Search This Blog

Sunday, July 10, 2022

IPO SIKU TU - 4

 







    Simulizi : Ipo Siku Tu

    Sehemu Ya Nne (4)





    "'Habari dada Jesca?, napenda kukutaarifu kuwa ile kazi uliyonituma nimeshaikamilisha tayari, ni kweli kama hisia zako zilivyokuwa, nimegundua Janet ni mzima na sehemu alipo pia nimefanikiwa kuitambua."' Ilikuwa ni taarifa ambayo ilimfanya Mama Beatrice atabasamu baada ya kuipokea kupitia ile simu aliyopigiwa kutoka kwa kwa mtu ambaye alimpatia kazi.

    Baada ya kupokea maelekezo yote hususani kuhusiana na jinsi ya kufika sehemu alipohifadhiwa Janet, Mama Beatrice hakuhitaji kupoteza muda, akachukua funguo za gari na kuingia kwenye gari yake ili aelekee sehemu aliyoelekezwa haraka iwezekanavyo.



    Katika nyakati zile za mchana, wakati mwanasheria Lucas akiwa anaelekea kwenda kumuona Janet kwa ajili ya kumueleza aliyoyagundua kupitia upelelezi wake wa siri anaoendelea kuufanya, mara anakutana na gari ndogo mbili, zenye rangi nyeusi zikiwa zimepaki nje kidogo ya hospitali aliyoifadhiwa Janet.Binafsi Lucas alianza kuingiwa na wasiwasi sana maana kila alipotazama mazingira ya pale nje, alitambua kuwepo kwa zile gari pale nje lazima kutakuwa na sababu.Lucas akijikuta moyo wake ukimsukuma kutenda jambo, akaingia ndani na kumchukua Janet haraka kwa ajili ya kumuhamisha sehemu ile.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Kwasasa dada Janet anafuatiliwa sana na maisha yake yapo hatarini mno hivyo ndio maana nilihitaji tumtoe pale hospitali haraka iwezekanavyo maana gari nilizozikuta zimepaki pale nje zilinifanya nipate wasiwasi kidogo." Ilikuwa ni kauli ya kijana Lucas akimueleza Nelson baada ya kufanikisha kumtorosha Janet sehemu aliyokuwepo awali na kumfikisha sehemu salama.

    Muda wote huo, Nelson alikuwa hajaelewa Lucas ana uhusiano gani na Janet maana hii ilikua ni mara yake ya pili kumuona baada ya kuonana nae ili siku ya kwanza ambapo alimkabidhi picha aweze kumfikishia Janet.

    "Nadhani hii sio mara yetu ya kwanza kuonana, pia nadhani si vibaya tukaweza kutumia fursa hii kufahamiana vizuri zaidi." Alizungumza Nelson na kumueleza Lucas.

    Kabla ya kumjibu Nelson, Lucas alipomtazama Janet kuna ishara alimpatia hivyo iliamua kujitambulisha si kama mwanasheria bali yeye ni rafiki wa marehemu Brian na ndio maana yupo karibu na Janet.Baada ya kufahamiana vizuri ndipo maongezi baina yao yakazidi kuendelea.



    Mama Beatrice alifika hadi katika chumba ambacho alielekezwa ndipo anapopatikana Janet lakini cha kushangaza hakukuwa na mtu yoyote aliyeweza kumkuta ndani yake.Akajaribu kuangalia mazingira ya pale ndani ili aone kama anaweza kugundua chochote lakini hakukuwa na ishara yoyote ambayo ingeweza kumjulisha kama ni kweli Janet alikuwepo mahali pale.Alipoendelea kutazama vizuri, ndipo alipoweza kuiona saa ya mkononi iliyonawili kwa rangi ya Shaba ikiwa kwenye sakafu, karibu na ukingo wa kitanda.Alipoitazama vizuri aliona kama ni saa ambayo alikuwa akiifahamu, akainama na kuikota ili aendelee kuitazama vizuri zaidi.

    Baada ya kukosa kumuona na kumpata Janet, Mama Beatrice alirudi nyumbani huku akitafakari sana yale yote aliyoambiwa na kuyashuhudia pale hospitali alipoenda.Mpaka inafika nyakati za jioni, bado mama Beatrice aliendelea kufikiri na kutafakari sana hususani kila alipoitazama ile saa ambayo aliokota pale maeneo ya hospitali maana alihisi kama ni ya mtu anayemfahamu.

    Wakati Mama Beatrice akiendelea kuyatafakari hayo, mara anaingia Nelson pale ndani.Kabla ya jambo lolote lile, mama Beatrice akatupa macho yake na kutazama katika mkono wa Nelson kama saa yake aliyovaa asubui atakuwa anayo, lakini Nelson hakuwa na saa yoyote aliyovaa kwa wakati ule na ndipo Jesca alipoanza kuhisi kitu juu ya mume wake.

    "Habari za mihangaiko mume wangu?" Mama Beatrice alimsalimu mume wake.

    "Nzuri mke wangu, siju na wewe tena hapa nyumbani."

    "Hapa nyumbani si kwema sana maana tangu nirudi nyakati za mchana mpaka muda huu, mjomba wako Angel hajarudi hapa nyumbani."

    "Ooh!, nilisahau kukujulisha Mama B, wakati leo mchana nikiwa kazini nilipokea simu ya dada yake marehemu Dk.Anthony, aitwaye Catherine, na akanitaarifu kuwa amekuja kumchukua Angel ili akaishi nae maana kaka yake alimuachia maagizo hayo.Hata hivyo jioni hii niliongea na Angel na anakuomba umsamehe kwa kuondoka bila kukuaga na pia anakupa salamu nyingi sana." Nelson alimueleza na kumtaarifu Mama Beatrice juu ya kuondoka kwa Angel japo huu wote ulikuwa ni uongo mtupu maana hakuhitaji atambue kama Angel amepata fursa ya kwenda kusoma nje ya nchi.

    Majibu ya Nelson hayakumuingia Akilini kabisa Mama Beatrice maana alijiuliza, inawezekanaje Angel aondoke ghafla namna ile bila maandalizi yoyote, akahisi lazima kuna kitu ambacho mume wake atakuwa amemficha kumueleza.



    Yakiwa majira ya usiku wa saa tisa na nusu, Angel, huku akiwa ameambatana na Madam Caroline pamoja na jopo lake aliloongozana nalo katika safari ile, wanawasili katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Marekani uitwao 'Los Angels International Airport'.Furaha ilikuwa kubwa sana kwa Angel kwa kuweza kukanyaga ardhi ya nchi ambayo siku zote aliishia kusoma habari zake na kuiona katika runinga.Wakiwa njiani kuelekea katika sehemu anayoishi Madam Caroline, mandhari aliyokuwa anaiona njiani ilizidi kumvutia sana Angel maana ilikuwa tofauti sana na ile aliyoizoea kuiona nchini Tanzania.

    Madam Caroline yeye ni mwanamke au mama ambaye hakubahatika kupata fursa ya kuwa na mtoto katika maisha yake hivyo hata jumba kubwa la kifahari ambalo alikuwa analimiliki, zaidi ya kuwepo wafanyakazi wa kumsaidia kazi mbalimbali hakuwa na mtu yoyote anayeishi nae.Kwa jinsi alivyotokea kumpenda Angel, Madam Caroline akaamua kumchukua Angel na kwenda kuishi nae nyumbani kwake japo utaratibu wa chuo chake, wanafunzi wote wageni ambao wamekusanywa na kuchukuliwa kutoka nchi mbalimbali ulimwenguni wanapoletwa huwa wanapelekwa kukaa katika Bweni kubwa lililopo chuoni.Kila kitu alichokuwa anakitazama Angel aliona kama ni ndoto kwake hususani akikumbuka maisha ya tabu aliyokuwa akiyaishi nyumbani kwa mama Beatrice.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ikiwa ni siku ya pili tangu waweze kufika na baada ya kupata mapumziko, siku hii Madam Caroline akamchukua Angel na kumpakiza katika gari yake illi akamuoneshe jinsi mazingira ya chuo yalivyo kabla hajaanza rasmi masomo yake.

    Chuo cha Stanford kilikuwa ni chuo kikubwa duniani na chenye hadhi ya kimataifa hivyo hata mazingira yake yalikuwa mazuri mno na yenye kumshawishi mwanafunzi aweze kujikita zaidi katika kusoma.Baada ya kumtembeza sehemu chache za chuo kisha madam Caroline akaamua kumpa fursa Angel aweze kutembeatembea mwenyewe ili aendelee kuyazoea mazingira ya pale ikiwemo kusalimiana na wanafunzi wenzake.Kila sehemu aliyokuwa anaitazama iliweza kumvutia vilivyo na binafsi alijiona mwenye bahati sana kupata fursa ya kusoma katika chuo kikubwa kama kile.

    Akiwa katika tembeatembea huku akiendelea kusalimiana na baadhi ya wanafunzi wenzake ambapo kwa upande mwingine ndio wenyeji wake wa pale chuoni, Mara Angel anasikia sauti ikimuita jina lake.

    "Angel!..Angel!?" Ni sauti ambayo ilisikika ikiita jina la Angel kwa mshangao.Aliposikia mara ya kwanza Angel akaipuuzia huku akihisi pengine yupo mwanafunzi eneo lile mwenye jina kama lake, lakini alipoisikia sauti ile ikiita kwa mara nyingine tena ndipo alipogeuka kutazama nyuma ili amshuhudie mtu aitaye.

    Ulikuwa ni mshangao mkubwa sana kwa Angel huku akishindwa kuamini kwa kile anachokishuhudia pale.Ni zaidi ya miaka miwili imepita tangu waweze kuachana lakini leo bila kutegemea, tena katika mazingira tofauti kabisa anaweza kumshuhudia.



    "Beatrice!, Ni wewe kweli Dada Beatrice!?" Ilikuwa ni sauti ya mshangao kutoka kwa Angel baada ya kumshuhudia Beatrice mbele ya upeo wa macho yake.

    Mshangao mkubwa ulikuwa kwa Beatrice maana alishindwa kuamini kama ni kweli anayemshuhudia pale ni Angel.

    "Angel!, umewezaje kufika huku!?" Aliuliza Beatrice kwa mshangao.Angel akamfuata Beatrice na kumkumbatia kwa furaha maana hakutegemea kama sehemu anayokuja kusoma kumbe ndiyo sehemu aliyokuwepo Beatrice.

    Baada ya kusalimana, wakapata muda kidogo wa kuweza kuzungumza machache na Beatrice alihitaji kufahamu kivipi Angel amaweza kufika pale chuoni kwao.Bila hiyana yoyote ile, Angel akamueleza kila kitu juu ya udhamini wake alioupata na pia kumjulisha kuhusiana na habari za familia yake.Beatrice alitabasamu na kumkaribisha sana Angel pale chuoni maana yeye tayari alishakuwa mwenyeji kwakuwa ni miaka miwili sasa imepita tangu afike pale na kuanza masomo.

    Beatrice kidogo yeye alishapiga hatua na alikuwa amebakiza mwaka mmoja tu wa kuweza kumalizia kusoma kozi ya awali na kama akifanya vizuri katika mitihani yake ya mwaka wa mwisho, basi atapata fursa ya kujiunga katika masomo ya kozi kubwa za pale chuoni.Upande wa Angel yeye ndio kwanza alikuwa anaanza hivyo moyoni mwake alijiapiza hatoweza kuitumia vibaya nafasi ile aliyoipata.



    Wakati wa mwanzo, Angel alipata wakati mgumu sana katika kuyazoea masomo maana kila kitu kilikuwa ni kigeni kwake.Hali ile haikumfanya Angel akate tamaa zaidi alizidi kuongeza jitihada katika kusoma na kupitia msaada wa Madam Caroline ambaye alikuwa akimpa matumaini na kumfundisha njia za kupita ili aweze kuyazoe mazingira yale haraka, kadri siku zilivyozidi kwenda Angel alianza kubadilika katika usomaji wake na kuanza kufanya vizuri katika mitihani mbalimbali aliyokuwa anaifanya.

    Kasi yake katika kusoma ilikuwa kubwa mno na ilimchukua muda mfupi tu kuweza kupata umaarufu pale chuoni maana kila orodha ya mwezi iliyokuwa inatolewa ya wanafunzi walioweza kufanya vizuri katika mitihani yao, Angel alikuwa ni mmoja wao tena katika nafasi za juu.Jambo lile lilikuwa likimfurahisha sana Madam Caroline na alijitahidi kumsimamia Angel ili aweze kuendelea na kasi aliyonayo na kutimiza ndoto alizonazo.



    Maisha aliyokuwa akiishi Angel yalikuwa ya kifahari sana maana yeye alikuwa ni mwanafunzi pekee ambaye alipata bahati ya kulelewa na kuishi kwa mmiliki wa chuo cha Stanford, Madam Caroline.Wanafunzi wengi aliokuwa anasoma nao walitokea kumpenda sana Angel maana alikuwa ni mwanafunzi mwenye tabia ya kupenda kushirikiana na kila mtu hususani katika suala la kimasomo.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Upande wa Beatrice, yeye alijikuta akianza kumuonea wivu Angel kutokana na maisha aliyokiwa anayaishi na wivu wake ulipitiliza mpaka ndani yake akawa na chuki dhidi ya Angel.

    "Mimi naamini kufeli mitihani ni moja ya hatua ambayo inatufanya sisi wanafunzi tuweze kujitafakari na kugundua tulipokosea hivyo Dada Beatrice huna haja ya kuhuzunika, zaidi kwasasani wakati unaotakiwa urekebishe pale palipo na ufa ili ufanye vizuri katika fursa hii nyingine uliyoipata." Yalikuwa ni maneno kutoka kwa Angel akimueleza Beatrice baada ya Beatrice kufanya vibaya katika mitihani yake kwa awamu ya pili mfululizo na kushindwa kujiunga katika kozi kubwa za pale chuoni japo chuo ilimpa fursa nyingine ya kurudia mtihani kwa mwaka mwingine tena.

    "Unayonieleza yote ni ya kweli Angel ila nadhani nami ningekuwa mtoto wa bosi kama wewe, nahisi nigefanya vizuri tu." Alizungumza Beatrice kwa hasira na kwa lengo la kumkebehi Angel.

    "Hapana dada Beatrice, mimi nadhani haijalishi mtu anatokea katika ya familia ya hadhi gani, kinachotakiwa ni kujitahidi katika kusoma maana ufahari wa mali ni tofauti sana na ufahari wa kichwani."

    "Heri yako wewe uliobarikiwa kuwa na fahari zote hizo mbili na unaefaulu kila siku maana mwenzetu wewe ni mtoto wa mkuu wa chuo, acha sisi walala hoi na tusiokua na fahari yoyote tuendelee kufeli." Alizungumza Beatrice na kumueleza Angel huku akiinuka alipoketi na kuondoka.

    Kauli hii aliyoitoa Beatrice ilimfanya Angel ajisikie vibaya mno moyoni mwake maana aliweza kugundua kumbe Beatrice ana chuki kubwa dhidi yake.



    "' Hivi mume wangu ungependa mtoto wetu atakayezaliwa tumpatie jina gani ikiwa kama atakuwa wa kike au wa kiume"'

    "'Mmh!, mimi naomba kama atakuwa kike tumpatie jina la Angel ili amrithi marehemu bibi yangu na pia kama atakuwa wa kiume, basi tumpatie jina la Andrew ili amrithi marehemu baba yangu."

    "'Sawa lakini!..Brian mume wangu!, angalia linakuja ilo!, Brianiiii..!!?"' Ilikuwa ni ndoto ambayo ilimjia Janet wakati akiwa amjipumzisha nyakati zile za jioni na ikimkumbusha tukio la ajali ambayo aliipata akiwa pamoja na marehemu mume wake.

    Kutokana na ndoto aliyokuwa anaiota, japokuwa bado alikuwa usingizini lakini machozi yakawa yanamtoka huku akitikisika huku na kule pale kitandani alipolala mpaka wahudumu waliokuwa karibu yake wakawa wanashangazwa na hali ile.Wakati akiendelea kuhangaika huku mdomo wake ukionekana kama unahitaji kusema neno, mara ikasikika sauti kutoka kinywani mwake ikiita jina la Brian kwa nguvu sana.



    Ni baada ya kupita takribani miaka kumi sasa tangu aweze kupoteza sauti yake lakini leo hii kwa mara nyingine iliweza kusikika, tena ikitamka na kuita jina la marehemu mume wake.

    Jambo lile lilimfanya kila mmoja aliyekuwepo eneo lile kushangaa sana maana walimtambua Janet siku zote ni mtu asiyeweza kuongea wala kutoa kauli yoyote ile kutokana na matatizo aliyoyapata lakini iliyosikika, ilikuwa ni sauti yake halisi kabisa.



    Baada ya daktari kufika na kuweza kufanya vipimo vya awali, aliweza kugundua zile sehemu za mwili ambazo awali mzunguko wa damu ulikuwa haufiki, sasa zilianza kufikiwa na damu na ndio maana baadhi ya viungo vilivyokuwa dhaifu vilianza kufanya kazi.Baada ya kuligundua lile, dakatari akaamuru Janet achukuliwe na kukimbizwa katika chumba cha mahabara haraka ili wakaweze kumfanyia vipimo zaidi.



    Ikiwa bado ni nyakati za jioni, Nelson akaamua kutoka nyumbani ili aelekee kwenda kumuona Janet katika hospitali aliyoifadhiwa.Kwakua alishaanza kumtilia mashaka muda mrefu, siku hii mama Beatrice nae akawa anamvizia mume wake atoke tu pale nyumbani ili aweze kumfatilia maana alimuhisi pengine anajua sehemu alipo Janet.

    Bila kutambua mkewe yupo nyuma yake akimfuatilia, Nelson alizidi kuongeza mwendo wa gari yake ili aweze kuwahi safari yake anayoenda.Baada ya muda mchache, Nelson akaweza kufika mpaka hospitali aliyoifadhiwa Janet, akapaki gari yake vizuri na kuingia ndani.

    Akiwa ameipaka gari yake kwa mbali kidogo kutoka katika hospitali, Mama Beatrice aliweza kuishudia vizuri sehemu ile aliyofika mume wake na moja kwa moja akili yake ikamtuma kuwa yawezekana pale ndipk alipohifadhiwa Janet.Baada ya kufanikiwa kuligundua lile, Janet akageuza gari yake na kurudi nyumbani.



    Alipofika ndani, Nelson alishangaa baada ya kutomkuta wala kumuona Janet katika chumba alichokuwa amehifadhiwa, wasiwasi ulianza kumjaa na akatoka haraka na kuelekea sehemu ya mapokezi ili akaulize kuhusiana na mgonjwa wake.

    Habari aliyotaarifiwa pale mapokezi ilikuwa ni njema sana na ikamfanya Nelson ajisikie kuwa na raha mno na kumshkuru Mungu maana aliona mwanga wa mafanikio kwa shemeji yake umeanza kuonekana.

    Alipotoka pale hospitali, Nelson akaamua kupitia katika Baa iliyokuwa inatambulika kwa jina la THE DREAMS BAR na ambayo ilikua karibu na ufukwe wa bahari ili aweze kupooza koo kutokana na mihangaiko ya kutwa nzima.

    Akiwa amejituliza peke yake katika meza aliyoketi na akiendelea kunywa kinywaji chake alicholetewa baada ya kuagiza huku macho yake akiwa ameyaelekeza kutazama kupwa na kujaa kwa maji katika bahari, mara anafika mtu mmoja katika meza yake na kumsalimu Nelson na kuketi katika kiti ambacho kwa muda ule kilikuwa hakikukaliwa na mtu.Nelson akamkaribisha yule mtu aliyejisogeza pale mezani kwake huku akihisi amepata mtu wa kuweza kuzungumza nae na kubadilishana mawazo, bila kutambua lipo jambo lililomfanya yule mtu afike pale.

    "Karibu kaka, heri umefika katika meza hii angalau tubadilishane mawazo kidogo maana muda mrefu nipo mwenyewe tu hapa." Aliongea Nelson.

    "Asante kaka ila nadhani sio rahisi sana wewe kuweza kunifahamu mimi, lakini mimi nakufahamu vilivyo." Alizungumza yule mtu na kumeeleza Nelson.Nelson alishangaa sana maana alishindwa kuelewa kwanini mtu asiyeweza kumtambua anamueleza maneno kama yale.

    "Unanifahamu kivipi kaka mbona mimi sikutambui!?"

    "Natambua unaitwa Nelson na una mke na mtoto mmoja anayeitwa Beatrice ambaye kwasasa yupo katika chuo cha Stanford kilichopo Marekani kwa ajili ya kimasomo." Aliongea yule mtu na kuzidi kumshangaza Nelson.

    Akili ya haraka nelsona akahisi yawezekana mtu aliye naye pale akawa ni mpelelezi maana alishindwa kuelewa amewezaje kumtambua yeye pamoja na mambo yake wakati yeye hamtambui na ile ndio mara yake ya kwanza kumuona.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Usiwe na shaka yoyote ile Nelson, mimi naitwa Dk.Steven Dawson kutoka katika hospitali ya KITUL, hii ni hospitali ambayo awali marehemu Dk.Anthony alikuwa anafanyia kazi hivyo mimi na yeye tulikuwa sambamba.nimejisogeza hapa kwa lengo la kukujulisha jambo ambalo limenifanya siku zote niishi nikiwa sina amani ndani ya moyo wangu na hii yote ilitokana na mkeo." Alizungumza yule mtu ambaye alijitambulisha kwa jina la Dk Steven na kuhitaji kumueleza kitu Nelson.

    Nelson alipata wasiwasi sana moyoni mwake na kujiuliza ni kitu gani hicho anachohitaji kuambiwa na Dk.Steven ambacho kinahusiana na mke wake.

    "Mke wangu tena!, nieleze ni jambo gani hilo linalomuhusu mke wangu!?" Aliuliza Nelson kwa shauku kubwa ya kutaka kujua.

    "Mke wako alisababidha nidhulumu haki ya mtu asiye na hatia yoyote, nafasi aliyokwenda kusoma binti yako nje ya nchi haikuwa ya kwake bali ilikuwa ni nafasi ya Angel, mtoto ambaye alilelewa na na rafiki yangu marehemu Dk.Anthony." Aliongea Dk.Steven na kuuweka ukweli wake bayana mbele ya Nelson.

    Dk.Steven hakuishia kutoa maelezo yake kwa kuzungumza tu bali akatoa baadhi ya karatasi za fomu mbalimbali ambazo zilikuwa zinaonesha jinsi marehemu Dk.Anthony alivyokua anafanya mawasiliano na watu mbalimbali kutoka chuo cha Stanford wakati akimtafutia Angel nafasi ya udhamini wa kimasomo.

    Nelson alishtuka na kushangazwa sana baada ya kuelezwa yale, akajaribu kujumuisha baadhi ya matukio yalikuwepo wakati wa kukamilisha udhamini wa Beatrice na hasa tukio lile la yeye kupewa fomu aijaze kama mjomba na sio baba mzazi wa Beatrice, ndipo anapogundua yote yale anayoelezwa na Dk.Steven yawezekana ni ukweli mtupu.



    "Katika maisha Angel, jua si kila mmoja atafurahia mafanikio yako maana binadamu wote hatupo sawa.Binafsi mimi nimepitia changamoto nyingi sana mpaka kufikia hapa nilipo lakini tumaini langu huwa linabaki kwa Mungu kwasababu yeye pekee ndiye anayeweza kunisimamia na kunipigania." Japo sio kwa kiswahili nyoofu sana, aliongea Madam Caroline na kumueleza Angel wakati wakiwa katika maongezi ya kawaida nyumbani.

    "Hata mimi Madam naamini katika hayo unayoyasema, lakini naweza nikakuuliza swali?"

    "Bila shaka Angel, niulize tu."

    "Uliwezaje kuupata utajiri wote huu ulionao wakati huna mume wala mtoto mpaka hivi sasa?." Aliuliza Angel na kumfanya Madam Caroline aachie tabasamu kabla ya kumjibu.

    "Umeuliza swali zuri Angel, ila naomba utambue sio mpaka uwe na mwanaume au mtoto ndio uweze kukamilisha malengo yako zaidi wewe weka jitihada pamoja na bidii yako katika yale uyafanyayo au uliyoadhimia kuyafanya na pia usithubutu hata siku moja ukaruhusu hata akatokea mtu na kukusimamisha katika njia yako ya kutafuta mwanga wa mafanikio.Lakini kwasababu umehitaji kujua, basi ngoja nikusimulie kidogo jinsi nilivyoweza kukamilisha ndoto zangu mpaka nimefikia hapa nilipo sasa." Alizungumza Madam Caroline na kuzidi kumueleza Angel maneno ya kumsaidia kuweza kutanua uwezo wake wa kufikiri, pia alihitaji kumsimulia kwa ufupi historia ya maisha yake na mpaka anaweza kuwa tajiri namna ile.



    "Katika maisha yangu, mimi sikubahatika kulelewa na wazazi wangu wote wawili maana walifariki baada ya kupata ajali gari wakati walipokwenda kuhudhuria harusi ya rafiki yao.Kipindi hicho mimi nilikuwa nina umri wa miaka saba.Baada ya Mama pamoja Baba kufariki, shangazi yangu mmoja ambaye alizaliwa pamoja na baba, akanichukua mimi na kuhitaji kunilea lakini kumbe lengo lake halikuwa kunilea mimi bali alikuwa akihitaji kuchukua mali zote za marehemu baba yangu.Mara baada ya kunichukua mimi, aliweza kufanikisha lengo lake na niliishi maisha ya tabu sana nyumbani kwake huku akinipa mateso makali na kufikia hatua mpaka akahitaji kuniua.Alipofikia hatua hiyo, ndipo nilipoamua kutoroka nyumbani kwake na kwenda kuishi mtaani kama watoto wengine waliokosa wazazi au walezi." Alizungumza Madam Caroline na kumueleza Angel.Machozi yalikuwa yanamtoka kwa wingi mno hivyo kabla ya kuendelea kuongea, Madam Caroline akanyamaza kidogo na kuchukua kitambaa chake kwa ajili ya kufuta machozi yale yaliyokuwa yanamtoka.

    "Pole sana Madam kwa yote hayo uliyopitia, lakini uliwezaje kuishi mtaani bila ya kuwa na mlezi wala mtu yoyote wa kuweza kukusaidia!?" Alizungumza Angel na kuuliza kwa shauku kubwa ya kutaka kujua.

    "Nikiwa mtaani, ndipo alipotokea mzee mmoja ambaye alikuwa kipofu, akanichukua na kunilea.Alinianzisha shule na kunisaidia mambo mengi mpaka nafikia umri wa kuanza kujitegemea mimi mwenyewe.Kutokana na yale aliyonifanyia yule mzee, ndio maana nami niliamua kuanzisha chuo hichi ili niwasaidie watoto wote wenye bidii ya kutafuta mafanikio." Alizungumza Madam Caroline na kuzidi kumueleza Angel.

    Historia fupi ile aliyozungumza Madam Caroline kuhusiana na maisha aliyoyapitia, ilimgusa sana Angel na aliona kumbe sio yeye pekee yake aliyeweza kupitia mateso na maswahibu makari kutoka kwa mama wa rafiki yake ambaye yeye alimchukulia kama Shangazi yake.

    Pia siku zote Angel hakuchoka kumkumbuka na kumuombea Janet, ambaye yeye binafsi moyoni mwake alimchukulia kama mama yake japo alikuwa hatambui ndiye mama yake halisi.



    Nelson alirudi nyumbani akiwa tofauti sana siku hii maana kila alipokumbuka maneno aliyoelezwa na Dk.Steven, mawazo yalizidi kumjaa sana na kumuona mke wake zaidi ya Shetani kwa yale aliyoyafanya.

    "Mbona leo hivyo, muda wote kazi kujisonya tu!, ulipotoka kwema huko!?" Aliongea Mama Beatrice na kumuuliza Nelson baada ya kumuona yupo tafauti kidogo siku hii.Nelson hakuweza kujibu chochote maana kwa wakati huo alikuwa amejawa na hasira mno dhidi ya mke wake.

    "Si naongea na wewe Baba B, au pengine huko ulipoenda hujamkuta huyo ulienda kumuona..!!?"

    "Nyamazaaa.!!, mwanamke uliyojawa na ushetani wee!, hivi unafikiri ni adhabu gani utakayostahili kwa unyama huu unaoendelea kuufanya!?" Alizungumza Nelson kwa sauti kali tena yenye kujaa hasira ndani yake.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Mbona sikuelewi Nelson!, kitu gani ulichokula leo!?"

    "Kwanini uliamua kumkatili Angel katika haki yake na kumpa binti yangu Beatrice mzigo wa dhambi usiomuhusu!?" Aliongea Nelson kwa hasira mno.

    Baada ya kugundua Nelson ameshatambua kila kitu juu ya yale aliyoyafanya katika ufadhili wa kimasomo alioupata Beatrice, Jesca aliangua kicheko cha nguvu huku akimpa pole mume wake kwa kushindwa kulitambua lile mapema.

    Kicheko kile cha Jesca au mama Beatrice kilimfanya Nelson apandwe na hasira mno, akainua mkono wake wa kulia na kumshushia kofi la nguvu mkewe mpaka Mama Beatrice akaanguka chini.

    "Nelson!, leo hii unathubutu kunyanyua mkono wako na kunipiga!?" Aliongea mama Beatrice huku akiwa pale chini alipoangukia.Nelson hakuweza kumjibu chochote zaidi akaamu kutoka nje na kuondoka kwa hasira.



    Ikiwa ni siku nyingine tulivu, siku hii mama Beatrice akaamua kufunga safari na kuelekea hadi katika hospitali ambayo aliweza kumshuhudia mume wake siku iliyopita akiingia.Baada ya kufika hospitalini, akaelekea sehemu ya mapokezi na kutoa maelezo ya kujitosheleza, kisha wahudumu wa pale mapokezi wakamuelekeza chumba anachopatikana Janet.



    Akiwa njiani kurejea nyumbani baada ya kutoka katika shughuli zake, mara Nelson anapokea ujumbe katika simu yake kutoka kwa namba asiyoifahamu ambao ulimshtua sana.

    "'Habari kaka Nelson, naomba nenda hospitali haraka, Janet yupo kwenye matatizo kwa sasa."' Ni ujumbe ambao uliingia katika simu ya Nelson.

    Baada ya kuweza kuusoma ujumbe huu, Nelson akaamua kupiga namba ile ili aweze kuongea na mtu aliyemtumia taarifa ile lakini namba ile ilikuwa haipatikani.Hakuhitaji kupoteza muda Nelson, akageuza gari yake haraka na kuanza safari ya kuelekea katika hospitali aliyoifadhiwa Janet.



    Akiwa amejipumzisha katika chumba chake baada ya kutoka katika chumba maalumu cha matibabu na akiwa hana ili wala lile Janet, mara anahisi kuingia kwa mtu pale chumbani kwake.Akili ya haraka akahisi pengie anayefika pale kwa nyakati zile atakuwa ni shemeji yake maana Nelson hupenda kuja kumtembelea nyakati kama zile.Alipotupa macho yake na kutazama vizuri katika mlango wa kuingilia katika chumba chake , Janet alishtuka na kushangaa sana kwa kile achokuwa anakishuhudia.

    Janet alijivuta na kuketi vizuri katika kitanda huku akishindwa kuamini kama ni kweli anayemuona mahali pale ni Jesca ambaye ni dada wa marehemu mume wake.Kila alipozidi kutazama, macho yake yalizidi kumthibitishia kuwa anayemshuhudi pale ni wifi yake.

    "Janet!!, hakika kweli milima haikutani ila binadamu tunakutana, kumbe ni kweli wewe mgumba bado upo hai!?" Alizungumza Jesca kwa mshangao mkubwa baada ya kufika karibu na sehemu alipo Janet.

    Janet hakuweza kujibu chochote kile maana alibaki ameduwaa tu huku kichwani kwake akijiuliza Jesca amewezaje kufika mahali pale.

    Jesca aliangua kicheko cha nguvu maana bado alikuwa haamini kama kweli leo ameweza kumuona wifi yake ambaye ni muda mrefu sasa umepita akiwa anahangaika kumtafuta ili amuangamize.

    "Hisia zangu siku zote zilinieleza kuwa bado upo hai na niliamini lazima Ipo Siku Tu itafika na nitaweza kukukamata, haya nieleze ukingo wa mbio zako uko wapi sasa!?, naongea na wewe kiziwi usiyetembea wala kusikia!" Alizungumza Jesca kwa kiburi kikubwa na kuangua kicheko cha nguvu huku akimuacha Janet akibaki kumtazama tu pale alipoketi.

    Wakati akiendelea kuongea maneno yake ya kujigamba na kashfa, mara Jesca alipoangaza macho yake kutazama huku na kule pale ndani, akaweza kuziona picha mbili ambazo zilimshtua sana zikiwa zimewekwa kwenye meza iliyo karibu na kitanda cha Janet.Picha ya kwanza ilikuwa ikimuonesha Jesca akiwa pamoja na marehemu mume wake na nyingine ilikuwa ni picha ya Angel.Mama Beatrice akasogea katika meza na kuzichukua picha zile huku akimuuliza Janet picha zile zimefikaje mahali pale.

    "Nakuuliza picha hizi umezitoa wapi!?" Aliuliza mama Beatrice lakini Janet alibaki kimya huku akimtizama.

    "Nakuuliza na hii picha ya huyu chokoraa imefikaje hapa!?" Aliuliza Mama Beatrice kwa hasira na baada ya kuona hakuna jibu lolote analojibiwa, akachukua ile picha ya Angel na kuipigiza chini kwa hasira mpaka kioo cha fremu yake kilivunjika.

    Kitendo kile kilimfanya Janet apate hasira mno na bila kutarajia, akasimama pale alipoketi na kumuwasha kibao mama Beatrice.

    "Mtoto wangu si chokoraa, Angel ni mwanangu aliyetoka katika tumbo langu." Alizungumza Janet kwa hasira mno.

    Wakati tukio hili likitokea, Nelson nae ndio alikuwa anawasili mahali pale lakini alijikuta akisimama ghafla baada ya kumshuhudia Janet akiwa amesimama mwenyewe na kuweza kuzungumza



    "Umenifanya maisha yangu yawe ya tabu kwa kipindi kirefu sasa, na ukaona haitoshi ukampa binti yangu mateso na kumfanya aishi maisha ya shida katika nyumba aliyojenga baba pamoja na mimi mama yake, lakini sasa ninaweza kutembea na sauti yangu ambayo ilipotea kwa ajili yako, Mungu ameamua kuniregeshea na lazima yale yote uliyoyafanya yatakurudia." Alizungumza Janet kwa hasira mno .

    Jesca yeye alibaki ameduwaa tu maana hakutarajia kama Janet anaweza kusimama na kuongea namna ili kwakuwa alikuwa akifikiri kuwa Janet ni bado dhaifu kama alivyokuwa awali.

    Sio Jesca pekee aliyekuwa ameshangazwa na lile, Nelson ndio alikuwa ameshangazwa sana na jambo lile maana kwa macho yake mawili ameweza kumshuhudia Janet akiweza kusimama mwenyewe, kutembea pamoja na kuongea.

    "Shemeji!, kumbe umeshapona kabisa!?" Nelson alimuuliza Janet kwa mshangao.

    "Mimi nakushukuru tu kwa msaada wako mkubwa ulionipatia shemeji ila kwa aliyonifanyia huyu mke wako, hakika siwezi kumsamehe kabisa na lazima nimrudishie maumivu yote niliyoteseka nayo kwa kipindi kirefu." CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Inamaana wee mchawi siku zote ulikuwa unaigiza ni mgonjwa kumbe ni mzima na unaweza kutembea kabisa!, basi wewe lazima ndio utakuwa umehusika na kifo cha kaka yangu." Aliongea Jesca kwa ajili ya kujikosha, nae Janet hakuhitaji kumchelewesha, akainua mkono wake na kumuwasha kibao kingine cha pili.Jesca naye akahitaji kuregesha kofi lile kwa Janet, ndipo Nelson alipoingilia kati na akamshika mkewe kwa nguvu na kumtoa pale ndani.

    Baada ya Nelson pamoja na mkewe kutoka nje, Janet akainama chini na kuikota picha ya binti yake kisha akaifuta na kuiweka vizuri huku moyoni mwake akijiapiza lazima amuweke sehemu mbaya Jesca kutokana na yale aliyomfanyia.



    Licha ya kupata nafasi ya upendeleo ili aweze kurudia mtihani kwa mara ya mwisho na kama atafeli kwa mara nyingine tena ndipo aregeshwe nchini kwao, Beatrice alijikuta akilisahau kabisa jukumu lililomfanya awepo pale zaidi muda mwingi aliutumia kutoka na wanaume mbalimbali wa pale chuoni na kwenda kufanya starehe mbalimbali.

    Jambo lile lilikuwa linamgusa sana Angel na alikuwa akimuhurumia sana rafiki yake na siku zote hakuchoka kumshauri aachane na yale anayoyafanya ili wajikite kwenye masomo maana kwasasa wote walikuwa darasa moja japo Beatrice alikuwa wa kwanza kufika pale chuoni.

    "Unajua hapa tulipo tupo ugenini dada Beatrice, mimi nakuomba achana na habari za wanaume ili tusome kwanza maana kumbuka hii ni nafasi ya mwisho kwako ambayo umepewa kurudia mtihani." Alizungumza Angel kwa upole na kumueleza Beatrice.

    "Hivi mbona wewe mtoto wa mkuu wa chuo una kidomodomo sana, kila wakati kujifanya unanishauri tusome mbona mimi sikuingilii katika maisha yako!?"

    "Hapana dada Beatrice, chuo kizima hapa unasifika kuwa mwanaume yoyote anayehitaji mwanamke basi atakuja kwako na kutimiza haja zake, binafsi mimi naumia sana maana wewe zaidi ya ndugu kwangu na ndio maana nakushauri yaliyo mema."

    "Kama umechoka kukaa na mimi hapa naomba uondoke sasa hivi!, eti 'nakushauri mema', mbona umeshindwa kuwashauri baba yako na mama yako wasikutelekeze na ukategemea kuishi kwa misaada siku zote katika maisha yako!?" Alizungumza Beatrice kwa kejeli na kumueleza Angel.

    Maneno haya yalikuwa makali mno kwa Angel, alijikuta akinyamaza ghafla huku machozi yakimtoka maana Beatrice alienda kumtonesha kidonda ambacho kila siku kilikuwa kinamuumiza moyoni wake.

    "Tusileteane uchuro hapa, ngoja mimi niondoke zangu ila kama utajisikia kuniona, njoo kule chumbani kwa Ramsey utanikuta." Alizungumza Beatrice na kuondoka huku akiwa amemuacha Angel akiwa amezama katika Dunia ya mawazo kutokana na yale aliyomueleza.

    Baada ya kumshauri sana na kumtaka rafiki yake apite njia sahihi lakini kutokana matusi aliyokuwa anatukanwa na kudharauliwa, Angel aliamua kumuacha Beatrice kama alivyo na badala yake aliamua yeye mwenyewe binafsi kuwekeza nguvu zake zaidi katika kusoma huku akiyazingatia mafundisho ya walimu wake pamoja na maelekezo yote aliyokuwa anaelekezwa na Madam Caroline.

    Walipofikia kufanya mitihani ya kumaliza muhula wa kwanza(Semistar one), matokeo yaliporudi Angel alikuwa ameongoza chuo kizima katika kozi yake aliyokuwa anaisomea na Beatrice alikuwa ni mwanafunzi aliyefanya vibaya mno.Lakini licha ya yote hayo kutokea, Beatrice hakujali zaidi aliendelea kutanua starehe na wanaume mbalimbali pale chuoni.



    Ikiwa ni siku ya mapumziko chuoni, siku hii Madam Caroline akaamua kumchukua Angel na kumpeleka katika Hotel yake kubwa iliyokuwa inapatikana katikati ya jini la New York.Walipofika hotelini, Madam Caroline alimtambulisha Angel kwa wafanyakazi wake kuwa ni binti yake hivyo wafanyakazi wote wakampa heshima Angel kama mtoto wa bosi wao.Baada ya kumuonyesha Hotel ile kubwa ya kifahari, Madam Caroline akamchukua Angel na kumpeleka katika mashamba yake makubwa ambayo yalikuwa yanalimwa zao la mahindi.

    Matembezi yao yaliweza kuchukua siku nzima na kila sehemu waliyoenda, Angel aliweza kuheshimiwa kuwa ni mtoto Bosi hivyo hata yeye alijisikia fahari moyoni mwake maana hakutarajia hata siku moja kama ataweza kuwa na hadhi kubwa kama ile.



    Muda wote Jesca au Mama Beatrice alionekana ni mtu mwenye kujawa wasiwasi mno maana alihisi lazima Janet atamuangamiza, kutokana na unyama wote ule alioweza kumtendea.

    Upande wa Janet, baada ya afya yake kuweza kutengemaa vizuri, harakati za kuitafuta haki yake ziliendekea huku akijaribu kukutana na watu mbalimbali ili wamsaidie kukipata kile anachokihitaji.

    "Naweza nikakueleza dada hilo unalolihitaji lakini nahofia sana usalama wangu!" Alizungumza kijana mmoja aitwaye Cassian ambaye siku ya leo Janet aliweza kukutana nae akiamini kuna jambo anaweza kumsaidia.

    "Naomba unisaidie kaka yangu na mimi nitakulinda na wala sitoweza kukutaja kabisa, nieleze ukweli tu ili niweze kutimiza ushahidi ninaoutafuta." Alizungumza Janet na kuendelea kumuomba Cassian amueleze jambo analolihitaji.

    "Sawa dada, mimi nitakueleza ila naomba usije ukaiiunja hii ahadi yako." Alizungumza yule kijana aitwaye Cassian na kujiweka vizuri ili amueleze Janet juu ya yale anayoyafahamu.

    "Mimi ndio nilikuwa dereva wa ile lori iliyowagonga siku ile wewe ukiwa pamoja na marehemu mume wako na aliyepanga mpango wote ule wa kukuwadhuru, alikuwa ni Jesca na lengo lake lilikuwa ni kuwaua ninyi nyote wawili.Ushahidi wa hili ninao katika flash yangu maana siku anayotupa kazi ile niliweza kumrekodi."

    "Jesca!, na katika hili pia anahusika!?" Alizungumza Janet kwa mshangao maana hakutarajia kusikia kuwa Jesca ndiye aliyeandaa mpango wote wa yeye pamoja na marehemu mume wake kupata ajali.



    Baada ya kupata maelezo yote, wakaweza kukubaliana na kupanga siku ya kuweza kukutana ili Cassian aweze kumkabidhi ushahidi wote alionao.Janet alifurahi sana na kumshukuru Cassian kwa msaada ule mkubwa aliompatia.



    Maisha ya kusoma kwa Beatrice yalizidi kuwa magumu kwasababu starehe zilikuwa zimemtawala kupita kiasi.Pamoja na Angel kukaa nae kando na kumuacha na mambo yake kama alivyo, lakini Beatrice aliamua kuandaa mpango kabambe ili amkomeshe Angel na kumchafulia sifa pamoja na jina lake alilonalo pale chuoni.



    Yakiwa majira ya jioni na kama ilivyo kawaida yake, Angel hupenda kujisomea mpaka nyakati za jioni na kuweza kuyapitia yale yote aliyofundishwa.Kutokana alikuwa na mtihani wa kujipima siku inayofuata, siku hii Angel alijikuta akijisomea mpaka kufikia mida ya saa mbili usiku.Wanafunzi wote walikuwa wamesharudi katika mabweni yao hivyo alibaki peke yake darasani maana yeye alikuwa akija kuchukuliwa na gari kutoka madam Caroline, kwasababu nyumbani kwa madam Caroline ndipo alipokuwa anaishi.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Akiwa hana hili wala lile huku akiendelea kujisomea, mara anapotupa macho yake kutazama katika mlango wa kuingilia darasani ,akamuona mtu kama Beatrice akichunguli pale mlangoni.Angel alijaribu kupaza sauti na kumuita Beatrice ili aweze kuhakikisha kama amuonaye pale ni yeye lakini cha kushangaza mtu yule aliyekuwa akichungulia akatoka pale mlangoni na kukimbia.Angel akaamua kutoka na kwenda mpaka katika mlango ili aweze kumshuhudia mtu aliyemuhisi kuwepo pale, lakini cha kushangaza alipofika hakuweza kumuona mtu yoyote yule.Alipoona ukimya ndiyo umetawala eneo lile, Angel akarudi hadi sehemu aliyokuwa ameketi na kukusanya vitabu vyake kwa ajili ya kuviweka kwenye begi lake ili aweze kutoka nje maana alisikia honi ya gari nje na akahisi pengine itakuwa gari ya Madam Caroline imekuja kumchukua.

    Akiwa anaendelea kuweka vitabu vyake ndani ya begi lake, mara wanaingia wavulana watatu ambao wote walikuwa ni wanachuo wa palepale.Angel hakuwa na shaka yoyote ile alipowaona maana alihisi pengine na wao wamekuja kujisomea kwa ajili ya kujiandaa na mtihani watakaoufanya siku inayofuata.Lakini jambo la kushangaza, wavulana wale wakasogea hadi sehemu alipokuwa Angel na wakamkamata kwa nguvu na kumfunga kitambaa mdomoni ili Angel asiweze kutoa sauti yoyote ile, kisha wakamlaza chini kwa kutaka kumuingilia bila ridhaa yake.Wakati wale vijana wakiwa katika harakati hizo, kabla hawajafanya lolote mara wakasikia sauti ya ukali pale darasani ikiwataka waache mara moja jambo wanalohitaji kulifanya.





    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog