Simulizi : Nisamehe Mama
Sehemu Ya Nne (4)
Mawazo yangu yote yalikuwa kuendesha biashara hata kama sikuwa nimesomea masomo ya biashara. Hilo nililiweka moyoni mwangu na siku moja majira ya mchana tukiwa tunakula niliamua kumuweka wazi mama yangu. Hii ni kwakuwa pesa ya kuanzisha biashara ilikuwepo.
"Mama naona nifungue duka kwasababu shule sina mawazo nayo tena." Maneno yangu hayo yalimshutua sana na hata kijiko alichokuwa amekiinuka kilianguka chini na mwili wake wote nikaona unatetemeka.
Nilishindwa kumuelewa ni kwanini alikumbwa na hali ile ghafla. Hakuongea lolote. Akajisukuma kwenye kibaiskeli na kuelekea chumbani kwake. Nikasikia akifunga mlango wake kwa nguvu hadi nikashtuka sana. Hata nami hamu ya chakula iliniisha.
Nilijiona nimemkosea sana japo alitakiwa aheshimu maamuzi yangu. Na hata kama ni kuyapinga, basi si kwa namna ile.
Nilikaa kwa muda sana pale sebuleni nikitafakari ni nini haswa kilichomsababishia hali ile lakini sikupata jibu. Usingizi ulipitia nikiwa nimekaa palepale kwenye kiti.
"Kubali kuitwa mwenye tamaa katika kutimiza yale uyafikiriayo mradi yawe katika njia nyoofu mbele za Muumbaji."
“Nilishtuliwa na baridi kali iliyoanza kupuliza majira ya usiku wa manane. Nikainuka na kuelekea chumbani kwangu. Nikajitupa kitandani lakini bado akili yangu iliwaza sana hali ya mama yangu pindi nilipomueleza nia yangu ya kufungua duka. Hadi napitiwa na usingizi kwa mara nyingine, mawazo yalikuwa ni yaleyale”.
“Tofauti na siku zote, siku iliyofuata nilichelewa sana kuamka. Jua tayari lilishaanza kuchomoza na kufanya mwanga upenye ndani ya nyumba.
Nikatoka kitandani na kuelekea sebuleni kwa lengo la kufanya shughuli ya usafi wa nyumba. Nilipofika sebuleni sikumkuta mama yangu kama nilivyokuwa nimezoea. Nikatoka hadi nje lakini nako nilimkosa. Nikaelekeaa chumbani kwake. Nikakuta bado mlango umefungwa kwa ndani. Nikagonga takribani dakika kumi ndipo nikasikia sauti yake.
Amani ikanirejea kwani nilishaanza kukata tamaa na kuamini uhai umeshamuondokea. Mama yangu alikuwa ni mtu mchangamfu sana lakini siku hiyo ilikuwa tofauti kabisa. Kila alipokuwa akiniangalia alidondosha machozi”.
"Mwanangu Steven. Katika mbio za kutafuta mafanikio ambayo kwa wote hatujui ni lini tutafafanikiwa, usiogope kuanguka. Wapo walioanguka zaidi ya mara kumi lakini leo hii ukiwaangalia kimafanikio wako imara vilivyo. Hii ni kwasababu waliinuka kila walipoanguka. Macho yao hayakufumbwa ili kuwapa utata wa hatua inayofuata. Uimara wao katika kufikiria uliwapatia mwanga wa yale waliyoyafanikisha." Maneno hayo aliyaongea mama yangu huku akiinuka.
Ni pale tulipomaliza kula chakula cha mchana siku ambayo jana yake nilimtamkia masuala ya kufungua duka. Alichokuwa akikilenga ni mimi kurudi shuleni. Hayo yalikuwa ni maneno ya mwisho kutoka kwa mama yangu. Maneno yenye kunitia faraja pamoja na kunifungua upeo wangu kifikra.
Tangu siku hiyo mama yangu alikuwa ni mtu wa kuniangalia tu na kuishia kutikisa kichwa chake kuonyesha kunisikitikia. Kilichokuwa kikipatia nguvu ya kutimiza azma yangu ni kwamba ile pesa tuliyopewa na ile kampuni ya uchimbaji, iliingizwa benki ambapo jina liliandikwa la kwangu. Nilikuwa na uhuru wa kuichukua nitakavyo. Ilikuwa ni shilingi milioni ishirini na tano.
Nilichokifanya ni kumueleza mama yake Sung'wa mpango wangu huo. Akaukubali na kuniambia nitashirikiana na Sung'wa lakini iwe siri yetu.
Kosa nililolifanya ni kukubali ushauri wa kwamba nifungue maduka mawili. Moja asimamie Sung'wa ili hata kama moja litatetereka, lingine liliinue.
Nikachukua kiasi cha shilingi milioni kumi na tano. Nikakigawa kati na kufungua maduka mawili yote ya bidhaa za aina moja lakini sehemu tofautitofauti.
Sikuwahi kuendesha mtaji hata wa shilingi laki moja nikajua faida na hasara. Je milioni saba na nusu nitatatambua faida na hasara? Mahesabu hewa niliyafanya. Mama yangu hakujua hilo. Miezi miwili tangu nifungue duka, nilianzisha tabia ya ulevi.
Nakiri tabia hii alinifundisha Sung'wa. Kuna siku hatukuwa tukirudi nyumbani kabisa. Ulevi ulipitiliza. Fedha hizo za ulevi zilitoka dukani.
Tabia ile ilipokomaa kiasi fulani, mama yangu ikaanza kumuumiza. Mbali na ushauri wake sikumsikiliza. Nyakati hizo ushauri nilikuwa nikiufuata wa mama yake Sung'wa.
Nakumbuka siku moja tulilewa kuliko maelezo. Sikurudi nyumbani kwetu, bali nilielekea nyumbani kwao na Sung'wa. Tulivyofika tu nikajitupa kwenye sofa na usingizi ukanipitia. Nilishtuliwa na sauti za mtu akilia kilio chenye kuashiria anafanya mapenzi.
Huwezi amini nilipofungua macho nilikutana na mama yake Sung'wa akiwa kifuani kwangu. Yuko uchi na mimi uchi. Pombe ilikata ghafla. Nikamsukumia pembeni lakini haikuwa imeondoa kile alichokuwa amekidhamiria.
Nasema hivyo kwasababu hakuwa amelewa kama mimi. Nikajiuliza ni nani alinibeba kunitoa sebuleni? Sikupata jibu ndugu msomaji wa mkasa huu. Wakati nikitafakari na machozi yakinidondoka, yeye alikuwa pembeni akiniangalia kwa macho yaliyojaa huba. Akadirika mpaka kuniita mpenzi. Sikumuongelesha chochote, nikainuka na kuvaa nguo zangu ili Sung'wa asijue kitendo kile.
Kufungua tu mlango ili nitoke, nikakutana uso kwa uso na Sung'wa. Nilichokishuhudia ni yeye kuanguka chini kama mzigo. Naamini kilichomfanya azimie ni kuniona natoka chumbani kwa mama yake huku nikifunga mkanda wa suruali yangu.
Sikumgusa, nikatoka na kurudi nyumbani. Nikafungua mlango kwa ufunguo wangu wa ziada. Nilipotizama saa yetu ya ukutani mshale ulielekeza saa kumi za usiku. Nikakaa pale sebuleni kwenye sofa nikiwa na mawazo lukuki. Sikukaa sana, mama yangu akatoka chumbani kwake na kusogea karibu yangu.
"Mara zote ukichezea nafasi zenye urahisi, jiandae kupambana na nafasi zenye utata." Maneno hayo aliyaongea mama yangu huku machozi yakimtiririka mashavuni mwake.
Alikuwa akiongea maneno ambayo yalianza kuonekana wazo. Hakunipatia nafasi ya kuongea, akarudi chumbani kwake. Akaniacha nikimuwaza Sung'wa niliyemuacha katika hali ya kupoteza fahamu. Sikujua kama amekufa ama lah!
Palipambazuka nikiwa palepale sebuleni. Nikamuandalia chai mama ndipo nikaelekea dukani kwangu. Inahitaji moyo kusimulia. Duka langu halikuwa na chochote kilichobakishwa na wezi. Lilikuwa limevunjwa.
Ilinibidi nikae chini huku machozi yakiwa fariji langu. Pole nilipokea nyingi kutoka kwa waliofika eneo lile lakini hazikusaidia chochote. Tegemezi langu lilibaki kwenye duka nililomfungulia Sung'wa ambaye nilimuacha amezimia nyumbani kwao.
Nguvu za kuendelea kubaki eneo lile sikuwa nazo tena. Nikawaachia polisi waifanye kazi yao ya upelelezi. Nilichokiona kinafaa ni kunywa pombe ili kuona kama nitapunguza mawazo. Nikaelekea baa ambayo mara nyingi ilikuwa na utulivu sana. Nilipofika nikaagiza bia ya safari. Nikaanza kuibwia moja moja hadi nilipokuwa chakari. Niliingia baa saa nne nikatoka saa kumi na mbili za jioni. Ni pombe tu hata chakula sikukigusa.
Nikarudi nyumbani hali yangu ikiwa si nzuri kabisa. Nilimkuta mama yangu sebuleni akiwa ameketi lakini macho yake yakionyesha wazi machozi. Machozi yenye kuashiria uchungu ndani ya nafsi yake kutokana na tabia yangu tangu kuachana na shule.
Sikumsalimia. Nikapitiliza hadi chumbani kwangu na kujibwaga kitandani. Sikujua kilichoendelea hadi niliposhtuliwa na sauti ya mama yangu akilia. Haraka nikainuka kitandani ambako nilimkuta mama yangu sebuleni akijilia sana. Masikini kumbe tangu chai niliyompatia asubuhi hakuwa amekula chochote hadi muda ule ambao saa ilisomeka saa tatu za usiku. Alikuwa akitetemeka mwili mzima. Nikajutia kitendo changu kile kilichomuweka mama yangu katika hali ile ya kutaabika.
Hakuwa akiongea zaidi ya kuangalia tu chini na kilio kikizidi kuwa kikubwa. Nikaingia jikoni na kuandaa uji ili kunyoosha utumbo wake.
"Mwanangu kamwe usiruhusu mawazo yako yakimbilie hatua ya kumi ilihali hata hatua moja hujaitimiza. Utavunjika kifikra kabla ya kufikia lile unalolikimbilia.
Hapo mwanangu utakata tamaa na huenda ukawa mwisho wako kupambana na mengi yakutatizayo katika mwanya wa kuyatafuta maisha yenye kufurahisha." Maneno ya mama yangu yalinisababisha nitoe machozi.
Ni maneno ambayo aliyaongea alipotuliza njaa yake. Tangu niwe na uwezo wa kutambua uzito wa ayasemayo mama yangu, sikuwahi kusikia maneno kutoka kwake yasiyokuwa na mafumbo ndani yake. Hakupenda kuniweka wazi. Alinijenga kimafumbo hivyo siwezi kumsahau kwa hilo.
Hadi nakusimulia hilo, sikuwa nimepata taarifa za kule kwao na Sung'wa. Nafsi yangu bado ilikuwa kwenye mashaka sana juu ya utatuzi wa kile kilichotokea usiku wa jana yake. Sikuhitaji kumshirikisha mama yangu. Nilitaka iwe siri yangu. Siku hiyo ikapita kwa namna ya machungu.
*******
Kesho yake nilichelewa sana kuamka. Mama yangu ndiye aliyeniamsha. Kama ilivyokuwa kawaida yangu kila asubuhi, nikaandaa chai na kuiweka mezani. Nilipokamilisha hilo, nikaingia bafuni kuoga. Lengo langu kuu ndani ya mawazo yangu lilikuwa ni kupata taarifa za kinachoendelea kwao na Sung'wa. Mbali na yote nilikuwa na uoga wa kwenda huko.
Nilichokifanya baada ya kuoga na kuvaa nguo zangu, nikatoka na kuelekea kwa rafiki yangu Shiwa. Nikamuomba aelekee huko ili ajue kinachoendelea. Akaondoka na kuniacha kwake ambapo alikuwa amepanga chumba chake. Hakuwa ameoa. Kwa muda wa nusu saa akarudi na kunipatia taarifa zilizonishtua.
"Nimefika pale lakini nikaambiwa na mlinzi niliyemkuta getini kwamba nyumba imeuzwa walioinunua walikuwa wanahamia rasmi mchana wa leo." Aliongea Shiwa pasipo kupepesa macho.
“Inamaana nyumba ilishauzwa siku nyingi au?
Mbona imekuwa ghafla?
Nini chanzo cha kuuzwa kwa nyumba hiyo?
Mbona Sung'wa hakuwahi kunipatia taarifa hizo na ni mtu ambaye langu analijua na inatakiwa lake aniweke wazi?”.Ni maswali niliyojiuliza mfululizo pasipo na majibu.
Kilichoniumiza kichwa ni kwamba matukio ya jana yake yalikuwa makubwa na ikawaje wahame haraka kiasi hicho?
"Mwanangu mama yake Sung'wa ametawaliwa na tamaa." Hiyo ni kauli aliyowahi kuniambia mama yangu. Siku hiyo ilijidhihirisha rasmi.
Hata muda wa kumuaga Shiwa niliukosa kutokana na mchecheto nilioupata. Nikatoka mbio hadi nilipokuwa nimemfungulia duka Sung'wa. Nilipofika nilishindwa kuhimili. Nikajikuta natua chini kama mzigo huku jasho likinichuruzika kwa kasi.
Kila sehemu ya mwili wangu ilitoa jasho na kuufanya mwili wangu kulowa mithili ya mtu aliyejitupa baharini na nguo zake bila kuvua.
Duka lilikuwa linamalizikia kuungua moto. Sikuwa na uhakika lakini nilipounganisha matukio pamoja na kauli ya mama yangu, niliamini kuna mchezo ulichezwa na mama yake Sung'wa ili kuyaangamiza mafanikio yangu.
Kibaya zaidi sikuwa na kielelezo cha kuwatia hatiani juu ya duka lile. Lakini hata ningekuwa na vielelezo ningeanzia wapi kuwatia hatiani ilihali wote wako pale wanalia kuashiria maumivu ya tukio lile? Vilevile kuna baadhi ya vitu ambavyo thamani yake haikuwa ikizidi laki tano vilikuwa vimeokolewa. Kama ni mchezo, ulichezwa kwa ustadi wa hali ya juu.
Ukilinganisha na upumbavu wangu kufungua duka na kumkabidhi Sung'wa bila kuwa na vielelezo vya umiliki, basi hali yangu ikawa ngumu sana kimawazo. Kila mtu aliamini duka lile ni mali ya Sung'wa pamoja na mama yake.
Nilipandwa na hasira sana kila niliposika pole wakipewa wao badala ya mimi mwenye mali. Nikaanza kumchukia Sung'wa kwa moyo wangu wote.
Nilitamani nimrukie na kumrarua mwili wake wote lakini isingekuwa busara hata kidogo. Nilichokifikiria kwa haraka ni kwamba ningejiweka kwenye matatizo zaidi. Ilihitajika niwe mtulivu ili niweze kupata maelezo kutoka kwa Sung'wa. Nikajikakamua kuinuka pale chini.
Nikazipiga hatua za kivivu hadi walipokuwa Sung'wa na mama yake. Lakini kabla sijafungua kinywa changu kuzungumza, Sung'wa akaniwahi na kuniuliza swali bila uoga mbele ya umati ule wa watu na kuwafanya watu waduwae. Unaweza kujiuliza ni kwanini waliduwaa lakini jibu ni kwamba aliuliza swali tofauti na kitu kilichokuwa kimewakusanya watu eneo lile.
"Unatambua maumivu ya usaliti?"Nilibaki kumuangalia tu bila kuongea lolote.
Kwa muda ule masuala yaliyotokea nyumbani kwao tena nikiwa katika hali ya ulevi sikuwa na habari nayo akilini. Nilichokuwa nakiwaza ni jinsi maduka yangu yalivyoniondokea ghafla pamoja na wao kuuza nyumba yao kimyakimya na kuhamia sehemu nisiyoifahamu.
"Kilio na kicheko ni vitu ambavyo havikwepeki siku zote za uhai wa mwanadamu japo hujitokeza kwa nyakati tofauti na katika mazingira tofauti." Nilimwambia Sung'wa ambaye muda wote huo alikuwa akionyesha hasira za wazi usoni mwake.
Nilishindwa kuchanganua muonekano wake kwamba anahusika katika mipango ya kuniangamiza kimaendeleo ama lah! Mama yake alikuwa akizidi kulia kwa uchungu huku akigalagala chini kudhihirisha uchungu ndani ya nafsi yake kutokana na kile kilichotokea.
Wakati nazidi kumstaajabu mama yake Sung'wa kwa jinsi alivyokuwa akigalagala kwenye mavumbi, nikashuhudia mama yangu akija eneo lile kwa kujisukuma kwenye baiskeli yoke ya walemavu wa miguu.
Mshtuko nilioupata ulisababisha nipoteze fahamu. Yote hii ni kuona siri niliyomficha muda mrefu hatimaye imefichuka.
Niliporejewa na fahamu zangu nilikuwa nyumbani sebuleni juu ya mkeka huku mama yangu akiwa pembeni yangu akilia. Ni ajabu kidogo lakini ndo ukweli wenyewe kwamba mtu akipoteza fahamu haraka hukimbizwa hospitali lakini mimi nilijikuta nyumbani. Nadhani mama aliamuru hivyo.
"Upelekapo mambo yako kasi pasipo kufikiria matokeo yake, andaa mapokezi ya maumivu ya ufinyu wa fikra zako." Ni maneno aliyoyatamka mama yangu pale nilipofumbua macho yangu.
Hata pole hakunipatia. Hakuniweka wazi kama alitambua kilichotokea. Nakiri mama yangu alikuwa mwingi wa mafumbo lakini kwa mwenye fikra za ufumbuzi alistahili pongezi. Alikuwa kwenye maumivu ya kuhangaikia kisicho na faida.
Maneno yake niliyasikia na yalinichoma vilivyo lakini sikuyapatia mwanya hata kidogo. Kilichokuwa akilini ni jinsi gani nitayaanza maisha upya baada ya kutetereka ghafla. Vilevile kumpata Sung'wa ili niweze kuongea naye kwa kina niweze kuhakikisha kama hawahusiki na lolote. Lakini nitampata wapi? Ni swali nililojiuliza mwenyewe pasipo kupata jibu.
"Naomba unisamehe mama. Lakini kumbuka kamba ya mbuzi haikosi fundo. Naamini hayo nd'o maisha yangu kwa sasa." Ni kama niliongea mwenyewe au aliyasikia lakini aliyapuuza kwa kuondoka mahali pale na kuelekea chumbani kwake.
Mwili wangu ulikuwa sawa. Sikuwa na uchovu wowote. Nikainuka na moja kwa moja nikaingia bafuni na kuoga. Yote hayo yakitendeka ilikuwa ni majira usiku. Nilipotoka bafuni ikawa ni wasaa mzuri kujibwaga kitandani.
Kesho yake nilihakikisha namuachia mazingira mazuri mama yangu ndipo nikatoka na kuingia mtaani ili kuona kama nitampata Sung'wa. Nikaelekea lilipokuwa duka. Nikawakuta mafundi wakijenga upya na wakati huo mmiliki alikuwa pale. Lakini maelezo aliyonipatia yalizidi kunichanganya zaidi.
"Hawa watu nasikia wameelekea Mwanza kuanza maisha mengine baada ya hii hasara waliyoipata."
Mwili mzima ulinilegea. Laiti ningekuwa nafahamu eneo waliloelekea, ningepanda gari siku hiyohiyo. Lakini hata kuikanyaga ardhi ya jiji hilo sikuwa nimewahi.
Kama nilivyofanya kwa Shiwa ndivyo nilivyofanya kwa mama yule. Niliondoka bila kuaga. Nikarudi nyumbani mawazo yakiwa lukuki kichwani mwangu.
Msaada wangu nilibaki nao ni ile milioni kumi liyokuwa imebaki benki. Kwakuwa tayari nilikuwa na uzoefu kiasi fulani katika biashara, sikuona sababu ya kuchelewa kufungua duka lingine.
Sikutaka kufanya ujinga kama ulioniteteresha mara ya kwanza. Nikafungua duka kubwa la takribani milioni nane pale nyumbani. Pamoja na ukarabati wa chumba nilicholiweka hilo duka, milioni tisa na nusu ikatimia. Benki nikabakiza shilingi laki tano pekee kama ulinzi wa akaunti yangu.
Maisha ya furaha yakadumu kwa miezi miwili tu na mwezi uliofuata kilio kikaibuka.
Zilikuwa zimepita siku nne tangu niingize mzigo mpya dukani kwangu. Nakumbuka siku hiyo niliuza hadi nikashangaa sana. Ndiyo maana msomaji wangu hapo kabla nilikwambia kicheko na kilio ni vitu ambavyo havikwepeki.
Ni dakika moja utacheka na dakika itakayofuata unaweza kulia pasipo kikomo. Majira ya usiku tukiwa tumelala, nilishtuliwa na vishindo vya watu nje. Niliinuka kitandani na kunyata hadi dirishani ambako niliangalia nje kupitia kioo. Siku hiyo msomaji wangu nilipoteza jicho langu la upande wa kulia. Kioo cha dirisha kilikuwa kinamruhusu aliye ndani kuona nje lakini wa nje haoni.
Nilijilaumu kusogea pale dirishani kwani kitu chenye ncha kali kilipasua kioo na moja kwa moja kikatua jichoni kwangu. Nilichoshuhudia ni damu iliyochanganyikana na maji kuanza kunichuruzika.
Kilichofuata ni mimi kuanza kupambana na maumivu ya jicho nikiwa najigalagaza sakafuni. Muda mfupi tangu nichomwe jicho, akaingia mwanaume mmoja mrefu aliyekuwa amefunika uso wake na hata mikono yake alikuwa ameivalisha gloves.
Hakuwa na muda wa maongezi marefu wala kuniongezea kipigo. Alichokihitaji ni kumuonyesha zilipokuwa fedha. Akili ilishaniruka hivyo sikufikiria mara mbili. Nikamuelekeza zilipo. Kwa madaha huku bastola yake ikiwa mkononi, akasogea nilipomuelekeza na kupekua. Akazichukua na kuziweka kwenye begi lake dogo alilokuwa nalo mgongoni kisha akaniachia pigo moja la teke ambalo liliniumiza mbavu zangu.
Hali ya ukimya ikatawala pindi mtu yule alipoondoka chumbani kwangu pamoja na fedha zangu ambazo hazikuwa chini ya shilingi milioni nne. Kiasi cha fedha ambacho ni cha kuweza kuniteteresha. Maumivu nikayaweka kando na kutembea kwa kupepesuka kuelekea chumbani kwa mama yangu kwani sikuwa na uhakika kama aliachwa salama.
Mlango wa chumba chake ulikuwa umefungwa. Nikagonga kwa muda ndipo nikasikia akijigeuza kitandani na kufuatiwa na sauti akiniuliza kuna nini hadi nimuamshe usiku ule. Nilistaajabu sana kwa kuona yote yaliyonitokea hajayasikia. Nilibaki nimeganda pale mlangoni bila kumwambia chochote kwani niliamini ningemuamshia presha.
Pamoja na kuhitaji kumficha ilishindikana kutokana na kwamba aliamka na kunikuta nikiwa nimesimama mlangoni huku nikiwa nimeshikilia jicho langu lililokuwa likiendelea kuchuruzika damu pamoja na majimaji. Hata yeye alistaajabu nilipomueleza kilichotokea.
Tulikaa sebuleni hadi pakapambazuka ambapo nilielekea polisi kutoa taarifa ya kilichotokea. Nikapokea PF3 kisha nikaruhisiwa kufika hospitali kwa ajili ya matibabu.
****
"Usiwasahau wale wote waliochangia mafanikio yako kwa namna yoyote ile."
****
Hazikupita dakika kumi tangu dokta amalize kunisafisha jicho langu na kunifunga bandeji. Wakaingia maaskari watatu wakiwa wameongozana na mwanamke mmoja mfupi. Alichoniambia mwanamke yule kilizidi kunichanganya akili. Eti nina mzigo wa wizi ndani ya duka langu. Nilikuwa najiamini kwa asilimia miamoja ya kuwa asemacho si cha kweli lakini tulipofika nyumbani, nilijikuta nakaa chini na kulia kwa kupaza sauti juu kutokana na maumivu niliyoyapata ndani ya nafsi yangu. Nikaamini maisha hayana kikokotozi ya kwamba ukibonyeza mbili mara mbili jibu utapatiwa sahihi.
"Katika safari ya kutafuta mafanikio ya maisha kuwa sawa na mtu anayetembea katika njia iliyojaa utelezi. Hakika hatapiga hatua kumi pasipo kuteleza. Lakini atelezapo atajiweka sawa na kuendelea na safari yake."
Nilihisi mikosi inaniandama kwa fujo. Baada ya maelezo yale, walinichukua hadi nyumbani na kunionyesha ”SeachWarrant”. Kilichonifanya nichoke zaidi kutoka kwa yule mwanamke ni kutaja alama alizoziweka kwenye bidhaa zake kabla ya kuanza kupekua.
Maaskari wakamruhusu kuanza kutafuta bidhaa zake. Ndiyo maana watu huwa wanajinyonga. Si bure msomaji wangu. Ni zaidi ya nusu aliyopekua na kukutana na alama alizozitaja. Mpaka vocha zilikuwa na alama hiyo. Mama yangu alilia sana pale nilipowekewa pingu na kuitwa muhalifu.
Nilikuwa na risiti mahali nilipochukulia mzigo lakini tulipofika huko risiti ilikuwa feki. Yani haikuwa ikifanana na zile walizokuwa wakipewa wateja tuliowakuta wakichukua mzigo. Sikuwa tayari kupelekwa kituoni kwani ningefungwa jela kutokana na kwamba ushahidi wa mali zile ulikuwa ukijidhihirisha wazi.
Nilichoomba ni wachukue mizigo lakini waniachie huru. Nashukuru yule mama hakutaka yafike mahakamani. Mama yangu pia naye alikuwa tayari kutoa hata nyumba yetu mradi nisiende jela. Yote hii kama unakumbuka mama yangu alikuwa ni mtu anayeogopa masuala ya kituoni.
Mimi sikuwa naogopa sana lakini kama ningefikishwa huko, pesa ya kunipambania sikuwa nayo. Hivyo mwisho ningeishia jela na huenda ningetakiwa kumlipa fedha yule mama kutokana na kumpotezea muda wake.
Gari aina ya fuso ikaletwa na kupakia mzigo wote ndani ya duka langu na kuacha shelfu peke yake. Huku jicho linauma, huku maumivu ndani ya nafsi yakinitafuna. Kumbe kuporomoka kwenye maisha ni ndani ya dakika moja unasahahulika kwenye ramani ya wenye mafanikio.
Nilikuwa kwenye wakati mgumu sana. Hata kukaa karibu na mama yangu sikutaka kwani alikuwa ameanza kukonda kutokana na kulia kila wakati na kuonyesha kunisikitikia. Hakika kauli zake zilikuwa zikifanya kazi. Yale aliyokuwa akinifumba yalikuwa yakijifumbua yenyewe pasipo uziada wa akili yangu. Nilitakiwa kupambana na utata wa maisha yaliyojaa umasikini.
***
Mwezi mmoja tangu niingie rasmi katika maisha ya kulima vibarua ili kumsaidia mama yangu ambaye kila ilipoitwa siku mpya hali yake ilikuwa ikizorota, alitokewa na kipele kwenye goti lake. Kilikuwa kidogo lakini kadri siku zilivyoenda kilikuwa kikiongezeka ukubwa huku kikimsababishia homa ya mara kwa mara.
Katika kuhangaika kutafuta tiba ni sehemu nyingi tulizipitia hasa za waganga wa kienyeji lakini haikusaidia. Hospitali pia tulizizunguka hasa zile ambazo gharama zake ni za chini kutokana na kwamba hospitali za bei ghali nisingeweza kumudu gharama. Tiba yake ingegharimu shilingi milioni moja na nusu ambapo mguu wake ulitakiwa kukatwa.
Pesa sikuwa nayo hivyo sikutaka daktari aliyeniambia hivyo afikishe taarifa hizo kwa mama yangu. Nilimshauri mama yangu tuuze nyumba ili tupate fedha za matibabu lakini alinikatalia katakata.
Nilijiona mkosaji mbele ya mama yangu kwani endapo ningekuwa msikivu na mnyumbulifu wa kauli zake, nisingeweza kushindwa kumpeleka katika hospitali ambazo zingeweza kumpatia huduma stahiki. Mama yangu kila aliponitazama alikuwa akisikitika huku machozi yakimtoka.
Kile kipele kikajenga usaha na pindi tulipokikamua kikaanza kujichimba chenyewe na kutengeneza shimo. Huruma ilizidi kunitanda kwasababu afya ya mama yangu ilikuwa ikitisha. Hakuwa tofauti na jani la mgomba lililokaushwa na jua kwa mwezi mzima. Kila siku nguvu zake zilikuwa zikimuisha na hata mikono yake ilikuwa ikitetemeka kwa kila alichokishika.
Nikabeba jukumu la kufanya baadhi ya vitu ambavyo alitakiwa kuvifanya yeye.
Siku moja majira ya mchana, tukiwa tumekaa sebuleni namlisha chakula, nilishangaa akikohoa kwa nguvu na kusababisha kile chakula kilichokuwa mdomoni kunirukia. Alizidi kukohoa na kilichonishangaza zaidi ni hali ya macho yake kuanza kubadilika na kuwa meupe. Mikono yake ikakakamaa mithili ya ukuni mkavu. Mdomo wake pia ukawa unatetemeka hali iliyozidi kunitia hofu nafsini mwangu.
Sikuwahi kushuhudia hali ya namna hiyo kwa mtu yeyote. Labda kwakuwa sikukulia katika mazingira ya familia kubwa au kwakuwa sikuwahi kuwa hospitalini hata kwa mwezi mmoja na kuona huwa inakuaje pindi roho ya mtu ikitaka kutengana na mwili wake.
Mbali na hayo mawazo yangu nikakumbuka ya kuwa kila mwanadamu amepangiwa aina ya kifo chake. Huyu atahangaika kabla ya kifo chake na yule atatulia pasipo purukushani yoyote. Baada ya muda kama wa dakika tatu, mama yangu alinyoosha mkono wake na kuuweka begani kwangu kisha akaniambia;
"Mwanangu kauli njema katika jamii nd'o mwanga wa maisha yenye usaidizi uwapo kwenye tabu. Moyo wako ujaze usikivu, unyenyekevu pamoja na upole." Huo ulikuwa mwisho wa kuyasikia maneno kutoka kinywani mwa mama yangu.
Mkono aliuweka mwenyewe lakini niliutoa mimi. Mama yangu aliondokewa na uhai mkono ukiwa begani kwangu.
Nililia mno na kuona mimi ndiye chanzo kifo cha mama yangu. Kama nisingekuwa mwingi wa pupa ningeweza kumpeleka hospitali yoyote ili akatibiwe. Nilichokitamka huku naondoa mkono wake begani kwangu ni “NISAMEHE MAMA.”
Siku mbili mbele, mazishi ya mama yangu yakafanyika na hatimaye nikabaki mpweke katika ulimwengu. Hakuwepo tena wa kunijenga kifikra. Lakini yote niliyataka mwenyewe. Sikuhitaji tena ushauri wa mtu yeyote. Katika nilichokifikiria. Nikamtafuta mteja na kuuza ile nyumba lakini kwa sharti la kutosawazisha kaburi la mama yangu. Nilipewa fedha ya kutosha takribani milioni thelathini. Nikalijengea vizuri kaburi lake.
Sikutaka kurudia kosa lililosababisha kumkosa mama yangu. Nikaweka benki shilingi milioni ishirini na tatu na kiasi kilichobaki nikaamua kuanzisha biashara ya nguo za mitumba katika jiji la Mwanza. Mwanzo ulikuwa mgumu lakini kauli zangu kuongeoa na wenyeji niliowakuta zilinifanya kuona ni hali ya kawaida.
Ni mwaka mmoja tu niliodumu katika biashara ile nikawa maarufu na hii ni kwasababu mtaji wangu ulikuwa mkubwa. Nikapata rafiki ambaye naye mtaji wake haukutofautiana sana na wa kwangu. Huyu ni Amiri.
Urafiki wetu ukakua na hatimaye tukawa tukienda wote NAIROBI kuchukua marobota ya nguo pamoja na viatu. Nikasahau unyama walionifanyia Sung'wa pamoja na mama yake. Mwaka uliofuata rafiki yangu akanishauri tununue kiwanja kila mtu cha kwake.
Hakika alikuwa rafiki mpenda maendeleo japo hadi wakati huo hakuwa anatambua kama benki ninamiliki fedha nyingine tofauti na ile iliyo katika mzunguko wa biashara. Wazo lake tukalitimiza na kila mmoja akamiliki kiwanja chake binafsi huku biashara yetu ikizidi kutuingizia kipato kikubwa. Maisha ni hatua na sisi tulianza kupiga hatua. Tukaanza kujenga ili kuachana na maisha ya kupangisha.
*****
"Uzuri au ubaya wa maisha yako hutokana na fikra zako uzipangiliavyo."
*****
Kwakuwa fedha haikuwa ya kubahatisha, nyumba zetu hazikuchukua muda zikakamilika ujenzi wake. Nikatamani mama yangu angekuwepo ili niyafute machozi yake niliyoyasababisha mimi kwa ufinyu wangu kiupambanuzi, lakini isingewezekana tena kuiona sura yake katika ulimwengu huu.
Miaka miwili tangu tuachane na maisha ya kupanga kwa kuhamia katika nyumba zetu binafsi, niliamua kununua gari langu dogo aina ya NOAH kwa ajili ya safari zangu ndogondogo na hata nikielekea kanisani siku ya jumapili.
Maisha yangu yakabadilika ghafla na kuonekana kijana mdogo lakini fedha si tatizo hata kidogo. Hakuna aliyeijua historia yangu kabla ya kuhamia jijini MWANZA. Laiti wangejua nadhani wangeniona wa tofauti sana.
Hiyo ilibaki kuwa siri yangu. Vilevile hakuna aliyethubutu kuniuliza kuhusu jicho langu bovu. Maisha yakazidi kusonga mbele na hisia za kuoa zikaanza kunitawala. Nikahitaji kuwa na mke halali wa ndoa lakini kila nilipomkumbuka Sung'wa, moyo wangu ulijawa na hofu fulani.
Si kwamba sikuwa nikifanya mapenzi. La hasha! Nilifanya lakini hakuna mwanamke niliyefanya naye mapenzi nyumbani kwangu. Sikuona sababu ya kujenga mazoea ya namna hiyo kwani wote hao hawakuwa kwenye mawazo yangu.
Katika maisha yangu nilijijengea msemo katika ufahamu wangu kwamba kila mbaya ana mbaya wake. Huu msemo siku moja majira ya mchana nikiwa nimesimama katika taa za barabarani kabla ya kuruhusiwa kuendelea na safari yangu ya kuelekea uwanja wa ndege, ulifanya kazi yake kikamilifu.
Ni pale taa ziliporuhusu foleni niliyokuwepo mimi ipite ndipo kioo cha gari langu kiligongwa kwa nguvu. Endapo angegonga taratibu ningepuuzia. Lakini ugongaji wake uliniamsha hasira na kunifanya nikishushe kwa kasi nikiwa na nia ya kumtolea kauli mbaya.
Nilipigwa na butwaa nilipoishuhudia sura ya mwanadada Sung'wa. Ikiwa imechakaa vilivyo. Mwili wake haukuwa wa kuvutia tena. Bali umedhoofu vilivyo. Hasira zangu juu yake zikaniyeyuka ghafla kutokana na hali niliyomkuta nayo.
Yeye pia alikumbwa na mshtuko uliosababisha sinia lake la karanga za kuchemsha, kuanguka chini. Nilizidi kutahamaki pasipo kukumbuka niko kwenye foleni na yapo magari yanahitaji kupita.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment