IMEANDIKWA NA : ISACK FLORIAN
*********************************************************************************
Simulizi : Ipo Siku Tu
Sehemu Ya Kwanza (1)
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kuishi maisha ya furaha, kudumisha amani, kujenga msingi bora wa familia na kushirikiana katika tabu na raha zote za hapa duniani mpaka kufa, hivi ni viapo ambavyo watu au wanandoa wengi huapa pale wanapounganishwa kuwa mwili mmoja katika kwenda kuyaanza maisha yao ya pamoja.Ni wanandoa wachache sana ambao huishi kwa kadri walivyoapa lakini wengi wao husahau viapo vyao na kuishi kinyume kabisa na Mungu atakavyo waishi.
Mr.Brian pamoja na mkewe, Mrs.Janet Brian, walikuwa ni wanandoa ambao walijitahidi kuishi vile atakavyo Mungu japokuwa changamoto na misukosuko ilikuwa mingi sana dhidi yao.Ni miaka kumi sasa imepita tangu waweze kuungana na kuwa pamoja, baraka kubwa ilikuwa katika maisha yao isipokuwa ni jambo moja tu lililokuwa linawatesa.Kutopata mtoto ndani ya familia yao, hii ni baraka ambayo bado Mungu alikuwa hajawajalia kuipata na ilizidi kuwatesa maana ndugu zao wengi walimshtumu Janet kuwa ni mwanamke asiye na uwezo wa kuzaa, yani ni Tasa.Ndugu, jamaa na watu wengi wa karibu wa Brian, walimshauri ni vyema akaamuacha Janet ijapokuwa tayari ameshafunga nae pingu za maisha, na atafute mwanamke mwingine ambaye ataweza kumzalia mtoto.Mawifi nao hawakua mbali katika hili, walimtazama Janet kama ni mwanamke asiyefaa kuwa pamoja na kaka yao na walizidi kumuhimiza ni vyema Brian akamuacha.
"Ni aibu gani hii kaka unataka kuileta katika familia yetu, Miaka kumi sasa imepita tangu uwe na huyu mgumba wako ambaye ameshindwa kabisa kukuzalia, hivi unafikiri mama na baba huko walipolala wanaridhia maisha haya unayoishi!"
"Hapana Jesca, ukiwa dada yangu wa pekee, hupaswi kabisa kuzungumza maneno kama hayo na tambua kila kitu huja kwa mpango wa Mungu."
"Mpango wa Mungu!, na je utakapokufa bila kuacha jina lako, mali zote hizi unataka kumuachia huyu Mgumba wako!?"
"Sasa huko unafika mbali mdogo wangu, sihitaji kumuona mke wangu akiteseka, mimi ndio mwenye maamuzi na hata kama hatutojaliwa kupata mtoto lakini siwezi kumuacha Janet mpaka kufa kwangu."
"Kama umeamua hivyo basi nami nakuahidi kaka, sitokanyaga tena hapa kwako mpaka utakapomuacha huyu mgumba wako." Alizungumza Jesca na kuondoka kwa hasira nyumbani kwa kaka yake.
Jesca na Brian walikuwa ni ndugu kabisa wa kuzaliwa tumbo moja, hivyo Brian alimuheshimu sana dada yake kwakuwa alikuwa ni wa pekee kwake.Maneno aliyozungumza Jesca yalikuwa mazito sana na yalimfanya Janet kudondosha machozi nyakati zote kila alipoyakumbuka na kuyafikiri na kupoteza kabisa amani ya moyo wake.Brian alijitahidi kumbembeleza mkewe na kumtaka asiwe na huzuni, muda utafika tu na wao siku moja watabarikiwa kupata mtoto.
"Nyamaza mke wangu na wala usiendelee kuyafikiri maneno haya aliyozungumza wifi yako, wewe ni mke wangu halali na sitoweza kuivunja ahadi yangu niliyoiweka kanisani." Alizungumza Brian na kumueleza mkewe.
"Hapana Brian!, Natambua unanipenda sana lakini utaishi katika maisha ya kugombana na ndugu zako mpaka lini!?, mimi naomba kama kuna uwezekano twende tukaivunje ndoa hii kanisani ili uishi kwa uhuru mume wangu."
"Unakumbuka kiapo tulichoapa mbele ya kanisa siku ile ya harusi yetu!?"
"Nakikumbukw vizuri Brian lakin...!!"
"Shiiiiii!!..Janet mke wangu!.siwezi kukivunja kiapo kile na pia tumeshapima kwa daktari na ametueleza hakuna mwenye tatizo lolote kati yetu, amini Mungu atatubariki tu nasi tutapata mtoto siku moja." Alizungumza Brian na kumkumbatia mkewe kwa lengo la kumfariji na kumtuliza.
Maneno mazuri ya Brian, yalimpa sana faraja Janet na akamuona ni mwanaume wa kipekee sana kwa kuweza kuvumilia kipindi chote cha miaka kumi bila ya kumzalia mtoto, tangu waanze kuishi pamoja baada ya kufunga ndoa yao.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Siku, miezi ilizidi kwenda, na baada ya miezi mitatu kupita, Brian pamoja na mkewe walirudi hospitali kama ilivyo kawaida kwa ajili ya kuangalia maendeleo yao.Siku hii daktari baada ya kuwapima, aligundua utofauti katika tumbo la Janet.
"Mr and Mrs.Brian"
"Ndio dokta."
"Vipimo vinaonesha tayari Janet hapo alipo ana kiumbe kipya tumboni mwake." Daktari aliwataari majibu ya vipimo vyao.
"What!, dokta Janet wangu ni mjamzito!!?" Brian alisimama na kuduwazwa na taarifa ile.
"Ndio Brian, mke wako kwa sasa ana ujauzito upatao wenye wiki mbili, hakika kweli Mungu amekisikia kilio chenu."
"Ooh!, 'Groly to God!..Groly to God!', nami naendwa kuitwa baba sasa..ahsante sana Mungu kwa kuturihidhishia ukuu wako kwetu" alizungumza Brian huku akionyesha furaha aliyokuwa nayo.
Machozi ya furaha yakawa yanamdondoka Brian, akamtazama mkewe ambaye naye alikuwa amekamata tumbo lake huku akishindwa kuamini kama ni kweli ameweza kushika ujauzito.
"Ee Mungu, hakika leo umenifanya kukuona wewe ni mfalme wa wafalme..mkuu wa kila jambo kwetu sisi wanadamu, ahsante baba yangu kwa kuniondolea aibu hii iliyokuwa inanitesa kwa muda mrefu mimi mjakazi wako." Alizungumza Janet huku machozi yakiwa yanamdondoka na akiwa ameyaelekeza macho yake kutazama juu.
Brian alimkumbatia mkewe kwa furaha na kuzidi kumshukuru sana daktari, maana yeye ndiye aliyekuwa mshauri wao mkuu katika jambo lile walilokuwa wanalihitaji kwa muda mrefu kutokea kwao.
"Tumshukuru sana Mungu katika hili Brian, na kwasasa mama atatakiwa kuanza kuhudhuria kliniki kwa kila tarehe atakayopangiwa kufika kwa ajili ya kuangalia maendeleo ya mtoto." Alisema daktari.
"Ahsante dokta, nakushukuru sana, tena sana maana bila ya wewe sidhani kama haya yote yangewezekana." Alizidi kumshukuru daktari, kisha wakaagana nae na kuanza safari ya kurejea nyumbani huku mioyoni mwao, yeye pamoja na mkewe, walikuwa wamejawa furaha isiyokuwa na kifani.
Wakiwa njiani, kwenye gari lao, nyimbo nzuri Brian aliendelea kuziweka na kumuimbia mkewe kama vile nyimbo inayojulikana kwa jina la 'MY LOVE' iliyoimbwa na kundi la Westlife, 'I WANT TO STAY WITH YOU MY WIFE' na 'SHOULD'V KISSED YOU' iliyoimbwa na msanii wa kimarekani, Chriss Brown.
Furaha iliwazidi mpaka wakajikuta wanajisahau kama wapo ndani ya gari, muda mwingi Brian alikuwa akiendesha gari huku akimkumbatia mkewe na kumbusu mara kwa mara kuonyesha jinsi gani alivyofurahi kwa mkewe kuweza kushika ujauzito.
Kilisikika kishindo kimoja tu cha nguvu, watu wote waliokuwa karibu na eneo lile, walitahaluki na kukimbilia eneo la tukio kwa ajili ya kwenda kuangalia usalama wa watu waliokuwemo ndani gari.
Lilikuwa ni roli kubwa lililosheheni mzigo wa mbao, liligonga na kuisambaratisha vibaya gari ndogo ambayo ndani yake alikuwemo Brian pamoja na mkewe.Damu ilikuwa imetapakaa kila mahali, hakuna sauti yoyote iliyokuwa inasikika maana gari ilikuwa imepondeka na kuharibika vibaya mno.
Wasamaria wema ambao walikuwepo karibu na mahali pale wakaweza kutoa taarifa sehemu husika na haikuchukua muda mrefu gari ya kubebea wagonjwa ikaweza kufika na kubeba miili ya watu waliokuwemo ndani ya gari.
Akiwa nyumbani kwake, Jesca pamoja na mumewe, siku hii Mume wake Jesca ambaye alikuwa anaitwa Nelson, alihitaji kumshirikisha jambo mke wake wakati wakiwa kwenye mazungumzo yao ya kawaida.
"Jesca mke wangu!" Aliita Nelson.
"Niambie mume."
"Japo sio sahihi sana mimi kuweza kuliingilia hili lakini leo nahitaji kukueleza kitu.Takribani miezi mitatu sasa imepita tangu ukate mawasiliano na kaka yako, hivi unafikiri haya ni maisha sahihi unayoishi na ukizingatia yule ni kaka yako wa pekee kabisa katika dunia hii!?"
"Nelson!, naomba uishie hapohapo na wala usingumze chochote kuhusiana na haya yanayoendelea kati yangu mimi na kaka yangu.Embu ngoja nikuulize swali moja, hivi kama mimi ninsingeweza kukuzalia huyu mtoto tuliyenaye kwa kipindi chote hichi tulichoishi pamoja, wewe ungeweza kuendelea kuishi nami mpaka sasa!?,"
"Kwanini isiwezekane!, wewe ni mke wangu halali tena na siwezi kukuacha kwasababu eti haujanizalia mtoto, na kumbuka kila kitu kinakuja kwa mapango wa Mungu hivyo kama hajanijalia kupata leo basi atanijalia kupata kesho." Alisema Nelson kwa utaratibu mzuri na kumueleza mkewe.
Baada ya kuzungumza maneno haya, Nelson akajikuta akipokea sonyo zito kutoka kwa mkewe.Jesca pamoja na Nelson wao katika ndoa yao walibahatika kupata mtoto mmoja wa kike ambaye walimpa jina la Beatrice na kwasasa mtoto yule alikuwa ana umri wa mwaka mmoja.
Wakiwa katika maongezi hayo, mara Jesca simu yake ya mkononi ikawa inaita na alipotazama namba ya mpigaji, ilikuwa ni namba ya kaka yake, Brian.Kwakuwa Jesca alikuwa ana hasira na kaka yake, akaamua kuiachi simu ile ikiita mpaka ilipokata yenyewe.Simu ikapigwa tena mara ya pili lakini Jesca hakuweza kuipokea simu ile.Ilipoita mara ya tatu, ndipo Nelson alipoamua kuichukua na kuipokea ili aweze kuzungumza na shemeji yake.Taarifa ambayo aliipokea Nelson, ilimfanya abaki mdomo wazi na kubaki ameduwaa huku akimtazama Jesca kwa mshangao sana, taratibu simu ikawa inamteleza mkononi na kudondoka mpaka chini maana nguvu zote zilimuisha.
Katika ajali ile iliyotokea, ilimpelekea Brian kupoteza maisha na Janet alikuwa katika hali mbaya sana na ilikuwa haijulikani kama anaweza kupona au kufa.Brian, yeye alifia palepale ajali ilipotokea hivyo mwili wake ulipofika hospitali, ulipelekwa moja kwa moja katika sehemu ya kuhifadhia maiti au kwa jina lingine ni sehemu inayoitwa Monchwari.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nelson alibaki kimya maana taarifa aliyoipata kutoka kwa mpigaji wa simu ile, ilikuwa inahusiana na tukio lililotokea kwa Brian pamoja mkewe.Alimtazama Jesca na kujiuliza ni vipi ataanza kumtaarifu.
"Mbona umekaa kimya na kiherehere chako cha kupokea simu zisizokuhusu.Nieleze sasa, amesemaje huyo mpuuzi mwenzako?" Alizungumza Jesca kwa dharau na kumueleza Nelson.
"Jesca mke wangu, naomba uwe unafikiri kwanza kabla kuzungumza maneno makari kama hayo, muda mwingine jitahidi kuwa na hekima." Alizungumza Nelson kwa upole sana.
"Embu nitokee kule, nisingekuwa na hekima wewe ungekuja kunioa mimi?." Alisema Jesca huku akiiupooza uji ulio kwenye bakuli kwa ajili ya kumlisha mtoto wake.
"Brian pamoja na mkewe wamepata ajali ya gari na tunavyozungumza kwa hivi sasa, Brian hayupo tena katika dunia hii." Nelson alimtaarifu Jesca
"Unasemaje!!?" Aliukiza Jesca kwa mshtuko mkubwa baada ya kupokea taarifa ile.
Machozi yakaanza kumtoka Jesca huku akilalamika na kuliita jina la kaka yake, Nelson akasogea karibu na mkewe na kuanza kumtuliza huku akimueleza maneno ya kumfariji.Wakati akiendelea kulia na kuomboleza kifo cha kaka yake mara Jesca akangusha kicheko cha nguvu mpaka kikamshangaza sana Nelson.
"Jesca! hivi unamatatizo gani wewe!, kipi sasa kinachokufanya ucheke!?" Aliongea Nelson kwa sauti ya ukari kidogo lakini ndio kwanza Jesca alizidisha kucheka.
"Japo ni huzuni kubwa kwangu kwa kumpoteza kaka yangu lakini kwa upande mwingine ni jambo jema maana mali zake zote zitakuwa chini yetu na yule mgumba, habari yake itakuwa imeisha sasa."
"Jesca!, Jesca!, Jesca mke wangu!!, kwanini unakuwa na fikra kama hizo!, yani badala uhuzunike kuhusiana na kifo cha shemeji lakini wewe unafurahia kuzichukua mali zake." Alizungumza Nelson, lakini Jesca hakujibu chochote kile zaidi aliendelea kucheka na kuinuka kwa ajili ya kuondoka pale sebuleni.
Taratibu kwa ajili ya maandalizi ya kumpelekea Brian katika makao yake ya milele ziliendelea pale nyumbani kwa marehemu huku watu wengi walionekana kuguswa sana na msiba ule maana Brian alikuwa mwenye kuishi vizuri na kila mtu.Siku inayofuata, ibada ya mazishi ya Brian iliazimishwa na mwili wake kupelekwa makaburini kwa ajili ya maziko.
Jesca, uso wake ulionekana kujawa na huzuni sana wakati wote, alibaki akilia kwa uchungu huku akilalamika kwanini kaka yake amemuacha peke yake.Kwa upande mwingine, pamoja na kulia kwakwe na huzuni aliyonayo lakini moyoni mwake alikuwa akifarijika sana maana kila alipotazama mali alizokuwa nazo kaka yake aliona sasa wakati wake umefika wa kuweza kuzimiliki yeye.
Upande wa Janet ambaye ni mke halali wa marehemu Brian, alikuwa katika hali mbaya sana na madaktri waliendelea kupambana kwa kadri wanavyoweza ili waweze kuokoa uhai wake ambao ulikuwa hatarini sana.Kupitia jitihada za madaktari, ilimchukua zaidi ya wiki mbili ndipo Janet alipoweza kufungua macho yake na kuweza kutazama nuru ya ulimwengu kwa mara nyingine tena.Matibabu yalizidi kuendelea juu yake, lakini kwa bahati mbaya ajali ile ilimpelekea Janet apoteze uwezo wa kuzungumza pamoja na miguu yake yote miwili kutokuwa na uwezo wa kufanya kazi tena, hivyo janet alikuwa ni mtu wa kitandani tu.Pamoja na yote kukumkuta hayo, madaktari walipofanya vipimo kwa ajili ya kuchunguza kama mtoto aliye tumboni atakuwa amepata athari yoyote ile, kwa bahati njema mtoto alikuwa salama na ukuaji wake uliendelea vizuri akiwa tumboni mwa mama yake.
Baada ya shughuli zote za msiba wa Brian kumalizika, mali zote zikabaki chini ya mikono mwa Jesca maana yeye ndiye mtu pekee aliyebaki kuweza kuzichukua mali zile za kaka yake na kuzisimamia kwakuwa Janet hakuwa na uwezo wa kuzungumza wala kutembea.Pia ilikuwa rahisi Jesca kuzipata mali zile maana aliahidi mbele ya kikao cha familia kuwa atamuhudumia wifi yake aliye hospitali mpaka atakapopata nafuu au kupona kabisa.
Baada ya kuhakikisha kila kitu kipo chini yake, Jesca hakusita kwenda kumuona wifi yake katika hospitali aliyolazwa na mara nyingi alipofika hospitalini, alizungumza maneno ya kujivuna na kumkashifu sana Janet.
"Maskini wifi yangu weeee!, kiko wapi sasa ulichokuwa unajivunia, jeuri na ngebe zako zote zimeisha sasa." Alizungumza Jesca na kumueleza Janet, baada ya kufika pale hospitali kwa ajili ya kumuona.Janet alibaki akimtazama kwa huzuni tu maana hakuwa na uwezo wa kuzungumza chochote kile.
"Yani jinsi ulivyo hautofautiani kabisa na shetani, hivi unafikiri mimi sitambui kuwa wewe ndiye uliyemuua kaka yangu ili urithi mali alizonazo!?, mchawi mkubwa wewe na kwa hili ulilolifanya, Mungu atakulaani katika maisha yako yote." Aliendelea kuzungumza Jesca na kumpelekea Janet adondoshe machozi kutokana na maneno makali aliyokuwa anaelezwa.
Janet alitamani azungumze kitu kwa ajili ya kumjibu wifi yake lakini sauti ilikuwa haitoki hivyo akaishia kucheza mdomo tu na kuzidi kulia kwa uchungu.
Baada ya kuonana na wifi yake, Jesca akatoka na kwenda kuzungumza na daktari ambaye alikuwa akijulikana kwa jina la Dk.Anthony.
"Karibu dada." Dk.Anthony alimkaribisha Jesca ofisini kwake.
"Asante dokta.Nimekuja kufahamu hali ya mgonjwa wangu, Je ana uwezekano wa kupona kweli!?"
"Mh!, hilo ni jambo gumu sana dada maana ajali ile imemuathiri sana Janet na imedhoofisha sehemu kubwa ya mwili wake na ukizingatia pale alipo ni mjamzito." Alizungumza Dk.Anthony na kumtaarifu Jesca.
"Dokta unasema!, Janet ni mjamzito!?" Aliuliza Jesca kwa mshangao mkubwa.
"Ndio dada, Tumshukuru sana Mungu maana pamoja na mwili wake kudhurika lakini mtoto alibaki akiwa salama na kutoweza kupata madhara yoyote yale."
"Una uhakika Dokta na hayo unayoyasema!?"
"Ni hakika nalo hilo dada na tutajitahidi kuweka uangalifu mkubwa kwake ili aweze kujifungua salama." Alisema Dk.Anthony na kuzidi kumueleza Jesca kuhusiana na ujauzito alionao Janet.
Taarifa ile haikuwa njema kwake kabisa Jesca na alihisi kama mtoto yule atazaliwa, basi itakuja kumuwia vigumu kwake kuweza kuendelea kuzimiliki mali za kaka yake.Hivyo Jesca, akahitaji kumuomba kitu Dk.Anthony.
"Hiyo ni taarifa njema ila kwa upande mwingine ni taarifa mbaya kwangu."
"Mh!, kwanini unasema hivyo dada!?"
"Samahani Dk.Anthony, nina ombi moja tu kwako na kama hutojali naomba nikueleze."
"Bila shaka dada, nieleze tu."CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Naomba iharibu hiyo mimba na ikiwezekana muue kabisa huyo mtoto aliye tumboni na pia kama utalikamilisha hili, nakuhakikishia nitakulipa pesa yoyote ile utakayohitaji." Alizungumza Jesca kwa ujasiri mkubwa na kumueleza Dk.Anthony.
Dk.Anthony alishtuka sana baada ya kusikia kauli ile kutoka kwa Jesca, alishindwa kuelewa kwanini anakuwa na roho ya kinyama kama ile wakati Janet ni wifi yake.
Dk.Anthony ndiye daktari ambaye alikuwa akiwasimamia na kuwashauri Janet pamoja Brian angali akiwa bado yupo hai, hivyo alitambua ni jinsi gani walivyokuwa wanataabika katika kutafuta mtoto.
"Nashindwa kuelewa kwanini unazungumza maneno kama hayo, embu nieleze dada, yote haya yanatokana na nini mpaka uzungumze kauli kama hiyo!?"
"Hakuna tatizo lolote lile dokta ila lengo langu ni kumsaidia wifi yangu katika maisha yake.Pale alipo hana kitu chochote katika mkono wake ambacho anaweza kukuitumia kumlea mtoto wake, hivyo ni bora ukamuangamiza mtoto mapema ili uweze kumsaidia."
"Kwanini iwe hivyo, ina maana marehemu mume wake hakuacha hazina yoyote ile ya kuweza kumsadia Janet katika kuyaendesha maisha yake!?"
"Janet alikuwa ni hawara tu na si mke halali kwa kaka yangu kwasababu hakukuwa na ndoa yoyote kati yao, hivyo mali za kaka yangu zote zinabaki kwetu sisi ndugu zake." Alizungumza Jesca kwa ujasiri mkubwa na kumueleza Dk.Anthony.
Dk.Anthony alishangazwa sana na yale aliyoyasikia pale, alimuona jinsi gani Jesca alivyokuwa na roho ya kinyama na kushindwa kabisa kuwa na ubinadamu hata kidogo kwa wifi yake.Pesa ambazo alikuwa ameahidiwa kulipwa baada ya kuikamilisha kazi ile, zilikuwa ni nyingi sana hivyo hii ikamfanya Dk.Anthony afikiri kidogo ni maamuzi yapi ayachukue katika lile.
Ilimchukua muda kidogo Dk.Anthony kuweza kulifikiri ombi lile la Jesca na baada ya kufikiri sana mwisho akaamua kufanya maamuzi ambayo aliyaona yapo sahihi upande wake.
"Sawa, nimekubali kuifanya kazi hii lakini kwa masharti." Alisema Dk.Anthony.
"Bila shaka, zungumza tu." Aliongea Jesca huku akiwa anatabasamu.
"Kwanza naomba uelewe shughuli hii tunayoenda kuifanya ni ngumu sana na maisha ya Janet yatakuwa yapo hatarini sana maana kwa kiasi fulani mimba yake imeshakuwa kubwa, hivyo naomba uwe tayari kwa lolote lile litakalotokea na ni muhimu jambo hili likawa siri kati yangu mimi na wewe tu."
"Asante sana Dokta na pia usiwe na shaka yoyote ile hata kama ikatokea Janet akapoteza maisha yake, cha muhimu ni lazima mtoto huyu afie hukohuko alipo.Nakutegemea sana Dk.Anthony na naamini hutoniangusha katika hili."
Yalikuwa ni maongezi kati ya Dk.Anthony pamoja na Jesca ambaye alijitahidi kwa kiasi kikubwa kuweza kumshawashi Dk.Anthony mpaka akaweza kukubali kuifanya kazi yake.Baada ya kumaliza maongezi yale, Jesca alitoka pale hospitali akiwa na furaha sana huku akiamini kupitia lile amemkomoa Janet kwa kila kitu.
Pamoja na kuafikiana na Jesca kuwa yupo tayari kuweza kuitenda kazi ile, moyoni mwake Dk.Anthony alikuwa na dhamira nyingine kabisa na hasa zaidi ya kumsaidia Janet aweze kujifungua salama.Dk.Anthony alidhamiria kumsaidia Janet katika jambo lile kwakuwa alikuwa akitambua changamoto nyingi ambazo Janet pamoja na marehemu mume wake walikuwa wanazipitia wakati wakiwa wanahangaika kutafuta mtoto hivyo ndio maana akaamua kuchukua uangalifu mkubwa kwa Janet na kuhakikisha huduma zote muhimu zinamfikia kwa wakati sahihi kwa lengo la kulinda ukuaji wa mtoto aliye tumboni.
Kwakuwa alihakikishiwa kuwa tayari kazi yake imekwisha kukamilika, Jesca hakuwa na shaka tena wala kupoteza muda wake kwenda kumuona Janet hospitali zaidi aliendelea kutanua mali zilizochumwa na marehemu kaka yake pamoja na wifi yake huku akiamini sasa ndio wakati wake wa kufanya kila alitakalo na hakuna mtu yoyote atakayekuwa kikwazo upande wake.
Siku na miezi ilizidi kukatika na hatimaye siku ya kujifungua kwa Janet ikawadia lakini cha kushangaza wakati wa kujifungua kwake, uchungu wake ulichukua muda mrefu sana mpaka ikawafanya madaktari waanze kuingiwa na wasiwasi kuhusiana na lile.Ilimchukua siku nzima Janet akiendelea kuugulia maumivu na uchungu aliokuwa anaupata, ndipo alipobahatika kujifungua mtoto mwenye jinsia ya kike.Kutokana uchungu wa kujifungua kwake kuchukua muda mrefu sana, ilimpelekea kupoteza damu nyingi pamoja na mwili wake kudhoofika sana licha ya kuwa alifanikiwa kujifungua salama.Yote kwa yote Dk.Anthony alimshukuru sana Mungu kwa Janet kuweza kujifungua salama zaidi akataka kuchukua uangalifu mkubwa kwa mtoto maana alitambua Janet hatokuwa na uwezo wa kumtunza na kumlea mtoto yule kutokana na hali aliyokuwa nayo hivyo alihitaji kutengeneza mazingira mazuri kwa ajili ya mtoto.Baada ya wiki mbili kupita tangu mtoto yule azaliwe na Janet akiwa amempatia mtoto wake jina la Angel kutokana na mazingira aliyompata, Dk.Anthony akamchukua mtoto yule na kumpeleka katika hospitali maalumu inayohusika katika kulea watoto wadogo ili akatunzwe katika mazingira mazuri na kwa usalama mkubwa.
Kadri siku zilivyozidi kwenda ndivyo Angel alivyoendelea kukua vizuri huku Dk.Anthony akijitahidi kutumia kiasi cha fedha ambacho alilipwa na Jesca baada ya kumdanganya kuwa amemkamilishia kazi yake kwa kupeleka mahitaji mbalimbali yaliyokuwa yanahitajika kwa ajili ya mtoto mpaka alipofikisha umri wa miaka sita ambapo Angel alihamishiwa katika kituo cha kulelea watoto yatima maana hospitali aliyokuwa analelewa hapo awali, ilikuwa inatunza na kulea watoto mpaka wanapofikisha miaka mitano tu.
Kipindi chote hicho Janet hakuweza kubahatika kumuona mtoto wake na kila alipojaribu kumuuliza Dk.Anthony ni wapi alipo mtoto wake, Dk.Anthony hakuwa tayari kumueleza zaidi alikuwa akimjibu kuwa Angel yupo salama na yupo sehemu sahihi hivyo asiwe na shaka yoyote ile.Dk.Anthony hakuhitaji Janet afahamu ni wapi alipo mtoto wake wala kumkutanisha nae kwa lengo la kumlinda Angel asije akapata tatizo lolote lile maana alihisi kama atagundulika yupo hai, maisha yake yatakuwa yapo hatarini sana.
Alipofikisha umri wa miaka saba, Angel alianzishwa darasa la kwanza katika shule moja isiyo ya kiserikali(Private school) ili akapate elimu itakayomsadia katika maisha yake ya baadae.Japokua umri wake ulikuwa ni mdogo lakini Angel alikuwa ni mtoto mwenye ufahamu mkubwa na aliweka jitihada zake katika kuitafuta elimu maana aliaminishwa ile ndio njia sahihi ya kupita kwa ajili ya kuitengeneza kesho yake itakavyokuwa.Utulivu mkubwa na hekima aliyojaliwa kuwa nayo, ilimpelekea Angel afanye vizuri katika masomo yake na tangu anaanza darasa la kwanza mpaka anafika darasa la nne, aliendelea kuwashangaza walimu wake maana hawakuwahi kushuhudia mtoto mwenye uwezo kama wake.Uwezo wake mzuri wa darasani, ulimfanya Angel ajizolee marafiki wengi pale shuleni japokuwa wengine walikuwa wema kwake na wengine hakuwa wema bali walitengeneza urafiki nae kwa ajili ya kukamilisha malengo yao binafsi.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ikiwa ni jioni moja na baada ya kumaliza ratiba ya masomo siku hii, Angel akiwa amejituliza nje ya shule kidogo huku akimsubiri Dk.Anthony afike mahali pale kumchukua na kumrudisha katika kitua anachoishi, mara anatokea mtu na kumsemesha.
"Hujambo binti mzuri?" Alizungumza yule mtu na kumuleza Angel.
"Sijambo mjomba, shikamoo." Alisema Angel na kumsalimu yule mtu ambaye ilikuwa mara yake ya kwanza kumuona katika mazingira yale ya shule yao.
"Marahaba mwanangu, mimi naitwa Anko Nea na wewe unaitwa nani?"
"Naitwa Malaika."
"Mh!, malaika!?, hapo umenidanganya mjomba si ndio enhee."
"Akuu! hata sijakudanganya ila hilo ndio jina langu." Alisema Angel na kumfanya yule mtu aliyejitambulisha kwa jina la Nea, atabasamu kidogo huku akiketi karibu na Angel maana alianza kunogewa na mazungumzo yale.
"Kwani wewe Anko Nea umesoma mpaka darasa la ngapi?"
"Mimi nimesoma mpaka chuo kikuu."
"Enheee!, haya niambie neno malaika kwa kiingereza linaitwaje?" Aliuliza Angel na kumfanya Nea aangue kicheko kikubwa maana hakuwahi kuuona mtoto mdogo mwenye uelewa mkubwa kama aliokuwa nao Angel.
Wakiwa wanaendelea kupiga stori mbalimbali huku Angel akiendelea kumsubiri Dk.Anthony, mara anafika Beatrice mahali pale.Beatrice alikuwa ni mwanafunzi mwenzake Angel ambaye wote walikuwa wanasoma darasa moja.Baada ya kufika pale, Beatrice akamsalimu baba yake ambaye alikuwa amefika pale shuleni kumchukua, kisha akazungumza neno ambalo lilimfanya Angel ahuzunike sana.
"Kwanini baba umekaa hapa na kuzungumza na maskini, mama yangu aliniambia nisije kuthubutu hata siku moja nikajenga ukaribu na maskini kama hawa." Yalikuwa ni maneno mazito kutoka kinywani mwa mtoto mdogo Beatrace.
Maneno haya yalimfanya Angel apate simanzi kubwa sana moyoni mwake, licha ya udogo alionao lakini akajikuta akiumia sana nafsini mwake mpaka kufikia kudondosha machozi.
Upande wa Nea yeye alibaki ameduwaa maana hakufikiri kama mtoto wake anaweza kuzungumza maneno makari kama yale.Pamoja na yote, Nea aliona jinsi gani sumu ya mkewe inavyoendelea kumtafuna mtoto wake taratibu hivyo akahitaji kufanya kitu ili aweze kuiondoa sumu ile mapema kwa Beatrice kabla haijaweza kumtawala kabisa.Akamchukua Beatrice na kumketisha karibu na alipoketi Angel ambaye muda huo alikuwa katika hali ya huzuni mno.
"Beatrice mwanangu."
"Ndio baba."
"Siku zote maneno tunayokueleza sisi wazazi wako ni ya kweli na tuna lengo la kukujenga ili uwe mtoto mzuri daima.Haijalishi uwe maskini au tajiri, lakini wote tunatakiwa tuishi kwa kupendana maana binadamu wote tuliopo hapa dunia ni sawa."
"Mh!, lakini mama mbona alinieleza kuwa sipaswi kabisa kukaa karibu na maskini kwakuwa tupo tofauti nao, sasa baba usawa wetu hapo unatokea wapi?"
"Swali zuri binti yangu, wewe na Angel wote mpo sawa kwasababu wote ni watoto wa Mungu na hakuna tajiri mkubwa hapa duniani kama utajiri alinao Mungu.Mungu humpenda na kumpa utajiri wake yule mtu anayependezwa nae hivyo ni vyema binti yangu uwapende wenzako ili Mungu aendelee kukupenda na kukupa utajiri wake."
"Kweli baba?, basi kuanzia leo mimi na Angel tutakuwa marafiki daima."
"Haswaaa!, umekuwa mwelevu sana binti yangu.Haya muombe msamaha mwenzako kwa maneno uliyoyasema kisha mshike mkono kuanzisha urafiki wenu siku ya leo."
Yalikuwa ni maongezi kati ya Nea pamoja na mtoto wake huku akimueleza maneno ya kumjenga na kumfundisha njia sahihi anayopaswa kupita, nae Beatrice akafanya kaba baba yake alivyomueleza.
Baada ya kupita zaidi ya mwaka mmoja na miezi kadhaa tangu aache kwenda kumuona Janet katika hospitali aliyokuwepo, siku hii Jesca aliamua kufunga safari na kwenda mpaka hospitali kwa ajili ya kwenda kuonana na Dk.Anthony.Alipofika hospitalini, kwa nyakati zile Dk.Anthony alikuwa ametoka kidogo hivyo ilimbidi Jesca amsubiri kidogo.
Baada ya kutoka kumchukua Angel katika shule anayosoma, akiwa njiani kumrudisha katika kituo cha watoto yatima ambacho kilikuwa kinatambulika kwa jina la ISLAF FOUNDATION mara Dk.Anthony anapigiwa simu ya dharura kutoka ofisini ambayo ilikuwa inamjulisha kuwa kuna majeruhi wa ajali ya gari wamefikishwa hospitalini wakiwa katika hali mbaya sana hivyo anahitajika arudi hospitali haraka iwezekanavyo.Mara baada ya kupata taarifa zile, Dk Anthony naye akaamua kurudi hospitali haraka kwanza kabla ya kumpeleka Angel.Walipofika hospitali, Dk Anthony akavaa mavazi yake ya kazi na kuingia katika majukumu yake ya kikazi huku akimueleza Angel amsubiri pale ofisini kwake mpaka atakaporudi.
Baada ya kukaa kwa muda kidogo tangu Dk.Anthony amuache pale ofisini,Kwakuwa alikuwa ni mtoto mdadisi sana hasa zaidi katika sehemu anayofika kwa mara ya kwanza, Angel akaamua kutoka ofisini na kuanza kutembea sehemu mbalimbali za pale hospitali huku akifika kuwasalimia baadhi ya wagonjwa ambao walikuwa wamelazwa pale hospitali.Katika tembea tembea yake, Angel akajikuta ameingia katika chumba kimoja ambapo alimkuta mama mmoja akiwa anahangaika kujiinua kitandani ili aweze kuketi.Angel akamuonea huruma sana mama yule, akasogea karibu na kitanda kile na kumsaidia kumuinua yule mama ili aweze kuketi bila kutambua yule amwonaye na kumsaidia pale ni mtu muhimu sana katika maisha yake.Baada ya kumsaidia kuketi, Angel akamsalimu yule mama, lakini cha kushangaza Mama yule hakuweza kumjibu chochote kwa kuzungumza zaidi alitikisa kichwa chake kumaanisha ameitikia salamu ile.Angel alipomtazama vizuri yule mama, akagundua hakuwa na huwezo wa kuzungumza ndio maana hata salamu yake alimjibu kwa kutikisa kichwa.Baada ya kuligundua lile, nafsini mwake alizidi kumuonea huruma sana yule mama na akachukua kitambaa chake na kuanza kumfuta jasho zilizokuwa zinamtiririka katika katika paji lake la uso.Mama yule akijikuta akitokea kumpenda sana Angel kwa yale yote aliyokuwa anamfanyia pasipo kujua yupo na mtoto wake wa kumzaa.Yakiwa hayo yanaendelea, mara anaingia Jesca katika kile chumba na kusogea mpaka sehemu alipokuwepo Angel pamoja na yule mama.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kitendo cha kumkuta Janet akiwa na mtoto karibu yake, kimlimfanya Jesca ashtuke kidogo na kuingiwa na wasiwasi.
"Shikamoo shangazi." Angel alimsalimu Jesca mara baada ya Jesca kufika pale walipo wao.
"Marahaba mwanangu, wewe ni nani na unafanya nini hapa?" Jesca aliitikia salamu ya mtoto Angel na kumuuliza swali.
"Mimi naitwa Angel na huyu hapa ni mama yangu hivyo nimekuja kumuona." Alijibu Angel kijasiri na kumpelekea Jesca ashtuke sana.
Kauli ile aliyozungumza Angel haikumshtua Jesca pekee bali hata Janet alishtuka sana pale alipoketi mpaka akajikuta mwili wake ukisisimka mno.
"Unamaanisha nini wewe binti kusema hivyo!, una maana huyu ni mama yako mzazi!?" Aliuliza Jesca kwa shauku kubwa ya kutaka kujua.
"Hapana shangazi, sio mama yangu mzazi ila binafsi huwa napenda kumuita mama mwanamke yoyote yule aliye mkubwa kama huyu mama kwasababu huwa naamini pengine anaweza kuwa na mtoto kama mimi."
"Oooh, basi ni vyema binti yangu lakini huyu mama hawezi kuwa na mtoto kama wewe maana yeye ni mgumba wa kutupwa na hatoweza kushika ujauzito katika maisha yake."
Yalikuwa ni maneno mithili ya kisu kikali kilichokwenda kuchoma katika moyo wa Janet vilivyo, machozi yakaanza kumtiririka huku akimtazama Jesca kwa uchungu sana japokuwa hakuwa na uwezo wa kufanya lolote lile.
Baada ya kurudi ofisini na kutoweza kumuona Angel pale alipomuacha, Dk.Anthony alianza kuhangaika huku na kule pale hospitali kwa ajili ya kumtafuta Angel ili amchukue na kumrudisha sehemu anayoishi.Alitembea sana na kuangaza huku na kule lakini hakuweza kumuona Angel mahali alipo.Hofu ikaanza kumuingia Dk.Anthony, ila alipofikiri sana akaweza kugundua kuna sehemu moja alikuwa hajaingia pale hospitalini hivyo akaamua kuelekea huko haraka ili akaone kama Angel atakuwa ameeleka huko.
"Naamini ni Mungu pekee hapa duniani humjalia kila mtu hitaji lake, hivyo shangazi kwa kuwa umenieleza kuwa huyu mama hawezi kuwa na mtoto katika maisha yake yote basi kuanzia leo huyu atakuwa mama yangu ili naye awe na faraja ndani ya moyo wake kuwa anaye mtoto." Aliongea Angel kwa weredi mkubwa na kumueleza Jesca.
Maneno mazuri ya mtoto mdogo Angel yaliweza kuchoma katika moyo wa Janet vilivyo mpaka akajikuta akidondosha chozi kutokana na faraja kubwa aliyokuwa anaipata ndani ya moyo wake maana hakutegemea kwa umri aliokuwa nao Angel kama anaweza kuongea maneno kama yale.
Maneno yale ya Angel, kwa upande mwingine yalimkera sana Jesca mpaka akajikuta akimuangisha sonyo zito Angel bila hata kujali udogo aliionao.
"Hivi unafikiri ukimfanya kuwa mama yako huyu ndio unafikiri utamfanya awe na raha!?, huyu baladhuri mkubwa na ataishi maisha ya tabu kama alivyo sasa mpaka kufa kwake." Alizungumza Jesca kwa sauti ya juu na iliyojaa hasira ndani yake, kisha akaanza kutoka pale ndani.
Alipofungua mlango Jesca kwa ajili ya kutoka nje, alikutana uso kwa uso na Dk.Anthony.
Dk.Anthony alishtuka sana maana hakutarajia kama anaweza kumkuta Jesca mahali pale.Kubwa ambalo lilimshtua zaidi, ni pale alipotupa macha yake kutazama ndani na kumuona Angel akiwa ameketi karibu na mama yake huku akimfuta jasho pamoja na machozi yaliyokuwa yanatiririka kutoka machoni mwa Janet.Wasiwasi mkubwa ulimjaa Dk.Anthony huku moyoni mwake akihisi pengine Janet ameshagundua kuwa Angel ni mtoto wake.
"Habari ya siku nyingi Dk.Anthony?" Jesca alimsalimu Dk.Anthony pale mlangoni waliposimama.
"Nzur!..nzuri Jesca karibu." Alijibu Dk.Anthony huku akipata kigugumizi cha ghafla kutokana na hofu aliyonayo.
"Asante Dokta, nina machache nahitaji tuzungumze."
"Sawa dada Jesca, tuelekee ofisini kwangu ili tukazungumze." Aliongea Dk.Anthony kisha akaongozana na Jesca kuelekea ofisini kwake ili wakaongee machache huku akimuacha Angel akiwa amejituliza pambeni mwa mama yake.
"Usilie mama na wala usiyaweke akilini haya aliyozungumza huyu shangazi, binafsi mimi naamini Mungu ndiye mpangaji wa kila kitu na mimi napenda unichukulie kama mwanao ili uwe unafarijika kila unionapo." Alizungumza Angel kwa utaratibu sana huku akiendelea kumfuta machozi Janet hata bila kutambua kuwa yupo na mama yake mzazi.
Janet alitokea kuvutiwa sana Angel, alimuona ni jinsi gani Angel alivyo mtoto mwelevu na aliojaliwa wema ndani yake.Alitamani azungumze neno lakini ilikuwa ngumu sauti yake kusikika kutokana na matatizo aliyonayo.Alijikuta moyoni mwake akifarijika sana kila alipokuwa anamtazama Angel, huku akijihisi kuwa na raha kubwa ndani yake, Janet akambusu Angel katika paji lake la uso na kumkumbatia.
"Samahani kidogo Dk.Anthony, nilipoingia katika chumba alicholazwa Janet nimeshangaa sana kumkuta akiwa na mtoto, je yule mtoto wa nani na kwanini yupo mahali pale?"
Lilikuwa ni swali gumu kwa Dk.Anthony kutoka kwa Jesca ila akajitahidi kukaza roho ili aweze kulijibu swali lile kwa usahihi.
"Yule ni mtoto wa mama mmoja ambaye amefika hapa hospitali kwa ajili ya kushughulikia uhamisho wa mgonjwa wake.Hivyo ameamua kumuacha mtoto wake hapa mara moja ili aweze kulishughulikia suala lake."
"Ooh, basi sawa.Ila kuna jambo lingine nahitaji tuzungumze kidogo."
"Bila shaka, zungumza tu."
"Baada ya mtoto sasa naomba afuate mama sasa."
"Unamaanisha nini kusema hivyo Jesca!?"
"Muda wa Janet kuendelea kuishi umeshaisha, sasa ni wakati wake wa kuifata familia yake mahali ilipo." Aliongea Jesca kwa ujasiri mkubwa.
Dk.Anthony alishtuka baada ya kusikia kauli hii kutoka kwa Jesca, akajikuta hasira kali ikimpanda huku akimuona Jesca ni kama shetani aliyopo mbele yake.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya kumaliza mazungumzo na kuagana na Jesca, huku kichwani mwake akiyafikiri makubaliano waliyoyafikia katika mazungumzo yao, kwa mwendo wa haraka Dk.Anthony akaelekea katika chumba alichokuwepo Janet kwa ajili ya kumchukua Angel.Alipofika mahali pale, Dk.Anthony alizidi kustaajabu baada ya kumkuta na kumuona Angel akiwa amelala usingizi miguuni mwa mama yake huku mama akiendelea kumpiga piga katika mgongo mithili kama anambembeleza mtoto mdogo.Aliposogea karibu zaidi na kitanda, Janet akatoa karatasi na kumpatia Dk.Anthony ili aweze kuisoma.Dk.Anthony alipoisoma ile karatasi, ilikuwa imeandikwa "'NIMEMKUMBUKA SANA MWANANGU, TAFADHALI NAHITAJI KUONANA NAE ANGALAU KWA MARA MOJA TU."'
Dk.Anthony alihuzunika sana baada ya kuusoma ujumbe ule, ila kwakuwa hakuhitaji Janet amfahamu mtoto wake kwa wakati ule zaidi akamueleza maneno ya kumtia moyo huku akimuahidi siku si nyingi atamletea na kumkutanisha mtoto wake.Baada ya kuongea na kumtuliza Janet, Dk.Anthony akamchukua Angel kwa ajili ya kumregesha katika kituo anachoishi.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment