Search This Blog

Sunday, July 10, 2022

IPO SIKU TU - 5

 







    Simulizi : Ipo Siku Tu

    Sehemu Ya Tano (5)





    Baada ya kufanikiwa kuupata ushahidi wote kuhusiana na ajali aliyoipata yeye pamoja na marehemu mume wake, siku hii Janet alikutana na mtu mwingine ambaye alimtaarifu kuhusiana na ajali aliyoipata marehemu Dk.Anthony.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Kweli dada Janet mimi sina ukweli mwingine zaidi ya huo niliokueleza ila naamini utaweza kuyapata mengi zaidi kama utaweza kumpata Daktari mmoja ambaye alikuwa rafiki mkubwa wa marehemu Dk.Anthony, jina lake huyo Daktari anaitwa Dk.Steven Dawson." Alizungumza kijana aitwaye John, ambaye kwa kiasi fulani alikuwa anafahamu ukweli kuhusiana na ajali aliyoipata marehemu Dk.Anthony.

    Janet alishtuka sana baada ya kutajiwa jina la Dk.Steven maana daktari huyu alikua akimfahamu kwa kiasi kikubwa.

    "Unamaanisha nini kumtaja Dk.Steven!, ina maana nae anahusika katika mpango wa kumuua Dk.Anthony!?."

    "Sio mpango huo tu dada Janet bali yapo mambo mengi tu Dk.Steven ameyafanya, ikiwemo kufanya mabadilisho katika udhamini alioupata Angel na kumpatia nafasi ile ya kwenda kusoma nje mtoto wa Jesca wakati ule udhamini, marehemu Dk.Anthony ndiye alikuwa amemtafutia Angel." Alizungumza kijana John na kuzidi kueleza mengi juu anayoyafahamu.

    Suala hili la mtoto wake kudhulumiwa haki yake liliweza kumgusa mno Janet maana kwake ile habari ndio ilikuwa mara yake ya kwanza kuipata.



    Alipotoka kuonana na John, Janet akaona hana budi kumtafuta Dk.Steven ili apate maelezo mengine ya ziada ambayo yataweza kumsaidia katika ushahidi wake anaouandaa.

    Janet akafunga safari na kufika mpaka katika hospitali ya KITUL, hospitali ambayo alikaa pale kwa muda mrefu sana wakati akiwa bado mgonjwa na akiwa chini ya usimamizi wa marehemu Dk.Anthony.Alipofika hospitalini, kila mmoja ambaye alikuwa akimfahamu Janet, alikuwa akimshangaa maana kwasasa Janet alikuwa anatembea mwenyewe na kuongea vizuri kabisa.Baada ya kusalimiana na watu kadhaa, Janet akaulizia kama Dk.Steven atakuwepo ofisini kwa wakati ule lakini taarifa aliyoipata ni kwamba Dk.Steveni hayupo tena katika Dunia hii na alifariki baada ya kuvamiwa na majambazi nyumbani kwake.



    Upande wa Jesca, nae akawa anatambua kivyovyote vile lazima Janet atafanya kitu dhidi yake hivyo akaanza kujihami mapema na kuendelea na mpango wake wa kuhitaji kumuua Janet.



    "Mnataka kunichafulia chuo changu!, Mnathubutu kutaka kufanya mambo machafu kama haya!?, Wakamateni haraka!" Ilikuwa ni sauti ya Madam Caroline ambaye alionekana kuwa na hasira mno baada ya kukuta tukio lile pale darasani wakati amefika kwa ajili ya kumchukua Angel.

    Baada ya kuisikia sauti ile ya madam Caroline, Beatrice ambaye alikuwa amesimama nje, upande wa dirishani huku mikononi mwake akiwa amekamata kamera kwa ajili ya kupiga picha na kuchukua tukio zima ambalo angefanyiwa Angel, woga pamoja na hofu kubwa ilimjaa pale aliposimama mpaka akajikuta akidondosha ile kamera aliyoishika.Kishindo cha kuanguka kwa kamera kikaweza kusikika pale ndani na ikamfanya madam Caroline agundue upande wa nje kutakuwa na mtu hivyo akatoa amri kwa vijana wake alioambatana nao kufika pale waende mara moja kumkamata mtu huyo aliyehisiwa kuwepo.

    -





    Beatrice ilimbidi atoke eneo lile haraka na kuanza kukimbia kwa ajili ya kurudi katika bweni lake.Wakati akiwa katika kukimbia mara anatokea mtu na kumshika mkono kisha akamvuta chemba, sehemu ambayo ilikuwa imezungukwa na ukuta.Hii iliwafanya wale watu waliotumwa na Madam Caroline kushindwa kumuona mtu yoyote pale nje.

    Baada ya Madam Caroline kuweza kujitokeza na kumuokoa katika hatari ile ya kubakwa, Angel akamkimbilia Madam Caroline na kumkumbati huku akilia kwa huzuni mno.Madam Caroline naye akamtuliza binti yake lakini jambo lile lilitokea kumkera sana maana haikuwahi kutokea hata mara moja katika chuo chake kufanyika kitendo kama kile kichotaka kutokea kwa Angel.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Siku ya pili Madam Caroline akakutana na wanafunzi pamoja na walimu wote wa chuo cha Stanford na kukemea vikali tukio lililotaka kutokea siku iliyopita pale chuoni, na akawaeleza wale wanafunzi wote watatu waliotaka kumfanyia ubaya Angel, wamefikishwa mahakamani na watahukumiwa kwenda jela.

    Yakiwa majira ya mchana na baada ya kutoka katika kusanyiko lililoitwa na Madam Caroline, Beatrice alikuwa amejituliza huku akiwa sambamba pamoja mpenzi wake aitwaye Ramsey, ambaye alikuwa ni mwanachuo wa palepale na mwenye asili ya kizungu.

    "Nakushukuru sana mpenzi wangu Ramsey kwa msaada mkubwa ulionipatia siku ya jana maana kama sio wewe sijui na mimi ningekuwepo wapi kwasasa." Aliongea Beatrice na kumshukuru mpenzi wake ambaye alijitokeza usiku uliopita na kumsaidia wakati akiwa anafuatwa na watu waliokuwa wametumwa na madam Caroline.

    "Pia sambamba na hilo lipo jambo lingine ambalo nahitaji kukutaarifu Ramsey." Aliendelea kuongea Beatrice na kumueleza mpenzi wake, nae Ramsey akawa tayari kusikiliza analotaka kuambiwa.

    "Hapa nilipo, mimi ni mjamzito na huu ujauzito nilionao ni wa kwako." Beatrice alimtaarifu Ramsey kuhusiana na ujauzito alionao.

    Baada ya kutaarifiwa hili, Ramsey akahamaki kwa hasira na kuja juu mpaka akafikia kukataa ujauzito ule alionao Beatrice huku akimueleza aende akamtafute mwanaume aliyempa ujauzito ule ndio amueleze yale.Beatrice alijitahidi kumuelewesha Ramsey ili aweze kumuelewa, lakini Ramsey hakuweza kukubaliana na lile na badala yake akainuka na kuondoka huku akiwa amempa onyo kali Beatrice kuwa asije akathubutu kumfuata tena maana uhusiano wao umeishia pale.

    Beatrice alibaki akihuzunika na kulia sana kwakuwa hakutegemea kama Ramsey angeweza akamkataa na kuukana ujauzito alionao namna ile.

    Akiwa katika hali hiyo ya huzuni Beatrice mara anafika mwalimu mmoja wa pale chuoni na kumtaarifu kuwa anahitajika kufika katika ofisi za chuo haraka iwezekanavyo.Hii ilimfanya Beatrice apate wasiwasi mkubwa maana alihisi pengine katika yale yaliyotokea usiku uliopita, nae tayari atakuwa ameshagundulika kuwa anahusika.

    Alipofika ofisini, alikuta walimu kadhaa ambao wanahusika kuunda bodi ya chuo, akiwemo na Madam Caroline ndani yake, walikuwa wameketi na wakimngoja yeye kuweza kufika mahali pale.

    Bodi ya chuo iligundua katika ujio wa Beatrice pale chuoni, kulikuwa na udanganyifu ndani yake maana kuna baadhi ya taarifa zake zilikuwa zinatofautiana.Baada ya kufika, Beatrice akaonyeshwa sehemu ya kuketi ili kazi ya kumuhoji ianze.

    "Naomba tutajie majina yako yote matatu kwa usahihi." Alizungumza mkurugenzi wa ile bodi na kumuuliza Beatrice.

    Beatrice alikuwa na hofu sana maana bado alishindwa kutambua kwanini anaulizwa maswali yale.

    "Naitwa Beatrice Brian Andrew."

    "Una umri wa miaka mingapi?"

    "Nina miaka kumi na nane."

    "Mbona fomu zako hapa zinaonesha una umri wa miaka kumi na saba!?"

    "Mimi!..labda..a.u pengine walikosea katika kujaza!."

    "Kwa asilimia kubwa, taarifa za fomu zako zina utofauti mkubwa sana na zile fomu ambazo zilitumwa katika maombi ya wewe kuja kujiunga hapa, sasa naomba utueleze ukweli ili tukusaidie la sivyo lazima wewe pamoja na familia yako mshtakiwe katika hili." Alizungumza Madam Caroline na kumtisha kidogo Beatrice ili aweze kueleza ukweli juu ya ujio wake.

    Baada ya kusikia suala la kushtakiwa yeye pamoja na familia yake, Beatrice aliogopa sana, huku machozi yakimtoka akaamua kuweka ukweli wote bayana juu ya kilichotokea na vitu vyote alivyovifanya mama yake mpaka yeye anafikia kuupata ufadhili ule wa kimasomo.Kila mmoja aliyekuwepo pale alishangazwa sana na lile na mwisho bodi ya chuo, baada ya kujiridhisha na maelezo aliyoyatoa Beatrice, wakafikia maamuzi ya kumfuta kabisa Beatrice chuo na kutomtambua kama Mwanafunzi wao na watamuandalia utaratibu wa kuweza kumrudisha katika nchi aliyotoka.

    Hili lilikuwa ni pigo kubwa sana kwa Beatrice na akashindwa kuamini kama pale ndio mwisho wake wa kuendelea kusoma pale chuoni na ukizingatia pale alipo tayari ameshika ujauzito.Alijitahidi kulia na kuomba apewe nafasi ya kuendelea na masomo lakini ombi lake lilikuwa ni gumu kukubaliwa kwasababu maamuzi yalikuwa yameshatolewa.

    Beatrice alitoka pale ofisini huku akiwa amechoka kila idara maana mawazo yalikuwa mengi sana kichwani mwake hususani kutokana na yale yaliyotokea.Baada ya kuhuzunika na kulia sana, ndipo anapopata akili ya kumfuata mtu mmoja ambaye alihisi ataweza kumsaidia katika lile.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nyakati zote Angel alikuwa anafikiria sana juu ya tukio ambalo lilitaka kutokea kwake na alizidi kuumia maana alishindwa kuamini kama ni kweli Beatrice anaweza kumfanyia jambo kama lile.Angel alikuwa ameshatambua kila kitu kuwa Beatrice ndiye aliyeandaa mpango wote wa yeye kuweza kubakwa japo jambo lile halikutimia.Alimuona Beatrice ni zaidi ya mnyama na alijikuta akitokea kumchukui sana kutokana na lile alilotaka kumfanyia.

    Akiwa anaendelea kuyatafakari hayo Angel, mara anapotazama mbele anamuona Beatrice akija upande wake huku uso wake ukionekana kulowana na machozi.Beatrice alipofika karibu na Angel, akapiga magoti chini na kulia kwa uchungu.

    "Najua umeshatambua kila kitu Angel, ila naomba unisamehe mimi kwa yote yale yaliyotokea jana na pia lile alikuwa kusudio langu kukutendea vile." Alizungumza Beatrice na kujutia kosa lake mbele ya Angel lakini Angel hakuweza kumjibu chochote zaidi alibaki akimtazama tu maana muda huo alikuwa na hasira nae mno.

    "Naomba unisamehe Dada yangu na pia nisaidie katika hili lilonikuta maana mwenzako nimeshafukuzwa chuo na hapa nilipo tayari nina ujauzito." Aliendelea kuongea Beatrice kwa unyonge na kumueleza Angel.

    Aliposikia kauli kuwa tayari Beatrice pale alipo ni mjamzito, kauli ile ilimshtua sana Angel, japokuwa alikuwa na hasira dhidi ya Beatrice lakini akajitahidi kukaza roho na kumpa nafasi ya kumsikiliza Beatrice ili amueleze matatizo yaliyomsibu.

    Beatrice hakuweza kuficha lolote lile, akaamua kumueleza Angel kila kitu kilichotokea na hila zote alizozifanya mama yake mpaka anafanikiwa kuipata nafasi ile ya udhamini ambayo alistahili kuipata Angel.

    "Ina maana nafasi uliyoitumia kuja kusoma hapa kumbe ilikuwa ni ya kwangu!?"Aliuliza Angel kwa mshangao.

    "Ndio dada Angel, mimi sikupenda itokee vile ila ni mama yangu tu alinilazimisha."

    Angel alishindwa kujizuia, taratibu machozi yakaanza kumtoka hususani kila alipokumbuka maisha ya tabu aliyokuwa anayapitia nyumbani kwa mama Beatrice kumbe mpango wake wa kuja kusoma nje ulikuwa umeshafanikiwa.

    "Jambo hili tayari limeshagundulika hapa chuoni na mimi nimeshafutwa na kutotambulika kama ni mwanafunzi wa hapa.Nakuomba dada Angel unisaidie kuzungumza na Madam Caroline iki aweze kuniruhusu niendelee na chuo." Aliongea Beatrice kwa unyonge na kumuomba Angel aende akazungumze na madam Caroline ili aweze kumruhusu aendelee na masomo.





    Beatrice aliendelea kulia kwa huzuni na kuzidi kumuomba Angel amsaidie katika lile ili ata angalau apate nafasi ya kufanya mtihani ambao ulikuwa karibuni kufanyika kwa ajili ya kumaliza kozi ya awali anayoisomea.

    Pamoja na maumivu aliyokuwa nayo kwa wakati ule, lakini Angel alikuwa ni binti aliyejaliwa kuwa na moyo wa huruma sana hivyo alijikuta akianza kuingiwa na imani na kumuonea huruma Beatrice kwa jinsi alivyokuwa anamuona.

    "Sawa Dada Beatrice, mimi nitajaribu kuzungumza na Madam lakini nieleze jambo moja tu, je aliyekupa huo ujauzito umeshamtaarifu!?."

    "Ndio nimeshamtaarifu lakini Ramsey ameikataa mimba hii..!!, nitafanya nini sasa!?, ni heri hata ningeyasikiliza yale uliokuwa unanishauri!" Aliongea Beatrice na kuzidi kujutia kutokana na yale yote yaliyomsibu.



    Ilipofika nyakati za jioni, Angel aliporudi nyumbani akajaribu kuzungumza na Madam Caroline ili aweze kumsamehe Beatrice na amruhusu aendelee na masomo.Japo lilikuwa ni jambo gumu sana kuweza kukubaliana na lile lakini kwa jinsi alivyokuwa anampenda Angel, Madam Caroline akakubali kutoa msamaha na kumruhusu Beatrice aweze kuendelea na chuo.



    Nyumbani kwa Nelson, amani ilikosekana kabisa maana muda wote Mama Beatrice alikuwa akimshtumu mumewe kwanini alikuwa anaenda kinyume nae mpaka afikie kumtunza na kumsaidia adui yake mkubwa ambaye ni wifi yake.

    "Umenisaliti kwa kiasi kikubwa Nelson yani kumbe siku zote humu nilikuwa nalea Mtoto wa yule mbwa!? Lazima utalipa kwa hili!"

    "Kelele wewe mwanamke!, hivi unafikiri ni nafsi ngapi zitakulilia wewe!, mangapi mambo machafu ambayo umeshayafanya mpaka sasa!?, lazimu Mungu akuhukumu hasa kwa ulivyosababisha kifo cha Dk.Anthony, mtu ambaye alijitolea kuilea familia iliyokuwa inateseka kwasababu yako."

    "Nelson! Nelson!, unathubutu kuniita mimi ni muuaji! una ushahidi gani ulionao mpaka unihukumu mimi ni muuaji!?" Alizungumza Jesca na kufoka kwa hasiri baada ya Nelson kumueleza kuwa yeye ndiye aliyehusika kumuua Dk.Anthony.

    "Mimi hapa ushahidi ninao wa kukuonyesha wewe ndiye uliyemuua marehemu mume wangu, Dk.Anthony pamoja na Dk.Steven ambaye aliamua kueleza uchafu wako wote ulioutenda." Ilikuwa ni sauti ya Janet ambayo ilidakia mazungumzo yale na kujibu swali la Jesca alilokuwa anamuuliza mume wake.Janet alifika mahali pale kwa ajili ya kukamilisha jambo.

    "Wewe Shetani umefuata nini hapa nyumbani kwangu!?" Aliuliza Mama Beatrice huku akiwa amemgeukia Janet na kumtazama kwa hasira.

    Kumbe Janet ujio wake pale hakuwa amekuja peke yake, ghafla wakaingia maaskari pale ndani na kumuweka chini ya ulinzi Jesca.Maaskari wakamkamata Jesca na kuondoka nae.

    "Naomba unisamehe shemeji kwa hiki nilichokitenda lakini binafsi kwangu ni vigumu sana kumsamehe Jesca kwa yote yale aliyonitendea japokuwa ni wifi yangu." Alizungumza Janet na kumueleza Nelson mara baada ya maaskari kumchukua Jesca na kuondoka nae.

    "Huna haja ya kuniomba msamaha shemeji, upo sahihi kabisa kwa hichi unachokifanya.Japokuwa Mama Beatrice ni mke wangu halali kabisa lakini anastahili kukipata hichi alichokipata kutokana na yale yote aliyoyatenda.Ila nafikiri mimi ndio nastahili kusamehewa kwako maana najihisi nami ni mtuhumiwa mbele yako kwa kushindwa kukusaidi lolote lile mpaka unafikia kuyafanya haya ukiwa mwenyewe." Alizungumza Nelson kwa uchungu sana na kumueleza Janet au Mama Angel.

    Mama Angel akamtaka Nelson asiwe na shaka yoyote ile zaidi akamshukuru kwa msaada wote aliokuwa anampatia japo Nelson alikuwa akijiona nafsini mwake kuwa hajatenda msaada wowote kwa Janet mpaka kufikia pale alipo.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Kesi iliweza kufikishwa mahakamani na kupangiwa tarehe rasmi ya kuweza kusikilizwa na kama ushahidi utaweza kujitosheleza, Jesca ataweza kuhukumiwa kifungo anachostahili kutokana na yale yote aliyoyatenda.Na kipindi chote hicho wakati tarehe ya kusikilizwa kesi ile ikisubiliwa, Jesca alikuwa amewekwa na kuhifadhiwa Mahabusu.

    Kadri siku zilivyozidi kukatika, Jesca akiwa Mahabusu akaweza kupatwa na ugonjwa wa matatizo ya kiakili hivyo hata ilipotimia siku ya kusikilizwa kesi yake, mahakama ikaamuru kuisogeza mbele tarehe ya kuisikiliza kesi ile ili Jesca aweze kupatiwa matibabu mpaka atakapotengemaa kiakili na kurudi katika hali yake ya kawaida.Janet aliweza kuliafiki lile kutokana na hali aliyokuwa akimuona nayo Jesca zaidi yeye aliendelea kuutunza ushahidi wake vizuri.



    Licha ya kupata nafasi ya kuweza kuendelea na masomo, lakini Beatrice tayari alikuwa ameshachelewa kurudi katika mstari maana ni muda mchache sana ambao ulikuwa umebaki kabla ya kuanza mitihani ya kumaliza kozi yao ya awali.Baada ya kufanya mtihani na matokeo yalipotoka, Beatrice hakuweza kupata alama za kumuwezesha kuendelea na chuo na safari ya kurudi Tanzania tayari ilikuwa imeshawadia upande wake.Upande wa Angel yeye alifanya vizuri sana na kuweza kuongoza katika matokeo yale kwa mara nyingine tena.



    "Nafikiri tangu awali hii haikuwa bahati yangu, hakuna chochote nilichokivuna zaidi narudi nyumbani nikiwa na huu ujauzito ambao sielewi nitaanza vipi kuwaeleza wazazi wangu." Alizungumza Beatrice kwa unyonge wakati alipoenda kumuaga Angel maana siku inayofuata ndio ilikuwa siku ya kuanza safari yake ya kurudi nyumbani.

    "Hapana dada Beatrice, mimi naamini kila kitu huwepo kwa mpango wa Mungu hivyo kufeli katika mitihani haimaanishi umepoteza kila kitu, pengine Mungu amekuandikia njia nyingine ya mafanikio utakayoweza kupita." Yalikuwa ni maneno kutoka kinywani kwa Angel na aliyazungumza kwa ajili ya kumfariji na kumtia moyo Beatrice.

    "Asante Angel ila naomba unisamehe na uyasahau yote yale mabaya ambayo nilikutendea."

    "Usijali Dada Beatrice mimi nimeshasamehe yote yaliyopita.Pia naomba zawadi hii kamkabidhi Anko Nelson na yeye atajua sehemu ya kuipeleka." Alizungumza Angel huku akitoa mfuko uliokua na kitu ndani yake na kumkabidhi Beatrice.

    Baada ya kuzungumza machache, Angel aliweza kumuaga rafiki yake na kumtakia safari njema huku akimuomba amfikishie salamu zake nyingi kwa mjomba pamoja na shangazi yake.

    Beatrice alijawa na huzuni sana huku akijutia kwa kuichezea nafasi ile adimu aliyoipata.



    Siku inayofuta, alfajiri na mapema Beatrice akaianza safari ya kurudi nyumbani, huku taarifa za kurudi kwake zikiwa tayari zimeshatumwa nchini kwake.



    Yakiwa majira ya asubui, Nelson akiwa njiani kuelekea ofisini kwake mara anapigiwa simu na kutaarifiwa kuhusiana na ujio wa mtoto wake.Nelson alishangazwa sana na lile maana ujio wa Beatrice ulikuwa wa ghafla mno.



    Yalipofika majira ya saa sita na nusu usiku, Nelson akawasili uwanja wa Ndege wa mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa ajili ya kumpokea binti yake maana alishataarifiwa hadi muda atakaowasili.

    Baada ya kusubiri kwa muda kidogo, ndipo Nelson alipoweza kumuona binti yake akiwasili sehemu ya mapokezi.Kitendo cha kumuona baba yake Beatrice akashindwa kujizuia, akuanza kuangusha kilio.Nelson alimpokea binti yake kwa furaha na alihisi kilio kile cha binti yake pangine kinatokana na kutoonana nae kwa muda mrefu.

    Walipofika nyumbani, Beatrice alishangaa kufikia katika nyumba tofauti na ile waliokuwa wakiishi awali.Pia Beatrice alijiuliza sana maana tangu afike hakuweza kumuona mama yake.

    "Yuko wapi mama, mbona hakuja kunipokea na wala simuoni mahali hapa?" Aliuliza Beatrice mara baada tu ya kuingia pale ndani.

    "Mama yako kidogo ameenda kumuangalia rafiki yake mmoja ambaye ni mgonjwa sana, hivyo ameamua kulala huko ili aweze kumsaidia." Alijibu Nelson japo wote ulikuwa ni uongo lakini aliamua kufanya vile ili binti yake asitambue lolote kwa wakati ule.

    "Sawa, lakini kwasasa mbona mpo kwenye makazi mapya, vipi kuhusu ile nyumba yetu ya zamani mmeshaiuza!?"

    "Naomba upumzike Beatrice mengi zaidi tutaongea kesho." Nelson aliamua kumkatisha binti yake na kumtaka apumzike huku akimueleza mengi zaidi wataongea siku inayofuata.



    Ilipowadia siku ya pili, Nelson akaweza kupata wasaa mzuri wa kuweza kuzungumza na binti yake na kumuuliza kuhusiana na safari yake aliyorudi.Beatrice nae akaamua kumueleza kila kitu baba yake kuhusiana na yale yaliyojiri ila kubwa zaidi ambalo lilimshtua Nelson ni pale Beatrice alipomueleza na kumtaarifu kuwa pale alipo ni mjamzito.

    "Unasemaje Beatrice!, wewe ni mjamzito!?"

    "Ndio baba!"

    "Yuko wapi kwasasa baba huyo kiumbe na Je uliweza kumtaarifu hili!?"

    "Nimemuacha huko nilipotoka baba na pia nilipomueleza, aliukataa!." Beatrice alimueleza baba yake huku akilia kwa uchungu.

    Nelson aliumia sana na yale maana hakutegemea kama binti yake kile ndicho atakachokivuna kule alipoenda.Kwakuwa yalikuwa yameshatokea, Nelson hakuwa na namna yoyote ile ya kufanya zaidi alimtaka binti yake atulie.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Majira ya mchana yalipowadia, Nelson akaamua kumchukua Beatrice na kumpeleka hadi katika hospitali aliyekuwepo mama yake, maana kwa wakati ule Jesca alikuwa ametolewa mahabusu na kuhifadhiwa katika hospitali ya watu waliokua na matatizo ya kiakili, hii ilitokana na hali aliyokuwa nayo.Beatrice alishangaa sana kwa hali ambayo alimuona nayo mama yake, akamuuliza baba yake ni kipi kilichotokea mpaka mama yake afikie katika hali kama ile, Nelson nae akamueleza kila kitu binti yake juu ya yale yaliyotokea mpaka mama Beatrice afikie katika hali ile.

    Baada ya kutoka kumtembelea mke wake na kumrudisha Beatrice nyumbani, Nelson akafika nyumbani kwa Janet, ambapo kwasasa alirudi katika nyumba aliyokuwa akiishi pamoja na marehemu mume wake hapo awali.Nelson akamjulisha mama Angel kuhusiana na ujio wa binti yake pamoja na kumkabizi zawadi ambayo alikuja nayo Beatrice, na ndio ile zawadi ambayo Beatrice alikabiziwa na Angel amfikishie Anko Nelson.

    Mama Angel alifurahi sana kwa zawadi ile aliyoiandaa binti yake, zilikuwa ni picha mbalimbali alizopiga Angel kule aliko pamoja na zawadi ya cheni ambayo katika kidani chake kulikuwa na picha mbili, moja ikiwa ni picha yake na nyingine ni picha ya Angel.

    "'Natumaini huko uliko upo salama mama yangu, mimi naendelea vizuri huku ila nimekukumbuka sana mama na nitajitahidi siku moja nije kukukamilishia ahadi niliyokuahidi kuitimiza.Nakupenda sana mama yangu"' ulikuwa ni ujumbe ambao uliambatana kuja na ile zawadi.

    Mama Angel alifurahi sana baada ya kupokea zawadi ile na kumuombea mema binti yake kule aliko.



    **************************



    Siku, miezi na miaka ilizidi kukatika na Angel aliendelea kufanya vizuri katika masomo yake na alikuwa amebakisha miezi michache kabla ya kumaliza mwaka wake wa mwisho wa masomo katika kozi yake yake aliyokuwa anaisomea.

    Wakati akiwa amebakiza miezi miwili tu kabla ya kufanya mtihani wake wa mwisho na kuhitimu masomo yake, mara madam Caroline anaugua ghafla na kupata ugonjwa ambao unamfanya ashindwe kufanya shughuli yoyote lile.Madaktari bingwa walijitahidi na kujaribu kuutibu ugonjwa unaomsumbua, lakini kila siku hali ya Madam Caroline ilizidi kuwa mbaya.







    Ugonjwa aliopata ulizidi kumtafuna na hatimaye haikuchukua muda mrefu Madam Caroline akaweza kufariki Dunia.Lile lilikuwa ni pigo kubwa katika chuo cha Stanford na Duniani kwa ujumla maana Madam Caroline alikuwa akitambulika sehemu nyingi ulimwenguni kutokana na ukubwa wa chuo chake alichokuwa anakimiliki.

    Pigo kubwa zaidi lilikuwa upande wa Angel maana alishamzoe kwa kiasi kikubwa madam Caroline na kifo chake kilimfanya awe na wakati mgumu sana hususani akijiuliza, atawezaje kuishi pasipokuwa na Madam Caroline ambaye alikuwa akiishi nae tangu afike pale nchini Marekani.

    Taratibu za mazishi zikaandaliwa na hatimaye mwili wa marehemu madam Caroline ukaweza kupumzishwa katika makao yake ya milele.



    Baada ya mwili wa marehemu madam Caroline kuzikwa, Angel hakuwa na namna yoyote ile ya kufanya zaidi alijitahidi kuizoea hali ile ya kuwa mpweke maana aliendelea kuishi katika nyumba ya marehemu Madam Caroline.Ilikuwa ni ngumu kwake kuweza kufuta fikra za kuweza kumfikiria madam Caroline, lakini alijitahidi suala lile lisije likamuathiri katika masomo yake hivyo akawa makini mpaka akafikia kufanya mitihani yake na kuweza kuhitimu masomo yake.Matokeo yalipotoka, Angel alionekana kufanya vizuri na kufaulu katika kiwango cha juu.Baada ya kuhitimu masomo yake Angel akawa tayari kujiandaa kwa ajili ya kurudi Tanzania maana hakuwa na cha ziada alichokuwa amebakisha pale Marekani.

    Akiwa katika maandalizi ya safari yake mara Angel analetewa taarifa ya kutakiwa kufika katika mahakamu kuu nchini Marekani.Angel naye akaweza kutii agizo lile na alipofika katika mahakama, akashangaa kwa taarifa ambazo alikutana nazo.Kumbe marehemu Madam Caroline kabla ya kufa kwake, alimuandika Angel kuwa ndiye atakayekuwa mrithi wa mali zake kikiwemo chuo cha kikubwa cha Stanford, majumba ya kifahari, mashamba na vitu vingine vingi vya thamani.

    Serikali ya Marekani ilishindwa kumkabidhi mapema Angel mali zile kwasababu sheria ilikuwa haiwaruhusu maana kwa wakati Madam Caroline anafariki, Angel bado alikuwa ni mwanafunzi hivyo iliwalazimu wamngoje mpaka amalize masomo yake na ndipo wakamkabidhi rasmi urithi wake au mali zote zilizokuwa zinamilikiwa na Madam Caroline.

    Angel alijiona kama yupo ndotoni maana hakutegemea kama madam Caroline ataweza kumuandika yeye ndiye mrithi wa mali zake na kumuachia utajiri mkubwa kama ule.Furaha ilikuwa kubwa sana kwake mpaka akafikia kudondosha machozi mbele ya mahakama na akainua macho yake na kutazama juu huku akiahidi kutoweza kumsahau marehemu Madam Caroline kwa jambo lile kubwa alilomfanyia.



    ***********************CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Kutokana na matibabu aliyoweza kuyapata, afya ya Mama Beatrice ikaweza kuimalika na kupona kabisa ugonjwa uliokuwa unamsumbua.Baada ya kupona ugonjwa wake, Jesca akaregeshwa mahabusu kwa ajili ya kungojea siku ya kusikilizwa kesi yake katika tarehe iliyopangiwa.



    Ilipowadia siku ya kusikilizwa kesi yake aliyoifungua, siku hii Janet akakusanya na kuweka sawa ushahidi wake wote alionao ili aende kuthibitisha mbele ya mahakama juu ya mashtaka yanayomkabili mama Beatrice.

    Akiwa ndani ya nyumba yake na akiendelea kuweka ushahidi wake vizuri, mara anasikia honi ya gari nje ya nyumba.Janet akahisi pengine watu wa kumpeleka mahakamani watakuwa wamefika kumchukua hivyo akajiandaa haraka na kutoka nje.Alipofika nje alipigwa na butwaa kwa alichokishuhudia, alikuwa ni Angel huku akiwa ameambatana na walinzi wake maana kwasasa alikuwa akitambulika kwa jina la Madam Angel kutokana na utajiri mkubwa alionao.Alifika pale nyumbani kwa mama yake huku akiwa ameambatana sambamba na Anko Nelson pamoja na Beatrice.

    Mshangao mkubwa ulikuwa kwa Madam Angel maana leo hii alimkuta mama yake akiwa tofauti kabisa na alivyomuacha awali wakati akielekea masomoni maana kwasasa Janet alikuwa anaongea pamoja na kutembea.

    "Angel binti yangu!"

    "Mama!, kumbe ni kweli umepona!?" Aliuliza Madam Angel kwa mshangao maana alishindwa kumuamini Anko Nelson alipomtaarifu kuwa kama mama yake amepona, lakini alipomshuhudia mwenyewe ndipo alipoweza kuyaamini yale aliyoambiwa.Madam Angel akamkimbilia mama yake na kumkumbatia kwa furaha.

    Madam Angel alifurahi sana kwa kuweza kumuona mama yake kwa mara nyingine tena, wakaingia ndani ili waweze kuongea mengi zaidi.Madam Angel akamsimulia kila kitu mama yake juu ya yale yaliyotokea na mpaka anafikia kuwa na utajiri namna ile.Mama nae alifurahi sana na kumshukuru Mungu kwa yote yale aliyoyapata binti yake.



    Beatrice nae akatumia fursa ile kuweza kumuombea msamaha mama yake ili Mama Angel abadilishe maamuzi aliyonayo na kumsamehe mama yake.

    "Najua mama yangu amekukosea sana na ametenda mengi maovu, lakini naomba kutumia fursa hii shangazi kumuombea msamaha mama yangu mbele yako.Msamehe mama na wala usiupelekee mahakamani huo ushahidi ulionao."

    "Hapana!, maumivu niliyoyapata kwa kipindi chote kwasababu ya mama yako wewe huwezi kuyajua! ngoja na mimi kwanza nimuoneshe Dunia ilivyo." Alizungumza Janet au mama Angel kwa msisitizo mno.

    Beatrice ambaye kwa wakati huu alikuwa na mtoto mdogo wa kiume, licha ya maneno yale aliyozungumza mama Angel lakini hakuchoka kuzidi kumbembeleza na kumuombea msamaha mama yake mbele ya mama Angel.

    Jinsi alivyokuwa analia na kuhuzunika Beatrice, Madam Angel alimuonea huruma sana na akaamua kutia neno na kumuomba mama yake akubali ombi la Beatrice na aweze kumsamehe shangazi yake.

    "Mama, Binadamu tumeumbwa kusamehe na kusahau yaliyopita, pamoja na yote aliyoyafanya shangazi Jesca lakini naomba umsamehe tu kwasababu naamini hakuna binadamu aliye mkamilifu na kupitia wakati huu mgumu alioupitia lazima atakuwa ameshajifunza jinsi Dunia ya wenye shida ilivyo." Aliongea madam Angel na kumueleza mama yake.

    Maneno ya Madam Angel yalifanya moyo wa mama kulegea japo alikuwa akihisi kupata maumivu makali moyoni mwake hasa zaidi kila alipokumbuka ubaya wote aliotendewa na Mama Beatrice, lakini yote kwa yote akakubali kumsamehe wifi yake na akawa tayari kwenda kuifuta kesi ile.

    Baada ya kila kitu kuisha na Janet kuamua kuifuta kesi aliyokuwa amemfungulia wifi yake, nae Mama Beatrice baada ya kuachiwa huru, akafika nyumbani kwa mama Angel na kujutia makosa yake yote na kumshukuru sana kwa kukubali kumsamehe.

    "Asante sana wifi yangu, hakika sikutegemea kwa yote niliyokutendea kama ungeniacha huru nmna hii."

    "Usijali Mama Beatrice, mimi nimeshasamehe yote yaliyopita na unaetakiwa kumshukuru zaidi ni binti yangu Angel maana yeye ndiye aliyesababisha mpaka wewe unakua huru."

    "Angel!, yuko wapi shangazi yangu nae nimuombe msamaha!?" Alizungumza mama Beatrice na kuhitaji kumuona Angel ili aweze kumuomba msamaha kwa mateso yote yale aliyompatia.

    Madam Angel naye akafika mahali pale nakuzungumza na shangazi yake pamoja na kukubali kumsamehe maana mama yake alishamueleza kila kitu kuwa yeye ndiye mama yake mzazi na mama Beatrice alikuwa ni shangazi yake kabisa, aliyezaliwa tumbo moja na marehemu baba yake.



    Madam Angel alishakuwa mtu kubwa sana duniani hivyo hata makazi yake yalikuwa nchini Marekani kutokana na miradi mingi aliyokuwa anaisimamia ambayo aliachiwa na marehemu Madam Caroline, Madam Angel akamchukua mama yake na kuondoka nae kwa ajili ya kurudi katika makazi yake huku akiwatakia maisha mema Anko Nelson pamoja na familia yake.



    Hapo ndio mwisho wa riwaya yetu inayotambulika kwa jina la IPO SIKU TU....natumaini yapo mengi uliyoyapata kupitia simulizi hii na pia si vibaya kama tukashirikishana na pia ningependa unishauri lolote lile hasa zaidi katika mapungufu uliyoyaona ili niendele kuboresha simulizi zangu zijazo........

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Changamoto na matatizo unayoyapitia sasa yasije yakakufanya ukakata tamaa katika maisha yako na kujiona kuwa ni mtu usiye na thamani, Amini IPO SIKU TU Mungu atakutazama na kukuondolea hayo yote unayopitia.



    MWISHO







0 comments:

Post a Comment

Blog