Search This Blog

Sunday, July 10, 2022

PENZI LILILOSABABISHA MAUTI - 4

 







    Simulizi : Penzi Lililosababisha Mauti

    Sehemu Ya Nne (4)

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    “Usijali mke wangu tumuombe sana Mungu kwani kwa Mungu hakuna kinachoshindikana,” nilimwambia huku nikijaribu kumkumbusha uwepo wa Mungu katika maisha yetu.

    “Namuomba sana Mungu azidi kutujaalia maisha mazuri pamoja na mtoto wetu aendelee kukua vyema ili siku moja ajivunie kuwa na wazazi kama sisi,” aliniambia Julieth.

    “Hilo ndilo jambo la msingi mengine huwa yanakuja yenyewe,” nilimwambia.

    “Ila kuna kitu nataka nikuombe mume wangu,” aliniambia Julieth huku akiwa ananitazama kwa macho ya kuniuliza nikwambie.

    “Kitu gani gani hicho?” nilimuuliza huku nikijiweka tayari kusikia hicho kitu.

    “Nataka unichagulie jina zuri ambalo ungependa nilitumie nitakapokuwa mtangazaji,” aliniambia.

    “Mimi napenda utumie jina lako hilo hilo.”

    “Hapana itabidi nibadilishe jina mume wangu ili liwavutie wengi hata nitakapokuwa natangaza wapende aina ya utangazaji wangu.”

    “Unataka ujiite jina gani sasa?”

    “Nataka unichagulie wewe,” aliniambia Julieth kisha nikapata kazi ya kuanza kufikiria jina ambalo ningeweza kumpa na likampendeza.

    Kichwani yalianza kunijia majina ya watangazaji lukuki ambao walikuwa wakivuma sana kwa aina ya utangazaji wao hata katika majina yao yalivutia mno.

    “Sasa nikuite nani?” nilimuuliza.

    “Fikiria jina lolote mume wangu,” aliniambia Julieth huku akiwa umeupindisha mdomo wake kuashiria kuwa alikuwa ameanza kukasirika

    “Ok ngoja nikuchagulie,” nilimwambia kisha nikanyamza kidogo nikafikiria halafu nikaendelea kuzungumza.

    “Jiite basi Julie Pretyy,” nilimwambia huku nikitabasamu, nilifahamu fika nilimpa jina ambalo halikumpendeza, nikaamini hatalipenda hata kidogo. Ajabu akaonekana kulipenda, alifurahi sana kusikia hivyo.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ooooh! My God jina zuri sana nimelipenda mume wangu,” aliniambia Julieth mke wangu huku furaha ikiwa imemtawala.

    Maisha yalibadilika kwa kiasi fulani kutoka katika maisha ya kushindia mlo mmoja kwa siku mpaka kufikia wakati ule ambapo tulikuwa tunauwezo wa kubadilisha mboga.

    Kila nililoamua kulifanya kwa mke wangu niliamua kulifanya kwa moyo mmoja wala sikutaka mtu wa kunishauri lolote katika hilo. Niliamini katika mapenzi ya dhati ambayo nilikuwa nayapata kwa mke wangu, mapenzi hayo ndiyo yaliyosababisha nikaamua kumsomesha mpaka kufikia wakati akamaliza na sasa alikuwa akisubiri kupata kazi.

    Alianza kuhangaika kutafuta kazi ya utangazaji katika vituo mbalimbali vya runinga na redio, kila alipokuwa akipeleka barua kwa ajili ya maombi ya kazi alikuwa akikosa, hilo likazidi kumuweka katika wakati wa mawazo, kuna kipindi alianza kukata tamaa, nikamsihi hakutakiwa kufanya hivyo kwani kila kitu kilikuwa na wakati wake hivyo asichoke kusubiri.

    “Siamini kama kweli ndoto yangu itatimia,” aliniambia.

    “Kwanini isitimie mke wangu muamini Mungu kila kitu kinawezekana,” nilimwambia.

    “Kila ninapoenda kuomba kazi nakataliwa halafu bado unaniambia kila kina wakati wake hivi ni wakati gani huo usiyoweza kutimia.”

    “Mke wangu hutakiwi kusema hivyo bali unachotakiwa ni kuwa na subira, kila kitu kitatimia,” nilimwambia.

    Julieth alizidi kuhangaika kutafuta kazi huku na kule, hakuchoka na kama Mungu siku moja aliweza kupigiwa simu na namba ya simu ya mezani. Ilikuwa ni simu iliyomtaarifu kuwa alikubaliwa kufanya kazi katika kituo kituo cha habari kilichojulikana kwa jina la HIZA TV.

    Taarifa hiyo ilileta furaha nyingine ndani ya nyumba bila kujua kuwa baadae nilikuwa naenda kumwaga machozi.

    Hatimaye mke wangu akafanikiwa kuanza kazi katika kituo hicho cha habari cha televisheni kilichokuwa maarufu sana. Nilifurahi sana kuona nimefanikiwa kuzitimiza ndoto za mke wangu kipenzi ambazo alionekana kuishi nazo kwa muda mrefu bila kutimia, hilo likanifanya nizidi kujivunia sana wala sikuona sababu ya kuacha kumpongeza mke wangu, nikampongeza kwa kumuahidi kuwa shabiki yake namba moja hasa katika kazi yake ya utangazaji redioni pamoja kwenye televisheni.

    Julieth alinishukuru sana, hakutaka kuamini kama kweli alifanikiwa kusoma na kwa wakati ule alikuwa ameanza kazi ya utangazaji. Kila alipokuwa karibu yangu alizidi kunishukuru sana.

    “Hapana mke wangu hupaswi kunishukuru kiasi hicho,” nilimwambia mke wangu.

    “Yani siamini mume wangu kama kweli nimekuwa mtangazaji, ndoto yangu imetimia,” aliniambia huku furaha ikionekana kutawala uso wake, alifurahi mno.

    Kwa kipindi hicho mtoto wetu Glory alikuwa ameshafika darasa la tano na katika upande wa malezi bora hatukuwa nyuma, tulihakikisha tunamlea katika malezi yaliyokuwa bora, hilo naweza kujivunia kwa wakati ule, niliishi vizuri na familia yangu wala hakukuwa na tatizo lolote.

    Tulikuwa bado tukiishi katika nyumba ya kupanga lakini maisha yetu yalikuwa mazuri, mahitaji yote muhimu tulikuwa tukiyapata tena kwa wakati.

    Sikuacha biashara yangu ya kuuza nguo za mitumba, niliendelea kuifanya huku nikiamini kuwa ilikuwa ndiyo kazi yangu mama ambayo ilinizalishia biashara nyingine ndogo ndogo.

                                                  ****

    Mke wangu alikuwa ni mtangazaji wa redio na TV katika vipindi vyake pendwa alivyokuwa akiviendesha. Alipendwa sana hasa kutokana na aina ya utangazaji wake, hilo lilinifanya nijivunie sana na kujiona kuwa mtabiri ambaye nilitabiri ukweli uliyoweza kutokea katika maisha ya kweli.

    Kazi yake utangazaji ikaanza kumuweka bize mke wangu mpaka akawa anakosa muda wa kusimamia biashara alizokuwa akiziongoza hapo awali. Ikabidi nisaidiane nae katika kuziongoza biashara hizo wala hakukuwa na tatizo lolote lile.

    Niliamini majukumu ya kikazi aliyonayo ndiyo yaliyokuwa yakimsababisha mpaka akawa anakosa muda wa kufuatilia biashara.

    “Mume wangu usione nakuwa mzembe kufuatilia biashara siku hizi nakuwa bize sana,” aliniambia Julieth huku akionekana kutingwa na majukumu ya kikazi.

    “Mke wangu naelewa hali uliyokuwa nayo kwasasa wala usijali,” nilimwambia.

    “Nafurahi mume wangu kwa kunielewa,” aliniambia.

    Hakukuwa na mtu niliyekuwa namuamini kama mke wangu, nilimuamini kupita kawaida wala sikuwa tayari kuona anatokea mtu anakuja kuuvunja uaminifu huo. Nilimpenda sana na pia nilimuheshimu kwa kila kitu.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Katika kumbukumbu zangu sikumbuki kama kuna siku niliwahi kumsaliti mke wangu wala kuwa na chembechembe zozote za kutaka kumsaliti, nilijiheshimu sana na ndoa yangu niliyokuwa naipenda kuliko kitu chochote kile.

    Uaminifu niliyokuwa nao kwa mke wangu ulimshangaza mpaka Chrispine japo yeye ndiye aliyekuwa mtu wangu wa karibu wa kunishauri mambo mengi sana kuhusu ndoa yangu.

    “Dominick kama ikitokea siku watu wakaamua kutoa tuzo za uaminifu basi  katika wanaume kumi bora wewe huwezi kukosekana,” aliniambia Chrispine huku akionekana kutabasamu.

    “Kwanini unasema hivyo?” nilimuuliza.

    “Sijui nikwambie nini ili kiukweli wewe ni muaminifu sana na ndoa yako,” aliniambia.

    “Ni kweli unajua unapoamua kuingia katika ndoa inabidi ukubali kuacha mambo yote ambayo hutakiwi kuyafanya wakati ukiwa ndani ya ndoa,” nilimwambia.

    “Julieth kapata mume aisee,” aliniambia Chrispine maneno ambayo yakatufanya wote tukacheka.

    Siku hiyo tulizungumza mambo mengi sana kuhusu maisha, ndoa, biashara ila lilipofikia suala la Chrispine kumsifia mke wangu juu ya kazi yake ya utangazaji aliyokuwa akiifanya pamoja na changamoto ambazo angeweza kukutana nazo kidogo nilianza kuingiwa na wasiwasi lakini baada ya dakika kadhaa kupita ule wasiwasi uliniondoka.





    “Mbona kama umesita kidogo?” aliniuliza Chrispine.

    “Hapana,” nilimjibu.

    “Ila inabidi uwe makini sana na mkeo unajua hawa viumbe hawakawi kubadilika sasa hivi ameshakuwa mtangazaji wa tv na redio, anakutana na watu wengi maarufu na wenye uwezo wa kifedha zaidi yako, inabidi uwe makini sana usipoangalia unaweza kuja kuyadondosha machozi baadae halafu ukakosa wa kukufuta,” aliniambia Chrispine.

    Sikutaka kuyachukulia maneno ya Chrispine kuwa kama ya kufikirika na kwamba yasingeweza kutokea kwa mke wangu, kwa kipindi kile ambapo alikuwa akinieleza kuhusu changamoto ambazo angeweza kukutana nazo mke wangu pamoja na aina ya watu mashuhuri aliyokuwa akikutana nao nilianza kuingiwa na wasiwasi, niliamini kuna ukweli ambao ulikuwa ukiishi katika maisha ya mke wangu ambapo kwa muda mfupi tangu alipoianza kazi yake ya utangazaji nilianza kuyaona mabadiliko makubwa sana.

    Alianza kuchelewa kurudi nyumbani na kila nilipokuwa nikimuuliza alinijibu kuwa alipangiwa ratiba ya kutangaza usiku redioni jibu ambalo likanifanya nikubali bila kipingamizi chochote.

    Nakumbuka kuna kipindi nilikuwa nikimsikiliza mke wangu redioni alipokuwa akitangaza na hata wakati mwengine kwenye Tv, nilijikuta nikianza kuwa mpenzi wa kusikiliza redio na kufuatilia vipindi vilivyokuwa vikirushwa kwenye Tv na yote sababu alikuwa ni mke wangu.

    Nilizidi kumuamini mke wangu hata ule wasiwasi wangu ambao ulikuwa umeanza kuniingia moyoni ukaanza kupotea, sikutaka kumuonyesha mke wangu tofauti yoyote, niliamua kuyapuuzia mawazo yote mabaya niliyokuwa nikimuwazia mke wangu.

    “Dominick mume wangu ni nini hivyo embu punguza wivu,” nilijiambia kisha nikajipiga kofi kuashiria kuwa nilikuwa katika mawazo ya kijinga.

    Nilimuamini mke wangu kwa kuwa hakukuwa na sinema iliyokuwa ikiendelea nyuma ya pazia ambayo sikuwa nikiifahamu, alikuwa akinieleza ukweli wa kila kitu kilichokuwa kikiendelea katika maisha yake.

    Ukweli wake aliyokuwa akinieleza juu ya wanaume waliyokuwa wakimsumbua ofisini ukanifanya nizidi kumuamini kabisa. Nikawa nakesha kumuombea kwa Mwenyezi Mungu azidi kumlinda na pepo baya la ngono ambalo lingeweza kumuingia. Sikuwa tayari kupokea maumivu ya usaliti moyoni.

    “Mume wangu niamini nakupenda sana na ndiyo maana nakueleza ukweli,” aliniambia Julieth.

    “Nakuamini sana mke wangu kuhusu hilo ondoa shaka kabisa,” nilimwambia huku nikiwa msisitizo wa maneno yangu.

    “Mkeo ni mzuri sana eti na ndiyo maana nasumbuliwa na wengi ila mimi najiheshimu na kujilinda mume wangu,” aliniambia  Julieth. Maneno yake ya upole yaliyoandamana na maana ya kile alichokuwa akinieleza yalizidi kuniteka vilivyo.

    Alipoanza kubadilisha mavazi yake ya heshima na kuvaa nguo fupi nilimuuliza lakini hakukuwa na jibu lingine alilonijibu zaidi ya kuniambia kuwa kazi yake ilimuhitaji awe katika mavazi yale ili azidi kuwavutia mashabiki wakipende kipindi chake. Sikutaka kujifanya mjuaji sana, niliamua kumuacha kama alivyo maadam aliniambia kuwa ananipenda na kuniheshimu basi hiyo ndiyo ilikuwa ngao niliyoishikilia siku zote.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Sasa kama alikuwa akinipenda kulikuwa kuna sababu gani za kutomuamini? Hilo ndiyo swali kubwa lililonijia katika kichwa changu, sikuwa na jibu kamili zaidi ndiyo kwanza nilizidisha mapenzi kwa mke wangu.

    Baada ya kupita miezi kadhaa siku moja majira ya usiku mke wangu alirudi nyumbani akiwa na gari aina ya Land cruiser Prado lenye rangi nyeusi. Nilibaki katika mshangao mara baada ya kumuona mke wangu. Sikushangazwa na uzuri wa mke wangu ambao kila siku ulizidi kuongezeka bali kitu kilichonishangaza ni aina ya gari alilokuja nalo. Nikakadiria hesabu ya miezi aliyokuwa nayo tangu alipoanza kazi yake ya utangazaji, alikuwa na miezi mitatu tu.

    “Yaani ndani ya miezi mitatu ndiyo anunue gari lenye thamani kubwa kiasi hiki?” nilijiuliza swali ambalo jibu lake alikuwa nalo mtu mmoja tu! alikuwa ni mke wangu. Sikutaka kupoteza muda niliamua kumuuliza.

    “Hili gari umetoa wapi?” nilimuuliza mara baada ya kushuka kwenye gari, nikashangazwa na kioja kingine. Ilikuwa ni udereva wake.

    “Unajua kuendesha gari siku hizi?” nilimuuliza tena na sasa yalikuwa ni maswali mawili aliyotakiwa kuyajibu.

    “Hee! Mume wangu hata salamu,” aliniambia huku akionekana kujiamini.

    “Nimekuuliza hili gari umetoa wapi?” nilimuuliza.

    “Nimehongwa,” alinijibu kwa dharau.

    “Unasemaje?” nilimuuliza kwa ghadhabu.

    “Unataka nikujibu nini wewe mwanaume,” aliniambia maneno ambayo yalinishangaza sana.

    Kwa sinema aliyonionyesha Julieth ni dhahiri alikuwa amebadilika, sikutaka kuamini kile nilichokuwa nikikishuhudia, nilimtazama mara mbilimbili huku nisijue ni nini nilitakiwa nifanye.

    Aliponiambia maneno yale hakutaka kuendelea kuzungumza na mimi, aliongoza moja kwa moja mpaka ndani. Niliendelea kushangazwa na sinema niliyokuwa nikiendelea kuishuhudia, nikalitazama lile gari hakika lilinifanya nibaki katika wakati wa maswali yaliyokosa majibu.

    “Ni nini hiki kinachotokea katika maisha yangu?” nilijiuliza kimoyomoyo kisha sikupata jibu lolote zaidi nilizidi kupandwa na hasira na nilijiapiza kuwa liwalo na liwe.

    Niliingia ndani huku hasira zikiwa zimenitawala kichwani mwangu, nikamkumbuka mwanangu Glory ambaye alikuwa tayari ameshalala, sikutaka kufanya vituko vyovyote mbele yake hata vya kuigiza, niliamua kufanya hivyo ni kutokana na malezi bora ambayo nilipanga kumpa, sikutaka niwe chanzo cha kuyaharibi maisha yake kwa kumuathiri kisaikolojia.

    Licha ya kuwa hasira zilikuwa zimenitawala lakini sikuwa na budi ya kuzipunguza, nakumbuka nilipanga kumpiga Julieth lakini nilishindwa kufanya hivyo. Nilipoingia chumbani nilimkuta tayari ameshalala tena usingizi haswaa! nikajiuliza iliwezekanaje huo usingizi ukampata kwa dakika chache ambazo alikuwa ameingia ndani tena sidhani kama hata kuoga alikuwa ameoga. Tukio hilo lilizidi kuniudhi.

    “Mke wangu,” nilimuita lakini hakuitika, nikanyamaza kama muda wa sekunde tano halafu nikamuita tena ndipo hapo alipoweza kuitika.

    “Unasemaje mimi nataka kulala nimechoka,” aliniambia maneno ambayo yalinizidi kunikwaza sana moyoni.





    “Unasemaje?” nilimuuliza.

    “Sitaki usumbufu nataka kulala nimechoka,” aliniambia kwa sauti ya dharau maneno ambayo yalizidi kunichoma moyoni mwangu. Siwezi kusema ni maumivu kiasi gani ambayo nilikuwa nikiyapata kwa wakati huo  ni kama vile kulikuwa na msomaji ambaye alikuwa akinisimulia simulizi nzuri ya kimapenzi na kwa wakati ule alikuwa ameufikia ukurasa uliyobeba maumivu makali mno.

    Nilivumilia mambo mengi sana na bado niliendelea kuyavumilia, naweza kusema kati ya wanaume waliyokuwa na mapenzi ya dhati kwa wake zao basi nilikuwa miongoni mwao. Licha ya mateso yote niliyokuwa nikipitia bado niliendelea kuvumilia huku nikijipa moyo yalikuwa na mwisho wake. Siku hiyo ikapita.

                                                                              ****

    Siku iliyofuata majira ya asubuhi mara baada ya Glory kwenda shuleni niliamua kumuuliza mke wangu kwa kile kilichokuwa kimetokea siku iliyopita.

    “Bado siamini kama umeninunia mke wangu hivi ni nini kimetokea?” nilimuuliza.

    “Huamini nini sasa?” aliniuliza.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mbona jana nakuuliza kuhusu gari ulilokuja nalo hujanijibu lolote?”

    “Unajua wewe ni mwanaume wa ajabu sana yani nakushangaa Dominick badala ya kunipa pole mkeo narudi kutoka kazini wewe una kazi ya kuulizia gari nimetoa wapi hivi umesahau kuwa mkeo sasa hivi nafanya kazi?” aliniuliza.

    “Julieth mke wangu mbona mapema sana yani miezi mitati tu! umeshanunua gari?”

    “Ni kitu gani ambacho unashindwa kukiamini hapo au unataka nizungumze lugha ipi ili uweze kunielewa.”

    “Jana unakumbuka nilipokuuliza ulinijibuje?”

    “Ndiyo nakumbuka.”

    “Kwanini ulinijibu vile?”

    “Unajua uliniudhi sana wewe hujui tu!” aliniambia Julieth kisha nikashindwa kuelewa ni kitu gani ambacho nilimuudhi.

    Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa kuchanganywa na mapenzi, mapenzi yalikuwa yakinipeleka puta, nilishindwa kuamua lolote kwa mke wangu, alikuwa ameiteka nafasi kubwa sana.

    Nilimkumbuka Mama yangu ambaye mpaka kufikia kipindi hicho sikuwa nafahamu lolote kuhusu yeye. Tangu alipoweza kunifukuza nyumbani kwake na kuniambia kuwa nisimtafute kwa namna yoyote huku sababu kubwa ikiwa ni mke wangu kwa kweli sikuweza kumtafuta.

    Nilikaa miaka mingi sana bila kuwasiliana na Mama yangu, nilifanya yote hayo nikiamini Mama yangu alikuwa na makosa. Kitendo cha kumchukia Mke wangu na kudai kuwa hakuwa mwanamke sahihi katika maisha yangu hakika kilinifanya nimchukie sana.

    Nilimchukia mara baada ya kupata ushauri wa rafiki yangu Chrispine. Maneno yake yalinifanya nijione kuwa bora zaidi ya kila kitu na sikutakiwa kumsikiliza Mama yangu kwa lolote lile ambalo alikuwa akiniambia.

    “Hivi nimefanya ujinga gani mimi?” yalikuwa ni majuto kwangu, nilianza kuona thamani ya maneno ya Mama yangu, Mama Dominick ambaye alikuwa ni mjane.

    Kwa kipindi cha miaka yote hiyo sikufahamu ni nini kilichokuwa kikiendelea katika maisha yake, nilimsusa kwa kiasi kikubwa sana na kwa kile kilichokuwa kimetokea katika ndoa yangu nilianza kuukumbuka uwepo wake, niliamini alikuwa na maneno mengi sana ya kunieleza mimi mwanaye.

    “Nataka nijiandae niende zangu kazini,” aliniambia Julieth kisha akafanya kama alivyoniambia.

    Bado nilizidi kuwa katika kiza kinene na sikujua ni nini kilichokuwa kikiendelea nyuma ya pazia.

    “Julieth embu naomba tuzungumze kuhusu hili suala kabla hujaondoka,” nilimwambia alipomaliza kujiandaa na kwa wakati huo alikuwa anataka kuondoka.

    “Nina haraka zangu please naomba tutazungumza nikirudi,” aliniambia huku akiitazama saa yake ya mkononi kuashiria alikuwa amechelewa.

    “Dakika chache nipe ili niweze kuzungumza na wewe,” nilimwambia.

    “Kwa sasa sina muda huo nina haraka labda tufanye kesho,” aliniambia.

    “Kwanini hutaki kunisikiliza.”

    “Sio sitaki tatizo lako sio muelewa,” aliniambia kisha akaondoka bila hata kuniaga.

                                                       ****

    Mateso ambayo nilikuwa nikiyapata kwa kweli siwezi kuyasimulia, nilianza kuwa mvivu katika kufanya kazi zangu hata katika biashara ya kuuza mitumba nilianza kuwa mtu wa kupata hasara kila kukicha, hilo lilimshangaza Chrispine ambaye yeye kwa wakati huo mambo  yake yalikuwa mazuri tu.

    “Una nini wewe?” aliniuliza siku moja alipoanza kuona tofauti.

    “Mbona nipo kawaida hakuna kitu,” nilimjibu.

    “Hapana kuna kitu sio bure unajua siku hizi sikuelewi kabisa maana hata katika biashara umekuwa ni mtu wa kuambulia hasara kuna nini?”

    “Chrispine.”

    “Niambie.”

    “Kuna vitu sivielewi kwa mke wangu.”

    “Vitu gani hivyo.”

    “Unajua mpaka sasa nahisi nipo njia panda.”

    “Kwanini?” aliniuliza.

    Nilianza kumsimulia kila kitu kilichokuwa kimetokea mpaka kufikia hatua mke wangu kumiliki gari ambalo hakuniambia lolote zaidi ya ugomvi na kunionyesha dharau.

    “Ndugu yangu pole sana,” aliniambia.

    “Bado sijapoa.”

    “Piga moyo konde ndugu yangu.”CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nashindwa kufanya hivyo Chris kiukweli nashindwa yani mpaka sasa sijui ni nini kinachoendelea.”

    “Vipi kuhusu mwanao?”

    “Hafahamu lolote na sitaki kwanza hafahamu.”

    “Ndugu yangu ukisikia kua uyaone ndiyo haya, sasa hapa itabidi uanze kumchunguza mkeo ili ujue ni nini kinachomchanganya maana ukiendelea kuwaza mwisho wa siku utavuruga kila kitu.”

    “Nitaanzia wapi?”

    “Jifanye mjinga muache akutawale ila inabidi uishi kiakili ukiendelea kumsoma naimani mwisho wa siku utafahamu kila kitu.”

    “Sijui kama nitaweza Chrispine unajua mpaka nimemkumbuka sana Mama yangu.”

    “Ni lazima umkumbuke hasa kwa hili lililotokea lakini unajua wanawake ni viumbe wa ajabu sana,” aliniambia Chrispine huku akionekana kusikitishwa na kile kilichonitokea.









    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog