwangaza kwa upya kwa familia hii ambayo ni kama dunia ilituterekeza. Tuliendelea kufanya ibada za kila siku, baadaye tukashauriana tumuite kiongozi wa ibada awe anashiriki nasi walau mara moja kwa wiki. Wakati huo mimi na Zita, tulianza kwenda kanisa moja la jirani kusali, kila Jumapili. Nilizungumza na mchungaji, akanielewa na kumpa jukumu kiongozi wake mmoja pale kanisani, akawa akija nyumbani siku za Jumamosi saa 12 hadi saa 2 usiku, tukishiriki ibada pamoja.
Madaktari uturuki walitutaka turudi baada ya miezi sita, lakini wakati huo baba hakupata nafasi, akashauri tusogeze miezi miwili mbele. Tuliporudi tena, hali ya kaka Bahati ilikuwa imeimarika zaidi sana kiasi kwamba mtu aliyemuona akiwa mgonjwa, hakumtambua kirahisi. Hivi sasa ninapoandika, kaka alisharudi kwenye afya yake ya awali, kabisa, na ninaweza kusema ni mzima na mwenye nguvu kuliko alizokuwa nazo awali. Ana afya na amani, ana uwezo mkubwa wa kufanya kazi zake, na kila nikimuangalia, naona muujiza mkubwa wa Mungu unaoishi na unaotembea.
Leo hii ni miaka kadhaa imepita tangu afanyiwe upasuaji, lakini hapo katikati kuna mambo mengi makubwa yametokea, kwa kaka Bahati, mahusiano yake, na hata kwangu pia. Ninachotaka kusema ni jinsi ambavyo maisha huweza kuwa machungu na magumu, ukapata maumivu na kutamani kufa, na hata wengine huchukua hatua za kujiua, lakini wanaokufa daima hawarudi bali huenda moja kwa moja, na hatujui yanayowatokea huko, ila naamini kuna maisha baada ya kufa. Kama umewahi kupata wazo la kujiua, kumbuka kwamba endapo maisha baada ya kufa yatakuwa machungu, hutakuwa na nafasi nyingine ya kuyabadilisha. Lakini maisha kabla ya kufa, yana kila nafasi ya kubadilika kuwa mema au mabaya.
Ikiwa uko katika hali nzuri sana ya maisha, usijisahau na kudhani ni milele yako, daima kuna mabadiliko, na pengine yako karibu nawe. Usalama wa maisha ya mtu uko kwa muumbaji wake, ninaamini Yeye ndiye pekee mwenye uwezo wa kufanya maisha yetu kuwa ya utoshelevu. Lakini pia endapo upo kwenye uchungu na ugumu kama ambao nilipitia, au zaidi ya huo, kumbuka bado Muumbaji wako ana mema mengi kwa ajili yako. Pia Yeye ndiye anajua watu sahihi kuweka kwenye maisha yako. Wakati tulipoangalia wenye mali na marafiki wa kaka kuwa ndio watakao simama pamoja nasi, lakini ni kaka Abdalah na dada Shanisa, ndio waliokuwa kama ndugu wa damu, bila kuchoka. Ukimkasirikia Mungu, na kujiweka mbali naye, unajichelewesha na mema yako.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kila hali unayopitia, si ya kudumu milele. Nilipompoteza mama yangu niliona kama nitakuwa mtu wa uchungu daima, lakini leo hii mimi ni mtu mwenye furaha sana. Mambo mengi yametokea katika maisha yangu na sikumbuki tena uchungu niliokuwa nao, imebaki historia tu.
MWISHO WA SEHEMU YA KWANZA
Najua unatamani kujua mengi zaidi, kuhusu hadithi hii, yenye uhalisia wa maisha ya watu wengi, lakini pia naamini umejifunza mengi katika hadithi hii ya ULIKUWA WAPI, TOLEO LA KWANZA. Nitakuletea TOLEO LA PILI hivi karibuni, nikikueleza zaidi kuhusu maisha ya kaka Bahati baada ya kupona, maisha yangu mpaka hii leo, Zita na taaluma yake na kaka Abdalah na dada Shanisa, na zaidi kuhusu baba zangu wadogo.
TOLEO LA PILI
Mimi: Dada mbona chenji uliyonirudishia ni pungufu?
Muuzaji: Shingapi imepungua?
Mimi: Elfu na mia tano
Muuzaji: Hiyo hapo
Nilishangaa kuona muuzaji anaongea kana kwamba tuna ugomvi, ilhali aliniita kwa juhudi nyingi akinikaribisha nikanunue nyanya kwake. Nilimtizama, nikitamani kumuonya kwa hasira, kwani nyanya zenyewe aliuza bei ghali kidogo zaidi ya wenzake. Huku nikifikiria nini cha kumwambia, niligundua ni sura ninayoifahamu. Mungu wangu! Ni yeye kweli? Nilijisemea akilini mwangu, nisiamini kile ninachokiona. Nina hakika hakunijua, na hata kama alinijua, hakutaka kabisa nifahamu kwamba amenitambua. Sikujua nianze vipi kumkumbusha, kwani angeona aibu sana na kujisikia vibaya, lakini kwangu ilikuwa fursa ya kipekee. Mpaka sasa sikuwa nimemsamehe kwa kile alichomfanyia kaka Bahati, na ingawa nilimuona katika hali mbaya sana ya kifedha, lakini sikuridhishwa na hiyo adhabu. Nilitamani mabaya zaidi yawe yamempata, kwani sikudhani kama anajutia alichokifanya.
Miaka mitano ilipita tangu kaka afanyiwe upasuaji, akaendelea kuwa sawa na mpaka kupona kabisa. Kwa msaada wa baba, mzee Magessa, maisha yalianza kuwa mazuri tena. Kaka alianza kujishughulisha na miradi yake, akafufua biashara yake ya kompyuta na vifaa vyake. Ndani ya muda mfupi sana, kila kitu kilibadilika, ingawa hatukuwa bado tumerudi katika hali ya awali, lakini maisha yalikuwa yameongezeka ubora kwa kiasi kikubwa. Kwa sasa nilijua kila kitu kuhusu biashara, na mimi ndiye niliyekuwa msimamizi mkuu wa biashara hiyo. Kaka aliniamini kwa kiasi kikubwa, na kuweka vitu vyote chini yangu. Sikubahatika kusoma kwa kiwango nilichotamani, lakini akili yangu ni nyepesi sana linapokuja suala zima la majukumu na pesa. Sikuwa na uzoefu wa biashara wakati naanza biashara na kaka, lakini haikunichukua muda mrefu kuweza kupata uzoefu katika kila eneo lihusulo biashara hiyo. Kwa sasa, kaka Bahati alinitegemea kama msimamizi mkuu wa biashara yake, hasa katika masuala ya wateja na wafanyakazi, kwani hayo ni maeneo yanayohitaji kutumia nguvu nyingi ya akili. Kwangu bado nilihisi kaka hatakiwi kuichosha akili yake kwa majukumu mengi, kwani sikutamani kabisa lile tatizo lijirudie hata kwa sehemu. Nilijitahidi sana kumpunguzia msongo wa mawazo, na kwa kiasi kikubwa nilifanikiwa katika hilo.
Baada ya kaka kupona, nilipata nafasi nzuri zaidi ya kumfuatilia Zita kitaaluma, nikagundua vitu ambavyo awali sikuvijua. Hakuwa akifanya vizuri sana shuleni, lakini pia hakufanya vibaya. Niligundua kuwa kuna vitu vingine amevifanya kipaumbele zaidi ya masomo, nilipofatilia shuleni. Mara kadhaa Zita alikusanya wanafunzi wenzake nje, au hata darasani, mwalimu akiwa hayupo, akaanza kuchekesha. Nilijua Zita ana uwezo mkubwa wa kuchekesha, kwani tangu zamani kabisa, aliwafanya watu wacheke kila alipokaa, lakini sikuchukulia kama hicho ni kipaji au kitu kinachoweza kumfanya mpaka akusanye watu. Hakuwahi kunihadithia, lakini niligundua wanafunzi wenzake walimpenda sana kwa tabia yake ya vichekesho. Hakuwa akikaa peke yake hata kwa muda mfupi, wanafunzi walimfuata kama nyuko wafuatavyo maua. Zita huangea sauti ya kipole, kana kwamba ni mtaratibu sana, kiasi kwamba huwezi kuamini kuwa sauti hiyo ya upole ina vituko vingi kiasi chake. Nilipofatilia zaidi niligundua kuna baadhi ya walimu wameshamgundua kuwa ni mchekeshaji sana, ingawa hafanyi hivyo mwalimu akiwepo darasani.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nakumbuka kipindi fulani nilialikwa shuleni kwao kwenye maafali, akiwa kidato cha pili, siku hiyo hata mimi sikuamini kuwa nina mdogo mwenye kipaji kikubwa namna hiyo. Kulikuwa na kipengele maalumu cha maonyesho ya vipaji, yaani talent show. Zita alishiriki kipaji cha uchekeshaji, au komedi, pamoja na wenzake wawili. Yeye alisimama wa mwisho kati ya hao wachekeshaji. Nilishangaa kuona kwamba pindi aliposimama tu, watu walianza kucheka, kabla hajafanya chochote. Alianza kuongea kana kwamba anasoma au ameandika mahali, kwani haikuwa rahisi kudhani kwamba vituko vyote vile alitoa kichwani. Kila alichoongea, watu walishika mbavu zao. Sikumuona kama mdogo wangu Zita ninayeishi naye nyumba moja, kwani vichekesho alivyotoa sikuwahi kuvisikia kwake wala kwa mtu mwingine yeyote. Muda wake ulikuwa dakika kumi tu, ambapo wenzake waliotangulia walipewa dakika pungufu ya zake, yaani tano. Alitumia muda wake vizuri sana, na kumaliza kwa wakati, lakini alipigiwa kelele nyingi, watu wakiomba aendelee. Nilimtizama, nikicheka sana, huku nikishindwa kuamini ni mdogo wangu anayefanya kadamnasi ya zaidi ya watu elfu mbili, wacheke kana kwamba wanamuangalia mchekeshaji maarufu duniani.
Kuanzia siku hiyo nilianza kuchukulia hiyo tabia ya Zita kama kipaji, nikiwaza ni namna gani kinaweza kikakuzwa na hata kumletea matokeo mazuri. Aliendelea na shule, na kumaliza, akapata daraja la tatu, kwa masomo ya sanaa. Nilimtafutia shule moja ya binafsi, akaendelea na kidato cha tano, masomo ya lugha. Akiwa shule hiyo, ndipo kipaji chake kilianza kuonekana kwa watu nje ya shule. Kuna mwalimu aliwahi kuniita na kunishirikisha kuhusu kipaji cha mdogo wangu, akiniambia kuwa anamtafutia mashindano ya vipaji vya uchekeshaji ili ashiriki na kukuza kipaji chake. Wasiwasi wangu ulikuwa atashuka kitaaluma, pengine hata kushindwa kupata ufaulu wa chini kabisa, lakini Yule mwalimu alisisitiza kwamba endapo tutapuuza kipaji hicho kikubwa, tutamnyima mtoto fursa ambayo wengi wanaitafuta duniani. “Vijana wenye uwezo mkubwa wa kuchekesha kama Zita ni wachache mno, hasa nchini kwetu. Kwa kipingi nilichomfahamu, kama mwalimu wa michezo na vipaji hapa shuleni, nimeona kipaji ambacho kusema kweli sikuwahi kukiona kwa mtoto yeyote aliyewahi kupita mikononi mwangu. Zita ana uwezo wa kuchekesha watu wa rika zote, na hata wenye huzuni au hasira. Huongea kana kwamba hataki kabisa kuzungumza, lakini kila neno analoongea, ni kichekesho. Zaidi ya hapo, yeye haoni aibu wala uwoga wa kuchekesha, na kila akipewa fursa ya kuwachekesha watu, huja na vitu vipya. Sijui akili yake huwa inawaza nini lakini kila anachokiona machoni pake, huweza kukiingiza katika vichekesho vyake.” Alisema mwalimu huyo huku akionesha ni jinsi gani kipaji cha mdogo wangu kilivyo cha kipekee na kinastahili kupaliliwa.
Zita alianza kushiriki mashindano na hata kuitwa kwenye maonyesho mbalimbali ya vipaji, akiwa kidato cha sita. Baada ya kumaliza kidato cha sita, alizidi sana kupata umaarufu kiasi cha kuwa anaitwa kwa malipo makubwa. Nakumbuka kwa mara ya kwanza, kuna mtu alimuunganishia, mkurugenzi wa kampuni moja kubwa nchini, akaitwa katika maonyesho ya vichekesho nchini Uganda, huku akishiriki pamoja na wachekeshaji mashuhuri sana. Kwa bahati, lugha haikuwa ikimsumbua, hivyo uwezo wake wa kuchekesha haukupotezwa na kubadili lugha na kutumia kiingereza. Nilisafiri naye kipindi hicho, kumtia moyo katika maonyesho hayo mapya na mageni kwake. Nilijisikia vizuri sana kuona anafanikiwa kuchekesha watu ugenini. Kulikuwa na mtanzania mwingine, lakini Zita ndiye aliyepewa fursa ya kushiriki maonesho mengine miezi mitano baadaye, nchini Kenya, huku wakimlipia kila kitu yaani malazi, na usafiri pamoja na kumpa pesa ya kutosha. Mwanzoni alifanya uchekeshaji kama kitu anachopenda, wala asifikiri kutengeneza pesa kupitia hicho kipaji, lakini siku zilivyosogea, pesa zenyewe zilianza kumfata, na sasa thamani yake ikaanza kuongezeka. Yeye ametumia historia ya maumivu ya maisha yake kama sehemu ya vichekesho vyake, na huwa nacheka sana ninaposikia akiwaweka kina baba wadogo katika komedi zake, ambazo nyingine nian hakika huwafikia kwani kwa sasa huonekana mara kwa mara kwenye vyombi vya habari. Kwa jinsi anavyoongea kwa upole, akianza vichekesho ambavyo ni sehemu ya maisha yake, watu hutaka kulia, lakini mwisho wake hucheka na kushikilia mbavu zao.
Kwa msaada wa Mungu, hivi ninavyoandika, mdogo wangu tayari ni mtu maarufu nchini na hata nje ya Afrika, kwani mwaka juzi kwa mara ya kwanza alipata mwaliko nchini Uingereza kuchekesha. Haijapita miaka mingi tangu aanze kufanya kipaji chache kama kazi yake ya kudumu, kwani baada tu ya kumaliza kidato cha sita, hakuwa akifanya shughuli nyingine yoyote zaidi ya kuchekesha, lakini ndani ya muda mfupi amefanikiwa kupata umaarufu mkubwa mno. Yeye hujiita Zitta Wanjie, na kwa sasa mpaka kwenye mitandao vichekesho vyake vimeenea na kuwa maarufu. Maisha yake sasa sio binti mdogo aliyeachwa na wazazi, aliyenyanyaswa na baba zake wadogo, aliyezurura mtaani, aliyemuangalia dada yake kama kila kitu, ambaye hakuweza kuvumilia kwa kumkosa dada yake kwa siku mbili, na mengine mengi, bali ni mwanamke mdogo tajiri na maarufu sana. Yeye hunitaja mara zote akisimama kuchekesha, hata kama siko katika maonesho. Huwa ananitambulisha kama ‘jeshi lake la kujitegemea’ na mara zote hunifanya nijihisi mtu maalumu sana. Kadiri anavyoendelea kuwa maarufu ndivyo na umaarufu wangu unaongezeka, na hiyo imetusaidia kwa kiasi kikubwa kukuza biashara zetu.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mara chache huwa napendelea kwenda kufanya manunuzi ya vitu vya ndani, siku za mwisho wa wiki. Kikawaida dada Shanisa huenda sokoni, au dada mwingine wa kazi tuliyemuajiri baada ya kaka kupona. Tulipoanza kufufua biashara, kuna kazi ambazo dada Shanisa na kaka Abdalah husaidia katika biashara, na hivyo kazi za nyumbani kuhitaji mtu, ikanilazimu kuajiri msichana wa kutusaidia. Siku moja nilienda na dada sokoni, Mabibo, kwani kuna vitu nilitaka kununua mwenyewe. Kuna sehemu huwa napenda kununua nyanya, maeneo ya Ununio, kwani huwa wanauza kutoka shambani kwa bei rahisi, hivyo mpaka tunamaliza manunuzi hatukuwa tumenunua nyanya. Lakini baada ya kutoka, nilikumbuka mara ya mwisho hatukupata nyanya Ununio, hivyo ikanilazimu kurudi ndani sokoni, kununua nyanya. Mimi hupendelea kuchagua nyanya mwenyewe kwani napenda ziwe nzuri sana, na zilizoiva. Nilirudi peke yangu mpaka sehemu walipojipanga wauzaji wa nyanya kama sita hivi, nikaangalia kwa haraka na kuona mama mmoja amepanga nyanya nzuri zaidi. Wakati huo, kama unavyojua sokoni, wauzaji wote waliniita kwa kunisihi niende kununua kwao, lakini nilichohitaji ni nyanya nzuri tu. Kuna ambao walitaja bei zao, nikaona ni nafuu sana, lakini nilimfuata mama huyu ambaye yeye bei yake ilikuwa juu kidogo. Nilipomfikia, na kuanza kumuuliza bei, licha ya kwamba awali aliniita kwa ushawishi, alionekana kunibadilikia na kuwa kauzu. Alijibu bei kana kwamba tuna ugomvi, akanifungia nyanya zangu, lakini katika kurudisha chenji alirudisha pungufu. Nilimuuliza kwanini amenirudishia hela pungufu, ila aliuliza tu imepungua kiasi gani, na kuniongezea kiasi kilichopungua.
Nikijiuliza kwanini mwanamke huyu mfanyabiashara amebadilika ghafla na kunionesha kama hanihitaji au nimejipendekeza tu kununua kwake, nikataka nimseme kidogo kwa tabia yake hiyo, nilimtizama usoni na kuhisi ni mtu ninayemfahamu. Alivaa blauzi ya rangi ya maziwa, lakini imepauka na kufubaa kana kwamba inataka kuwa ya kahawia. Chini alivaa kitenge kilichochoka sana, na kichwani alisuka mabutu yaliyoonekana yamesukwa kama wiki nzima au zaidi, iliyopita. Alionekana kuwa mwanamke mwenye shida sana kifedha, sio msafi na aliyezeeshwa na matatizo, ingawa hakuonekana kuwa na umri mkubwa sana. Nilimtizama kwa makini akijaribu kama kukwepesha uso wake, huku nikijiuliza kama ni yeye ninayemdhani au nimemfananisha. Kumbukumbu zangu kwa watu ninaowafahamu huwa si dhaifu. Nina uwezo mkubwa sana wa kukumbuka sio tu sura, bali hata jina na mahala nilipoonana na mtu, hata kama imepita miaka ishirini tangu tuonane. Nadhani ni kati ya watu wachache wenye uwezo mkubwa sana wa kukumbuka watu. Hata sikumoja, mtu hawezi kunifanyia kitu, aidha kizuri au kibaya, nikamsahau. Hata kama nimemuona mara moja tu, maadamu nimemuangalia na ameingia kwenye akili yangu, basi lazima nitamkumbuka tukionana tena.
Nilijua ninayemuona ndiye, na wala sijamfananisha, japo kila kitu kumuhusu yeye kilibadilika kabisa. Hakuwa yule mwanadada mrembo, aliyetaka aitwe anti Ketty, bali alikuwa mwanamke mwenye shida zinazoonekana mpaka kwenye ukucha wa mguu wake, asiyestahili hata kutumia neno anti kwenye jina lake. Ngozi yake ilipauka na kuwa nyeusi kabisa, nikagundua kumbe ule weupe aliokuwa nao ulikuwa wa mkorogo. Hakuwa na nywele zenye dawa, zilizobadilishwa nywele bandia kila wiki, bali sasa nywele zake za asili zilisukwa mabutu sio ya jana wala juzi, bali yaliyoshakaa kichwani pake muda mrefu. Nilipomtizama vizuri kichwani, niligundua kuwa huenda sehemu anayolala si safi, au labda hata kujijali kwa kuosha nywele na kusuka mpya kwake ni gharama. Nguo alizovaa nilishindwa kuelewa amezivaa kwa muda gani mfululizo. Ni kama mtu ambaye hakuwa na nguo zaidi ya hizo, kwa muda usiopungua miezi sita mfululizo, hivyo akilazimika kuzifua na kuzisubiria zikauke ili azivae tena. Nguo zilipauka na kuchoka sana, kiasi kwamba kama angepata nguo nyingine zaidi, angetupa zile haraka sana. Sikuuona uzuri wake hata kidogo, sikuona ile sura iliyoonesha utajiri, ile sura yenye kuvutia ambayo ilimpagawisha kaka. Nilijiuliza, “Nini kimemkumba huyu mwanamke, na mali zote zile alizomdhulumu kaka?”
Ilibidi niahirishe nilichotaka kumwambia na badala yake kumuuliza, “Dada samahani, nadhani ninakufahamu.” Akajibu kifupi, “Sijui”. “Wewe ni anti Ketty, mke wa kaka Bahati, sijakufananisha najua.” Nilimwambia, nikimaanisha zaidi kama mtu asiyetaka kudanganywa. Alinitazama kwa aibu sana, akashindwa kukataa wala kukubali. Nilipoona hajibu, nilimsalimia tu, “habari za siku? Vipi maisha?” Alinijibu kuwa kila kitu kiko sawa, nikamuaga na kuanza kuondoka. Nikiwa tu nimegeuza mgongo wangu, aliniita jina langu, “Zawadi,” nikageuka tena kwa haraka na kumfuata. “Tafadhali nipatie namba yako ya simu.” Akatoa kikaratasi na kalamu, akaandika namba yangu, akiniacha na maswali kuwa nini hasa anataka kwangu. Kusema ukweli nilijihami sana, nikijiandaa kwa mashambulizi endapo angenitafuta. Sikuwa najua nitamfanya nini haswa, lakini nilitamani nimtukane. Kama nisingekuwa nimeyabadili maisha yangu na kuwa karibu na Mungu, nina hakika huyu mwanamke angejuta kukutana tena na mimi, kwani ningeyaharibu maisha yake ambayo tayari yalikuwa yameharibika.
Nilirudi nyumbani, nikamuhadithia kaka Bahati na kaka Abdalah na dada Shanisa tuliokuwa tunaishi nao. Kila mtu alisema lake, isipokuwa kaka. Yeye alionekana kuchukuliwa na hisia nilipomuelezea, asiweze kusema chochote. Baadaye alisema, “Najua Mungu atakuwa amemlipa mabaya mengi mno, lakini ukweli ni kwamba simuhurumii. Nimejikuta nakumbuka jinsi nilivyompenda kwa dhati, nikamthamini na kumfanya awe mtu wa maana kati ya watu. Ninyi wenyewe hamkujua kuwa Ketty hakusoma, elimu yake ni darasa la saba nalo alifeli, na tangu namfahamu maisha yao yalikuwa duni kabisa, huku mama yake akijitahidi kumpatia mahitaji yake na kumfanya aonekane binti wa maana. Nilimpenda Ketty, kwa uzuri wake hasa, wa sura, rangi na umbo, lakini pia kwa huduma zake nzuri. Wakati nakutana naye, alifanya kazi kwenye mgahawa mmoja niliopenda sana kwenda kula mchana, kama mtu wa usafi. Alinihudumia kwa uchangamfu, akiwa amevaa nguo zake safi na kunipa tabasamu nzuri mara zote alipokuja kusafisha meza yangu. Nilimchunguza kwa miezi kadhaa, nikiangalia kama angefaa kuwa mke, na hatimaye nikaanza mahusiano naye. Alionesha kunipenda na kufurahishwa sana na uhusiano wetu, hata kunishawishi kufanya maamuzi ya kumuoa. Sikujua naoa janga kubwa la maisha. Ketty ameufanya moyo wangu kuwa mgumu kama jiwe, na baridi kama barafu, kwani ni kwa mara ya kwanza nilimthamini mwanamke na kufanya maamuzi ya kuwa na uhusiano wenye kesho (future), lakini ndio mara ya kwanza kuumizwa na mwanamke pia. Sina hamu tena ya kupenda, na hata kama Ketty angekuja kwangu kwa magoti na kulia sana, sina nafasi hata tone ndani ya moyo wangu ya kumfanya sio tu mpenzi, bali hata rafiki wa mbali.”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilielewa sana kaka alichomaanisha. Sikuwa nimebahatika kupenda kabla, nadhani pia moyo wangu niliufunga mlango unaoitwa mapenzi. Sikutamani kupenda na kuumia, sikutamani kupewa ahadi za uwongo. Kuna mara kadhaa wanaume walionesha kunitaka, wengine waume za watu, wengine vijana tu, wengine wa imani tofauti na mimi na wengine dini tofauti na hata dini yangu, lakini sikujali wala kuangalia ni nani anayenitaka. Nilikuwa na msimamo mmoja tu, “Sitaki mapenzi bado.” Sikuwa binti mdogo wakati huo, na mdogo wangu Zita tayari alikuwa kwenye mahusiano na mtu ambaye sasa ni mume wake. Mahusiano niliyoyaona kwa kaka Bahati na Ketty yaliniogopesha kuhusu mapenzi. Nilijiuliza, kama mtu anaweza kumfanyia hivyo mwanaume anayelala naye chumba kimoja, anayemvulia nguo mara zote, na aliyeweka ahadi kanisani kwamba atakuwa naye siku zote, je, kuna mapenzi ya dhati kati ya mwanamke na mwanaume? Niliamini moyo wangu una uwezo mkubwa wa kupenda na kujali, lakini nilihofia huyo nitakayempa moyo huenda asiwe salama kwangu. Pia nilihofu juu ya afya na maisha ya kaka Bahati sana. Kiukweli sikutaka kabisa kumuacha, wala sikutaka apate mawazo. Nilihofia kuwa endapo nitaolewa, nitashindwa kusimamia kazi zake vizuri, na hata kumjali kwa karibu. Mara kadhaa kaka alinisisitiza kuwa nahitaji kuwa na mume na kuishi maisha yangu, lakini nilimwambia wakati bado. Kwangu umri haukuwa kigezo cha kuwahi kuolewa, na hata ningefikisha miaka 40, sikuwa naona kama nimechelewa. Niliamini nitakapokuwa tayari, nitapata mtu sahihi na nitaolewa tu. Kwa maisha yangu yote, tangu nibakwe na baba mdogo, wanaume kwangu hawakuwa watu rafiki kabisa. Yaani ukiacha kaka Bahati, baba na kaka Abdalah, ninaweza sema hakuna mtu mwingine yeyote wa jinsia ya kiume niliyekuwa naye karibu.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment