Search This Blog

Sunday, July 10, 2022

DUNIA ISIYO NA HURUMA - 2

 





    Simulizi : Dunia Isiyo Na Huruma

    Sehemu Ya Pili (2)



    Mara baada ya milio ya risasi kusikika pale walipokuwa na wanajeshi kudondoka chini, hakukuwa na mtu aliyesubiri, kila mmoja akaanza kukimbia kuyaokoa maisha yake.

    Kwa Solange na mama yake, wakaanza kukimbia upande mwingine wa Kaskazini, upande tofauti na Didier alipokimbilia pamoja na msichana Sophia. Si kwamba Solange hakumuona kaka yake akikimbia na Sophia, alimuona na alijaribu kumuita ili asimame lakini kutokana na milio ya risasi iliyokuwa ikisikika mahali hapo, hakukuwa na mtu aliyekuwa tayari kusimama.

    “Didier...Didier...” aliita Solange lakini sauti yake ilimezwa na milio ya risasi iliyoendelea kusikika mahali hapo.

    Alimshika mama yake mkono, hakutaka kumuachia, wao na kundi kubwa la watu wakaanza kukimbia upande mwingine kabisa. Kila mmoja alipiga kelele, wengi wakapigwa risasi na kudondoka chini lakini wao waliosalimika, hawakutaka kusimama, waliendelea kukimbilia porini zaidi.

    Solange alitaka kukimbia kwa kasi zaidi kuelekea porini, kila alipowaangalia wenzao walikimbia kwa kasi kubwa hali iliyosababishwa kuachwa umbali mrefu. Mama yake ndiye alikuwa mzito, alikuwa mwanamke mwenye umri wa zaidi ya miaka hamsini, hakuwa na mbio, kukimbia kwake ilikuwa ni kujivutavuta sana.

    “Solange....” aliita mama yake, ndiyo kwanza walikuwa wamekimbia kama kilometa moja.

    “Abeee...”

    “Siwezi kukimbia zaidi,” alisema mama yake huku akionekana kuchoka.

    “Kwa nini? Mama! Tukimbie tuyaokoe maisha yetu, tukimbie mama, vumilia,” alisema Solange huku akimvuta mama yake, milio ile ya risasi iliyokuwa ikisikika mahali hapo, iliwatisha.

    “Acha nife...” alisema bi Shamarima maneno yaliyomshtua Solange.

    “Ufe? Siwezi kukuacha ufe, huwezi kufa mama,” alisema Solange huku akimwangalia mama yake usoni, machozi yalikuwa yakimbubujika.

    Bi Shamarima alimaanisha alichokizungumza, alikuwa mwanamke mzee ambaye miguu yake ilianza kupoteza nguvu, kitendo cha kukimbia kidogo, alichoka, miguu iliuma na hakuona kama alitakiwa kukimbia zaidi.

    Alitaka kuishi lakini hakuwa radhi kuendelea na safari yake ya kukikimbia kifo. Alimwambia binti yake kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wa safari yake, asingeweza kuendelea mbele zaidi.

    Alimwambia Solange aendelee na safari lakini msichana huyo hakutaka kusonga mbele, alikumbuka vilivyo kwamba walimpoteza baba yao, alikimbia upande mwingine tofauti na kaka yake, mpaka kipindi hicho hakujua kama kaka yake alikuwa salama huko alipokimbilia au aliuawa kama wengine, kwake, kumuacha mama yake mahali hapo lilikuwa jambo lisilowezekana.

    “Siwezi kukuacha mama,” alisema Solange huku akilia kama mtoto.

    “Kimbia uyaokoe maisha yako Solange, okoa maisha yako binti yangu,” alisema bi Shamarima huku kwa muonekano wake tu, alionekana kukata tamaa.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alichokifanya Solange ni kumuinua mama yake pale alipokuwa huku lengo lake likiwa ni kuondoka kusonga mbele zaidi. Ilikuwa kazi kubwa, mama yake alikuwa mzito mno, hivyo akashindwa kabisa.

    Huku akijifikiria ni kitu gani alitakiwa kufanya, hapohapo akasikia risasi zikipiga karibu na miti ilikuwa karibu naye, akaogopa, akajua kwamba wale watu waliokuwa wakipiga risasi walikuwa wamewasogelea kabisa, hivyo akaona ilikuwa ni lazima akimbie.

    “Kimbia Solange...kimbia, acha nife,” alisema bi Shamarima huku akimsukuma Solange.

    Iliuma, ilimuogopesha, ilikuwa picha mbaya ambayo hakuwahi kuiona maisha yake yote, hakuendelea kubaki mahali hapo, kwa kuwa mama yake alimwambia akimbie kuyaokoa maisha yake, hakuwa na jinsi, alichokifanya ni kukimbia kusonga mbele.

    Wakati akiwa njiani, kama hatua sitini kutoka pale alipomuacha mama yake, milio ya risasi ikasikika nyuma yake, kilio kikubwa kikasikika, aliifahamu sauti hiyo, ilikuwa ya mama yake, moja kwa moja akajua kwamba watu hao walimfikia mama yake na kumpiga risasi, moyo wake ukamuuma mno. Hakusimama, aliendelea kusonga mbele zaidi.

    Hakujua alipokuwa akielekea, yeye alichokijua ni kukimbia kuyaokoa maisha yake tu. Njiani, alikuwa akilia, kifo cha mama yake kilimhuzunisha, wakati mwingine alikuwa akijuta, hakuona kama mama yake alitakiwa kuachwa porini peke yake na kuuawa, hakika kila alipokumbuka, moyo wake ulimuuma mno.

    Upande huo alipokuwa akikimbilia ilikuwa ni Tumba, Kaskazini mwa nchi ya Rwanda, kilometa zaidi ya mia mbili kutoka jijini Kigali, alipita sehemu iliyokuwa na maporomoko makubwa, tambarare, milima lakini kote huko hakuwa tayari kusimama, alidhamiria kusonga mbele zaidi.

    Baada ya saa nne za kukimbia ndipo akakutana na kundi kubwa la watu wakiwa wamepumzika chini ya miti. Watu hao walikuwa zaidi ya mia moja, pembeni yao walikuwa na viroba vilivyokuwa na nguo zao huku wengine nguo hizo zikiwa zimefugwa katika khanga walizokuwa nazo.

    Wengi walikuwa wasichana wadogo, na wazee walikuwepo ila ni wale ambao kidogo walionekana kuwa na nguvu ya kukimbia.

    Vijana walioongozana nao, wengi walipanda juu ya miti kutafuta matunda kwa ajili ya kula, hakukuwa na mtu aliyekuwa na chakula, porini hapo, na walikimbia kwa umbali mrefu pasipo kula chochote kile.

    Solange akaufuata mti mmoja na kukaa chini, machozi yalikuwa yakimbubujika, moyo wake ulihisi maumivu makubwa, hakuamini kama kile kilichokuwa kikitokea, yeye ndiye aliyekuwa akikipitia.

    Pale chini alipokaa, alimuomba Mungu ili abadilishe kila kitu kilichokuwa kikiendelea, yaani kama ni matukio halisi basi yabadilike na kuwa ndoto, hakutaka kuona kile kilichokuwa kikitokea kiwe maisha halisi.

    Nchi yake ya Rwanda, iliyokuwa na watu wenye upendo na amani, ghafla ilibadilika, machafuko waliyokuwa wakiyasikia kutoka kwa watu wengine, leo hii nao walianza kuyapitia machafuko hayo.

    Watu walichinjana kama hawakuwa wa nchi moja, wale wasiokuwa na uwezo wa kutumia silaha yoyote, wale wasiotaka kumwaga damu ndiyo waliokuwa wakikimbia, walikuwa tayari kuwa wakimbizi lakini si kuuawa, tena na watu waliokuwa wakiishi nao nchi moja.

    “Wewe ni Solange?” ilisikika sauti ya mwanaume mmoja aliyekuja mahali pale alipokuwa amekaa Solange huku akiwa amekiinamisha kichwa chake.

    Solange akauinua uso wake na kumwangalia mtu huyo aliyemuuliza swali hilo, alipomwangalia usoni mwanaume huyo, hakumfahamu, alikuwa mgeni machoni mwake, kwa haraka sana akaanza kuvuta kumbukumbu zake kuona kama alikwishawahi kumuona mwanaume huyo sehemu yoyote ile, hakukumbuka chochote kile.

    “Wewe ni nani?” aliuliza Solange hata kabla ya kujibu swali alilouliza.

    “Huwezi kunifahamu. Ninaitwa Michael Buchumi,” alisema mwanaume yule.

    “Michael yupi?”

    “Ni mtoto wa mvuvi masikini, mzee Buchumi, si kama wewe binti wa tajiri mkubwa,” alisema Michael huku akikaa chini na kuanza kuangaliana na msichana Solange.

    “Nikusaidie nini Michael?”

    “Solange, natumaini tupo safari moja, si ndiyo?”

    “Safari moja! Kwenda wapi?”

    “Kwani wewe unakwenda wapi?”

    “Sijui! Nimekimbia kukiepuka kifo, sijui ninakwenda wapi.”

    “Oooh! Solange! Hapa ni porini, kilometa nyingi kutoka Kigali. Natumaini baada ya muda tutaingia Tumba,” alisema Michael.

    “Mungu wangu! Tumba?”

    “Ndiyo! Hatuna cha kufanya, ni lazima tukimbie, ikiwezekana kuingia Demokrasia ya Kongo,” alisema Michael.

    “Demokrasia ya Kongo? Hapana! Siwezi kwenda huko.”

    “Kwa nini?”

    “Hujui kwamba hata nao wana mapigano na waasi wa M23?”

    “Najua, ila tutafanyaje?”

    “Siwezi kwenda huko.”

    Huo ndiyo msimamo aliouweka, japokuwa kila mtu katika kundi hilo alisema kwamba ilikuwa ni lazima wakimbilie nchini Kongo lakini maneno ya Solange aliyomwambia Michael yakawafumbua macho watu wengine, kukimbilia kwenda Kongo ilikuwa ni sawa na kukikimbilia kifo kwani hata huko napo bado kulikuwa na mapigano ya serikali ya nchi hiyo na waasi wa Kundi la M23.

    Watu walipokumbushwa kuhusu kundi hilo la waasi, kila mmoja akabadilika, hakukuwa na aliyetamani kukimbilia nchini humo tena, wengi wakabadilisha mawazo na kuona kwamba ilikuwa ni afadhali kukimbilia nchini Uganda, nchi ambayo waliamini hakukuwa na mapigano yoyote yale.

    “Basi tutakimbilia Uganda,” alisema Michael.

    “Hakuna tatizo,” aliitikia Solange.

    Walikaa kwa muda wa saa tano, usiku wa saa tatu, kundi hilo la watu likaanza safari ya kuelekea nchini Uganda, kusafiri kwao nyakati za usiku ilionekana kuwa nafuu kwao kwa kuamini kwamba ndiyo ilikuwa nyakati tulivu ambapo hata wapiganaji nao hawakuwepo. Hivyo safari ikaanza huku Solange na Michael wakiwa wameambatana pamoja.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Didier alidhamiria kurudi kule walipotoka, hakuwa radhi kuona akiondoka na wakati familia yake ilikuwa nyuma yake. Alichanganyikiwa lakini hakutaka kuelewa, alichokuwa akitaka kukiona ni dada yake, Solange na mama yake ambaye alikuwa na uhakika kwamba walipata matatizo kule walipokuwa.

    Milio ya risasi iliendelea kusikika lakini hakutaka kubaki, hakutaka kusonga mbele, alikuwa tayari kufa lakini mpaka kuhakikisha anakufa mbele ya dada yake na mama yake.

    Watu walimsihi sana lakini Didier hakukubaliana nao, upendo mkubwa aliokuwa nao kwa ndugu zake haukuelezeka hata kidogo. Sophia alijitahidi kumzuia kwa maneno, hakuelewa, alijitahidi kumzuia kwa kumshika mkono lakini bado haikusaidia hata kidogo.

    “Sophia, songa mbele, narudi nyuma kwa ajili ya familia yangu,” alisema Didier huku kibubujikwa na machozi.

    “Didier, naomba usirudi, utakufa, utakufa Didier...” alisema Sophia.

    “Hakuna amani, kuna wengi wamekufa Sophia, sipo tayari, kama kufa, acha nife lakini si kumuacha mama yangu na dada yangu,” alisema Didier.

    “Watakuwa wamekufa...naomba tusonge mbele....”

    “Wamekufa! Basi acha nikaone hata maiti zao, sipo radhi kuona zikiliwa na wanyama wa porini,” alisema Didier.

    Hakutaka kubaki mahali hapo, alichokifanya ni kuondoka, tena huku akikimbia kurudi kule walipotoka. Moyo wake ulikuwa na huzuni kubwa, hakukubali kuona akisonga mbele na wakati nyuma yake kulikuwa na familia yake.

    Alipita katikati ya miti mikubwa, alipita mpaka katika nyasi ndefu lakini hakusimama, alitaka kufika barabarani haraka iwezekanavyo. Kadiri alivyozidi kukaribia ndivyo milio ya risasi ilivyozidi kusikika masikioni mwake, hakutaka kusimama, dhamira yake ilikuwa ileile, kufika barabarani kwa lengo la kuwaona ndugu zake.

    “Paaa...paaa...” milio kadhaa ya risasi ilisikika, risasi zile zilimkosa na kupiga kwenye magome ya miti.

    “S'il vous plaît ne me tuez pas,” (Tafadhali msiniue,) alisema Didier kwa sauti ya juu huku akionekana kuogopa.

    “Qui es-tu?” (Wewe nani?)

    “Didier...”

    “Un Tutsi ou Hutu?” (Mtusi au Mhutu?) ilisikika sauti ya mtu huyo.

    Wakati akizungumza na mtu huyo kwa sauti, Didier alikuwa amejificha kichakati, nyuma ya mti mmoja, alikuwa akitetemeka, japokuwa sauti ya mtu huyo ilisikika nyuma yake lakini alihisi kwamba mtu huyo hakuwa peke yake kwani hata zile risasi zilizomkosakosa, zilisikika kwa mpigo hali iliyoonyesha wapigaji walikuwa zaidi ya mmoja.

    “Un Tutsi ou Hutu?” (Mtusi au Mhutu?) mwanaume huyo aliuliza tena, mara hii kwa sauti ya juu yenye hasira.

    “Un Hutu.” (Mhutu)

    Wakati anatoa jibu hilo, tayari wanaume wale walimfikia pale alipokuwa, hofu yake ilikuwa ni juu ya Watusi, alihisi kwamba watu hao walikuwa Watusi na kuona kwamba ilikuwa ni lazima auawe mara moja kutokana na mapigano ya kikabila yaliyokuwa yakiendelea.

    Alipowaona watu hao kwamba ni Wahutu wenzake, akashusha pumzi ndefu na kujiona akiwa katika mikono salama kwani kabila moja hawakuwa wakiuana, kila mmoja alipamba kwa kuwaua watu wa kabila jingine.

    Walimwangalia Didier, alionekana kijana mdogo, si zaidi ya miaka ishirini na tano, uso wake ulijawa hofu na kwa mbali kijasho chembamba kilikuwa kikimtoka. Didier alipowahesabu wanaume wale, walikuwa watano, tena wote wakiwa na bunduki mikononi mwao.

    “Unajua kutumia bunduki?” aliuliza jamaa mmoja.

    “Hapana!”

    “Ushawahi kuua?” aliuliza jamaa mwingine.

    “Hapana!”

    “Kuchinja kuku je?”

    “Sijawahi!”

    “Daah! Sawa! Kuanzia leo utaua na kufanya mambo mengine.”

    “Nitaweza?”

    “Usijali, utaweza tu. Chukua hii!” alisema mwanaume mmoja, akamkabidhi bunduki moja, ilikuwa AK 47.

    Japokuwa alikuwa na safari yake ya kwenda kuwatafuta ndugu zake lakini hakwenda tena huko, alionekana kuwa na hofu ya kuwaambia watu wale kwamba wamuache kwa sababu alikuwa na safari zake.

    Akaungana nao na kuanza safari mpya ya kwenda asipopafahamu, ila alijua kwamba ni upande wa Magharibi. Kichwa chake hakikutulia, kila wakati aliwafikiria ndugu zake, alitamani kuonana nao lakini hakuwa na nafasi hiyo tena.

    “Tunataka tuiweke nchi hii mikononi mwetu,” alisema jamaa mmoja, kidogo alitaka ukaribu na Didier, huyo alijitambulisha kwa jina la Jackson.

    “Kwa kuua?”

    “Ndiyo! Wakati mwingine amani haiwezi kupatikana pasipo kutoa damu! Hawa Watusi wametutesa sana, lazima tuwamalize, ikiwezekana kizazi chao chote,” alisema Jackson.

    “Mmh! Sawa! Na huku tunakwenda wapi?”

    “Kuwatafuta Watusi.”

    “Wapo wapi?”

    “Popote walipo, sisi tutawaua tu, hatujui wapo wapi, ila popote walipokuwa, tutawaua,” alijibu Jackson kwa sauti ya kutamba, alipoongea hayo, akaanza kutoa tabasamu kubwa.

    Wakati huo walikuwa wakipita porini huku kule walipokuwa wakielekea ikiwa ni Bicumbi, sehemu ambayo ilitawaliwa na mapigano mengi na Watusi wakiwa wengi sehemu hiyo.

    Hakukuwa na sababu ya kusimama njiani, kama kububujikwa na machozi, alibubujikwa sana lakini hakutaka kuwaambia watu hao kilichokuwa kikiendelea moyoni mwake.

    Kuwa nao, ilikuwa ni sawa na kulazimishwa, hakuwa tayari kutangulizana nao kwani alijua kwamba ilikuwa hatari ila hakuwa na jinsi, kwa wakati huo, alikuwa tayari kwa kila kitu, hata kama angeletewa mtu na kuambiwa aue, ilikuwa ni lazima kufanya hivyo kwani alikuwa chini ya watu fulani.

    Ilipofika usiku, wakapumzika, watu wale wakatoa vyakula kutoka katika mabegi waliyokuwa nayo na kuanza kula, walipomaliza, walilala. Usingizi haukuweza kuja, kila alipojaribu kulala, alihisi kulikuwa na watu wakija na kumuua.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mbali na hilo, pia mawazo juu ya wazazi wake yalimtesa mno, kila alipojaribu kuvuta usingizi na kulala, ilishindikana kabisa.

    Mpaka sauti za ndege zilipoanza kusikika kwamba tayari alfajiri ilikuwa imeingia, hakuwa amelala kabisa, alikesha kama popo. Wenzake walipoamka, safari ikaanza tena, hawakutakiwa kwenda sehemu nyingine yoyote zaidi ya Bicumbi, sehemu iliyokuwa na Watusi wengi ambapo huko ndipo walipotaka kuitafuta amani kwa kumwagaji wa damu.

    Kutoka maeneo ya Rutonde hapo walipokuwa mpaka Bicumbi ilikuwa ni umbali wa kilometa sitini, hivyo walitakiwa kutembea na kupumzika mara kwa mara. Njiani, hawakubahatika kukutana na watu wengine kwani hata njia walizopita zilikuwa ni za kujificha sana.

    Kuanzia saa moja asubuhi mpaka saa kumi na mbili jioni, wakaanza kuona dalili za uwepo wa watu kule walipokuwa wakielekea na kuhisi kwamba tayari walikaribia hapo Bicumbi.

    Nyumba mbalimbali mbovu zikaanza kuonekana, hapo, hawakutakiwa kukukuruka, kuingia kwa papara kwani sehemu kubwa ya Bicumbi ilikuwa ikikaliwa na Watusi wengi.

    Walitembea kwa tahadhari, tena kwa kujifichaficha, kila walipopita, maiti za watu zilizagaa, zilianza kuharibika na kutoa harufu kali iliyowafanya muda wote kuziba pua zao.

    Sehemu yote ilikuwa kimya, watu walizikimbia nyumba zao kwa sababu ya mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyokuwa yakiendelea. Picha iliyoonekana mahali hapo, ilimsikitisha mno Didier na kuona kwamba tangu azaliwe, hakukuwa na siku ambayo aliona kitu kibaya na chenye kumchoma moyo wake kama kile alichokuwa akikiona mahali hapo.

    Walizunguka hapo Bucumbi bila kuchoka, lengo lao kwa wakati huo lilikuwa ni kuwaona Watusi na kuwaua. Hakukuwa na kitu kingine zaidi ya maiti na mbwa waliokuwa bize wakila maiti hizo.

    Walijaribu kuingia ndani ya nyumba moja baada ya nyingine ili kuona kama kungekuwa na watu lakini humo ndani waliambulia patupu.

    Hakukuwa na mpango wa kurudi nyuma, walidhamiria kusonga mbele, waliendelea kwenda mpaka walipofika sehemu ambayo kulikuwa na kanisa la kijiji mbele yao.

    Kote huko walipokuwa wakipita, maiti zilikuwa nyingi, tena damu zikiwa mbichi kabisa hali iliyoonyesha kwamba watu hao waliuawa kipindi kifupi kilichopita. Wakahisi kwamba kule kwenye kanisa lile lililokuwa mbele yao kulikuwa na watu, hivyo wakaanza kulisogelea.

    Mwendo wao ulikuwa ni wa kunyata, tena wakiangalia huku na kule kwani wakati mwingine walihisi kwamba Watusi walijificha sehemu hivyo kama wangeonekana basi wote wangeuawa.

    “Andaeni bunduki zenu, nimesikia minong’ono,” alisema jamaa mmoja, alitwa Chonji, ndiye aliyeonekana kuwa mkubwa wa msafara ule.

    Kanisa ambalo lilikuwa mbele yao halikuwa kubwa, lilikuwa dogo tena lililojengwa kwa udongo upande mmoja, walipoukaribia mlango, hawakutaka kuufungua kwa kuhisi kwamba inawezekana humo ndani kulikuwa na watu wenye risasi, walichokifanya ni kuanza kulimiminia risasi mfululizo palepale nje.

    “Paa...paaa...paaa...paaa...” milio ya risasi ilisikika mfululizo ila katika risasi zote hizo, hakukuwa hata na risasi moja iliyotoka katika bunduki ya Didier.

    Mara baada ya kuhakikisha kwamba tayari waliwamaliza watu wote waliokuwa ndani ya kanisa lile, wakaufuata mlango na kuingia ndani. Walichokikuta, wenyewe walikifurahia na kuanza kupongezana. Mbele yao kulikuwa na maiti za watoto, wanawake wajawazito na wanaume wengine, wote hao, hakukuwa hata na Mhutu, wote walikuwa Watusi.

    Wakagongesheana mikono na kukumbatiana. Kwa Didier, kile alichokuwa akikiona, hakukiamini kabisa, hakuwahi kuua na wala hakuwa na mpango wa kufanya hivyo ila kwa kile kilichokuwa kikiendelea, kilimuweka katika wakati mgumu na kuona kwamba muda wowote ule naye angeweza kuua.

    Alilia na kulia lakini hilo halikusaidia, kwa sababu alikuwa katika kundi hilo la watu, ilikuwa ni lazima kulia, wenyewe walikuwa na msemo usemao ‘UA WATUSI UWALINDE NDUGU ZAKO’.

    “Jackson....” alimuita mshikaji wake.

    “Niambie...”

    “Haya mambo mpaka lini?”

    “Kwani wao si ndiyo wameanza! Kama wameanza, acha sisi tumalize...” alisema Jackson.

    “Ninaumia sana, sipendi kuua na sijawahi kuua kabisa....” alisema Didier.

    “Utajifunza tu, hakuna anayefundishwa kuua...utajua tu mbele ya safari...” alijibu kijana huyo.

    Hawakutaka kuendelea kubaki mahali hapo, walichokuwa wakikitaka, tayari walikikamilisha hivyo walitakiwa kusonga mbele. Mawazo juu ya familia yake hayakumuisha, kila wakati alimfikiria mama yake na dada yake, hakujua mahali walipokuwa ila alijiahidi kwamba ilikuwa ni lazima awatafute, hata kama ingechukua miaka kumi, alihakikisha anawatafuta mpaka anawapata.

    “Ni lazima niende Tanzania,” alisema Didier.

    “Kufanya nini?”

    “Kuishi...nchi yetu imekwishachafuka...”

    “Didier, acha ujinga, tena ukisikiwa na hawa wenzetu, watakuua...” alisema Jackson.



    Nchi ilikuwa ya kwao, babu zao walipigana usiku na mchana kuwaondoa wakoloni, baada ya kufanikiwa katika hilo, miaka ikapita na hatimaye, wao wenyewe wakaanza kupigana, wakauana, nchi nzima ilitapakaa damu.

    Kundi kubwa la watu wakiwemo Solange na Maichael liliendelea na safari, walipita porini, hakukuwa na mtu aliyesimama, muda huo, kila mmoja alitaka kuiokoa nafsi yake na nchi y Auganda ndiyo ilionekana kuwa kimbilio lao kubwa.

    Kutoka hapo walipokuwa mpaka Uganda ilikuwa ni zaidi ya kilometa mia tano lakini pamoja na hayo yote, wote kwa pamoja waliamini kwamba wangefika huko salama na kuanza maisha mapya.

    Solange hakuacha kulia, bado moyo wake ulimuuma mno kila alipomfikiria mama yake. Alikufa kifo kibaya cha kupigwa na risasi, mbali na mama yake huyo, pia hakujua kaka yake alikuwa wapi, hakujua kama huko alipokuwa alikuwa salama au naye aliuawa kama watu wengine.

    Duniani, akajiona peke yake, mbele yake aliliona giza kubwa likiwa limetanda. Hakutegemea kabla kama kuna siku angeishi katika maisha kama aliyokuwa akiishi kipindi hicho.

    Hakukuwa na magari tena, ule utajiri wa baba yake, waliuacha Kigali walipotoka, katika kipindi hicho, hakukuwa na kitu chochote kilichoonekana kuwa muhimu katika maisha yao zaidi ya roho zao.

    Wanawake waliowabeba watoto wao, walimsikitisha mno, kila alipowaangalia, walikuwa watu waliokata tamaa ambao roho zao walizikabishi kwa Mungu tu. Safari hiyo ilisonga mpaka walipofika sehemu iliyokuwa na mashimo makubwa mno, nayo, ilitelekezwa, hawakujua kulikuwa na nini mpaka kuwa na mashimo makubwa kiasi hicho, tena porini kama hapo.

    “Hii ni nini?” aliuliza Solange.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Niliwahi kumsikia rais akizungumza kuhusu machimbo ya madini yaliyokuwa huku porini, kweli inawezekana yakawa haya?” aliuliza Michael.

    “Labda...tufanye nini?”

    “Tuvukeni!”

    “Kweli ni salama katika maisha yetu?”

    Watu walikuwa wakihoji, hakukuwa na mtu aliyekuwa na amani muda huo. Idadi kubwa ya watu waliokuwa muda huo ilionyesha dhahiri kwamba wasingekuwa salama, iwe isiwe ilikuwa ni lazima kuonekana na hatimaye kuua

    Rais Juvenal Habyarimana ambaye aliuawa katika ndege siku chache zilizopita ndiye aliyewaambia wananchi kwamba porini huko kulikuwa na machimbo ya madini ambayo hayakutakiwa kuchimbwa kwani hiyo haikuwa sehemu salama kutokana na kuwa msituni sana.

    Pamoja na kuambiwa hivyo, wananchi hawakusikia, waliendelea kuchimba tena kwa kusaidiana na makampuni makubwa kisiri. Hukohuko, wanawake wengi wakaanza kubakwa, wengine wakaanza kuuawa, watu waliokuwa na bunduki kali, wakavamia machimbo hayo na kuanza kuua watu ovyo.

    Hiyo haikuwa sehemu salama hata mara moja. Na hata mapigano yalipoanza, ilisadikiwa kwamba kuna baadhi ya watu walikimbia lakini wengine walibaki. Hakukuwa na aliyekuwa na uhakika, sehemu hiyo ilionekana kuwa hatari sana.

    Kundi lile la watu lilipofika karibu na eneo hilo, hawakutaka kutoka kwa kuhofia kwamba inawezekana kulikuwa na watu, wakajificha porini, walichokifanya ni kuwatuma wanaume wanne, wapite mpaka kule kwenye mashimo, ili kama kutaonekana salama, kundi zima lipite ila kama hakutokuwa salama, basi wasipite, wageuze na kurudi walipotoka.

    “NA wewe unatakiwa kwenda!” alisema mzee mmoja, alimwambia Michael.

    “Mimi?”

    “Ndiyo! SI peke yako, wenzako hawa watatu, tunataka kujua kama sehemu hii ni salama...” alisema mzee huyo.

    Huo ndiyo uamuzi uliofikiwa, vijana wanne walichaguliwa kuwa kama chambo, walitakiwa kutoka hapo porini na kuanza kuvuka katika njia iliyokuwa na mashimo hayo. Hawakuwa na jinsi, wakaondoka na kuanza kuvuka huku Michael akiwa amekwishamwambia Solange kwamba hana uhakika kama angevuka, moyo wake ulihisi kwamba kuna watu walikuwa wamejificha hivyo kuwasubiri, kama wangepita katika njia hiyo yenye mashimo hayo, basi wamiminiwe risasi na kufa.

    “Kama nitakufa...jua kwamba nilitamani kuishi na kufika Uganda,” alisema Michael.

    “Usijali! Mungu atakuwa pamoja nawe...” alisema Solange.

    Watu wote wakatulia na wanaume wale kuanza kupiga katika njia ile iliyokuwa na uwanja mkubwa. Kwa jinsi ilivyoonekana tu, hakukuwa na amani hata kidogo. Huku wakipiga hatua, tayari tumbo la Michael likaanza kuuma, wote wanne walikuwa wakitetemeka, hakukuwa na kingine kilichofanyika zaidi ya kuanza kusali, tayari walijiona kuwa wafu waliokuwa wakitembea.

    ****

    Yalikuwa machimbo mapya kabisa ambayo yaligunduliwa na Mzungu mmoja, aliyekuwa mtalii ambaye alifika Rwanda kwa ajili ya utalii, Mzungu huyo aliitwa Sam Donald.

    Mara baada ya kugundua machimbo hayo yaliyokuwa na almasi, akapeleka taarifa katika serikali ya Rwanda iliyokuwa chini ya rais Juvenal Habyarimana. Rais alikubaliana naye vizuri na hivyo sehemu hiyo kuwekwa alama na yeye kurudi nchini Uingereza.

    Bwana Donald aliporudi nchini Rwanda mwaka mmoja uliofuata, akakuta sehemu ile aliyoigundua, tayari watu walianza kuchimba madini tena huku kukiwa na kampuni zilizotoka nchini China ambazo zilikuwa ni za mahasimu wao wakubwa.

    Ilimchukiza, akarudi nchini Uingereza huku akiwa na hasira kubwa. Alipofika huko, akatoa taarifa na kitu walichokifanya Waingereza ni kuanza fitina, hawakutaka kumuona Mchina akikaa hapo, walijua kwamba wangenufaika sana.

    Fitina zao za kuzungumza na viongozi wa serikali ya rwanda zikafanikiwa na hivyo Mchina kufukuzwa ikiwa ni miezi sita tangu waanze kazi katika migodi hiyo. Kilichotokea baada ya hapo ni mafarakano, na baadaye, waasi wa serikali ya Rwanda, wakachukua migodi hiyo.

    Wakati watu wakiendelea na uchimbaji migodi huku majeshi ya serikali yakiwa yamepigwa mikwara kukanyaga katika machimbo hayo, ndipo hali ya hatari ikaingia nchini Rwanda, milio ya risasi ikaanza kusikika kila kona hali iliyohatarisha amani na hivyo wachimbaji wengi kukimbia.

    Waasi hao ambao walikuwa na jukumu la kusimamia kila kitu mahali hapo, hawakukimbia, hawakuwa tayari kuiona migodi yao ikipotea, almasi zikichukuliwa kisa tu vita.

    Walichokifanya, hawakukimbia bali wakajificha sehemu ambapo waliona vizuri kule machimbo yao yalipokuwa. Huko, walikuwa na bunduki nzito, AK 47 na silaha nyingine kali.

    Baada ya kujificha huko, baada ya siku mbili, tena huku macho yao yakiwa makini kuimarisha ulinzi katika machimbo hayo, wakaona watu wanne wakivuka kuelekea upande wa pili.

    Waliwaangalia vizuri, walionekana waoga, wasiojiamini ambao walihitaji msaada mkubwa. Hilo hawakutaka kujali, walichokijua wao, kila mtu aliyeonekana mbele yao alikuwa adui yao, yaani mwananchi ambaye aliungana na serikali ambayo ilikuwa adui yao mkubwa.

    Walichokifanya, wakaandaa bunduki zao. Hawakuwa na mchezo, hawakumpenda mtu yeyote yule na ndiyo maana suala la kutoa roho ya mtu kwao lilifanyika kwa haraka pasipo kipingamizi chochote kile.

    “Wapigeni risasi...” ilisikika amri kutoka kwa kiongozi wao, hawakuwa na budi, walichokifanya, wakazikoki bunduki zao tayari kwa kuwafyatulia watu hao wanne akiwemo Michael.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ITAENDELEA



0 comments:

Post a Comment

Blog