Search This Blog

Friday, July 15, 2022

NAMTAKA MPENZI WANGU ARUDI - 5

 







    Simulizi : Namtaka Mpenzi Wangu Arudi

    Sehemu Ya Tano (5)

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wazazi wa Dickson hawakuamini baada ya kuona kwamba mtu aliyefungua kesi ile mahakamani dhidi ya mtoto wao alikuwa msichana Linda. Walimfahamu msichana huyo, alikuwa mpenzi wa mtoto wao ambaye kila siku alionekana kuwa na shauku ya kuolewa na kijana wao.

    Hawakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea nyuma ya pazia. Walijaribu kumpigia simu kwa lengo la kuzungumza naye ili kama ikiwezekana basi afute kesi ile mahakamani lakini msichana huyo hakuwa akipokea.

    Hilo liliendelea kuwatia wasiwasi kwamba kijana wao alikuwa akienda kufungwa. Wao kama wazazi walikuwa wakifanya kazi kwa nafasi yao, walimtafuta sana msichana huyo kwenye simu na hata kwenda nyumbani kwao mara kwa mara lakini huko napo hawakubahatika kuonana naye.

    Kesi ile iliwatia tumbo joto, walikaa kama na mzee Gwamaka na kukubaliana kuwa hawakutakiwa kumwambia ukweli Nandy kwa kuwa angeumia sana hasa baada ya kuambiwa kwamba mpenzi wake alisimama mahakamani kwa kuwa alikuwa amebaka.

    Waliendelea kumfariji msichana huyo kitandani alipokuwa. Alikonda mno, alionekana kukosa tumaini, hakuwa na uhakika wa kupona na alijiona kabisa akiendelea kuteseka kitandani hapo kwa maisha yake yote duniani.

    Marafiki zake, washirika wengine walikuwa wakimtembelea pale kitandani alipokuwa, kila mtu aliyekuwa akimwangalia, alimuonea huruma, Nandy huyu hakuwa yule wa zamani, mrembo, mwenye sauti kali ya kumuimbia Mungu.

    Alibadilika, alifanana na mtu aliyekuwa akiumwa Ukimwi. Watu waliokuwa wakimuona walimfariji na kumwambia kwamba Mungu angemponya na kusimama tena kitu ambacho kwake kilionekana kuwa kigumu kufanyika kwa kuwa tu alilala kitandani kwa muda mrefu.

    “Unaamini kwamba Mungu ni mponyaji?” aliuliza mchungaji Tumaini huku akimwangalia nandy.

    “Ninaamini mchungaji!”

    “Kwa moyo wako mmoja?”

    “Nilifundishwa kumwamini Mungu tangu utotoni, katika maisha yangu yote ninamuamini Mungu kwamba ni mponyaji mchungaji,” alisema Nandy.

    “Basi atakwenda kukupona kitandani hapa!”

    “Naamini mtumishi wa Mungu!”

    Huo ulikuwa mwezi wa tatu tangu alale kitandani, moyo wake ulikata tamaa na wakati mwingine kuhisi kama Mungu alimuacha ateseke kitandani pale kwa kuwa alijiingiza kwenye maisha ya dhambi.

    Hakuacha kumlilia mpenzi wake, Dickson, alijua dhahiri kwamba kulikuwa na kitu kibaya kilichokuwa kikiendelea ambacho hakutakiwa kukijua.

    “Baba!” alimuita baba yake.

    “Naam binti yangu!”

    “Unaweza kunisaidia kitu kimoja?”

    “Kipi hicho?”

    “Unaweza kuniambia ukweli wako wote?”

    “Ndiyo binti yangu, siwezi kukudanganya!”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Dickson yupo wapi? Kwa nini yupo mahakamani? Ana kesi gani?” aliuliza Nandy huku akimwangalia baba yake, mzee Gwamaka.

    Hilo lilikuwa swali gumu kujibika, mzee huyo akanyamaza na kuangalia chini. Walikubaliana kwamba hawakutakiwa kumwambia Nandy ukweli juu ya kilichokuwa kikiendelea.

    Nandy hakunyamaza, alimwambia baba yake kwamba alihitaji kuujua ukweli kwani alichoka kusubiri na mbaya zaidi kila mtu aliyekuwa akimuuliza hakuonekana kuwa tayari kumjibu.

    “Amefungwa?” aliuliza Nandy.

    “Hapana!”

    “Sasa yupo wapi? Au ameniacha tena ili nife?” aliuliza.

    “Hapana binti yangu! Dickson hawezi kukuacha!”

    “Sasa yupo wapi?”

    “Atakuja!”

    “Najua! Yupo wapi kwa sasa?” aliendelea kuuliza.

    Maswali hayo aliyokuwa akiyauliza yakaanza kumliza kitandani pale. Alihisi kitu chenye ncha kali kikiuchoma moyo wake. Alimkumbuka Dickson, kwake, mwanaume huyo alikuwa kila kitu.

    Hakuambiwa kitu chochote kile, maumivu yale yaliyokuwa moyoni mwake yaliendelea kubaki vilevile. Dickson aliyekuwa akimuendesha kwenye kiti chake, hakuwepo tena, kazi hiyo alikuwa akiifanya baba yake

    Siku zikakatika mpaka kufikia siku ya kesi hiyo kusikilizwa mahakamani kwa upande wa shahidi. Wazazi wa Dickson walikwenda mahakamani kama kawaida.

    Walipoingia katika viunga vya mahakama, macho yao yalitua kwa Linda ambaye naye alifika kwa ajili ya kusikiliza kilichokuwa kikiendelea.

    Alikuwa na Amina, muda mwingi alimkumbusha kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wake endapo tu asingezungumza kile walichokuwa wamekubaliana na mbaya zaidi Kudra na mwenzake walikuwa mahakamani hapo ili kama angekwenda kupingana nao, basi wangeondoka naye na kwenda kumuua.

    Siku hizo Linda alionekana kuwa tofauti, hakuwa kama yule msichana ambaye walikuwa wakimfahamu kutokana na upole wake, katika siku hizo alibadilika na kuwa mtu mwingine kabisa.

    Muda mwingi alionekana kuwa na hasira na alidhamiria kumfunga Dickson gerezani kwa sababu tu alikataa kukubaliana naye kuoana na wakati alikuwa akimpenda kwa moyo wa dhati.

    Baada ya dakika kadhaa basi kubwa kutoka magereza likafika mahali hapo na moja kwa moja watuhumiwa ambao siku hiyo walikuwa wakisomewa kesi zao kuanza kuteremka, na miongoni mwa watuhumiwa hao alikuwemo Dickson.

    Alionekana kuwa mnyonge, mikononi alikuwa na pingu, alipoteremshwa, macho yake yakaanza kuangalia huku na kule, kwa mbali aliwaona wazazi wake, alitamani kuwafuata na kuwauliza kuhusu hali aliyokuwa akiendelea nayo mpenzi wake.

    Alimkumbuka Nandy, kwake, kila siku msichana huyo alikuwa akizunguka kichwani mwake, alihitaji sana kumuona na kumjulia hali kwani aliamini kwamba kusingekuwa na mtu ambaye angemjali kama alivyokuwa akimjali kabla ya kukamatwa.

    Baada ya kuingizwa mahakamani, haraka sana kesi zikaanza kusikilizwa na kesi ya kwanza kabisa ilikuwa yake kwa kuwa kilichokuwa kikihitajika ni ushahidi tu.

    Baada ya jaji kuingia, akaanza kuisoma kesi hiyo tangu ilipoanzia na mpaka ilipofikia na kitu pekee kilichokuwa kikisubiriwa kwa hamu ni ushahidi juu ya ile video iliyokuwa ikionekana, na mtu pekee ambaye alitakiwa kutoa ushahidi ni yule msichana aliyekuwa akionekana kwenye video ile, Amina.

    Jaji akapewa taarifa kwamba msichana huyo alikuwemo mahakamani na hivyo alitakiwa kwenda kizimbani na kusema ukweli juu ya kile kilichokuwa kimetokea.

    Hilo halikuwa tatizo, kwa unyonge, Amina akainuka na kuanza kuelekea katika kizimba kile huku akichechemea hali iliyomfanya kila mmoja kujua kwamba alikuwa na maumivu katika miguu yake.

    Alipofika, akasimama na kujitambulisha, akajiapiza huku akinyanyua mkono wake wa kulia huku katika mkono wake wa kushoto akiwa ameshika Kitabu Kitakatifu cha Kuran.

    “Na Allah anisaidie,” alisema baada ya kumaliza kujiapiza.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mahakama ilitakiwa kuzungumza kila kitu kilichotokea siku hiyo mpaka kubakwa na mtuhumiwa. Kabla ya kuanza kusimulia, Amina akayapeleka macho yake na kumwangalia Dickson.

    Aliumia mno, mwanaume huyo alikuwa amepungua kupita kawaida, kwa kusoteshwa rumande amefanyiwa kisa tu kumuacha mwanamke ambaye aliamini hakuwa wa ndoto yake

    Amina hakutaka kumuona Dickson akifungwa gerezani kwa kosa ambalo hakulifanya, japokuwa aliambiwa kwamba angeweza kuuawa lakini alikuwa radhi lakini si kuona mwanaume huyo akichukuliwa na kwenda kufungwa.

    Alichokifanya ni kuanza kusimulia kila kitu kilichotokea, jinsi alivyokwenda hotelini kuonana na Dickson kisha kukubaliana kwenda chumbani na kuanza kufanya mapenzi.

    Watu wote mahakamani walikuwa kimya, walimsikiliza msichana huyo alivyokuwa akisimulia huku akilia kwani hakupenda kabisa kumuona Dickson akifungwa, kama Kudra na mwenzake walitaka kumuua alikuwa tayari kufa.

    “Hakunibaka! Nilifanya naye mapenzi kwa hiyari yangu. Niliambiwa nijifanye kama nakataa, kwa mara ya kwanza sikujua maana ya mtu aliyenituma lakini baadaye nikagundua kwamba aliniambia nifanye vile kwa kuwa ilitakiwa nionekana kwamba nabakwa,” alisema Amina, kila mmoja alikuwa kimya, akaendelea:

    “Baadaye ndiyo nikaambiwa jinsi hali ilivyokuwa, nilishangaa, nilimwambia mtu huyo kwamba sikuwa tayari kwa kuwa nilikuwa nampenda Dickson lakini akanilazimisha sana, akahisi kwamba nisingezungumza kile alichotaka nizungumze hivyo akatuma watu waniteke na kunitesa, nikaunguzwa na kisu cha moto,” alisema Amina, hiyo haikutosha, akaanza kuonyesha majeraha yake mapajani. Wanawake waliokuwa humo wakaanza kutokwa na machozi, kwa jinsi Amina alivyokuwa amejeruhiwa kulimuumiza kila mtu.

    “Nilionywa kwamba kama nisingesema kwamba nimebakwa basi ningeuawa! Hakimu, watu hao wapo hapa, ninatoa ushahidi na wanasikia na ninategemea baada ya hapa wanakwenda kuniua kama walivyoniahidi,” alisema Amina, watu wote humo ndani kuanza kuangalia.

    “Unaweza kuwaonyesha watu wenyewe?” aliuliza jaji.

    “Ndiyo!” alisema Amina na kuwanyooshea vidole Amina na vijana wake wawili, polisi wakawasogelea watu hao, akaendelea:

    “Kiukweli sikubakwa, sikubakwa kabisa. Kama ningekuwa nimedhalilishwa kingono namna hiyo, ningekuwa muwazi, ila sikubakwa bali nilitumika kwa manufaa ya msichana huyo aliyetaka kuona yeye akiolewa na Dickson,” alisema Amina na kunyamaza.

    Ndani ni kama kulikuwa na msiba, watu walishindwa kuvumilia, walikuwa wakimwangalia Amina, hawakuamini kuona msichana huyo akiwa amepitia mateso makubwa kiasi hicho.

    Jaji mwenyewe kule alipokaa alishindwa kuvumilia, machozi yakaanza kujaa machoni mwake na kuanza kutiririka mashavuni kwani kile alichokisikia kilimuumiza mno.

    Hakutaka kuchelewa, akamuita polisi mmoja ambapo akaambiwa kwamba ilikuwa ni lazima kwa watu hao watatu kukamatwa kwa makosa waliyokuwa wameyafanya, yaani yule shahidi aliyekuwa ameletwa mahali pale, alitoa ushahidi wake lakini wa kuwaingiza watu hao matatizoni.

    Alipomaliza, kesi ikaendelea kwa jaji kuanza kuipitia tangu mwanzo ilipoanza mpaka hapo ilipoishia na kilichokuwa kimebaki kilikuwa kimoja tu, kutolewa hukumu ya kesi hiyo.

    “Kama tulivyomsikia shahidi ambaye alikuwa na nguvu kwenye hitimisho ya kesi hii, hakubakwa, na sasa sioni ni kwa namna gani naweza kuendelea na hii kesi. Kwa mamlaka ya mahakama, ninamuachia huru ndugu Dickson kwa kuwa mahakama haikumkuta na hatia yoyote ile,” alisema hakimu na kuifunga kesi hiyo.

    Dickson kule alipokaa, hakuamini alichokisikia, kwake ilionekana kuwa kama ndoto. Akasimama na kuwafuata wazazi wake, alipowafikia, akawakumbatia na neno la kwanza kabisa kuzungumza nao ni kutaka kujua hali aliyokuwanayo mpenzi wake.

    “Nandy! Mama! Nandy anaendeleaje?” aliuliza Dickson huku macho yake yakiwa mekundu mno kutokana na kulia sana.

    “Anaendelea vizuri!”

    “Ninahitaji kumuona!” alisema.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alipomaliza, akamsogelea Amina na kumkumbatia. Alimshukuru kwa kila kitu, hakuamini kama angeweza kumtetea kwa kile kilichokuwa kimetokea, alipomaliza, watu wakatoka nje na hivyo mahakama kujiandaa na kesi nyingine.

    Linda alipokaa, aliuinamisha uso wake kwa aibu, hakuamini kilichokuwa kimetokea, kwake, kilionekana kuwa kama ndoto, alitamani kubadilisha kila kitu na kumrudisha Dickson kizimbani na kumuhukumu kifungo cha miaka thelathini yeye mwenyewe.

    Kwa aibu, akasimama na kuanza kutoka nje. Alipofika katika uwanja wa mahakama, polisi wakamfuata na kumkamata, hakuwa yeye tu bali hata vijana wake nao wakakamatwa na kurudishwa mahakamani, jaji yuleyule akaanza kuwasomea mashtaka kwa kile kilichokuwa kimetokea.

    Dickson hakutaka kubaki mahali hapo, kulikuwa na kitu kimoja tu alichohitaji kukifahamu muda huo nacho kilikuwa ni afya ya mpenzi wake ambaye alimuacha kitandani kwa muda wa wiki kadhaa.

    Akawachukua wazazi wake, wakapanda ndani ya gari na kuanza kuelekea nyumbani. Njiani walikuwa wakizungumza naye mambo mengi lakini mawazo yake yalikuwa kwa Nandy tu, alihitaji kumuona msichana huyo, kwake, hakukuwa na kitu chochote kile kilichokuwa na thamani zaidi ya huyo Nandy.

    Walipofika, wakateremka, wakakuta geti likiwa wazi, walishangaa, wakaingia ndani, hakukuwa na mtu, mbaya zaidi hata mlinzi hakuwa mahali hapo.

    Dickson akaufungua mlango na kuingia ndani, moja kwa moja akaelekea katika chumba alichokuwemo Nandy, hakuwemo humo, kitanda kilikuwa kitupu.

    “Nandy! Nandy amekufa,” alisema huku akilishika shuka la kile kitanda alichokuwa amelalia Nandy.

    Alichokifanya ni kuanza kuita, akaita na kuita, alichanganyikiwa, si yeye tu bali hata wazazi wake nao walichanganyikiwa. Walipotoka nje, wakakutana na mlinzi ambaye alikuwa amerudi nyumbani hapo huku akiwa anahema kwa nguvu kama mtu aliyetoka kukimbia mbio ndefu.

    “Cosmas...kuna nini? Nandy yupo wapi?” aliuliza Dickson, tayari moyo wake ulikuwa na hofu kupita kawaida.

    “Nandy? Nandy?” aliuliza mlinzi, kila alipotaka kuzungumza, mdomo ulikuwa mzito kufunguka.



    Nandy hakuwa na furaha hata kidogo, bado kichwa chake kilikuwa kikimfikiria mpenzi wake, Dickson ambaye muda huo hakuwa akijua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea.

    Alitulia kwenye kitanda kile, alikuwa mtu wa kulala tu, hakuweza kuusogeza mwili wake kivyovyote vile, kama alivyokuwa kipindi cha nyuma ndivyo alivyokuwa mpaka kipindi hicho.

    Baba yake ndiye aliyekuwa na majukumu ya kila kitu, ndiye aliyekuwa akimtoa kitandani hapo na kumgeuza, ndiye aliyekuwa akimlisha na kumfanyia mambo mengine.

    Dickson, mwanaume wake wa dhati hakuwepo nyumbani na kitu pekee alichokuwa akikihitaji kipindi hicho ni kumuona tena mbele ya macho yake.

    Baada ya kukaa kwa siku kadhaa, pale kitandani akaanza kujisikia vibaya, siku hiyo hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea, kwa mara ya kwanza maumivu makali yakawa yanaupata mgongo wake.

    Akaanza kupiga kelele za kuhitaji msaada, alikuwa akiumia kupita kawaida na pale kitandani mwili ukawa kama unapanda na kushuka.

    Sauti yake ilisikika na mlinzi aliyekuwa getini, haraka sana akaelekea chumbani, hali aliyoikuta ilimuogopesha, kwa jinsi msichana huyo alivyokuwa kitandani pale ilionyesha kwamba alikuwa katika siku yake ya mwisho kuvuta pumzi ya dunia hii.

    Mlinzi hakujua afanye nini kumsaidia zaidi ya kumpigia simu mzee Gwamaka ambaye akafika mahali hapo haraka sana.

    “Vipi?” aliuliza mzee huyo, bado Nandy alikuwa kwenye hali ileile.

    “Sijui nini kimetokea! Nimemkuta akiwa hivi, Mungu wangu! Anakufa?” aliuliza mlinzi huyo huku akitetemeka.

    Nandy akaanza kutapika, mwisho kabisa mapovu yakaanza kumtoka. Alitisha kitandani pale na muda wowote ule alionekana kukata roho.

    Mzee Gwamaka huku akiwa amechanganyikiwa akamnyanyua, akamtoa nje, mlinzi akaita Bajaj, ilipokuja, wakamuingiza ndani na kuanza kuondoka naye kuelekea hospitali.

    Walipofika, machela ikaletwa, akapokelewa na kisha kuanza kusukumwa kuelekea ndani. Huko, akalazwa na kuanza kupewa huduma ya kwanza kabla ya matibabu kamili kuanza.

    Mzee gwamaka na mlinzi walikuwa nje kwenye benchi, kila mmoja alionekana kuwa na hofu na kuhisi kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wa Nandy kuendelea kuishi.

    Pale walipokuwa, mzee Gwamaka aliikutanisha mikono yake na kuanza kumuomba Mungu, hakutaka kushuhudia mtoto wake akifa kitandani, alimuomba Mungu kwamba amponye kwa kuwa asingekuwa na mtu yeyote katika maisha yake.

    “Mungu! Naomba usimchukue Nandy, nitabaki na nani mimi ukimchukua? Ni kweli anateseka, lakini naomba usimchukue, ninampenda sana binti yangu,” alisali mzee Gwamaka huku akiangalia juu.

    Machozi ya uchungu yakaanza kumtoka kiasi kwamba hata mlinzi alimuonea huruma kwa kile kilichokuwa kikiendelea.

    Wakati wakiendelea kuwa mahali hapo, mlinzi akakumbuka kwamba hakuwa amelifunga geti kwa ufunguo hicyo alitakiwa kurudi nyumbani na kulifunga. Akamuaga mzee Gwamaka na kurudi nyumbani huku akikimbia.

    Huko ndipo alipokutana na Dickson pamoja na wazazi wake, alishangaa, hakuamini kama mwanaume huyo angetoka huko alipokuwa, alipoulizwa mahali alipokuwa Nandy, kwanza akatulia.

    “Niambie! Nandy amekufa? Mbona hujibu, niambie Cosmas,” alisema Dickson huku akianza kutokwa na machozi.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Akawaambia kilichotokea, Dickson aliposikia, hakutaka kubaki mahali hapo tena, akatoka na kuanza kukimbia kuelekea hospitalini ambapo hakukuwa mbali kutoka mahali hapo.

    Njiani, kichwa chake kilikuwa kikimfikiria msichana huyo tu, alikuwa tayari kupoteza kitu chochote katika maisha yake lakini si kumpoteza Nandy ambaye alikuwa mtu muhimu kupita kawaida.

    Alimpoteza kwa mara ya kwanza, kilichotaka kutokea kilikuwa ni kumpoteza kwa mara ya pili tena milele kitu ambacho Dickson hakutaka kukubaliana nacho hata kidogo.

    Hakuchukua dakika nyingi akafika katika hospitali hiyo, watu walikuwa wakimshangaa, alikuwa akitoka jasho huku akihema kama mbwa aliyekimbia mbio ndefu, akamkuta mzee Gwamaka akiwa amejiinamia kwenye benchi.

    “Baba! Baba...niambie nini kinaendelea!” alisema Dickson huku akiwa amemsogelea mzee huyo ambapo baada ya kunyanyua uso, akashangaa kumuona Dickson.

    “Dickson!”

    “Baba! Niambie nini kinaendelea! Nandy anaendeleaje?” aliuliza.

    “Ndiyo namsubiri daktari!”

    Dickson akatulia kwenye benchi, akaungana na mzee huyo kwenye dimbwi la mawazo, walikaa hapo kwa dakika kama arobaini ndipo mlango ukafunguliwa na daktari mmoja kutoka ambapo akawaambia awafuate ofisini kwake.

    “Ila anaendeleaje?” aliuliza Dickson aliyekuwa na presha ya kutaka kufahamu kilichokuwa kikiendelea.

    “Twendeni ofisini kwanza!”

    “Amekufa?”

    “Mtayajua huko!”

    Dickson ndiye aliyekuwa na presha kubwa ya kutaka kufahamu kilichokuwa kikiendelea kwa mpenzi wake, baada ya mwendo mdogo, wakafika katika ofisi hiyo na kukaa katika viti.

    “Huyu binti yako amepooza, si ndiyo?” alianza kwa kuuliza daktari.

    “Ndiyo!”

    “Ooh! Pole sana. Tumemchunguza kwa makini na kugundua kwamba ana tatizo liitwalo Sciatica,” alisema daktari.

    “Ndiyo nini hilo?”

    “Hili ni tatizo linalotokea kwenye uti wa mgongo wakati pingili za uti zimekuwa zimefinywa kwa kipindi kirefu. Hapo kuna sehemu kwenye uti wa mgongo inaitwa Lumbar stenosis ambayo hiyo huchukua mawasiliano kutoka sehemu moja ya uti wa mgongo na kupeleka sehemu nyingine,” alisema daktari.

    “Dokta! Hayo majina unatuchanganya, hebu tuambie moja kwa moja, nini kinaendelea,” alisema Dickson.

    “Ni kwamba mgonjwa wenu amepata tatizo la kwenye pingili, hii imesababishwa na kulala kwa kipindi kirefu, anatakiwa wakati mwingine ageuzwe na hata kukalishwa,” alisema.

    “Lakini tunafanya hivyo!” alisema mzee Gwamaka.

    “Basi mnafanya kidogo sana. Kwa siku, muacheni akae kitako hata kwa saa nne, si saa nyingi awe amelala tu,” alisema.

    “Lakini atapona?”

    “Uti wa mgongo au hili tatizo aliloletewa hapa?”

    “Tatizo hili!”

    “Hili linapona! Hakuna tatizo!”

    “Na uti wa mgongo kwa ujumla?”

    “Bado kwa kweli! Nimeangalia pingili zake, aisee inaweza kuchukua miaka na miaka,” alisema daktari huyo bila kuwaficha chochote kile.

    Daktari aliwaambia mambo mengi kuhusu ugonjwa wa Nandy lakini mwisho wa siku akawaeleza ukweli kwamba msichana huyo asingeweza kupona tena.

    Hilo liliwauma lakini hawakuwa na la kufanya. Baada ya saa moja, daktari akawachukua na kuwapeleka katika chumba alicholazwa Nandy. Walipoingia na Nandy kuwaona, uso wake ukajawa na tabasamu pana, hakuamini kama kweli mpenzi wake angekuwa uraiani kama alivyomuona.

    Dickson akatembea haraka kumfuata Nandy pale kitandani, alipomfikia, akamuinamia na kumbusu shavuni huku kila mmoja akionekana kuwa na furaha.

    Siku hiyo alilala hospitalini hapo, usiku walikuwa wakiongea mambo mengi, walifurahishana huku Dickson akimwambia Nandy kwamba kuna siku angeweza kusimama tena na kukimbia kama zamani.

    “Hivi ulikwishawahi kusoma stori ya Musa?” aliuliza Dickson.

    “Nimesoma sana mpaka mapigo saba ambayo Mungu aliipiga Misri,” alijibu Nandy.

    “Na ulisoma jinsi Waisrael walivyofika katika bahari ile Nyekundu?” aliuliza.

    “Ndiyo!”

    “Kuna muujiza gani Mungu aliufanya kupitia Musa?”

    “Aliigawa bahari na Waisrael wakavuka katikati. Unamaanisha nini?”

    “Ninamaanisha kwamba Mungu wetu tunayemuabudu ni mkuu, Mungu wetu ni Muweza, hakuna mtu au roho yoyote ile ambayo itashindana na Mungu aliye hai. Unaposikia Mungu, jua unamzungumzia Mungu mwenye miujiza, Mungu asiyeshindwa, asiyesinzia wala kulala, Mungu ambaye anaweza kuifinyanga dunia na kuitupilia mbali ndani ya sekunde moja tu,” alisema Dickson.

    “Kweli kabisa.”

    “Kama Mungu amefanya hayo yote, yeye ni nani mpaka ashindwe kuunganisha uti wako wa mgongo?” aliuliza Dickson.

    “Hashindwi! Na hatowahi kushindwa!”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nandy! Unachotakiwa ni kufanya kitu kimoja tu, unatakiwa kuamini, Mungu huwa hashindwi, kuna watu wanaponywa Ukimwi, kuna watu wanafufuliwa, kuna watu wanaponywa magonjwa hatari kama kansa, huyo ndiye Mungu ambaye ninakwambia usiku wa leo kwamba hashindwi na hajawahi kushindwa, yeye anajua mfumo mzima wa mwili wako, damu inatoka wapi, inakwenda wapi na anajua vitu kwenye mwili wako ambavyo hata madaktari hawavijui, hebu jaribu kufikiria ni Mungu wa aina gani huyo,” alisema Dickson huku machozi yakimlenga, alipokuwa akizungumzia matendo makuu ya Mungu, alihisi nafsi yake ikielekea katika sehemu nyingine kabisa, sehemu yenye raha, amani, sehemu yenye tumaini, hali ambayo hakuwahi kukutana nayo katika maisha yake.

    “Amen! Mungu ataniponya.”

    “Mungu hajawahi kushindwa. Kuna siku Nandy utasimama kwa miguu yako na kumwambia kila mtu kwamba Mungu hajawahi kushindwa!” alisema.

    “Amen!”

    “Mungu hajawahi kushindwa!”

    “Amen!”

    “Mungu hajawahi kushindwa!”

    “Amen”

    “Utasimama kwa miguu yako na kuiambia dunia kwamba MUNGU HAJAWAHI KUSHINDWA.”

    “Amen!” alisema Nandy kwa sauti juu iliyokuwa na imani kubwa katika maisha yake kwamba Mungu huyo aliyeigawanya bahari Nyekundu, hakuwahi kushindwa.

    “Kuna siku utasimama!”

    “Naamini! Kuna siku nitasimama tena, nitamuimbia Mungu na kucheza mbele yake! Ninaamini hilo,” alisema Nandy kwa ushujaa mkubwa.





    Moyo wa Dickson haukuacha kuuma, alimwambia Nandy kuhusu kumuamini Mungu kwa kila kilichokuwa kikiendelea kwamba kuna siku angepona kabisa na kutembea kama ilivyokuwa zamani.

    Msichana huyo akaamini, hakuona kama Mungu angeweza kushindwa kitu chochote kile, katika maisha yake, hakukuwa na mtu au kitu alichokiamini zaidi ya Mungu.

    Pale kitandani walipomaliza kuzungumza maneno kuhusu nguvu za Mungu, wakashikana mikono na kuanza kusali huku wakimpa shukrani Mungu kwa kile ambacho waliamini kuwa angekwenda kukifanya baada ya siku chache.

    “Mungu! Tunakushukuru kwa kila kitu tulichokuwanacho, tunashukuru kwa haya maisha, tunashukuru kwa baraka hizi, tunashukuru kwa zile baraka ambazo bado hazijafika mikononi mwetu, tunashukuru kwa kila kitu, pia tunashukuru kwa uponyaji unaokwenda kumpa Nandy katika siku chache zijazo,” alisali Dickson huku akiwa ameshikana mkono na msichana huyo.

    Maisha yaliendelea kama kawaida, kila siku Dickson alikuwa ndani ya chumba hicho, yeye ndiye aliyekuwa na kazi ya kumuogesha, kumbadilisha nguo, kumtembeza huku na kule kwenye kibaskeli chake na kumfanyia kila kitu ambacho alitakiwa kufanyiwa.

    Kila ilipofika siku ya Jumapili, Dickson ndiye aliyekuwa akimwandaa msichana huyo na kuelekea kanisani. Huko, huku akiwa kitandani bado Nandy aliendelea kumuimbia Mungu.

    Kila mtu aliyekuwa akimwangalia, alimshangaa, alibadilika, alikonda kupita kawaida, katika maisha yake, kitu ambacho alikuwa akikitegemea ni kwamba siku moja angepona na kutembea kama zamani.

    Watu walimuombea, walimuomba Mungu kufanya uponyaji katika kitanda kile lakini bado Nandy aliendelea kuwa katika hali ileile.

    Baada ya miezi minne mingine, mchungaji kutoka nchini Marekani, Richard Turnbull akafika nchini Tanzania na kuandaa mkutano mkubwa wa Injili.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hiyo ikaonekana kuwa nafasi nyingine ya Mungu kufanya miujiza kwani miongoni mwa wachungaji waliokuwa na nguvu kutoka kwa Mungu alikuwa mchungaji huyo.

    Kila alipokuwa akiandaa mikutano, wagonjwa waliponywa, viwete walitembea, viziwi walisikia na miujiza mingine mingi.

    Dickson akamchukua Nandy na kuanza kushiriki naye katika mkutano huo huku akiwa kwenye kiti chake. Wakati wagonjwa walipotwa na kuombewa, naye Nandy akataka kwenda kuombewa, lakini kitu cha ajabu ambacho kilimshtua ni kwamba Dickson hakutaka kumpeleka.

    “Nipeleke nikaombewe,” alisema Nandy huku akimwangalia Dickson.

    “Hapana! Moyo wangu unakuwa mzito!”

    “Kwa nini? Ninataka kupona, Dickson, naomba unipeleke nikaombewe,” alisema Nandy huku akimwangalia Dickson, kwake, hiyo ndiyo ilikuwa nafasi yake ya kipekee ya kupokea uponyaji.

    Bado Dickson alikuwa akikataa, Nandy alilia lakini hakutaka kulazimisha, hakutaka kumkasirisha Dickson, mpaka mkutano unaisha siku hiyo na kurudi nyumbani, Nandy hakuonekana kuwa kwenye hali ya kawaida.

    Hiyo ilikuwa siku ya kwanza, siku ya pili ya mkutano ikaingia, hali ilikuwa vilevile, siku ya tatu na mpaka mkutano unaisha katika siku ya saba bado Dickson hakutaka kumpeleka Nandy kwenda kuombewa zaidi ya kukaa na kusikiliza Neno la Mungu.

    Wakarudi nyumbani, Dickson alijua kwamba Nandy alikuwa amekasirika, alijua kwamba aliumia ila kitu alichokifanya ni kumchukua na kumpeleka nje, akaanza kumuendesha katika kibaskeli chake mpaka ufukweni ambapo hakukuwa mbali na walipokuwa wakiishi.

    “Nandy! Kuna kitu ninataka kuzungumza nawe,” alisema Dickson huku akimwangalia Nandy.

    “Kitu gani?”

    “Niliisikia sauti ikiniambia moyoni mwangu kwamba sikutakiwa kukupeleka pale mbele katika mkutano na kuombewa. Nina uhakika ilikuwa ni sauti ya Mungu, ilisikika kwa upole mno moyoni mwangu tofauti na sauti nyingine, ila ilikuwa na nguvu ya ajabu,” alisema Dickson huku akimwangalia Nandy.

    “Ilisemaje?”

    “Iliniambia mengi, cha msingi kabisa ni kwamba Mungu anataka kupandikiza nguvu ya imani mioyoni mwetu. Kwa jinsi tulivyomuomba, tunatakiwa kumwamini kwamba atatenda muujiza, si mpaka mchungaji wa kimataifa amtumie kufanya miujiza, hata sisi pia tunaweza kufanya miujiza,” alisema Dickson huku uso wake ukiwa kwenye tabasamu pana.

    “Nina imani, kuna siku atafanya muujiza,” alisema Nandy.

    “Ila kuna kingine!”

    “Kipi?”

    “Nandy! Wewe ni msichana wa kipekee, katika maisha yangu nimefikiria jambo moja muhimu, ninahitaji unipe nafasi moja tu,” alisema Dickson.

    “Ipi?”

    “Ya kuwa mume wako!”

    “Unataka kunioa?”

    “Ndiyo!”

    “Mimi?”

    “Nandy! Kwani wewe una nini?”

    “Mimi ni mgonjwa, siwezi kufanya lolote lile!”

    “Umesahau nilichokwambia kuhusu imani?”

    “Nakumbuka!”

    “Basi kumbuka kwamba wewe si mgonjwa tena, kuna siku utainuka na kuishangaza dunia,” alisema Dickson huku akimwangalia mpenzi wake huyo.

    Kwa furaha Dickson akamkumbatia Nandy na kurudi nyumbani huku wakizungumza mambo mengi yaliyokuwa yakiendelea katika maisha yao.

    Dickson hakutaka kubaki na jambo hilo moyoni mwake, alichokifanya ni kuwaambia wazazi wake kwamba alidhamiria kumwambia kuhusu mpenzi wake huy.

    Wazazi wake waliposikia, hawakuamini lakini kwa yote hawakumzuia kijana wao kumuoa Nandy kwa kuwa kila walipokuwa wakimwangalia, alionekana kuwa na mapenzi ya dhati kwa mpenzi wake huyo.

    Hakuishia kuwaambia wazazi wake tu bali alimwambia mpaka mzee Gwamaka kile kilichokuwa kikiendelea. Mzee huyo hakuamini, kwake ilionekana kama ndoto kwani pamoja na Dickson kumpenda mno binti yake bado hakutakiwa kumuoa kwa kuwa alikuwa kwenye hali ile.

    Akamwambia kijana huyo ukweli kuhusu binti yake, hilo halikuwa tatizo kwa Dickson, hata kama mpenzi wake alikuwa kwenye hali hiyo, alikuwa radhi kumuoa lakini si kuona akiondoka tena mikononi mwao.

    “Nitamuoa, hata kama hatorudi katika hali yake maisha yote bado nitahitaji kumuoa,” alisema Dickson huku akimwangalia mzee Gwamaka.

    Huo ulikuwa uamuzi wake, hakutaka mtu yeyote amuingilie, alichokifanya ni kumwambia mchungaji, naye alishangazwa lakini hakuwa na jinsi.

    Akatangaza kanisani, na baada ya miezi miwili, watu hao wakaoana huku Nandy akiwepo kwenye kiti, akavarishwa pete na hatimaye kuwa mume na mke.

    Moyo wa Dickson ukaridhika, kwake hakuangalia afya, kwake hakuangalia watoto, kitu ambacho alikiangalia kwake ni upendo wa dhati kwa msichana huyo.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kila alipokuwa akimwangalia, hakuacha kumwambia kwamba alikuwa akimpenda kupita kawaida. Baada ya shere ya harusi kumalizika, wakaondoka na kuelekea Zanzibar kwa ajili ya kula fungate.

    Ndoa aliyofunga na Nandy ikawa gumzo Tanzania nzima, hakukuwa na mtu aliyeamini kama kweli mwanaume huyo aliyekuwa na sura nzuri aliamua kufunga ndoa na msichana aliyekuwa kitandani huku akiwa amepooza.

    Wanaume wengi wakatakiwa kujifunza, kwenye mapenzi, hukutakiwa kuangalia afya, kwenye mapenzi hukutakiwa kuangala watoto, kila kitu kilipangwa na Mungu kwani kulikuwa na watu wengi waliokuwa na afya, watoto lakini bado mioyo yao iliumizwa kila siku, bado macho yao yalitoa machozi na kutiririka mashavuni mwao kila siku.

    “Jamani huyu kaka ana moyo wa chuma,” alisema msichana mmoja huku akiwaonyeshea gazeti wenzake.

    “Mmh! Amemuoa mwanamke amepooza?”

    “Ndiyo! Yaani hatofanya naye mapenzi, hatomzalia, lakini kidume kimeoa hivyohivyo,” alisema msichana huyo.

    “Mmh!”

    “Yaani nyie acheni. Ila mkaka yupo bomba, handsome la maana, huyu ukimpata hata kazini huendi, kumwangalia tu chumbani inatosha kujisikia umelipwa mshahara,” alisema msichana huyo.

    “Hahaha!” wote wakabaki wakicheka.

    ***

    Kesi ilikuwa ngumu kwa Linda, mahakamani pale kesi ile iliendelea kila ilipokuwa wiki na hatimaye yeye na wenzake wakakutwa na kesi ya kujibu na hivyo hukumu ilipotoka, wakafungwa gerezani miaka sita kwa kosa la kutaka kuua kwa kukusudia.

    Hiyo ilimuuma mno Linda, hakuamini kama msichana mrembo kama yeye, mwenye elimu yake, kutoka katika familia ya kitajiri alikuwa akienda gerezani.

    Hilo lilimuuma kupita kawaida, aliondolewa mahakamani huku akilia, wazazi wake ambao walikuwa wakifuatilia kesi hiyo tangu mwanzo mpaka ilipomalizika, hawakuamini kama mahakama ingetoa hukumu hiyo ambayo kwao ilionekana kuwa kubwa kupita kawaida.

    Linda akaanza maisha ya gerezani, alikosa penzi, akakosa kila kitu kizuri na mwisho wa siku kujikuta akiwa gerezani.

    Moyo wake ulichoma mno na baada ya miezi kadhaa akiwa huko, akapata nafasi ya kusoma gazeti na kuiona habari iliyokuwa imetawala katika magazeti mengi kwamba mwanaume mwenye sura nzuri, mtoto wa kitajiri aliamua kumuoa mwanamke aliyekuwa kitandani amepooza.

    Moyo wake uliumia. Kilichomuumiza si Dickson kumuoa Nandy bali kilichomuumiza ni kuona msichana Nandy akiwa kitandani kwa ujinga aliokuwa ameufanya.

    Akajikuta akisikia hukumu nzito moyoni mwake, hakutaka kuona akiendelea kuumia kiasi kile bali alichokifanya ni kuchukua karatasi na kutaka kuwaandikia barua wawili hao, alihitaji kukiri kusababisha maisha ya msichana huyo kuwa kitandani lakini pia alihitaji kuwaomba msamaha kwa kila kitu kilichotokea. Baada ya dakika kadhaa, akapata kalamu na karatasi na kuanza kuandika barua hiyo kwenda kwa watu hao.



    Dickson na Nandy walikuwa wakirudi jijini Dar es Salaam wakitoka katika Visiwa vya Zanzibar ambapo walikwenda kwa ajili ya fungate yao.

    Mioyoni walikuwa na furaha tele kwani baada ya kupitia vikwazo mbalimbali hatimaye wawili hao walikuwa wameoana na kuwa pamoja.

    Ndani ya boti kila mtu alikuwa akiwaangalia, hawakuamini kama watu hao ndiyo walikuwa wameoana huku mwanaume waliyekuwa wakimwangalia, aliyekuwa na sura nzuri ndiye aliyeamua kumuoa mpenzi wake huyo huku akiwa amepooza.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Walionekana kuwa na furaha kupita kawaida, mule ndani walikuwa wakizungumza mambo mengi na watu wengine, hawakusita kuwaambia kuhusu muujiza wa Mungu ambao angeufanya baadaye katika mwili wa Nandy.

    Kila mtu aliiona imani yao, hawakutaka kuwa na hofu na kitu chochote kile kwani kwa kila kilichokuwa kikiendelea waliamini kwamba ulikuwa ni mtihani tu ambao mwisho wa siku kulikuwa na matokeo yake.

    Walipofika Dar es Salaam, wakapokelewa na ndugu, jamaa na marafiki na kuelekea nyumbani. Maisha kama wanandoa yakaanza, kila siku Dickson alikuwa akienda kazini alipokuwa akisimamia biashara nyingi za baba yake na kurudi jioni.

    Mapenzi yalikuwa motomoto, kila alipokuwa akirudi nyumbani alikuwa na zawadi kwa ajili ya mke wake huyo ambaye mpaka katika kipindi hicho hakukuwa na maendeleo yoyote mwilini mwake zaidi ya kuwa vilevile kama alivyokuwa kipindi cha nyuma.

    Baada ya kukaa kwa siku kadhaa ndipo Dickson akapigiwa simu kutoka katika Kituo Kikuu cha Polisi na kuambiwa kwamba kulikuwa na mzigo wake kutoka gerezani.

    Hakujua ulikuwa ni mzigo wa nini, hakujua alipelekewa na mtu gani. Muda huo aliopigiwa simu alikuwa akirudi nyumbani kwake, akakatisha safari, akakata kona na kuelekea huko.

    Njiani alikuwa na mawazo mengi, alichanganyikiwa, alijitahidi kukumbuka kama kulikuwa na mtu aliyekuwa akimfahamu huko mpaka kutumiwa mzigo wake lakini hakukumbuka kitu chochote kile.

    Alipofika huko, akapewa bahasha ndogo ambapo kwa ndani kulikuwa na barua, hakutaka kufungulia hapo, akarudi kwenye gari, akaondoka, alipofika njiani kwenye foleni, akaifungua na kuanza kuisoma.

    Ilitoka kwa Linda, msichana aliyekuwa amefungwa kifungo cha miaka sita gerezani. Dickson aliisoma barua ile, ilikuwa ni ya kugusa, iliyousisimua mwili wake, machozi yalishindwa kuzuilika, yakaanza kutiririka mashavuni mwake.

    Maneno yaliyoandikwa katika barua ile ilimgusa kupita kawaida. Alipomaliza, akauegemea usukani na taa ziliporuhusu, akaondoka mahali hapo.

    Alipofika nyumbani, kitendo cha Nandy kumuona tu akagundua kwamba kulikuwa na kitu, hakumzoea mume wake kuwa kwenye hali aliyokuwanayo, macho yake yalikuwa mekundu yaliyoonyesha ni kwa jinsi gani alikuwa amelia sana.

    “Kuna nini mpenzi?” aliuliza Nandy kwa sauti ya chini.

    Dickson hakujibu kitu, alichokifanya ni kuingiza mkono mfukoni na kumpa barua ile Nandy, akaipokea na kuanza kuisoma kwa umakini. Barua ile iliandikwa hivi...

    Kwako Dickson.

    Ninaomba msamaha kwa kila kitu kilichotokea baina yangu na yako. Ninaamini kwamba ni shetani ndiye aliyekuwa akiniendesha pasipo kujua kwamba hakukuwa na kitu kilichokuwa kikitesa duniani kama kumlazimisha mtu anayekupenda akupende.

    Ninakuomba msamaha kwa hayo yote, kwa kuulazimisha moyo wake unipende msichana ambaye sikua chaguo lako, ninakuomba msamaha kwa hatua niliyochukua kwa kukusingizia kubaka, ni kitu ambacho kinaniumiza moyoni mpaka leo hii. Dickson, ninaomba msamaha sana.

    Nandy anaendeleaje? Ni msichana mwenye sura nzuri ambaye ananijia kichwani mwangu kila siku, ni msichana ambaye ninakiri kwamba anastahili kuwa mke wako maisha yako yote.

    Dickson, ninaomba uzungumze na Nandy, ninaomba umwambie anisamehe kwa kila kitu kilichotokea. Bila mimi, bila upumbavu wangu, bila wivu wangu wa kijinga leo hii Nandy angekuwa anatembea.

    Niliumia nilipoona umenikataa, nikaamua kuchukua uamuzi mgumu wa kuyaondoa maisha ya msichana huyo. Ajali aliyoipata, haikuwa ya bahati mbaya, ilikuwa ni ajali ya kupangwa ambayo nilitaka niyaondoe maisha yake.

    Dickson! Moyo wangu unauma, ninajiona kuishi katika dunia ya peke yangu, ninajiona kuishi jehanamu kwenye maumivu makali ya nafsi yangu.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ninajuta! Kwa kila kitu nilichokufanyia wewe na Nandy, ninastahili adhabu yoyote, hata kama nitauawa, ninastahili kwa kuwasababishia maisha mliyokuwanayo sasa hivi.

    Dickson! Ninahitaji msamaha wako niwe na amani! Najua siwezi kubadilisha kitu chochote kile, najua siwezi kumpa afya Nandy, ila pamoja na hayo, ninahitaji msamaha wenu, ninahitaji muupoze moyo wangu kwa kunisamehe kwani najiona nina msalaba wa dhambi kichwani mwangu, nimechoka, ninahitaji muutue kwa kunisamehe tu.

    Nimehukumiwa miaka sita gerezani, ni michache, kwa yale niliyowafanyia ninastahili hata kuhukumiwa kifo, Dickson! Ninahitaji msamaha wenu, ninahitaji kusamehewa japokuwa kwa yale niliyowafanyia inawezekana hayastahili kupokea msamaha wenu.

    Ni mimi, Linda!



    Mpaka anamaliza kuisoma barua ile, machozi yalikuwa yakimtoka Nandy, hakuamini kama Linda ndiye aliyemfanya kuwa kitandani akiteseka. Akamuita Dickson, akamsogelea na kumwambia amkumbatie, Dickson akafanya hivyo.

    “Dickson! Pamoja na mateso ninayopata, pamoja na maisha yote ninayopitia, kwa moyo wangu mmoja, NIMEMSAMEHE LINDA!” alisema Nandy huku uso wake ukiwa kwenye tabasamu na machozi yakitiririka mashavuni mwake.

    “Kweli?”

    “Mungu ametufundisha kuhusu kusamehe! Yesu aliwasamehe watu waliomtesa, walimchoma mkuki, walimzomea na kumtemea mate na kumuua, mimi ni nani mpaka nissisamehe! Dickson, kama bado hujamsamehe Linda, naomba umsamehe ili awe na amani,” alisema nandy huku akiwa amekumbatiwa na mpenzi wake.

    Dickson akamwambia wazi kwamba naye pia alimsamehe, hakuishia hapo tu, naye akamwandikia barua na kumwambia kuhusu msamaha, kwamba hawakuwa na kinyongo chochote kile.

    Kwa kile alichokifanya Linda si kumkomoa Nandy bali alimsaidia kwani kipindi alichokuwa akipata ajali, Nandy alikuwa akienda kujiua, kwa maana hiyo, kama asingepata ajali hiyo kipindi hicho angekuwa marehemu.

    Hayo ndiyo yaliyoendelea. Mungu aliwapa muda mrefu wa kusubiri, Nandy aliendelea kukaa kitandani kwa miaka mitatu mfululizo ndipo mabadiliko yakaanza kuonekana mwilini mwake.

    Kitu cha kwanza kabisa kufanya kazi kilikuwa ni vidole vyake vya miguu, vilianza kuchezacheza. Alishtuka, hakuamini, akamuita dada wa kazi na kumwambia ampigie simu Dickson.

    “Mwambie vidole viecheza,” alisema huku akionekana kutokuamini.

    “Unasemaje dada? Vidole vimecheza?” aliuliza dada wa kazi huku akionekana kutokuamini.

    “Ndiyo! Mpigie simu kumwambia aje,” alisema Nandy.

    Hayo yalikuwa ni mabadiliko ya mwanzo, yakaendelea kutokea zaidi na zaidi, baada ya wiki mbili, Mungu akazidi kufanya miujiza mwilini mwake, akaendelea kuonyesha nguvu zake kwa kupitia imani ambayo alijiwekea msichana huyo.

    Kuanzia kiunoni kushuka chini kukaanza kufanya kazi, ilikuwa ni furaha tele kwa msichana huyo. Pale kitandani alipokuwa alikuwa akimuimbia Mungu matendo makuu aliyokuwa akiyafanya mwilini mwake.

    Alitamani kuinuka na kurukaruka, kwa kilichokuwa kikiendelea mwilini mwake hakuamini na baada ya miezi miwili, Nandy akapona kabisa.

    Kilichokuwa kimemponya hakikuwa uwezo wa madaktari, kilichomponya hakikuwa ujanja wake wala kitu chochote zaidi ya imani yake na nguvu ya msamaha aliyokuwanayo moyoni mwake.

    “Nitayazungumzia matendo ya Mungu maishani mwangu,” alisema Nandy huku akiwa amesimama mbele ya kanisa, alishika kinasa sauti huku machozi yakimbubujika.

    Alikonda sana, hakujali, kitu pekee alichokuwanacho kichwani mwake ni kwamba aliponywa ugonjwa uliokuwa ukimsumbua kwa miaka mingi.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mume wake alikuwa pembeni yake, kila alipomwangalia, alimuona mwanaume shujaa aliyekuwa tayari kufanya lolote lile kwa ajili yake.

    Hapohapo kanisani, akamsogelea na kumkumbatia, akaliambia kanisa kwamba miongoni mwa watu waliopata bahati ya kuwa na mume jasiri, aliyejua kupenda, alikuwa yeye.

    “Ni imani ndiyo iliyoniponya,” alisema kila alipokuwa akiulizwa. Hakuacha kulia kwa furaha, kila alipokuwa akiyakumbuka matendo makuu ya Mungu, alibaki akimsifu tu.



    MWISHO.

0 comments:

Post a Comment

Blog