Simulizi : Penzi Lililosababisha Mauti
Sehemu Ya Pili (2)
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Maisha yaliendelea huku nikiendelea kubaki na siri moyoni mwangu, ilikuwa ni siri ile ya maneno aliyoniambia Mama yangu, aliniambia kuwa sikutakiwa kuendelea kuishi na mke wangu hasa katika kipindi kile cha ujauzito hivyo nilitakiwa kumrudisha nyumba kwao kwa ajili ya kuilea mimba mpaka pale ambapo angeweza kujifungua ndiyo nilitakiwa kumrudisha na kuendelea kuishi naye. Hilo lilizidi kuniumiza sana akili yangu.
Dominick mimi fundi simu wa Kariakoo sikushindwa kutafuta pesa ya kuweza kuihudumia mimba, sasa kwanini Mama yangu aniambie nilitakiwa kumrudisha kwao, kwani ameona nini?
Lilipotoka swali hilo likajitunga swali lingine basi ikawa ni tafarani tu! nikazidi kujiona kuwa mjinga wa kuendelea kuificha siri ambayo mwisho wa siku ningeweza kuzikwa nayo.
Baada ya wiki moja kupita niliamua kumueleza ukweli mke wangu, nilimuelezea kila kitu kilichokuwa kimetokea, sikutaka kumficha lolote, nilimwambia kwa kuwa nilimuamini, alikuwa ni msikivu hivyo sikutegemea tofauti yoyote ambayo ingeweza kujitokeza.
“Mume wangu,” aliniita mara baada ya kumuelezea kila kitu tulipokuwa nyumbani.
“Naam,” nilimuitikia huku nikimtazama, hakuonekana kubadilika kwa lolote lile, sura yake ya kitoto bado iliendelea kuwa katika vazi lake la upole.
“Mama ameongea kitu cha umuhimu sana,” aliniambia Julieth kwa sauti ya upole.
“Cha umuhimu kivipi?” nilimuuliza.
“Ameona mbali,” alinijibu.
“Kivipi?”
“Wewe hautaweza kunihudumia kwa kila kitu, kuna vingine utashindwa wakati utakapokuwa kazini ni bora niende nyumbani tu! kule watakuwa karibu sana na mimi hasa katika hiki kipindi cha ujauzito wangu.”
“Kwahiyo unataka kuniambia umekubaliana na Mama mkwe wako?”
“Ndiyo tena ameongea kitu cha umuhimu sana,” aliniambia Julieth huku akionekana kuwa sawa, hakuonyesha kukasirika kwa lolote lile.
Nilijaribu kumkatalia lakini lilipokuja suala la king’ang’anizi kwa kweli nilishindwa, Julieth hakutaka kuona wazo la Mama yangu ninalipuzia.
“Mama ni mama Dominick embu tusimpuuzie yeye ni mtu mzima,” aliniambia Julieth.
“Lakini mke wangu.”
“Hakuna cha lakini, kilichobaki hapo wewe nipe nauli niende nyumbani,” aliniambia Julieth.
****
Baada ya siku ya tatu kupita niliamua kwenda kumkatia tiketi ya basi Ubungo mke wangu ambapo siku iliyofuata alitakiwa kusafiri kwenda mkoani Kilimanjaro na basi la KIMOTKO.
Ilikuwa ni moja kati ya safari iliyoniacha katika wakati wa maumivu sana, nilimzoea sana mke wangu, alikuwa ndiyo kila kitu katika maisha yangu.
Hatimaye siku ya safari ikawadia, Julieth mke wangu akaweza kusafiri kuelekea nyumbani kwao Kilimanjaro. Nakumbuka nilipokuwa Ubungo nikimuaga machozi yalikuwa yakinilengalenga mwisho yakaanza kunibubujika.
“Nakupenda sana mke wangu, nitakukumbuka sana,” nilimwambia nilipokuwa nikimuaga.
“Hata mimi nitakukumbuka sana mume wangu, huwezi kuamini yani natamani nisiondoke lakini sina jinsi acha niende nikailee mimba yako nikirudi nitakuletea furaha ya maisha yako,” aliniambia Julieth maneno aliyoyatamka kwa hisia. Nilishindwa kujizuia nikaamua kumkumbatia, akatulia vyema katika kumbato langu.
“Niambie kitu kimoja kabla hujaondoka,” nilimwambia nilipokuwa nimekumbatiana nae.
“Nakupenda sana na ninakuahidi nitamlea vizuri mwanao,” aliniambia huku akilipapasa tumbo lake. Nilimtoa katika lile kumbato kwa wakati huo muda wa kuondoka basi ulikuwa umefika. Nikamsindikiza kwa zawadi ya mabusu huku moyoni nikiahidi kumtunzia thamani yake kama mke wangu wa ndoa.
****
Nilianza kuyaamini maneno ya Mama yangu, niliamini alikuwa sahihi kuniambia maneno yale ya kunikaripia. Hakika nilijiona kuwa mjinga sana hasa kwa kujaribu kupingana na maneno ya Mama yangu, Mama aliyeniweka miezi tisa tumboni mwake kisha akanizaa kwa uchungu.
Nilihisi kuwa mkosaji na niliamua kwenda kumuomba msamaha kwa yale yote yaliyokuwa yametokea. Alinisamehe lakini ulikuwa ni msamaha wa masharti.
Alikuwa amenitafutia mwanamke mwingine ambaye alihitaji nimuoe haraka iwezekanavyo na kila kitu alikuwa ameshakiandaa kama maandalizi ya kumuoa mwanamke huyo ambaye alijulikana kwa jina la Evelyne.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hakutaka kunipa nafasi ya kujielezea lolote kwa wakati huo alipokuwa akinieleza kuhusu Evelyne, alijua fika nisingeweza kukubali kirahisi hivyo aliamua kutumia cheo chake kama Mama katika kunikandamiza.
“Dominick ukitaka nikusamehe na haya yote yaishe yani nisiwe na kinyongo chochote basi kubali umuoe Evelyne, roho yangu itaridhika,” aliniambia Mama kwa msisitizo.
Nilikuwa katika wakati mgumu sana ndugu msomaji, nilihisi kuchanganyikiwa baada ya kuambiwa maneno hayo. Nikamkumbuka mke wangu ambaye alisafiri siku chache zilizopita pamoja na ahadi zangu nilizomuahidi, nilimuahidi mambo mengi sana lakini kubwa ilikuwa ni kumtunzia thamani yake ya ndoa kama mke wangu halali, sikutaka kumfanyia lolote baya ambalo baadae lingeweza kumpa maumivu makali mno, nilizithamini mno hisia zake, niliuthamini uwepo wake katika maisha yangu.
Nilianza kuona ahadi zangu zikiteketea moja baada ya nyingine, msamaha wa Mama yangu wenye masharti ndani yake kwa kweli ulizidi kuniweka katika wakati wa mawazo, nilikuwa nikiwaza mambo mengi sana lakini hakukuwa na kitu nilichowahi kuking’amua.
“Mama kumbuka lakini nina mke na tayari ana ujauzito wangu,” nilimwambia Mama maneno yaliyomfanya abadilike, alikuwa amekasirika.
“Mke wako mimi simtambui,” alisema Mama huku akiwa katika mnuno usiyomithilika.
“Mama,” nilimuita.
“Hakuna cha Mama hapa ninachotaka ni ukubali kumuoa Evelyne,” aliniambia Mama.
“Nimuoe kivipi Mama na wakati tayari nina mke wangu,” nilimjibu.
“Dominick umekuwa mwanangu yani unanijibu kama mwanao, naona umekuwa sasa baba, umekuwaeeeh,” aliniambia Mama huku akinipigia makofi ya kunidhihaki. Eti! Alikuwa akinipongeza kwa ukuaji wangu mpaka nimefikia hatua namjibu ninavyojisikia.
“Hapana Mama sio kama nakujibu ninavyojisikia lakini waka…” nilimjibu lakini kabla sijamaliza sentensi yangu ghafla! alinikata kauli.
“Lakini nini?” aliniuliza.
“Nampenda sana Mke wangu,” nilimjibu.
“Hivi ni nini unachoking’ang’ania kwa huyo mwanamke au amekupa nini mwanangu. Mimi nahisi sio bure kuna kitu hapa yule mwanamke atakuwa amekuloga,” aliniambia Mama huku akionekana kuithibitisha kauli yake kana kwamba alimuoma mke wangu wakati akiniloga.
Haikuwa kazi rahisi hata kidogo katika kunibadilisha mawazo yangu ya kumpenda Julieth kisha yakabadilika na kuwa chuki, nimchukie Julieth mwanamke wa maisha yangu. Hakika hiyo ilikuwa ni ndoto tena ndoto ya kufikirika kamwe isingeweza kutimia abadani.
Evelyne alikuwa ni msichana mrembo aliyejaaliwa kila sifa za kumshawishi mwanaume rijali. Sikutaka kulijali lile wowowo lake kubwa atembeapo nyuma alikuwa akiacha lawama wala sikutaka kuijali ile elimu yake pamoja na kazi aliyokuwa nayo, nilichokuwa najali kwa wakati huo ni uwepo wa Julieth wangu, mama wa mwanangu mtarajiwa. Sijui aliingia vipi mkataba na Mama yangu mpaka akaamini kuwa ningeweza kumuoa.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hilo lilikuwa ni jambo gumu sana, sikutaka kukubali kirahisi japo Mama yangu aliniambia kuwa asingeweza kunisamehe lakini haikuwa tatizo kwangu, niliendelea kubaki na msimamo wangu, sikutaka kukubaliana na jambo lile kwani kwa kukubali kwangu kungeweza kusababisha maumivu kwa mwanamke ambaye alikuwa akinipenda sana.
“Naomba unisamehe Mama, siwezi kufanya hivyo,” nilimwambia Mama yangu.
“Huwezi nini Dominick na wakati nimeshakwambia msahau kuhusu huyo mke wako,” aliniambia Mama.
“Mama kwanini unashiriki kuiangamiza ndoa yangu?” nilimuuliza.
“Unasemaje?” aliniuliza kwa ghadhabu.
“Mama kwanini unataka nimuache mke wangu?” nilimuuliza swali ambalo lilionekana kumkera sana, alikasirishwa mno na ni hapo ambapo hakutaka kuniona, aliamua kunifukuza na kuniambia nisimtafute tena katika maisha yake, nisimjue tena akazidi kwenda mbali akaniambia nitafute Mama mwingine ambaye angeweza kuyafurahia maisha ya ndoa yangu. Mama yangu alitokea akanichukia. Kuna kipindi niliwaza kuwa kama kweli yule alikuwa ni Mama yangu mzazi aliyenizaa sasa kwanini anichukie kiasi kile? Nilijiuliza swali ambalo sikuweza kupata jibu. Ndoa yangu ambayo aliikubali mwanzoni na kuipa baraka zote leo aliikataa na kuanza kunitafutia mwanamke mwingine, nikazidi kuwa katika maumivu makali mno, kuna wakati nilihisi wenda nilikuwa nikiigiza katika moja ya sinema ya kusikitisha na muda wowote muongozaji wa sinema hiyo angeweza kuniambia neno “Cut,” na hivyo ningesimama lakini haikuwa hivyo, nilikuwa katika maisha halisi, maisha ya changamoto niliyokuwa nikipitia ya ndoa yangu.
Niliamua kumuita Chrispine katika ofisi yangu kisha nikamsimulia mkasa mzima uliyokuwa umetokea na lile tukio zima la Mama yangu kunifukuza na kuniambia kuwa nitafute Mama mwingine ambaye angeweza kuifurahia ndoa yangu.
“Unajua bado nipo njia panda,” aliniambia Chrispine huku akionekana kuchanganyikiwa, wakati huo nilikuwa nikitengeneza simu ya mteja ambayo ilikuwa na tatizo la kubadilisha Screen.
“Upo njia panda kivipi?” nilimuuliza.
“Kwani Mama yako anachokitaka hasa ni nini?” aliniuliza.
“Anataka nimuoe Evelyne,” nilimjibu.
“Duh! Ndugu yangu kweli hapo upo katika wakati mgumu ila kuna kitu itabidi nikushauri.”
“Kitu gani?”
“Kuwa na maamuzi, unajua sifa kubwa ya mwanaume sio kula au kunyanyua vyuma hapana bali ni kuwa na maamuzi tu! maamuzi ndiyo yatakayoweza kukufanya ukabiliane na matatizo yote hayo yanayokuandama katika maisha yako,” aliniambia Chrispine.
Kwa kweli sikuwa tayari kumsaliti mke wangu, sikutaka kukubaliana na Mama yangu katika mpango wake wa kunishawishi nimuoe Evelyne mwanamke aliyenichagulia na kudai kuwa ndiye alikuwa chaguo sahihi la maisha yangu. Akili yangu haikutaka kukubaliana na hilo kabisa na kila nilipojaribu kulitafakari bado liliendelea kuniumiza tu! sikutaka kuamini kama zile zama za kuchaguliana mke au mume bado zilikuwepo.
Ama kweli wenye maneno yao waliposema kuwa kuwa uyaone hawakukosea, hakika nilikuwa katika ukubwa wa kuyaona maajabu yasiyosimulika.
Yote yaliyokuwa yametokea niliamua kuyachukulia kuwa kama changamoto za kimaisha ambazo mtu yoyote anaweza kukumbana nazo hata hivyo sikutaka kuonyesha kukata tamaa, niliendelea kuipigania ndoa yangu.
Sikuacha kuwasiliana na mke wangu kipindi alipokuwa nyumbani kwao akiendelea kuilea mimba, kila nilipomkumbuka nilimpigia simu na kuzungumza mambo mawili matatu kuhusu maisha yetu nay a mtoto ambaye tulikuwa tunatarajia kumpata, nilizungumza na wazazi wake pamoja na ndugu zake ambao walionekana kunipenda sana, hakukuwa na tofauti yoyote katika mazungumzo yetu na mara zote nilipozungumza nao sikuacha kuwaambia kuwa nilikuwa nikiwapenda sana na waendelee kumtunza mke wangu, kauli yangu hiyo kwao ilikuwa ni kituko, iliwaacha na kicheko kikubwa sana. Nakumbuka ndugu zake wengine walikuwa wakiniambia Julieth alikuwa amepata mume.
Maneno ya ndugu zake mke wangu pamoja na upendo wao ndiyo ulinifanya nizidi kusahau yale matatizo yaliyokuwa yakiniandama, kuna wakati sikutaka kuyakumbuka kabisa.
Naikumbuka ile sauti ya mke wangu Julieth iliyokuwa na upole uliyopitiliza, alipokuwa akizungumza na mimi sikujutia, nilitamani muda wa maongezi usiishe haraka kwani alikuwa akinifariji sana.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Usijali mume wangu ni muda mchache umebakia nitakuzalia mwanao,” aliniambia mke wangu kwa sauti legevu iliyoniacha katika weweseko la kimapenzi.
“Natamani sana mwanangu awe ni wa kiume,” nilimjibu huku nikiivuta pumzi nzito na kuiachia kwa pupa.
“Kwanini umependa awe wa kiume na asiwe wa kike?” aliniuliza Mke wangu.
“Kwasababu nataka nimuite jina la marehemu baba yangu,” nilimwambia.
“Jamani mimi nataka awe wa kike,” aliniambia.
“Akiwa wakike sitakuwa na rafiki hapo.”
“Kwahiyo wewe unataka rafiki?”
“Hahaha! Ndiyo ili nicheze naye na fujo zote anifanyie mimi.”
h“Kwani akiwa wakike hataweza kufanya hivyo?”
“Muda wote atakuwa kwa mama yake huo muda wa kucheza naye nitaupata wapi,” nilimwambia mke wangu maneno yaliyomfanya akacheka sana.
Hakuacha kuniambia kuwa katika maisha yake alikuwa akijivunia kuwa na mimi, nilikuwa nikimfanya awe ni mtu wa kutabasamu kila wakati. Maneno yangu, vituko vyangu vya kwenye simu vilimfanya kila mara anitafute, kuna wakati alinipigia simu kisha akaniambia kuwa ananipenda sana, nikatabasamu halafu na mimi nikamjibu kuwa nampenda pia, jibu hilo likamfanya afurahi sana, wakati huo nilikuwa katika ofisi yangu nikiendelea kuzitibu simu mbovu za wateja wangu.
****
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment