Simulizi : Sipendi Ujinga Mimi
Sehemu Ya Tatu (3)
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mdidi akafata maelekezo aliyopewa na vijana wale na baada ya dakika kama kumi akawa amefika alipoelekezwa, lakini kila alipotazama hakuweza kugundua nyumba ya Mzee Kilonda ni ipi. Kwa bahati akatokea msichana mmoja mrembo na aliyependeza kwelikweli, akiwa anakuja njia ile aliyosimama Mdidi, msichana yule akamtazama Mdidi kwa jicho la udadisi Mdidi pia akasubiri msichana yule amkaribie ili aweze kumuuliza,
“Samahani dada yangu naomba kuuliza”
“Who are you and what do you want to ask? (wewe ni nani na wataka kuuliza nini?)” Msichana yule akauliza kwa dharau mno, huku akimpandisha na kumshusha Mdidi.
Mdidi akamtazama msichana yule asijue amjibu nini maana alijikuta akikereka na dharau alizoonesha mdada yule.
“You miss the target, am not that cheap as you think,(umeingia chaka mie sio mrahisi kama unavyodhani)” aliendelea kuongea msichana yule.
“Inaonesha kuwa hujiamini hata kidogo,” Mdidi akasema.
“Am confidently enough to do anything as long as I am not breaking rules and regulations, (najiamini sana kiasi cha kuweza kufanya lolote ndani ya sheria na taratibu)”
“Kwanini umejibu kitu usichoulizwa, unahisi nimekutaka, nimekutamani au kukupenda? Kwanini usinge subili nikuulize kwanza ndivyo ujibu, am not here to ask for your heart, (sipo kwa ajili ya kuomba faragha kwenye moyo wako),” Mdidi akajibu kwa jeuri.
Msichana yule akajisikia vibaya kwa jibu alilopewa na Mdidi kwani kwake ilikuwa kawaida kwa wavulana wa mtaa ule hata wa kutoka mbali na mtaa ule kusimama sehemu ile ile aliyosimama Mdidi na kutupa ndoano zao walau wapate nafasi ya kuwa na mrembo yule.
Mdidi akutaka kuendelea kumsemesha yule msichana akamtazama kisha akaweka sawa begi lako na kumwambia,
“Thanks for your time”
Akamuacha akiendelea kutafakari ule mgogoro mfupi uliotokea baina yake na Mdidi asiamini, kwani wanaume wengi wa kila rika ubabaika pindi wamuonapo sasa imekuaje kwa huyu mbona hakushtuka, ikabidi aghairi safari yake na kurudi alipotokea.
Mdidi baada ya kuachana na yule msichana akakutana na mtu mwingine mbele na kuulizia kwa mzee Kilonda na akapewa maelekezo yote. Akaenda hadi nyumba aliyoelekezwa akashangaa sana kukuta ni nyumba yenye hadhi ya kati na kwa kutazama mara mbili watu waishio humo wanapesa japo si ya kufanya makubwa ila ile ya kuamua leo kula maharage kesho nyama ilikuepo, kitu kingine kilichomshangaza ni kuwa Mzee kilonda alipendwa sana na kila mtu aliyekuwa akiishi eneo ilo akavuta kumbukumbu ya maneno aliyoambiwa na mtu wa mwisho kumuuliza,
“Bila shaka utakuwa una shida usiogope mueleze kila kitu naamini atakusaidia kwani mzee Kilonda ni moja kati ya wazee wapenda Amani na utulivu, anapenda watu waishi kwa upendo na kuthaminiana”
Mdidi akavuta tena kumbukumbu ya maneno ya Yahaya aliyoyasema juu ya Mzee kilonda na mambo yote yaliyotokea katika mtaa wa Faru,
“Aah!! Yule mzee nuksi sana yeye ndiye chanzo cha majanga yote hapa, kuna siku alitaka kuamulia ugomvi na bahati haikuwa kwake kwani mama Salehe alimchambua na kumpa maneno mazito, watu wengi walimfukuza na kumwita mzee yule mchawi. Jioni ya siku iyo ndiyo mambo yote yakaanza kutokea kifo cha Salehe, Upendo na Vijana wale 10”
Kumbukumbu izo zikazidi kumchanganya Zaidi Mdidi akawaza au labda amekosea nyumba lakini hapana kwani kwa maelezo yote hapo ndipo kwa mzee kilonda, hakuweza kuikariri sura yake vizuri kwani ile siku aliyopita karibu na banda la Yahaya machipsi ilikuwa giza lishaingia tayari na hakuweza kumuona vizuri.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mawazo yake yakakatishwa baada ya mlango kufunguliwa na kutoka bibi mmoja aliye na nguvu za kutosha mbali na uzee wake, kwa mawazo ya haraka haraka akahisi uenda yule ni mke wa mzee Kilonda.
“Shikamoo bibi”
“Marahaba mjukuu wangu ujambo!”
“Sijambo bibi”
“Haya karibu ndani”
Ukaribisho ule ukaanza kumpa Amani ya moyo na kuamini kuwa kile alichokiwaza au watu wa mtaa wa faru walichoamini sicho. Mdidi akaingia ndani na kukaa kwenye kiti,
“Samahani bibi”
“Bila samahani”
“Sijui mzee Kilonda nimemkuta”
“Tufahamiane kwanza mjukuu wangu”
“Aah! Samahani sana bibi yangu nimeghafirika kidogo, mimi naitwa Mdidi natokea mtaa wa Faru na nipo hapa kwa ajili ya kuongea na babu”
Bibi alishtuka kidogo kusikia Mdidi anatokea mtaa wa Faru kwani kilichomtokea mume wake huko anakifahamu vizuri, akavuta pumzi ndefu na kuendelea kumuuliza,
“Ayah! Niambie una shida gani hadi utake kuonana na mzee Kilonda?”
Swali likawa gumu Zaidi akawaza je aseme kuwa ni kwa ajili ya kashfa zile za uchawi au atumie njia gani, lakini wakati akiendelea kuwaza hayo wakasikia sauti ya mzee Kilonda akiongea na mjukuu wake kwa sauti kuu,
“Yaani babu hamu ya kutoka imeniisha”
“Kwanini mjukuu wangu?”
“Nimekutana na mtu mmoja hivi wa ajabu ajabu ameniharibia siku yangu yote”
“Mhmhm mkwe nini?”
“Aah! Babu acha utani bhana!”
Kwa maongezi hayo yalitosha kumpa majibu japo kwa uchache Mdidi kuhusu mzee Kilonda ni mtu wa aina gani. Mzee akiwa na mjukuu wake wakaingia ndani msichana yule akapigwa na butwaa alipokutanisha macho yake na Mdidi,
“Babu naona hali ya hewa imeharibika humu ndani”
“Kauli gani hiyo unayoitoa mbele ya mgeni,” Mzee Kilonda aliongea kwa sauti ya chini kumkanya mjukuu wake.
“Karibu kijana,”
“Asante, shikamoo!”
“Marahaba! Kwema utokako alafu mbona hauna hata kinywaji, we Catherine njoo mara moja!”
“Hapana babu sijisikii kutumia chochote kwa sasa kwani hata bibi alinikaribisha kinywaji nikamueleza kuwa niko sawa tumboni”
“Kwangu mgeni ni Baraka ivyo sipendi mtu aingie na kutoka pasipo kupata chochote kitu toka kwenye nyumba yangu, naamini hata bilauri moja ya sharubati haitoathiri kitu”
Maneno yale yalimuingia vilivyo Mdidi akajikuta akikubali ombi la mzee Kilonda,
“Na iwe kama ulivyo nena mzee wangu”
Baada ya muda mfupi Catherine akawa kashaleta kinywaji na maongezi kati ya Mdidi na Mzee kilonda yakaendelea,
“Wewe ni mmoja kati ya wazee wachache sana wa dunia ya leo walio jaliwa busara na hekima, mimi nipo kwa niaba ya serikali nafanya utafiti katika kata ya Mnyamani na mitaa yake”
“What’s the purpose of your research, (nini dhumuni la utafiti wako)”
“Actually, I intended to assess socio-economic as well as psychological factors which contributed to poor academic performance among the pupils and students in their final exams specifically to those who lives in Mnyamani ward, (nimedhamiria kufanya utafiti juu ya sababu zinazowafanya wanafunzi wengi kufanya vibaya katika mitihani yao hasa wale waishio kata ya Mnyamani).
“Kho! Kho! Kho!” Mzee Kilonda akakohoa kidogo kisha akakaa sawa na kumtazama kwa makini Mdidi hakutegemea kama anaweza kukutana na kijana wa haiba ile.
“Is there anything I can do to your research? (naweza kusaidia lolote katika utafiti wako)”
“Ofcourse yes! , ( bila shaka ndio)”
“Haya nakusikiliza kijana”
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hadi kufika hapo hali ilikuwa tofauti sana na alivyotegemea, Mdidi akajikuta akiwaza ni kwa namna gani ataweza kuingizia habari ya kina mama Salehe kwa mzee yule ambaye alioonekana kuwa makini na kujua vitu vingi sana hivyo haikuwa rahisi kumuadaha.
“Naweza kukuhoji leo au tufanye siku nyingine ambayo wewe utakuwa na nafasi,” alisema Mdidi.
“Wewe unaonaje?” aliuliza mzee Kilonda.
“Naomba nikuachie dodoso yangu uisome kwa umakini na uijaze”
“Hapo sawa, rudi baada ya siku mbili naamini utafikia lengo”
“Asante mzee wangu”
Mdidi hakuwa na la ziada kwa siku iyo kwani kwa kiasi kikubwa alifahamu kuwa mzee Kilonda si yule watu wa mtaani kwake wanavyomfikiri, ikabidi aage na kuanza kuondoka lakini kabla hajaondoka mzee Kilonda akamtaka asubiri kidogo ili aweze kumsindikiza, akamuita mjukuu wake,
“Cathy…. Cathy..!”
“Abee babu!”
“Ebu njoo tumsindikize mgeni mara moja”
“Aah! Jamani babu si uende tuu”
“Twende! Hatufiki mbali”
“Sawa nakuja”
Mdidi alivutiwa sana na ukaribu uliopo kati ya babu na mjukuu wake, familia ile ilionesha kuwa na upendo wa hali ya juu, walionesha kumpatia mjukuu wao malezi bora mno.
“Twaweza kwenda sasa,” aliongea mzee Kilonda baada ya Cathy kufika.
Wakaanza kutembea huku kila mmoja akiwa kimya asimuongeleshe mwenzie, Mdidi alitamani kusikia mzee yule akiongelea habari zilizotokea siku za nyuma lakini hakujua ni kwa namna gani ataweza anzisha iyo mada.
“Hivi wewe kaka, unaishi wapi naona unamchosha babu yangu kutembea,” Cathy akavunja ukimya kwa kumuuliza Mdidi swali hilo.
“Naishi mtaa wa Faru”
“Faru..!” mzee kilonda akashtuka kusikia jibu la Mdidi.
“Ndio naishi faru karibu na kijiwe kimoja kinaitwa Kafapandu”
Mzee Kilonda akashusha pumzi ndefu, akapunguza mwendo na hatimaye kusimama kabisa. Fikra zake zikaenda mbali sana akajikuta akimshika mjukuu wake mkono kisha akamtazama Mdidi na kumwambia.
“Nadhani sisi tuishie hapa”
“Are you ok? (uko sawa),” Cathy akamuuliza babu yake.
“Yeah! Am fine, (niko sawa)”
“Sasa mbona umebadirika ghafla kusikia Mdidi anaishi Faru au bado zile kumbukumbu zipo?” Cathy akauliza.
“Hapana! Ila namhurumia sana kijana huyu naona anaishi katika mazingira magumu mno”
“Usiwaze kuhusu mimi babu nimepazoea tayari,” alijibu Mdidi huku akifurahi moyoni baada ya kuona kuna uwezekano mkubwa akafanikiwa kukitambua kile alichotamani kukijua kwa mzee Kilonda.
“Kwanini umesema naishi katika mazingira magumu?”
“Watu wa mtu ule wamekosa busara na hekima, wengi wametawalia na fikra potofu zilizochagizwa na Imani za kishirikina,” alisema Mzee Kilonda huku akimtazama Mdidi.
Mzee Kilonda akasimulia tukio zima kuhusu ugomvi wa mama Juma na mama Salehe, hivyo yeye kama mtu mpenda Amani na utulivu aliona si busara kwa wanawake wale kugombana hadharani akaamua aingilie kati kuwasuluhisha lakini kilichotokea ni kukashifiwa na kudharaulika. Mzee Kilonda alieleza huku akionesha masikitiko makubwa kwa jamii ile, Mdidi akapata suluhisho la maswali yaliyotatiza akili yake kwa muda mrefu.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya kuachana na mzee Kilonda, Mdidi akarejea nyumbani na kukuta watu wengi wamejaa, wakati akiendelea kutafakari kulikoni akasikia watu wakishangilia kama vile wanaangalia mpira.
“Ndiooo!”
“Mpe huyo hawezi kukuchukulia mume na nyumbani kwako akaja”
“Hahahahaha! Hatupendi ujinga sisi”
Zilikuwa sauti za wanawake waliokusanyika eneo hilo, Mdidi akasogea na kuangalia Vizuri akakuta ni mama Salehe akipigana na mumewe huku akimshtumu kutoka nje ya ndoa. Baba Salehe ni mwanaume mpole asiye na maneno mengi, ndoa yake na mama Salehe ilifungwa miaka 4 iliyopita lakini hata siku moja hakuwahi kuifurahia ndoa yake, tabia za mkewe zilimfanya ajisikie vibaya mbele za watu, alijitahidi kumkanya mara kwa mara lakini haikufua dafu kwani mama Salehe alijaliwa mwili mkubwa na alikuwa na maneno mengi, hakuwa na heshima mbele ya mumewe. Hali hii ikampelekea baba Salehe atafute mwanamke mwingine kwa siri bila mkewe kujua, hivyo hakiona kero huwa anakwenda kuliwazwa na mwanamke huyo mpya. Kama waswahili wasemavyo “penzi kikohozi kulifa huliwezi” baba salehe alidata akadatika taratibu hakaanza kupunguza mawazo na mkewe na ndio hapo mama Salehe akagundua na kuanza kufatilia nyendo za mumewe. Hatimaye akawakuta na kuwavuta kibabe hadi nyumbani kwake hapo ndiyo timbwili likaanza.
“Hivi wewe mwanaume umekosa nini hadi kuamua kuchepuka na huyu kinuka mkojo”
“Wewe koma tena ukomaye, mumeo hapa ndio kafika”
“Paka tukiongea wewe panya ukae kimya sawa eenh! Naongea na mume wako”
“Huhuhuhu! Eti mume wako! Angekuwa mume wako ungemfungia ndani bibi eenh! Ukamuacha anatangatanga wajanja tukamchukua,” alijibu yule msichana kwa kujiamini sana.
Baba Salehe alivyoona hivyo akaamua ajikaze kiume na kumchukua mchepuko wake na kumtaka aondoke eneo lile lakini mama Salehe akamzuia, na kumnasa kibao mumewe.
Mdidi alikuwa karibu akiyashuhudia hayo ukweli akashindwa kuvumilia ile hali ikabidi aingilie kati kuamulia ugomvi ule.
“Uungwana si maneno pekee bali vitendo, leo hii mnavyogombana hadharani mnawafunza nini hao watoto wadogo wanaowatazama! Kwani hamna njia nyingine ya kusawazisha tofauti zenu hadi hii ya kugombana hadharani,” alisema Mdidi baada ya kufika alipo Mama Salehe na yule msichana.
“Kaka nakuheshimu! Achana na mambo yasiyokuhusu,” aliongea yule msichana.
“Ndiooo! Janaume zima kuingilia vitu visivyo muhusu puuuu!” waliongea watu wengine kwa sauti kumshushua Mdidi.
“Hahahahahahahaha!” Mdidi akacheka na kuwafanya watu wote wanyamaze kuangalia nini kinachomchekesha lakini wasikione.
“Mhmhm! Jamani isije kuwa yeye pia ni mchawi yakawa kama yalivyokuwa kipindi kile,” wakasikika vijana wawili wakiongea kwa sauti ya chini.
“Mmesimama kwenye mlango wa chumba changu, mnawezaje kusema sihusiki wakati mmezuia njia, nahitaji kupumzika na kama ulivyo na haki ya kupiga kelele name pia nina haki ya utulivu, tumelipa wote kodi sasa tafadhali naomba mkatafute pa kugombania ila sio hapa,” alisema Mdidi huku akianza kupiga hatua fupi fupi kuelekea ulipo mlango wa chumba chake.
“Yaani wewe mtoto! Usione nimekaa kimya ila mimi ni mtu mzima na akili zangu, mume wangu mwenyewe hakunyanyua mdomo wake juu yangu wewe nani hasa kunisema hivi?” mama Salehe akambwatia Mdidi ambaye alishaanza kufungua mlango kuingia ndani.
Ikabidi asimame na kumuangalia mama Salehe kwa tabasamu zito bila kusema lolote, watu wote wakashangaa mno kwani walitegemea Mdidi ataonesha kukasirika hata kujibishana na mama Salehe.
“Vipi mama! Umemaliza au nisubili uendelee kuongea,” alisema Mdidi
“Nakuonya kwa maneno, siku nyingine ntakufunza kwa vitendo fyuuuuuu!” aliongea mama Salehe kwa hasira.
“Dada hapo alikuwa sahihi kama kweli yule ni mwanaume wako uliyeapa kumpenda kwa shida na raha, usingemuacha akatangatanga. Familia bora hujengwa na uhusiano thabiti baina ya mtu mume na mtu mke lakini hiyo pia haikuwa sababu ya kutosha kwa wewe dada kumkubali mwanaume asiye wako. Lakini muamuzi wa mwisho ni moyo, moyo wa mumeo ukihama kwako hata ufanye nini hauwezi kurudi labda akose tulizo la muda mrefu”
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya kuongea maneno yale akaingia ndani, huku nje kila mmoja akawa hana la kuzungumza baadhi ya watu walionekana kuyaelewa maneno ya Mdidi.
“Daah! Kweli asee tumepoteza saa nzima kuangalia huu ujinga, ningekuwa namenya viazi vyangu sasa hivi ningekuwa nan doo hata mbili,” alisema Yahaya huku akivuta hatua ndefu kuondoka eneo hilo.
Watu wakatawanyika ukimya na utulivu ukarejea kwa muda. Kwa upande wa mama Salehe hali haikuwa shwari hata kidogo akatoka moja kwa moja hadi kwa shoga yake mama Ashura,
“Vipi shoga mbona hai hai!”
“Mhmhm! Mwenzangu yaliyotokea huko nadhani umeyasikia”
“Nitaachaje kutosikia shosti! Na mtaa huu kuna redio mbao kama utitiri, ila nawe umekosea, mtoto mdogo yule unajibishana naye wa nini? Ona sasa alivyokuabisha”
“Sasa ningefanyaje shoga yangu?”
“Yaani mume akuchukulie na kebehi akufanyie mweeeh! Alafu nasikia sijui kuna mkaka gani naye akawa anamtetea”
“Ndio shosti yule mkaka naona ananifatilia kitambo tuu, mara amsaidie mama Juma, leo kamtetea yule kishankupe mchukua mabwana za watu”
“Usikae kimya shosti wangu fanya mambo uwaoneshe dunia ilivyo”
“Sawa shosti mwambie basi mtaalamu wako afanye mambo”
“Huhuhuhuhu! Nilikuwa nasubiri ruksa yako tuu! Niliwalipueeee”
“Hatupendi ujinga sisi,” walisema pamoja huku wakicheka.
“Mdidi tumfanyaje,” mama Ashura akauliza.
“Nataka awe shoga wanaume wenzie wampumulie maana kazidi kuchimba mambo yasiyomuhusu”
“Huhuhuhuhuhu! Apoo ndio napokupendea shoga angu, haufumbii macho ujinga,” aliongea mama Ashura.
“Na yule kishankupe nataka nimlaze kitandani mwaka mzima,” aliongea mama Salehe kwa hasira mno huku akiuma meno.
“Mhmhmh! Kivipi shoga yangu?” aliuliza mama Ashura.
“Binafsi natamani apate gonjwa la ajabu ikiwezekana apararaizi”
“Mhmhmh! Mama Salehe wewe”
Mama Ashura alishangazwa kidogo na chuki aliyoijenga rafiki yake juu ya wale maadui zake, hata hivyo hakuweza kukataa kutoa msaada kwa shosti wake,
“Sawa mambo yataenda kama ulivyonuia, itabidi twende kwa mtaalamu kesho asubuhi na mapema ili tuwahi kukamilisha shughuli hii nzito”
“Asante shosti kwa sapoti yako”
“Usijali! Hatulei ujinga sisi lazima tuwafunze”
Wakaendelea kuongea mengi, huku mama Salehe akitamani siku ipite kwa haraka ili malengo yake yatimie, akawaza vingi sana moyoni mwake na akijikuta akitabasamu tuu.
Siku iliyofata ilikuwa ni siku ya kwenda kuchukua dodoso kwa mzee Kilonda, ivyo baada ya kifungua kinywa Mdidi akaanza safari ya kuelekea mtaa wa 8. Hakutumia muda mrefu baada ya mwendo wa nusu saa akawa amefika kabisa nyumbani kwa mzee Kilonda, akabisha hodi na kukaribishwa ndani. Mdidi akahisi hali ya tofauti na siku ile ya kwanza alipokuja, nyumba ilikuwa imepooza sana,
“Vipi za huko utokako?” mzee Kilonda akauliza baada ya kusalimiana na Mdidi.
“Kwema mzee wangu! Sijui ninyi?”
“Aah! Kwetu ni kwema kiasi”
“Wamaanisha nini?”
“Yule mjukuu wangu anaumwa sana”
“Aah! Nini Zaidi?”
“Daktari amesema ana malaria kali mno”
“Asee! Poleni sana”
“Asante tushapoa”
“Yupo hapa nyumbani au bado yupo hospitali?”
“Yupo ndani huko na bibi yake kula kwenyewe hataki basi tabu tupu”
“Naweza kwenda kumuona”
“Utamuona tuu, ila ngoja tumalize kilichokuleta kwanza”
“Sawa haina shida”
Mzee Kilonda akachukua bahasha ya kaki iliyokuwa juu ya meza kisha akatoa dodoso aliyokwisha ijaza na kumkabidhi Mdidi. Mdidi akaipokea na kuipitia, akalidhishwa na majibu aliyotoa mzee Kilonda, akairudisha ile dodoso kwenye bahasha na kutoa shukrani zake,
“Nashukuru sana babu! Kwa hakika umenisaidia sana katika hili”
“Usijali mjukuu wangu, mimi pia napenda kuona vijana wakielimika na kwenye mapungufu lazima tupaze sauti zetu kuongea bila kuogopa”CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ni watu wachache wenye mambo haya, wazazi wengi hufikiri kuwa jukumu la watoto zao kuwa na elimu bora ni la walimu au serikali,” aliongea Mdidi.
“katika dunia ya leo mzazi yuko ladhi kukopa kiasi chochote cha pesa kwa ajili ya sare za harusi au zawadi za kicheni pati, lakini si rahisi kwake kuazima pesa kwa ajili ya kununua kitabu ili mtoto wake ajisomee, angalia miziki ya kishenzi ilivyotawala leo hii mtoto anawajua waimba muziki kuliko maana fupi ya baolojia au uraia, watoto wanashindana kukata viuno na wazazi wanawashangilia wakati wenzetu huko wanashindana kugundua vitu,” alisema mzee Kilonda kwa uchungu mno akionesha kuumizwa na mambo yanayotokea katika jamii inayomzunguka.
“serikali ata ijitahidi vipi lakini bila msaada wa walezi au wazazi watoto hawawezi kufanya vizuri darasani, mtoto toka anazaliwa hadi anakua, masikioni mwake anasikia matusi, akisogea mbele anaona kamali, akirudi huku anakuta vigenge vya wavuta bangi je unafikili mtoto yule atafikilia kusoma katika mazingira hayo” aliendelea kuongea mzee Kilonda huku Mdidi akimsikiliza kwa makini na kuandika baadhi ya vitu kwenye kijitabu kidogo alichonacho.
“kwenye sababu za kijamii utaona nimeandika malezi mabovu toka kwa wazazi au walezi, makundi rika, mapenzi ya utotoni, utoro na nyingine nyingi kama sababu zinazo wafanya watoto kufeli pia kwenye uchumi utaona nimeandika upungufu wa vifaa vya kufundishia, miundo mbinu kuwa dhaifu, kipato kidogo cha wazazi na ajira za utotoni na mwisho kwenye sababu za kisaikolojia kuna hofu ya mitihani, kutokuwa na mawazo ya kina, kutojiamini na nyinginezo”
“Daah! Mzee sikutegemea kama unaweza kuchambua mambo kiasi hiki, ukweli umenifungua sana kiakili na naamini utafiti wangu utakuwa bora”
“Shaka ondoa kijana wangu, wakati wowote mimi nipo unakaribishwa”
Baada ya maongezi hayo mafupi, ikabidi Mdidi anyanyuke na kuongozana na mzee Kilonda hadi chumba alichopo mgonjwa. Hali ya Cathy haikuwa njema sana kwani ndani ya siku mbili alionekana kudhoofika mno, Mdidi akasogea hadi alipo mwanadada yule na kuongea naye,
“Vipi Cathy wajionaje na hali”
“Kama unavyoniona Mdidi,” alijibu Cathy kwa sauti ya chini sana.
“Je unakula kweli?”
“Mhmh! Chakula hakipandi kabisa”
“Sasa unafikiri utapona vipi bila kula?”
“Nitapona tuu”
“Acha ujinga basi, itabidi ule wewe huoni huruma kwa bibi na babu yako wanavyokuhangaikia” Mdidi akaongea kisha akachukua uji uliokuwa kwenye chupa na kumimina kwenye bakuli kisha akamwinua Cathy na kumkalisha vizuri kitandani.
Mzee Kilonda alivyoona vile ikabidi amfinye mkewe aliyekodoa macho kuangalia nini kama mjukuu wake atakubali kula au la,
“Kho! Kho! Kho! Wee mwanamke embu kaniletee dawa yangu mimi nipo sebuleni,” alisema mzee Kilonda huku akiondoka.
Bibi naye alielewa vizuri kile mumewe alichomaanisha ikabidi atoke na kutimiza agizo la mumewe,
“Kunywa kidogo upate nguvu,” alisema Mdidi huku akipeleka kijiko mdomoni kwa Cathy.
“Siwezi kulishwa na mtu nisiyemfahamu”
“Acha ubishi basi, hata mimi sikufahamu wewe kunywa kwa heshima ya bibi na babu yako” alisema Mdidi huku akimtazama Cathy.
Nguvu ya maneno yenye busara na ushawishi mkubwa yakamfanya Cathy akubali kunywa uji ule, akajikuta anaumaliza bila shida yeyote. Mdidi akaendelea kupiga soga za hapa na pale ambazo kwa namna moja au nyingine zilimchangamsha sana mrembo yule. Kadri muda ulivyozidi kwenda ndivyo Cathy alijikuta akipata nguvu walau ya kuinuka na kuongea kwa mchangamfu,
“Thanks for your care, I real appreciate it may God bless you abundantly. (Asante kwa kujali, Mungu akubariki)”
“Never mention! (Usijali)”
“Mdidi sikutegemea Kama una moyo wa huruma kiasi hiki”
“Binadamu tumeumbwa kusaidiana leo kwako kesho kwangu, kwa hiyo usiwaze sana jitahidi kula ili dawa zifanye kazi vizuri,” alisema Mdidi huku akiutazama uzuri wa msichana yule kwa karibu Zaidi japo alikuwa akiugua lakini uzuri wake haukujificha ata kidogo.
Baada ya kusema hayo Mdidi ikabidi aage tayari kwa kurejea kwake, lakini Cathy hakutamani hata kidogo aende, alitamani kuwa karibu na Mdidi.
“Ndiyo unondoka?”
“Yeah! Nitakuja kukuona siku nyingine”
“Nikuombe kitu”
“Omba tuu”CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Utakubali?”
“Kama kipo ndani ya uwezo wangu nitakubali”
“Nataka ukae na mimi walau kwa siku ya leo hadi jioni,” alisema Cathy huku akitazama chini.
Mdidi akafikiri kidogo kisha akamtazama Cathy aliyesubili jibu kwa shauku kuu, Mdidi akatabasamu na kukohoa kidogo kisha akasema,
“Utajisikiaje endapo nitakubali?” Mdidi akauliza.
“Nitafurahi nahisi hata hii Malaria itaisha”
“Na utajisikiaje endapo nitashindwa kutimiza ombi lako?”
“Nahisi homa itazidi”
“Basi zidiwa sasa nikuone maana ombi lako siwezi litimiza, ila kabla ujazidiwa ngoja nimuite bibi yako akuone”
“Mhmhmhm! Mdidi wewe”
Bila kupoteza muda Mdidi akatoka na kuaga kwa babu na bibi wa Cathy na kuahidi kurudi siku nyingine kumjulia hali mjukuu wao,
“Asante sana Mdidi, leo umefanya kitu kikubwa sana katika maisha yetu, Mungu akuongoze na kukubariki”
“Amina! Msijali sana wazee wangu”
***********************
Mama Salehe baada ya kutoka kwa mtaalamu na kupewa dawa, akarudi nyumbani na kunyata hadi karibu na chumba cha Mdidi, akachungulia kwenye tundu dogo lililopo mlangoni na kugundua kuwa Mdidi hayupo, ila aliamini kuwa hayupo mbali na eneo ilo sababu mlango wake ulikuwa wazi, akarudi na kukaa kwenye ngazi iliyopo mlangoni mwake. Kumbukumbu za masharti ya mzee Bang’ala zikashuka kichwani mwake.
“Hakikisha hii dawa anaitambuka pindi tu atokapo msalani, kuwa makini asitambuke mtu asiyehusika maana madhara yake yatagharimu uhai wako”
“Tawile babu,” alisema mama Salehe kukubaliana na sharti lile.
“Hii dawa unatakiwa uiwashe kwa ukuni wa moto kipindi kile upepo unapotokea kusini na hakikisha unalitaja jina la yule mwanamke mara saba na kutema mate kila unapomaliza kutaja jina lake”
Mawazo yake yalikatishwa baada ya kuhisi kuna mtu chooni, alipochunguza vizuri akagundua aliyekuwa chooni ni mwanaume, akavuta fikra za haraka na kujua kuwa aliyekuwa chooni ni Mdidi, hivyo bila kupoteza muda akaingia ndani kwake na kuchukua dawa kikaratasi cha unga mweusi na kunyata hadi kwenye ngazi za kuingilia chooni, akaunyunyiza unga huku akitamka maneno flani yasiyosikika baada ya hapo akarudi ndani kwake huku akichungulia kuona nini kitatokea.
Baada ya dakika 2 Mdidi akawa anatoka msalani huku akiwa ameshika ndoo, mama Salehe akaanza kujawa na tabasamu huku akiamini lengo lake linatimia, Mdidi akapiga hatua fupi kushuka ngazi lakini kabla hajamalizia ngazi ya mwisho akajikuta akiteleza na kuanguka chini ile ndoo aliyoishikiria ikamponyoka na maji yaliyobaki yakamwagika. Mdidi alishangazwa na hali ile kwani alijikuta akiwa chini kwa Zaidi ya dakika 3, huku akishindwa kuelewa kile kilichotokea.
Kichwa kikawa kizito sana, ghafla akahisi mwili unashikwa ganzi, baridi kali likafanya aanze kupoteza uwezo wake wa kuona, upepo mkali ukazuka na akapoteza fahamu….
*****************************
Katika mwezi wa 5 waujauzito wa mwanamke mmoja asiye na umaarufu katika kata yaSharifu Shamba, wilayani Ilala, Mkoa wa Dar es salaam. Muelekeo wa kuwa na maisha bora ulikuwa kizungumkuti katika familia ya mama huyo wa watoto wawili huku akimtarajia watatu miezi michache baadaye.
Maisha ya kupanga yalikuwa magumu sana kwa mwanamama huyo, kipato kidogo alichokipata mumewe hakikuweza kukidhi mahitaji yote hivyo ikamlazimu ajinyime Zaidi ili watoto wake waweze kupata chochote kitu kuridhisha matumbo yao.
Ugumu wa maisha haukuweza kusababisha asitoe tabasamu tamu awapo mbele za watu, ucheshi wake ulihadaa nyoyo za watu wengi na katu hamna aliyewaza kuwa kuna siku mwanamama huyo anakosa hata kikombe cha chai. Katika hali ile aliweza kuwa na urafiki na majirani wengi na hiyo ikapelekea watoto zake kujenga ukaribu na watoto wa nyumba za jirani. Muda mwingi baada ya masomo waliutumia kucheza na wenzao na kumuacha mama yao katika hali ya upweke usio na huzuni.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Mtoto aliye tumboni mwa mama yule ananyota kali sana, kama tutampata kabla hajaliona jua itakuwa faida kwetu,” alisema bibi mmoja wa kizaramo aliyefahamika kwa jina binti Shomvi.
“Siku zote umekuwa na macho makali sana, nasubili maelekezo kujua nini kifanyike kumchukua kiumbe yule,” alisema mama mmoja wa makamo anayeishi na binti Shomvi katika paa moja.
Mlali ambaye ni mama wa watoto wawili, alisifika Zaidi kwa ukarimu, moyo wake wa kutoa kwa wengine ulimfanya abarikiwe na kupokea Zaidi japo si mali ila maneno yaliyo mtia nguvu na kumjaza ujasiri siku hadi siku. Moyo wake huo uliwapa mwanya maadui walio na nia mbaya juu ya kiumbe kilicho tumboni mwake.
“Nitakupa dawa! Kesho asubuhi hakikisha unaifanya kazi ya kukichukua kiumbe kile, mara nyingi mama yule hupenda kwenda bombani saa 2 asubuhi, fanya kila uwezalo umtwike ndoo yake ya maji na kazi itakuwa imeisha,” alisema binti Shomvi na kuingia ndani.
Mama Amina aliyekutwa na maswahiba yakufiwa na mume sambamba na watoto zake wote wawili miaka kadhaa iliyopita, katu hakupenda kumwona mwanamke mwenzake akiwa na matarajio ya kupata mtoto, hivyo maneno ya binti Shomvi yalimfanya afurahi na kutamani muda uende hili aweze kuifanya kazi ile.
“Sijutii kumuua mume wangu na kuwatoa sadaka wanangu sembuse wewe Mlali, nisiye na undugu nawe ata wa kusingiziwa….!” Alisema mama Amina.
Dakika zikasogea, saa zikakimbia hatimaye giza likaingia, Mlali ambaye pia alitambulika kama mama Mdidi aliandaa chakula mezani na kukifunika, akajilaza kwenye kiti kilichopo pembeni kidogo na meza ya chakula, usingizi ukampitia,
“Mtoto huyu ni nuru kubwa katika familiayako, wengi wanamuinda ila usiogope pambana kadri uwezavyo mwanao atakuwa salama”
“Ni wakina nani hao wanao muinda mwanangu angali tumboni,”
“Mama Aida! Mama Aida!,” kabla hajajibiwa akasikia sauti ikimuita alipotazama nyuma kuona nani anamuita akashtuka toka usingizini na kukuta mume wake kipenzi akiwa amerudi toka kazini.
Moyo ulimuenda mbio kuliko kawaida, maneno aliyoyasikia toka ndotoni yalimtia hofu sana, alitamani ajue nani na nani ni maadui zake lakini njia za Mungu si za mwanadamu, yafanyikayo usiku mwanga utayaumbua.
“Vipi mke wangu mbona unahema ivyo”
“Hamna kitu baba Aida! Umefika muda gani?”
“Kama dakika 10 zilizopita”
“Pole na kazi mpenzi”
“Asante! Mama watoto”
Baada ya kujuliana hali wakajongea kwa pamoja mezani tayari kwa kupata chakula cha usiku, kwa kuwa hakukua na chakula cha kutosha iliwalazimu wale sahani moja,
“Vipi Aida na kaka yake wako wapi?”
“Wameshalala”
“Ooh! Wamekula lakini?”
“Ndio niliwapakulia wakala”
Waliendelea kula huku wakiongea mambo kadha wa kadha juu ya maisha yao na watoto zao kwa ujumla.
********************************
Ni asubuhi nyingine iliyotawaliwa na mawingu mepesi yaliyopendezesha anga la jiji la Dar es salaam. Kama ilivyo ada kwa mama Aida kwenda bombani kila ifikapo saa mbili asubuhi. Mama Amina hakuwa mbali alisogea karibu kuhakikisha anapata nafasi yakumtwika ndoo mama Mdidi pale tu atakapohitaji, bahati ilionekana kuwa upande wake kutokana na hali ile ya ujauzito hakuweza kukaa foleni na pindi tu alipojaza ndoo yake mama Amina akawa amefika tayari kwa kumtwika. Hakupoteza muda ikabidi ainame na kuinyanyua ndoo.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kabla hajainyanyua akatokea mama mwingine na kupaza sauti iliyomshtua mama Amina, na kufanya aache kile alichokusudia kufanya,
“Mwanahizaya usiye na haya wewe! Unataka kumfanya nini mwanamke mwenzio,” alisema Yule mama.
“Eenh! Bibi wee msiba haukuhusu kilio cha nini?”
“Ondoka hapa na uchawi wako! Mfyuuuu!”
Mama Amina baada ya kuona amegundulika akaanza kujibalaguza na alipopata upenyo akaondoka zake na kuacha gumzo huku nyuma.
“Sio watu wote wenye nia ya kukufanyia wema!”
“Sielewi unachokizungumza”
“Tukio lile la kukutwishwa ndoo lina maana ya kukivua kiumbo kilicho tumboni mwako, kama angefanikiwa basi mtoto ungemkosa”
Mama Aida alishtuka sana kusikia vile, akajikuta akiishiwa nguvu na kukaa chini,
“Usiwaone wanavyokuja na kucheka pamoja nawe, binadamu sio wema, wanausongo na wewe,” aliendelea kusema Yule mama huku akinyanyua ndoo ya mama Aida.
“Twende nikusindikize nyumbani”
“Sijui nikushukuruje ndugu yangu, umekuwa msaada mkubwa kwangu, isingalikuwa wewe leo hii basi ningalimpoteza mwanangu, mungu akubariki na kukuzidishia,” alisema mama Aida.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment