Search This Blog

Sunday, July 10, 2022

IPO SIKU TU - 3

 







    Simulizi : Ipo Siku Tu

    Sehemu Ya Tatu (3)



    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Mtoto ambaye kila siku upo nae na ambaye unamjali na kumpenda sana, huyo ndiyo mtoto wako shemeji yangu." Aliongea Nelson na kumtaarifu Janet.

    Janet akabaki ameduwaa maana hakuelewa Nelson anamaanisha nini kuzungumza maneno yale.

    "Angel ndiye mtoto wako.Hili ninalokueleza shemeji, nina uhakika nalo asilimia mia kwasababu nililifuatilia na kulithibitisha pia."

    Baada ya kupokea taarifa hii, machozi ya furaha na yenye uchungu ndani yake yakawa yanamdondoka Janet huku akishindwa kuamini kama binti aliyekuwa akimpenda na kumjali sana mithili kama mwanae, kumbe ndiye mtoto wake halisi aliyetoka tumboni mwake.

    "Naamini machozi yadondokayo kutoka machoni mwako, ni ya furaha baada ya kufanikiwa kumtambua binti yako.Angel yeye haelewi chochote kuhusiana na haya na hajatambua kama wewe ndiye mama yake mzazi, hivyo naomba jambo hili liendelee kubaki kuwa siri maana Dk.Anthony alifanya hivi kwa nia nzuri kabisa." Aliongea Nelson na kumueleza Janet huku akimtaka asije akamueleza Angel kama yeye ndiye mama yake mzazi maana aligundua Dk.Anthony alifanya vile kwa lengo la kumlinda Angel asije akapata madhara yoyote yale kama ikatokea akagundulika ni mtoo wa Mr na Mrs Brian.

    Janet hakuwa na jibu lolote la kuweza kumwambia Nelson, zaidi alibakia kudondosha machozi ya furaha huku akisubiri ujio wa Angel kwa hamu kubwa siku hii baada ya kufahamu ni mtoto wake halisi.

    Baada ya kuweza kumfahamisha shemeji yake kila kitu alichoweza kukigundua, Nelson hakuwa na la ziada zaidi akamuaga Janet na kuondoka huku akiwa amemsisitiza sana asije akamueleza chochote Angel kuhusiana na yale yote aliyomueleza.



    Baada Nelson kuondoka, ulipita muda wa nusu saa tu Angel naye akawasili katika sehemu ile aliyohifadhiwa mama yake ili aweze kumsalimu.Siku hii Angel hakuwa na furaha kabisa moyoni mwake kutoka na kukosa ufadhili ambao alidhani utamsaidia katika kusoma kwake.Lakini wakati akiwa njiani kuelekea kwenda kumuona mama yake, moyoni mwake akajieleza atajitahidi kutoonesha hali yoyote ya unyonge mbele ya mama yake.

    Kitendo cha kumuona Angel akiingia mahali pale, moyo wake Janet ulilipuka kwa furaha maana leo alikuwa akimtazama binti yake kwa sura nyingine kabisa tofauti na ya siku zote.Alitamani hata asimame pale kitandani alipoketi ili aweze kwenda kumlaki na kumkaribisha mahali pale lakini ilikuwa ngumu kutokana na hali aliyokuwa nayo.

    Angel alipofika karibu na mama yake, mama akamkaribisha kwa furaha huku uso wake ukionekana kujawa na tabasamu nyakati zote.

    "Shikamoo mama." Angel alimsalimu mama yake.

    Salamu hii iliweza kupenya vilivyo masikioni mwake, baada ya kuitwa mama, Janet alijikuta mpaka machozi yakimdondoka kwasababu salamu ya Angel katika siku hii ilikuwa na uhalisia ndani yake.Angel akabaki anashangaa na kujiuliza kwanini mama yake anadondosha machozi baada ya yeye kumsalimia.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Akiwa amejituliza nyumbani baada ya kutoka kwenda kumuona Janet kwa siri, mke wake akahitaji kuzungumza nae ili aweze kumshirikisha jambo fulani.

    "Kuna jambo dogo hivi nahitaji kukushirikisha mume wangu." Alizungumza Jesca na kumueleza Nelson.Nelson naye akawa tayari kusikiliza analotaka kuambiwa.

    "Nadhani unatambua kuwa binti yetu amepata ufadhili katika masomo yake na anatarajia kwenda nje ya nchi hivi karibuni, sasa kuna fomu imekuja hapa naomba ubandike picha zako katika fomu hii na uijaze kama ukiwa mjomba ake na sio baba yake." Alizungumza Jesca na kumueleza mume wake.

    Maneno haya yalimshangaza Nelson maana alishindwa kuelewa ni kipi Jesca alikuwa amekimaanisha mpaka afikie kuzungumza vile.



    "Unamaanisha nini kwa mimi kuweza kuijaza fomu hii kama mjomba wakati Beatrice ni mwanangu!?"

    "Naomba unisamehe mume wangu kwa kushindwa kukufahamisha hili mapema ila naomba ufahamu wale wadhamini walikuwa wanatafuta mtoto yatima hivyo nami nikaamua kuipigania nafasi ile na kuandika binti yetu amefiwa na mzazi mmoja, yani hana baba ili tuweze kuipata nafasi ile." Alizungumza Jesca na kumueleza mumewe.

    "Hapana mama Beatrice!, huu ni upumbavu, unawezaje kumuandika binti yetu yatima wakati sisi wazazi wake wote wawili bado tupo hai!?, siwezi kufanya huo upuuzi unaoutaka!." Aliongea Nelson kwa ghadhabu mno na kumueleza mkewe.

    "Nakubali nilikosea mume wangu kwa kulifanya hili bila kukushirikisha hapo awali, lakini naomba unisamehe katika hilo na pia tafadhali jaza fomu hii ili binti yako asiipoteze nafasi hii ya kipekee na adimu kuipata."

    "Nimesema sitoweza kufanya hivyo!, binafsi nishaanza kuwa na wasiwasi kuhusiana na huo udhamini wenu, yawezekana kuna jambo limejificha nyuma yake!." Aliongea Nelson kwa hasira na kuzidi kumueleza mkewe.Kauli hii iliyoiongea Nelson ilimuuzi sana Jesca maana hisia za Nelson zilikuwa zinaendana na ukweli.

    Wakati hayo yakiendelea pale sebuleni huku Nelson akiwa amegoma kabisa kuijaza ile fomu, mara anaingia Beatrice mahali pale na kwenda kupiga magoti karibu na sehemu alipokuwa baba yake na kuanza kulia huku akimbembeleza baba yake aweze kukubali kuijaza fomu ile.

    "Tafadhali baba, mimi ni binti yako wa pekee na unayenitakia mema na mafanikio kila kukicha, naomba baba kubali kuisaini na kuijaza fomu hii ili nisipoteze nafasi hii niliyoipata ambayo ni adimu sana kutokea." Aliongea Beatrice kwa unyonge na kumueleza baba yake.

    Machozi pamoja na unyonge aliokuwa anauonesha Beatrice mbele ya baba yake, ulimfanya Nelson taratibu moyo wake kuanza kufunguka maana alikuwa hapendi kumuona binti yake akiwa katika hali ya huzuni.Nelson kachukua ile fomu na kuanza kuijaza kama akiwa mjomba wa Beatrice lakini moyoni mwake alijisikia vibaya mno maana mkewe hakuwa amemshirikisha jambo lile tangu awali.



    Baada ya kukaa na kuongea na mama kwa muda kidogo, Angel akajikuta usingizi ukimchukua na kulala karibu na mama yake huku kichwa chake akiwa amekilaza mapajani mwa mama yake.Muda wote Janet alijiwa na furaha sana kila alipokuwa akimtazama Angel huku akijaribu kuvuta picha na kulinganisha baadhi ya viungo vya mwili wa Angel na marehemu mume wake.

    "'Angalia mume wangu Brian, leo hii mtoto wako amejilaza hapa mapajani mwangu na kwa hili naamini sasa hivi nawe unayo furaha huko ulipo kama niliyonayo sasa."' Alijisemea moyoni mwake Janet kwa kuhisi kama anaongea na Brian, marehemu mume wake.

    Angel nae wakati akiwa amejipumzisha pale kwa mama yake, ndoto njema ikamjia usingizini.Alikuwa akiota yupo katika bustani nzuri iliyopendeza na kunawiri kwa maua mazuri huku akicheza na kuimba kwa furaha pamoja na mama yake.Wakati akiwa anaiota ndoto hii, muda wote uso wake ulikuwa katika hali ya tabasamu mpaka ukamfanya mama ashangae sana.

    Alipozinduka usingizini, Angel akaamua kumsimulia mama yake yale yote yaliyomjia ndotoni, mama naye alifurahi sana baada ya kufahamishwa yale maana alihisi ile itakuwa ni furaha ya Mungu pamoja na marehemu mume wake kwa yeye kuweza kumuona mtoto wake.

    Kwakuwa tayari muda ulikua umeshaenda, baada ya kuweza kumuona na kuzungumza na mama, Angel akamuaga mama yake na kurudi nyumbani.



    Yakiwa ni majira ya jioni, familia yote ilikuwa imejipumzisha sebuleni baada ya kupata chakula kwa pamoja huku maongezi mbalimbali yakiendelea baina yao.Katika maongezi yale, mara nyingi Beatrice pamoja na mama yake wakawa wanazungumzia kuhusiana na safari ya Beatrice kuelekea nchini Marekan kwa ajili ya kwenda kusoma kupitia ufadhili alioupata.Kwa upande mwingine maongezi yale yalikuwa yakimuumiza sana Angel maana alijiona ni yeye pekee asiyekuwa na bahati katika maisha kwa kukosa ufadhili wa kumsomesha kama ilivyo kwa Beatrice.Ni Nelson pekee ambaye aliweze kuligundua lile hivyo akawa anapoteza mada ile na kuzungumza mambo mengine ili Angel asiendelee kujisikia vibaya.

    Siku ya tatu ilipowadia, kila kitu kikawa tayari na Beatrice akaweza kusafiri kuelekea nchini Marekani kwa ajili ya kwenda kuanza masomo yake.



    Baada ya Beatrice kuondoka, Angel alibaki kuwa mpweke sana maana Beatrice ndiye alikuwa mtu wake wa karibu zaidi pale nyumbani.Alijitahidi kuizoea hali ile ya upweke huku akiendelea kujiandaa kuingia shule ambayo alipangiwa na Serikali kujiunga nayo kwa ajili ya kuanza kidato cha kwanza.Pia kitendo cha Beatrice kuondoka pale nyumbani, Mama Beatrice alifungua ukurasa mpya wa mateso dhidi ya Angel hususani pale Nelson asipokuwepo pale nyumbani.

    "We kenge!, umejikalisha hapo kuangalia Tv, umeshamaliza kuosha vyombo vilivyopo pale jikoni?" Jesca au Mama Beatrice alimuuta Angel na kumuuliza.

    "Ndio shangazi, kila kazi uliyonipa tayari nimeshaimaliza." Alijibu Angel kwa unyenyekevu maana hali ile ya kufanyishwa kazi nyingi na kuitwa majina yasiyofaa alishaanza kuizoea.

    "Shangazi, siku zote hizi huwa najiuliza kwanini umebadilika ghafla namna hii na kunichukia mimi mara baada tu ya dada Beatrice kuondoka, naomba unieleze shangazi ni kosa lipi mimi nimelifanya kwako ili nikuombe msamaha!?"CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Nyamaza!, mbwa mkubwa weee!, unafikiri hii ni sehemu ya kuwalisha bure machokoraa wanaohangaika kama wewe!?, lazima uwajibike hapa na ole wako nikusikie ukifungua hilo domo lako na kumueleza mume wangu haya yote yanayoendelea hapa nyumbani asipokuwepo, nitakubutua mpaka utaje jina la mama yako mzazi!, ebu nitokee hapa na sasa hivi nenda kule stoo ukafanye usafi." Yalikuwa ni maneno makari sana kutoka kinywani mwa Jesca au Mama Beatrice akimueleza binti mdogo, Angel.

    Haya ndio yalikuwa maisha mapya kwa Angel, muda wote alikuwa ni mtu wa kuhuzunika, kunyanyasika na kulia tu lakini pamoja na yale yote kufanyiwa, Angel hakuthubu hata siku moja kuweza kufungua kinywa chake na kumueleza Anko Nelson kwa kuhofia na kumuogopa shangazi yake.



    Alifika stoo ambayo ilikuwa imejaa vitu mbalimbali vilivyosheheni vumbi kutokana na kukaa kwa muda mrefu bila kutumika wala kusafishwa, Angel akaanza kufanya usafi kama alivyoagizwa na shangazi yake.Muda wote nafsini mwake alikuwa akihuzunika na kusononeka sana kutokana na yale yote aliyokuwa anayapitia pale nyumbani.

    Akiwa katika harakati za kusogeza baadha ya vitu ndani ya ile stoo ili aweze kufanya usafi vizuri, ghafla inadondoka picha moja kutoka katika kiroba ilimohifadhiwa na kioo cha fremu yake kupasuka.Angel akainama na kuikota picha ile ili aweze kuiregesha sehemu yake husika.Alipoikamata picha ile Angel, alipigwa na butwaa baada ya kushuhudia jambo ambalo lilimshangaza sana.



    Ilikuwa ni picha ya Janet ambaye yeye amemchukulia kama mama yake, akiwa yupo pamoja na mumewe Mr.Brian katika siku yao waliyofunga ndoa.Jambo ambalo lilikuwa linamshangaza Angel ni kumuona mama yake kwenye ile picha, akabaki akijiuliza sana kwanini picha ile ameikuta mahali pale.

    Akaisafisha na kuifuta vumbi ili aweze kuiona vizuri zaidi, ni kweli sura aliyokuwa anaiyona katika picha, ilikuwa ni sura halisi ya Janet pamoja na mumewe.Bila kutambua wale anaowaona pale ndio baba pamoja na mama yake mzazi na ndio wamiliki halali wa nymba ile anayoishi, Angel anaamua kuichukua picha ile na kwenda kuihifadhi chumbani kwake huku mengi zaidi aliona atakwenda kumuuliza mama yake pale atakapokwenda kumuona.



    Maisha ya manyanyaso na kusimangwa kila wakati, yalizidi kuendelea kwa Angel lakini busara na hekima kubwa aliyojaliwa kuwa nayo , alijitahidi kuyavumilia yote yale anayoyapitia bila ya kumueleza mtu yoyote.

    "Mbona katika mkono wako una jeraha tena, umeumia na nini mjomba?" Nelson alimuuliza Angel baada ya kumuona akiwa na jeraha mkononi kwake.

    "Niliumia wakati namsaidia shangazi kazi za hapa nyumbani, lakini usiwe na shaka Anko hili ni jeraha dogo tu." Alijibu Angel lakini wote ule aliouzungumza ulikuwa ni uongo mtupu maana jeraha lile alilipata baada ya kushushiwa kipigo na shangazi yake.

    Nelson alipolitazama Jeraha lile alilokuwa nalo Angel, lilikuwa ni jeraha kubwa kiasi hivyo akaona ni vyema aende kumnunulia dawa za kuweza kumsaidia kulitibu.

    "Nilikuwa nasubiri tu ufungue domo lako na uropoke, ungenitambua vizuri." Alizungumza mama Beeatrice na kumueleza Angel mara tu baada ya Nelson kutoka pale ndani.

    Angel akatoka na kuingia chumbani kwake huku akilia na kuhuzunika sana.

    "Uko wapi Anko Anthony?, kwanini uliondoka mapema na kuniacha mimi katika dunia iliyojaa mateso namna hii!?, basi ungenieleza tu ni wapi walipo wazazi wangu nami niondokane na tabu zote hizi, rudi Anko!..njoo uniokoe mimi Anko! Rudi Ankoooo.!!" Alilalamika na kulia sana Angel huku akiwa ameilalia picha ya Mr&Mrs.Brian ambayo alikuwa ameiweka pale kitandani baada ya kuichukua kule stoo.

    Haikupita muda, Nelson akaingua pale chumbani kwa Angel huku mkononi mwake akiwa amekamata dawa ambazo alikwenda kuzinunua ili Angel aweze kuzitumia kwa ajili ya kutibu jeraha alilonalo.Mara baada ya kuingia, Nelson akashangaa kumkuta Angel akiwa analia, akamsogelea haraka ili aweze kujua sababu ya kilio chake.

    "Tatizo nini Anko!, mbona unalia na kuhuzunika namna hiyo!?"

    "Hakuna shida Anko ila ni maumivu makari tu ya hili jeraha ndio yananifanya nilie." Aliongea Angel kwa unyonge huku akifuta machozi ambayo yalikuwa yanatiririka mashavuni mwake.

    "Pole mjomba, naomba utumie hizi dawa nilizokuletea naamini zitakusaidia kupunguza maumivu unayoyapata na kuponyesha kabisa hilo jeraha." Alizungumza Nelson huku akimkabidhi Angel dawa alizokuja nazo ili aanze kuzitumia.

    Pamoja na kuwepo pale na kuzungumza na Angel lakini mpaka anatoka pale ndani, Nelson hakuweza kufanikiwa kuiona picha iliyokuwa kitandani kwakuwa hakuwa na wazo lolote la kuweza kutazama sehemu ile.

    Licha ya kukosa amani moyoni mwake kutokana na yale yote anayoyapitia pale nyumbani, ni sehemu moja tu ambayo Angel alikuwa akifarijika na kujihisi naye ni mtu anayethaminika katika dunia hii, mwanamke ambaye moyoni mwake amempa thamani ya kuwa mama yake, huyu ndiye mtu pekee ambaye Angel alikuwa akimpenda na kumthamini sana na kila siku alijitahidi kwenda kumtembelea na kumjulia hali.



    Ikiwa ni siku tulivu, majira ya asubui na mapema, huku begi lake lililosheheni madaftari pamoja na vitabu mbalimbali akiwa amelibeba mgongoni, Angel anawasili katika shule ya sekondari Dakawa kwa ajili ya kuripoti na kuanza rasmi masomo yake kwa hatua ya kidato cha kwanza.Shule ya sekondari Dakawa ilikuwa ni shule ya kiserikali na ambayo ilikuwa inafaurisha wanafunzi wake kwa kiwango cha wastani wa kawaida tu.

    Siku hii Angel alikuwa na furaha mno kwa kuweza kushiriki masomo kwa mara ya kwanza pamoja na wenzake kwa hatua nyingine ya kimasomo.

    Wakati wa kurudi nyumbani ulipowadia, kabla ya kurudi nyumbani, Angel akaona ni vyema kwanza akapitia kwenda kumuona na kumjulia hali mama yake.



    Mama alipomuona binti yake amefika mahali pale, moyoni mwake alijawa na furaha mno tena baada ya kumshuhudia akiwa amevalia sare ya shule.Angel alimkimbilia mama yake na kumkumbatia kwa furaha.

    "Nimefurahi kukuona ukiwa salama mama yangu, tena leo nimekuletea zawadi moja nzuri sana ambayo naamini utaipenda na kuifurahia." Alizungumza Angel na kumueleza mama yake baada ya kumsalimia.

    "Sasa mama naomba ufumbe macho wakati nikiwa naitoa zawadi yangu." Aliongea Angel na kumtaka mama yake afumbe macho ili aweze kuitoa na kukabidhi zawadi aliyomletea.

    Angel akakamata begi lake na kulifungua, kisha akatoa picha ya Janet akiwa pamoja na marehemu baba yake huku akiwa ameinunulia fremu mpya baada ya ile ya mwanzo kupasuka.Baada ya kuitoa na kuikamata vizuri mikononi mwake, akamueleza mama yake sasa afungue macho ili aweze kuishuhudia zawadi aliyomletea.



    Baada ya kufumbua macho, akajikuta akibaki ameduwaa kwa kile alichokuwa anakishuhudia, machozi yakaanza kumtiririka Janet huku akishindwa kuamini kwa kile alichokuwa anakishuhudia pale.Alitamani kuzungumza kitu lakini ilikuwa ngumu sauti yake kuweza kusikika zaidi alibaki kuishia akichezesha mdomo tu.

    "Bila shaka huyu utakuwa ni wewe mama, je huyu aliye pembeni yako ni nani!?" Alizungumza Angel na kumuuliza mama yake huku akiwa amenyoosha kidole chake kuelekeza sehemu alipo marehemu Brian katika ile picha.Janet akaichukua ile picha na kuikumbatia huku kilio kikizidi kumtawala.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Hii picha nimeikuta pale nyumbani kwa Anko Nelson pamoja na shangazi hivyo nikaamua kukuletea uione, lakini mama hii picha ilifikaje nyumbani au ulimpa Anko Nelson akutunzie?, na kama aliichukua kwanini ameenda kuiweka stoo ya vitu vichafu!?" Yalikuwa ni maswali magumu kutoka kinywani mwa Angel akimuuliza mama yake na ni miswali ambayo yalimfanya Janet azidi kusikia uchungu moyoni mwake.

    Jinsi Janet alivyokuwa anahuzunika na kulia kwa uchungu, ilimpelekea Angel kuguswa sana na hali ile anayomuona nayo mama yake, imani ikamuingia moyoni mwake na akamsogelea na kumkumbatia ili aweze kumtuliza huku nafsini mwake akijutia na kujilaumu kwanini aliichukua ile picha na kumletea.

    Janet hakuhitaji kumueleza chochote binti yake kuhusiana na ile picha, zaidi alihitaji kubaki nayo maana ile ilikuwa ni kumbukumbu ya tukio muhimu sana katika maisha yake.



    Ikiwa mida ya jioni, baada ya kutoka kumuona na kumjulia hali mama yake, Angel akaanza safari ya kurejea nyumbani.Alipofika nyumbani akamkuta shangazi yake akiwa ameketi sebuleni akitazama runinga, Kwa hekima na unyenyekevu mkubwa Angel akamsalimu shangazi yake lakini badala ya kuitikiwa akajikuta akiadhibiwa kofi zito mpaka likampelekea kudondoka chini.

    "Mbwa mkubwa weee!, muda wote ulikuwa wapi mpaka nyakati hizi ndio urudi nyumbani!, naongea na wewe chokoraa usiye na baba wala mama!?" Alizungumza mama Beatrice kwa ukari na kumfokea Angel.

    "Nisamehe shangazi, nimechelewa kurudi nyumbani kwasababu sikuwa na ela yoyote ya ziada ambayo ningeitumia kulipia nauli ya gari zaidi ya ile uliyoichukua asubui niliyoachiwa na Anko Nelson." Aliongea Angel kwa unyonge mkubwa huku akijisomba pale chini alipoanguka na kuinuka.

    "Keleleee!, ngedere kasoro mkia weee!, nenda kabadilishe miguo yako hiyo haraka na uende ukaoshe vyombo sasa hivi kabla ya mume wangu hajarudi."

    Hakuwa na namna Angel, licha ya uchovu alionao ilimbidi atekeleze kama Shangazi yake alivyomuagiza.

    Maisha ya Angel hususani pale nyumbani yalizidi kuwa ya shida, kila aliporudi shuleni hakuwa na nafasi ya kupumzika zaidi ya kufanyishishwa kazi ngumu na shangazi yake.Hii ilimpelekea Angel awe na wakati mgumu sana katika kuitafufa elimu yake, alijithadi kuitumia nafasi ndogo aliyokuwa anaipata kuweza kujisomea huku moyoni mwake akiamini elimu ndio njia sahihi itakayoweza kumuongoza na kumbadilisha katika maisha anayoishi nyakati zile.

    Maarifa aliyojaliwa kuwa nayo pamoja na bidii yake kubwa katika kusoma kwa muda ule mchache aliokuwa anaupata, ilimpelekea Angel awe na wastani mzuri sana wa ufaulu katika masomo yake mpaka walimu wengi wa shule ya Sekondari ya Dakawa walibaki wakishangazwa na uwezo wake maana haikuwa kutokea pale shuleni mwanafunzi mwenye wastani mzuri wa ufaulu kama aliokuwa nao Angel.Sio katika kusoma tu, pia Angel alikuwa ni mwanafunzi mwenye hekima pamoja na unyenyekevu kwa mtu yoyote pale shuleni yani awe na umri mkubwa au mdogo kwake.Walimu pamoja na baadhi ya wanafunzi wenzake walimpenda sana maana alikuwa ni mwanafunzi mwenye kupenda kushirikiana na kila mtu hususani katika kusoma.Kasi yake ilizidi kuwa kubwa na mpaka anafanikiwa kuingia kidato cha pili hakuna hata somo moja ambalo alishuka wastani wa B.



    "Habar za jioni?" Ilikuwa sauti ya mwalimu mkuu wa shule ya sekondari Dakawa aliyekuwa akitambulika kwa jina la Mwl.David Mzovu akiwasalimu wanafunzi wake wa kidato cha pili nyakati za jioni huku mkononi mwake akiwa amekamata karatasi za matokeo.Wanafunzi walijibu salamu ya mwalimu wao na kutulia kwa ajili ya kumsikiliza.

    "Haya mnayoyaona ni matoke ya mtihani wenu wa taifa mlioufanya hivi karibuni kwa ajili ya kuhitimu elimu ya kidato cha pili na kuingia kidato cha tatu.Wengi wenu mmeonekana kufanya vizuri na kupata nafasi ya kuendelea kidato cha tatu japokuwa kuna wachache wamefeli." Aliendelea kuzungumza Mwl.Mzovu na kuwafanya wanafunzi waingiwe na hofu kuhusiana na matokeo yao.

    Angel alikuwa ni mmoja ya wanafunzi walio katika kusanyiko lile hivyo naye hofu ya matokeo ilikuwepo ndani yake huku akiongeza umakini wa kumsikiliza mwalimu mwake.

    "Kwasasa muda umeenda sana hivyo matokeo yenu mtayakuta kesho yakiwa tayari yameshabandikwa katika ubao wa matangazo lakini jambo pekee ambalo naweza nikawajurisha sasa, kwa mara ya kwanza shule yetu imeweza kutoa mwanafunzi aliyeongoza kitaifa.Hakika walimu wote tumefurahishwa sana na hili na lazima kama shule tumuandalie zawadi huyu mwanafunzu, naomba nimtaje jina ili asogee mbele hapa muweze kumuona." Aliendelea kuongea Mwl.Mzovu huku moyoni mwake akiwa na raha mno maana katika historia ya shule ile haikuwa kutokea mwanafunzi aliyefanya vizuri kama mwanafunzi aliyekuwa anamzungumzia.



    "Angel Brian, naomba usogee hapa nilipo mimi ili wanafunzi wenzako waweze kukushuhudia." Alizungumza Mwl.Mzovu na kumtaja Angel kuwa ndiye mwanafunzi aliyefanya vizuri zaidi mtihani ule kwa taifa zima.

    Ilikuwa ni furaha iliyoje kwa Angel baada ya kusikia jina lake ndilo lililoitwa pale, machozi ya furaha yakawa yanamtoka huku wanafunzi wenzake wakimpongeza kwa kumpigia makofi mengi maana walitambua yeye pekee ndiye atakayetajwa kutokana uwezo mkubwa alionao tangu awali.Alipofika na kusimama mbele kabisa(sambamba na mahali aliposimama mkuu wake wa shule), Mwl.Mkuu akamtaka Angel azungumze lolote lile mbele ya wanafunzi wenzake naye akawageukia na kutoa neno la shukrani kwao huku akiwaomba wazidi kushirikiana kwa pamoja katika kusoma maana mapambano bado yanaendelea.Wanafaunzi wenzake wakampongeza kwa kumpigia makofi mengi, Mwl.Mzovu nae akaamua kutoa zaidi tsh.30,000 na kumkabidhi Angel mbele ya wanafunzi wenzake kwa ajili ya kuonyesha raha aliyonayo kwa Angel kuweza kuitangaza vizuri shule yao.



    Akiwa amejipumzisha katika nyakati zile za jioni, mara anamuona binti yake akiwasili mahali pale.Moyoni mwake alijisikia faraja sana Janet maana likuwa anampenda sana mtoto wake.Angel naye huku siku hii akiwa na raha isiyo na kifani, alimkimbilia mama yake na kwenda kumkumbatia kwa furaha.

    Angel akamsalimu mama yake kisha akamjurisha yale yote yaliyojiri shuleni.Mama alifurahi sana na kujivunia kuwa na binti mweredi kama alivyo Angel.Mama akageuka katika meza iliyokuwa karibu na kitanda chake na kuchukua picha ile aliyopiga na marehemu mume wake na kuishika huku usoni mwake akiwa ameachia tabasamu la kutosha.Binafsi Angel alifurahi sana kumuona mama yake katika hali ile maana nyakati zote alipenda kumuona akiwa na furaha.

    "Inaelekea mama umemkumbuka sana huyu mume wako, lakini binafsi huwa najiuliza sana, kwasasa Baba yuko wapi wako maana tangu ukiwa katika hospitali ile ya Dk.Anthony mpaka hivi leo, sijawai kumuona hata siku moja akija kukutembelea?" Aliongea Angel na kumuuliza mama yake huku macho yake akiwa ameyaelekeza kutazama picha iliyopo mikononi mwa mama yake.

    Mama alibaki akitabasamu tu maana moyoni mwake alisikia raha sana kwakuwa Angel alikuwa akimuulizia baba yake bila ya yeye mwenyewe kutambua.Akamshika binti yake na kumsogeza karibu yake zaidi na kumlaza kifuani kwake.

    '"Tazama mume wangu, leo damu yako inakuulizia wapi ulipo!, naamini kwasasa unayo furaha yakutosha huko ulipo mume wangu, oooh! mume mume wangu Brian, pumzika kwa amani"' Janet alijisemea moyoni mwake na kujifariji huku akiwa bado amemkumbatia binti yake.

    "Anko Anthony alinieleza elimu ndio njia pekee ninayopaswa kupitia ili siku moja nije kuyakamilisha yale yote ninayoyawaza hivyo nami nitayakumbuka na kuyatendea kazi maneno yake daima na lengo langu, kwa gharama yoyote ile lazima nikutibu na kukuponyesha kabisa mama ugonjwa huu uliokufanya siku zote uishie kukaa hapa kitanda." Alizungumza Angel kwa hisia na kumueleza mama yake.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Maneno yale ya Angel yalimgusa sana mama, hakika aliamini ule usemi usemao Damu ni nzito kuliko maji maana kwa jinsi upendo aliokuwa anauonyesha Angel kwake, mithili kama alikuwa akitambua yeye ni mama yake mzazi.



    Taarifa za kufanya vizuri katika mitihani yake ya kuhitimu kidato cha pili, Nelson alizipokea kwa furaha mno na akampongeza sana Angel kwa kazi nzuri aliyofanya, lakini kwa upande wa Jesca ambaye Angel ni shangazi yake, alishangazwa sana na lile maana hakutegemea kama Angel ataweza kufanya vizuri katika masomo namna ile kutokana na wakati mgumu aliokua anampatia pale nyumbani.

    "Hongera sana mjomba, yani umenifanya leo niwe na furaha mno na natumaini kwa kasi hii uliyonayo naamini utafika mbali sana." Alizungumza Nelson kwa furaha na kumpongeza Angel, mara baada ya Angel kurejea pale nyumbani.

    "Asante Anko Nea, naamini hizi zote ni neema kutoka kwa Mungu na nitazidi kumtegemea yeye ili siku moja niweze kuyakamilisha yale yote ninayoyawaza."

    "Safi sana mjomba, Mungu atakusaidia na utafika mbali tu."

    Aliendelea Nelson kutoa pongezi zake kwa Angel.

    Wakati wote huo Nelson akizungumza na kumpongeza Angel, mama Beatrice yeye alikuwa amejituliza pembeni na hakuthubutu kufungua kinywa chake na kutoa neno la pongezi kwa Angel kwa kufanya vizuri katika mitihani.



    Maisha aliyokuwa anayapitia nyumbani hayakumfanya Angel apoteze tumaini la kuyafikia malengo aliyonayo zaidi aliendelea kujitahidi kuitafuta elimu kwa kasi kubwa maana aliamini ule ndio mtaji pakee utakaomsaidia katika maisha yake ya baadae.



    Ikiwa ni siku nyingine tulivu, baada ya kutoka katika mihangaiko yake ya kila siku, Nelson anafika sehemu alipohifadhiwa shemeji yake kwa ajili ya kumsalimu.Janet akamkaribisha Nelson mahali pale kwa furaha, wakasalimiana kwa kupeana mikono kisha Nelson akawa na machache ambayo alihitaji kumueleza shemeji yake na lengo kuu lililomfanya afike pale kwa nyakati zile.

    "Nashukuru shemeji yangu kwa kuweza kukuta ukiwa salama.Dhumuni ambalo limenifanya nifike mahali hapa kwa nyakati hizi za jioni, kuna kitu ambacho nilihitaji kuja kukukabidhi." Alizungumza Nelson na kumueleza shemeji yake huku akifungua begi lake la mkononi na kutoa bahasha kubwa yenye rangi ya kaki na kumkabidhi Janet.

    Janet hakuelewa ni kitu gani kilichopo ndani ya ile bahasha lakini baada ya kufungua, alishindwa kuamini kwa kile alichokiona.



    Zilikuwa ni picha za matukio mbalimbali katika siku ambayo Janet aliweza kupata ajali pamoja na marehemu mume wake.Kitu ambacho kilimshangaza Janet ni baadhi ya matukio ambayo aliyashuhudia katika zile picha kama vile, wakati akitoka hospitali yeye pamoja na marehemu mume wake, sehemu waliyopata ajali na mpaka picha za mwili wa marehemu mume wake wakati ukiwa umelala chini baada ya ajali ile kutokea.Hii yote ilionyesha ni wazi, ajali waliyoipata ilikuwa ni ya kusababishwa.

    Sio Janet pekee aliyekuwa anashangazwa na lile bali hata Nelson ambaye amezileta mahali pale, alibaki ameduwaa maana kumbe nae alikuwa haelewi kichomo ndani ya ile bahasha kwasababu alikabidhiwa na mtu aweze kuifikishia kwa Janet.

    Huzuni ilikuwa imemtawala sana Janet maana zile picha zilimkumbusha tukio ambalo hawezi kulisahau kabisa maishani mwake.

    "Hiyo bahasha nilikabidhiwa na kijana mmoja ambaye alijitambulisha kwangu kwa jina la Lucas, alinieleza nikufikishie wewe bila ya kufunguliwa na mtu yoyote.Binafsi nilishangaa sana shemeji lakini yeye alinieleza nitakapokutajia jina hili utaweza kumtambua." Alizungumza Nelson na kumueleza shemeji yake.

    Janet hakuweza kujibu lolote lile zaidi alimuomba Nelson amletee kibiriti.Nelson hakuelewa kwanini shemeji yake amemuomba amletee kibiriti lakini hakuhitaji kulifikiria sana lile zaidi akatenda kama alivyoambiwa.Baada ya kuletewa kibiriti, Janet akachukua zile picha na kuziregesha ndani ya ile bahasha kisha akaiwasha moto na kuitupa pembeni.Kilikuwa ni kitendo ambacho kilimshangaza sana Nelson maana hakujua kwanini shemeji yake ameamua kuzichoma picha zote zile ambazo kwa upande mwingine zingemsaidia katika kutafuta haki yake.

    "Kwanini shemeji umeamua kuzichoma hizi picha!?, binafsi nahisi huyu mtu alikuwa na maana kubwa kunipatia nikuletee, yawezekana pengine ajali mliyoipata wewe shemeji Brian ilikuwa imepangwa!" Alizungumza Nelson kwa na kumueleza Janet.

    Lucas alikuwa ni mwanasheria wa familia ya Mr.Brian hivyo nyakati zote alikuwa akiwasiliana na Janet kwa siri maana alikuwa akifuatilia jinsi tukio zima la ajali aliyoipata marehemu Brian pamoja na mkewe ilivyotokea na pia jinsi mali za wateja wake zilivyopotea na ndio maana Nelson alipotaja jina la Lucas, Janet alishaelewa kila kitu na pia alikuwa na sababu za kuzichoma picha zile.

    Baada ya Nelson kumuuliza kwanini ameamu kuzichoma zile picha, Janet akachukua karatasi na kuandika kuwa, kwasasa furaha ya binti yake ndio kitu pekee ambacho anakihitaji hivyo hana sababu za kukaa na zile picha maana zingezidi kumuumiza tu kwa kumkumbusha yale yote yaliyopita.



    Ikiwa ni siku nyingine tulivu, yakiwa majira ya mchana, Angel alikua amejituliza darasani pamoja na wanafunzi wenzake wakiendelea kujisomea wenyewe maana kwa wakati huo hakukuwa na mwalimu yoyote darasani.Wanafunzi wote wakiwa wanaendelea na ratiba zao binafsi, mara anaingia mwalimu mmoja wa kike ambaye alikuwa akijulikana kwa jina la Mwalimu Lucy na kutoa tangazo kuwa wanafunzi wote wanahitajika kufika sehemu ya makutano(Assemble) haraka kwa ajili ya kutangaziwa kuhusiana na ugeni mkubwa ambao ulifika pale shuleni kwao.

    Baada ya walimu pamoja na wanafunzi wote wa shule ya sekondari Dakawa kuweza kukusanyika sehemu ya makutano, ndipo mwalimu mkuu wa shule aliposogea sehemu ya makutano huku akiwa ameambatana na wageni waliotembelea pale shuleni.Baada ya kufika, Mwl.Mzovu akawasalimu wanafunzi wake kisha akahitaji kuongea machache hususani nw ugeni ule uliotembelea pale shuleni.

    "Mnaouna mbele yenu hapa, huu ni ugeni mkubwa kutoka nchini Marekani ambao umetutembelea hapa shuleni kwetu hii leo, naomba tuwe watulivu ili tuweze kusikiliza kile walichokuja kutueleza." Alizungumza Mwl.Mzovu na kuwakaribisha wageni ili wazungumze mbele ya wanafunzi yale waliyokuja nayo.

    "Naitwa Thomas Dickson, mimi ni balozi wa chuo kikubwa kinachotambulika kwa jina la 'Stanford University' kutoka nchini Marekani." Alijitambulisha kijana mmoja mwenye asili ya Kitanzania ambaye aliambatana kufika na ule ugeni

    Baada ya kijana aitwaye Dickson kujitambulisha kisha akachukua fursa ile kumkaribisha kiongozi wao wa msafara nae aweze kujitambulisha mbele ya walimu pamoja na wanafunzi wa shule ya sekondari Dakawa na kuzungumza machache, hususani kuhusiana na lile lililowafanya wafike pale shuleni.

    "Kwa majina naitwa Madam Caroline Laurian, mimi ni mmiliki wa chuo cha STANFORD UNIVERSITY kilichopo nchini Marekani na nimefika hapa Tanzania kwa ajili ya kuwajulisha kuhusiana na Sponsorship(Udhamini), kutoka chuoni kwetu" Alizungumza na kujitambulisha kiongozi wa msafara wa wale wageni na kuzungumzia suala la udhamini wa kimasomo wanaoutoa chuoni kwao.Madam Caroline alikuwa ni mama mwenye asili ya kizungu hivyo hata kiswahili chake alichokuwa anakizungumza kilikuwa si kinyoofu sana japo alikuwa anaeleweka kile alichokuwa anazungumza.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Chuo cha Stanford, kilikuwa ni chuo kikubwa sana kutoka nchini Marekani na chenye kukusanya wanafunzi wengi kutoka nchi mbalimbali ulimwenguni.Viongozi pamoja na mabalozi wa chuo hiki walikuwa na utaratibu wa kuzunguka katika mabara na mataifa mbalimbali kwa ajili ya kuwachukua wanafunzi waliofanya vizuri katika mitihani ya kitaifa kwenye nchi zao na kuwaendeleza kwa kuwapa udhamini.

    Baada ya kujitambulisha na kuzungumza machache pia Madam Caroline alieleza sababu kuu kabisa iliyowafanya wafike pale shuleni, ni kutokana na kuwepo kwa mwanafunzi aliyeongoza na kufanya vizuri katika mtihani wa kuhitimu kidato cha pili kitaifa, ambaye ni Angel.

    "Mpaka sasa, nimezunguka katika mataifa mengi sana lakini nadiriki kusema sijawahi kuona mwanafunzi wa kike aliyefaulu kwa wastani wa juu sana kama mwanafunzi aliyetoka hapa shuleni kwenu ambaye anaitwa Angel, kwakweli nawapongeza sana walimu wa hapa na pia si vibaya kama angepita mbele huyu mwanafunzi ili niweze kumuona." Alizungumza Madam Caroline japo sio kwa kiswahili nyoofu, lakini alichokuwa amekizungumza kiliweza kueleweka.

    Takribani wanafunzi, walimu na wageni wote waliinua mikono yao na kumpigia makofi mengi ya pongezi wakati Angel akisogea mbele kabisa ya kusanyiko lile.Hii ilimfanya Angel ajisikie kupata raha isiyo na kifani moyoni mwake mpaka akajikuta machozi ya furaha yakimdondoka.Madam Caroline akampokea Angel na kumkumbatia kwa furaha na kumtaka azungumze chochote mbele ya wanafunzi wenzake, lakini Angel alishindwa kuongea lolote lile kutokana na kuzidiwa na kilio.

    Baada ya wageni kumaliza kuwasilisha yale waliyokuja nayo, mkuu wa Shule naye akazungumza machache na kuwataka wanafunzi wake wayazingatie yale yote waliyoelezwa na ule ugeni uliotembelea pale shuleni kwao kisha akatoa matangazo mengine na kuwaruhusu wanafunzi wote warudi madarasani kuendelea na vipindi huku Angel akiwa amefuatana na wale wageni kuelekea ofisini maana walihitaji kuzungumza nae.



    Lengo la Janet kuzichoma picha zile mbele ya shemeji yake, alikuwa haitaji mtu yoyote atambue kama kuna upelelezi wa siri ambao anaufanya kupitia kwa mwanasheria wake aitwaye Lucas.Japokuwa Nelson alikuwa karibu naye na aliyejitoa kumsaidia kwa kila jambo, lakini kwa upande mwingine Janet alikuwa hamuamini sana kwasababu Nelson alikuwa akiishi na wifi yake, ambaye ni adui mkubwa katika maisha yake.

    Wakiwa katika maongezi ya kawaida, mara anaingia Angel mahali pale huku akiwa ameambatana na ule ugeni uliotembelea shuleni kwao.Angel alifika na kumsalimu mjomba pamoja na mama yake, kisha akawatambulisha kwa wageni aliyokuja nao.Madam Caroline pamoja na jopo lake, nao wakasalimiana na Janet pamoja na Nelson na wao kujitambulisha pia, kisha wakaeleza lengo la wao kufika pale.

    "Basi kama nilivyowaeleza hapo awali, sisi tumetoka nchini Marekani, katika chuo cha STANFORD na mimi ndiye mmiliki wa chuo hicho.Nimevutiwa sana na uwezo wa darasani aliokuwa nao binti yenu hivyo nahitaji kumfadhili na niende nae ili akasome katika chuo changu na ndio maana tumekuja kumuona mama yake ambaye yeye mwenyewe Angel ndiye ametuongoza mpaka kufika sehemu hii.." Yalikuwa ni moja ya maneno ya madam Caroline katika maongezi yake akiwaeleza Janet pamoja na Nelson.

    Janet alishangaa sana kwa Angel kuweza kuwaeleza wale wageni kuwa yeye ndiye mama yake mzazi, akageuka na kumtazama Nelson na kuhisi pengine atakuwa ameshamfahamisha Angel kila kitu, lakini kumbe Angel alikuwa hafahamu chochote ila moyoni mwake aliamua kumpa Janet hadhi ya kuwa mama yake mzazi maana yeye tangu azaliwe alikuwa hatambui ni wapi alipo mama yake.

    "Kutokana na umri wake alionao, kwanza ataanzia kusoma masomo maalumu kwa muda wa miaka mitatu na hii ni kwa ajili ya kumjenga kabla ya kuingia katika kozi kubwa kabisa za chuo." Aliendelea kuzungumza Madam Caroline na kuzidi kufafanua kuhusiana na udhamini watakaompatia Angel.

    Ilimbidi Nelson ndiye azungumze na wale wageni badala ya Janet, na hii na kutokana matatizo aliyonayo Janet.Ile ilikuwa habari njema sana kwa kila mmoja na bila ajizi yoyote ile Janet pamoja na Nelson wakakubali Angel aweze kupata ufadhili ule katika masomo yake.Baada ya maongezi yote kukaa sawa, Madam Caroline akatoa fomu ambayo inatakiwa ijazwe na mazazi wa mwanafunzi na kumkabidhi Janet ili aweze kuijaza.

    Baada ya kila kitu kuwa sawa, Madam Caroline akatoa shukrani zake za dhati kwa familia ya Angel kwa kuweza kukubaliwa ombi lake la kumfadhili na kumchukua Angel.Mwisho kabisa, Madam Caroline akamalizia kwa kumpa Angel wiki moja ya kufanya maandalizi ya safari wakati wao wakiendelea kukamilisha taratibu nyingine hususani taratibu za kiserikali pamoja na kumuandalia Visa ya kusafiria.



    Ilikuwa ni siku ya furaha sana kwa Angel, kila wakati kinywani mwake hakuchoka kutamka na kuimba, "Glory to God!, Glory to God!..Asante Mungu!".Pia Angel aliweza kuyazingatia maneno aliyoelezwa na mjomba wake maana Nelson alimueleza ni lazima awe msiri katika lile na wala asije akathubutu kumueleza shangazi yake jambo lile, ambaye ni mama Beatrice.



    Zikiwa zimebaki siku mbili pekee kabla ya kuweza kusafiri, siku hii Nelson akamchukua Angel na kuhitaji kumpeleka mahali kama shemeji yake alivyomuagiza.

    Wakiwa ndani ya gari, Angel alijitahidi kumuuliza Anko Nelson aweze kumueleza ni sehemu gani wanayoenda maana alimchukua na kumtaka aingie kwenye gari bila ya kumfahamisha chochote kile.Nelson hakuhitaji Angel afahamu chochote kile kuhusiana na sehemu wanayoenda kwa wakati ule hivyo alikuwa akimjibu kwa kuyakwepa maswali yake.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Safari ilizidi kuendelea na baada ya mwendo wa gari kwa muda wa nusu saa, walifika sehemu moja ambayo ilikuwa imezungukwa na makaburi kila mahali kisha Nelson akasimamisha gari.

    "Anko!, tumekuja kufanya nini huku makaburini au kuna ndugu yako amezikwa mahali hapa!?" Aliuliza Angel kwa mshangao huku akishindwa kuelewa kwanini Anko Nea amempeleka pale makaburini.

    "Usijali mjomba, lipo jambo la muhimu sana ambalo mama yako ametaka uje kuliona mahali hapa kabla hujaondoka kuelekea masomoni, hivyo Anko naomba tushuke ndani ya gari ili nikupeleke."

    "Mama!, ina maana Anko umemuona mama yangu!?" Aliuliza Angel kwa mshangao mkubwa baada ya Nelson kumueleza kuwa mama yake ndiye aliyemuagiza amlete mahali pale.

    "Oooh, hapana Anko, simaanishi mama yako mzazi bali ni yule mama aliye pale hospitali." Aliongea Nelson na kumfahamisha Angel.

    Baada ya maelezo haya mafupi, Nelson akamchukua Angel na kumuongoza hadi katika kaburi lililoandikwa kwenye msalaba wake jina la Brian Andrew, ambapo kaburi hili ndilo kaburi alimozikwa mume wake Janet.Walipofika katika lile kaburi na ndipo Nelson alipoamua kumueleza ukweli Angel juu ya kaburi lile.

    "Angel binti yangu?"

    "Ndio Anko"

    "Hili unaloliona hapa ndilo kaburi la baba yako mzazi.Japokuwa utakuwa na wakati mgumu sana kuweza kulielewa hili, lakini naomba utambue Brian Andrew ambaye ndiye baba yako mzazi, yeye alishafariki siku nyingi zilizopita baada ya kupata ajali mbaya ya gari akiwa pamoja na mama yako." Aliongea Nelson na kumueleza Angel.

    Zilikuwa ni taarifa ambazo zilimshangaza sana Angel maana siku zote yeye alikuwa akitambua jina la baba yake lakini hakuwa kumuona Sura yake na kila alipokuwa akimuuliza marehemu Dk.Anthony kuwa ni wapi walipo wazazi wake, Dk.Anthony alikuwa akimjibu na kumueleza kuwa wazazi wake wapo na siku moja ataweza kuwaona tu.

    "Marehemu Dk.Anthony hakuhitaji kukueleza lolote kuhusiana na hili kwasababu alihitaji kwanza ujikite zaidi katika kusoma, lakini kuanzia sasa naomba utambue baba yako ni marehemu na hili ndilo kaburi lake." Alizungumza Nelson na kuzidi kumjulisha Angel.

    "Samahani Anko Nea, Je naweza kukuliza swali?"

    "Bila shaka Anko, niulize tu."

    "Kama baba yangu alishakufa siku nyingi zilizopita na hili ndilo kaburi lake, Je mama yangu yuko wapi kwasasa au nae ni marehemu!?" Kwa sauti ya unyonge huku machozi yakimtoka na kuchiriza mashavuni mwake, alizungumza na kuuliza Angel.

    Anko Nelson hakuwa na jibu lolote katika lile zaidi alisogea karibu na Angel na kumshika begani kwa lengo la kumpa matumaini katika yale.Angel aliangukia kaburi la baba yake na kuanza kulia kwanguvu na kwa uchungu sana maana leo ndio anapata fursa ya kujigundua kuwa pale alipo ni yatima.

    "Baba! baba!, kwanini hukuhitaji hata kuniona mimi mwanao kabla haujaondoka! amka baba! mimi Angel, mtoto wako nimekuja kukuona..Baba!.Babaaaa..!!" Yalikuwa ni moja ya maneno ya uchungu na masikitiko kutoka kinywani mwa Angel mbele ya kaburi la baba yake.



    Baada ya kwenda kuliona kaburi la baba yake na kumsalia ili marehemu Brian aweze kupumzika kwa amani kule alipo, Nelson akamchukua Angel na kurudi nae mpaka sehemu alipohifadhiwa Janet.Alipofika kwa mama yake, Angel alifikia kulia tu huku akilalamika mbele ya mama yake kuwa yeye ni yatima na hatambui kwanini Mungu alimchukua baba yale mapema na kutompa fursa ya kumuona na kukaa nae angalau hata kwa muda mdogo tu.Janet alijitahidi kumbembeleza binti yake japo yeye ndiye aliyemuomba Nelson ampeleke Angel akalishuhudie kaburi la baba yake.Wakati akiendelea kumbembeleza binti yake, Janet alijikuta akishindwa kujizuia kulia maana jambo lile lilikuwa linamgusa hata yeye pia.



    Ikiwa ndio siku rasmi ya kusafiri kuelekea masomoni, Angel akachukua fursa ile kufika shuleni kwa ajili ya kuwashukuru na kuwaaga walimu pamoja na wanafunzi wenzake wa shule ya sekondari Dakawa, kisha akatoka na msafara wake unaomsindikiza katika safari yake mpaka kufika kwa mama yake ili nae pia aweze kumuaga.

    "Nitakukumbuka sana mama yangu mpendwa, natamani niendelee kubaki nawe lakini naamini hata hili ninaloenda kulifanya ni jambo jema kwetu na natumani Ipo Siku Tu nitakuja kukutimizia ile ahadi niliyokuahidi." Alizungumza Angel kwa unyonge wakati akimuaga mama yake.

    Janet hakuwa na lolote la kumueleze mtoto wake zaidi akavua cheni yake aliyoivaa shingoni, cheni hii alinunuliwa na marehemu mume wake ikiwa kama zawadi kwake baada ya kufunga ndoa yao, kisha akamvisha ile cheni binti yake na kumbusu katika paji la uso kwa ajili ya kumtakia baraka njema katika masomo na safari yake anayoenda na pia huku machozi ya huzuni yakimtoka maana ata yeye atamkumbuka sana binti yake kutokana na upendo mkubwa uliokuwepo baina yao.

    Baada ya kuagana na mama, kisha Angel akaenda kumuaga Anko Nelson ambaye alikuwa amesimama kando kidogo ya Janet.Angel akamshukuru sana Anko Nelson kwa msaada mkubwa aliokuwa amempatia tangu aondokewe na mlezi wake ambaye ni marehemu Dk.Anthony na pia Angel akamuomba ajitahidi kutovunja makubaliano yao maana Anko Nelson alimuahidi atamsaidia kumtafutia mama yake mahali alipo ili siku atakayorudi kutoka masomoni aweze kuonana nae.Kauli ile ya Angel ambayo alikuwa akimsisitiza Anko Nelson asisahau kumtafutia mama yake, ilimfanya Janet asikie huzuni sana moyoni mwake mpaka kufikia kutamani kumueleza ukweli binti yake ili aondoke huku akitambua kuwa yeye ndiye mama yake mzazi, lakini ilikuwa ni ngumu kufanya vile kwasababu ambazo zilikuwa ni za msingi.

    Baada ya kumaliza kuagana na familia yake, Angel akachukuliwa na watu wa msafara wake na kupakizwa kwenye gari na kuanza safari ya kuelekea uwanja wa ndege wa Julius Kambarage Nyerere kwa ajili ya kuanza safari yao ya kuelekea nchini Marekani.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Akiwa amerejea nyumbani kutoka katika shughuli zake za kibiashara, Mama Beatrice anazunguka huku na kule pale ndani kumtafuta Angel maana kuna kazi alihitaji kumpatia aifanye kwa wakati ule.Alijitahidi kumuita na kumtafuta kila mahali lakini ni ukimya tu ulionekana kutawala pale ndani.Baada ya kuhangaika sana, ndipo alipoamua kuingia katika chumba cha Angel huku akihisi pengine atakuwa amelala maana muda wake wa kwenda shule ulikuwa bado haujawadia.Alipofungua chumba cha Angel na kuingia ndani, alistaajabu baada ya kukuta kabati la kuwekea nguo likiwa lipo wazi tena likiwa halina hata nguo moja pamoja na baadhi ya vitu ilivyokuwepo pale ndani.Akili ya haraka, Mama Beatrice akahisi pengine Angel atakuwa ametoroka kutokana na maisha ya tabu aliyokuwa anampatia pale nyumbani.

    Akiwa katika tahaluki hiyo, mara Jesca au Mama Beatrice, anapokea simu ambayo ilimfanya ashtuke kidogo na baadae kuachia tabasamu zito.





    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog