Simulizi : Ndoto Za Kipepeo
Sehemu Ya Tano (5)
“Sakarani mkubwa! Funga bakuli lako,” Oli alifoka baada ya kumkabidhi mkewe konde zito kati ya shavu na jicho. Mama Tora maumivu yalimpata na kulifanya jicho kuvimba. Aliufunga mdomo angali Oli naye aliivuta shuka na kulala. Alimwacha mkewe akiugulia.
Asubuhi iliyofuata, Carolina aliamka. Alifanya usafi kila mahali alipotazamiwa kufanya na kuandaa chai. Hadi anamaliza kumchemshia maji mama Tora, alikuwa bado hajamtia machoni. Oli ndiye alikuwa wa kwanza kuamka tofauti na mazoea yaliyokuwepo. Oli alipoondoka Carolina ilimpasa kumsemesha mama yake.
“Mama, mbona huamki?” aliita Carolina na kuhoji.
“Naamka mwanangu. Nipelekee maji bafuni nioge ili niende hospitalini.”
“Maji yapo tayari mama. Nilikuwa nakungoja wewe tu.”
“Haya nakuja,” alisema mama Tora. Alinyanyuka kitandani na kujivuta akielekea bafuni. Wakati akitoka mlangoni Carolina alimtazama na kustaajabu.
“Mama! Umefanya nini?”
“Nilijigonga ukutani wakati nikiwa nataka kwenda msalani usiku. Unajua umeme ulikuwa umekatika,” mama Tora alimdanganya Carolina. Kwa kuwa alizisikia vurumai usiku, alijiongeza.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Pole mama. Labda sasa nikuchemshie maji mengine ili upakanyage hapo kwa maji ya moto,” alisema Carolina.
“Asante mwanangu. Naomba nikimaliza kuoga unisindikize mahali.”
V
“Wapi? Hospitalini?”
“Hapana. Wewe jua utanisindikiza mahali. Uelekeo utaujua hukohuko mbele ya safari,” alieleza mama Tora.
“Haya, ngoja nimwandalie Tora na baba chai ingali bado mapema,” alisema Carolina. Aliharakisha kuandaa chai nakuiweka mezani. Alikitwaa kikombe naye alijipatia chai kukifungua kinywa chake. Vile vile mama Tora alipomaliza kuoga alipata chai yake kadri alivyojisikia.
****
Roy alitoka kijijini Tuamoyo kama alivyokuwa amekusudia. Alikuwa na muda tangu awasili tena Tumaini ambako maisha yake yalimchukua. Muda huo alikuwa na mambo mawili fikrani mwake; aliwaza namna ya kumpata Carolina na hapohapo aliwaza kama maombi yake ya kujiunga na jeshi la polisi yangeweza kukubalika. Kwa kuwa alikuwa na muda wa kutosha, maneno yote aliyosimuliwa na mzee Majaliwa kule kijijini alikusudia kuyafanyia kazi. Ilimpasa kuunganisha jambo moja juu ya jingine ndipo angebaini kule Carolina alikuwa. Ilikuwa ni wakati mzuri wa kumtafuta Carolina.
Kwa kuwa mji wa Tumaini ulikuwa mkubwa na ulijaa kila aina ya watu, halikuwa jambo jepesi kumtafuta mtu na kumpata kadri ya matamanio. Mji wa Tumaini ulikuwa si wa kutafutana kwa wepesi. Watu hawakufahamiana hata kama walikaa mtaa mmoja. Kila mmoja alikuwa na hamsini zake kadri maisha yalivyomwelekeza kufanya. Vilevile Roy wakati akiendelea na mpango wa kumsaka Carolina aliendelea na kibarua alichokuwa akikifanya. Kwani baada ya kuhitimu masomo ya kidato cha nne, alianza kuchukua bidhaa madukani na kuzisambaza kama mchuuzi aliyeenda kila kona ya mji akitafuta wateja. Kazi ile ilimfanya akutane na kuonana na watu wengi. Mji mzima wa Tumaini aliugonga mihuri kwa nyayo zake akijitafutia riziki. Maisha yake hayakuwa haba maana mwenda bure si mkaa bure bali huenda akiokota.
Kila hatua aliyoipiga ilikuwa ni kujitafutia riziki na kumtafuta Carolina. Alipoenda sokoni alijitahidi kuangaza akimtafuta mama mwenye sifa zile ambazo alitajiwa na mzee Majaliwa kule kijijini. Akilini aliwaza, siku akimkuta mama mnene, mweupe mwenye kidani puani, basi ingekuwa mwanzo wa kumpeleleza. Haja yake ilikuwa moja tu, ni kumkuta akiwa katika kibanda cha matunda hasa maembe. Safari yake kila wakati kukatiza na kuvizunguka vibanda havikumkutanisha na mama wa namna ile.
Achilia mbali niaye kutaka kuliona japo lile gari aina ya Pajero, nayo haikumsaidia. Magari aina ya Pajero pale mjini yalikuwa mengi kwa idadi. Asingeweza kumparamia kila mtu ambaye alikuwemo ndani ya magari yale akiwa na lengo tu la kujua kule aliko Carolina. Lilikuwa jambo gumu.
Fikra zake zilikuwa zikimzidishia mkanganyiko wa njia sahihi ya kufuata. Ni kweli alikuwa kapewa majina mawili ya mahali ambako kulihisiwa ndiko makazi ya kudumu ya waliomchukua Carolina. Majengo na Ushirika ndiyo majina ambayo alitembea nayo Roy akilini. Mizunguko ya biashara zake ilimfikisha kote, si Majengo wala Ushirika, kote alifika tena kwa kurudiarudia. Kilichomtatiza ni kukutana na majumba yaliyozungushiwa kuta ndefu ambapo haikuwa rahisi kujua wamiliki wake. Kazi aliyoiingia ilimhitaji kuwa mpelelelezi mweledi kuweza kuupata ukweli.
Upande wa Carolina na mama yake uliwachukua kuipa kisogo nyumba yao. Mama Tora alitangulia wakati Carolina alifuata kwa nyuma. Walivaa nguo ndefu zilizofunika miili yao kutoka unyayoni hadi unywele kichwani. Kilichokuwa kikionekana ni uso na macho pekee. Walikatiza mtaa baada ya mtaa. Watu waliokuwa nje ya majumba yao wengi hawakuacha kuwashangaa punde tu walipotoka ndani.
“Watu wa mtaa huu huwa nawashangaa, pamoja na kuweka kuta kwenye majumba yao, bado hutoka nje nakujianika kwa umbea. Hata huwa sielewi kwa nini waliweka kuta za kuwasitiri,” alisema mama Tora.
“Ni kawaida mama. Mimi nadhani kuta ni kwa ajili ya usalama tu. Mengine ambayo ni asili ya watu hayamzuii mtu kutoka nje,” alijibu Carolina.
“Usalama wa wapi? Nani aliwaambia kuna vita nchi hii hadi wajikinge kwa kuta ndefu. Kama kifo kipo palepale, kikifika hakuna atakayekwepa. Kama tabia yenyewe hutembea na mtu, haiwezi kubadilishwa kwa ukuta,” aliongeza mama Tora.
“Kwani mama wewe unadhani kuta ziliwekwa kwa nini?” alihoji Carolina.
“Kuficha maovu tu ya walimwengu. Pia ni ubinafsi unaowasumbua watu wa mji huu. Wanadhani kuna mtu atawaendea na kuwaomba. Ukiweka ukuta ina maana hutaki nduguyo hata jamaa yako akuone wala afike kwako. Uchoyo huo. Kama si hivyo basi kuna mambo ambayo wanayaficha. Kinachonishangaza, unakuta mtu kajenga nyumba yake nzuri ya kuvutia tena ya kifahari, lakini ukuta mrefu umeificha. Nini maana yake?” alisema mama Tora.
“Tumanini karibu kote watu wenye kipato naona wanaishi hivi,” alisema Carolina.
“Kwanza hata baba yako hapo nyumbani huwa namwambia kila siku, vunja ukuta tujuane na watu. Kuta ndefu kama gereza unadhani kuna ujamaa tena namna hii, hakuna. Kila mtu na ukuta wake kajitenga na jirani. Lini mtafahamiana kama si uhayawani,” alisema mama Tora.
“Ndivyo ilivyo mama. Wakati wa ukuta, siku kutakuja mtindo mwingine nao hautakuwa na jema. Kila jambo kwa binadamu linao wakati wake.”
“Kweli mwanangu. Sasa nakupeleka ambako hujawahi kufika. Huko tutazungumza kwa faragha maana nisipokuambia leo basi ujue hakuna siku tena utayasikia hayo kutoka kwangu,” alisema mama Tora.
“Mama, kwani wapi huko tuendako?”
“Nitakujibu tukifika. Nimeamua twende kwa miguu ili uweze kupakumbuka wakati ukiwa peke yako,” alisema mama Tora. Walitembea kwa muda mrefu kidogo hadi walifika sehemu ambayo walikuwa wakielekea. Moja kwa moja mama Tora na Carolina walifika kwenye nyumba ambayo ilikuwa na chumba kimoja na sebule. Mama Tora aliufungua mlango na kuingia ndani. Carolina alibaki kustaajabu kuona yaliyokuwa yakiendelea. Aliingia ndani na kumkuta mama Tora akiwa kaketi kwenye kochi. Alipoketi Carolina alibaki kimya akiangaza macho yake kila upande. Nia yake ilikuwa ni kuona japo mtu ambaye alikuwa maeneo yale. Hakumwona mtu!
“Carolina mwanangu, karibu.”
“Asante mama. kwani hapa pia ni kwenu?”
“Hapana. Hapa ni kwangu na si kwetu. Labda kwetu mimi na wewe?” alieleza mama Tora.
“Una maana gani kusema hivyo?”
“Naomba nisikilize kwa makini. Nitakayokueleza hapa uyatie akilini mwako na kamwe usije kwenda kinyume na ninachokueleza. Naamini wewe ni binti unayejitambua na unaelewa jinsi ya kutimiza ndoto zako,” alisema mama Tora.
“Ndiyo mama, nakusikiliza,”
“Sawa. Hiki kijumba ni mali yangu. Nilijenga kwa nguvu zangu wakati nikiwa bado naponda kokoto na mama yangu. Baada ya mama yangu kufariki na mimi kupata mchumba, nililazimika kukiacha. Nilimkabidhi kijana mmoja aishi hapa ambaye naye Mungu kamjalia kapata kwake. Ameshajenga na kuoa. Sasa! Tangu aondoke hapa sikuwa nimepata mtu wa kumkabidhi. Baada ya kutafakari sana, hatimaye niliyakumbuka maneno ya marehemu mama yangu. Alisema; nyumba hii kwa kuwa nilimjengea yeye isije ikaenda mikononi mwa mtu ambaye hana chembe ya upendo. Alisisitiza pia kuwa, nisipoishi mimi basi nimpatie mtu yeyote ambaye atakuwa na sifa alizotaka awe nazo. Iwe kabla ya kifo changu. Sasa baada ya kuwa nimemaliza miaka na mme wangu hadi kuwa tumekuwa na maisha tunayoyaishi sasa, sioni haja ya kuendelea kuwa na hiki kijumba,” alieleza mama Tora wakati Carolina akiwa kasikiliza kwa makini. Alikuwa kama mtu asiyeelewa.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Jambo jingine linalonifanya niuchukue uamuzi huu leo, ni ukweli wa mambo hapo nyumbani. Nimekuwa nikiishi nawewe kwa kipindi kirefu sasa. Ugomvi uliojitokeza unaelekea kuzalisha mambo mengi magumu. Hivi uonavyo, jicho hili sikujigonga ukutani wala mlangoni. Nakuambia siri hii kwa kuwa moyo wangu umekuhifadhi, nimepigwa usiku sababu ya kukutetea wewe. Baba yako hataki uendelee kuwepo hapo nyumbani,” alieleza mama Tora.
“Hataki! Kwani nimemkosea nini? Pole mama! Pole!” alisema Carolina kwa huzuni.
“Tena yuko tayari hata kukuua kwa jinsi alivyokuwa akijiapiza mbele yangu. Kama mimi ambaye nimekuwa nikichangia kitanda naye kwa miaka mingi ameweza kunitenda hivi, je wewe atashindwaje kutaka kuiona damu yako ikimwagika?” alieleza mama Tora.
“Ee Mungu! Anataka kuniua? Nitarudi kijijini kwetu mama. Nitarudi sitaki kukusababishia matatizo,” alisema Carolina.
“Hapana Carolina. Naomba nisikilize kwanza.”
“Sawa mama, nasikiliza.”
“Nyumba hii haijui Tora wala baba yake, naijua mimi na marehemu mama yangu enzi za uhai wake. Sasa baada ya kuwa nimefika kijijini ulikokuwa unaishi na wale wazee, ukichanganya na wema wako kwa kipindi chote nilichokaa nawe, nashawishika! Umenishawishi kuwa, kwao moyo wako, unaweza kuwa mlezi mwema wa jamii ambayo imepitia mateso na manyanyaso kama yako na yangu. Umri wangu unasogea. Sijui kesho itakuwaje. Sijui litakalo amriwa na mme wangu wakati wowote. Namjua ni mtu wa visasi. Nipo tayari kufa ili kukutetea. Hivyo kuanzia leo, nakukabidhi nyumba hii. Ni mali yako!” alihitimisha mama Tora. Carolina alikuwa kimya asiyeelewa maneno aliyokuwa akiyasema mama Tora. Alipigwa bumbuwazi.
“Mama, kwa nini? Kwa nini unafanya jambo hili kwangu ambaye tena si sehemu ya familia yako?”
“Mama aliahidi na mimi natimiza. Lazima nyumba hii iende kwa yatima ambaye atapata nyumbani wakati wa kuziunga chembechembe za matumaini ili kujikomboa. Amini Carolina. Hapa ni kwako. Na hivi nisemavyo, leo usiku nakutaka uondoke nyumbani.”
“Asante mama. Mungu atakuzidishia. Sasa nitakaa na nani, maaana!”
“Utakaa na utakaye kukaa naye. Lakini uwe mwema kadri ya wema ninaokutendea. Nipatwapo mahangaiko najua utaninyanyua na kunitetea. Nipatwapo kiu utanituliza kwa maji. Usijisahau na kutekwa na starehe za ulimwengu. Asiyefunzwa na mamaye, hufunzwa na ulimwengu. Naomba jitunze hadi mwisho wa dahari. Pia nakukabidhi nyaraka hizi. Nimeshabadili kila kitu kuhusu umiliki. Zitunze na ikibidi uzipeleke benki wakutunzie,” alieleza mama Tora wakati akimpatia Carolina nyaraka.
“Asante sana mama. Mungu akuweke na akuzidishie kila utakacho,” Carolina alishukuru. Alipiga magoti wakati chozi likimiminika kwa saada iliyomtembelea. Hakuamini kilichomtokea. Japo alikuwa bado na maswali mengi, hakuweza kuhoji bali aliishia kunyamaza. Mwenye saada habahatishi, kudra zake humjaza wakati wa dhiki!
Wakati ambao mama Tora alikuwa akimkabidhi Carolina nyumba, Tora na baba yake walifanya kutano. Ilikuwa ni kutano ambalo lililenga kutafuta mbinu ambayo itamtoa Carolina katika nyumba yao. Oli alijua kuwa, uwepo wa Carolina ulikuwa wa kipepelezi zaidi hivyo hakuwa na amani tena.
Maazimio ya kikao chao yalikuwa ni kummaliza Carolina usiku uliokuwa unafuata. Walikubaliana kukodi vijana ambao wangeingia ndani na kummaliza Carolina kimyakimya. Oli alimshauri Tora kwenda kuwatafuta vijana ambao wangetekeleza zoezi hilo. Janja waliyokubaliana ni kwamba, wakati Tora akiwa anarudi ndani, angeliegesha lango kuu la kuingilia ili wafikapo watekeleze unyama huo na kuepa bila kugundulika. Mpango ulipangwa na kupangika.
Siku hiyo haikukataa kuisha. Ilikuwa mchana hatimaye jioni ilibisha hodi. Carolina alikuwa mchangamfu siku hiyo. Aliandaa chakula kizuri kama kawaida yake. Walipakua na kula pamoja mezani kama familia. Siku hiyo Tora alionesha uso wenye bashaha akimfurahia Carolina kama hakuwa amekosana naye. Oli naye alionesha kumpenda zaidi Carolina kuliko siku zote, lilikuwa tabasamu la mamba. Akilini mwa Carolina kulikuwa na wazo, vilevile mama Tora alikuwa na lake, kila upande walikuwa wamepanga yao.
Usiku wa saa tatu ulivyofika, Oli alimtaka Tora kwenda dukani kumtafutia matunda. Alifanya vile baada ya kulifungua jokofu na kukuta hakuna tunda hata moja. Hata hivyo haikuwa nia ya dhati kwake. Ndicho walikubaliana na mwanaye ili kuutekeleza mpango wao. Baada ya kula chakula na kuvitoa vyombo, Tora hakuwa amewasili kutoka kule alienda. Carolina alivisafisha vyombo na kuvipanga kabatini usiku ule kama kawaida yake. Alimpelekea mama Tora maji ya kuoga. Mama Tora aliyekuwa akingojea maji yapelekwe bafuni alikuwa na wazo la kumnong’oneza Carolina.
“Carolina!”
“Abee mama!”
“Niletee kitenge changu hapo nilipokuwa nimeketi.”
“Sawa mama, naleta,” Carolina alienda hadi kwenye kiti ambapo alikuwa ameketi mama Tora. Alikichukua kitenge na kukipeleka moja kwa moja hadi kwa mama yake.
“Sikiliza. Nenda kapange nguo zako vizuri. Usiweke kwenye begi. Zifunge nguo kama furushi kwenye kitenge hiki. Atakapobisha hodi Tora, mfungulie. Lango usilifunge, liegeshe. Tora akiingia ndani, utakaposikia mlango wetu nimeufunga, ondoka haraka uende zako. Pesa yako pamoja na ziada nimekuwekea kitandani utavikuta. Kuwa mwangalifu. Usirande mtaani mwanangu. Uwe makini sana dhidi ya yeyote,” mama Tora alimnong’oneza Carolina. Kama alivyoagizwa, Carolina alitekeleza. Alijiandaa kadri ya maelezo ya mama yake.
Siku ambayo Carolina alipatiwa makazi mapya na mama Tora, Roy alikuwa mwenye furaha isiyo na kifani. Alikuwa amepokea barua iliyomruhusu kwenda kujiunga na mafunzo ya kijeshi ili apate kulitumikia jeshi la polisi. Alikuwa akihitajika huko haraka iwezekanavyo hivyo hakuwa tena na nafasi ya kuhangaika kumtafuta Carolina. Aliamini Carolina alikuwa salama na ipo siku ambayo wangekutana naye. Japo alimhusudu sana, umbali uliwaweka kila mmoja na fikra ya kutafuta maisha ya ndoto yake. aliamini kuwa maisha si kutafutana bali ni kutafuta, kama Mungu alipanga wakutane ipo siku wangeweza kukutana. Wote wawili walikutwa na saada.
Baada ya kufanikiwa kutoroka, Carolina moja kwa moja alienda hadi kwenye nyumba aliyokuwa kakabidhiwa. Usiku ule Tora na baba yake walijua ungekuwa wa mwisho kwa Carolina. Tofauti na matarajio yao, mambo yalikuwa sivyo. Walitarajia nyumbani kwao kungekuwa na msiba. Akilini Tora alijua angeenda tena Tuamoyo mara hiyo ni kuupeleka mwili wa Carolina kwani hapakuwa na mtu aliyepafahamu huko zaidi ya mama yake. Mama Tora hakuwa na wasiwasi, aliujua mchezo aliokuwa kaufanya na Carolina. Asubuhi ilipowadia, Oli alimkurupua mkewe kutoka usingizini.
“Katarina, nenda kamwamshe binti yako anichemshie maji nataka kuwahi mjini.,” alisema Oli.
“Kulikoni usiku usiku, huko mjini unakwenda kumfumania nani? Watu wote mji huu hulala mpaka jua litoe vidole kuwaamsha. Lakini nisitake kujua sana uendako,” alisema mama Tora. Alijikongoja kukiachia kitanda na kujizoazoa hadi mlangoni. Aliufungua mlango kisha kutoka nje akiwa anajua fika kuwa Carolina hakuwemo ndani.
“Carolina wewe! Carolina!” aliita mama Tora kila baada ya kuita na kuugonga mlango kwa nguvu. Oli na Tora walijawa furaha nafsini mwao wakijua tayari Carolina alitiwa adabu. “Wewe Carolina!” aliita mama Tora wakati akiusukuma mlango. “Mbona hakuna mtu humu ndani?” alijiongelesha mama Tora. “Baba Tora, mbona chumba kitupu? Ameenda wapi asubuhi hii?” alihoji mama Tora.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hayumo ndani?” alihoji Oli. Alitembea harakaharaka kuelekea chumbani pale.
“Mbona hata hili geti liko wazi!” alidakia Tora aliyekuwa getini. Naye alitembea hadi kwenye chumba kilichokuwa cha Carolina. Tora aliingia ndani pamoja na baba yake. Waliangaza macho na kuona kila kilichokuwa cha Carolina hakikuonekana.
“Hata nguo zake zote na viatu havipo. Atakuwa katoroka huyu binti. Wasichana wa siku hizi! Yawezekana kabisa kapata mwanaume wa kumhadaa. Tumaini ni mji mkubwa, nasijui ambako atakuwa ameelekea,” alieleza Oli. Fikrani hakuwa na amani. Hali aliyoiona haikumpa jawabu la kile alikuwa akikitarajia. Alitarajia kumkuta Carolina akiwa mfu ama mahututi baada ya kushughulikiwa kwa mapanga na vijana aliokuwa amewaandaa na mtoto wake. Nafsini alianza kumshuku Tora kuwa huenda alimzunguka na kumtorosha Carolina. Hakuwa na imani tena na mwanaye.
“Nitawaambiaje wenye mtoto! Mtafuteni na akipatikana arudishwe kwa wazazi wake,” alisema mama Tora.
“Tora, toa gari tujaribu kumfuatilia huko kwao. Carolina si mwenyeji katika mji huu. Lazima atakuwa kaifuata njia kwenda nyumbani,” alisema Oli. Tora aliiwasha gari na kuanza kuifuata njia iendayo Tuamoyo. Waliifuata njia ileile iliyomleta Carolina mjini. Kwa kuwa ilikuwa safari ya haraka, walienda wakimkagua kwa macho kila waliyemkuta njiani. Njia nzima mpaka wanaingia Tuamoyo, hawakumwona Carolina wala wa kufanana naye.
“Sasa niache kabla hujafika kwenye mji wa hao wazee. Nenda kaulize kama Carolina amefika lakini usioneshe kuwa kuna matatizo yoyote,” alisema Oli. Tora alisimamisha gari kumruhusu baba yake kushuka. Toka hapo Tora aliendesha gari taratibu hadi mahali ambapo Carolina alikuwa akilelewa. Maua na Majaliwa walikuwa wamejianika kwenye jua la asubuhi. Walipoliona gari walipatwa mshtuko. Kutahamaki gari lilikuwa mbele yao. Alishuka kijana mrefu, mwemba mwenye uso mrefu. Alitembea mpaka walipokuwa wameketi. Aliwasabahi nao waliitikia likiwa swali lao la kwanza ni kule Carolina alikuwa.
“Carolina aliaga kuwa anakuja huku, sasa kwa kutaka kupata uhakika kama alifika ndipo nikaona nije kuhakikisha na nirudi naye,” alisema Tora.
“Hapana babu! Huku hajafika bado. Kama aliondoka bila usafiri huenda akawa bado yupo njiani. Kuna tatizo lolote huko kwani?” alihoji Maua.
“Hapana. Alikuwa amewakumbuka sana na alipaswa awe hapa kwa ajili ya likizo. Inawezekana atafika. Kama atafika, basi mjuzeni nitakuja kumchukua baada ya siku tatu,” alisema Tora.
“Sawa babu. Mungu atamfikisha salama na tutamjulisha. Tushamkumbuka sana. Angalau sasa hata fununu hizi zinatutia moyo kuwa yupo anakuja kutuona,” alisema Majaliwa.
“Sasa mimi natoka, nina haraka kidogo. Nikikutana naye nitamwahisha ndipo nirudi. Sasa shikeni hizi zitawafaa,” alisema Tora. Muda huo aliwakabidhi Majaliwa na Maua kila mmoja noti ya shilingi elfu kumi alizokuwa kapewa na baba yake. walipokea na walimshukuru.
Tora aliondoka. Hakuwa amemwona Carolina hata dalili ya kuwepo pale haikuwepo. Moja kwa moja aliendesha gari hadi kwa baba yake na kumpakiza kwenye gari. Walianza kurudi taratibu uliko mji wa Tumaini.
“Umewapatia ile hela nilikupa.”
“Ndiyo, nimewapatia. Lakini Carolina hajafika huku bado,” alieleza Tora.
“Jambo hili haliniingii akilini. Carolina ametoroka, kwa nini ametoroka? Alijua kuwa usiku atavamiwa? Kama alijua nani alimwambia habari hizo? Bado Carolina ni mgeni ndani ya mji.
Atakuwa kaenda wapi? Nashawishika yupo mwenyeji, tena mtu wa ndani kalifanya jambo hili,” alieleza Oli.
“Unahisi anaweza kuwa nani?” alihoji Tora.
“Huyu atakuwa ni mwanangu! Hakika atakuwa yeye bila shaka,” alijibu Oli.
“Hapana mzee, mwanao wa wapi?”
“Nina mashaka sana na wewe. Huenda badala ya kuwaambia vijana wenzako wamtoe roho Carolina uliwaambia wamtoroshe. Huna sababu ya kujitetea. Nimejua hufai kuwa mwanangu,” alilaumu Oli.
“Jambo hili hata mimi linanikanganya sana. Wapi Carolina amekimbilia. Au hawa jamaa badala ya kummaliza palepale waliona wasilete kesi nyumbani wampele sehemu za mbali?” alisema Tora.
“Labda iwe hivyo. Lakini hadi na nguo zake zote?” alitaharuki Oli.
“Yaweza kuwa walitaka kupoteza kabisa ushahidi,” alieleza Tora.
“Basi inafaa tukatulie siku chache tusubiri. Atapatikana akiwa mfu ama mahututi. Inafaa tuwe na subira, lakini tuwe makini sana,” alisema Oli.
Safari yao iliyokuwa ya harakaharaka hatimaye iliwafikisha tena mjini baada ya muda mrefu kuwa njiani. Mama Tora yeye alijua fika kilichokuwa kikiendelea. Kwa kuwahadaa, alikuwa akilia na kukosa utulivu. Oli alimsihi atulie kwanza ndipo waende kutoa taarifa kituo cha polisi. Carolina muda huo alikuwa katulia kwenye nyumba alikokuwa kapatiwa makazi na mama Tora.
Hakuna afahamuye siku na wakati ambao bahati yenye kumjaza ramsa itamfika. Kila mmoja hutafuta pasipo uhakika wa lini agano la kuzaliwa litatimia. Carolina naye maisha yalimchukua kama bembea kwa mtindo huo. Kama kiungo kilicho bora katika mchanganyiko wa chakula na vyote viliwavyo kwa viungo duniani, yeye alikosa chumvi ambayo ni elimu. Alitaka kuipata elimu bila kujali angeipata wapi. Hatimaye, maisha ya ndoto za Carolina yalianza kumpandisha taratibu kuyaelekea mafanikio. Japo alipitia misukosuko iliyouchosha moyo na mwili, hakukubali kukata tamaa. Juhudi zake ziliisukuma kudra kumfuata na kumwandama kama mwanga wa jua.
Katika maisha yake hakutaka kuwa mtumwa wa mawazo ya waliomtangulia. Aliona vema kuyaanza maisha ya kuishi kwa vitendo na kuacha porojo za mawazo yake. Hakuamini kuwa ulimwengu ulikuwa na watu waliozaliwa kwa madaraja, wenye nacho na wengine wakosaji. Aliamini alikuwa bora na muhimu kwa kila wakati. Ukiachilia saada iliyomkuta akajipatia nyumba bila malipo,
Carolina alikuwa na pesa nyingi iliyomtosha kuyalipia masomo yake. Fedha aliyokuwa amejitunzia na nyingine iliyokuwa hisani na ujira kutoka kwa mama Tora, ilimfanya akae kitako kupanga namna bora ya kuzitumia. Alitaka fedha zitumike kuyanyanyua maisha yake.
Japo aliamini kuwa, mwenye kiraka haliliwi njaa, kusoma ndilo lilikuwa chagua lake la kwanza. Carolina angesoma nini wakati alikuwa bado mshamba wa shamba asiyejua thamani ya ulimwengu? Alichagua kilichomfaa. Nia ya Carolina ilimfanya kwenda moja kwa moja hadi kwenye chuo cha uhazili kilichokuwa mjini Tumaini. Wakati huo aliishi kwa kuificha sura asitambulike na yeyote. Kadri ya nia yake, chuo cha uhazili kilimpokea na kumshauri kujiunga na masomo ya uhazili ngazi ya kwanza. Alikubali. Haikumchukua muda mrefu Carolina kuanza kuyaelewa masomo aliyosajiliwa nayo. Nusu mwaka baadaye, Carolina alikuwa tayari kuhitimu na kuivuka ngazi hiyo kwa kishindo. Hakutaka kuivuruga akili yake kwa lolote. Aliamini, mshikambili moja humponyoka. Ustawi wa mwili na akili yake vilimjenga na kumfanya mtu mwenye staha.
Tangu atoroke, Carolina alikuwa akionana na mama Tora kwa nadra tena kwa siri kubwa. Njia yake ilikuwa nyoofu isiyopinda kwa mambo ya dunia. Baada ya kuwa amehitimu masomo yake kwa ngazi ya kwanza, alipata fursa ya kuendelea na ngazi ya pili. Hatua hiyo haikumfanya atumie jasho jingi kuimaliza kwani alifanikiwa kufaulu kwa kiwango kikubwa kuliko cha awali. Carolina alikuwa kipanga, pamoja na kuupoteza muda mwingi akiwa na misukosuko ya maisha, hakuweza kuipoteza dira yake.
Kuhitimu kwa mafanikio katika uhazili kulimfanya Carolina apate nafasi ya kazi. Moja kwa moja idara ya mahakama ya mji wa Tumaini ambapo alifanya mazoezi ya vitendo ilimhitaji. Si tu kwa kuwa na haiba ya kuvutia bali ubora wa kazi zake ulijieleza. Aliajiriwa kama karani katika ofisi ya Hakimu mfawidhi wa mji wa Tumiani.
*****
Miaka mingi ilikuwa imepita Tunu, mtoto wa Koi tangu aipe kisogo ndoa na kukimbilia mjini. Mji wa Tumaini ulimpokea na kumtupa katikati ya shughuli za anasa. Alikuwa akihudumu kwenye nyumba moja ya kulala wageni ambapo pia palikuwa na baa ya pombe. Pamoja na kuwa alitoweka na kumwachia mmewe mtoto mdogo, kuna wakati alikuwa anawaza na kumkumbuka sana. Hali ile iliendelea mfululizo kumkalia Tunu akilini kisha siku moja ilimlazimu kumwandikia barua mmewe. Kikubwa alichokuwa akitaka kukijua ni kuhusu maendeleo ya mtoto wake. Damu ni nzito kuliko maji!
Baada ya kuiandika barua, Tunu aliwapatia wafanyabiashara waliokuwa wakienda hadi kijiji cha Sihiri. Eneo hilo kulifanyika mnada ambao uliwavutia wengi kwenda kuzinadi bidhaa zao. Ilikuwa rahisi kwa mmewe kuipata barua kwani ukoo wake ulikuwa maarufu kijijini pale.
Ilipofika jioni, mmewe Tunu alikuwa na barua mkononi. Aliisoma ikamtia simanzi moyoni. Aliamua pia kumpatia mkwewe ili naye ajue kule mwanaye alikuwa. Koi baada ya kuisoma barua alikata shauri kusafiri hadi Tumaini. Alikuwa na hamu ya kumwona mwanaye. Mbali na kumwona, alitaka kumjulisha yaliyoipata familia yao hasa kifo cha mama yake. Kwa sababu usiku uliingia, Koi aliamua kuondoka alfajiri iliyofuata kuelekea hadi mjini Tumaini.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wakati Koi anapanga kuingia Tumaini, familia ya Oli haikupata utulivu tangu Carolina autoroke mji. Hawakuisha kukwaruzana kila siku ambayo jua lilichomoza. Mama Tora na mmewe walikuwa kama paka na panya, hawakupikika tena chungu kimoja. Oli alimlaumu mkewe kumletea mzuka nyumbani kwake ambaye ni Carolina. Tuhuma hiyo ilitokana na kutopatikana kwa Carolina kwa kipindi chote tangu atoroke. Oli alijua fika kuwa, Carolina hakuwa mtu mwema na kuna wakati alihisi alikuwa Lola aliyejigeuza ili apata kulipiza kisasi cha yale walimtendea miaka mingi iliyokuwa imepita.
Mbali na Oli kuwa katika mtafaruku na mkewe, Tora mambo hayakuwa shwari. Hakulisikia la mama wala la abu yake, alikuwa akiishi kwa amri yake akiponda starehe kuliko kazi. Kwake alilipokea jua kwa kiroba cha konyagi na aliliaga kwa mzinga wa chang’aa ili kujiliwaza. Alikuwa mlevi aliyetopea na mwili wake ulidhoofika. Kituo chake kikubwa cha kileo kilikuwa ni mahali ambapo Tunu, mtoto wa Koi alikuwa. Tora na Tunu walifahamiana sana. Tora akiwa mteja wakati Tunu alikuwa mhudumu. Maisha yaliwapepeta!
Serikali ya Tumaini baada ya kuona watu wake wengi hasa vijana wakipotea na kuangamia kwa vileo, ilitunga sheria zilizolenga kukomesha tabia hiyo. Uongozi wa mji ulisambaza sheria hizo kwa vipeperushi na matangazo ya redio kila kona ya mji wa Tumaini. Kila ambaye angepatikana akitumia kileo ama kuonekana eneo la starehe kama baa majira ya asubuhi na mchana wakati wa uzalishaji, alipaswa kukamatwa na kufikishwa mahakamani. Adhabu kali ilipangwa kumpata kila mvunja sheria iliyokuwa ikilenga kuwafanya wote kushiriki katika uzalishaji.
Mazoea aliyokuwa nayo Tora hayakumfanya kuisikia na kuielewa ilani ile. Kwake ilikuwa sawa na kumpigia zumari mbuzi na kumtaka aimbe mashairi kwa sauti ya kuvutia. Tora alipuuza. Kiguu na njia aliondoka kwao asubuhi na mapema hadi kwenye baa aliyokuwa akihudumu Tunu. Huko alimkuta Tunu akifanya usafi ili kuyaandaa mazingira tayari kuwahudumia wateja wake.
“Tunu mtoto mzuri, nakuona unazidi kuwakawaka. Japo hunitaki basi nipatie mpenzi jini aniliwaze,” alisema Tora. Wakati huo alikuwa kamfikia Tunu na kusimama mbele yake.
“Tora nawe, asubuhi hii mpenzi jini atakuliwazaje? Ngoja angalau jua lichomoze. Kwanza hata chai hujatia mdomoni unamtaka mpenzi jini, huoni atakuelemea?” alisema Tunu.
“Mpenzi jini haishi utamu. Ukimpenda naye anakupenda maradufu. Si kama nyinyi binadamu macho juujuu mifukoni mkisaka noti. Mpenzi jini hana bei lakini hakunyimi raha mpaka kisogo kinasisimka,” alisema Tora.
“Tora hapana. Hujasikia jinsi serikali ya Tumaini imetangaza sheria mpya? Vileo vyote na vituo vya burudani havipaswi kufunguliwa wakati wa uzalishaji. Sasa unataka kunitia majaribuni wewe,” alieleza Tunu.
“Sikiliza wewe, sheria zilitungwa ili zivunjwe. Zisipovunjwa unadhani zitakuwa sheria tena? Za kuambiwa unatakiwa uongeze na zako. Utaacha kuchuma pesa wakati imejileta yenyewe asubuhiasubuhi. Sasa unataka kuwaona wajinga waliosema biashara asubuhi, jioni ni mahesabu?” alisema Tora. Sauti yake ilijaa mkwaruzo.
“Siwezi babu eeeh! Kisa cha kuswekwa rumande! Wewe nenda kalale hiyo konyagi sijui penzi jini wako utamkuta jioni,” alisema Tunu.
“Kweli masikini hana lake,” alisema Tora wakati akizitoa fedha zilizokuwa mfukoni mwake. “Ona! Hizi zote nilitaka ziishie hapa. Nimeona niwahi asubuhi na mapema maana nikianza mchana sitazimaliza. Sasa chagua moja, unanihudumia ama hutaki?” alisema Tora wakati akizionesha fedha hadharani.
“He! Tora, hebu nione. Hela zote hizo umezitoa wapi?” alihoji Tunu wakati mate yakimmiminika kuzitamani.
“Nakula urithi kabla wazazi wangu hawajafa. Huwezi kujua wataanza wao au mimi. Sasa nimeamua kula urithi ningali mzima. Nimezikuta chumbani kwa mzee nikazizoa. Sasa kwani nimefanya kosa?” alisema Tora.
“Hela zote hizo kweli! Ungemwachia hata kidogo,” alisema Tunu.
“Kidogo za nini? Kwanza achana na hayo. Shika hizi nihudumie. Hii ni ya kwako ufe nayo, elfu ishirini tia mfukoni. Hii shika niletee mpenzi jini najificha huku unipe chumba kimoja nitulie,” alieleza Tora. Tunu alipoziona pesa hakutaka kuzubaa. Macho yalimtoka wakati akimshika mkono Tora hadi kwenye chumba kimoja kilichokuwa kikitumiwa na wahudumu wa baa ile.
“Sasa tulia humu. Mpenzi jini nakuletea sasa hivi. Akikuliwaza sasa sitaki utoke nje, inabidi ulale hapa kitandani tulii mpaka utakapojisikia sawa. Unanielewa mpenzi!” alisema Tunu wakati akimtekenya Tora kwa uchokozi. Hatimaye mzinga wa konyagi ulikuwa mkononi mwa Tora. Alipoupokea na kutabasamu.
“Leo mpaka huyu aliyenyanyua mikono aishushe ndipo nitasema basi,” alisema Tora. Alianza kujimiminia kileo. Mpenzi jini alimwingia mwilini wakati Tunu akiwa karibu naye akimhudumia. Baada ya muda mfupi kupita, mpenzi jini alipanda akilini kwa Tora. Nyimbo za kila aina zikajaa fikrani akijiona yuko juu ya jukwa anasakata rumba. Tora hakuvumilia, aliufungua mdomo na kuanza kuimba kwa nguvu. Hakuishia kuimba, alinyanyuka na kuanza kukata mauno bila aibu. Chumba wakati ule hakikumtosha, alinyanyua miguu kutoka nje. Mkononi alishikilia mzinga wa konyagi wakati mifuko yake ilijaa viroba ambavyo alikuwa akivimiminia mdomoni kwa zamu. Akili ilivurugika. Alipopiga hatua na kufika mbele ya baa, Tunu alisikia tambo na kelele. Alitoka alipokuwa na kumfuata ili amrudishe.
“Tora nilisema, rudi ukalale.”
“Kalale wewe. Kwani mimi mgonjwa hadi nilale!” alisema Tora kwa kufoka yangali maneno yakikwama kutoka mdomoni. Tunu alimvuta kwa nguvu kumrudisha. Wakati anamvuta alijaribu kuiingiza mikono yake mfukoni kwa Tora kuzichukua pesa zote alizokuwa nazo. Tora alibaini hila ile japo alikuwa kalewa.
“Niache sijalewa. Mpenzi jini ananiliwaza tu ujue,” alisema Tora. Tunu alikazana kumvuta wakati Tora alikazana kugoma akiisimika miguu yake kama mbuzi alazimishwaye kwenda asikokutaka.
“Ala! Sijalewa kahaba wewe! Sijalewa, rudisha hela yangu nasema,” alifoka Tora baada ya kubaini Tunu amezichomoa fedha zote. Wakati Tunu akitaka kuondoka amwache Tora aende zake, alikuwa kachelewa. Tora aliisukuma chupa ya konyagi iliyokuwa mkononi na kuipasua juu ya kichwa cha Tunu.
“Mamaaa!” Tunu alilia kwa nguvu. Watu waliokuwa karibu walimiminika na kumkuta Tora akitaka kuondoka. Walimkamata nakumfunga kamba mikononi. Taarifa zililifikia jeshi la polisi ndipo walifika kuwachukua Tora na Tunu. Wote waliwekwa chini ya ulinzi japo Tunu alipelekwa hospitalini kwanza kwa ajili ya kulitibu jeraha lilokuwa kichwani kwake.
Ilipofika mchana, taarifa zilimfikia Oli kuwa kijana wake alikuwa matatani. Taarifa hiyo ilimstaajabisha sana na kumfanya asiweze kuelewa kilichokuwa kimetokea kama ni cha kweli. Fununu za kuwa Tora huwa analewa na kufanya mambo ya aibu mitaani, hakuwa akizisadiki. Kila aliyemjuza alimwona kama shambenga-mchonganishi. Siku hiyo hakuwa na la kufanya. Kwa kuwa mkewe alikuwa kwenye kibanda cha biashara, hakutaka kupoteza muda kumsumbua. Aliondoka moja kwa moja kuelekea kilipo kituo cha polisi alikokuwa akishikiliwa Tora.
Mchana huo Koi alikuwa kawasili mjini Tumaini. Kwa maelekezo ya barua aliyoiandika Tunu, moja kwa moja aliulizia kwa watu wema. Umaarufu wa sehemu ile ulimfanya afike bila kusumbuka. Haikuwa siri tena, walimjuza jinsi ilivyokuwa imetokea hadi Tunu kushikiliwa na jeshi la polisi japo alipata jeraha kubwa kichwani. Shauku aliyokuwa nayo Koi ilipotea. Kinyume cha furaha aliyokuwa nayo kilikuwa maumivu na uchungu mkubwa. Nafsi yake ilijaa fadhaa akitaka kukata tamaa juu ya uzao wake.
Uchungu wa mwana aujuaye mzazi, Koi alijikaza na kuelekea kilipokuwa kituo cha polisi. Ilikuwa nia yake kwenda kujua kilichokuwa kikiendelea sehemu ile. Kikubwa alitaka kujua afya ya mwanaye na kisha angejua sababu iliyomfanya Tunu atiwe ndani wakati alitendewa unyama. Kituo cha polisi hakikuwa mbali, hatimaye alifika. Moja kwa moja aliongoza hadi yalipokuwa mapokezi. Alipoona mtu wa mapokezi akiwa anamhudumia mtu mwingine, aliamua kuketi. Aliingoja zamu yake ndipo naye aweze kufika dirishani kuhudumiwa.
“Ha! Nani? Oli!” alisema Koi kwa mshangao baada ya kuwa wamekutanisha nyuso zao na macho moja kwa moja. Koi alitoka mapokezi na Oli akielekea mapokezi.
“Alaaa! Koi! Ni wewe kweli au jinamizi?” alisema Oli. Nafsini mwake alifurahi kukutana na rafiki yake wa siku nyingi.
“Kweli milima haikutani, lakini binadamu hukutana. Za siku nyingi jamaa yangu?” alihoji Koi wakiwa wameshikana mikono. Hawakujali tena kama kulikuwa na jambo la kuhuzunisha lilikuwa likiendelea. Baada ya kuwa wamejali sana maongezi yao, askari mmoja aliwataka kupisha mahali pale ili wapate kufanya mazungumzo yao bila kuwabugudhi watu wengine. Walitii nao walienda chemba.
“Kweli umri ukienda mwili hubadilika sana. Umekuwa pandikizi la baba. Miaka ni mingi sana hata sijui ilikuwa mwaka gani,” alisema Koi.
“Kweli ni miaka mingi mno. Vipi tena kituoni muda huu, kuna heri kweli?” alihoji Oli.
“Sote yatupasa kuulizana, kulikoni?” alisema Koi. Kwa pamoja walicheka kidogo.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kwa kuwa umeanza kuniuliza, niwe wa kwanza kukujibu. Bwana nimefika kutoka shamba muda si mrefu. Nia yangu ikiwa ni kumwona binti yangu ambaye miaka mingi yupo mjini hapa. Cha kusikitisha nilivyofika tu, wenyeji wake pale Mshikemshike wakanijuza kuwa yupo kituoni. Inasemekana kapigwa chupa na mlevi na hali yake si salama. Ndipo nikaamua kufika hapa haraka nijue kinachoendelea,” alieleza Koi.
“Alaaa! Mshikemshike ile baa maarufu hapa mjini! Kweli shida. Lakini matatizo huwapata wote, wanyama na binadamu. Pole sana. Usemalo ni sawa na langu. Nimefika hapa baada ya kupata taarifa kuwa kijana wangu anashikiliwa na polisi. Walionipa taarifa walidai kuwa kamjeruhi mtu kwa chupa na alikuwa amelewa. Palepale usemapo, Mshikemshike,” alieleza Oli. Wakati huo wote walibaki kuduwaa wakitazamana.
Hatimaye Koi na Oli walikutana tena baada ya miaka mingi. Kilichowaachanisha ni Majaliwa. Kipindi kile cha kumhujumu Majaliwa, Oli alikuwa na jukumu la kumswaga fahali hadi mnadani na kumuuza ili wajipatie fedha. Oli alivyotoweka hakurudi tena Hamaniko hadi wasaa waliokutana kituo cha polisi cha Tumaini. Penye tatizo hapakuwa na la kungoja. Koi na Oli waliongozana tena hadi mapokezi ili kupata taarifa sahihi za watuhumiwa. Walielezwa majina na kila taarifa zilizo wahusu. Oli alitambua kuwa kijana wake Tora ndiye alimpiga kwa chupa Tunu na kumjeruhi kwichwani. Vilevile Koi alijua fika kuwa binti yake Tunu ndiye alipata jeraha baada ya kupigwa chupa na kijana ambaye aliitwa Tora. Pande mbili za marafiki wa zama zilikuwa zimehitilafiana. Sheria haikubagua na wala haikuutambua urafiki wa wawili wale. Ilipaswa kuchukua mkondo wake.
Oli na Koi waliendelea kusogoa wakingoja Tunu kuwasili pale kituoni. Tunu alipofikishwa hospitalini alishonwa kwa nyuzi saba na aliruhusiwa kuongozana na polisi hadi kituo cha polisi. Hati ya mashitaka iliandaliwa sambamba na ya mtu aliyemjeruhi. Hakupata bahati ya kuongea na baba yake zaidi ya kutazamana naye kwa mbali. Alijawa mshangao!
Baada ya kuwa wamehojiwa na kuandikwa hati za mashitaka ililazimu ofisi ya upelezi kuziwasilisha hati hizo mahakamani kwa ajili ya shauri kusikilizwa. Mkuu wa idara ya upelelezi wa makosa ya jinai katika kituo hicho alikuwa ni kijana mdogo kwa umri. Aliyabeba majalada na kwenda hadi ilipokuwa mahakama ya hakimu mfawidhi kuyawasilisha. Alipofika kwenye ofisi ya karani wa hakimu, palikuwa na msongamano wa watu wengi. Wote walikuwa wakipatiwa huduma ambayo iliwafanya kuwa pale. Kwa busara zake mpelelez,i aliamua kungoja watu wahudumiwe ndipo angeweza kuhudumiwa kwa kufuata utaratibu. Alingoja hadi watu walipopungua ndipo alinyanyuka kuingia ndani ya ofisi alimokuwa karani yule.
“Karibu!” aliitikia kalani akiwa bado hajakinyanyua kichwa chake kumtazama mtu aliyekuwa kasimama mbele yake. Alikuwa makini akijaza taarifa kwenye jalada moja lililokuwa mkononi mwake. Mara macho yalienda kwenye shajara na kutua kwenye kalenda akiangalia tarehe.
“Samahani, naomba keti nikuhudumie,” aliongea karani. Bado alikuwa akikamilisha kujaza taarifa kwa usahihi zaidi. Muda huo mpelelezi wa makosa ya jinai alikuwa kaketi. Alikuwa kainama kwenye majalada yake aliyokuwa akiyawasilisha. Alikagua karatasi moja baada ya nyingine ili kuhakiki kama taarifa alizokuwa akiwasilisha zilikuwa sahihi.
Hatimaye karani alimaliza kujaza taarifa. Aliunyanyua uso kumtazama kijana aliyekuwa kamkaribisha na kumtaka aketi kitini. Bado mpelelezi hakuwa amemaliza lakini jicho la karani lilikuwa likimtazama. Alikuwa kavaa suti nyeusi ambapo ndani alivaa shati jeupe. Mguuni alikuwa na kiatu cheusi kilichochongoka kwa mbele. Alikuwa na nywele fupi nyeusi tiii! Mkononi alikuwa na saa iliyojaa nakshi ya dhahabu.
“Kaka, nikuhudumia tafadhali!” Alisema karani.
“Sawa, asante,” alijibu kijana yule mpelelezi wakati akiunyanyua uso wake kumtazama karani. Mtumishi yule wa ofisi ya hakimu alivaa blauzi nyeupe iliyong’aa kama theluji. Shingoni alitupia skafu na sketi yake ilikuwa nyeusi. Kupitia uvungu wa meza, alionekana kuvaa kiatu cheusi kilichoushika mguu wake vizuri. Kichwani kulikuwa na nywele ndefu nyeusi zilizoshuka hadi mabegani kuelekea mgongoni, zilikuwa ndefu. Masikioni kulikuwa na hereni zikining’ia kama pilipili tawini. Midomo yake ilikuwa ua waridi changa likingoja jua kuchanua. Macho yake yalionekana kujawa usingizi japo hakuwa akihisi kulala wakati huo. Moja kwa moja karani alikutanisha macho na mgeni aliyehitaji kuhudumiwa.
“Nani!” alitamka karani wakati akinyanyuka kutoka kitini. Alisimama akitafakari kidogo. Kijana mpelelezi naye alisimama akiwa kafumwa na mshangao. Hakuweza kutoa neno kama karani alivyokuwa kaduwaa. Walibaki kutazamana. Hatimaye tabasamu lilichanua mdomoni kwa karani. Vishimo vya huba mashavuni kwake vliajitangaza. Kinywa alikiacha wazi na kuyafanya meno yake meupe mdomoni kuonekana. Fahamu za kukumbukana zikatua kama radi kwa kila mmoja. Karani alikiacha kiti na kuzunguka kuelekea alipokuwa kasimama kijana mpelelezi. Alimkumbatia bila kuyajali macho ya watu.
“Roy!” alitamka karani akiwa himayani mwa kijana yule.
“Caro!” alitamka mpelezi wa makosa ya jinai. Walibaki wamekumbatiana kwa muda. Hadi wakati ule kila mmoja alikuwa akivuta pumzi ya manukato yaliyokuwa yameufunika mwili wa mwenzake. Baada ya kukumbuka walikuwa ofisini ndipo Carolina lijitoa himayani mwa Roy. Hawakuisha kushangaana.
“Roy ni wewe? Hata siamini.”
“Amini ni mimi. Hata mie siamini kama ni wewe. Tangu lini upo hapa?”
“Nina muda sasa. Yapata miezi sita nipo katika ofisi hii. Kwa hapa Tumaini ninamuda mrefu sasa.”
“Nawewe kulikoni na majalada mkononi?”
“Yanakuja kwa mheshimiwa,” alijibu Roy. Aliunyosha mkono kumpatia Carolina majalada mawili. Carolina aliyapokea. Hakuwa na utulivu muda ule. Alihisi kurukwa na akili baada ya kumwona Roy.
“Tulia ifanye kazi yako kwanza, nahitaji nipate mrejesho kama kesho yatashungulikiwa,” alisema Roy wakati akiwa na tabasamu mdomoni. Carolina alizidisha umakini kwenye majalada yale. Aliyapatia namba na kujaza taarifa zake kwenye shajara ya mahakama. Alinyanyuka na kuyafungia majalada kwenye kaisiki lililokuwa pembeni yake. Dakika chache alizitumia pia akiwa makini akijaza taarifa za majalada kwenye kompyuta kutoka kwenye shajara. Alipomaliza kujaza, aliiruhusu printa kutapika karatasi moja yenye maandishi. Aliichomoa na kumkabidhi Roy.
“Kumbe wewe ndiye Mkuu wa idara ya upelelezi hapa Tumaini?”
“Umejuaje hata sijakuambia?”
“Ulimwengu ushapiga hatua. Hakuna siri siku hizi, tunafanya kazi kisasa zaidi. Nimeingiza tu taarifa za majalada yako nikakutana na kila kitu juu yako. Hongera sana.”
“Hongera nawewe. Kwa kuwa upo kazini na mimi nipo kazini, tutawasiliana baada ya muda wa kazi. Kazi kwanza, mengine tutayapatia muda wa kuteta.”
“Sawa Roy. Lakini…….”
“Tutawasiliana baadae. Namba yangu ni hiyo kwenye majalada. Nitafute baada ya kazi. Tafadhali usiache nataka leo tuzungumze kwa undani,” alisema Roy. Carolina hakutaka kumpoteza Roy machoni. Alitamani aendelee kubaki mahali pale lakini hakuwa na jinsi. Roy naye alikuwa akihisi vilevile. Walihisi wangeweza kupotezana tena. Kwa kuwa wakati ni ukuta, Roy ilimpasa kurudi ofisini kwake na Carolina ilimpasa kuhudumu kwenye ofisi aliyoajiriwa. Kila mmoja moyoni alikuwa na faraja kwa kile ambacho kilitokea. Kukutana kwao kulikuwa hakutarajiwi.
Baada ya Roy kutoka, Carolina aliinakili namba ya simu ya Roy. Alitaka kujua kama namba ile ilikuwa hai na ingeweza kuwaunganisha hapo baadaye. Alipojaribu kuipigia, simu iliita. Aliamua kumtumia arafa kumjulisha: Roy, namba yangu hiyo-Carolina. Roy alipoipata aliihifadhi baada ya kuwa amemshukuru kwa kumpatia namba ya kuwasiliana naye.
Carolina alianza kuyapanga majalada tayari kuingoja kesho kufika. Baada ya pekuapekua yake, alipoyafikia majalada ambayo yaliwasilishwa na Roy. Kabla ya kumaliza kuyahakiki alipatwa mshangao. ‘Tora bin Oli! Jalada hili ni la Tora yule mtoto wa mama mfadhili wangu!’ Carolina alitafakari sana. Alilichomoa na kuliweka pembeni. Aliendelea na jalada lililokuwa likifuata, nalo likampa mshangao uleule. ‘Tunu binti Koi! Huyu naye atakuwa na uhusiano na Koi wa Hamaniko. Yawezekana kabisa ni Tunu ambaye tumekua naye lakini akaolewa mara tu baada ya darasa la saba. Ee Mungu, nini kinatokea hapa?’ aliwaza Carolina. Aliwaza sana. Iweje kwa siku moja apate kuonana na Roy, hapohapo apate taarifa zinazowahusu watu wengine wanne aliowafahamu. Alibaki njia panda lakini aliamua kuupa wakati nafasi kutoa majibu.
Ilifika jioni Tora na Tunu bila kufikishwa mahakamani. Taarifa ambazo Koi na Oli walizipata kutoka ofisi ya mpelelezi ziliwafanya kwenda nyumbani. Koi aliongozana na Oli hadi nyumbani kwake. Huko walimkarimu na kumfanya apate mshangao mkubwa tofauti na alivyotarajia. Tofauti na Koi, Oli alikuwa na maisha mazuri.
Wakiwa kwa Oli, wawili hao waliteta mengi. Jambo kubwa likiwa ni jinsi ya kuweza kuwanasua wanao kutoka katika mikono ya sheria. Kwa fikra zao, walikubaliana kutolifikisha jambo hilo mahakamani. Walitaka yaishe kwani waliohitilafiana walikuwa ni ndugu wasiokuwa wakifahamiana. Usiku ule walilala wakiwa na jambo la kuamka nalo.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Carolina na Roy baada ya kuzifunga ofisi jioni ile hatimaye walikutana. Carolina ilimpasa kwenda moja kwa moja hadi ambako Roy alikuwa amepatiwa nyumba na ofisi yake. Ilikuwa nyumba nzuri yenye mvuto. Roy alikuwa peke yake. Mbali na kupatiwa nyumba nzuri ya kuishi, alipatiwa gari zuri la kutembelea ili kurahisisha kazi zake. Kilichompeleka Carolina kilikuwa ni kubadilishana mawazo na kujua kile kilitokea kwa kipindi chote walichoachana hadi wanakutana mahakamani.
“Karibu sana Carolina. Hapa ndipo ninaishi kwa sasa,” alisema Roy.
“Asante Roy, nimefarijika sana kukuona.”
“Naam, kulikoni hadi mahakamani, tena mbele ya ofisi ya mheshimiwa?”
“Yote si kwa juhudi zangu, Mungu ndiye anajua ilivyokuwa. Kwa juhudi zangu tu nisingeweza kufika hapa nilipo.”
“Nimefurahi sana kukutana na wewe leo. Miaka mingi imepita bila kujuliana hali. Nilirudi kijijini nikajuzwa kuwa upo Tumaini. Baada ya kurudi hapa nilijaribu sana kukutafuta, lakini sikubahatika kupata japo fununu. Ningali nikijaribu, nilipata nafasi ya kwenda masomoni baada ya kuomba kujiunga na jeshi la polisi. Huko nilikaa zaidi ya miezi tisa. Baada ya kurudi hapa ili nipangiwe kazi katika kituo chochote cha polisi, tena bahati iliniandama,” alieleza Roy.
“Bahati tena, kweli mwenye bahati…..” alisema Carolina.
“Ndiyo! Niliteuliwa kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kujifunza mambo maalumu ya usalama hasa upelelezi kuhusu. Na sasa niliporudi tu, nikakuta kila kitu kipo tayari kwa ajili yangu. Na huwezi kuamini, majalada niliyoyaleta kwako leo ndiyo kazi yangu ya kwanza. Mungu akiamua kukunyanyua basi hakuna awezaye kukukalisha,” alieleza Roy.
“Hongera sana. Endelea kumtumainia Mungu kwani ndiye aliyetufikisha hapa. Kwangu bila shaka wajua, sina tegemeo zaidi ya Mungu pekee,” alisema Carolina.
“Asante Carolina. Sasa najiona nimekamilika baada ya kukuona. Naona unazidi kuwa …..”
“Shhhhhh! Tafadhali usiseme kitu,” Carolina alimnyamazisha Roy kwa kumpachikia kidole mdomoni.
“Haya, acha ninyamaze maana nisiposema utanisemea.”
“Ndiyo! Sema na moyo wako usitamke hadharani,” alisema Caro. “Sasa, hebu tuachane na porojo,” aliongeza Carolina.
“Nipe habari, mimi leo ni msikilizaji tu. Si umenikataza kusema.”
“Utasema ninayotaka useme. Hivyo nisikilize kwanza. Sikia, leo umeleta majalada mawili ofisini kwa ajili ya kesho.”
“Ndiyo!”
“Umefanya uchunguzi wa kina kuhusu majalada hayo?”
“Bila shaka. Pale kuna mashauri yamebebana. Nilichobaini ni kuwa, kuna shauri kuhusu uuzaji wa kileo kwa wakati uliopigwa marufuku na sheria. Shauri jingine linahusu uuzwaji wa kileo ambacho pia kimepigwa marufuku, kiroba. Na shauri la tatu ni utumizi wa kileo kilichopigwa marufuku, kiroba. Shauri jingine ni uuzaji wa kileo kilichopigwa marufuku. Shauri la tano ni shambulio la kuudhuru mwili. Hivyo mashauri yote haya yanashughulikiwa na sheria zetu kwa ukamilifu,” alieleza Roy.
“Sawa, umetoa ufafanuzi mzuri. Lakini kuna kitu nahisi hujakichunguza katika majalada yote mawili,” alisema Carolina.
“Nimbie mapema nisije kuwa naharibu kazi yangu,” alisema Roy kwa wasiwasi. Aliketi vema kumsikiliza Carolina.
“Wala usihofu. Wanaohusika na majalada umebaini ni akina nani?” alieleza Carolina.
“Ndiyo, huwezi kuwasilisha hati ya mashitaka pasipo majina sahihi ya wahusika. Bila shaka umeyaona,” alisema Roy.
“Sawa yapo. Je, unawajua ni akina nani?” alihoji Carolina.
“Hapana. Kwa mujibu wa kazi zangu, si lazima kumfahamu sana mtuhumiwa ndipo ashitakiwe. Nafahamu taratibu tu ndizo lazima kuzingatiwa,” alieleza Roy. Carolina alicheka kidogo na kumfanya Roy ataharuki.
“Roy, majina yote yaliyopo kwenye hati zile yamenitia wasiwasi ndipo nikaamua kukuuliza.”
“Majina gani tena Caro! Mbona unanijaza wasiwasi.”
“Koi na Oli. Hujawahi kuyasikia majina haya?” alihoji Carolina. Roy alitafakari kidogo.
“Hebu niweke wazi nijue. Nisijekuwa nafanya nisilolijua,” alisema Roy.
“Katika majalada yale, watuhumiwa wote wawili, Tora na Tunu nawafahamu. Tena yaonesha kuwa mvulana ni mtoto wa Oli na msichana ni mtoto wa Koi.”
“Koi! Yule wa kijiji cha Hamaniko?”
“Ndiyo! Humkumbuki Tunu tuliyekuwa naye darasa moja. Baada tu ya kumaliza darasa la saba hata matokeo hayakutoka alimwozesha bintiye kwa lazima?”
“Alaa! Sasa ndo napata picha. Je, huyo mvulana unamfahamu?”
“Roy nakwambia kweli, mvulana namjua kuliko msichana. Ni mtoto wa aliyekuwa tajiri yangu nilipokuwa kijakazi. Hata kutoka kwao yeye ndiye alisababisha nitoke,” alieleza Carolina.
“Alifanya nini hadi ukalazimika kuondoka?”
“Hayo tuyaache tutayazungumza wakati mwingine. Tuzingatie lililopo mbele yetu.”
“Lililopo mbele yetu ni pamoja na hilo. Historia ya mtuhumiwa inaweza kunisaidia kuendesha shauri hili. Wewe sema alikufanya nini ama alitaka kukufanya nini?” alihoji Roy. Carolina alilazimika kumsimulia Roy kisa kizima. Alimweleza yote yaliyompata tangu aingie Tumaini hadi kipindi hicho ambapo walikutana baada ya kuonana mahakamani. Ilikuwa simulizi iliyomkera na kumuuzi sana Roy. Nafsini Roy alijawa wivu akitamani kumtia mkononi Tora aliyetaka kumfisadi Carolina.
Mazungumzo yao hayakuwa ya kuumaliza usiku. Carolina aliaga na ndipo Roy alimchukua kwa gari yake hadi kule alikuwa akiishi. Kila mmoja siku ilimalizika akiwa na furaha nafsini mwake.
Ukumbi wa mahakama ulijaa watu hadi uliwatapika. Hakimu mfawidhi wa mji wa Tumaini alikuwa mbele ya watuhumiwa. Karani naye alikuwa sambamba na mwendesha mashitaka wa serikali kwa ajili ya kuyataja mashitaka yaliyokuwa mezani. Tunu na Tora walikuwa wamesimama kizimbani kuyasikiliza waliyotuhumiwa nayo. Nyuma pembeni kulikuwa na wanaume wawili walioonekana kulingana kwa kimo na umri. Mmoja alionekana kuwa na sura angavu, sura iliyoonesha dhahiri kuwa hakuwa akiishi katika maisha ya vumbi. Mwanaume mwingine alikuwa mnyonge usoni. Tangu mavazi na siha alikuwa dhoofu. Hakuwa na tumaini machoni zaidi ya kujawa wasiwasi. Si wasiwasi wa alichokiona pale, bali hakuwa na jana nzuri kabla ya kufika alipo. Walikuwa ni Oli na Koi.
Wanaume hao wawili hawakuisha kumtupia macho karani wa mahakama. Kila mmoja alikuwa na yake fikrani. Wote walijaribu kuvuta kumbukumbu ya kule ambako waliwahi kuiona sura ya karani yule wa mahakama. Kwa kuwa kila mmoja hakuwa na uhakika, hawakuhitimisha kumtambua karani yule. Jambo lililowatatiza ni muda. Walipounganisha matukio ya historia ya mtu waliyemfahamu na yule aliyembele yao, hisi zao hazikuwaruhusu kumbatiza mtu yule kuwa ni Carolina aliyekuwa duni. Walihisi labda alifanana lakini hakuwa ndiye.
“Huyo karani unamfahamu?” alihoji Koi kwa kunong’ona.
“La hasha! Hata mimi nilitaka kukuuliza, lakini namfananisha tu.”
“Anafanana sana na Carolina!” alisema Koi. “Lakini naona macho yanaongopa. Atakuwa siye.”
“Carolina! Inaweza kuwa ni yeye. Lakini mbona……..” alisema Oli kisha alikatisha maneno yake. Mahakama ilikuwa tayari kung’oa nanga.
“Koooooooorti!” aliipaza sauti askari aliyekuwepo nyuma ya watuhumiwa. Watu wote walisimama na baada ya muda zilipofuatwa taratibu zote za kuanza kusikiliza mashauri, watu waliketi. Wengine walikuwa wima wakichungulia kupitia madirishani. Oli na Koi walikuwa bado wamesimama.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Wadhamini wa Tunu binti Koi, wote wawili wanatakiwa waje hapa,” alisema karani wa mahakama. Alikuwa akichorachora kwenye karatasi. Alipomaliza alimpatia hakimu jalada la kwanza kati ya aliyokuwa nayo mkononi. Muda huo Koi na Oli walikuwa mbele ya meza ya karani wakisikiliza walichoitiwa. Karani aliongea nao kwa sauti ya chini, aliwapatia vijikaratasi wakatoka navyo. Wakati wanaongeleshwa na karani, walipata muda wa kumtazama vizuri karani. Oli alibaini fika kuwa yule alikuwa Carolina. Hatimaye walirudi sehemu walizokuwa wamesimama.
Taratibu za kimahakama zote zilizingatiwa. Hakimu na mwendesha mashitaka walikuwa bega kwa bega. Karani naye alikuwa makini kuweka kumbukumbu alizoona zinafaa. Hapakukosa kituko mahakamani pale.
“Kila mmoja anatakiwa kujibu kadri ya uelewa wake,” alisema hakimu. “Kweli au sikweli,” aliongeza hakimu. Alikuwa kawatazama Tora na Tunu baada ya kuwa yamesoma maelezo kwa muda mrefu tena kwa kina. Tunu alisomewa makosa mawili na Tora aliomewa matatu.
“Tora.”
“Kweli mheshimiwa.”
“Tunu!”
“Si kweli mheshimiwa,” Tunu alikana mashitaka yote. Tora aliafiki kila kosa alilokuwa ameulizwa. Hali ya kupishana kwa kauli zao kuliwafanya watu waliokuwa wamefurika mahakamani kuangua kicheko. Hakimu baada ya kuwahoji aliinama na kuanza kuchorachora kwenye karatasi zilizokuwa kwenye majalada yale. Alipomaliza alimtazama mwendesha mashitaka kwa sekunde kadhaa.
“Mwendesha mashitaka!”
“Mheshimiwa, kuahirishwa kwa shauri.”
“Nafasi ya dhamana ipo wazi kwa watuhumiwa wote. Kila mmoja alete wadhamini wawili wenye mali isiyoweza kuhamishika,” alisema hakimu. Hatimaye mahakama iliahirishwa. Hakimu na jopo lake waliondoka kwenye ukumbi wa mahakama. Tunu na Tora walichukuliwa kwenda mahabusu. Koi na Oli hawakutimiza masharti ya dhamana.
Baada ya kuwa mahakama imeahirishwa, Oli alitaka kudodosa zaidi. Alitaka kujua kama kweli yule aliyekuwa mbele yao kama karani alikuwa ni Carolina au la. Aliondoka hadi kwenye ofisi ya karani ili kuuliza muda ambao mahakama ingeanza kusikiliza mashauri siku iliyokuwa inafuata. Alipofika huko, Carolina alijidai hakuwa anamfahamu Oli. Alipofika ofisini hakuhangaika kujua kuwa ndiye au siye. Alipotazama kwenye kitambulisho alichokuwa kakivaa karani yule moja kwa moja alisoma na kubaini kuwa alikuwa ni Carolina. Hatimaye aliondoka kwenda kuungana na Koi wakaenda zao nyumbani.
Walipofika nyumbani, walimsimulia mama Tora mambo yote yalivyokuwa yakiendelea. Hawakuacha kumjuza kile walikuwa wamekibaini mahakamani. Uwepo wa Carolina kama karani kuliwafanya kutokuwa na imani na taratibu zote za mahakama, walihofia kuhujumiwa na Carolina.
Muda wa kazi ulipomalizika, Roy na Carolina tena walikutana kwa mazungumzo. Ilimlazimu Roy kumbeba Carolina kumpeleka nyumbani kwake. Siku hiyo walikaa kitako kuyajadili mambo mbalimbali yaliyokuwa yakiwahusu. Sebule ya Carolina baada ya kufanya kazi kwa miezi sita ilikuwa ya kisasa, ilivutia na kuyaburudisha macho. Pamoja na yote, Roy hakuwa amelisahau ombi lake la kumtaka Carolina kuwa wake wa huba. Carolina naye aliingiwa akilini na tabia njema za Roy, japo alimzungusha na kuikwepa mitego yote aliyotegewa, nafsini alikuwa kamhifadhi. Wakiwa katikati ya maongezi, waliusikia mlango unagongwa.
“Nani anagonga?” aliuliza Roy.
“Ondoa wasiwasi.”
“Isijekuwa ni bwana’ko.”
“Wala! Hivyo unadhani nishakuwa kirukanjia?”
“Si hivyo. Naogopa isije ikawa habari hapa mjini.”
“Ngoja nimsikilize.” alisema Carolina wakati akielekea kuufungua mlango.
“Karibu! Pita moja kwa moja ndani.” Alimkaribisha mgeni na kusabahiana.
“Roy, huyu ndiye mama yangu mzazi niliyekuambia.”
“Naam! Karibu sana mama. Nafurahi kukufahamu.”
“Asante mwanangu! Nimefurahi leo Caro kukukuta na mkwe wangu.”
“Umejuaje mama kuwa huyu ndiye mkweo?”
“Jicho la mtu mzima halifundishwi kuona. Nimeona nikajua. Pia sijawahi kusikia wala kuona mtu yeyote akiwa hapa.”
“Yawezekana akawa japo……”
“Haya yaishe nilikuwa nachombeza tu,” alidakia mgeni. Kwa pamoja waliangua kicheko.
“Nimekuja mbiombio nataka kukuuma sikio. Sijui nisema ama tutoke nje kidogo?”
“Usiwe na mashaka mama. Mgeni wangu asikutie shaka. Huyu ni mwema zaidi yangu. Sema tu, hakuna shida.”
“Sawa. Baba yako na rafikiye wanavikao visivyoisha hapo nyumbani. Leo wamerudi tu kutoka mahakamani wakaketi. Wanachozungumza ni juu yako. Nimejaribu kuwasikiliza kwa makini, wanadai mahakama haitatenda haki kwa sababu yako. Hivyo mahakama ikitenda kinyume na matakwa yao, chamoto utakiona. Sasa kaa ujipange. Walipofahamu kuwa upo mahamani limewashuka shuuu! na Ukweli sijui uliwakosea nini?”
“Mama usijali. Lakini ahsante sana kwa taarifa. Nitajua jinsi ya kuenenda.”
“Lakini pia……..basi siku nyingine sasa!”
“Nooh! Sema! Niambie mama. kama kunachochote sema. Mimi ni mwanao japo si wa damu Tora. Hupaswi kunificha jambo.”
“Nilikuwa nahitaji fedha kidogo ya kunisukuma. Baba yako siku hizi haeleweki. Kila kuki………”
“Inatosha mama usiendelee. Shika hela hii itakufaa kwa kesho asubuhi na mchana. Kesho jioni, muda kama huu uje nitakupatia fedha ya kutosha kuendesha maisha yako. Wala usiwaze kuhusu pesa mama. Changu chako mama yangu. Pole sana,” alisema Carolina wakati akitoa noti mbili za elfu kumi kumi kutoka kwenye mkoba wake. Mama Tora alizipokea na kuzifunga kwenye ncha ya kitenge. Aliaga kuondoka. Carolina alimfungulia mlango na kumsindikiza hatua chache.
“Unapaswa uchukue usafiri ili uwahi nyumbani. Usiku unazidi kuwa mkubwa,” alishauri Carolina. Mama Tora alirudi nyumbani.
Jambo ambalo alikuwa kalieleza kwa Carolina halikuwa siri. Wakati anaondoka kwenda kwa Carolina usiku ule baada ya kuwatengea chakula, Oli alilisikia lango la geti likipiga kelele. Mama Tora hakulifunga akitarajia kurudi mapema. Kelele zile za geti zilimtoa Oli ndani hadi langoni. Muda huo aliangaza macho na kuita lakini mkewe hakusikia. Alipochungulia nje kwa mbali aliona amkewe akiwahi pikipiki na kuipanda. Oli naye aliamua kuchukua pikipiki akamfuata kwa nyuma. Alifuata kwa nyuma kwa kumvizia hadi alipobaini alifika na kuingia kwenye nyumba asiyojua mhusika wake. Wakati wakiwa ndani, Koi aliyasikia yote. Alikuwa kajibanza nyuma ya dirisha. Alipohakikisha kakipata kilichompeleka mama Tora kule, alirudi haraka kabla ya mkewe.
“Waume, mmeona kimya nilitoka mara moja,” alisema mama Tora baada ya kuingia ndani. Alipoangaza macho kwenye meza ya chakula vyombo havikuwepo. Oli na Koi walikuwa wameketi wakiangalia runinga. Oli hakujibu kitu isipokuwa Koi ndiye aliitikia kwa kicheko na kutabasamu.
“Mwenzako anagubu huyu! Kanikosa sekunde moja basi midomo kaivuta. Huwa hataki kabisa niutoe mguu wangu hapa,” alisema mama Tora.
“Shemeji, lazima abiria achunge mzigo wake. Kwani ulienda wapi?” alihoji Koi. Swali hilo lilimfanya Koi kutega sikio kwa makini kusikiliza jibu.
“Nilikimbia kibandani shemeji. Wakati nafunga nilisahau enti zangu za mauzo ya leo. Isitoshe kesho namimi nataka kwenda mahakamani kusikiliza hatima ya mwanangu,” alieleza mama Tora.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Sawa shemeji. Umefanya vizuri kuifuata. Huwezi kujua, usiku ni mrefu.”
Mama Tora aliingia chumbani na alipotoka alielekea bafuni kuoga. Walilala mzungu wanne. Usiku mzima ulimalizika, Oli na mkewe hawakusemeshana. Koi alionekana kufura hasira. Mam Tora alijua ni kwa sababu tu ya kuwa aliondoka kwa muda mfupi. Usilolijua ni sawa na usiku wa giza, Oli alifahamu na kusikia kila alichokisema mama Tora alipokuwa kwa Carolina. Alijipa muda wa kuchunguza zaidi!
*****
Asubuhi ilifika, Carolina na Roy waliamka na kuoga bafuni pamoja. Usiku wao ulikuwa mzuri kila mmoja aliufurahia. Walielekea kazini. Usiku ule uliwakutanisha na kufahamiana vilivyo. Hakuwepo kati yao ambaye hakumfahamu mwenzake. Roy wakati akiendesha gari, njia nzima aliiwaza heshima kubwa aliyotunukiwa na Carolina. Hakuwahi kuota kukutana na Carolina akiwa mwanamwali. Lilikuwa jambo ambalo lilimfanya azidi kumpenda Carolina mbali na fikra zote alizokuwa nazo tangu amkute akiwa kafunikwa macho na Koi kule bustanini. Hakuwa na lolote la kuweza kumtoa kasoro tena kwa awali iliyomvutia. Aliuahidi moyo wake kuilinda heshima aliyotunukiwa.
Moja kwa moja Roy aliiendesha gari na kwenda kumshusha Carolina mahakamani ambako ilikuwa ofisi yake. Carolina tabasamu usoni lilimtoka kwa kulazimisha. Si kwa kuwa alikuwa na hasira, alikuwa na furaha iliyofifishwa na maumivu ya kuagana na usichana wake. Hakuwa na haiba kama siku nyingine, ingekuwa kwa hiari yake, siku hiyo asingeweza kwenda kazini. Lakini kwa kuwa ilikuwa kazi ya kuajiriwa, alilazimika kwenda kuyatimiza majukumu yake.
Roy alipoondoka ofisini kwa Carolina, moja kwa moja alienda hadi ofisini kwake. Tofauti na Carolina alivyojisikia, yeye alikuwa na furaha nafsini mwake. Kilichokuwa kikimuumiza ni pale alipowaza zawadi anayostahili kumpatia Carolina. Kila zawadi aliipanga lakini aliiona kuwa thamaniye ilikuwa ndogo kulinganisha na kile alitunukiwa. Bado ilimpasa kuumiza kichwa akipate cha kumfaa msiri wake.
Mahakama ilivyoketi, taratibu zote zilizingatiwa. Ulifika wakati wa hakimu kutoa hukumu kwa yaliyowasibu Tora na Tunu. Hakimu aliketi kitini akitafakari na kuandika. Alipekuapekua karatasi zilizokuwa mkononi mwake na kuzisoma moja baada ya nyingine. Miwani yake mikubwa ilikaa machoni vizuri. Aliwatazama kwa mpigo Tora na Tunu waliokuwa wamejikunyata kwa hofu. Oli na Koi walikuwepo sehemu ileile ambayo siku iliyopita walisimama. Mahakama muda huo ilikuwa kimya. Macho yote ya waliokuwa hapo yalikuwa kwa hakimu na wakati yaliwatazama kwa mpigo Tora na Tunu.
“Baada ya mahakama kuzipitia hoja za upande wa mashitaka na upande wa utetezi, nalazimika kuyahitimisha mashitaka yote. Watuhumiwa walipofikishwa hapa walituhumiwa kwa makosa matano kwa pamoja. Tora bin Oli alishitakiwa kwa kutenda jumla ya makosa matatu. Makosa hayo ni; moja, kutumia kinywaji kilichopigwa marufuku, kiroba. Pili, ni kutumia kilevi kwa wakati usiofaa, wakati wa uzalishaji kinyume na sheria za mji wa Tumanini zinazowataka watu wake kutumia kileo au kufanya starehe baada ya saa za kazi. Na kosa la tatu linatokana na bwana Tora kumshambulia bi. Tunu kwa chupa. Kwa upande wa bi. Tunu, alikabiliwa na makosa mawili. Kosa la kwanza ni kuuza kilevi haramu kilichopigwa marufuku, kiroba na kosa la pili ni kufungua biashara na kuuza kilevi saa za uzalishaji,” aliongea hakimu. Mahakama ilikuwa kimya ikisikiliza kitakachotokea.
“Kwa maana hiyo, makosa yote yanabeba dhana mbaya ya jinai. Yakiwa na maana kuwa yanalenga kuuhujumu uchumi wa taifa la Tupendane, katika mji wa Tumaini kwa makusudi,” alieleza hakimu. Koi na Oli walitazamana. Hawakuwa na neno la kusema bali walipaswa kusikiliza uamuzi wa mahakama.
“Makosa haya kwa mujibu wa katiba, sheria na kanuni, kifungu cha sheria “A” kipengele (c) na ibara ndogo ya pili (2) iliyopitishwa kwa marekebisho ya dharula mwaka 2000, na Bunge la Jamhuri ya watu wa Tupendane, ni wazi mahakama inahitimisha shauri kwa haki juu ya niliyoeleza kwa usawa. Mzani lazima uwe na ulinganifu usiegemee upande mmoja, awe tajiri hata maskini, haki yake ataipata,” alidodosa hakimu. Watu wote mahakamani walikuwa kimya wakisikiliza. Hamu yao ilikuwa kuisikia hukumu, kuachiwa au kutiwa hatiani kwa watuhumiwa.
“Kwa mamlaka niliyopewa na kwa hekima na uzalendo juu ya ustawi wa Jamhuri ya watu wa Tupendane, na kwa matakwa ya kanuni za mji wa Tumaini, napaswa kutoa hukumu sasa,” alisema hakimu kisha kunyamaza kidogo. Mikono yake ilipekuapekua karatasi, alisoma kila ukurasa juu juu na kuhitimisha kimyakimya.
“Bi. Tunu kwa makosa yote mawili, atakwenda jela kwa miaka mitatu na akitoka alipe faini ya shilingi milioni mbili,” alisema hakimu kwa kuyadondoa maneno. Mahakama ilizizima kwa miguno. Watu walinong’ona chinichini. Koi hakuwa imara tena, alinyong’onyea. Hakuweza kutamka zaidi ya kumwegemea Oli ambaye alikuwa makini kungoja hukumu ya mwanaye. Tunu alikuwa kapigwa ganzi, alisimama wakati machozi yakimshuka na kuchuruzika mashavuni. Baada ya kelele kupungua, kulitawala ukimya tena.
“Kwa upande wa Tora bin Oli, makosa yake matatu yanamtia hatiani. Atatumikia kifungo na kazi ngumu gerezani kwa miaka saba bila faini baada ya kutoka. Adhabu zote zinapaswa kuanza sasa. Hakuna nafasi ya rufaa katika mahakama yoyote!” Hakimu bwana Kifenenge alihitimisha. Mahakama ilipigwa butwaa. Oli na Koi walitazamana kimyakimya. Wakati huo hakimu alitoka na baraza lake na kuuacha ukumbi wa mahakama.
Tora na Tunu walichukuliwa moja kwa moja na kupelekwa katika gereza la kilimo katika mji wa Tumaini. Japo walilia na kumwaga machozi, hawakuweza kuibadili hali iliyowapata. Mguu wa mama Tora pale mahakamani ulikuwa mbaya. Oli kila alipomtazama hakuisha kumtazama kwa macho ya hukumu. Mama Tora baada ya kuyasikia yaliyompata mwanaye, macho hayakuwa makavu. Pamoja na kuwa hakuwa na mahaba na mwanaye, uchungu wa mwana ulimkata akayaporomoa machozi.
Oli na Koi walipaswa kuondoka mahakamani wakiwa wanyonge. Mambo yaliwakataa. Mama Tora kwa kujisahau alikwenda hadi kwa Carolina na kumkumbatia. Jambo hilo lilimzidishia hasira Oli na kutaka kuujua uhusiano wao dhahiri. Hakuweza kuvumilia, moja kwa moja alienda hadi walipokuwa mama Tora na Carolina.
“Hayajaisha bado!” alisema Oli kumwambia Carolina. Alimvuta mkono mke wake wakaondoka. Muda wote alimlaumu mkewe kuwa alishiriki kuihujumu familia. Aliapa kulipa kisasi kwa yeyote aliyehusika. Pamoja na mama Tora kulaumiwa, waliporudi nyumbani hakuwa na furaha. Koi na Oli hawakuacha kuketi na kuteta. Hukumu dhidi ya wapendwa wao iliwanyong’onyesha na kuwafanya kumchukia kila mtu. Fikrani, walijua kulikuwa na shinikizo alilolifanya Carolina kama njia ya kulipa kisasi kwa niaba ya mama yake. Waliyoyawaza hayakuwepo akilini mwa Carolina. Katika tafakari yake, Oli alianza kumshuku mkewe kuwa alikuwa na jambo la siri.
“Koi, napata wasiwasi sana na mienendo ya mke wangu.”
“Kwanini unasema hivyo?”
“Mke wangu simwelewi, yapo mengi ambayo anayafanya na kunifanya nitie mashaka. Sasa Tora katiwa hatiani na miaka saba inamtafuna. Bila aibu, anakimbia kwenda kumkumbatia adui. Huoni kama anahusika na amebakiza kuniua ili arithi mali zangu zote? Tora akitoka huko hatakuwa na nguvu tena. Mimi sijui kama nitakuwa hai. Sasa ninachokiona, huyu mwanamke anataka kuniua ili achukue chake mapema. Na njama hizi fika anazisuka huyu jini Carolina. Nikifa lazima atabaki mke wangu ambaye ni rafiki yake. Kumuua mwanamke ni sawa na kumponda sisimizi kwa kinu. Hatachelewa kummaliza na hapo ndipo Carolina atajihakikishia umiliki wa mali zangu zote,” alieleza Oli.
“Inawezekana usemayo yakawa kweli, lakini unahakika gani kama shemeji anahusiana kwa karibu na Carolina?”
“Hakuna siri. Kumbuka jana alitenga chakula hapa na kutuacha. Niliposikia lango kuu likipiga kelele nilifuatilia hatua kwa hatua. Alikokwenda nilimfuata, kibaya zaidi nilisikia kila walichozungumza. Ninahisi ndiko kwa Carolina huko. Sasa najaribu kuwaza, kabla hata siku haijaisha, badala ya kuomboleza kifungo cha mwanaye, anasherehekea. Na leo lazima atakwenda tena huko sababu jana waliahidiana kupeana hela. Unadhani pesa anazopatiwa zinanunua nini kama si chambo ya kutaka kumhadaa?” alisema Oli.
“Yawezekana hivyo? Kama hali iko hivyo, inapaswa kuchukua hatua ingali mapema. Ukute wanapanga kukumaliza na muda wenyewe yaweza kuwa sasa.”
“Sasa anahangaika nini, angenitilia sumu maramoja ningekauka. Unashuri nifanye nini, maana nimepanga kuwamaliza wote kwa pamoja. Wakikutana tu kupeana hela, hukohuko nitawaangamiza. Najua hakuna atakayejua,” alisema Oli.
“Fanya hivyo. Kabla adui hajakumaliza, mmalize!” Alisema Koi. Walikubaliana uamuzi wa kuchukua ili kuukata mzizi wa fitina. Mama Tora hakuwa na taarifa yoyote juu ya kile kilipangwa. Alichokuwa akikiwaza ni kuusubiri muda ufike ili aweze kwenda kwa Carolina kujipatia ile pesa aliyokuwa ameahidiwa. Alipika chakula harakaharaka. Chakula kilipokuwa tayari, aliwatengea. Mama Tora aliaga kwa mmewe. Alisema anakwenda dukani kuangalia kama kulikuwa salama baada ya kutwa nzima kutokuwa huko. Hakumkatalia. Baada ya kumruhusu, Oli alitazamana na Koi. Walitazamana na kutingisha vichwa kwa sikitiko. Mama Tora aliondoka!
Mama Tora alipotoka, Oli alimchungulia na kumwona akielekea njia ile ambayo usiku uliotangulia pia aliipita. Oli tayari alitambua kule mkewe alikuwa akielekea. Aliingia ndani hadi chumbani. Alitafakari jinsi ya kufanya na hatimaye alikata shauri kuwahi. Alivaa viatu vyake vya kufunika, vikubwa vyenye soli ngumu na virefu. Koi hakwenda peke yake, alimchukua rafiki yake na kumpakiza kwenye gari. Walipokaribia mahali walipokuwa na mashaka napo, Oli aliliegesha gari mbali kidogo na pale. Aliteremka na kumwacha Koi. Hakwenda moja kwa moja kwenye nyumba ile, ilimpasa kwenda hadi kwenye duka lililokuwa karibu na pale.
“Naomba vocha mbili za alfu-alfu.”
“Nikwangue zote?” aliuliza muuza duka.
“Kwangua moja, nyingine usikwangue,” alisema Oli. Alipokea vocha alizonunua. Zilikuwa vocha mbili za elfu moja moja ambazo zilikuwa hazijaachanishwa. Alibonyezabonyeza vitufe vya simu yake kuijaza vocha kwenye simu. Alipomaliza aliitia simu na vocha kwenye mfuko wa shati. Hatimaye aliondoka hadi kule alikusudia kuelekea.
Alipoifikia ile nyumba, Oli alizunguka moja kwa moja upande wa nyuma. Alisikia sauti ya runinga ikiporomoa muziki. Alipochungulia, alimwona mkewe akiwa kaketi kwenye kochi akitazama matukio yaliyokuwa yakirushwa na runinga ile. Alitulia dakika chache akichunguza lakini hakuonekana mtu akiungana naye pale. Oli aliamini kuwa Carolina alikuwa chumbani ambako taa ilikuwa haijawashwa. Alikata shauri! Aliufikia mlango na kugonga taratibu.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nakuja mwanangu subiri,” alisema mama Tora. Alinyanyuka na kuufikia mlango kisha kuufungua. “Pole, karibu!”
“Asante!” aliitikia Oli. Alimtazama mkewe aliyekuwa kajaa hofu akijaribu kuuficha uso wake. Oli alitafakari kwa haraka na kugundua kuwa lazima Carolina alikuwa nje. Alijua mambo yaliharibika, hivyo aliamua kumfanyia ufirauni mkewe. Alimzoa pale alikuwa kasimama kwa mguu wake. Mama Tora alijihami akijaribu kumkimbia mmewe. Kona kwa kona alijaribu kwenda. Alipanda kwenye makochi ili amkwepe lakini ilikuwa vigumu. Oli aliizima taa ya sebuleni. Alitulia kidogo ndipo alipomnasa mkewe na kumporomoa sakafuni. Oli alilikamata koo la mkewe na kumtua chini kama mzigo. Aliuziba mdomo wake kwa kitambaa. Alimkandamiza akaziba njia ya pumzi kooni. Aliitengua shingo kwa kuinyonga upandeipende. Alimwachia mkewe akazunguka sakafuni na kutulia pale gizani. Wakati wa purukushani zile aliusikia mshindo wa simu. Ilianguka chini hivyo alipapasa kuitafuta. Hakuweza kuiona! Aliwasha taa na kuiokota kisha aliizima tena taa na kutoka harakaharaka.
Oli alielekea sehemu alipokuwa kaliegesha gari. Akiwa analikaribia, alipishana na pikipiki iliyokuwa imembeba mtu ambaye alihisi kuwa ni Carolina. Aliingia kwenye gari na kuliondoa. Wakati wanapishana, Carolina naye alihisi mtu yule kuwa ni Oli. Alienda moja kwa moja hadi nyumbani kwake. Alipofika alistaajabu kuona mlango ukiwa wazi na taa ikiwa imezima. Alipoingiza mguu wake ndani, aliiwasha taa. Hamadi! Mama Tora alikuwa kajaa sakafuni. Carolina alipigwa butwaa akabaki mdomo wazi. Aliuchapua mguu wake hadi pale mama Tora alikuwa kalala. Alimtazama pasipo kumgusa ndipo alipogundua kuwa hakuwa anapumua.
Carolina alitoka nje akiwa mtulivu. Hakutaka kupiga kelele. Alitafakari akitafuta njia ya kuweza kulitatua tatizo lile. Baada ya sekunde chache akiwa nje ya nyumba, aliamua kumpigia simu Roy. Alimtaka kufika kwake haraka. Roy alipoikata simu, kama alivyoombwa aliingia kwenye gari. Moja kwa moja alifika nyumbani kwa Carolina. Alimkuta Carolina akiwa nje. Hakuwa na utulivu, alikuwa kama mtu aliyevamiwa na siafu. Moja kwa moja Roy alitoka kwenye gari na kutembea hadi kumfikia Carolina alipokuwa kachutama. Alichutama na kumshika bega.
“Mbona huna furaha, kuna tatizo?” alihoji Roy. Carolina aliendelea kuporomoa machozi. Alipogundua Carolina alikuwa katikati ya kilio ilimtaka kufanya udadisi.
“Nyanyuka njoo!” alitamka Carolina wakati akielekea mlango kwake. Carolina hakuingia ndani alibaki mlangoni na kumwacha Roy kuingia ndani. Roy alipomwona mwanamke akiwa chini aligutuka.
“Kafanyaje?”
“Mimi sijui. Alifika hapa kama nilivyomwahidi jana. Sasa sikuwa na pesa ya kutosha ndani nikalazimika kwenda ATM kutoa pesa. Niliporudi nilikuta hali hii ila taa ilikuwa imezimwa,” alieleza Carolina. Roy alizunguka mle ndani akichunguza. Alimtazama mama Tora tena na tena bila kumshika.
“Naomba niletee tochi, mwanga wa taa zako hautoshi,” alisema Roy. Carolina aliingia chumbani na kurudi na tochi. Roy alimmulika mama Tora shingoni. Aling’amua jambo. “Kuna mtu kamnyonga.”
“Kanyongwa! Nani kafanya hivi?”
“Hupaswi kutaharuki. Kuwa na utulivu maana imeshatokea. Nawewe utakuwa wa kwanza kuisaidia polisi kwa jambo hili. Lakini ukweli ukipatikana utakuwa huru,” alieleza Roy. Carolina hakuamini maneno aliyoyasikia kutoka kwa Roy. Wakati huo Roy alipiga simu kituo cha polisi kuomba gari na askari. Wakati akisubiri gari kufika, Roy alizunguka pale sebuleni. Alipotazama kwenye makochi, alikichukua kitambaa kilichotandikwa juu yake. Alikichunguza kitambaa na kuona alama ya unyayo wa kiatu ukiwa kama mhuri. Alikikunja na kukiweka tayari kwa ushahidi. Alichukua tochi na kuiwasha akimulika sakafuni, napo aliona zile alama za unyayo wa kiatu. Alitoka kuizunguka nyumba akimulika kwa makini. Alipofika nyuma, aliona nyayo za viatu zikiwa kwenye mfereji uliopokea maji machafu kutoka ndani ya bafu la Carolina. Alirudi!
“Bila shaka tutampata mhusika. Lakini kwa nijuavyo, utakuwa chini ya ulinzi hadi apatikane. Hii ni kwa sababu hapa ni kwako na hakuna mtuhumiwa wa awali zaidi yako.”
“Mimi tena nishikwe wakati sikuwepo! Roy nisaidie mpenzi. Siwezi kulala rumande bila sababu.”
“Taratibu za kazi yangu zinanitaka iwe hivyo. Wakija polisi utaenda nao. Nitafanya upelelezi kwa muda mfupi. Hadi kesho atapatikana aliyehusika. Amini ninachosema, mazingira nimeshayaona.”
“Asipopatikana!” alihoji Carolina.
“Atapatikana. Najua hujahusika. Kwani ulimgusa baada ya kumkuta hivi?” alihoji Roy.
“Hapana. Sijamgusa kabisa.”
“Inakupasa uwe mtulivu na ushirikiane na polisi. Usiwe na mchecheto tafadhali.”
“Sawa, nitakuwa mtulivu,” alisema Carolina. Wakati huo gari la polisi lilikuwa mbele ya nyumba ya Carolina. Majirani nao walikuwa wamefika na kuzunguka eneo lile.
Taratibu za kijeshi zilizingatiwa kumtoa mama Tora kutoka sehemu ile. Baada ya kuwa ameondolewa na kupandishwa kwenye gari. Roy aliamuru askari wawili kubaki pale hadi asubuhi ifike ili taratibu za ziada za kipelelezi ziweze kufanyika. Carolina alilipanda gari la polisi na kuondoka hadi kituoni kama mtuhumiwa wa kwanza. Mama Tora tayari alikumbwa na umauti.
Baada ya kufikishwa katika kituo cha polisi, Carolina alihojiwa. Katika maelezo yake alitakiwa kutaja mtu ambaye alimhisi kuhusika kwenye tukio hilo. Carolina hakuacha kutaja. Alimtaja Oli kuwa ndiye mshukiwa wa kwanza kwani wakati ule anarudi kutoka kuchukua pesa, alipisha na mtu aliyemfananisha naye. Na pia gari alilolipita njiani lilikuwa ni kama lile ambalo Oli alikuwa akilimiliki.
Baada ya kutajwa kwa Oli, usiku uleule walitumwa maaskari. Waliongozana na Carolina ambaye alipafahamu mahali alipokuwa akiishi. Walipofika walimchukua na kumwacha Koi akiwa peke yake kwenye nyumba ile. Safari ya kurudi kituoni ilifanyika haraka. Baada ya kuhojiwa usiku ule Oli alikataa katakata. Badala yake alilalamika na kuapa kumtafuta aliyesababisha kumuua mkewe. Wapelelezi waliamua kumpa muda ili kuingoja asubuhi kufika ili waweze kuupata ukweli. Ilikuwa patashika ya kumsaka muuaji.
Asubuhi iliyofuata, Roy hakuweza kuketi chini. Aliondoka moja kwa moja hadi nyumbani kwa Carolina. Alizunguka tena pale nje akitazama kwa makini nyayo za viatu zilizokuwa zimekanyaga eneo oevu la nyuma ya nyumba ya Carolina. Wakati huo aliweza kuona nyayo zikiwa zimeacha alama iliyoonekana kwa kukoleza. Alipiga alipiga picha unyayo wa kusho na wa kulia kwa kutumia simu. Aliandika maelezo mafupi kwenye shajara yake.
Alitoka nyuma ya nyumba na moja kwa moja alielekea mlangoni. Aliusukuma mlango na kuingia sebuleni. Maaskari waliokuwa wakilinda pale mmoja aliingia ndani kumsindikiza, mwingine alibaki nje kwa ajili ya usalama. Roy aliikagua sakafu kwa makini, michirizi ya tope iliyoachwa baada ya kiatu chenye tope kukanyaga ilionekana dhahiri. Alichunguza kila taratibu lakini hakuona kingine zaidi cha kuweza kumsaidia katika upelelezi wake. Aliamua kutoka ili aondoke zake.
Alipiga hatua mbili akiukaribia mlango, wakati akitaka kupiga hatua ya tatu nafsi yake ilimkemea na kumnong’oneza, ‘usiondoke, rudi ndani kuna kitu. Alitii. Aligeuka na kutembea hadi kwenye meza na kusimama mbele. Macho aliyasafirisha kwa kila kochi lakini bado kiahiria kipya cha ushahidi hakukiona. Aliisukuma meza kwa mguu wake ikahama mpaka kwenye ukutani. Alitazama chini na kukiona kisu kidogo. Alikishika kisu na kukichunguza lakini kwake hakikuwa na umuhimu. Alikirudisha kwa kukirusha. Alipotazama sakafuni kwa makini, aliiona vocha. Upande mmoja ulikuwa umekwanguliwa na upande mwingine haukuwa umekwanguliwa. Aliichukua na kuigeuzageuza, huku anatafakari. Hatimaye aliamua kuifungua shajara yake na kuipachika ile vocha ndani. Aliandika maelezo kidogo kwenye ukurasa ilipokuwa vocha. Alipomaliza, aliifunga shajara na kuondoka.
Wakati anarudi kituoni, Roy aliwaza njia nzima. Alijaribu kutafakari juu ya mtu aliyehusika kumuua mama Tora. Alijitahidi kujiuliza pia, sababu zilizomfanya muuaji atekeleze unyama huo. Hakuishia hapo, alijiuliza, kwa nini mama Tora auawe wakati akiwa kwa Carolina na si mahali pengine? Kila alipojaribu kuunganisha matukio, hakupata kubashiri. Kufika kwake kituo cha polisi kulimfanya aongoze moja kwa moja hadi ofisini kwake. Aliwaagiza maaskari waliokuwepo pale kumpeleka Carolina kwa ajili ya mahojiano juu ya swala lile. Carolina alipofikishwa, walianza mahojiano.
“Kwanza pole sana.”
“Asante!” alijibu Carolina kwa makato. Alikuwa anajikuna mwilini. Vipele vingi viliota mikononi sababu ya mbu waliomdokoa usiku kucha.
“Nieleze, kwa nini katika maelezo yako unamshuku Olin a si mwingine?”
“Kwa sababu nilimwona akiwa kwa mguu akielekea kwenye lile nadhani lilikuwa gari lake.”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Unadhani! Kwa nini udhani pasipo uhakika?”
“Kwa sababu kulikuwa na giza sikuweza kuuona uso wake. Lakini umbile lake na gari ndivyo vinanifanya niamini hivyo. haiwezekani mtu wa kukisia iwe kwa gari na umbile.” Alieleza Carolina.
“Unadhani kwa nini amemuua mama Tora?”
“Labda kwa sababu alikuwa na mawasiliano na mimi. Lakini hata mahakamani, baada ya kutolewa hukumu ya majalada yale mawili, mama Tora alikuja kunisalimia. Baada ya pale na Oli alikuja kumvuta mke wake. Kabla hajamvuta kutoka kwangu alisema maneno yanayonitia wasiwasi sana.”
“Alisemaje?”
“Alisema, hayajaisha!”
“Kwa nini unaamini maneno hayo yanahusiana na kifo hiki?”
“Kwa kweli aliyasema akiwa na hasira. Na kama unakumbuka juzi usiku alipokuja, alieleza mambo kadhaa kuwa hawaelewani. Na kutoelewana kwao ni sababu yangu. Huyu mama amekuwa akinitetea na kila hatua ameniweka karibu, sasa nadhani anaona akimuua atakuwa ameukata mzizi wa fitina.”
“Kwa nini asiukate mzizi wa fitina kwa kukuua wewe amuue mkewe tena aliyeoana naye miaka mingi. Huoni kama unamshuku kwa makosa?”
“Hapana Roy, mimi naamini hata kumuua mkewe peke yake ilitokea kama bahati tu mimi nikawa nimetoka. Yawezekana kabisa angenikuta angetuua wote.”
“Hapo kwako kuna mtu zaidi yako ambaye kati ya siku za wiki hii alikuja kama fundi bomba au fundi ujenzi?”
“Hapana. Sijawahi kuleta fundi yeyote mwezi huu wa tatu. Mimi nadhani Oli alitaka kuniangamiza pia sababu ya kuwa amegundua asili yangu. Nadhani unaelewa mambo yaliyotokea kwa marehemu mama yangu. Watuhumiwa wa kwanza ni yeye na Oli. Na sasa wako pamoja, huwezi kujua wamepanga nini tena.”
“Sawa. Lakini wameshachelewa kama ndivyo. Hivi huwa unatumia vocha za kukwangua kwenye simu yako?”
“Vocha! Hapana. Huwa nanunua moja kwa moja kwenye simu kupitia akaunti yangu ya benki.”
“Unaweza kukumbuka labda kuna siku alikuja mgeni kwako ukaagiza vocha kwa ajili yake?”
“Hapana. Hata wageni wangu huwanunulia muda wa maongezi mtandaoni. Huwa sipendi vocha za kukwangua kabisa. Tangu ninunue simu, sijawahi kukwangua vocha,” alieleza Carolina.
“Sawa, ni hayo tu.”
“Mbona hivyo, kuna nini?” alihoji Carolina.
“Bado upelelezi unaendelea. Lakini naamini hadi jioni tutakuwa tumepata ukweli.”
“Jitahidi Roy, sehemu hii haifai kabisa kwa binadamu.”
“Usitie hofu, kazi inaendelea vema,” alijibu Roy. Alimwita askari kumchukua Carolina ili kumrudisha rumande. Carolina alipoondoka, Roy alimwita askari aliyekuwa anashughulika na Oli. Alimtaka ampatia jalada la Carolina. Alitumia muda mwingi kuyasoma maelezo ndani ya jalada lile. Hatimaye baada ya kumaliza kusoma, alitaka kupelekewa mtuhumiwa namba mbili ambaye ni Olin a jalada lake. Ilikuwa mara ya kwanza kwa Oli kuonana na Roy katika mizunguko yake. Alipokuwa mbele ya Roy, Oli alitulia na kuhisi kijana yule mdogo asingeweza kumfanya chochote. Tangu Oli afikishwe ndani ya chumba kile, hakumsikia Roy akizungumza kitu zaidi ya kumtazama na kuendelea kuandika kwenye jalada. Hatimaye Roy aliuvunja ukimya.
“Jina lako unaitwa nani?”
“Naitwa Oli bin Tora.”
“Unaweza kueleza, kwa nini upo hapa?”
“Sijui, lakini itakuwa kwa sababu ya kifo cha mke wangu.”
“Kwa nini umemuua mkeo?”
“Mini sijamuua.”
“Hujanijibu. Kwa nini umemuua mkeo?”
“Sijaua? Unajuaje kama nimemuua mimi?”
“Unaikumbuka siku uliyo muoa mkeo ilikuwa juma ngapi?”
“Swali gani? Zamani hiyo wewe ungekumbuka?”
“Mna watoto wangapi?”
“Mmoja.”
“Kwa siku huwa unaoga mara ngapi?”
“Maswali gani unaniuliza. Tatizo lako bado mtoto. Niache niende kama huna maswali ya kunihoji.”
“Mimi ndiye nakuhoji. Kazi yako ni kunijibu. Kuhusu aina ya maswali ya kukuhoji ni uamuzi wangu.”
“Unalijua jina kamili la mkeo?”
“Mama Tora! Eeeeh……”
“Mara ya mwisho kugombana na mkeo ilikuwa lini?”
“Sijui bwana! Maswali hovyohovyo. Uliza taratibu nipate kujibu taratibu,” aling’aka Oli. Roy alikuwa akiandika kila jibu na kila kitendo alichokionesha Oli.
“Huwa unavaa viatu vya aina gani?”
“Viatu, vya kawaida tu.”
“Vya kawaida ni viatu vya aina gani?”
“Hivi vya kufunika, watu wengine akili zenu ni kama za watoto. Unaniuliza navaa viatu wakati unajua hata hapa nimekuja na viatu. Au kwa kuniona hapa sina viatu unaniona mshamba,” alieleza Oli kwa ukali.
“Unavaa viatu namba ngapi?”
“Sijui. Waagize mbwa wenzio wavilete. Kwa kuwa unajua kusoma utajua ni namba ngapi,” alieleza Oli. Roy alimwita askari aliyekuwa karibu na kumtaka kuvileta viatu vya Oli. Vilipofikishwa Roy alivishika mkononi.
“Hivi ndivyo viatu vyako?”
“Ndiyo!”
“Una viatu vingine vya kufunika kama hivi?”
“Hapana. Nina viatu vya wazi vingi. Cha kufunika ni hiki peke yake,” alijibu Oli. Roy aliandika maelezo yote. Oli alikuwa akitabasamu kwa dharau. Roy alikitoa kitambaa kile chenye alama ya tope na kukiweka mezani. Alikichukua kiatu na kukitazama sehemu ya kukanyagia. Alichukua simu yake na kupiga picha sehemu ya soli. Alikibandika kiatu juu ya kitambaa kile kupima ulinganifu wake. Tope lililokuwepo kukizunguka lilikauka lakini lilikuwa bado lipo. Oli aliyatumbua macho akiwa kajawa na mshtuko. Alichokifanya Roy hakukitarajia. Hatimaye Roy alitingisha kichwa kuonesha kuna kitu alibaini. Alitabasamu!
“Ulivaa viatu hivi na kupita kwenye tope ukiwa wapi?”
“Sikumbuki.”
“Sawa, unamfahamu Carolina?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ndiyo.”
“Unamfahamje?”
“Alikaa kwangu.”
“Unafahamu anapoishi baada ya kutoka kwako?”
“Ndiyo! Ah…sipajui!” alijibu Oli kwa kujikanganya. Roy aliandika.
“Una simu ya mkononi?” alihoji Roy.
“Ndiyo, nitakosaje simu ulimwengu huu!” alijibu Oli.
“Unaikumbuka namba yako ya simu?”
“Ndiyo, naikumbuka.”
“Nitajie,” alisema Roy. Oli alitaja namba yake na Roy aliiandika kwenye maelezo aliyokuwa akiyachukua.
“Simu yako iko wapi?”
“Nimekabidhi mapokezi,” alijibu Oli. Roy aliagiza simu ya Oli iwasilishwe kwake.
“Simu yako ni hii?” Roy aliionesha.
“Ndiyo!”
“Huwa unatumia vocha za aina gani?”
“Vocha za kukwangua,” alijibu Oli. Roy alitabasamu. Alimtazama machoni kwa muda mrefu akiwa na utulivu.
“Mara ya mwisho kuweka vocha kwenye simu yako ilikuwa lini?” Roy alihoji. Oli alibaki kimya.
“Hujanisikia swali?”
“Nimesikia, sikumbuki.”
“Una uhakika hukumbuki?”
“Nakumbuka sasa. Jana kama sikosei.”
“Uliweka saa ngapi na vocha ya shilingi ngapi?”
“Jioni, ni ya shilingi elfu moja. Tena nilikuwa nayo hapa!” alisema Oli. Alianza kujikagua kwenye mfuko wa shati lake. Roy alikuwa akimtazama kwa makini. “Siioni, ningekupa maana nilinunua mbili. Nilitumia moja, nyingine nilibakisha,”alijieleza Oli. Roy bado alikuwa kamkazia macho yake. Aliifungua shajara na kuichukua vocha aliyokuwa nayo.
“Vocha yenyewe ni hii?”
“Ewaaa! Ndiyo! Uliipataje?”
“Hupaswi kujua,” Roy alijibu wakati akiiwasha simu ya Oli. Alijaribu kuiingiza ile vocha iliyotumika kwenye simu ya Oli. Baada ya muda ilimletea taarifa kuwa vocha hiyo ilitumika. Ujumbe ule ulitaja tarakimu tatu za namba ya simu iliyoitumia. Roy alipozilinganisha tarakimu zile zilifanana na tarakimu tatu za mwishoni mwa namba ya simu ya Oli. Roy alitabasamu. Wakati huo Oli alianza kuingiwa wasiwasi. Hali ya uchangamfu usoni ulifutika. Mwili ulinywea akawa mnyonge kupita kiasi. Roy aliandika maelezo yake vizuri.
“Unalo jambo lolote la kusema kabla sijafunga mjadala na wewe?” alihoji Roy.
“Sina neno,” alijibu Oli akiwa mnyonge. Akilini mwake kengele ya hadhari ilimjuza kuwa alizidiwa ujanja na kijana yule.
“Sawa. Ahsante kwa ushirikiano wako,” alisema Roy. Alimwita askari wa zamu ili kumchukua Oli.
Baada ya kuhitimisha zoezi zima la kumhoji, Roy alijawa na tabasamu usoni. Aliondoka moja kwa moja hadi ofisini ili kuwasiliana na kampuni la simu ambalo Oli aliutumia. Alitaka kudhibitisha kama kweli namba ya Oli ndiyo ilitumia vocha ile aliyoiokota ndani kwa Carolina.
Ilichukua muda mfupi taarifa alizoziomba Roy zote alipatiwa. Ni kweli namba ya Oli iliitumia vocha iliyookotwa sebuleni kwa Carolina. Tayari Roy alifanya utaratibu wa kumtoa Carolina. Kabla hajaruhusiwa kuondoka kituoni alikuwa na dokezo. Alimjuza Roy kuwa ni vema wangeenda nyumbani kwa Oli ili kumkamata mwanaume mwingine ambaye yawezekana akawa anajua juu ya mauaji hayo. Roy aliafiki na haraka gari ya polisi ilienda hadi nyumbani kwa Oli. Koi hakuwa na wasiwasi, alijua jambo lile lisingemhusu moja kwa moja na hata kama angehojiwa angekataa kwani hakuona wala kusikia.
Maaskari walipofika walimtia mbaroni Koi. Walimchukua moja kwa moja hadi kituoni lakini hawakumhifadhi rumande. Walimpeleka sehemu waliyokuwa wakiita gereji. Sehemu ile ilikuwa mahsusi kuwahoji watuhumiwa sugu ambao walikuwa wagumu kusema ukweli wa waliyoyafahamu. Baada ya kufikishwa gereji, Koi alihojiwa maswali machache.
“Unaitwa nani?”
“Naitwa Koi”
“Koi mkojo, ulijizaa peke yako?”
“Hapana. Koi bin Kihiyo”
“Naam, jina lenyewe linaonyesha wewe ni kihiyo kwelikweli,” alimkejeli askari yule. “Mara ya mwisho kuua ilikuwa lini?”
“Kuua nini?”
“Pumbavu! Hupaswi kuuliza swali. Unapaswa kujibu. Sema siku ya mwisho kuua ilikuwa lini?”
“Sijawahi kuua.”
“Hara kuku au mdudu hujawahi kuua?”
“Nishaua sana, kama kuku!”
“Kuua mtu je?”
“Hapana. Sijawahi kabisa na sitaua.”
“Unamjua Oli?”
“Namjua, ni rafiki yangu.”
“Anaishi wapi?”
“Anaishi Majengo, Tumaini hapa.”
“Wewe kwenu wapi?” Koi alinyamaza kidogo. Alipigwa kofi kali.
“Hamaniko!”
“Umekuja Tumaini lini?”
“Juzi tu. Ninasiku tatu au nne leo.”
“Kwahiyo umekuja kwa ajili ya kuua mke wa rafiki yako?”
“Hapana.”
“Naomba useme ukweli kabla sijawasha mashine, unaiona hii. Leta mchezo utaondoka hapa jogoo hawiki tena.” askari alionesha nyaya za umeme zilizokuwa zinatoa cheche baada ya kukutanishwa. Unajua kwa nini ulifuatwa baada ya kuwa Oli amechukuliwa?”
“Sijui. Labda mniambie sababu.”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Oli amesema kuwa wewe ndiye amekukodi kuja kusaidia kuua mke wake. Kasema alikulipa milioni moja na bado una mdai laki tano akumalizie ndipo uondoke.”
“Muongo! Si kweli, anaongopa. Mimi sijamuua mke wake kabisa.”
“Kama amekutaja kuwa umemuua mkewe, tuambie sasa ni nani. Mpaka sasa wewe amekutaja. Hata sisi tunaamini kuwa wewe umeua kwa sababu ushahidi katupa Oli.”
“Hapana afande. Kaua!”
“Nani?”
“Yeye, Oli.”
“Uliona au …….”
“Sikiliza, aliniacha kwenye gari akaondoka lakini..” Koi alieleza jinsi walivyopanga hadi kuondoka kwenda eneo la tukio. Kila taarifa ilikuwa wazi.
Alipomaliza kuhojiwa, Koi alitwaliwa hadi chumba kingine. Ilikuwa zamu ya Oli kwenda kukili kwa kinywa chake kuwa alihusika. Walipomweleza kuwa rafikiye Koi aliwaeleza bila kuficha jinsi walipanga kwenda kumuua Carolina na mama Tora, Oli alikataa katakata na kusema walimsingizia. Oli fikrani alijua fika kuwa Koi alikuwa kaondoka nyumbani baada ya kuona polisi wakimchukua yeye. La hasha! Mawazo yake yalikuwa kinyume. Alipowabishia sana walimtoa Koi na kumleta mbele yake. Oli aliinama na kukitingisha kichwa baada ya kumtazama Koi akiwa na pingu mkononi.
“Koi, yamekwisha! Umenikoka motoni kwa mafuta yangu mwenyewe,” alisema Oli kisha machozi yalianza kumporomoka. Kwa namna Roy alimhoji na majibu aliyoyatoa pamoja na maneno waliyomwambia kuwa Koi aliyasema, aliishiwa nguvu. Carolina aliachwa huru. Oli na Koi walirudishwa rumande kungoja hati ya mashitaka na hatimaye kufikishwa mahakamani.
*****
Nenda rudi kwa siku nne mfululizo mahakamani ilijibiwa kwa kishindo. Siku hiyo saa saba za mchana, mahakama ilihitimishwa kwa kuisoma hukumu ya kihistoria. Kifungo cha maisha jela kilikuwa stahiki kwa Oli na rafikiye Koi. Walipotolewa kwenye ukumbi wa mahakama waliingizwa ndani ya gari kwa ulinzi mkali wa polisi. Msafara wa kuwapeleka gerezani uling’oa nanga kutoka mahakamani. Koi alipokuwa akiyaangaza macho ndipo aliiona sura ya Roy kwa karibu akiwa na Carolina. Alijaribu kutabasamu lakini hakuweza. Oli alikuwa akipumua kwa shida kutokana na kibuhuti baada ya hukumu ambayo hakuitegemea. Japo alijitahidi kuwaza na kujipa tumaini, huzuni ilizidi furaha.
Taarifa ya kuhukumiwa kifungo cha maisha kwa Oli na Koi ilisambaa kama upepo jangwani. Kuanzia mjini Tumaini hadi vijijini kote walipata taarifa. Wakati huo Carolina na Roy walikuwa na chereko mioyoni mwao. Japo Oli na Koi walihukumiwa, furaha haikutosha kumpoza Carolina dhidi ya machungu ya kumpoteza mama Tora, kipenzi chake. Roy alihisi aliifanya kazi yake ilivyompasa kufanya. Ilikuwa hatua nzuri ya mafanikio katika kazi yake mpya ya upelelezi. Jinsi alivyokuwa ameiandaa hati ya mashitaka na jinsi shauri lilivyosomwa, liliwavutia watu wengi. Mpangilio wa matukio, hoja na ushahidi vilikuwa vya kuvutia.
Jua lilipotua, Carolina na Roy walikwenda kupumzika. Ilikuwa shangwe tena, walijumuika kwa Roy wakipongezana. Roy bado hakuwa amepata zawadi ya kumfaa Carolina kwa heshima aliyomtunuku. Aliyakumbuka mambo yote yaliyotokea katika maisha yao wakati wakiwa kijijini Hamaniko. Japo Roy alikuwa na misukosuko, fikrani alihisi Carolina ndiye alipaswa kuitwa shujaa wa mapambano.
Dunia ilipofumbua macho na kuzitoa tongotongo kwa miale ya jua, Carolina alimtaka Roy kumrudisha nyumbani kwake. Ilikuwa siku ya jumamosi ambapo hawakuwa na lazima ya kwenda kazini kwa shinikizo bali kwa hiari kama kulikuwa na viporo vya kukamilisha. Carolina hakukaidi kumpeleka mpenziwe. Siku hiyo Carolina aliitumia kufanya usafi wa nyumba na samani ili kuyaweka mazingira salama.
Roy aliporudi kwake, naye alifanya usafi wa nyumba na kilakitu ambacho alihisi kilihitaji mkono wake kukisafisha. Alipomaliza aliondoka hadi katikati ya mji kujitwalia mahitaji yake. Alipokuwa anarudi, alikuwa akiwaza jinsi atakavyofanya ili kuweza kumfurahisha Carolina kwa kipindi cha maisha yake yote. Alipanga na kupangua kila wazo lililomjia fikrani, hatimaye alipata wazo mujarabu na kuufanya moyo wake kutabasamu na kucheka kwa nguvu. Alipopata kifungua kinywa, alikitandika kitanda vema na kuichukua simu yake. aliandika ujumbe na kuutuma. Aliandika,
‘Mpenzi, ghafla nahisi kuvamiwa na ugonjwa nisioufahamu. Nauhisi mwili kuishiwa nguvu. Pumzi zinanipotea, na sasa naelekea hospitali. Nikitoka huko nitakujulisha. Hali yangu ni mbaya!’
Roy aliutuma ujumbe kwa Carolina ambaye alikuwa na simu yake mkononi wakati ule. Ujumbe uliingia moja kwa moja kwenye simu, aliufungua na kuisoma. Uso wake ghafla ulikosa furaha. Alitafakari kwa sekunde chache kisha naye aliamua kuujibu. Aliandika,
‘Tatizo nini Roy, anyway napaswa kuja nikusindikize. Huwezi kwenda peke yako. Nimepata mshituko na sasa furaha yangu imetoweka. Itakuwa nini Roy mpenzi?.....lakini tangulia haraka nisikuchelewashe mambo yakawa magumu zaidi. Unijulishe kila hatua. Nakupenda, pona haraka nakuhitaji. Nakupenda sana Roy!’ Carolina aliutuma ujumbe, Roy aliusoma na kutabasamu. Aliandika kumjuza mpenziwe,
‘Usihofu, nitakuwa sawa. Nitakujulisha kila hatua.’ Roy aliutuma ujumbe na kungoja kijibiwa. Haikuchukua muda mrefu, Carolina alimjibu,
‘Asante, nitafurahi mpenzi.’
Carolina alipoutuma ujumbe, aliendelea kumalizia kazi zake. Roy naye aliendelea na alichokuwa akifanya. Aliungoja muda upite ndipo amjuze Carolina hatima ya afya yake. baada ya saa moja kupita, ilikuwa muda muafaka kwa Roy kumtumia ujumbe mpenzi wake. Wakati huo aliingia ndani kwake. Alipanda kitandani na kuivuta shuka. Aliichukua simu na kuutuma ujumbe kwa Carolina.
‘Nimefanyiwa uchunguzi kwa kina, ninatatizo kubwa huenda maisha yangu yakakatika muda wowote. Naomba kama unaweza uje nyumbani kuniona. Nimekata tamaa!”Aliutuma ujumbe huo kwa Carolina naye aliupokea na kuusoma. Haraka hakutaka kuujibu kwa maandishi. Alijiandaa na kutoka mbio akiwa na wasiwasi mkubwa. Hofu yake ilikuwa juu ya afya ya Roy ambaye alikuwa ameungana naye kwa huba kipindi kifupi tu baada ya kukutana wakiwa mahakamani.
Carolina hakukawia kufika, alipofika kwa Roy, moja kwa moja aliingia ndani. Aliita na alipobaini kuwa Roy alikuwa kitandani alienda moja kwa moja kumpa pole.
“Roy, pole mpenzi. Tatizo ni nini?”
“Nimechunguzwa, naumwa ugonjwa ambao haujulikani kwa jina. Hauonekani kwa vipimo vya kitabibu. Kila kipimo wamejaribu, lakini imeonyesha sina tatizo.”
“Unasemaje?”
“Sina tatizo. Lakini nilipo hapa siwezi kufanya chochote, mwili wangu haujiwezi. Sijui kama nitapona,” alieleza Roy.
“Usiseme hivyo, unanifanya nishindwe kujua la kufanya.”
“Usihangaike, najua sitapona.”
“Hapana, sema nifanye nini ili uweze kupona. Inapaswa upelekwe hata nje ya nchi huenda ukapata tiba.”
“Hapana, usisumbuke nitapona tu,” alisema Roy. Alizidi kujikunyata pale kitandani akilalama kwa maumivu makali. Carolina furaha ilimpotea, machozi hayakukawia kumfunika machoni. Hakuwa na hatua ya kuchukua zaidi ya kusononeka. Hakuisha kulalama na kumlaumu Mungu kuwa alimuumba ili ahangaike. Alilia!
Baada ya kuona Carolina amezidi kulia kwa huzuni, Roy aliita akiwa kajifunika gubigubi. Carolina aliacha kulia na kumsikiliza mpenziwe.
“Unasemaje Roy?” alisema Carolina wakati mkono wake unapangusa kamasi kutoka puani kwake.
“Naomba nisaidie dawa, ipo pale juu ya meza kwenye bahasha. Tafadhali fanya haraka.” Carolina aliifuata haraka bahasha iliyokuwa juu ya meza. Alimpatia Roy bila kuifungua.
“Niifungue, kwani ni dawa gani?” Carolina alihoji.
“Usiifungue, niletee maji kwenye kikombe niimeze,” alijibu Roy. Dawa hii inaitwa ROCALIN.”
“Rocalin ndo dawa gani?” alihoji Carolina akiwa anaelekea kumpatia Roy maji. Roy hakumjibu.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Naomba usiketi. Naomba simama kishike kikombe cha maji mkono wa kulia,” alisema Roy. Alikuwa ameifungua bahasha na alikuwa na kitu alichokikumbatia kwenye kiganja chake.
“Hebu niione hiyo dawa ikoje?” alihoji Carolina akiwa na wasiwasi.
“Hutakiwi kuiona kwa sasa. Kwanza usinitazame ninavyo imeza. Fumba macho nitakwambia nikiiweka mdomoni,” alisema Roy.
“He! Dawa gani mpaka nifumbe macho Roy. Haya bwana, ngoja nifumbe macho,” Carolina alifumba macho. Roy aliweka kitu mdomoni mwake.
“Fumbua macho tayari,” alisema Roy akiwa kama mmeza nofu mdomoni.
“Haya, nimefumbua macho. Nipe niione hiyo dawa,” alisema Carolina.
“Haya pokea,” alisema Roy. Carolina aliutoa mkono wa kushoto kuipokea ile dawa aliyoambiwa. Mkono wa kulia alikuwa kashika kikombe cha maji. Roy alikishika kiganja cha Carolina kwa kuutumia mkono wake wa kushoto. Mkono wa kulia uliipokea dawa aliyokuwa nayo mdomoni. Alikishika na kukinyanyua kidole cha shahada. Carolina alikuwa kapigwa bumbuwazi.
“Caro, dawa yangu itakayonifanya niishi kwa furaha siku zote ni hii. Inaitwa ROCALIN. Naomba uipokee na ukubali kuwa tabibu wangu kwa maradhi yasiyo na tiba hospitalini,” alisema Roy.
“Roy, kwa nini lakini? Umenishtua sana. Kwa hiyo huumwi tena chochote!”
“Ugonjwa wangu ni hofu ya kukupoteza. Dawa yake ni kuwa nawe wakati wote. Naomba ukubali kuwa mke wangu, nakupenda sana Carolina,” alisema Roy kwa unyenyekevu. Alipiga goti chini akimkazia macho Carolina ambaye alikuwa analia, si kwa huzuni bali kwa furaha.
“Roy, ni radhi kuwa wako siku zote. Nyanyuka Usiniabubu, afaaye kuabudiwa ni Mola peke yake,” alisema Carolina wakati akimnyanyuka Roy.
“Asante Carolina, hii ndiyo Rocalin, tiba ya moyo wangu,” alisema Roy na kumvisha Carolina pete ya uchumba. Carolina hakuyaamini macho yake. Aliendelea kulia na kumkumbatia Roy kwa furaha. Ilikuwa furaha isiyokuwa na mfano. Hatimaye alinyamaza na kutoa yake ya moyoni.
“Rocalin! Maana yake ni nini?”
“Roy na Carolina.”
“Asante mpenzi, nakupenda na nitakupenda daima dumu,” alieleza Carolina.
Maisha ya wawili wale, yalichukua sura mpya. Kutoka huzuni hadi chereko. Hawakuwa wakiota kuyafikia maisha hayo zaidi ya kuzungukwa na hamaniko kama kilivyokuwa kijiji chao. Kwa juhudi na kudra walifanikiwa kupiga hatua kujinasua matopeni na kujiweka kwenye kilele cha furaha.
Ulipita mwezi mmoja, walijiandaa kwenda Tuamoyo kama walivyokuwa wamepanga. Safari yao ilikuwa ya mafanikio kwani kila walichokipanga kilifanikiwa. Majaliwa na Maua walikuwa na furaha kujumuika na wajukuu waliowapenda. Walifurahi kusikia uamuzi wa Roy na Carolina kutaka kuoana. Baraka za wazee wale zilikuwa juu yao, nao waliwabariki.
Safari ya Carolina kwenda kijijini haikukoma walipofika Tuamoyo pekee. Waliambatana na walezi wao kwenda hadi kijijini Hamaniko kwenda kuona makaburi ya wazazi wao na kutaka baraka zao kwa uamuzi waliokuwa wameuchukua. Hamaniko iliyokuwa na hamaniko ilitabasamu kwa ujio wao. Chuki ziligeuka furaha wakiwashangaa na kuwashangilia. Cherekochereko zilikuwa juu ya ardhi iliyojaa huzuni. Iliwapasa kuifunga ndoa yao ya jadi katikati ya kijiji cha Hamaniko kama kumbukumbu mhimu kwa wazazi waliowapoteza. Ndoa ilifana na kijiji kizima kilifikwa na furaha kwa tabasamu la wawili wale. Familia yao ilianza kwa kishindo kwani kila mmoja aliwarushia baraka za kufanikiwa. Hatimaye, chereko zilihitimishwa kwa nasihi kutoka kwa Carolina. Alipokuwa akisimama kuzungumza, kila mwanakijiji alikuwa kimya akitaka kuyasikia maneno ambayo Carolina alilenga kuzungumza nao. Alisema,
“Lola mama yangu, apumzike kwa amani.
Dendego mkwe wangu, alinijua ningali mashakani, apumzike kwa amani, upendo wake mkubwa kwangu nitauenzi.
Hamaniko ndiye baba yangu, japo alinipenda nizaliwe juu yake, hakunionesha wa nasaba yangu. Sitaacha kumtambua Hamaniko kuwa ndiye baba yangu wa damu.
Mlezi wangu Malecha na mama wa hiari kwangu, Rabi awazidishie furaha. Pasipo ninyi hata leo nisingeweza kusimama hapa kuutoa ushuhudu huu adhimu kwa maisha ya mwanadamu. Mlipambana kunilea kama mtoto halali kwenu, lakini kwa yaliyotokea njiani, sina budi kuwasamehe. Wema wenu ulizidi ubaya, najua mlipitiwa hadi leo nikawa nje ya miliki zenu. Mungu atawajaza na kuwasamehe kwa dua zangu njema kwenu. Pia, namwomba Mola ampunguzie adhabu na kumweka sehemu salama kaka yangu kipenzi Saraganda, hakika alikuwa nuru kwangu. Alinipigania akitaka nisome na kufanikiwa ili niweze kujitegemea. Katikati ya vita ya kunilinda, alikumbana na vikwazo vingi hadi kifo kilipomfika akiyakatisha maisha sababu yangu. Alitaka sana nifabikiwe. Sina budi kusema asante na Mungu amrehemu.
Furaha yangu katika mji wa Malecha kwa walezi wa hiari kwangu, isingekamilika pasipo kuwa na rafiki kipenzi. Huruma! Nashukuru na kufurahi kukuona leo uko mbele yangu ukitabasamu kwa furaha baada ya kuniona nikiwa mwenye furaha pia. Wewe ulikuwa tulizo la nafsi yangu, mshauri na mganga tabibu kila nilipopata jeraha tuwapo safarini kutekeleza maagizo ya mji. Wewe ni kipepeo mchanga, dunia bado inakuhitaji kutia juhudi ili uweze kuyafikia maisha ya ndoto zako. Kumbuka, simulizi za kipepeo na kinyonga wakati ule ilisipokea kama hekaya za jinamizi, zisizo na ukweli bali na masimulizi ya kuupitisha wakati, leo tena nakuasa, jichunge na ujilinde. Mungu atakupa njia nawe uifuate kwa uaminifu.
Fahari ya kijiji hiki haiwezi kusimama juu ya mlima bila kuzitangaza mila zake. Hamaniko ni kijiji cha mashaka ninayotaka leo nyote mtambue. Mume hata mke watambueni kuwa ni watu sawa. Si kwa maumbile na siha bali kwa amali na vipawa. Awaye yeyote anahaki sawa kama kifo, hakibagui. Wathaminini watoto wa kike, waleeni kwa elimu msiukumbatie ukale na kuuacha usasa. Je, leo hii nani aaminiye kama ndimi Carolina nipo mbele yenu leo kukibadilisha kijiji cha Hamaniko? Nadhani nyote mtakuwa mashahidi. Malecha na babu yangu Majaliwa, kwa kusukumwa na mila za kijiji hiki, waliamua kumtelekeza mtoto wa kike, kisa hawezi kuwa mrithi wa amali na fahari zao, leo hali imegeuka. Nanyi binti wa Hamaniko, tieni bidii kwenye masomo mijiwekee vikwazo nafsini mwenu na kuamini hamtaweza kuyafikia matamanio yenu kwa juhudi zenu, mnaweza.
Pamoja na chereko zote hapa leo, nimesikitika kuiona Hamaniko ikiwa katika hali mbaya kwa mazingira. Hamaniko inalia kwa ukame. Hamaniko inalia kwa njaa. Hamaniko inalia kwa magonjwa. Tofauti kabisa na enzi za usichana wangu mchanga ilipokuwa na mito iliyomwaga maji kila mahali, mimea ilikuwa kijani kibichi na watu walikuwa wakila na kusaza. Sasa yote yamepita na kusahaulika. Haya yote ni matatizo ya kibinaadamu, yatupasa sote kuchukua hatua. Binafsi na mume wangu tutakuwa mabalozi wazuri wa kuifanya hamaniko kisiwa cha furaha. Tutaanzisha na kusimamia miradi ya utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti kila kona ya Hamaniko ili iweze kuirudisha haiba ya kijiji hiki. Tutawekeza juhudi na amali katika miradi ya vijana ili kuwaelimisha jinsi ulimwengu uanbadilika kwa kasi ili badala ya kukaa na kuzikumbatia mila angamizi, waweze kubuni na kujitengenezea maisha ya fahari kwa miradi mbalimbali. Tutajitahidi kuwa na kituo cha afya na kuishauri serikali ya nchi ya Tupendane, kutoka makao makuu pale Tumaini iweze kuongeza uwekezaji katika miradi ya kijamii hasa elimu na afya ili kuwafanya vijana wengi kuyafikia mafanikio na kukifanya kijiji hiki sehemu kubwa ya maendeleo ya nchi. Majukwaa ya sheria na usalama wa raia yataundwa na kuwa na matawi kwa kila kijiji hasa hapa Hamaniko. Mtu asijichukulie sheria mkononi.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kwa hayo niliyoyasema, utekelezaji wake utakuwa wa haraka. Nawaomba sana, vijana kwa wazee, mshirikiane nasi kwa moyo mkunjufu. Pendekezo langu kabla sijatia nanga kwa maneno yangu, kijiji hiki kibadilishwe jina na kuwa Ramsa, yaani furaha.” Carolina alihitimisha, kijiji kizima kililipuka kwa chereko baada ya kuingiwa na tumaini jipya.
Kweli, maisha ni mzani na baada ya dhiki ni faraja.
TAMATI
Asanteni sana kwa kusoma Riwaya hii ya kipekee.
0 comments:
Post a Comment