Search This Blog

Sunday, July 10, 2022

DUNIA ISIYO NA HURUMA - 4

 





    Simulizi : Dunia Isiyo Na Huruma

    Sehemu Ya Nne (4)





    ILIPOISHIA...

    Wakafika sehemu iliyokuwa na inzi wengi, pembeni ya mti mmoja mkubwa, wakausogelea mti ule, walipoufikia na kuona nini kilikuwa chini ya mti huo, kelele kubwa, zilizojaa uoga zikaanza kusikika kutoka kwa msichana Solange, alichokiona, hakuamini.



    SONGA NAYO..



    Milio ya risasi ilikuwa ikisikika kila kona, hakukuwa na mtu aliyebaki mahali hapo, si Didier wala Jackson, kila mmoja alikuwa akitimua mbio kuyaokoa maisha yake.

    Risasi zile ziliwakosakosa, hawakutakiwa kusimama, kwa jinsi walivyokuwa wakiwaona baadhi ya wanakijiji waliyokuwa wakiuawa kwa risasi zile, waliogopa na kuona kwamba kama wasingefanya haraka basi nao wangeweza kuuawa.

    Rwanda iliendelea kujidhihirisha kwamba watu wake hawakuwa na huruma tena, hakukuwa na mtu aliyekumbuka kwamba watu waliokuwa wakiwaua walikuwa ndugu zao.

    Didier na Jackson waliendelea kusonga mbele, upande waliokuwa wakienda ni mwingine kabisa, hawakukumbuka kwamba walikuwa njiani kuelekea nchini Tanzania.

    “Ongeza kasi...” alisema Jackson.

    “Sawa! Kazana, wanakuja...” alisema Didier huku akikimbia kwa kasi ajabu.

    Walipotokea, ilikuwa ni sehemu kubwa iliyokuwa wazi, ilionyesha kwamba sehemu hiyo ilikuwa ni shamba kubwa la mpunga, hivyo wakaingia na kuendelea na safari yao.

    Hawakuwa peke yao, watu waliokuwa na uwezo wa kufika huko walikuwa wanaume wenye mbio tu, wanawake, watoto wote waliuawa na watu wale waliokuwa wamevamia kijiji kile.

    Walipita katika mashamba yale kwa kasi ya ajabu, waliendelea kukimbia kuusonga mbele, hakukuwa na mtu aliyesimama, kila mmoja alikimbia kuyaokoa maisha yake.

    Wakati wakiwa wamekimbia kwa dakika zaidi ya kumi katika mashamba yale ya mpunga ndipo walipoyamaliza na kuingia tena porini. Ilikuwa ni safari ya pori kwa pori, hakukuwa na mtu aliyekuwa radhi kusimama njiani.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Siku hiyo, mpaka inaingia jioni, wao walikuwa ni watu wa kukimbia pori kwa pori. Ilikuwa ni bora kukimbia hivyo, hawakutaka kufa, bado walitaka kuendelea kuishi. Ilipofika saa moja usiku, wakajikuta wakiwa wamefika katika ziwa kubwa ambalo hakujua ilikuwa sehemu gani.

    “Hili ni ziwa?” aliuliza Didier, aliyekuwa akimuuliza, yeye mwenyewe hakujua.

    “Sijui! Subiri!”

    Alichokifanya Jackson ni kuyafuata maji hayo na kuyaonja. Ni kweli yalikuwa ni maji ya ziwa. Wakajua kwamba walifika katika moja ya ziwa nchini humo ila tatizo ni kwamba hawakujua lilikuwa ziwa gani.

    Wakati wakiendelea kuwa hapo huku wakijifikiria ni kwa jinsi gani wangeweza kuvuka, ndipo wakagundua kwamba ndani ya ziwa lile kulikuwa na miili ya watu waliokuwa wameuawa.

    Hiyo iliwachosha na kuwaogopesha, wakaona kila kona nchini Rwanda kulikuwa na miili ya watu tu. Hakukuwa na amani tena, kama watu hao walikuwa wameuawa, ina maana kulikuwa na mambo mawili.

    Jambo la kwanza ni kwamba sehemu hiyo kulikuwa na maadui lakini jambo la pili ni kwamba watu hao walitaka kuvuka ziwa hilo, je walikuwa wakitumia chombo gani kuvukia?

    “Subiri kwanza....”

    Jackson akaanza kuangalia huku na kule, alichokuwa akikitafuta ni boti au mtumbwi ambao ungewawezesha kuvuka katika ziwa hilo. Huku wakiwa wanajifikiria ni kitu gani walitakiwa kufanya, ghafla wakaanza kusikia milio ya risasi kutoka huko porini.

    Hiyo iliwashtua, hawakutaka kubaki hapo ufukweni, ili kuyaokoa maisha yao ilikuwa ni lazima kuingia ndani ya ziwa hilo. Hawakutaka kuchelewa, kwa haraka sana wakaingia na kuanza kukimbia humohumo ziwani, walipofika maji ya kuzama, wakavuta pumzi ndefu na kuzama chini.

    Watu saba waliokuwa na bunduki wakafika ufukweni hapo, walionekana kuwa na hasira mno, waliangalia huku na kule kuona kama mahali hapo kulikuwa na mtu yeyote yule aliyekuwa hai, hakukuwepo na mtu yeyote zaidi ya ile miili.

    Wakashindwa kuamini kama zile zilikuwa maiti, walitaka kujiridhisha hivyo kuzisogelea na kuanza kuzipiga risasi kadhaa vichwani, walipoamini kwamba zile zilikuwa maiti, wakaangalia huku na kule, walipowakosa watu wengine, wakarudi porini.

    Walipohisi kwamba watu hao tayari waliondoka mahali hapo, wakaibuka na kuangalia huku na kule, pumzi zao zilifika katika hatua za mwisho kabisa, walikuwa hoi na hata uhemaji wao mahali hapo ulikuwa ni ule wa harakaharaka.

    “Tufanye nini?” aliuliza Didier.

    “Hakuna chochote cha kufanya zaidi ya kupiga mbizi tu...”

    “Ila hili ni ziwa gani?”

    “Sijui chochote kile, kwa sababu milima ile kule tunaiona, hakuna jinsi, tupige mbizi, pipote tutakapotokea, tutaendelea na safari,” alijibu Jackson.

    “Sawa...hakuna noma.”

    “Poa! Wewe si unajua kuogelea?”

    “Sana tu, hilo wala usihofu..”

    Hawakutaka kuchelewa, kilichofuata ni kuanza kupiga mbizi, hawakutaka kubaki hapo, waliamini kwamba inawezekana hilo lilikuwa ziwa ambalo lilipakana na nchi nyingine hivyo kulivuka na kwenda upande mwingine kwao ilikuwa ni ushindi mkubwa.

    Walizidi kusonga mbele, kuna kipindi walichoka, wakabaki wakielea juujuu, walipopumzika vya kutosha safari iliendelea. Haikuwa na kazi nyepesi hata kidogo lakini waliendelea kupiga mbizi kwa kupumzikapumzika na baada ya saa moja na nusu, kidogo wakaanza kukaribia nchi kavu kwani hata milima waliyokuwa wakiiona kwa mbali, ilionekana ikiwa karibu.

    Wakapata nguvu mpya na kuendelea kusonga mbele zaidi mpaka walipoanza kukanyaga mchanga wa ziwani. Hiyo ikawapa nguvu zaidi, wakaelekea mpaka nchi kavu.

    Kitu cha kwanza kabisa walichokifanya ni kulala kifudifudi, walichoka sana, walimshukuru Mungu kwa kuona kwamba walikuwa wameingia nchi nyingine kabisa.

    Walibaki hapo huku wakiwa wamelala tu, baada ya dakika thelathi, wakainuka na kusonga mbele kuifuata ile milima mikubwa iliyokuwa mbele yao. Wakati wakitoka katika ufukwe wa ziwa hilo, wakaona kibao kilichoandikwa kwa Kifaransa kilichosomeka ‘Lec Cyambwe’ ikiwa na maana ya Ziwa Cyambwe...wakashangaa, wakagundua kwamba bado walikuwa nchini Rwanda.

    Ila kilichowafariji, wakagundua kwamba ziwa hilo lilikuwa Mashariki mwa nchi ya Rwanda ambapo kama ungekwenda mbele zaidi, ungekutana na milima iliyokuwa ikitenganisha Rwanda na Tanzania. Hivyo wakaanza kuifuata milima ile ambao kama wangefanikiwa kuvuka, basi wangetokea mkoani Kagera.

    “Asante Mungu! Ni lazima tuivuke milima ile,” alisema Jackson huku akionekana kutokuamini. Safari ndefu ya kuisogelea milima ile ikaanza tena.

    ****

    Walipofika kulikuwa na mti mmoja mkubwa, chini ya ule mti kulikuwa na maiti ya mtu aliyekuwa na ulemavu wa ngozi (albino). Solange hakunyamaza, aliendelea kupiga kelele za uoga kwani kitu alichokiona mbele yake, kilimtisha mno.

    Ni kweli aliziona maiti nyingi huko nyuma lakini kwa hapo maiti ile iliyokuwa chini ya mti ule ilimtisha mno. Pembeni ya maiti ile kulikuwa na tunguli nyingi ambazo zilionyesha kwamba hata maiti ile ilipelekwa pale kwa ajili ya kutolewa kafara.

    Kilio chake kilisikika mno, alichokifanya Michael ni kumsogelea na kisha kumkumbatia huku akimwambia kwamba walitakiwa kuendelea na safari yao kwani huo haukuwa mwisho.

    “Tuondoke, bado safari ni ndefu,” alisema Michael.

    “Inauma sana...”

    “Najua, lakini tunapaswa kusonga mbele,” alisema Michael.

    Hilo ndilo lililobaki, walichokifanya ni kusonga mbele zaidi huku tayari ikiwa inaingia saa nne asubuhi. Hawakutaka kusimama, walidhamiria kufika mbele zaidi, walipita huko porini mpaka walipofika sehemu ambayo kidogo ilionekana kuwa na matumaini ya kuwepo watu kwani kulikuwa na mashamba makubwa, pia kulikuwa na matrekta.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Walichoifanya ni kusogea kule kulipokuwa matrekta na kuanza kuangalia ndani. Walihisi kwamba kungekuwa na watu lakini ukweli ni kwamba hakukuwa na mtu yeyote, yale matrekta yaliachwa baada ya wakulima kusikia milio ya risasi na tetesi kwamba huko walipokuwa kijijini kwao, watu waliuana.

    “Hakuna mtu!”

    “Kweli?”

    “Ndiyo!”

    Walichokifanya ni kuanza kutafuta chakula kwani waliamini kama mahali hapo kulikuwa na watu kipindi cha nyuma basi walijua ilikuwa ni lazima kuwe na chakula.

    Katika kuangaliangalia kwao, wakafanikiwa kuziona chupa za chai, hawakujua kulikuwa na nini lakini walipozifungua, wakaona uji wa ulezi ila ulikuwa umeharibika.

    “Tufanyeje?” aliuliza Solange.

    “Tunywe hivyohivyo, haina jinsi,” alisema Michael.

    Hawakuwa na jinsi, mahali hapo walipokuwa hawakuwa na chakula chochote kile, kile kilichoonekana mbele yao, kilionekana kufaa kabisa. Pasipo kujiuliza kitu chochote kile, wakaanza kunywa uji ule. Haukuwa na ladha nzuri lakini wakavumilia kwani ili kuyaokoa maisha yao, ilikuwa ni lazima kunywa uji ule.

    Walipomaliza, hawakutaka kuendelea kubaki mahali hapo, bado walikuwa na safari ndefu ya kuelekea nchini Uganda. Kama kawaida yao, wakaanza kukimbia kuelekea upande wa Kaskazini ambako ndipo kulipokuwa na nchi hiyo.

    Kuanzia muda huo, walikuwa wakikimbia huku wakati mwingine wakisimama na kupumzika. Walikuwa wamechoka sana lakini bado kukimbia ndiyo ilionekana kuwa salama kwao. Safari iliendelea, hakukuwa na muda wa kurudi nyuma tena, ilipofika saa kumi na moja jioni ndipo walipoingia katika kijiji kingine kiitwacho Kivuye, kilometa mia moja kabla ya kuingia nchini Uganda kwa kupitia njia za panya.

    Hiyo ilionekana kuwa nafuu kwao, hawakutaka kusubiri, walisonga mbele kwani kwenye kijiji hicho, kama kawaida hawakukuta mtu yeyote yule zaidi ya maiti zilizokuwa zimetapakaa kila sehemu.

    Walisonga mbele, ilipofika saa kumi na mbili na nusu wakati giza linaanza kuingia, wakaamua kupanda juu ya mti na kulala huko huku wakisubiri siku nyingine iingie na safari yao iendelee kama kawaida.





    Kila mmoja alibaki akiwa ameduwaa, hawakuamini kama ziwa lile walilolivuka lilikuwa Ziwa Cyambwe. Walibaki wakiangalia huku na kule, hawakuonekana kuamini kwani kutoka hapo mpaka jijini Kigali ilikuwa mbali sana.

    Hawakutaka kukaa sana hapo ufukweni, waliifahamu Rwanda na wakajua kwamba walikaribia kuingia nchini Tanzania, hivyo wakaendelea na safari yao.

    Njia haikuwepo, iliwalazimu kupita pori kwa pori. Muda wote walikuwa wakiomba Mungu wasikutane na wanyama wabaya kwani kama wangekutana nao, ingewapasa warudi nyuma kitu ambacho hawakutaka kuona kikitokea hata mara moja.

    Pori lilikuwa kubwa, waliendelea kuvuka mbele mpaka kufika sehemu moja ambayo walihisi kwamba kulikuwa na uwepo wa watu kwani kulikuwa na barabara iliyojaa majani lakini waliweza kuziona alama za matairi ya gari kwa mbali.

    “Hapa tusonge mbele, sijajua tunaelekea wapi, ila tusonge mbele,” alisema Jackson.

    Waliendelea mbele mpaka walipofika katika sehemu iliyokuwa na kibao kilichosomeka Kimisi Game Reserve yaani Hifadhi ya Wanyama ya Kimisi. Waliisikia hiyo hifadhi ya wanyama na hivyo kugundua kwamba tayari waliingia nchini Tanzania.

    Kitu cha kwanza kabisa walichokifanya ni kupiga magoti na kisha kumshukuru Mungu. Hawakuamini kama kweli walikuwa wameingia nchini Tanzania.

    Japokuwa hifadhi hiyo ilikuwa na wanyama wakali, hawakutaka kujali, kitendo chao cha kuingia nchini humo waliona kuwa katika mikono iliyo salama, sasa kazi ikawa ni kuvuka hifadhi hiyo na kusonga mbele.

    Wakajifunga mikanda na kuanza safari yao huku ikiwa tayari saa tisa alasiri. Walikuwa na njaa lakini hawakutaka kujali, muda huo, ilikuwa ni bora kuendelea na safari lakini si kusimama au kurudi nyuma.

    Njiani, wakaanza kupishana na wanyama wala majani kama nyumbu, pundamilia na wengineo. Hawakusimama, hawakurudi nyuma, waliendelea kusonga mbele.

    Walipofika umbali kama kilometa kumi kutoka pale walipokiona kibao kile, wakashtuka mara baada ya kusikia mlio wa gari nyuma yao. Kitu cha kwanza kabisa walichojisi ni moja ya magari ya vijana wale waliokuwa na bunduki ambao walikiteketeza kijiji kile.

    Wakabaki wakiwa na hofu kubwa ila kabla hawajaamua nini cha kufanya, wakasikia mlio mkubwa wa risasi, sauti za watu zikasikika zikiwataka watulie na wapige magoti chini.

    “Hawa ni majangili, hawa ni majangili, wamiminie risasi haraka,” alisikika mwanaume mmoja, huyo mwingine ambaye walijua kwamba alikuwa na bunduki, akaanza kuikoki bunduki yake tayari kwa kufanya kile alichoambiwa na mwenzake.

    ****

    Asubuhi waliamshwa na sauti za ndege zilizokuwa zikisikika katika pori zima. Wakashtuka kutoka usingizini na kuanza kuangalia huku na kule. Walikuwa juu ya miti kama walivyolala usiku uliopita.

    Kabla ya kuteremka kutoka mtini, Michael akaanza kuangalia huku na kule, hasa sehemu ambayo walitakiwa kwenda na kuingia nchini Uganda. Huko, hakukuonekana kuwa na makazi ya watu wowote wale, kulionekana kuwa na pori kila mahali hali iliyowafanya kukata tamaa kabisa.

    Hawakutaka kubaki mitini, walichokifanya ni kuteremka na kuendelea na safari yao. Kama kubaki nchini Rwanda, hawakutaka, ilikuwa ni bora kuendelea mbele, na kama kufa basi wafe porini na si kuuawa na watu amao kila siku waliwaambia kwamba ni ndugu zao.

    Safari ndiyo kwanza ilianza, ilikuwa ndefu, wote wawili walikuwa na njaa kali lakini hakukuwa na chakula, miti mingi iliyokuwa huko porini, hakukuwa na miti ya matunda hivyo kuwawia ngumu sana kupata chakula cha kula.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Walichokifanya ni kuendelea mbele, ilikuwa ni lazima waingie nchini Uganda ambapo kwao ilionekana kuwa sehemu salama. Safari ilikuwa ndefu sana, walitembea mpaka kuhisi kwamba muda wowote ule wangeanguka na kufa au miguu kuingia tumboni kwani ilichoka lakini bado waliendelea na safari kama kawaida.

    Milio ya risasi ilisikika kwa mbali nyuma yao, bado walijua kwamba mapigano yalikuwa yakiendelea na hiyo milio ndiyo iliyowaambia kwamba ni lazima waendelee na safari, kama wangekutana na wanyama wakali, basi waliwe na kufa lakini si kurudi nyuma kukutana na ndugu zao ambao hawakuwa na huruma hata kidogo.

    Wakati wakiwa wametumia masaa kumi njiani kwa siku hiyo ndipo kidogo wakakutana na barabara ya vumbi, walijua kwamba iwe isiwe ilikuwa ni lazima sehemu hiyo kuwe na magari yanayopita hivyo walichokifanya ni kuanza kutembea pembezoni mwa barabara ili hata kama kuna gari lingetokea, wapewe msaada na kusonga mbele.

    Barabara ilikuwa ndefu, walitembea mpaka kufika kipindi wakachoka, hakukuwa na msaada wowote ule, wakahisi miguu yao ikilegea, ikalegea na kulegea na hapohapo kuanguka chini, hawakujua nini kilichoendelea, macho yao yakajaa giza na hapohapo kupoteza fahamu.

    *****

    “We are Rwandans, We are Rwandans...” (Sisi ni Warwanda...Sisi ni Warwanda...) alisema Didier kitu kilichowafanya wale watu waliofika na bunduki mahali pale kumwambia mwenzao asubiri kwanza.

    “What are you doing in this reserve?” (Mnafanya nini katika hifadhi hii?) aliuliza mwanaume mmoja kwa sauti ya juu kabisa.

    Huo ulikuwa muda wa kujitetea, hakukuwa na kitu kingine walichokifanya zaidi ya kuwaambia kwamba nchi yao ilikuwa kwenye machafuko na hivyo walikuwa wakikimbia kuyaokoa maisha yao.

    Taarifa za machafuko ya nchini kwao hayakuwa siri, yalijulikana dunia nzima, watu wengi walihuzunika hasa baada ya kuona makabila mawili ya nchi moja yakiingia katika mapigano makubwa yaliyowamaliza watu wengi.

    Kwa kuwa nao walikuwa Warwanda, walinzi wa hifadhi hiyo wakawachukua na kuondoka nao. Walionekana kuchoka na kuwa na njaa, hivyo walichokifanya ni kuwapeleka katika kambi yao na kuwapa chakula na maji. Hiyo ilikuwa furaha kwao, hawakuamini kama walikuwa wamefanikiwa kuingia nchini Tanzania, nchi ambayo waliamini kulikuwa na amani ya kutosha kama nchi yao kabla ya kuingia katika machafuko.

    “Mpo katika mikono salama, na poleni kwa yote yaliyowakuta,” alisema mwanaume mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Omari.

    “Asante sana...”

    “Inabidi tuwachukue na kuwapeleka katika kambi ya wakimbizi. Kuna Warwanda wengi sana wameingia, litakuwa jambo la msingi sana kama mtakwenda huko na kukutana na ndugu zenu,” alisema Omari.

    “Hakuna tatizo, tutafurahi sana.”

    Kitu cha kwanza kilichoingia kichwani mwa Didier ni ndugu zake tu. Aliwakumbuka, alivyoambiwa hivyo alihisi kwamba huko angekutana na ndugu zake akiwemo mama yake na dada yake, Solange.

    Alikuwa na hamu ya kwenda huko. Alizunguka sana, alipitia misukosuko hivyo aliamini kwamba kitendo cha kwenda huko kambini kungekuwa na asilimia mia moja kukutana na ndugu zake hao.

    Siku hiyo walitakiwa kulala mahali hapo, asubuhi ilipofika, wakaondoka na Omari kuelekea katika kambi hiyo ambayo haikuwa mbali sana kutoka katika hifadhi hiyo ya wanyama.

    “Hapa ni wapi?” aliuliza Didier.

    “Tanzania...”

    “Mkoa gani?”

    “Kagera!”

    Safari ilikuwa ikiendelea kuelekea katika Kijiji cha Karanga ambapo huko kulikuwa na kambi ya wakimbizi. Njiani, Didier na Jackson walikuwa na kazi ya kusimulia kile kilichokuwa kimetokea nchini kwao, Rwanda na namna walivyoumia baada ya kuwapoteza watu wengi.

    Kila mtu aliyekuwa akiwasikiliza, aliumia, hawakuamini kama nchi ndogo kama Rwanda ingekuwa na mauaji ya kimbali namna hiyo. Walichukua saa nne ndipo walipoingia katika kijiji hicho ambapo moja kwa moja wakapelekwa katika kambi ya wakimbizi iliyokuwa hapo Karanga.

    Huko, kulikuwa na wakimbizi wengi, hawakuwa wale wa kutoka nchini Rwanda tu bali wengine walitoka burundi, Kongo na nchi nyingine ambazo zilikuwa katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.

    Kwa sababu naye alifika hapo huku akiwa na matumaini ya kuwaona ndugu zake, alichokifanya ni kuanza kuwatafuta kila kona huku akiuliza kwa watu wengine. Hakukuwa na mtu aliyewaona ndugu zake, waliwafahamu sana kwa kuwa walikuwa familia ya tajiri mkubwa nchini Rwanda ila kuwaona ndani ya kambi hiyo, hawakuwaona.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Au watakuwa wameuawa?” alijiuliza Didier na kuanza kulia, moyo wake ukaanza kusikia maumivu makubwa mno.

    Hapo ndipo alipoanza maisha upya, alikuwa mtoto wa tajiri mkubwa nchini Rwanda lakini kwa wakati huo, naye alikuwa ndani ya kambi ya wakimbizi huko Karanga, Kagera nchini Tanzania. Maisha hayakuwa kama nchini Rwanda japokuwa walipewa kila kitu, alikosa kuwa na uhuru, mawazo yalimsonga, hakuonekana kuwa na raha hata mara moja.

    Kila siku idadi ya wakimbizi ilikuwa ikiongezeka mahali hapo. Alikuwa makini kuwaangalia wote walioingia, alihisi kwamba angeweza kuwaona watu aliokuwa akiwatafuta.

    Baada ya wiki moja kukatika akiwa kambini hapo, ghafla akamuona mtu ambaye alihisi kumfahamu, alikuwa msichana, japokuwa alimuona kwa nyuma lakini alikuwa na uhakika kwamba alikuwa mwenyewe, huku akionekana kuwa na furaha, akaanza kumfuata msichana huyo.

    Moyoni mwake alihisi furaha kubwa, hakutegemea kumuona mtu huyo mahali hapo. Hatua zake aizozipiga zilikuwa za harakaharaka sana, hakuchukua sekunde nyingi, akamfikia, akamshika bega kwa nyuma huku akimuita jina lake, alipogeuka, kweli alikuwa yeye, hisia zake zilikamilika kwa kuona kwamba huyu ndiye yule aliyemhuhisi, hapohapo tabasamu pana likaanza kuonekana usoni mwake, msichana huyo akageuka na kumwangalia.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog