IMEANDIKWA NA : NIHZRATH NTANI
*********************************************************************************
Sehemu Ya Kwanza (1)
KISA CHA KWELI
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kwa kumbukumbu ya wazazi wangu.
"Wakati mikono yangu haiwezi tena kuwagusa niwapendao, nitaendelea kuwakumbuka kwa sala zangu. Wakati macho yangu hayawezi tena kuwaona wapendwa wangu, sura zao kamilifu huibuka katika album ya picha ya familia yetu. Wakati masikio yangu hayawezi tena kusikia sauti tamu za niwapendao, bado minong'ono yao huendelea kama kitulizo na burudisho la muziki mtamu masikioni mwangu. Kweli wale tuwapendao hawafi kamwe bali huendelea kuishi kwa muda wote ambao tunawakumbuka , kuwaenzi na kustahimili ukiwa lakini bado tutaendelea kuwa pamoja nao
Uungwana na utulivu wao upo hai wakati wote, macho yao malegevu, lakini ya huruma yataendelea kuniangalia. Tabia zao za unyenyekevu na utaratibu nitazikumbuka. Nitakumbuka pia ushauri wao waliokuwa wakinipa na utaendelea kuwa kama mwongozo mzuri kwangu, familia yetu na marafiki pia. Wamekwenda, nitawaonaje mimi?"
Utangulizi: Nimekuwa mwanaume mtu mzima sasa, pengine ni wakati sahihi kuitoa simulizi hii ili jamii ipate kujifunza. Niliitaka simulizi hii niifanye kama riwaya, pengine hadithi nzuri ya kupendeza lakini yote ilishindikana kwa sababu kazi hii si ya kubuni ingenipa shida sana katika kutengeneza matukio ya riwaya. Nikataka kuandika kama tamthiliya lakini nako sikuweza kuzingatia muundo wa uandishi wa tamthiliya nikajikuta naandika simulizi isiyo tamthiliya, riwaya ama hadithi. Nina hakika mara tu utakapomaliza kuisoma simulizi hii utakuwa umejifunza jambo muhimu sana katika maisha yako. Majina yaliyotumika katika simulizi hii si ya kubuni lakini hayahusiani na simulizi hii. Majina halisi yamefichwa kwa sababu maalumu. Twende nami mpaka mwisho wa stori hii......
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
....................
Nikiwa ndio kwanza nimetoka kutuma barua ya maombi yangu ya kazi, kwenda kwenye kampuni moja inayohusika na usafirishaji wa mizigo ndani na nje ya nchi. Asubuhi hii ilinikuta niko maeneo ya Posta, jijini Dar es salaam. Kuwepo kwa mvua za rasha rasha zilinifanya nijumuike na watu wengi kujificha pembezoni mwa korido za ofisi zilizoko maeneo hayo. Hata hivyo, baada ya muda fulani mvua zile zilikata.
Nikaanza kujivuta kusogea stendi ili nipate usafiri wa kurudi nyumbani ninapoishi pale maeneo ya Ukonga Airport. Kwa muda ule wa asubuhi ya saa nne hakukuwa na shida yoyote ya usafiri kama ilivyo adha la jiji la Dar Es Salaam, magari yalikuwa mengi. Wakati nalifuata basi moja kati ya mabasi machache yaliyokuwepo kituoni hapo yanayokwenda njia ya Gongolamboto. Nikajikuta namgonga kwa bahati mbaya mdada nisiyemfahamu.Mungu wangu!
Bila kutarajia, macho yangu yakajikuta yakiangalia baadhi ya nyaraka zilizosambaa ardhini kutokana na kitendo kile nilichokifanya bila kukusudia, nikajikuta mwili wangu ukiinama na kuziendea nyaraka zile na kuzikusanya kwa uangalifu mkubwa. Sikuwa najua nini kilichoifadhiwa ndani ya nyaraka zile. Kwa unyonge niliyainua macho yangu na kumtazama binti yule kwa mara ya kwanza, nakiri kabla ya hapo sikuwa nimemtazama vizuri binti huyu.
Macho yangu yakatua kwenye uso wa binti yule, Lalaula! nikashtuka! ni kama nimeshikwa na bumbuwazi kwa muda wa sekunde chache, mapigo ya moyo wangu yalikimbia kwa maili nyingi. Kitendo kile kilifanyika kwa haraka mno. Hata hivyo niliweza kumkabidhi binti yule nyaraka zile, na alipozipokea tu alinisindikiza na tusi na msonyo juu yake, nikabakia kufadhaika kwenye macho ya watu wengi, mvulana mimi!.
Wakati macho yangu yakimsindikiza binti yule akitokomea ndani kabisa ya Bank ya CRDB tawi la Azikiwe lililopo jirani na eneo hilo la Posta hapa jijini Dar es Salaam. Nami nikajivuta na kuingia ndani ya Bus, na kukiendea kiti cha kati kati upande wa dereva kisha nikakaa hapo. Dakika chache baadae basi lile likaanza safari. Mawazo ya binti yule yakaanza kunitawala. Hakika alikuwa binti mzuri ajabu na mrembo hasa wa kupendeza ambaye nakiri sikuwahi kukutana na msichana mzuri kama yule kabla. Kila kitu kilichotokea kwa dakika zile chache zikawa zinajirudia mawazoni mwangu. Nikajikuta najiuliza kwanini binti yule atawale mawazo yangu?.Nikakosa jibu.
*****************
Milio ya 'coins' kama ilivyo ada ya makonda wengi wanavyozichezesha pesa hizi za 'silver' kwa mtindo wa kipekee kabisa, ilinigutusha kutoka katika lindi la mawazo kwa wakati huo. Konda alikuwa ananikumbusha nimpe pesa yake, huku macho yangu yakitazama nje, nikaja gundua tupo kwenye foleni ya kuvuka mataa pale Tazara. Haraka nikaingiza mkono wangu mfukoni ili nitoe akiba yangu nimlipe konda yule.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hamadi! mikono yangu ilirudi patupu, hakukuwa na pochi wala pesa. Nikajikuta natafuta kila mahali ndani ya mifuko ya suruali yangu kama mtu aliyechanganyikiwa kwa muda huo lakini majibu yalikuja yale yale, pochi haikuwepo. Nikajikuta nababaika huku nisijue cha kufanya. Wakati huo huo konda alikuwa yupo makini na mimi akisubiria nimpatie haki yake. Kwa mara nyingine tena, nikawaza! nikawaza! nikahofu kufadhaika ndani ya Bus. Kwa ujasiri wa kiume nilimjibu konda yule, nimeibiwa pochi na pesa iliyokuwemo. Konda hakunielewa hata kidogo, akaanza kutoa maneno ya kashfa na ya udhalilishaji juu yangu, huku akisema ni tabia za vijana wengi kusingizia kuibiwa mara wanapodaiwa nauli. Nikafadhaika!
Maneno yale yalinifanya niwaze sana, nikaanza kujiuliza nikiwa msomi wa shahada moja ya elimu ya teknolojia, leo nadhalilika kwa kutokuwa na shilingi mia nne tu ya nauli? Konda yule akawa anaendelea kusisitiza kuhitaji nimlipe nauli yake. Dada mmoja kama malaika akajitokeza pasipo tarajia;...wakati nikiwa nimebakia nafikiria kumwambia konda anisaidie huku nikiwa na hofu kutokana na matamshi yake dhidi yangu, nikajikuta nadhamiria kumuomba anishushe.
Hata hivyo kabla ya kuyasema hayo, nikasikia sauti ya kike kutoka nyuma ya kiti changu ikimwambia konda akate nauli yake na yangu. Haraka niliyageuza macho yangu na nikajikuta yanagongana na ya msichana mrembo wa haja. Bahati kubwa hii? Nilijiuliza. Haraka nilimjibu "Asante" nae akaachia tabasamu machoni mwake huku akinijibu "husijali kaka", Wakati huo huo konda alikuwa anarudisha chenji kwa yule dada. Safari ikaendelea.
Nikajikuta mawazo yangu yanamkumbuka yule dada niliyemgonga pale posta, nikaanza kuhisi kuwa tukio lile lilipelekea kuibiwa pochi yangu bila kufahamu, sikumbuki ni muda gani nilibiwa lakini najua kuna mvulana alikuja na kumuuliza yule dada tatizo mahali pale. Wakati naendelea kuwaza...nikaanza kuwaza maisha yangu chuoni.
Nikawakumbuka marafiki ambao tulikuwa tukiambizana vyumbani wakati huo tukiwa hosteli kwa furaha na kupeana matarajio makubwa ya kuwa tukimaliza chuo, tutapata kazi nzuri, tutaishi maisha mazuri na hata kuwa na familia nzuri. Kila kitu kilikuwa kinakuja kama tamthiliya fulani ndani ya mawazo yangu, nikajikuta nachukia mfumo wa ajira ya nchi yangu hata mfumo wa elimu pia, elimu inayomfanya mhitimu afikirie kuajiriwa kuliko kujiajri. Walimu wetu chuoni hawatuambii ukweli hali halisi ilivyo baada ya kuhitimu elimu yetu. Nikajikuta najichukia mwenyewe badala ya walimu hao.
Nikaanza kuwakumbuka wazazi wangu waliokuwa kijijini mkoani Mbeya, wamejenga matarajio mema juu yangu,lakini ni mwaka wa pili sasa nahangaika kutafuta kazi bila mafanikio, kila mahali nilipotuma maombi yangu hakuna nilipoitwa kwa usaili. Maisha ya kuishi kwa watu yalielekea kunichosha, hata hivyo si mimi tu hata walezi wangu walianza kunichoka. Nikaanza kuchukia ni kwanini nilitumia muda wangu mwingi kusoma, kusoma kusiko na faida?
Kutokuwapo na kazi yenye kuniingizia kipato kukapelekea nimpoteze 'My Girlfriend' Binti yule wa Kimanyema niliyekuwa nafikiri ananipenda kwa dhati, kumbe alikuwa ananidanganya. Mwanamke niliyempata Chuoni, nilimpenda kweli kweli lakini baadae aliniacha kwa sababu sina pesa. Wako wapi wanaosema pesa haina umuhimu katika mapenzi?.Mnajidanganya.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nikaanza kuyakumbuka matendo yake kwangu, nyakati fulani alilia kwa ajili yangu hasa nilipomuuzi, alinihakikishia kuwa mimi ni wake na yeye ni wangu mpaka ndoa na hakuna kitakachotutenganisha. Kumbe nilikuwa napumbazwa ndani ya dimbwi la mahaba. Mahaba yaliyokuja kuniumiza baadae. Nikajikuta nikiwachukia viumbe hawa wanaoitwa wanawake. Hata hivyo, bado moyo wangu haukuepa maumivu yale.
Sauti ya konda ilinigutusha kutoka katika lindi la mawazo yale, tayari gari limewasili kituoni, kituo kilicho pembeni na uwanja wa ndege. Haraka nilishuka nikaanza kutembea. Sijui ni kitu gani kilinifanya nigeuke nyuma kabla ya kuvuka barabara. Nikajikuta nabakia na mshangao mkubwa! .Ndio! macho yangu yakakutana na binti yule mwokozi wangu, binti aliyenionea huruma na kunilipia nauli ndani ya Bus . Haraka nilimpa tena asante kwa msaada wake, binti yule akanijibu "nisijali", nilimuuliza wapi anapoelekea, alinijibu yeye ni mgeni mahali hapo na amekuja kumsubiri mgeni wake kutoka nje ya nchi, hata hivyo amewahi sana, atafika hapo masaa mawili baadae.
Binti yule aliniomba nimuoneshe mahali panapopatikana chips nzuri apate kula, ni baada ya kumwambia mimi ni mwenyeji mahali hapo. Nikachukua jukumu la kumsindikiza, nilimpeleka kwenye Cafe zilizoko pale karibu na kituo cha tax. Baada ya kufika pale nilianza kumuaga kwa minajili ya kuondoka. Binti wa ajabu alipinga uamuzi wangu, akaniomba tuwe pale tupate wote chakula na kinywaji kisha angeniruhusu kuondoka kama sitajali. Kumbuka sikuwa nimetia chochote tumboni kwa wakati huo, hakika sikujivunga.....nikavuta kiti na kukaa.
Kuwepo kwangu na binti yule mahali pale kukapelekea kutambuana, alinifahamisha kuwa anaitwa Nadia, ni sekretari wa kampuni moja ya Bima nchini na yupo pale kwa ajili ya kumpokea rafiki yake mmoja. Nilijitambulisha kwake kuwa naitwa Richard Kamba. Nilimuelezea maisha yangu kwa ufupi, hata hivyo sikuwa natambua kwanini namuelezea maisha yangu mtu nisiyemfahamu? Hata hivyo nguvu fulani iliniambia nimefanya jambo sahihi kwa wakati ule.
Baada ya muda tuliachana na binti yule, alinipa 'Bussines Card yake', akinisisitiza kuwa nikifika nyumbani nimpigie, maana simu yangu nayo ilikuwa imeibiwa kwa tukio lile la Posta. Vile vile alinipatia noti ya elfu tano, bahati ilioje? kwa dakika zile nikajikuta nasahau yote uso ukajaa tabasamu. Nilipofika nyumbani nilioga na kupata chakula nilichokikuta, kazi ya kutazama vipindi vya television ikachukua nafasi yake kama ilivyo siku zote. Hiyo ndio ilikuwa kazi kubwa nikiwa nyumbani, kushinda kwenye tv.
Baadae nilipokumbuka kumpigia simu Nadia, nikatafuta 'Bussines Card' ile bila mafanikio, sikumbuki wapi nilipoiweka, nilitafuta mwishowe nilikata tamaa. Na sikuiona tena.
Maisha ya hapo nyumbani hayakuwa yenye furaha kwa upande wangu hata kidogo, sikuwa na kazi ya kufanya na muda mwingi niliutumia kukaa sebuleni na kutazama tamthiliya za kifilipino na baadhi ya filamu za Bongo movie yalikuwa maisha yangu ya siku zote. Maisha ya mtu hasiye na kazi.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mwaka sasa, bado ningali natafuta kazi na hakuna mahali nilipowahi kuitwa hata kwenye usaili tu. Walezi wangu walianza kunichoka taratibu hapo nyumbani nilianza kufikiria kurudi kijijini, mahali walipo wazazi wangu, hata hivyo bado moyo wangu haukuwa radhi kurudi Tukuyu. Sikuweza kukata tamaa. Tukio la ajabu likatokea....
***********************
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment