Search This Blog

Sunday, July 10, 2022

PENZI LILILOSABABISHA MAUTI - 1

 







    IMEANDIKWA NA : JUMA HIZA



    *********************************************************************************



    Simulizi : Penzi Lililosababisha Mauti

    Sehemu Ya Kwanza (1)





    Based on True Story.



    Niliamua kufunga pingu za maisha na Julieth kwasababu alikuwa ni mwanamke niliyempenda sana. Alikidhi kila aina ya vigezo ambavyo nilikuwa nikivihitaji kwa mwanamke hasa yule ambaye nilitarajia kufunga naye pingu za maisha.

    Nakumbuka alivumilia mambo mengi sana, wakati wa mateso, huzuni na hata wakati mwingine wa furaha bado alikuwa na mimi. Sikutaka kumpoteza katika maisha yangu nilihakikisha naitimza ahadi yangu niliyomuahidi ya kumuoa.

    Julieth alijaaliwa uzuri wa sura ya kitoto, macho makubwa legevu ya kurembuwa, umbo namba nane lililokuwa linawapagawisha wanaume wengi waliyokuwa wakimtazama kwa macho ya matamanio.

    Nilikuwa nikipata kesi lukuki za wanaume ambao walikuwa wakimsumbua lakini wote hawakuweza kupata nafasi. Julieth alikuwa akinipenda sana, hakutaka kufanya kitu kibaya ambacho kingeweza kunigharimu maisha yangu. Alikuwa akizijali  sana hisia zangu.

    “Dominick mpenzi mimi siwezi kukusaliti nakupenda sana na ninakuahidi hutojutia kunipenda katika maisha yako,” yalikuwa ni maneno ya Julieth aliyokuwa akipenda kuniambia, wakati huo kichwa chake alikuwa amekilaza kifuani mwangu.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nilizidi kumuamini sana Julieth na hii ndiyo sababu iliyonipelekea mpaka nikaamua kumkabidhi dhamana ya moyo wangu, moyo ambao sikumbuki kama uliwahi kupenda hapo kabla. Ilikuwa ndiyo mara yangu ya kwanza kupenda na niliangukia mikononi mwa Julieth, mwanamke niliyekuwa nikimfananisha na kito cha thamani ambacho niliahidi kukitunza mpaka pale mwisho wa pumzi zangu utakapofika. Nilimpenda sana Julieth Mushi.

    Ingawa maneno ya Mama yangu, ndugu na marafiki hayakuwa mbali kipindi ambacho nilikuwa nataka kumuoa Julieth lakini hayakufanya niache kufanya kile ambacho nilidhamiria kwa wakati ule, kwa kuwa niliamini sisi ndiyo tulikuwa tumependana kwa dhati itokayo moyoni basi maneno ya watu hayakuweza kusitisha kile tulichokuwa tumepanga.

    Kazi yangu ya ufundi wa simu niliyokuwa nikiifanya katika ofisi yangu ndogo iliyokuwepo mtaa wa Kariakoo ukijumlisha na Julieth ambaye hakuwa na kazi yoyote ilichangia kuzalisha maneno mengi kila kukicha, wengi wao hawakutaka kuamini kama kweli nilikuwa naoa tena nilikuwa naenda kumuoa mwanamke ambaye hakuwa amesoma wala hakuwa na kazi yoyote, katika maisha yake ya kielimu alibahatika kusoma mpaka darasa la saba tu!. Ugumu wa maisha  ndiyo uliyochangia Julieth kutoendelea na elimu yake ya sekondari, wazazi wake hawakuwa na uwezo wa kuendelea kumsomesha. Huo ndiyo ulikuwa mwisho wa elimu yake. Hakika nilichekwa sana, nilitukanwa kila aina ya tusi lakini katu sikutaka kuwasikiliza, nilisimamia katika kile nilichokuwa nakiamini.

    “Nakupenda sana Julieth wangu,” nilimwambia Julieth huku nikimtazama kwa macho ya huba, alionekana kuwa mpole sana.

    “Sawa unanipenda Dominick lakini Mama yako anaonekana kutonipenda, utawezaje kuishi na mimi?” aliniuliza Julieth swali lililokuwa na maana kubwa sana, ni kweli mama yangu alionekana kutompenda lakini sikutaka hilo liendelee kuwa tatizo litakalosababisha kuvunjika kwa uhusiano wetu.

    “Julieth mimi ndiyo niliyokupenda Mama yangu asiwe kikwazo cha kukufanya utokwe na imani ya mapenzi yangu,” nilimwambia.

    “Hata kama Dominick lakini nitawezaje kuishi na Mama yako na wakati hanipendi?”

    “Julieth mpenzi wangu naomba uniamini kuwa nakupenda kwa dhati wala usiwe na wasiwasi wowote kuhusu Mama yangu usijali nitaongea naye na kila kitu kitakuwa sawa” nilimwambia maneno ambayo yalionekana kumuingia vyema, alikuwa ni muelewa sana.

                                                                         ****

    Maneno ya Mama yangu bado yaliendelea kuwa tatizo katika mapenzi yangu kila siku nilikuwa nikigombana na Mama yangu kuhusu Julieth mwanamke ambaye alionekana kuwa takataka, hakuwa na kazi yoyote hivyo kila kitu kwake kilionekana kuwa kibaya. Mama yangu alikuwa akimsema sana Julieth, alinidharau kwa maamuzi ambayo nilikuwa nimeyachukua.

    “Dominick mwanangu hivi una akili kweli wewe, utaendaje kumuoa mwanamke ambaye hana kazi wala nini” aliniambia Mama yangu huku akionekana kukasirishwa na kitendo nilichokuwa nimekifanya.

    “Lakini mama nampenda sana,” nilimjibu huku nikimtazama usoni, alionekana kuwa na hasira mno.

    “Utampendaje mwanamke ambaye hana mbele wala nyuma. Mwanangu wewe mwenyewe embu angalia kazi unayoifanya halafu bado unaenda kuoa mwanamke ambaye hana maisha hivi unafikiri maisha yako yatakuwaje?” aliniuliza Mama.

    “Mama mapenzi hayaangalii kazi nzuri wala maisha mazuri bali moyo ndiyo unaopenda na moyo ukipenda kamwe huwezi kuukataza uache kupenda,” nilimjibu huku nikiwa nimeyaelekeza macho yangu chini, sikutaka kumtazama Mama yangu usoni. Nilimuonea haya.

    “Ati! nini! Unasamaje Dominick? Mimi na marehemu Baba yako hatukupendana kama unavyosema bali ni wazazi wetu waliamua kutuchagulia na kwa wakati ule Baba yako alikuwa na maisha mazuri tu! Sasa huo unaouita moyo hapa sijui ni moyo wa aina gani?”

    “Mama ni moyo wa mapenzi na ukishapenda umependa kweli wala huwezi kuubadilisha. Nampenda sana Julieth na yeye ndiye mwanamke wa ndoto zangu,” nilimwambia.

    Bado niliendelea kuushikilia msimamo wangu wa kumpenda Julieth mwanamke niliyekuwa nampenda kuliko kitu chochote kile wala siwezi kuficha kitu katika hilo.

    Ingawa Mama yangu alionekana kutokukubaliana na mimi kumuoa Julieth lakini ilifikia kipindi akaamua kukubali hapa ni baada ya kuniona nimezidi kuwa kin’gang’anizi.

    Hatimaye Dominick mimi niliyezaliwa miaka ishirini na Saba iliyopita nikaamua kufunga ndoa rasmi na Julieth na huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa kuhama maisha ya nyumbani, nikayaanza maisha mapya ya ndoa yangu. Maisha ambayo kiukweli mwanzo yalianza kama hadithi nzuri ya kimapenzi lakini kadri siku zilivyokuwa zikisonga mbele hadithi hiyo iliweza kubadilika na kuwa miongoni mwa hadithi za kutisha ambayo iliweza kuniacha na uadui mkubwa sana dhidi ya viumbe ambavyo vimefanya niishi  maisha ya kutoitamani kesho yangu.

                                                          ****CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nilikuwa nikiishi Magomeni mtaa wa Mwinyimkuu, nilifanikiwa kupanga nyumba yenye vyumba viwili. Maisha ya ndoa yalionekana kuwa mazuri sana, yalibadili mfumo mzima wa maisha yangu ukitofautisha na mfumo ule wa maisha tegemezi niliyokuwa nikiishi nyumbani kwetu Kimara kwa Mama Dominick.

    Mke wangu Julieth alikuwa ni zaidi ya mke mwema kwangu, hakukuwa na tofauti yoyote katika maisha yetu ya ndoa, kila siku nilizidi kujifunza mambo mengi sana hususani yale ya ndoa.

    Nilijifunza juu ya uvumilivu, upendo, upole na busara katika kufanya maamuzi. Vitu hivi ndiyo ngao ambayo niliitumia katika kuishi vizuri na ndoa yangu.

    Japo kazi yangu ya ufundi simu haikuwa ikiniingizia kipato kikubwa lakini hiyo haikuwa sababu ya kunifanya nishindwe kuwa mwaminifu wa ndoa yangu, nilikuwa mwaminifu haswaa wala siongopi ninapoyasema haya. Nayamaamisha kutoka katika kitako cha moyo wangu.

    Julieth alikuwa ndiye mshauri wangu, alikuwa akinishauri mambo mengi sana hata yale ambayo nilikuwa siyafahamu pia aliweza kunijuza. Alikuwa na kipaji cha kuniongoza vyema katika maisha yangu, hakupenda kuona naanguka kimaisha hivyo kila kitu kilichokuwa kikiendelea katika maisha yangu yeye alikuwa ndiye rubani wangu, alikuwa akiniongoza. Hakika elimu yake ya darasa la saba aliitumia katika dhana ya kipekee sana wala sikutaka kuamini.

    “Mume wangu pole na kazi,” aliniambia Julieth wakati ambao nilikuwa nimerudi nyumbani, ilikuwa ni majira ya jioni.

    “Asante sana mke wangu,” nilimwambia kisha kabla sijakaa kwenye kochi alinipokea kwa kumbato na kunivua begi lililokuwa mgongo mwangu, lilikuwa ni begi lenye vifaa vyangu muhimu vya kazi.

    Upendo ulitawala katika maisha yangu, nilihisi kupendwa sana na hii ndiyo sababu iliyopelekea nikazidi kuyasahau yale matusi na maneno ya kejeli niliyokuwa nikiambiwa na ndugu pamoja na marafiki zangu juu ya Julieth mke wangu, walikuwa wakimsema kuwa alikuwa ni mwanamke ambaye hakuwa amesoma.

    Kwa upendo aliyokuwa akinionyesha Julieth kwa kweli nilimchukulia kuwa kama zaidi ya msomi, sikuhitaji msomi mwingine ukimtoa Julieth pambo la moyo wangu, furaha ya maisha yangu.

    “Nakupenda sana Julieth wangu,” kinywa changu hakikuacha kumkumbusha maneno haya kila siku, ilikuwa ni desturi yangu. Haikuweza kupita siku bila kumsifia Julieth kutokana na uzuri aliyokuwa nao, nakumbuka kuna baadhi ya sifa nilikuwa nikiongezea chumvi. Hahaha! Ila wanasema yote haya ni mapenzi tu! mapenzi yanahitaji mambo mengi sana yanayoleta furaha ila chunga shubiri isije ingia katika mapenzi yako, utatamani dunia igeuke miguu juu kichwa chini, hutatamani kupenda tena.

    “Wewe ndiye mwanamke wa maisha yangu, nakufananisha na kila kitu ninachokihitaji katika maisha yangu. Sijutii kukuchagua katika maisha yangu. Naomba utambue kuwa wewe ni zaidi ya kiungo muhimu katika mwili wangu,” nilimwambia maneno ambayo yalijawa na ushawishi wa utamu wa mapenzi ya dhati .

    “Dominick nakupenda pia mume wangu,” aliniambia Julieth.

    Maisha yetu yalitawaliwa na furaha sana, utamu wa maisha ya ndoa ukanifanya nisahau kabisa shida nilizokuwa nazo, nikazidi kunawiri japo maisha hayakuwa mazuri sana lakini kiupande wa pili wa sarafu wale waliokuwa wakinitazama walikiri kuwa hakika ndoa ilinipenda.

    “Aisee Dominick umebadilika kabisa ndugu yangu,” aliniambia Chrispine rafiki yangu ambaye urafiki wetu ulikuwa kama ndugu, nilikuwa nikisaidiana naye mambo mengi sana, hata katika suala hili la mimi kumuoa Julieth alihakikisha anasimama kidedea mpaka nafanikiwa kumuoa. Alikuwa akifanya kazi katika duka la kuuza Compact Disk (Cd) Kariakoo.

    “Ah! Wapi wewe acha mambo yako, huoni jinsi nilivyokondeana hivi?” nilimuuliza swali la kiutani huku kicheko kikishika hatamu yake, nilikuwa nikicheka kwa wakati huo.

    “Sasa unacheka nini wakati nakwambia ukweli,” aliniambia Chrispine huku akinitazama, nikazidi kucheka sana.



    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    “Hahaha! Shemeji yako anafanya kazi yake bhana,” nilimwambia maneno ambayo yakamfanya atokwe na tabasamu pana.

    “Naam! Hilo ndiyo neno ambalo nilikuwa nataka kulisikia kutoka kwako,” aliniambia.

    “Hii ndiyo kazi ya shemeji yako.”

    “Hata mimi naona ndugu yangu unapendeza tu!”

    “Hahahaha!”

    Kila neno alilokuwa akilizungumza Chrispine lilikuwa likinichekesha sana, nilizoea kuzungumza naye kwa utani.

    Alipenda kuona nikiishi maisha mazuri ya ndoa yangu, hakupenda kuona nikinyanyasika na mapenzi naweza kusema alikuwa ni mtu ambaye alikuwa akinipa somo kubwa kuhusu maisha ya ndoa.

    Katika maisha yake aliwahi kubahatika kuoa lakini kutokana na mkasa uliyowahi kumtokea hakuweza kuendelea kuishi na mke wake, waliachana.

    Aliwafahamu sana wanawake, alifahamu kila kitu kuhusu wanawake na hata kipindi ambapo nilikuwa nikiambiwa na watu kuwa nimuache Julieth nikamuoe mwanamke mwingine hakuweza kukubaliana nalo.

    Kwa maisha ya furaha ambayo alikuwa akiona nikiishi baada ya kuoa hakika alifurahi sana, sikumbuki kama kuna neno baya ambalo aliwahi kuniambia ila ninachokikumbuka mimi aliwahi kuniambia kuwa nimuheshimu sana mke wangu.

    “Inabidi umuheshimu sana mke wako Dominick, usikubali hata siku moja katika maisha yako itokee ukamuudhi, utakuwa umefanya makosa makubwa sana, jitahidi atamani kuwa na wewe kila siku za uhai wake,” aliniambia Chrispine siku moja tulipokuwa kwenye mgahawa mmoja mtaa wa Kariakoo tukipata chakula cha mchana, alionekana kuwa na mengi sana ya kuniambia siku hiyo.

    “Nimekuelewa sana ndugu yangu,” nilimwambia huku nikikitikisa kicha changu kumuonyesha kuwa nilimuelewa sana.

    “Unajua wanawake ni viumbe wa ajabu sana, mimi napenda kuwaita sometime jua sometime mvua,” aliniambia maneno aliyoyafumba.

    “Kwanini?” nilimuuliza.

    “Hawatabiriki yani unaweza ukahisi ni jua kumbe ni mvua aisee,” aliniambia maneno ambayo yalikuwa na fumbo ndani yake, sikuweza kulifumbua kwa haraka, ikabidi nimuulize kuwa alikuwa na maana gani hasa, wakati huo alikuwa akicheka.

    “Sasa hapo ni lipi usilolielewa Dominick?”

    “Umesema jua mara mvua sijui unamaanisha nini?”

    “Inabidi utumie akili nyingi sana kuishi na hawa viumbe aisee hawachelewi kukupa kovu la maisha,” aliniambia Chrispine huku akikipigapiga kijiko katika sahani, alikuwa akitabasamu, sikujua tabasamu lake lilimaanisha nini hasa, nikamuuliza tena.

    “Kuna nini?”

    “Mkeo anakupenda sana.”

    “Ndiyo nalifahamu hilo.”

    “Basi jitahidi kuishi naye vizuri ila usiombe wale waliyokutabiria mabaya yakakutokea kweli utahisi dunia imekuelemea.”

    “Sawa nimekuelewa.”

    “Mpende sana mkeo Dominick naamini wewe ni mpambanaji, pigania penzi lako, pigania ndoa yako usikubali kumpoteza mkeo kwa maneno ya ndugu na marafiki,” aliniambia kisha akanyamaza kidogo halafu akaendelea tena kuzungumza.

    “Kuna kitu kimoja inabidi ujifunze,” aliniambia.

    “Kitu gani hicho?” nilimuuliza.

    “Ishi maisha ya kumpenda kila mtu,” aliniambia Chrispine.

    Maneno ya Chrispine yalizidi kunijenga sana, yalikuwa yakiniimarisha vyema, nilisimama imara na ndoa yangu ambayo kila siku nilikuwa nikiifurahia.

    Nakumbuka Mama yangu hakuwa akimpenda Julieth hata kidogo hapo awali lakini kupitia maneno na ushauri wa Chrispine niliweza kuutumia katika kumfanya Mama yangu akampenda Julieth, sikumbuki kama ni kweli alimpenda ama la lakini ninachokikumbuka alikuwa akimpenda, yale maneno mabaya aliyokuwa akiyasema kuhusu Julieth yalimuisha.

    Ukurasa wa maisha ya ndoa yangu ulikuwa ni wa aina yake, tuliishi kwa upendo sana na mke wangu, alijivunia kuwa na mimi hata mimi pia nilijivunia kuwa na yeye maishani, alikuwa ni hakimu wa moyo wangu, kila kitu ambacho alikuwa akiamua nilikifuata bila kupinga, waliokuwa wakinitazama waliniambia kuwa nimelogwa. Sikutaka kuyapa nafasi maneno yao yatanitawale, nilichokuwa nikikitazama kwa wakati ule ni maisha mazuri yaliyogubikwa na amani niliyokuwa nikiishi na mke wangu.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Siamini kama Mama yako amekubali kabisa mimi kuolewa na wewe,” aliniambia Julieth siku moja usiku tulipokuwa kitandani.

    “Inabidi uamini sasa Mama yangu anakupenda sana,” nilimwambia huku nikimbusu katika paji la uso wake, alitabasamu kisha nikaitumia mikono yangu vyema katika kumpapasa mgongoni mwake, alikuwa na mwili laini sana uliyonisisimua kimapenzi.

    “Furaha yangu sasa naweza kusema imerudi,” aliniambia Julieth kwa sauti ya chini, ilikuwa na utulivu wa aina yake.

    “Kwani ilienda wapi?” nilimuuliza kiuchokozi, akatabasamu wakati huo nilikuwa nikiendelea kumpapasa.

    “Umeshaanza vituko vyako,” aliniambia.

    Haikuchukua dakika nyingi mwisho nikajikuta tayari nimeshazipandisha hisia za Julieth, alionekana kuweweseka kimapenzi, alikuwa akihangaika katika kifua changu. Sikumbuki ni nini kilitokea ila nilishangaa Julieth akiwa juu yangu tena akiwa uchi wa mnyama, kitendo kilichofuata hapo ilikuwa ni kufanya mapenzi usiku kucha.

    Mchezo huo haukukoma tuliendelea kila siku, Julieth alinisifu kuwa katika maisha yake hakuwahi kumpata mwanaume ambaye alikuwa akimfikisha safari yake kama nilivyokuwa nikifanya mimi, hilo lilizidi kunifanya nijione kuwa hodari hasa katika mchezo ule ambao ndiyo kama silaha ya ndoa.

    “Sitokuacha mume wangu kipenzi,” aliniambia Julieth siku moja tulipomaliza kufanya mapenzi.

    “Hata mimi siwezi kukuacha wewe ndiyo hodari wa raha zangu,” nilimwambia.

    “Naomba ujiheshimu sana mume wangu, jilinde siku hizi maradhi ni mengi sana,” aliniambia Julieth kwa sauti ya kipole, alikuwa akideka.

    “Najiheshimu sana Mke wangu wala usiwe na mashaka katika hilo mumeo ni mwaminifu sana,” nilimwambia.

    “Nitafurahi sana kama ni kweli hayo uyasemayo mume wangu.”

    “Kama usiponiamini mimi ni nani mwingine ambaye utamuamini?” nilimuuliza.

    “Nakuamini Mume wangu,” alinijibu.

    “Nakupenda sana,” nilimwambia.

    “Nakupenda pia mume wangu,” aliniambia.

    Maisha yetu yaliendelea mpaka pale siku moja Julieth aliponiambia kuwa alikuwa ni mjamzito, taarifa hizo ziliweza kunifurahisha sana, nikahisi kuitimiza ndoto ya maisha yangu, ilikuwa ni ndoto ya kupata mtoto.

    “Mke wangu unasema kweli?” nilimuuliza mke wangu huku nikionekana kutoamini kabisa, nilihisi alikuwa akinitania.

    “Ndiyo mume wangu nina ujauzito wako,” alinijibu Julieth huku uso wake ukiunda tabasamu pana.

    “Siamini kwa kweli, unaujauzito?” nilimuuliza tena safari hii nilisimama na kwenda kumkumbatia kwa furaha, nilipokuwa nimemkumbatia sikuacha kumwambia kuwa nilimpenda sana na kwa zawadi ile aliyokuwa amenipa katika maisha yangu ilinifanya nizidi kumpenda sana. Niliahidi kuongeza mapenzi.

    “Huu ujauzito una muda gani?”

    “Mwezi mmoja.”

    “Asante mke wangu, umeitimiza ndoto yangu.”

    “Ndoto yako?”

    “Ndiyo.”

    “Ndoto gani?”

    “Kwa muda mrefu nilikuwa nikitamani siku moja kuitwa baba, sikujua itakuwa ni siku gani lakini katika hili la leo ulilonifanyia katika maisha yangu kwa kweli nashindwa nikushukuru vipi ila nakuahidi kuwa nitakupenda sana na nitakutunza maisha yako yote, nitapigania uwepo wako katika maisha yangu,” nilimwambia.

    Wakati wa furaha ukazidi kutawala maisha yangu, maisha ya ndoa yangu, nilizidi kumpenda sana mke wangu kwa maana yeye ndiye alikuwa mwanamke wangu wa kwanza kumpenda katika maisha yangu na vilevile ndiye alikuwa mwanamke wangu wa kwanza kunipa taarifa za ujauzito wangu. Moyo wangu ulikuwa katika furaha kubwa sana.

    “Siamini, siamini Julieth,” nilijiambia maneno haya nilipokuwa peke yangu chumbani, wakati huo nilikuwa nimejilaza kitandani huku nikiukunjakunja mto. Hakika nilijiona kuwa kidume tena kidume haswaa.



    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Nilikumbuka kumwambia Mama yangu juu ya habari zile za ujauzito wa Julieth, alionekana kufurahishwa na taarifa hizo. Hakuacha pia kunihusia juu ya maisha mapya ya familia ambayo nilikuwa natarajia kwenda kuyaanza.

    “Dominick mwanangu hongera ila jiandae kwa maisha mapya ya familia unayokwenda kuyaanza,” aliniambia Mama nilipokuwa nikizungumza naye kwenye simu.

    “Asante Mama ila hata hivyo najiandaa najua sasa tunakwenda kuongezeka katika familia yangu,” nilimwambia Mama kisha nikajichekesha kwa makusudi kabisa ajabu Mama yangu alikuwa kimya, hakunionyesha hali yoyote ya kuniunga mkono.

    “Ila Dominick mwanangu kuna jambo nataka kukueleza,” aliniambia Mama kwa sauti ya chini.

    “Jambo gani hilo mama?” nilimuuliza.

    “Ni kuhusu huyo mke wako,’ alinijibu.

    “Amefanyaje tena?”

    “Hajafanya kitu ila hivi ni kweli kabisa umefurahia mkeo kukubebea ujauzito wako?”

    “Ndiyo Mama kwani kuna ubaya?”

    “Hakuna ubaya ila nahisi kama unaenda kujibebesha mizigo.”

    “Najibebesha mizigo kivipi Mama mbona sijakuelewa?”

    “Huyo unayemuita mkeo hana kazi yoyote anakutegemea wewe umfanyie kila kitu bado hapohapo anakuletea mtoto hivi huoni kuwa hiyo ni mizigo unajibebesha?”

    “Hapana Mama usiseme hivyo huyu ni mke wangu na suala la mimi kumuhudumia ni wajibu wangu mbona sioni kama kuna tatizo hapo?”

    “Dominick mwanangu wewe bado ni mtoto kwangu na utabaki kuwa mtoto siku zote, kwa macho ya haraka unaweza kusema sio tatizo lakini kiukweli ni tatizo tena ni tatizo kubwa sana, unakwenda kubeba majukumu mazito mwanangu.”

    “Sasa Mama unanishauri nifanyaje?”

    “Hapo cha kukushauri mwanangu mrudishe kwao aende kwanza kuilea mimba mpaka pale atakapojifungua ndiyo arudi nyumbani wakati huo utakuwa umeshamuandalia mazingira mazuri ya kumlea mtoto wenu.”

    “ Hapana Mama siwezi kufanya hivyo.”

    “Dominick mwanangu nakuonea huruma,” aliniambia Mama kwa sauti iliyoonyesha kuwa na masikitiko makubwa sana.

    Niliamua kuyakatisha mazungumzo kwa kumdanganya kuwa salio nililokuwa nimejiunga lilikuwa limeisha hivyo muda wowote simu ingeweza kukatika. Naam! Haikuchukua sekunde chache kisha niliweza kukata simu, niliamua kufanya hivyo kwa kuwa sikutaka kuzungumza na Mama yangu kwa wakati huo, maneno yake yalionekana kunikwaza moyoni.

    Sikupenda kumuona mtu yoyote akimzungumzia vibaya mke wangu, nilihakikisha nasimama imara katika kuipigania ndoa yangu. Sijui ni nini kilitokea mpaka Mama yangu akabadilisha mawazo yake, alikuwa akimchukia tena mke wangu. Nilipokuwa nikiendelea kutafakari juu ya chuki iliyojipandikiza upya kwa Mama yangu dhidi ya mke wangu Julieth ghafla! simu yangu iliingia ujumbe mfupi. Nilipoufungua na kuusoma ulikuwa ni ujumbe kutoka kwa Mama yangu, alikuwa ameniandikia hivi,

    “MWANANGU NAONA UMELOGWA SASA YANI HUTAKI KABISA KUNISIKILIZA MIMI MAMA YAKO NILIYEKUZAA SIJUI UTAMSIKILIZA NANI MWINGINE AU UNATAKA MIZIMU YA BABA YAKO IFUFUKE IJE IKUAMBIE NDIYO UTAELEWA?”

    Nilipomaliza kuusoma ujumbe huo hakika ulionekana kunitisha sana, sikutaka kumjibu lolote kwa maana niliamini fika hata kama ningeamua kumjibu lolote kama swali la kumuuliza majibu yangekuwa ni yaleyale.

    Kichwa changu bado kiliendelea kutawaliwa na mawazo lukuki, nilizidi kuwaza na kuwazua, kupanga na kupangua lakini mpaka kufikia wakati huo sikujua ni nini nilitakiwa kufanya. Kila nililokuwa nikiliwaza lilizidi kuniumiza kichwa changu, nilipagawa.

    Bado wimbi la mawazo liliendelea kuvuma katika upeo wa fikra zangu, nilizidi kuwaza mambo mengi sana kuhusu ndoa yangu ambayo tayari ilikuwa imeingia dosari.

    “Kwanini mama unanifanyia haya, kwanini hutaki kufurahia maisha ya ndoa yangu?” nilijiuliza wakati huo mikono yangu ilikuwa imeshikilia picha iliyokuwa ndani ya fremu, ilikuwa ni picha yangu na mke wangu tuliyopiga siku ya ndoa yetu. Macho yangu yaliitazama lile vazi la shela alilokuwa amevaa mke wangu kisha na mimi nikiwa katika vazi la suti adhimu, tulikuwa tumekumbatiana huku furaha ikiwa imetutawala.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Machozi hayakuwa mbali kwa wakati huo, yakaanza kunidondoka tone moja kisha tone la pili na haikuchukua sekunde kadhaa kusababisha mvua ya machozi ya uchungu iliyoninyeshea kutiririka mashavuni mwangu, nilikuwa nikilia kwa wakati huo.

    Mama yangu alikuwa kikwazo cha furaha ya ndoa yangu, kila kitu kilichokuwa kikiendelea alionekana kuwa nacho kinyume, alikikosoa.

    “Nimekukosea nini mimi Mama kwanini hutaki kuniunga mkono katika hili, kwanini hutaki kushiriki furaha ya maisha yangu au nimefanya makosa kukueleza taarifa za ujauzito wa mke wangu?”

    Kila swali nililokuwa nikijiuliza halikuweza kupata majibu zaidi machozi ndiyo yaliyokuwa yameshika hatamu yake, yalizidi kunitiririka mashavuni bila kuyafuta.

    Wakati ule ambao nilikuwa nimeishikilia picha huku machozi yakiendelea kunidondoka ghafla! mke wangu Julieth akatokea, alinikuta nikilia.

    “Mume wangu kuna nini kimetokea?” aliniuliza Julieth kwa sauti iliyogubikwa na upole wa hali ya juu, alionekana kushangazwa na hali aliyonikuta nayo kwa wakati ule.

    “Hakuna kitu,” nilimjibu huku nikiyafuta machozi yangu kisha nikairudisha ile picha ukutani.

    “Hakuna kitu na wakati nimekukuta unalia?” aliniuliza huku akionekana kutoelewa lolote lile.

    Naam! Ni kweli alikuwa hajui lolote lililokuwa limetokea hata hivyo sikutaka kumuweka wazi, niliamua kumficha ukweli, niliamua kufanya hivyo ni kutokana na hali ambayo alikuwa nayo.

    “Hakuna kitu nipo sawa,” nilimwambia kisha nikajaribu kutengeneza tabasamu pana katika uso wangu, nilifanikiwa kutabasamu.

    “Mbona unalia?” aliniuliza wakati huo alinisogelea kisha akaanza kunifuta machozi kupitia viganja vyake, nilipomtazama alionekana kuonyeshwa kuguswa na tukio lile japo hakuwa akijua ni nini hasa kilichokuwa kimetokea.

    “Nimemkumbuka marehemu baba yangu laiti kama angekuwepo naamini hata yeye angefurahia kwa tukio hili lililotokea, angefurahi kuwa babu mtarajiwa,” nilimwambia maneno ya uongo ambayo yalijitunga ghafla! kichwani. Muonekano wangu wa majonzi ukichanganya na hayo maneno niliyomwambia yakasaini ukweli ambao alikuwa akiutaka kuufahamu japo ulikuwa ni ukweli wa kutunga.

    “Mume wangu usiseme hivyo utakufuru,” aliniambia huku akionekana kuniamini kabisa ila ni kama alikuwa akiwaza kitu na mara baada ya kukiwaza akaamua kuniambia.

    “Halafu nimesahau kukwambia,” aliniambia huku akionekana kufurahi.

    “Umesahau kuniambia nini?” nilimuuliza huku nikimtazama, wakati huo machozi yalikuwa yamekoma kunidondoka.

    “Nimeongea na mama,” alinijibu.

    “Mama yupi?” nilimuuliza.

    “Kwani wewe una mama wangapi?” aliniuliza.

    “Wawili,” nilimjibu.

    “Yupi na yupi?” aliniuliza tena swali ambali likanifanya nitabasamu.

    “Mama Julieth na Mama Dominick mzaa chema, sasa sijui wewe umeongea na mama yupi hapo?” nilimjibu kwa kumuuliza swali.

    “Nimeongea na Mama Dominick,” alinijibu.

    “Anasemaje?” nilimuuliza.

    “Amefurahi tu! kusikia kuwa nina ujauzito ila ameniambia kuna zawadi anataka kunipa.”

    “Zawadi gani tena.”

    “Hata sijui mume wangu ila amefurahi huyo,” aliniambia Julieth huku uso wake ukiwa katika tabasamu pana, tabasamu ambalo likazidi kuniweka katika bumbuwazi, kichwani likanijia swali. Lilikuwa ni swali juu ya huyo Mama Dominick ambaye alikuwa akiniambia alifurahishwa na taarifa hizo kiasi kwamba ikafikia wakati wa kutaka kumpa zawadi.

    Ni zawadi gani hiyo ambayo anataka kumpa mke wangu?

    Na je huo upendo anaouzungumzia mpaka akafurahishwa na taarifa za ujauzito wake ulitokea wapi?

    Nikazidi kuwa katika kizungumkuti, sikujua ni nini kilichokuwa kinakwenda kutokea katika ndoa yangu. Nikakumbuka yale maneno aliyoniambia Mama yangu pamoja na ule ujumbe alinitumia, vilikuwa ni vitu viwili tofauti na yale maneno ya Julieth aliyokuwa akiniambia kwa wakati huo.

    “Unasema umeongea na Mama Dominick, Mama yangu!” nilimuuliza Julieth huku nikionekana kushangazwa na maneno yake.

    “Ndiyo nimeonge na Mama yako,” alinijibu huku akionekana kutokuwa na tatizo lolote, alikuwa akijiamini na jibu lake.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Vipi na Mama yako pia umemwambia?”

    “Ndiyo niliwaambia wote ila kwa ufupi hakuna tatizo lolote mume wangu.”

    “Una uhakika?”

    “Ndiyo mbona umeshangaa?” aliniuliza.

    “Hapana hakuna kitu,” nilimjibu.

    Nilizidi kuwa katika fumbo zito, nisijue ningeweza kulifumbua vipi kwani tayari akili yangu ilikuwa imechoka. Nikazidi kubaki kujiuliza maswali lukuki ambayo hayakuweza kupata majibu, kiufupi nilitawaliwa na mawazo.

    “Ina maana Mama yangu alikuwa akinitania au?” nikajiuliza tena hapo nilikuwa nikijichekesha kama mwendawazimu, sikutaka kumuonyesha tofauti yoyote mke wangu.







    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog