Simulizi : Darkness Of Comfort (Giza Lenye Faraja)
Sehemu Ya Tatu (3)
Watu wale walikuwa wakiendelea kulifuata gari lao huku wakiwa wamembeba Richard, kitu walichokuwa wakikitaka mahali hapo ni kumpeleka sehemu mtoto huyo na kisha kumuua, hayo ndiyo yalikuwa maagizo waliyopewa na mzee Tai Peng.
Bado Richard alikuwa akipiga kelele za kuomba msamaha huku akiwataka watu wale wamuonee huruma na kumuachia lakini hakukuwa na mtu aliyeelewa, walichokuwa wakikitaka mahali hapo ni kutekeleza maagizo waliyokuwa wamepewa, hivyo tu.
Huku wakiendelea kupiga hatua kulifuata gari lao, ghafla wakaanza kusikia kelele za watu, wale watoto wa mitaani waliokuwa mahali hapo, wakageuka kuona ni kitu gani kilikuwa kikiendelea, wakashtukia wakianza kupigwa mawe mfululizo.
Hawakurusha mawe peke yake, bali kila kitu kilichoonekana kuwa ni silaha, walikitumia kuwarushia watu hao. Kadiri kelele zilivyoendelea kusikika na ndivyo ambavyo watoto hao wa mitaani pamoja na wahuni kadhaa walivyoendelea kuwasogelea huku wakiendelea kuwarushia mawe na silaha nyingine.
Walipoona kwamba kadiri walivyokuwa wakipiga hatua na ndivyo watu wale walioonekana kuwa na hasira walivyozidi kusogea, kwa kuyaokoa maisha yao, wakamuachia Richard na kuanza kukimbia.
Hiyo haikuwa sababu, japokuwa walikuwa wamemuachia mtoto huyo lakini bado walikimbizwa huku wakirushiwa mawe yao. Mpaka wanalifikia gari lao, kila mmoja alikuwa hoi, wengine walikuwa wamejeruhiwa vibaya, gari likawashwa na kuondolewa mahali hapo.
“Wale ni wakina nani?” aliuliza Shu Yan huku akimuinua Richard.
“Sijui ni wakina nani.”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Walikuwa wakitaka nini kutoka kwako?”
“Sijui Shu Yan.”
Kuanzia usiku wa siku hiyo Richard akaanza kuishi kwa wasiwasi mwingi, hakuwa mtu wa kujiachia kiholelaholela tu, kila kitu kilichokuwa kimetokea kilimtia hofu kubwa moyoni mwake.
Mpango wa kuomba mitaani kwa ajili ya kutafuta fedha za kuelekea katika Jimbo ya Yunnan haukuwepo tena kwa upande wake, Shu Yan ndiye aliyekuwa akitafuta nauli hiyo.
Baada ya wiki moja, fedha zilizokuwa zikihitajika zikapatikana na hivyo kuamua kuhama katika Jimbo hilo na kuelekea Yunnan.
Hawakuwa na ndugu yeyote yule, walikuwa wawili tu na waliahidiana kusaidia akatika kila kitu. Ndani ya treni, hawakuwa na fedha, zote walizitumia katika nauli ya kuwasafirisha kutoka Chuxiong mpaka huko Yunnan.
Japokuwa walikuwa na njaa lakini hawakuwa na cha kufanya, walikuwa wakivumilia tu mpaka pale walipoingia ndani ya jimbo hilo huku tayari wakiwa wametumia masaa manne.
Maisha mapya yakaanza huko. Shinda iliwatafuta mno na hawakuwa na kitu kingine zaidi ya kuendelea kuomba mitaani. Mtoto wa bilionea ambaye aliogelea fedha, leo hii alikuwa mtoto wa mitaani aliyeishi kwa kuombaomba tu.
Wazazi wake walikuwa wameuawa na hivyo kubaki peke yake tu. Kwa nchini China, hakuwa na ndugu yeyote, watu wengi aliokuwa akiwafahamu na ambao alijua fika kwamba walikuwa ndugu zake walikuwa nchini Tanzania tu.
Wakati mwingine alitamani kurudi katika nchi hiyo ili hata kama itatokea atakufa basi afe akiwa ndani ya nchi hiyo. Hilo halikuwa jambo jepesi kutokea, umasikini aliokuwa nao ulikuwa ni wa kupitiliza.
Mwezi mzima walikuwa ndani ya jiji hilo, alikuwa amekwishazoeana sana na Shu Yan kiasi kwamba kila alipokuwa akimwangalia, alimuona kuwa ndugu yake wa damu, tofauti ilikuwa rangi tu.
“Nataka nipambane mpaka niwe na fedha kama baba yangu,” alisema Richard.
“Kumbe baba yako alikuwa na fedha?”
“Ndiyo. Alikuwa na fedha sana, tena bilionea,” alisema Richard huku akiwa amejiinamia chini.
“Sasa kwa nini hakukuachia hizo fedha?”
“Sijui kwa nini, inaniuma sana, mimi siyo mtu wa kuzurura mitaani na kuomba msaada Shu Yan. Nilizaliwa katika familia yenye fedha sana,” alisema Richard.
“Pole sana.”
“Asante. Hivi umekwishawahi kumsikia mzee fulani anaitwa Walusanga Ndaki?” aliuliza Richard.
“Ndiyo. Ni mzee tajiri sana, alikuwa akitusaidia sana watoto wa mitaani. Alifariki mwezi uliopita, amefanya nini?” alisema Shu Yan na kuuliza swali.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ndiye baba yangu.”
“Baba yako?”
“Ndiyo.”
“Acha utani. Mzee Walusanga ni baba yako?”
“Ndiyo.”
“Sasa imekuwaje mpaka upo hapo mtoto wa bilionea?” aliuliza Shu Yan huku akionekana kupigwa na mshangao.
Hapo ndipo ambapo Richard akaanza kusimulia kila kitu kilichokuwa kimetokea katika maisha yake ya nyuma kabla wazazi wake hawajafariki. Kila alipokuwa akihadithia, Shu Yan alikuwa makini akimsikiliza tu.
Alisimulia zaidi mpaka siku ya mwisho kumuona mama yake huku baba yake akiwa hajarudi nyumbani kwao.
“Pole sana.”
Maisha ya Yunnan hayakuwa mepesi kama walivyotegemea, yalikuwa ni maisha magumu yaliyowafanya kulala siku nyingi na njaa kuliko kula. Hawakukata tamaa, bado walikuwa pamoja huku maisha ya kuombaomba mitaani ikiendelea kama kawaida yao.
Hawakuwa na pa kulala, kila siku walilala mitaani ila baada ya kukutana na binti aitwaye Lucy Liu, akawaambia kwamba hawakutakiwa kuteseka kwa kukosa pa kulala bali kulikuwa na jumba moja kubwa la ghorofa ambalo lilitengwa kwa ajili ya kuishi kwa watu wasiokuwa na nyumba.
Hawakutaka kuuliza, wakataka kupelekwa katika jumba hilo, Lucy akawapeleka na walipofika, wakaanza kupanda juu. Ndani, kulikuwa na idadi kubwa ya watoto, wengi wao walikuwa wakilala koridoni tu.
Hayo ndiyo yakawa makazi yao mapya, kila siku walipokuwa wakitoka katika mizunguko yao, walirudi mahali hapo na kulala katika korido kwa kubanana na watoto wengine.
“Ni lazima baba yako atakuwa ameacha fedha, inakupasa kujua hizo fedha zipo wapi,” alisema Shu Yan.
“Nitajuaje?”
“Sijui, ila ni lazima ujue,” alijibu Shu Yan.
Hayo ndiyo yalikuwa maneno aliyokuwa akiyazungumza Shu Yan kila siku. Alijua fika kwamba Richard alikuwa mtoto wa bilionea na hivyo hakutakiwa kuishi maisha aliyokuwa akiishi katika kipindi hicho.
Kila alipokuwa akimwangalia Richard, aliuona utajiri wa wazi machoni mwake, kijana huyo hakutakiwa kuwa hivyo kwa kuwa alitoka katika moja ya familia ya kitajiri sana.
Baada ya mwezi mmoja kumalizika, usiku wa siku moja, walipokuwa wakijiandaa kulala koridoni, Shu Yan akamvuta Richard pembeni na kuanza kuongea naye, maneno mengi aliyoyaongea siku hiyo ni kwamba ilikuwa ni lazima wamtafute wakili wa baba yake kwa kuamini kwamba mtu huyo angekuwa akifahamu mengi kuhusiana na fedha hizo.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hilo halikuwa na tatizo, kwa kuwa alikuwa akimfahamu wakili wa baba yake, akaahidi kumtafuta ili amwambie ukweli juu ya utajiri wa baba yake.
“Tukimpata huyo, basi tutakuwa tumetoka kwenye umasikini,” alisema Shu Yan.
“Kweli?”
“Ndiyo. Cha msingi tuanze kumtafuta kesho.”
“Hakuna tatizo.”
“Sawa. Ngoja niende chooni. Nikirudi tutaongea mengi mahali pa kuanzia kesho kabla ya kulala,” alisema Shu Yan.
“Sawa. Nakusubiria,” alisema Richard.
Shu Yan akainuka na kuelekea chooni huku akimuacha Richard akiwa na baadhi ya watoto wengine wa mitaani koridoni pale.
Isiku wa siku hiyo katika kipindi ambacho Shu Yan alikuwa chooni na Richard kuwa koridoni ndiyo ulikuwa usiku ambao tetemeko la ardhi likatokea na jumba hilo kuangushwa huku baadhi ya watu wakifariki dunia na mamia kujeruhiwa vibaya.
Mpaka ilipofika kesho asubuhi, bado Shu Yan hakujua Richard alikuwa wapi. Japokuwa alijitahidi sana kumtafuta lakini mahali alipokuwa kulionekana kuwa mtihani mkubwa na mgumu kupafahamu.
“Upo wapi Richard, njoo tena kwangu, hata kama umekufa, nitataka kuuona mwili wako,” alijisema Shu Yan, naye alikuwa miongoni mwa watu walionusurika katika tetemeko hilo la ardhi.
Tetemeko la ardhi linatokea katika Jimbo la Yunnan nchini China, watu wengi wanapoteza maisha na wengine kujeruhiwa baada ya majengo makubwa kuanguka. Katika tetemeko hilo, msichana wa Kichina Shu Yan anampoteza rafiki yake kipenzi mweusi, huyu anaitwa Richard.
Alijaribu kufuatilia kila sehemu kuona kwamba inawezekana akawa majeruhi, akamkosa, akajaribu kuziangalia maiti zote, napo hakuwepo, anabaki na sintofahamu.
Upande wa pili, kabla ya tukio hilo, baba yake Richard, mzee Walusanga alikuwa tajiri mkubwa nchini China, alimiliki majumba ya kifahari na biashara nyingi ambazo zilimpatia fedha kila siku.
Huku maisha yakiendelea, anatokea tajiri mwingine wa Kichina, huyu anaitwa Tai Peng. Kitu anachokitaka ni kuchukua utajiri wa mzee Walusanga, anachokifanya, anamuua yeye na mke wake, bi Diana na kisha kuanza kumtafuta Richard kwa ajili ya kumuua kwani bila kufanya hivyo aliona kwamba kungeweza kutokea tatizo lolote na hata huo utajiri wa mzee Walusanga asiupate.
Amewatuma vijana wake kumtafuta mtoto huyo ambaye hana baba wala mama lakini ameachia utajiri mkubwa, wanapofika mitaani, wanafanikiwa kumpata. Huku wakimchukua na kuanza kuondoka naye, watoto wa mitaani na wahuni wanawapiga mawe, wanamuachia na kukimbia.
Shu Yan ambaye alikuwa rafiki mkubwa wa Richard, anamshauri walihame jimbo la Chixong na kwenda Yunnan, wanakwenda huko huku lengo lao likiwa ni kutafuta maisha kwa kuombaomba mitaani.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Bwana Tai Peng alionekana kuwa na hasira, hakuamini kile kilichokuwa kikizungumzwa na vijana wake kwamba walifanikiwa kumkamata Richard lakini bahati mbaya watoto yatima na wahuni wengine wa mitaani walikuwa wakiwarushia mawe na vitu vingine vilivyowapelekea kumuacha mtaani na wao kuondoka.
Kila alipokuwa akiwaangalia watu wale, aliyauma meno yake kwa hasira, akajikuta akianza kujipapasa kiunoni, akaichukua bunduki yake na kuwamiminia risasi vijana wake.
Macho yake yalibadilika, mwili wake ulikuwa ukitetemeka kwa hasira, hakuamini kwamba mchakato wake mzima wa kumtafuta Richard na kumuua ulikuwa umeshindikana kwa mara ya pili.
Huyo ndiye alikuwa mtu pekee aliyebaki katika dunia hii na ambaye alikuwa na uhitaji wa kutumia uwezo wake wote, nguvu zake zote kuhakikisha kwamba mtoto huyo anauawa na mambo mengine kuendelea.
Huku akiwa anamfikiria Richard, kulikuwa na kitu kingine kilichokuwa kikikiumiza kichwa chake, hiki kilikuwa ni jinsi ya kuupata utajiri mkubwa aliokuwa akiumiliki marehemu mzee Walusanga.
Alihakikisha kwamba anatumia kila njia ili kujua ni kwa namna gani angeweza kupata kiasi hicho cha fedha kilichokuwa katika akaunti zake zote, kitu pekee ambacho alikiona kufaa sana kwa wakati huo ni kumuita kijana aliyekuwa mkali wa kompyuta, ambaye aliwahi kuweka historia ya kuiibia serikali ya China kiasi kikubwa cha fedha kwa kutumia kompyuta, huyu aliitwa Pin Pong.
“Siwezi kufanya kazi hiyo, nipo serikalini, wizi wa namna hiyo ni hatari kwangu,” alisema Pong mara baada ya kuitwa na bwana Tai Peng.
“Usijali. Mtu mwenye akaunti hiyo amekwishakufa, hakuna mtu yeyote anayefuatilia, ukifanikisha, nakupa dola milioni mbili,” alisema mzee Tai Peng, alionekana kuwa na uchu wa kuzitaka fedha hizo.
“Ila serikali itajua.”
“Itajuaje? Itaanza vipi kujua?”
“Kwa hiyo unasema mwenye akaunti kafariki?”
“Ndiyo.”
“Na ndugu zake?”
“Nao wamefariki.”
“Mmmh!”
“Ndiyo hivyo. Ninahitaji unisaidie kufanya hivyo.”
“Sawa. Hakuna tatizo. Kitu cha kwanza kabisa unachotakiwa kukifanya ni kuniandalia kiasi changu cha fedha kama malipo na kisha nitakufanyia hiyo kazi yako, sawa?” alisema Pong na kuuliza.
“Hakuna tatizo.”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kuhusu fedha, wala halikuwa tatizo kwa bwana Tai Peng, kwa wakati huo, kitu pekee alichokuwa akikitaka ni kupata fedha kutoka katika akaunti ya mzee Walusanga.
Hakufikiria ni kwa jinsi gani angemuacha Richard katika maisha ya kimasikini, hakujali kama Richard angeishi vipi, kitu ambacho alikuwa akikijali kwa wakati huo na ambacho kwake kilionekana kuwa muhimu ni maisha yake na ya familia yake tu.
Siku iliyofuata, asubuhi na mapema Pong alikuwa mahali hapo na alikuja na vitu vyote ambavyo alitakiwa kuvitumia siku hiyo, cha kwanza kabisa kilikuwa laptop yake.
Ujio wake ndani ya nyumba hiyo ulikuwa siri kubwa, hakutaka mtu yeyote afahamu kitu chochote kile, kwa sababu alikuwa amekwishakatazwa na serikali ya China kufanya wizi wa mtandaoni na hivyo kumpa ajira yenye malipo makubwa, hakutakiwa kujihusisha na wizi huo, kwa hiyo hata kuingia ndani ya nyumba hiyo bado ilikuwa siri kubwa.
“Ninaanza kazi, japokuwa imepita kipindi kirefu, acha niingie mzigoni,” alisema Pong na kisha kuanza kazi.
Japokuwa alikuwa akitumia kompyuta yake ndani ya sebule hiyo huku akiwa amezungukwa na watu zaidi ya saba, mbele yao kulikuwa na televisheni kubwa yenye inchi zaidi ya sitini ambayo ilikuwa imeunganishwa na kompyuta ile huku ikichukua kila kitu kilichokuwa kikiendelea katika kompyuta ile.
Bwana Tai Peng alikuwa mwenye furaha tele, kila alipokuwa amesimama mahali pale, alitamani kushangilia kwa furaha kwani ndani ya muda mfupi alikuwa akienda kuwa zaidi ya milionea.
Imani yake kubwa ilikuwa kwa Pong aliyekuwa mtaalamu wa masuala ya kompyuta ambaye alisoma mpaka kichwa kikamuuma, aliyajua masomo yote, kuanzia network, programming na mengineyo.
Kazi haikuwa ndogo, kila wakati alikuwa akikuna kichwa chake kuashiria kwamba kile alichokuwa akikifanya hakikuwa kidogo bali kilihitaji utulivu wa hali ya juu. Kitu alichokifanya ni kuingia katika Benki ya Chinesse na kisha kuingiza namba za akaunti ya mzee Walusanga.
Hapo, kompyuta ikaanza kusubiri, akaunti yake ikaja na kuanza kuingiza codes za benki hiyo, hapo napo akaanza kusubiri. Kijasho chembemba kikaanza kumtoka, moyoni mwake alikuwa akimuomba Mungu amfanikishe katika kile alichokuwa akikifanya.
Kwa bwana Tai Peng, muda wote alikuwa na presha, bado alikuwa haamini kama dakika chache zijazo, akaunti yake ingeingiza zaidi ya dola bilioni arobaini. Mwili wake ulikuwa ukitetemeka kwa furaha, kama ilivyokuwa kwa Pong, hata naye kijasho kilikuwa kikimtoka.
“Huleeeeee, nishaningia kwenye akaunti yake, ngoja isome kuna kiasi gani nikutumie,” alisema Pong kwa furaha huku mikono yake ikiwa juu, data zikaanza kujikusanya, wote walitaka kujua kulikuwa na kiasi gani ili fedha ziamishwe, yaani kwa kizungu tungesema ‘Money Transfer’
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Je nini kitaendelea?
Je mtaalamu Pong ataweza kuzihamisha fedha hizo?
Je Richard atapona?
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment