IMEANDIKWA NA : NYEMO CHILONGANI
*********************************************************************************
Simulizi : Dunia Isiyo Na Huruma
Sehemu Ya Kwanza (1)
Mara baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe kuingia nchini Rwanda, watu wengi wakakimbia na kuziacha nyumba na fedha zao. Wengi waliuawa, vita vya Watusi na Wahutu vilishika kasi nchini humo kiasi kwamba hakukuwa na mtu aliyetamani kubaki ndani ya nchi hiyo.
Maelfu ya Wanyarwanda wakawa wakimbizi katika nchi za jirani kama Tanzania, Kenya na Burundi, amani waliyokuwa wakiiringia ikaingia doa, furaha waliyokuwa nayo kipindi cha nyuma, ikapotea, sauti za upendo zilizokuwa katika kila pembe ya nchi yao zikapotea na kila walipopita, ni sauti za risasi, mabomu na mapanga ndizo zilizosikika.
Watu walilia, fedha hazikuwa na thamani tena, watu waliacha vitu nyumbani kwao, hakukuwa na aliyekumbuka ndugu yake, kwa wanawake waliokuwa na watoto, mara baada ya kusikia milio ya risasi, wakawakimbilia mbwa na kuwabeba migongoni kwa kuhisi kwamba walikuwa watoto wao, walipogundua kwamba walibeba mbwa, walikuwa umbali wa kilometa zaidi ya kumi na tano.
Kilikuwa kipindi kibaya, chenye maumivu kilichoweka madoa katika mioyo ya Wanyarwanda wengi, wale waliokuwa matajiri wa kutupwa, hawakukumbuka waliacha kiasi gani cha fedha katika akaunti zao, walichokikumbuka kwa wakati huo ni kuyaokoa maisha yao tu.
Wakati milio ya risasi ikianza kusikika, katika jumba moja kubwa la kifahari, lililojengwa kwa thamani kubwa, jumba lililozungushiwa ukuta mkubwa na kwenye eneo la jumba hilo kukiwa na magari ya bei mbaya, watu waliokuwa ndani ya jumba hilo walikuwa kwenye majonzi mazito.
Mzee Jerome Mugenzi, mmoja wa matajiri wakubwa nchini Rwanda alikuwa kitandani, familia yake ya watoto wawili na mkewe ilikuwa imemzunguka. Mzee huyo alikuwa katika hatua za mwisho za kuvuta pumzi ya dunia hii, na hata kuongea kwake ilikuwa ni kwa shida sana.
Kila mmoja alikuwa akilia, kwa kumwangalia tu ingekuwa rahisi kugundua kwamba mzee huyo hakuwa na zaidi ya saa moja la kuishi kwani ugonjwa wa moyo uliokuwa ukimsumbua kwa miaka na miaka, kipindi hicho ulikuwa katika hatua za mwisho kumuua kitandani hapo.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hawakwenda hospitali, milio ya risasi ilisikika kila kona, waliogopa, kama kufa, walikuwa radhi kumuona mzee huyo akifa kitandani pale lakini si kwenda nje ya nyumba hiyo, hali iliyokuwa huko ilimtisha kila mmoja.
Mke wake, Bi Shamarima alikuwa akilia, hakuamini kile alichokiona, mumewe, aliyempenda kwa mapenzi ya dhati, alikuwa hoi, katika hatua za mwisho za kuishi.
Alitamani kile kilichokuwa kikiendelea mahali pale kiwe ndoto ili baadaye atakapoamka kila kitu kiwe upya, lakini kile hakikuwa ndoto, lilikuwa tukio halisi ambalo liliendelea ndani ya nyumba yao na hata ile milio ya risasi iliyokuwa ikisikika nje, ilikuwa halisi, nchi hiyo ndogo ilikuwa kwenye machafuko ya wenyewe kwa wenyewe.
Mzee Mugenzi, bilionea mkubwa nchini humo alizungukwa na familia yake, watoto wake wawili na mke wake mpendwa aliyekuwa akimpenda kwa moyo wa dhati, kila mmoja alikuwa akilia, walitamani kuyaokoa maisha ya baba yao lakini hilo lilishindikana, ugonjwa aliokuwa akiumwa, ulimtafuna sana kiasi kwamba kitandani pale alionekana kama mfu anayepumua.
“Please don’t leave us,” (tafadhali usituache) alisema Bi Shamarima huyo huku akilia kama mtoto.
“There is nothing I can do, I have to die,” (hakuna ninachoweza kufanya, ninatakiwa kufa) alisema mzee Mugenzi kwa sauti ya chini iliyosikika kama mtu aliyekata tamaa ya kuishi.
Maneno yake yalimuumiza kila mtu, wote watatu wakaanza kububujikwa na machozi, kila walipomwangalia mzee huyo kitandani pale walishindwa kuvumilia.
“Didier, take care of your mother and your sister, Solange,” (Didier, Mlinde mama yako na dada yako, Solange) alisema Mzee Mugenzi.
“I will dad,” (Nitawalinda baba) alisema Didier huku akiyafuta machozi yaliyokuwa yakimtoka.
“Solange, I am dying, I could take care of you to death, but, this is my last breath, your brother will take care of you for me,” (Solange, ninakufa, ningekulinda mpaka kifo chako lakini hii ni pumzi yangu ya mwisho, kaka yako atakulinda kwa ajili yangu) alisema Mzee Mugenzi.
Solange hakujibu kitu zaidi ya kububujikwa na machozi. Hapohapo akamwangalia mkewe.
“My wife Shamarima, I can say nothing, I just love you to the en.....” (mke wangu, Shamarima, sina la kusema, ninakupenda mpaka mw...) alisema Mzee Mugenzi lakini hata kabla hajamaliza sentensi yake, akabaki kimya, mapigo ya moyo yakaacha kudunda, akafariki dunia kitandani pale tena mbele ya familia yake.
Hakukuwa na mtu aliyeamini, machozi yaliwatoka zaidi na sauti ya vilio kusikika humo chumbani. Mioyo yao iliwauma mno, hawakuamini kile walichokiona, mtu waliyempenda, baba yao alifariki dunia na kusingekuwa na uwezekano wa kurudi tena.
Walijaribu kumuamsha kitandani pale lakini hakuamka, walitamani kumuona akifumbua macho yake na kuangalia tena lakini haikuwa hivyo, mzee yule alibaki kimya kitandani, hakuzungumza wala kutingishika, alikuwa amefariki dunia na kuiacha familia yake.
“Dad, please wake up, open your eyes and look at us,” (Baba, tafadhali amka, fumbua macho yako ututazame) alisema Solange huku akilia kama mtoto.
“Please my husband, open your eyes, please,” (tafadhali mume wangu, fumbua macho yako) alisema Bi Shamarima huku akibubujikwa na machozi.
Walilia na kulia lakini machozi yao hayakubadilisha kitu chochote kile, ukweli ulibaki palepale kwamba mzee huyo bilionea alifariki dunia kitandani pale huku akiwa ameacha utajiri mkubwa duniani.
Huku kila mmoja akilia kwa maumivu makali ya moyo tena wakimuita kitandani pale aweze kuamka na kuwaangalia, ghafla, wakaanza kusikia milio ya bunduki kutoka nje ya nyumba yao, watu zaidi ya watano waliokuwa na bunduki wakaingia ndani ya eneo la nyumba hiyo kwa kuvunja geti, walichokifanya ni kuanza kuzipiga risasi gari za kifahari zilizokuwa katika sehemu ya maegesho.
“Ils sont tous des Hutus, tuer tout le monde dans cette maison,” (wote ni Wahutu, ueni kila mtu ndani ya nyumba hii) ilisikika sauti ya mwanaume mmoja kwa Lugha ya Kifaransa, vishindo vya watu kuanza kusikika vikiusogelea mlango wa kuingia ndani.
Mitaani hakukukalika, watu walikimbia huku na kule kuyaokoa maisha yao. Rwanda ile ya kipindi cha nyuma haikuwa hii, kila kitu kikabadilika, watu waliokuwa wakitaka kuiongoza nchi hiyo kikabila wakasababisha vurugu zilizowafanya watu kukimbia kila kona kutafuta amani.
Watu walipigwa risasi hovyo mitaani, watoto walitelekezwa na wazazi kukimbia zao, hali ilitisha, milio ya risasi iliyokuwa ikisikika kila kona iliwafanya watu kutetemeka na hofu kuitawala mioyo yao.
Idadi kubwa za maiti zilikuwa barabarani, damu zilitapakaa kila kona, picha ya Jiji la Kigali ilibadilika, ilitisha, ilisisimua, nyumba nyingine zilichomwa moto.
Mtaani ilikuwa vita, vijana wa Kihutu walitembea mitaani huku wakiwa na mapanga na wengine wakiwa na bunduki, walipokuwa wakiwaona Watusi, waliwafuata na kuwashambulia kwa risasi na hata kuwakatakata kwa mapanga.
Hiyo haikuwa kwao tu, hata kwa vijana wa Kitusi nao walitembea barabarani huku wakiwa na bunduki, wengine wakiwa na mapanga, walipowaona Wahutu, waliwafuata na kuwashambulia kwa risasi na mapanga.
Mtaani hakukukalika, watu walizidi kuuana kana kwamba hawakuwa watu wa nchi moja. Kutokana na nchi hiyo kuwa ndogo, watu walifahamiana, Watusi waliingia ndani ya nyumba za Wahutu na kuwaua huku nao Wahutu wakiingia ndani ya nyumba za Watusi na kuwaua.
Katika harakati hizohizo za kuvamiana nyumbani na kuuana ndiyo iliwapelekea vijana wa Kitusi waliokuwa na bunduki na mapanga kuifuata nyumba ya bilionea Mugenzi kwa lengo la kuingia ndani na kumuua yeye na familia yake kwani walifahamu fika kwamba watu hao walikuwa Wahutu.
Walipofanikiwa kuingia ndani ya eneo la nyumba hiyo, kwanza wakayapiga risasi magari yake kisha kuingia ndani kabisa. Walianza sebuleni, hakukuwa na mtu yeyote yule, kila mmoja alikuwa amekimbia kuyaokoa maisha yake, hawakuishia hapo, walichokifanya ni kwenda katika vyumba vingine, huko napo palikuwa patupu.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ils sont tous des Hutus, tuer tout le monde dans cette maison,” (Wote ni Wahutu, ueni kila mtu ndani ya nyumba hii) alisema mwanaume mmoja.
Hawakutaka kuishia katika vyumba hivyo tu, walichokifanya ni kwenda katika vyumba vingine kwani walihisi kwamba kulikuwa na ambavyo hawakuwa wameingia.
Hakukuwa na chumba kingine zaidi ya kimoja tu kilichowapelekea kukifuata, walipoufikia mlango, wakaingia ndani. Mbele yao, kitandani alilala mwanaume mmoja, alionekana kama mtu aliyekuwa hai lakini walipomsogelea na kuyasikiliza mapigo ya moyo wake, alikuwa amekwishakufa.
Walimfahamu mwanaume huyo, ndiye aliyewafanya kuingia humo ndani huku wakiwa na hasira naye, maiti hiyo ilikuwa ni ya bwana Mugenzi, hawakutaka kuridhika, walichokifanya, maiti hiyohiyo wakaanza kuishambulia kwa risasi kitandani pale huku wengine wakiikatakata kwa mapanga.
“Il est déjà mort,” (amekwishakufa) alisema jamaa mmoja huku akiwa na uso uliojawa na tabasamu pana.
“Où est sa famille?” (familia yake iko wapi?)
“Il sera ici présentes, la recherche, ne peut échapper,” (itakuwa humuhumu ndani, tuitafuteni, haiwezi kutoroka) alisema jamaa mwingine ambaye alionekana kama kiongozi wao.
Hicho ndicho walichokifanya, hawakutaka kuona wakitorokwa, walijua fika kwamba watu waliokuwa wakiwatafuta walikuwa ndani ya nyumba hiyo hivyo walichokifanya ni kutoka ndani ya chumba kile na kuanza kuwatafuta.
Katika sehemu zote zilizojificha kama kwenye dari walipiga risasi ili hata kama walikuwepo humo basi wafe, nyuma ya kabati, hawakutaka kuangalia, walichokifanya ni kupiga risasi mfululizo kwa kuamini kwamba ni lazima wangekufa tu.
Walipekuwa nyumba nzima, watu hao hawakupatikana, hawakutaka kubaki nyumbani hapo, walichokifanya ni kutoka nje huku wakikubaliana kwamba familia ya mzee Mugenzi ilikuwa imekwishatoroka kutokana na upekuzi wao mkubwa walioufanya ndani ya nyumba hiyo kutokuzaa matunda.
*****
Maisha yao yalikuwa kwenye hatari kubwa, watu wale waliofika mahali hapo huku wakiwa na bunduki waliwaogopesha mno, wakabaki chumbani mule huku wakitetemeka.
Kulikuwa na vitu vitatu walivyotaka wavifanye lakini ilikuwa ni lazima kifanyike kitu kimoja, kama kubaki chumbani mule na kama kuuawa wauawe pamoja na mzee Mugenzi, kutoroka chumbani na kuuacha mwili wa mzee wao au kuubeba na kukimbia nao ili wakauzike mbele ya safari.
Walibaki wakiulizana harakaharaka na jibu la mwisho kabisa alilolitoa Didier ilikuwa ni lazima wakimbie, wauache mwili wa baba yao ndani ya chumba kile kwani hata kama wangekimbia nao, wasingefika nao mbali.
Hakukuwa na mtu aliyempinga, wazo lake alilolitoa lilionekana kuwa sahihi, hivyo walichokifanya ni kuondoka chumbani mule, hawakupitia mlango wa mbele kwa kuamini kwamba huko ndipo kulipokuwa na wauaji waliongia, bali walichokifanya ni kupitia mlango wa nyuma.
Geti la nyuma ya nyumba ndilo lilionekana kuwasaidia, wakalifungua kisha kutoka nje, kilichofuata baada ya hapo ni kukimbia tu. Kila mmoja alihuzunika, walishindwa kuyazuia machozi yao kukububujika mashavuni mwao, walilia na kulia, waliendelea kusonga mbele kwani kwa kipindi hicho, kukimbia kwao ndiyo ulionekana kuwa usalama wa maisha yao.
Njiani hali ilitisha, kila walipopita, maiti za watu zilitapakaa kila kona, mbwa na ndege walikuwa wakiitafuna miili hiyo. Harufu kali ilisikika puani mwao, iliwapa shida lakini kwa kipindi hicho cha hatari, hakukuwa na mtu aliyediriki kusimama.
“Tunakwenda wapi Didier?” aliuliza mama yake, bi Shamarima.
“Popote pale ambapo kuna amani, hatuwezi kusimama njiani, kama kufa, acha tufe tukiwa safarini,” alijibu Didier huku safari ikiendelea.
Hawakukutana na mtu yeyote aliyekuwa akitembea, kila walipopita, ni milio ya ndege na mbwa ndiyo iliyokuwa ikisikika. Walizidi kusonga mbele mpaka walipolifikia kanisa kubwa la Roman Catholic, kulikuwa na ukimya mkubwa, hawakutaka kusimama, hapo ndipo kulipoonekana kuwa sehemu ya kujifichia, wakaingia katika eneo la kanisa hilo na kuufuata mlango.
“Tugonge tufunguliwe,” alisema Solange.
“Tugonge, hakuna kugonga, tuingieni moja kwa moja, hakuna mtu,” alisema Didier huku wakiusogelea mlango wa kanisa lile.
Walipoufikia mlango mkubwa wa kuingia ndani, Didier akajaribu kuufungua lakini mlango ulikuwa umefungwa kwa ndani. Wakajaribu kugonga ili kama kulikuwa na watu ndani basi wawafungulie lakini hakukuwa na mtu yeyote aliyekuja na kuufungua.
Hawakuishia hapo, walichokifanya ni kuzunguka nyuma ya kanisa huku wakiita ili waweze kupewa msaada. Ukimya mkubwa ulikuwa ndani ya kanisa hilo, haikusikika sauti ya kitu chochote kile.
Waliita mpaka wakachoka na mlango haukufunguliwa, hawakuwa na jinsi, walichokifanya ni kuanza kuondoka ili kwenda kutafuta hifadhi sehemu nyingine kwani walihisi kama wangeendelea kubaki mahali hapo basi wauaji wangefika na kuwaua.
Wakati wakiwa wamekwishafika barabarani kuendelea na safari yao, wakasikia mlango mkubwa wa kanisa ukianza kufunguliwa, kwa haraka sana wakarudi pale mlangoni.
Mtu aliyefungua alikuwa padri wa kanisa hilo. Aliwaangalia watu hao na kuwakaribisha ndani, wakaingia, kilichowashangaza ni kwamba humo ndani kulikuwa na watu zaidi ya mia mbili, walikuwa wa makabila mawili tofauti, Watusi na Wahutu, watu wote hao walionekana kujawa na hofu mioyoni mwao.
“Hali inaendeleaje huko?” aliuliza padri, hata kabla Didier hajajibu swali hilo, dada yake, Solange akaanza kulia.
“Nyamaza Solange. Tumefika sehemu salama,” alisema Didier huku akimbembeleza dada yake.
“Hali ni mbaya padri, watu wameuawa kinyama, picha inatisha, tumuombe Mungu tu atunusuru,” alisema Didier na hapohapo padri akafanya ishara ya msalaba kwa kupeleka vidole kwenye paji la uso, kifuani na mabegani.
Watu waliokuwa ndani ya kanisa lile wakawasogelea pale walipokuwa, walitaka kusikia kile walichokuwa wakimueleza padri, walitaka kufahamu kilichokuwa kikiendelea mitaani.
Hapo ndipo Didier akaanza kuwaambia hali halisi, Kigali ile ilikuwa imechafuka na mitaani kulijaa miili ya watu waliokufa. Kila mtu aliyesikia hilo, alibaki akilia kwa uchungu kwani ile ilikuwa nchi yao wenyewe, lakini katika kipindi hicho, walikuwa wakikimbia hovyo, amani haikuwepo tena mahali hapo.
“Jamani, tunatakiwa kutulia humu mpaka hali itakapotulia,” alisema padri.
“Na vipi kuhusu chakula, tutakufa njaa,” alisema jamaa mmoja, alikuwa Mtusi, mrefu na mweusi tii.
“Humu kanisani huwa tuna ghala, lilijengwa mwaka 1988 na lilikuwa maalumu kwa kuhifadhia chakula na maji, lipo humu na limejaa vyakula, nadhani si tatizo,” alisema padri maneno yaliyomfanya kila mtu kushukuru.
Humo ndipo walipotakiwa kuanza maisha upya, nje hakukuwa na amani hata kidogo, humo ndani, tena kanisani ndipo kulionekana kuwa sehemu yao ambayo wangekaa katika kipindi chote mpaka pale ambapo mapigano yangeisha.
“Solange...” ilisikika sauti ya msichana mmoja, Solange alipogeuka, macho yake yakatua kwa msichana mmoja wa Kitusi, alikuwa mzuri wa sura.
“Sophia...” aliita Solange, wakakimbiliana na kukumbatiana.
Kila mmoja alionekana kuwa na furaha, machozi yaliwabubujika, hakukuwa na aliyeamini kwamba amekutana na mwenzake. Wawili hao walisoma shule moja, shule ya matajiri iliyokuwa pembeni kidogo mwa Jiji la Kigali.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wazazi wa Sophia waliuawa wakiwa njiani kuyakimbia mapigano. Kama alivyokuwa Solange, hata Sophia naye alitoka katika familia ya kitajiri.
“Upo na nani hapa?” aliuliza Solange.
“Nipo peke yangu, wazazi wangu wamepigwa risasi na kufa, tulivamiwa nyumbani, ni mimi peke yangu ndiyo nimenusurika,” alisema Sophia huku akiendelea kububujikwa na machozi, hayakuwa ya furaha tena bali maumivu makali.
“Pole sana. Hapa nipo na mama pamoja na kaka yangu,” alisema Solange.
Wawili hao wakaonana ndani ya kanisa hilo, huo haukuwa muda wa kuwa na furaha, kila mmoja alikuwa na huzuni tele, matukio yaliyokuwa yakiendelea yalitisha na mara kwa mara ilitangazwa kwenye redio kwamba watu walitakiwa kukaa kwenye sehemu salama.
Waliendelea kukaa ndani ya kanisa hilo mpaka ilipofika usiku. Saa mbili kamili tu, watu wakashtuka baada ya kusikia mlango mkubwa ukianza kugongwa kifujofujo.
Kila mtu aliyekuwa ndani akashtuka, wote wakabaki kimya, ugongaji ule haukuwa wa kawaida, wote wakagundua kwamba kulikuwa na tatizo.
“Tufungue mlango?” aliuliza mzee mmoja, alikuwa akimuuliza padri kwa sauti ya chini.
“Hapana! Subiri kwanza,” alisema padri.
Watu hao hawakuacha kugonga, waliendelea zaidi, walipoona kwamba mlango haufunguliwa, hapohapo milio ya risasi ikaanza kusikika mlangoni, mlango ukapigwa risasi, kitasa kikatoka na mlango kufunguka.
Wanaume saba, warefu na weusi tii wakaingia ndani ya kanisa hilo. Kwa kuwaangalia tu wala isingekupa wakati mgumu kugundua kwamba watu hao walikuwa Watusi. Nyuso zao hazikuonekana vizuri ila kwa jinsi walivyokuwa, walionekana kuwa na hasira mno.
“Washa taa,” ilisikika sauti ya mwanaume mmoja, hapohapo taa zikawashwa.
Watu hao wakaonekana mbele yao, walikuwa Watusi, mwanaume mmoja ambaye ndiye alikuwa kiongozi alikuwa mtoto wa waziri wa afya nchini humo aliyeitwa Mazikuti ambaye kila siku baba yake akitaka sana mambo ya kikabila huku akitaka kabila la Wahutu likae kimya kwa sababu hawakuwa na elimu kama wao, aliwataka Wahutu wote wawe wafanyakazi na wao wawe mabosi.
Leo hii, mtoto wake alikuwa miongoni mwa watu walioleta fujo kwa kuua watu wengi. Mwili wake ulijawa damu, katika mkono wake wa kushoto alishika bunduki kubwa aina ya AK 47 huku mkono wa kulia akiwa na panga lililokuwa na michirizi ya damu.
“Wahutu huku, Watusi kule,” ilisikika sauti ya Mazikuti, mkono aliokuwa akiwaelekezea watu walipotaka kukaa ulikuwa ule alioshika upanga. Hakukuwa na mtu aliyesogea upande wowote ule.
“Paaa..paaa..paa...” ilisikika sauti ya risasi mahali hapo, alipiga risasi juu kama kuwatisha watu hao.
“Wahutu huku na Watusi kule,” alisema tena maneno yaliyomuogopesha Didier na familia yake, kwani wao walikuwa Wahutu, na watu walioingia humo ndani walikuwa Watusi. Wakakiona kifo kikiwa mlangoni.
Hiyo ilikuwa ni amri, Wahutu na Watusi walitakiwa kusimama kimakundi tofauti ili wale waliokuwa Wahutu wauawe kanisani hapo. Kila mmoja alibaki akitetemeka, hakukuwa na mtu aliyetaka kuona wenzake wakiuawa kanisani hapo, hivyo hakukuwa na mtu aliyekwenda upande wowote ule.
“Nimesema Wahutu kule na Watusi huku,” alisema Mazikuti kwa sauti kubwa huku uso wake ukionyesha hasira kubwa.
“Hatuwezi kujitenga, sisi ni wamoja katika mwili na roho,” alisema padri kwa kujiamini.
“Unasemaje?” aliuliza Mazikuti, alionekana kukasirishwa na maneno hayo, hakutaka kupoteza muda, akamnyooshea bunduki, kilichofuata baada ya hapo ni sauti za risasi, padri akaanguka chini, damu nyingi zilimtoka kifuani, pale chini, hakutingishika, alitulia tuli.
Hilo likamuogopesha kila mtu, ilionyesha kabisa kwamba Mazikuti hakutania hata kidogo, alichotaka kukifanya mahali hapo ni kuwaua Wahutu, kabila ambalo hakulipenda maisha yake yote.
Kifo cha padri yule kiliwafanya watu wote kuogopa, hapohapo wakaanza kujitenga, wakaanza kukaa kimakundi kama walivyoambiwa.
“Nakupenda Solange,” alisema Sophia huku akimuachia mkono aliokuwa amemshika na kwenda upande mwingine, ule wa Watusi walioambiwa waende.
Watusi tisini wakajitenga na kuwaacha Wahutu katika upande mwingine, walikuwa ni wengi zaidi ya wale waliokuwa wamekwenda upande mwingine. Wahutu wale waliokuwa na bunduki ambao waliongozwa na mtoto wa waziri, wakaamriwa wapige magoti tayari kwa kuwaua.
“Mungu! Naomba unisamehe kwa dhambi nilizotenda,” alisema Didier kwa sauti ya chini, Watusi wale wakawanyooshea bunduki, hapohapo milio ya risasi ikaanza kusikika, kilichotokea ni sauti za vilio na damu kutapakaa kila kona kanisani hapo.
Machafuko makubwa ya ukabila yaliyotokea nchini Rwanda yalivuma kila sehemu, kila mtu aliyesikia taarifa juu ya machafuko hayo alibaki akishangaa tu. Rwanda ilikuwa nchi ndogo, yenye watu wachache lakini kitendo cha watu haohao wachache kupigana tena kwa sababu ya uongozi, kiliwashangaza watu wengi.
Umoja wa Afrika (AU) haukutulia, walichanganyikiwa kwani hiyo ndiyo nchi pekee ambayo kwa mwaka huo, 1994 ilikuwa kwenye machafuko ya wenyewe kwa wenyewe baada ya kitu kama hicho kutokea katika nchi nyingine zamani ikiwemo Siera Leone.
Mara baada ya tukio hilo kutokea, kikao cha dharura kikaitishwa na viongozi kujadili ni kitu gani kilichotakiwa kufanywa. Uamuzi mmoja tu ndiyo uliotolewa kwamba wanajeshi wa umoja huo ndiyo walitakiwa kwenda nchini Rwanda kuhakikisha kwamba amani inarudi tena na machafuko yanakwisha mara moja.
Zaidi ya wanajeshi laki moja wakaondoka kuelekea nchini humo, hakukuwa na mtu aliyeuawa, walikuwa mahali hapo kuhakikisha kwamba amani inarudi tena na kuwa kama zamani.
Wakaanza kurandaranda ndani ya nchi hiyo, walitembea kimakundi na kila sehemu. Kile walichokiona kwenye televisheni ndicho walichokishuhudia ndani ya nchi hiyo. Miili mingi ya watu ilikuwa barabarani, hali ilimsikitisha kila mtu aliyeiona miili ile.
Watoto ambao waliwapoteza wazazi wao na hawakuwa na pa kukimbilia, walikaa karibu na maiti za wazazi wao na kuanza kulia kwa uchungu mkubwa, hawakutaka kuondoka, hawakuwa tayari kuiacha miili ya wazazi wao barabarani.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/--
Wanajeshi waliokuwa katika kikundi walichokipa jina la Spider 15 walizunguka katika mitaa mbalimbali mpaka walipofika nje ya kanisa moja kubwa la Roman Catholic, walitaka kulipita lakini mara baada ya kusikia milio ya risasi ndani, hawakutaka kuondoka, walichokifanya ni kuandaa bunduki zao na kuanza kutembea kwa mwendo wa kunyata kuelekea kanisani humo.
“Nimesema Wahutu kule na Watusi huku,” ilisikika sauti ya mwanaume mmoja ndani ya kanisa hilo.
Tayari walijua kwamba kulikuwa na hatari ndani ya kanisa hilo, hatua zao za kunyata zikaongezeka zaidi mpaka kuufikia mlango mkubwa wa chumba na kujibanza pembeni huku macho yao yakiwa kanisani mule.
Walichoweza kukiona ni idadi kubwa ya watu ambao walikaa kimakundi, kundi moja lilikuwa la watu waliopiga magoti huku kundi jingine likiwa la watu waliosimama.
Vilio vilitawala kila kona, mbele ya kundi la watu waliopiga magoti, mbele ya kulikuwa na watu waliokuwa na bunduki mikononi mwao. Walikwishajua kile kilichotaka kutokea, kwa staili ya kikomandoo, ya kubimbilika wakaanza kuingia kanisani mule na kuanza kuwamiminia risasi watu wale.
Lilikuwa ni tukio la haraka sana, ni ndani ya sekunde kumi tu, hakukuwa na mtu yeyote aliyesimama, wote walikuwa chini, damu ziliwatoka migongoni na kisogoni, hapohapo wakapoteza uhai.
“Mko katika mikono salama....” alisema mwanajeshi mmoja huku akiwaangalia watu wale.
Hiyo ndiyo ilikuwa salama yao, wanajeshi wale waliowaokoa walionekana kuwa mashujaa wao. Wakachukuliwa na kupelekwa nje ya kanisa lile tayari kwa kuanza safari kuelekea Kibungo, Mashariki mwa Rwanda ambapo waliambiwa kwamba kulikuwa na utulivu.
“Solange, siamini Mungu kama tumenusurika,” alisema Didier huku akiwa pembeni ya mdogo wake, Solange na Sophia.
“Mungu ni mweza, najua atatuongoza na kutulinda mpaka Kibungo,” alisema Solange.
Walikuwa wakitembea huku wakiwa karibukaribu sana, katika kila hatua waliyokuwa wakipiga, walifarijiana kwamba wangefika salama Kibungo. Mioyo yao ilijawa tumaini kubwa, wanajeshi zaidi ya watano ambao walikuwa wakiwalinda, tena wakiwa mbele yao kuliwapa uhakika kwamba wangefika salama.
Walipofika Makwete, kilometa kumi kabla ya kuingia Kibungo, tena ikiwa katika barabara iliyozungukwa na msitu mkubwa, ghafla milio ya risasi ikaanza kusikika kutokea msituni, kila mmoja akashtuka, wanajeshi wote waliokuwa wakiwaongoza walikuwa chini, damu ziliwatoka, vilio vikasikika, hakukuwa na sababu ya kubaki mahali hapo, kundi la watu hao mia mbili wakaanza kukimbia kuelekea msituni, kwa jinsi Didier alivyochanganywa na milio ile ya bunduki, badala ya kumshika Solange mkono, akajikuta akimshika Sophia pasipo kujijua na kuanza kukimbia naye porini.
Kila mmoja alikimbilia katika upande aliouona kuwa salama katika maisha yake. Milio ya risasi iliendelea kusikika nyuma yao, hakukuwa na mtu aliyesubiria, wasiokuwa na mbio, wakaachwa wakiuawa mahali hapo, watoto ambao hawakujua ni nani walitakiwa kumfuata, wakajikuta wakipigwa risasi na kufa.
Didier hakutaka kusimama, alimshikilia vilivyo Sophia na kusonga naye mbele. Hakuwa amegundua kwamba yule aliyemshika hakuwa mdogo wake, Solange bali rafiki yake Solange, Sophia, alichokitaka mahali hapo ni kuyaokoa maisha yao tu.
Walikimbia kwa takribaki kilometa tano porini, tena huku wakipita katika miti mikubwa, wakakutana na ziwa Mugesera ambalo walitakiwa kulivuka na kutokea upande wa pili ambapo ndipo kulipokuwa Kibungo. Mahali hapo hawakuwa peke yao, kulikuwa na watu wengine zaidi ya kumi ambao nao walinusurika kuuawa kule barabarani.
“Solange, ni lazima tuvuke ili tuwe salama,” alisema Didier huku akiliangalia ziwa lile pasipo kugundua kwamba yule aliyekuwa akimwambia hivyo hakuwa Solange bali Sophia.
“Didier....”
“Naam...”
“Mimi si Solange, ni Sophia...” alisema Sophia.
Hapohapo Didier akayageuza macho yake na kumwangalia mtu huyo, kweli hakuwa Solange kama alivyofikiria bali alikuwa rafiki wa mdogo wake, Sophia. Hapohapo, pasipo kutegemea Didier akajikuta akipiga magoti chini na kuanza kulia, hakuamini kile kilichokuwa kimetokea, yaani kwa mwendo mrefu kutoka barabarani mpaka kufika pembezoni mwa ziwa lile, yule aliyemshika mkono na kukimbia naye akiamini kwamba alikuwa mdogo wake, kumbe hakuwa Solange bali Sophia.
“Solange yupo wapi?” aliuliza Didier huku akiangalia huku na kule na wakati mwingine kuita, alionekana kuchanganyikiwa.
“Sijui yupo wapi!”
“Hapana! Siwezi kusonga mbele, ni lazima turudi kumfuata Solange na mama,” alisema Didier huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Turudi?”
“Ndiyo! Siwezi kusonga mbele pasipo Solange na mama,” alisema Didier huku akionekana kumaanisha alichokisema.
Sophia akatumia muda huo kumbembeleza Didier kwamba ilikuwa ni lazima wavuke ziwa hilo kusonga mbele kwani huko walipotoka hakukuwa na amani hata kidogo, milio ya risasi ilitawala na kulikuwa na watu wabaya ambao wangeweza kuwaua.
Didier hakutaka kuelewa kabisa, alikuwa radhi kufa lakini lakini si kuwaacha ndugu zake wakiuawa peke yao. Alichokifanya Sophia ni kuwaambia watu wengi kile alichotaka kukifanya Didier, wengi walimwambia kwamba hakutakiwa kurudi nyuma, alitakiwa kusonga mbele kwani huko nyuma kulichafuka mno.
“Siwezi kuendelea. Baba alikufa kwa kuwa sikuwa na uwezo wa kumuokoa, siwezi kuwaona niliobaki nao wakifa, kama nina uwezo wa kuwaokoa, acha nifanye hivyo, sisongi mbele, hapa nitarudi nyuma tu,” alisema Didier, machozi yalimbubujika kwa uchungu.
“Didier, naomba tusonge mbele.....”
“Haiwezekani Sophia, siwezi, ni lazima nirudi,” alisema Didier, akaanza kupiga hatua kurudi nyuma ambapo milio ya risasi iliendelea kusikika.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment