IMEANDIKWA NA : ANDREW CARLOS
*********************************************************************************
Simulizi : Niache Nilie
Sehemu Ya Kwanza (1)
Msimuliaji: Esther
Mpenzi msomaji, kabla sijaanza kusimulia kisa cha kusikitisha kilichotokea katika maisha yangu, napenda kukuambia kwamba dunia ina mambo mengi mabaya na mazuri ambayo nilipokuwa mdogo sikuweza kufikiri kama yapo.
Nasema hivyo kwa sababu nilikuwa nasoma na kusikia habari za watu waliokumbwa na mikasa ya kutisha, lakini sikudhani kama siku moja nami ningepatwa na masaibu hayo.
Kabla sijaanza kusimulia mkasa ulionikuta napenda kukuelezea historia fupi ya maisha yangu kisha uungane nami katika kisa cha kuhuzunisha kilichonikuta.
Kwa jina naitwa Emiliana Ernest. Nilizaliwa mwaka 1990, katika familia yetu, mimi ni mtoto pekee kwa wazazi wangu.
Kwa mujibu wa mama, awali maisha yetu yalikuwa ya amani na upendo kwani baba na mama walikuwa wananipenda na kunilea kwa upendo wa dhati.
Kama inavyofahamika watu hususan wanandoa hawawezi kuishi bila kukutana na vikwazo, mama alisema yeye na baba ambaye sikumfahamu waliingia kwenye mgogoro uliosababisha watengane ambapo kila mmoja alikwenda kuishi kivyake.
Mama yangu aliyekuwa mjasiriamali aliendelea na biashara zake na baba aliyekuwa akifanya kazi ya umakanika aliendelea na kazi yake.
Wakati mama anaendelea na maisha yake, aliolewa na mwanaume mwingine na baba naye alioa. Hivyo kwa upande wa mama nina ndugu wanne.
Kwa baba nina ndugu watatu na mimi ni wanne. Baada ya kutengana kwa wazazi wangu, nilienda kuishi na bibi yangu mzaa mama, Martha Wawaya Chuwa huko Rungwe mkoani Mbeya.
Niliishi na bibi yangu hadi alipoamua kurudi Moshi katika Kijiji cha Uru alikozaliwa, bibi alinipa mapenzi ya hali ya juu.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Waswahili husema ng’ombe wa maskini hazai na akizaa huzaa dume, wakati nikiwa namtegemea bibi kwa kila kitu kwa bahati mbaya bibi aliugua na kufariki dunia.
Kifo cha bibi lilikuwa pigo kubwa sana kwangu kwani alifariki na kuniacha nikiwa binti wa miaka tisa, hakika nilipata pigo ambalo sitalisahau mpaka nitakapoondoka hapa duniani.
Kufuatia kifo cha bibi, sikuwa na jinsi nilikubaliana na hali halisi iliyotokea. Tulimzika bibi yangu. Na tangu hapo maisha yangu yakaanza kuwa magumu. Kwani nilianza kuishi mikononi mwa watu ambao sikuwa nimewazoea.
Baadaye nilienda kuishi kwa babu yangu ambaye ni kaka yake marehemu bibi yangu aliyekuwa akiishi katika Kijiji cha Uru Kitandu. Kutokana kumzoea sana marehemu bibi, ilinichukuwa muda mrefu kuyazoea mazingira mengine.
Hata hivyo, kule nyumbani kwa babu sikupungukiwa kitu chochote, nilikula, kununuliwa nguo na mahitaji mengine na maisha yalikwenda kama kawaida.
Baada ya kukaa kwa babu kwa muda, wazazi wangu walinifuata ambapo tulikaa kikao cha pamoja. Katika kikao hicho babu alikuwa mzungumzaji mkuu.
Nakumbuka babu aliniita na kusema: “Emiliana, hawa ni wazazi wako, huyu ni baba yako na huyu ni mama yako.”
Nilifurahi sana kukutana na wazazi wangu ambao walitengana nikiwa mdogo sana, hata wao walifurahi kuniona.
Babu alipotoa kauli hiyo, aliniambia kwamba kwa kuwa wazazi wangu waliachana nikiwa mdogo sikumfahamu baba yangu ndipo alinitambulisha kwake.
Baada ya kunitambulisha alisema: “Emiliana wazazi wako wamekuja kukuchukua, sasa ni uamuzi wako kuchagua wapi ukaishi, kwa mama au kwa baba yako?”
Kufuatia kauli ya babu, niliduwaa ndipo nilimuuliza babu: “Babu unasema nichague niende nikaishi na mzazi yupi wakati wote ni wazazi wangu?”
Babu alinifahamisha kwamba walikuwa hawaishi pamoja ndiyo maana aliniuliza nichague ningeenda kuishi kwa nani!
Ukweli ni kwamba nilikuwa sijawahi kuishi na mzazi hata mmoja nikiwa nina akili za kikubwa, hivyo sikujua mapenzi ya baba wala ya mama.
Nilimjibu babu kwamba nitaenda, kuishi na baba yangu. Basi babu akampa masharti baba kwamba akitaka kunichukua alete mbuzi mmoja.
Baba alikubali kufanya hivyo, muda wa chakula ulikuwa umefika tukala ndipo baba aliaga kwamba anarudi Arusha alikokuwa akiishi kwa ajili ya kufanya utaratibu wa kurudi tena Moshi akiwa na mbuzi.
Nilimsindikiza baba hadi kituo cha mabasi ambapo tuliagana akaelekea Arusha, kitendo cha kukutana na mzazi wangu huyo ambaye nilikuwa simfahamu kilinipa raha sana!
Baada ya muda si mrefu, baba alikuja kunichukua Moshi ambapo aliongozana na mama mmoja, pia alikuwa na mbuzi aliyeagizwa na babu.
Tulipomaliza kusabahiana, baba alimtambulisha yule mwanamke aliyeongozana naye kwamba ni dada yake aliyeitwa Elizabeth Martini Tairo.
Nilifurahi sana kwani kwa upande wa baba sikumfahamu hata ndugu mmoja, licha ya awali kusalimiana naye, kwa furaha ya kukutana na shangazi yangu nilimsalimia tena.
Baada ya muda baba alimkabidhi babu mbuzi wake ambapo alifurahi sana kisha kwa amani alimruhusu baba kuondoka nami.
Chakula kilipokuwa tayari, tulikula ndipo niliingia chumbani nikafungasha nguo na vitu vingine vilivyonihusu tayari kwa safari ya Arusha.
Muda wa kuondoka ulipowadia, tuliiaga familia ya babu ambapo walitusindikiza hadi kituoni ambapo tulipata usafiri wa kuelekea Moshi mjini, kwa ujumla siku hiyo nilifurahi sana.
Tulipofika Moshi mjini baba aliniita na kuniambia;
“Mwanangu nakupenda sana na si unajua kuwa mimi ni baba yako?” Nikamjibu; “Ndiyo wewe ni baba yangu na pia hata mimi nakupenda sana.”
Akaniambia yeye anakwenda Arusha hivyo nibaki pale Moshi mjini kwa shangazi yangu angekuja kunichukua baada ya siku mbili, sikuwa na kipingamizi nilikubaliana naye.
Licha ya kumjibu hivyo, furaha na amani niliyokuwanayo ilitoweka nikajikuta nabubujikwa machozi.
Baba na shangazi walinisihi ninyamaze lakini niliendelea kulia kisha nilimuuliza baba, mbona wakati ananichukua kwa babu alisema tunakwenda kuishi kwake Arusha iweje aniache Moshi kwa shangazi!
Kufuatia swali langu, hakuwa na jibu zaidi ya kuniambia; “Nenda tu mwanangu kesho kutwa nitakuja kukuchukua.”
Alipotoa kauli hiyo nikanyamaza na kumsindikiza kwenda kupanda basi kisha akaondoka kuelekea Arusha, mimi na shangazi tukarudi nyumbani huku moyoni nikiwa sina raha!
Baada ya kufika nyumbani kwa shangazi aliniambia maneno haya: “Hapa ndiyo umefika, utakaa hapa na kusoma hapa hapa.”
Nilikubali kwani sikuwa na jinsi, hata kama ningekataa ningeenda wapi kwa sababu sikuwa na nauli ya kurudi kijijini kwa babu yangu.
Shangazi alinionyesha chumba ambacho ningekitumia kulala, baada ya kuingia nilianza kulia na kujiuliza kwa nini baba alinidanganya kwamba tunaenda kuishi kwake Arusha kisha kuniacha dada yake.
Ingawa bado nilikuwa mdogo, jambo hilo lilinihuzunisha sana lakini sikuwa na la kufanya zaidi ya kuanza maisha mapya pale kwa shangazi ambaye siku hiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza kumuona.
Shangazi yangu alikuwa ni mwalimu wa shule ya msingi iitwayo Mwereni iliyopo Moshi hivyo alienda kuniandikisha darasa la kwanza. Nilianza masomo rasmi nikiwa na umri wa miaka tisa.
Shauku ya kuwa na baba ilinitoka, sikumuwaza tena badala yake nilimzoea sana shangazi ambaye nilimuona kama mama yangu mzazi.
Awali shangazi alinipenda sana lakini nikiwa darasa la nne upendo ulitoweka akaanza kunifanyia visa ambavyo vilinifanya nimkumbuke baba yangu.
Shangazi aliendelea kunifanyia visa ambavyo nilivivumilia hadi nilipofika darasa la sita ndipo kitovu changu ambacho kilikuwa kikinisumbua tangu utotoni kikaanza kuniuma tena.
Kufuatia tatizo hilo, nilianza kuzimia ovyo hali ambayo ilimpa wakati mgumu shangazi yangu. Alipoona sikuwa na dalili za kupata nafuu aliamua kunipeleka Arusha kwa Mmasai mmoja kwa ajili ya matibabu.
Nilipofikishwa kwa mtaalam huyo wa tiba asili wa mambo yalikuwa hivi;
Masai : Wewe ni mtoto wa ngapi kwenu?
Jibu : Ni mtoto wa kwanza kwa wazazi wangu
Masai: Tatizo ni nini?CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Jibu: Kitovu kinanisumbua sana na pia wakati wa baridi huwa kinavimba chenyewe. Basi alichukua dawa na kunichua na nyingine akanipa kwa ajili ya kunywa nyumbani.
Baada ya kutoka kwa yule Mmasai, shangazi alinipeleka kwa baba ambapo nilimueleza juu ya tatizo la kuumwa kwangu, akanipa pole.
Hata hivyo, nilipotaka kumweleza kuhusu mateso niliyokuwa nayapata kutoka kwa shangazi niliogopa, kulipokucha tulimuaga ambapo aliahidi kuja kunisalimia Moshi.
Nilipofika Moshi niliendelea kutumia dawa huku nikienda shuleni kama kawaida, tulipofunga shule baba alimpigia simu shangazi na kumweleza alihitaji niende nikamsalimie Arusha ningerejea Moshi shule zitakapofunguliwa.
Kitendo cha baba kunihitaji niende Arusha kilinifurahisha sana na nilifurahi zaidi baada ya shangazi kukubaliana naye kwamba niende huko.
Baada ya siku mbili niliondoka Moshi kuelekea Arusha ambapo baba alinipokea vizuri alinitambulisha kwa mkewe na wadogo zangu, licha ya kukaa huko kwa mwezi mmoja sikudiriki kumweleza baba kuhusu mateso niliyokuwa nayapata kwa shangazi.
Jambo la kuhuzunisha ni kwamba, tangu mwaka 1999 nilipoanza kuishi na shangazi sikuwahi kumuona mama yangu tuliyeachana naye Moshi kijijini kwa babu.
Niliendelea kuishi na shangazi yangu na kupata kumonio ya kwanza na kipaimara nikiwa kwake, wakati huo nilikuwa naabudu katika Kanisa Katoliki.
Nikiwa kwa baba yangu, maisha yaliendelea vizuri kwani nilipata mapenzi ya wazazi kwani mama mdogo alinipenda na kunijali kama alivyofanya kwa watoto wake.
Likizo ilipoisha amani ilitoweka ghafla kwani nilijua narudi tena kwa shangazi yangu kuendelea kutuseka, siku hiyo nilipoteza uchangamfu niliokuwanao.
Usiku tulipomaliza kula, tukiwa tumeketi sebuleni baba aliniita na kusema: “Mwanangu hautarudi tena Moshi utabaki na utasoma hapa hapa.
Kauli ya baba ilinifanya niruke kwa furaha kisha nilimshukuru kwa uamuzi huo, ambapo alisema nisijali kwa hilo.
Baada ya kufungua shule na kupita siku kadhaa bila kuniona, shangazi alimpigia simu baba na kuhoji sababu za kutorudi Moshi ambapo mazungumzo baina yao yalikuwa kama ifuatavyo:
Shangazi: Kaka mbona simuoni Emmy na shule zimefunguliwa?
Baba : Mtoto nimemwambia lakini amegoma.
Shangazi: Kwa nini agome tuseme mtoto anakuzidi akili?
Baba: Nimeogopa.
Shangazi: Kwa nini uogope kuna tatizo gani?
Baba: Mwanao ameongea jambo la kutisha.
Shangazi: Jambo gani na linahusu nini?
Baba: Mtoto amesema kuliko arudi kwako ni bora afe.
Shangazi: Kweli Emmy ametamka hivyo?
Baba: Ndiyo.
Shangazi: Haya bwana sina la kusema, akakata simu.
Shangazi yangu aliendelea kuyatafakari maneno yale. Na hivyo ilimlazimu kufunga safari na kunifuata Arusha kwa baba lakini baba na mama waliniambia hata akija mjibu hivyo hivyo.
Waliponiambia hivyo, sikuwajibu chochote na maisha yaliendelea hadi shangazi alipoamua kuja ambapo alinikuta mimi na mama mdogo kwani baba alikuwa kazini.
Akiwa amesimama nje alimuuliza mama mdogo nilikuwa wapi? Wakati huo nilikuwa napika jikoni.
Shangazi : Vipi wifi.
Mama mdogo: Safi wifi, karibu.
Shangazi : Asante lakini siingii ndani.
Mama mdogo: Kwa nini wifi?
Shangazi: Emmy yuko wapi?
Mama mdogo: Yupo.
Walipokuwa wakiendelea kuongea nilitoka jikoni na nilimkuta shangazi kasimama huku mama kasimama mlangoni, kwa kweli kitendo hicho sikukifurahia kwani alipaswa kumpatia kiti.
Shangazi aliponiona alinisalimia kwa kusema: Hujambo mwanangu?
Nilimwambia sijambo kisha nilimwamkia ambapo aliitikia salamu yangu na kuniuliza mbona sijarudi kwake wakati shule zilikuwa zimefunguliwa!
Nilinyamaza kimya, mama mdogo aliwahi kumjibu kwamba mtoto amesema kuliko arudi kwako ni bora afe tumzike hapa. Shangazi akageuka na kuniambia ni kweli Emmy? Nimekufanya nini au nimekukosea nini? Nilizidi kunyamaza bila kujibu lolote lile zaidi nilizidi kuona machozi yakinitoka kwani sikuwahi kuyatamka yale maneno aliyoambiwa.
Nilitamani kumwambia ukweli kuwa yale maneno niliambiwa akija niyatamke lakini sikuweza, nilibaki nimenyamaza tu huku nikiendelea kumwangalia shangazi yangu.
Shangazi alipoondoka, nililia sana ndipo mama mdogo alinifuata na kuniambia kwa nini shangazi yangu aliponiuliza nilikaa kimya?
Akaniambia; “Mjinga wewe, pumbavu kabisa.”
Nilizidi kulia kwa yale maneno waliyomtamkia shangazi yangu. Baba aliporudi salamu aliyopewa na mama mdogo ilikuwa: “Huyu mtoto wako ni mpumbavu na mjinga,” baba akauliza kwani kuna tatizo gani? Mama akamwambia, “dada yako Eliza amekuja hapa na alipofika alimhoji mwanao kuhusu kutorudi Moshi lakini huyu mpuuzi hakujibu kama tulivyomwambia.”
Baba akajibu; “Muache atajua na upumbavu wake.” Nilijua baba atanitetea na kuwa upande wangu lakini haikuwa hivyo. Tangu hapo maisha yalianza kubadilika.
Baba sikumuelewa, nilianza kumuuliza habari za shule lakini aliniambia toa ujinga wako hapa. Muda wa shule ulifika sikwenda. Ndipo nilipoona giza la utata machoni mwangu na katika maisha yangu.
Upendo ulipotea, baba hakunipenda tena nilichukiwa kupita kiasi na hata wale ndugu zangu hawakunipenda tena. Maisha yaliendelea kubadilika na kuwa magumu. Muda wa kwenda shule ulizidi kwenda na mimi bado nikawa nyumbani tu. Baadaye baba alikwenda kunitafutia nafasi katika Shule ya Msingi Ngarenaro. Alipata nafasi na kuniandikisha hapo. Nilianza kwenda shule kwa shida na kwa manyanyaso makali mno. Shule waliyonipeleka walituruhusu kusuka nywele, hivyo na mimi nilianza kusuka na ndugu yangu pia alikuwa akisuka tangu mwanzo, yaani tangu nilipoenda kwa baba nilimkuta akisuka.
Nilienda shule na kusoma bila uhamisho kutoka katika shule niliyotokea. Walimu wakawa wakali ambapo mwalimu mkuu siku moja aliniuliza;
“Mbona unasoma bila uhamisho? Mwambie mzazi wako alete uhamisho kutoka shule uliyotokea.” Nikasema sawa mwalimu nitafanya hivyo. Niliendelea na darasa la sita. Nilipofika nyumbani nilimweleza baba. Baba akaniambia, “toa upuuzi wako hapa pumbavu kabisa toka mbele yangu.”
Nilikosa amani kwani sikusikilizwa tena na wazazi wangu, amani ilizidi kupotea ndani yangu, furaha haikuwepo tena giza la utata lilizidi kuwa kali kwangu. Nilisoma kwa shida bila maelewano kuwa na maelewano na wazazi wangu.
Hata nilipopata matatizo nilisita kuwaeleza kwani nilisha chukiwa pale nyumbani, muda ulizidi kwenda na baada ya mwezi wa saba kupita visa vilianza.
Ilikuwa hivi:-
Baba alianza kuninyima kukaa na watoto wake ambao ni ndugu zangu na kuwaeleza kuwa mimi ni mchawi na uchawi huo nilifundishwa na bibi yangu ambaye ni mama wa mama yangu.
Nilitengwa na kunyimwa kutembea na wadogo zangu kwa madai kwamba ningewaroga. Baada ya muda wakaniambia ninyoe zile nywele nilizokuwa nikisuka na kuambiwa, “kwa nini wewe uje juzi tu nywele zako zikue kuliko za ndugu yako? Nyoa.” Nikaenda kunyoa na nikaambiwa nikishanyoa nilete zile nywele sikujua walipozipeleka, nikaanza kuishi maisha ya shida nilishindwa kuongea yaani nikawa bubu kwa wiki moja. Baadaye nilinyimwa kwenda shule na hata kanisani sikwenda tena nikawa nakaa nyumbani tu. Wakitoka wananifungia, nje hadi watakaporudi. Nilimwambia baba mbona mnanikataza kutoka na nyie na kila mnapoondoka mnanifungia nje ya geti? Baba alinijibu, “tumwachie mchawi nyumba? Na pia hatuwezi kuongozana na mchawi njia moja.” Nilikuwa wakulia kila siku amani, upendo, furaha viliondoka moyoni mwangu. Baada ya wiki moja niliweza kuongea na nikaanza kwenda shuleni hakika maisha yalikuwa magumu sana.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Manyanyaso yaliongezeka
Nilitengewa vyombo vyangu vya chakula, kikombe changu sahani na kijiko. Nilitengwa nisilale na ndugu zangu nililazwa sebuleni peke yangu na kupewa shuka yangu ya pekee. Kila chakula kilipopakuliwa nilipeleka sahani yangu ili niwekewe chakula na hata chai ilipokuwa tayari nilipeleka kikombe pia. Sikuruhusiwa kukaa mezani na wenzangu, nilikaa chini saa ya chakula. Niliendelea kupata usumbufu shuleni lakini sikuweza kumueleza baba yangu kwani nilishamuogopa nilinyamaza tu. Siku moja nikiwa natoka shuleni nilikutana na mama yangu mdogo aitwaye Mary Mwakalinga alinikaribisha nyumbani kwake wakati tunaelekea ndani nilimwambia haya;
Emmy: Mama mdogo acha tu niende nitakuja kukutembelea siku nyingine.
Mary: Hapana twende mara moja.
Emmy: Hapana mama mdogo nitakuja kesho.
Basi niliachana naye nikaelekea nyumbani kwetu kesho yake nilienda shule na nilipotoka nilielekea kwa mama mdogo tena kwani nilimueleza kuwa nitaenda kwake na bahati nzuri nilimkuta.
Emmy: Shikamoo mama mdogo.
Mary: Marahaba, za tangu jana?
Emmy: Nzuri tu.
Mary: Ulikuja lini Arusha?
Emmy: Tangu likizoya mwezi wa sita
Mary: Habari nyingine…
Emmy: Mama mdogo tangu nimekuja kwa baba nimekuwa nikifanyiwa vitendo vya ajabu na vyakikatili sana.
Mary: Vitendo gani tena? Yule si baba yako?
Emmy: Ni kweli, lakini sijui amekuaje na isitoshe nimekuwa nikiota ndoto mbaya na za kutisha.
Mary: Hebu nieleze.
Emmy: Nililala siku moja nikamwota bibi yangu yule ambaye nilikuwa nikiishi naye na niliota akiwa amevaa vazi jekundu kifuani mwake lile vazi limeipigwa liki lakini kwenye hiyo liki kuna mkato yaani liki imekata kosa. Hadi sasa sijaelezwa ile ndoto ilinimaanishia nini. Na siku iliyofuata niliota katika kile chumba nilichokuwa na lala kuna mtu ambaye amekaa chumba kizima yaani mtu anayetisha jitu ambalo halieleweki na halina kichwa. Lakini nilishtuka usingizini, na niliposhtuka nikaamka na kukaa. Nilipokaa na kuwa macho bado nilizidi kuliona lile jitu na nilipopiga kelele sauti haikutoka. Nilikaa na kuanza kulia ingawa sauti haikutoka. Pumzi ilizidi kuwa ngumu kuipata nilizidi kulia bila msaada wowote kupata.
Baada ya hapo nilimaliza maelezo kwa mama yangu mdogo. Mama mdogo akaniambia basi tuombe, tuliomba na kuvunja kila aina ya nguvu za shetani. Na tulipomaliza maombi mama mdogo akanipa zawadi ya kanga peya mbili nikamuuliza ni nani kanipa akaniambia ni mama yako mkubwa yule wa Mbeya ndiye aliyekutumia na alizituma muda mrefu. Namshukuru Mungu kwa kukuona. Nikazipokea kisha niliagana naye na kuondoka uku nikimwambia tutaonana kesho. Nilianza safari kuelekea nyumbani na nilipofika nilimkuta mama mdogo ambaye kwangu ni mama wa kambo akiwa anaendelea na shughuli zake za kushona masweta kisha akaniuliza nimepitia wapi? Nikamwambia hamna mama, akaniambia, “unafikiri nilivyokuuliza mi mjinga?” Nikamwambia sijapitia mahali popote mama, mazungumzo yalizidi kuwa mengi na akiendelea kunibadilikia yaani akiendelea kuwa mkali kwangu nilizidi kukosa raha na amani ndani yangu.
Mama: Nakuuliza kwa mara ya mwisho, ulienda wapi?
Emmy: Kimya
Mama: Sema ukweli, nikusamehe. Nilizidi kuwa kimya sikumjibu lolote lile. Aliamka pale alipokuwa ameketi na kusimama na alinipokonya mfuko niliokuwa nimeubeba ambao ulikuwa ni zile kanga nilizopewa na mama yangu mdogo ambaye ni mdogo wa mama yangu mzazi. Alipochukua ule mfuko akaangalia ndani na kuziona zile kanga, kisha akaniangalia usoni, akaniambia, “nilikuuliza umepitia wapi ukawa kimya na je hizi kanga umezitoa wapi?” Nikamwambia, “nilipotoka shule nilikutana na mama yangu mdogo na ndiye aliyenipa hizi kanga alipokuwa ananipa sikuingia hata ndani alinipa na mimi nikaondoka.” Akasema, “unanifanya mimi mjinga?” Nikamwambia hapana mama, basi akaniambia ngoja baba yako arudi ndiyo utaweza kujieleza kwa sasa naona huwezi kujieleza.
Niliingia ndani na kuvua nguo za shule, na nilipotoka, nje nilienda kuchukua vyombo vya kuosha na wakati, nachukua vyombo akanikataza nisivichukue. Nilipata uchungu na kuanza kulia huku nikiendelea kumkumbuka marehemu bibi yangu. Bado maisha kwangu yalizidi kuwa magumu na ya utata zaidi.
Nilitamani sana kwenda kwa mama yangu mzazi lakini sikupafahamu kabisa. Ingawa kwa mama mdogo ambaye ni mdogo wa mama yangu nilishamfahamu lakini ilikuwa bado ni ngumu kwangu kwani wazazi niliokuwa naishi nao walishaanza kunifuatilia kila kona. Basi baba alirudi kutoka kazini na kitendo cha kumuona tu moyo uliuma gafla. Nilimpokea na kumsalimia, aliingia ndani nami niliendelea na kazi zangu. Majira ya usiku tulipata chakula cha na baada ya kumaliza kula mama akamuelezea baba kuhusu ile safari niliyopita kwa mama mdogo na kumwambia kuhusu zile kanga nilizopewa. Baba akaniuliza, “hizo kanga za kichawi ulizozileta ndani kwangu ziko wapi wewe shetani?” Nikamwambia baba si za kichawi, kama unavyosema akaniambia, “wakati naongea usiwe unanijibu hata siku moja, shetani mkubwa wewe.” Nilizidi, kuumia zaidi kwani yule ni baba yangu mzazi ambaye angetakiwa awe mtetezi wangu wa karibu sana kwangu lakini alizidi kuwa adui kwangu. Niliingia chumbani na kwenda kuzileta kanga hizo na baada ya kuzileta alimkabidhi mama naye akaelekea kwenye mti wa mparachichi uliokuwa karibu sana na mlangoni na kuziweka juu. Baba akaniuliza, “nani alikupa ruhusa ya kwenda kwa mama yako mdogo?” Nikamjibu hakuna aliyeniambia. Akaendelea kusema, “kama hamna nini kilikupeleka huko?” Nilipoona maswali yamekuwa mengi niliomba msamaha na kukiri kuwa nimekosea na kumwahidi sintarudia tena. Baba hakuweza kunisikiliza hata kidogo na sapoti nyingi za hasira ziliindelea kutolewa na mkewe. Baba alianza kunishambulia bila huruma alinipiga sana huku nikimuomba msamaha lakini hakunisikiliza hata kidogo kwa sababu sikuwa na wakunitetea. Nilitamani kukimbia lakini sikuweza huku mama akisema hawezi kumtetea mchawi. Nilizidi kuumia kwa lile neno. Baba hakuweza kunihurumia mwanaye alizidi kunipiga ingawa nilitia sana lakini bado kilio changu hakusikia hata kidogo. Alinipiga sana lakini cha ajabu sikuyasikia maumivu hata kidogo alipokuwa akinipa kipigo japo nilikuwa nalia. Naweza kusema hamu yake yakuendelea kunipiga ilimwisha, basi akaniacha na kuniambia, “rudia tena uwone nitakacho kufanya ewee mchawi, umenielewa?” Nilikubaliana naye lakini moyo uliniuma sana.
****
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/“Ni bora nisingekuwa na mzazi kuliko haya yanayonipata” nilikuwa nawaza moyoni huku nikuvuta sura au taswira ya marehemu bibi yangu ambaye niliishi naye kwa upendo wa hali ya juu. Mawazo ya kujiua yalinijia moyoni mwangu nikaanza kutafuta sumu ili ninywe nitoweke juu ya huu ulimwengu. Nilifikia uamuzi huo baada ya kukosa furaha ya maisha ya kuishi na wazazi wangu na ghafla nilianza kumchukia baba yangu ikawa kila nilipomuona moyo wangu ulizidi kukosa amani zaidi. Wadogo zangu nao walianza kunibeza huku wakinicheka na kuniambia, “dada gani wewe baba alikupiga jana hatukuiti dada tena, baba amesema atakukomesha, kwanza mama yetu ametuambia kuwa wewe ni mchawi, usitembee na sisi wala usile na sisi tena usilale na sisi, kumbe wewe mchawi aaa.” Niliumia sana na nilizidi kulia huku nikijuta kuzaliwa, nilizidi kukosa amani ndani ya moyo wangu, nilikonda kadiri siku zilivyozidi kwenda. Mbali na kutaka kujinyonga pia nilitamani heri ningekuwa yatima huenda watu wema wangejitolea kunilea kupewa mapenzi ya dhati.
Kulipokucha ndipo nilipoanza kusikia maumivu ya kipigo cha usiku nilichopigwa na baba yangu. Cha ajabu wakati ananipiga hadi anamaliza kunipiga sikusikia chochote ila asubuhi ilifika wakati nikashindwa kukaa pia mwili ulikuwa umevimba na majeraha yalionekana zaidi mwilini mwangu. Hakuna aliyeongea na mimi wala kunipa pole zaidi ya kunicheza na kuendelea kunibeza hali iliyosababisha nianze kulia kwa uchungu huku nikimuwaza mama yangu mzazi ingawa sikufahamu alipokuwa anaishi. Siku zilizidi kwenda hamu ya kuishi ikiendelea kutoweka ndani yangu, mawazo mabaya yakizidi kukimbilia kwenye ufahamu wangu, akili, ikizidi kuchoka. Siku msahau muumba wangu nilizidi, kumwomba Mungu anisaidie na kuniepusha na ugumu wa maisha niliokuwa nikipitia. Nilihisi giza la utata katika maisha yangu kwani tangu marehemu bibi yangu kufariki sikupata kuishi maisha ya furaha tena na wala amani sikuipata. Maisha yaliendelea kuwa magumu kwangu nakupelekea niwe binti wakulia tu kila kukicha. Niliichukia familia ya baba yangu yote sikutamani hata kuwaona. Sikuwa na lakufanya kwani bado nilikuwa nikiishi nao. Kweli ni bora kukosa kila kitu katika ulimwengu huu kuliko kukosa amani na furaha na upendo katika maisha. Nilihisi nitaishi maisha ya amani na ningepata furaha kwa wazazi wangu na pale nilitarajia ningeonyeshwa upendo wa dhati lakini hali ilikuwa tofauti kama nilivyokuwa nikiwaza katika ufahamu wangu na kujikuta kila kitu kwangu nikikiona kibaya hata kile kizuri sikukithamini hata kidogo. Ndipo niligundua kuwa hakuna anayejua thamani ya maisha yangu kwa hapa duniani zaidi yake Mungu aliyeniumba. Kutokana na mateso makali niliyokuwa nayapata kutoka kwa baba kilipelekea niwe na hali ya kuwachukia wanaume wote kwani nilijua wanatabia kama ya mzazi wangu na kufikiri hata nikitoka kwa baba na kwenda mahali pengine mambo yataendelea kuwa yaleyale. Nilikatazwa kwendwa kanisani kwa madai kuwa mimi mchawi na kupewa kazi ya kuwa mlinzi wa nyumbani. Kilikuwa ni kipindi kigumu sana kwangu kwani hatima ya maisha yangu sikujua itaishia wapi. Siku moja nilimuomba baba niende kanisani lakini alikataa katu katu lakini mama mdogo aliahidi kunipeleka. Kweli baada ya muda mama alianza kunipeleka kanisani na kuanza kufanyiwa maombi. Nilisali katika kanisa moja lililopo Ngulelo mkoani Arusha. Nilihudhuria kanisani kwa muda mrefu huku nikiendelea kufanyiwa maombi kanisani hapo.
Siku moja niliitwa na mchungaji wa kanisa hilo kwa ajili ya mazungumzo zaidi na yalikuwa marefu lakini yaliniumiza kwa upande mwingine.
Mchungaji: Emmy hujambo?
Emmy: Sijambo mchungaji Bwana Yesu asifiwe.
Mchungaji: Ameni.
Mchungaji: Nimekuita kuna mazungumzo kati yangi mimi na wewe.
Nilinyamaza na kujiandaa kuyasikiliza mazungumzo aliyoniitia.
Moyo ulianza kukosa amani hata kabla ya mazungumzo yenyewe, moyo ulianza kuzungukwa na machozi ya uchungu.
Ilikuwa hivi:
Mchungaji: Emmy tumechoka kukuombea wewe na ujue tumefika mwisho hakuna mtu ambaye atapiga magoti tena na kusema anakuombea wewe. Kwani wewe hausikii na ukitaka kuendelea kuishi hapa na kusali katika kanisa langu naomba ukafanye haya nitakayo kwambia. Nikamwambia sawa mchungaji.
Aliniambia kuwa;
“Kuna kitu umechimbia pale mlangoni kwa baba yako sasa nahitaji uende ukakifukue hapo, sawa?” Nilimwambia mchungaji sijafanya kitu kama hicho lakini yeye aliendelea kusisitiza kuwa yeye ni mtumishi wa Mungu anajua anachofanya na Mungu anamuonyesha mengi. Nikamwambia tena mchungaji sijachimbia chochote na maneno hayo ni mageni kwangu. Lakini yeye aliendelea kusisitiza kuwa anachokisema ni kweli na kama sitaki niseme. Nilinyamaza kimya sikuwa na lakuongea, nilisikia uchungu na moyo ulizidi kuniuma kwa yale mazungumzo. Akaniambia; “nakupa siku tatu tu uwe umeshachimbua hivyo vitu sawa?” Nilinyamaza. Akanimbia nisipochimba atawatuma watumishi wake waje wachimbe hapo nyumbani. Nilinyamaza kimya huku machozi yakinitoka na nilipata uchungu sana moyoni. Baaya kukataa akaniambia niondoke nami nilisimama na kuondoka nikiwa nimeongozana na mama mdogo. Tuliondoka na kuelekea nyumbani, wakati tunaelekea nyumbani mama mdogo aliniambia; “kumbe umechimbia uchawi wako nyumbani kwangu ndiyo maana nashindwa kuishi kwa amani na familia yangu.” Katika mazungumzo yangu na mchungaji nilimwambia kuwa wakati baba ananunua kiwanja sikuwepo na kipindi anajenga nilikuwa sijafika na wakati wanahamia mimi sikuwepo. Lakini mchungaji hakuniambia chochote kile kuhusu jambo hilo zaidi yakuniambia nienda kuchimba hicho alichoniambia nimekichimbia nyumbani kwetu. Tulipofika nyumbani mama mdogo alinigeuzia kibao kisha akawa mkali na kunitaka nikachimbue uchawi wangu niliouchimbia nyumbani kwake. Nilimwambia hakuna nilichochimbia na mchunguaji sijui maneno hayo ameyatoa wapi mpaka wanilazimishe kuchimbua vitu ambavyo sijaviweka na wala sivijui. Mama mdogo alisema mtumishi wa Mungu si mwongo hata kidogo hivyo ninachotakiwa nienda kuchimba huo ushetani wangu. Mchungaji alisema kitu hicho nilikichimbia mlangoni upande wa kusohoto pembeni ya korido kidogo. Basi mama mdogo aliingia jikoni na alipotoka alitoka na panga, akanikabidhi na kuniambia nichimbe vitu hivyo nami nilijikuta naliaa kwa uchungu kwani alinilazimisha nifanye hivyo haraka kabla watumishi wa Mungu hawajafika maana nitapata shida sana. Aliendelea, kunilazimisha nichimbe ile sehemu niliyoambiwa. Baada ya kuona kipigo kimeanza nilianza kuchimba ile sehemu niliyoambiwa na mama mdogo. Nilianza kuchimba mpaka nilipofika kwenye msingi wa ile nyumba na kukutana na kimfuko cheusi kilichofungwa vifundo vitatu na kilikuwa ni kirefu.
****
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment