Simulizi : Nisamehe Mama
Sehemu Ya Tatu (3)
Akajitoa lile koti na kukufunika halafu akaniambia nimfuate wakati huo alikuwa akipiga hatua za kutoka nje ya darasa lile. Nikamuona ni mtu kati ya wenye kuwa na fikra za utambuzi juu ya neno maisha.
Mwanangu maisha ni sawa na barafu. Kamwe haiwezi kubaki katika kuganda endapo itasogezwa kwenye joto. Lazima itayeyuka. Na ikirudishwa kwenye baridi hapana shaka itarudi katika hali yake ileile.
Katika maisha unaweza kuvuma au kuvumishwa kwasababu ya kitu fulani lakini tambua wakati ukifika vyote vitayeyuka na waweza kuanguka daima usisimame tena hata kama upeo wako kifikra uko juu kiasi gani.
Mwanangu Steve, katu usisite kumsamehe yeyote yule kwani hata wewe wapo utakaowakosea ama ambao uliwahi kuwakosea. Haijalishi kosa lako lina uzito kiasi gani.
Nikainuka na kumfuata yule mlinzi.
Pamoja na kujivika roho ya ujasiri lakini moyo wangu haukuwa na amani hata kidogo. Yote hii ni kwasababu yako mwanangu. Nilihitaji kuona ukiwa salama hata kama usalama wako utanigharimu.
Nikamuona akiingia kwenye darasa lingine. Na mimi nikaingia. Akakutandikia hilo koti na hapohapo likawa kama blanketi kwako. Alipohakikisha uko salama eti ananisogelea. Hakujali hata hali yangu ilivyokuwa katika ugumu. Sikujua hata nguvu zilitoka wapi. Nikasukuma moja ya dawati ambalo lilimuumiza mguu na kumsababisha apige ukelele mmoja tu na kutulia.
Nilihisi kuchanganyikiwa sana baada ya tukio hilo. Nikakutoa pale chini na kuhama haraka eneo lile kwani halikuwa salama tena kwa upande wangu. Kwa jinsi nilivyokuwa, sikutofautiana na wale wanatalii katika mlima Kilimanjaro. Hata ungenipatia maji ya yanayochemka na kuingiza mkono nisingehisi kuungua.
Nilikuwa katika tabu iliyopitiliza. Kila kiungo kilitetemeka kwa baridi. Nikatembea hadi kanisani ambapo nililala barazani.
Kabla hakujapambazuka nikarejea hapa nyumbani ambapo nilikuta nyumba yetu haionekani kutokana na kufunikwa na maji. Nikiwa najiuliza cha kufanya ili usiku wa siku hiyo nisipatwe na tabu, nikasikia makelele ya wanafunzi shuleni. Nikatambua hali si shwari na muda wowote nitakamatwa".
"Mama naomba nikukatishe kidogo kwa sababu utumbo nahisi unawaka moto".Steven alivumilia lakini hatimaye alimkatisha mama yake.
"Mwanangu wewe! Ila ipo siku hutahisi njaa japo sikuombei hivyo kama ilivyonitokea mimi siku hiyo." Aliongea mama yake na Steven wakati huo Steven alishanyanyuka kwenda kujipatia chakula jikoni.
Alitumia dakika tano tu kumaliza kula. Yote hii ni kwasababu ya hamu juu ya mkasa wa maisha alioupitia mama yake. Mkasa ambao ulikuwa ukizidi kumteka kila dakika ndani ya ufahamu wake.
Alitoka shule saa kumi lakini chakula alikipata saa moja. Alichokifanya baada ya kumaliza kula, akarudi ndani na kuketi pembeni ya mama yake ili aendelee kupata uhondo.
“Uhu! Uhu!”.Alikohoa kidogo ndipo akaendelea kumpatia mwanaye kile alichokianzisha;
"Usiogope kujikwaa pindi upambanapo na vikwazo vya maisha. Vikwazo ambavyo mara zote husababishwa na binadamu mwenziyo ambaye amejawa na roho ya wivu. Upigapo hatua tano, geuka nyuma na utizame wapi panastahili kurekebishwa.
Mwanangu kamwe usikubali kuyumbishwa kifikra kwani utawapatia nafasi ya kukanyaga juu yako wale wapendao kukuona ukitaabika kila wakati.
Yale makelele yaliendelea kusikika na wanakijiji walianza kuelekea huko shuleni ili kujua ni kitu gani kinaendelea. Mapigo ya moyo yalianza kunienda mbio japo sikuwa nimetambua kama alikufa ama lah! pale nilimpomsukumia kwenye dawati lililosababisha anguke na kutulia kimya.
Sikuwa tayari kukamatwa na polisi na vilevile sikuwa tayari kutiliwa shaka juu ya jambo hilo. Lakini kilichokuwa kikinitia matumaini ni kwakuwa usiku ule hakuna aliyeona nikiingia na kutoka katika viunga vya shule ile kwasababu ulikuwa ni usiku wenye kiza totoro.
Lakini je, kama atakuwa hai si atasema mimi ndiye chanzo cha yeye kukutwa katika hali ile? Hakuna kitu kilikuwa kikiutetemesha mwili wangu kama jela au kituo cha polisi. Sikuwahi kufika lakini wale waliokuwa wakitoka hulo hawakusita kutoa simulizi za waliyokutana nayo huko magereza.
Mbali na kuwaza pasipo majibu ya haraka, nikapiga moyo konde na kujichanganya na waliokuwa wakielekea huko shuleni. Kwa waliomsogelea walisema mapigo yake ya moyo yanadunda kwa mbali.
Hapo angalau nikapata ahueni kwani kifo lingekuwa tatizo lingine tena kubwa kuliko maelezo. Hakupelekwa hospitali pindi alipofika Bi Hellen ambaye alikuwa mganga wa kijiji chetu. Akampatia dawa alizozijua yeye na fahamu zilimrejea mlinzi yule. Alipoulizwa kilichotokea nilihisi kama naota. Akasema ni vibaka walimvamia. Amani ikarejea na naamini hakujua kama ni mimi kwani hata nilipokutana naye mtaani hakuniuliza chochote."
"Pole sana mama'angu kwa magumu uliyoyapitia. Lakini hapa tunapoishi uliachiwa na nani? Na mbona unaonekana kumchukia Sung'wa". Ni maswali mawili mfululizo yalimtoka Steven pindi mama yake alipokoma kuhadithia.
"Mwanangu katika kutimiza yale uyafikiriayo, jiweke mbali na wenye moyo iliyojawa na tamaa. Mama yake Sung'wa amejawa na tamaa hivyo sitapenda uwe kwenye mahusiano na binti yake.
Najua utaona kama nakunyanyasa kimaamuzi yako lakini kumbuka ni moja ya kukulinda na wale waonyeshao uzuri kitabasamu na kiubaya moyoni ambako si rahisi kugundua endapo fikra na upeo wako utakuwa ukipepesa mita kumi ilihali wao wanapepesa mita hamsini."
"Lakini mbona amekuhudumia bila kinyongo?"
"Utakuwa huna fikra pevu endapo utadanganyika na cheko pamoja na tabasamu la mwanadamu. Hata sekunde moja usiogope kuchukiwa ikiwa malengo yako yanaelekea kuyumbishwa pasipo na sababu ya msingi kwani utajiweka katika utata unaoweza kuigharimu roho yako ili kuutatua."
"Moja umenijibu japo umeniweka kwenye utata kwani naumuona Sung'wa ni mtulivu. Lakini napaswa kuheshimu yale uyatamkayo kama wewe ulivyostahimili tabu ukiwa na mimi."
"Vyema kama umenielewa. Ngoja nikujibu na lililobakia. Miezi mitatu tangu nitoke kwa mwenyekiti katika suala la nyinyi kuachwa kituoni, hali ya maisha Maganzo nzima ilibadilika na kuwa ngumu kuliko maelezo.
Wakati huo bado hukuwa unaweza kuvumilia njaa. Vibarua ambavyo vilikuwa vikinipatia kodi ya chumba pamoja na matumizi yangu na wewe vikaadimika na hatimaye vikapotea kabisa. Ikiwa imebaki siku nne mbele nidaiwe kodi ya nyumba, nikapata taarifa ya kwamba huko Bariadi hali ya maisha inaridhisha.
Nilikuwa na elfu moja kwenye pindo la kaka yangu. Fedha ambayo isingeniwezesha kusafiri au kupanda usafiri wowote. Njia pekee ya kuniwezesha kufika huko ilikuwa ni kwa miguu japokuwa umbali ulikuwa mrefu.
Sikujali hilo ili wewe usije nyanyasika ilihali mzazi wako nipo. Nikanunua mkate. Nikajaza maji kwenye kidumu cha lita tano. Hapo nikawa tayari kwa safari.
Siku iliyofuatia saa kumi na moja alfajiri, nikaanza safari yangu kwa miguu wewe ukiwa mgongoni." Alipofika hapo akatulia kisha akamuuliza swali Steven,
"Unakumbuka nilikwambia ipo siku hutahisi njaa?"
"Nakumbuka mama"
"Nikiwa njiani nikakutana na dada mmoja ambaye alikuwa amekaa pembezoni mwa barabara huku akionekana kuchoka sana. Hali yake kiafya ilikuwa imezorota mno. Nikamsogelea na kutaka kujua kulikoni. Nikakutana na kitu kilichonitoa machozi."
Alipofikia hapo hakuendelea tena, akamtaka Steven akalale ili kupumzika kwani tangu atoke shule hakuwa amepata mapumziko.
Steven akarudi sebuleni na kukunjua kigodoro chake. Akajitupa kuisaka siku mpya japo kimang'amung'amu kutokana na hali ya mama yake kiafya.
Alishtuliwa asubuhi na mapema na sauti ya mama Sung'wa aliyekuwa akigonga mlango. Akanyanyuka na kukunja matandiko yake, ndipo akausogelea mlango na kuufungua.
Akamsalimia huku mama yule akiiingia chumbani kwa mama yake ili kumjulia hali. Alikaa pale hadi majira ya saa mbili alipoondoka huku akiwa amewapatia maelezo ya dawa zile za kienyeji.
Siku hiyo ilikuwa ni siku ya jumamosi. Hivyo Steven alikuwa tu nyumbani. Na hata kama ingekuwa ni siku ya mwanzo au katikati ya wiki, isingejalisha kwani mitihani ya kuhitimu alishamalizana nayo.
"Utajisikiaje ukimuhurumia mtu halafu huruma hiyo iwe chanzo cha tabu kwa upande wako?" Ni swali aliloulizwa Steven na mama yake baada ya kumaliza kunywa chai.
"Nitajisikia vibaya sana."
"Hapana mwanangu. Msaada toa endapo uwezo wa kutoa upo kwani na wewe zitafika nyakati za kuwa na uhitaji. Haijalishi utakugharimu ama lah!"
"Asante kwa kunijenga mama. Na ilikuaje kwa yule dada uliyemkuta pembezoni mwa barabara."
"Wananiua kisa ujauzito wake." Ndivyo alivyoniambia kwa sauti iliyoambatana na kitetemeshi.
“Nikajiuliza wakina nani wanamuua ilihali yu peke yake mahali pale? Kabla sijamuuliza nikamuona ananinyooshea mkono huku akiomba nimpatie kile nilichokuwa nimekishika mkononi ambacho ni mkate,tena vikiwa vimebaki vipande vichache mno ambapo nilikuwa nimevigusa saa saba za mchana.
Hivyo pale hata mimi nilikuwa navitamani lakini wewe ungekula nini? Alikuwa na njaa. Wakati huo kiza kilikuwa kinaanza kuingia. Nikimaanisha nimeshatembea takribani masaa kumi na nne.
Nikamuangalia kwa muda nikaona heri kumpatia hata vipande viwili pamoja na maji. Vikabaki vitatu ambavyo vilitakiwa kuliwa na wewe ila mimi nivumilie hadi nifike niendako”.
Alipomaliza kula akaniambia,
"Nilifikiri wanawake wote wana roho za kinyama kumbe hapana. Wewe umenisaidia japo hunifahamu lakini umenisaidia katika nyakati zangu za mwisho. Mimi ni wa kufa tu."
“ Hapo akanionyesha kitu kilichonifanya nikuweke chini ili nimuangalie vizuri nikiwa nimeinama karibu yake. Zilikuwa ni damu zikimtoka sehemu zake za siri. Akaniwahi kabla sijamuuliza chanzo cha hali ile”.
"Kawahusie wale wanawake wapendao kuachia nyeti zao kwa wanaume wasiotambua thamani zao kwao. Wakumbuke kudhibiti hisia zao ili yasiwakute haya yanayoniua.
Nilimpenda kwa kiwango cha kupitiliza pasipo kutambua uthamani wangu kwake. Kumbe hakunipenda na alikuwa na mwanamke mwingine ambaye nilikuwa nikimuona pale kwake mara mojamoja sana na aliwahi kunitambulisha ni mtoto wa shangazi yake.
Hatukuwa tumeoana na sikuwa nikilala kwake. Mara nyingi alikuwa akiniambia anahitaji mtoto. Nikataka kumshtukiza. Nikamuachia anichezee nikiwa kwenye siku za hatari na kweli mimba ikanasa.
Mwezi mmoja hali yangu ilivyobadilika nikaenda hospitali ndipo nikagundulika nina mimba. Nikajawa na furaha ya aina yake. Nikajiona nitakuwa wa thamani zaidi katika nafsi yake. Kumbe hakuwa kama nilivyokuwa nikimuona akicheka na kutabasamu.
Nilidanganyika na tabasamu lake. Likanigharimu.
Nilipotoka pale hospitali ikiwa majira ya mchana nikarudi nyumbani.Ilipofika jioni. Nikaelekea kwake ili kumpatia taarifa zile.
Nilipofika kwake nilikuta hali ya utulivu sana. Pale palikuwa kama kwangu, nikasukuma mlango na kuingia. Huwezi amini dada'angu niliwakuta yeye na yule aliyeniatambulisha kama mtoto wa shangazi yake wanafanya mapenzi.
Niliishiwa nguvu na kujikuta naanguka chini japo sikupoteza fahamu. Sikutaka kumficha. Nikamwambia hali yangu mbele ya huyo mwanamke wake. Sikujua kama nilikuwa najifukia nikiwa hai.
Akiwa uchi yule mwanamke alinirukia na kunikanyaga tumbo langu kwa nguvu. Hata yule niliyezoea kumuita mume wangu akacheka na bila huruma akanikanyaga kwa teke na kuanza kunisukumia nje huku akiniita mchawi.
Kilichonigharimu ni kwamba uhusiano wangu ulikuwa ni wa kificho. Hakuna hata rafiki yangu mmoja aliyekuwa akitambua uhusiano ule kwani ndugu sikuwa nao. Watu wa Shinyanga wanavyoamini uchawi nilijua litatokea balaa eneo lile. Nikajiinua pale japo maumivu ya tumbo langu yalikuwa makubwa mno. NAKUFA...". Yule dada alikuwa akinihadithia huku nikimuona anatetemeka kwa nguvu.
“Nikashangaa ameacha kuongea na kutulia pasipo kujitikisa. Sikutaka kumgusa, nikaweka sikio langu karibu na moyo wake ambapo mapigo yake ya moyo sikuyasikia. Nilishtuka sana na nilichohisi kwa haraka ni kwamba alipoteza maisha palepale. Hata hakuwa amemaliza kunihadithia lakini sikuwa na namna.
Usalama wangu pale kama ningekutwa na polisi ulikuwa mdogo. Kwanini nijiweke matatani? Nikafanya ishara ya msalaba kisha nikamuacha mahali pale na kuendelea na safari yangu. Lakini katika pointi niliyoinasa kwake ni kwamba mapenzi ya siri ni hatari sana. Wakati nakutana na dada yule nd'o nilikuwa nimeivuka Maswa.
Roho yangu ilikuwa kwenye maumivu sana. Nilitamani hata ningemfahamu huyo mwanaume aliyempa mimba ili nimwagie hata tindikali kwenye macho lakini nisingeweza kumfahamu. Safari yangu ikaanza kuyumba miguu ilipoanza kuniuma kwasababu ya kutembea umbali mrefu. Njaa haikuwa mbali na utumbo wangu. Sikuwa na chochote cha kuituliza kwani kilibaki kipande kimoja tu cha mkate baada ya vile viwili kuliwa na wewe.
Umbali kama wa kilometa mbili tangu nimuache dada yule, miguu ikaniuma sana hali iliyonifanya nishindwe kuendelea kutembea. Wakati huo nilikuwa nimefika sehemu iliyoonyesha kuwa pori kwani hapakuwepo na nyumba.
Ni vichaka pekee pamoja na miti mifupimifupi. Nikatoka barabarani na kuingia kwenye moja ya kichaka. Nikatandika khanga yangu na sweta nililokuwa nalo nikakufunika wewe. Hao mbu walioibuka humo kichakani nahisi walikuwa wa kutumwa.
Mbu, njaa pamoja na maumivu ya miguu ni vitu ambavyo vilinisulubu usiku kucha. Sikufumba jicho langu kwa ajili ya usingizi. Nilikuwa nikiwafukuza mbu wasiukabili mwili wako. Hakika nilikuwa katika nyakati zinazokomaza fikra. Nilikomaa vilivyo kifikra.
Kabla hakujapambazuka nikatoka mule kichakani na kuendelea na safari yangu japo bado miguu ilikuwa ikiuma. Mwanga utokao angani ulipoimulika ardhi niliweza kugundua miguu yangu ilikuwa imevimba. Hilo halikukomesha safari yangu.
Majira ya saa saba za mchana, nilikuwa pale kwenye kiwanda cha kusafisha pamba kilichoko Bariadi. Moyo wangu ukalipuka kwa furaha kwani niliamini tayari nimefika. Nikakipita na baada ya saa moja nilikuwa kwenye kibao kilichoandikwa Ngulyati. Kibao ambacho kipo katikati ya mji wa Bariadi”.
"Nianzie wapi?" Ni swali ambalo nilijiuliza.
“Cha muhimu ilikuwa ni kuokoa tumbo langu kwa njaa. Nikatembea hadi sehemu iliyoonekana ikifuka moshi huku watu wakiingia na kutoka. Naweza kushukuru kwamba nilipata msaada wa chakula pasipo malipo yoyote kutoka kwa huyo mmiliki wa hoteli ambaye alikuwa ni mwanamke.
Nilipomaliza kula nikamueleza ni wapi yanapatikana mashamba kwa wingi ili nikapate kibarua huko. Akanielekeza sehemu moja inaitwa Kidinda. Naamini kwa waliowahi kuishi Bariadi wanakifahamu hicho kijiji.
Huko ndiko nilikutana na Sabo. Mzee ambaye aliniachia hii nyumba pamoja na lile shamba letu baada ya kifo chake. Yeye alikuwa mwenyeji na ndiye aliyeniajiri. Akanipatia hadi hifadhi. Alikuwa ni mwema na mkarimu kwangu.
Miguu ilinisumbua sana lakini aliweza kunihudumia hadi ikapona. Ukamuita baba na yeye akakuita mtoto wake. Mimi nikamuita mume wangu. Maisha yakasogea na baada ya miaka miwili ya kuishi Bariadi, akaniambia turudi Maganzo. Wazo lake hilo sikuliafki kwani mateso niliyokuwa nimeyapata yalikuwa makubwa. Lakini aliponihakikishia kutoteseka nikamkubalia.
Kumbe alikuwa ana kiwanja ambacho nd'o hiki. Tukafunga safari tena kwa gari na si kwa miguu kama ilivyokuwa kwa upande wangu wakati wa kuelekea huko. Tulipofika huku nyumba hii ilikuwa imeshajengwa. Tukaishi hapa na wewe akakuandikisha shule lakini siku zote hizo nilizoishi naye nilikuwa sijawahi kumuuliza historia yake.
Kilichonishangaza ni pale alipoanzisha tabia ya ulevi. Kule hakuwa akinywa hata kidogo. Nikaingia uoga kwani kuna siku alikuwa harudi nyumbani.
Mbali na ulevi wake hakuwahi kunyanyua mkono wake kunipiga. Ilikuwa ni vigumu sana kumtambua. Hata nilipomkwaza hakuonyesha kuchukia. Mara zote alipenda kucheka na tabasamu halikuwahi kukauka usoni mwake. Niseme alikuwa ni wa kipekee sana”.
*******
"Tumeishi na wewe kwa muda sasa, lakini hukuwahi kuniambia historia yako ilihali ya kwangu nilishakusimulia pasipo kificho,kwa nini?" Ni swali nililomuuliza siku moja majira ya mchana tulipotoka shambani.
“Wakati huo tulikuwa tumemaliza kula chakula. Alichonijibu ni hiki”.
"Nikirejea kutoka Maganzo mjini nitakusimulia japo inahitaji moyo kuisikiliza. Na vilevile inaweza kuchukua uhai wangu." Akaondoka na kuniacha hamu ikiwa juu ya kile kinachohitaji uvumilivu kukisikiliza na ni kwanini aseme inaweza kuchukua uhai wake.
“Nilimsubiri sana ili tuelekee shambani kama ilivyokuwa kawaida lakini nilichoka kusubiri,ikanibidi nielekee shambani mwenyewe. Niliporudi bado hakuwa amerejea.
Nikapika chakula cha jioni tukamgojea ili tuweze kula pamoja lakini hali ilikuwa ni ileile. Tukala na kulala. Majira ya saa kumi za usiku yakasikika makelele kuashiria kuna jambo. Nikafungua mlango kisha nikatoka na kuungana na watu wengine hadi yalipokuwa yakitokea hayo makelele. Sikuamini”.
"Mara zote fikra komavu huwa chanzo cha urahisi wa yale yenye utata".Mama yake Steven aliendelea kumsimuli mwanaye.
“Alikuwa ni Sabo huku damu zikiwa zimetapakaa mahali pale alipokuwa amelala. Alikuwa amecharangwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake.
Kila mmoja aliogopa kumsogelea. Ni mwanamke lakini mimi ni zaidi ya mwanaume katika kulikabili jambo lenye kuhitaji ujasiri.
Nilimsogelea na kuanza kugaragara juu ya mwili wake. Zile damu zikatapakaa mpaka kwenye nguo zangu. Hata nami nikawa sawa na yeye.
Ni kwamba tayari roho yake ilishajitenga na mwili wake. Hilo halikuhitaji uthibitisho wa daktari. Baada ya muda ambao nilishalia na macho yangu kuvimba, ikatakiwa polisi wapatiwe taarifa ili mwili upate kufanyiwa uchunguzi.
Akajitolea kijana mmoja aliyeelekea kituo cha polisi alfajiri ile kutoa taarifa. Haukupita muda mrefu,maaskari wakafika na kukamilisha taratibu zao ndipo nikaondoka nao hadi kituoni. Niliulizwa maswali mengi lakini pointi yangu iliyowagusa ni pale nilipowaambia kwamba mchana wa jana yake aliniambia kwamba historia yake inaweza kumgharimu maisha yake”.
" Wewe ni mtu wake wa karibu sana. Je kabla halijatokea hili alikuwa kwenye mpishano wa kauli na mtu yeyote?".Ni swali nililoulizwa na mmoja wa maaskari.
Nilipomjibu ya kuwa sikuwahi kushuhudia hilo labda katika vilabu vya pombe aliyokuwa akinywa, akanitaka tuelekee nyumbani kwa uchunguzi zaidi.
“Nilitaka kubisha kwasababu hakuuliwa nyumbani lakini nikaona haina busara. Nikaongozana na maaskari watatu hadi nyumbani huku mwili wa marehemu ukipelekwa hospitali. Wakati huo kulishapambazuka.
Walikagua kila kona ya nyumba ili kuona kama kuna chochote kingeweza kuwasaidia lakini hawakuambulia chochote. Wakaniaga na kunitaka kuelekea hospitali kwa ajili ya kufanya taratibu za kuuchukua mwili wa marehemu.
Walipoondoka, majirani ambao walikuwepo pale nyumbani wakaanza kupanga ratiba za msiba. Kesho yake mazishi yakafanyika na suala lilibakia kwa maaskari wakisema uchunguzi unaendelea.
Hapo tayari walishakamatwa zaidi ya watu watano ambao nao walikuwa wakijihusisha na ulevi sehemu moja na yeye. Pamoja na kukamilisha mazishi yake, akili yangu haikuwa imetulia hata kidogo. Nilijiuliza sana ni kina nani walimsababishia kifo lakini jibu halikupatikana.
Kilichoniweka katika utata ni kuniambia kitu kilichoendana na ukweli. Lakini hakuwa amenihadithia. Je kuna siri gani kwenye maisha yake? Ni nani wa kunipatia jibu la swali langu? Hayupo.
Nikaendelea kubaki na utata wangu juu ya kifo chake cha kikatili. Hakuwa na ndugu hivyo nikamiliki kila kilichomhusu. Wale waliokamatwa wakaachiwa kutokana na kutopatikana na hatia. Maisha yakazidi kusonga pasipo misukosuko yoyote. Nikamsahau kabisa Sabo kwenye maisha yangu kwani nisingeweza kumuona tena. Sikutaka kuwa na mwanaume tena na ndiyo maana unaniona hivi peke yangu”.
Hadi mama yake Steven anamaliza mkasa wake, tayari ilishatimu majira ya mchana. Steven akaingia jikoni. Akaandaa chakula pasipo na dukuduku lolote moyoni mwake juu ya historia ya mama yake yote alihadithiwa bila kufichwa.
"Nitawaheshimu wanawake wote wale wenye kuleta watoto duniani na si wale wawaangamizao kwani hawatambui tabu ya aina yoyote katika suala zima la malezi". Ni maneno aliyokuwa akijisemea Steven akiwa anaendelea kupika.
Akiwa anamalizia kupika, akaonekana mama Sung'wa akija huku akicheka. Bila shaka kulikuwa na jambo lililokuwa likimsababisha awe katika furaha ya aina ile.
"Shida kwisha." Aliongea mama Sung'wa huku akicheka.
"Kuna nini?" Aliuliza Steven.
"Subiri utaona baada ya muda mfupi." Aliongea mama Sung'wa ambapo hazikupita dakika tano likaja gari likiwa na watu wanne ndani yake. Watatu waafrika na mmoja mchina.
Walikuwa wamekuja kukagua eneo lile kwa ajili ya kazi yao ya uchimbaji madini. Waliteta mengi na kabla hawajaaga na kuahidi ununuzi wa nyumba na si kujenga, waliwaachia kiasi fulani cha fedha. Fedha hizo alizitoa yule mchina.
"Wingi wa mali haumaanishi umeepuka tabu. Tabu zipo na hazizuiliki haswa kama zilipangwa zikukabili.
Hata uwe na fedha kiasi gani, zitafika nyakati za wewe kuziona mali si chochote kama thamani yako. Kamwe usithamani mali kuliko utu. Hutajizika.
Wale uwatemeao mate na kuwaona hawana thamani kisa mali zako, ndiyo hao watakaokufukia. Thamani ya mtu si pesa bali ni kile kilicho ndani yake. MOYO.
Utambue kuheshimu jamii". Aliongea mama yake na Steven pindi wageni wale walipoondoka. Maneno yale yalimfanya kucheka mama Sung'wa lakini hakueleza kwanini alicheka.
Yeye pia hakukaa sana, akaaga na kuondoka.
*STEVEN ANASIMULIA*
“Ahadi ya uchimbaji wa madini eneo lile tulilokuwa tukiishi ilikamilishwa. Tulinunuliwa nyumba pale Shinyanga mjini lakini hatukuwa tena majirani na kina Sung'wa. Japo sikusita kuonana na Sung'wa kwa siri.
Kiukweli nilikuwa nampenda sana yule msichana. Hatukuwa tumefanya mapenzi. Kila mmoja alikuwa akimuogopa mwenzake.
Mbali na hilo, tuliamini mapenzi si ngono. Bali mapenzi ni hisia zetu zinasema nini. Nilizirutubisha hisia zangu kwa Sung'wa na yeye akafanya hivyo kwa upande wangu. Mama yangu hakuwa akisimama. Alitembea na baiskeli ya walemavu. Matokeo ya mitihani yalipotoka, nilihisi kuchanganyikiwa.
Matokeo yangu yakanifanya nijone sina thamani tena katika ulimwengu wa wanadamu. Nilikuwa nimefeli.
Haikuwa rahisi kuamini kama ni mimi niliyefanya mitihani kwa umakini mkubwa. Nililia sana hadi wenzangu wakanishangaa. Kilichonifanya haswa nilie ni jinsi gani mama atayapokea matokeo yangu. Hakika ilikuwa ni vigumu hadi anielewe.
Ile kauli ya kufeli mtihani si kufeli kimaisha kwa upande wangu niliiona ya kipuuzi. Machozi yangu hakuna aliyeyajali kwani wengine walikuwa kwenye furaha na wengine kwenye huzuni kama mimi.
Nilijifikiria sana kujiondoa uhai kwa kukaa katikati ya barabara ghafla ili gari linigonge lakini nikakumbuka pesa ya kuniwezesha kimaisha ipo kutokana na ile kampuni iliyotuhamisha eneo letu.
Pamoja na kwamba ilikuwepo ahadi ya kusoma kwa kupitia mgongo wa kampuni sikuona kama kuna umuhimu wa kurudi darasani. Yote hayo niliyawaza wakati nikirejea nyumbani ili niweze kumueleza mama matokeo yangu.
Umbali haukuwa mrefu lakini nilitumia zaidi ya saa moja hadi kufika nyumbani. Kila niliyekuwa nikipishana naye njiani nilimuona kama mbaya wangu katika maisha yangu yajayo. Hata wale waliokuwa wamenizoea katika hali ya ucheshi na tabasamu muda wote, siku hiyo hawakuamini. Nilibadilika ghafla na uso wangu ulitawaliwa na makunyanzi yaliyofunikwa na machozi”.
"Siamini mama". Ni kauli niliyoitoa pindi nilipofika nyumbani na kumkuta mama yangu barazani kwenye kibaiskeli chake cha tairi tatu. Wakati huo nilikuwa nimejilaza sakafuni.
"Huamini nini mwanangu?"
"Nimefeli mama." Kauli yangu hiyo ya kiujasiri niliitoa huku macho yangu yakiwa yanamuangalia usoni.
Nilitegemea angepata mshtuko mkubwa lakini haikuwa hivyo. Alianitizama pale chini nilipokuwa nimejilaza kwa takribani dakika kadhaa ndipo akafungua kinywa chake na kuanza kuniweka katika hali ya kawaida kwani nilikuwa nimekata tamaa.
"Usitegemee hata siku moja kuwa dunia itasimama. Nikimaanisha haitazunguka katika mhimili wake.
Kadri inavyozunguka ndivyo siku zinasonga mbele. Katika siku hizo zipo zenye kuhitajika uvumilivu katika magumu yake. Vilevile zipo zenye kukufanya uione dunia ni kisiwa cha starehe.
Mwanangu usisite kusimama haraka pindi ukianguka katika mbio zako za kuelekea katika taa imulikayo maisha yenye furaha. Kumbuka si wewe tu iliyefeli mtihani. Wapo na wenzako walio katika kulia hata zaidi yako. Simama na uanze kupiga hatua za kusawazisha yale mambonde yaliyosalia." Aliyasema hayo mama huku akilia.
Machozi yake hayo naamini aliyatoa kwa kuona amenitaabikia muda mrefu lakini bahati yenye kuatisha tamaa ikasimama pale nilipokuwa nimeweka mguu mmoja. Huku mguu wa pili ukiwa hauna nguvu hata chembe. Hapo naamanisha mama yangu hali yake kiafya ilikuwa si nzuri hata kidogo. Mama yangu ndiye alikuwa mguu wangu wa pili pamoja na jicho langu la pili.
"Najiona asiye na thamani tena mama katika hili."
"Steven fungua upeo wako na utambue ya kuwa maisha hayana hatua moja. Ukishindwa ya kwanza ipo inayofuata. Usikubali kunyong'onyeka nafsi yako kwani muda upo na unatosha kwa wewe kufukia pale ulipofukua pasipo kutarajia."
Maneno ya mama yangu yalikuwa yenye kunitia faraja lakini hayakuniingia hata kidogo. Nilimkubalia tu ili asinione nimekuwa mtata mbele yake. Hilo likapita. Hata kwa upande wa Sung'wa naye alikuwa kama mama yangu maneno yake yalikuwa yaleyale japo ya kwake hayakuwa na uzito mkubwa.
"Elimu ni kupanua upeo wa akili na si kuondoa ujinga kama wasemavyo wengi. Wapo wenye elimu zenye viwango vya juu lakini ukikaa nao dakika kumi utaona ni heri wale ambao hawajaenda hata shule.
Wale wasio na elimu watakupa mwanga mzuri katika kupambana na maisha kuliko hao watakaong'ang'ania maisha bila elimu ni sawa na kuingia ziwani na mtumbwi pasipo kasia. Kizuri zaidi shule utaenda kwa fedha za wafadhili." Nakumbuka maneno hayo aliyatamka Sung'wa,msichana ambaye mama yangu hakuwa akimpenda. Faraja zote nilizisikiliza kwa umakini lakini katu sikuwa tayari kurudi shuleni.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment