Simulizi : Penzi Lililosababisha Mauti
Sehemu Ya Tano (5)
Nilishindwa kuelewa ni kitu gani nilitakiwa kufanya kwa mke wangu, alibadilika ghafla! na sikufahamu ni nini kilisababisha mpaka akawa katika hali ile.
Mwanzoni nilionekana kuipenda kazi ya mke wangu kwasababu nilishikiri kwa kiasi kikubwa katika kumsomesha mpaka kufikia hatua akapata kazi na miezi mitatu kupita baada ya kupata kazi ndipo mabadiliko yalipoanza.
Niliporudi nyumbani sikuweza kupata usingizi kabisa muda wote nilikuwa nikiifikiria ndoa yangu ambayo ilikuwa imeshaingia doa. Nilimtazama mwanangu Glory kama mboni yangu muda wote yeye ndiye alikuwa mfariji wangu kwa wakati ule.
Kuna kipindi kilifika Mke wangu akaanza tabia ya kutorudi nyumbani, hilo lilizidi kuniumiza sana na nilipomuuliza siku iliyofuata aliporudi nyumbani alidai kuwa amechoka na kazi yake ya utangazaji hivyo nimuache apumzike.
Wimbi la mawazo lililoambatana na upepo wa upweke ukanipitia, nilikuwa mnyonge mithili ya mkiwa. Sikuweza kufanya kazi, sikuweza kula, sikuweza kupata usingizi muda wote nilikuwa nikimuwaza mke wangu. Ama kwa hakika ndoa iikuwa imeniweka mahali pabaya sana. Nilishindwa kuwaza na kuwazua lolote.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Baba mbona una mawazo, una waza nini?” lilikuwa ni swali la mwanangu Glory aliloniuliza usiku mmoja ambao Mama yake hakuwa amerudi nyumbani.
“Hakuna kitu mwanangu nipo sawa, enhee! Halafu hujaniambia leo shuleni mmejifunza nini?” nilimjibu kisha nikamuuliza swali la kuzuga.
“Tumejifunza jinsi ya kumpa huduma ya kwanza mgonjwa aliyezimia.”
“Unajua ni hatua gani muhimu ambayo anatakiwa kufanyiwa?”
“Anatakiwa kupata hewa nyingi hivyo mwalimu ametufundisha inabidi tuhakikishe amepata hewa ya kutosha.”
“Vizuri sana mwanangu bila shaka umelielewa vyema somo hilo.”
“Ndiyo Baba halafu wiki ijayo tunaanza kufanya mitihani ila Baba nataka likizo niende nikamsalimie Bibi,” aliniambia Glory maneno ambayo yalinishtua sana. Kwa umri aliyokuwa nao sikutaka kuamini kama aliweza kukumbuka uwepo wa Bibi yake ambaye hakuwahi kumuona hata mara moja.
“Usijali nitakupeleka mwanangu,” nilimwambia.
Sikumaanisha kile nilichokizungumza bali niliamua kumwambia maneno hayo kama kumdanganya kwa kumridhisha ili asiendelee kunisumbua.
“Baba mbona Mama hajarudi?” aliniuliza tena swali lingine lililoniweka katika hasira kali mno, kutokana na hasira nilizokuwa nazo nikajikuta nampiga kibao mwanangu na kuanza kumtolea maneno makali ya kumfokea juu ya maswali yake yasiyokuwa na vichwa wala miguu.
Alianza kulia huku akilitaja jina la Mama yake, nikapata kazi ya kumbembeleza, hakuweza kunyamaza kirahisi na kila nilipokuwa nikijaribu kumbembeleza alizidi kulia huku akilitaja jina la Mama yake.
“Julieth kwanini unanifanyia haya lakini?” nilijiuliza kwa ghadhabu.
Usiku huo ulikuwa ni wa kilio kwa mwanangu Glory pamoja na maumivu kwa upande wangu, nilijiona kuchanganyikiwa kwa maamuzi ya kukurupuka niliyokuwa nmeyachukua. Hata nilikuwa sielewi ni nini nilichokuwa nakifanya. Siku hiyo ikapita.
****
Siku iliyofuata niliweza kumuomba msamaha mwanangu kwa kosa la kumpiga usiku wa siku iliyopita, hakuwa amenikosea bali nilikuwa katika hasira. Kwa kumdanganya ilinibidi nimpe noti ya shilingi elfu mbili nikamwambia ilikuwa ni zawadi yake na hakutakiwa kunichukia mimi Baba yake ambaye nilikuwa nampenda sana.
“Mama yuko wapi?” aliniuliza.
“Mama leo atarudi jana alibanwa na kazi halafu ameniambia akirudi atakuletea zawadi,” nilimwambia.
“Baba kweli?” aliniuliza
“Ndiyo mwanangu,” nilimjibu.
Nilimwambia ajiandae ili aweze kwenda shuleni kisha akafanya kama nilivyomwambia na baada ya kumaliza kujiandaa nilimwandalia chai akaweza kwenda shule.
Akaniacha na upweke kama ilivyokuwa kawaida yangu, nikaendelea kuiwaza ndoa yangu jinsi ilivyokuwa ikielekea mahali pabaya.
Nilimpigia simu Chrispine kisha nikamueleza kuwa sikuwa sawa kwa siku hiyo hivyo nisingeweza kutoka kwenda mahali popote pale, nikajaribu kumpa maelekezo ya kunisaidia mambo mawili matatu ya juu ya biashara zangu.
“Sawa nitafanya kama ulivyoniambia ila Dominick ndugu yangu mapenzi yasikupeleke puta kiasi hicho yani imefikia hatua mpaka kutoka unashindwa?”
“Nahisi kichwa kinaniuma Chrispine sipo sawa kabisa.”
“Ndugu yangu una matatizo makubwa embu jioni fanya tuonane tuzungumze kitu,” aliniambia Chrispine.
“Sawa,” nilimjibu kisha nikakata simu.
Tangu Chrispine aliponiambia nianze mpango wa kumfuatilia mke wangu ili niweze kufahamu ni nini kilichokuwa kinaendelea nyuma ya pazia kwa kweli nilishindwa kufanya hivyo. Niliamini kuwa endapo ningeweza kumchunguza na kufanikiwa kufahamu kitu kilichokuwa nyuma ya pazia hakika nilikuwa nikishiriki katika mpango wa kuupondaponda moyo wangu kutokana na maumivu makali ambayo ningeweza kuyapata.
Jioni ya siku hiyo mara baada ya Glory kurudi kutoka shule nilihakikisha amekula kabisa, ameandaa nguo zake za shule kisha nikaweza kumuaga huku nikimuahidi kuwa sitachelewa kurudi nyumbani.
Nilienda kukutana na Chrispine Magomeni Mikumi katika baa moja iliyojulikana kwa jina la Deluxe Bar. Tulipokutana niliagiza bia aina ya Grant’s kitendo ambacho kilimshangaza sana Chrispine. Yeye aliagiza soda na baada ya kuhudumiwa na muhudumu mazungumzo yetu yalianza.
“Unakunywa pombe siku hizi?” aliniuliza.
“Ndiyo nakunywa,” nilimjibu.
“Unajua umebadilika sana,” aliniambia.
“Nadhani unajua sababu iliyosababisha mpaka nimekuwa hivi,” nilimwambia.
“Kwanza umeanza kutekeleza kile nilichokuambia?” aliniuliza.
“Kitu gani?”
“Kumchunguza mkeo.”
“Hapana.”
“Kwanini?”
“Nimeshindwa kufanya hivyo Chris.”
“Unapoelekea ni mahali pabaya inabidi ujitoa kiume upambane mpaka ujue ni nini kilichomsibu mkeo.”
“Hivi kwa hapa nilipofikia unadhani nitaweza kweli?”
“Kwanini ushindwe Dominick ni mambo mangapi umeweza kuyafanya katika maisha yako ukayafanikisha kwanini hili jambo dogo la kumchunguza mkeo ushindwe?”
“Sitaki kufanya huo ujinga hata mara moja,” nilimwambia kwa ukali kisha nikaanza kunywa pombe kwa pupa mithili ya mtu aliyekuwa na kiu kikali, nilikunywa pombe zisizokuwa na idadi mpaka nikapoteza fahamu.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilipata fahamu na kujikuta nipo ndani ya chumba kimoja, nilikurupuka na kushangaa mahali pale nilifikaje. Kumbukumbu zangu za mara ya mwisho nilikumbuka nilikuwa baa na Chrispine tukizungumza na baada ya hapo sikukumbuka tena kitu kilichoendelea. Kichwa kilianza kuniuma, nilipoamka nilijihisi kuwa mzito sana. Nilipokuwa nikiendelea kujiuliza maswali yalikosa majibu mara Chrispine akaingia ndani.
“Hapa nimefikaje Chrispine?” nilimuuliza Chrispine alipokuja na kukaa pembeni yangu.
“Ina maana unataka kuniambia umesahau kila kitu kilichotokea jana?” aliniuliza.
“Sikumbuki ila si tulikuwa baa?” nilimuuliza.
“Sema tulikuwa baa,” aliniambia.
“Mbona nipo hapa nyumbani kwako?”
“Ushukuru ulikuwa na mimi sijui kama ungekuwa peke yako ingekuwaje?”
“Kwanini?”
“Dominick embu acha kujitoa ufahamu ina maana unataka kuniambia umesahau kila kitu kilichotokea jana?”
“Sikumbuki kweli.”
“Ok, jana ulikunywa sana pombe mpaka ukapoteza fahamu,” aliniambia Chrispine kisha nikakumbwa na bumbuwazi.
Nilihisi kama hakukuwa na ukweli katika yale aliyokuwa akinieleza, nikabaki nikiendelea kumkodolea macho huku nisiwe na la kusema. Yaani mapenzi yalikuwa yamenichanganya mpaka nikafikia hatua ya kunywa pombe, sikutaka kuamini kabisa.
Niliingiwa na hofu nilipomkumbuka mwanangu Glory, sikujua alikuwa katika hali gani, nilikumbuka siku iliyopita nilimuahidi kutoka na kutochelewa kurudi matokeo yake niliamka katika siku nyingine tena nikiwa nje na nyumbani kwangu.
“Sijui Glory atakuwa salama?” nilimuuliza.
“Kwani ulimuacha na nani?”
“Peke yake.”
“Mama yake hakurudi?”
“Sijui kama alirudi,” nilimjibu Chris kisha akatikisa kichwa chake, alionekana kunihurumia sana, kila alipokuwa akinitazama alizidi kunionyesha sura iliyogubikwa na masikitiko makubwa.
“Dominick hivi utaendelea kuishi maisha haya mpaka lini?”
“Sijui Chris, sijui kwa kweli.”
“Unajua nahisi kama nimekukosea sana.”
“Kwanini?”
“Nakumbuka mimi ndiyo mtu ambaye nilikuwa kipaombele sana katika kukushauri na kukupigania katika mahusiano yako hata hii ndoa yako mimi ndiye niliyekushauri umuoe huyu mwanamke, najua kwa mateso unayoyapita hivi sasa ni lazima utafika muda utanichukia ni lazima unichukie maana hata huyu mwanamke amesababisha mpaka umegombana na Mama yako,” aliniambia Chris.
Maneno ya Chris yalizidi kuniumiza sana, nilikumbuka mambo mengi ambayo yalitokea katika maisha yangu, jinsi ambavyo nilipigana kiume mpaka nikahakikisha nafanikiwa kumuoa Julieth japo alisababisha mpaka nikagombana na Mama yangu lakini hilo sikutaka kujali.
Licha ya mapenzi yote ambayo nilimuonyesha na kumthamini kama mke wangu wa ndoa lakini ghafla! alikuja kubadilika. Alibadilika katika kipindi ambacho nilikuwa nampenda sana, sikutarajia kama angeweza kubadilika katika kipindi kile nilichokuwa namuhitaji zaidi.
Sikutaka kuweka mlolongo mrefu wa mazungumzo kati yangu na Chrispine, aliponiambia kuwa alikuwa akinionea huruma kwa yale yaliyokuwa yakinitokea nilimwambia asijali hivyo abaki na amani, niliamini kile kilikuwa ni kipindi cha mpito na muda wowote kingeweza kufika mwisho.
Nilimuaga Chrispine kisha nikaondoka kuelekea nyumbani kwangu, barabarani nilikuwa mwingi wa mawazo sana, kuna muda nilikuwa nikiongea peke yangu kama mwendawazimu.
Nilipofika nyumbani nje nililiona gari alilodai mke wangu kuwa ni lake, nikalitazama kwa muda wa sekunde kadhaa kisha nikaingia ndani, nikamkuta mke wangu akiwa amekaa sebuleni, alionekana kunisubiri kwa hamu kubwa sana. Wakati huo Glory alikuwa ameshaenda shule.
“Umetoka wapi?” bila hata salamu aliniuliza huku akiwa ameikunja sura yake kwa ghadhabu.
“Bila hata salamu mke wangu?” nilimuuliza kwa sauti ya upole.
“Salamu ya kazi gani sasa au itakusaidia nini, nimekuuliza umetoka wapi?” aliniuliza.
“Nimetoka kwa Chris,” nilimjibu.
“Kwa Chris?” aliniuliza.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ndiyo,” nilimjibu.
“Kwahiyo unataka kuniambia jana umelala huko huko?”
Kila swali nililokuwa nikimjibu mke wangu nilimjibu kwa sauti ya upendo lakini nilishagazwa na muonekano wake, alionekana kutawaliwa na hasira na yote ilisababishwa na kutorudi kwangu nyumbani, nilipomuuliza kuhusu mwanangu Glory alishindwa kunijibu alikuwa shule mwisho tukaingia katika ugomvi.
Alidai kuwa amenichoka na hivyo hakutaka kuendelea na mimi tena, kama ni ndoa basi ule ndiyo ulikuwa mwisho wake wa uvumilivu. Hakutaka kuendelea kuumiza akili yake juu ya vitu ambavyo havikuwa na msingi katika maisha yake.
Sio siri nilishangazwa na maamuzi aliyokuwa ameyachukua mke wangu, nikazidi kumuona kuwa mwanamke wa tofauti sana hasa ukilanganisha muonekano wake, kazi yake pamoja na mambo aliyokuwa akiyafanya vilikuwa ni vitu viwili tofauti.
Kwakweli nilizidi kuchanganyakiwa kutokana na uamuzi aliyokuwa ameuchukua mke wangu, nilikuwa nampenda sana japo alianza kunifanyia visa lakini sikutaka kuupunguza upendo niliyokuwa nao kwake. Kwa wakati ule ambapo alikuwa ameniambia amenichoka na kutaka tuachane nilijaribu kumsihi asichukue maamuzi hayo kwani tayari tulikuwa tumejaaliwa kupata mtoto katika maisha yetu na alikuwa akitutegemea kwa kila kitu, sikutaka Glory apoteze muelekeo wa maisha yake baada ya kuachana kwetu, nikajaribu kumsihi mara mbilimbili asichukue uamuzi huo mgumu ambao ungeweza kumuathiri kisaikolojia.
“Tafadhali mke wangu naomba usichukue uamuzi huo, mimi bado nakupenda sasa kwanini unataka kunipa hukumu nisiyoistahili?” nilimuuliza kwa sauti ya kulalamika, nilikuwa nikiyalalamikia mapenzi ya mke wangu na kwa wakati huo hakuonekana kujali, alikuwa amenikinai.
“Sitaki Dominick naomba tuachane nimekuchoka,” aliniambia huku akinionyesha hasira za waziwazi.
Kuna wazo lilinijia kichwani na nilihitajika kulifanyia kazi kwa wakati huo ili kuinusuru ndoa yangu ambayo ilikuwa inaendea kuangamia.
MSAMAHA hili ndilo wazo lililonijia kichwani kwa wakati huo, nilichoamua kukifanya ni kuanza kumuomba msamaha mke wangu. Niliamua kufanya hivyo ilimradi amani ya mapenzi yetu ya ndoa irejee kama hapo awali lakini naweza kusema haikuwa kama nilivyodhani.
****
Huo ndiyo ukawa mwanzo wa kuyapokea maumivu mengine yaliyouumiza moyo wangu wa mapenzi, Julieth aligeuka kuwa ncha ya kisu kikali na kisha akawa ananichomachoma moyoni mwangu. Nilikuwa nikiyapokea maumivu makali ambayo sikuyatarajia katika maisha yangu. Hatimaye ya mapenzi niliyoyafananisha na simulizi nzuri ya kimapenzi iliweza kugeuka kuwa simulizi ya kusikitisha.
Kipindi ambacho Julieth alikuwa amebadilika na kuwa mbogo ndani ya nyumba nilianza kuyasikia maneno ya chinichini ya watu wakisema alikuwa akitembea na wanaume mbalimbali wenye pesa ambao ndiyo walikuwa wakimuhonga magari pamoja na pesa.
Sikutaka kuamini macho yangu pale nilipoziona picha za Julieth mitandaoni akiwa kitandani na mwanamuziki maarufu wa nyimbo za bongo fleva aliyekuwa akijulikana kwa jina la Gibson David lakini jina la kisanii alikuwa akitumia “G Malove”.
Nilihisi kuchanganyikiwa baada ya kusikia Julieth alikuwa katika mahusiano ya kimapenzi na Gibson na kibaya zaidi alikuwa ana ujauzito wake. Maumivu hayakuishia hapo tu, Mwanamuziki huyo alimpangia nyumba pamoja na kumfungulia biashara mbalimbali mke wangu.
Kilichokuwa kimetokea katika maisha yangu kilimsikitisha sana rafiki yangu Chrispine, alinionea huruma sana kutokana na madhila niliyokuwa nimeyapata.
Hakutaka kuamini kama Dominick niliyekuwa nikiishi maisha ya kuifurahia ndoa yangu wakati huo nilikuwa nikiteseka, nikinyanyasika, nikiumizwa na ndoa yangu.
Ulifika wakati nilikosa mtetezi wa kunitetea si kwa Chrispine tu! bali hata kwa upande wa Mama yangu mzazi hatukuwa na mawasiliano mazuri, tuligombana na sababu kubwa alikuwa ni mke wangu.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hutakiwi kuendelea kuwa mnyonge inabidi ufanye maamuzi katika hili,” aliniambia Chrispine.
“Hivi kweli mke wangu anaweza akanifanyia unyama huu?” nilimwambia Chrispine kisha nikamuuliza swali ambalo lilinifanya nidondokwe na machozi, nilikumbuka mambo mengi niliyowahi kuyafanya kwa mke wangu lakini yalionekana kuwa ni bure, hayakuwa na faida yoyote kwa wakati huo.
“Najisikia vibaya sana ndugu yangu najua unapitia katika wakati wa maumivu kiasi gani lakini huna budi kukubaliana na hali halisi, yule mwanamke ni muuaji kweli, hana utu kabisa,” aliniambia Chrispine.
“Lakini angeniambia mapema kuwa amenichoka, nimewekeza dhamana ya upendo, uvumilivu na kujitoa lakini mwisho wa siku amekuja kunilipa maumivu, amenilipa dharau nadharaulika mimi kila kona, naonekana labda pengine simridhishi mke wangu na ndiyo sababu amenisaliti,” nilimwambia Chrispine huku machozi yakiendelea kunibubujika mashavuni mwangu.
“Usiseme hivyo,” aliniambia Chrispine.
“Kwanini anasahau wema wangu wote niliyomtendea katika maisha yake, kwanini anasahau kwamba tuna mtoto mdogo ambaye anatutegemea, kwanini anachukua kunipa hukumu hii? Anasahau kuwa yeye ndiyo chanzo cha mimi kugombana na Mama yangu, kwanini amesahau mapema kiasi hiki?” nilimuuliza Chrispine huku nikiendelea kudondokwa na machozi mfululizo.
Nililia sana, niliumia mno wala maumivu yangu sidhani kama kulikuwa kuna mtu wa kuyatibu kwa wakati ule. Nilitokea nikayachukia mapenzi, nikayawekea uadui mkubwa mno.
Niliyekuwa namsikia akiyasifia mapenzi nilimuona kuwa kipofu asiyeona mbele ni kitu gani kilichokuwa kinakwenda kumtokea, mimi nilikuwa mfano bora wa kuwasimulia yale yaliyowahi kunikuta katika maisha yangu, nilikuwa kipofu wa mapenzi.
Nakumbuka nyumba niliyopanga kujenga kisirisiri, ilinishinda mwisho wa siku nikaamua kuiuza.
****
Baada ya mambo yote hayo kutokea katika maisha yangu niliamua kwenda nyumbani kwa Mama yangu kwa lengo kwa kuomba msamaha. Nilichokutana nacho baada ya kwenda nyumbani kwa Mama yangu huku nikiwa na mwanangu ni kaburi ambalo niliambiwa alizikwa hapo miaka miwili iliyopita.
Kiukweli sikutaka kuamini kwa kile nilichokuwa nikielezwa na majirani, nilihisi kuchanganyikiwa, hakukuwa na kitu kingine zaidi ya machozi ya uchungu, nilimlilia Mama yangu ambaye alikufa bila kusema neno lolote na mimi, alikufa huku akiwa ananichukia, niliumia mno.
****
Niliporudi nyumbani kwangu sikuonekana kuwa mwenye furaha hata kidogo, nilikuwa mnyonge sana na kila wakati taswira ya kaburi la Mama yangu ilikuwa ikinijia kichwani.
Sijui niseme nini ila naweza kusema nilichanganyikiwa na kila nililokuwa nalifanya haikuwa ni akili yangu kwa wakati huo.
Usiku wa siku hiyo mke wangu hakurudi tena nyumbani, nikabaki nikitabasamu huku nikiamini alikuwa na huyo mwanamuziki wake.
“Kwako Chrispine,
Najua utashtushwa na aina ya maamuzi ambayo nimeamua kuyachukua, sina maana kwamba nimeshindwa kuyavumilia hapana ila imebidi iwe hivi.
Najisikia kufanya mauaji na sitaki kusabababisha mauaji kwa damu isiyokuwa na hatia. Najiona nikielekea mahali pabaya sana na hakuna wakunisaidia.
Nimeteseka sana katika kupigania maisha ya mke wangu lakini mwisho wake amekuja kunilipa zawadi ya maumivu, amenipa jeraha la mapenzi na sijui kama nitaweza kupona.
Najua nitaishangaza dunia kwa maamuzi yangu haya ninayokwenda kuyachukua lakini kabla sijayachukua naomba uyafanyie kazi haya nitakayokuandikia.
Hakikisha unasimamia vyema biashara zangu, hakikisha unabaki na mwanangu Glory, naamini ninamuacha katika mikono salama.
Nachukua maamuzi ya kujiua lakini nitakapokufa hakikisha nazikwa pembeni na kaburi la Mama yangu pengine kwa kufanya hivyo nitapata wasaa wa kuzungumza naye na kumuomba msamaha kwa mara nyingine. Atanisamehe.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Maiti yangu chonde tafadhali hakikisha mke wangu haisogelei, sitaki tukio hili litokee katika msiba wangu kwa maana yeye ndiyo chanzo cha yote haya na kama utapata bahati ya kuisoma barua hii basi usiache kumwambia mke wangu kuwa nakufa huku nikiwa namchukia sana.”
Ilikuwa ni barua iliyoambatana na simulizi ya maisha aliyoiandika Marehemu Dominick, kila mtu alisikitishwa na kifo chake alichokisababisha mwenyewe.
Aliamua kujiua kwa kujichoma na kisu tumboni. Kifo chake kilisababishwa na MAPENZI.
Hii ni simulizi ya maisha iliyowahi kutokea, nimeamua kukusimulia kile nilichokishuhudia katika safari ya maisha ya mhusika huyu ambaye kiukweli kifo chake kimewaumiza wengi mno.
Imeandikwa na JUMA HIZA.
MWISHO.
0 comments:
Post a Comment