Search This Blog

Friday, July 15, 2022

ULIKUWA WAPI - 2

 







    Simulizi : Ulikuwa Wapi

    Sehemu Ya Pili (2)



    Mshahara wangu wa kwanza haukuwa mwingi lakini kwa kipindi hicho, na kwa maisha niliyoishi, niliuona ni mwingi sana. Nilitoa pesa ya nauli tu na kula milo miwili kwa siku, iliyobaki nikampelekea mzee Magessa kuanza kupunguza deni. Siku hiyo sitaisahau kwa mshangao nilioupata, nilipompa baba Magessa ile pesa. Aliishika bahasha yangu ya pesa baada ya kumpa, akanishikisha mkononi mwangu, tukiwa tumekaa kwa kutazamana ofisini kwake, kisha akaniambia, “Sihitaji unilipe, ila nenda kawafanyie vivyo hivyo wengine wenye mahitaji.”



    Nilibaki nimemshangaa kama dakika nzima, nisijue nini cha kumjibu. Sikuamini kwamba kweli anamaanisha nisimlipe hata senti moja. Sikuwahi kufikiri kwamba wema wote ule alionifanyia, alimaanisha kunisaidia tu, bila malipo kabisa. Nilitamani nimbembeleze akubali nimlipe ili nitue mzigo niliokuwa nao, lakini neno alilosema niliona alimaanisha malipo makubwa zaidi ya ambayo ningemlipa. Sikutaka kumpa ahadi yoyote ya kutimiza alichoniambia, lakini machozi yalinitoka huku nikimwambia neno moja tu, ‘Nitafanya hivyo’ halafu nikapokea ile pesa na kuirudisha mfukoni.”



    Baada ya hiyo habari ya mzee Magessa ambayo binafsi niliona kama hadithi ya malaika wake, aliendelea kutueleza kwanini tunatakiwa kusamehe kwa kutuelezea maisha yake baada ya hiyo kazi yake ya kwanza. “Nilifanya kazi yangu ya kwanza kwa bidii sana kwani ndiyo ilinitoa kwenye kuombaomba. Lakini kilichonifanya nitie bidii zaidi, ukiacha baba, mzee Magessa, ni uchungu na maumivu niliyosababishiwa na ndugu zangu. Mzee Magessa alipokataa mshahara wangu, nilihifadhi zile pesa, nikasubiri baada ya miezi mitatu huku nikiendelea kuhifadhi pesa kiasi cha kutosha kana kwamba nina deni la kulipa. Nilipopata nafasi ya kuchukua likizo fupi ofisini, nilisafiri kurudi kijijini nilipotoroka, kwa lengo la kwenda kumuona kaka yangu na kumsaidia. Wakati natoroka Manyara nilimuaga kaka, najua alikuja kuwambia na wengine lakini haingedhuru nikiwa tayari nimetoroka.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Namshukuru Mungu, nilimkuta kaka yangu salama na maendeleo yake yalinitia moyo sana. Alianza kufanya shughuli ndogo ndogo za kumpatia kipato, akawa akiendelea na maisha japo ya kimasikini.

    Kaka alifurahi mno kuniona, na kuona kuwa maisha yangu yameendelea kulinganisha na wakati tunatengana. Nilianza kufanya mpango wa kumuhamisha pale nyumbani kwani licha ya kuwa alifanya shughuli zake binafsi, lakini alilazimishwa kutumia pesa zake zote kwa matumizi ya nyumbani. Pia siku zote walimfanya kama mtoto mdogo, tena mwenye tatizo, na sio kama mtu mzima. Walimuamulia kila kitu, walimgombeza na kumsimanga na hata watoto wa baba mkubwa aliowazidi sana, yaani umri wangu au wadogo kwangu, nao walimdharau.



    Nilifanikiwa kumuhamishia kaka Dar es Salaam, tukaanza kuishi pamoja kwenye chumba nilichopanga. Kipindi chote hicho nilikusudia kulipa kisasi kwa kila aliyenifanyia ubaya, kwa kadiri nitakavyoweza. Ndugu zangu baada ya kuona nainuka walianza kunitafuta. Unajua mali za wizi tena wa urithi huwa hazidumu hata kidogo. Karibu ndugu wote walikuwa sio wenye pesa tena, yaani utadhani baba hakuacha kitu. Jinsi walivyonitafuta ndivyo nilivyozidi kuwachukia. Niliwatukana, nikawajibu hovyo, niliwadharau sana, na hakuna niliyeongea naye kwa adabu. Nilianza kufurahia kila baya lililotokea kwenye maisha yao, na naweza kusema Mungu sio Athumani, yaliwapata mabaya haswaa. Baba mkubwa niliyeishi naye alipata ugonjwa wa kupooza, alifiwa na watoto wake wawili, alikimbiwa na mke wake, yaani tafrani. Wengine hivi ninavyoongea vijana wao wameishia kuwa wavuta bangi, watumia madawa ya kulevya, wengine wamefariki yaani kama wanatembelea laana. Lakini cha ajabu nafsi yangu haikuwa ikiridhika na kila baya lililotokea, ingawa nilifurahia moyoni.



    Nakumbuka kuna siku, nikiwa na miaka nane ofisini, nimeshapanda cheo na kuwa na nafasi nzuri zaidi, alikuja jamaa mmoja kutoka Afrika Kusini kwa ajili ya mafunzo ya uongozi kwa wafanyakazi. Nilihudhiria ile semina ya wiki moja, iliyofanyika hoteli moja hapa Dar. Kitu kilichonisaidia sana kwenye yale mafunzo ni kile alichosema katika mada ya KUJITAMBUA. Yule bwana alizungumza kuhusu nguvu ya msamaha, na namna kutosamehe kunavyoweza kuharibu hata utendaji wako wa kazi. Katika vitu alivyosema ni kuwa, tunapobeba uchungu na visasi tunayaathiri maisha yetu wenyewe, tunachelewesha maendeleo yetu wenyewe, tunawaumiza wapendwa wetu na kujiumiza sisi wenyewe.



    Huyu mtu alinifungua kugundua kuwa naishi maisha yasiyo na furaha wala utoshelevu, kwani kila nilipojaribu kupiga hatua, moyoni mwangu nilibeba watu. Kaka yangu Martin alikuwa amejitahidi kunifanya nisamehe, kwani alijua kisasi kinanitesa, lakini alishindwa. Nilifanya kazi kwa bidii lakini sikuwa na maendeleo makubwa. Nilifanya vitu vya kunifurahisha lakini sikuwa na furaha. Sikuwa na namna bora zaidi ya kulipa kisasi zaidi ya kutamani mabaya yawapate, lakini hata yalipowapata, sikuridhika. Niligundua jinsi ambavyo hata mahusiano yamenishinda kwa ajili ya kisasi. Mpaka nakuja kupata hii semina, nilishaisi miaka mingi mno ya uchungu.

    (Kaka Martin wakati huo alikuwa ameshajitegemea na kuoa, lakini alihamia mkoani Morogoro).



    Niliamua kuanzia wakati huo kujifunza kusamehe, na kwa kiasi kikubwa sana nimefanikiwa, ingawa imenilazimu kuishi bila kuingia kwenye mahusiano kwa kipindi kirefu ili nihakikishe naweza tena kuishi na mwanamke bila kumuumiza.”



    Siku hiyo nadhani kaka Bahati alisahau kwamba sisi ni wadogo zake wadogo ambao bado hatuelewi mambo mengi ya maisha bado. Aliongea na sisi kama watu wazima, lakini licha ya umri wetu hasa wa Zita ambaye alikuwa bado mdogo kabisa, mambo aliyotueleza yalitusaidia sote kusamehe. Nadhani alimaanisha kututaka kuachilia mambo maovu tuliyofanyiwa, huku tukiamini Mungu ndiye hulipa kisasi. Nililia siku hiyo, huku nikiiambia nafsi yangu kusamehe na kuachilia. Unajua kama hujawahi kujaribu kumsamehe mtu aliyekukosea sana, huwezi ukaelewa nini ninamaanisha. Nilihitaji kutoa uchungu na machozi, kuwaachilia wale niliowabeba moyoni, hasa baba mdogo Naise. Sikutaka niishi maisha yangu yaliyobaki kwa mateso kwa ajili ya kutosamehe.



    Tuliishi na kaka Bahati kwa miaka miwili bila shida yoyote, maisha yenye raha na utoshelevu, huku kipindi cha likizo, yule binti aliyemsomesha akija kusalimia na baadae kwenda kwa wazazi wake Morogoro. Kaka Bahati aliajiriwa kwa miaka kama kumi na kidogo, kisha akaanza kujiajiri, akafungua duka kubwa la kompyuta, akawa akiingiza kompyuta kutoka nje. Hiyo biashara ilimpatia pesa sana, kwani pia alikuwa akitoa huduma za kiteknolojia za kompyuta. Ndani ya miaka hiyo miwili tuliyoishi naye, kaka Bahati alipata mchumba, akatutambulisha kwake, akawa akija pale nyumbani mara kwa mara.



    Baadaye alitushauri atutafutie shule ya bweni kwani kwa sasa tuna uwezo wa kuendelea na masomo kama watoto wengine. Wazo hilo kwangu halikuwa baya, kwani niliamini anafanya hivyo kwa nia njema ya kutusaidia kimasomo, lakini niliogopa sana maisha mapya ambayo tungeyaanza shuleni. Kaka Bahati alinitoa wasiwasi kwamba wanafunzi ni watu wema, na walimu pia hivyo hatutapata shida tukiwa shuleni. Tulianza kusoma shule moja mkoani Moshi, ya wasichana, ambayo ilikuwa nzuri tu na hatukupata shida kama nilivyohofia mwanzo.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Likizo ya pili baada ya kuanza kusoma Moshi tulikuta kaka Bahati anakaribia kuoa, hivyo tukashiriki maandalizi ya harusi, mwezi huo harusi ikafanyika. Baada tu ya harusi, yeye na mke wake walisafiri, nasi pia tukarudi shule. Maisha yaliendelea, tukarudi likizo nyingine baada ya miezi sita. Kipindi hiki tulikuta mambo tofauti kidogo. Ule uhuru tuliokuwa nao pale nyumbani ni kama kiasi ulipungua, lakini haikunisumbua. Akili yangu ilishakua ya utu uzima kidogo, nikielewa kuwa yule mke wa kaka Bahati hatuchukulii kama ndugu zake wa damu. Nilielewa pia kwamba huenda yeye ndio sababu ya kaka kutoa wazo la kutupeleka shule ya bweni. Baada ya kipindi kile kaka Bahati kuongea nasi kuhusu kusamehe, nilianza kuizoesha akili yangu kutohisi watu vibaya, kuwa mtu chanya na kutohukumu kirahisi, hivyo hata mke wake, anti Ketty, sikumuhisi kwamba huenda anatuchukia zaidi ya kudhani kuwa pengine si mtu mwepesi kuzoea watu. Anti Ketty (kama alivyotaka tuwe tunamuita), hakuonesha mazoea na sisi kabisa. Alianza kutufanya tujihisi kwamba si wanafamilia wa nyumba ile, ingawaje kaka Bahati alijitahidi sana kupingana na hiyo hali.



    Nakumbuka tukiwa likizo hiyo, kuna wakati aliondoka sebuleni tukiwa tumekaa pamoja na kwenda kujifungia chumbani. Wakati mwingine hata chakula alienda kulia chumbani. Mara kadhaa, kaka alijaribu kumfata lakini alirudi peke yake. Kusema kweli hakututesa kwa lolote, kwa chakula wala malazi, bali ni ile hali ya kuonesha kutofurahia uwepo wetu ndiyo ilinipa wasiwasi. Tulirudi shule, muda ukapita, tukitumiwa pesa za matumizi kwa wakati bila shida. Mimi ni mpenzi wa kuandika tangu zamani, hivyo mara kadhaa nilikuwa nikimuandikia kaka Bahati barua. Nilifanya hivyo kabla hata sijaenda shule ya bweni, nilipenda kuandika barua fupi kumshukuru. Kwangu hii niliona ni njia sahihi zaidi kumuonesha jinsi gani moyo wangu una shukurani. Kuna wakati alijibu kifupi tu, “Asante mdogo wangu” na mara zingine hakujibu kwa kuandika.



    Nilipokuwa shule karibu barua zangu zote alijibu japo kwa kifupi. Kwangu huyu alikuwa kaka, baba, na ndugu pekee wa kiume. Nilihisi kama tulizaliwa na mama mmoja au aliachiwa jukumu la kutulea na wazazi wangu, lakini niliamini ni kama malaika Mungu alimleta kwenye maisha yetu kwa wakati sahihi kabisa.



    Kuna wakati baada ya kurudi shule, tulikaa muda mrefu bila kupata mawasiliano yoyote toka nyumbani. Nilimtumia barua kaka Bahati kumjulisha kuna mahitaji fulani shuleni kwa ajili ya sherehe. Shule tuliyosoma iliadhimisha siku ya wazazi mara moja kila mwaka, na sherehe hizo zilikuwa kubwa kwani zilijumuisha pia na sherehe za mahafali. Wazazi wa watoto wote walifika pale. Sherehe ya kwanza ya wazazi tukiwa shuleni hapo alikuja kaka Bahati na mke wake, wakati huo wakiwa wachumba bado.



    Kulikuwa na mahitaji maalumu kwa ajili ya sherehe hizo hivyo mbali na walimu kutuma barua kwa kila mzazi, ya mualiko na kumuorodherea mahitaji, nilimtumia pia barua kaka kumwambia mimi binafsi. Kaka Bahati hakuwa na kawaida ya kuchelewa hata kidogo ilipokuja uhitaji wa kitu chochote kwa ajili yetu, lakini nilishangaa mwezi mzima ulipita bila majibu. Nikaandika tena barua nyingine kwa kudhani kwamba hakuipata ile ya kwanza. Sikumtegemea sana kujibu kwa maandishi, bali niliamini angetuma hela zote na vitu vyote kwa haraka sana. Lakini hata barua ya pili hakujibu pia.



    Nilisubiri muda wa kutosha, nilipoona kimya, niliamua kumfuata mama mlezi wa wasichana, matroni, kumuomba simu ili niwasiliane na nyumbani, lakini mara mbili nilizopiga, simu yake haikupokelewa. Kaka Bahati hakutujengea mazingira ya kupiga simu kwani alihisi zinaweza kutuletea shida katika masomo. Hofu yake ilikuwa kama tungemtafuta kwenye simu tusimpate, ingeweza kutupa hofu na kupoteza umakini darasani. Kwake, barua ilikuwa njia bora zaidi aliyotaka niwe nikiitumia, na kuna wakati baada ya kupata barua zangu, yeye mwenyewe alipiga simu kwa matroni na kuomba kuongea na mimi. Haikuwa kawaida kupita miezi mitatu tukiwa shule, tusipate mawasiliano naye kabisa. Lakini kipindi hiki ilipita miezi mitatu, ikafika wakati wa likizo fupi ambazo kikawaida hatukuwa tunarudi Dar es Salaam.



    Kaka alituunganisha na rafiki yake aliyeishi hukohuko Moshi, tukawa tukiishi kwake likizo zote fupi. Safari hii wakati wa likizo haukuwa mzuri kabisa kwangu. Nilitamani ndani ya muda huo mfupi niende Dar kujua kama kuna kilichompata kaka yetu. Kwa huyo rafiki yake kaka Bahati, siku zote hapakuwa na shida, na waliishi na sisi vizuri bila kutunyanyasa. Nilijaribu kumwambia mke wake kuwa nahitaji kuwasiliana na kaka Bahati kwani amekuwa kimya sana, wakanipa simu kupiga, akapokea mke wake, anti Ketty. Nilimsalimu, akanijibu lakini alijibu kama mtu anayeongea na mtu asiyemfahamu, ikabidi nijitambulishe, akasema “Ndio, najua”. Nilianza kujieleza huku nikitamani anipe kaka Bahati niongee naye. “Nimejaribu kuwapigia nikiwa shule anti, lakini simu haikupokelewa. Mnaendeleaje?” “Vizuri!” alijibu kifupi. Nikamuuliza kama naweza kuongea na kaka Bahati, akanipa jibu ambalo lilinifanya nikae kwanza chini kwa mshtuko. “Bahati anaumwa, hawezi kuongea.”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Niliogopa sana, nikaanza kumuuliza maswali zaidi ambayo alijibu kwa mkato tu na mengine hakujibu. Niliuliza tatizo ni nini, ameanza lini, anaumwa kiasi gani na maswali mengine kadhaa. Lakini aliniambia kwa kifupi kuwa nitajua zaidi nikirudi likizo ndefu. “Kwasasa tulia msome, ukija likizo ndefu utaelewa zaidi. Lakini anaumwa na hawezi kuongea wala kujibu barua zako.”

    Jinsi anti Ketty alivyoongea, ni kama alizungumza na mtu ambaye hawezi kusumbuliwa na habari ya kaka Bahati kuumwa. Akilini nilijiuliza kama kweli anajua ni kiasi gani nampenda na kumjali kaka Bahati. Alichukulia kirahisi kweli, nadhani kwa sababu alijua sisi si ndugu wa damu labda. Wakati huo Zita alikuwa pembeni yangu akisikiliza. Alipoona nimeishiwa nguvu na kuanza kutoa machozi, yeye alilia zaidi yangu, kiasi cha kunifanya nijikaze na kumtuliza.



    Zita alihisi kwamba sasa tunakwenda kumpoteza kaka Bahati, huku akiamini kila anayekuwa karibu yetu huishia kufa. Mdogo wangu alimchukulia kaka Bahati kama baba yake kabisa, kiasi cha kuwa huru kwake kama mtoto anayependwa na baba. Mke wa rafiki wa kaka Bahati, anti Tesa, alitufariji kidogo kisha akatutaka twende kuoga na kulala. Wiki nzima hiyo ya likizo nilikuwa kama mgonjwa, nisijue nini cha kufanya. Sikuweza tena kupiga simu kuulizia hali ya kaka, wala sikuweza kuwaomba kina anti Tesa watusaidie. Nilichogundua, wenyewe hawakusumbuliwa sana na habari ya kuwa kaka Bahati anaumwa. Sikujua kuwa huenda wao wana taarifa zaidi kuliko sisi lakini hawakutaka kutuambia.



    Nilijaribu kumdodosa anti Tesa, lakini unajua si watu wote wako kama kaka Bahati. Watu wengi hawawezi kuweka mazoea hata ya kuwa na mazungumzo ya kawaida na watoto wasiowahusu. Kiumri, hatukuwa watu wa kuweza kujenga urafiki nao, ila pia kwao hatukuwa na undugu wowote. Kuishi kwetu pale ni kwa sababu ya heshima na mahusiano waliyokuwa nayo na kaka tu, na sio zaidi ya hapo. Nakumbuka muda mwingi tuliokaa pamoja ni wakati wa kula na labda wakati mchache tukiangalia luninga, ila nisingethubutu kuzungumza kitu zaidi ya yale ambayo wangeniuliza tu. Hali ya ukimya kati yetu haikunisumbua, isipokuwa wakati huu ambao nilihitaji kujua kuhusu kaka yangu na sikuweza. Nilijaribu mara nyingine kumuuliza rafiki yake mwenyewe tukiwa mezani, anko Faraja, naye akanipa jibu nisilolielewa, “Sijui ana tatizo gani lakini simu yake hapokei.”



    Siku ziliisha, nikarudi shule, nikawa nikiugulia sana moyoni. Nilitumaini kuna siku kaka Bahati atajibu barua zangu au labda atapiga simu, lakini haikutokea. Nilikuwa nikilia, karibu kila siku, bila matumaini. Sherehe ziliwadia, watoto karibu wote wakawa na wazazi wao siku hiyo, isipokuwa mimi na Zita. Zita alishiriki michezo ya maigizo, ila mimi sikuweza kushiriki chochote. Katika sherehe hizo, ilibidi nichukue baadhi ya pesa za matumizi tulizopewa wakati wa kuja shule, kutoka kwa matroni, nimlipie Zita mahitaji yake ya sherehe, lakini nikawaambia walimu kuwa sikuweza kununua vitu vingine.



    Nakumbuka siku moja, siku kadhaa kabla ya hiyo sherehe, wenzangu wakiwa bize sana na mazoezi ya hapa na pale, mwalimu wa michezo alinifata akaanza kuniuliza maswali. Sikuweza kumjibu vizuri zaidi ya kulia, na kumwambia kuwa mzazi wetu hataweza kuja wala hakuweza kutuma mahitaji yetu, ni mgonjwa. Mwalimu alinihurumia, nikaitwa ofisini badae, nikajieleza kidogo na kutiwa moyo. Walichukua namba ya kaka Bahati na kupiga tena simu lakini haikuwa inapatikana. Hapo ndipo nilihisi huenda ameshakufa, tumefichwa. Nilijihisi narudia maisha ya mateso yale niliyoishi. Nililia, nilikonda kipindi hicho na hata ufaulu wangu darasani ukashuka sana.



    Baada ya siku ya wazazi, hazikuwa zimebaki siku nyingi, tukafunga shule. Kikawaida, kuna basi ambazo zilituchukua kila ilipofika likizo, kutupeleka nyumbani kutoka shuleni. Wazai wote ambao watoto wao husoma nje ya Moshi, hulipia usafiri wa basi hizo mwanzoni kabisa wa muhula au wakati wa kulipa ada. Siku ya kuondoka, nilitamani hata ningepaa kufika Dar es Salaam. Safari yangu ilikuwa ndefu mno, nikiwaza nitakuta hali gani nyumbani. Tulisafiri kutoka Moshi, na kufika Dar mida ya jioni. Nilizoea kupokelewa na kaka lakini siku hiyo ilibidi tuchukue taxi hadi nyumbani.



    Nilifika, nikagonga bila kuitikiwa, nikafungua mlango ambao haukuwa umefungwa kwa funguo kisha tukaingia ndani. Nilimuuliza dada aliyekuwa jikoni, baada ya kumsalimu, kama kuna shida yoyote, akanijibu kwa hali ya huzuni kabisa, “Bosi anaumwa.” Moyo wangu uliogopa sana, nikajua kuna tatizo kubwa, kwani wakati dada anasema, machozi yalimlenga. Kwa mtu yeyote aliyemfahamu kaka Bahati kwa ukaribu, lazima angempenda na kumtakia mema. Yeye hakumdharau mtu, bali alimpenda na kumuheshimu kila mtu. Wafanyakazi wake wa ndani au wa kazini wote aliwachukulia kama watu wenye thamani kabisa, kana kwamba si bosi wao mkubwa. Kama kuna watu nimewahi kukutana nao wanaojua kuishi na watu vizuri, kaka Bahati nadhani anashika namba moja.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Niliulizia alipo, nikaambiwa yuko chumbani. Kabla hajaoa, tuliruhusiwa kuingia chumbani kwake, na mara nyingi nilikuwa nikimfanyia usafi. Lakini alipoingia kwenye mahusiano na kukaribia kuoa, aliomba tusiwe tunaingia chumbani kwake mara kwa mara. Alikuja kuniambia, alipokaribia kuoa kabisa, kuwa anti Ketty hapendelei mtu yeyote aingie chumbani kwake hivyo tusifanye hivyo tusije tukamkwaza. Kati ya vitu nilivyompendea kaka Bahati, ni uwazi wake. Yeye si mnafiki hata kidogo na mara zote alizungumza ukweli. Kitu kilichomuudhi alisema bila uwoga, alitufundisha kuwa njia sahihi ya kujitetea na kutoruhusu watu wakuonee, ni kuwa muwazi na mkweli, hivyo mara zote nilikuwa huru sana kwake nikiamini nikimkosea ataniambia ukweli tu.



    Nilimuuliza dada kama anti Ketty yupo, akasema siku hizi mara nyingi huondoka mapema na kurudi usiku. Nikaogopa, kwani nilijua kaka anakua peke yake muda mwingi. “Huwa namuhudumia mchana wote, wakati mwingine mpaka jioni. Pia Abdalah (kijana wa kazi) humuhudumia vizuri. Kwa sasa mtu yeyote anaweza kuingia chumbani kwao, kwani muda wote dada Ketty hayupo.” Alinijibu dada. Sikusubiri maelezo zaidi, nilikimbia chumbani kumuangalia, akanifuata Zita nyuma yangu.



    Sitasahau nilichokiona nikimtazama kaka Bahati. Sikujua nitazame juu nimlaumu Mungu, au nikae chini niomboleze. Kaka Bahati ni mtu mwenye mwili wa wastani kidogo, ila sio mwembamba kabisa. Rangi yake ni nyeupe, mrefu na mwenye uzito kama wa kilo themanini au zaidi hivi. Hupendelea kufanya mazoezi, hivyo ana mwili fulani mzuri wa kiume. Nilipomuangalia akiwa kitangani, nadhani kama ningemkuta wodini hospitali, bila kuambiwa ndiye, nisingemtambua. Alikuwa amekonda sana, sana yani, mpaka amekuwa kama kijana mdogo. Rangi haikuwa ile nyeupe, ilififia sana akawa kama maji ya kunde, na pia mdomo ulienda upande, macho nayo kama yameenda upande kama mtu mwenye makengeza. Alikuwa amelala chali, tulipoingia, akageuza kichwa kututazama. Hakuweza kuongea, alitoa sauti ya kuguna tu, akanyoosha mkono wake wa kulia kunipa. Nilimshika mkono, nikapiga magoti chini, na kuanza kulia. Kwakweli nilishindwa kujizuia kulia mbele yake. Zita ndio akalia zaidi kana kwamba ni msiba umetokea. Alinishika mkono kwa nguvu sana, machozi yakimtoka yeye pia, nadhani akitamani kutuzuia kulia.



    Tulikaa chumbani mule mpaka dada akaja kututoa, akaanza kutubembeleza akitufariji kuwa atapona tu. Siku hiyo niliona maisha hayako sawa hata kidogo. Haikuniingia akilini mtu mwema kama kaka Bahati aumwe kiasi hicho. Roho iliniuma sana, nikakaa tu chumbani nikilia sana. Sikuweza kula chakula wala usiku sikupata usingizi. Anti Ketty alirudi nadhani saa nne usiku, sisi tukiwa chumbani, hivyo hatukuonana naye. Kesho yake napo aliondoka asubuhi kabla hatujatoka chumbani. Yaani siku tatu nzima tangu tufike pale, hatukuonana naye, mpaka siku ya Jumapili, ambapo tulionana asubuhi wakati wa chai. Akatusalimia kana kwamba tumeonana naye jana, asituulize hata habari za shule. Baada tu ya chai, aliondoka tena, na siku hiyo hakurudi.



    Nilimuuliza dada kuhusu matibabu, akasema kuna daktari amekuwa akija pale nyumbani, lakini anaona siku hizi naye haji mara kwa mara. Nilianza kuwaza kama mtu mzima zaidi, nikajiongeza akilini na kujua kuwa anti hana uchungu juu ya mumewe kama niliokuwa nao mimi. Niliondoka na kwenda hospitali moja ambayo tulikuwa tukitibiwa. Kuna daktari ambaye kaka tulikuwa tukienda naye, aliongea naye kirafiki, nikaona watakuwa marafiki hivyo nikamtafuta ili aje kumuona. Kupata nafasi ya kuja nyumbani ilikuwa shida sana, ila alifanikiwa baada ya muda. Kaka Bahati alipata msaada wa matibabu lakini ilionekana ana ugonjwa mkubwa zaidi ya ambavyo nilidhani. Zilihitajika gharama kubwa zaidi na ingawa alikuwa na pesa nyingi sana, lakini anti Ketty ndiye aliyekuwa na maamuzi juu ya upatikanaji wa pesa zote kwa wakati huo. Kuna wakati alionesha ushirikiano ila muda mwingi hakupatikana na hivyo kufanya matibabu yawe ya shida sana.



    Muda wa kurudi shule ulifika ila hatukuweza kuondoka. Maisha pale nyumbani yalianza kubadilika, anti Ketty akidai ameshatumia pesa nyingi sana kumtibu kaka Bahati na hivyo pesa zimeisha. Ratiba zake hazikuwa za kushinda nyumbani, alitoka kila siku akidai anatafuta pesa na kuna wakati hakurudi, mara kadhaa nilisikia akizungumza na watu, muda mwingi aliokuwa nyumbani, hata usiku wa manane na kuna ambao nilimsikia akiongea nao, “anaendea vizuri ila yupo tu, madaktari wamesema hawezi kupona.” Hiyo sentesi iliniumiza sana, nikitamani nimwambie kuwa anachosema si sahihi. Kuna baadhi ya rafiki zake walikuja kumuona, lakini hakukuwa na mwenye msaada zaidi ya kumletea vitu ambavyo hata kula hawezi. Ni kama walianza kumkatia tamaa na hao marafiki zake. Nilitamani kama yule baba yake mzee Magessa angekuwepo nchini, lakini yeye na familia yake walihamia nje ya nchi, nchi ya Poland kabla hata hatujafahamiana na BahatiCHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Kaka yake mkubwa na kaka bahati alikuja tukiwa hapo nyumbani, akaanza kushughulikia matibabu. Kipindi amekuja kidogo anti Ketty alionesha adabu, akawa akiwahi kurudi nyumbani na kujidai anashughulika na matibabu ya mumewe, lakini alilalamikia suala la pesa akidai kuwa mumewe alikuwa na miradi yenye madeni makubwa hivyo hakuwa na hela wanazoweza kutumia muda mrefu bila kufanya kazi. Alidai kwamba yeye huhangaika kusimamia miradi, ila mumewe hakumtengenezea mazingira ya kusimamia miradi hiyo endapo yeye ni mgonjwa au amekufa. Binafsi tangu namfahamu anti Ketty, nilisikia mara kadhaa wakizungumza na kaka juu ya miradi na biashara zao kama watu wanaofanya biashara pamoja. Anti Ketty alimfanya shemeji yake amuamini na kuona kama mdogo wake alikuwa na ukatili fulani kwa mkewe. Nakumbuka kuna siku aliongea sentensi, ikanifanya nishindwe kujizuia na kutaka kusema mbele ya anti na kaka mkubwa kuwa wanachomuwazia kaka Bahati si kweli, ila nikaogopa. Wakiwa katikati ya maongezi, kaka mkubwa alisema, “Yaani Bahati nilidhani alishaachilia visasi vyake, kumbe mpaka kwenye ndoa bado ameonesha tabia za uchungu na kisasi alizokuwa nazo ujanani. Aliwaumiza sana mabinti akiwa kijana mdogo, kwajili ya hivyo visasi vyake, sasa nilidhani sasa hivi amekua, amebadilika.”



    Niliinuka pale sebuleni na kukimbia chumbani, nikalia sana yaani. Mtu pekee aliyewahi kunionesha upendo ambao ni wazazi tu wangeweza kunionesha, alikuwa kitandani kwa zaidi ya miezi sita, bila msaada wowote, huku hata ndugu yake wa damu akimuona ni mtu mbaya. Niliumia sana, nikitamani nikamshtaki anti Ketty polisi, kwa kitendo alichomfanyia, lakini hata kama ningepata ujasiri huo, sikuwa na ushahidi. Baada ya muda kaka mkubwa alirudi Morogoro, huku akiamini anti Ketty humuhudumia vizuri. Yeye alikuwa na kazi lakini hakuwa mtu mwenye kipato kikubwa, kwani hata mtoto wake alisomeshwa na kaka Bahati.



    Maisha yaliendelea kubadilika, huku anti Ketty akijiachia na mara kadhaa kutolala nyumbani. Tulishinda na kaka Bahati chumbani, wakati mwingine nikalazimisha atolewe nje tukisaidiana na Abdalah na dada, ili angalau apate jua, ingawa kumtoa ilikuwa kazi kubwa mno. Ilifika wakati maisha yakaanza kuwa magumu kwa hali ya uchumi kiasi cha kuanza kupata shida ya mahitaji ya kawaida. Kaka Bahati aliumwa, mwaka ukaisha, mwaka wa pili nao ukaisha, na mwaka wa tatu, akiwa ni mtu tu wa kulala, kuogeshwa na kusaidiwa kila kitu. Nawashukuru mno wafanyakazi wake wa ndani, kwani ilifika kipindi anti Ketty aliondoka na nguo zake, akidai anasafiri kikazi na hakurudi tena. Dada, pamoja na kaka Abdalah, walimuhudumia mno kaka kwa kipindi kirefu, bila malipo yoyote.



    Mimi na Zita ilibidi tuache shule, lakini mwaka wa pili wa kuugua kwake nilimtafutia Zita shule ya serikali ili walau mdogo wangu asome, amalize darasa la saba. Mimi niliamua kuanza kutafuta kazi za hapa na pale au hata kuomba ili tupate pesa za chakula ndani. Dada alitoa wazo la kuanza kuuza baadhi ya vitu vya ndani, ili tupate pesa za kuendelea kuishi huku tukimuhumia mgonjwa. Kaka Abdalah alisaidia, tukauza luninga zote tatu zilizokuwepo pale nyumbani, tukauza vitu vingi, pesa zikawa zikisaidia matumizi na dawa za vitamini za kaka Bahati, ila pia zikanipatia mtaji wa biashara ndogo ndogo za kutembeza bidhaa.



    Nilipata wazo la kuuza gari mbili zilizokuwa zimepaki pale nyumbani, lakini hatukujua kadi zake zilipo, hivyo zikawa zikikaa tu pale, huku mara kadhaa kaka Abdalah akiziwasha ili zisiharibike. Nilivyoendelea kukua, nikawa nikipata mawazo mapya ya namna ya kuendesha maisha kwa vitu vilivyopo, nikafikiria kukodisha magari lakini hayakuwa na vibali kwani yalishakaa muda mrefu, pia hayakuwa katika hali nzuri tena. Nikafikiria pia kuwa nyumba tuliyoishi Salasala, ni nzuri mno, tunaweza kupata mpangaji, sisi tukahamia nyumba ya kawaida. Nilipoongea na dada na Abdalah, wakakubali wazo langu, tulianza kutafuta mpangaji. Tulihangaika kama miezi sita bila kupata mpangaji, baadae tukampata, tukakubaliana naye kwa malipo ya miezi sita, kisha alipolipa hiyo pesa tukatafuta nyumba maeneo ya Tegeta, uswahilini kabisa, nyumba ya vyumba viwili na sebule, kisehemu kidogo cha kupikia kwa nje ila nilitafuta yenye choo ndani ili isiwe shida sana kwa kaka Bahati kupelekwa chooni.



    Kwenye nyumba hiyo mpya, yeye alilala na kaka Abdalah, sisi watatu tukalala chumba kingine. Tuliishi kama ndugu, sote watano, huku kila mmoja wetu akimchukulia kaka Bahati kama mtu aliyejitoa sana kwake hivyo kwa sasa anapotuhitaji zaidi hatuwezi kumtupa.Nilijitahidi siku zote apate chakula sahihi cha kula, na walau glasi ya maziwa kila siku, hivyo kwa kiasi kulikuwa kuna maendeleo kidogo kidogo ya afya yake, akaanza kuweza kunyanyuka na kukaa akisaidiwa.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Siku, miezi na miaka ilipita tukiendelea kuishi pale. Zita akamaliza darasa la saba akafaulu kuingia kidato cha kwanza shule ya serikali. Ikanipa moyo kwani sikuwa na pesa za kumsomesha shule ya binafsi. Hali ya kaka Bahati iliendelea kuimarika kwa kasi ndogo mno, lakini angalau kuna wakati tulikaa naye, akacheka tulipoongea, japo hakuweza kuzungumza zaidi ya maneno machache tu, nayo akiyasema kama mtoto mdogo. Tulifanikiwa kutengeneza magari mawili kwa ile pesa tuliyopangishia nyumba, tukawa tukipata wateja kuyakodisha japo kwa gharama ya chini sana. Hali ya maisha baada ya kupangisha nyumba na kuanza kukodisha magari ilikuwa na nafuu kidogo, tukaanza kupata pesa za kumpeleka kaka hospitali, lakini bado tumaini la kupona kwake halikuonekana zaidi ya hayo mabadiliko ya taratibu sana.



    Kuna wakati walitaka afanyiwe uchunguzi wa kichwa, lakini gharama ikawa kubwa sana, tukaahirisha mpaka msimu ujao tuliopokea kodi ya nyumba. Baada ya kufanyiwa uchunguzi huo, yaani MRI, alionekana ana tatizo kichwani ambalo hapa nchini haliwezi kutibika.

    Nilivyoendelea kukua, hizo habari za kaka kuumwa, niliona ni za kichawi tu, kwani sikuelewa kwanini awe na tatizo linaloshindwa kutibika na miaka yote hiyo halimuui wala haponi. Nilimlaumu anti Ketty siku zote, nikiamini ndiye muhusika mkuu wa hilo suala kwani hakuonekana kuguswa kabisa na kuumwa kwa kaka Bahati. Kama ningeulizwa ni kitu gani natamani zaidi ya kaka yangu kupona, ningesema ni anti Ketty naye apate ugonjwa kama wa kaka Bahati. Nafsi yangu ilimchukia huyo mwanamke kuliko bamdogo Naise aliyenibaka. Sikuona kama kuna mtu mwenye roho mbaya duniani zaidi yake, na labda adhabu pekee ambayo ingemfaa ni kupata ugonjwa wa namna ile na kukosa hata mtu mmoja wa kumuhudumia. Lakini kwa wakati huo sikuwa najua hata ni wapi anapatikana wala maisha yake yako katika hali gani. Nilihisi atakuwa na maisha mazuri tu, yenye furaha na amani, akifurahia mali za kaka Bahati, roho ikaniuma mno.



    Wakati tunahama, vitu vingi nilifanya kuhamisha kama vilivyo, bila kukagua ndani, likiwemo begi dogo lililokuwa chumbani kwa kaka, nililofungua na kuona kuna vitabu vingi tu. Siku moja niliamua tu nianze kupekua vile vitabu mule ndani nione ni vya aina gani. Wazo langu lilikuwa ni kutafuta vitabu vya hadithi za kuvutia niwe namsomea kaka Bahati, ili kuichangamsha akili yake. Nilipekua sana, nikipata vitabu vingi vya kiingereza tu na wala sikuona cha kunifaa. Lakini chini ndani ya kile kibegi, niliona kijitabu cha kuandikia cha mwaka, maarufu kama dayari (diary) ya miaka zaidi ya kumi iliyopita. Nilishawishika kupekua ndani ya ile dayari, nione vilivyoandikwa na kaka Bahati. Kuna baadhi ya vitu niliona ameandika, vikanifikirisha ikiwemo na siku aliyokutana na anti Ketty, ambavyo sitavizungumzia, lakini niliona baadhi ya namba za simu na anuani za barua pepe.



    Nilipokagua kwa makini niliona anuani moja ya baruapepe imeandika magessasr@hotmail.com . Akili ilinikumbusha kuwa huyu ni baba mzee Magessa, mtu pekee ambaye kaka Bahati alimchukulia kama baba yake mzazi na alikuwa na uhakika na upendo wake, kwani aliiandika kwenye mabano 'baba'. Nilifarijika kuona hiyo anuani, huku nikiwa na matumaini kuwa itakuwa bado inafanya kazi. Kwa uelewa wangu, niliwahi kusikia kwamba barua pepe ni njia bora zaidi ya kuwasiliana na mtu wa nje ya nchi, kwani mara nyingi watu hubadilisha namba za simu lakini si anuani ya baruapepe.



    Siku hiyo hiyo niliondoka pale nyumbani kwenda kutafuta sehemu ninayoweza kutuma baruapepe, nikaipata sio eneo la mbali sana. Nililipia, nikamuomba muhudumu aje anisaidie namna ya kumuandikia mtu baruapepe, akanisaidia kufungua akaunti yangu kwanza ili iwe rahisi kuanzisha mawasiliano na huyo mtu ninayetaka kumuandikia. Nilipofanikiwa, muhudumu alinishauri niongeze muda wa nusu saa zaidi ya kutumia kompyuta, ili nisikatizwe kabla sijamaliza kuandika, kwani pia sikuwa na kasi nzuri ya kuandika kwenye kompyuta. Niliongeza kiasi cha pesa, nikaongezewa dakika, nikaanza kuandika.



    “Baba, mzee Magessa, shikamoo. Naitwa Zawadi, sina hakika kama kaka Bahati alishakwambia kuhusu mimi, ila ni binti niliyechukuliwa kusaidiwa na kaka Bahati Gideon Ndegi miaka tisa iliyopita, mimi pamoja na mdogo wangu Zita. Nimebahatika kupata anuani yako ya baruapepe, hivyo nimeona vyema nikuandikie baruapepe kuhusu yanayoendelea kwa afya ya kaka Bahati. Bahati amekuwa akiumwa kwa muda wa miaka zaidi ya mitano sasa, na hali yake sio nzuri. Matatizo mengi mno yametokea tangu aanze kuumwa ikiwemo mkewe kumfilisi mali zake na kumtoroka. Tumejaribu kutafutiza pesa za kumtibisha, ila taarifa ya mwisho tuliyoipata ni kuwa ana tatizo kubwa kichwani ambalo haliwezi kutibiwa hapa nchini. Nimeandika kuomba msaada kwa ajili ya matibabu ya kaka Bahati, kwani amekuwa akiishi katika mateso, akihudumiwa kwa kila kitu, kwa muda mrefu sana. Nitashukuru kusikia kutoka kwako. Asante sana.”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Niliondoka hapo nikiamini baada ya siku mbili au tatu barua yangu hiyo itajibiwa, lakini nilirudi baada ya siku tatu, nisikute majibu yoyote. ilipita wiki nzima tena nikaenda lakini sikukuta majibu. Muhudumu alishauri kuwa huenda nimekosea anuani, lakini nilihakikisha nikaona sijakosea kabisa. Alisema kitu kingine, kikanifanya nipate wasiwasi na kama kukata tamaa kuwa nilichofanya ni kazi bure. “Kama anuani ni ya muda mrefu sana, inawezekana mtumiaji haitumii tena, alishafungua anuani nyingine, pengine alipoteza namba ya siri” alisema yule muhudumu. Nilipoteza matumaini yaliyokuwa yameanza ndani yangu, nikarudi nyumbani moyo ukiwa umeshuka kabisa. Baada ya kupata anuani ya mzee Magessa, nilipata tumaini kuwa kaka yangu anaenda kupona kwani niliamini mzee huyu angefanya juu chini kaka Bahati akatibiwe nje ya nchi. Nilipoona sijibiwi na hiyo taarifa ya muhudumu nilianza kufikiri kwa upya ni namna gani kaka yetu anaweza tena kuwa mzima, nisione njia kabisa. Nilikaa chumbani, nikalia sana siku hiyo, nikiiaminisha akili yangu kuwa hayo ndiyo maisha yake daima.



    Siku moja dada alitoa wazo la kwenda kwa mganga wa kienyeji tukiwa tumekaa watatu nje, kaka Bahati amelala ndani na Zita yuko shule. Tulianza mjadala kwa kufikiri kwamba huenda kaka Bahati alirogwa na mkewe, nikagundua sote watatu tulikuwa na mtazamo sawa, tukimuhisi hivyo anti Ketty. Dada alisema kama amerogwa basi tiba sahihi itapatikana kwa mganga wa kienyeji na ndio sababu siku zote hospitali hakuna kilichofanyika. Nilishawishika kuwa wazo hilo linaweza likawa na maana, tukakubaliana kwamba tuanze kumpeleka kwa waganga. Mimi ndiye niliyekuwa na ushawishi mkubwa kwa kaka Bahati, na hata wakati ambapo angekataa kula au kunywa dawa, basi mara zote nikimshawishi, angekubali. Niliamua nitaongea naye juu ya wazo la kutafuta waganga wa jadi watusaidie juu ya afya yake, kwani pamoja na ugonjwa wake kumuharibu kiasi kile, akili yake ilikuwa inafanya kazi vizuri tu, na tusingeweza kumfanyia maamuzi kama hayo. Ilikuwa ni lazima tumueleweshe na akubali mwenyewe kwanza.



    Niliingia chumbani muda ule ule, na kuanza kuzungumza naye kwa kirefu kiasi kuhusu ugonjwa wake na kuwa tunahisi ni ushirikina umefanyika, japo sikumwambia kuwa tunamuhisi mke wake ndiye aliyemroga. Alikubaliana na mimi kwa ishara, nikaendelea kusema kwamba kama amerogwa hospitali ni ngumu kumtibu, pia akakubali. Nikampa wazo la kwenda kwa waganga ili atibiwe huko, huku nikimpa shuhuda za waganga waliowahi kutatua matatizo ya watu, kulingana na maelezo niliyopewa na kaka Abdalah na dada. Hapo niliona sura yake imebadilika, akaonekana kupata huzuni sana kwa hiyo taarifa. Mimi najua sana kuongea, nina uwezo mkubwa wa kutumia maneno yangu kumshawishi au kumbembeleza mtu. Nilianza kuzungumza na kaka Bahati kwa kumbembeleza sana, nikimshawishi kuwa kwa mganga tutapata suluhisho la ugonjwa wake. Jinsi nilivyoendelea kumshawishi, ndivyo alivyoonesha huzuni sana, kiasi cha kuanza kutoka machozi huku akitikisa kichwa ishara ya kukataa. Nilimuelewa na kumtuliza, nikamuhakikishia kuwa hatutaenda kwa mganga kwani yeye hajakubali, akajitahidi sana kuongea maneno mawili, nikamsikiliza kwa makini, nikagundua ametamka "Magessa, Mungu."



    Sikuelewa kwa haraka anamaanisha nini kusema hayo majina mawili, lakini nilimtuliza tu na kumuahidi kuwa hakutakuwa na habari ya waganga, nikatoka kwenda kuwambia wenzangu kuhusu majibu ya kaka Bahati. Kidogo moyo wangu haukufurahia jibu lake, lakini sikutaka kabisa kumuudhi, na hasa alipoonesha huzuni na kulia, nilijisikia vibaya sana, nikamuhurumia. Binafsi niliona miaka mingi aliyokaa akiwa mgonjwa ingemshawishi kufanya lolote lile kwa ajili ya afya yake, ilimradi tu ajaribishe kama atapona. Tulianza tena kujadili, nikawambia alivyotaja hayo majina mawili, nikahisi labda anamaanisha Magessa au Mungu ndio watakaomponya lakini sikupata ushirikiano. Kesho yake, kuna wakati niliingia chumbani kwake, asubuhi, akaonesha ishara ya kutaka tuongee, nikakaa, akaanza kutamka tena yale maneno, Magessa, Mungu. Nilipata shida sana kumuelewa, nikijaribu kutoa maelezo tofauti kumuuliza kama ndicho anachomaanisha, bila mafanikio. Baadaye nikapata wazo, nikamuuliza, “Unamaanisha Mungu wa baba Magessa ndiye atakuponya?” Akajibu kwa furaha sana, kuonesha kukubaliana na mimi. Nikatamani aeleze sasa anataka tufanyeje, kwani baba Magessa yuko nje ya nchi na hatuwezi kumpata, sisi hatujui namna sahihi ya kumuomba huyo Mungu mpaka muujiza wa kupona utokee. Siku zote tumekuwa tukiomba kaka Bahati apone lakini hakuna kinachotokea, hivyo kwa uelewa wangu sikuwa naona kama kuna nafasi ya Mungu kumponya.



    Wiki mbili zilipita nikiwaza ni namna gani tutafanya ili kumsaidia kaka. Nilifikiria labda tuanze kumpeleka kanisani lakini kusema kweli sikuamini kwamba kunaweza kukawa na msaada. Sikujua kanisa sahihi la kumpeleka, sikuamini kwamba ataombewa na kupona papo hapo, hivyo niliona tutamsumbua tu. Kumtoa tu nje ilikuwa kazi kubwa, kumpeleka kanisani ingekuwa kazi kubwa zaidi, na labda ingekuwa ni mara moja tunampeleka kisha apole siku hiyo hiyo, lakini nilijua tungetakiwa kumpeleka kila Jumapili labda. Siku moja niliamua nikaangalie tena kama huenda ikawa imetokea bahati baruapepe yangu imejibiwa. Alinishauri dada kuwa labda ilitokea tu mzee Magessa alikuwa na shughuli nyingi, lakini sasa ameiona na kujibu, basi nikafanya hivyo. Sikuwa na matumaini kabisa ya kukuta nimejibiwa, nilifanya kujaribisha tu.



    Nakumbuka siku hiyo nilifika mtandaoni, kwanza nilikuta watu wengi sana, kompyuta zimejaa, hivyo ikabidi nisubiri kama dakika 20 mtu aondoke. Halafu mtandao ulikuwa unasumbua sana kiasi kwamba ilibidi yule muhudumu aniongezee nusu saa ya ziada tofauti na muda niliolipia, kwani zilipita dakika zaidi ya ishirini nashindwa kupata mtandao. Nilipofanikiwa, nikaangalia nisione barua ya baba Magessa, nikaumia sana, lakini niliona kuna baruapepe yenye anuani nisiyoijua. Niliifungua hiyo kwa haraka, na hiki ndicho nilichokuta.



    “Zawadi binti yangu, kaka yako Bahati aliniambia kuhusu wewe na mdogo wako. Amekuwa akisaidia vijana wengi sana, ingawa haishi nao kama ninyi, na mara nyingi huniambia, akinikumbusha kuwa ni malipo yangu. Nimeshtuka mno kupata taarifa za kuumwa kwake kwani siku nyingi sana nimekuwa nikimtafuta bila mafanikio. Nakumbuka kuna siku nilipiga simu yake ikapokelewa na mkewe, akaniambia Bahati amepumzika, nipige badae, lakini nilipopiga tena hakupatikana, mpaka leo. Bahati hakuwahi kutopokea simu zangu hata ningepiga usiku wa manane, wala hakuwahi kukaa miezi mitatu bila kuwasiliana na mimi, hivyo siku zote hizi nilikuwa nikijiuliza nini kimempata sipati jibu. Nimejaribu kumtumia baruapepe kadhaa, bila majibu. Mwaka huu nilikuwa napanga kuja Tanzania, na moja ya sababu ingenileta ni yeye. Nashukuru sana kwa kuwasiliana na mimi, ingawa ile anuani uliyotumia niliiacha siku nyingi, yaani sijui hata nini kimenituma leo kuiangalia tena, nikafufua nenosiri kwani nilishapoteza. Nadhani ni Mungu ameniongoza.”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nilisoma majibu ya baba Magessa machozi yakinitoka, nilihisi kama naota. Kabla hata sijamaliza kuisoma, nilijua tayari jibu la kaka Bahati limepatikana. Sikuwa na wasiwasi na huyu mzee na msaada wake, niliamini Mungu amemuhurumia kaka yangu na ameamua kumjibu kwa namna hii. Mwishoni wa barua yake mzee Magessa aliandika, “Ukitaka kuwasiliana namimi tena tumia anuani hii niliyotumia. Kuna mambo naweka sawa halafu miezi mitatu ijayo nitakuja Tanzania. Naomba ufanye juu chini ununue simu, hata ya bei rahisi kabisa, kisha unitumie namba yako ambayo nitawasiliana nanyi. Sitaki kukuuliza maswali kuhusu hali ya Bahati, ila ninaamini atapona.” Nilimjibu kumshukuru sana, nisiamini kama ni kweli ni yeye aliyejibu ile baruapepe. Nilirudi nyumbani nikiwa na furaha mno, sana yaani, siku tatu baadaye kuna pesa nikapata, nikanunua simu ya bei nafuu kabisa. Nilienda mtandaoni na kumtumia namba siku hiyo hiyo.



    Nilimuhadithia kaka Bahati kuhusu barua niliyomtumia baba Magessa na majibu yake, nikamuelezea kuanzia mwanzo nilivyohangaika na kukata tamaa, nilipomwambia kuwa amejibu na atakuja, siwezi kuelezea hisia alizoonesha. Tangu naanza kumuuguza, sikuwahi kumuona kaka Bahati na furaha kama siku ile. Alifurahi sana, alijaribu kuongea maneno ingawa yalikuwa magumu kueleweka, lakini aliongea kwa furaha, alicheka, machozi ya furaha yakimtoka. Alinishika mkono, akabusu mkono wangu, kunionesha kiasi gani anashukuru. Aliomba kutolewa nje, tukamtoa, akatumia muda mwingi amekaa kwenye kiti tofauti na siku zote. Kuanzia siku hiyo hata ulaji wake haukuwa wa kusumbua kabisa. Moyo wake ulichangamka, na alifanya kila kitu bila kulazimishwa au kubembelezwa kama awali, mfano kula, kunywa dawa, na mazoezi. Miezi mitatu kwetu ilionekana kama wiki chache tu, kwani zilikuwa siku zenye furaha na matumaini makubwa.



    Nilipokea simu ya kwanza toka kwa baba Magessa, nikamuelezea kwa kirefu kabisa kuhusu ugonjwa wa kaka Bahati. Nilieleza juu ya mke wake, na pia kuhusu dada na kaka Abdalah tuliosaidiana nao kumuhudumia kaka Bahati. Pia nilimwambia kuhusu hali ya maisha, jinsi ilivyotulazimu kuhama, kuacha shule na kila kitu. Niliona nimepata mtu ambaye anamjali kaka kama mimi na labda ni mtu pekee ambaye ningeweza kumwambia matatizo yote kwa uhuru, na kusema kweli alionekana kuwa sehemu kabisa ya shida zetu ingawa alikuwa mbali. Wiki chache baadaye alitutumia pesa kwa njia fulani wanayotuma pesa toka nje ya nchi, yaani Western union, kiasi cha dola 2000, yaani milioni tatu na kadhaa kwa thamani ya dola ya wakati huo, kwa ajili ya matumizi ya pale nyumbani. Kipindi hiki, kila pesa ikija ilikuwa inakuta mlolongo wa matatizo hivyo kiasi hicho cha pesa kilifanyika mkombozi mkubwa sana.



    Siku iliwadia, baba mzee Magessa akanitaarifu kwamba kesho yake ndipo angekuwa safarini kuja nchini, sote tukawa tukimsubiri kwa hamu. Lakini kesho yake jioni alipiga simu, kuniambia kuna dharura kubwa imetokea ya kifamilia hivyo ingempasa asogeze mbele safari yake kama wiki tatu au mwezi tena. Hapo sasa niliona ng’ombe wa masikini hazai. Nilijisemea moyoni kwamba haya ndiyo maisha yetu na sote tutakufa katika shida hizi. Akili iliniambia kwamba baada ya huo mwezi kuna dharura nyingine itatokea, na hivyo hatakuja. Nilitamani nisimwambie kaka Bahati, ambaye alikuwa na furaha na msisimko kuhusu ujio wa mzee Magessa, lakini ilibidi nitafute namna ya kumueleza ukweli tu, ili ajipe muda zaidi wa kusubiri. Tuliendelea kusubiri, huku nikiiaminisha akili yangu kwamba hatokuja, ili nisiwe na matumaini hewa.



    Aliposema kuhairisha safari, mawasiliano pia yalianza kuwa hafifu kidogo, ikawa ikipita zaidi ya wiki hajapiga simu. Ulipita mwezi mzima, nikashindwa kumuuliza tena anakuja lini, nikisubiri kama yeye mwenyewe atasimamia ahadi yake ya kuja, lakini zilipita tena wiki mbili, hajaniambia chochote. Hapo nikawa sasa nimekata tamaa kabisa, najipanga kuendelea kuishi tu. Kaka Bahati japo naye alionesha huzuni na kukata tamaa lakini mara kadhaa alijitahidi kuwasiliana nasi akituambia kuwa Magessa atakuja. Inaonekana imani yake juu ya ujio wa mzee Magessa ilikuwa kubwa kuliko yangu. Sikutamani aendelee kumngoja kwa matumaini kwani nilihisi angeumia sana asingekuja.



    Siku moja ya Jumamosi, mida ya saa tano asubuhi, niko jikoni naandaa supu ya maziwa kwajili ya kaka, nilipokea simu, namba siifahamu.



    Kwenye simu: Halo?

    Mimi: Halo, nani?

    Kwenye simu: Mimi ni dereva wa taxi, nina mgeni wako, naomba unielekeze mnapoishi.

    Mimi: Sawa, subiri nikupe mtu akuelekeze



    Hapo nilikimbia kumtafuta kaka Abdalah, nikampa simu bila maelezo zaidi ya kumuomba awaelekeze hapo nyumbani, huku nikisubiri amalize nimuulize ni kina nani. Sijui akili yangu ilikuwa inawaza nini, lakini nilihisi kaka Abdalah atajua ni mgeni gani analetwa. Nilihisi na kutamani awe mzee Magessa, lakini sikutaka kujipa hayo matumaini kwani ni lazima angenitafuta kabla ya kuanza safari, nilijisemea. Kaka Abdalah alitoa maelekezo tu, kisha simu ikakatwa hivyo wala hakujua ni mgeni gani anakuja. Sote tukawa tukisubiri kumuona huyo mgeni, ila sikumjulisha kaka Bahati.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Eneo tuliloishi ni uswailini, lakini panaelekezeka hasa kwa mtu mzoefu kama dereva taxi. Zaidi ya saa nzima, tulimsubiri huyo mgeni. Nilipoivisha supu, tulimtoa kaka uwani, tukawa tumekaa naye, mimi na Zita. Zita mdogo wangu ni mtu mwenye hadithi nyingi sana za vituko. Mara nyingi akikaa na kaka Bahati humchekesha kwa hadithi za wanafunzi wenzie, hivyo muda mwingi aliokuwa anakuwa nyumbani, akiwa hana kazi za shule, nilipenda akae naye ili amchangamshe. Tukiwa uwani, kibarazani tumekaa, gari ilipaki mbele kabisa ya nyumba, akashuka mwanaume mmoja mtu mzima, wa miaka kama 60 hivi, mrefu, mwenye mwili wa wastani. Akaja moja kwa moja alipokaa kaka Bahati, huku kaka akimuangalia, na kutoka machozi. Yule mwanaume alimshika kaka mikono yote miwili, akamuinua, akamkubatia kwa muda mrefu kabisa, naye akitokwa na machozi. Nilijua huyu ndiye baba mzee Magessa. Nilimpisha kiti, wakakaa baada ya kukumbatiana, tukasalimiana naye pia, alinikumbatia na mimi, akitusalimia mimi na Zita kama watu anaotufahamu.



    Niliona siku hiyo kaka Bahati alivyotamani kueleza furaha yake, kumuona mzee Magessa, lakini hata kuandika hakuwa anaweza. Alijaribu kuongea maneno machache tu, akimshika mkono mzee, na kumbusu mara kadhaa, nikamwambia baba kuwa anaonesha kiasi gani anakushukuru. Tulimuhudumia baba, kwa supu kama ile tuliyompikia kaka Bahati. Mzee Magessa ni mtu rahisi sana kujichanganya. Humpi chakula akakataa, hajali sana anakaa katika mazingira gani, na nadhani kama mule kungekuwa na chumba cha ziada, angelala pale, japo ni mazingira duni sana kulinganisha na maisha aliyozoea. Tofauti na nilivyotegemea, hakuonekana kushangazwa na hali ya pale ndani, wala muonekano wa kaka Bahati. Alikuwa mwenyeji na mzoefu ndani ya muda mfupi sana, akaanza kutupa hadithi za huko ughaibuni alikotoka.



    Ujio wa mzee Magessa ulituchangamsha sana pale nyumbani, hasa kaka Bahati. Ile hali ya ugonjwa na udhaifu uliopitiliza ikapunguzwa na uchangamfu wake. Jioni ya siku hiyo baba, mzee Magessa alilazimisha tutoke kwa ajili ya chakula cha jioni. Kwa mara ya kwanza, tangu aanze kuumwa, kaka Bahati alitoka kwenda kwenye hoteli nzuri kula chakula. Siki hiyo nilikumbuka kaka alivyokuwa akitutoa kwa chakula cha mchana, au cha jioni , au matembezi tu ya mwisho wa wiki, mara kwa mara. Nilikumbuka pia mara ya mwisho tulitoka tukiwa na mke wake, anti Ketty, akaanza kutueleza jinsi gani anampenda yule mwanamke. Kaka kiasili ni mtu muwazi, asiyejua kuficha hisia zake, aidha za upendo, hasira, furaha au zozote zile, na nina hakika mkewe alijua ni kiasi gani alimpenda. Sikuelewa ni kwanini mwanamke huyo aliamua kumlipa ubaya mwanaume aliyempenda kiasi kile.



    Baada ya chakula, tulirudi nyumbani na taxi kisha mzee akaenda hoteli fulani nzuri jirani alipofikia. Kitu kilichonifurahisha zaidi tulipokaa kwa chakula cha jioni siku ile, tukiwa sote watano pamoja na mzee Magessa, ni namna ambavyo baba alifanikiwa kumpa matumaini kaka Bahati ya kupona na kuendelea na maisha. Nakumbuka alizungumza maneno haya na kaka kwa hisia kabisa, bila kujali kama anauwezo wa kumjibu au la.



    “Bahati kijana wangu, hakuna mbegu njema inayopandwa kwenye udongo mzuri ambayo isiyoota na kuzaa matunda. Unakumbuka uliponifuata kuanza kunirudishia ile pesa niliyotumia kukusomesha, kitu nilichokwambia? Nilisema, nenda ukawafanyie hivyo wengine. Si kwamba nilikuwa na pesa nyingi za kutupa ndio sababu nilikataa pesa zako, au labda nilishindwa kuzichukua na kusaidia watu wengine mimi binafsi, lakini nilitaka kupanda mbegu njema ndani yako. Watu wengi wanashindwa kufikia ndoto na malengo yao kwa kukosa fursa. Nilihitaji nikupe fursa ya kutimiza ndoto zako, halafu nikupe fursa ya kusaidia wengine kutimiza ndoto zao. Fursa ya kwanza ni yenye manufaa kwako binafsi zaidi, lakini fursa ya pili ina manufaa kwako, na kwa wahitaji na wenye shida. Watu ambao dunia haiwaoni, watu ambao hutoa machozi mbele za Mungu wakihisi wameachwa na kukataliwa. Kusaidia mtu wa namna hiyo, hubadilisha machozi yake ya kilio kuwa machozi ya kukuombea wewe uliyemsaidia. Najua mimi ni kati ya watu umekuwa ukiwajali na kuwaombea sana kwenye maisha yako, na ninajua mafanikio makubwa niliyonayo leo ni kwa ajili ya maombi yako na ya wengine niliowahi kuwasaidia.



    Mungu si dhalimu, asahau sadaka zako ulizotoa kwa kusaidia watu, au apuuze maombi ya wengi uliowasaidia. Wengine ni kweli tunawasaidia na kuwatoa kwenye shida zao, lakini hawakumbuki fadhila wala hawana shukrani, nao ni wengi sana. Lakini mimi naamini kila msaada unaoutoa bila kutaraji malipo, ni sadaka mbele za Mungu, na hata mwanadamu asipoona uzito wake na kushindwa kushukuru, Mungu hupokea sadaka hiyo na kukubarikia. Ninachokuhakikishia ni kwamba, hapa ulipopita ni kwa sababu njema, lakini hautakaa hapo milele. Sio kwa sababu mimi nimekuja, lakini kwa sababu Mungu anakupenda.”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Maneno yake yalifanya si tu kaka Bahati atoke machozi, ila pia sote tuliomsikiliza akizungumza. Niligundua ni kwanini mzee huyu huonekana mwenye afya na kijana zaidi ya umri wake ulivyo. Kichwa chake kilijaa mvi lakini muonekano wa ngozi yake ulikuwa kama wa kijana mdogo. Kaka Bahati aliwahi kuniambia umri wake nyuma, lakini ilikuwa nikimlinganisha na watu wa umri wake ni kama wamemzidi miaka kama kumi hivi. Moyo wake ulikuwa mwema mno, wenye huruma. Ni mzee mwenye macho yenye kuona shida za watu, mwenye mikono mikubwa kufikia wahitaji na mwenye masikio yanayosikia vilio vya wengi. Huyu baba aliithamini kila shilingi yake, ingawa alikuwa na pesa nyingi; hivyo hakuwa mtu wa kufuja mali. Lakini hakuona thamani kubwa ya kitu chochote zaidi ya uhitaji wa mwanadamu. Hakuogopa kutoa, bila kujali anayempa atamlipa, atamfaa au atamsaidia, na bila kujali ni msaada mkubwa kiasi gani. Kila mara moyo wake ulipomuongoza kutoa, alifanya hivyo bila kubagua. Tangu naanza kumsikia kwa kaka Bahati, nimesikia mambo mengi sana mema kumuhusu, lakini baada ya kumuona na kumfahamu zaidi, niligundua ni kati ya watu wenye mioyo ya utoaji wa ajabu, anayejitoa si tu kwa mali, bali pia kwa utu wake.



    Siku iliyofuata asubuhi sana mzee Magessa alikuja, akaanza kushughulikia kwa upya matibabu ya kaka. Tulienda hospitali ya Aghakan, tukaonana na daktari wa mishipa ya fahamu. Baada ya vipimo kadhaa, alishauri kama itawezekana apelekwe nje ya nchi kwa upasuaji. Ilionekana ana tatizo la kichwa lakini sehemu lililogusa ni mishipa makini sana ya fahamu na kama pataguswa vibaya basi anaweza kupoteza maisha au abaki hivyo milele. Lakini alisema kuna nafasi ya kupona kama atapata wataalamu na maabara makini zaidi za upasuaji. Niliona uso wa mzee Magessa umeonesha hofu kidogo baada ya maelezo ya daktari, lakini tukiwa njiani tunarudi nyumbani alianza kunitia moyo, akiniahidi kwamba kaka atapona tu. Mara kadhaa hatukutaka kumsumbua kaka Bahati, isipokuwa siku za vipimo, vinginevyo mimi na mzee Magessa tulikuwa tukifuatilia mambo mengine ya hospitali yakiwemo majibu. Kulingana na yule daktari mtaalamu wa Aghakani, kwa nchi yetu, hata kama wataalamu wa kufanya huo upasuaji wanapatikana, lakini maabara zetu bado sio za hali ya juu sana, na pia gharama ingekuwa kubwa zaidi kuliko kumpeleka nchi kama India au Uturuki, ambapo kuna maabara nzuri zaidi pia.



    Mzee Magessa alianza kushughulikia namna ya kumpeleka kaka nje kutibiwa. Aliwasiliana na baadhi ya watu wake, kukawa na machaguo matatu ya hospitali nzuri zaidi za matibabu. Kulikuwa na India, Uturuki na Thailand, ambapo ndipo ingewezekana kwenda kwa gharama nafuu, na kwa matibabu mazuri kwa haraka. Mwisho iliamriwa ataenda Uturuki, zikafanywa taratibu zote, nikaacha mambo sawa pale nyumbani, tukasafiri mimi, kaka Bahati na baba. Ilikuwa mara yangu ya kwanza kusafiri nje ya nchi, tukafika nchi nzuri sana hata zaidi ya mara kumi ya Tanzania, kuanzia uwanja wa ndege, lakini sikuwa na muda wa kushangaa wala kuangalia uzuri wa mji ule mpya. Hamu na shauku yangu ilikuwa ni kumuona kaka yangu akiwa mzima tena. Nilitamani nisikie wataalamu wa nchi ile wanasemaje kuhusu afya ya kaka.



    Tulienda hospitali fulani katika mji mmoja unaitwa Antalya, hospitali kubwa kuliko zote nimewahi kuona kabla. Hiyo hospitali ilikuwa na hoteli yake pembeni, tuliyoishi kaka akiwa ameanza kufanyiwa vipimo. Vilifanyika vipimo mpaka kupata majibu, wiki ile ya kwanza yote ikawa imeisha, lakini mwishoni mwa wiki, tulionana na daktari, aliyetuelezea kwa undani kuhusu tatizo la mgonjwa wetu na kutushauri tufanye maamuzi mapema afanyiwe upasuaji. Majibu hayakutofautiana sana na ya nyumbani, Tanzania, ingawa yale yalionesha mpaka ni kiasi gani tatizo limeathiri sehemu za mwili wake. Kulingana na maelezo ya daktari, kulikuwa na nafasi ya kupona au kufa wakati wa upasuaji, kwani ingewalazimu kugusa sehemu muhimu sana za fahamu. Ilitakiwa kaka apasuliwe katika muunganiko wa uti wa mgongo na ubongo, upasuaji ambao ni wa kitaalamu sana na wenye hatari kubwa. Kaka hakutakiwa kabisa kuwa na hofu wala msongo wa mawazo katika maandalizi ya upasuaji wake, hivyo katika vikao vyetu na daktari yeye hakuwepo. Mzee Magessa alijitahidi kuzungumza naye bila kumuonesha hatari iliyopo kwa maisha yake, au ya kupoteza viungo vyake. Siku ya upasuaji ilipopangwa, baba alikaa kuzungumza na kaka tena akimtoa hofu juu ya matibabu.



    “Bahati mwanangu, safari ya kuelekea afya yako ndiyo tunaianza siku mbili zijazo. Kumbuka kama ambavyo jina lako lilivyo, maisha yako ni yenye bahati, na wewe binafsi ni bahati kwa watu, hivyo bado una siku nyingi za kuishi ukiwa na afya. Usiruhusu akili yako ikwambie kwamba utakufa, au utaendelea kuwa mlemavu. Naamini utapona kabisa, na maisha yako yaliyobaki yatakuwa ya furaha kuliko ya awali. Ondoa kinyongo chochote ndani yako, juu ya mke wako, kaka yako na hata marafiki waliokutelekeza, ukijua kwa hakika Mungu ndiye aliyeshikilia hatima ya maisha yako.” Mzee Magessa alimwambia hayo maneno akimsaidia kujiandaa na upasuaji. Kwangu niliona kama sio tu anamuandaa na upasuaji, bali anamuandaa na maisha baada ya upasuaji. Kitendo cha kumwambia aondoe kinyongo kabisa kwa wote waliomuumiza, akilini kilinifanya nihisi kama huenda baba anahofia kaka Bahati atapoteza maisha, hivyo asiye akafa na kinyongo. Hayo mawazo yalinipa hofu kubwa mno.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nakumbuka usiku mmoja kabla ya siku ya upasuaji nilienda kujisaidia kama mara kumi hivi, nikiharisha kwa hofu. Nilitamani nimwambie mzee Magessa kuwa tusikubali upasuaji kwani kaka atakufa. Hakukuwa na faida kwangu, kwa upasuaji huo endapo kaka yangu angekufa. Sikutamani kuishi bila kumuona, na hata kama ingenilazimu kumuhudumia akiwa katika hali ile mpaka uzee wake, kwangu ilikuwa ni sawa kabisa. Niliogopa mno, kiasi kwamba sikujua saa nane ambazo daktari alituambia wangetumia kumpasua, ningekuwa katika hali gani.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog