Search This Blog

Sunday, July 10, 2022

NISAMEHE MAMA - 2

 







    Simulizi : Nisamehe Mama

    Sehemu Ya Pili (2)



    "Unadhani wote wanaoingia madarakani wanania ya kuwatumikia wanahohehae kama unavyodhani wewe?" Aliniuliza mwenyekiti wa kijiji. Sikuwa na neno kwani ningeweza hata kumtusi tusi ambalo lingesababisha nitozwe faini au nipelekwe gerezani kwa miezi sita kwa mujibu wa sheria ya matusi. Alipoona ukimya wangu akazidi kubwabwaja;

    "Nyie vinyambevinyambe ndiyo maana huwa mnauliwa. Badala uangalie maisha yako pamoja na hicho kicherema chako mgongoni unaanza kuwa mwingi wa udadisi wa yasiyokuhusu.

    Kawataarifu na wenzako ya kuwa mkitaka kuchagua kiongozi wa umma muangalieni kwanza kipato chake kama kinatosheleza. Siyo mnamchagua mtu kama mimi sina moja ukategemea nitahitaji kubaki hapo kwenye sifuri. Nitahitaji kupata kumi na nd'o utakuwa unakwisha muda wangu wa kukaa madarakani." Alimaliza kuongea mwenyekiti maneno ambayo yaliuchoma vilivyo moyo wangu. Lakini aliweza kunipa mwanga wa roho za viongozi.

    “Wakanifukuza kama mbwa na mimi sikutaka kufuatilia suala hilo tena,lakini baadaye nilipata taarifa kuwa kituo kile kilisambaratika na baadhi ya watoto waliingia mtaani na kuwa machokoraa.

    Wale wadogo walichukuliwa na wale waliowapeleka pale kama ilivyokuwa kwangu kukuchukua wewe..

    Kituo kilisambaratika kwa sababu fedha zilizokuwa zimetumwa ziendeshe kituo,ziliingia mifukoni mwa wachache”.Yule mama aliendelea kumsimulia mwanaye mkasa uliokuwa umemsibu katika maisha yake.

    “Nikarudi kwenye chumba nilichokuwa nimekipangisha kwani tayari ilishafika majira ya jioni. Nikakuacha ndani ukiwa umelala na mimi nikaelekea dukani kununua unga kwa ajili ya chakula cha usiku.

    Huko ndiko kulinifanya nikuonyeshe goti langu. Ndiyo siku ambayo niliteguka goti langu. Lakini mbali na kuteguka walifanikisha azma yao." Machozi yaliombatana na kamasi pamoja na kwikwi yakatawala ndani ya nyumba ile. Steven alilia kwasababu alijua kilichomkuta mama yake japo hakuwekwa wazi.

    Wote walilia sawa. Hapakuwepo na wa kumbembeleza mwenzake.

    "Mwanangu usiku ni mkubwa na kesho unatakiwa ukafanye mtihani." Aliongea mama yake huku akinyanyuka na kuelekea chumbani kwake huku akimuacha Steven ambaye alikuwa akilala sebuleni.

    Steven akatandika kigodoro chake kilichochoka na kulala juu yake lakini katu usingizi haukumchukua mapema. Mawazo yalikuwa mengi haswaa.

    Ilikuaje hadi leo hii tunaishi kwa amani na mimi naenda shule? Hili eneo alilipata wapi kama anasema alikuwa amepanga? Kama alinunua ni wapi alipata fedha?

    Ni maswali yaliyokuwa yakizunguka kichwani mwa Steven hadi akapitiwa na usingizi. Kesho yake aliwahi kudamka kabla ya mama yake. Akajiandaa na kumuaga mama yake ndipo akaelekea shuleni.

    ***

    Kama kawaida yake alitakiwa kuelekea shambani kwa ulikuwa ni msimu wa kilimo cha mahindi. Akiwa anaeleke shambani asubuhi ile akakutana na mama Sung'wa ambaye alikuwa akitabasamu.

    "Mwenzangu bado unahangaika tena na kulima wakati pesa imeiva?"

    "Imeivaje sasa?"

    "Leo nd'o tunatakiwa kujaza fomu juu ya ule mpango niliokwambia. Yaani baada ya kujaza fomu kwa mwenyekiti zikapelekwa hakuna utata tena. Ni kufaidi maisha." Alisisitiza mama Sung'wa.

    "Kuhusu hayo mafomu atayajaza Steven na siyo mimi."

    "Basi jitahidi akitoka shule mripoti kwa mwenyekiti wetu ili mjaze hizo fomu za kukubali."

    Mjadala wao ukakomea hapo. Lakini mama yake na Steve hakurudi nyumbani. Akaelekea shambani kwake.

    Shuleni Steven aliifanya mitihani ile kwa umakini kama ilivyokuwa ile ya awali. Waliporuhusiwa Steven hakutaka hata kuagana na marafiki zake kama alivyokuwa akifanya mara zote.

    Shauku ilikuwa kubwa moyoni mwake ya kutaka kufahamu ilikuwaje hadi wakawa pale. Historia aliyokuwa akisimuliwa na mama yake, ilikuwa inamvutia na kumfanya amuone mama yake ni mwanamke shujaa,tena anayestahili kushukuriwa kila muda. Hata mama yake pia alishangaa kuona mwanaye kawahi sana.

    "Steve mwanangu mbona leo umewahi mno? Au kuna tatizo?"

    "Hakuna tatizo mama na vilevile baraka zako zinaniifanya akili yangu kuona maswali ya mitihani ni mepesi sana. Ila kikubwa ni furaha ya yale aliyoyasema mama Sung'wa." Alidanganya Steve huku akiweka vifaa vyake alivyotoka navyo shule kwenye moja ya kona pale sebuleni.

    "Vizuri mwanangu. Tena umenikumbusha maana mama Sung'wa nilipokutana naye asubuhi, aliniambia natakiwa kujaza mafomu kwa mwenyekiti wetu. Lakini nikamwambia wewe ndiye utakayeifanya hiyo kazi. Ndipo akaniambia ukitoka shule tusisite kuripoti kwa mwenyekiti."

    "Yaani mama'angu kama hilo litafanikishwa, naamini tabu hizi za mvua ikinyesha usiku hakuna kulala zitakuwa zimekoma." Aliongea Steven kwa furaha lakini ikageuka machozi kwa mama yake.

    "Mwanangu Steve una miaka mingapi sahivi?" Aliuliza huku akilia.

    "Kumi na saba mama."

    "Mwanangu Steve jifunze kukabiliana na huzuni endapo huna uwezo wa kuigeuza ikawa furaha."

    "Unamaanisha nini mama unaposema hivyo?"

    "Ashindwaye kesho ni yule ambaye hakuweka mipango yakinifu leo. Itizame leo kwa jicho la ziada. Usiifikirie kesho ambayo hujui itaanza vipi na itaisha vipi. Najua nakuweka kwenye mafumbo lakini kula kwanza chakula halafu tuelekee kwa mwenyekiti. Tukirejea nitakufumbua niliyokufumba."

    Steven hakuona sababu ya kuendeleza maswali ilihali alishaambiwa atafumbuliwa kile alichofumbwa. Alichokifanya ni kuelekea bafuni. Akaoga ndipo akachukua chakula jikoni na kutuliza njaa yake.

    "Mama yangu wewe! Nikipata fedha nitafungua hoteli kubwa yenye hadhi ya kimataifa halafu niandike maandishi makubwa. NATENZA MAGIC HOTEL.

    Hii ni kwasababu ukipika natamani nisishibe ili niendelee tu kusikilizia ladha ya ukipikacho." Alimtania mama yake ambaye aliishia kucheka.

    Alipomaliza kula hata hakupumzika kama wanavyoshauri wataalamu wa masuala ya afya. Miguu na njia wakaelekea kwa mwenyekiti. Steven akajaza mafomu kama ilivyokuwa ikielekezwa kupitia maandishi,ambapo walitakiwa kuhama eneo lile na kujengewa nyumba nyingine mahali popote ambako wangehitaji.

    Vilevile watoto wa familia husika kusomeshwa japo Steven alikuwa mwenyewe. Akatamani angekuwa na wadogo zake au wakubwa zake.

    Baada ya kujaza akamkabidhi mwenyekiti ambaye aliahidi kuwapatia taarifa ya kitakachoendelea. Wakaagana na kurudi nyumbani,wakati huo ilishatimu majira ya saa kumi na mbili jua likianza kuchwea.

    Mama akachukua jukumu la kupika wakati huo Steven akichukua madaftari yake ya Biology pamoja na History kwani nd'o masomo ambayo alitakiwa kuyafanyia mitihani kesho yake.

    Masaa mawili pekee nd'o aliyatumia kupitia masomo yale.

    Hadi anamaliza kupitia masomo yale, chakula kilikuwa tayari. Wakaanza kupata mlo huo na baada ya kumaliza mama yake Steven akaendelea na simulizi yake kwa mwanaye.

    "Kamwe mwanangu usikubali kufanya kosa la kufikiria kile ambacho huna uhakika nacho. Kumbatia kile kilichokuwa tayari. Kile usichokuwa na uhakika nacho kifikirie kama si chako.

    Mwanangu leo hii unasema mpango wa kujengewa nyumba ukikamilia tutakuwa tumeepuka tabu ya mvua pindi inyeshapo. Lakini kumbuka huu ni mwaka wa kumi na mbili tunaishi hapa. Hii ni nyumba iliyotusitiri kwa miaka hiyo yote. Kama ningeiona haifai nadhani leo hii tungekuwa tunaitwa hayati.

    Nakwambia hayo mwanangu si kwamba umenikasirisha kwa kauli yako. Hapana! Ila tu lengo langu kuu ni wewe kuwa mwingi wa fikra za kile kilichoiva na si kile ambacho hata huna mategemeo ya kukipika." Akanyamaza ghafla kisha akarudia kuita.

    "Steven mwanangu."

    "Naam, mama."

    "Mwaka mmoja tangu nikabidhiwe nyumba hii, nakumbuka ilikuwa ni siku ya Jumatatu. Siku hiyo sitaisahau kamwe mwanangu.

    Ila nastahili kusema MUNGU ni mwingi wa mitihani kwa waja wake. Mitihani ambayo inahitaji uvumilivu wa hali ya juu kuishinda. Ila katika hilo lililotokea nilitamani nikuue kisha nijiue na mimi ili kuepukana na tabu hiyo.

    Mchana wa siku hiyo hali ya hewa ilikuwa nzuri sana. Jua liliwaka kama kawaida lakini ilipotimu majira ya saa moja, mawingu yalitanda na kuifunika nuru iliyokuwa imeanza kuimulika ardhi.

    Mawingu yale yakasababisha kiza kinene kana kwamba ulikuwa usiku wa manane. Mbwa wakaanza kubweka kwa nguvu na kuifanya mioyo yetu kuingiwa na taharuki. Muda mfupi baadaye upepo mkali ukaanza kuvuma huku anga likianza kuachia radi pamoja na miungurumo.

    Kabla hilo halijapita, matone ya mvua yakaanza kudondoka na baadaye mvua iliyoambatana na mawe.

    Kama hiyo haitoshi, paa la hii nyumba yetu likang'olewa na ule upepo uliokuwa ukiendelea kuvuma pasipo huruma.

    Mwanangu Steven kumbuka kuwaheshimu wanawake wote wanaojitolea maisha yao kubeba mimba na hatimaye kujifungua.

    Baada ya paa kuezuliwa, mvua ikaanza kufanya makao ndani. Wakati huo ulikuwa na umri wa miaka minne. Ukaanza kulia kilio cha juu mpaka nikahisi una tatizo limekupata. Hapakustahili tena kutusitiri. Nikakufunika kwa blangeti ukiwa kifuani mwangu. Mimi nikawa kinga yako ili yale mawe yaliyoambatana na mvua yasikuumize ila mimi nikaumizwa.

    Nikajongea kwa mwenyekiti wetu kipindi hicho alikuwa na miezi mitatu tu tangu apatiwe madaraka. Nikagonga hodi ili aweze kutupatia msaada.

    Mwanangu dunia hii tunaishi wengi, na matatizo ni moja ya upande wa maisha lakini kuna wakati inafika unaona kama umeumbwa mwenyewe.

    Kijiji kina wakazi wengi lakini niliona kama naishi mwenyewe ndani ya kijiji kizima”.

    “Umeambiwa hapa ni kutuo cha watoa misaada kwa masikini?” Ni swali aliloniuliza mwenyekiti pindi alipofungua mlango na mimi kumueleza shida yangu.

    “Nilishindwa kumjibu na nikabaki nikimtizama tu. Alipoona nimenyamaza akataka kufunga mlango wake. Nikauzuia na kumuomba akuhifadhi wewe peke yako halafu mimi aniache nife kwasababu sina thamani tena.

    Hakujibu zaidi ya kuusukuma kwa nguvu na kusababisha nianguke na kuteguka mkono wangu. Nikainuka huku wewe ukizidi kulia. Mvua nayo haikuwa imekoma. Tena nd'o ilikuwa ikizidi kunyesha kwa nguvu.

    Nikaona isiwe tabu. Kama amenigomea kuingia ndani kwake, basi ngoja nijibanze barazani. Hazikupita dakika mbili, mbwa wake akabweka kwa nguvu na kumfanya atoke”.

    “Unahitaji kuniletea mikosi ndani ya familia yangu?” Akaniuliza huku akiwa amenimulika na kurunzi yake yenye mwanga mkali.

    “Unadhani ningemjibu nini?

    Nikamuomba akuonee huruma wewe. Bado hakunielewa.

    Akanifukuza kana kwamba hakuwa akinifahamu.

    Hata angekuwa hanifahamu lakini hana moyo wa ubinadamu? Au roho yake imeumbwa kwa chuma? Jibu ni hapana. Ila ni ubinafsi tu.

    Nikaona njia sahihi ni kwenda kujihifadhi shuleni. Taratibu nikaanza kutembea na muda huo mwili wangu ukaanza kutetemeka kutokana na hali ile isiyovumilika labda katika kipindi kama nilichokuwamo mimi. Kipindi cha mateso na wingi wa mitihani.

    Mita chache kabla sijafika, kundi kubwa la mbwa likanivamia na kuanza kunishambulia. Wale mbwa hadi leo hii huwa sielewi kama walitumwa ama lah!

    Mbwa hawaogopi mvua wala mawe yaliyokuwa yakidondoka".

    Hapakuwepo na sababu ya kumchosha mwanaye Steve ambaye bado alikuwa akikabiliwa na mitihani.

    Akakomea hapo kwa usiku huo na kumtakia mwanaye usiku mtulivu. Akamuaga na kuingia chumbani kwake huku sebuleni Steven akibaki njia panda.

    Mbwa walimvamia tena akiwa na mimi. Ilikuaje hadi tukapona? Steve alijiuliza kabla ya kupotelea katika usingizi.

    Saa kumi na moja alfajiri alishtuliwa na sauti ya mama yake akilia kama kuna kitu kinamkaba. Akasikilizia kwa umakini kwa kudhani labda yu ndotoni. Haikuwa ndoto bali kitu halisi.

    Akainuka na kuwasha kurunzi yake ndogo. Akaelekea chumbani kwa mama yake. Akamshuhudia mama yake akirusha miguu huku na kule kama mtu anayetaka kuakata roho. Akamsogelea na kuanza kumuita kwa sauti ya juu.

    “Mama.. Mamaaa. Mamaaa...” Hakuelewa ni kitu gani kinamsibu.

    Aliita sana lakini mama yake hakutoa sauti ya kumuitikia. Akazidi kurusha miguu yake pamoja na mikono huku kifua chake akikipandisha na kukishusha kwa kasi.

    Alichokifanya Steven ni kutoka mbio hadi kwa mama Sung'wa. Akabisha hodi lakini mapigo yake yakiwa yanamuenda mbio sana.



    Baada ya dakika chache mlango ukafunguliwa. Akatokeza mama Sung'wa vidole vyake vikiyapikicha macho.

    "Mama yangu anakufa." Ni kauli aliyoitoa Steven pasipo kumsalimu mama yule aliyekuwa kampita umri mama yake.

    Lakini si kwamba ni kwasababu ya dharau. Hapana! Hali ya akili yake haikuwa sawa hata kidogo. Kumpoteza mama yake ilikuwa ni sawa na kupoteza kila kitu kwenye maisha ulichokiangaikia kwa miaka sabini.

    "Kuna nini kimemtokea??"

    "Mama yangu anakufa." Alirudia kauli ileile na wakati huo akimvuta mama Sung'wa ili akaone ni kitu gani kinaweza kufanyika kwa haraka ili kuokoa uhai wa mama yake.

    Mama Sung'wa ikabidi arudi ndani kwanza. Akajitanda khanga ndipo wakaongozana kwa mbio hadi nyumbani kwao na Steven lakini mkononi akiwa na mwiba ambao Steven hakuelewa kazi yake hadi. Wakakuta hali ya mama yule katika sintofahamu. Alikuwa katulia tuli pasipo kurusha mikono wala miguu kama ilivyokuwa awali.

    "Nipatie kiberiti." Aliongea mama Sung'wa. Naye Steven akatekeleza kama alivyoagizwa.

    Mama Sung'wa akawansha njiti ya kiberiti na kuichoma ncha ya mwimba ule ulioanza kutoa moshi. Akausogeza karibu na pua ya mama yake na Steven. Wakati huo Steven hakuwa sawa kabisa. Alishika hiki mara kile. Yaani ni kama alikuwa nusu ya mwendawazimu. Baada ya muda mfupi tangu moshi ule uanze kuingia katika pua za mama yule, akapiga chafya mfululizo.

    Kitendo cha kupiga chafya kikarudisha amani ndani ya nafsi ya mwanaye japo hakuwa ameongea.

    "Kwanini tusimpeleke hospitali??" Aliuliza Steve.

    "Hapana wala usitie shaka katika hili. Atakuwa sawa kipindi kifupi kijacho". Muda wa kuelekea shuleni tayari ulishawadia lakini kwa jinsi alivyokuwa akimpenda mama yake, hakuwa tayari kuelekea shule pasipo kuisikia kauli ya mama yake.

    "Mwanangu Steven." Ilimtoka sauti iliyojaa kitetemeshi pindi chafya zilipokoma.

    "Pole sana mama." Alitamka Steven huku akimsogelea na kumshika mkono wake.

    "Bado hujaenda shule?" Alimuuliza mwanaye swali ambalo halikustahili hata kidogo kwani alikuwa akimuona mahali pale.

    "Mama nisingeweza kwenda shule mapema ilihali hali yako si nzuri. Kwanza inatakiwa tuelekee hospitali ila wakaangalie ni nini tatizo." Alijibu Steven.

    "Ni kweli mwanangu uyasemayo lakini mimi mara nyingi natumia miti shamba kwani hii si mara ya kwanza mimi kukumbwa na hili. Wewe nenda shule ukamalizie mitihani yako. Nitakuwa salama kwa uwezo wa aliyeniumba."

    Alipenda sana kuzifuata kauli za mzazi wake. Akajiandaa na kuelekea shuleni japo kwa shingo upande.

    Akamuacha mama yake katika mikono ya mama Sung'wa. Njia nzima alikuwa akiwaza sana juu ya nguzo yake muhimu aliyoiona ni muhimu zaidi ya mboni ya jicho lake. Aliamini hata akipofuka macho yake yote lakini kama mama yake yupo hakuna kuhangaika kutembea na fimbo.

    Hadi anaingia katika viunga vya shule yao, bado alihisi kama yuko pembeni ya mama yake akimwambia pole. Hakuongea na mtu yeyote. Hata marafiki zake walipomsogelea hakufungua kinywa chake. Hakuwa tofauti na bubu.

    Walipozidisha usumbufua alihama eneo lile alilokuwepo na kwenda sehemu nyingine hadi muda wa kuingia kwenye ukumbi wa kufanyia mtihani ulipowadia. Siku Hiyo Steven na watahiniwa wenzake walikuwa wanahitimisha safari yao ya mitihani. Ni somo moja ambalo walitakiwa kulifanya. Phyisics.

    ***

    Nyumbani baada ya Steven kuondoka, mama yake akajaribu kuinuka akisaidiwa na mama Sung'wa ambaye tangu alipomuomba Steven kiberiti, hakuwa ameongea tena neno lolote lile. Ni heri asingejaribu kuinuka huenda angebaki salama. Aliponyanyua tu mgongo akahisi kama uti wake wa mgongo kuvunjika mithili ya mtu anayevunja ukuni mkavu.

    Maumivu aliyoyapata hayastahili kuhadithiwa kwako msomaji wa mkasa huu kwani yalikuwa makubwa mno. Kama unazo kumbukumbu nzuri ziwe za kuhadithiwa au kwa waliokuwepo enzi za miaka ya tisini na nane kurudi nyuma, ni wachache sana waliokuwa wakiamini dawa za mahospitalini tofauti na sasa.

    Hata mama yake Steven pamoja na wanakijiji wenzake walikuwa miongoni wa wanaoamini dawa za kienyeji kuliko za hospitali. Mbali na hilo, miguu yake nayo ikaanza kuuma na hatimaye ikaanza kuonyesha kuvimba. Mama Sung'wa akamuacha kwa muda na aliporudi alikuwa na dawa kwenye mfuko. Akazichemsha na kumpatia anywe. Angalau maumivu yakapungua.

    Alipomaliza taratibu zote juu ya mtihani ule, Steven akarejea nyumbani kiunyonge sana. Akamkuta mama yake akiwa amelala huku mama Sung'wa akiwa pembeni yake. Hali ya mama yake ilimhuzunisha vilivyo. Hakuwa na namna zaidi ya kushauri waelekee hospitali.

    Ushauri ambao ulipingwa kwa nguvu zote na mama yake pamoja na mama Sung'wa. Baada ya muda mfupi akaongezeka na mtu mwingine. Huyu ni Sung'wa. Msichana mbichi kabisa wa miaka kumi na tano.

    Alikuwa ni mzuri kiasi chake na hata Steven alikuwa akimpenda japo hakuwahi kumtamkia. Steven alimpenda lakini mama yake ndani ya moyo wake hakuwa akimpenda Sung'wa hata kidogo. Na hata alipowaona wakiwa wote hakufurahia hata kidogo. Sababu aliijua yeye mwenyewe ni kwanini alimchukia.

    "Mwanangu Steven."

    "Naam mama."

    "Hali yangu si nzuri kama unavyoniona mwanangu. Si kwamba nampangia MUNGU lakini nahisi kifo chako hakipo mbali. Wanadamu tumeumbwa na moyo unaofanana lakini tofauti katika matendo. Tumejawa na wingi wa tamaa zisizo na manufaa hata kidogo. Wengi wetu tupo tayari kuua mradi kufanikisha yale tunayoyafikiria. Lakini katu mwanangu usijejaribu kuua kisa maisha yako kuwa na ugumu. Mara zote ufinyu wa fikra zetu huwa chanzo cha maisha yenye utata."

    **

    Ujio wa Steven kutoka shuleni, ukamfanya mama Sung'wa kuaga na kuahidi kurudi kesho yake asubuhi.

    "Kama kutatokea tatizo kubwa Steven usisite kuja kuniita" Aliongea mama Sung'wa.

    "Kwaheri Steven." Alimalizia Sung'wa wakati huo wakiondoka. Lakini jicho la mama yake na Steven lilimuangalia kwa hasira Sung'wa.

    Walipoondoka tu, mama yake Steven akamtaka mwanaye amsikilize kwa makini hata kama njaa inamsibu lakini akae na kumsikiliza. Steven akatii ndipo mama yake akaanza kumhadithia huku akilia. Hakujali maumivu aliyokuwa nayo. Alichohitaji ni kumalizia hadithi yake ili hata kama uhai utauacha mwili, basi asimuache mwanaye katika dukuduku.

    "Kundi lile la mbwa likaanza kunishambulia. Nilipiga kelele sana huku nikijaribu kujiokoa lakini haukupatikana msaada.

    Nilikung'ang'ania kwa nguvu zote mwanangu ili usiumizwe na yale makucha pamoja na meno yao yaliyokuwa yakinirarua mimi. Mwanangu mwili mzima nikawa sawa na matope. Nilijitahidi vya kutosha hadi nilipopoteza uwezo wa kuparangana na hatimaye fahamu zilinipotea.

    Nilipozinduka, mvua ilikuwa imekata lakini nilikuwa eneo lilelile huku upepo ukiendelea kuvuma na hata anga bado lilikuwa limetanda mawingu hivyo kuzidi kusababisha kiza. Maumivu yalikuwa makali sana. Kila sehemu yenye nyama kwenye mwili wangu ilikuwa ikiniuma.

    Sikusikitika kwasababu ya maumivu yangu. La hasha! Kilichonisikitisha ni kwamba lile vurumai lilikuwa limenitenganisha na wewe. Takribani dakika kumi nilizitumia kulia huku nikitambaza mikono yangu huku na kule ili kuona kama nitakupata. Nikiwa nimeshakata tamaa kwa kudhani umechukuliwa na maji ambayo yalikuwa yakitiririka, nikasikia sauti yako ukilia. Nguvu zikanijaa ghafla.

    Nikakusogelea lakini mwanangu hali yako haikuwa njema hata kidogo. Ulikuwa ukitetemeka sana hadi nikaingiwa na uoga. Lile blanketi halikuwepo tena. Nadhani lilichukuliwa na maji.

    Sauti yangu ilifika mbali pindi nilipopiga kelele lakini hakuna hata jirani mmoja aliyetoka kutoa msaada. Majirani ambao mara zote tulikuwa tukicheka na kufurahi wakati wote,lakini siku hiyo nilizitambua roho za wanadamu. Wanapenda kulia wakati wa furaha ili kuficha undani wa miyo yao kiubinadamu.

    Mwanangu Steven amini MUNGU yupo. Na pasipo uwepo wake leo hii si wewe tu hata mimi pia tusingekuwa tunaendelea kuvuta pumzi hii tusiyoitolea gharama yoyote ile.

    Ningeweza vipi kukusitiri na baridi ile ilihali hata mimi nguo yangu ilikuwa imelowa? Mikono yangu tu yenyewe kukugusa ulikuwa ukishtuka kwasababu ilikuwa imekakamaa kuliko chuma kilichochomelewa. Nikajikakamua na kutembea hadi shuleni. Nikaingia kwenye moja ya darasa. Nikatulia humo hadi pale nilipohisi ujio wa mtu. Hii ni kutokana na kishindo kilichokuwa kikipenya katika ngoma za masikio yangu.

    Haikuwa kuhisi tena bali uhalisia pale mwanga wa kurunzi ulipopenya katika chumba kile. Alikuwa ni mlinzi. Nikaanza kuomba asiingie lakini wala haikusaidia. Akaingia na kutembea hadi sehemu ambayo nilikuwa nimekaa na kujikunyata huku wewe ukiwa kifuani mwangu ili upate joto". Historia ile ilizidi kupenya na kuingia hadi katika moyo wa Steven. Hakika mama yake alimfananisha na chuma,tena kile chuma cha mkoloni wa enzi za miaka ya 1880.

    Alikuwa akizidi kuhadithia lakini akakatishwa na kikohozi. Kikohozi kilichomsababisha kutapika hadi damu. Haikuwa mara yake ya kwanza kutapika damu lakini kwa Steven ilikuwa ni mara yake ya kwanza kuona hali ile kwa mama yake.

    "Kweli mama yangu unaumwa."

    "Haijalishi ni wangapi watakukejeli na kukuonyesha dharau za wazi katika kutimiza yale uliyojiwekea au yale yaliyo katika fikra zako kwa wakati huo.

    Mara zote dharau ziwe chachu ya wewe kuinuka pale ulipojikwaa na kusimama kwa nguvu moja huku ukiamini utafika wakati wale waliojivika kofia ya kiburi mbele ya fikra zako watakupigia makofi kama ishara ya uimara wako wa juhudi zako zisizoyumbishwa na mawimbi ya kukata tamaa". Aliongea mama yake Steven huku akijaribu kuinuka. Akashindwa.

    Na kilichokuwa kinamuinua pale ni ili akapate kujisaidia haja kubwa. Steven akabeba jukumu la kumletea kitu kitakachomsaidia kumaliza haja ile palepale.

    Mimba ni sawa na mbegu unayoipanda leo ukitegemea mavuno baada ya muda fulani. Tambua mbegu hiyo haiwezi kutoa matunda bora pasipo kuipalilia. Kama mama yake na Steven asingekaza roho yake hapana shaka siku hiyo asingepata msaada. Nani atakuletea beseni ujisaidie haja kubwa ilihali umri wako unaruhusu uwe na mtoto mkubwa wa kukufanyia hayo?

    Haijalishi magumu yapi utakumbana nayo lakini kumbuka mtoto ni sawa na ngazi katika maisha yako ya baadaye. Na ngazi bora ni ile iliyogongewa kwa misumari na siyo kwa kufungwafungwa na kamba. Vilevile mtoto ni sawa na mchezo wa kamari ya kwamba unaweza kupata au ukakosa. Wapo wengi waleao watoto kwa tabu lakini matokeo yake huambulia kashfa kutoka kwa hao waliosababisha wang'ate magodoro.

    Alipomaliza haja yake Steven aliyekuwa ametoka nje, akaitwa na kuondoa mahali pale huku mama yake akilia. Alilia kwasababu bila mwanaye huyo angeadhirika.

    "MIMI NI SHUJAA" Alijisemea mama yake na Steven pindi mwanaye akiwa hajarudi. Tangu aliporejea kutoka shule hakuwa ameweka chochote tumboni mwake lakini hakuhisi njaa. Bado alikuwa njia panda na yale aliyokuwa akihadithiwa na mama yake. Yalimvutia mno na kumuhuzunisha pia.

    "Sikuhangaika bure mwanangu Steven"

    "Kwanini unasema hivyo mama."

    "Mwanangu ni wachache sana wanaowatupa watoto wao au kutoa mimba lakini mara zote huwa kuna chanzo. Hakuna anayefanya hivyo pasipokuwa na sababu ya msingi. Ni dhambi lakini kuna wakati inambidi mwanamke afanye hivyo ili kunusuru kitu fulani. Lakini mimi mwanangu pamoja na tabu zote nilivumilia na leo hii nimepokea matunda ya mateso yangu kwako".

    "Umeruhusiwa na nani kuingia humu ndani?". Aliniuliza yule mlinzi kwa ukali huku uso wake ukiwa umechora michirizi ya makunyazi kuashiria amechukia.

    Sikuwa namuona usoni lakini kwa jinsi alivyouliza niliamini amekasirishwa na kitendo changu cha kuingia kwenye lile darasa.

    "Hapana baba'angu hakuna aliyeniruhusu bali hizi tabu zangu ambazo zinaniadhibisha mimi na huyu mtoto." Nilimwambia ndipo akatusogelea zaidi na kukuondoa wewe mikononi mwangu.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog