Search This Blog

Sunday, July 10, 2022

NOTHING WITHOUT YOU (SI KITU BILA WEWE) - 2

 





    Simulizi : Nothing Without You (Si Kitu Bila Wewe)

    Sehemu Ya Pili (2)





    Ilipoishia





    Taarifa ile ilionekana kumchanganya kupita kiasi.

    Moyo wake uliamini kwamba kitu chochote ambacho kingefanyika ndani ya jiji la Dar es Salaam basi kilikuwa na uwezo mkubwa sana kusikika Tanzania nzima kutokana na kuwa na vyombo vingi vya habari. Alitamani ajitangaze ili Tanzania nzima kumfahamu yeye ni nani na alikuwa na malengo gani katika maisha yake. Muda wote alijisikia kuruka ruka kwa furaha, safari ya kwenda Dar es Saaam ilionekana kumchanganya kupita kiasi.

    “Safari yenyewe inaanza lini?”

    “Kesho kutwa” Bi Stumai alimwambia.





    Songa nayo sasa..







    Bado Bi Anna alikuwa akiifikiria safari ya kuelekea Dar es Salaam. Kila siku alikuwa akiiota safari hiyo ambayo kwake ilionekana kuwa kama tukio kubwa ambalo lilikuwa linakwenda kutokea. Vijana wengi ambao walikuwa wamefika Dar es Salaam na kurudi kule kijijini walikuwa wakielezea uzuri wa Dar es Salaam pasipo kuzungumzia mambo mengine machafu ambayo yalikuwa yamekithiri.

    Kila mtu akaonekana kutaka kuhakikisha kwa macho yake kile ambacho alikuwa akiambiwa lakini tatizo lilikuwa ni kutokupata fedha za kwenda Dar es Salaam na kuliona kwa macho yao jiji hilo ambalo lilionekana kuwa na mambo mengi.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Masaa aliyaona yakikawia, kichwa chake kilikuwa kikiendelea kufikiria safari hiyo ambayo bado ilikuwa ikiendelea kukaa kichwani mwake. Bi Anna bado alionekana kuwa na hamu ya kuwa pamoja na familia yake kwani aliamini kama tu angekuwa na hata mtoto wake Patrick pamoja nae, basi nae angekuwa na nafasi kubwa ya kuelekea Dar es Salaam kusafisha macho.

    Siku moja kabla ya safari, Bi Anna hakulala usiku, kichwa chake kilikuwa kikiifikiria safari hiyo ambayo kwake ilionekana kuwa kama muujiza mkubwa. Kila wakati ambao alikuwa akpata usingizi kidogo, alikuwa akishtuka na kuangalia nje kuona kama kumepambazuka.

    Masaa yaliendelea kukatika huku mabegi yake yakiwa tayari kwa ajili ya safari. Alamu ya simu yake ikaanza kusikika, akaamka na kuanza kujiandaa. Wala hazikupita dakika hata tano, wanawake wanne wakaingia ndani ya nyumba hiyo na baada ya muda wakaanza kumsindikiza katika kituo cha mabasi ambapo akapanda basi na saa kumi na mbili kamili basi kuanza safari ya kuelekea Dar es Salaam.

    Bi Magdalena alibaki akiangalia dirishani huku kumbukumbu zake zikimrudisha nyuuma kabisa katika kipindi ambacho alikuwa pamoja na familia yake. Alimkumbuka sana marehemu mumewe ambaye aliuawa baada ya kuhisiwa kuwa ni mchawi, kumbukumbu zake hazikuishia hapo, alimkumbuka na mtoto wake, Patrick huku akionekana kutokuwa na uhakika kama alikuwa hai au nae alikuwa ameuawa siku ile.

    Basi liliingia katika kituo cha Ubungo Terminal saa moja usiku, Bi Anna akateremka na kuanza kupiga hatua kuwafuata wanawake wawili ambao walikuwa wamesimama huku wakionekana kumwangalia katika mtazamo wa kutaka kumuuliza kitu.

    “Bila shaka wewe ndiye Bi Anna” Mwanamke mmoja alimwambia Bi Anna huku uso wake ukiwa umejaa tabasamu.

    “Ni mimi” Bi Anna alijibu.

    Hakukuwa na sababu ya kupoteza muda kituoni hapo, kitu walichokifanya ni kukodisha teksi na moja kwa moja kuanza safari ya kuelekea hotelini. Ndani ya dakika thelathini wakawa wamekwishafika katika hoteli ya La Vista Inn ambako moja kwa moja wakaelekea ndani ambako walikuwa wamechukua chumba kimoja.

    Bi Anna alibaki akikiangalia chumba kile mara mbili mbili. Televisheni kubwa ilikuwa imewekwa ukutani, taa mbalimbali zilizokuwa na mianga tofauti zilikuwa zikiendelea kumulika katika chumba hicho. Bi Anna aliendelea kushangaa, kila kitu kwake kilionekana kama ndoto ambako baada ya muda fulani angeamka kutoka katika usingizi mzito.

    Muda wote Bi Anna aliuona mguu wake kukanyaga kitu cha tofauti ambacho hakuwa na ukakika kama alikwishawahi kukikanyaga toka azaliwe. Kapeti lililokuwa na manyoya lilikuwa limetandikwa katika sakafu ya chumba kile. Kila kitu ambacho alikuwa akikiangalia kilionekana kuwa kigeni machoni mwake.

    “Kesho utakuja kuchukuliwa na gari kupelekwa katika mkutano ambao utachukua siku tatu” Mwanamke mmoja alimwambia Bi Anna.

    “Saa ngapi?”

    “Saa tatu asubuhi”

    Wanawake wale wakaondoka chumbani mule na kumwacha Bi Anna peke yake. Muda wote alikuwa akikiangalia chumba kile. Dhahiri alijiona kuwa katika ulimwengu mwingine ambao ulikuwa ulimwengu wa maajabu. Akakifuata kitanda na kukalia, akazidi kujisikia utfauti.

    Kijijini Chibe alizoea kulalia kitanda cha kamba mpaka pale alipohamia Shinyanga mjini ambako kulikuwa na nyumba ambayo alipangiwa, huko ndipo ambapo alipoanza kulali kitanda ambacho kilikuwa na mvuto. Kitanda ambacho alikuwa amekikalia kwa wakati huo chumbani hapo kilionekaa kuwa tofauti na vitanda vyote ambavyo alikuwa amevilalia katika maisha yake kwani kitanda kile kilikuwa na mvuto wa juu ambao hakuwahi kuuona.

    “Mmmmh! Hadi saa tatu nitakuwa nimeamka kweli! Nisije nikachelewa” Bi Anna alijisemea.

    Bi Anna akajiandaa na kuelekea bafuni, mshangao wake ukaongezeka zaidi na zaidi. Akili yake ikahama kabisa na kujiona alikuwa katika ulimwengu mwingine wa tofauti kabisa. Sinki kubwa la kuogea lilikuwa likionekana vizuri machoni mwake.

    Akaanza kulisogelea na kulishika huku akionekana kuogopa kwa kuona kwamba angelichafua. Akafungua koki ya bomba na maji kuanza kutoka. Kia kitu ambacho alikiona katika usiku huo kilionekana kumshangaza kupita kiasi, bado alijiona kuwa mwanamke ambaye alikuwa na bahati kubwa katika maisha yake.

    Asubuhi ilipofika, Bi Anna akaamka na moja kwa moja kuletewa kifungua kinywa na baada ya kumaliza, akapelekwa katika ukumbi wa Diamond Jubilee kwa ajili ya mkutano wa wanawake wa kitaifa ambao ulikuwa ukifanyika mahali hapo.

    Wanawake zaidi ya mia saba walikuwa wamekusanyika katika ukumbi huo huku wakiendelea kupiga stori. Walikuwa wapo tayari kwa kuanza mkutano lakini Waziri wa wanawake na watoto, Bwana Hidifonce Mayemba hakuwa amefika mahali hapo.

    Zilipita dakika thelathini, gari moja la kifahari likaanza kuingia katika eneo la ukumbi ule ambapo wanawake wote wakaamriwa kutoka ukumbini na kwenda kumkaribisa waziri Mayemba. Vigeregere vilikuwa vikisikika kutoka kwa wakinamama hao katika kipindi ambacho Bwana Mayemba alikuwa akipiga hatua za taratibu kuelekea ukumbini huku akiwapungia mkono.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mkutano ukaanza rasmi huku baadhi ya waandishi wa habari wakiwa wamekusanyika mahali hapo kwa ajili ya kupiga picha na kuandika kila kilichokuwa kikiendelea mahali hapo. Mara baada ya Waziri kuelekea ukumbini, mkutano ukaanza mara moja.

    Kila mwanamke alikuwa akiongea kile kitu ambacho alikuwa amekiandika au kuandikiwa katika karatasi. Maneno mazito yalikuwa yakiongelewa mahali hapo, maneno ambayo yalikuwa yakimaanisha kwamba wanawake walikuwa wakitaka kupewa nafasi kubwa katika jamii.

    Waziri Mayemba alikuwa akiandika mambo mengi ambayo yalikuwa yakizungumziwa mahali hapo, hakutaka kupitwa na kitu chochote kile. Wanawake tisa walikuwa wameongea na ni Bi Anna tu ndiye ambaye alikuwa amebakia kwa ajili ya kuwawakirisha wanawake wote wa kanda ya ziwa.

    Bi Anna aliongelea mambo mengi ambayo yalionekana kumgusa kila mtu aliyekuwepo mahali hapo. Alionekana kuwa kama mwanamke ambaye alikuwa na elimu ya juu, kuanzia ngazi ya digrii. Maneno aliyoongea yalikuwa mazito ambayo mara kwa mara yaliwafanya watu waliokusanyika mahali hapo kutikisi vichwa vyao.

    “Tunahitaji kushirikishwa katika jamii kwa kila kitu, hatutaki kubaguliwa na kuonekana kama hatuna mchango wowote ule katika jamii. Tunataka tupewe haki sawasawa na wanaume hata kama wao walichangia kwa asilimia kubwa kututafutia uhuru” Bi Anna alimalizia na kuondoka kuelekea kitini kwake. Makofi mazito na vigeregere vilikuwa vikiendelea kusikika ukumbini hapo, Bi Anna alionekana kuongea maneno makali kwa jamii.

    Waziri Mayemba alibaki akishangaa, muda wote alikuwa akimwangalia Bi Anna huku akionekana kumsnagaa. Ni kweli alikuwa ameongea maneno mazito ambayo kila mtu aliyeyasikia ni lazima angemuona mwanamke huyo kuwa msomi lakini kuna kitu ambacho kilikuwa kikimfanya kumshangaa zaidi Bi Anna, uzuri wake.

    Ni kweli Bwana Mayemba alikuwa amewaona wanawake wengi lakini kwa Bi Anna alionekana kuwa tofauti kabisa. Uzuri wake ulionekana kumvutia kuliko kawaida, alimwangalia katika kila hatua ambayo alikuwa akitembea mpaka kitini kwake.

    Akabaki akiwa akimshangaa tu, macho yake yalikuwa yameganda usoni mwa Bi Anna ambaye hadi katika kipindi hicho, moyo wake ulikuwa umetekwa kupita kiasi. Mpaka Bwana Mayemba anakaribishwa mbele kwenda kufunga mkutano, hakuwa amesikia kabisa, bado macho yake yalikuwa yakimwangalia Bi Anna.

    “Mheshimiwa....” Mwendesha mwenyekiti alimuita kwa mara ya tatu.

    Bwana Mayemba akaonekana kushtushwa kutoka katika lindi la mawazo. Akasimama huku uso wake ukiwa na tabasamu pana. Wala hakutaka kuongea sana kwani bado alijiona kutaka nafasi zaidi ya kutaka kuongea na Bi Anna.

    Baada ya dakika kadhaa, mkutano ukafungwa na wanawake wote kwenda nje. Waandishi wa habari wakaanza kumfuata waziri Mayemba na kuanza kumhoji maswali kadhaa. Kila kitu alicholizwa, alikijibu haraka haraka, katika kipindi hicho alikuwa akitaka kuachiwa nafasi ili amfuate Bi Anna.

    “Nadhani nimemaliza” Bwana Mayemba aliwaambia waandishi wa habari na kisha kuanza kumfuata Bi Anna ambaye alikuwa amesimama pembeni.

    Kadri alivyokuwa akizidi kumsogelea Bi Anna na ndivyo ambavyo mapigo yake ya moyo yalivyozidi kumdunda zaidi na zaidi. Hakuonekana kujiamini kabisa, akaanza kuusikia mwili wake ukipigwa na kijibaridi cha mbali.

    “Habari za mchana” Bwana Mayemba alimsalimia Ni Anna huku akimwangalia usoni.

    “Nzuri tu. Karibu Mheshimiwa” Bi Anna alimwambia Bwana Mayemba.

    Bwana Mayemba hakutaka kutoa jibu la haraka haraka, akabaki akimwangalia Bi Anna kwa umakini. Uzuri wake ukaonekana kumvutia zaidi na zaidi. Akatamani kumwambia ukweli mahali hapo ili amkumbatie na kumbusu, alionekana kulitamani joto la mwanmke huyo ambaye alikuwa akionekana kuwa na kila aina ya mvuto machoni mwake.

    “Samahani kama nitakuwa nakusumbua” Mzee Mayemba alimwambia Bi Anna

    “Usijali Mheshimiwa”

    “Hivi una nafasi jioni ya leo?”Bwana Mayemba alimuuliza Bi Anna ambaye akaonekana kuanza kusikia aibu kutokana na macho ya Bwana Mayemba kuwa usoni mwake muda wote.

    “Ndio” Bi Anna alijibu kwa kifupi.

    “Ningependa kupata chakula cha usiku pamoja nawe” Bwana Mayemba alimwambia Bi Anna.

    “Usijali Mheshimiwa” Bi Anna alijibu.

    Huo ndio ukawa mwanzo wa mawasiliano kati yao. Katika siku tatu ambazo Bi Anna alikuwa jijini Dar es Salaam muda mwingi alikuwa pamoja na Bwana Mayemba huku wakielekea katika sehemu mbalimbali kutembea.

    Bi Anna alijiona kuwa na bahati hasa mara baada ya Bwana Mayemba kumwambia kuhusu kile ambacho kilikuwa kinaendelea moyoni mwake. Bi Anna hakuleta kipingamizi chochote kile, kitendo cha kutoka out kwenda kutembea tayari kilikuwa kimfanya kuvutiwa na Bwana Mayemba.

    “Na vipi kuhusu mkeo?”

    “Mke wangu alifariki miaka miwili iliyopita, wala hatukufananikiwa kupata mtoto hata mmoja” Bwana Mayemba alimwambia Bi Anna.

    “Pole sana”

    “Usijali. Nimkwishapoa. Vipi kuhusu wewe?”

    Swali hilo ndilo ambalo lilimfanya Bi Anna kuelezea kila kitu ambacho kilikuwa kimetokea maishani mwake. Ilionekana kuwa kama hadithi fulani ambayo ilikuwa ikisisimua kupita kiasi. Bwana Mayemba alimwangalia Bi Anna mara mbili mbili, hakuamini kama mwanamke huyo alikuwa amepitia katika maisha magumu kiasi hicho.

    “Hivi kweli kuna watu wana roho mbaya namna hiyo hapa Tanzania?” Mzee Mayemba aliuliza huku akionekana kushangaa.

    “Wapo. Wamejaa vijijini kwetu”

    Mara baada ya wiki moja kukatika ndipo Bi Anna akarudi mkoani Shinyanga. Hakutumia basi tena, safari hii alikatiwa tiketi ya shirika la ndege la Precious na kurudi Shinyanga.

    Mawasiliano ndicho kilikuwa kitu ambacho kilikuwa kikiendelea katika maisha yao. Kila siku mapenzi ya watu hawa wawili yalikuwa yakionekana kuongezeka kiasi ambacho hata wao wenyewe walionekana kujishangaa. Mipango mingi wakaipanga maishani mwao, ni kitu kimoja tu ndicho ambacho kilikuwa kikisubiriwa, ndoa.



    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    *******************







    Siwema alikuwa akikimbia kuelekea mbele zaidi. Machozi bado yalikuwa yakimtoka, moyoni aliumia kupita kiasi. Vibao ambavyo alipigwa na baba yake vilionekana kumkasirisha kupita kiasi. Hakutaka kurudi tena kijijini kwao, aliona ni bora kuendelea na safari, kutafuta maisha mapya.

    Kila wakati taswira ya Patrick ilikuwa ikionekana kichwani mwake, wakati mwingine alikuwa akitabasamu huku akijiona kuwa mtu wa bahati kupendwa na mtu kama Patrick. Alimpenda Patrick kuliko mvulana yeyote katika maisha yake, aliyatoa maisha yake kwa ajili yake na ndio maana hata aikuwa radhi kuutoa usichana wake kwa mvulana huyo.

    Pori lilikuwa na giza kubwa lakini macho ya Swema yalionakana kuwa na nguvu ya kuona kila kitu ardhini. Aliruka vishimo na magogo kadhaa. Woga wote ambao alikuwa nao ulikuwa umemtoweka, hakuogopa giza tena kwa wakati huo.

    Mara kwa mara Siwema alikuwa akipumzika chini ya miti na kisha kuendelea na safari kama kawaida. Hakujua alikuwa akielekea upande gani, kitu ambacho alikuwa akikijali ni kuukimbia mkono wa baba yake, mzee Abdallah ambaye alionekana kukasirika kuliko kawaida.

    Siwema alikimbia zaidi na zaidi huku masaa yakiendelea kukatika, kwa mbali macho yake yakaanza kuona mwanga wa taa kadhaa. Siwema akaachia tabasamu kwani tayari alikwishaona kuwa mahali pale ndipo ambapo angepata msaada wa kulala na kisha kesho kuendea na safari ambayo hakuwa akiifahamu.

    Akajikuta akipata nguvu ya ziada na kuzidi kukimbia zaidi na zaidi kuelekea kule ambako kulionekana kuwa na nyumba chache. Kadri alivyozidi kukimbia na ndivyo ambavyo matumaini yalivyozidi kuongezeka moyoni mwake.

    Akafika katika uwanja mkubwa ambao kwa mbele kulikuwa na nyumba kadhaa. Siwema akaanza kupiga hatua kuzifuata nyumba zile huku macho yake yakiangalia huku na kule. Hakukuwa na mtu yeyote nje zaidi ya ng’ombe ambo walikuwa wamefungiwa zizini.

    Siwema akaanza kupiga hatua huku akiangalia katika kila upande. Mara ng’ombe wakaanza kupiga kelele. Siwema akaonekana kushtuka, akasimama na kuanza kuangalia kila upande huku akionekana kuanza kushikwa na wasiwasi.

    Wanaume kama nane wakatokea kutoka katika vichaka walipokuwa wamejificha na kuanza kumsogelea Siwema kwa kasi. Hakukuwa na mtu aliyemuuliza kitu chochote kile zaidi ya kumvamia na kuanza kumshambulia kwa kumchapa fimbi mfululizo na kumpiga kwa marungu waliyokuwa wameyashika.

    Siwema akadondoka chini na kuanza kulia. Hakukuwa na mtu aliyeonekana kujali, bado walikuwa wakiendelea kumshambulia kwa nguvu huku wakionekana kuwa na hasira. Siwema alikuwa akitokwa na damu katika sehemu kubwa ya mwili wake, mbele yake akaanza kuona giza ambapo baada ya muda, hakuonekana kujua kitu chochote kilichokuwa kikiendelea.

    “Tumewakomesha sasa. Huyu ni wa kwanza, kuna wengi watakuja, kazi yetu itakuwa ni hii hii, kuwaua tu” Kijana mmoja aliwaambia wenzake huku wakipongezana kwa furaha kwa kitendo kile cha kumpiga Siwema mpaka kutokujitambua.

    “Mhhhhhh...!” Kijana mmoja alisikika akiguna hali iliyomfanya kila mtu kumwangalia.



    *********************************************





    Kila mtu alikuwa akimwangalia mganga ambaye alikuwa amemaliza sala yake ya kuikabidhi damu ya Patrick mikononi mwa miungu yake. Akayarudisha macho yake kwa Patrick na kukishika vizuri kisu chake kilichokuwa na makali pande zote mbili.

    Akakipeleka shingoni mwa Patrick huku akijiandaa kumchinja kama kawaida yake. Muda wote huo Patrick alikuwa akisali sala yake ya mwisho huku machozi yakiendelea kumtoka, hakuamini kama siku hiyo ndio ilikuwa siku yake ya mwisho kuvuta pumzi ya dunia hii.

    Kila mmoja aliyekuwa mahali hapo alishtushwa na mlio wa simu ambayo ilikuwa ikiita. Mganga akaacha kile ambacho alikikususdia kukifanya na macho yake kumwangalia kila mtu huku akitaka kujua ni nani ambaye alikuwa ameiacha simu yake ikiwa imewashwa.

    Kila mmoja akamwangalia Bwana Mayasa ambaye alikuwa akijipapasa na kuitafuta simu yake. Hakukuwa na mtu aliyesema kitu chochote kile, kwani bosi ndiye ambaye alikuwa amefanya kosa kwa kuiacha simu yake ikiwa imewashwa.

    Bwana Mayasa akaonyesha ishara ya kuomba msamaha na kuipokea simu ile na kuipeeka sikioni. Kila mmoja alikuwa kimya akimwangalia Bwana Mayasa ambaye muda wote wa maongezi alionekana kama mtu ambaye alishtushwa na kitu fulani.

    “Unasemaje?”

    “Ndio hivyo mkuu. Yaani hapa ninapoongea, wako njiani wanakuja huko” Sauti ya kijana fulani ilisikika simuni.

    Bwana Mayasa akaonekana kuchanganyikiwa upita kiasi, akakata simu ile na kuanza kumwangalia kila mtu mahali pale. Mganga akataka kuendelea kwa kukirudisha kisu chake shingoni mwa Patrick kwa ajili ya kumchinja kama ambavyo ilikubaliwa.

    “Ngoja kwanza” Bwana Mayasa alimwambia mganga ambaye alionekana kushtuka.

    Hakukuwa na mtu ambaye alikuwa akiamini kama Bwana Mayasa angeweza kumsimamisha mganga ambaye alitaka kfanya kile alichotaa kukifanya. Hawakuelewa sababu iliyompelekea kumsimamisha mganga kwani jambo hilo halikuweza kutokea toka miaka kumi iliyopita katika kipindi kazi hiyo ilipoanza.

    “Wanakuja” Bwana Mayasa alimwambia mganga.

    “Wanakuja? Wakina nani?” Mganga aliuliza huku akiwa ameacha kufanya kile alichotaka kukifanya.

    “Mapolisi. Wanakuja kufanya uchunguzi mashimoni. Usifanye hivyo, acha kwanza kwani hali inaweza kuwa ya hatari kwetu” Bwana Mayasa alimwambia mganga.

    “Kwa hiyo hawa watoto tuwafanye nini bosi?” Godwin alimuuliza Bwana Mayasa.

    “Waacheni waondoke”

    “Hauoni kama siri hii inaweza kujulikana?”

    Bwana Mayasa akaonekana kushtushwa kutoka katika hai fulani. Tayari aliona kama angewaacha Patrick na Aziz basi ni lazima watoto hao wangekwenda kutangaza kile ambacho kilikuwa kikitokea mashimoni. Kukaonekana kutokuwa na sababu ya kuwaacha watoto hao hai, ilikuwa ni lazima wawaue ili kuilinda siri hiyo.

    “Basi wapotezeni. Ila msifanyie hapa mgodini, nendeni nao porini, tena mbali kabisa na hapa ili miili yao iende ikaliwe na wanyama wa mwituni kupoteza ushahidi” Bwana Mayasa aliwaambia.

    Hakukuwa na cha kupoteza, kila kitu kikaanza kufanyika haraka haraka. Patrick na Aziz wakabebwa juu juu na kupelekwa nje ya shimo lile. Patrick akajiona kuwa na bahati kubwa, hakuamini kama kweli walikuwa wamenusurika kutoka katika mdomo wa kifo.

    Wakapakizwa garini na moja kwa moja Godwin na Ally kuingia garini na safari ya kuelekea porini kuwaua Patrick na Azizi kuanza.

    Patrick na Aziz walibaki kimya garini, bado walikuwa wakiona kuwa katika hali ya hatari. Manyunyu yakaanza kudondoka na hatimae mvua kubwa kuanza kunyesha. Patrick akaonekana kukosa tumaini, tayari alijiona kuelekea kuuawa pamoja na rafiki yake, Aziz.

    Godwin na Ally muda wote walikuwa wakifurahia tu, bunduki zilikuwa zikiandaliwa vizuri kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wasingechukua hata dakika moja katka kukamilisha kile ambacho walikuwa wanakwenda kukifanya.

    Gari likakatwa kona na kuingia porini. Mvua ambayo ilikuwa imenyesha ilisababisjha matope ardhini lakini kutokana na gari lao kuwa na nguvu, liliweza kupita bila tatizo lolote lile.

    Safari iliendelea zaidi na zaidi mpaka katika sehemu ambayo ilionekana kuwa wazi kidogo, wakasimamamisha gari lao na kisha kuteremka.

    “Vipi hapa! Kunafaa?” Godwin alimuuliza Ally.

    “Pako mzuka. Kama vipi tuwateremshe tuwaue fasta fasta tukaendelee na kazi zetu” Ally alimwambia Godwin.

    Patrick na Azizi wakateremshwa kutoka garini na kuwekwa chini. Kila mmoja alikuwa akilia mara baada ya kumuona Godwin akiikoki bunduki yake kwa mbwembwe. Tayri walijiona kutokuwa na nafasi ya kunusurika kutoka katika mikono ya watu hao ambao walionekana kuwa hatari katika maisha yao.

    “Nani aanze kufa? Huyu Mpemba au huyu mswahili?” Godwin alimuuliza Ally ambaye alikuwa ameegemea gari akivuta sigara.

    “Anza na mpemba” Ally alijibu.

    Godwin akamnyooshea Aziz buduki tayari kwa kumfyatulia risasi. Muda wote Azizi alikuwa akilia, tayari alijiona kuwa muda huo ndio ambao alikuwa akienda kufa na kuungana na wazazi wake ambao walikufa kipindi kirefu kilichopita.

    “Paaa...paaa...paaa..paaa...” Milio ya risasi ikasikika mahali hapo.

    Patrick alikuwa akilia, hakuamini kama huo ndio ulikuwa mwisho wa kumuona Azizi maishani mwake. Sasa aliiona zamu yake ikifuata.





    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    *****





    Mikakati ya harusi kati ya Bi Anna na Bwana Mayemba ilikuwa ikiendelea kufanyika. Waandishi wa habari hawakuwa mbali, kila siku ilikuwa ni lazima waizungumzie harusi hiyo ambayo ilitarajiwa kufanyika baada ya wiki moja.

    Miezi sita ambayo walikuwa wamekaa katika uhusiano iliwatosha sana kuchunguzana na hata kuzoeana. Kupena zawadi ndio ilikuwa sehemu ya maisha yao, mara kwa mara Bi Anna alikuwa akiondoka Shinyanga na kuelekea Dar es Salaam kwa ajili ya kuonana na mwanaume ambaye siku chache zijazo angekuwa mume wake wa ndoa.

    Kila siku wakilikuwa wakiwasiliana simuni hali ambayo iliyafanya mapenzi yao kuongezeka zaidi na zaidi. Kila mmoja alijiona kuwa na uhitaji wa mwenzake, mkoani Shinyanga, ofisini hakukukalika kabisa, kila siku Bi Anna alikuwa akitaka kuelekea Dar es Salaam kuonana na mpenzi wake, Bwana Mayemba.

    Michang ikaanza kuchangishwa, kila mtu alitoa kwa moyo kwani walikuwa na hamu ya kuwaona wapendao hao wakiingia katika maisha mapya ya ndoa. Mavazi ya bwana harusi na Bibi harudi yalikuwa yameandali vizuri kwa kukodishwa JM Fashion iliyokuwa Kinondoni.

    Magazeti mengi yalikuwa yakiandika habari ya harusi hiyo, mitandao mingi ya internet walikuwa wakiitangaza harusi hiyo ya Mheshimiwa, waziri wa Wanawake na Watoto, Bwana Mayemba. Jina la Bi Anna likazidi kupata umaarufu, sasa alikuwa akijlikana Tanzania nzima kwa sababu tu alikuwa akienda kuoewa na mtu ambaye alikuwa akijulikana nchini Tanzania.

    Bendi ya matarumbeta ikaagizwa kutoka nchini Afrika Kusini kwa ajili ya kuja kutumbuiza katika harusi hiyo. Kadi zaidi ya elfu tatu zikatengeneza kwa ajili ya kupewa kila mtu ambaye angetoa mchango wake. Magazeti yote nchini Tazania yalikuwa yakiandika habari za harusi hiyo ambayo ilikuwa ikitarajiwa kufanyika mwezi mmoja utakaofuata.

    Mchungaji kutoka Ghana akaitwa maalumu kwa ajili ya kuja kufungisha harusi hiyo ambayo ilikuwa ikizidi kusambaa kadri siku zilivyozidi kwenda mbele. Kila mtu masikio yake alikuwa ameyaweka karibu na vyombo vya habari kwa kutaka kujua siku ambayo hrusi hiyo ilitakiwa kufungwa.

    Hamu ikazidi kuongezeka mioyoni mwa watu hasa mara baada ya kutangazwa siku ambayo ilitakiwa kufanyika harusi hiyo. Viongozi mbalimbali wakaziandaa zawadi zao tayari kwa kuwapa maharusi katika siku ya harusi ambayo ilikuwa imebakia siku ishirini na moja kabla ya kufungwa katika kanisa la Praise and Worship.

    Siku ziliendelea kukatika huku watu wakizidi kuisubiri siku hiyo ambayo ilitangazwa kama siku ambayo ingeweka historia kwa kufanyika harusi kubwa na ya gharama kuliko harusi zote ambazo zilitokea kufanyika nchini Tanzania.

    Siku ziliendelea kukatika kama kawaida. Bwana Mayemba akaonekana kuwa na shauku zaidi. Ofisini hakutulia, mara kwa mara alikuwa akiwapigia marafiki zake mbalimbali na kuwataarifu juu ya harusi yake ingawa alijua fika watu hao walikuwa wakifahamu kila kitu.

    Bwana Mayemba akavuta kiti chake na kutulia, akayapeleka macho yake katika saa kubwa iliyokuwa ukutani ambayo ilikuwa ikionyesha kwamba tayari ilikuwa saa tatu usiku. Huku akiandika majina ya watu ambao walitakiwa kupewa kadi hasa wale ambao walikuwa serikalini, mara simu ya mezani ikaanza kusikika ikiita.

    Bwana Mayemba akaonekana kukasirika. Akatamani kuacha kuipokea simu ile lakini kutokana na kelele ambayo ilikuwa ikipiga, akaamua kuifuata na kuipokea. Akaupeleka mkonga wa simu sikioni na kuita.

    “Naongea na nani?” Bwana Mayemba aliuliza mara baada ya kuitikia simu ile.

    “Hautakiwi kunifahamu kwa sasa, ninajua kuwa umenisahau. Ila sitoweza kukusahau milele” Sauti ya msichana ilisikika.

    Mzee Mayemba akaonekana kushtuka, sauti ile ilionkana kumchanganya kupita kiasi. Akajaribu kuvuta kumbukumbu juu ya mahali ambayo aliisikia sauti ile, kila alipojaribu kukumbuka, hakuweza kukumbuka chochote kile.

    “Wewe ni nani?” Bwana Mayemba aliuliza huku akionekana kuwa na hasira.

    “Unanifahamu Mayemba. Ila kuna kitu nataka kukuambia” Sauti ya mwanamke yule ilisikika.

    “Kuna kitu unataka kuniambia! Kitu gani?” Mzee Mayemba aliuliza huku akionekana kuanza kuchanganyikiwa. Tayari kijasho chembamba kikaanza kumtoka, tayari wasiwasi ukaanza kumpata, akajaribu kuvuta kumbukumbu ya maisha yaliyopita, hakupata jibu lolote lile.

    “Ni lazima nitaipinga harusi yako. Harusi haitofungika” Mwanamke yule alisikika.

    “Utapinga harusi isifanyike? Wewe ni nani na kwa nini unataka kufanya hivyo?” Mzee Mayemba aliuliza huku akionekana kuchanganyikiwa zaidi ya kipindi kilichopita.

    “Utanifahamu siku hiyo” Sauti ya mwanamke yule ilisikika na simu kukatika.

    “Halooo...Halooo...” Mzee Mayemba aliita lakini hakukuwa na mtu yeyote aliyejibu.

    Mzee Mayemba akaurudisha mkonga wa simu mahali pake. Akarudi kitini na kutulia. Uso wake ulikuwa ukionekana ni kwa jinsi gani alikuwa na mawazo wakati huo. Akili yake haikuwa sawa kabisa, alionekana kuchanganyikiwa kupita kawaida.

    Kazi ambayo alikuwa akiiifanya ya kuandika kadi mbalimbali hakuifanya tena, akaiacha na kutulia kochini. Kadri dakia zilivyozidi kwenda mbee na ndivyo wasiwasi ulivyozidi zaidi na zaidi. Sauti ya msichana yule ilijirudia mara kadhaa kichwani mwake lakini wala hakupata jibu.

    Furaha yote ambayo alikuwa nayo katika kipindi kilichopita ikayayuka, huzuni na mawazo ndivyo ambavyo vilikuwa vimeutawala moyo wake kwa wakati huo. Kwa uchovu mkubwa, akainuka na kuanza kuelekea chumbani kwake ambako akajilaza kitandani na kutulia.

    Mawazo hayakumuisha kichwani mwake, kila wakati sauti ile ilikuwa ikisikika masikioni mwake. Alibaki akiwa amechanganyikiwa, bado hakuweza kupata jibu lolote juu ya sauti ile ya mwanamke yule. Usingizi wala haukupatikana, akabaki akiangalia darini tu.

    Kuanzia siku hiyo, furaha yote aliyokuwa nayo ilikuwa imepotea, hakuonekana kuwa na furaha ingawa mara kwa mara alikuwa akijilazimisha kuonekana kuwa na furaha. Mbele yake aliiona aibu ikiiwa inamnyemelea, kitendo cha harusi yake kutaka kupingwa kanisani kilionekana kumfanya kuwa na mawazo kupita kawaida.

    Siku ziliendelea kukatika na hatimae siku ambayo ilikuwa ikisubiriwa kwa hamu kuwadia. Magari zaidi ya mia mbili yalikuwa yamepaki katika kanisa la Praise And Worship, kanisa ambalo lilikuwa kubwa kuliko makanisa yote Afrika Mashariki.

    Idadi ya waumini pamoja na watu wengine ambao walikuwa wamehudhuria harusi hiyo hapo kanisani ilikuwa zaidi ya watu elfu mbili. Kila kona kulikuwa na kamera za waandishi wa habari na za watu binafsi ambao walitaka kupiga picha harusi hiyo.

    Kwaya moja baada ya nyingine zilikuwa zikiimba kanisani hapo kwa ajili ya kuvuta muda wa kuwasubiri maharusi ambao walikuwa njiani kuelekea kanisani hapo. Kila mtu ambaye alikuwa kanisani hapo alikuwa akionekana kuwa na furaha isipokuwa mwanamke mmoja tu ambaye macho yake yalikuwa mekundu hali iliyoonyesha kwamba alikuwa amelia kwa kipindi kirefu.

    Dakika ziliendelea kwenda huku vigeregere vikizidi kupigwa kanisani hapo. Zilipita dakika thelathini, gari la bwana harusi likasimama katika eneo la kanisa hilo. Mzee Mayemba akateremka na kuanza kupiga hatua kuelekea kanisani huku akiongozana na mpambe wake.

    Zilipita dakka tano, gari la bibi harusi, Bi Anna likaanza kuingia mahali hapo hali iliyowafanya wakinamama kuanza kupiga vigeregere. Bwana Mayemba akamfuata Bi Anna na kisha kuanza kuelekea nae mbele ya kanisa.

    Muda wote Mzee Mayemba alikuwa akionekana kutokuwa na furaha, tabasamu la bandia ndilo ambalo lilikuwa likionekana usoni mwake. Muda wote macho yae yalikuwa yakiangalia kila kona kanisani mule kumtafuta mwanamke ambaye alikuwa amempigia simu usiku wa siku ile.

    Mara baada ya maharusi kufika mbele ya kanisa, mchungaji Samuel Mwashambwa akaanza kuhubiri, alihubiri kwa dakika tano, alipomaliza akaziomba pete ambazo zililetwa moja kwa moja mpaka pale alipokuwa.

    “Nitakwenda kufungisha ndoa hii, ndoa ambayo kila mtu alikuwa na hamu ya kuiona” Mchhungaji alisema na kuendelea.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kwa mamlaka ambayo nimepewa, nitakwenda kuifungisha ndoa hii mchana wa leo” Mchungaji aliwaambia.

    Kanisa zima lilikuwa kimya likimsikiliza mchungaji ambaye alikuwa akiendelea kuongea. Alichukua dakika mbili, akaanza kuliangalia tena kanisa lile na kutulia.

    “Kabla ya kuifungisha ndoa hii, kuna mtu mwenye kipingamizi chochote cha kuzuia ndoa hii isifugwe?” Mchungaji aliuliza.

    Kanisa zima lilikuwa kimya, watu wakaanza kuangalia huku na kule kuona kama kulikuwa na mtu yeyote ambaye alisimama. Mchungaji akarudia kwa mara ya pili, Bwana Mayemba akaanza kuwaangalia washirika ambao walikuwa kanisani mule.

    Moyo wake ukashtuka kupita kiasi mara baada ya kumuona mwanamke ambaye alikuwa akimfahamu vilivyo ambaye historia ya maisha yake ilikuwa ndefu sana. Bwana Mayemba akaonekana kuwa na wasiwasi, mwili wote ukamnyong’onyea.

    Mwanamke yule alikuwa akilia huku akimwangalia Bwana Mayemba kwa hasira, alionekana kama kutaka kusimama na kuongea kitu ambacho alikuwa nacho moyoni. Bwana Mayemba akatamani kumsimamisha mwanamke yule asisimame.

    “Kuna mtu ana kipingamizi cha ndoa hii kutokufungwa?” Mchungaji alilirudia swali lake.

    “Nakuomba Maria usisimame. Niko tayari kumlea mtoto. Nakuomba Maria usisimame” Bwana Mayemba alisema kimoyo moyo huku akionekana kuwa na wasiwasi juu ya Maria kusimama na kuipinga harusi hiyo.



    ***********************************





    Serikali ilionekana kuchanganyikiwa kutokana na idadi ya watoto ambayo ilikkuwa ikipotea mara kwa mara Tanzania. Ulinzi mbalimbali uliwekwa katika maisha ya watoto wengi lakini bado watoto hao walikuwa wakiendelea kupotea.

    Kamanda mkuu wa jeshi la polisi Tanzania, Bwana Nehemia Kiki alionekana kuchanganyikiwa kuliko kawaida. Kesi mbalimbali ambazo alikuwa akizipata kutoka kwa wakinamama mbalimbali kuhusiana na watoto ambao walikuwa wakiendelea kupotea zilionekana kumchanganya.

    Akaamua kujitoa na kupambana kwa nguvu zote. Maoni mbalimbali ya wakinamama yakaanza kukusanywa mitaani. Kazi ilionekana kuwa kubwa lakini alionekana kufanikiwa kwa kiasi kikubwa sana. Maoni mengi kutoka kwa wakinamama yakawa yamekwishakusanywa na kupelekwa ofisini mwake.

    Alianza kuyasoma maoni yale huku akionekana kuwa makini kupita kawaida. Alipitia karatasi mbalimbali huku akionekana kuanza kuhisi kitu fulani kichwani mwake. Karatasi za maoni zilikuwa nyingi lakini alizipitia kwa haraka haraka usiku kucha na ndipo alipozimaliza.

    “Inawezekana hupelekwa katika migodini na baharini” Kamanda Nehemia alijisemea na kuzihifadhi zile karatasi.

    Kwa haraka haraka akaanza kusambaza taarifa katika vituo mbalimbali vya polisi nchini. Upelelezi ukatakiwa kufanyika kwa haraka sana katika migodi yote nchini pamoja na sehemu ambazo walikuwa wakitumia katika uvuvi wa samaki.

    Mapolisi walijipanga vilivyo, ingawa taarifa ilikuwa imetolewa usiku wa saa tatu lakini kila kitu kilitakiwa kufanyika kwa haraka sana. Kila polisi alikuwa akimuogopa kamanda Nehemia kutokana na ukali wake aliokuwa nao kazini na hiyo ndio ilikuwa sababu ambayo iliwafanya mapolisi wote kutekeleza kile ambacho alikuwa akikitaka kifanyikike.

    Mkuu wa polisi mkoani Shinyanga, Bwana Haji mara baada ya kupewa taarifa ile, akaanza kulifanyia kazi jambo lile usiku ule ule. Kwa haraka akainuka kutoka kitandani na moja kwa moja kutoka nje ambako akachukua gari lake na kuanza kuelekea katika jengo la kituo kikuu cha polisi cha mkoa wa Shinyanga.

    Huko akatoa taarifa juu ya kila kitu ambacho alikuwa ameambiwa simuni. Mapolisi zaidi ya kumi wakaingia katika magari mawili na kisha safari kuanza kuelekea Mwadui kuanza. Dakika zilizidi kusogea zaidi na zaidi huku manyunyu ya mvua yakianza kudondoka ardhini.

    Mapolisi wote ambao walikuwa ndani ya magari yale walikuwa wameshika bunduki zao. Manyunyu bado yalikuwa yakiendelea kudondoka hali ambayo baada ya muda, mvua kubwa ikaanza kunyesha. Matope yakaanza kuonekana barabarani hasa katika barabara hiyo ya vumbi ambayo ilikuwa ikielekea katika mji wa Mwadui.

    Magari yalikuwa katika kasi kubwa, walitaka kuingia mgodini hapo kwa kushtukiza ili kusiwe na mtu yeyote ambaye angetambua kama usiku huo walikuwa wakielekea katika mgodi huo. Mapolisi waliliona gari lao haliendi kabisa, kiasi ambacho walitamani liote mabawa na kupaa.

    Kwa mbali wakaanza kuziona taa za gari ambalo lilikuwa likionekana kuja kwa kasi. Gari lile likazidi kusogea na hatimae kupishana nalo. Hakukuwa na mtu yeyote ambaye alikuwa na wasiwasi na gari lile, bado walikuwa wakiendelea na safari yao ya kuelekea Mwadui.

    “Simamisha gari” Ilikuwa ni sauti ya kamanda Haji ambaye alikuwa amemwambia dereva.

    Gari likasimamishwa, kamanda Haji akataka gari lile ligeuzwe na kuanza kulifuatilia gari lile walilopishana nalo huku gari lile jingine la polisi likiendelea na safari ya kuelekea Mwadui. Tayari kamanda Haji akaonekana kulitilia mashaka, alitaka kulifuatilia kuona ni kitu gani kilikuwa kinaendelea katika gari lile.

    “Zima taa za gari. Tunataka tulifuatilie kigiza giza” Kamanda Haji alimwambia dereva ambaye alifanya kama alivyoambiwa.

    Waliendelea kulifuatilia gari lile ambalo lilikuwa likiendeshwa kwa mwendo wa kasi ambao uliwashangaza hata hao wenyewe. Wasiwasi ukazidi kuwaingia mioyoni mwao, tayari waliona kwamba kulikuwa na kitu ambacho kilikuwa kinaendelea kuhusiana na lile gari.

    “Bunduki mnazo vizuri?” Kamanda Haji aliwauliza mapolisi watatu ambao alikuwa nao katika gari lile aina ya Difenda.

    Gari lile likakata porini hali ambayo ikawapa uhakika asilimia mia moja kwamba gari lile lilikuwa la watu wabaya ambao walikuwa wakikorofishana na mapolisi mara kwa mara. Mara baada ya kufika katika sehemu ile, nao wakakata kona kuelekea kule gari lile lilipokuwa likielekea.

    Bado mvua kubwa ilikuwa ikiendelea kunyesha huku baridi kali likiwapiga wale mapolisi watatu ambao walikuwa nyuma. Walitembea kwa mwendo fulani, wakalikuta gari lile likiwa limepakiwa pembeni. Kwa staili ya kikomando, wakateremka na kuanza kuelekea kule ambako walikuwa na uhakika wenye gari lile walipokuwa.

    Kwa kutumia mwanga wa gari lile la wauaji, wakafanikiwa kuwaona watoto wawili wakiwa chini. Mikono yao ilikuwa imefungwa kamba huku midomoni wakiwa wamewekewa gundi ya nailoni iliyowafanya kutokuongea vizuri.

    Mmoja wa wale vijana akachukua bunduki yake na kuanza kuiangalia kama alikuwa akiichunguza. Kamanda Haji na mapolisi wenzake wakagundua kwamba mahali hapo kulikuwa na hatari kitu ambacho kiliwafanya kuandaa vizuri bunduki zao.

    “Tuanze na nani hapa? Huyu mpemba au Mswahili?” Kijana mmoja alisikika akimuuliza mwenzake.

    “Anza na mpemba”

    Godwin akaishika bunduki yake vilivyo na kumuelekezea Azizi pale chini alipokuwa. Azizi alikuwa akilia huku akionekana kutaka kuachiliwa na kuondoka mahali pale alipokuwa pamoja na Patrick. Huku Godwin akiwa amejiandaa kumfyatulia risasi Aziz, risasi mfululizo zikaanza kusikika, Godwin na Ally wakaanguka chini huku damu zikiwatoka.

    Patick alikuwa akilia kwa uchungu, tayari alijua kwamba rafiki yake, Azizi alikuwa ameuawa na sasa ilikuwa ni zamu yake. Mapolisi wanne wakatokea mahali hapo kutoka vichakani na kuwafuata Patrick na Aziz ambao walikuwa wakilia.

    “Mungu wangu! Angalia, yaani ni watoto wadogo kweli, sijui kwa nini walitaka kuwaua” Polisi mmoja aliwaambia wenzake.

    “Hawa ndio watatuambia ukweli ka nini watoto wanapotea na kupelekwa migodini. Cha msingi wafungueni kambana tuondoke nao” Kamanda Haji alisema huku bado mvua ikiendelea kunyesha. Mara baada ya kufunguliwa kamba ambazo zilikuwa zimewafunga pamoja na gundi ambazo zilikuwa zimefunika midomo yao, moja kwa moja wakachukuliwa na kupelekwa garini huku nguo zao zikiwa na matope.

    Kamanda Haji alionekana kufurahia, tayari alikuwa na uhakika wa kujua juu ya kitu ambacho kilikuwa kikiwasumbua Watanzania. Aliamini kuwa Patrick na Azizi ni lazima wangewaambia ukweli juu ya kile ambacho kilikuwa kikitokea migodini.

    “Endesha kwa kasi, nina hamu ya kuwahoji watoto hawa” Kamanda Haji alimwambia dereva ambaye aliongeza kasi.

    Gari liliendeshwa kwa kasi lakini kutokana na matope mazito ambayo yalikuwa yametanda katika barabara ile ya vumbi kutokana na mvua ile kubwa, wakashangaa kuona gari lao likikwama katika matope. Dereva alijitahidi zaidi na zaidi lakini wala gari halikutoka mahali pale.

    “Kwa hiyo tufanye nini?” Kamanda Haji aliuliza.

    “Inabidi mteremke na mlisukume” Dereva aliwaambia.

    “Kwa hiyo wasukumaji tuwe mbele au nyuma?”

    “Nendeni nyuma” Dereva aliwaambia.

    Mapolisi wale watatu pamoja na kamanda Haji wakaelekea nyuma ya gari lile na kuanza kuliasukuma huku dereva akijaribu kukanyaga moto. Kazi ilionekana kuwa bure hali ambao ilimfanya dereva awaambie waelekee mbele na kulisukuma kurudi nyuma. Wote wakaenda mbele ya gari lile na kuanza kulisukuma.

    Patrick pamoja na Azizi walikuwa wakitetemeka kwa barini, mvua bado ilikuwa ikiendelea kunyesha. Patrick akaanza kuangalia katika kila upande kama mtu ambaye alikuwa akiangalia noma, alipoona hali iko fresh, akamsogelea Azizi.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Tuondoke. Tukimbie” Patrick alimwambia Azizi ambaye alionekana kushtuka.

    “Tukimbie? Tukimbie nini sasa na wakati hawa ni mapolisi” Azizi aimuuliza Patrick.

    “Bado hatuko salama Azizi, ni lazima tuishi maisha ya kuangaika angaika tu. Hawa hawatotusaidia kabisa” Patrick alimwambia Azizi ambaye alionekana kama kuchanganyikiwa na maneno ambayo aliongea Patrick.

    “Bado unanichanganya Patrick! Hawatotusaidia?”

    “Ndio. Wao wanataka kutuhoji tu. Hebu jifikirie wakishamaliza kutuhoji watatupa sehemu ya kuishi au watatuacha tuondoke?” Patrick aliuliza.

    “Watatuacha tundoke”

    “Basi haina maana. Tuondoke Azizi” Patrick alimwambia Azizi huku akimshika mkono.

    Hakukuwa na muda wa kuchelewa, kutokana na mapolisi wale kuwa mbele ya gari lile, hawakuweza kuwaona Patrick na Azizi ambao walikuwa nyuma ya gari lile aina ya Difenda. Patrick na Azizi wakaanza kukimbia kuelekea Porini. Hawakujua walikuwa wakielekea wapi ila wao kitu walichokijua ni kuondoka, hawakutaka kuishi na mtu yeyote yule, walitaka kuangaika kivyao.

    Mara baada ya kusukuma gari lile na kuona imeshindikana, wakaamua kurudi tena nyuma ya gari kwa ajili ya kusukuma. Wote wakapigwa na mshangao, Patrick na Aziz hawakuwa garini pale hali iliyoonekana kuwachanganya.

    “Mungu wangu! Wamekimbia! Ingieni vichakani, watakuwa hawajafika mbali, zifuateni alama za miguu yao. Tunawahitaji watoto hawa. Yaani wao ndio wa kutueleza kila kitu” Kamanda Haji aliwaambia mapolisi huku akionekana kuchanganyikiwa. Polisi wote wakaingia vichakani kwa ajili ya kuwatafuta Patrick na Azizi kwa kufuatilia alama za miguu yao.



    **********************************





    Watu wote waliokuwa na mapanga. Marungu na fimbo walikuwa wakimwangalia kijana ambaye alikuwa ametoa mguno. Mguno wake haukuwa wa kawaida hata kidogo ulisikika katika hali ambayo ilimaanisha kwamba kulikuwa na kitu.

    Akaichukua tochi yake ambayo alikuwa ameifunga katika mkanda wake kiunoni na kuiwasha kisha kummulika Siwema, kila mwanaume akaonekana kuogopa, hawakuamini kama mtu ambaye walikuwa wakimshambulia alikuwa msichana. Kila mmoja akaonekana kuogopa.

    Damu zilikuwa zikiendelea kumtoka Siwema, pale chini alikuwa kimya, hakutingishika hata kidogo. Wanaume wote walibaki kimya kwa muda huku wote wakionekana kupigwa na butwaa kubwa. Mmoja mmoja akaanza kupiga hatua kurudi nyuma.

    “Sasa mnakwenda wapi? Mnataka kukimbia?” Mzee Mkude ambaye alikuwa mwenyekiti wa kijiji kile aliwaambia wanaume ambao walikuwa wakipiga hatua kurudi nyuma.

    “Hakuna mtu yeyote kuondoka. Tumbebeni tumpeleke katika hospitali ya kijiji” Mzee Mkude aliwaambia na kisha kumbeba Siwema na kuanza kumpeleka katika hospitali ya kijiji.

    Wala hakukuwa mbali sana kutoka mahali hapo, ni ndani ya dakika tano wakawa wamekwishafika katika hospitali hiyo ambapo moja kwa moja wakaanza kupiga hatua kuelekea katika sehemu ya mapokezi. Hakukuwa na mtu yeyote katika sehemu ile ya mapokezi, wakaanza kuiya ambapo baada ya dakika kadhaa, dada aliyekuwa amevalia nguo nyeupe tupu akatikea mahali hapo.

    “Karibuni” Dada yule aliwakaribisha huku akiwasha taa.

    “Asante” Mzee Mkude alijibu.

    Mshtuko mkubwa ukampata dada yule wa mapokezi mara baada ya macho yake kutua katika mwili wa Siwema. Mwili ulikuwa unatisha ambao hakuweza kuuangalia mara mbili. Aliuhisi mwili wake ukitetemeka kwa hofu. Ni kweli alikuwa amewaona watu wengi wakiwa wamejeruhiwa, lakini kwa Siwema ilikuwa ni zaidi ya kujeruhiwa.

    Mwili wake ulikuwa umechanwachanwa na fimbo pamoja na mapanga ambayo alikuwa ameshambuliwa nayo. Mwili ulikuwa umevimba, marungu ambayo alikuwa amepigwa pasipo mpangilio, yalionekana kumvimbisha kupita kiasi.

    “Kuna nini tena? Mbona huyo binti yuko hivyo?” Yule dada wa mapokezi aliuliza huku akionekana kushangaa.

    “Ajali. Ajali mama” Mzee Mkude alimwambia dada yule wa mapokezi huku akionekana kuogopa.

    “Ajali! Ajali ya nini?”

    “Si unajua mambo ya kulinda mifugo yetu usiku. Tulivyomuona tulifikiri mwizi na ndipo tukaanza kumshambulia” Mzee Mkude alimwambia dada yule.

    Bado yule dada alionekana kusisimka mwili wake kupita kiasi. Siwema alionekana kuumia kupita kawaida kiasi ambacho ingekuwa ngumu sana kupata matibabu katika hospitali ile. Kitu alichokifanya ni kuondoka moja kwa moja kwenda kwenye chumba kimoja, aliporudi, alirudi na mwanaume mmoja mweusi aliyekuwa na ndevu nyingi.

    “Naomba uwapeleke Nzega” Dada wa pale mapokezi alimwambia mwanaume yule.

    Japokuwa ilikuwa ni moja ya kazi yake, mwanaume yule wala hakuwa na kipingamizi japokuwa alikuwa akionekana kuchoka kupita kiasi. Aliwaangalia mzee Mkude na wenzake, hasira zikamshika kwani aliona kama anasumbuliwa.

    Macho yake alipoyaamisha na kuyapeleka kwa Siwema ambaye alikuwa amelazwa benchini, yeye mwenyewe akaanza kufanya haraka haraka. Hali ya Siwema ilionekana kumtisha kila mtu. Akawaambia wambebe na kisha kumpeleka katika gari aina ya Pick Up na kisha kuwasha gari lile.

    “Ninaokwenda nao ni nani na nani?” Mwanaume yule dereva aliuliza.

    Mzee Mkude na wanaume wengine wawili wakajitokeza na kuingia garini huku watu wengine wakiondoka mahali hapo. Kila wakati walikuwa wakimwangalia Siwema ambaye alionekana kuwa katika hali mbaya kupita kawaida, damu ambazo zilikuwa zikimtoka zikaanza kuchuruzika katika bodi la gari lile.

    Kwa kawaida kutoka katika kijiji cha Ukenyenge mpaka Nzega mkoani Tabora ilikuwa ni lazima utumie masaa matatu kama tu ungetumia gari. Barabara haikuwa nzuri hata kidogo, kila sehemu kulikuwa na mashimo. Dereva hakuendesha gari lile katika mwendo wa kawaida, alikuwa akiendesha kwa mwendo wa kasi huku lengo lake likiwa ni kufika Nzega haraka.

    Ndani ya masaa mawili ndio wakaanza kuingia Nzega huku ikiwa imetimia saa kumi alfajiri. Walipoingia katika barabara ya lami, dereva aliongeza kasi zaidi mpaka wakaingia katika hospitali ya Nzega. Kutokana na kutokuwa na mtu nje ya eneo la hospitali, wakamteremsha Siwema na kuanza kuelekea nae ndani ya hospitali ile.

    “Mmmhh! Mbona hivyo jamani” Dada aliyewapokea mapokezi aliwauliza.

    “Kwanza jaribu kutusaidia halafu maswali baadae dada” Derva alimwambia dada yule ambaye akaufungua mlango na wao kumuingiza Siwema. Moja kwa moja wakampeleka mpaka chumbani ambako akalazwa na kisha mzee Mkude kuelekea Mapokezini kumwandikisha.

    Masaa yalikuwa yakisogea mpaka datari mkuu kuingia. Moja kwa moja akapewa taarifa juu ya mgonjwa ambaye alikuwa ameletwa alfajiri. Daktari akaanza kuelekea katika chumba kile ambako baada ya muda akarudi huku uso wake ukiwa umejaa huzuni.

    Mwili wa Siwema na kwa jinsi ambavyo alikuwa amejeruhiwa ulionekana kumshtua kupita kiasi. Micharazo ilikuwa ikionekana vizuri mwilini mwake huku alama za kukatwa katwa na panga zikionekana kwa mbali. Akaanza kuwaangalia mzee Mkude pamoja na wenzake na kisha kuwaita ofisini.

    Mzee Mkude alielezea kila kitu kilichotokea lakini huku akidanganya kuhusu kijiji walichotokea. Daktari alibaki kimya akimsikiliza, alipoona ameridhika na maelezo yake, akawaambia waende wakasubiri benchini.

    “Mbona umemdanganya kuhusu sehemu tulipotokea?” Kijana mmoja kati ya wale wawili aliokuja nao aliuliza.

    “Hii kesi. Tena kesi kubwa. Hapa ni lazima tuondoke haraka iwezekanavyo” Mzee Mkude aliwaambia.

    Huo ndio uamuzi uliofikiwa, hawakutaka tena kubaki hospitalini pale, tayari waliona kuwa kesi ilikuwa ikiwajia kama tu wangediriki kusubiri kujua ni kitu gani kingeendelea. Hakukuwa na yeyote ambaye alikuwa tayari kusubiri, kwa mwendo wa haraka haraka wakatoka katika jengo lile na kukimbia huku wakimwacha Siwema akiwa hana mtu yeyote anayemfahamu pale Nzega.

    *****

    Bado mvua ilikuwa ikiendelea kunyesha, mawingu mazito yalikuwa yametawala angani. Ardhi ilikuwa na matope mengi kupita kiasi lakini hakukuwa na mtu yeyote aliyesimama. Bado walikuwa wakiendelea kukimbia kwa kasi, hawakutaka kutiwa mikononi mwa wale mapolisi ambao waliwaokoa kutoka katika mikono ya wauaji.

    Zilipita dakika thelathini, mvua ile ikakatika. Wakaanza kutembea kwa mwendo wa kasi mpaka kufika katika sehemu ambayo ilikuwa na kilima kimoja ambacho hakikuwa kikubwa sana. Wakaanza kupandisha kilima kile kwa mwendo wa kasi.

    Giza nene bado lilikuwa limetanda huku kadri walivyokuwa wakikipandisha kilima kile na ndivyo ambavyo baridi lilivyozidi kuongezeka. Walitamani kama wangekuwa na makoti mazito ambayo yalikuwa na kazi ya kuzuia baridi, lakini walikuwa na fulana tu.

    Wakafika pale kilimani na kuanza kuangalia kwa chini. Ni miti mirefu ndiyo ambayo ilikuwa imetawala huku giza kubwa bado lilikuwa limetanda katika eneo hilo. Wakaamua kuufuata mti ambao ulikuwa katika kilima kile na kupumzika huku wakipaona mahali hapo kuwa salama kwa ajili ya maisha yao.

    Waliendelea kubaki kilimani pale, masaa yaliendelea kukatika huku kiubaridi kikizidi kuwapiga mahala hapo. Kila mmoja alikuwa akitetemeka kwa sababu ya baridi lile ambalo lilizidi kuwapiga zaidi na zaidi. Hakuna aliyepata usingizi ingawa walikuwa wamechoka kupita kiasi.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kwa mbali mwanga ukaanza kuonekana, wakaangalia tena chini ya kilima kile, kwa mbali walikuwa wakiona mwanga wa taa za gari ambazo zilikuwa zimesimama.

    “Unaoa mianga ile?” Patrick alimuuliza Aziz ambaye alianza kuangalia vizuri.

    “Naiona. Nafikiri zile zitakuwa nyumba”

    “Zile sio nyumba Azizi, ile ni mianga ya taa. Itatubidi tuondoke mahali hapa kuelekea kule, nadhani pale tutaomba msaada wa kufikishwa mjini” Patrick alimwambia Aziz na kisha kuanza kushuka kilima kile.

    Kutokana na kilima kile kuwa na miti mingi pamoja na kona ambazo zilionekana kuwa kama njia zilizosahaulika kupitwa, walitumia zaidi ya dakika arobaini hadi kufika chini ya kilima kile na kuanza kuelekea kule ambako waliyaona mataa yale ya gari.

    Umbali ulikuwa ni tofauti na jinsi ambavyo walijua kabla. Walitembea zaidi na zaidi huku kila mmoja akiwa na uhakika wa kufika pale ambako taa za gari zilipoonekana. Walitembea kwa mwendo mrefu kupita kawaida. Mwanga ukaanza kutokeza, bado walikuwa wakizidi kutembea. Kila mmoja alionekana kuchoka, masaa mawili walikuwa wameyatumia lakini kitu cha ajabu hawakuwa wameifikia sehemu ile iliyokuwa na magari yale.

    Kila mmoja alionekana kukata tamaa huku wakiona labda walikuwa wamekosea njia. Patrick akaanza kuufuata mti mrefu ambao ulikuwa katikakati ya miti mingi mifupi na kisha kuanza kuuparamia. Alienda juu zaidi na zaidi huku Azizi akimsubiria chini.

    “Inaonekana si mbali sana kutoka hapa” Patrick alimwambia Aziz mara baada ya kuteremka.

    “Unasema kweli?”

    “Ndio. Nimesikia honi kadhaa. Nafikiri si mbali sana kutoka hapa” Patrick alimwambia Azizi na kuendelea na safari yao.

    Miili yao ilikuwa michafu kupita kawaida. Matope yalikuwa yamezitawala suruali zao. Bado waliendelea kupita katika matope lakini hakukuwa na yeyote aliyeonekana kujali. Kwa kipindi hicho, kitu ambacho walikuwa wakikitaka ni kufika Shinyanga Mjini, sehemu ambayo wangetafuta kazi yoyote ya kufanya ili wajiingizie fedha.

    Wakajikuta wakitumia masaa matatu kutoka kilimani mpaka kufika katika sehemu ambayo wakaanza kusikia sauti za watu wakiongea huku wengine wakipiga kelele. Wakaonekana kupata nguvu, wakaanza kupiga hatua za haraka haraka kusogea kule kulipokuwa na kelele zile.

    Wakatokea katika sehemu ambayo ilikuwa na mkusanyiko mkubwa wa watu. Daladala zilikuwa katika kila sehemu mahali hapo. Wakinamama walikuwa wameshika matenga makubwa yaliyokuwa matupu. Utingo wa daladala tofauti walikuwa wakiendelea kuitia abiria ambao walikuwa wakiingia katika magari hayo mmoja baada ya mwingine.

    Jua lilikwishaanza kuchomoza mahali hapo, kitu ambacho walikuwa wakikitaka ni kujua kwamba walikuwa wapo katika kijiji gani na kwa namna gani ambayo wangeweza kufika Shinyanga mjini. Wakapitisha macho yao katika sehemu mbalimbali maeneo hayo, watu walikuwa wakionekana kuwa bize kupita kawaida.

    Kadri sekunde zilivyoendelea kwenda mbele na ndivyo ambavyo idadi ya watu ilipozidi kuongezeka mahali hapo. Macho yao yakatua katika mzee mmoja ambaye alikuwa amesimama nje ya hiace yake huku mkononi akiwa na sigara akivuta. wakaanza kupiga hatua na kumfuata.

    “Tunaomba kuuliza. Hivi hiki ni kijiji gani?” Patrick aliuliza mara baada ya kumsalimia.

    Mzee yule hakujibu kitu, alibaki akiwaangalia kwa macho yaliyoonekana kukasirika, alionekana kutokuwa na haja ya kuwajibu. Hisia zake zote alikuwa amezipeleka katika sigara ile ambayo alikuwa akiingiza moshi mdomoni na kuutoa. Patrick alibaki akimshangaa mzee yule ambaye bado alikuwa akiendelea kuvuta sigara kwa staili ile ile ya kuuingiza moshi na kuutoa hali iliyoonekana kukumpa raha.

    “Tunataka kufika Shinyanga mjini. Nauli shilingi ngapi?” Patrick aliuliza mara baada ya kumuona mzee yule akiwa amenyamaza.

    “Umesema mnataka kufika wapi?” Mzee yule aliuliza huku akionekana kuwa na mshangao.

    “Tunataka kufika mjini” Azizi alijibu.

    “Hivi mnajua huu ni mkoa gani?”

    “Shinyanga” Azizi alitoa jibu ambalo lilionekana kumshangaza mzee yule.

    “Shinyanga! Hapa si Shinyanga” Yule mzee ambaye alikuwa akijulikana kama mzee Masharubu alijibu.

    “Hapa si Shinyanga?”

    “Ndio. Hapa ni Mwanza. Na hapa mko katika kijiji cha Misungwi” Mzee Masharubu alijibu.

    Kila mmoja akaonekana kushtuka, hawakuamini kama masaa nane ambayo walitembea porini, walikuwa wametembea mpaka katika jiji la Mwanza. Kila mmoja akabaki akiwa ameduwaa.

    “Tunataka kwenda mjini” Patrick alimwambia mzee Masharubu.

    “Mna nauli?”

    “Kwani ni shilingi ngapi?”

    “Elfu moja kwa kila kichwa” Mzee Masharubu alijibu.

    Patrick akamvuta Aziz pembeni na kuanza kuongea nae huku yule mzee akiwaangalia. Patrick akaanza kujipekua mfukoni mwake, akajikuta ana shilingi mia mbili tu. Tayari akaona mambo kuwa magumu kwa upande wake. Azizi akajipekua mfukoni, alijikuta kuwa na shili mia nne tu. Jumla walikuwa na shilingi mia sita.

    Tayari waliona ugumu wa kupanda daladala. Wakapanga kwenda kumuomba msaada mzee Masharubu ambaye alionekana kutokuwa na mzaha na kazi yake.

    “Tunaomba utusaidie. Tuna shilingi mia sita” Patrick alimwambia mzee Masharubu kwa sauti iliyojaa unyenyekevu.

    “Shilingi mia sita! Hili gari ni la baba yenu?”

    “Hata ukitushusha njiani, tutashukuru mzee wetu” Patrick alimwambia mzee Masharubu ambaye alibaki akiwaangalia kwa hasira.

    “Hivi mnajua kwa nauli hiyo mtaishia wapi?”

    “Hapana”

    “Nitawashushia Kigongo, kilometa thelathini hadi mjini”Mzee Masharubu aliwaambia.

    “Kilometa thelathini kutoka hapo Kigongo hadi Mjini?” Azizi aliuliza huku akionekana kushtuka.

    “Ndio” Mzee Masharubu aliwaambia.

    Wote wakaonekana kukatishwa tamaa. Walikuwa wametembea porini kwa takribani kilometa themanini, tena kwa kukimbia muda mwingi hadi kufika mahali hapo. Kila mmoja alionekana kuchoka. Kama wangepanda katika daladala hiyo na kushushiwa Kigongo basi ingewachukua kutembea kwa miguu mpaka mjini hali ambayo waliiona kutowezekana kabisa kwa jinsi walivyokuwa wamechoka.

    Walijaribu kumuomba mze Masharubu awasaidie lakini akaonekana kuwa mgumu kufanya hivyo, yeye kitu alichokuwa akikiangalia ni fedha tu. Kama angewasaidia Patrick na Azizi kwa kile kiasi cha fedha ambacho walikuwa nacho basi alijiona angepata hasara sana kwa sababu tu mafuta yalikuwa yamepanda bei.

    “Tunaomba utusaidie mzee” Patrick alimuomba mzee Masharubu ambaye alionekana kukasirika zaidi.

    “Hebu tokeni hapa kabla sijawafanya kitu kibaya” Mzee Masharubu aliwaambia kwa hasira.

    Patrick na Azizi hawakuwa na jinsi, wakaanza kupiga hatua kuondoka mahali hapo kuyafuata magari mengine ambayo yalikuwa yakipakia abiria. Mara wakasikia sauti ya mzee Masharubu akiwata, wakageuka na kumwangalia.

    “Mnasema mnakwenda wapi?” Mzee Masharubu aliwauliza.

    “Mjini” Patrick alijibu.

    “Nitawapelekeni” Mzee Masharubu aliwaambia.

    Uso wa mzee Masharubu ulikuwa ukionekana kuwa na tofauti kubwa. Hasira zote ambazo alikuwa nazo katika kipindi kichache kilichopita hazikuonekana tena, kwa wakati huo uso wake ulikuwa umetawaliwa na tabasamu pana.

    Patrick na Azizi wakaonekana kuishangaa hali ambayo alikuwa nayo mzee Masharubu, hawakujua furaha yake ilikuwa imetokea wapi na wakati kipindi kichache kilichopita alikuwa amefula kwa hasira. Moja kwa moja akawachukua na kuwaingiza katika daladala yake huku akiwa amewaweka katika viti vya pale mbele.

    Muda wote uso wake ulikuwa ukionyesha tabasamu. Akamuita mwanamke ambaye alikuwa akiuza mandazi na kuwanunulia mandazi Patrick na Azizi. Wote wakabaki wakishangaa, kila walipokuwa wakijiuliza juu ya furaha ya ghafla aliyokuwa nayo mzee Masharubu, walikosa jibu.

    “Msijali. Nitawasaidia kama watoto wangu”Mzee Masharubu aliwaambia huku akiongeza zaidi tabasamu.

    Abiria walizidi kuongezeka ndani ya daladala ile. Matenga yaliwekwa juu ya gari lile huku garini kukiwa kumetawaliwa na harufu kali ya shombo ya samaki. Abiria walipojaa ndani ya daladala ile, dereva, mzee Masharubu akawasha gari na kuliondoa mahali hapo. Kadri sekunde zilipokuwa zikizidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo furaha ya mzee Masharubu ilivyozidi kuongezeka.

    “Siamini.........!” Mzee Masharubu alijisemea moyoni huku tabasamu pana likizidi kuonekana usoni mwake.



    *********************************

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Alikuwa na umbo namba nane, uso wake ulikuwa mwembamba. Mwendo wake haukuwa wa kasi, alikuwa akitembea taratibu kana kwamba alikuwa akiogopa kujikwaa. Miguu yake ilikuwa ikimtamanisha kila mtu ambaye alikuwa akimwangalia machoni mwake.

    Uso wake ulikuwa mzuri kiasi ambacho hakukuwa na mvulana ambaye alidiriki kumwangalia mara moja msichana huyu ambaye alionekana kuwa na uzuri wa peke yake. Alipokuwa amenuna, alionekana mzuri, alipokuwa amekasirika bado alikuwa akionekana mzuri, kila alipokuwa akicheka, uzuri wake ulikuwa ukiongezeka maradufu.

    Katika maisha yake alijitambua kwamba alikuwa mzuri na alijua sana kama angepata usumbufu mkubwa kutoka kwa wavulana mbalimbali ambao walikuwa wakiishi mtaani kwao. Mawazo yake ndiyo ambayo yalijenga picha kamili ya baadae. Wavulana wengi walikuwa wakimtaka kimapenzi msichana huyu ambaye alikuwa na vishimo viwili mashavuni mwake, vishimo ambavyo vilikuwa vikionekana kila alipokuwa akicheka au kutabasamu.

    Msichana huyu hakuwa na doa lolote mwilini mwake, aliishi kama yai nyumbani kwao huku akipata malezi ambayo yalimfanya kujitenga kabisa na wavulana. Kusimamishwa na kutongozwa ndio ilikuwa sehemu ya maisha yake ambayo aikuwa akiishi lakini kamwe hakumtukana mwanaume ambaye alikuwa akimtongoza.

    Kila alipokuwa akiambiwa maneno matamu ya mapenzi, alibaki akicheka na kutabasamu tu hali ambayo iliwapa moyo wavulana wengi, lakini kitu cha ajabu, jibu lake lilikuwa tofauti na tabasamu lake. Wavulana walitumia njia zote kuwa na msichana huyu shuleni lakini hakukuwa na mvulana yeyote ambaye alibahatikia kuwa rafiki yake.

    Wanafunzi wengi wa kiume walikuwa wakitembelea shule ya sekondari ya Mbezi High huku sababu kubwa ikiwa ni kutaka kumuona msichana huyu ambaye alikuwa akisifika kwa uzuri kuliko msichana yeyote katika shule zote za Dar es Salaam.

    Msichana huyu alikuwa akivutia kupita kawaida, alionekana kama msichana wa ndoto ambaye wala hakuwa akiishi katika ulimwengu huu. Kila mvulana ambaye alibahatika kukutana nae, hakika alikiri nafsini mwake kukutana na msichana mzuri ambaye kamwe asingeweza kukutana na msichana kama huyo maishani mwake.

    Alijipenda na kujithamini, hakutaka kumpa mvulana mwili wake auchezee. Muda mwingi alikuwa akishinda chumbani kwake akijisomea hali ambayo ilikuwa ngumu sana kumuona mitaani. Halikuwa jambo la kushangaza kama tu wavulana wa mtaani kwao walikuwa wakimuona msichana huyo mara moja kwa wiki.

    Kila siku alikuwa akiepelekwa shuleni kwa gari na kurudishwa na gari. Ni mara chache sana alikua akielekea dukani, sehemu ambayo wanaume walipata nafasi kumsimamisha na kuanza kuongea nae.

    Wavulana walikuwa wakigombana mitaani kwa sababu yake ingawa hakukuwa na mvulana yeyote ambaye alibahatika hata kumshka mkono wake. Misele nyumbani kwao haikuisha, kila siku wavulana walikuwa wakipitapita nyumbani kwao ili mladi tu kumuona.

    Msichana huyu alipata wakati mgumu pale alipofungua akaunti yake katika mtandao wa Facebook. Ingawa hakuwa ameweka picha yake, watu wengi walikuwa wakimuomba urafiki kiasi ambacho alipata marafiki zaidi ya elfu tano ndani ya mwezi mmoja tu huku idadi kubwa ikiwa wavulana.

    Kila siku wavulana walikuwa wakimtumia meseji mbalimbali za kumtaka kuweka picha yake kwani wao walikuwa wakisikia sifa zake tu. Akaamua kuiweka picha yake ambayo kwake yeye aliiona kuwa picha mbaya kuliko zote.

    Picha ile ikaonekana kuleta kizaazaa, kila mvulana alikuwa nayo katika kompyuta yake huku wengne hadi wakiiweka katika simu zao. Alionekana kuwa na uzuri wa tofauti kabisa kabisa, alionekaa kuwa kama mwanadamu ambaye hakuzaliwa katika dunia hii.

    Alilelewa vizuri na wazazi wake. Baba yake alikuwa mchungaji wa kanisa la Praise And Worship lililokuwa Kinondoni alipokuwa akiishi huku mama yake akiwa Mhasibu katika Benki ya CRDB. Msichana huyu alikuwa akiishi katika mazingira ya dini, Biblia ndicho kikawa kitabu ambacho alikuwa akikipenda sana kukisoma.

    Kila siku alikuwa mtu wa kusali chumbani kwake akimuomba Mungu Awe nae katika maisha yake, Amlinde na kumuongoza katika njia ambayo alipaswa kwenda. Dini ndio ambayo ilikuwa ikimuongoza msichana huyu ambaye kadri siku zilivyokuwa zikiendelea kwenda mbele na ndivyo uzuri wake ulivyozidi kuongezeka.

    *****

    Bado safari ya kuelekea Mwanza Mjini ilikuwa inaendelea. Muda wote mzee Masharubu alikuwa akionekana kuwa na furaha. Utajiri ulionekana kuanza kumnyemelea, maisha ya kimasikini ambayo alikuwa akiishi aliyaona kuwa na mwisho wake siku hiyo.

    Mara baada ya kufika Mjini, moja kwa moja akawachukua Patrick na Azizi na kuanza kuelekea nao katika mghahawa ambao ulikuwa karibu kwa ajili ya kupata kifungua kinywa pamoja nao. Patrick na Azizi bado walikuwa wakiendelea kujiuliza maswali vichwani mwao juu ya furaha ambayo alikuwa nayo mzee Masharubu lakini hawakupata jibu lolote lile.

    “Mnataka kazi?” Mzee Masharubu aliwauliza mara baada ya kumaliza kunywa chai.

    “Ndio. Tunahitaji kazi mzee, tunaomba utusaidie” patrick alimwambia mzee Masharubu huko nyuso zao zikionyesha kweli kwamba walikuwa wakihitaji kazi.

    Mzee Masharubu akaanza kuondoka nao kuelekea nao pembezoni mwa ziwa Viktoria, katika sehemu ambayo ilikuwa na mitumbwi mingi. Akawaambia wasubiri nje ya kibanda ambacho yeye akaingia ndani na baada ya muda, akatoka huku akiongozana na mwanaume mmoja aliyekuwa na ndevu nyingi nyeupe.

    Mzee yule akaanza kuwaangalia na kujitambulisha kuwa aliitwa mzee Baku, mzee maarufu ambaye alikuwa akimiliki mitumbwi mingi ya kuvulia samaki usiku. Akawahakikishia kuhusu kazi ambazo walitakiwa kufanya na kupewa malipo mazuri.

    Patrick na Azizi hwakuonekana kuamini hata kidogo, kupata kazi kwa haraka sana kulionekana kuwafurahisha kupita kiasi. Wakabaki wakikumbatiana kwa furaha, hawakuamini kama nao walikuwa wakielekea kufanya kazi na kuanza kulipwa mshahara.

    Mara baada ya utambulisho ule, mzee Masharubu na mzee Baku wakarudi ndani ya kibanda kile huku wakiwaacha Patrick na Azizi wakiwa na furaha kubwa kupita kiasi. Wakaelekea mpaka katika chumba ambacho waliamini hakukuwa na mtu ambaye alkuwa akiwasikia.

    “Kwa hiyo? Nimekuletea mizigo miwili ya bureeee...” Mzee Masharubu alimwambia mzee Baku.

    ”Chukua milioni mbili kwanza” Mzee Baku alimambia.

    “Acha biashara ya kitoto wewe. Kwani nimekuletea gunia la mkaa hapa!”

    “Nitakupa nyingine baada ya kazi kufanyika”

    “Mtaifanya lini sasa?”

    “Leo usiku”

    “Sawa”

    Hayo yalikuwa mangezi mafupi ambayo yalikuwa yameongelewa ndani ya chumba kile. Walipokubaliana, mzee Masharubu akatoka na kuondoka huku akiwaacha Patrick na Azizi wakiwa kama waajiriwa wapya katika sehemu hiyo ambayo ilihusika katika uvuvi wa samaki katika ziwa hilo.

    Mzee Baku alijitahidi kufanya kila kitu ambacho kilikuwa kinawezekana kuwafanyia ili wasiweze kugundua ni kitu gani ambacho kilikuwa kinaendelea mahali hapo. Kila mfanyakazi ambaye alifika mahali hapo, Patrick na Azizi walitambulishwa kama wafanyakazi wapya.

    Uchangamfu ambao ulitolewa kwao na wafanyakazi wengine kuliwafanya kujisahau kabisa, wakaonekana kumzoea kila mtu kupita kawaida, hawakuwa na hofu hata kidogo, walimuona kila mfanyakazi kuwa kama ndugu zao ambao walitoka nao kutoka Shinyanga.

    Siku hiyo ilionekana kuwa ya furaha kwao, walikula na kunywa mpaka kuacha chakula. Hawakuwahi kuishi maisha ya furaha katika maisha yao kama siku hiyo. Walijisikia kuwa katika hali ya tofauti sana ambayo wala hawakuwa wameitegemea kabla.

    Muda ulizidi kwenda mbele, huku masaa yakizidi kusogea. Wote walitaarifiwa kwamba kazi ingeanza siku hiyo hiyo. Ili kuwavutia zaidi kazini, mzee Baku akawagaiwia shilingi elfu tano kila mmoja, fedha ambazo zilizichanganya akili zao kupita kiasi.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Walitaarifiwa kwamba nao walitakiwa kwenda ziwani usiku kwa ajili ya kuvua samaki pamoja na wavuvi waliokuwa chini ya mzee Baku. Ingawa mara ya kwanza walikuwa akiogopa, waliwekwa chini na kutolewa woga wote waliokuwa nao.

    “Kwanza hakikisheni wanapanda mitumbwi tofauti” Mzee Baku aliwaambia vijana wake.

    “Ndio”

    “Na hakikisheni wasijue kitu chochote kile. Mganga alikuja na kunipa hii dawa. Kazi inatakiwa kufanyika haraka iwezekanavyo. Damu zao zinahitajika sana” Mzee Baku aliwaambia.

    “Sawa mzee”

    Vijana wale wakaondoka na kuelekea nje ya nyumba ile ambako wakaachukua Patrick na Azizi na kuwapa makoti mazito. Wakapandishwa katika mitumbwi tofauti na kisha safair ya kuanza kuelekea ziwani kuanza.

    Lugha ambayo ilikuwa ikitawala mahali hapo ni Kisukuma, lugha ambayo Patrick na Azizi hawakuelewa kabisa. Mitumbwi ikazidi kwenda zaidi na zaidi huku wakiziandaa nyavu zao kwa ajili ya kuzitupia ziwani. Taa zao za chemri zilikuwa zikiendelea kuwaka katika boti zile ambazo ziliuwa mbali mbali.

    Kisukuma kilizidi kuongelewa mtumbwini mule, Patrick hakuwa akielewa kitu chochote kile. Nyavu zikashushwa, kijana mmoja akachukua mfuko wa nailoni ambao ulikuwa na vitu kadhaa ndani yake. Patrick alikuwa akifuatilia kila kitu, hakuonekana kuwa na wasiwasi wowote ule, alionekana kumuamini kila mtu mtumbwini humo.

    Mtumbwi ulifika mbali sana, kila upande ambao alikuwa akiangalia hakuona kitu. Mtumbwi ambao alikuwa Azizi pamoja na wavuvi wengine haukuwa ukionekana tena machoni mwake. Patrick akanza kuogopa, hali ya kutisha ziwani ikaonekana kuanza kumtia hofu.

    Mawimbi yalikuwa yakipiga kwa mbali, hali ya ziwa ilionekana kuwa nzuri kuliko siku nyingine ambapo maimbi makubwa yalikuwa yakipiga. Wavuvi wale walikuwa wakimwangalia Patrick ambaye tayari alikuwa akionyesha wasiwasi mkubwa.

    Kwa kutumia mwanga wa mwezi walikuwa wakionana vizuri katika mtumbi ule. Uso wa Patrick ambao ulikuwa umejaa wasiwai ulikuwa ukionekana vizuri kwa kila aliyekuwa akimwangalia. Mvuvi yule ambaye alichukua mfuko ule wa nailoni akaufungua na kutoa kikaratasi kimoja ambacho kilionekana kufungwa vitu fulani kwa ndani.

    Ndani ya kikaratasi kile kulikuwa na unga mweusi. Akaumimina mkononi mwake na kisha kuanza kuongea maneno ya taratibu kwa sauti ya chini ambayo alihakikisha hakukuwa na mtu yeyote ambaye angeweza kumsikia. Alipomaliza, akayapeleka macho yake usoni mwa Patick. Kwa kasi ya ajabu, akampulizia unga ule machoni na kisha kumsukuma ziwani.

    Patrick akaanza kutapatapa kwa kurusha mikono yake katika kila upande. Kila alipotaka kuzama, alijitahidi kuulegeza mwili wake na kubaki juu. Mtumbwi ule ulikuwa umekwishaondoka mahai pale. Patrick alikuwa akipiga kelele lakini hakukuwa na dalili ya mtu yeyote au mtumbwi ziwani pale.

    Patrick akaanza kuchoka, baridi lilikuwa likimpiga kupita kiasi. Akaonekana kukubaliana na hali ambayo ilikuwa ikimkumba mahali pale, ghafla akaanza kuzama. Patrick alijaribu kujirudisha juu lakini hakuweza, alizidi kuzama kwenda chini zaidi mpaka pale alipoanza kujiona akiishiwa pumzi.

    Macho yake yakaanza kupoteza muelekeo, mara akaanza kuona giza na baada ya sekunde kadhaa, hakujua kitu chochte ambacho kiliendelea baada ya hapo, alikuwa nusu ya mfu.









    *****









    Kijana Hidifonce alikuwa akionekana kijana mtanashati kuliko vijana wote ambao walikuwa wakiishi Kinondoni. Kila siku alikuwa akionekana msafi pasipo kujalisha kama alikuwa akikaa nyumbani au alikuwa akielekea ofisini.

    Hakuwa mtu wa kushinda nyumbani, kazi ya uasibu ambayo alikuwa akiifanya bandarini ndio ambayo ilikuwa ikimfanya kuwa bize kupita kiasi. Muda wake wa kukaa nyumbani ulikuwa ni Jumamosi na Jumapili tu. Kila kitu ambacho kilikuwa kikitokea mtaani kwao wala hakuwa akipata taarifa.

    Ingawa muda mwingi alikuwa akiutumia kazini lakini Hidifonce alikuwa akijitahidi kuongea na vijana wenzake hasa alipokuwa akirudi nyumbani.

    Utanashat wake pamoja na ucheshi ambao alikuwa nao ulimfanya kupata marafiki wengi mtaani kwao ambao mara kwa mara alikuwa akikaa nao na kubadilishana mawazo.

    Hakuwa na mpango wa kuoa katika kipindi hicho, bado alihitaji muda wa kukaa peke yake zaidi, wasichana hawakuwa sehemu ya maisha yake kwani kila alipokuwa akielekea kazini, alikuwa akikutana nao na ambao walikuwa wazuri kuliko wale ambao alikuwa amewazoea kuwaona mtaani.

    Kila alipokuwa akikaa na marafiki zake alikuwa akilisikia jina la msichana mmoja likitajwa sana katika midomo ya vijana hao, msichana huyu alikuwa Mary Christopher, binti wa mchungaji Christopher wa kanisa la Praise And Worship lililokuwa Kinondoni.

    Sifa zilikuwa nyingi kiasi ambacho nae akatamani kumuona msichana huyo ambaye alikuwa ameteka mioyo ya vijana hao. Kushinda ofisini na kurudi usiku ndiko ambako kulimfanya kutokumuona msichana huyo ambaye aliuhisi uzuri wake kuwa mkubwa kupita kiasi.

    Kila siku alikosa raha kila alipokuwa akisikia sifa za Maria. Akaanza kumtengeneza Maria wake kichwani kwake, umbo zuri la kuvutia pamoja na sura nzuri ilikuwa ni picha nzuri ya Maria ambayo aliitengenaza kichwani mwake.

    Kila Jumamosi na Jumapili ambazo alikuwa akishinda nyumbani, Maria hakuwa akionekana mtaani jambo ambalo lilimfanya kila siku kuwa na shauku ya kumuona Maria. Tayari akili yake aliiona kuanza kumpenda msichana ambaye wala hakuwa amemuona machoni mwake.

    Siku ziliendelea kukatika huku Maria akizidi kuzungumziwa kila siku. Kila siku Hidifonce ambazo alikuwa akirudi kutoka nyumbani, sifa za Maria zilikuwa zikiongezeka. Hakuwa na jinsi hali iliyompelekea nae kuanza kwenda kanisani katika kanisa lile ambalo alikuwa akisali Maria.

    Huko napo wala haikuwezekana kumuona Maria, kwa kuwa alikuwa muimbaji wa kikund kimoja cha kwaya kanisani hapo, hakuwa akionekana kwa urahisi kwani mara kwa mara walikuwa wakiitwa katika makanisa mengine kwa ajili ya kumsifu Mungu.

    Hidifonce bado alionekana kuchanganyikiwa, kiu aliyokuwa nayo ya kutaka kumuona Maria iliendelea kumkamata kila siku. Macho yake yalikuwa na kiu ya kutaka kumuona Maria ambaye alisadikiwa kuwa mzui kuliko wasichana wote ambao walikuwa wakiishi Kinondoni.

    “Unasema haujawahi kumuona Maria?” Kijana mmoja alimuuliza Hidifonce ambaye alikuwa pamoja nao.

    “Ndio. Kwani yuko vipi? Uzuri wake uko vipi?’ Hidifonce aliuliza.

    “Hauelezeki. Yaani kama nikikwambia ni mzuri sana naona kama nakudanganya. Yeye ni mzuri hata zaidi ya sana” kijana yule alitoa jibu ambalo lilimfanya Hidifonce kuwa na hamu zaidi ya kumuona Maria.

    Hidifonce alikuwa akijilaumu pasipo kuwa na sababu, kitendo cha kutokumuona Maria machoni mwake kilionekana kuwa kama kosa kubwa ambalo hakuwahi kulifanya maishani mwake. Akaanza kujitahidi kurudi nyumbani apema ili mladi tu amuone Maria lakini napo haikuwezekana.

    “Maria mwenyewe huyo hapo” kijna mmoja alisikika akiwaambia wenzake.

    Kwa kasi ya ajabu, Hidifonce akayainua macho yake na kumwangalia Maria. Mapigo ya moyo wake yalikuwa yakidunda kwa kasi kutokana na mzunguko wa damu yake kuwa mkubwa. Hidifonce hakuonekana kuamini kabisa kama msichana ambayealikuwa akipita mbele yake alikuwa binadamu au malaika ambaye alishushwa duniani.

    Mshtuko ukampata Hidifonce, macho ya Maria yalikuwa hayajatoka usoni mwake. Walibaki wakiangaliana kwa muda huku Maria akiendelea kupiga hatua kulifuata geti la nyumba yao. Hidifonce hakujua ni kitu gani ambacho kilikuwa kinaendelea, Maria akalifungua geti na kabla hajalifunga, akayapeleka macho yake usoni mwa Hidifonce na kisha kufunga geti.

    Kila mmoja alibaki akiwa ameduwaa. Hawakuelewa ni kwa nini Maria na Hidifonce walikuwa wakiangaliana namna ile, tena katika mwangalio ambao ulikuwa umejaa mahaba mazito. Hidifonce alibaki kimya kwa muda huku akianza kumfikiria Maria.

    Kabla ya kumuon Maria, tayari alikuwa amemtengeneza Maria mzuri kichwani mwake lakini kwa Maria ambaye alikuwa amemuona, alikuwa mzuri hata zaidi ya Maria yule ambaye alikuwa amemtengeneza kichwani mwake.

    “Mbona umeangaliwa sana Hidifonce?” Hamidu alimuuliza Hidifonce.

    “Hata mimi mwenyewe nashagaa. Labda ananifahamu” Hidifonce alijibu.

    “Hilo si tatizo, na wala sina tatizo na kukuangali. Ila mimi najaribu kuutafakari ule muangalio. Macho yalikuwa yamekaa kimahaba kabisa alipokuwa akikuangalia” Hamidu alimwambia Hidifonce.

    Siku ziliendelea kukatika. Hidifonce hakuweza kumuona tena Maria ingawa moyo wake ulikuwa na hamu kubwa ya kumuona. Majukumu kazini yalikuwa yamembana kupita kiasi. Kila siku muda wake wa kurudi nyumbani ulikuwa usiku.

    “Nitamtafuta tu, nimetokea kumpenda sana binti huyu” Hidifonce alijisemea.





    ******************************************************





    ****** Je nini kitaendelea?





    ******* Je huo ndio mwisho wa Patrick ziwani Victoria?





    *******Je Siwema atapona au ndio mwisho wake?





    ******* Je kijana Hidifonce ataweza kumuona Maria? Na Bwana Mayemba ataweza kufunga ndoa na Bi Anna?

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    *****ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog