Simulizi : Darkness Of Comfort (Giza Lenye Faraja)
Sehemu Ya Pili (2)
Diana alikuwa ndani ya nyumba na mtoto wake, uso wake ulionyesha wasiwasi mwingi, halikuwa jambo la kawaida kwa mumewe kumpigia simu na kutokupokea, na kama kuna siku kitu kama hicho kilitokea, basi alikuwa akimtaarifu kwa njia ya meseji kwamba alikuwa kwenye kikao au sehemu yoyote ile.
Siku hiyo ilikuwa ni ya tofauti sana, alikuwa mtu mwenye mawazo, kila kitu kilichokuwa kikiendelea kilimtia wasiwasi mno. Maswali hayakuisha kichwani mwake, hakujua mumewe alikuwa wapi, kitendo cha simu yake kuita mpaka kukata, kilimtoa amani kabisa.
Ingawa ilikuwa ni usiku sana lakini hakupata hata lepe la usingizi, kila alipojigeuza huku na kule, kichwa chake kilikuwa kikimfikiria mume wake tu. Alipoona kwamba ameshindwa kabisa kulala, akatoka nje ya chumba chake na kuelekea sebuleni, huko, bado aliendelea kuwa na mawazo lukuki.
“Jamani, naomba unipigie simu mume wangu uupoze moyo wangu,” alisema Diana huku akiiangalia simu yake.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hakukuwa na kitu kilichobadilika, bado hali iliendelea kuwa vilevile. Ilipofika saa nane usiku, mara akasikia minong’ono ya watu nje ya nyumba yake, akashikwa na wasiwasi lakini hata kabla hajachukua uamuzi wowote ule, akafungua pazia na kuchungulia nje. Hakuona mtu.
Moyo wake haukuwa na amani hata kidogo, tayari akahisi kwamba kulikuwa na kitu kilichotaka kutokea, alichokifanya ni kuelekea chumbani kwa mtoto wake, Richard, alikuwa amelala fofofo.
Akamsogelea kitandani pale na kukaa karibu yake. Mapigo yake ya moyo yalikuwa yakidunda mno.
Baada ya dakika ishirini, akasikia mlio wa risasi, akashtuka, Richard aliyekuwa amelala, akaamka na kushangaa kumuona mama yake akiwa pembeni yake.
“Kuna nini mama?” aliuliza Richard.
“Sijui kuna nini, amka,” alisema bi Diana.
“Baba yupo wapi?”
“Hajarudi.”
“Hajarudi?”
“Ndiyo. Njoo huku,” alisema bi Diana na kumvuta mtoto wake mpaka chooni.
Chooni kulionekana kuwa pa kawaida sana lakini kulikuwa kumetengezwa shimo kwa siri ambalo juu yake lilifunikwa na bati gumu. Halikuwa jambo jepesi kugundua kwamba ndani ya choo hicho kulikuwa na shimo, hata Richard mwenyewe, siku hiyo alikiona kitu hicho kuwa kigeni.
“Mama, kuna nini?” aliuliza Richard wakati mama yake akilitoa bati hilo gumu lililoendana na sakafu.
“Ingia humu.”
“Mama. Niambie kwanza kuna nini.”
“Ingia tu.”
Richard hakuwa na jinsi, kwa sababu aliambiwa aingie, akaingia, akashuka ngazi mpaka chini na mama yake kubaki juu huku akiwa amelirudishia bati lile.
Hapo, kidogo moyo wake ukapata ahueni, kitendo cha kuona kwamba mtoto wake alikuwa sehemu salama kikamuondolea asilimia kadhaa za hofu moyoni mwake.
Wala hazikupita dakika nyingi, mlango ukafunguliwa watu wanne waliokuwa na bunduki kuingia ndani huku wakiongozana na mmoja wa walinzi, bi Diana akajua fika kwamba kidole cha mlinzi ndicho kilichotumika kuufungua mlango huo uliokuwa ukifungwa kwa mashine maalumu mpaka mtu uweke alama ya kidole.
“Hebu twende huku,” alisema jamaa mmoja, sura yake ilikuwa imefichwa na kinyago.
Bi Diana alikuwa akitetemeka kwa hofu, kijasho chembamba kikaanza kumtoka, kila alipokuwa akiwaangalia watu wale, hawakuonekana kuwa na huruma. Wakamchukua na kuanza kuondoka naye mahali hapo.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nje, walinzi wote waliokuwa wakilinda mahali hapo walikuwa chini, damu zilikuwa zikiwatoka, walikuwa wamekufa baada ya kupigwa risasi za kichwa na kifua, kwa jinsi picha ilivyokuwa ikionekana mahali pale, bi Diana alibaki akilia tu.
Njiani, bi Diana alikuwa akiomba msamaha tu lakini hakukuwa na mtu yeyote aliyemuelewa. Gari liliendeshwa kwa mwendo wa kasi mpaka katika sehemu ambayo ilikuwa na kipori fulani na kisha kuteremshwa.
Bado alikuwa na wasiwasi mwingi. Aliposhikwa mkono na kupelekwa kule alipotakiwa kwenda, akamuona mume wake akiwa chini, damu zilikuwa zikimtoka, akashindwa kuvumilia, akaanza kumsogelea, alipomfikia, akamkumbatia na kuanza kulia naye.
“Mume wangu, mume wangu, kuna nini?” aliuliza bi Diana huku akianza kububujikwa na machozi.
Bwana Walusanga hakuweza kuongea, alibaki akigunaguna tu kwa maumivu makali. Uso wake ulikuwa umevimba, damu ziliendelea kumtoka, alitia huruma mahali pale alipokuwa.
Huku wakiwa wamekumbatiana, wakasikia maagizo yakitolewa kwamba hata mtoto wao, Richard alikuwa akihitajika mahali hapo kwa ajili ya kufanya kazi ambayo ilikuwa imebakia.
Wakashtuka, wakabaki wakilia tu huku wakiwa wamekumbatiana, hawakuamini kama mwisho wa kila kitu ungekuwa namna hiyo. Wakati mwingine walikuwa wakijuta kuwa nchini China, ni heri wangekuwa nchini Tanzania, hata kama wangeuawa, basi wangeuawa ndani ya nchi yao.
“Tumuombe Mungu wasimpate Richard,” alisema bi Diana huku akiwa hana uhakika kama Richard hatoweza kupatikana.
****
Wanaume watatu wakarudi ndani ya nyumba hiyo, ilikuwa ni saa tisa usiku na hakukuwa na mtu yeyote aliyekuwa akifahamu kile kilichokuwa kimeendelea ndani ya nyumba hiyo. Walichokifanya ni kuzama ndani na kisha kuanza upekuzi wao.
Walianza na vyumbani, kote huko, Richard hakupatikana, hawakuishia hapo, walikwenda jikoni na kufungua makabati yote lakini hakukuwa na mtu yeyote zaidi ya wafanyakazi wa ndani waliokuwa wamewafunga kamba.
“Richard yupo wapi?” aliuliza jamaa mmoja huku akionekana kuwa na hasira.
“Hatujui yupo wapi,” alijibu mfanyakazi mmoja.
“Mnamfichaeee, nitawapiga risasi.”
“Kweli tena hatujui.”
Wanaume wale hawakutaka kuishia hapo, walichokifanya ni kuendelea kumtafuta Richard ndani ya nyumba hiyo. Walimtafuta mpaka inafika saa kumi na moja alfajiri lakini hawakuweza kumpata, walichokifanya ni kuondoka zao. Hawakujua kama Richard alikuwa katika shimo lililokuwa bafuni.
****CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Richard alikuwa akitetemeka kupita kawaida, bado aliendelea kushangaa kwa sababu gani mama yake alikuwa amemuingiza ndani ya shimo lile huku baba yake akiwa hajarudi nyumbani hapo japokuwa ilikuwa usiku mzito.
Alibaki shimoni mule huku kichwa chake kikijaza maswali mengi yasiyokuwa na majibu. Baada ya dakika kadhaa, akasikia sauti za watu, mama yake akaanza kulia, tayari akajua kwamba kulikuwa na hatari, hivyo akasogea karibu zaidi ili aweze kusikia vizuri.
Mara kwa mara mlango wa chumbani ulikuwa ukifunguliwa na kufungwa huku sauti za watu wale zikiendelea kusikika, alichokifanya ni kuondoka mahali hapo.
Huku machozi yakimbubujika mashavuni mwake, Richard akaanza kupiga hatua ndani ya bomba lile, kulikuwa na giza totoro lakini hakuonekana kujali, hakujua bomba lile lilipoishia, kitu alichokuwa akikitaka ni kujiona akiwa amefika sehemu salama tu.
Maji machafu yalikuwa yakipita kuelekea mbele kabisa huku sauti za panya zikisikika katika shimo hilo. Mwili wake ulikuwa ukitetemeka lakini hakuwa radhi kurudi nyuma kwani tayari alijua kwamba hali ya amani haikuwa salama nyumbani.
Baada ya dakika kadhaa, akaanza kusikia sauti ya mawimbi, hapo akajua kwamba tayari alikuwa amefika baharini. Akaongeza kasi yake ya kutembea, akatokea katika bahari ya Sicbuan. Hapo ndipo safari yake ndefu maishani mwake ilipoanza, akaanza kukimbia pembezoni mwa bahari, alipoelekea, hakupafahamu, ila alijua kwamba alikuwa baharini, machozi yaliendelea kumtoka lakini hakusimama, alikuwa akiyaokoa maisha yake.
***
Vijana wakarudi kwa bosi wao, japokuwa walikuwa wameagizwa kurudi mahali hapo pamoja na mtoto, hawakuwa naye. Bwana Tai Peng alionekana kukasirika, hakuamini pale alipoambiwa kwamba mtoto Richard hakuwa amepatikana.
Huyo ndiye alikuwa mtu muhimu sana, aliamini kwamba endapo angemuua bwana Walusanga na mke wake, bi Diana bado isingekuwa imejitosheleza kwa sababu kulikuwa na mtu mwingine aliyebaki.
“Mmemkosa vipi?” aliuliza bwana Tai Peng huku akionekana kukasirika.
“Hatujui mkuu.”
“Mlitafuta vyumba vyote?”
“Ndiyo. Lakini tukamkosa.”
“Aagghh! Watatuambia ukweli tu,” alisema bwana Tai Peng.
Bwana Tai Peng akayarudisha macho yake kwa bi Diana, alikuwa akilia huku akiwa amemkumbatia mume wake kipenzi aliyekuwa hajiwezi. Bwana Tai Peng akamchukua bi Diana na kumsimamisha, akaanza kumwangalia usoni, akachukua bunduki yake na kumuelekezea bwana Walusanga.
“Una dakika moja tu ya kutuambia mtoto wako yupo wapi,” alisema bwana Tai Peng huku akiwa amemuelekezea bunduki bwana Walusanga.
Bi Diana hakusema kitu, alikuwa akilia tu. Alimpenda sana mtoto wake, hakutaka kuona akiuawa na wakati alikuwepo. Japokuwa mumewe alikuwa ameelekezewa bunduki na njia mojawapo ya kumuokoa ilikuwa ni kusema ukweli mahali mtoto Richard alipokuwa lakini hakutaka kuwa muwazi.
“Una sekunde thelathini za kutuambia mahali alipokuwa mtoto,” alisema bwana Tai Peng huku akiikoki bunduki yake.
Bi Diana alikuwa akilia tu. Ingawa alikuwa akimpenda sana mtoto wake lakini pia alimpenda mno mume wake. Hakutaka kuona akiuawa, kila alipotaka kusema ukweli mahali mtoto wake alipokuwa, alinyamaza.
“Paaaaaaa,” ulisikika mlio wa risasi, bwana Walusanga alikuwa akipiga kelele huku risasi ile ikiwa imepenya mguuni mwake na kuutoboa mfupa.
Maumivu aliyoyasikia bi Diana moyoni mwake yalikuwa ni zaidi ya maumivu ya mguu aliyoyasikia bwana Walusanga. Uso wake ukabadilika, akashikwa na hasira, akatamani kumrukia bwana Tai Peng, amkabe na kumuua.
“Una sekunde kumi nyingine, tuambie mtoto alipo,” alisema bwana Tai Peng huku akiwa ameielekezea bunduki katika mguu mwingine wa mzee Walusanga.
“Usiwaambie, kama kuniua waache waniue, usiwaambie,” alisema bwana Walusanga kwa maumivu mkali.
Kama alivyoambiwa na mume wake ndivyo alivyofanya, hakutaka kueleza ukweli mahali alipokuwa mtoto wake. Bwana Walusanga aliendelea kumiminiwa risasi mahali pale, ilipotoka miguu, ikahamia mikono na mwisho kummalizia risasi ya kichwa lakini bado bi Diana hakuthubutu kuzungumza ukweli japokuwa alitamani kufanya hivyo.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Bado na wewe. Tuambie mtoto wako yupo wapi.” Alisema bwana Tai Peng huku akiwa amemnyooshea bi Diana bunduki ile.
“Una sekunde thelathini tu,” aliongezea bwana Tai Peng.
Ulikuwa ni usiku sana lakini Richard hakutaka kusimama, alikuwa akiendelea kusonga mbele pembezoni mwa bahari ile. Upepo mkali bado uliendelea kuvuma huku kukiwa na giza totoro.
Hakukuwa na mtu yeyote ufukweni hivyo hakuweza kusimama, aliendelea kwenda mbele zaidi na baada ya dakika kadhaa, kwa mbali akawaona watu waliokuwa wamewasha moto huku wakiwa pembeni wakiota moto ule.
Wakati akiendelea kupiga hatua kuwafuata watu wale, mawazo yake yakaanza kurudi nyuma katika kipindi ambacho mama yake alimwambia aingie ndani ya shimo nay eye kubaki juu. Kichwa chake kilikuwa na maswali yasiyokuwa na majibu, kwa nini alimuingiza shimoni na watu wale waliofika mahali pale walikuwa wakina nani, kila alipojiuliza, alikosa jibu.
Alipowafikia watu wale, wote wakashtuka, haikuwa kawaida kumuona mtu ufukweni hapo tena usiku kama huo, walichokifanya ni kumuita na kuanza kumuuliza maswali machache.
“Unatoka wapi?” aliuliza mwanaume mmoja.
“Nimetoka kule,” alijibu Richard huku akiinyoonyeshea kidole nyia aliyotokea.
“Umefikaje hapa?”
“Nilikuwa nakimbia.”
“Unakimbia nini?”
Richard hakujibu swali hilo, akaanza kumkumbuka mama yake na machozi kuanza kumbubujika mashavuni mwake. Watu wale wakabaki wakimshangaa, wakamwambia wamsogelee zaidi na hapo ndipo Richard akaanza kuwahadithia.
“Nililetwa huku na mjomba wangu, aliniambia kwamba kulikuwa na sherehe ya watoto huku ufukweni, tulipofika kule, kuna watu wakanifuata na kunichukua, walinipeleka kule kwenye majani kwa lengo la kuniua,” alisema Richard, kila alichokuwa akikizungumza, kilikuwa ni uongo.
“Ikawaje?”
“Nikafanikiwa kuwatoroka.”
“Wapo wapi? Bado wapo kule?”
“Sijajua.”
“Hebu twende tukawaangalie,” alisema mwanaume mmoja, akasimama, akachukua bunduki iliyokuwa pembeni yake.
Kama alivyofanya, na wenzake wakafanya vilevile, nao wakasimama na kuchukua bunduki zao na kumtaka Richard awapeleke kule aliposema kwamba kulikuwa na watu waliokuwa wakitaka kumuua.
Richard akabaki akitetemeka, hakujua kama wale watu aliokuwa akiwaambia hivyo walikuwa wanajeshi, alichokifanya, akajitoa hofu na kuanza kuondoka nao kuelekea huko, walipofika, hakukuwa na mtu.
“Watakuwa wametoroka tu. Mjomba wako yupo wapi?” alisema mwanaume mmoja na kuuliza.
“Sijui, sijajua kama wamemuua au vipi,” alisema Richard.
Kitu alichokihitaji mahali hapo ni msaada tu, akawaambia watu hao na wao kumuongoza mpaka nje kabisa huku wakisema kwamba ule ufukwe ulikuwa ni wa kijeshi na hivyo hakukutakiwa kuonekana mtu yeyote ambaye hakuwa mwanajeshi.
Alipofikishwa barabarani, Richard akaondoka huku akipita pembezoni mwa barabara. ALitembea kwa muda wa dakika arobaini na tano, kwa mbali, mbele yake akauona moto ukiwa umewashwa, akaanza kuusogelea, alipofika eneo lile, kulikuwa na watoto wengi waliokuwa wamelala huku mapipa yakiwa yamesimamishwa, hayo ndiyo yaliyokuwa yamewashwa moto.
Alipofika eneo hilo, Richard akanyata na kwenda sehemu kulipokuwa na maboksi na kisha kukaa hapo.
Machozi hayakukoma machoni mwake, bado yaliendelea kumbubujika mfululizo, kila wakati alikuwa mtu wa majonzi tu, kumbukumbu za kile kilichokuwa kimetokea bado kilimuumiza kwa kuona kwamba ni lazima kulikuwa na kitu kibaya kwani hakikuwa kitu cha kawaida kwa mama yake kumwambia aingie shimoni.
“Kuna kitu, ila ni nini na kwa nini hata baba hakurudi nyumbani?” alijiuliza Richard.
Hicho kilikuwa kitu kingine ambacho kiliuumiza moyo wake. Siku zote baba yake alikuwa akiwahi kurudi nyumbani lakini siku hiyo ilikuwa tofauti kabisa, baba yake alikuwa amechelewa kurudi tofauti na siku nyingine.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Siku hiyo kila kitu kilionekana kuwa tofauti kabisa kwake. Matukio yote yaliyokuwa yametokea yaliacha maswali mengi yasiyokuwa na majibu kichwani mwake.
Mtoto wa kitajiri, usikuwa wa leo alikuwa katika kundi la watoto wa mitaani, shida ambazo alikuwa akizisikia, leo alikuwa akijionea mwenyewe. Alimuomba Mungu amuepushe na vitu vibaya vyote ambavyo vingeweza kutokea maishani mwake na mwisho wa siku amruhusu kukutana tena na wazazi wake, kila alichokuwa akikiomba, kilionekana kuwa kama muujiza kutokea.
Usiku huo alikaa hapo na hakutaka kuondoka. Mawazo yake bado yalikuwa yakiwafikiria wazazi wake tu. Asubuhi ya siku inayofuata ilipofika, kila mtoto wa mtaani aliyekuwa akimwangalia Richard alibaki akimshangaa.
Hakuonekana kuwa kama wao, hakuonekana kuwa na maisha magumu kama waliyokuwa wakiishi. Hakukuwa na mtu aliyemsogelea, kila mmoja alikuwa akimuogopa.
Mtu pekee ambaye alipata ujasiri wa kumsogelea alikuwa msichana ambaye alijitambulisha kwa jina la Shu Yan. Alipomuona Richard amekaa kiunyonge, akapiga hatua na kumfuata, alipomfikia, akaanza kuzungumza naye.
Richard hakuonekana kuwa kwenye hali ya kawaida, alikuwa mkimya na mwenye huzuni tele, kwa Shu Yan ilikuwa ngumu sana lakini mwisho wa siku, Richard akaufumbua mdomo wake.
“Ninaitwa Richard,” alijibu Richard.
Wakaanza kuzungumza kwa kirefu, muda wote, Shu Yan alionekana kujifikiria kitu, maswali kibao yalikuwa yakimiminika kichwani mwake juu ya kijana huyo. Hakuonekana kuwa kama watoto wengine, alikuwa tofauti kabisa.
Hiyo ndiyo ikawa siku ya kwanza kwa Richard kuanza maisha yake mitaani. Baada ya siku mbili, akaziona taarifa kwenye magazeti kwamba baba na mama yake walikuwa wameuawa na miili yao kutupwa ufukweni.
Ilikuwa taarifa mbaya kwake, alijitahidi kuyazuia machozi yasimtoke lakini mwisho wa siku akashindwa, akajikuta akianza kububujikwa na machozi huku moyo wake ukiwa kwenye maumivu makali.
“Mbona unalia?” aliuliza Shu Yan.
“Hakuna kitu. Ninasikitika sana kujiona nikiteseka mtaani, hivi ni lini na sisi tutakuwa na fedha?” aliuliza Richard huku akijitahidi kuuficha ukweli.
“Usijali, tuendelee kuomba tu. Ila naomba tubadili sehemu,” alisema Shu Yan.
“Tubadili sehemu! Kivipi?”
“Twende mji mwingine kabisa.”
“Mji gani?”
“Tuondoke hapa tuelekee Chuxiong na tuelekee Yunnan, nadhani huko tutafanikiwa zaidi kwani hapa kuna watoto yatima wengi,” alisema Shu Yan.
“Tutafikaje huko?”
“Tuombe kwa wiki hii, baada ya hapo, tutapata nauli na kuelekea huko,” alisema Shu Yan.
“Sawa.”
Walikuwa ni marafiki wawili waliokuwa wamezoeana sana, kila sehemu mmoja alipokuwa na mwenzake alikuwa mahali hapo. Walilala pamoja huku wakiomba pamoja mitaani.
Ukaribu wao ukawashangaza watu wengi, halikuwa jambo rahisi kumkuta Mchina akiwa karibu na mtu mwenye ngozi nyeusi kama walivyokuwa wawili hao. Ukaribu wao ukaanzisha maswali mengi lakini hawakuonekana kujali.
Japokuwa baadhi ya maeneo kulikuwa na ubaguzi mkubwa wa rangi lakini hiyo haikufanya wawili hao kuachana, kila walipokuwa waliendelea kuwa pamoja.
“Hivi wazazi wako wapo wapi?” aliuliza Richard.
“Mpaka sasa hivi sijajua, nilipata taarifa kwamba nilitupwa mtaani, niliokotwa na kupelekwa katika kituo cha watoto yatima, baadae nikatoroka,” alijibu Shu Yan.
“Kwa nini ulitoroka?”
“Nilitaka kuwa huru, nilitamani kuwa na fedha zangu, hicho ndicho kilichonifanya nitoroke,” alijibu Shu Yan.
Siku hiyo waliendelea kuulizana maswali mpaka ilipofika saa sita usiku, wakalala katika maboksi kama kawaida yao.
“Usiku mwema.”
“Nawe pia.”
Usiku huo hukuwa wa kawaida, ilipofika saa nane, minong’ono ya watu fulani ikaanza kusikika mahali hapo. Richard akayafumbua macho yake, wanaume wanne walikuwa wamesimama mbele yake huku wakiulizana maswali.
Mapigo ya moyo wa Richard ukaanza kudunda kwa nguvu, ghafla, wakamvamia na kumnyanyua juujuu, Richard akaanza kupiga kelele. Watu wale hawakujali, waliendelea kumbeba na kuanza kuelekea naye sehemu ambayo walipaki gari, walikuwa ni vijana kutoka kwa bwana Tai Peng, walikuwa wametumwa kumchukua Richard na kisha kumuua kama wazazi wake.
****
“Paaaaa…..” mlio wa risasi ukasikika mahali hapo, bi Diana akaanguka chini na kufariki dunia.
Bwana Tai Peng akaichukua bunduki yake na kuanza kuifutafuta, hilo ndilo lilikuwa lengo lake, kitu alichokuwa akikitaka ni kuwaua watu hao na mwisho wa siku kujichukulia fedha zake.
Mtu pekee ambaye alikuwa akikisumbua kichwa chake kwa wakati huo alikuwa Richard tu. Alichokifanya ni kuwaagiza vijana wake ili waende kumtafuta mtoto huyo, popote ambapo wangemkuta ilikuwa ni lazima wamuue nay eye kupelekewa mwili tu.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Popote mtakapompata, muueni na mniletee mwili wake tu,” alisema bwana Shu Yan kwa hasira.
Vijana hao wakaondoka na kuelekea mitaani, huko, walikuwa na kazi moja ya kumtafuta Richard tu. Halikuwa jambo jepesi kwao, walijitahidi kuzunguka kila kona lakini hawakuweza kumpata.
“Tufanye nini?” jamaa mmoja alimuuliza mwenzake.
“Sijiu. Ila tuendelee kumtafuta. Ni lazima tumpate na lazima tumuue,” alisema kijana mwingine.
Hawakukata tamaa, waliendelea kumtafuta zaidi. Kadri walivyozidi kuzunguka huku na kule wakimtafuta na kumkosa na ndipo hasirza zao zilizidi kuongezeka zaidi. Kwa kuwa Richard alikuwa mtoto mweusi, hapo ndipo walipoanza kuulizia.
Hakukuwa na mtu aliyekuwa akimfahamu, kwa kila mtu aliyeulizwa, alisema kwamba hakuwa akimfahamu mtoto huyo. Baada ya kusumbuka kwa wiki nzima ndipo walipokuja kusikia tetesi kwamba kulikuwa na mtoto mweusi ambaye naye alijiunga na kundi la watoto wa mitaani ambao kazi yao kubwa ilikuwa ni kuombaoba tu.
“Twendeni huko,” alisema jamaa mmoja, wakachukua gari na kuanza kuelekea huko.
Walipofika, wakalipaki gari lao kwa mbali, wakaweza kumuona Richard akiwa na msichana mmoja wa Kichina huku wakipiga stori tu. Kutokana na wingi mkubwa wa watu, hawakutaaka kumfuata, bali walisubiri mpaka giza litakapoingia na ndipo wamfuate.
Baada ya masaa mawili, giza likaanza kuingia, bado hawakuona kama huo ulikuwa muda sahihi wa kumfuata mtoto huyo, ilipofika usiku wa manane, wakaandaa bunduki zao na kuanza kumfuata huku wakionekana kuwa makini sana.
Walipomfikia, wakamvamia, wakambeba juujuu na kuanza kuondoka naye kuelekea ndani ya gari. Hakukuwa na mtu aliyejua, ila kelele za Richard ndizo zilizowafanya watu wengine kushtuka kutoka usingizini, walipoangalia, mtoto huyo alikuwa amebebwa juujuu na watu waliokuwa wamevalia suti, walikuwa wakilifuata gari lao.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Je nini kitaendelea?
Je Richard atauawa?
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment