Simulizi : Namtaka Mpenzi Wangu Arudi
Sehemu Ya Nne (4)
Alichokisema Linda ndicho alichokifanya, siku iliyofuata akaamka asubuhi na mapema na kwenda katika Kituo cha Polisi cha Osterbay na kufungua jalada la kesi huku akimshutumu Dickson kwa kumbaka msichana ndani ya chumba cha hoteli.
Polisi hao wakataka kujiridhisha na hivyo kuangalia video ile. Kwa jinsi ilivyoonekana ilikuwa rahisi sana kujua kama Dickson alikuwa akimbaka Amina kitandani walipokuwa.
“Hii ni kesi kubwa sana! Huyu msichana yupo?” aliuliza polisi mmoja huku akimwangalia Linda.
“Amejaa tele!”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Basi mlete kwanza tuzungumze naye.”
Hilo halikuwa tatizo kabisa kwa Linda, akawasiliana na Amina na kumwambia kilichokuwa kimetokea polisi na hivyo mtu aliyekuwa akihitajika alikuwa yeye tu.
Hakukuwa na tatizo lolote lile, kwa sababu tayari alikuwa amekula pesa za msichana huyo, hakuwa na jinsi kushirikiana naye. Siku hiyohiyo akaelekea katika kituo hicho cha polisi ambapo akawaambia polisi kwamba kweli alikuwa amebakwa na mwanaume huyo chumbani.
“Alikubaka hotelini?” aliuliza polisi mmoja.
“Ndiyo!”
“Duuh! Sasa wewe ulifuata nini kule?”
“Aliniita kwa ajili ya kuzungumza mambo ya biashara!”
“Mzungumzie chumbani?”
“Ndiyo!”
“Kitandani?”
“Ndiyo!”
“Hata akili yako haikuhisi chochote kile binti?”
“Hapana!”
“Basi kuna baadhi ya mishipa yako haifanyi kazi inavyotakiwa,” alisema polisi huyo kwa utani ulioonekana kuwa na shaka tele.
Haraka sana Amina akaandkika maelezo yake aliyoonyesha kwamba alibakwa na Dickson ambaye katika kipindi hicho hakuwa nchini Tanzania.
Moyo wake ulimuuma mno, hakuamini kama kweli yeye ndiye angethubutu kufanya kitendo kama kile, kwa sababu ya pesa, alikuwa tayari kufanya jambo lolote lile kumuangamiza mwanaume aliyekuwa akimpenda ambaye kwa kipindi hicho alikuwa kwenye hali mbaya baada ya mpenzi wake kupata ajali.
Alimuuliza maswali mengi Linda kuhusu Dickson lakini kwa wakati huo msichana huyo hakutaka kujibu chochote kile. Alishangaa kwani alihitaji kupata maelezo ya kina kabla hawajafika mpaka mahakamani lakini bado msichana huyo hakutaka kumpa ushirikiano.
“Linda...” aliita Amina.
“Naomba uniache kwanza. Nimechanganyikiwa mno,” alisema Linda huku akiendesha gari.
“Sawa. Hebu nijibu swali moja,” alisema Amina.
“Lipi?”
“Hivi kweli Dickson alikuwa mpenzi wako?”
“Ndiyo!”
“Na alikuwa akikupenda?”
“Ulisema swali moja, si ndiyo? Naomba nipumzishe kichwa changu,” alisema Linda na kutilia umakini katika uendeshaji wa gari lake.
Moyo wake uliwaka kwa hasira, hakuridhika japokuwa Nandy alikuwa kitandani akiteseka, alikuwa na uhakika kwamba msichana huyo angekufa kitandani pale lakini kwa kuwa Dickson alikuwa na msichana huyo, akakosa furaha mkabisa.
Alimfikisha Amina mpaka Manzese alipokuwa akiishi na yeye kuondoka zake. Njiani, hakuacha kumfikiria Dickson, alijua kwamba kulikuwa na watu wengi waliokuwa wakiumia katika mapenzi lakini kwa maumivu aliyokuwa akiyasikia kipindi hicho, alijiona kuwa mwanamke wa kwanza aliyekuwa akiumia kuliko wote.
Ndani ya gari akaanza kutokwa na machozi yaliyokuwa na maumivu makubwa, alilia mno kiasi kwamba mpaka kichwa kikaanza kumuuma. Alipofika nyumbani, akalipaki gari na kuelekea chumbani kwake
Siku hiyo hakutaka kuzungumza na mtu yeyote yule, alihitaji kupumzika, alihitaji kuyauguza maumivu yaliyokuwa yakiushambulia moyo wake. Kila alipokaa, ni picha ya Dickson ndiyo iliyokuwa ikimjia kichwani mwake.
Mama yake aligundua kwamba binti yake hakuwa sawa, akaingia chumbani na kumuuliza kilichokuwa kikiendelea, alishindwa kumuhadithia, alibaki kimya huku akilia tu.
“Tell me! What is going on?” (niambie! Nini kinaendelea?) aliuliza mama yake huku akimsogelea, alipomfikia, akamkumbatia.
“Nothing!” (hakuna kitu)CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Why are crying for nothing?” (kwa nini unalia na wakati hakuna kitu?) aliuliza mama yake.
Linda akashindwa kulijibu swali hilo, akabaki kimya huku akiendelea kulia kilioo cha kwikwi, hakutaka kabisa kuufungua mdomo wake na kumwambia mama yake kile kilichokuwa kikiendelea, maumivu aliyokuwa akiyasikia akataka yabaki milele ndani ya moyo wake.
Ndege ikatua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Chennai uliokuwa nchini India. Haraka sana gari la wagonjwa kutoka katika Hospitali ya Apollo likasogezwa mahali husika na wazazi wa Dickson na mzee Gwamaka kuanza kuteremka.
Baada ya kufika chini, kitanda cha mgonjwa, Nandy kikaanza kuteremshwa kutoka ndani ya ndege huku Dickson akisaidiana na wahudumu wa ndege hiyo kumteremsha.
Baada ya kufikishwa chini, akaingizwa ndani ya gari la wagonjwa lililokuwa mahali hapo na safari ya kuelekea hospitalini kuanza.
Muda wote huo, Dickson alikuwa pembeni yake, moyo wake uliendelea kuwa kwenye majonzi tele, aliumia, hakukuwa na kitu ambacho kiliichanganya akili yake kama kuugua kwa mpenzi wake.
Hawakuchukua muda mrefu wakafika hospitalini, akateremshwa na kuanza kuingizwa ndani ya hospitali hiyo.
Kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumpeleka katika chumba cha mapumziko kwa ajili ya madaktari kupitia ripoti yake ili kuangalia kwa undani tatizo lililokuwa likimkabili ambalo lilimfanya kuwa kitandani.
Baada ya nusu saa, jopo la madaktari kumi na mbili likakutana ndani ya chumba kimoja cha mkutano na kuanza kuijadili ripoti ya Nandy ambayo ilitumwa kutoka nchini Tanzania.
Kila daktari aliyeona ripoti ile alishtuka, hakukuwa na aliyeamini kama kungekuwa na mtu aliyepata majeraha makubwa ya uti wa mgongo kama ilivyokuwa kwa Nandy.
Uti wa mgongo ulivunjika hali iliyoonyesha kwamba ilikuwa ni lazima apooze kitandani pale alipokuwa. Kila mmoja alimsikitikia lakini hawakuwa na jinsi kwani kama uti wa mgongo ulivunjika vibaya namna ile, wasingeweza kuurudisha katika hali yake kwa kipindi kifupi, ingeweza kuchukua miaka zaidi ya hamsini mpaka kuwa sawa.
Uti wake wa mgongo ukagawanywa kwa sehemu kuu tatu. Sehemu ya kwanza ya juu ilikuwa ikianzia C1 hadi C4, sehemu hii waliiweka alama ya bluu na iliitwa High-Cervical Nerves iliyokuwa na pingili nne.
Mgonjwa anapokuwa amevunjika katika sehemu hii ya kuanzia C1 hadi C4 inamaana kwamba katika mwili wake angepooza miguu, mikono, asingekuwa na uwezo wa kula au kuoga yeye mwenyewe na ilikuwa ni lazima atafutiwe mtu wa kumfanyia mambo hayo yote, asingekuwa na uwezo wa kuendesha gari, kwa kifupi alitakiwa kuwa chini ya uangalizi kwa saa ishirini na nne.
Mbali na hicho, pia kulikuwa na pingili nyingine walizoziwekea rangi ya kijani. Hizo ziliitwa Low-Cervical Nerves ambazo zilianzia C5 hadi C8.
Mgonjwa anapovunjika pingili hizo, kwake isingekuwa vigumu sana kufanya mambo mengine kwani angeweza kunyanyua mkono, kutembea na wakati mwingine hata kuzungumza kama kawaida lakini tatizo kubwa ambalo angekutana nalo ni kwenye mfumo wote wa upumuaji, asingeweza kupumua kwa kawaida, ilikuwa ni lazima kutumia mashine maalumu kupumua.
Kulikuwa na pingili nyingine walizozipa rangi nyekundu, hizi ziliitwa Thoracic Nerves walizozipa T1 hadi T5. Hizi nazo kama zingevunjika basi mgonjwa angepata matatizo katika kifua chake, miguu na mikono ingepooza ambapo kwa kitaalamu hujulikana kama paraplegia.
Walipitia kila kitu kwa umakini mkubwa na tatizo kubwa lililotokea kwa Nandy ni kwamba pingili nyingi zilikuwa zimevunjika hali iliyoonyesha hatari kubwa katika maisha yake.
Baada ya saa saba, kikao kikamalizika na hivyo kuanza kazi ya kumshughulikia mgonjwa huyo ambaye alipelekwa katika hospitali hiyo huku akiwa hajitambui.
Kila mtu aliyemwangalia pale kitandani alipokuwa, alimuonea huruma, alidhoofika mwili kwa siku chache tu, alipokuwa amelala, hakuweza kuyafumbua macho yake na ilikuwa ni rahisi kusema kwamba alikuwa amefariki dunia kutokana na ukimya wake.
Pale chumbani, Dickson alikuwa pembeni yake, moyo wake haukuacha kuuma, machozi hayakukatika mashavuni mwake, wakati mwingine alikuwa akijilaumu kwa kumuacha Nandy na kwenda kuwa na mwanamke mwingine ambaye aliamini kwamba hakuwa chaguo lake hata kidogo.
Alimwangalia msichana huyo, wakati mwingine alihisi kwamba alifariki dunia pale kitandani kutokana na ukimya aliokuwanao, kitu pekee ambacho kilimpa uhakika kwamba Nandy hakuwa amefariki dunia ni mashine ya Medical EKG Heart Rate Monitor ambayo ilionyesha namba moyo wake ulivyokuwa ukifanya kazi kwa kupanda na kushuka.
“Mungu! Naomba uchukue kila kitu kwangu lakini naomba uniachie Nandy! Ni msichana mdogo mno, mwenye ndoto zake za kuwa muimbaji mkubwa wa injili, Mungu, kwa nini usininyang’anye kila kitu na kuniachia Nandy?” aliomba Dickson huku akimwangalia msichana huyo aliyekuwa kimya kitandani.
Maisha yaliendelea, kila siku Dickson na wazazi wao walikuwa wakielekea hotelini na kurudi hospitalini hapo. Hakukuwa na nafuu kwa msichana huyo, hali yake iliendelea vilevile kiasi kwamba kuna wakati wote walihisi kuwa msichana huyo alikuwa amefariki dunia lakini madaktari walishindwa kuwaambia ukweli.
Kila siku madaktari walikuwa wakimchukua na kumpeleka katika chumba maalumu cha matibabu na kuanza kumtibu humo. Zoezi kubwa walilokuwa wakilifanya lilikuwa ni kuunyoosha mgongo wake, zile pingili ambazo zilikuwa zimeachana zirudi na kuungana tena kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma.
Kuzinyoosha lilikuwa zoezi kubwa na gumu, madaktari walihangaika mpaka kufanikiwa kuzinyoosha na kitu pekee kilichobaki kilikuwa ni kuziacha ziungane na kuwa kama zamani zoezi ambalo lingeweza kuchukua hata zaidi ya miaka hamsini.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Atapona?” lilikuwa swali alilouliza Dickson mara kwa mara.
“Ndiyo! Atapona japokuwa itamchukua muda mrefu sana!” alijibu daktari.
“Kama miezi mingapi?”
“Miezi kama mia sita!”
“Unasemaje?”
“Miezi mia sita. Hicho ni kipindi kifupi sana kwa mtu kama yeye lakini wengine wanaweza kuchukua miezi mingi zaidi ya hiyo,” alisema daktari.
Dickson akachoka, akahisi miguu yake ikinyong’onyea na kukaa chini. Kichwa chake kilifanya hesabu harakaharaka kwamba miezi hiyo mia sita aliyokuwa ameambiwa ilikuwa ni sawa na miaka hamsini.
Pale chini alipokuwa akaanza kulia, hakuona tumaini tena, alikata tamaa na kuhisi kabisa kuwa mpenzi wake huyo angekufa akiwa pale pale kitandani.
“Hawezi kufa akiwa kitandani, kuna siku atasimama na kutembea tena,” alisema Dickson huku akilia kwa sauti kubwa kiasi kwamba kila mmoja aliyekuwa hospitalini hapo akahisi kuwa mgonjwa wake alifariki dunia.
Siku zilikatika na baada ya miezi mitatu na nusu, hatimaye muujiza ukaonekana kwa Nandy, akayafumbua macho yake na kuanza kuangalia huku na kule.
Kitu pekee alichokuwa akikikumbuka ni kupata ajali mbaya akiwa kwenye pikipiki, baada ya hapo hakujua ni kitu gani kiliendelea.
Akaanza kuyapeleka macho yake huku na kule, mashine ya kupumulia ilikuwa puani na mdomoni mwake, kwa juu yake aliiona dripu ikiwa inaning’inia, hakutaka kujiuliza, kwa jinsi ajali ile ilivyokuwa imetokea, alijua kabisa kwamba hapo alipokuwa ilikuwa ni hospitalini.
Akajaribu kuinuka kitandani pale, akashindwa, mwili wake ulikuwa haufanyi kazi kabisa. Kiuno kilikataa kutingishika, alijaribu kuitingisha mikono yake, akashindwa kabisa, ilikuwa ni kama mtu aliyepigwa sindano ya ganzi.
Hakujua ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea, mwili wake ulikosa mawasiliano na ubongo na kitu pekee alichokuwa na uwezo wa kukitingisha kilikuwa ni kichwa chake tu.
“Nini kimetokea?” aliuliza kwa sauti kubwa iliyowafanya manesi wawili kuingia chumbani hapo.
Walipomuona Nandy amefumbua macho, mmoja akatoka na kwenda kumuita daktari. Ulikuwa ni mwezi wa tatu tangu afikishwe hospitalini hapo, alikuwa kimya, alipoteza fahamu na hatimaye siku hiyo aliyafumbua macho yake na kuangalia tena.
Daktari alipofika, akatoa tabasamu pana. Alishangaa, manesi waliokuwa mbele yake walikuwa Wahindi na hata daktari aliyekuwa ameingia ndani ya chuma hicho alikuwa Mhindi pia.
“Where Am I?” (nipo wapi?) aliuliza Nandy.
“In the hospital!” (hospitalini)
“Agha Khan?”
“No! Apollo, India,” (Hapana! Apollo, India) alijibu daktari huyo.
“Doctor! What is wrong with me? I can’t move my legs, hands, what is wrong with me?” (Dokta! Nina tatizo gani? Siwezi kuisogeza miguu yangu, mikono, nina tatizo gani?) aliuliza Nandy huku akiwa kitandani pale.
Daktari hakumjibu, alimwangalia, aliangalia mapigo ya moyo wake, mtungi wa gesi, alipoona kwamba ana uwezo wa kupumua pasipo mashine hiyo, akakitoa kifaa cha kupumulia na kisha kuandika maelezo machache na kutoka ndani ya chumba hicho.
Akaingia ofisini mwake na kuwaita wazazi wa binti huyo waliyekuwa wamemleta, wakaelekea huko wakiwa na Dickson na kuanza kuwaambia kuhusu hali ya mgonjwa.
Hakukuwa na aliyeamini waliposikia kwamba Nandy aliyafumbua macho yake na kuzungumza. Kila mmoja alihisi kama alikuwa kwenye ndoto moja ya kusisimua na baada ya dakika kadhaa angeamka kutoka kitandani.
Miezi mitatu yote walikuwa hospitalini hapo wakisubiria muujiza, walimuomba Mungu na mwisho wa siku akawajibu kwa kumrudishia pumzi msichana huyo huku akiwa kitandani.
Kila mmoja alikuwa na hamu ya kumuona Nandy ndani ya chumba kile, walizungumza na daktari lakini mawazo yao yote yalikuwa kwa msichana huyo tu.
Walipomaliza, daktari akawachukua na kuondoka nao kuelekea katika chumba kile. Moyo wa Dickson ulikuwa na shauku kubwa kumuona Nandy. Alimuomba sana Mungu, alihitaji kumuona akiyafumbua macho yake tena, kiu yake kubwa ilikuwa ni kusimama mbele ya msichana huyo na kuongea naye.
Walipoingia, moja kwa moja wakaanza kupiga hatua kumfuata huku nyuso zao zikiwa kwenye tabasamu pana. Nandy, alipomuona baba yake, akatabasamu lakini macho yake yalipohamia kwa Dickson, akaanza kupiga kelele huku akimtaka kijana huyo atoke haraka sana ndani ya chumba hicho.
“Dickson tokaaaaaaa.....sitaki kukuonaaaa...tokaaaaaaa....” alipiga kelele Nandy huku akimwangalia Dickson kwa hasira, machozi yakaanza kutiririka mashavuni mwake.
Dickson hakuamini alichokuwa akikisikia, alibaki akimwangalia Nandy kitandani pale ambapo aliendelea kumwambia kwamba ni lazima aondoke ndani ya chumba kile.
Moyo wake ulimuuma mno, machozi yakaanza kumtoka na kutiririka mashavuni mwake. Ni kweli alimkosea msichana huyo, alimuumiza mno lakini alimsaidia sana mpaka kufika nchini India na kuanza kupewa matibabu.
Nandy hakuwa akijua hilo, alipoteza fahamu kwa miezi mitatu hivyo hakujua ni kwa namna gani mwanaume huyo alikuwa amemsaidia kufika mahali hapo.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hakutaka kubisha, huku akionekana kuumia sana akageuka na kuanza kutoka ndani ya chumba hicho tena kichwa chake akiwa amekiinamisha chini.
“Ninakuchukia, ninakuchukia Dickson,” alisema Nandy wakatik Dickson alipokuwa akitoka ndani ya chumba hicho.
Akaelekea nje na kukaa kwenye viti vilivyokuwa mahali hapo, aliumia moyoni mwake lakini baada ya kugundua kwamba msichana huyo alikuwa amefumbua macho yake baada ya miezi mitatu kupita, akaanza kumshukuru Mungu, akapiga magoti chini na kuinyoosha mikono yake juu.
Mule ndani, baba yake, mzee Gwamaka na wazazi wa Dickson wakaanza kumtuliza na kumtaka kunyamaza huku wakimwambia ni kwa jinsi gani Dickson alifanikisha kwa yeye kuwa mahali hapo.
Nandy hakutaka kukubali, hakuwaamini, alipoambiwa kwamba alikuwa kitandani hapo kwa muda wa miezi mitatu kwake aliona ni uzushi tu kwani kile kilichotokea kwenye ajali ile kilionekana kuwa kama siku iliyopita.
“Aliniacha, alinitesa, siwezi kuwa naye,” alisema Nandy huku akilia.
“Hutakiwi kusema hivyo! Mungu husamehe, kwa nini hutaki kusamehe binti yangu?” aliuliza mzee Gwamaka.
“Lakini aliniumiza sana!”
“Yesu aliumizwa, alichapwa mijeledi, alitemewa mate, alizomewa, aliitwa mwizi, alizihakiwa na kutundikwa msalabani Goligotha, lakini palepale msalabani alisema kwamba Mungu awasamehe, yaani alisamehe pamoja na kufanyiwa vyote hivyo, sisi ni nani mpaka tusisamehe?” aliuliza mzee Gwamaka huku akimwangalia binti yake.
Nandy alikuwa kimya, maneno aliyoongea baba yake yaliingia moyoni mwake na kumkumbusha maneno ya kwenye Biblia kwamba alitakiwa kusamehe saba mara sabini.
Moyo wake ukalowa, hakuwa na ubishi tena, alijua kabisa kwamba hata kama alifanyiwa mambo gani alitakiwa kusamehe kwa kila kitu kilichotokea.
Akamwambia baba yake kwamba alikubali kumsamehe Dickson lakini hakutaka kuwa naye tena, yaani katika maisha yake, alitakiwa kubaki peke yake, bila kuwa na mwanaume mwingine mpaka kifo chake.
“Hakuna tatizo!” alisema mzee Gwamaka.
Hapohapo mzee huyo akatoka ndani na kwenda kumuita Dickson, alipofika kwenye korido, bado mwanaume huyo alikuwa amepiga magoti, alimshukuru Mungu kwa kile kilichokuwa kimetokea.
Kwake, kitendo cha Nandy kuyafumbua macho yake kilionekana kuwa muujiza mkubwa kama kuuhamisha mlima na kuupeleka baharini.
Hapohapo mzee Gwamaka akamfuata na kumshika bega na kumwambia kwamba alikuwa akihitajika na Nandy. Haraka sana akasimama, akaingia ndani ya chumba kile na kumfuata Nandy pale kitandani.
Kitu cha kwanza kabisa kukifanya ni kupiga magoti na kuanza kumuomba msamaha. Aliyajua makosa yake, kwa jinsi msichana huyo alivyokuwa akimpenda, hakutakiwa kumuacha kama alivyokuwa amefanya.
Aliomba sana msamaha huku akilia kama mtoto mdogo, alimwambia wazi kwamba katika maisha yake yote asingeweza kufanya ujinga kama aliokuwa ameufanya, alikuwa tayari kumfanyia kila kitu lakini si kumuacha tena.
“Nandy! Naomba unisamehe, najua nimekukosea, najua sistahili msamaha, nilikuumiza sana lakini naomba unisamehe mpenzi,” alisema Dickson huku akiwa amepiga magoti chini, macho yake yalikuwa mekundu mno.
“Dickson! Why did yo...” (Dickson! Kwa nini uli....) aliuliza Nandy lakini hata kabla hajamalizia sentensi yake, akaanza kulia.
Dickson akainuka na kuusogeza uso wake karibu na uso wa msichana huyo, akachukua fulana yake na kuanza kuyafuta machozi yake.
Moyo wake ulimumia mno, pale kitandani alipokuwa, Nandy alishindwa kufanya jambo lolote lile, machozi yale aliyokuwa akifutwa na Dickson yakaurudisha moyo wake na kuhisi kabisa kwamba ukianza kuanguka katika mapenzi mazito ya mwanaume huyo.
“Dickson! Nimepooza mpenzi,” alisema Nandy huku akimwangalia mwanaume huyo.
“Najua! Inawezekana Mungu alipanga hivi, hata kama umepooza, nakuahidi kitu kimoja kwamba sitokuacha,” alisema Dickson huku akiwa ameukaribisha uso wake karibu na wa Nandy.
“Unanipenda pamoja na hali niliyokuwanayo?”
“Ninakupenda sana Nandy! Siwezi kukuacha kwa kuwa umepooza, nitakupenda hata kama kuna siku utaondoka ndani ya dunia hii,” alisema Dickson.
“Nimepooza Dickson!”
“Najua! Ninakupenda katika hali hiyohiyo uliyokuwanayo,” alisema.
Alimaanisha, moyoni mwake hakukuwa na msichana aliyekuwa na nafasi zaidi ya Nandy, alikuwa tayari kufanya kila kitu katika maisha yake lakini si kumuacha msichana huyo.
Aliongea naye mambo mengi kitandani pale, yale machozi yakakauka na kuanza kucheka pamoja mahali hapo kitu kilichowafurahisha wazazi wao.
Siku zikaendelea kukatika, kila siku madaktari walikuwa wakiingia na kuangalia hali ya Nandy. Walichokifanya ni kumnunulia Nandy kiti cha mataili ambacho walimtaka kukitumia katika maisha yake.
Hiyo ikawa nafasi ya Dickson kumtoa na kuanza kuzunguka naye huku akimuendesha kwenye kiti kile. Kila siku hiyo ndiyo ilikuwa ratiba yao, walitoka asubuhi na kwenda kwenye bustani, huko walizungumza mambo mengi huku wakipanga mipango yao ya maisha ya baadaye.
“Nandy!” aliita Dickson.
“Abeee.”
“Will you marry me?” (utakubali nikuoe?) aliuliza Dickson, hapohapo akapiga magoti mbele ya Nandy na kumuonyeshea pete iliyokuwa kwenye kikabati chake.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nandy alipoiona, akashindwa kuvumilia, palepale alipokuwa akaanza kulia, hakuamini kuona mwanaume huyo akiwa na shauku ya kutaka kumuona japokuwa alikuwa kwenye hali mbaya kama aliyokuwa nayo.
Alitamani kuinyanyua mikono yake na kumkumbatia lakini alishindwa kusogeza kiungo chake chochote kile. Akakubaliana naye huku akilia, akatingisha kichwa chake na kumwambia kwamba alikuwa tayari kuolewa na yeye lakini bado kulikuwa na tatizo kwamba alikuwa amepooza.
“Sijali!”
“Ila sitoweza kufanya mapenzi na wewe!”
“Sijali!”
“Sitoweza kukuzalia watoto!”
“Pia sijali!”
“Dickson! Kwa nini usitafute mwanamke mwingine?”
“Siwezi! Nilianza kukupoteza Nandy! Kwa sasa, sitoweza kukupoteza tena. Kwako sihitaji watoto, sihitaji kufanya mapenzi, nikiwa na wewe tu najisikia amani, najisikia furaha, najiona kukamilika kama mwanaume,” alisema Dickson, akachukua mkono wa Nandy na kumvisha pete ya uchumba huku wazazi wao wakiwa kwa mbali wakiangalia.
Ulikuwa ni ushujaa mkubwa kwa Dickson, kwake hakutaka kujali kitu chochote kile, alichokuwa akikiangalia ni kuwa na msichana huyo tu.
Baada ya kukaa miezi miwili, wakaondoka na kurudi nchini Tanzania. Njiani walikuwa wakizungumza mambo mengi mno, walikuwa wakifurahia pamoja japokuwa kwa msichana Nandy hakuweza kufanya kitu chochote kile.
Walipofika, maisha yakaanza upya. Dickson hakutaka kuona Nandy akikaa peke yake, alichokifanya ni kumuhamisha nyumbani kwao na kuanza kuishi na yeye. Hakutaka kusoma tena, alichokifanya ni kusimamia biashara za baba yake.
Akamuajiri msichana wa kazi za ndani aliyeitwa Maria ambaye huyo alitakiwa kukaa na Nandy na kumuhudumia kwa kila kitu.
Wakati akiwa ameishi nchini Tanzania kwa siku tatu, ghafla akashtukia akipokea ugeni kutoka katika Kituo cha Polisi cha Osterbay na kuambiwa kwamba alikuwa akihitajika huko kwa kuwa kulikuwa na kesi ya kubaka iliyofunguliwa.
“Nilibaka?” aliuliza, alisahau kabisa kuhusu Amina.
“Ndiyo!” alijibu polisi mmoja na kumfunga pingu, wakaanza kuelekea kituoni.
Wakati akiwa ndani ya gari la polisi ndipo kumbukumbu ya tukio hilo lilipomjia kichwani mwake. Alikumbuka namna alivyotumiwa video akiwa anafanya mapenzi na Amina ambaye alionekana kama alikuwa akimbaka.
Moyo wake ukawa na hasira zaidi na Linda kwani aliamini kwamba msichana huyo ndiye aliyekwenda kituoni na kufungua kesi hiyo.
Alipofikshwa huko, akatupwa selo na kuambiwa asubiri kwani kesi yake hiyo nzito ilikuwa ikiandaliwa tayari kwa kupelekwa mahakamani ambapo ingeanza kusikilizwa na kama angekutwa na hatia, alitakiwa kufungwa gerezani kwa miaka isiyopungua thelathini.
Wazazi wa Dickson walipewa taarifa juu ya kile kilichokuwa kimetokea, walishangaa, kwao lilionekana kuwa jambo geni kwa mtoto wao kukamatwa na kupelekwa polisi huku akishutumiwa kwa kosa la ubakaji alilokuwa amelifanya miezi mitatu iliyopita.
Wakaondoka na kuelekea katika kituo hicho ambapo huko wakajitambulisha kwa polisi na kutaka kujua kile kilichokuwa kimetokea.
Polisi hao waliwaambia kwamba kulikuwa na msichana mmoja aliyekwenda kituoni hapo kufungua kesi ya ubakaji aliyokuwa ameifanya miezi mitatu iliyopita.
Walichokitaka ni kuonana na msichana huyo na kuzungumza naye kwani kitu hicho kwao kilionekana kuwa kigeni na hawakuwa na uhakika kama mtoto wao alifanya kosa hilo kwa kuwa walimwamini, alikuwa mcha Mungu ambaye aliishi katika mazingira ya dini kila siku.
Linda akapigiwa simu na kuambiwa kwamba mwanaume aliyekuwa amemfungulia kesi tayari alikuwa amekamatwa na hivyo kwenda katika kituo hicho.
Msichana huyo aliposikia hilo, moyo wake ukawa na furaha, akawa na amani na kuona kwamba alikuwa amemaliza kila kitu na hivyo kitu kilichokuwa kimebaki kilikuwa ni kuzungumza na Amina ili amwambie kwamba alitakiwa kujiandaa.
“Kila kitu tayari, yule mwanaume amekamatwa,” alisema Linda.
“Mwanaume gani?”
“Dickson! Yaani umesahau?” aliuliza Linda.
Amina alisahau kila kitu kilichotokea, siku hiyo alipoambiwa kuhusu mwanaume huyo, kumbukumbu zake zikaanza kurudi nyuma na kuikumbuka sura ya mwanaume huyo.
Bado alikuwa mzuri, alihisi kabisa kwamba kama angekwenda mahakamani na kutoa ushahidi kwamba alibakwa kitu ambacho hakikuwa kweli, aliona kabisa maisha yake yasingekuwa kama yalivyokuwa, yangebadilika kwa kuwa nafsi yake kila siku ingekuwa ikimsuta.
“Siwezi! Siwezi kutoa ushahidi wa kumfunga,” alisema Amina.
Hilo ndilo alilopanga, hakutaka kumwambia Linda, mwanamke huyo alitumia kiasi kikubwa cha pesa kuhakikisha kila kitu alichopanga kinakwenda kama kilivyotakiwa hivyo kama angekataa kwamba hakubakwa basi alihisi kungekuwa na jambo baya ambalo lingetokea.
Wakati akifikiria kuhusu hayo, Linda akampigia simu na kumwambia kwamba walitakiwa kuonana kwa kuwa kuna mambo mengi walitakiwa kuyazungumza kabla ya kupanda mahakamani.
Hilo halikuwa tatizo, haraka sana wakaonana Magomeni katika Mgahawa wa Young Boys na kuanza kunywa juisi. Waliongea mambo mengine mengi, walifurahia pamoja lakini mwisho wa siku Linda kumwambia kile kilichowafanya kuwa mahali hapo.
“Ninachohitaji ni kuona anafungwa gerezani tu,” alisema Linda huku akimwangalia Amina.
“Kwani tatizo hasa nini?”
“Ni mapenzi tu!”
“Na unampenda?”
“Sana tu!”
“Sasa kwa nini unataka kumfunga?” aliuliza Amina.
Kwa kipindi hicho hilo ndilo swali lililokuwa likimkasirisha moyoni mwake, hakutaka kuulizwa kuhusu sababu bali alichokuwa akikitaka ni kuona Dickson anafungwa gerezani tu kwa kuwa aliamua kumuacha na kumchukua mwanamke mwingine.
“Hilo hutakiwi kulifahamu! Shika hii bahasha, nadhani tutaonana mahakamani,” alisema Linda na kumpa bahasha ile.
Akaondoka, Linda akabaki peke yake mahali hapo. Alikiinamisha kichwa chake, alikuwa akipitia katika kipindi kigumu kupita kawaida.
Moyo wake ulikuwa umegawanyika, upande mmoja ulimwambia kwamba uamuzi wa kumfunga Dickson gerezani ulikuwa mbaya na hakutakiwa kuufanya hata siku moja katika maisha yake lakini upande mwingine wa moyo wake ulimwambia kwamba hakukuwa na tatizo, alitakiwa kufanya kile alichoambiwa kufanya.
“Mungu wangu! Nifanye nini mimi?” aliuliza.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Akaifungua bahasha ile kubwa ya kaki. Ndani, akakutana na noti za shilingi elfu kumi, vilikuwa vibunda vinne, kila kibunda kilikuwa na milioni moja.
“Pesa! Hizi pesa ni kwa lengo la kumfunga mtu?” alijiuliza.
Mpaka anaondoka mahali hapo hakuwa na jibu sahihi la kile alichotakiwa kufanya. Bado moyo wake ulikuwa kwenye wakati mgumu mno, wakati mwingine alitamani hata kutoroka na kwenda sehemu ambayo kusingekuwa na mtu mwingine ambaye angemuona.
Akiwa njiani, akapokea meseji kutoka kwa Linda na kumwambia kwamba alitakiwa kufanya kile alichotakiwa kwa kuwa zoezi hilo lilimfanya kutumia kiasi kikubwa cha pesa kuhakikisha mwanaume huyo anapotea.
Wakati wakiyapanga mambo hayo yote, bado Dickson alikuwa selo akiendelea kusota. Moyo wake ulimuuma kuwa mbali na mpenzi wake, Nandy, alibaki akilia huku moyo wake ukijuta kwa uamuzi wa kumchukua Amina na kufanya naye mapenzi hotelini.
Siku hiyo alilala humo selo huku usiku mzima akionekana kuwa na mawazo tele. Kwa kuwa ilikuwa ni Jumapili, alitakiwa kubaki mpaka Jumatatu ambapo kesi yake ilitakiwa kwenda mahakamani na hivyo kusomewa mashtaka.
Nyumbani, Nandy alikuwa akijiuliza maswali mengi, aliona jinsi mpenzi wake alivyokamatwa na polisi na kupelekwa kituoni, hakujua ni kitu gani kiliendelea huko, hakujua mpenzi wake alikuwa na kosa gani mpaka polisi hao kwenda kumchukua.
Pale kitandani alipokuwa, hakuacha kuuliza, kila aliyemuuliza hakumpa jibu la uhakika, kulionekana kama kuna kitu ambacho kilitokea ambapo walimficha kumwambia.
“Baba! Kuna nini?” aliuliza Nandy huku akimwangalia mzee Gwamaka.
“Hakuna kitu!”
“Unanificha! Naomba uniambie ukweli!”
“Hakuna kitu binti yangu!”
“Na Dickson yupo wapi?”
“Aliitwa polisi mara moja!”
“Kuna nini huko?”
“Nandy binti yangu! Hakuna kitu, naomba uniamini!” alisema mzee Gwamaka.
Japokuwa aliambiwa maneno mengi kwamba hakukuwa na kitu kibaya kilichokuwa kimetokea lakini moyo wake haukuwa na amani hata kidogo.
Alihisi kwamba kulikuwa na kitu kibaya kilichokuwa kimetokea ambacho wazazi hawakutaka kumwambia ukweli. Usiku wa siku hiyo hakulala, alibaki akimfikiria mpenzi wake, alitamani kuchukua simu na kumpigia lakini hakuwa na uwezo wa kufanya kitu chochote kile.
Jumatatu ilipofika, karandinga likafika kituoni hapo na kumchukua Dickson kisha kumpeleka mahakamani. Ndani ya karandinga hilo alikuwa kimya, kichwa chake kilikuwa kikiyafikiria maisha yake lakini zaidi alikuwa akimfikiria mpenzi wake.
Hakujua ni kitu gani kingetokea kama angefungwa gerezani na mpenzi wake kubaki nyumbani. Aliumia, kwa hali aliyokuwanayo Nandy hakutakiwa kuachwa hata mara moja, hata kama ingetokea siku moja akafa basi alikuwa radhi kuona akifa mbele ya macho yake.
Alipofika, akateremshwa huku akiwa na pingu yake, akapelekwa ndani ya mahakama huku akiwa na watuhumiwa wengine. Alipokwenda kusimama kizimbani, akaanza kuangalia huku na kule.
Macho yake yalikuwa yakiangalia huku na kule, ghafla yakatua usoni mwa Linda aliyekuwa amekaa mbele kabisa. Msichana huyo hakuonekana kuwa na tatizo lolote lile, pale alipokaa uso wake ulikuwa na tabasamu pana kuonyesha kwamba kile kilichokuwa kikiendelea, kilimfurahisha kupita kawaida.
Siku hiyo ilikuwa ni ya kusomwa kwa kesi yake, alisimama kizimbani huku akiwa ameuinamisha uso wake chini. Alikuwa akilia, moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali na hakuamini kama siku hiyo alisimama mahakamani kusomewa mashitaka kwa kesi iliyokuwa ikimkabili.
Siku hiyo kesi ikaahirishwa na kupangwa tarehe ambayo ingeanza rasmi kusikilizwa. Linda aliondoka mahakamani hapo huku akijiona shujaa, alijiona bingwa kuliko watu wote katika dunia hii.
Alitembea kwa kujiamini mpaka alipolifikia gari lake na kuingia, hakutaka kubaki mahali hapo, akaondoka zake huku njiani akimpigia simu Amina na kumwambia kwamba kazi ilibaki kwake.
“Sijui kama nitaweza,” alisema Amina.
“Kwa nini ushindwe?”
“Mmh! Nitaweza kweli?”
Mpaka kufikia hapo tayari Linda akaona kama angegeukiwa na msichana huyo. Alitumia pesa nyingi kuhakikisha kila kitu kinawekwa sawa, wakati wakiwa wamemla ng’ombe mzima na kubaki mkia, akaanza longolongo kwamba aliona ugumu mbele yake.
Linda hakutaka kusubiri, hakutaka kuona akigeukiwa, akawapigia simu vijana wake na kuwaambia kwamba Amina alitakiwa kutekwa, apelekwe sehemu, ashikiliwe kwa siku mbili mfululizo huku akipewa vitisho kwamba kama asingefanya kile kilichotakiwa kufanywa basi angeuawa kwa kuchomwa moto.
“Hilo tu bosi?” alisikika jamaa akiuliza upande wa pili.
“Ndiyo! Yaani mumshikilie, mumpe vitisho, mumtese mpaka ashike adabu, na mmwambie kabisa kwamba kama hatofanya kile kinachotakiwa, basi mtamuua,” alisema Linda.
“Haina shida madam!”
“Sawa. Nawatumia milioni kumi!”
“Poapoa.”
Simu zikakatwa.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Linda alizaliwa katika familia ya kitajiri, wazazi wake walikuwa na pesa nyingi na ndiyo maana elimu zake zote alichukulia nje ya nchi barani Ulaya na Marekani.
Mbali na pesa za baba yake, naye alikuwa mfanyabiashara mzuri tu, maisha yake yalizungukwa na pesa na kila alipokuwa ni lugha ya pesa tu ndiyo aliyokuwa akiizungumza.
Alikuwa na kila kitu alichokuwa akikihitaji, wakati mwingine aliona kwamba alikuwa na uwezo wa kupata kila kitu kwa kuwa alikuwa na pesa. Aliamini kwamba unapokuwa na pesa unaweza kupata mapenzi ya dhati, unapokuwa na pesa unabadilisha hata chuki kuwa penzi na ndiyo maana alimuihitaji sana Dickson.
Kutumia pesa kwa vijana wale kwa kazi aliyotaka kuifanya hakukuwa na tatizo, alihitaji furaha ya milele, alihitaji kujiona akitabasamu mbele ya kioo na kitu pekee alichoamini kwamba kingempa tabasamu hilo hakikuwa kingine bali pesa.
Vijana hao baada ya kutumiwa pesa hawakutaka kubaki walipokuwa, wakaambiwa mahali alipokuwa akiishi Amina na kuanza kuelekea huko. Hakukuwa na tatizo kumpata, wasifu wake kwamba alikuwa na wowowo kubwa, mzuri wa sura, mweupe vilikuwa vitu vilivyowapa uhakika wa kumpata kwa urahisi kabisa.
Wakaondoka mpaka Manzese Midizini walipokuwa wameelekezwa, walifika mpaka nje ya nyumba ya akina Amina ambapo kulikuwa na duka na kujifanya kununua kitu huku wakimuulizia Amina kwa muuza duka huyo.
“Amina yupo?” aliuliza jamaa mmoja aliyeitwa Kudra.
“Ametoka sasa hivi!”
“Amekwenda wapi tena?” aliuliza.
“Sijui! Alikuja jamaa yake, akamchukua na kuondoka naye, kurudi nadhani ni usiku,” alijibu muuza duka.
“Poa haina noma.”
Kwa kuwa walipata uhakika kwamba msichana huyo angerudi usiku hawakutaka kuwa na hofu, wakaondoka na kuwasiliana na Linda na kumwambia kile walichoambiwa na muuza duka.
Hakukuwa na tatizo lolote lile, akawaambia kwamba wafanye kila liwezekanalo na mwisho wa siku msichana huyo apatikane kwani kama angefika mahakamani huku akiwa hajapewa mkwara wowote ule ilikuwa ni lazima aseme ukweli kwamba hakubakwa.
“Yaani hakikisheni anapatikana, sawa?” alisema Linda.
“Sawa.”
Usiku wakarudi Manzese Midizini, hawakutaka kwenda mpaka nyumbani kwa akina Amina, walichokifanya ni kwenda katika baa fulani iliyokuwa jirani na mahali hapo na kutulia.
Ilipofika majira ya saa tano usiku wakaliona gari moja aina ya Toyota Vitz ikielekea nyumbani kwa akina Amina na kusimama. Hakuteremka mtu yeyote yule mpaka baada ya dakika tano mlango ukafunguliwa na Amina kuteremka.
Kwa jinsi alivyokuwa amevaa, hawakuwa na maswali kwamba huyo alikuwa mwenyewe au mtu mwingine. Alikuwa na wowowo, mzuri, mweupe ambaye kila alipokuwa akitembea ni kama wowowo lilitaka kudondoka.
Akaagana na mwanaume aliyekuwa ndani ya gari na kuelekea ndani ya nyumba hiyo. Walipohakikisha mwanaume huyo ameondoka, Kudra akaelekea kule na kumuulizia muuza duka.
“Ameingia sasa hivi!”
“Naomba uniitie,” alisema.
Hilo halikuwa tatizo, kijana huyo akamuita Amina ambaye alifika hapo nje na kukutana na Kudra. Alichokisema mwanaume huyo ni kwamba aliwahi kuonana naye na kuzungumza mengi halafu msichana huyo akamuelekeza nyumbani kwao na hivyo kumfuata.
Kwa Amina, hilo halikuwa tatizo, alikuwa mwanamke aliyependa sana wanaume, kwake, kutoa namba ya simu hakukuwa na tatizo lolote lile, alikuwa tayari kufanya kitu chochote kile lakini mwisho wa siku apate pesa.
Hakuwa akimjua mwanaume huyo lakini akajikuta akianza kutoa tabasamu na kumuuliza maswali ambayo yalikuwa mepesi mno kujibika kwa Kudra.
“Sasa ndiyo unifuate usiku jamani?” aliuliza kwa sauti yake nyembamba.
“Nilikuja mchana, hukuwepo. Muulize dogo,” alisema Kudra, hapohapo muuza duka akadakia.
“Alikuja, ulikuwa umeondoka!”
“Umesikia! Hatuwezi kukaa sehemu kuongea?” alimuuliza.
“Mmh! Usiku huu?”
“Ndiyo! Kidogo tu!”
“Hapana!”
Alichokifanya Kudra ni kuingiza mkono mfukoni, akatoa bunda la pesa na kuchomoa shilingi elfu ishirini na kumpa muuza duka na kumshukuru kwa msaada wake wa kumuitia Amina na kuzungumza naye.
Pesa hizo zilikuwa kama mtego, Amina alipoziona, moyo wake ukanyong’onyea, tamaa ikamshika kiasi kwamba mpaka yeye mwenyewe akajikuta akijilaumu kwa kukataa kutoka na mwanaume yule kwenda kuzungumza.
“Lakini isiwe mbali,” alisema Amina na wakati alikaa kabla, tayari Kudra akajua kabisa pesa zililainisha kila kitu.
“Pale tuu baa.”
Akamchukua na kuondoka naye. Amina alikuwa akijichekeshachekesha tu, pesa iliharibu kila kitu, akamsahau mwanaume aliyekuwa amemleta nyumbani pale na gari, aliangukia katika penzi la mwanaume mwingine kabisa.
Wakaelekea katika baa ile ambapo akakutana na mwanaume mwingine aliyetambulishwa kama rafiki wa Kudra na kuanza kuongea. Usiku huo ulikuwa ni wa kupombeka tu, walikuywa sana pombe, chakula. Amina aliamua kumchuna, alihisi kwamba kwa usiku huo angemaliza kibunda chote cha pesa kitu ambacho hakikuwa kweli kabisa.
Pombe zikamchukua, akaanza kupiga pombe kali kiasi kwamba mpaka inafika saa saba usiku, hakuwa akielewa kitu chochote kilichokuwa kikiendelea mahali hapo.
“Dullah! Kwanza tukamle uroda, mimi siwezi kuvumilia na hilo wowowo,” alisema Kudra.
Wakamchukua, wakamuingiza ndani ya gari na kumpeleka katika jumba moja waliloliandaa. Njiani, kila mtu alikuwa akifikiria kufanya mapenzi na msichana huyo, aliwatamanisha, wowowo lake, mapaja yake makubwa na meupe, kifua chake kidogo kiliwachanganya kupita kawaida.
Walipofika, hawakutaka kuchelewa, wakamlaza kitandani na kuanza kufanya naye mapenzi usiku mzima na walipomaliza, wakamfunga kamba.
Asubuhi ilipofika, Amina akashtuka, mwili wake ulikuwa ukijisikia uchovu kupita kawaida. Alishangaa mahali alipokuwa, alikuwa kitandani huku akiwa amefungwa kamba katika kitanda hicho cha chuma.
Hakujua ni mahali gani na alifikije. Akaanza kuvuta kumbukumbu, akakumbuka kwamba usiku uliopita alizungumza na mwanaume aliyekuwa na pesa ambaye alimchukua na kumpeleka baa na kuanza kunywa naye huku akiwa na rafiki wa mwanaume huyo na baada ya hapo hakujua ni kitu gani kilikuwa kimeendelea.
Kitandani pale kulikuwa na mipira ya kiume iliyokuwa imetumika. Hiyo ilionyesha kwamba mwanaume aliyekuwa amemleta chumbani pale alifanya naye mapenzi pasipo kujitambua.
Akaanza kupiga kelele mfululizo. Mara mlango ukafunguliwa na Kudra kuingia huku akiwa na bakuli la supu, akakaa kitandani na kumwangalia Amina.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Vipi? Mbona unatupigia kelele?” aliuliza Kudra huku akimwangalia Amina.
“Nimefanya nini? Naomba mniache niondoke,” alisema Amina huku akianza kulia katika kitanda kile alipokuwa amefungwa.
“Hujafanya kitu! Subiri!” alisema Kudra, hakutaka kubaki ndani ya chumba hicho, akatoka.
Amina akabaki peke yake, hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea mpaka mwanaume huyo na mwenzake kumchukua na kumfunga kamba ndani ya chumba hicho.
Alibaki akilia, mahali alipokuwa hakukuwa na dalili za kupata msaada wowote ule. Alijutia uamuzi wake wa kukubaliana na mwanaume yule na kumfuata kule alipokuwa kisa tu pesa alizokuwa amezishika.
Baada ya dakika kadhaa, Kudra akarudi chumbani humo akiwa na jiko la mkaa lililokuwa na moto huku kwa ndani akiwa ameweka kisu kilichokuwa kikiunguzwa na moto ule.
Amina akatetemeka, akahisi kabisa huo ndiyo ulikuwa mwisho wake. Akaanza kuomba msamaha japokuwa hakujua ni kosa gani alikuwa amelifanya. Kudra hakuzungumza kitu, alikuwa akiendelea kufanya mambo yake huku akinywa juisi.
Akamuita mwenzake ambaye akaja mahali hapo haraka sana na kuanza kuongea naye. Akamwambia kwamba ilikuwa ni lazima kuanza kazi yao kwani muda ulikuwa ukienda na kama wangechelewa kila kitu kingeharibika.
“Upo hapa kwa sababu moja tu,” alisema Kudra.
“Naomba mnionee huruma!”
“Upo hapa kwa sababu unataka kumgeukia bosi wetu mahakamani. Video inaonyesha kwamba umebakwa lakini unataka kumsaliti mahakamani na wakati amekulipa pesa nyingi sana,” alisema Kudra.
Hapo ndipo Amina akapata majibu juu ya kilichokuwa kikiendelea. Alikuwa mahali hapo kwa sababu ya Linda ambaye alihitaji kumsikia akizungumza uongo mahakamani kama walivyokuwa wamekubaliana.
Alilia sana, aliamini kwamba alikuwa akifanya kila kitu kwa ajili ya kumsaidia msichana huyo lakini mwisho wa siku akawatuma watu wamteke na kumfungia ndani ya chumba hicho.
Japokuwa alilia sana lakini hakuachwa. Baada ya kumwangalia na kumsikiliza alivyokuwa akipiga kelele, Kudra akachukua kisu kile kutoka kwenye jiko na kukaa kitandani.
“Ili usizungumze ni lazima tufanye hili kwanza, tunaanza miguuni, tunapanda juu mpaka mapajani, mwisho wa siku tunamalizia kwenye kizazi chako, cha muhimu ni kutuambia kwamba utasema kile tunachohitaji wewe kusema mahakamani,” alisema Kudra.
“Nitasemaaaaaaa...” alisema Amina huku akitetemeka.
“Unatudanganya, kwanza acha tucheze huu mchezo unaoitwa burn burn,” alisema Kudra, hapohapo akakichukua kisu kile kilichokuwa kimeunguzwa mpaka kuwa chekundu na kumuwekea Amina kwenye mguu wake wa kulia kwenye nyama za nyuma ya mguu.
Amina akapiga kelele za maumivu, kisu kilimuunguza kupita kawaida, Kudra hakutaka kuacha, alihakikisha kwamba pindi watakapomwachia msichana huyo mahali hapo basi aende kufanya kile walichotaka akifanye.
Kama alivyomwambia ndivyo alivyofanya, akaanza kupanda juu, kila hatua alikuwa akimuunguza mno. Kisu kilipokuwa kikipoa, kilirudishwa kwenye jiko, wakawa wanapiga stori, kilipopata moto akakichukua na kumuunguza msichana huyo mpaka kwenye paja hali iliyompa maumivu makali Amina kiasi kwamba akahisi kama Kudra alikuwa ameukata mguu wake.
Amina alikuwa kwenye maumivu makali, mapaja yake yaliunguzwa kwa kisu kile kilichokuwa cha moto, alilia sana, aliomba msamaha na msaada lakini hakukuwa na mtu aliyemsikiliza.
Moyo wake uliumia, aliendelea kujuta kwa kile kilichokuwa kimetokea, hakuamini kama kushirikiana na Linda kucheza mchezo ule mchafu ungemfanya kuwa mahali hapo akipokea mateso makali namna hiyo.
Mashavu yake yalilowanishwa na machozi, alijua kwamba angeonewa huruma na kuachwa lakini wanaume wale ndiyo kwanza waliendelea kumtesa zaidi kiasi kwamba akahisi dunia chungu.
Walimuuliza maswali mengi juu ya kile kilichokuwa kikiendelea mahakamani, walimwambia wazi kwamba hawakutaka kusikia akikataa kuwa hakubakwa, alitakiwa kuzungumza uongo na kukubaliana na mahakama kama alibakwa kitu ambacho alikubaliana nao kwa asilimia mia moja.
“Nimekubali, nitafanya mnavyotaka,” alisema Amina, alikuwa hoi, hata sauti aliyokuwa akiitumia aliongea kwa chini sana.
“Na ukitugeuka, tutakuleta tena ndani ya hiki chumba na kukumaliza kabisa, huwezi kucheza na akili zetu,” alisema Kudra.
Amina akafunguliwa kamba alizokuwa amefungwa na kutolewa nje ambapo akapakizwa ndani ya gari na kuanza kurudishwa nyumbani.
Njiani, alikuwa akiambiwa kwamba ilikuwa ni lazima azungumze kile walichomtaka kuzungumza kwani vinginevyo kama wangerudi kwa mara ya pili wasingekuwa na huruma naye hata kidogo.
Amina akakubaliana nao, alipofikishwa nyumbani, akateremshwa na kuelekea pembeni, akakaa na kuanza kuugulia maumivu makali ya mapaja yake.
Pale chini alipokuwa alikuwa akilia kama mtoto, alishindwa kutembea vizuri kwani kwa jinsi mapaja yake yalivyokuwa yameunguzwa ilikuwa ni balaa.
Kwa waliokuwa wakimfahamu wakamfuata na kumuuliza kilichokuwa kikiendelea, hakutaka kuufumbua mdomo wake na kuwaambia kilichotokea kwani alihisi kabisa kitu ambacho kingefuata ni kutekwa na kuuawa kama alivyoambiwa.
Hapo nje, akabebwa na kupelekwa ndani, alipoingia tu, simu yake ikaanza kuita, akaichukua na kuangalia kioo, namba ya Linda ilikuwa ikionekana.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Moyo wake ulichukia, hasira zikampanda, hakuamini kama msichana huyo angempigia simu tena kwani kwa njama alizokuwa amezifanya ziliubadilisha moyo wake kabisa na kuona kwamba Linda hakuwa msichana mwenye huruma kama vile alivyokuwa akihisi hapo mwanzo.
Akaanza kuzungumza naye, msichana huyo alimwambia kwa kile alichokipata kutoka kwa vijana wake kilikuwa kama trela na picha lenyewe lingekuja baada ya kusema mahakamani kwamba hakubakwa.
Moyo wake ulimchoma mno, hakutaka kuona akitoa ushahidi wa uongo mahakamani lakini kutokana na vitisho vikali alivyokuwa akipewa vilimfanya kuwa na hofu na kuona kabisa kwamba mauti ilikuwa ikimjia mbele yake.
“Dada Linda, nitafanya unachokitaka,” alisema Amina huku akionekana kuwa na hofu.
“Na usipofanya! Yaani ndiyo nitakuonyeshea sura yangu ya kishetani inafananaje,” alisema Linda kwa sauti iliyokuwa na hasira tele.
***
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment