Simulizi : Kwa Nini Mimi?
Sehemu Ya Tatu (3)
ILIPOISHIA….
Thomas alishtuka baada ya kuangalia saa akaniambia
"we Anne huna njaa? Mbona umeongea kwa muda mrefu bila kula? Twende tukale kwanza,halafu tutaendelea".Aliongea Thomas na bahati nzuri Thomas alikuwa amepika chakula mpaka cha jioni, tukala chakula halafu nikaendelea kumsimulia.
ENDELEA NAYO..
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
MAISHA YA MTAANI NI MAGUMU SANA HIVYO YATUPASA TUWAONEE HURUMA WATOTO WA MTAANI NA IKIWEZEKANA KUWASAIDIA KABISA..
[ANNE ANAENDELEA KUSIMULIA]
Nilivyofika Iringa sikutaka kwenda kwa kaka John nikawa nafanya vibarua mbalimbali huku jioni nilikuwa nalala kwenye stendi ya mabasi yaendayo mikoani.Ila kuna kipindi nilianza kusumbuliwa na ndoto za mara kwa mara, wazazi wangu walikuwa wakinitokea na kunisihi nirudi nyumbani.Mwanzoni nilidharau zile ndoto. Kwa muda wa miezi mitatu ile ndoto ilikuwa ikinisumbua sana.Nikaamua kwenda nyumbani maana siku hiyo sikuwa na raha kabisa.
Kufika nyumbani sikuamini nilichokiona, nyumba yetu ilikuwa imebomolewa na kulikuwa na nyumba mpya ikijengwa.Majirani waliponiona walikuwa wakinionea huruma huku wakitingisha vichwa vyao kuonesha masikitiko.Mama Lucy, jirani yetu akanidokezea kuwakaka John alimuuzia nyumba mwarabu mmoja baada ya kukopa sana na kudaiwa.Kwa hiyo aliamua kuuza nyumba ili alipe madeni. Kwa kweli nilichanganyikiwa sana kitu kilichopelekea kupoteza fahamu. Nilikuja kushtuka baada ya kumwagiwa maji na watu wengine walikuwa wakinipepea.
Watu wengi walinipa pole, wakaniambia kaka yangu alikuwa amepanga maeneo ya Gangilonga.Niliwashukuru majirani kwa msaada walionipa nikaondoka taratibu nikiwa nina mawazo mengi. Niliamua kwenda Gangilonga maana majirani walinielekeza mpaka nyumba.
Nilifika mpaka kwenye nyumba aliyopanga kaka John, wifi alishtuka sana akaniuliza nimepajuaje pale nikamjibu kupitia watu.Kaka John alikuwa hayupo hivyo nilikaa pake kumsubiri kaka John.
Nakumbuka nilikaa pale kwa muda wa masaa matatu ndipo kaka alipokuja.Kaka John alivyoniona alishtuka sana mpaka akadondosha mfuko aliokuwa ameushika. Akaniuliza
"Anne umepajuaje hapa?"nikamjibu kupitia watu, na hapo hapo nikamuwahi sikutaka apumzike,nikamuambia ahsante sana kwa kuuza nyumba ya urithi.Sihitaji hela yoyote kutoka kwako umeniudhi sana.Nilikuwa naongea hayo huku nalia, na nilikuwa nimemkwida kaka John. Wifi alijaribu kunituliza, nikamsukuma pembeni kisha nikimwambia
"hayakuhusu tafadhali tuache wifi".Kaka alijaribu kunituliza huku akiniambia
Anne mdogo wangu nipo tayari tugawane sehemu ya pesa. Nami nikamjibu kuwa, sitegemei hela yako na sipo tayari kupokea hata senti moja kutoka kwako.Nililia kwa sauti huku nikiwalaumu kaka zangu wote kuwa hawaeleweki.
“Kwa heri kaka John”.Hayo ni maneno niliyoyatoa baada ya kulia sana. Kaka John alijitahidi kuniuliza kwanini nimesema wao hawaeleweki?.Nikamwambia kaka Zakaria anafanya biashara ya madawa ya kulevya na ni mtumiaji mzuri.Kisha nikamwambia kaka John asiangaike kunitafuta naenda kutafuta maisha yangu.Baada ya hapo nikaondoka.
Nikaingia mtaani. Mtaa ukanichekea kisha ukanipokea kwa shangwe na nderemo nyingi.Makazi yangu yakawa stendi ya mkoa. Tulikuwa vijana wengi sana tuliokuwa tunalala pale stendi.
Kuingiliwa kimwili bila ridhaa yangu ikawa ni kawaida tu!.Kuwaibia vitu vya thamani watu mbalimbali ilikuwa ni jadi yangu, na nilikuwa naenda kuviuza kwa bei rahisi ilimradi nipate hela ya kuingiza kitu kinywani.
Kuna siku tulienda kuiba kwa muhindi.Kiukweli sitasahau siku hiyo.
Siku hiyo ilikuwa ya arobaini kwangu.Nilivyokamatwa nilipigwa sana mpaka nikapoteza fahamu.Nilikaa hospital kwa muda wa miezi sita. Kaka John ndiye alikuwa anakuja kuniona.Akanibembeleza sana nikakae nae, lakini niligoma katakata.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kaka alimalizana na Mhindi, akafuta kesi hivyo nikawa huru.Kwa mara nyingine nikarudi mtaani. Safari hii niliamua kubadilika,nikawa nafanya vibarua,na sikuwa naiba tena.Nilikaa sana pale Iringa, ila nikaona maisha ya Iringa hayalipi nikajipanga kurudi Dar-es-salaam tena kwenda kujaribu maisha kama yatanifaa. Sikupanga kufikia kwa kaka Zakaria hata kidogo.
Wakati nawaza hayo sikuwa na nauri. Nikajiuliza nitafikaje Dar?Mfukoni nilikuwa na shilingi elfu tano tu!.Ghafla nikaijiwa na wazo la kwenda barabarani kuvizia malori yanayotoka Zambia maeneo ya Makambako nimuombe dereva yoyote anipe lifti.
Nilifanikiwa kuomba lifti mpaka Makambako, jioni ya siku hiyo nikaona gari moja dogo likiwa limefunguliwa huku maboksi yakipangwa vizuri ndani ya gari. Niliingia ndani ya gari lile kwa kujificha kisha nikajibana kwenye maboksi.Bahati nzuri wahusika wa kwenye gari hawakuniona hiyo ndiyo ikawa safari yangu ya pili kuja Dar.
Wahusika wa hilo gari walifanikiwa kupanga maboksi vizuri kwenye gari hilo aina ya Land Cruise.Tukafanikiwa kuondoka Makambako salama, na nakumbuka ilikuwa ni mida ya saa mbili usiku kwa vile nilikuwa nimevaa saa mkononi ndio maana nilijua muda tulioondoka.Nililala usingizi ingawa nilikuwa nimejibana kwenye maboksi yale. Usingizi ulikuwa mtamu sana,nilikuja kushtuka mtu akiwa amenisimamia mbele yangu,kumbe walikuwa wamesimama sehemu wakishusha mizigo.Yule mtu alishtuka na akaanza kuniita,
“wewe binti wewe binti”.Kwa uwoga nikaanza kutetemeka.Akanivuta nje, alinipiga vibao viwili, kasha akaniambia kuwa hawahitaji kesi ya kuua tafadhali.Akaniambia,
“Nakupa dakika mbili sitaki kuiona sura yako mbele yangu toka haraka sana, hiyo sehemu uliokaa haina hewa”.Thomas siyo siri, nilikimbia kama sina akili nzuri, sikuelewa ninakoelekea ni wapi.Nakumbuka nilitembea barabarani kama masaa mawili hivi.
Hapo Thomas aliangalia saa akashtuka akaniambia
"Anne sasa hivi ni saa saba usiku nakuona umechoka na hadithi ya maisha yako ni ndefu tutaendelea kesho nenda ukalale".Nilimtakia Thomas usiku mwema kisha kila moja akaenda kulala.
Ilikuwa ni Jumapili asubuhi na mapema, Thomas aliniambia tujiandae twende tukasali.Thomas aliniuliza nasali wapi? Nikamjibu Roman Catholic. Bahati nzuri na yeye alikuwa akisali huko huko,hivyo tukaongozana kwenda kanisani kusali.
Tulivyotoka kusali tulikunywa chai.Na kisha nikamwambia Thomas kuwa, apumzike naingia jikoni mimi.Thomas akacheka sana akaniambia,
”ndio raha ya kuwa na nyumba yenye mwanamke. Haya mama ingia jikoni mie leo pua zangu zitakuwa zimesimama juu kwa kusikilizia harufu".Nilitabasamu nikaenda jikoni. Siku hiyo niliamua kupika pilau ambayo nilihakikisha inaweza kutosha mpaka jioni.
Kwa kweli siku hiyo nilipika chakula kizuri maana nilimaliza ujuzi wangu wote wa upishi alionifundisha marehemu mama yangu kwenye pilau ile.Thomas hakuvumilia ilibidi aniambie tu
"Anne itabidi uwe unanipikia siku zote pilau, chakula kitamu sana sijawahi kula hapo kabla”.Tulivyomaliza kula tukapumzika kwa muda wa saa moja na baada ya hapo nikaendelea kumsimulia,Thomas historia ya maisha yangu.
[ANNE ANAENDELEA KUSIMULIA]
Nilikimbia sana sikuona lami ilipoanzia wala ilipoishia,na sikumbuki nilitumia muda gani katika kukimbia.Nilifika sehemu ilikuwa ni chini ya mti huku nikiwa nimechoka sana. Nikalala usingizi mzito sana pale chini ya mti. Nilivyokuja kushtuka tumbo lilikuwa halina kitu, njaa ilikuwa inanikong'ota ile mbaya.Nilitembea nikafika sehemu moja MAMA LISHE waliokuwa wanauza chakula. Nikawasalimia,kisha mama mmoja aliniangalia akaniambia.
"Tafadhali sema shida yako tunawateja wengi tunaowahudumia".Nikamwambia
"Naomba chakula njaa inaniuma sana".Huku machozi mengi yalikuwa yananitoka.Yule mama alicheka sana akaniambiaCHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Hapa siyo kanisani hatutoi misaada".Bahati nzuri kuna mzee mmoja alikuwa anaingia hapo kwa mama lishe kwaajili ya kula chakula. Alisikia maongezi yote.Akamwambia yule mama
"Wewe mama kuwa na huruma hata kidogo jamani, kwani sahani moja itakuletea hasara gani?.Mpe huyo binti chakula nitakilipia”. Kisha yule mzee akaniita niende kukaa pale kibandani. Nilimshukuru sana yule mzee. Chakula kililetwa, nilikifakamia kwa haraka sana kutokana na njaa iliyokuwa imenikamata vya kutosha.Yule mzee aliniangalia kwa huruma sana, akamwita yule mama akamwambia,
"Muongezee tena Sahani nyingine ya wali na mletee soda pamoja na maji ya kunywa".Kwa kweli nilimshukuru sana yule mzee. Nilikula kile chakula chote nikakimaliza.Baada ya hapo yule mzee akajitambulisha anaitwa Mchungaji Jakson, anaishi Dar-es-salaam.Nikamuuliza,
"Kwani hapa ni wapi?"akaniambia.
"Hapa panaitwa kibaha, kwani wewe umetokea wapi?".Nikamuelezea historia yangu yote. Mchungaji Jakson akaniambia.
"Anne usijali tutaishi wote pamoja nyumbani kwangu.Nitakwenda kukutambulisha nyumbani kwangu. Wewe umeshakuwa ni sehemu ya familia yangu".Kweli niliondoka na mchungaji Jakson nikaenda hadi kwake.Tulivyofika kwake akanitambulisha kwa mke wake,wakati huo watoto wake walikuwa wamekwenda shule.Walivyorudi nikatambulishwa kwao. Walikuwa wapo Sekondari, mmoja anitwa Eric alikuwa yupo kidato cha nne,na Erica alikuwa yupo kidato cha pili.Walinipokea vizuri tukawa tunaishi pamoja,hapo nikawa sehemu ya familia ya mchungaji Jackson.
Kwa kweli familia ya mchungaji Jakson ilinipenda sana,na mimi niliwapenda sana.Ingawa nilikuwa"Roman Catholic", lakini ilipenda sana kuabudu kanisa la mchungaji Jakson.Mchungaji Jakson alijua kuhubiri, mara nyingi alivyokuwa akihubiri niliona ananilenga sana.Na mara nyingi nilikuwa nikilia, lakini mchungaji Jakson alipenda kunitia moyo akiniambia huku, akinibembeleza,
"Anne usilie hayo ni majaribu hata Ayoub alipatwa na majaribu akayashinda. Soma kitabu cha Ayoub katika agano la kale”.Hivyo kupitia faraja ya mchungaji nilikuwa nafurahi tena nikawa naendelea na shughuli nyingine kama kawaida.Eric na Erica, nilikuwa nipo karibu nao nikiwaelekeza masomo pindi walipokuwa nyumbani pale ninapopata muda wa ziada. Hata hivyo mchungaji Jakson hakujisikia vizuri kuniona muda mwingi nikikaa nyumbani.Akanitafutia nafasi katika chuo cha VETA ,nikaanza kusomea ufundi wa kushona nguo.
Kufikia hapo, nikanyamaza kumsimulia Thomas hadithi yangu.
“Sijui MUNGU hapendi jamani”.Nilijikuta nikisema hivyo, Thomas akanizuia kwa kuniambia,
"Anne tafadhali usiseme hivyo unamkufuru MUNGU".
Nikaendelea.
Mchungaji Jakson alipatwa na ajali mbaya ya gari wakati anatoka kuhubiri.Kwa kweli alihumia sana na alisafiri mwenyewe, mke wake alimuacha nyumbani.Hivyo alilazwa hospital ya muhimbili kwa muda wa wiki moja.Alikuwa ameshakata kauri, hakuwa akijitambua wala kuongea. Nililia sana, nilifunga kwa muda wa siku saba nikimuombea mchungaji Jakson.Lakini MUNGU alimpenda sana Mchungaji Jakson, alishatimiza ile kazi aliyomtuma alimchukua.
Oh! Oh! mchungaji Jakson alifariki dunia,nililia huku nikijifuta machozi. Thomas alinikumbatia akinibembeleza huku, akinipiga piga mgongoni, akiniambia
"pole,pole Anne jikaze, hayo ndiyo majaribu ya dunia MUNGU yupo pamoja nawe nitakusaidia”.Nikanyamaza na nikaendelea kusimulia.
Baada ya mchungaji Jakson kufariki ndugu walikusanyika na kupanga mipango ya mazishi.Hatimaye baada ya siku mbili mchungaji Jakson alipumzishwa katika nyumba yake ya milele.
Kwa kawaida baada ya mazishi ndugu wanakusanyika na kukaa kikao na kupanga mambo mbalimbali.Baadhi ya ndugu walinishangaa kwanini niko pale.Mke wa marehemu mchungaji Jakson akanigeuka huku akiniambia.
"Anne hautambuliki kama wewe ni mtoto wa hapa hivyo inabidi uondoke".Baadhi ya ndungu walinishangaa zaidi uwepo wangu pale. Wakajadiliana hatimaye wakaamua kuniambia niondoke pale kwa vile mimi siyo sehemu ya familia, hivyo kile kikao hakinihusu.Nikapewa siku moja nikusanye kila kilicho changu na kuondoka kabisa. Kiukweli nililia sana,Eric na Erica walilia nao walilia zaidi huku wakimwambia mama yao aache roho mbaya,na zaidi walimuambia kuwa mimi nilikuwa nawasaidia masomo yao. Lakini mke wa mchungaji Jakson hakukubali.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nikaondoka pale kwa mchungaji Jakson huku nikiwa sijui ninakoelekea. Nilitembea mpaka Ubungo kwenye kituo cha daladala, nikawa nimekaa naziangalia daladala nyingi zikiwa zinapita.Nilikaa kwa muda mrefu nikijiuliza nitakwenda wapi na pale kwa marehemu mchungaji Jakson nimeshafukuzwa.Ghafla wakati nipo kwenye mawazo hayo, ikaja daladala ikasimama jirani yangu, akashuka konda akawa anasema"kariakoo,kariakoo miatatu vipi dada twende".Hapo hapo likanijia wazo la kwenda kariakoo. Nikapanda daladala nikaenda kariakoo.
Ndipo nilipoanza maisha mapya nikiwa ndani ya Karikoo, nikilala kwenye vibaraza vya wahindi na kuwalipa walinzi ujira mdogo.Bahati nzuri nilikutana na mama Hadija aliyekuwa MAMA NTILIE, ndiyo nilikuwa namsaidia kazi, huku akiwa ananilipa ujira ambao haukukidhi haja za maisha yangu,lakini nilimshukuru kwa yote.Na siku uliyoniokota pale barabarani, Mama Hadija alikuwa amenipa hela za kwenda kununulia mafuta.Kuna vibaka wawili walikuwa wameniona wakanifuatilia na kuniambia wananisindikiza,kufika mbele wakanigeuzia kibao.Wakaniambia niwape zile hela nilizopewa na mama Hadija, nilisita kuwapa wakanitolea kisu na kuanza kunitishia ndipo nikawapa zile hela.Walivyochukua tu zile hela, wakaanza kupiga kelele huku wakiniambia mimi ni mwizi. Watu wengi wakaja wakanipiga mpaka nikapoteza fahamu mpaka pale uliponikuta na kunisaidia kunipeleka kwa Dokta Hans.Hiyo ndiyo historia ya maisha yangu Thomas.Nilimaliza kwa kumwambia hivyo Thomas.Thomas alihuzunika sana akaniambia,
"tupo pamoja Anne, usijali sitakutupa kuanzia leo wewe utaishi hapa pamoja name. Nilifurahi sana,nikamshukuru sana Thomas huku nikimwambia,
"Thomas Mungu ndiye atakae kulipa".Thomas akaitikia
"amina"
******
Siku iliyofuata mimi na Thomas tuliongozana kuelekea kariakoo kwenye kibanda cha mama Hadija.Mama Hadija alipotuona alifurahi sana akaniambia.
"Anne mwanangu nilishakata tamaa na wewe nikajua umenikimbia na kutoroka baada ya kukupa hela zangu."
Nilimsimulia yaliyonikuta mama Hadija alilia sana.Baadaye akamshukuru Thomas kwa msaada wote alionisaidia.Kisha nikamwambia mama Hadija kuanzia leo na kuendelea nitakuwa naishi na Thomas.Thomas alinunulia Simu nikampa namba zangu. Thomas akamkabidhi Mama Hadija pesa taslimu shilingi laki mbili za kuendeleza biashara. Mama Hadija alitushukuru sana.Baada ya hapo tukaagana na mama Hadija nikamuhaidi mama Hadija kumtembelea mara kwa mara.
******
Maisha kwa Thomas hayakuwa mabaya, alinifungulia saluni na duka la vipodozi nikawa msimamizi mkuu na vyote vilikuwa mali yangu.Na maisha ya nyumbani kwa Thomas yalikuwa mazuri,alinielekeza kugusa kila mahali isipokuwa chumba kimoja aliniambia nisikifungue kabisa.Wakati mwingine nilimuuliza Thomas kwanini anaishi peke yake,na ndugu zake wako wapi?alinijibu kuwa ikifika siku nitawajua nisiwe na wasiwasi.Hayo ndio yalikuwa maisha yetu ya kila siku.
Siku moja usiku Thomas alirudi jioni akaniomba nijiandae tuna mtoko.Nilijiandaa vizuri,na kwa kweli nilipendeza sana. Nilivaa gauni la rangi ya pinki, viatu vyeusi na pochi la pinki.Hata Thomas aliponiona hakusita kunisifia. Tukaingia kwenye gari na kuanza safari hadi Serena hotel.
Siku hiyo ilikuwa mara ya kwanza kuingia kwenye ile hotel kwa upande wangu.Muhudumu alikuja haraka baada ya kuingia pale na tukamuagiza chakula.Wakati tunaendelea kupata vinywaji na chakula,Thomas alianzisha mazungumzo kwa kuniita
"Anne"nikaitika.Akaniambia,
"Anne nimeishi na wewe kwa muda wa miezi sita, ni muda mrefu sana, na nimegundua hauna mwanaume.Ukweli nimekupenda, nimegundua wewe unafaa kuwa mke wangu".Aliongea hayo huku akiniangalia, nilihisi aibu nikainamisha macho yangu chini.
Sikutaka tuangaliane na Thomas.Thomas akafungua mdomo wake tena na akaniuliza,
"je upo tayari?"nilipigwa na butwaa nikashindwa nijibu nini huku midomo yangu ikitetemeka.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment