Simulizi : Mimi Ni Mwenye Dhambi Nisamehe Mungu
Sehemu Ya Tatu (3)
Mara baada ya kumaliza kidato cha nne katika shule ya Uhuru mkoani Kilimanjaro, msichana Catherine Mushi akarudi nyumbani kwa ajili ya kusubiria matokeo yake ya kidato cha nne. Siku zote katika maisha yake ya nyumbani, Catherine alikuwa mtu wa kuendelea kuwa karibu na Samuel ambaye alionekana kuwa na mapenzi ya dhati kwake.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/--
Ukaribu wao wa kimapenzi ambao walikuwa nao nyumbani ulikuwa ukiendelea kama kawaida jambo ambalo kwao likaonekana kuwafurahisha na kuyakomaza mapenzi yao hayo ambayo katika kipindi hicho yalionekana kuwa juu sana. Katika maisha yake, Catherine hakujutia kitendo chake cha kuwa na Samuel, kwake alionekana kuwa mwanaume bora ambaye angeweza kumhitaji katika kipindi chote cha maisha yake.
Mara kwa mara alikuwa akionana na Samuel huku wakati mwingine wakiongea simuni kama kawaida yao. Hakutaka kupiga hatua za kurudi nyuma, kila siku walikuwa wakitaka kupiga hatua kwenda mbele zaidi katika mahusiano yao ambayo yalionekana kukua kila siku. Katika kichwa cha Catherine bado kulikuwa na kitu ambacho kilikuwa kikimsumbua sana kwa wakati huo, matokeo ya kidato cha nne.
Japokuwa alikuwa huru na mwanaume ambaye alikuwa akimpenda sana lakini bado Catherine hakuonekana kuwa na amani. Matokeo ambayo yalitarajiwa kutoka baada ya miezi kadhaa yalionekana kumsumbua sana kichwa chake. Hakuwa amesoma vya kutosha, maisha ya kutoroka usiku na kwenda katika kumbi za starehe ndio maisha ambayo alikuwa ameishi sana shuleni Uhuru mkoani Kilimanjaro.
Baada ya miezi kukatika na hatima matokeo kutoka, kile ambacho kila siku alikuwa akikitarajia ndicho ambacho kilikuwa kimetokea. Kama ilivyokuwa kwa wenzake watatu, Samuel, Sadiki na Mariamu ndio ambayo ilikuwa imemtokea hata yeye mwenyewe, alikuwa amefeli vibaya. Hilo likaonekana kuwa pigo la kwanza katika maisha yake, lilikuwa ni pigo kubwa na baya ambalo halikuweza kubebeka kwa urahisi moyoni mwake.
Hapo ndipo maisha ya majuto yalipoanza kumkumba. Mara kwa mara alikuwa akijutia aina ya maisha ambayo alikuwa akiishi shuleni kule katika kipindi cha nyuma. Maisha ya anasa ambayo alikuwa akiishi na wenzake ndio ambayo yalikuwa yamemletea matokeo yale ambayo yalionekana kumkasirisha kila mtu nyumbani kwao.
“Yaani mimi napoteza fedha zangu halafu mtoto anakwenda kufanya umalaya tu” Mzee Mushi alimwambia Catherine huku akionekana kuwa na hasira.
“Msamehe, bado anahitaji nafasi zaidi ya kuyarekebisha mambo yake” Mama yake, Bi Maria alimwambia mumewe, mzee Mushi ambaye katika kipindi hicho alionekana kuwa mkali hata zaidi ya mbogo aliyejeruhiwa.
“Wewe ndiye utalifanya hili kichwa kuwa nyanya. Leo hii ametuletea sifuri humu ndani, huyu si ataweza kutuletea hata UKIMWI ndani ya nyumba hii” Mzee Mushi alimwambia kewe, Bi Maria.
“Bado tumpe nafasi” Bi Maria alimwambia mumewe.
“Nafasi. Wewe unafikiri huyu tukimpa nafasi atabadilika, hivi unafikiri hili likichwa likipewa nafasi litabadilika?” Mzee Mushi alimuuliza mke wake huku akiendelea kuwa na hasira.
“Naomba unisamehe baba. Nitabadilika” Catherine alimwambia baba yake.
Kama kumchapa alikuwa amekwishamchapa vya kutosha na katika kipindi hicho fimbo hazikuonekana kubadilisha kitu chochote kile. Kwa sababu mke wake alikuwa akimtetea sana juu ya kile ambacho kilikuwa kimetokea, mzee Mushi hakuwa na jinsi zaidi ya kukubali kumpa nafasi binti yake kwa kuamini kwamba angeweza kubadilika na hatimae kufanya vizuri.
“Nafasi ya mwisho kwako kuingia darasani. Ukishindwa bora uolewe tu” Mzee Mushi alimwambia Catherine.
“Nitajitahidi baba” Catherine alimwambia baba yake.
Baada ya mwezi mmoja Catherine akaanza masomo katika shule ya Mbezi Beach huku lengo lake likiwa ni kuyarudia masomo ambayo alikuwa ameyasoma na mwisho wa siku kurudia mitihani yake. Katika kipindi chote hicho cha kurudia masomo yake Catherine alionekana kuwa makini katika masomo yake, hakutaka kurudia makosa ambayo alikuwa ameyafanya ambayo yalimpelekea kufanya vibaya katika masomo yake.
Kazi ya kusoma kwake ilikuwa imeongezeka zaidi na alitakiwa kupigana nayo vilivyo. Katika upande mmoja alikuwa akiyasomea masomo ambayo alikuwa amefeli lakini kwa upande mwingine alikuwa akiendelea na masomo ya kidato cha tano ili endapo kama atakuja kufaulu mitihani yake basi aweze kuingia moja kwa moja kidato cha sita.
Katika kipindi hicho hakutaka kuwasiliana na Samuel, aliona kwamba endapo angewasiliana na mwanaume huyo basi hali ile ya kutokusoma ingeweza kujirudia tena na hivyo kufanya vibaya katika masomo yake. Kichwa chake alikuwa amekituliza katika kusoma, hakutaka kuyapa nafasi maisha ya anasa tena, ndani ya moyo wake alikuwa ameamua kwa asilimia mia moja kwamba alikuwa akitaka kusoma tu.
Ubongo wake ukashtuka na kisha kuanza kujiweka kama zamani. Ubize wa kusoma ambao alikuwa akijipa kila siku ndio ambao ulianza kumfanya kuanza kurudi kama alivyokuwa zamani, kipindi ambacho hakuanza kuishi maisha ya anasa shuleni Uhuru mkoani Kilimanjaro. Walimu wakautambua uwezo mkubwa ambao alikuwa nao Catherine, ulikuwa ni uwezo ambao ulimfanya mara kwa mara kuongoza katika masomo yake.
Wazazi wake wakaonekana kuwa na matumaini kwa binti yao, juhudi ambazo alikuwa akizionyesha katika masomo yake zikaonekana kuanza kuzaa matunda. Kila siku alikuwa mtu wa kujifungia chumbani na kusoma, mambo ya anasa na kutamani kufanya mambo yasiyokuwa na maana akawa ameachana nayo na katika kipindi hicho alikuwa akifikiria kitu kimoja tu, kusoma na kutimiza ndoto zake ambazo alikuwa akiziota kila siku, ndoto za kuwa mwanasheria mkubwa nchini Tanzania.
Mwaka ulipokatika, akamaliza masomo yake aliyokuwa akiyarudia na alipofanya mitihani akawa amefaulu vizuri jambo ambalo lilimfanya kuingia kidato cha sita huku akiwa na alama zote ambazo alitakiwa kuwa nazo katika matokeo yake.
“Naona kama ndoto zangu zinakaribia kutimia Scola” Catherine alimwambia rafiki yake wa karibu ambaye mara kwa mara alikuwa akipenda kusoma nae.
“Kila kitu kitakwenda kutimia, cha msingi ni kuongeza juhudi tu. Mbona unaweza sana tu Catherine” Scola alimwambia Catherine ambaye alionekana kufarijika.
“Nitataka kuwa mwanasheria katika nchi hii” Catherine alimwambia Scola.
“Kama ukipigana na kusoma sana, utakuwa tu, hakuna kinachoshindikana chini ya jua” Scola alimwambia Catherine ambaye aliendelea kusoma zaidi na zaidi.
Catherine akaonekana kubadilika kabisa, shuleni hapo akaonekana kuwa mkali zaidi ya wanafunzi wote ambao walikuwa kidato cha sita. Katika kipindi hicho aliona kusoma ndicho kilikuwa kitu pekee ambacho kingemfanya kutimiza ndoto zake za baadae, ndoto za kuwa mwanasheria nchini Tanzania. Wanafunzi wengi wa kike na wa kiume walikuwa wakivutiwa na Catherine ambapo mara kwa mara walikuwa wakitamani kuwa karrbu nae na kisha kuwafundisha.
Shuleni hapo, wanafunzi wengi waliambiwa kuiga tabia za Catherine ambaye kila siku alionekana kuwa moto shuleni hapo. Catherine hakutaka kuyakumbuka maisha yake ya nyuma ambayo alikuwa amepitia, kitu ambacho alikuwa akikitaka kwa wakati huo ni kuyafikiria maisha yake ya mbele na kutimiza malengo yote ambayo alikuwa amejiwekea moyoni mwake.
“Vipi kuhusu mapenzi?” Fatuma alimuuliza Catherine.
“Mapenzi hayafai katika kipindi ambacho unahitaji muda wa kusoma” Catherine alimwambia Fatuma.
“Kwa nini? Ulikwishawahi kuumizwa nini?”
“Hapana. Namshukuru Mungu kwa sababu mpaka leo sijawahi kuonja maumivu ya mapenzi maishani mwangu” Catherine alimwambia Fatuma ambaye akabaki akiachia tabasamu.
“Mmmh! Sawa. Ila kuna tu alikuwa akitaka kuongea na wewe” Fatuma alimwambia Catherine.
“Nani?”
“Edmund”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kuongea na mimi kuhusu nini?”
“Wala sijui au nikuitie umsikilize” Fatuma alimwambia Catherine.
Edmund alikuwa miongoni mwa vijana wa shule ile ambao walikuwa wakivutiwa sana na uzuri wa Catherine. Kila siku Edmund alikuwa mvulana wa kumwangalia sana Catherine ambaye alikuwa akisoma nae darasa moja. Kwa Catherine, katika kipindi hicho hakuwa akiyatamani mapenzi, alijua kwamba mapenzi hayo hayo yalikuwa yamempotezea muda wake mwingi sana na hivyo hakutakiwa kurudi kule alipotoka.
Japokuwa Edmund alikuwa akimpenda sana Catherine lakini moyo wake ulikuwa umejaa woga mwingi. Hakuwa akiamini kama angeweza kusimama na Catherine na kisha kumueleza ukweli juu ya alivyokuwa akijisikia kwamba alikuwa akimpenda sana. Kila siku alibaki kuwa mtu wa kumwangalia Catherine na kumsifia moyoni kwamba alikuwa msichana mzuri ambaye alitakiwa kuwa na mtu kama yeye.
Edmund hakuwahi kumsogelea Catherine na kumwambia ukweli juu ya jinsi alivyokuwa akijisikia. Kwanza alikuwa akimuogopa sana msichana huyo ambaye alionekana kujiamini kupita kawaida. Kila alipokuwa akisimama mbele ya mvulana yeyote yule Catherine alionekana kuwa msichana imara, msichana asiyetetereka hata kidogo jambo ambalo lilikuwa likiwatia hofu wanaume wengi shuleni hapo.
Wale wanaume ambao hawakuwa wakiogopa kitu chochote wakajitoa mhanga na kisha kumfuata Catherine na kumueleza ukweli juu ya jinsi walivyokuwa wakijisikia mioyoni mwao. Kwa Catherine hakuonekana kuwakubali, kila siku katika maisha yake aliyaona mapenzi kutaka kuzima ndoto zake ambazo alikuwa amejiwekea toka alipokuwa kidato cha kwanza. Ni kweli kabisa mapenzi yalikuwa yamechukua nafasi moyoni mwake na hatimae kumfanya kufeli vibaya masomo yake, katika kipindi hicho hakutaka tena kuwa na mwanaume yeyote yule.
“Nayachukia mapenzi” Catherine alimwambia Scola.
“Kwa nini?”
“Yanaweza kukufanya kutokukamilisha ndoto zako” Catherine alimwambia Scola.
“Mmmh! Ila wavulana wengi wanakupenda hapa shuleni” Scola alimwambia Catherine.
“Najua. Mara kwa mara Fatuma amekuwa akiniambia hivyo”
“ Sasa haukuchukua hata hatua?”
“Hatua gani?”
“Kuwa hata na mmojawapo”
“Hapana. Hilo ni jambo gumu sana. Siwezi kuwa na mwanaume yeyote yule shuleni hapa” Catherine alimwambia Scola.
Japokuwa Catherine alikuwa akiendelea kuonyesha msimamo wake lakini wanaume hawakukoma, kila siku walikuwa wakimfuata lakini Catherine hakuonekana kukubaliana na mwanaume yeyote yule. Edmund hakutaka kukata tamaa, japokuwa wavulana wengi walikuwa wakikataliwa na Catherine lakini kila siku katika moyo wake alikuwa na uhakika wa asilimia mia moja kwamba kuna siku msichana huyo, Catherine angekuwa wake na hivyo kufanya mambo mengi kama wapenzi.
Mchungaji
Mpelele hakuelewa ni kitu gani kilikuwa kikiendelea, kila alipokuwa akimpigia
simu mtoto wake, Samuel hakuwa akipatikana simuni kabisa. Wasiwasi ukamwingia
moyoni mwake kwa kuona kwamba inawezekana kulikuwa na jambo baya ambayo lilikuwa
limemtokea mtoto wake. Alipomuuliza mke wake, Bi Magreth, nae alisema kwamba
kila alipokuwa akimpigia simu, simu haikuwa ikipatikana.
Jambo hilo
likazidi kumtia wasiwasi zaidi hali ambayo likamfanya kushauriana na mke wake
waelekee shuleni kwao, Makongo kwa ajili ya kuuliza ni kitu gani ambacho
kilikuwa kikiendelea. Katika kipindi hicho, mchungaji Mpelele hakuwa na wasiwasi
na mtoto wake kwani katika kipindi ambacho alikuwa akienda kuanza shule kwa
ajili ya kurudia mitihani yake, tayari mtoto wake, Samuel alikuwa amekwishaamua
kubadilika kwa kuanza kumtumikia Mungu.
Walipofika shule, moja kwa
moja wakaanza kuelekea katika ofisi za walimu ambapo wakahitaji kuonana na
mwalimu mkuu na kisha kuruhusiwa kuelekea katika ofisi ya mwalimu huyo.
Walipoingia, hawakuwa na muda wa kupoteza, wakajitambulisha kama wazazi wa
Samuel na walifika mahali hapo kwa ajili ya kumuona mtoto wao,
Samuel.
Kwanza mwalimu mkuu akaonekana kushtuka, akawaangalia vizuri,
uso wake ukaonekana kubadilika, mshangao wa wazi ukaonekana machoni mwake.
Hakuamini kama kweli Samuel alikuwa mtoto wa mchungaji, uso wake ulionyesha
dhahiri kushangazwa na cheo cha mchungaji Mpelele.
“Kumbe wewe ni
mchungaji?” Mwalimu mkuu aliuliza huku akionekana kushangaa.
“Ndio.
Mimi ni mchungaji wa kanisa la Praise And Worship hapo Mwenge” Mchungaji Mpelele
alimwambia mwalimu mkuu.
“Dah! Unajua kuna wakati naona kama siliamini
hili” Mwalimu mkuu aliwaambia.
“Kwa nini?”
“Kumbe Samuel ni
mtoto wa mchungaji?”
“Ndio. Kuna nini? Tunaweza kumuona?” Mchungaji
Mpelele alimuuliza mwalimu.
“Hayupo shuleni”
“Hayupo
shuleni?”
“Ndio. Huu mwezi wa pili hajafika shuleni hapa” Mwalimu mkuu
aliwajibu.
“Unatuchanganya mwalimu. Inakuwaje Samuel kutokuwa shuleni
hapa kwa kipindi kirefu namna hiyo?” Mchungaji Mpelele aliuliza.
“Huo
ndio ukweli. Ila mbona mnauliza kwa kushangaa sana?”
“Kwa sababu sisi
tunajua anakuja shule kila siku”
“Kwani kila anapofika nyumbani huwa
anawaambia nini?”
“Hakai nyumbani”
“Sasa mbona na nyie pia
mnanichanganya”
“Hakai nyumbani. Alihitaji muda wa kukaa katika
hosteli yoyote ile kwani aliamini kwa kufanya hivyo angekuwa makini na masomo”
Mchungaji Mpelele alimwambia mwalimu mkuu.
“Duh! Hii kali mchungaji.
Ndio kwanza nimeanza kuisikia kwako kwamba mwanafunzi wa sekondari anakaa
hosteli” Mwalimu mkuu alimwambia mchungaji Mpelele na Bi
Magreth.
“Hatuwezi kuonana na mwalimu wa dini?”
“Wa nini
tena mchungaji”
“Inawezekana akawa anafahamu kidogo kuhusu
Samuel”
“Kivipi?”
“Kwa sababu Samuel ni mcha
Mungu”
“Mcha Mungu! Kuanzia lini?”
“Toka alipoondoka
nyumbani”
“Mcha Mungu kivipi tena? Hapo unanichanganya
mchungaji”
“Mcha Mungu kama unavyoelewa wewe
mwalimu”
“Sidhani kama Samuel alikuwa mcha Mungu kama ninavyoelewa
mcha Mungu anavyokuwa. Mcha Mungu huwa hanywi pombe, mcha Mungu huwa afanyi
ngono” Mwalimu alimwambia mchungaji.
“Kwa hiyo una maana kwamba Samuel
alikuwa akinywa pombe na kufanya ngono?” Mchungaji Mpelele aliuliza huku
akionekana kuchanganyikiwa.
“Ndio”
“Shuleni hapa
hapa?”
“Ndio”CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Majibu ya mwalimu
mkuu yakaonekana kuwachanganya wote, wakabaki kimya, kila mmoja akaonekana
akifikiria lake kichwani mwake. Hawakuyaamini maneno yale ambayo mwalimu mkuu
alikuwa ameyasema mbele yao, hawakuamini kama mtoto wao Samuel alikuwa ameanguka
tena dhambini.
Mchungaji Mpelele akaona koti lake la suti kama linampa
sana joto, akalivua na kisha kuanza kujipepea kwa kitambaa chake huku kijasho
kikiwa kinamtiririka kupita kawaida. Kwa mke wake, Bi Magreth, alikuwa kimya,
nae alionekana kuchanganyikiwa kwa kile ambacho alikuwa amekisikia kutoka kwa
mwalimu mkuu. Hapo ndipo walipoamini kwamba shetani alikuwa akiendelea kufanya
kazi kwa mtoto wao na si kwamba alikuwa amemaliza kazi zake juu
yake.
“Haiwezekani” Mchungaji Mpelele alisema huku akionekana
kuchanganyikiwa.
“Hatuwezi kuongea na marafiki zake?” Bi Magreth
alimuuliza mwalimu.
“Toka aje katika shule hii alikuwa na rafiki yake
mmoja tu” Mwalimu alijibu.
“Huyo huyo tunataka kuongea
nae”
“Nae ameondoka pamoja nae. Yaani Samuel alipoacha kuja shule tu,
hata nae rafiki yake akaacha kuja shule. Natumaini watakuwa pamoja kwa sasa”
Mwalimu alimjibu.
“Rafiki yake yupi?”
“Anaitwa Sadiki
Hamidu” Mwalimu mkuu alijibu.
Jina hilo halikuwa geni sana masikioni
mwao, walikuwa wamekwishawahi kulisikia mara kadhaa kutoka mdomoni wa mtoto wao,
Samuel. Mpaka kufikia hatua hiyo, walikuwa na kitu kimoja tu ambacho walikiona
kwamba kilitakiwa kufanyika. Wakataka kuonana na wazazi wa Sadiki na kuzungumza
nao ili wafahamu kama nao mtoto wao alikuwa kama Samuel au ilikuwaje.
Alichokifanya mwalimu mkuu ni kuwataka wote wafike shuleni hapo kesho huku yeye
akifanya mawasiliano na Ustadhi Hamidu kumtaarifu kuhusu kuja shuleni
hapo.
Walichokifanya mara baada ya kuondoka shuleni hapo ni kuelekea
katika hosteli ya St’ Peter ambayo ilikuwa Kinondoni kwa ajili ya kuonana na
Samuel ambaye alikuwa amechukua chumba katika hosteli hiyo. Ndani ya gari kila
mtu alikuwa akiwaza lake, maneno ambayo aliongea mwalimu mkuu yalionekana
kumchanganya kila mmoja.
“Ila naona ni kama kitu kisichowezekana” Bi
magreth alimwambia mume wake, mchungaji Mpelele.
“Kwa
nini?”
“Kweli Samuel anaweza kuyarudia maisha ambayo alikuwa akiishi
kipindi cha nyuma?”
“Anaweza. Mtu husimama na kuanguka pale ambapo
anasimama mguu upande. Shetani ana nguvu sana, sisi kama wanadamu hatuwezi
kupigana nae na ndio maana tunasema vita vyetu vya nyama na damu” Mchungaji
Mpelele alimwambia mke wake, Bi mage.
Baada ya dakika kadhaa wakafika
nje ya jengo la hosteli ya St Peter ambapo wakateremka na kisha kuanza
kuusogelea mlango wa kuingia katika jengo lile. Walichokifanya mara baada ya
kuingia ndani ya jengo lile ni kuwafuata wanachuo kadhaa ambao walikuwa wamekaa
pembeni kwa lengo la kuwauliza.
“Dah! Hao watu toka mwezi uliopita
walitimuliwa hapa” Kijana mmoja miongoni mwa vijana hao
aliwaambia.
“Waliwatimua! Kisa nini?”
“Walikuwa na tabia
chafu sana. Walikuwa wakipenda sana kunywa pombe, kula mirungi, kuvuta sigara
mpaka kuleta wanawake ndani” Kijana huyo alijibu.
“Unamaanisha mambo
hayo alikuwa akiyafanya Samuel?” Mchungaji Mpelele aliuliza huku akionekana
kutokuamini.
“Ndio. Samuel Mpelele pamoja na rafiki yake, Sadiki
Hamidu” Kijana yule alijibu.
“Baada ya kutoka hapa watakuwa wameelekea
wapi?”
“Hatujui. Labda angekuwepo rafiki yao waliyekuwa anakaa nao
chumba kimoja angekuwa anafahamu”
“Rafiki yao nani?”
“Huyu
anaitwa Cosmas ila bahati mbaya nae mwenyewe alihama mahali hapa” Kijana yule
aliwaambia.
Akili zao zikazidi kuchanganyikiwa zaidi. Hapo wakaonekana
kuamini kwamba kijana wao alikuwa amepotelea katika mikono ya shetani na
yalihitajika maombi zaidi kwa kumrudisha tena. Wote wakaonekana kukata tamaa,
hawakuamini kama kijana wao, Samuel angeweza kupotealea katika mikono ya shetani
kwa mara nyingine tena.
Usiku hawakulala vizuri, hawakuwa na amani
mioyoni mwao, kitu ambacho walikuwa wakikitaka ni kufahamu mahali ambapo mtoto
wao alipokuwa katika kipindi hicho. Nusu saa kabla ya kulala, wakashikana mikono
na kisha kuanza kuomba. Sala yao kwa Mungu ilikuwa moja tu, kumrudisha Samuel
nyumbani hapo na kumbadilisha kwa mara nyingine
tena.
****
Siku iliyofuata saa tano asubuhi wakaanza safari
ya kuelekea shuleni hapo kwa ajili ya kuonana na wazazi wa Sadiki ili kujua ni
kitu gani ambacho kilikuwa kikiendelea. Walipofika shuleni hapo, moja kwa moja
wakaanza kupiga hatua mpaka katika ofisi ya mwalimu mkuu. Walipoingia, ukiachana
na mwalimu mkuu, macho yao yakatua kwa ustadhi Hamidu ambaye alikuwa amevalia
kanzu huku akiwa na kofia ya kiislamu pamoja na Tasbih mkononi mwake huku mke
wake, Bi Aisha akiwa amevalia baibui kubwa nyeusi ambayo ilikuwa imemfunika
mpaka miguu yake huku kichwani akiwa amejisitiri na kilemba kilichoonekana
kumpendezesha sana.
“Karibuni” Mwalimu mkuu aliwakaribisha mara baada
ya kuingia ndani ya ofisi ile.
Moja kwa moja wakakaa vitini na kisha
mwalimu mkuu kuanza kutoa utambulisho mahali hapo na kisha kuanza kuelezea kila
kitu ambacho kilikuwa kikiendelea katika maisha ya watoto wao.
Ustadhi
Hamidu na mkewe hawakuonekana kushtuka sana hali ambayo iliwaonyesha kwamba
walikuwa wakifahamu baadhi ya mambo ambayo yalikuwa yakiendelea kwa mtoto wao.
Japokuwa hawakuonyesha mshtuko mkubwa lakini nyuso zao zilionyesha kuumizwa na
kile ambacho kilikuwa kimetokea kwa kijana wao.
“Mtoto wangu alimkataa
Allah! Sina uhakika kama Allah ataendelea kuwa nae” Ustadhi Hamidu alisema huku
akionekana kukata tamaa.
“Usiseme hivyo ustadhi” Mwalimu mkuu
alimwambia ustadhi Hamidu.
“Huo ndio ukweli. Tumeshangaa sana, hatujui
ni mahali gani ambapo Sadiki alikuwa amejikwaa, hatujui kama ni yeye ndiye
chanzo au kuna sehemu sisi kama wazazi tulifanya makosa. Mabadiliko yake
yamekuja kwa haraka sana” Ustadhi Hamidu aliongea huku akionekana kuwa na
maumivu makali moyoni.
“Hiyo ni sawa na Samuel. Yaani tuliona
amebadilika bila kujua ni kitu gani kilikuwa chanzo cha mabadiliko yake”
mchungaji Mpelele aliwaambia.
Kila mmoja akaonekana kukata tamaa na
mtoto wake, hakukuonekana kuwa na dalili za watoto wao kurudi katika maisha kama
ambayo walikuwa wakiishi zamani, maisha ya kumtumikia Mungu. Mara baada ya
maongezi mafupi hapo ndipo mchungaji Mpelele alipowaambia kile ambacho aliambiwa
katika hosteli ya St Peter kwamba vijana wao hawakuwepo katika hosteli ile kwani
walikuwa wamefunkuzwa.
Ustadhi Hamidu pamoja na mkewe, Bi Aisha
wakaonekana kuchanganyikiwa, maneno ambayo aliongea mchungaji Mpelele
yakaonekana kuwachanganya zaidi kwani waliona kwamba mtoto wao, Sadiki alikuwa
ametoweka moja kwa moja na kujiingiza katika maisha ya mitaani. Mioyo yao
ikazidi kuumia zaidi na zaidi, katika kipindi hicho, wazazi wa pande zote mbili
wakaonekana kuumizwa kupita kawaida, tayari waliona kwamba shetani alikuwa
amewazidi nguvu watoto wao na hatimae kujiingiza katika maisha ya anasa moja kwa
moja.
Siku hiyo ikaonekana kuwa mbaya kwa wazazi wa pande zote mbili,
walibaki wakiwa na huzuni sana huku mioyo yao ikizidi kumuomba Mungu awalinde
watoto wao na mwisho wa siku waje kumtumikia Mungu kama ilivyokuwa katika
kipindi cha nyuma.
Walipoondoka mahali hapo, wakajiahidi kuanza
kuwatafuta watoto wao huku wakiwa wamebadilishana namba za simu kwa ajili ya
kufanya mawasiliano pale ambapo wangesikia kitu chochote kile kuhusiana na
watoto wao juu ya mahali walipokuwa katika kipindi hicho.
“Allah!
Naomba uniangalie mtumishi wako. Hili pigo ulilompiga Sadiki ni kubwa sana.
Naomba umsamehe kwa kila kitu na kumrudisha kundini na aendelee kumtangaza Mtume
Mohammad S.A.W” Ustadhi Hamidu alisema huku akiangalia juu, alionekana kukata
tamaa na kuonekana katika hali ambayo alimtegemea Mungu
tu.
Bado biashara ya kuuza madawa ya
kulevya ilikuwa ikiendelea kama kawaida huku Khaled akiendelea kuwatuma katika
nchi mbalimbali barani Afrika hasa katika nchi ambazo zilikuwa katika ukanda wa
Mashariki. Kila siku walikuwa wakiifanya kazi ile ambayo kwao ikaonekana kuwa
nyepesi kabisa.
Madawa ya kulevya yalikuwa yakisafirishwa na kiasi
kikubwa cha fedha kuingizwa katika akaunti ya Khaled ambaye alikuwa akizidi
kutanuka kibiashara zaidi nchini Tanzania. Baadhi ya polisi ambao walikuwa
wanafiki walionekana kuiangusha Serikali, mara kwa mara walikuwa wakipokea
rushwa njiani na kuyaruhusu madawa kupita bila tatizo lolote lile. Kwa sababu
Khaled alikuwa na mnyororo mkubwa wa kufanya biashara zake, alihakikisha kwamba
vijana wake hawapati tatizo lolote lile njiani jambo ambalo lilimfanya kufanya
biashara bila vizingiti vyovyote vile.
Katika kipindi chote ambacho
walikuwa wakiendelea kusafirisha madawa ya kulevya, akili zao zilikuwa
zikifikiria kitu kimoja tu, kumpindua Khaled katika kipindi cha baadae mara
baada ya kuanza safari za Ulaya na kufahamiana na wateja wote ambao walikuwa
wakinunua madawa yale ya kulevya.
Hilo ndilo dhmuni ambalo lilikuwa
mioyoni mwao, unyonyaji ambao alikuwa akiufanya Khaled kwao waliuona kuwa mkubwa
sana kwani walikuwa wakiyahatarisha maisha yao kupita kawaida. Hawakumeza
madawa, usafirishaji wao ulikuwa ni wa kawaida sana hasa katika kipindi hicho
cha zamani, kipindi ambacho madawa wala hayakuwa yakisafirishwa kwa wingi
sana.
Kila siku maongezi yao yalikuwa ni kumzungumzia Khaled, bado
walikuwa na tamaa ya kumiliki biashara nzima ambayo Khlaed alikuwa akiifanya,
kitendo cha kuona fedha nyingi zikiingizwa ndani ya akaunti ya Khaled
zikaonekana kuwatamanisha kupita kawaida.
Bado walikuwa wakiendelea
kufanya kazi kama kawaida lakini akili zao zilikuwa zikifikiria dhuluma tu. Wote
kwa pamoja walikuwa wakihitaji kuwa na fedha nyingi, wawe na utajiri mkubwa
ambao ungewafanya kuwa huru kufanya kila kitu ambacho walitakiwa
kukifanya.
“Lazima tumuue” Sadiki alimwambia Samuel.
“Hilo
lilikwishapita tangu kitambo. Au kama una jingine” Samuel alimwambia
Sadiki.
“Na lazima tuchukue utajiri wake. Yaani fedha zake ziwe zetu.
Au hilo wazo baya?” Sadiki alimuuliza Samuel.CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Wazo zuri sana.
Kitendo cha kumuua tu kinamaanisha kwamba tunataka kila kitu kiwe chini yetu. Ni
lazima tufanye hivyo” Samuel alimwambia Sadiki.
“Tumekwishaanza kujua
michongo yote ya hapa Afrika. Unazikumbuka namba za bwana Khusa yule mzee wa
Afrika Kusini?” Sadiki alimuuliza Samuel.
“Yeah! Nilichukua
mawasiliano yake”
“Na yule mzee Pokwane wa pale
Zimbazwe?”
“Wote nilichukua mawasiliano yao. Yaani kwa kifupi, watu
wote ambao tulifanikiwa kwenda kuwauzia madawa nilichukua mawasiliano yao”
Samuel alimwambia Sadiki.
“Basiiii. Hicho ndicho kilikuwa kitu cha
muhimu sana. Cha msingi kuna safari hizo za Ulaya, Asia na Brazil inabidi
tuzizoee pamoja na kuwafahamu watu kadhaa wanaohusika na madawa hapa nchini”
Sadiki alimwambia Samuel.
Akili zao zilikuwa zimekwishabadilika
kabisa. Walikuwa wakiendelea kufanya biashara ya kuuza madawa si kwamba walikuwa
wakipenda kuifanya kwa sababu ilikuwa ikiwapatia fedha ila katika kipindi hicho
walikuwa wakitaka kufanya kitu kimoja tu, kumdhulumu Khaled madawa yale na kisha
kumuua.
Kwa jinsi tamaa ya fedha ambayo ilikuwa imewaingia mioyoni
mwao wala hakukuwa na woga kabisa wa kumuua mtu yeyote yule, walichokuwa
wakikiangalia kwa wakati huo kilikuwa ni fedha tu. Kila siku walikuwa
wakiongelea fedha, tena hawakuwa wakiongelea kiasi kidogo cha fedha, walikuwa
wakiongelea mamilioni ya fedha.
“Ninawaamini sana” Khaled aliwaambia
mara baada ya kuhitaji kuongea nao.
“Asante bosi kwa kutuamini. Unajua
tumefanya kazi pamoja nawe kwa mwezi wa sita sasa, haujatuangusha, umekuwa
ukitulipa kiasi kizuri cha fedha, hatuna shaka juu ya hilo” Samuel alimwambia
Khaled huku moyo wake ukiwa tofauti na maneno ambayo alikuwa akiyaongea kipindi
hicho.
“Safi sana. Mmekuwa mkijitoa sana kwa ajili yangu. Ni kweli
kwamba katika kipindi cha nyuma nilitamani sana kuwa na wafanyakazi kama ninyi,
kila siku nilikuwa naomba Mungu kuwa na wafanyakazi kama ninyi, mwisho wa siku,
amejibu maombi yangu kwa kuwaleta mahali hapa” Khaled aliwaambia huku akionekana
kuwa na furaha.
Hapo hapo Khaled akasimama na kisha kuelekea kwenye
jokofu na kuchukua pombe kali ya John Walker na kisha kurudi mezani pale,
akachukua glasi ambazo zilikuwa mezani na kisha kuanza kuwamiminia pombe ile.
Katika kipindi chote hicho uso wa Khaled ulikuwa ukionyesha furaha, kwake,
Samuel na Sadiki walionekana kuwa wafanyakazi bora ambao alitakiwa kuwa nao
katika kipindi kirefu sana.
Kwa sababu alikuwa binadamu, hakuweza
kufahamu kile ambacho kilikuwa kikiendelea katika mioyo ya watu hao ambao
alikuwa akiwaamini kupita kawaida. Hakujua kama ndani ya mioyo ya watu hao
walikuwa wakifikiria kumdhulumu mali zake na kisha kumuua na kuiacha biashara ya
madawa ya kulevya mikononi mwao.
“Hiki ndicho kipindi ambacho nilikuwa
nakisubiria kwa hamu sana” Khaled aliwaambia huku akionekana kuwa na
furaha.
“Kipindi gani bosi?” Samuel Alimuuliza.
“Kipindi cha
nyie kwenda barani Ulaya” Khaled aliwaambia.
“Sawa sawa. Na sisi hiki
ndicho kipindi ambacho tulikuwa tukikisubiria kwani tunaamini kama tutafanikiwa
kupeleka mizigo huko, utaingiza kiasi kikubwa na sisi wadogo zako kutuangalia
kwa jicho la tatu” Samuel alimwambia Khaled.
“Sawa sawa. Unalosema ni
kweli kabisa. Ila naomba kabla hamjakwenda huko, kuna mzigo nata mpeleke nchini
Kenya” Khaled aliwaambia.
“Hakuna tatizo. Tutakwenda tu. Unataka
tupeleke lini?” Samuel alimuuliza.
“Kesho kutwa. Cha msingi jiandaeni.
Ni mzigo mkubwa ambao unahitaji uangalizi mkubwa sana” Khaled
aliwaambia.
“Usijali mkuu”
****
Kila siku Edmund
alikuwa akijisikia kuwa wa tofauti moyoni, alikuwa akitamani sana kuongea na
Catherine na hatimae amwambie kile ambacho alikuwa akijisikia moyoni mwake.
Kwake, Catherine alionekana kama malaika aliyekuwa na uzuri wa tofauti, kila
alipokuwa akimuona mapigo yake ya moyo yalikuwa yakidunda kupita
kawaida.
Mara kwa mara alikuwa akipanga kwamba siku hiyo ilikuwa ni
siku ya kumwambia Catherine juu ya alivyokuwa akijisikia lakini kitu cha ajabu,
siku hiyo ilikuwa ikipita bila kutamka neno lolote lile. Katika maisha yake,
hakuzoea kabisa kuongea na msichana yeyote yule, hakuwahi kumtongoza msichana
yeyote, kwa kifupi, Edmund alikuwa bikira wa kiume.
Mapenzi juu ya
Catherine yalikuwa yakimtesa kupita kawaida, katika kipindi hicho ndicho ambacho
alipata kufahamu kwamba mapenzi yalikuwa yakitesa sana moyoni hasa pale ambapo
ulikuwa ukimpenda mtu ambaye wala hakuwa na habari na wewe. Kila siku akawa mtu
wa kuumia tu, Catherine alizidi kuonekana mzuri machoni mwake jambo ambalo
lilikuwa likimvutia zaidi na zaidi.
Wanaume wengi walikuwa wakiendelea
kujitosa kwa msichana huyo lakini hakuonekana kumkubalia mtu yeyote jambo ambalo
lilizidi kumuogopesha Edmund kwa kuona kwamba kulikuwa na uwezekano hata yeye
mwenyewe angeshindwa kumuingiza Catherine katika mikono yake. Watu ambao
walikuwa wakimfuata Catherine walikuwa watu wenye uwezo mkubwa kuongea, walikuwa
watu ambao kila walipokuwa wakisimama na msichana walionekana kuwa na ushawishi
mkubwa, ila hao watu wote kwa Catherine wakaonekana kuwa si kitu jambo ambalo
lilimfanya Edmund kuona kwamba kama angekwenda yeye, pia mambo yangekuwa vile
vile.
“Nitamfuata tu” Hayo yalikuwa maneno ambayo mara kwa mara
yalikuwa yakitoka mdomoni mwa Edmund lakini hakuwa akiyatendea
kazi.
Siku ziliendelea kukatika mpaka zilipofikia siku za mwisho za
kufanya mitihani ya taifa ya kidato cha sita. Kama kuvumilia Edmund alikuwa
amevumilia vya kutosha na katika kipindi hicho aliona bora kulipasua jipu ambalo
kwake lilionekana kuiva. Alichokifanya wiki moja kabla ya kuanza mitihani ni
kuanza kumfuata Catherine ambaye alikuwa amejikalia darasani
akijisomea.
Kadri Edmund alivyokuwa akipiga hatua kumfuata Catherine
na ndivyo ambavyo mapigo yake ya moyo yalivyokuwa yakizidi kumdunda zaidi na
zaidi huku kwa mbali kijasho chembamba kikianza kumtoka. Mpaka anamfikia
Catherine katika sehemu ile amliyokuwa amekaa, alionekana kuhofia kupita
kawaida.
“Mambo!” Edmund alisalimia huku kwa mbali akionekana
kutokujiamini.
“Safi. Karibu” Catherine alimkaribisha Edmund ambaye
akajitahidi kuonyesha tabasamu usoni mwake.
“Asante” Edmund alimwambia
Catherine.
Mpaka kufikia mahali hapo Edmund akaonekana kuishiwa
maneno, akabaki kimya huku akijifikiria ni neno gani ambalo lilitakiwa kufuata
baada ya hapo, hakujua ni maneno gani matamu ambayo yalitakiwa kutoka mdomoni
mwake na kusikika masikioni mwa Catherine. Kichwani alikuwa akiendelea
kujifikiria, kwake tayari ugumu ukaanza kuonekana kwa kuona kwamba kazi ya
kuongea na msichana ilikuwa kubwa sana.
“Nakupenda” Edmund alijikuta
akisema baada ya ukimya wa muda mrefu kidogo.
Catherine akaonekana
kushtuka, kwanza akaacha kazi ya kusoma na kisha kuyapeleka macho yake usoni mwa
Edmund. Catherine alionekana kupigwa na mshangao, neno ambalo lilitoka kinywani
mwa Edmund likaonekana kumshtua kupita kawaida, alichokifanya ni kutoa
tabasamu.
“Umesemaje?” Catherine alimuuliza Edmund huku akionekana
kushtuka.
“Nakupenda” Edmund alijibu.
“Kivipi? Kama rafiki?
Nakupenda pia” Catherine alimwambia Edmund.
“Hapana. Ninakupenda,
ninamaanisha nimeangukia katika mapenzi yako” Edmund alimwambia
Catherine.
“Upo sawa kweli leo Edmund?”
“Nadhani nipo sawa
zaidi ya siku zote”
“Hapana. Haupo sawa”
“Kwa
nini?”
“Kwa hicho ulichoniambia”
“Kwani kigeni masikioni
mwako?”
“Hapana, si kigeni ila kwa mtu kama wewe, ni kigeni kabisa na
sikutarajia kukisikia” Catherine alimwambia Edmund.
Kwanza Edmund
akabaki kimya. Alijua fika kwamba alikuwa ameharibu kwa kumwambia Catherine moja
kwa moja juu ya kile alichokuwa akijisikia moyoni mwake ila kwa wakati mwingine
alijiona kutakiwa kumwambia zaidi Catherine kwa kuamini kwamba angeweza hata
kufanikiwa kumteka msichana huyo ambaye alikuwa akiutesa sana moyo
wake.
“Kuna tatizo mimi kukupenda?” Edmund alimuuliza
Catherine.
“Hakuna tatizo”
“Sasa mbona
umeshtuka?”
“Umekuja moja kwa moja”
“Najua. Huwa
nisingependa niongee maneno mengi sana na kuanza kutoa ahadi nyingi ambazo
ningeshindwa kuzitimiza mara tu ungekubali kuwa pamoja nami. Sitaki uwe pamoja
nami kwa sababu ya maneno yangu na kinafiki yatakayokuonyesha kukujali au
kukuthamini, nisingependa uwe mpenzi wangu kwa sababu nimekuwekea ahadi ambazo
ningeziona kutoweza kuzitimiza maishani mwangu, nimekwambia moja kwa moja,
nisingependa kuongeza neno wala kupunguza neno” Edmund alimwambia
Catherine.
“Mmmh! Sikujua kama upo
hivi”
“Kivipi?”
“Una maneno mengi”
“Hapana.
Ninajaribu kukwambia ukweli tu” Edmund alimwambia Catherine.
Kadri
alivyokuwa akiongea na Catherine na ndivyo ambavyo alikuwa akipata ujasiri zaidi
na zaidi mpaka kufikia kipindi ambacho akajiona kuwa huru kuzungumza neno lolote
kwa msichana huyo mrembo. Edmund hakutaka kutoka nje ya mazungumzo, kila
alichokuwa akikiongea mahali hapo kilikuwa kikihusiana na mapenzi, maneno ambayo
yakaonekana kuwa tofauti masikioni mwa Catherine, hayakuonekana kuwa kama maneno
ya wavulana wengine ambao aliwaona kumfuata kitamaa.
“Naomba
nikufikirie” Catherine alimwambia Edmund mara baada ya kuona kabanwa
kotekote.
“Nahisi haitokuwa rahisi kunifikiria katika kipindi kama
hiki. Tuna mitihani mbele yetu, utaweza kunifikiria na wakati huo huo unatakiwa
kufikiria mitihani?” Edmund alimuuliza Catherine.
“Ni ngumu kupanga
maamuzi ya haraka Edmund”
“Najua. Ila na ni ngumu kuamua kunifikiria
na majibu yako kuwa ya kuniumiza. Naomba uniambie hapa hapa, nataka kufahamu
kama upo tayari kuwa na mimi au la” Edmund alimwambia
Catherine.
“Nitakujibu simuni. Namba yangu si unayo
hapo?”
“Hapana”CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Basi ichukue”
Catherine alimwambia Edmund huku akimgawia simu.
Siku hiyo ndio
ilikuwa siku ya kwanza kwa wawili hao kuongea kuhusiana na mahusiano ya
kimapenzi. Japokuwa Catherine alionekana kuwa mgumu kwa wanaume wengine lakini
kwa Edmund akajihisi kuwa wa tofauti kabisa, akahisi mapenzi yakianza kujitokeza
moyoni mwake. Kwa sababu Edmund alikuwa amekuja moja kwa moja bila kuzungumza
maneno mengi,
Catherine akapata uhakika kwamba mwanaume huyo alikuwa
na mapenzi ya dhati kwake kiasi ambacho akaamua kumkabidhi moyo wake usiku wa
siku hiyo katika kipindi ambacho walikuwa wakiongea simuni. Japokuwa walikuwa
wameahidiana kwamba mapenzi yao yangekuwa siri, wkajikuta wakigundua kwamba
mapenzi yalikuwa ni kikohozi, tena kikohozi kizito kwani ndani ya wiki hiyo
hiyo, wanafunzi wengi wakafahamu kwamba wawili hao walikuwa kwenye mahusiano ya
kimapenzi jambo ambalo liliwashangaz wengi kwani Edmund alionekana kuwa muoga wa
wanawake.
“Naomba unipende katika kipindi chako chote cha maisha yako”
Catherine alimwambia Edmund kwa sauti ya chini katika kipindi ambacho walikuwa
wakijisomea, siku moja kabla ya kuanza mitihani ya Taifa ya kidato cha
sita.
“Usijali. Nitakupenda katika maisha yangu yote, nakuhakikishia
hakuna kitakachotenganisha upendo wangu kwako zaidi ya kifo” Edmund alimwambia
Catherine bila kufahamu ni kitu gani kingetokea katika maisha yao ya mbele,
hakukuwa na mtu aliyejua kama maisha yao ya mbele ya mahusiano yale yangekuwa ni
machozi na maumivu yasiyokwisha mioyoni mwao.
Mapenzi yalikuwa matamu
kama ungempata mtu asiyeweza kukusaliti, ila kwa mahusiano yao, kuna mambo mengi
yangeweza kutokea, mambo ambayo kwao hawakuwa wakiyafahamu kwa sababu tu
yalikuwa mbele ya muda, endapo wangeyafahamu, kusingekuwa na mtu ambaye
angetamani kuwa katika mahusiano ya
kimapenzi.
Kila mmoja alikuwa
akijiandaa na safari ya kuelekea nchini Kenya kama walivyokuwa wameambiwa na
bosi wao, Khaled ambaye alikuwa akiwajali kwa kila kitu. Maandalizi yalikuwa
yakiendelea lakini vichwa vyao kwa wakati huo vilikuwa vikifikiria kitu kingine
kabisa. Bado walikuwa na kiu kubwa ya kumdhulumu Khaleed fedha zote ambazo
alikuwa nazo pamoja na kuichukua biashara ile ya madawa ya kulevya kwani tayari
waliona kwamba ilikuwa moja ya biashara zilizokuwa na fedha nyingi kupita
kawaida.
Baada ya siku mbili, Khaled akawagawia gari jingine na kisha
kuwaletea vibali vyote ambavyo vilikuwa vikihitajika katika safari tayari kwa
kuelekea nchini Kenya kwa kupitia Tanga. Hilo kwao wala halikuwa tatizo kabisa,
mzigo mkubwa wa madawa ya kulevya walihakikisha wangefika nao salama mpaka
katika mikono ya mtu ambaye alikuwa akiyahitaji na hatimae kurudi salama nchini
Tanzania.
Mzigo ulikuwa mkubwa kiasi ambacho wakati mwingine walikuwa
wakifikiri kukimbia nao, wauuze na kisha kuzichukua fedha na kufanyia mambo yao.
Tamaa ndicho kitu ambacho kilikuwa kimewatawala, kitu ambacho walikuwa
wakikifikiria ni fedha tu. Walijua fika kwamba biashara ile ingewaingizia kiasi
kikubwa cha fedha endapo ingekuwa mikononi mwao na si mikononi mwa mtu
mwingine.
Walichokuwa wakikifanya kwa wakati huo ni uvumilivu tu,
hawakutaka kuwa na presha ya kufanya kile ambacho walikuwa wakikusudia kukifanya
kwa haraka sana, walitakiwa kusubiri zaidi na zaidi lakini walijua kwamba ni
lazima kile ambacho walikuwa wamekipanga kufanyika tena kwa ufasaha. Walijua
fika kwamba kwa safari za hapa hapa Afrika wala hazikuwa na fedha nyingi sana
bali kama wangepata nafasi za kusafiri mpaka Ulaya na Amerika ya Kusini ndipo
ambapo wangetengeneza fedha zaidi.
Pamoja na hayo yote, vile vie
walikuwa wakitaka kuzifahamu njia nyingi za kuweza kufanikisha kuipeleka mizigo
hadi Ulaya na Marekani ya Kusini huku pia wakitaka kufahamiana na wanunuzi ambao
walikuwa tayari kununua mzigo wa kiasi chochote kile.
“Naona kama
tunachelewa” Sadiki alimwambia Samuel.
“Hatuchelewi, kinachotakiwa kwa
sasa ni kufahamu njia pamoja na wateja, hilo tu” Samuel alimwambia
Sadiki.
“Kwa hiyo mzigo hasa utakuwa ukitoka wapi?” Sadiki alimuuliza
Samuel.
“Kwa nchi za huko, mara nyingi nilikuwa namsikia bosi akisema
kwamba mzigo alikuwa akiuchukua Pakistan na kisha kuanza kuusambaza” Samuel
alimwambia Sadiki.
“Kwa hiyo Pakistan ndio kitovu cha kila
kitu?”
“Yeah!”
“Basi huko ndipo penyewe. Tufanye juu chini
mpaka tujue jinsi ya kuyapata madawa kutoka katika nchi hiyo” Sadiki alimwambia
Samuel.
Safari yao ilikuwa ikiendelea. Kitu ambacho walikuwa
wakikitaka kwa wakati huo ni kuelekea mpaka Tanga, huko wangeweza kuunganisha
mpaka Mombasa kwa kupitia Manza Bay mpaka kuingia Mombasa kwenyewe. Ndani ya
gari walikuwa wakipiga stori za hapa na pale huku akili zao bado zikiendelea
kufikiria kuhusu dhuluma ambayo walitaka kumfanyia Khaled.
Safari ile
iliendelea zaidi, njiani, kama kawaida yao walikuwa wakitumia fedha kwa kila
polisi wa barabarani ambaye alikuwa akionekana kuwa na mashaka juu yao. Fedha
kwao haikuonekana kuwa tatizo lolote lile, walikuwa wakijiona kushinda kila kitu
katika dunia hii, hata dini zao hawakutaka kuzikumbuka, walionekana kusahau kama
walikuwa wametoka katika familia zilizokuwa zikimuabudu Mungu mchana na
usiku.
Wakaingia Tanga, hawakutaka kuendelea na safari, walichokifanya
ni kutafuta hoteli na kisha kupumzika huku wakitaka siku inayofuatia basi waweze
kuendelea na safari yao mpaka Mombasa. Usiku, muda wote walikuwa katika ukumbi
wa muziki wa Kunani ambapo huko walikuwa wakicheza na wanawake wazuri huku
wakizitumbua fedha vilivyo. Fedha zile zikaonekana kuwavutia wanawake ndani ya
ukumbi ule, wao wakaonekana kuwa mabosi waliotoka jijini Dar es
Salaam.
“Kweli kuwa na fedha raha sana. Yaani mtu unapata
unachokitaka” Sadiki alimwambia Samuel ambaye alikuwa amekumbatia chupa kubwa ya
pombe kali.
“Ndio maana kila siku nasisitiza kwamba huyu mpumbavu
Khaled ni lazima tumchukulie kila kitu kutoka katika mikono yake. Ikiwezekana
tumuue kabisa” Samuel alimwambia Sasiki.
“Ila kuna umuhimu wa kumuua
kweli? Wakati mwingine nafikiria bora tuchukue kila kitu halafu tumuache hai,
nadhani hilo litakuwa pigo kubwa zaidi” Sadiki alimwambia
Samuel.
“Hilo ni kosa. Tena kosa kubwa sana. Huwezi kumuacha hai,
anafahamiana na watu wengi sana, anaweza kuwasiliana nao na kisha kufanya mpango
wa kutuua. Cha msingi tumuue ili kila kitu kiwe poa. Au unaogopa kupata dhambi?”
Samuel alimwambia Sadiki na kisha kuuliza.
“Dhambi! Dhambi ndio nini
sasa? Toka lini mtu akaogopa dhambi na wakati ulimwengu tunaoishi ni ulimwengu
wa maovu. Siogopi dhambi ila nilijaribu tu kukwambia kitu ninachokihisi. Cha
msingi, tufanye kama ulivyosema. Tumuue” Sadiki alimwambia
Samuel.
“Hapo tupo pamoja na tutaendelea kuwa pamoja” Samuel
alimwambia Sadiki.
“Ila bado nina swali. Sijui kwa nini kwenye suala
hili ninakuwa na maswali mengi namna hii” Sadiki alimwambia
Samuel.
“Swali gani tena?”
“Tutamuuaje? Nadhani kwa kifo
chochote kile tutakachotumia kumuua, watu watajua kwamba tupo nyuma ya kila
kitu” Sadiki alimuuliza Samuel.
“Hahah! Hilo mbona jambo dogo sana.
Tutamuua na hakuna mtu atakayejua kwamba kauawa” Samuel alimwambia
Sadiki.
“Ndio nataka kufahamu, kifo cha aina gani?” Sadiki alimwambia
Samuel.
“Ajali. Tutamsababishia ajali. Hilo tu” Samuel alimwambia
Sadiki.
“Kivipi?”
“Kwa sasa kuelezea ni ngumu sana. Ngoja
mishe ikamilike na utajionea. Utafurahia wewe mwenyewe” Samuel alimwambia
Sadiki.
Wote wakaendelea kukubaliana, katika kipindi kirefu walikuwa
wakimzungumzia Khaled tu, unyonyaji ambao alikuwa akiwafanyia ukaonekana
kuwaumiza kupita kawaida hali ambayo iliwafanya kupanga mikakakti ya kumuua,
mikakati ambayo wala hawakutaka mtu yeyote afahamu hilo.
Usiku huo,
bado walikuwa wakiendelea kunywa kama kawaida, wanawake ambao walikuwa nao
katika ukumbi wa starehe wakaachana nao huko na hawakutaka kwenda nao hotelini
kutokana na kuhofia kuonekana kwa mzigo wao wa madawa ya kulevya. Wakabaki
wakinywa pombe usiku wa siku hiyo tena zile pombe kali ambazo ziliwalevya kupita
kawaida na kisha kulala.
Asubuhi, wakaamka na kuanza kujiandaa na
safari ya kuelekea Mombasa ambapo wala hakukuwa mbali sana kutoka Tanga.
Walipomaliza kujiandaa kwa kila kitu, wakalifuata gari lao ambalo walilipaki
katika eneo la hoteli hiyo na kisha kuondoka mahali hapo. Kwa wakati huo, kila
mmoja alijiona kuwa mchangamfu, uchovu wa pombe ambao walikuwa nao katika
kipindi hicho ukaonekana kutoweka miilini mwao.
Safari iliendelea kama
kawaida, kutokana na uzoefu ambao walikuwa nao kuwa mkubwa katika usafirishaji
wa madawa ya kulevya katika nchi za hapa Afrika, wala hawakuweza kupata tatizo
lolote lile hasa kwa polisi ambao kwao walionekana kuwa watu wenye njaa, watu
ambao kama ungewapa kiasi kidogo cha fedha basi wangeweza kukuachia na kuendelea
na safari bila kulikagua gari lako.
Walikuwa wamebakisha kilometa
ishirini kabla ya kuingia Manza bay, sehemu iliyokuwa kaskazini mwa mkoa wa
Tanga, sehemu iliyokuwa na wanawake wengi wazuri. Huku safari ikiendelea zaidi,
mbele yao wakawaona polisi watatu ambao walikuwa na bunduki mikononi mwao.
Wakaonekana kushtuka lakini kutokana na kuujua udhaifu mkubwa wa polisi,
hawakutakiwa kuwa na wasiwasi kabisa.
Gari lilipoanza kukaribia kule
ambapo polisi wale walipokuwa, polisi mmoja akawapungia mkono katika ishara ya
kuwaambia kwamba walitakiwa kusimama. Kila mmoja akaanza kuwa na wasiwasi,
kwanza eneo lile halikuonekana kuwa na kawaida ya kuwepo kwa polisi yeyote yule,
kila walipokuwa wakijaribu kujiuliza juu ya sababu zilizowafanya polisi wale
kuwa mahali pale katika kipindi hicho, walikosa jibu.
“Mnaelekea
wapi?” Lilikuwa swali moja ambalo aliwauliza polisi, usoni hakuonekana kuwa na
mtu mwepesi kushawishika.
“Tunaelekea mpakani. Tunataka kuingia Kenya”
Samuel alisema huku akionekana kutokuwa na wasiwasi kabisa.
“Okey!
Shukeni kutoka garini kwanza” Polisi yule aliwaambia.
“Tushuke kutoka
garini?”
“Ndio”
“Kuna nini tena mkuu?” Sadiki aliingilia kwa
kuuliza swali.
“Tunataka kupekua gari lenu, kila ninavyowaangalia
naona kama mmepakia bangi humu” Polsi yule aliwaambia.
Kila mmoja
akaonekana kushtuka, hawakuamini kama polisi yule angeweza kuwaambia jambo lile.
Tayari waliona kwamba ilikwishakuwa noma mahali pale, kwa haraka sana
alichokifanya Samuel ni kuingiza mkono mfukoni mwake, kama kawaida, akatoa pochi
na kisha kuifungua, akatoa kiasi cha shilingi laki mbili.
“Sihitaji
rushwa. Nimesema shukeni ndani ya gari” Polisi yule aliwaambia huku akionekana
kuanza kukasirika.CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Tunaomba utusaidie
mkuu. Tunaomba utusadie tunawahi kwenye msiba” Samuel alimwambia polisi yule
ambaye hakutaka kuelewa kitu chochote kile.
Polisi aliendelea
kuwaambia kuteremka kutoka garini lakini wao waliendelea kubembeleza zaidi
kwamba walikuwa wakiwahi kwenye msiba uliokuwa umetokea nchini Kenya katika mji
wa Mombasa. Kelele ambazo alikuwa akizipiga polisi yule kwa kuwataka kuteremka
kutoka garini ndizo ambazo zikawafanya polisi wengine watatu ambao nao walikuwa
na bunduki kusogea mahali hapo.
Kitu cha kwanza alichokiwahi polisi
yule ni kuchukua ufunguo wa gari, kwa Samuel na Sadiki tayari mambo yakaonekana
kuwa mabaya kwao. Katika kipindi chote hicho magari mengine yalikuwa
yakiruhusiwa kupita kitu ambacho kikawafanya kugundua kwamba ule ulikuwa mchezo,
kuna mtu alikuwa amewaambia polisi kuhusu wao.
“Teremkeni garini”
Polisi yule aliwaambia huku akiishikilia vizuri bunduki yake.
Katika
kipindi hicho hakukuwa na mtu aliyeonekana kubisha, tayari mambo yakaonekana
kubadilika, kitendo cha polisi yule kukataa kiasi cha shilingi laki mbili
kilionekana kuwasababishia matatizo. Mara walipoteremka, polisi wawili wakaanza
kulipekua gari lao, wala hawakuchukua muda mrefu, wakafanikiwa kuyakuta madawa
ya kulevya yakiwa yamewekwa katika mfuko wa nailoni.
“Nilijua tu”
Polisi yule aliwaambia wenzake.
Tayari wakaonekana kuingia katika
mikono ya sheria, mzigo ambao walikuwa wakiusafirsha kuelekea nchini Kenya ukawa
umekamatwa katika eneo la kilometa ishirini hata kabla hujaingia Manza Bay. Kila
mmoja akabaki kuwa na wasiwasi, tayari hali ikaonekana kubadilika, kila
walipokuwa wakijiuliza ni nani hasa ambaye alikuwa amewaambia polisi kuhusiana
na mzigo ambao walikuwa nao wakakosa jibu.
Wote wakachukuliwa na kisha
kupakizwa ndani ya gari, wakawekwa chini ya ulinzi na kisha safari ya kurudi
Tanga mjini kuanza. Hali haikuonekana kuwa ya kawaida kabisa,, gari ambalo
walikuwa wakilitumia polisi wale lilionekana kuwa tofauti kabisa, halikuwa kama
magari ya polisi wengine, Defender, gari ambayo walikuwa wakiitumia ilikuwa Land
Cruiser.
Tofauti na mawazo yao kwamba wangepelekwa katika kituo cha
polisi, gari lile likafunga breki ndani ya jengo moja kuu kuu na kisha
kuteremshwa. Kwanza hata kabla ya kuingizwa ndani, wakaanza kupigwa, walipigwa
kipigo kikali, kipigo ambacho kiliwaacha hoi mahali pale na kisha kuingizwa
ndani. Kwa kipindi kichache, kila mmoja alikuwa amevimba, damu zilikuwa
zikiwatoka, huku pingu zikiwa mikononi mwao, wakaanza kuingizwa ndani ya jumba
lile kuu kuu.
“Sisi ni watu wa usalama wa taifa, tupo mahali hapa kwa
ajili ya kuweka usalama katika taifa hili. Huwa hatupendi ugomvi na hatupendi
kuongea sana. Tunachokitaka ni kitu kimoja tu, tuambieni huu mzigo ni wa nani”
Polisi mmoja aliwaambia kwa sauti ya chini iliyojaa upole, sauti ambayo
ilisikika kutaka kufahamu ukweli.
Hakukuwa na mtu ambaye alisema
chochote kile, walibaki kimya huku wakiangaliana. Kumtaja bosi wao, Khaled
lilionekana kutokuwa jambo jepesi kufanyika mahali hapo, waliona ni vyema wapate
mateso yoyote yale lakini si kumtaja Khaled kwamba ndiye ambaye alikuwa bosi wao
na ndiye ambaye alikuwa amewatuma madaya yale ya kulevya kuyapeleka nchini
Kenya.
“Ukimya wenu unamaanisha kwamba hautaki amani mahali hapa.
Sawa. Hakuna tatizo” Polisi yule alisema.
Hapo hapo akamuita mwanaume
mmoja ambaye akafika mahali hapo, alipowaangalia nyusoni, kwanza akaanza kucheka
kidharau, akaanza kuvua fulana yake, mwili wake ambao ulikuwa umejazia ukawa
wazi. Misuli ilikuwa imetapakaa mwilini mwake.
“Nafasi ya mwisho.
Hatutokuwa tayari kusikia kitu chochote baadae” Polisi yule aliwaambia lakini
hakukuwa na mtu aliyekuwa tayari kuzungumza kitu chochote kile.
“Kwa
hiyo bado hamtaki amani? Sawa” polisi yule alisema na kisha kusimama
pembeni.
Hapo ndipo mateso yalipoanza rasmi, walipigwa ngumi za kila
aina huku wakiwa wamefungwa kamba katika viti vilivyokuwa katika eneo hilo.
Mwanaume yule alionekana kuwa na ngumi kali na nzito, ni ndani ya dakika
ishirini, kila mmoja alikuwa hoi, kila mmoja alikuwa ameviomba lakini hakukuwa
na mtu ambaye alikuwa radhi kutamka mtu ambaye walikuwa wamewatuma mzigo
ule.
Hiyo haikuonekana kutosha, walichokifanya polisi wale ni kuchukua
spana na kisha kuanza kuzibinya sehemu zao za siri. Wakapatwa na maumivu makali
ambayo hawakuwahi kuyapata kabla. Walibaki wakipiga kelele za maumivu, polisi
wawili ambao walikuwa wakiwabinya korodani zao kwa kutumia spana wakaongeza
zaidi na zaidi kiasi ambacho kila mmoja aliona kwamba zingepasuka lakini bado
Samuel na Sadiki hawakuonekana kuwa tayari kumtaja mtu ambaye alikuwa amewatuma
kuyapeleka madawa ya kulevya nchini Kenya.
Kila mateso ambayo walikuwa
wakipewa mfululizo mahali pale yalionekana kutokutosha kabisa, walipewa mateso
ya kila namna kiasi ambacho hata walipofunguliwa kamba hakukuwa na mtu ambaye
alikuwa na uwezo wa kusimama mahali pale. Mateso hayakuisha, waliendelea
kupatiwa mateso mpaka kufika kipindi ambacho waliihisi miili yao kufa ganzi
lakini bado hawakuwa tayari kuzungumza kitu chochote
kile.
Kilichofanyika mahali hapo ni kuletwa jenereta ambalo
likaonganishwa nyaya fulani nyembamba na kisha jenereta kuwashwa na kuchanwa
kidogo miilini mwao na zile nyaya kupitishwa. Hayo yakawa maumivu mengine ambayo
yalikuwa ni zaidi ya yale ya mara ya kwanza. Miili yao ikaanza kupigwa shoti,
adhabu ile ilichokua zaidi ya dakika thelathini lakini bado hakukuwa na mtu
ambaye alikuwa tayari kumtaja mtu ambaye alikuwa amewatuma madawa yale ya
kulevya.
“Kwa hiyo tufanye nini? Manake vijana wanaonekana kuwa
wabishi” Polisi mmoja alimuuliza mwenzake.
“Mmmh! Sijui tufanye nini.
Kati ya watu wote ambao tumewahi kuwapa adhabu, hawa watu wameonekana kuwa
wavumilivu sana. Yaani wamewashinda hata majambazi sugu” Polisi mmoja
aliwaambia.
“Haina jinsi. Kamuite bosi” Polisi mmoja alisema na kisha
polisi mwingine kuondoka mahali hapo.
Kila kilichokuwa kikizungumzwa
mahali hapo kilikuwa kikisikiwa vizuri masikioni mwa Samuel na Sadiki lakini
hawakuwa na nguvu za kuongea kitu chochote kile wala kusogeza viungo vyao kwani
walikuwa wamepewa adhabu vya kutosha.
Baada ya dakika kadhaa, polisi
yule akarudi mahali pale, huyo mtu ambaye walikuwa wakisema kwamba ni bosi wao
na ndiye aliyekuwa nyuma ya kila kitu walikuwa wakimjua sana kwa kumwangalia,
alikuwa Khaled ambaye akafika mahali hapo huku akiwa ameachia tabasamu pana na
huku akipiga makofi kama ishara ya kuwapongeza.
****
Khaled
alikuwa na lengo la kuwatuma Samuel na Sadiki nje ya bara la Afrika kwa ajili ya
kusafirisha madawa kwa wateja wake ambao alikuwa akiwaamini sana. Ile ilionekana
kuwa kazi kubwa, vijana wengi walikuwa wakihofia sana kusafirisha madawa kwa
sababu ulinzi katika viwanja vya ndege ulikuwa mkubwa kiasi ambacho wengi
walikuwa wakikamatwa na kisha kupewa mateso ambayo yaliwafanya kuwataja watu
ambao walikuwa wamewatuma.
Khaled alijua fika kwamba nae alikuwa
mbioni kuwatuma vijana wake kusafirisha madawa, biashara ambayo walionekana
kujitolea kwa asilimia zote. Khaled hakutaka kukurupuka, kitu ambacho alikuwa
akikitaka mahali hapo ni kuhakikisha kwamba vijana wake wanasafirisha madawa na
hata kama watakamatwa basi wasiweze kumtaja.
Kitu ambacho alikiona
kufaa sana kufanyika mahali hapo kilikuwa ni kuwaandaa watu ambao hao wangefanya
kazi ambayo alikuwa akiitaka. Alitaka Samuel na Sadiki wakamatwe katika kipindi
ambacho watakuwa wakipeleka madawa ya kulevya nchini Kenya na hatimae wapewe
mateso makali, kitu ambacho alikuwa akikitaka ni kuona kama vijana wake
wangeweza kumtaja au wangenyamaza.
Vijana watano wakaandaliwa kwa
ajili ya kufanya kazi ile, akafanya mipango ya kupatikana kwa mavazi ya polisi
na kisha kuwaambia kukaa katika barabara ambayo ilikuwa ikielekea mpakani mwa
Tanzania na Kenya kupitia Manza bay. Vijana wale akawalipa vizuri na akaandaa
sehemu ambayo watu wake walitakiwa kupelekwa na kisha kupewa mateso makali huku
lengo lake likiwa lile lile, kuangalia kama wangeweza kutoa siri
ile.
“Na kama ikitokea wametoa siri?” Kijana mmoja
alimuuliza.
“Haina haja, sitokuwa na kazi nao, waueni” Khaled
aliwaambia.
“Sawa bosi. Hakuna tatizo” Kijana yule alimwambia na kisha
kuondoka mahali hapo.
Kama ilivyokuwa imepangwa na ndivyo ilivyotokea,
Samuel na Sadiki wakakamatwa na kisha kupelekwa katika jumba kuu kuu na kupewa
mateso huko. Mateso yalikuwa makali sana, waliwaandhibu kwa kadri walivyoweza
lakini hakukuwa na mtu ambaye alikuwa tayari kumtaja mtu ambaye alikuwa
amewatuma kuyasafirisha madawa yale kuelekea nchini Kenya. Ndani ya saa moja ya
mateso, wote walikuwa hawako tayari kuzungumza juu ya mtu ambaye alikuwa nyuma
ya biashara ile.
“Hawajanitaja?” Khaled alimuuliza kijana ambaye
alikuwa amekuja kumuita baada ya kila kitu kukamilika.
“Kuhusu vijana.
Pale umewapata aisee. Kwa mateso tuliyowapa, kweli wana moyo. Wapo tayari kufa
lakini si kukutaja” Kijana yule alimwambia Khaled ambaye akatoa tabasamu
pana.
Hapo akaanza kuelekea katika chumba kile cha mateso, alipowaona
vijana wake kwa jinsi walivyokuwa wanaoneka, Khaled akatoa tabasamu pana na
kupiga makofi kwa kuona kweli walikuwa wamepewa mateso makubwa lakini mwisho wa
siku hawakuwa radhi kumtaja. Hapo ndipo Khaled akatoa amri wapewe maji na kisha
kuanza kufutwa damu zilizokuwa zikiwatoka na kuwataka kupelekwa garini na kuanza
kuelekea katika moja ya nyumba yake hapo Tanga.
Ndani ya gari, Khaled
alikuwa akijisifia kwamba alikuwa amepata vijana ambao walikuwa radhi kufanya
nae kazi bila matatizo yoyote yale na si vijana wa wafanyabiashara wengine ambao
kila walipokuwa wakibananishwa kidogo tu, walikuwa wakiweka kila kitu wazi.
Safari yao hiyo ilichukua dakika chache wakawa wamekwishafika katika nyumba hiyo
ambapo wakapelekwa ndani na kisha daktari ambaye alikuwa ameajiriwa kufika na
kuanza kupewa huduma.CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Iliwachukua wiki
nzima na ndipo Samuel na Sadiki wakaweza kupata nafuu na kurudiwa na nguvu zao
kama kawaida. Kila wakati Khaled alikuwa akijisifia kuwa nao, alikuwa
akiwapongeza kwa hatua kubwa ambayo walikuwa wameipiga, hatua ambayo iliwafanya
kupokea mateso makali lakini hawakuwa radhi kumtaja.
“Kila kitu
kilikuwa mpango wangu. Nilitaka mpate mateso ili nione kama mngenitaja” Khaled
aliwaambia huku akiachia tabasamu pana.
“Kwa sababu gani ulifanya
hivi?” Samuel alimuuliza.
“Mnatakiwa kuanza safari za masafa marefu,
huko mnaweza kukutana na vitu vingi, mnaweza kukamatwa pia na kulazimishwa
kunitaja na ndio maana nimeamua kufanya hivi ili nione mngefanyaje” Khaled
aliwaambia.
Kila mmoja akashusha pumzi, ugumu wa kutokumtaja Khaled
ukaonekana kuwasaidia kwa kuamini kwamba endapo wangemtaja basi mtu huyo
angeamua kuwaua. Kazi ya kupeleka madawa katika nchi zilizokuwa nje ya Afrika
wakawa wameipata kwa jasho na damu na kwa upande wao wakaona kwamba kazi ile
ilitakiwa kuwalipa zaidi kutokana na mateso yale ambayo walikuwa
wameyapata.
“Sawa. Tumekuelewa. Kwa hiyo lini tutaanza kazi hiyo?”
Sadiki aliuliza huku akiwa amemkazia macho Khaled.
“Wiki ijayo. Kila
kitu kipo tayari. Safari ya kwanza itakuwa ni kwenda nchini Malaysia, kila kitu
nitawaambia” Khaled aliwaambia.
“Hakuna tatizo. Na vipi kuhusu kuvuka
uwanja wa ndege?”
“Kwa hapa kwetu si tatizo. Mtavuka kwa kupitia
mlango wa V.I.P” Khaled aliwaambia.
Kila kitu ambacho kilikuwa
kimepangwa ndicho ambacho kilitakiwa kufanyika kwa wakati huo. Samuel na Sadiki
wakabaki na maswali mengi vichwani mwao kwamba ni kwa namna gani wangeweza
kutumia mlango maalumu wa V.I.P na wakati wao hawakuwa na cheo chochote kile au
kuwa watu maarufu lakini swali hilo wakaliacha juu ya Khaled ambaye alionekana
kufahamu kila kitu.
Kila mmoja kwa wakati huo alikuwa na hamu ya
kuanza masafa ya mbali kwa ajili ya kupeleka madawa ya kulevya. Vichwani mwao
hawakusahau kwamba katika kila kitu ambacho walikuwa wakikifanya ilikuwa ni
lazima kukamilisha mpango wao wa kumdhulumu Khaled na kisha kumuua ili biashara
yote ya madawa ya kulevya iwe chini yao.
Siku zikaendelea kukatika
mpaka kufikia siku yenyewe, siku ambayo walitakiwa kupanda ndege na hatimae
kuelekea nchini Malaysia kwa ajili ya kuyauza madawa ya kulevya. Kila mmoja
katika kipindi ambacho walikuwa wakielekea uwanja wa ndege alikuwa akitetemeka,
hofu ilikuwa imewajaa mioyoni mwao kwa kuona kwamba wangeweza kukamatwa katika
uwanja wa ndege.
Walipofika uwanja wa ndege, Khaled akawaambia
wamsubirie huku yeye akiteremka na kisha kuelekea katika jengo la uwanja ule.
Khaled alionekana kuwa bize kwa wakati huo huku akitembea kwa haraka haraka kana
kwamba kuna kitu ambacho alikuwa akikitaka kifanyike kwa upesi sana. Samuel na
Sadiki walibaki garini huku mabegi yao yakiwa tayari, kitu walichokuwa
wakikisubiria kilikuwa ni ruhusa tu kutoka kwa bosi wao,
Khaled.
Zilipita dakika arobaini, Khaled alionekana akiwafuata sehemu
ile huku uso wake ukiwa na tabasamu pana, tabasamu ambalo lilionyesha mafanikio
makubwa ya kile kitu ambacho alikuwa amekwenda kukiulizia. Alipolifikia gari
lile, akaufungua mlango na kuingia ndani.
“Kila kitu kipo poa kama
nilivyotaka kiwe. Yaandaeni mabegi yenu” Khaled aliwaambia huku tabasamu
likiendelea kuwepo usoni mwake.
Samuel na Sadiki wakajiandaa tayari
kwa kuanza safari fupi ya kuelekea katika jengo lile. Kila kitu kilipokuwa
tayari, wakatoka na kuelekea ndani ya jengo lile. Walipokuwa wamekaa katika viti
vya wasafiri, Khaled hakuonekana kutulia, bado alikuwa akiangaika huku na kule.
Sadiki na Samuel walionekana kuwa wageni katika kusafirisha madawa kwenda nje ya
Afrika na ndio maana katika kipindi hicho alitakiwa kusimamia katika kila
kitu.
Saa kumi na mbili abiria ambao walikuwa wakitaka kusafiri kwa
kutumia ndege yao wakaambiwa kuelekea katika ndege hiyo. Kwa haraka haraka
Khaled akawapa ishara ya kunyanyuka mahali pale na kuwataka kumfuata. Huko
wakakabidhiwa kwa mwanaume mmoja ambaye alivaa tai, mwanaume ambaye alionekana
kuwa nadhifu na kisha kuanza kuondoka nao na kuwapitisha katika mlango wa
V.I.P.
Kuhusu kuvuka na madawa ya kulevya ambayo yalikuwepo ndani ya
mabegi yao wala haikuwa kazi kubwa sana, walikuwa wamefanikisha kwa kiasi
kikubwa sana. Wakaendelea kupiga hatua mbele zaidi mpaka wakaungana na wasafiri
wengine na kisha kuingia ndani ya ndege ile na safari kuanza huku kila mmoja
akishusha pumzi ndefu.
“Mmmh! Unaweza kujisaidia haja kubwa” Samuel
alimwambia Sadiki huku akishusha pumzi nzito.
“Huo ndio ukweli. Sasa
kule tukifika itakuwaje?” Sadiki aliuliza.
“Bado sijajua. Ila ngoja
tusikilizie na tutafahamu” Samuel alimwambia Sadiki.
“Cha msingi
kumuomba Mungu tu”
“Hilo la maana. Ila hii kazi ni ya hatari sana na
ndio maana nikakwambia ni bora iwe mikononi mwetu kwamba hata kama tukikamatwa
tumekamatwa kwa kupitia biashara yetu” Samuel alimwambia Sadiki.
“Ila
si tulikubaliana tumuue?”
“Ndio. Ni lazima tumuue na kisha kuchukua
biashara hii”
Kwa wakati huo walikuwa wakiongea mambo mengi ambayo
yalikuwa yakitakiwa kufanywa kwa mikono yao wenyewe. Vichwa vyao kwa wakati huo
vilikuwa vikifikiria fedha tu, kiasi cha fedha ambacho alikuwa akiingiza Khaled
kila siku kilionekana kuwachangaya kupita kawaida. Kila mmoja alikuwa akitamani
kuingiza fedha ambazo Khaled alikuwa akiingiza kwa kufanya biashara ile ya
madawa ya kulevya, kwao, kiasi kile kilionekana kuwa kikubwa sana ambacho
kingeweza kuyabadilisha maisha yao moja kwa moja.
CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment