Simulizi : Dunia Isiyo Na Huruma
Sehemu Ya Tatu (3)
Bado walikuwa kwenye Kijiji cha Bucumbi, walikuwa wakizunguka huku na kule, kila mtu waliyemuona, walimuua pasipo huruma yoyote ile. Hawakuwa watu wa kukubali, waliwachukia Watusi kwa sababu walidai kwamba watu hao walikuwa na maringo, walijiona kwamba wao ndiyo wao.
Hawakuwapenda, walitaka kuwaua Watusi wote pasipo kuangalia umri wala dini. Safari yao iliendelea, hawakuwa na mahali maalumu pa kwenda, walichokuwa wakifahamu ni kuzunguka kila kona wakiwatafuta Watusi ili wawaue.
Wakati wakiwa wametembea kwa takribani kilometa tano, tena porini na ndipo walipofanikiwa kufika katika sehemu iliyokuwa na Mto mkubwa wa Manyiru ambao uliunganisha mpaka nchini Uganda.
Walitakiwa kuvuka mahali hapo, walitakiwa kuelekea upande wa pili na kwenda upande mwingine ambapo huko wangejua ni ni cha kufanya. Huo haukuwa mto wa kawaida, pembeni, ulikuwa mkubwa na mrefu ambao hawakutakiwa kuvuka hivihivi, walitakiwa kutumia mitumbwi ambayo ilikuwa pembeni ya mto huo.
“Ni lazima tuvuke mto huu...” alisema mkuu wa msafara.
“Sawa...ila nasikia kuna mamba na umekuwa kwenye historia ya watu wengi kuliwa na mamba, hasa wavuvi,” alisema Jackson.
“Ndiyo! Ila ni lazima tuvuke...ili tuendelee kuua Watusi wengi, ni lazima tuvuke hapa,” alisema kiongozi huyo.
“Basi sawa...”
Walichokifanya ni kuandaa mitumbwi ile na kuanza kuvuka, lengo lao lilikuwa lile lile kuvuka kuelekea upande wa pili. Hakukuwa na mtu aliyetaka kubaki nyuma, mitumbwi miwili iliyokuwa mahali hapo ilitosha kabisa kuwapeleka ng’ambo.
Katika muda wote wa kuvuka mto huo, Didier alikuwa kimya, hakuwa mzungumzaji, alikuwa kimya huku muda mchache sana alikuwa akizungumza na Jackson.
Wengine, walikuwa tofauti na yeye, walikuwa wazungumzaji sana, walipiga stori na kupongezana kwa kazi kubwa lakini yeye, alikuwa kimya kabisa. Mawazo juu ya familia yake yalimsumbua, hakukuwa na kitu alichotamani kukiona kipindi hicho zaidi ya mama yake aliyekuwa marehemu na dada yake, Solange.
“Nimeikumbuka familia yangu...” Didier alimwambia Jackson.
“Kweli?”
“Ndiyo!”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Usijali! Kila mtu ameikumbuka familia yake...”
“Na nyie pia mna familia?”
“Ndiyo! Unadhani hatuna familia? Tunazo!’
“Sasa mbona sijawahi kusikia hata mkizizungumzia?”
“Ni kwa sababu zimepotea, hatujui zilipo, tunaamini Watusi wamewaua na ndiyo maana usiku na mchana tunazunguka huku na kule kuwatafuta Watusi wote tuwaue...” alisema Jackson.
“Na mna mpango wa kurudi Kigali?”
“Kufanya nini? Bado tupo kwenye mapambano mazito, ni lazima tupambane...” alijibu Jackson.
Wote walikuwa kimya, ni sauti za ndege tu ndizo zilizokuwa zikisikika. Wakati wakiendelea kuuvuka mto ule, wakaonekana kushikwa na machale, wakahisi kwamba mahali hapo hawakuwa peke yao bali kulikuwa na watu wengine wakiwafuatilia.
“Kuna kitu...” alisema kiongozi wao.
“Hata mimi ninahisi...kwa nini ndege wanakimbia porini?” aliuliza jamaa mwingine.
“Hebu inameni....” alisema kiongozi wao na kweli wakafanya kama walivyoambiwa huku bunduki zao zikiwa tayari kabisa.
Wakati wakiwa makini kabisa kuangalia kule walipokuwa wakienda, ghafla milio ya risasi ikaanza kusikika kutoka kule kwenye miti ambapo ndege kadhaa walikuwa wakikimbia.
Hilo ndilo walilolitegemea kwamba humo porini kulikuwa na watu, hasa maadui, hivyo nao wakaanza kurusha risasi. Mto wa Manyiru ukabadilika na kuwa uwanja wa vita, risasi zikazidi kurushwa mahali hapo.
Mitumbwi ile ikashambuliwa, risasi kadhaa zikapigwa, watu wawili, kutoka katika kundi lao wakapigwa risasi na kufa papo hapo. Walikuwa kwenye wakati mgumu, walikuwa wakipambana na watu kutoka kule porini, hawakuwaona kabisa, walijipigia risasi kwa kubashiri tu mahali walipokuwa.
“Tunazidiwa...” alisema kiongozi wao.
“Tufanye nini?” aliuliza Jackson, walikuwa wamebaki watatu, kiongozi wao, Jackson na Didier.
“Tujitoseni mtoni...”
“Ila kuna mamba...”
“Bora kupambana na hao, ila si risasi...” alisema kiongozi huyo, hapohapo akajitosa baharini.
Didier na Jackson, nao hawakutaka kusubiri, wakajitosa huku risasi zikiendelea kurushwa. Hawakutaka kuibuka, wakaanza kupiga mbizi za chini kwa chini pasipo kujali kama humo kulikuwa na mamba au la! Kwao, kupambana na mambo ilikuwa ni afadhali kuliko risasi za moto.
****
“Paa..paa...paa...” milio ya risasi ikaanza kusikika kutoka katika mashimo ya machimbo yale ya almasi. Japokuwa wapigaji walikuwa watatu lakini kitu cha ajabu kabisa hakukuwa na risasi yoyote iliyopenya katika mwili wa mtu yeyote yule.
Kwa kasi kubwa, Michael akalala chini huku mikono yake ikiwa kichwani, akaanza kutambaa mithili ya nyoka. Wale wengine ambao alikuwa akivuka nao mahali pale, walikuwa wakikimbia kurudi porini, hilo ndilo lilikuwa kosa kubwa walilolifanya, wakashtukia wakipigwa risasi hata kabla hawajafika huko porini.
Watu wengine waliobaki kule porini, hakukuwa na mtu aliyebaki, wote wakaanza kukimbia kurudi nyuma, kile walichokikimbia, ndicho walichokutana nacho kule walipokuwa wakielekea.
Msichana Solange hakutaka kurudi, hakutaka kwenda peke yake, ilikuwa ni lazima amsubiri Michael kwani mwanaume huyo alionekana kuwa msaada mkubwa kwake kutokana na kumpoteza kaka yake, Didier na mama yake ambaye aliuawa katika mapigano hayo.
“Michael....Michael...” aliita Solange kwa sauti kubwa huku akilia.
Michael hakusimama, aliendelea kutambaa tena kwa kasi kubwa kurudi kule porini. Alifanikiwa kwani ingawa wale watu waliojificha waliendelea kumimina risasi lakini hawakuweza kumuona Michael ambaye alitambaa mpaka alipofika porini.
“Tukimbie...” alisema Michael, alikuwa akimwambia Solange.
Hawakutaka kusubiri mahali hapo, hakukuwa na amani tena, hali ilibadilika, hivyo wakaanza kukimbia huku mwanaume huyo akimshika mkono Solange. Walikimbia hovyo, japokuwa walijikwaa na kuumia lakini hawakutaka kusimama, safari yao ilikuwa mbele tu.
Walibaki wawili, kundi lote la watu mia mbili lilipotea machoni mwao. Hawakujua ni mahali gani walitakiwa kwenda, hali ilitisha sana na hata walipokuwa wakikimbilia, hawakujua kama ilikuwa ni Magharibi, Mashariki, Kaskazini au Kusini.
Walikimbia kwa takibani dakika thelathini, wakafika katika kijiji ambacho hawakukijua, wakaingia humo na kuanza kutembea kwa mwendo wa tahadhali kubwa. Kama ilivyokuwa katika vijiji vingine, napo ndani ya kijiji hicho maiti za watu zilikuwa nyingi, zilitoa harufu mbaya kwani tayari zilianza kuoza.
Ndege wa angani na mbwa walikuwa wakizila maiti hizo. Ziliharibika vibaya na kila wakati Solange alipokuwa akiziona maiti hizo, alikuwa akilia, moyo wake ulimuuma mno, hakuamini kama kuna siku angeweza kuona maiti kwa wingi kiasi hicho, mambo kama hayo alikuwa akiyaona kwenye televisheni tu.
“Nyamaza Solange, bado tuna safari ndefu, hatujui hapa ni wapi, hatujui tunapoelekea, tusonge mbele tu, hakuna amani tena,” alisema Michael huku wakizidi kusonga mbele.
Sehemu walipokuwepo ilikuwa ni Mbogo, kijiji kilichokuwa kilometa sabini kutoka katika Jiji la Kigali. Walikuwa wakielekea upande wa Kaskazini, sehemu ilipokuwa nchi ya Uganda ila wao hawakujua mahali walipokuwa wakienda.
Walizidi kwenda mbele mpaka walipofika sehemu iliyokuwa na barabara ya vumbi. Wakabaki wakiwa wamesimama pembeni mwa barabara hiyo, walikuwa wakijiuliza kama ilikuwa sahihi kuvuka na kuelekea upande mwingine au watembee barabara kwa barabara.
“Ni bora tutembee barabara kwa barabara,” alisema Solange.
“Kwa nini?”
“Tunaweza kupata hata msaada wa gari. Hatujui huku tunapoelekea ni wapi, kama tutatumia barabara, itakuwa rahisi kwetu,” alisema Solange.
“Hapana!”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hapana! Kwa nini?”
“Tuvuke barabara na tuingie porini,” alisema Michael.
“Kwa nini? Hutaki msaada?”
“Ninahitaji! Ila nini kitatokea kama tutakutana na Watusi, hauoni kama tunaweza kuuawa?” alihoji Michael.
“Michael, nimechoka, ninahitaji msaada,” alisema Solange hukuu akionekana kuchoka kweli.
“Najua, msaada tutapata ila si barabarani. Tuondoke, tukifuata barabara tutauawa, Rwanda si sehemu salama kwa sasa,” alisema Michael.
Huo ndiyo ulikuwa ukweli, kila sehemu mapigano yalikuwa yametawala, hakukuwa na sehemu iliyokuwa na amani kwa kipindi hicho. Kila kona, watu walikuwa wakisubiri kwa mapanga, bunduki ili watakapowaona watu ambao walikuwa tofauti na kabila lao basi wawaue kwa kuwapiga kwa mapanga.
Wazo alilolitoa Michael ndilo lililofanyika, walichokifanya ni kuvuka barabara na kuendelea mbele. Hawakutakiwa kupita sehemu yoyote ile zaidi ya porini tu.
Walikwenda kwa miguu mpaka giza lilipoanza kuingia. Hawakutaka kuendelea zaidi, kila mmoja alichoka na njaa ziliwauma mno. Walichokifanya ni kupumzika katika sehemu iliyokuwa na nyasi nyingi.
“Michael...” aliita Solange.
“Naam...”
“Nasikia njaa...nahisi nitakufa kwa njaa,” alisema Solange.
“Huwezi kufa...kama utakufa, labda kwa kifo kingine ila si nja,” alisema mwanaume huyo.
Hiko ndicho kilikuwa kipindi cha kuonyesha uanaume wake, hakutaka kubaki mahali hapo, akamwambia Solange kwamba anaelekea sehemu fulani kwenda kutafuta chakula.
Alichokifikiria ni kupata matunda na si chakula kama chakula, alipoondoka, akazunguka kila kona, alitembea huku na kule, kwa bahati sana kwake akakutana na mti wa mpera, akaufuata na kuanza kuuparamia na kuchuma matunda hayo.
Alipomaliza, hakutaka kuubaki mahali hapo, harakaharaka akaanza kurudi. Giza lilikuwa kubwa, lakini akafanikiwa kufika pale alipomuacha Solange. Kitu ambacho kilimshangaza kabisa, alipofika mahali hapo, msichana huyo hakuwepo.
Alichanganyikiwa, hakujua alikimbilia wapi, hakujua kama kulikuwa na watu walikuja na kumchukua au la. Kuchanganyikiwa huko kukamfanya kuanza kuita, aliita na kuita, tena kwa sauti kubwa, kitu kilichomshangaza na kumtia wasiwasi, msichana Solange hakuitikia na wala hakuhisi kama kulikuwa na dalili za msichana huyo sehemu fulani.
Moyo wake ukakata tamaa na kuhisi kwamba watu walimuona na hivyo kumteka na kuondoka naye kwenda kumbaka. Moyo wake ulimuuma mno.
Maji ya mto ule hayakuwa masafi, yalikuwa machafu, tena kulikuwa na tope jingi lakini hawakutaka kujali, hali ilikuwa ngumu, hakukuwa na mtu aliyeogopa mamba katika kipindi kibaya kama hicho, kama kufa, walikuwa tayari kuuawa na mamba lakinii si kuona wakipigwa risasi na wauaji wale.
Wakaanza kupiga mbizi za chini kwa chini. Walikuwa wakisonga mbele huku risasi zikiendelea kumiminwa bila mpangilio. Kutokana na maji ya mto ule kuwa machafu, hawakujua watu hao walikuwa sehemu gani, walichokifanya ni kupiga risasi mfululizo tu.
Wote watatu walisonga mbele, chini kwa chini pasipo kuibuka hata unywele. Walisonga mbele mpaka kama umbali wa nusu kilometa, wakaibuka huku wakiwa wamechoka mno.
Hakukuwa na mtu yeyote aliyewaona mahali hapo walipoibukia, wakabaki wakiangaliana huku wakipongezana kwa kazi kubwa waliyofanya ya kuogelea kutoka kule walipokuwa.
Hakukuwa na mtu mwenye bunduki, wote walikuwa mikono mitupu. Wakati wapo pembeni ya mto walipokuwa wamelala kwa kujipumzisha, ghafla, katika tendo la haraka mno, kiongozi wao wa msafara akajikuta akiumwa mguu, kuinuka kuangalia kilikuwa kitu gani, alikuwa mamba aliyetoka mtoni, akamng’ata mguu na kuanza kumvuta mtoni.
Meno ya mamba yule yalimshilia vilivyo, Didier na Jackson walitamani kumsaidia lakini kutokana na ngu ya mamba hasa awapo majini, wakashindwa kabisa kufanya hivyo.
Kiongozi yule akapelekwa katika maji mengi, huko, kulikuwa na mamba wengine ambao wote wakamvamia na kuanza kumtafuta. Picha waliyokuwa wakiiona, iliwaogopesha mno, sehemu ambayo kiongozi huyo alipokuwa aking’atwang’atwa, maji yalibadilika, damu zikatapakaa kuonyesha kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wake.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Tufanye nini?” aliuliza Didier huku akionekana kuwa na hamu ya kutaka kumsaidia.
“Hatuwezi kufanya hivyo! Hatuna bunduki yoyote ile,” alijibu Jackson.
“Kwa hiyo?”
“Tuondoke!”
Hawakuwa na jinsi, ilikuwa ni lazima kuondoka mahali hapo, mikononi hawakuwa na kitu, kumsaidia kiongozi wao ilikuwa ngumu kwani hawakuwa hata na bunduki mikononi mwao, na hata kama wangekuwa nazo, zingefanya kazi kutokana na kulowanishwa na maji.
Safari ikaendelea, hawakujua ni mahali gani walipokuwa wakielekea, hawakujua ilikuwa upande gani, wao walichokijua ni kusonga mbele tu.
Hapo walipokuwa ilikuwa ni Rutobwe na walipokuwa wakielekea ilikuwa ni Kibilira, Magharibi mwa nchi ya Rwanda upande wa nchi ya Kongo, kilometa mia moja kutoka katika Jiji la Kigali.
Walitembea na kutembea kwa tahadhali kubwa, mioyoni mwao walikuwa wakiomba Mungu wasikutane na aduio yeyote yule kwani pasipo hivyo walijua kwamba wangeweza kuuawa.
Walitembea porini mpaka walipofika katika barabara ya vumbi ambapo wakakutana hapo wakakutana na kibao kilichoandikwa Kibilira 80km. Hapo ndipo wakapata picha kwamba upande walipokuwa wakielekea ilikuwa ni nchini Kongo.
Walikuwa na wasiwasi mno kwani Kongo na Rwanda kwa kipindi hicho hali ilikuwa vilevile tu, zilifanana kutokana na mapigano yaliyokuwa yakiendelea kila siku kwa serikali na kundi la waasi la M23.
“Tuchague, twende Kongo au tubaki hapahapa Rwanda?” aliuliza Jackson huku akionekana kuwa na hofu kubwa.
“Vyovyote vile, kotekote ni kufa tu, ingekuwa nafuu kama tungekimbilia nchini Tanzania, vinginevyo, hizi nchi nyingine ni kufa tu,” alisema Didier.
“Kwa hiyo tuishie hapa na tuelekee Tanzania?”
“Haina jinsi, kama itawezekana, twende huko...”
“Ila ni lazima tupitie Kigali!”
“Hapana! Tupite pori kwa pori, tutafanikiwa tu. Kwa ufahamu wangu, hii Kibilira ipo upande wa Magharibi, kwa maana hiyo turudi upande wa Mashariki ilipo Tanzania, ni mbali mno lakini hatuna jinsi, kama tutakufa njiani, basi Mungu amepanga na kama tutafika salama, basi tumshukuru yeye,” alisema Didier.
Huo ndiyo uamuzi walioufikia, ilikuwa ni lazima kuondoka mahali hapo na kurudi kule walipotoka, ila kwa njia nyingine na kuelekea nchini Tanzania, hawakutaka kusubiri, wakaanza kuelekea huko.
Kama kawaida yao hawakutaka kupita barabarani, walipita porini, walitembea mno mpaka ilipofika usiku ambapo wakalala juu ya miti, asubuhi ilipofika, wakaamka na kuanza kuondoka kuendelea na safari yao.
Njaa iliwauma mno lakini hawakuwa radhi kusimama sehemu yoyote ile, walikuwa wakisonga mbele na kila hatua waliyokuwa wakipiga, pua zao zilianza kusikia harufu ya damu.
Iliwabughudhi pua zao, hawakusimama, waliendelea mbele na baada ya kufika umbali fulani, wakahisi harufu ile ya damu ikiongezeka zaidi, wakajua kwamba hapo walipokuwa kulikuwa na dalili za kuwa na maiti sehemu.
Walipotembea kama hatua mia mbili mbele, macho yao yakatua katika shimo moja kubwa ambalo ndani yake kulikuwa na maiti zaidi ya mia tatu zikiwa zimetupwa humo ndani.
“Mungu wangu!” alijikuta akisema Didier, alishindwa kuvumilia, hapohapo machozi yakanza kumtoka.
Walichokuwa wakikiangalia hakikuwa ndoto, kilikuwa kitu halisi kilichokuwa kikiendelea katika maisha yao. Kila kona porini humo, maiti zilitapakaa, hali ilionyesha kwamba nchi hiyo ilichafuka kwa kiasi kikubwa na mbaya zaidi watu waliokuwa wakiuana, walikuwa ndugu, waliozaliwa katika hospitali moja, ila leo hii, kila mmoja alikuwa akimuwinda mwenzake.
Hawakutaka kubaki mahali hapo, kama kulia, walilia sana, waliendelea mbele, baada ya umbali kama nusu kilometa hivi, wakafanikiwa kuingia katika kijiji kimoja, kilikuwa ni Gigarama, hapo, kulikuwa na ndogo ya watu ambao walionekana kutoka mafichoni.
Kila mtu aliyejitokeza, alikuwa akimuita ndugu yake, waliwatafuta ndugu zao, hawakuwaona hivyo kujua kwamba tayari waliouawa na watu waliokuwa wakiendeleza mapigano kila kona nchini Rwanda.
Hawakutaka kuendelea na safari, kitu cha kwanza kilikuwa ni kutafuta chakula kisha kuendelea na safari yao ya kuelekea nchini Tanzania. Hawakuwa na uhakika kama hapo walipokuwa palikuwa ni sehemu salama, walikuwa na hofu mno, walikaa kwa tahadhali.
Baada ya kujitambulisha, wakaungana na wanakijiji hao ambao waliwapa chakula na kuanza kula. Walipanga kulala mahali hapo ila iliipofika saa nane mchana, ghafla wakaanza kuona magari kama kumi kwa mbali yakija katika kile kijiji walichokuwa.
Katika magari hayo, walionekana vijana waliokuwa na bunduki na mapanga, walikuwa wakija kwa kasi katika kijiji kile. Wanakijiji walipoyaona magari hayo yakija kwa kasi, hawakutaka kubaki, wakaanza kukimbia, vijana hao wakaanza kurusha risasi hovyo, wengine walipigwa na wengine ziliwakosa.
Didier na Jackson hawakutaka kubaki mahali hapo, nao wakaanza kukimbia kuelekea porini.
****
Michael alichanganyikiwa, hakujua msichana Solange mahali alipokuwa. Alimwambia kwamba alikwenda kutafuta chakula kwani alikuwa akihisi njaa, alipata mapera na aliporudi mahali hapo, msichana huyo hakuwepo.
Alijaribu kumuita, alitembea huku na kule akimtafuta msichana huyo tena kwa kumuita lakini hakuitikia. Kichwa chake kilijaa maswali, akaanza kujiuliza kama msichana huyo alikuwepo sehemu amejificha au kulikuwa na watu waliofika mahali hapo na kisha kumchukua.
“Hakuacha kuita, aliendelea kufanya hivyo tena huku akienda huku na kule lakini majibu yalikuwa yaleyale, msichana huyo hakuweza kuitikia. Michael akakata tamaa, akahisi kwamba lazima kulikuwa na watu waliofika mahali hapo, wakamchukua msichana huyo na kuondoka naye.
Wakati akiwa amekata tamaa kabisa, akamsikia msichana huyo akimuita, kutoka ule upande alipomuacha, akaanza kwenda huko huku akikimbia.
“Nipo hapa Michael,” alisema msichana huyo, alikuwa juu ya mti amejificha, akaanza kuteremka.
“Mbona ulipanda mtini?” aliuliza Michael huku akimshangaa msichana huyo.
“Nilihisi kuna watu wanakuja, nikaogopa hivyo kupanda mtini na kujificha,” alisema Solange.
Kwa sababu mapera alikuwa nayo mkononi, akamgawia msichana huyo na kuanza kula. Hakikuwa chakula kizuri sana lakini hakuwa na jinsi, hapo porini hakukuwa na piza wa baga, hakukuwa na mayai wala maandazi, kile kilichopatikana mahali hapo ni hicho ambacho alianza kula.
Usiku wa siku hiyo hawakuendelea na safari, walibaki porini hao huku wakiwa wamekumbatiana usiku mzima. Solange alikuwa na mawazo mno, kila kitu kilichokuwa kikiendelea kwake kilionekana kama ndoto fulani ambapo baada ya mua angeshtuka na kujikuta akiwa kitandani.
Moyo wake ulimuuma mno, nchi yao ilikuwa ya amani na upendo lakini kwa kipindi hicho, nchi nzima ilitapakaa damu. Kitu kingine kilichomfanya kuwa na mawazo ni kaka yake, Didier ambaye mpaka kipindi hicho hakujua alikuwa wapi.
Mama yake alifariki dunia, alilifahamu hilo lakini hata kumpata kaka yake lingekuwa jambo jema, lingemfurahisha na kumfanya kuwa na furaha maisha yake yote.
“Sijui Didier yupo wapi,” alisema msichana Solange huku akiwa kifuani mwa Michael.
“Tutampata tu, wala usijali, cha msingi kwanza ni lazima twende Uganda,” alisema Michael.
“Kama naye ameuawa, sitokuwa na furaha maisha yangu yote...”
“Wala hajafa, tutakutana naye tu.”
Michael alikuwa na jukumu la kumfariji msichana huyo aliyeonekana kukata tamaa. Dakika ziliendelea kwenda mbele, baada ya saa moja, kila mmoja akapitiwa na usingizi mzito.
Sauti za ndege ndizo zilizowashtuka, wakayafumbua macho yao na kuangalia huku na kule, walikuwa porini. Hawakutaka kuendelea kubaki mahali hapo, ilikuwa ni lazima kukimbia, kusonga mbele na kwenda Nyamugali.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Bila shaka huku tunapoelekea ni Nyamugali,” alisema Miichael.
“Umejuaje?”
“Ndiyo hivyo! Ni safari ndefu sana, ushawahi kufika huko?” aliuliza Michael.
“Hapana.”
“Ni mji fulani mkubwa, ni kilometa mia moja kutoka hapo mpaka Kivuye, sehemu ambayo ipo karibu sana na Uganda,” alisema Michael.
“Kwa hiyo tunatembea?”
“Kama kawaida. Ni lazima tufike huko. Beba mapera, sidhani kama njiani tutakuta chakula kingine,” alisema Michael na safari kuanza tena.
Wote walichoka lakini hakukuwa na mtu aliyekuwa radhi kusimama, safari yao ilikuwa yenye kuchosha sana lakini hawakutaka kubaki mahali hapo. Ilikuwa ni lazima kuondoka, kuikimbia nchi yao yenyewe kutokana na mapigano yaliyokuwa yakiendelea nchini humo.
Kuanzia saa kumi na mbili asubuhi walianza kukimbia, hakukuwa na muda wa kusimama, walipochoka, walikuwa wakikimbia. Pori lilitisha sana, walifika katika sehemu zenye kuogopesha mno, lakini hawakujali, waliendelea kusonga mbele.
Ilipofika majira ya saa nane mchana, wakafika sehemu iliyokuwa na miti michache, kwa muonekano tu, ilionyesha kwamba sehemu hiyo ilikuwa ikifikiwa sana na watu, hivyo wakaanza kutembea kwa tahadhali kubwa.
Walipoifikia umbali fulani, wakaanza kusikia harufu kali ya kitu kilichooza. Wakaziba pua zao, hawakujua ni kitu gani lakini harufu ile ilivyozidi kuwa kali zaidi, wakajua kwamba inawezekana sehemu hiyo kulikuwa na mwili wa mtu aliyekuwa ameuawa kama ilivyokuwa huko walipotoka.
“Nafikiri kuna watu wameuawa...” alisema Michael.
“Hata mimi nahisi hivyohivyo...” alisema Solange na kuendelea kupiga hatua.
Wakafika sehemu iliyokuwa na inzi wengi, pembeni ya mti mmoja mkubwa, wakausogelea mti uule, walipoufikia na kuona nini kilikuwa chini ya mti huo, kelele kubwa, zilizojaa uoga zikaanza kusikika kutoka kwa msichana Solange, alichokiona, hakuamini.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment