Simulizi : Kwa Nini Mimi?
Sehemu Ya Nne (4)
ILIPOISHIA
Siku hiyo ilikuwa mara ya kwanza kuingia kwenye ile hotel kwa upande wangu.Muhudumu alikuja haraka baada ya kuingia pale na tukamuagiza chakula.Wakati tunaendelea kupata vinywaji na chakula,Thomas alianzisha mazungumzo kwa kuniita
"Anne"nikaitika.Akaniambia,
"Anne nimeishi na wewe kwa muda wa miezi sita, ni muda mrefu sana, na nimegundua hauna mwanaume.Ukweli nimekupenda, nimegundua wewe unafaa kuwa mke wangu".Aliongea hayo huku akiniangalia, nilihisi aibu nikainamisha macho yangu chini.
Sikutaka tuangaliane na Thomas.Thomas akafungua mdomo wake tena na akaniuliza,
"je upo tayari?"nilipigwa na butwaa nikashindwa nijibu nini huku midomo yangu ikitetemeka.
ENDELEA
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
PENZI LA KWELI DAIMA UANZA NA HISIA KALI, LAKINI UNAPOTOKEA MTAFARUKU HUWA NI CHUNGU KAMA SHUBIRI.
Niliinama kwa aibu kwa muda wa dakika mbili,ndipo nilipofungua mdomo na kumwambia Thomas naomba unipe muda wa wiki moja nifikirie kwanza.
Thomas akaniambia , sawa wewe ndio mwamuzi wa mwisho siwezi kukulazimisha.Akasema atasubiri siku ya uamuzi aone itakuwaje.Tuliendelea na habari nyingine huku tukipata chakula na vinywaji tulivyoagiza na baada ya kumaliza, tukarudi nyumbani huku nikikumbuka kuwa nilimuomba Thomas anipe muda wa wiki moja nijifikirie halafu nimpe jibu.
Kwa muda wote wa wiki moja nilikaa nikijifikiria Thomas alivyonisaidia, mpaka nilipo sasa. Nikaona kweli Thomas anafaa kuwa Baba wa watoto wangu na sikuwa na kipingamizi kuhusu ilo.
Ilikuwa ni jumamosi tulivu siku hiyo nilipanga nimpe jibu Thomas. Nilijiandaa vizuri baada ya chakula cha mchana kisha nikamuomba Thomas twende Ufukwe Wa Coco kupunga upepo.Thomas alinikubalia na tukaanza safari. Njiani tulikuwa tukiongea mambo mbalimbali ya hapa na pale.Thomas alikuwa ni muongeaji mzuri sana na mcheshi, sikuchoka kumsikiliza muda wote. Mara nyingi nilifurahia soga zake.Tukafika ufukweni na tukachagua sehemu nzuri ambapo kulikuwa na Hotel, tukakaa.Huku tukiendelea na maongezi ya hapa na pale nikaanza kumwambia Thomas.
"Nimekaa kwa muda mrefu na wewe, nimekuchunguza na kukuangalia mwenendo wa tabia zako na nimeridhia ombi lako uliloniambia wiki iliyopita la wewe kutaka kuwa na mimi,nimekubali niwe mtu wako wa karibu”.Ndugu msomaji Thomas alichanganyikiwa akaniambia.
"Would you marry me?"Yaani tutaoana? Na mimi nikamjibu,
"Yes I will marry you even today"Yaani ndiyo tutaona hata leo.
Thomas alifurahi sana. Hapo hapo akanyanyuka akanikumbatia na kunibusu huku akiniambia.
"Anne nakuhaidi sitakutenda, nitakupenda daima, utakuwa ni mke wa maisha mpaka hapo kifo kitakapotutenganisha”.
Siku hiyo tulivyorudi nyumbani nililala chumbani kwa Thomas.Kilichoendelea humo ndani ni siri ya watu wawili.Hapo ndipo tulipofungua pazia letu rasmi la mapenzi,huku Thomas akisisitiza ni lazima tufunge ndoa ya bomani kwanza wakati akihangaikia ndoa ya kanisani.
Niliendelea vizuri na biashara zangu na kila mara Thomas alikuja kunitembelea kazini kwangu.Mara nyingi tuliongozana na Thomas katika matembezi mbalimbali,kifupi tulikuwa kama kumbikumbi.Vitendo vile vilisababisha hata watu wa mtaani waanze kutuonea wivu. Katika saluni yangu nilikuwa na mfanyakazi aliekuwa ananisaidia aliitwa Joyce.
Joyce alikuwa ni sawa na rafiki yangu.Mara nyingi alikuwa akiniambia kuwa nisimuache Thomas, kwa sababu tunapendeza kweli, mapenzi yetu yamekuwa mfano wa kuigwa hapa mtaani.
******
Baada ya miezi miwili tulifunga ndoa ya bomani huku wasimamizi wakuu wakiwa ni Daktari Hans na mke wake Jane. Siku hiyo nilipendeza sana ingawa katika hiyo harusi yetu sikumuona hata ndugu moja wa Thomas.Nilivyomuuliza Thomas kuhusu ndugu zake aliniambia
"hakuna umuhimu wa ndugu zangu kuwepo hapa, tunachotaka ni ndoa na tumeshafunga".
Harusi yetu ilifana sana, kaka yangu John na wifi walikuja kuhudhuria. Lakini kwa bahati mbaya sikufanikiwa kumpata kaka Zakaria. Hata nilivyokwenda kwake wapangaji wenzake waliniambia kuwa alihama, wana muda mrefu hawajamuona na hawajui amehamia wapi.Nilikwenda kule kijiweni kwake, mateja wa kijiwe kile walinipa jibu lile lile kuwa hawajui alipoenda.
Ingawa nilikuwa naolewa na kuonesha furaha lakini sikuwa na amani ya roho kabisa, nilipenda ndugu zangu wote washereheke harusi yangu na mafanikio yangu. Mara nyingi nilikuwa namfikiria kaka yangu Zakaria amekwenda wapi?
Basi baada ya kutoka bomani tulikwenda kwenye ukumbi kwa ajili ya kusheherekea harusi yetu.Watu walikuwa wamejaa sana. Nilimuuliza Thomas hela zote za kuwalisha wale watu amezipata wapi? maana Thomas hakutaka vikao vya harusi vifanyike na wala kuundwa kwa kamati ya harusi yetu.Alichonijibu ni kuniuliza huku ananielekeza na baadaye kulipoteza swali nililomuuliza,
“Kwani hujui mimi ni mfanyabiashara maarufu? Na ninajulikana sana. Hawa ni baadhi ya marafiki zangu, nimependa wajumuike nasi, wengine utawajua taratibu mke wangu.Tafadhali chukua kinywaji unywe tushereheke harusi yetu”.
Sherehe iliendelea 'MC' aliipamba sherehe katika ukumbi ule uliyokuwa umepambwa ukapambika.Hakika watu walikula na kusaza, kwa kifupi harusi yetu ilipendeza sana
******
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya harusi maisha yaliendelea.Thomas akazidisha upendo kwangu na mara nyingi alikuwa akiniambia kuwa kila siku ananiona mpya. Tukazidisha mahaba motomoto kadiri muda ulivyoenda.
Siku hiyo Nilimuuliza Thomas kwanini amenizuia nisikifungue kile chumba kilichofungwa cha pale nyumbani?Thomas alikasirika sana akaniambia
"Hivi wewe Anne unakosa nini kwangu mpaka uniulize hayo maswali.Kwani hauli chakula? Hauvai?
Sitaki uniulize tena hilo swali la kuhusiana na hicho chumba.Chumba ni cha kwangu na mwenye mamlaka nayo ni mimi siyo wewe, sawa?”.
Siku hiyo Thomas alikuwa amekasirika sana. Aliondoka nyumbani muda ule wa mchana.
Nilimsubiri sana, lakini siku hiyo Thomas hakurudi kabisa nyumbani bali alirudi asubuhi siku ya pili akiwa amelewa. Alipitiliza mpaka chumbani akalala.Niliogopa kumuuliza alikuwa wapi maana ningeanzisha ugomvi mwingine.Tuliendelea na mapenzi yetu vizuri lakini niliona Thomas amebadilika kweli, hakuwa Thomas yule wa zamani niliekuwa namjua.
Siku hiyo nilikuwa saluni ninashughuli zangu, nikapigiwa simu na mlinzi kuwa nyumbani kuna mgeni anadai ni mdogo wake Thomas.Nilimwambia mlinzi ampe kiti akae anisubiri mimi nifike pale nyumbani, mimi ndie nitakaetoa maamuzi.Nilitoka haraka pale saluni, nikaenda kwenye gari yangu aina ya Escudo ambayo Thomas alinipa kama zawadi baada ya kumkubalia tufunge ndoa.
Nilipofika nyumbani nikamuona msichana ayekuwa amefanana sana na Thomas.Pasipo kuuliza bila ubishi nikajua kabisa yule ni mdogo wake Thomas.Alikuwa amebeba begi dogo, akanisalimia akajitambulisha anaitwa Eve. Akaniambia kwao walizaliwa watano, ndugu zake watatu wamefariki vifo vya kutatanisha.Hivyo wamebaki yeye na Thomas,Thomas ndiye alikuwa anajiweza lakini haijali familia yao.Nilimueleza ukweli Eve kwa kumuambia kuwa,kila nikimuambia Thomas anitambulishe kwa ndugu zake anakuwa mkali.
Eve akaniambia kwa kuniomba kama wifi yake, nimsaidie kumuambia kaka Thomas awakumbuke.Nilimuonea huruma sana Eve.
Nikampigia simu Thomas, nikamueleza mdogo wake amefika nyumbani.Thomas alichanganyikiwa akaniuliza mara ya pili.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Umesema yupo hapo nyumbani?"
Nikamjibu "Ndio kwani vipi?"
Akaniambia"Nakuja".
Akakata simu huku mimi nikabaki nikiwa sielewi Thomas anakuja nyumbani kwa lipi? Wakati nimekaa nikiwaza kwanini Thomas amebadilika vile kwenye simu.Eve alikuwa amemaliza kunywa kinywaji nilichompa akawa ananiita.
"Wifi,wifi"mpaka akaja kunitingisha nikashtuka, nikamwambia Eve nilikuwa mbali kidogo nikiwaza maisha tu ya kawaida.
Wakati tukiendelea na maongezi ghafla Thomas aliingia ndani akiwa amekasirika.Moja kwa moja akamfuata Eve, akamshika nywele akawa anazivuta.Huku akiongea kwa hasira akasema,
“ Nakuuliza wewe mpumbavu, nani amekwambia uje kwangu?, Nani amekutuma?".Nikamuwahi Thomas nikamwambia.
"Huyo ni ndugu yako wa damu, lakini kwanini unamfanyia hivyo?.Thomas akaniambia kwa ukali,
"Anne kama unanipenda nenda chumbani tafadhali na uniletee virago alivyokuja navyo huyu mpuuzi. Nampa nauli sasa hivi arudi kwao alipotoka."
Nililia sana nikamwambia Thomas kuwa amuache alale hata kwa usiku wa leo ataondoka kesho.Thomas akasema kwa hasira hatakiwi kulala hapa atanisababishia matatizo makubwa.Basi Thomas alimchukua Eve kwa nguvu akampa nauli na hela ya kwenda kulala hotelini.Wakati naenda kumchukulia Eve mizigo yake, ndani ya mfuko nilimwekea elfu hamsini na nikamwandikia namba zangu za simu nikamuwekea kwenye nguo zake.Nilimuonea huruma sana. Hivi ndivyo Eve alivyofukuzwa na kaka yake pale nyumbani.
****
Baada ya miezi miwili nikahisi dalili za kuumwa, nilikuwa nasikia dalili za uchovu na kutapika na kichefuchefu kisichoisha.Thomas akanipeleka kwenye hospital ya dokta Hans.
Dokta Hans alichukua vipimo vyote akaniambia nirudi kuchukua majibu siku ya pili.Kesho yake Thomas alikuwa na mkutano hivyo aliniacha niende mwenyewe hospitalini.Dokta Hans alifurahi sana akanipa majibu yangu huku akiniambia.
"Anne hongera ndoa imejibu.Una ujauzito wa mwezi mmoja”. Nilifurahi sana nikampigia simu Thomas hapo hapo.Nilivyomueleza Thomas juu ya ujauzito wangu,Thomas alibadilika akasema
"Anne haiwezekani ushike ujauzito, hiyo mimba lazima uitoe”.
KUKICHUKIA KIUMBE ULICHOKIWEKA TUMBONI SIYO VIZURI MPAKA KUFIKIA HATUA YA KUKITOA. NA UPENDO KWA NDUGU ZAKO NI JAMBO LA BUSARA KATIKA MAISHA YA SASA.
Nilitoka pale hospitali kwa Dokta Hans nikiwa nina mawazo sana.Furaha yangu yote ya kushika ujauzito ikawa imefutika.Nilivyofika nyumbani sikutamani kula chakula hata kidogo.Nikaingia kitandani, sikumbuki hata nililala kwa muda gani. Nilishtuka Thomas akiwa amesimama pembeni ya kitanda akinitingisha kwa nguvu huku akiita jina langu.
“Anne, Anne, hamka tafadhali tuongee"Niliamka na kukaa kitako pale pale kitandani huku nikimuangalia Thomas.Thomas alianza kwa kusema
"Anne kama unanipenda mimi mume wako, tafadhali itoe hiyo mimba. Mimi sipo tayari kuilea wala kuchangia gharama zozote”.Nikamjibu huku nikionesha msisitizo kwa nisemacho,
"sitoi hii mimba,na nitailea mimi mwenyewe”. Kwa mara ya kwanza nilimuona Thomas akinipigia magoti huku akilia.
"Anne nionee huruma tafadhali, niko chini ya miguu yako, itoe hiyo mimba tuishi kwa raha”. Na mimi machozi yakawa yananitoka mengi kama mvua ya El-nino nikamjibu Thomas.
"Sitatoa hii mimba, ni dhambi kubwa sana kukitoa kiumbe cha MUNGU. Lakini kwani hii mimba inakosa gani?.Nipo tayari kutumia gharama zozote zile kuilea hii mimba kama hauitaki”.Thomas hakunijibu kitu. Alinyanyuka pale alipokaa na kuondoka.
Aliniacha nikiwa ninalia huku nimekaa pale kitandani. Nililia sana mpaka sauti ikakauka na hapo hapo nikapitiwa tena na usingizi.Nilikuja kushtuka saa tano usiku, kuangalia pembeni ya kitanda sikumuona Thomas.Nikampigia simu,simu yake ikawa inaita haipokelewi.Nikanyanyuka nikaenda mpaka getini kumuulizia mlinzi kama Thomas amemuachia maagizo yoyote.Yule mlinzi alichonijibu ni kuwa alimuona Thomas akiingia kwenye gari na kuondoka, hajamuachia maagizo yoyote.Nilibaki nimechanganyikiwa huku nikijawa na wasiwasi,ikanibidi niingie ndani kulala.
Asubuhi nilivyoamka sikuwa na amani kabisa, nilijaribu tena na tena kumpigia simu Thomas lakini nilichosikia ni sauti ya mashine inayosema namba unayopiga haipatikani.Nikazidi kuchanganyikiwa na kuanza kuwapigia simu marafiki wa Thomas na kuwauliza kama wamemuona.Walichonijibu ni kuwa, hawajamuona Thomas muda kidogo umepita.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilikaa nyumbani zaidi ya siku mbili nikiwa sina raha,na Thomas hakuonekana nyumbani katika hizo siku mbili. Sikuwa naelewa yuko wapi, ndipo siku ya tatu mlinzi alinifuata akaniuliza kama nilishakwenda kazini kwa Thomas kumwangalia. Nikakumbuka kuwa nilikuwa sijaenda.
Hapo hapo nikatoka nje kwa gari yangu na kuanza kuelekea kazini kwa Thomas. Niliendesha kwa kasi ya ajabu sana. Mpaka kufika kazini kwa Thomas ni mwendo wa saa moja lakini siku hiyo nilitumia nusu saa tu mpaka kufika ofisini kwa Thomas.Nilivyofika kazini kwa Thomas, nilikuta wafanyakazi wakiendelea na kazi zao.Walinisalimia lakini sikuwajibu kitu kilichowafanya wabaki wananishangaa tu.
Nikafika mpaka mapokezi, niliwasalimia baadhi ya wafanyakazi waliokuwa pale,kisha nikawauliza
"Thomas yupo?" Secretary akaniambia.
"Yupo ngoja nimpigie simu"nikamjibu yule secretary
"Unampigia simu kwa nini?Kwani haujui mimi ni nani kwake?"kabla hajanijibu kitu nikawa nimeshaelekea ofisini kwa Thomas.
Nilivyoingia kwenye ofisi ya Thomas, hali niliyomkuta nayo Thomas ilinisikitisha sana.Ofisi ya Thomas ilikuwa imevurugwa mno.Kulikuwa na chupa za konyagi mbili na glasi, alikuwa akiendelea kunywa pombe.Pembeni yake alikuwa amekaa rafiki yake alikuwa akijitahidi kumbembeleza Thomas aache kunywa pombe lakini Thomas hakuwa akikubali kuacha kunywa, alichokuwa anasema ni
"Anne unaniua uko wapi?Namtaka Anne wangu jamani".Rafiki yake Thomas aliponiona tu, alifurahi akasema.
"Afadhali shemeji umekuja labda utaweza kumbembeleza huyu mtu mpaka akakuelewa, mimi nimeshindwa".Thomas aliponiona akaanza kufurahi huku akiniambia
"Karibu mke wangu".Yule rafiki yake Thomas akasema
"Ngoja niwapishe mimi natoka mara moja".Thomas alinivuta tukaenda kukaa kwenye kiti cha ofisini, halafu akaniambia.
"Anne unanipenda kweli? na unataka tuendelee kuishi pamoja?"nikamjibu
"Ndio nakupenda mume wangu".Akaniambia
"Basi itoe hiyo mimba tutaendelea kuishi kama zamani.Nilibaki nikiwa ninalia machozi yaliyokuwa yakimiminika kwa fujo mpaka nikawa sioni.Nilibaki nikijiuliza nafsini mwangu nifanye nini?.Nichague mimba au Thomas?.
Nilimuonea huruma sana Thomas. Alikuwa amebadilika sana,ngozi ya mwili wake ilipauka,nywele zake zilikuwa hazijapitishwa chanuo nafikiri Ilikuwa ni siku ya pili sasa.Ikabidi nimkubalie
"Ndiyo nipo tayari mume wangu kuitoa hii mimba".Machozi yalikuwa yakinitiririka huku nikijilaumu kwa kumkosea MUNGU wangu.Thomas aliruka kwa furaha akanikumbatia kwa nguvu akaniambia,
"I love you my Anne"Sikujibu kitu zaidi yakumuambia Thomas twende nyumbani kwa ajili ya kupumzika. Thomas akakubali,kisha tukaanza safari ya kuelekea nyumbani.Kesho yake tukaenda hospitali kwaajili ya kutoa mimba,lakini haikuwa hospital ya Dokta Hans.
Nililia sana wakati napanda kitandani kwa ajili ya kutolewa mimba huku nikimuomba MUNGU wangu anisamehe kwa dhambi ambayo sikukusudia.Nilisikia maumivu makali sana wakati wa lile tendo.Tulipofanikiwa Dokta alinipa pole na dawa za kunywa kwa ajili ya kutuliza maumivu.
Tukarudi nyumbani na Thomas huku akiwa na furaha kuu usoni pake. Alikuwa amechanua tabasamu ambalo nilikuwa sijapata kuliona, wakati mimi muda wote nilikuwa nalia. Thomas aliniambia
"Anne usilie, nakupenda mke wangu, ahsante kwa kunisikiliza".Nilikasirika nikamwambia
"Thomas umeniacha na majonzi ambayo yatanitesa kwa muda wa miaka kumi na nne mpaka kuja kusahau”.Nikamkumbuka padri mmoja aliwahi kutufundisha kanisani wakati wa mafundisho ya kipaimara.Alisema kuwa, mwanamke akishatoa mimba anakaa kwa muda wa miaka kumi na nne mpaka kuisahau hiyo dhambi.Na kama akizaa motto kabla ya hiyo miaka kumi na nne kufika, basi ataathiriwa na ule ujauzito wa kwanza aliokwisha toka.Hivyo yampasa akae kwa miaka kumi na nne ndiyo azae mtoto aliye salama.
Yule padri alitufundisha athari za mtoto aliyezaliwa kabla ya muda huo kuwa ni, kumchukia mzazi au kujichukia yeye mwenyewe.Nilibaki nikikumbuka na kutafakari mafundisho ya yule padri huku nikilia.
Tulivyofika nyumbani nikamuambia Thomas sihitaji kukaa pale nyumbani.Bali nahitaji kwenda mbali kwaajili ya kupumzika.Thomas akaniambia nichague sehemu ya kwenda atanipeleka bila ya hiyana, nikachagua nyumbani kwao Thomas.
Thomas akashangaa lakini ikabidi akubali kunipeleka kwao kwa vile alijua nilikuwa nimekasirika.Nikamuomba namba ya wifi yangu Eve niwasiliane naye, akaniambia hana.Nikamuambia fanya kila njia ili Eve ajue kama naenda nyumbani. Akaniambia kuna jirani yao atampa taarifa,yeye ndiye ataenda nyumbani kutoa taarifa.
Baada ya siku mbili tulifunga safari na kwenda Kilimanjaro nyumbani kwa akina Thomas.
****JE, WALIVYOFIKA KILIMANJARO ILIKUWAJE?
NA ANNE ALIPOKELEWAJE NA ALIIKUTAJE HALI YA KULE?
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment