Search This Blog

Friday, July 15, 2022

NAMTAKA MPENZI WANGU ARUDI - 3

 







    Simulizi : Namtaka Mpenzi Wangu Arudi

    Sehemu Ya Tatu (3)



    “Tatizo nini mpenzi? Kuna kitu gani kinaendelea?” aliuliza Nandy, aliishangaa hali aliyokuwanayo mpenzi wake huyo.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Dickson akabaki kimya, machozi yakaanza kumtoka na kutiririka mashavuni mwake. Aliumia mno, Nandy alibaki akishangaa, hakujua kilichokuwa kikiendelea kwa mpenzi wake huyo.

    Alimbembeleza na kumwambia amwambie ukweli juu ya kilichokuwa kikiendelea mpaka kuwa katika hali ile lakini Dickson hakusema kitu zaidi ya kuendelea kulia tu.

    Alikuwa kwenye hali hiyo kwa dakika kumi nzima, akajifuta machozi na kumwangalia Nandy tayari kwa kumwambia kile kitu alichokuwa amemuitia.

    “Nandy!” alimuita msichana huyo.

    “Nipo hapa mpenzi!”

    “Kwanza naomba unisamehe sana, najua kuna siku utajua ukweli wa kila kitu, ila naomba unisamehe sana,” alisema Dickson, akanyamaza, akaangalia chini, aibu nzito ikautawala uso wake.

    “Kuna nini? Unanitisha!”

    “Nisamehe kwa kukupoteza muda wako!”

    “Niambie kuna nini,” alisema Nandy, akaanza kuogopa.

    “Sistahili kuwa mume wako! Sistahili Nandy,” alisema Dickson na kuanza kutokwa tena na machozi.

    Moyo wa Nandy ukapiga paa, hakuamini alichokisikia, alimwangalia Dickson, alihitaji kuona kama kijana huyo alikuwa akimaanisha alichokuwa akimwambia au la.

    “Unasemaje?”

    “Naomba tuachane, naomba unisamehe kwa kukupotezea muda wako. Nahitaji kuwa huru, ninahitaji kuwa na furaha maisha yangu, najua kuna siku utakuja kujua kila kitu, ila naomba tuachane Nandy, ukipata mwanaume mwingine wa kukuoa, acha akuoe, ila naomba unisahau, naomba usahau kila kitu kuhusu mimi,” alisema Dickson kwa sauti ndogo.

    Nandy alichanganyikiwa, alimwangalia Dickson mara mbili-mbili, hakuamini alichokuwa akikisikia. Yeye mwenye machozi yakaanza kumtiririka, alihisi kama alikuwa ndotoni ambapo baada ya muda fulani angeamka na kujikuta akiwa kitandani.

    Dickson yuleyule aliyekuwa amemwambia kwamba anampenda, Dickson yuleyule aliyemthamini na kumruhusu autoe usichana wake ndiye ambaye alikuwa mbele yake na kumwambia kwamba waachane.

    Alihisi kichwa kumuuma, alihisi kitu chenye ncha kali kikiuchoma moyo wake, pale alipokuwa akaanza kutetemeka, japokuwa mgahawa huo ulikuwa ufukweni tena wakipigwa na upepo mkali wa baridi, akaanza kutiririkwa na kijasho chembamba.

    “Dickson...” aliita Nandy.

    “Naomba uniache Nandy! Sistahili kuwa mume wako,” alisema Dickson, hakutaka kubaki mahali hapo, akasimama na kuanza kuondoka.

    Nandy akasimama pia, akaanza kumfuata Dickson huku akimuita. Kila mtu aliyekuwa hapo akabaki akishangaa, ilikuwa sehemu tulivu, kulikuwa na wapendanao ambao walikuwa wakiongea mambo yao lakini kelele za kuita za Nandy zilimshtua kila mtu mahali hapo.

    “Dickson....Dickson...” aliita, Dickson akapotea machoni pake, akashindwa kusonga mbele, akahisi miguu yake ikikosa nguvu, kizunguzungu kikamuanza, hakupiga hatua zaidi, hapohapo akaanguka na kupoteza fahamu. Hakujua ni kitu gani kiliendelea baada ya hapo.



    Nandy alipata fahamu akiwa hospitalini, akayafumbua macho yake na kuangalia huku na kule, hakujua mahali alipokuwa lakini baada ya kuona dripu iliyokuwa ikining’inia juu yake, haikuwa ngumu kugundua kwamba alikuwa hospitalini.

    Akaanza kufikiria ni kitu gani kilitokea mpaka kufika mahali hapo. Alichokumbuka ni kwamba alikuwa na mpenzi wake, Dickson, walikuwa wakizungumza lakini mwanaume huyo alimwambia kwamba hakutaka kuwa naye tena kwa sababu alikuwa amepata mwanamke mwingine.

    Hapohapo kitandani alipokuwa, akaanza kulia, hakuamini kama yeye ndiye aliyeambiwa hivyo na mwanaume huyo aliyekuwa akimpenda, mwanaume aliyemuona kuwa kila kitu kwake, mwanaume ambaye alikuwa ndoto ya maisha yake, mwanaume ambaye alipanga kuwa mume wake hapo baadaye.

    Moyo wake uliuma mno, pale kitandani alipokuwa, akaanza kulia, maumivu hayakupungua, yalizidi, baada ya dakika chache, nesi mmoja akafungua mlango na kuingia ndani.

    Alipomuona Nandy analia kitandani pale, akamsogelea na kuanza kumbembeleza kwa kumtaka kunyamaza. Hakunyamaza kwani kila alipokuwa akiikumbuka sura ya Dickson alizidi kulia.

    “Kwa nini Dickson ameniacha? Kwa nini amepata mwanamke mwingine? Kwa nini? Kwa nini ameniacha?” aliuliza Nandy huku akilia.

    Hazikupita dakika nyingi baba yake, mzee Gwamaka akaingia ndani ya chumba hicho, alipomuona binti yake, akauinamisha uso wake chini, maumivu aliyosikia moyoni mwake yalikuwa makubwa mno.

    Akamsogelea na kuanza kumbembeleza, alijua kwamba binti yake alipoteza fahamu alipokuwa akizungumza na mwanaume, hakujua mwanaume huyo alikuwa nani kwani wale waliokuwa wamempigia simu na kumpa taarifa hawakumwambia kitu chochote kile zaidi ya hali aliyokuwanayo binti yake.

    Nandy alipomuona baba yake, kilio kikazidi, mzee Gwamaka akasogelea kitanda kile na kukaa karibu ya binti yake huyo ambaye alibaki akilalamika kwa kutaka kujua tatizo lilikuwa nini mpaka Dickson kumuacha.

    Mzee Gwamaka aliposikia hilo, akazidi kuumia, hakutaka kabisa kumuona mwanaye akiingia kwenye uhusiano wa kimapenzi kwa kuwa aliamini kwamba kuna siku angeumia sana, alitamani binti huyo aendelee kukaa peke yake lakini baada ya Dickson kutokea na kumuonyeshea uaminifu mkubwa, akamruhusu kuwa karibu na binti yake.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mvulana huyohuyo aliyemwamini ndiye aliyekuja kumuumiza binti yake na kumliza kitandani hapo. Hakuamini, alijilaumu na wakati mwingine kujiona akiwa amefanya kosa kubwa mno.

    Hakutaka kubaki na maumivu, alipotoka hospitalini hapo breki ya kwanza ilikuwa ni nyumbani kwa wazazi wa Dickson, alipofika, akaanza kuwaambia kilichokuwa kimetokea.

    “Haiwezekani! Dickson hawezi kumuacha Nandy,” alisema mama yake huku akimwangalia mzee Gwamaka.

    “Amemuacha, na hata alipopoteza fahamu, hakutaka kujali, akaondoka zake. Kwa nini kijana wenu amefanya hivi?” aliuliza mzee Gwamaka huku akionekana kuwa na hasira mno.

    Wazazi wa Dickson hawakutana kubaki nyumbani walichokuwa ni kwenda mpaka hospitalini kwenda kujua ukweli kama kile alichokizungumza mzee Gwamaka kilikuwa kweli au la.

    Walipofika huko na kuonana na Nandy, akawahadithia kilichokuwa kimetokea, hawakuamini, walimfahamu Dickson, alikuwa na mapenzi ya dhati kwa Nandy kiasi kwamba kwao lilionekana kuwa jambo lisilowezekana hata kidogo kwa mtoto wao kumuacha Nandy.

    Wazazi wake hawakutaka kusubiri, walichokifanya ni kumpigia simu kijana wao kwa lengo la kutaka kumsikia akizungumza hayo kwa mdomo wake. Walipompigia simu, aliwaambia kama alivyomwambia Nandy kwamba hakutaka kuwa naye kwani alipata msichana mwingine ambaye alipanga kumuoa.

    “Una akili Dickson?” aliuliza baba yake kwa hasira swali ambalo hakupanga kuliuliza hata siku moja.

    “Moyo baba! Siwezi kumuoa msichana ambaye moyo wangu haupo kwake, naomba mniache, kama ambavyo hakukuwa na mtu aliyekuchagulia mama, na mimi naomba msinichagulie,” alisema Dickson na kukata simu.

    Walichanganyikiwa, kile walichoambiwa na Dickson hakikuwaingia akilini kabisa. Hawakutaka kubaki hospitalini hapo, wakaondoka kurudi nyumbani kwao.

    Njiani, walikuwa wakizungumza mambo mengi kuhusu kijana wao. Alibadilika ghafla, hakukuwa na mtu ambaye aliamini kama angeweza kuchukua uamuzi kama huo ambao ulionekana kuwa wa ghafla sana.

    Kwao ilikuwa ni aibu nzito, wakati mwingine walijiona kama takataka kwa mzee Gwamaka ambaye alimwamini kijana wao kwa asilimia mia moja kwamba angeweza kumuoa Nandy.

    Wakati wao wakifikiria kuhusu uhusiano huo, Dickson alikuwa bize na Linda, muda wote alikuwa na msichana huyo ambaye alionekana kuwa na furaha tele.

    Walikuwa wakiyafurahia mapenzi, kwa Dickson moyo wake ulikuwa tofauti kabisa, alifanya kile alichokitaka msichana huyo kwa kuwa aliogopa kupelekwa polisi kwa kosa la kumbaka Amina chumbani.

    “Nataka tukale fungate nchini Ufaransa, kuna hoteli moja nzuri sana inaitwa La Petit, kama tukienda kule, natumaini itapendeza sana,” alisema Linda huku akimwangalia Dickson.

    Kwa kumwangalia tu lisingekuwa jambo jepesi kugundua kwamba tabasamu lile alilokuwa akilionyesha usoni mwake lilikuwa tofauti kabisa na moyo wake. Alimchukia msichana huyo kwa nguvu zote lakini hakuwa na jinsi.

    Baada ya kukaa kwa kipindi cha wiki moja, Linda akalilia kwenda kutambulishwa kwa wazazi wa Dickson kwa kuwa alikuwa na malengo naye.

    Dickson akawa na hofu, hakujua wazazi wake wangempokeaje kwani walimpenda Nandy kuliko msichana mwingine yeyote yule.

    Kabla ya kwenda huko akawapigia simu wazazi wake na kuwaambia kwamba alikuwa njiani kwenda kuwatambulisha mchumba wake ambaye angefunga naye pingu za maisha.

    Japokuwa wazazi hao walikuwa na hasira lakini katika suala kama hilo wakaituliza mioyo yao na kukubaliana na mtoto wao kwa uamuzi aliokuwa ameuchukua.

    “Una uhakika huyo ni msichana wako wa dhati?” aliuliza baba yake, alitaka kufahamu kabisa kama kijana wake aliamua kwa moyo mmoja au alilazimishwa.

    “Nimeamua baba! Huyu ni mwanamke wangu wa ndoa!”

    “Una uhakika?”

    “Ndiyo!”

    “Na anakupenda?”

    “Ndiyo baba!”

    “Na wewe unampenda?”

    “Kupita maelezo!”

    “Sawa.”

    Wakaelekea nyumbani kwao na walipofika huko, akaonana na wazazi wake huku akiwa na Linda na kuanza kuzungumza naye. Aliwaambia kwamba huyo ndiye alikuwa mchumba wake ambaye alitaka kufunga naye ndoa.

    Hakuishia hapo, aliwahadithia maisha yao tangu zamani, jinsi walivyokuwa wamesoma wote, kupendana na hata msichana huyo alipoondoka kwenda Ulaya kusoma.

    Hilo likawafanya wazazi wake kuhisi kwamba kweli Dickson alikuwa akimpenda msichana huyo, walichokifanya ni kukubaliana naye na kutoa baraka zote kama wazazi japokuwa mioyo yao haikumkubali Linda hata kidogo na walihisi kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea ambacho Dickson hakutaka kuwaambia.

    “Na mmepanga kuoana?” aliuliza mama yake.

    “Ndiyo mama! Tunatarajia kufunga ndoa baada ya miezi miwili,” alisema Dickson maneno yaliyowashtua.

    “Miezi miwili?”

    “Ndiyo!”

    “Mbona haraka sana?”

    “Kwa sababu tumeamua, tumeishi sana maisha ya ujana, wasije wakatokea akina Nandy wengine,” alisema Dickson.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Sawa. Haina shida. Tunawatakia maandalizi mema,” alisema baba yake.

    ***

    Nandy alikuwa na maumivu makali moyoni mwake, hakuamini kile kilichotokea kwamba mpenzi wake, Dickson alikuwa amemuacha na kumchukua mwanamke mwingine.

    Kila siku alikuwa mtu wa kulia tu, hakuamini kama kweli yeye ndiye aliyekuwa akipitia maisha hayo. Wakati mwingine alipiga magoti na kumuomba Mungu msamaha, alihisi kwamba hayo ndiyo yalikuwa matokeo yake ya kuchanganya mambo ya kidunia na kiroho.

    Hakuwa na furaha, hata alipokuwa akienda kanisani na kuimba mbele ya kanisa, alionekana kabisa kutokuwa na furaha hata kidogo.

    Hali yake ikazua maswali mengi, wengi wakataka kufahamu sababu ya msichana huyo kubadilika ghafla lakini hakukuwa na mtu yeyote yule aliyegundua kitu chochote kile.

    Kilichotokea kilikuwa siri yake na baba yake. Japokuwa aliumizwa na Dickson lakini moyo wake haukuwahi kumchukia kijana huyo, alimpenda, yeye ndiye aliyemuonyesha jinsi dunia ya mapenzi yalivyo, ndiye mwanaume aliyemvua nguo yake na kufanya mapenzi kwa mara ya kwanza.

    Aliyakumbuka maisha yaliyopita aliyoishi na Dickson, moyo wake uliumia mno na wakati mwingine alijiahidi kuwachukia wanaume, kuyachukia mapenzi lakini kitu cha ajabu kabisa alishindwa kabisa kumchukia Dickson.

    Siku zikaendelea kukatika, moyo wake uliamini kwamba mwanaume huyo angerudi tena kwake na kuanza kuyapanga mambo yao kwa mara nyingine lakini hilo lilishindikana.

    Alitamani kuifuata namba ya mwanaume huyo katika simu yake, alijaribu kufanya hivyo lakini alishindwa kabisa, kila alipotaka kuifuata, kwanza aliiandika pembeni, alipoifuta baadaye akaisevu tena.

    Yalikuwa ni maisha ya mateso makubwa, mapenzi yalimuendesha kupita kawaida. Siku zilizidi kukatika. Kwa kumuonyeshea Linda kwamba alikuwa akimpenda, Dickson akawa anaweza status za mapenzi kwenye Mtandao wa WhatsApp, akawa anaweka picha nyingi akiwa na msichana huyo kitu ambacho kilimuumiza sana Nandy.

    Mwili wake ukadhoofika, alikonda kutokana na mawazo aliyokuwanayo. Wengi walimjadili na kuhisi kwamba alikuwa mgonjwa lakini zaidi ya kukonda hakuwahi kwenda hospitalini.

    Kila siku kazi yake ikawa ni kumuomba Mungu tu, alimwambia kwamba alitamani kuyabadilisha maisha yake, kitu cha kwanza alichohitaji Mungu akifanye kilikuwa ni kuubadilisha moyo wake, amuondoe Dickson moyoni mwake na kuliweka neno lake, mistari mingi ya Biblia ambayo aliamini kwamba ingembadilisha lakini hilo lilishindikana.

    Baada ya kumalizika mwezi mmoja, akatumiwa ujumbe na Dickson kwamba alitarajiwa kufunga ndoa na Linda hivyo alitakiwa kuhudhuria harusi hiyo ambayo ingefungwa katika Kanisa la Mtakatifu Yehova lililokuwa Mwenge, jijini Dar.

    Ulikuwa ni ujumbe wenye kuuma sana, siku hiyo alilia zaidi ya alivyolia siku alipoachwa na mwanaume huyo. Akajifungia chumbani, alihitajika kwenda kanisani kwa ajili ya mazoezi ya kwaya lakini akashindwa kabisa kutokana na maumivu aliyokuwanayo kipindi hicho.

    Kwake, hayo yote yalionekana kuwa majaribu makubwa. Hata alipoanza kwenda chuo, hakuona raha ya kusoma kwa kuwa alikuwa akimuona sana Dickson huko kitu kilichomfanya kuumia mno.

    “Mungu! Siwezi kuishi! Nimeshindwa, nimeshindwa Mungu! Maumivu yamenizidi,” alisema Nandy.

    Hakuona sababu ya kuendelea kuishi tena, kama kuumia, aliumia kupita kawaida, alichokuwa amekifikiria kilikuwa ni kujimaliza tu.

    Kichwa chake kikafikiria sehemu ambayo angeweza kujimaliza vizuri, kilichokuja kichwani mwake kilikuwa ni kwenda katika Ghorofa la LAPF lililokuwa Makumbusho, apande mpaka juu kabisa na kujirusha.

    Alipopata wazo hilo, hakutaka kubaki chuoni, akatoka, akachukua bodaboda na kumwambia dereva ampelekea Makumbusho.

    Safari ikaanza, njiani alikuwa akimuomba Mungu msamaha kwa uamuzi aliokuwa ameuchukua, hakutaka kuendelea kuishi huku akiwa na maumivu moyoni mwake, ili awe na furaha, amani ilikuwa ni lazima kujimaliza.

    Pikipiki ilikuwa ikiendeshwa kwa mwendo wa kasi. Ilipofika Mwenge, dereva akakata kushoto na kuchukua Barabara ya Ally Hassan Mwinyi na kuanza kuitafuta Bamaga.

    Wakati dereva akiwa kwenye mwendo wa kasi, kwa mbele yake akaiona gari ikija kwa mwendo wa kasi. Hakuogopa, alikaa upande wake akiwa anaendesha kwa mwendo wa kasi pia.

    Wakati gari lile la upande mwingine lilipokuwa limekaribia, dereva wa gari hilo akayumba, akahama njia na kwenda katika upande ule uliokuwa pikipiki ile, hapohapo wakakutana uso kwa uso.

    Ulisikika mzinga mkubwa, gari likabondeka kwa mbele, pikipiki ikarushwa, dereva na Nandy wakarushwa, na kwa sababu Nandy hakuwa amevaa helmenti, akafikia kichwa kwenye lami, damu zikaanza kumtoka, kama jinsi alivyokuwa amefikia, akatulia hivyohivyo juu ya lami, hakutingishika hata kidogo.

    “Mungu wangu!” alisema jamaa mmoja huku wakiwakimbilia watu hao.

    Dereva alivunjika miguu na kiuno huku Nandy kwa kumwangalia harakaharaka, alikuwa amevunjika shingo na alionekana kuumia sana kichwani na mgongoni akiwa amechunika kutoka na mwili wake kuburuzika kwenye lami kabla ya kufikia pembeni kidogo ya mtaro na kutulia hapo.

    “Jamani huyu mwanamke naye vipi? Mzima?” aliuliza jamaa mmoja.

    “Huyu amekufa! Jamani simamisheni gari tuupeleke mwili huu hospitali,” alisema mwanaume mwingine aliyekuwa amemsogelea Nandy pale alipokuwa.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Nandy alifikishwa katika Hospitali ya St. Magreth iliyokuwa Kijitonyama akiwa hajitambui, kila mtu aliyemwangalia hakuamini kama kungekuwa na mtu ambaye angeumia vibaya kama ilivyokuwa kwake.

    Mwili ulijaa damu, kichwani ndiyo ilikuwa balaa kiasi kwamba hata sura yake haikuwa ikionekana kabisa, yote ilitapakaa damu.

    Manesi wakamchukua na kumpeleka katika chumba cha wagonjwa mahututi ambapo huko akaoshwa na kupelekwa katika chumba cha upasuaji, ilikuwa ni lazima kuokoa maisha ya binti huyo kwani alikuwa kwenye hatari ya kuyapoteza maisha yake.

    Watu waliokuwa wamempeleka mahali hapo walikuwa wakisubiri taarifa rasmi kwa madaktari kwani tayari walijua kwamba alikufa hivyo walisubiri uthibitisho kutoka kwa madaktari tu.

    “Ni ndugu yenu huyu?’ aliuliza nesi mmoja huku akiwaangalia watu waliompeleka Nandy hospitalini hapo.

    “Hapana! Tumemsaidia tu! Vipi? Amekufa?” aliuliza jamaa mmoja.

    “Hapana ila hali yake ni mbaya sana!” alijibu nesi huyo.

    Wale waliokuwa wakishughulika na Nandy ndani ya chumba kile walikuwa bize, kwa jinsi alivyokuwa ameumia ilikuwa ni lazima afanyiwe upasuaji wa kichwa ambao kwa kitaalamu uliitwa Craniotomy.

    Kwa kuwa hospitali hiyo haikuwa kubwa, Nandy alitakiwa kuhamishwa na kupelekwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambapo huko wangemfanyia vipimo vyote ili hata kama upasuaji wa kichwa ungefanyika basi ingekuwa ni rahisi kujua ni kitu gani kilitakiwa kufanyiwa kazi.

    Haraka sana simu ikapigwa kitengo cha usafirishaji, gari likaandaliwa na ndani ya dakika kadhaa kupandishwa garini na kupelekwa katika hospitali hiyo huku akiwa hajitambui.

    Walipofika, akateremshwa na kupelekwa ndani ya hospitali hiyo. Akachukuliwa na moja kwa moja kuingizwa katika chumba ambacho alitakiwa kufanyika hatua ya kwanza ya kuangalia tatizo lililokuwa kichwani mwake.

    Hapo, akachukuliwa na kuingizwa kwenye mashine ya MRI (Magnetic Resonance Imaging) na kugundulika kwamba kulikuwa na donge la damu katika ubongo wake, lilikuwa limeganda kiasi kwamba liliyahatarisha maisha yake.

    Alitakiwa kupasuliwa kichwa na donge lile litolewe kwani kwa jinsi hali ilivyokuwa ikionyesha, ilionekana kuwa mbaya sana kama tu wasingefanya kila liwezekanalo kuhakikisha donge lile la damu linatolewa.

    Haraka sana daktari bingwa kwa upande wa upasuaji wa kichwa, Dk. Ezekiel Ndaki akapigiwa simu na kufika mahali hapo haraka sana. Nandy akachukuliwa na kupelekwa katika chumba maalumu cha upasuaji na kuanza kufanyiwa kazi.

    “We have to perform Craniotomy very fast,” (ni lazima tumfanyie upasuaji wa kichwa haraka) alisema daktari huyo.

    “Will she be okey?” (atapona kweli?) aliuliza nesi mmoja huku akionekana kuogopa.

    “Is this your first time to help me?” ( hii ni mara yako ya kwanza kunisaidia?) aliuliza Dk. Ndaki.

    “Yeah!”

    “Are you scared?” (unaogopa?)

    “A little bit!” (kidogo tu) alijibu, Dk. Ndaki akatabasamu kidogo.

    Nandy alizungukwa na madaktari, manesi waliokuwa mahali hapo kwa ajili ya kumfanyia upasuaji, pale kitandani alikuwa kimya, hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea.

    Upasuaji ukaanza, vifaa vyote vilivyokuwa vikihitajika vikawekwa tayari na kila mmoja kuwa makini katika kazi hiyo kwani kukifumua kichwa cha mgonjwa na kulitoa donge la damu lililokuwa kwenye ubongo haikuwa kazi ndogo kwani walitakiwa kuwa makini na kutokuichana mishipa iliyokuwa ikisafirisha damu kupeleka kichwani na kurudishwa katika moyo.

    Kichwa kikachanwa na fuvu la kichwa kupasuliwa, kilichoonekana kilikuwa ni ubongo ambao ulikuwa na donge kubwa la damu.

    Dk. Ndaki akaanza kuhangaika kulitoa donge hilo. Haikuwa kazi ndogo kwani kila alipokuwa akilisogelea, lilikwenda pembeni.

    Lilimsumbua mno lakini mwisho wa siku akawa amefanikiwa kulikamata kwa kifaa maalumu na kulitoa huku tayari wakiwa wametumia muda wa saa tatu mpaka kumaliza.

    Dk Ndaki akashusha pumzi nzito, alimshukuru Mungu na hivyo akatakiwa kurudishwa katika chumba kilichokuwa mashine ya MRI na kufanyiwa tena uchunguzi kwani waligundua kwamba mbali na kupasuka kichwa pia kulikuwa na uwezekano wa kuwa na tatizo jingine.

    Katika uchunguzi wao wa kina wakagundua kwamba Nandy alikuwa amevunjika uti wa mgongo na ndiyo maana hata alipokuwa amefikia katika barabara hakuweza kutingishika kwa kuwa uti huo haukuwa ukipeleka mawasiliano kichwani.

    Madaktari wote hawakuamini, hakukuwa na kitu walichokuwa wakikiogopa kama kuvunjika kwa uti wa mgongo, kwa maana hiyo hata kama mgonjwa huyo angepona, bado kungekuwa na tatizo kubwa katika maisha yake, mwili wake usingeweza kufanya kazi tena, angepooza kitandani maisha yake yote na ni kichwa tu ndicho ambacho kingetingishika.

    “Mungu wangu!” alisema daktari mmoja huku machozi yakimlenga, ripoti ya taarifa ya Nandy ilimuumiza mno kana kwamba alikuwa mtoto wake wa kumzaa.

    Wakati madaktari wakiendelea kumshughulikia msichana huyo, huku upande wa pili baba yake, mzee Gwamaka alikuwa bize akimtafuta binti yake.

    Alijaribu kumpigia simu lakini haikuwa ikipatikana, moyo wake ulikuwa na hofu, hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea, alichanganyikiwa, aliwapigia ndugu, jamaa na marafiki lakini kote huko walisema kwamba hawakujua mahali alipokuwa.

    Haraka sana akampigia simu Dickson na kumuuliza kuhusu binti yake, alimwambia kwamba hakuwa amekutana naye kwa siku mbili hivyo hakujua kitu chochote kile.

    “Kwani hajarudi nyumbani?” aliuliza Dickson.

    “Ndiyo! Si kawaida yake, saa mbili sasa hivi lakini hajarudi,” alisema mzee Gwamaka.

    Japokuwa hakuwa na Nandy kwa sababu ya Linda lakini taarifa hizo zilimshtua mno, hakutaka kubaki chuoni, akaondoka na moja kwa moja kuelekea nyumbani kwa kina Nandy, alipofika huko, hakumkuta mzee Gwamaka na alipouliza alijibiwa kwamba alikwenda nyumbani kwa mchungaji.

    Akaelekezwa na kuelekea huko. Moyo wake ulimwambia kwamba kulikuwa na tatizo lililokuwa limetokea. Njiani, hakumfikiria Linda, akaanza kumfikiria Nandy ambaye kwake alionekana kuwa kila kitu japokuwa Linda aliingilia kati.

    Alipofika huko, akamkuta mzee huyo akiwa amchanganyikiwa, simu ya msichana huyo haikuwa imepatikana hivyo kuunganisha nguvu kumtafuta msichana huyo.

    Mzee Gwamaka hakumpenda Dickson, alimchukia kwa kuwa alimuumiza binti yake lakini kwenye hali kama aliyokuwanayo, hakuwa na jinsi, akaungana naye na kuanza kwenda huku na kule kumtafuta msichana huyo.

    Ilipofika majira ya saa sita usiku, wakaamua kuzunguka kwenye hospitali mbalimbali na kuulizia kama alifikishwa huko akiwa maiti. Wakaelekea katika mochwari za hospitali zote lakini hakukuwa na majibu.

    “Twende Muhimbili,” alisema Dickson.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wakaelekea huko, sehemu ya kwanza kabisa kufika ilikuwa ni mochwari ambapo huko wakaenda na kuanza kumtafut Nandy, walimkosa, hilo liliwachanganya sana na kwenda kuulizia kwa manesi ndipo wakapewa taarifa kuhusu wagonjwa walioletwa hospitalini hapo siku hiyo.

    “Kuna msichana?” aliuliza mzee Gwamaka.

    “Wapo sita hivi.”

    “Majina?”

    Akawatajia lakini akawaambia kwamba wawili hawakuwa wakijulikana. Wakataka kuwaona hao wawili, wakapelekwa kwa mmoja, walipomwangalia, hakuwa Nandy.

    “Na huyo mwingine?”

    “Huyo yupo mahututi, tangu aletwe hospitali hajanyanyuka, alipata ajali mbaya sana,” alisema.

    “Ajali mbaya?”

    “Ongeza sana.”

    Wakataka kumuona msichana huyo. Hawakuruhusiwa kumuona kwa kipindi hicho mpaka baada ya daktari kufika kwa lengo la kumjulia hali.

    Akawaambia kuhusu watu hao kwamba walitaka kumuona mgonjwa huyo kwani walikuwa wakimtafuta ndugu yao aliyekuwa amepotea na mpaka muda huo, saa nane usiku hawakujua mahali alipokuwa.

    Kwa kuwa walikuwa wamechoka na walionekana kutaka kujua kuhusu ndugu yao, wakachukuliwa na kupelekwa katika chumba hicho.

    Kwa mbele walimuona msichana akiwa kitandani, hakuwa akitingishika, aliwekewa dripu huku akipumua kwa kutumia mashine ya gesi. Kichwa chake kilizungushiwa bandeji, kwa kumwangalia pale alipokuwa ilikuwa rahisi sana kugundua kwamba mtu huyo alikuwa mahututi.

    Wakaanza kumsogelea, walipomfikia na kumwangalia usini. Alikuwa Nandy. Mzee Gwamaka akahisi miguu yake ikipigwa ganzi, hakuweza kusimama, akajikuta akikaa chini na kuanza kulia.

    Dickson, hakuamini alichokuwa akikiangalia, kwanza akahisi kwamba alikuwa akiota, Nandy, msichana aliyekuwa akimpenda kwa moyo wote hakuamini kama siku hiyo angekuwa katika hali aliyokuwanayo kipindi hicho.

    Alishindwa kuyazuia machozi yake, moyo wake ulimuuma mno, akapata hasira kali dhidi ya Linda, japokuwa ilikuwa ni ajali tu lakini akahisi kama yeye ndiye aliyehusika katika ajali hiyo kwa kuwa tu hakumtakiwa kuwa na msichana huyo.

    “Nandy!” aliita Dickson huku akimsogelea na kumwangalia vizuri.

    Nandy hakuyafumbua macho yake, aliyafumba na kutulia, kwa jinsi alivyokuwa ametulia ilikuwa rahisi sana kusema kuwa msichana huyo alifariki dunia.

    “Nandy...Nandy...Nandy! Forgive me,” (Nandy...Nandy...Nandy...nisamehe) alisema Dickson huku akitokwa na machozi.

    Dokta hakutaka waendelee kubaki ndani ya chumba hicho, akawachukua na kutoka nao. Akaelekea nao ofisini na kuanza kuwaambia kuhusu mgonjwa wao.

    Wote wawili walikuwa wakitokwa na machozi, waliumia, pamoja na kuwa katika hali ya huzuni lakini walitakiwa kuambiwa kitu kingine ambacho kingewatia huzuni zaidi.

    “Kuna jambo jingine kuhusu mgonjwa wenu,” alisema Dk. Ndaki huku akiwaangalia kwa zamu.

    “Tatizo gani?”

    “Mgonjwa wenu....kwanza alipata ajali, donge la damu liliganda kwenye kichwa chake lakini tulifanikiwa kulitoa baada ya kumfanyia upasuaji wa kichwa. Ila kuna tatizo jingine ambalo mnatakiwa kulifahamu,” alisema dokta, hapo, akanyamaza, wote wakabaki wakimwangalia.

    “Lipi?” aliuliza Dickson.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ni kwamba mgonjwa wenu amevunjika uti wa mgongo,” alisema dokta, wote wakabaki wakimwangalia.

    “Uti wa mgongo kwa maana hatoweza.....”

    “Kufanya lolote lile, atapooza, maisha yake yote yatakuwa kitandani tu,” alisema daktari, palepale kwenye kiti wote wawili wakaanza kulia kwa sauti kubwa kama watoto wadogo.



    “Eti uko wapi?” ilisikika sauti ya mwanamke kwenye simu.

    “Kijiweni!”

    “Upo na wenzako au?”

    “Yeah! Kama kawaida yetu. Umeadimika sana, usharudi kutoka Uingereza?”

    “Ndiyo! Kitambo fulani! Naomba tuonane kuna kitu nataka tuzungumze,” ilisikika sauti ya msichana huyo.

    “Sawa.”

    Aliyekuwa akiongea kwenye simu alikuwa msichana Linda. Moyo wake ulikuwa umewaka kwa hasira, hakutaka kukubali kuona kile ambacho kilitarajiwa kutokea kikitokea.

    Alichokuwa akikifikiria ni kuupa moyo wake furaha ya milele, hakutaka kuona mtu yeyote anakuja na kuivuruga furaha aliyokuwanayo. Alijua kwamba alimpoteza Dickson kwa mara ya kwanza kabla ya kumrudia, hakutaka kuona akimpoteza kwa mara nyingine tena.

    Alikuwa tayari kufanya kila kitu lakini mwisho wa siku kuwa na mwanaume huyo milele yote. Ili aishi kwa furaha, kulikuwa na mtu mmoja tu ambaye alitakiwa kuondoka duniani, huyo alikuwa Nandy.

    Alikutana na kijana aliyekuwa amezungumza naye kwenye simu na kuanza kupanga mipango. Alichomwambia kijana huyo ni kwamba alitaka kumshuhudia Nandy akifa tu.

    Alimwambia jinsi mipango ilivyotakiwa kufanyiwa kazi, yeye na wenzake walitakiwa kwenda mpaka chuoni na kumteka msichana huyo, waondoke naye na kwenda kumuua sehemu na mwili wake kuuweka kwenye kiroba.

    Jamaa huyo aliyeitwa kwa jina la Hamisi akasikiliza maelezo ya Linda na kuona kabisa kungekuwa na ugumu wa kumuua msichana huyo kwa mauaji aliyokuwa ameyapanga, kama kweli walitaka kumuua basi wamuue kidigitali, kusiwe na mtu yeyote ambaye atagundua kama msichana huyo ameuawa.

    “Kivipi?” aliuliza Linda.

    “Tutengeneze ajali! Tumuue kwenye ajali, hilo tu,” alisema Hamisi.

    Wazo hilo lkaingia kichwani mwa Linda na alichomwambia ni kwamba walitakiwa kulifanya jambo hilo haraka sana.

    Akawapa picha ya Linda ambayo aliiba katika simu ya Dickson na hivyo Hamisi na wenzake kuanza kwenda chuoni kumtafuta msichana huyo.

    Walipewa data zote kuhusu Nandy, hakukuwa na kitu kilichowachanganya, wakafanikiwa kumuona msichana huyo chuoni hapo na hivyo kuanza kujipanga kutekeleza adhima yao.

    Siku zikaendelea kukatika mpaka kufika siku ambayo walitakiwa kummaliza Nandy. Wakajigawa, kwa kuwa alikuwa akisoma chuo na kurudi nyumbani kwa usafiri wa bodaboda basi wangeweza kummaliza kwa kumgonga na gari.

    Wakajipanga na magari yao, walitakiwa kufanya kila linalowezekana lakini mwisho wa siku majibu yatoke kwamba msichana huyo alikuwa amefariki dunia.

    Walikuwa vijana sita, walijua kwamba msichana huyo alikuwa akiishi Kurasini hivyo kama alitakiwa kuondoka hapo ilikuwa ni lazima kutumia Barabara ya Mandela kuelekea nyumbani kwao.

    Wakamweka mtu mmoja kwenye gari alilolipeleka mpaka Mabibo Hostel, mwingine akapelekwa mpaka Barabara ya Shekilango karibu kabisa na kuingia katika Barabara ya Morogoro, mwingine akawekwa katika Barabara ya Sam Nujoma, huyo alitakiwa kuwasiliana na wenzake kama gari lingekwenda Mbezi Beach au Makumbusho, lakini mbali na hao, pia kuna mwingine akawekwa Kimara, yote hiyo ilikuwa ni kumvizia msichana huyo katika barabara zote.

    Wakati wao wakiwa wamejipanga, Hamisi alikuwa chuoni akimfuatilia msichana huyo. Alijifanya kuwa bize, mgongoni alikuwa na begi lake, alikuwa na muonekano kama mwanachuo.

    Nandy alipotoka darasani, kama kawaida yake akaelekea sehemu ya bodaboda, akachukua na kuondoka mahali hapo. Hamisi hakujua mahali alipokuwa akienda, naye akachukua pikipiki yake aliyokwenda nayo na kuanza kuwafuatilia.

    Ilipofika Barabara ya Sam Nujoma, bodaboda ile ikakata kushoto hali iliyoonyesha kwamba ilikuwa ikienda Makumbusho au Mbezi Beach.

    Kichwa chake kilikuwa kinajiuliza sababu ya msichana huyo kwenda huko. Muda ulikuwa umekwenda na alitakiwa kurudi nyumbani lakini cha ajabu, alikuwa akielekea upande mwingine kabisa.

    Alipofika Mwenge, bodaboda ikakata kona kulia, ikachukua Barabara ya Ali Hassan Mwinyi kuelekea Makumbusho.

    “Anakuja upande wenu. Dereva kavaa fulana nyeusi, kampakiza dada mwenye blauzi ya pinki,” alisema Hamisi na hivyo dereva wa gari lililokuwa Bamaga akaliwasha na kuanza kuelekea Mwenge huku akiwa kwenye mwendo wa kasi.

    Kwa jinsi ajali ile ilivyotokea, hakukuwa na mtu aliyehisi kwamba ilikuwa imetengenezwa. Nandy aligongwa na gari lakini kitu cha ajabu dereva wa gari lile alikuwa amekimbia.

    Baada ya nusu saa, Hamisi ambaye aliishuhudia ajali ile akampigia simu Linda na kumwambia kile kilichokuwa kimetokea, alimuelezea mazingira ya ajali hiyo na hata jinsi Nandy alivyokuwa ameumia vibaya.

    “Linda...” aliita Hamisi.

    “Niambie!”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Yule dada akipona, naenda kuogelea baharini kule Morogoro,” alisema Hamisi huku akiwa na uhakika kwamba Nandy hawezi kupona.

    “Kwani imekuwaje?”

    “Ungebahatika kumuona, ungejiuliza kagongwa na treni au ajali ya gari na pikipiki,” alisema Hamisi huku akionekana kuwa na furaha kwani alikuwa na uhakika wa kulipwa malipo yao yaliyobaki kwa kazi kubwa waliyokuwa wameifanya.

    ***

    Mzee Gwamaka hakukumbuka kuhusu ubaya wa Dickson, kitu pekee alichokuwa akikiangalia ni hali ya mtoto wake tu. Alikuwa kitandani, tangu siku ya kwanza alipokuwa amepelekwa hospitalini hapo mpaka siku ya tatu hakuwa amefumbua macho yake.

    Nandy alikuwa kwenye hali mbaya, ingekuwa rahisi kusema kwamba tayari alikuwa amefariki dunia kwani hakuwa ametingishika tangu siku ya kwanza alipofika mahali hapo.

    Dickson hakutaka kuondoka hospitalini, siku zote hizo tatu ambazo Nandy alikuwa hospitalini hapo alikuwa pembeni ya kitanda alicholalia. Muda wote alikuwa mtu wa kulia tu, macho yake yalikuwa mekundu kupita kawaida.

    Linda alimpigia simu kwa lengo la kuzungumza naye lakini hakupokea, kwa wakati huo, alikuwa tayari kwa kitu chochote kile, alikuwa tayari kufungwa gerezani kwa kosa la kutaka kubaka lakini hakutaka kuona akimpoteza Nandy, msichana aliyekuwa akimpenda kwa moyo wa dhati.

    Wazazi wa Dickson ndiyo waliokuwa wakigharamia kila kitu hospitalini hapo, walitamani kumuona kijana wao akiwa na furaha, kitendo cha kumuhudumia Nandy kwa kila kitu waliamini kwamba kingeweza kumfanya Dickson kuwa na furaha moyoni mwake.

    Washirika wa kanisa alilokuwa akisali walifika hospitalini hapo na kumuona Nandy, kila aliyemuona alisikitika, ilikuwa ni vigumu kuamini kile kilichokuwa kikionekana kitandani, Nandy yuleyule aliyekuwa na sauti kali ya kumuimbia Mungu leo hii alikuwa kimya kitandani.

    Wachungaji kutoka katika makanisa mbalimbali nao walimiminika hospitalini, walimfahamu Nandy, alikuwa binti maarufu makanisani, alimsifu sana Mungu, kitendo cha kupata ajali ile kiliwashtua sana na hilo ndilo lililowapeleka hospitalini huko kumwangalia.

    Japokuwa alikuwa amelazwa kwa siku tatu lakini hakukuwa na maendeleo yoyote yale, alikuwa vilevile kama alivyoletwa huku kila siku akila na kujisaidia kwa kutumia mipira iliyokuwa imefungwa mwilini mwake.

    “Nandy mpenzi....” alisema Dickson huku akimwangalia Nandy kitandani pale.

    “Najua nimekukosea, hukustahili kuumizwa kama nilivyokuumiza, najuta kwa kuchukua uamuzi wa kijinga namna ile. Mimi ni mwanaume ambaye nilitakiwa kuonyesha uanaume wangu hata kama ningeambiwa kwamba nafungwa gerezani milele.

    “Nandy! Najua hii yote ni kwa sababu yangu! Kwa nini nimekuumiza? Kwa nini nilikubali kukuacha? Mimi ni mpumbavu, mimi ni shetani, sikutakiwa kukulipa wema kwa ubaya. Ulinionyesha mapenzi, yaani yote yale nimekuja kukuacha kwa sababu ya uoga? Yaani uoga wangu ndiyo ulinifanya nikuache na kukuumiza namna hii? Nandy! Ninakupenda, nipo hapa, sitoondoka hospitalini mpaka siku ambayo utafumbua macho yako na kuniangalia tena,” alisema Dickson huku akiwa pembeni ya kitanda alicholalia Nandy.

    Kwa jinsi alivyokuwa akiongea ilikuwa ni rahisi kugundua kwamba alikuwa ameumizwa moyoni mwake. Machozi yalikuwa yakimtoka, yalitiririka mashavuni mwake na kulowanisha shati lake kifuani na kuonekana kama alimwagiwa maji.

    Macho yake yalikuwa mekundu sababu ya kulia sana. Hakulia siku hiyo tu, kwa siku tatu mfululizo alikuwa akilia na hakutaka kuondoka hospitalini hapo, alikuwa tayari kupoteza kila kitu lakini si kumuacha Nandy akiendelea kuteseka.

    Marafiki zake walifika na kumpa pole, walimuonea huruma rafiki yao, kwa jinsi alivyokuwa akilia, alionekana kuumia kupita kawaida. Alitia huruma, alionekana kukata tamaa, hakuonekana kuwa na imani kwamba kuna siku Nandy angeweza kuamka kitandani hapo.

    Siku zikaendelea kwenda mbele, mpaka mwezi unakatika bado Nandy aliendelea kuwa kitandani hapo huku akiwa kimya kabisa. Alikuwa akipumulia mashine ya gesi, mipira ikiwa imechomekwa mwilini mwake kwa ajili ya chakula na kwenda haja.

    Baada ya kuona hakukuwa na maendeleo yoyote yale, wazazi wa Dickson wakaamua kwa pamoja kwamba msichana huyo alitakiwa kusafirishwa na kupelekwa nchini India kwa matibabu zaidi.

    “Baba! Unadhani huko kunaweza kumrudisha mpenzi wangu?” aliuliza Dickson.

    “Tuna imani hiyo! Atarudi na kuungana nawe kwa mara nyingine,” alisema baba yake huku naye akilengwa na machozi kwani kila alivyomwangalia Dickson kwa jinsi alivyokuwa ameumizwa, alijisikia uchungu moyoni mwake.

    Wakakumbatiana! Waliendelea kubaki hospitalini hapo huku Nandy akiendelea kulala kitandani huku akiwa hajitambui.

    Jopo la madaktari kila siku lilikuwa likikutana katika chumba cha mkutano na kujadili hali ya Nandy. Hakukuwa na mabadiliko yoyote yale, uti wa mgongo ulikuwa vilevile, kichwani hakuwa amepata nafuu kama walivyokuwa wakitegemea.

    Baada ya kusikia kwamba wazazi walikubaliana kumsafirisha mgonjwa mpaka nchini India kwa matibabu zaidi, wakashukuru Mungu kwani walihisi kabisa kwamba hiyo kidogo ingewasaidia.

    Haraka sana wakaanza kufanya mawasiliano na Hospitali ya Apollo iliyokuwa Chennai nchini India na baada ya wiki moja, harakati za safari zikaanza kufanyika, mgonjwa akaandaliwa na siku iliyofuata safari ya kuelekea nchini India ikaanza.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Bado Dickson alikuwa pembeni mwa Nandy, kulia ilikuwa sehemu ya maisha yake, pale alipokuwa hakuyatoa macho usoni mwa Nandy, alikuwa akimwangalia huku moyo wake ukiwa na mambo mengi mno.

    Ili kuonyesha kwamba alikuwa ameumizwa sana na kile kilichokuwa kikiendelea, akawa anaweka posti katika mtandao wa WhatsApp kwa status na kuelezea hisia zake, jinsi alivyokuwa mpumbavu kuachana na msichana huyo, alivyokuwa akimuomba msamaha na mambo mengine mengi.

    “Huyu mwanamke ni shetani! Nipo tayari kwa lolote sasa,” aliandika kwenye status moja WhatsApp huku akiwa ameweka picha ya msichana huyo.

    Linda alipoiona tu, akajua sasa kwamba vita vilikuwa vimeanza na hakuwa na dalili za kuolewa na mwanaume huyo.

    “Kama kamwaga ugali, namwaga mboga!” alisema Linda kwa hasira huku akiwa amevimba na uso kutawaliwa na ndita.



    Amina hakutaka kabisa kuwasiliana na Dickson kwa kuwa kile alichoambiwa na Linda akifanye alikifanya kwa mafanikio makubwa. Moyo wake ukaridhika na hivyo kuendelea na maisha yake.

    Picha ya Dickson haikutoka kichwani mwake, alimpenda mwanaume huyo kwa moyo wa dhati, tabasamu lake lilikichanganya kichwa chake na muda mwingi alikuwa akipambana kumtoa kijana huyo asikisumbue kichwa chake lakini ilishindikana kabisa.

    Kwa kitendo chake cha kuacha kuwasiliana na Dickson kilimuuma mno, kwake, mwanaume huyo alionekana kuwa kama malaika ambaye hakutakiwa kupotezwa na mwanamke yeyote yule.

    Kuwa na Dickson, hakukuhitaji pesa kwani kumwangalia yeye tu kuliyafanya maisha yako kuonekana kukamilika, hata kama unamiliki baiskeli tu, lakini kuwa naye ilikuwa ni sawa na kujiona ukimiliki Prado.

    Hata kama ulikuwa na njaa ndani ya nyumba na hakuna chakula, kuwa na Dickson pembeni ilikuwa ni sawa na kuliangalia sinia pembeni lililokuwa na pilau la kutosha.

    Moyo wake ulimuuma mno kutokuwasiliana na mwanaume huyo kwani kwake japokuwa alitembea na wanaume wengi lakini kwa Dickson alionekana kufa na kuoza.

    Baada ya siku kadhaa akaamua kuweka laini yake kwenye simu yake kwani aliamu kuachana nayo kwa kipindi fulani baada ya kuona akitafutwa sana na Dickson.

    Alipoiweka tu, kitu cha kwanza kilikuwa ni kuingia kwa meseji nyingi za mabwana zake na huku wengine wakilalamika kuachwa na wakati walikuwa kwenye mapenzi ya dhati.

    Hakutaka kujali kuhusu meseji hizo, haraka sana akaenda WhatsApp na kulitafuta jina la Dickson, alipolipata, macho yake yakatua katika picha ya msichana fulani aliyekuwa amelala kitandani huku dripu ikining’inia juu yake.

    Moyo wake ukamshtuka, picha aliyokuwa akiiona ilimtisha sana, aliiangalia kwa sekunde thelathini kisha kuingia katika sehemu ya ‘status’.

    Huko akakutana na picha za msichana mrembo aliyekuwa na sura yenye furaha huku kukiwa na ujumbe uliosindikizia picha hiyo uliosema ‘Nalikumbuka tabasamu lako’. Hakuishia hapo, picha zikaanza kubadilika na baada ya picha tatu, akamuona msichana huyo huyo akiwa amelala kitandani huku akiwa na dripu kwa juu yake.

    Msichana huyo alikuwa Nandy. Alisikitisha pale alipokuwa, Amina mwenye hakuweza kuangalia kwa muda mrefu, akaitoa na kuangalia picha nyingine.

    Huko ndipo akapata jibu ya kila kitu kilichokuwa kikiendelea. Aliziona picha za Linda ambapo pia kulikuwa na ujumbe kuhusu msichana huyo, Dickson akimlalamikia kwa kulazimisha penzi na wakati hakuwa na mapenzi yake lakini mbaya zaidi, akaandika kwamba hakuogopa polisi hata kama alipanga kumfanyia jambo baya sana.

    Hapo, akahisi kitu, akagundua kabisa kwamba inawezekana jambo baya alilokuwa akilizungumzia Dickson lilikuwa ni lile alilokuwa amemfanyia ambalo kwa kifupi walipokuwa chumbani wakifanya mapenzi ilionekana kama msichana huyo alikuwa akibakwa.

    Moyo wa Amina ukamuuma kupita kawaida, hakuamini kama mipango ya msichana huyo ilikuwa hivyo. Hasira kali ikamkaba kooni, chuki ikajitokeza moyoni mwake dhidi ya Linda ambaye hakujua alikuwa mahali gani.

    Ilipofika majira ya saa 2:06 usiku simu yake ikaanza kuita na alipoichukua na kuangalia jina, mpigaji alikuwa Linda. Kwanza akakunja sura yake, hakumpenda kwa kuwa alimfanya kushiriki katika jambo ambalo hakufahamu ni kwa namna gani video zile zingekwenda kutumia. Akaamua kuipokea.

    “Nini?” aliuliza Amina mara baada ya kupokea simu.

    “Upo wapi?” lilikuwa swali kutoka kwa Linda.

    “Nyumbani!”

    “Nakwenda mahakamani kufungua kesi. Yule mshenzi amenibadilikia kwa sababu ya malaya wake,” alisema Linda huku sauti yake ikisikika kama mtu aliyekuwa na hasira mno.

    “Mshenzi gani?”

    “Dickson!”

    “Weee! Dickson mshenzi! Mshenzi gani anakuwa na sura nzuri kama ile?” aliuliza Amina, yaani muda huo hakutaka kusikia lolote lile baya kuhusu Dickson.

    Linda akaanza kumuhadithia kila kitu kilichokuwa kimetokea. Alionekana kukasirika mno na moyo wake ulidhamiria kufanya jambo moja tu, kumfunga Dickson hata kama alikuwa na mapenzi makubwa kiasi gani juu yake.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Japokuwa Amina alishirikiana naye lakini katika jambo hilo hakutaka kushirikiana naye tena, moyo wake ulibadilika na kuhisi kabisa kwamba alihitajika kumsaidia Dickson hata kama Linda angepata mahakamani na kumshtaki mwanaume huyo.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog