Simulizi : Dunia Isiyo Na Huruma
Sehemu Ya Tano (5)
Hatua zake alizozipiga zilikuwa za harakaharaka sana, hakuchukua sekunde nyingi, akamfikia, akamshika bega kwa nyuma huku akimuita jina lake, alipogeuka, kweli alikuwa yeye, hisia zake zilikamilika kwa kuona kwamba huyu ndiye yule aliyemhuhisi, hapohapo tabasamu pana likaanza kuonekana usoni mwake, msichana huyo akageuka na kumwangalia.
****
Alikuwa msichana Sophia, alipomuona, hakuamini kama angeweza kukutana na msichana huyo nchini Tanzania, kabla ya kuzungumza chochote kile, wakakumbatiana huku wakilia kama watoto.
Kumbukumbu zao zikaanza kurudi nyuma, porini walipokuwa wakikimbia kwa ajili ya mapigano yaliyokuwa yakiendelea. Kila mmoja alionekana kukata tamaa kuonana na mwenzake kwani mapigano yalikuwa makubwa na kipindi kile, Didier alisema anarudi kuwatafuta ndugu zake, upande ambao milio ya risasi ilikuwa imetawala.
“Uliwaona?” aliuliza Sophia.
“Sikuwaona, imeniuma sana, najua watakuwa wameuawa,” alijibu Didier huku akishindwa kabisa kuyazuia machozi yake kutiririka mashavuni mwake.
“Watakuwa hawajafa, Mungu atakuwa amewalinda tu,” alisema Sophia huku akijaribu kumfariji mwanaume huyo.
“Kwa nini sikuwaona? Kule niliporudi, milio ya risasi ilikuwa ikitawala kila kona, ukiniambia kwamba hawajafa, nitakuona unanidanganya tu,” alisema Didier huku akiendelea kulia kama kawaida.
Huo ukawa mwanzo wao, wakawa wanaishi pamoja huko kambini. Yeye, Sophia na Jackson wakawa watu waliokuwa na ukaribu siku zote, wakawa watu wa kuamka pamoja, kufanya kazi pamoja na mambo mengine kuendelea.
Kila siku walikuwa watu wa kufuatilia taarifa ya habari, televisheni ziliwekwa kila kona mahali hapo, bado mapigano yalikuwa yakiendelea, kila mmoja alitaka kuwa kiongozi wa nchi hiyo.
Hilo halikuwa suala la kuwatupia lawama Wazungu kwani wao wenyewe ndiyo walianza mapigano hayo huku Kabila la Watusi wakidai kwamba wao ndiyo walikuwa na elimu hivyo ngazi zote za juu zilitakiwa kuwa chini yao kitu ambacho siku zote Wahutu walikikataa.
Kilichokuwa kikiendelea nchini mwao, kiliwaliza kila siku, ndugu zao waliuawa kinyama, watu walitafutwa kwa mapanga mitaani, waliokuwa na bunduki ambao waliwaona watu wasiokuwa kabila lao waliwaua kinyama.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Mazikuti ndiye kiongozi wao,” alisema Didier, alimkumbuka mtoto wa aliyekuwa Waziri wa Afya nchini Rwnada.
“Kiongozi wa nini?” aliuliza Jackson.
“Watusi...ameua watu wengi sana,” alisema Didier.
“Na yeye yupo wapi?”
“Aliuawa, ila kama machafuko yanaendelea, kutakuwa na wengine tu,” alisema Didier huku akionekana kuwa na uhakika na alichokuwa akikiongea mahali hapo.
Siku zilikatika, baada ya mapigano kudumu kwa kipindi fulani, majeshi ya Umoja wa Mataifa, UN yakaingilia kati kwa kutuma wanajeshi kadhaa ambao walitapakaa nchini Rwanda na kumaliza mapigano hayo yaliyodumu kwa miezi kadhaa.
****
Walikuja kupata fahamu saa tatu baadaye, waliposhtuka, wakajikuta wakiwa hospitalini huku mikononi mwao kukiwa nadripu zilizokuwa zikipitisha maji taratibu katika mishipa yao.
Walijua kwamba hapo palikuwa ni hospitalini lakini walifikaje? Kumbukumu zao ziliwaambia kwamba mara ya mwisho kabisa walikuwa njiani, katika barabara ambapo walikuwa wakielekea sehemu wasipopajua, ila ghafla wakaanguka chini.
Ndani ya chumba kile walikuwa wawili tu, walibaki wakiangaliana huku wakionekana kushangaa. Mara mlango ukafunguliwa na nesi mmoja aliyevalia gauni refu jeupe kutokea, alipowaona wameamka tu, uso wake ukajawa na tabasamu pana.
“Tupo wapi?” lilikuwa swali la kwanza alilouliza Michael.
“Mpo Chondo, nchini Uganda,” alijibu nesi huyo.
“Tumefikaje hapa?”
“Kuna watu waliwaleta, nyie ni wakina nani?” alijibu nesi na kuuliza swali.
“Sisi ni Wanyarwanda, tumekuwa tukikimbia usiku kucha kuepuka machafuko yaliyotokea nchini mwetu,” alijibu msichana Solange.
“Poleni sana, tuligundua kwamba mmekuwa na njaa kwa kipindi kirefu hivyo kuwawekeeni dripu zenye glucose ambazo tunaamini zitaipa nguvu miili yenu,” alisema nesi huyo huku akizitoa dripu zile zilizokwisha maji na kuweka nyingine zilizokuwa na glucose.
Mioyoni mwao walimshukuru Mungu, hawakuamini kama walifanikiwa kufika nchini Uganda kama walivyotaka, walibaki wakimshukuru Mungu kwa kufika salama nchini humo.
Baada ya kukaa kwa saa nane, ndipo wakatolewa, wakachukuliwa na polisi kisha kupelekwa katika kambi ya wakimbizi ya Nyamigeni iliyokuwa hapohapo nchini Uganda.
Bado wakimbizi kutoka nchini rwanda waliendelea kuingia nchini humo. Machafuko hayo yaliyokuwa yakisikika dunia nzima yaliwahuzunisha watu kwani wale waliokuwa wakipigana, hawakuwa maadui, walikuwa ndugu wa damu wenye kiu ya kutaka uongozi nchini humo.
Baada ya kuingia katika kambi hiyo, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumtafuta kaka yake, alijua kwamba naye alikimbia kukimbia machafuko yale, alipokwenda, hakuwa akijua hivyo alihisi kwamba Didier alikuwa katika kambi hiyo.
Alizunguka mahali pote, aliwaangalia mpaka wakimbizi waliokuwa wakiingia kila siku lakini hakuweza kumuona kaka yake huyo. Moyo wake ulinyong’onyea, akahisi kwamba kaka yake huyo tayari aliuawa kule porini alipokuwa.
Kila siku akawa mtu wa kulia, alimkumbuka kaka yake huyo, Michael ndiye alikuwa mtu pekee aliyemfariji usiku na mchana na kumtia nguvu kwamba kaka yake huyo hakufa bali alikuwa sehemu na siku si nyingi wangeonana.
Japokuwa mwanaume huyo alimfariji lakini Solange hakuelewa, alichanganyikiwa, hata kula hakula tena, kila siku akawa mtu wa kumfikiria kaka yake, Didier tu.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Uwepo wa wanajeshi kutoka Umoja wa Mataifa ulisaidia kwa kiasi kikubwa mno, mapigano yaliyokuwa yakiendelea, yakaacha na watu kuanza kujipanga kwa ajili ya maisha mapya.
Mapigano hayo ambayo yalianza tarehe 7 mwezi wa nne mwaka 1994, yalidumu mpaka tarehe 18 mwezi wa saba mwaka huo huku zaidi ya watu milioni moja wakiuawa.
Japokuwa serikali ya Rwanda ilitangaza kwamba hakukuwa na mapigano tena, kila kitu kilichotokea kilitakiwa kusahaulika na wale walioikimbia nchi yao warudi lakini hakukuwa na mtu aliyetaka kurudi. Bado mioyo yao ilikuwa na hofu tele, huko walipokuwa, japokuwa walikuwa ukimbizini lakini kwao ilionekana kuwa bora zaidi ya kurudi katika nchi yao wenyewe.
Didier na Solange huko walipokuwa, hawakutaka kurudi tena, kila siku nchi zilizokuwa zimewahifadhi wakimbizi ziliwaambia wakimbizi hao warudi nchini mwao lakini hakuna aliyekubali, kwao, bado mioyo yao ilijua kuwa muda wowote ule mapigano hayo yangeanza tena.
Siku ziliendelea kwenda mbele huku watu hao wakitafuta kila siku. Didier hakujua kama mdogo wake, Solange alikuwa nchini Uganda katika kambi moja huko na pia Solange hakujua kama kaka yake huyo alikuwa nchini Tanzania.
Baada ya kukaa kwa miezi mitatu zaidi tena kila mmoja akiwa amekata tamaa ya kumuona ndugu yake ndipo serikali za nchi hizo ziliamua kuwarudisha wakimbizi hao nchini mwao.
Hawakutaka kurudi huko lakini hawakuwa na jinsi. Nchi ilichafuka mno, maiti zilienea kila kona katika kipindi cha mapigano lakini kwa wakati huo, maiti zote zilizikwa katika makaburi makubwa kwa pamoja.
“Kweli turudi Rwanda?” aliuliza Didier.
“Haina jinsi, unadhani tutakwenda wapi tena?”
“Mmh! Sawa! Haina jinsi, ila ningependa kubaki hapahapa Tanzania kwa maisha yangu yote,” alisema Didier.
“Hapa si nyumbani kumbuka. Kwa sababu serikali imetuhakikisha amani na usalama, hatuna jinsi, turudi tu,” alisema Jackson.
Hicho ndicho kilichotokea, wakimbizi wote wakaanza kurudishwa nchini Rwanda. Nchi haikuwa ya mapigano tena, ilikuwa nchi ya amani huku kila mmoja akitakiwa kusahau yote yaliyotokea huko nyuma.
Mara baada ya kufika nchini Rwanda, moja kwa moja Didier akarudi mpaka nyumbani kwao. Nyuma ilikuwa kwenye mazingira mabaya, alipoyaona, kumbukumbu zake zikarudi nyuma kabisa, siku ya kwanza mapigano yalipotokea na baba yake kufa ndani ya nyumba hiyo.
Kitanda kilekile alicholalia baba yake siku ya mwisho ya uhai wake, kilikuwa chumbani mulemule, machozi yalikuwa yakimbubujika tu. Japokuwa walikuwa na utajiri, ila furaha ilikuwa kila kitu katika maisha yake.
Alimzoea Jackson, alikuwa rafiki yake mkubwa, hakutaka kumuona akiondoka, akataka kuishi naye. Mbali na Jackson, pia kulikuwa na msichana Sophia. Huyu hakuwa na ndugu yeyote yule, wazazi wake waliuawa na hakuwa na pa kulala, hivyo Didier akaamua kuanza naye maisha ndani ya nyumba hiyo.
Kila siku akawa mtu wa kwenda kanisani, huko, aliwaombea ndugu zake, Mungu awape maisha ya raha ya milele Mbinguni pasipo kujua kwamba mdogo wake, Solange alikuwa hai.
*****CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Solange hakuwa na jinsi, mara baada ya serikali ya nchini Uganda kutangaza kwamba wakimbizi kutoka nchini Rwanda walitakiwa kurudi nchini mwao, mara moja wakachukua mizgo yake na kuanza kurudi huko.
Njiani, muda mwingi alikuwa akimuuliza Michael kama kukubali kurudi nchini humo ulikuwa uamuzi sahihi, kitu alichokisema Michael ni kwamba ilikuwa ni bora kufa nchini mwako kuliko kufa ugenini, hivyo walitakiwa kurudi huko.
Walipofika nchini Rwanda, hawakuwa na pa kwenda zaidi ya nyumbani kwa kina Solange. Walikuwa wawili tu kwani hata huyo Michael hakuwa na mtu yeyote yule, ndugu zake walikufa katika mapigano hayo.
Mara baada ya kurudi nyumbani, hali ilionekana kuwa tofauti kabisa, nyumba ilionekana kuwa kwenye hali ya usafi. Solange hakuhisi kama kulikuwa na mtu na aliona hali hiyo kutokuwa ya kawaida kwani kama walioondoka kwa kipindi kirefu, ilikuwaje nyumba hiyo iwe na mazingira masafi kiasi hicho?
Wakaanza kuusogelea mlango, walipoufikia, wakaufungua na kuingia ndani. Macho ya Solange hayakuamini alichokiona mbele yake, Didier alisimama mbele ya kabati ndogo akiangalia picha zao walizopiga kipindi cha nyuma. Hakuonekana kuwa na furaha hata mara moja, usimamaji wake tu ulionyesha ni jinsi gani alikuwa na majonzi.
“Didier...” aliita Solange.
Didier alipogeuka na kumuona mtu aliyemuita, hakuamini, akaacha kutazama picha zile na moja kwa moja kumsogelea Solange na kumkumbatia, wote wakadondoka chini, machozi yalikuwa yakiwatoka.
Walipotezana kwa kipindi chote, hawakuamini kama ingetokea siku hiyo wakaja kuonana tena. Walilia kwa pamoja, kila kitu kilichokuwa kikiendelea kilionekana kama wapo ndotoni ambapo baada ya kipindi fulani wangeamka na kujikuta wakiwa kitandani.
“Mama yupo wapi?” aliuliza Didier.
Swali hilo lilijibiwa kwan kilio kutoka kwa Solange, Didier hakutaka kutafuta nini kilitokea, kilio hicho kilimaanisha kwamba mama yao aliuawa msituni katika kipindi walichokuwa wakikiikimbia nchi hiyo.
Hicho ndicho kilichotokea. Baada ya kuwa na hali ya amani, watu waliohusika katika mapigano hayo wakakamatwa na kufikishwa mbele ya sheria.
Miongoni mwa watu hao waliokamatwa walikuwepo mchungaji wa Kanisa la Pentekoste, Jean Uwinkindi ambaye alihukumiwa kifungo cha maisha jela, Ladislas Ntangazwa, Claude Muhayimana, Innocent Musabyimana na wengine wengi ambapo wengine walihukumiwa kifo huku wengine wakihukumiwa vifungo vya maisha gerezani.
Huo ulikuwa mwanzo mpya, Rwanda ikabadilika, mapigano yakabaki kuwa kumbukumbu yao mpaka leo hii. Kwa Didier na Solange, wakaamua kuishi na marafiki zao, Michael, Jackson na msichana Sophia.
Utajiri mkubwa wa baba yao, wakautumia kufungua taasisi zilizojihusisha na kuwahudumia watoto yatima na wajane huku wakisaidia kuleta chakula kutoka nchini Tanzania kwa ajili ya Wanyarwanda waliokuwa katika matatizo mengi.
Hawakuangalia kuingiza fedha, waliangalia kutoa zaidi kwani waliamini kwamba kuwasaidia watu wengine ilikuwa bora zaidi ya kuingiza mamilioni kila siku.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya miaka miwili kupita, hapo ndipo walipoamua kuungua biashara kubwa, zilizowaingizia kiasi kikubwa cha fedha na kuufanya utajiri huo wa familia kuongezeka kila siku. Wakaanzisha kampuni kubwa zilizowatangaza sana Afrika Mashariki na Kati. Wakati yote hayo yakiendelea, ndugu zao wa hiari waliendelea kuwa pamoja nao wakisaidia katika kila hatua mpaka pale ambapo Didier alipoamua kumuoa Sophia na Solange kuolewa na Michael.
Kilichoendelea baada ya hapo, ni historia tu.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment