Simulizi : Penzi Lililosababisha Mauti
Sehemu Ya Tatu (3)
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya miezi tisa kutimia Julieth alifanikiwa kujifungua mtoto wa kike ambaye niliamua kumuita jina la Glory. Nilimpongeza sana mke wangu kwa zawadi ile ambayo alikuwa amenipatia katika maisha yangu, nilimwambia kila aina ya maneno mazuri siku hiyo.
“Yani mke wangu siamini, hivi ni kweli leo naitwa baba?” nilimuuliza Mke wangu nilipokuwa nikizungumza naye kwenye simu, wakati huo alikuwa bado yupo hospitalini.
“Ndiyo mume wangu amini sasa hivi unaitwa baba,” alinijibu mke wangu kwa sauti iliyokuwa na furaha.
“Asante mke wangu ila pia pole najua umeumia kwa ajili yangu, nakupenda sana laazizi wangu,” nilimwambia.
“Asante mume wangu,” alinijibu kisha na huo ndiyo ulikuwa mwisho wa mazungumzo yetu.
Nilitawaliwa na furaha sana, sikutaka kuamini kama kweli nilikuwa naitwa baba kwa wakati ule. Huo ulikuwa ni ukweli ambao ulizidi kuniweka katika wakati wa furaha muda wote, sikutaka kuamini kwa kweli.
“Dominick, Dominick unaitwa baba,” nilijiambia kisha nikaanza kucheka kama mwendawazimu.
Japo ilikuwa imepita miezi mingi tangu Mama yangu aliponifukuza nyumbani kwake na kuniambia kuwa nisimtambue lakini sikuacha kumpigia simu na kumueleza tarifa zile, alionekana kuzipuuzia kisha hakutaka kubaki kimya akaniambia kuwa namba ile niione kuwa kama kituo cha polisi, nisiizoee. Alifika mbali akaanza kumtukana mke wangu pamoja na mwanangu, malaika ambaye alikuwa hajui lolote kuhusu baba wala bibi katika hii dunia.
Nilizidi kushangazwa na matusi aliyokuwa akiyatoa Mama yangu dhidi ya mke wangu na mwanangu, nikajiuliza juu ya makosa ambayo walikuwa wameyafanya mpaka wakafikia hatua ya kutukanwa, hakukuwa na kosa lolote bali lilikuwa ni gubu la Mama yangu.
“Mama mbona unanitukania mke wangu na mwanangu kwani wamekukosea nini?” nilimuuliza Mama yangu baada ya matusi kumkoma.
Hakunijibu lolote mwisho akaamua kunikatia simu, kitendo kile kikaniweka katika hali ya sintofahamu, chuki alizokuwa nazo Mama yangu zikazidi kunishangaza. Nikajiuliza kama kweli yule alikuwa ni Mama yangu mzazi sasa kwanini anifanyie yale au hakuthamini uwepo wangu kama mtoto wake. Inamaana hakutaka kujua lolote kuhusu mwanaye, ukimya wangu wa miezi yote niliyokaa kimya tangu pale aliponifukuza hakutaka kujua lolote, hakutaka kunisikiliza japo kwa sekunde kadhaa ambazo ningezitumia vyema kuzungumza naye.
Niliguna mara baada ya kukatiwa simu kwa wakati ule, nilihisi kukosea namba, akilini nikajiambia kuwa labda yule hakuwa Mama yangu mzazi hivyo nikarudia kuitazama ile namba vyema. Naam! Ilikuwa ni namba ya Mama yangu Mzazi, sikutaka kuamini kama bado alikuwa na chuki na mke wangu tena chuki zake zilipitiliza kiasi kwamba akawa anamchukia na mwanangu ambaye hakuwa na hatia yoyote. Nilijaribu kumpigia simu kwa mara nyingine lakini haikupolewa mwisho akaamua kunizimia kabisa simu, ikawa haipatikani.
Sikutaka tena kuishughulisha akili yangu kuendelea kuwaza mambo ambayo yalikuwa yanaendelea kuniumiza kwa wakati ule ambao nilikuwa katika furaha, niliamua kuyaacha kama yalivyo na kama tatizo alikuwa ni Mama yangu nilipanga kutomsumbua tena kwa kumpigia simu wala kumtafuta kwa njia yoyote ile kama alivyokuwa akitaka nifanye. Nilifahamu fika kwa kuendelea kumsumbua ningezidi kujitafutia matatizo mengine.
****
Baada ya kupita miezi mitatu niliowaomba wazazi wa mke wangu niweze kumrudisha mke wangu na mwanangu kisha maisha yetu yaendelee kama kawaida. Hawakuonekana kunipinga kwa lolote, walinikubalia ombi langu kisha wakaniruhusu nimchukue mke wangu.
Baada ya kufanikiwa kumrudisha mke wangu pamoja na mwanangu nyumbani maisha yaliendelea vizuri, nilikuwa nikifanya kazi yangu ya ufundi simu huku nikitegemea kipato nilichokuwa nikikipata kiniwezeshe kuilea familia yangu ambayo ilikuwa imeongezeka.
Nilimpenda sana mwanangu Glory ambaye kila nilipomtazama kwa mbali nilikuwa nikiiona taswira ya Mama yangu mzazi, alifanana sana Mama Dominick.
Maisha yaliendelea huku mwanangu naye akizidi kukua vyema. Bado niliendelea kumficha mke wangu juu ya kile kilichokuwa kimetokea kwa Mama yangu lakini ni kama vile nilikuwa nikijaribu kuificha siri ambayo tayari ilikuwa ikifahamika na wengi, nilijidanganya.
Siku moja mke wangu aliniuliza swali ambalo liliniweka katika wakati mgumu sana wa kuweza kulijibu. Aliniuliza juu ya ukimya aliyokuwa nao Mama yangu pamoja na tukio la kutokuja kumuona mjuu wake. Lilikuwa ni swali gumu ambalo liliniwia vigumu kutoa jibu kwa uharaka, nilibaki kimya huku nikiendelea kumtazama usoni kana kwamba sikuwa nimemsikia swali alilokuwa ameniuliza.
“Mume wangu,” aliniita.
“Naam,” nilimuitikia.
“Mbona Mama yako hataki kuja kumuona mjuu wake?” aliniuliza.
“Labda itakuwa ni ubize wake lakini atakuja kumuona usijali,” nilimjibu kwa kumdanganya uwongo ambao haukuwa na mashiko hata kidogo.
“Ubize inamaana ndiyo akose hata nafasi ya kuja kumuona halafu mbona nikimpigia simu hapokei kuna nini?” aliniuliza tena akinitazama kwa macho yaliyogubikwa na kila aina ya wasiwasi.
“Hapokei?” nikamuuliza huku nikijifanya kushangazwa.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Vipi kwani wewe ulizungumza naye?”
“Ndiyo na tena aliniambia atakuja kumuona mtoto,” nilimwambia huku nikijitahidi kutomuonyesha tofauti yoyote ambayo ilikuwa imetokea na mwisho aliweza kuniamini, akaridhika na maneno yangu.
Maisha yaliendelea huku kila siku swali likiwa ni lile lile kuhusu Mama yangu, kwa kweli kuna kipindi nilikwazika moyoni hasa baada ya mke wangu kuzidi kung’ang’ania ujio wa Mama yangu. Kuna kipindi tulikuwa tukiingia katika ugomvi na sababu kubwa ilikuwa ni Mama yangu. Mke wangu alikuwa hajui ni kitu kilichokuwa kikiendelea, kuna wakati nikatamani nimueleze ukweli wa kile kilichokuwa kimetokea lakini nafsi yangu ilisita nikahisi ningeweza kuzua ugomvi ambao kwa kweli ningeshindwa kuuamua.
Kuendelea kuwaza na kujiuliza maswali lukuki bila kupata majibu yake ni sawasawa na kuteka maji katika tenga. Niliamua kumueleza Chrispine kuhusu janga lile lililokuwa limeikumba ndoa yangu kiasi kwamba kuna kipindi furaha ilikuwa ikitoweka kabisa.
“Unajua kuna kitu kimoja unakosea Dominick,” aliniambia Chrispine huku akionekana kunisikitikia.
“Nakosea nini sasa?” nilimuuliza.
“Julieth kwani ni nani yako?” aliniuliza swali ambalo jibu lake lilikuwa wazi kabisa, nilihisi kama alikuwa akinikejeli.
“Ni mke wangu inamaana hujui?” nilimjibu kwa kumuuliza swali.
“Nafahamu ila inawezekana ukawa umesahau kuwa Julieth ni mkeo ukahisi labda ni mpenzi wako,” aliniambia maneno yaliyoniacha njia panda.
“Una maana gani?” nilimuuliza.
“Kwa ninavyojua mimi mpaka mnaamua kuishi kama mke na mume katika ndoa basi maana nyie ni kitu kimoja sasa kutakuwa kuna maana gani ya ndoa wakati matatizo yako unayafanya kuwa siri usiyotaka hata mkeo kufahamu au unataka kuniambia unaamini katika ule msemo wa kipumbavu eti! Changu ni changu?” aliniuliza.
“Hapana sio kama naficha lakini,” nilimwambia lakini kabla sijamaliza akanikata kauli.
“Lakini nini?”
“Namjua vizuri mke wangu, sitaki kumuumiza.
“Kuna vitu vya kuficha lakini si kama hili, mueleze ukweli mkeo ili aweze kujua ni cha kufanya wakati mwingine unaweza ukaona upo sahihi kuficha lakini baadae itakuja kukugharimu maisha ohoo,” aliniambia Chrispine maneno yaliyokuwa na maana kubwa sana.
Nilijiona kuwa sahihi kwa kile nilichokuwa nikikifanya, kumficha mke wangu ukweli wa jambo lile, niliamua kuuvunja ukimya nikapanga kumueleza mke wangu ukweli wote uliyokuwa umetokea mpaka kufikia hatua Mama yangu kunitafutia mwanamke mwingine ambaye alinilazimisha nimuoe, kwa kweli sikujua nilitakiwa nianzie wapi kumuelezea mke wangu ambaye alikuwa hafahamu lolote.
Nilikuwa nimepanga kumueleza ukweli mke wangu wala sikutaka tena kumficha, maneno ya Chrispine yaliiingia vilivyo mpaka nikajiona kuwa nilikosea. Nilianza kwa kumuomba msamaha kwa kosa nililokuwa nimelifanya, akaonekana kushangazwa na msamaha wangu, alinitazama kama mtu aliyekuwa katika mshangao wa kuitazama sinema ya kutisha. Nilifahamu nilikuwa nimemuacha njia panda hasa baada ya kumuomba msamaha wa kosa ambalo sikulikiri mbele yake.
“Unaniomba msamaha kwani umenikosea nini mume wangu?” aliniuliza huku akiendelea kunishangaa, sikutaka kumuacha aendelee kuwa katika mshangao ule sajari na hali ya sintofahamu iliyokuwa imemkumba ghafla! nikaamua kumuelezea kila kitu kilichokuwa kimetokea.
Hakutaka kuamini hata kidogo kwa kile nilichokuwa nikimueleza kuhusu Mama yangu na mambo aliyokuwa akinifanyia, akabaki akiwa ameyatoa macho yake mithili ya mtu aliyekuwa katika kabali nzito baada ya kusikia kuwa nilitafutiwa mwanamke ambaye nililazimishwa nimuoe kipindi kile ambacho alikuwa nyumbani kwao akiilea mimba.
Kama ilivyokuwa kawaida yake machozi hayakuwa mbali, yalianza kumdondoka huku midomo yake ikionekana kumchezacheza, alikuwa na maneno ya kuniambia lakini yalikwamishwa na kilio kilichomkumba ghafla! Nikapata kazi ya kumbembeleza mpaka pale alipotulia ndipo alipoweza kuzungumza.
“Dominick kwanini mama yako ananichukia kiasi hiki nimemkosea nini mimi?” aliniuliza kwa sauti dhaifu iliyokaribisha kilio kingine, akaanza kulia tena, nikamsihi anyamaze huku nikimfuta machozi yake.
“Dominick hivi nimemkosea nini mimi mama yako?” aliniuliza huku machozi yakiendelea kumbubujika mashavuni mwake. Nilipomtazama alinisikitisha mno, nikajikuta maumivu yakianza kunichoma katika moyo wangu.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hapana mke wangu usiseme hivyo,” nilimwambia kwa kumkataza, sikujua hata nilikuwa namkataza nini wakati ukweli nilikuwa tayari nimeshamueleza.
“Dominick mama yako hanipendi, hampendi hata huyu mwanao hivi unafikiri tutaishi vipi?” aliniuliza huku machozi yakiwa yamemjaa katika macho yake.
“Julieth mke wangu najua Mama yangu hakupendi lakini mimi ndiye ninayekupenda hivyo naomba usijisikie kuwa mnyonge, umesikia mke wangu,” nilimwambia lakini hakunijibu lolote, alibaki kuwa kimya huku akiwa ameyaelekeza macho yake chini, machozi bado yalikuwa yanaendelea kumbubujika.
Haikuchukua sekunde chache akainua kichwa chake kisha akanitazama, maneno yangu yalionekana kumuumiza sana.
“Dominick najuta hata kumzaa huyu mtoto,” aliniambia huku akiyafuta machozi yake.
“Mke wangu ndiyo maneno gani hayo unanayoniambia kwanini hutaki kuwa mwelewa, nimekwambia usijali lolote,” nilimwambia.
“Hivi kwa haya yote uliyonieleza bado niendelee kuishi na wewe kweli au unasubiri mama yako aje aniue ndiyo ufurahi?”
“Julieth mke wangu.”
“Naomba uniache,” aliniambia huku akionekana kujawa na hasira, hakutaka hata nizungumze lolotr, hakuwa tayari kunisikiliza tena.
Nilianza kujilaumu kwa uamuzi ule niliyokuwa nimeuchukua wa kumueleza ukweli mke wangu, moyo wangu ukaanza kumchukia Chrispine, nilimuona kuwa kama adui mwingine wa ndoa yangu yani ushauri kwa wake badala uiokoe ndoa yangu ndiyo kwanza ulienda kuiharibu na kwa wakati ule nilikuwa katika ugomvi na mke wangu.
Nilijitahidi kuomba msamaha lakini hakukuwa na msamaha, nilichukiwa ghafla! na mke wangu hata ile furaha ambayo ilikuwa imetawala katika maisha yetu ikapotea, hakukuwa na aman tena.
“Kwanini hutaki kunielewa mke wangu?” nilimuuliza wakati huo nilikuwa nimepiga magoti.
“Nikuelewe nini Dominick we nenda kamuoe huyo mwanamke aliyekutafutia mama yako,” aliniambia huku hasira pamoja na wivu vikiwa vimemtawala.
“Nakupenda wewe mke wangu huyo mwanamke kama ningekuwa nina nia ya kumuoa ningemuoa tangu ulipokuwa nyumbani lakini sikuwa tayari kufanya hivyo, nakupenda mke wangu,” nilimwambia.
“Nimesema Dominick naomba uniachee,” aliniambia.
“Kumbuka tuna mtoto hivi kama tukianza kugombana wakati huu unafikiri mtoto atakuwa katika misingi ipi?”
“Dominick sitaki kukugombanishe na Mama yako nende ukamuoe huyo mwanamke ili umridhishe mimi niache na maisha yangu.”
“Hiyo ndoto isiyoweza kutimia, siwezi kukuacha wala siwezi kuruhusu ukapotea katika maisha yangu, wewe ni mke wangu tafadhali naomba unielewe.”
“Nikuelewe nini?”
“Nakupenda.”
“Na mama yako je?”
“Mama yangu asikuumize kichwa, sisi tuishi maisha yetu kama yeye hataki basi ila sisi ndiyo tumependana na tayari tupo katika ndoa hivyo hawezi kufanya lolote,” nilimwambia.
“Niahidi,” aliniambia hapa alikuwa tayari ameshaacha kulia.
“Sitokuacha kamwe katika maisha yangu mpaka mwishi wa pumzi zangu,” nilimwambia.
“Kweli?” aliniuliza.
“Namaanisha,” nilimwambia.
Tuliendelea na Maisha yetu huku huku mawazo ya mama yakiendelea kufutika, sikutaka Mama yangu aendelee kuwa kikwazo cha ndoa yangu, nilifanya kila niwezalo ilimradi ndoa yangu iendelee kuwa salama.
Baada ya kupita mwaka mmoja nilihisi kuwa na kila sababu ya kubadilisha kazi, majukumu yaliongezeka na kama unavyojua tena swala la kulea mtoto siyo kazi ya mzahamzaha. Pale Kariakoo nilipokuwa nikifanya kazi yangu ya ufundi simu haikuwa ikinilipa sana kama hapo awali, maisha yalibadilika na kila siku ilikuwa ni afadhali ya jana.
Kuna kipindi tulikuwa tukishindia uji siku nzima huku pesa niliyokuwa nikifanikiwa kuipata nilikuwa nikiichanga kwa ajili ya kulipa kodi ya chumba. Maisha yalikuwa magumu sana, ukichanganya na uwepo wa mtoto tuliyekuwa naye ndiyo kwanza kichwa kilizidi kuniuma.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilimueleza mke wangu juu ya mpango wangu wa kubadilisha kazi akaonekana kuniunga mkono lakini pia hakuacha kunishauri,
“Kwanini usiangalie kazi ambayo inalipa ndiyo uifanye?” aliniuliza.
“Ni kazi gani hiyo?” nilimuuliza.
“Kuna biashara nimeifikiria,”aliniambia.
“Biashara gani hiyo?”
“Kwanini usifanye biashara ya kuuza mitumba nasikia inalipa,” aliniambia mke wangu.
Kwa kweli biashara hiyo ya kuuza mitumba ilionekana kuniingia akilini, nilitabasamu baada ya kusikia hivyo, sikuacha kumshukuru mke wangu ambaye ndiye aliyenipa wazo lile, hakutaka kunishukuru zaidi aliniambia kuwa lile lilikuwa ni jukumu lake kama mke kuhakikisha nafanikiwa katika maisha.
“Hivi mtaji wake ni shilingi ngapi?” nilimuuliza.
“Inategemea na uwezo wetu ila kwa kuanza itabidi ukanunue mzigo pale Ilala sokoni kwa bei rahisi halafu utakuwa unaenda kuwauza wateja mitaani mpaka pale ambapo tutapata mtaji kisha na sisi tutakuwa tukinunua kwa jumla na kuziuza kwa upana,” aliniambia mke wangu maneno ambayo niliyapitisha katika serikali ya ubongo wangu.
****
Niliamua kufanya rasmi biashara ya kuuza nguo za mitumba mitaani, biashara ambayo ilifanya watu wengi wanishangae kipindi ambapo nilikuwa nikianza hata rafiki yangu Chrispine alinishangaa sana na kuniona kuwa nilifanya maamuzi ya kukurupuka bila kuhitaji ushauri.
Kama walivyosema wahenga kuwa katika wengi kuna mengi pia ndivyo ilivyonitokea kipindi ambapo naanza kufanya biashara yangu ya kuuza nguo za mitumba mitaani.
Nilianza kusikia maneno ya watu wakisema kuwa nilifilisika kiasi kwamba niliamua kuacha kazi yangu ya ufundi simu Kariakoo nikawa muuza mitumba. Kila mtu alikuwa na lake la kusema.
Miongoni mwa maneno ambayo siwezi kuyasahau katika maisha yangu nayakumbuka mpaka leo katika kumbukumbu zangu ni siku moja nilisikia watu wakinizungumzia vibaya, walikuwa wakisema kuwa nililogwa na mke wangu ambaye alikuwa hana kazi yoyote Ati! Limbwata la mke wangu ndiyo lilikuwa linaniongoza niende kufeli katika maisha yangu ili tuwe sawa.
Maneno hayo yaliniumiza sana moyoni, sijui ni kwanini ila nilishangaa nikikosa uvumilivu, machozi yakaanza kunidondoka mfululizo. Nilikuwa nikilia machozi yaliyochanganyika na maumivu yaliyo ndani ya moyo wangu.
Siku moja majira ya usiku niliamua kumueleza mke wangu juu ya maneno niliyoyasikia kwa watu wakitusema vibaya lakini mke wangu mimi aliyeumbwa na upole, roho yake iliyochanganyika na ustahimilivu hakuacha kunena japo maneno ya kishujaa akiniambia mimi mume wake ambaye uvumilivu ulikuwa tayari umeshanishinda, kama ni maji basi yalikuwa yamenifika kooni.
“Mume wangu najua sio wote watakao tupenda kuna wengine watatuchukia hata hivyo hutakiwi kukata tama kumbuka tuna mtoto na anatutegemea kwa kila kitu, mimi sina kazi yoyote mume wangu angalau wewe umepata nafasi hii ya kuuza mitumba basi ifanye kwa bidii ili baadae izae matunda,” aliniambia mke wangu wakati huo alikuwa akiandaa chakula mezani, alikuwa amepika ugali na mboga ya kisamvu.
“Miongoni mwa vitu ambavyo najivunia katika maisha yangu ni kuwa na wewe katika maisha yangu, sijuitii kukuita mke wangu kwani kila ninapolitamka neno hili linanipa picha halisi ya mwanamke sahihi aliyeumbwa kwa ajili ya maisha yangu,” nilimwambia huku nikimtazama alipokuwa akininawisha mikono tayari kwa kula chakula alichokiandaa usiku ule.
“Ni wajibu wangu kama mkeo kuhakikisha nakuwa mstari wa mbele kutetea hitaji la moyo wako, kutetea ndoto yako na kuhakikisha kila ulilolipanga nakuwa nyuma yako kwa kila hali mpaka litimie,” aliniambia alipomaliza kuninawasha mikono kisha na nikampokea jagi pamoja na lile beseni dogo aliloninawishika, nikamnawisha.
“Asante mume wangu,” aliniambia mara baada ya kumaliza kumnawisha mikono yake, akaketi chini kisha tukaanza kula kwa pamoja, nilianza kwa kumlisha tonge moja, akacheka wakati huo mtoto wetu alikuwa ameshalala.
“Glory ameshiba kweli?” nilimuuliza mke wangu nilipomkumbuka mwanangu.
“Ndiyo nilimnywesha uji, ameshiba sana,” alinijibu mke wangu kisha tukaendelea na zoezi letu la kula ugali na mboga ya kisamvu iliyopikwa ikapikika.
Kila nilipokuwa nikimtazama Julieth usoni nilizidi kuiona taswira ya mwanamke mvumilivu ambaye alivumilia mambo mengi sana japo kuna kipindi alionekana kuchoka na kukata tamaa lakini hiyo haikuwa sababu ya kufanya mapenzi yetu yafutike, ndoa yetu ivunjike, hilo lilikuwa ni jambo gumu mno kuweza kutokea.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Niliendelea na biashara yangu mpaka pale ambapo nilifanikiwa kupata mtaji uliyoniwezesha na mimi kununua mabeli nikawa nauza kwa jumla jumla. Ilikuwa ni hatua nzuri niliyoipiga katika biashara yangu hiyo ukilinganisha na mwanzo ambapo nilipoanza.
“Hivi umewezaje kufanya haya yote?” lilikuwa ni swali la Chrispine huku akionekana kutoamini kwa hatua niliyokuwa nimefikia katika biashara yangu ya kuuza mitumba. Alikuwa bado akiendelea kuuza Cd katika duka lake Kariakoo, kwa upande wake biashara ilionekana kuwa ngumu mno.
“Ni mipango ndugu yangu,” nilimwambia.
“Mipango ipi tena wakati naona sasa hivi mambo yako sio mabaya,” aliniambia Chrispine huku akicheka.
“Kwa kweli mimi sikuwahi kuamini kama nitafanikiwa kufika hadi huku ila yote haya shemeji yako ndiyo kafanya mpaka yametimia,” nilimwambia kisha akaonekana kama kutoelewa lolote, nikaamua kumuelewesha kwa kirefu, akaonekana kuvutiwa na biashara ile niliyokuwa nikiifanya.
“Itabidi na mimi nianze kuuza mitumba aisee kule biashara imekuwa ngumu,” aliniambia Chrispine maneno ambayo alionekana kuyamaanisha kwa kila kitu.
Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa kufanya biashara ya kuuza mitumba na Chrispine, aliamua kuniongezea mtaji na sasa tukawa kitu kimoja, tukaamua kufungua duka la pamoja Kariakoo, tukawa tunauza na kununua kwa wingi. Biashara ikaonekana kukuwa kila siku na tulikuwa tunapata faida kubwa sana.
Baada ya kupita miaka mitano biashara ya kuuza mitumba ilikuwa imetupa mafanikio makubwa sana. Nilikuwa nimefanikiwa kufungua duka langu la nguo pia niliamua kumfungulia mke wangu saluni ya kike pamoja na mgahawa na biashara zote hizo nilimuweka yeye ndiyo aongeze. Julieth alifurahi sana hakutaka kuamini kama kweli na yeye alikuwa anaitwa boss.
Wakati huo Mtoto wetu Glory alikuwa na umri wa miaka saba na tayari alikuwa ameshaanza kusoma darasa la kwanza katika shule ya msingi ya Ali Hassan Mwinyi.
“Jamani Dominick mume wangu nakupenda sana,” aliniambia huku akiwa amenikumbatia kwa furaha nilipomueleza kuwa biashara zote alitakiwa aziongeze.
“Nakupenda pia mke wangu,” nilimwambia kisha nikambusu shingoni.
Nakumbuka mpaka kufikia wakati huo nilikuwa nimefanikiwa kununua kiwanja maeneo ya Vikindu na nilikuwa katika mipango ya kuanza kujenga, sikutaka kumwambia mke wangu kwa haraka, nilipanga kumfanyia Surprise kama wazungu wanavyosema.
Baada ya miezi kadhaa kupita huku biashara zikiendelea kupamba moto mke wangu alianza kuonekana kuhitaji kitu katika maisha yake, kuna kitu alionekana kukisubiri kwa muda mrefu sana na hakikuweza kutimia, aliamini kwa wakati ule ndiyo ulikuwa muda muafaka wa yeye kunieleza ili niweze kumtimizia.
Alitamani sana kuwa mwandishi wa habari, ndoto yake kubwa ilikuwa ni siku moja kuwa mwandishi wa habari mkubwa sana hapa Tanzania. Hakutaka kunificha lolote lile lililokuwa likiendelea kumuumiza moyoni mwake, alinieleza kila kitu na mipango yake ya kurudi shule ili aweze kuitimiza ndoto yake hiyo ambayo aliishi nayo kwa muda mrefu sana.
“Una uhakika utaweza kufanya vizuri?” nlimuuliza mara baada ya kunielezea malengo yake kwa wakati ule.
“Ndiyo mume wangu natamani sana kuwa mwandishi wa habari wa kidunia,” alinijibu huku akionekana kuwa na munkari kupita kawaida.
“Umepanga uanzie wapi sasa?” nilimuuliza.
“Itabidi nirudi shuleni ili nitafute cheti cha form four halafu nikajiunge na chuo kinachofundisha masomo ya uandishi wa habari,” alinijibu huku akionekana kudhamiria kufanya kweli yale aliyokuwa akinieleza.
Kwa kweli nilishindwa kumkatalia mke wangu kwa yale aliyokuwa akinieleza, maneno yake niliyachukulia kuwa kama zaidi ya taarifa muhimu ambayo nilitakiwa kuisikiliza kwa umakini na kuizingatia.
Niliamua kumkubalia kwa kila kitu alichokuwa akikihitaji kwa wakati ule kisha nikaanza kupanga mipango ya kumrudisha shule mke wangu. Niliamua kumpeleka katika elimu ya watu wazima Qualifying Test (QT) ambapo aliweza kusoma na baadae kufanikiwa kumaliza na kupata cheti cha kidato cha nne. Hiyo ilikuwa ni zaidi ya furaha kwa mke wangu, hakutaka kuamini kama alifanikiwa kusoma na kupata cheti cha kidato cha nne.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Upendo ulizidi kuongezeka pale ambapo niliamua kumpeleka chuo cha uandishi wa habari kilichojulikana kwa jina la Daresalaam school of Journalisim kilichopo Ilala. Akafanikiwa kusoma kozi ya uandishi wa habari na utangazaji kwa muda wa miaka mitatu akamaliza.
Furaha ikazidi kumtawala mke wangu ambaye alitamani sana siku moja kuonekana kwenye runinga akitangaza habari au kipindi chochote ambacho angeweza kupewa akiendeshe.
“Kuna siku utaniona kwenye runinga mkeo nikitangaza taarifa ya habari,” aliniambia Julieth tulipokuwa tukitazama taarifa ya habari.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment