IMEANDIKWA NA : CARRY CARLOS
*********************************************************************************
Simulizi : Painful Memories
Sehemu Ya Kwanza (1)
Jua lilikuwa linachomoza katika kipindi ambacho kijana Edmund alikuwa akiamka kutoka kitandani kwake. Mwanga wa jua ambao ulikuwa ukipenya ndani kupitia dirishani ndio ambao ulimshtua kutoka usingizini. Akaamka na kisha kukaa kitandani huku macho yake akiyapeleka katika saa ya ukutani, ilikuwa saa moja na robo asubuhi.
Edmund akainuka na kuanza kujiangalia kwenye kioo kilichokuwa chumbani mule, alijiona kuwa vile vile pasipo kuwa na mabadiliko yoyote yale, uso wake bado ulikuwa ukionekana kutokuwa na furaha hata kidogo. Akachukua taulo alilolitundika katika msumali mlangoni na kisha kulivaa. Akauchukua mswaki wake ambao aliuweka dirishani, akachota maji kwenye ndoo ndogo iliyokuwa hapo chumbani na kisha kuelekea bafuni kupiga mswaki.
Baba mwenye nyumba wake, mzee Hamadi akaonekana kukasirika, hakuonekana kumpenda kabisa Edmund, kila siku alikuwa akimchukia kupita kiasi. Ucheleweshaji wa ulipaji wa kodi ndani ya nyumba yake ndio ambao ulimfanya kumchukia Edmund kupita kawaida. Kwake, Edmund alionekana uwa msumbufu sana ambaye hakulipa kodi katika muda muafaka.
Japokuwa Edmund alikuwa amemuahidi kumlipa fedha zake ndani ya wiki inayofuatia lakini mzee Hamadi hakuonekana kuridhika kabisa, alizihitaji fedha zake zaidi ya kitu chochote kutoka kwa Edmund. Mzee Hamadi hakuyatoa macho yake kwa Edmund, alikuwa akimwangalia mpaka pale ambapo akapotea machoni mwake mara baada ya kuingia bafuni.
“Hii mijitu mingine inakera sana. Yaani akinilipa, sitaki tena aendelee kukaa ndani ya nyumba yangu” Mzee Hamadi alijisemea huku akipiga hatua kuelekea chumbani kwake.
Huyu alikuwa kijana mwenye sura ya upole ambaye alikuwa mkimya kupita kawaida, Edmund Zilikana. Edmund alikuwa kijana masikini, hakuwa na fedha za kutosha kabisa kutokana na maisha yake kutegemea kazi ndogo ndogo ambazo alikuwa akizifanya hasa sokoni Tandale.
Kila siku alikuwa mtu wa kuamka asubuhi na kuelekea sokoni ambako huko alikuwa akipata nafasi ya kubeba magunia ya nafaka mbalimbali ambayo yalikuwa yakiletwa sokoni kwa magari makubwa ya kubebea mizigo. Sokoni huko ndipo ambapo alipokuwa akibeba magunia hayo na kupata kiasi cha fedha ambacho kilikuwa kikiyaendesha maisha yake ya kila siku.
Kwa wakati huo alikuwa akiishi peke yake, wazazi wake walikuwa wamekwishafariki na wala hakuwa na ndugu yeyote ndani ya jiji la Dar es Salaam. Kila siku alikuwa akijitahidi kupigana na maisha magumu ambayo yalikuwa yakimkabiri maishani mwake. Alitamani sana kupata mafanikio ambayo yangemuwezesha kukaa chini na kula chakula kizuri kama ambavyo watu wengine walivyokuwa wakifanya.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Fedha, kwake ikaonekana kupotea, tangu kuzaliwa kwake, hakuwahi kushika hata kiasi cha shilingi laki mbili na kujivunia kwamba fedha ile ilikuwa yake. Maisha kwake yakaonekana kuwa kama jehanamu. Alijua fika kwamba ili kujiondoa katika maisha hayo magumu ilimpasa kupigana kwa nguvu zote.
Kila siku alikuwa akiendelea kupigana na maisha magumu lakini hali wala haikuonekana kubadilika. Hapo ndipo alipouona ubaya wa kuwa masikini, hapo ndipo alipoanza kuuchukia umasikini ambao ulionekana kumshusha thamani kwa kiasi kikubwa sana. Kila alipokuwa akipita, alijiona kutokuthaminiwa, alitamani kuwa na maisha mazuri ambayo yangejumuisha kuwa na nyumba yake mwenyewe, gari lake mwenyewe na hata kuwa na mwanamke mzuri ambaye angeweza kutengeneza familia pamoja nae.
Kila kitu ambacho alikuwa akikihitaji kikaonekana kuwa kama ndoto kukipata, alimuona Mungu kumtenga, kila siku lawama zake zilikuwa kwa Mungu kwa kumuumba katika dunia hii ambayo ilijaa mateso makali. Pamoja na kuwa na maisha hayo yote lakini kamwe Edmund hakutaka kukata tamaa, kila siku aliendelea kupigana japokuwa hakuonekana kuushinda umasikini.
Sokoni Tandale ambapo ndipo alipokuwa akifanyia kazi ya kubeba magunia napo kukaonekana kuwa na tabu. Mara kwa mara ugomvi ulikuwa ukitokea hasa katika kipindi ambacho magari yalikuwa yakifika katika soko hilo. Kila mbebaji alikuwa akitaka kubeba mizigo ambayo ilikuwa ikishushwa katika magari hayo.
Kila siku maisha yalionekana kuwa magumu na yalizidi kuwa magumu zaidi na zaidi. Alipokuwa akirudi nyumbani usiku na kulala, mwili wake ulikuwa ukichoka kupita kawaida. Kiasi cha fedha ambacho alikuwa akikipata alikuwa akikigawa sehemu mbili tu. Sehemu ya kwanza ilikuwa ni kwa ajili ya chakula na sehemu nyingine ilikuwa ni kwa ajili ya kodi.
Hakuona haja ya kununua nguo nyingi. Angezivaa wapi? Wakati gani na wakati alikuwa akiondoka asubuhi na kurudi usiku tena akiwa ametoka kubeba magunia ambayo yalikuwa yakimchosha kupita kawaida? Asilimia kubwa ya maisha yake kwa siku alikuwa akiyatumia kuwa sokoni ambako alikuwa akiendelea kufanya kazi zake kama kawaida.
Elimu yake ya kidato cha nne haikuonekana kumsaidia hata mara moja. Alijaribu kutafuta kazi sehemu mbalimbali lakini wala hakufanikiwa, kazi nyingi ambazo zilikuwa zikitangazwa zilikuwa zikichukuliwa na ndugu wa wafanyakazi wa kampuni au ofisi husika. Katika maisha yake, alijiona kuwa mtu mwenye bahati mbaya ambaye wala hakuwa na bahati yoyote ile.
“Utanibebea kwa shilingi ngapi hapa mpaka Kwa Mtogole?” Mwanamke mmoja alimuuliza Edmund huku gunia la mchele likiwa mbele yake.
“Elfu saba” Edmund alijibu huku akiliangalia gunia lile lililokuwa na uzito wa kilo mia moja.
“Mbona nyingi hivyo?”
“Si unaona mzigo wenyewe mama. Kilo mia moja hiyo” Edmund alimwambia mwanamke yule huku akilishika shika lile gunia.
“Hata kama kijana wangu. Hiyo ni fedha nyingi sana” Mwanamke yule alimwambia Edmund.
“Sawa. Wewe una shilingi ngapi mama yangu?”
“Elfu tano”
“Da! Sawa. Acha nikubebee” Edmund alimwambia yule mwanamke na kisha kuwaita marafiki zake ambao walimsaidia kumtwisha mzigo ule na safari ya kuelekea mtaa wa kwa Mtogole kuanza.
Mzigo ule ulikuwa mzito sana, mwendo wa Edmund ulikuwa ni wa haraka sana kwani aliamini asingeweza kuchoka haraka. Kutokana na mwendo wa Edmund kuwa wa haraka haraka, mwanamke yule alikuwa mbele huku akikimbia kimbia. Kutoka pale sokoni mpaka katika nyumba hiyo ambayo alitakiwa kuufikisha mzigo huo walitumia dakika kumi, wakafika na kuingia ndani.
Edmund alikuwa akihema kwa nguvu kana kwamba alikuwa ametoka kukimbia mbio ndefu. Akaomba maji na kuletewa na kijana wa mwanamke yule. Alipomaliza kunywa maji, akaanza kulivuta gunia lile la mchele mpaka sehemu husika na kisha kuaga.
Hayo ndio yalikuwa maisha yake ya kila siku, kubeba mizigo mikubwa kutoka sehemu moja kwenda nyingine alionekana kuyazoea japokuwa hakuwa akiyapenda kabisa. Siku ile ndio ikawa mwanzo wa mazoea kati yake na mwanamke yule ambaye alijitambulisha kama Mama Hussein japokuwa alikuwa akipenda sana kuitwa Bi Husna.
Mara kwa mara Bi Husna alipokuwa na mzigo ambao ulikuwa ukihitaji mbebaji alikuwa akimtafuta Edmund ambaye alikuwa akiubeba mzigo huo. Ukaribu huo ukaanza kuwa wa karibu zaidi, Edmund akaanza kumuona Bi Husna kuwa kama mama yake wa kumzaa huku Bi Husna akimuona Edmund kuwa kama mtoto aliyetoka tumboni mwake.
Siku ziliendelea kukatika, wiki zikaendelea kusogea huku nayo miezi ikiendelea kusonga mbele. Bi Husna akaonekana kuvutiwa na ufanyaji wa kazi wa Edmund jambo ambalo alilimfanya kutamani sana kukaa nae chini na kuongea nae juu ya jambo moja. Kila siku alipokuwa akitaka kumwambia Edmund, aliona kwamba huo haukuwa muda sahihi wa kufanya hivyo, alijiona kuhitaji kuvuta subira.
Siku ambayo alipanga kumwambia juu ya jambo hilo ikafika, alichokifanya ni kumuita Edmund na kisha kukaa nae sebuleni. Muda wote macho yake yalikuwa yakimwangalia Edmund kana kwamba alikuwa akimchunguza au alikuwa akitafuta mapungufu fulani mwilini mwa Edmund.
“Umekula?” Bi Husna aliuliza.
“Ndio” Edmund alijibu.
“Umeshiba?”
“Ndio”
“Sawa” Bi Husna aliitikia na kisha kuanza kumwangalia Edmund usoni.
“Hautakiwi kuishi maisha hayo Edmund. Unahitaji kuwa na maisha bora zaidi ya hapo. Kuna kitu nimekifikiria juu yako” Bi Husna alimwambia Edmund ambaye akajiweka vizuri kochini.
“Kitu gani?”
“Kukutafutia kazi. Kazi ambayo inaweza kuyasaidia maisha yako na kuyaweka kwenye unafuu” Bi Husna alimwambia Edmund.
“Sawa. Nitashukuru sana”
“Elimu ya Sekondari si unayo kama ulivyoniambia?”
“Ndio”
“Basi sawa. Nitajaribu kuongea na mdogo wangu na nitakwambia anasemaje juu ya hilo” Bi Husna alimwambia Edmund.
Tangu mwaka huo uanze, siku hiyo ndio ambayo ilionekana kuwa ya furaha kuliko siku zote, kitendo cha Bi Husna kumuahidi kumuombea kazi kilionekana kumpa faraja. Njia nzima alikuwa akifikiria kuhusiana na kazi ambayo alikuwa akienda kutafutiwa, alimuomba Mungu kwamba iwe kazi bora ambayo ingeyabadilisha maisha yake na kumfanya kuishi kama ambavyo alitaka kuishi kila siku.
Hakutaka kuendelea kubaki sokoni, alichokifanya ni kuanza kuelekea nyumbani. Alipofika akaingia chumbani kwake na kutulia. Akaanza kumfikiria Bi Husna, alionekana kuwa mwanamke ambaye alikuwa na malengo makubwa na maisha yake, akaona kulikuwa na sababu zote za kuanza kumthamini na kumsikiliza mwanamke yule.
Siku zikakatika lakini Bi Husna alikuwa kimya, hakuonekana kabisa machoni mwa Edmund. Kila siku Edmund alikuwa mtu wa kuangalia huku na kule sokoni na hata kwenda nyumbani kwake lakini napo Bi Husna wala hakuonekana. Jambo lile likamfanya Edmund kukosa amani, furaha ikatoweka moyoni mwake.
Akili yake ikaanza kufikiria mambo mengine, jambo la kwanza ambalo alikuwa amelifikiria kuhusiana na Bi Husna ni kwamba mwanamke yule alikuwa akitaka kujionyesha kwake kwamba alikuwa na uwezo mkubwa wa kuyabadilisha maisha yake na kuyaweka kama vile ambavyo alitaka yawe. Kila kitu ambacho alikuwa akikifikiria juu ya Bi Husna kilionekana kuwa kitu kibaya, akaonekana kuanza kuutoa uaminifu wake kwa mwanamke yule.
Siku zikaendelea kukatika mpaka kufikia siku ambayo Bi Husna akaja tena kuonekana machoni mwake. Edmund akaonekana dhahiri kukata tamaa, hakutarajia kama angeweza kumuona tena Bi Husna. Alichokifanya Bi Husna ni kumuita na kuanza kuongea nae japokuwa mwanamke huyo alionekana kuwa na haraka.
“Jiandae. Kesho saa mbili asubuhi inabidi tuwe sehemu husika. Vaa vizuri, hakikisha una kopi za cheti chako na kitambusho cha kupigia kura. Wahi. Nipitie nyumbani mapema” Bi Husna alimwambia Edmund na kuondoka mahali hapo.
Edmund hakutaka kuendelea kubaki sokoni, alichokifanya ni kuondoka mahali hapo na kuelekea nyumbani ambako akaingia chumbani na kujilaza. Swali la kwanza ambalo lilimjia kichwani mwake ni juu ya sehemu ambayo angeweza kupata nguo za kuvaa kwa ajili ya kuelekea huko ofisini. Aliyakumbuka maneno ya Bi Husna ambayo yalimtaka kuvaa vizuri, hakujua ni nguo gani ambazo angezivaa.
“Gilbert. Yeah!” Edmund alijisemea.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/Hapo hapo akasimama na kuanza kutoka nje ya chumba kile na safari ya kuelekea nyumbani kwa rafiki yake, Gilbert kuanza. Lengo la kwenda kwa rafiki yake huyo lilikuwa moja tu, kuazima nguo ambazo angezivaa tayari kwa kuanza safari ya kueleka katika sehemu ambayo aliambiwa aende pamoja na Bi Husna.
Usiku hakulala. Alibaki akiyaangalia mavazi ambayo alikuwa ameyaazima kwa Gilbert. Toka azaliwe hakuwahi kuvaa tai, ila mavazi yale ambayo alikuwa ameyaazima yalikuwa yamejumuisha na tai. Alibaki akitabasamu, hakujua angependeza namna gani siku inayofuata.
Asubuhi na mapema akaamka, akajiandaa na kisha kuelekea nyumbani kwa Bi Husna ambaye akamkuta tayari amkwishajiandaa. Akamsalimia na kisha wote kuanza kuelekea kituoni ambako wakachukua daladala huku lengo lao likiwa ni kuelekea Posta.
Safari ilichukua dakika ishirini, wakasimama nje ya jengo moja kubwa ambalo lilikuwa na bango kubwa lililoandikwa PHOTOMANIA IMAGE EFFECT kwa nje. Wakaanza kuingia ndani ya jengo lile na kuelekea katika sehemu ya mapokezi.
“Karim nimemkuta?” Bi Husna alimuuliza dada wa mapokezi mara baada ya salamu.
“Nani? Bosi? Ndio yupo” Msichana yule alijibu na kisha Bi Husna na Edmund kuanza kuelekea ndani ya ofisi ya Karim.
Wakakaribishwa vizuri na kutulia katika viti. Wakaanza kuongea mambo tofauti tofauti huku Karim akionekana kuwa mchangamfu muda wote. Edmund alionekana kutokujiamini kama alikuwa ndani ya ofisi kubwa na nzuri kama ile hali ambayo ilimfanya Karim kuligundua hilo.
“Karibu Edmund” Karim alimkaribisha Edmund huku akitoa tabasamu.
“Asante”
“Hii ni kampuni ambayo inashughulika sana na upigaji picha mbalimbali hasa za wasichana warembo na wanamitindo, tunashughulika pia na upambaji wa harusi, kukodisha mavazi pamoja na mambo mengi tu” Karim alimwambia Edmund kama kumpa taarifa juu ya mahali alipokuwa huku Edmund akitikisa kichwa chake juu na chini.
“Niliongea na dada yangu na kunieleza kuhusu wewe. Nimefahamu mengi kuhusu wewe kupitia yeye. Usijali hata kidogo, kazi zipo tena nyingi tu ila inategemea wewe unataka kazi gani” Karim alimwambia Edmund huku tabasamu pana likizidi kuonekana usoni mwake.
“Yoyote tu” Edmund alijibu.
“Acha utani Edmund. Kuna kazi nyingine hazitakiwi kufanywa na mtu kama wewe hasa uliyefika Sekondari. Unaweza kuchagua kati ya kazi hizi na kuniambia ungependa kazi gani” Karim alimwambia Edmund huku akimpa karatasi ilikuwa na orodha ya kazi tofauti tofauti.
Edmund akaanza kuiangalia karatasi ile kwa makini huku akiisoma kazi moja baada ya nyingine. Muda huo Karim alikuwa akiongea mambo mengine na Bi Husna. Edmund alikuwa kwenye utulivu mkubwa sana, alipomaliza, akamrudishia Karim karatasi ile.
“Namba tatu”
“Sekta ya kufanya usafi. Sawa” Karim alimwambia Edmund.
Hiyo ndio ilikuwa siku ya kwanza kwa Edmund kuingia katika ofisi kubwa na nzuri kama ile. Siku iliyofuata akatakiwa kufika ofisini hapo ambapo makubaliano ya mshahara yakafanyika na kisha kuanza kazi rasmi.
Edmund akaamua kujituma na kuipenda kazi yake, bado alionekana kuwa na hasira na umasikini ambao ulikuwa umemuandama kwa kipindi kirefu sana. Kila siku alikuwa akifika asubuhi na mapema ofisini hapo na kuanza kazi ya usafi mara moja. Edmund akaanza kuonekana kuwa kivutio, ufanyaji wake wa kazi ukaonekana kumfurahisha kila mfanyakazi wa ofisi ile ambaye alikuwa akimwangalia.
“Yaani ninachokitaka ni kupigana na huu umasikini tu. Kufagia vyoo sio tatizo, ninachotaka ni kupata changu tu mwisho wa mwezi” Edmund alikuwa akijisemea mara kwa mara alipokuwa akiingia chooni kufanya usafi.
****
Kampuni ya upigaji picha ya PHOTOMANIA IMAGE EFFECT ilikuwa ni kampuni kubwa ambayo ilikuwa imejipatia umaarufu mkubwa kuliko makampuni yote ambayo yalikuwa yakifanya kazi ya upigaji picha nchini Tanzania. Kila siku watu mbalimbali walikuwa wakija ndani ya kampuni hiyo na kisha kupiga picha ambazo zilikuwa zikionekana kuwa na ubora wa juu.
Kamati ya urembo nchini Tanzania iliingia mkataba na kampuni hiyo kwa ajili ya upigaji picha kwa warembo wao ambao walikuwa wakiingia katika kinyang’anyiro kila mwaka. Picha nzuri ambazo zilikuwa katika kiwango cha juu ndizo ambazo ziliwafanya watu wengi kumiminika ndani ya kampuni hiyo kwa ajili ya upigaji wa picha.
Vile vile kampuni hiyo ilikuwa inajishughulisha na ukodishaji wa nguo za maharusi. Suti pamoja na mashela ambayo yalikuwa yakipatikana humo yalikuwa yakiwavutia watu wengi kiasi ambacho mara kwa mara kamati nyingi za harusi zilikuwa zikiweka oda maalumu katika kampuni hiyo.
Kampuni hiyo wala haikuishia hapo, bado ilikuwa ikiendelea kujiimarisha na kuliteka soko la Dar es Salaam. Wakaanzisha mambo ya upambaji wa kumbi mbalimbali hasa katika shughuli maalumu kama harusi, sherehe pamoja na shughuli nyingine. Watu wengi jijini Dar es Salaaam walikuwa wakivutiwa na kampuni hiyo ambayo ilizidi kujitengenezea jina kadri siku zilivyozidi kwenda mbele.
Kati ya watu ambao walikuwa wakipenda sana kwenda katika jengo la kampuni hiyo na kupiga picha alikuwepo msichana Uki Msantu. Mara kwa mara msichana huyo alikuwa akielekea katika jengo la kampuni hiyo na kupiga picha mbalimbali ambazo alizitengenezea fremu na kuziweka chumbani kwake.
Kila siku Uki alikuwa akitamani kujiingiza katika mambo ya urembo, kwake, upigaji picha ilikuwa ni moja ya sehemu ambayo alikuwa akipenda kujiona ni kwa jinsi gani alikuwa msichana mzuri aliyejaa mvuto mkubwa. Maneno mengi ya watu ambao walikuwa wakiuzungumzia uzuri wake ndio ilikuwa moja ya sababu iliyompelekea kupiga picha mara kwa mara ndani ya jengo la kampuni hiyo.
Uzuri wa msichana Uki ulikuwa gumzo ndani ya jiji la Dar es Salaam, vijana wengi ambao walikuwa wakikutana nae walikuwa wakivutiwa nae. Kwa mara ya kwanza alipoamua kujiingiza katika mambo ya urembo, vyombo vingi vya habari vikaanza kumtangaza kiasi ambacho akaanza kuwa gumzo midomoni mwa watu.
Picha zake nyingi ambazo alikuwa akizipiga katika kampuni hiyo zilikuwa zikiwekwa katika majarida mbalimbali ambayo yalikuwa yakitengenezwa jijini Dar es Salaam. Mvuto wa Uki ukawapelekea watu kutaka agombanie urembo wa Tanzania lakini Uki hakuweza kukubaliana nao.
Kwanza, hakupenda kuingia katika mambo ya urembo moja kwa moja, kwake, kuwa mwanamitindo kulionekana kumtosha kabisa. Pili, ukali wa baba yake ndio ulikuwa ukimtisha kuingia kwenye urembo mpaka kufikia ngazi za juu. Baba yake, Bwana Msantu alikuwa mkali, hakupenda binti yake aingie katika mambo ya urembo au kugombania kuingia katika ngazi kubwa ya urembo nchini Tanzania.
Ingawa alimruhusu binti yake aingie kwenye uanamitindo lakini Bwana Msantu hakufurahishwa na uamuzi wa binti yake. Kila siku alikuwa akijitahidi kumfurahisha binti yake hivyo aliona lisingekuwa jambo la usahihi kama angemkatalia pia kujiingiza katika mambo ya uanamitindo.
Shughuli za kutoka usiku kwa ajili ya kufanya kazi ya uanamitindo katika kumbi mbalimbali ndizo ambazo zikamfanya Bwana Msantu amuandae mtu maalumu ambaye alikuwa na bunduki kwa ajili ya kumlinda binti yake. Alihakikisha binti yake anapatiwa ulinzi wa kutosha kwani kulikuwa na watu wengi ambao walikuwa wakimtamani Uki.
“Ukiona mtu haeleweki eleweki, mpige risasi haafu kesi ya mauaji nitasimamia mimi mwenyewe” Bwana Msantu alimwambia kijana wake ambaye alimuweka kuwa mlinzi wa binti yake.
Bwana Msantu alikuwa mtu tajiri ambaye utajiri wake ulikuwa ukifikia zaidi ya trilioni moja. Alikuwa amejenga nyumba nyingi za kifahari pamoja na kununua magari mengi ya gharama kama Aston Martin na magari mengine ya kifahari.
Mzee huyo alikuwa akimiliki makampuni makubwa nchini Tanzania kama kampuni ya kutengenezea magazeti iliyojulikana kama SIMPAPER MEDIA, pia alikuwa akimiliki kampuni kubwa ya vinywaji ya BAVARIAN huku ikiwa inatengeneza soda pamoja na bia.
Mzee huyo hakuishia hapo, alikuwa akimiliki hoteli kubwa tatu zilizokuwa na hadhi ya kuitwa nyota tano ambazo ziliitwa UKILIA. Hoteli hizo zilikuwa katika sehemu tatu tofauti, hoteli ya kwanza ilikuwa ndani ya jiji la Dar Es Salaam, ya pili ilikuwa ndani ya jiji la Kampala huku nyingine ikiwa katika jiji la Nairobi.
Ukiachilia utajiri huo, pia Bwana Msantu alikuwa akimiliki boti zaidi ya kumi ambazo zilikuwa zikifanya safari kutoka Dar es Salaam kuelekea Zanzibar, boti ambazo alizipa jina la UKILIA kama alama ya jina la binti yake mpendwa. CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Katika maisha yake, Bwana Msantu alikuwa na mwanamke mmoja tu, Bi Nasra ambaye alikuwa amezaa nae mtoto mmoja ambaye alikuwa Uki. Baada ya kumpata Uki, mzee huyo hakuwa na uwezo wa kuzalisha mbegu zilizokuwa na nguvu kwa mkewe.
Uki ndiye alikuwa mtoto wake pekee ambaye alikuwa akimchunga hata zaidi ya mboni yake, ilikuwa ni rahisi kwa mzee huyo kumkasirisha yeye na kukuacha kuliko kumkasirisha binti yake ambaye alikuwa akimpenda sana. Kwake, Uki alionekana kuwa kila kitu, hakutaka mtu yeyote amsogelee binti yake, alijitahidi kumtunza katika maisha ya kifahari ambayo yangempa heshima katika kila kona ambayo angepita.
Pamoja na ulinzi wote ambao alikuwa akimpa binti yake lakini hakuweza kumzuia kuingia katika mahusiano na kijana Rahman, mtoto wa tajiri Adamu ambaye alikuwa akimiliki vituo kadhaa vya mafuta nchini Tanzania.
Wawili hawa walikutana katika jumba la sinema la Cinemax, huko wakaanza kuzoeana kwa kuongea, kila mmoja alionekana kuwa mchangamfu kwa mwenzake. Wakafika hatua ya kupeana namba simu hali iliyomaanisha kwamba hawakutaka ukaribu wao uishie mahali hapo.
Nyumbani wakaanza kuandikiana meseji na wakati mwingine kuongea. Bado walikuwa marafiki wa kawaida lakini kadri muda ulivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo urafiki wao ukazidi na hatimae kuingia katika mahusiano ya kimapenzi.
Kila moja alimpenda na kumthamini mwenzake, walikuwa pamoja katika kila sehemu walizokuwa. Katika kipindi ambacho Uki alikuwa akielekea katika maonyesho ya mavazi kama mwanamitindo, Rahman alikuwa pamoja nae.
Ukaribu wao ukaanza kusikika katika kila kona ya jiji la Dar es Salaam. Hakukuwa na mtu yeyote ambaye alionekana kushangaa kutokana na watu hao wote kuwa watoto wa matajiri ambao walikuwa wakitikisa nchini Tanzania.
Uhusiano huo ulipomfikia Bwana Msantu, alionekana kukasirika kupita kawaida, hakutarajia kama binti yake angeweza kujiingiza katika mahusiano. Alichokifanya kwa wakati huo ni kumuita Uki na kumwambia kuhusu uhusiano uliokuwa ukiendelea. Uki hakutaka kujificha, alimuelezea baba yake kila kitu na katika kipindi hicho alikuwa ndani ya mapenzi mazito na kijana Rahman Adamu.
Uki akataka maisha yake ya uhusiano yaachwe kama yalivyokuwa, Bwana Msantu hakutaka kuendelea kuyafuatilia. Kutokana na kutamani binti yake awe na furaha muda wote na ndio ilikuwa sababu iliyomfanya kumuacha kuendelea na uhusiano wake huku akimtaka kuwa makini kwa kila kitu.
Uki akajiona kuwa huru, uhusiano wake ukaongezeka zaidi kwa Rahman ambaye alikuwa akimuonyeshea mapenzi ya dhati. Vyombo vingi vya habari vikaanza kuwatangaza, picha zao mbalimbali zilikuwa zikitolea magazetini jambo ambalo wala hawakuonekana kujali sana zaidi ya kuwafanya kuwa maarufu zaidi na zaidi.
Siku zikaendelea kukatika mpaka pale ambapo mabadiliko yalipoanza kujionyesha, ukaribu ambao alikuwa nao Rahman kwa Uki ukaonekana kuanza kupungua. Uki hakuonekana kuelewa sababu ambayo ilisababisha hali ile jambo ambalo likamfanya kuanza kufanya uchunguzi kimya kimya.
Kitu cha kwanza akaanza kuipekua simu ya Rahman katika kipindi ambacho alikuwa akielekea bafuni kuoga. Meseji nyingi za kimapenzi zilikuwa simuni mule huku zikiwa zimetumwa kwa wanawake mbalimbali. Hali ile ikamuumiza sana Uki.
Kuanzia siku hiyo akawa msichana wa kulia tu. Mapezi yale ambayo kila siku yalikuwa yakimpa furaha yakaanza kumtesa. Rafiki yake pekee ambaye alikuwa akimfariji katika kipindi hicho alikuwa msichana Esta ambaye alikua nae toka utotoni, walisoma pamoja mpaka kipindi hicho walikuwa pamoja.
Hali ilimfanya kuanza kupungua, mawazo yalikuwa yakimwandama kupita kawaida, kila siku akawa mtu wa kulia tu. Furaha kwake ikabaki kuwa kama historia, alizikumbuka siku zote za nyuma ambazo alikuwa akilia na kuyafurahia mapenzi, kwa kipindi hicho furaha yote ilikuwa imefutika kabisa.
Rahman hakuonekana kuyajali machozi ya Uki ambayo kila siku alikuwa akilia, kwake maisha yalikuwa yakiendelea kama kawaida. Akaanza kutembea na wasichana mbalimbali, hakukuwa na msichana yeyote ambaye alimkatalia, fedha za baba yake zikaonekana kuwa silaha kubwa sana kwa wanawake.
Alilala na msichana yeyote ambaye alikuwa akitaka kulala nae, alizitumia fedha za baba yake kuwahonga wasichana ambao walikuwa wakimpa starehe ambayo alikuwa akiitaka. Mara kwa mara Uki alikuwa akimpigia simu na kumuomba msamaha japokuwa hakuwa na kosa, Rahman alionekana kuwa na maringo kwa Uki, hakumtaka tena, kile ambacho alikuwa akikitaka katika mwili wa msichana yule alikuwa amekwishakipata.
Uki akawa msichana wa kushinda ndani, majonzi aliyokuwa nayo yalikuwa ni zaidi ya msiba. Kila siku alilia kupita kawaida, kila siku alijitahidi kumpigia simu Rahman lakini mvulana huyo hakuonekana kujali. Kitendo cha kupigiwa simu na Uki kila siku kikamuongezea kiburi kwa kujiona kwamba alikuwa akipendwa na msichana huyo jambo lililomfanya kuendelea kuwafuata wasichana wengine kadri alivyoweza.
****
Uki akajitahidi kusahau kila kitu kilichotokea kati yake na Rahman lakini bado hali ile haikuweza kusahaulika moyoni mwake. Mapenzi makubwa ambayo alikuwa nayo juu ya Rahman yakaonekana kumganda moyoni mwake. Hakujua angefanya nini, mapenzi yalikuwa yamemuumiza kupita kawaida.
Akaanza kuyachukia mapenzi, wanaume kwake wakaonekana kuwa viumbe vya ajabu ambavyo wala havikutakiwa kithaminiwa. Rahman alikuwa ameubadilisha moyo wake na kumuingizia chuki kubwa moyoni mwake. Hakutaka tena kujiingiza katika mahusiano, wale wanawake ambao walikuwa wakizeeka bila kuwa katika mahusiano ya kimapenzi akaanza kuwaona kwamba waliamua kufanya uamuzi mzuri ambao ulitakiwa kuigwa na kila msichana.
“Usiyachukie mapenzi Uki. Jaribu kumchukia yule ambaye amekufanya wewe kuyachukia mapenzi” Esta alimwambia Uki.
“Hauwezi kuubadili moyo wangu Esta. Ninawachukia wanaume na ninayachukia mapenzi pia” Uki alimwambia Esta huku akiwa katika uso ulioonyesha maumivu makali.
“Hata kama Uki. Hautakiwi kufanya hivyo. Bado una nafasi ya kuingia katika mahusiano hata na tu mwingine” Esta alimwambia Uki kwa sauti ya chini.
“Unasemaje? Uki mimi niingie tena kwenye mahusiano na mwanaume. Mimi Uki huyu huyu eti niingie kwenye mahusiano na mwanaume, labda sio mimi” Uki alimwambia Esta huku akijinyooshea kidole.
Huo ndio msimamo ambao Uki alikuwa ameuweka. Kamwe hakutaka kujiingiza tena katika mahusiano na mwanaume yeyote yule, alitamani aendelee kuwa vile vile kama alivyokuwa. Kila siku alikuwa akimuomba Mungu aubadilishe moyo wake, amsahaulishe na vitu vyote ambavyo vilikuwa vimetokea katika maisha yake ya nyuma kuhusiana na mahusiano ya kimapenzi.
Maombi yake ya kila siku yalikuwa ni kutaka kusahaulishwa kwa kila kitu kilichotokea huku akimuomba Mungu ampe moyo wa kutokupenda tena maishani mwake. Kwa kuwa uhusiano ule ulikuwa ukijulikana na kila mtu jijini Dar es Salaam basi hata ulipokuja kuvunjika watu walifahamu pia.
Vyombo vya habari hasa vya magazeti vilikuwa vikiandika kuhusu kuvunjika kwa uhusiano huo ambao ulidumu kwa muda wa mwaka mmoja tu. Kila siku Uki alipokuwa akiziona habari zile alikuwa akilia, zilikuwa zikimkumbusha kitu ambacho kilikwishatokea katika maisha yake na ambacho hakutaka kukikumbuka tena.
“Nitamsahau tu” Uki alijifariji katika kipindi ambacho aliamua kuzichukua picha zote alizopiga na Rahman na kuamua kuzichoma moto.
****CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Edmund bado alikuwa akiendelea kufanya kazi kama kawaida yake. Ndani ya miezi mitatu ambayo alikuwa amefanya kazi ndani ya kampuni hiyo tayari maisha yake yakaanza kubadilika. Alikuwa akila vizuri, mshahara ambao alikuwa akiupata ulikuwa umeanza kubadilisha maisha yake.
Alichokifanya ni kuzidi kufanya kazi kwa juhudi zote, aliipenda sana kazi yake kwa kuwa ilikuwa ikimuingizia fedha sana. Kila siku alikuwa akiamka asubuhi na mapema na kuwahi kazini ambako alikuwa akifanya usafi wa kufagia kuanzia mapokezini mpaka chooni. Japokuwa ilionekana kuwa kazi ya kipuuzi sana kwa watu wengine lakini kwa Edmund kazi hiyo ilionekana kuwa muhimu sana.
“Unajitahidi sana kufanya usafi. Hongera” Msichana wa mapokezini, Belinda alimwambia Edmund ambaye alikuwa akiendelea kufagia.
“Labda kwa sababu naipenda kazi yangu Belinda” Edmund alimwambia huku akiachia tabasamu.
Kadri alipozidi kubadilika kimuonekano wake mwilini na ndivyo ambavyo wasichana walivyoanza kuvutiwa nae. Wasichana wengi ambao walikuwa wakifika mahali hapo kwa ajili ya kupiga picha hawakuweza kuzificha hisia zao kwa Edmund. Belinda ndiye alikuwa mtu pekee ambaye alikuwa na uwezo mkubwa wa kuwaonganisha pamoja na Edmund.
Edmund hakuwa tayari kuingia katika mahusiano. Kwanza alihitaji kufanya kazi kwa muda mrefu sana, alijiona kama angediriki kuingia katika mahusiano basi ufanyaji wake wa kazi ungeweza kupungua kwa kiwango kikubwa sana. Kwake, alihitaji kujiweka mbali na mahusiano ya kimapenzi japokuwa kila siku alikuwa akipokea salamu mbalimbali kutoka kwa Belinda zikiwa zimetumwa na wasichana mbalimbali.
“Sasa nani aliyejua kama leo ni siku yangu ya kuzaliwa?” Edmund alimuuliza Belinda huku akionekana kukasirika.
“Mmh! Sijui” Belinda alijibu.
“Hapana. Utakuwa umewaambia tu kwa sababu hakuna mtu yeyote niliyemwambia zaidi yako” Edmund alimwambia Belinda.
Mifuko ya zawadi mbalimbali za siku ya kuzaliwa ilikuwa mikononi mwake Belinda ambaye aliambiwa ampe Edmund. Wala haukuwa mfuko mmoja tu, ilikuwa mifuko mingi ambayo ilimuonyeshea kwamba kulikuwa na wasichana wengi ambao walikuwa wamemtumia.
Edmund hakutaka kuziacha zawadi zile, akazichukua na muda wa kurudi nyumbani ulipofika akarudi nazo. Mara baada ya kufika nyumbani, kitu cha kwanza ambacho alikifanya ni kuanza kuifungua mifuko ile. Zawadi mbalimbali pamoja na keki za thamani zilikuwepo ndani ya mifuko ile pamoja na picha mbalimbali za wasichana ambao walikuwa wamemtumia zawadi zile.
Edmund hakutaka kujali, kwake mapenzi hakuwa ameyapa kipaumbele, alichokifanya ni kuchukua keki zile na kuzila huku akitamani siku nyingine aletewe tena. Mawazo yake yalikuwa yakiifikiria kazi yake tu, tayari akayaona mafanikio makubwa yakiwa mbele yake, alipenda sana kuwa na maisha mazuri kama watu wengine, hakuupenda umasikini hata mara moja.
Mara kwa mara alikuwa akielekea nyumbani kwa Bi Husna. Mwanamke huyu alimchukulia kama mama yake. Kila siku alipokuwa akienda kumtembelea alikuwa akimshukuru kwa kile ambacho alikuwa amemfanyia, cha kumtafutia kazi sehemu ambayo ilimuweka kuwa karibu na watu wengi.
Siku zikazidi kupita mpaka kufika siku ambayo aliamua kununua simu. Hakutaka namba yake awe nayo mtu yeyote nje ya ofisi ile lakini jambo hilo hakuweza kulizuia. Ni ndani ya wiki moja akaanza kupigiwa simu na wasichana mbalimbai wakimtaka mahusiano. Edmund akaonekana kushangaa, hakuwa na uhakika kama bosi wake, Karim au wafanyakazi wengine wangeweza kutoa namba yake zaidi ya mtu mmoja tu, Belinda.
Kila alipokuwa akimuuliza Belinda alikuwa akikana ila mwisho wa siku akaamua kumwambia kwamba yeye ndiye alikuwa akiitoa kwa malipo makubwa, yaani wasichana walikuwa wakiitaka huku wakimlipa kiasi kizuri cha fedha. Belinda hakutaka kuacha viasi vile vya fedha jambo ambalo lilimfanya kumpa namba ya Edmund kila msichana ambaye alikuwa akiitaka.
“Sasa hizo fedha wanazokupa mbona hata mimi haunipi?” Edmund alimuuliza Belinda.
“Nitakupa vipi na wakati wewe ndiye una nafasi kubwa za kuzichukua kutoka mifukoni mwao?” Belinda alimuuliza Edmund na wote kuanza kucheka.
Edmund hakutaka kujali, alichokifanya kwa wakati huo ni kuendelea na kazi yake kama kawaida. Kila baada ya masaa matatu alikuwa akielekea chooni na kusafisha. Usafi ndicho kitu ambacho kilikuwa kikimfanya kuonekana kijana nadhifu hata kwa wasichana ambao walikuwa wakiingia ndani ya jengo lile. Kama ambavyo alivyotamani choo kiwe kisafi kila wakati na ndivyo ambavyo alitamani hata naye awe msafi kila wakati.
“Naomba ufunguo wa stoo’ Edmund alimwambia Belinda alipomfuata pale mapokezini. Kwa kuwa Belinda alikuwa na wateja wawili mahali hapo wala hakutaka kuongea kitu chochote kile zaidi ya kuinama, kuifungua droo ya meza na kutoa funguo kumpa Edmund.
Edmund akauchukua ufunguo ule na kuanza kuondoka mahali pale huku akiurusha rusha ufunguo juu na kuudaka. Kwake maisha yalionekana kuwa ya raha kila siku. Hakuwa na kitu chochote ambacho alikuwa akikifikiria zaidi ya kazi yake ambayo ilikuwa ikimfanya kuwa na furaha kila siku.
“Uki unaulizwa” Esta alimwambia Uki ambaye alikuwa pale mapokezini.
“Unasemaje?” Uki aliuliza huku akimwangalia Belinda.
“Umevutiwa nae nini nikupe namba yake? Naona unamwangalia sana” Belinda alimwambia Uki ambaye kipindi kichache kilichopita alikuwa akimwangalia sana Edmund aliyefika mahali pale kuchukua funguo.
“Hapana. Usijali. Tunataka kupiga picha” Uki alimwambia Belinda.
Kama kawaida wakaelekezwa kule ambapo walitakiwa kwenda. Uki alionekana kubadilika, akaonekana kuanza kufikiria mambo kadhaa hali ambayo ilimfanya Esta kuligundua lile. Esta hakutaka kuuliza kitu chochote kile, walipofika sehemu husika, wakalipa na kisha kuanza kupiga picha na kuondoka mahali hapo.
“Kuna kitu nimesahau. Naomba unisubirie mara moja” Uki alimwambia Esta na kisha kuanza kurudi ndani ya jengo lile na safari yake kuishia mapokezini.
“Samahani kama nitakuwa ninakusumbua” Uki alimwambia Belinda.
“Kuna nini?” Belinda aliuliza.
“Unamfahamu yule kijana aliyekuja hapa?”
“Ndio. Ni mfanyakazi mwenzangu”
“Unaweza kuniitia niongee nae mara moja?”
“Hapana. Ana kazi kubwa ya kufanya usafi, huwa ahitaji kusumbuliwa kabisa” Belinda alimwambia Uki.
“Kwa hiyo siwezi kuonana nae?”
“Haiwezekani. Au kama unataka nikupe namba yake ya simu” Belinda alimwambia Uki.
“Sawa. Nipe” Uki alisema huku akiitoa simu yake.
“Una shilingi ngapi?”
“Za nini?”
“Za namba”
“Yaani namba tu unataka niinunue?”
“Ndio. Wanawake wote ambao wanahitaji namba yake huwa ninawauzia. Hii ni amri kutoka kwake mwenyewe. Kama hauna fedha basi endelea na safari yako” Belinda alimwambia Uki ambaye alionekana kushangaa.
“Sawa. Unauza kwa shilingi ngapi?”
“Elfu kumi na tano” Belinda alijibu.
Uki hakutaka kuchelewa, tayari alionekana kuwa kama mtu ambaye alihitaji kitu fulani. Alichokifanya kwa wakati huo ni kuingiza mkono wake katika mkoba wake na kutoa kiasi cha shilingi elfu ishirini na kisha kumpatia Belinda. Alichokifanya belinda ni kuchukua simu yake na kisha kumpatia Uki namba ile ya simu ya Edmund.
“Anaitwa nani?”
“Edmund”
“Asante” Uki alimwambia Belinda na kuondoka mahali hapo.
Wala hazikupita dakika nyingi, Edmund akatokea mahali hapo huku mkononi akiwa ameushika ufunguo na kumgawia Belinda. Uso wa Belinda ulikuwa ukionekana kuwa na furaha hali ambayo ilimfanya Edmund kumshangaa. Kila alipokuwa akijaribu kumuuliza siri ya furaha yake Belinda hakutaka kuongea kitu chochote zaidi ya kuendelea kutabasamu tu.
“Kuna nini?” Edmund alimuuliza.
“Namba yako ya simu”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Imefanya nini tena? Au umeiuza kama kawaida yako ili nisumbuliwe usiku?” Edmund aliuliza huku akiachia tabasamu.
“Ndio. Maisha magumu haya bila ujanja ujanja wa mjini hauwezi kuishi”
“Sasa umemuuzia nani?”
“Msichana”
“Msichana gani?”
“Uki”
“Ndiye nani huyo?”
“Acha kunitania. Haumjui Uki? Ngoja” Belinda alimwambia Edmund na kisha kuinama chini, akaifungua droo yake na kutoa magazeti kadhaa na kumuonyeshea picha za Uki.
“Huyu msichana kama nimewahi kumuona sehemu fulani hivi!” Edmund alisema.
“Si umesema haumfahamu?”
“Aaah! Nimeshakumbuka. Kumbe nilikuwa nimemuona mahali hapa kipindi kile nilichokuwa nimekuja. Si ndio huyu?”
“Ndiye mwenyewe”
“Du!”
“Kuna nini tena?”
“Ngoja nisubiri simu yake nione ataniambia nini. Ila ni mzuri sana” Edmund alimwambia Belinda.
“Achana na uzuri Ed. Kuna kingine cha ziada”
“Kipi?”
“Kuhusu utajiri. Baba yake ni tajiri mkubwa sana. Nadhani hii ni bahati ambayo Mungu ameamua kukupa kimafumbo. Ukicheza, bahati itaondoka mikononi mwako” Belinda alimwambia Edmund.
“Kwa hiyo nifanye nini?”
“Mungu wangu! Yaani ukubwa wote huo unaiuliza swali kama hilo! Wewe unavyoona unatakiwa ufanye nini?”
“Nimeshakuelewa” Edmund alimwambia Belinda na kuondoka mahali hapo.
****
Usiku kwake ukaonekana kuwa mrefu kufika. Kila wakati Edmund alikuwa akimfikiria Uki, msichana ambaye alikuwa amepewa namba yake na Belinda. Kila wakati macho yake yalikuwa yakiangalia saa yake, mshale wa dakika ulionekana kwenda taratibu sana tofauti na siku nyingine. Alitamani muda uende haraka haraka ili Uki aweze kumpigia simu na kuanza kuongea nae.
Uzuri wa uki tayari ulikuwa umemvutia, akauhisi moyo wake ukianza kumpenda msichana huyo ambaye kwake alionekana kukamilika kwa kila kitu. Kila alichokuwa akikifanya kama kupoteza muda ili masaa yaende haraka haraka haikuweza kusaidia, bado alikuwa akiona masaa yakienda taratibu sana.
Uzuri wa Uki ukaonekana kumchanganya akili yake. Japokuwa alikuwa na tabia ya kuwakatalia wasichana mbalimbali lakini kwa Uki ikaonekana kuwa ngumu kufanya hivyo. Japokuwa alikwishaambiwa kwamba msichana yule alikuwa mtoto wa tajiri lakini wala hakutaka kujali. Kwake aliyachukulia mapenzi kuwa mapenzi na utajiri kuwa utajiri tu.
Akili yake haikuufikiria utajiri uliokuwepo katika familia ya Bwana Msantu, kwake alikuwa akifikiria mapenzi tu. Uki alionekana kumvutia kupita kawaida. Alichokifanya ni kutafuta magazeti ya siku zilizopita ambayo yalikuwa na picha ya Uki na kisha kuelekea nayo chumbani.
Alijilaza kitandani huku macho yak yakiangalia picha zilizokuwepo katika magazeti yale. Mapenzi yake kwa Uki yakazidi kuongezeka zaidi na zaidi. Kitendo cha kuona kwamba Uki alikuwa ameachana na mpenzi wake aliyekuwa nae kilionekana kumpa faraja kupita kawaida.
Mara simu yake ikaanza kuita. Kwa haraka haraka akaichukua na kuanza kukiangalia kioo cha simu ile. Namba ambayo ilikuwa ikimpigia kwa wakati huo ilikuwa namba ngeni kabisa simuni mwake. Huku akionekana kuachia tabasamu, akakibonyeza kitufe cha kijani na kisha kuipeleka simu sikioni huku uso wake ukiendelea kuwa na tabasamu pana.
“Hallow” Aliita mara baada ya kuipokea simu ile.
“Hallow. Samahani. Naongea na Edmund hapo?” Sauti nzuri ya msichana ilimuuliza.
“Ndio” Edmund alijibu haraka haraka bila hata kujiuliza.
“Ok! Samahani. Ninaweza kukuona?”
“Wapi?”
“Hapa Magomeni”
“Sawa. Kwanza naongea na nani?”
“Lucy”
“Lucy! Lucy ndiye nani?”
“Msichana niishie Mikocheni. Nilipewa namba yako na msichana ambaye unafanya nae kazi’ Lucy alijibu.
Edmund hakutaka kupoteza muda, alichokifanya ni kuikata simu ile. Lucy hakuonekana kukubali hata kidogo, akaendelea kupiga zaidi na zaidi lakini Edmund hakutaka kuipokea simu ile. Kwa wakati huo mawazo yake yalikuwa kwa Uki tu, hakutaka kuisikia sauti ya msichana mwingine yeyote zaidi ya Uki ambaye tayari alikuwa amekwishauteka moyo wake.
Aliendelea kuisubiria simu ya Uki. Dakika na masaa yalizidi kusogea mbele lakini wala hakukuwa na simu iliyopigwa kutoka kwa Uki zaidi ya wasichana wengine ambao walikuwa wakimtaka kimapenzi.
Mpaka inafika saa saba, hakuwa amepata simu kutoka kwa Uki jambo ambalo lilionekana kumkosesha furaha kabisa. Hali iliendelea kuwa vile vile, mpaka anapata usingizi saa nane, wala hakuwa amepata simu kutoka kwa Uki, msichana ambaye alikuwa ameuteka moyo wake kupita kawaida.
Asubuhi ilipofika akaelekea kazini na kuendelea na kazi zake kama kawaida. Kichwa chake bado kilikuwa na mawazo mengi, alimfikiria Uki kupita kawaida. Belinda aliweza kuigundua hali ambayo alikuwa nayo lakini kila alipomuuliza, Edmund hakumwambia ukweli.
“Bosi anakuita” Mfanyakazi mwingine wa kike, Aisha alimwambia Edmund ambaye akaanza kupiga hatua kuelekea ofisini.
“Kuna kazi ya ziada nataka kukupa mara moja” Karim alimwambia.
“Kazi gani bosi?”
“Kuna picha kadhaa zipo ndani ya hii flash disc, kuna sehemu nataka uzipeleke kwa ajili ya kutengenezewa fremu” Karim alimwambia Edmund.
“Nizipeleke sehemu gani?”
“Pale posta ya zamani. Kwenye lile jengo iliyokuwepo na maduka kadhaa ya Nguo. Ukifika hapo, utakuta sehemu wameandika NYEMO THE PRINCE, ndio hapo hapo”
“Sawa”
Karim akampa Edmund maelekezo yote ambayo alitakiwa kuyafuata na kisha kuanza safari ya kuelekea alipoagizwa huku akitumia usafiri wa kampuni. Moyoni mwake hakujisikia vizuri kabisa, kitu ambacho alikuwa akikitaka ni kuendelea kubaki pale ofisini kwa kuamini kwamba Uki angerudi tena mahali pale.
Alipofika, akaingia ndani ya lile jengo na kuanza kuitafuta ofisi ambayo alikuwa ameelekezwa na kisha kumgawia mhusika ile flash disc. Akaambiwa asubiri na baada ya dakika thelathini kila kitu kilikuwa tayari na kukabidhiwa picha zile ambazo zilikuwa katika fremu.
Edmund hakutaka kuondoka bila kuziangalia picha zile, alichokifanya ni kuifungua bahasha ile ya kaki na kisha kutoa fremu zile tano za picha na kuanza kuziangalia. Mapigo yake ya moyo yalikuwa yakidunda kupita kawaida, hakuamini kwamba picha zile ambazo alikuwa amezishika zilikuwa ni picha za Uki ambazo alikuwa amepiga peke yake pamoja na rafiki yake, Esta.
“Samahani. Nitolee picha nyingine mbili za hizi hapa” Edmund alimwambia mhusika huku akimpa picha mbili za Uki.
“Nisitengenezee fremu pia au?”
“Yeah! Ni Kiasi gani kila moja?”
“Elfu kumi”
“Poa. Nitolee” Edmund alimwambia.
Baada ya nusu saa nyingine akawa na fremu mbili za ziada ambazo zilikuwa na picha za Uki. Kila alipokuwa akiziangalia picha zile alikuwa akitabasamu tu, hakuamini kama msichana mzuri kama yule alikuwa amevutiwa nae kiasi ambacho alichukua mpaka namba yake ya simu.
Huku akiiangalia picha moja kati ya zile garini, mara simu yake ikaanza kuita. Akaichukua kutoka mfukoni na moja kwa moja kuipeleka sikioni. Sauti ya kike ikasikika sikioni mwake, akaonekana kukasirika kwani alija fika alikuwa mmoja wa wanawake ambao walikuwa wakimpigia simu mara kwa mara.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nahitaji kuonana nawe” Sauti ya msichana yule ilisikika.
“Kwanza naongea na nani?”
“Uki Msantu” Uki alijibu.
Jibu lile likaonekana kumchanganya Edmund, alibaki kimya kwa muda huku akiwa hajui aongee kitu gani. Simu ambayo alikuwa ameisubiria usiku kucha ndio ilikuwa imeingia katika kipindi hicho. Ukimya bado ulikuwa ukiendelea.
“Hallow!” Uki aliita baada ya kuona ukimya wa muda mrefu.
“Nipo kazini kwa sasa”
“Kwa hiyo siwezi kukuona hata baadae?”
“Baadae ya saa ngapi?”
“Kwani kazini huwa unatoka saa ngapi?”
“Saa kumi na mbili”
“Basi naomba tuonane saa mbili usiku”
“Sawa. Ila sehemu gani?”
“Popote. Kwani wewe unakaa wapi?”
“Uswahilini”
“Uswahilini? Wapi?’
“Tandale”
“Kwa Mtogole?”
“Hapana. Ni ndani ndani zaidi”
“Basi ningependa tuonane katika baa ya Kingstone” Uki alimwambia Edmund.
“Ndio iko wapi baa hiyo?”
“Kijitonyama”
“Sawa” Edmund alijibu na kisha kuagana.
Moyo wake ulikuwa umefarijika kuita kiasi, kitendo cha kupigiwa simu na msichana ambaye alikuwa ameuteka moyo wake kilionekana kumfurahisha. Akatamani aruke kwa furaha katika kiti kile alichokuwepo. Akamwangalia dereva ambaye alikuwa akimuendesha, alitamani amgawie hata shilingi elfu kumi.
“Vipi tena? Mbona furaha hivyo? Umeongezewa mshahara nini?” Dereva alimuuliza.
“Hapana”
“Sasa nini siri ya furaha yako?”
“Wewe acha tu” Edmund alijibu.
Furaha ya Edmund ikawa imerudi upya. Kila wakati akaanza kuangalia saa yake, muda kwake ukaonekana kuchelewa kufika huku mshale wa dakika ukienda taratibu sana. Katika kipindi hicho alikuwa akitaka kuonana na Uki tu.
Kila wakati alikuwa akiiangalia namba ya simu ya Uki, alitamani ampigie ili aisikie sauti yake tu kwa mara nyigine tena. Ingawa alikuwa ameongea nae katika saa moja lilipita lakini akawa na hamu kubwa ya kutaka kuisikia sauti ile kwa mara nyingine tena.
Mpaka anatoka kazini saa kumi na mbili bado akili yake ilikuwa ikimfikiria Uki. Alipofika nyumbani akaanza kujiandaa tayari kwa safari ya kuelekea katika baa ya Kingstone iliyokuwa Kijitonyama kwa ajili ya kuoanana na msichana mrembo, Uki.
Kutoka Tandale mpaka Kijitonyama wala hakukuwa mbali, ni mwendo wa miguu wa dakika kumi na tano akawa amekwishafika katika baa hiyo na kukaa katika sehemu ambayo ilikuwa wazi. Mhudumu akatokea mahali hapo na kumwambia kwamba alikuwa akihitajika na msichana mmoja ambaye alikuwa amekaa katika kiti kilichokuwa sehemu iliyokuwa na mwanga hafifiu wa taa.
Edmund akasimama na kuanza kuelekea kule alipokuwa amehitajika. Moyo wake ukajihisi kupata faraja hasa baada ya kumuona Uki mahali hapo. Alitamani amsogelee na kumkumbatia pamoja na kummwagia mabusu mfululizo.
Uso wa Uki ulikuwa ukimuonyeshea tabasamu pana ambalo lilimfanya Edmund achanganyikiwe zaidi na zaidi. Akakaribishwa mahali pale na chakula kuagizwa na kisha kuanza kula. Katika kipindi hicho Uki alikuwa akimuuliza maswali mfululizo Edmund hasa kuhusiana na uhusiano wa kimapenzi ambao alikuwa nao au alioupitia kabla ya siku hiyo.
Ni ndani ya dakika thelathini, wakazoeana kupita kawaida kana kwamba walikuwa wamekutana mara kadhaa siku za nyuma. Katika kipindi hicho, Uki hakutaka kuzificha hisia zake za kimapenzi ambazo zilikuwa moyoni mwake juu ya Edmund, akamuelezea kila kitu ambacho alikuwa akijisikia moyoni mwake.
Edmund hakutaka kujifikiria, akamkubalia Uki ombi lake la kutaka kuanzisha uhusiano wa kimapenzi pamoja nae. Huo ndio ukawa mwanzo wa mahusiano hayo ya kimapenzi, mahusiano ambayo yalimfanya kila mmoja kuwa na furaha, mahusiano ambayo yalianzisha chuki kwa watu wengine, mahusiano ambayo yalikuja kuwagharimu katika maisha yao ya baadae.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment