IMEANDIKWA NA : ANDREW CARLOS
*********************************************************************************
Simulizi : Sitaki Tena
Sehemu Ya Kwanza (1)
Nakumbuka Levina mimi nilikuwa na miaka Kumi na Nne tu. Wazazi
wangu walikuwa wakinipenda sana na walipenda kuniachia huru hata pale nilipokuwa nacheza na rafiki zangu michezo mbalimbali ya utoto. Nilikuwa napenda
sana kucheza michezo tofauti nawenzangu si unajua tena utoto, na
mchezo mkubwa niliokuwa nikiupenda ni huu wa rede (ule wa
kukwepa mpira pindi unaporushiwa).
Naendelea kukumbuka siku hiyo nikiwa mimi na rafiki
zangu tukicheza. Sikuamini macho yangu na ni vigumu
kuamini mpaka sasa kwa kile nilichotenda badala ya
kuuokota mpira nirushe kwa mwenzangu, ile haraka niliyokuwa nayo ndani ya
ule mchezo nilijikuta nikiokota jiwe bila kujitambua nilichokuwa
nimeokota huku nikidhania kuwa ni mpira na kumrushia Jeni na kwa bahati
mbaya lilimpata Jeni kichwani na kuzimia palepale. Juhudi zilifanywa haraka haraka
na majirani huku mimi nikiwa pembeni sijui cha kufanya . Mchozi
ukinitiririka uku kijasho chembamba kikipenyeza katika paji la uso wangu kupitia
shingoni na lile jasho likichochea mkojo ulioanza kunitoka taratibu palepale huku
nikitazama kinachoendelea.
“..Panda na wewe twende…nimesema panda huko husikii?”
Aliongea na mimi Mama mmoja kwa ukali huku akinitolea mijicho kana kwamba labda alikuwa ni
mtoto wake lakini haikuwa hivyo kwani alikuwa ni mpita njia aliyekuwa shuhuda wa lile tukio.
Nilipanda taksi pamoja na wale majirani iliyokuwa imekodiwa haraka kwa ajili ya kumkimbiza
Jeni hospitali. Kadri tulivyokuwa tunakaribia hospitali ndivyo mapigo yangu ya moyo
yalikuwa yakinienda kasi mithili ya yule mwanariadha wa Jamaika anayeitwa 'Bolt'. Huku nikiomba
miujiza yeyote itokee ili Jeni apone turudi nyumbani,. Niliendelea kulia tena kwa sauti
ya juu huku kamasi likinitoka na tulipokaribia kufika hospitali niligeuza kichwa changu nakumuangalia mama mmoja aliyekuwa
pembeni yangu akimshikilia Jeni. Alikuwa akitikisa kichwa huku akimwambia dereva
apunguze mwendo kwani haina haja tena kuwahi tena hospitali. Aliendelea kumsisitizia kuwa mtu
waliyekuwa wakimuwaisha ameshapoteza maisha.
“Jeni amekufaaa..amekufaaa…
Hapana… hapana… Mama yangu weeee...Mama...Baaabaaa uko
wapi jamanii Mama yangu weee”
Nilizidisha kupaza sauti kwa kulia niliposikia
yale maneno. Sikuweza kuamini kama kweli Jeni amekufa mpaka
nilipoona tunaelekea mochwari ndipo nilipoamini Jeni alikuwa tayari keshapoteza
maisha. Damu nyingi zilikuwa zikimtoka eneo la kichwani na puani.
“Umeshaua? ndio umeuwa naongea na wewe kinyago uliyefanya makusudi haya!”
Aliongea yule Mama akinikazia sura.
“Sijau..”
Kabla sijamalizia kujibu nilishangaa napigwa kofi kubwa la
usoni mpaka nikajihisi kizunguzungu.
“Tena ishia hapo hapo mwanaidhaya mkubwa wewe na tunakupeleka polisi moja kwa moja mbwa
wewe ukaozee huko huko ndio utanyooka!”
*********************
Taarifa za mimi kufanya lile tukio tena kwa bahati mbaya zilitawanyika Mtaani kote na hakuna hata mmoja aliyeweza kuamini kwani taarifa hata zilipofikiwa wazazi wangu nao hawakuweza kuamini
kilichonitokea. Walikuja pale kituoni japo kunitoa kwa dhamana lakini ilishindikana
kutokana nakuwa hakuna dhamana kwa kesi yoyote ya mauaji. Nilishiwa nguvu, na kulegea
viungo vyote hali iliyonisababishia kupoteza fahamu kutokana na kukataliwa dhamana.
BAADA YA SIKU (NNE) 4
Sikuweza kupata hata lepe la usingizi takribani siku mbili kutokana na kulia sana, kichwa kiliniuma
sana. Ilikuwa ni asubuhi na mapema pale askari alipotuamrisha tupande gari la polisi kutoka pale kituo kidogo cha polisi Kurasini na kuelekea kituo kikubwa cha polisi pale MSIMBAZI KARIAKOO. Safari ilianzia kituo kidogo cha Kurasini nilipokuwa nimechanganywa na wenzangu niliowajua pale pale na wao walikuwa na makosa tofauti tofauti. Tulikikatiza Sheli ya BP mpaka raundi ‘about’ ya Kamata. Sehemu zote tulizopita bado machozi yalikuwa yakinitoka huku yakiandamana na mafua makali yaliyo nipata pale kurasini kituoni. Kwikwi ilibana sana na haikuwa kwasababu ya kiu ya maji bali ilikuwa ni kwikwi ya kulia kwa muda mrefu.
“Embu nyamaza hukoo. Haupo kwa Baba yako wala Mama yako.Tena unyamaze?.”
Aliongea kwa hasira askari mmoja aliyeonesha kukasirishwa na kitendo changu cha kulia muda
mrefu bila kunyamaza.
“Hivi we mtoto husikii? Kwani sisi ndio tumekutuma uue?”
Aliendelea kunikalipia Yule askari. Mpaka tunaingia pale kituoni ‘MSIMBAZI’
macho yalikuwa mekundu na yamenivimba sana huku sauti ikinikauka kutokana na kulia kwa
muda mrefu. Nikawekwa lokapu ya kituo kikubwa cha MSIMBAZI.
*** ***
Nilikuwa katika basi lenye namba PT 10319 ambalo lilikuwa likikatisha mitaa ya kariakoo
likiwa linatokea kituo kikubwa MSIMBAZI huku nikiwa katika orodha ya
mahabusu waliokuwa wamewekwa pale MSIMBAZI kituoni kuelekea mahakama kuu
pale KISUTU kwa ajili ya kusikilizwa kesi yangu kwa mara ya kwanza.
Kila moja alikiwa amefungwa pingu mikononi. Nywele pamoja na nguo zangu
zilikuwa chafu sana kutokana na uchafu wa pale kituo cha Kurasini na msimbazi.
Huku basi la polisi likiwa linakata kona ya kuingia mahakamani . Macho yangu yalikuwa haraka kuangaza
huku na kule labda huenda ningeweza kumuona hata mama au baba. Ghafla macho yangu yakafanikiwa kumuona mama yangu akiwa amejifunika khanga upande mmoja wa paji la uso wake kuashiria kuwa alikuwa ameumia upande mmoja wa uso wake. Nikiwa bado katika hali ya kustaajabu nilijikuta nikipigwa na afande. Teke!
“Embu tembea hukoo...Unashangaa shangaa nini? Kwani hujui kama hapa ni
mahakamani?”
Nilipiga moyo konde nakuugulia maumivu ndani ya moyo wangu. Kwa mstari mmoja tulishuka na kuelekea kwenye vyumba ila mimi niliingizwa chumba
maalumu kilichoandikwa maneno makubwa mlango wa kuingilia
“CRIMINAL ONLY”. Kwa haraka haraka sikuweza kutambua lile
neno linamaana gani kwakuwa ndio kwanza nilikuwa niko form one ila nilichoweza
kuambulia neno moja tu lililoandikwa “ONLY” kwani nilipenda sana kuangalia ile
tamthiliya ya kifilipino iliyokuwa inaitwa ‘only you’ nikijua inamaanisha ‘Wewe
Pekee..’
Niliingizwa mpaka ndani ya kile chumba. Sikuwa mbali na fikra zangu kwani kile chumba kilikuwa peke yake kwa ajili ya kesi za mauaji kama yangu ndio huwa zinasomwa hapa. Niliendelea kustaajabu watu waliovalia majoho marefu. Akili yangu napo ikafanya kazi kwa haraka nakutambua kuwa watakuwa mawakili wangu
nisiowafahamu ila niliamini tu Baba ndio aliwatafuta. Kwani alikuwa akiongea nao kwa ukaribu kabla mimi sijaingizwa mule ndani. Chumba kilikuwa kidogo sana na watu walimiminika wakiwa ni pamoja na majirani, ndugu na marafiki huku kesi ikitaka kuanzwa kusomwa niligeuka nyuma nikajikuta macho yangu yakikutana na mama mmoja. Kwa hasira na jazba niliokuwa nayo nilijikuta
Nikitoa fyonyo kali na la kupaza sauti ya juu.Wote mle ndani wakawa kimya ghafla
wakinitazama.
“xé@shh.. mbea mkubwa we!” Nikatoa maneno makali.
Kisha nikamtemea mate huku hasira zikinipanda kutokea miguuni kuelekea kichwani na mikononi. Nilijikuta nikitaka kumpiga lakini mikono yangu ilikuwa ndani ya pingu. Hivyo hasira ikazidi mara mbili huku nikihema kwa kasi iliyoambatana na makamasi yaliokuwa
yakinichilizika mithili ya umande unapokutana na majimaji au konokono anapokuwa anaachia kofia yake. Nikanyanyua mguu wangu wa kulia tayari kwa kumtupia mateke yule mtu,lakini kwa bahati nikawa tayari nimeshathibitiwa na mapolisi. Hakuwa mwingine bali alikuwa ni yule Mama tuliepanda naye taksi kumuwahisha Jeni hospitali yule aliyekuwa akinisema ovyo kwenye gari pia ndo alienipeleka Kunikabidhi polisi. Nikiwa bado naendelea kumtolea macho huku nimekunja uso wangu kwa hasira
mithili ya Bi Kidude akiwa jukwaani anaimba. Nilipokea vibao mfululizo kutoka kwa askari aliyekuwa akifuatilia tukio mule ndani.
“Hata kesi haijaanza umeanza kuonyesha we nunda eenh... hatimaye hakimu aliingia
“Na lazima utaozea jela tu wewe.”
Maneno yale yalivuta hisia nyingi sana ndani ya moyo wangu, Moyo ukavumilia yote hayo. Mwili ulininyong'onyea ghafla. Nikaanza kutetemeka japo nilikuwa mdogo kiumri lakini nilikuwa tayari nimeshakomaa kifikra na pia jasiri ndani ya muda mfupi.
******
Muda wa hakimu kuingia mule ndani ulifika. Hakuwa mtu wa masihara hata kidogo kwani
aliingia haraka haraka na kuuliza jina langu kamili kisha akaandika andika pale kwenye kitabu
alichokuja nacho.Akaniambia kuwa inabidi nirudi tena ndani kwani kesi yangu bado ipo kwenye upelelezi hivyo nitarudishwa tena pale mahakamani baada ya wiki Tatu au Nne. Nguvu zilizidi kunipotea, akili nayo ilishajichokea. Nilitoka pale kwa ghadhabu huku askari akiwa nyuma yangu, nilikuwa na hasira na vitu vitatu. Kwanza sijapata fursa ya kuongea na wazazi wangu kwa muda mrefu kwani kwenye kesi kama hizi mtuhumiwa huwa hana hata ruhusa ya kuongea na mtu
yoyote. Pili nilikuwa na hasira ya kuhairishwa kwa kesi yangu na
tatu ni hasira ya yule mama aliojifanya yupo mstari wa mbele katika kunifuatilia kujua mwisho wangu.
“Ole wake siku nikitoka?”
Nilijikuta nikijisemea kimoyomoyo huku dukuduku likiwa limenijaa
moyoni.
“Ipo siku tu, Atanijua mimi ninani?”
Nilipandishwa kwenye basi la polisi tayari kwa safari ya kurudishwa tena rumande.
Usiku ule tangu nirudishwe tena rumande kwangu haukuwa mzuri kabisa Akili na viungo vya mwili wangu vilikuwa vimechoka sana, yote hiyo ni kutokana na kulia na kupigwa
pigwa, ovyo na maaskari. Sikuweza kupata hata chembe ya usingizi kila nilipofikiria kilichonikuta.
“Hivi kweli nimeua? mimi nimeua? miiiimi.?”
Hilo ndio swali nililojikuta nikijiuliza usiku kutwa bila kupata majibu. Nilitamani nishuhudie rafiki yangu kipenzi Jeni akizikwa pengine labda ndio ningeshawishika na kuamini kama kweli nimeua lakini hiyo
haikuwezekana. Hakika usiku uliendelea kuwa mrefu sana kwangu. Mawazo mengi yalikuwa tayari yameshatawala kichwa changu pengine hata umri wangu haukuniruhusu kufikiri sana lakini tayari nilikuwa na fikra tena za kikubwa zaidi kwa mda mfupi tu tangu niwekwe rumande. Sauti za bundi popo na mbwa ndizo zilikuwa zinakipaa sana kuzunguka huku na kule katika lile eneo la kituoni. Wenzangu walikuwa tayari wameshalala fofo hawajielewi hiyo yote ni kutokana na shuruba shuruba za humu ndani.
Mpaka ilipotimia saa tisa za usiku usingizi ulikuwa tayari umeshanipitia. Lakini kitu kilichokuja
kunishtua ni kaubaridi kalikokuwa kakipenyeza ndani ya gauni nililokuwa nimevaa. Miköno yangu miwili ndio ilikuwa mto. Mwili wote ulikuwa ukinitetemeka mithili kifaranga cha kuku kikinyeshewa na
mvua. Kifupi palikuwa na baridi sana nadhani ni kwasababu sakafu ndio ilikuwa kitanda changu.
Taaratibu nilianza kujihisi kama kuna kitu kinanipapasa kupitia mapajani mwangu. Sikuwa na wasiwasi kwani nilijiamini sana kuwa tupo wanawake tu na kama askari ndio walikuwapo mchanganyiko wakiume kwa wakike. Kila muda ulivyokuwa ukisogea ndivyo na hisia zilikuwa zikibadilika ndani ya kichwa changu. Taratibu niliweza kulifungua jicho langu la upande wa kushoto kuangaza huku na huku kujua kitu gani kinachonipapasa. Mshtuko!
“shhhhhhhh……....!!!!!! nyamaza...!!!!!!!! na ole wako ufungue domo lako?”
Ilikuwa ni sauti ya askari wa kike niliyekuwa nikimfahamu kwa sura. Alikuwa kanishika mapaja yangu kwa nguvu huku akiwaamuru askari wenzake ambao walikuwa wakiume wafanye haraka haraka.
Moyo ulinipasuka, nguvu ziliniishia, hasira zilinikaa ghafla. Nilijihisi kukosa pumzi kutokana na kuzibwa mdomo kwa muda mrefu.
Hatimaye wale askari waliokuwa takribani watatu walifanikiwa kuniingilia tena kwa
nguvu kwa zaidi ya nusu saa pale huku wakiniacha na damu nyingi zikinitiririka katika sehemu zangu za siri. Nikapoteza fahamu kwa kuchoka na kuishiwa nguvu.
BAADA YA MWEZI
Hatimaye upelelezi ulikuwa umeshakamilika na nilikuwa tayari niko kizimbani. Nywele
zilikuwa hazitamaniki. Miguuni sikuwa hata nandala, mavazi nayo yalikuwa yameshachoka na kuchafuka kwani toka mwezi ule nibakwe Levina mimi sikuwa hata na nguo nyingine ya kubadilisha. Mwili ulikuwa
tayari umeshadhohofika kutokana na msosi mbaya tuliokuwa tunapewa. Hakika yalikuwa ni mateso makubwa na si jambo dogo akilini kwangu.
Kama kawaida ya kesi nyingine nadhani hii ni kutokana na shauku iliowataka watu wajue ni
nini kitakachofuatia katika kesi yangu. Umati mkubwa sana
wa watu ulikuwepo ukishuhudia kesi yangu kiasi cha kunifanya moyo wangu
ulipuke kwa huzuni. Macho yangu yalikuwa yakiangaza huku na kule na kwa ghafla nilifanikiwa
kumuona Baba na safari hii hakuwa na mawakili kama ambavyo nilitegemea bali
alikuwa kakalia kibaiskeli cha kupakia wagonjwa walemavu wa miguu huku akikokotwa na Dada aliyekuwa amevalia mavazi meupe wazo lilinijia palepale na kugundua kuwa ni lazima atakuwa ni Nesi..
“Lakini kwanini amekuwa vile? au atakuwa amepooza nini?”
Nilijiuliza mengi kichwani bila kupata majibu.
Muda wa kuanza kusoma kesi yangu ulifika. Pande zote mbili zilikutana ikiwa ni pamoja na mashahidi wa pande zote mbili.
“Wewe ndio binti Levina?”
“ndio mimi.”
“Unakumbuka mnamo tarehe moja mwezi wa pili tisini na tisa
ulifanya kosa? na unakumbuka Uliweza kuua tena kwa kukusudia?”
“Ndio”
Hayo ni kati ya maswali
niliokuwa nikiulizwa na kuyajibu. Hatimaye yalikusanywa maswali na majibu yote kuashiria kesi
imeeleweka na kuhukumiwa kifungo cha miaka kumi gerezani.
“Mwanangu...! mwanangu..! Kweli unafungwa mwananguu?”
Hayo yalikuwa maneno ya mwisho kwa Mama yaliyofanya na watu wengine waachie vilio pale pale huku nikibakiwa na roho ya kishujaa na kijasiri bila hata kutoka mchozi.
BAADA YA MIAKA MITANO
Vurugu zilizokuwa zikiendelea katika Gereza la wafungwa watoto watukutu lililopo mbeya,
ndizo zilizosababisha watoto wengi kupoteza maisha na wengine kupata ulemavu wa maisha kutokana na mgomo waliokuwa wameuanzisha kutokana nakupewa chakula kidogo sana tena kichafu, milipuko ya magonjwa kama kipindupindu, msongamano wa wafungwa kiasi cha wengine kufariki kwa kukosa hewa wakati wa kulala usiku.
Namba CG.016/007369, ndiyo namba iliyokuwa inasomeka katika sare yangu ya gerezani .
Tayari maisha nilikuwa nimeshayazoea mule gerezani. Taarifa kutoka nyumbani nilikuwa nikiletewa na afande mmoja ambaye tayari nilimzoea. Siku ile nilipo hukumiwa pale mahakamani hali ya Baba yangu kiafya haikuwa nzuri na hakukaa muda mrefu akawa amepoteza maisha. Mwenyezi mungu amlaze mahala pema peponi.
Na sasa Mama ndio mzazi wangu pekee aliyebaki hata kama nitatoka gerezani siku yeyote. Ucheshi, ufanyaji kazi kwa nguvu, bidii na kujituma zaidi ndicho kitu kilichokuwa kikiwavutia maaskari wengi pale kiasi kwamba nikapendwa sana na kuaminika.
“Levinaaa... Levinaaa....Wewe Levina Christian?”
Aliniita askari wa zamu lakini
sikuweza kumsikia vizuri kwa sababu ya makelele ya wenzangu
waliokuwa wakipigana mule ndani.
“Abeee afande,nilimuitikia”
“Embu fanya haraka kuna mgeni wako kaja kukutembelea fanya ukamuone”
“Sawa afande...”
Mapigo ya moyo yalikuwa yakinienda mbio. Halmashauri ya kichwa changu
iliweza kupambanua haraka haraka na kujua atakuwa ni Mama yangu tu.
“lakiiini...mbona afande hakuniambia kama ni Mama au la! maana Mama yangu anamjua
angeniambia tu?”
Ndio maswali niliokuwa nikijiuliza nikiwa njiani kuelekea chumba cha wageni ghafla,
* ** * * *
Gervas Phota ni mtoto wa pili katika familia ya mzee Phota waliokuwa wakiishi kurasini,jijini Dar.
Alikuwa ni kipenzi sana cha wazazi wake kwani walimpenda na kumkazania sana katika elimu.
Akiwa kidato cha Nne katika shule ya sekondari Tosamaganga mjini Iringa.
Habari za Levina kuhukumiwa jela zilimfikia na kumsikitisha kwa kuwa alimfahamu sana kwani waliishi jirani pia walikuwa wakicheza wote toka utotoni.
Kasi ya kusoma darasani ilipungua. Mawazo yakawa mengi na kitu kilichomchanganya zaidi ni pale alipopata taarifa kutoka kwa wenzake kuwa Levina ameamishiwa katika gereza la watoto watukutu mkoani Mbeya ambapo sio mbali sana kutokea Iringa alipokuwa akisoma Gervas.
“Unasema kweli Davis?”
"Mimi ndio nakupa ‘live’ yupo hapo tena nasikia kakonda sana..”
“...Basi ngoja mwezi huu nifanye juu chini nimuibukie mana nashindwa hata kusoma mwana"
Hayo yalikuwa maneno ya Gervas akizungumza na na rafiki yake Davis kupitia simu.
Siku moja Gervas alipotumiwa pesa zake kwa ajili ya matumizi madogo madogo alijibana na kuingia katika mnada na kununua baadhi ya nguo akiamini zitamtosha Levina. Alinunua vitu vingi ikiwamo sabuni za kuogea na mswaki.
Ilipotimia saa Kumi alfajiri hakutaka kupoteza muda akatoroka shuleni bila kujali kama akikamatwa itakuwaje. Akiwa na akili moja tu ya kufika gerezani,haikuchukuwa muda mrefu ndani ya masaa mawili alikuwa tayari yupo katika geti la gerezani..
“Shikamoo afande!.. Samahani Afande nimekuja kumtembelea ndugu yangu”
Kabla Gervas hajamalizia kuongea alidakia yule askari..
“Anaitwa nani?”
“Levina Christian...!!”
“..Pita katika chumba cha hapo pembeni utakutana na kidirisha kidogo msubiri utaongea naye kupitia hako katobo”
************
“Sasa mbona simuoni mgeni wangu?”
Nilijikuta namgeukia yule afande aliyekuja kuniita na kuniambia kuwa nina mgeni.
“Umeanza kisilani chako enhee?
Au unataka ukalime heka tatu peke yako sasa hivi...? Enhee!”
Nikabaki kimya huku nikiendelea kumtolea macho ya ukali yule Askari ambaye alikuwa anajulikana 'Jesca Tester' kutokana na kuwa mkorofi kwa wafungwa wabishi hata kipindi kingine huwa anakorofishana na maaskari wenzake..
“Si naongea na wewe kinyamkera?,
Haya na huyu hapa ni mgeni wa nani sasa?”
Nikajinyamazia kimya huku nikikaa katika kajidirisha cha kuongea na wageni, nikimuacha yule askari akiendelea kubwabwaja pale.
“Na Nakupa dakika kumi tu uwe umeshamalizana naye na upotee hapa, Sawa?”
“Sawa mkuu nimekuelewa!”
Nilimjibu kwa heshima huku nikianza mazungumzo na yule mgeni wangu pale.
Gervas; “Sijui umeshanikumbuka?”
Levina; “Hapana“
Gervas ; “Naitwa Gervas Phota..Tumeishi wote kurasini na kucheza,”
kabla hajamalizia kuongea tayari akili yangu ilishaweza kuchambua fasta na kumjua.
Levina; “We si mtoto wa mzee Phota pale jirani na nyumbani kwetu?”
Gervas; “Haswaaa..! Ndiye mimi kumbuka tulikuwa wadogo sana lakini kwa bahati mbaya sikuweza kuwepo kuanzia siku ya tukio, Kipindi cha kesi yako mpaka leo kwa sababu nilipelekwa shule mapema mno.
Levina; “Usijali Gervas yote hayo nimaisha namshukuru mwenyez mungu mpaka nilipofikia hapa kwani nimebakiza miaka sita tu niwe huru”
“Muda umekwisha, haya we Levina inuka uwafuate wenzako shambani, inuka!”
aliongea yule askari ‘Jesca’ ambaye muda wote wa maongezi alikuwa akitusimamia.
Haraka haraka nilimuona Gervas akatoa kijimfuko kilichoashiria kina nguo. Kisha akatoa na noti ya shilingi elfu kumi akanipatia. Yule askari akampa shilingi elfu tatu na kuniaga kwa kuniahidi kuwa atakuwa akinitembelea mara kwa mara.
Siku hiyo sikuweza kupata hata lepe la usingizi kwani nilijihisi tayari nipo nyumbani kwa zile nguo nilizoletewa na Gervas. Nilijikuta machozi yakinitoka japokuwa yalikuwa ni machozi ya furaha kwangu.
Ikawa haipiti mwezi lazima Gervas aje kunitembelea na kuniachia japo chochote. Nikaamini kuwa mtetezi wa maisha yangu ni Gervas na mama yangu pekee japo tangu nilipoletwa huku gerezani hajawahi kuja kuniona. Moyo wa upendo taaratibu ulianza kunijia kwani hakukuwa na mtu aliyejionesha kunijali kama Gervas.
BAADA YA MIAKA 2
Nakumbuka siku hiyo Gervas alikuja kunitembelea lakini safari hii alionekana kuwa tofauti na siku nyingine kwani alikuja na furaha ambayo sikuitegemea na hakuweza kukaa sana ila akachukuwa mkono wake wakati ananiaga alinipa kitu nilihisi itakuwa kama kawaida yake ya kuniachia pesa lakini haikuwa pesa ila ilikuwa ni kijikaratasi kilichokuwa na ujumbe mfupi.
Niliagana na Gervas kisha nikaenda kutafuta eneo lililokuwa tulivu,taaraibu nikaanza kufungua ile karatasi ghafla moyo ukanilipuka,
“Mpendwa Levina, natumai u mzima wa afya kwani mara nyingi huwa tunaonana,
nashukuru mwenyezi mungu mpaka hapa tulipofikia kwani umenifanya nijue mengi yanayotendeka humu ndani kwa kifupi nimejuana na kuzooena na maaskari wengi hapa,
Levina mimi na wewe tumetoka mbali na sitapenda nikuache uendelee kuteseka hapo gerezani,
Mwezi huu Rais atatoa msamaha ikiwa ni pamoja na gereza lenu lakini msamaha wenyewe utalenga wale wenye ulemavu nilichokifanya ni….
kabla sijamalizia kusoma alitokea afande ‘Jesca Tester’ na kunifokea,
“hivi wewe Levina muda wote umekaa hapo umewakimbia wenzako kule, unafanya nini?”
Nika kaa kimya,
aliendelea kuongea Afande kwa sauti ya ukali,
“na kwanini umekuja kujitenga peke yako huku?”
“Nisamehe Afande sitarudia tena. Wakati namjibu ghafla kile kikaratasi kikadondoka chini,akakiona,
“haya lete hicho ulichoangusha, nimesema letee!”
*********
Nilijikuta nachukua kile kikaratasi na kumpatia afande Jesca nikiamini kuwa hajui kusoma kwani huwa mara nyingi akitumiwa ujumbe kwenye simu yake huwa ananitafuta nimsomee.
Alikichukuwa kile kikaratasi akakigeuza geuza kisha akanirudishia,
“acha upuuzi wako nenda kwa wenzako sawa?"
"Sawa"
nilimuitikia lakini kishingo upande huku akili yangu ikinituma nielekee chooni nikakimalizie kukisoma,taratibu nikaongoza hadi chooni nikakifungua kwenye gauni kilipokuwa na kumalizia kukisoma, enhe ikawaje vilee,
“…..lakini msamaha wenyewe utalenga wale wenye ulemavu nilichokifanya ni kutoa ada yangu yote niliyotumiwa shilingi laki mbili na kuwahonga polisi kisha wakalipitisha jina lako kwenye orodha ya watakao kuwa huru”
Hapohapo nikakichukuwa
Kile kijikaratasi na kukichana chana kisha nikakitupia katika tundu la choo, nikitoka na furaha ya hali ya juu huku nikijiona mshindi.
BAADA YA WIKI MOJA
Ilikuwa ni asubuhi na mapema tukiwa tumejipanga mstari halmashauri ya kichwa changu ikawa imeshafanya kazi nakutambua ni kitu gani kilituleta katika eneo lile,
kama kawaida ya Afande kimbele mbele afande ‘Jesca’ alikuwa tayari akiwanyosha watu mistari huku akiwapiga na kuwafokea wale waliojifanya ni wabishi.
Tayari maafande takribani Nane walikuwa mbele yetu huku mkuu wa gereza akiwa kashikilia karatasi bila kuchelewesha muda akaongea kilichotuleta eneo lile na kuanza kutuita majina naweza kusema sikuamini kilichotokea kuwa kama ndoto kwani ni kweli na mimi nilikuwa katika ile orodha ya walioachwa huru,
“nashindwa kujua nimfanyie nini huyu kaka,
Gervas...! Gervas...! Nakupenda na Nitazidi kupenda daima”
nilijisemea kimoyomoyo huku nikipiga ishara ya msalaba na kukusanyika na wenzangu huku tukitokea lango kuu,
*** * * *
Gari aina ya ‘Land Rover’ yenye namba T643 ABK iliyokuwa imebeba magunia ya mpunga kutoka Tunduma kuelekea Dar es salaam huku ikiwa imepakiza abiria wa nne tu, wawili wa kiume na wawili wa kike,nikiwamo katika hilo gari kwa mwendo wa taratibu huku nikiwa na mawazo mengi yalionijaa akilini mwangu ikiwa ni pamoja na hofu juu ya safari kama tutafika salama, muda huo ilikuwa imeshatimia saa mbili za usiku, tulikuwa tunakaribia kufika Iringa, mawazo gongana yaliniandama ndani ya kichwa changu hasa kwa kuzingatia kuwa bado nilikuwa sijajiamini kwa kile kilichonitokea kama kweli niko huru ama la!
Huku nikiendelea kuwa katika dimbwi la mawazo usingizi ukanipitia..
“..lete Jeki fasta,waambie na hao wadada washuke huko nyuma!”
sauti ya dereva wa ile gari akiongea na mwenzake ndiyo
ilinishtua sana kwani gari lilikuwa limeharibika kilomita chache kabla hatujaingia Iringa mjini.
Baridi lilikuwa kali sana, nilijihisi kama mwili umeganda sikuwa na nguo yoyote ya kubadilisha, hivyo sikuwa na jinsi zaidi ya kujilaza pembeni ya lile gari huku nikitetemeka mdomo na meno yakiumana kama nimepigwa ganzi.
Nikiwa pale chini natafuta tena usingizi huku dereva akiendelea kutengeneza lile gari, kwa mbaaali niliona mwanga mkubwa ukitumulika huku unasogea taaratibu, akili yangu na wale wenzangu haikuwa mbali kwani lilikuwa ni gari lakini ilipofika karibu yetu dereva wetu akawa ameipungia mkono isimame kwa ajili ya kuomba spana, ilisimama kisha wakashuka wanaume watano waliokuwa wamevalia makoti meusi huku mikononi wameshika Panga na Bunduki wakitufuata eneo tulilokuwa.
“Wote mikono juu”
“Na ole wake mtu asimame au aongee hata neno moja”
Aliongea mmoja wa wale wanaume aliekuwa anasura ya kikomavu iliyojikunja kunja mithili ya mchekeshaji wanaomwita 'King'wendu', huku kavalia miwani meusi na mdomoni akivuta sigara na kutupulizia moshi.. Tukiwa bado tupo pale chini tukitetemeka na kuogopa pia tulikuwa kama tumeshajitolea kwa lolote litakalotupata..
Ghafla milio ya risasi ikaanza kurindima kuelekea kwenye matairi ya lile gari letu yakapasuka yote manne kisha wakamchukuwa dereva na wenzake wakawachinja mbele ya macho yangu kisha wakaondoka na kuniacha na mwenzangu niliyetokanaye gerezani, Roho ya Ujasiri, ukatili na ukakamavu niliokuwa nayo toka nipo kifungoni ilinisaidia sana kwani sikuogopa hata kidogo kilichonitokea muda mfupi uliopita nilimchukuwa mwenzangu na kutokomea naye msituni.
Nikiwa nimemshika mkono mwenzangu Pendo, tulikuwa tayari tumeingia msitu wa Ruaha ambao kiukweli ulikuwa ni mkubwa sana na uliojaa na miti mirefu,hatukuweza kuogopa kitu kwani maisha ya gerezani yalikuwa tosha kwa mimi na Pendo kuwa wajasiri,wakatili na wakakamavu muda wote.
"Nimechoka,nimechoka siwezi kuendelea tena Pendo,tupumzike hapa"
Nilimwambia pendo huku nahema nikitokwa jasho usoni kwa mwendo tuliokuwa tunatembea haraka haraka hakika ulikuwa ni mwendo mrefu sana.
“Sasa ukiendelea kudeka deka mimi nakuacha, au unapenda kubakia hapa porini?”
Alisema Pendo kwa ukali kudhihirisha kuwa alikua amechoshwa na kitendo cha mimi kupumzika,nilijikaza na kuinuka tayari kwa kuendelea na safari lakini..
“…Pendo! Pendo! Mama yangu wee mguu wangu!”
Nilijikuta namuita Pendo asiondoke kwani mguu wangu kwa upande wa nyuma ulikuwa umeshachanika na damu nyingi zilikuwa zikinitiririka, Pendo hakuwa na jinsi kwani aliona kubaki na mimi katika ule msitu kungemchelewesha kufika kwao kwani safari yake ilikuwa inaishia Dodoma.
“Pendo..! Pendo..! usiniache Pendo..! nitabaki na nani tena Pendo!”
aliniacha nikiwa katika hali mbaya huku machozi yakinitoka,na kukata tamaa,nakuona bora ningemsubiri Gervas aje kunichukuwa. Ulikuwa tayari ni usiku sana nahisi ilikuwa imetimia kwenye saa nane au tisa kwani giza tororo ndilo lilitawala sana, nikiwa bado katika dimbwi la mawazo na hasira nyingi pale chini huku milio ya wanyama wakali ikipaza huku na kule, ghafla nikaanza kusikia mshindo wa kitu kama kinakuja tena kwa kasi ya ajabu, kadri mlio ulivyokuwa unazidi kuwa mkubwa mapigo yangu ya moyo yalizidi kunipelekesha,nilihema mpaka nikajihisi nimeishiwa pumzi sikuwa na lakufanya zaidi ya kujitoa kwa lolote litakalonipata kutokana na mguu kuumia vibaya kutokana na kujiumiza na kipande cha bati kwenye gari wakati tunakimbia kujiepusha na yale majambazi waliotuteka kulee.
Hatimaye nikaanza kutambua kitu kilichokuwa kinakuja kwani mwanzoni nilijua labda atakuwa Pendo amerudi kuja kunichukuwa lakini haikuwa hivyo kwani alikuwa mnyama mkubwa mweusi aliyefanania na nyati ila alikuwa akija kwa mwendo wa taratibu huku akinifuata katika eneo nililokuwa nimekaa.. Mwili ulinitetemeka sana hofu kubwa ilinitanda ndani ya kichwa changu, nilitetemeka sana huku mchozi ukiwa unanitoka ukiambatana na mkojo kwa kasi, Maumivu ya ule mguu yakatoweka kutokana na kile kilichokuwa mbele yangu.
“jamani..! jamani..! jamani..! nisaidieni nakufaa..! nakufaa..!”
Nikiwa bado nalia pale mara,
ghafla nikamulikwa mwanga mkubwa nikaangaza huku na huku nikaweza kuwaona watu wakiwa wamenizunguka.
“Wewe ni nani? Na unafanya nini hapa?”
Aliongea mmoja wa watu wale waliokuja pale nilipokuwa baada ya kupiga makelele kwa kuona mnyama akinifuata kumbe hakuwa mnyama wa kunidhulu bali alikuwa ni ng'ombe aliyechelewa kuingizwa Zizini na katika lile eneo walikuwapo wanaishi watu,
“naitwa Levina nimetokea mbeya ila gari yetu ilipata ajali tukawa tumevamiwa na majambazi hivyo nikaamua nikimbilie huku msituni,kwani hapa ni wapi?”
Niliwajibu hapo hapo huku nikishusha pumzi na kuwauliza swali bila hata ya kuonyesha woga wa aina yoyote,
“hapa ni kijiji cha ‘LIAMKENA’ tupo katikati na hili pori la msitu wa Ruaha, haya mbebeni tumpeleke nyumbani na wewe John swaga huyo ng'ombe turudini nyumbani” aliamrisha mmoja wao kwa sauti ya juu.
Safari ya kutoka katika ule msitu mpaka kuingia katika kijiji cha 'Liamkena' usiku wa manane ilifanikiwa kwani nilipofika tu wakaanza kunitibia kidonda changu kwa kutumia dawa za kienyeji huku wanakijiji wengine kutoka katika kijiji kile wakija kunishangaa si kwakuwa nilikuwa natisha bali walistaajabu kuokotwa usiku wa manane kwenye ule msitu ulioaminika kuwa na wanyama wakali tena wengi,
Ndani ya siku moja nikawa tayari nimeshazoea mazingira huku akili yangu nashauku kubwa nikiielekezea nyumbani na jinsi gani nitampata Gervas na kumshukuru kwa yote aliyonitendea.
Hali ya kidonda changu haikuwa mbaya kwani kilianza kufunga taratibu, ila wanakijiji walipenda niendelee kubaki mpaka nipone kabisa jambo ambalo lilipingana na halmashauri ya kichwa changu,
Ilipofika saa tano usiku huku kijiji chote kikiwa kimerindima kwa giza nene. Sikuwa na hata chembe ya usingizi. Jicho langu liliweza kupenyeza kupitia katundu kadogo kadirisha kalichokuwa kametengenezwa kwa kutumia miti. Niliweza kujua mara moja sehemu ya kutokea hivyo nikachana kipande cha gauni langu na kukifunga katika eneo lakidonda changu kisha nikachukuwa mishale na upinde huku upande wa kulia kwangu nikashikilia panga tayari kwa kuingia tena msituni huku nikitafuta barabara ya kutokea,nilifanikiwa kutoroka na kuingia msituni. Akili yangu na mwili wangu vikawa kama vimeshapigwa ganzi kwani sikuwa muoga hata kidogo. Nilitembea taratibu lakini nikaona kama nachelewa hivyo nikaanza kukimbia wakati nakimbia niliweza kusikia kama kuna watu wananikimbiza nyuma yangu kama sivyo basi nitakuwa nimeingia katika ulimwengu wa wanyama pori tena wale wakali nikasimama na kujificha nyuma ya mti kisha taratibu nikachomoa mshale japo nilikuwa sijui kuutumia lakini niliweza kuuelekezea upande wa ile sehemu niliyotoka na kuhisi kile kitu kitakuwa kinatokea upande huo. Niliunyosha na kufanikiwa kuuachia,nikasikia sauti ya kitu kikilia kwa vikwifukwifu.
“nakufaa mama niokoe...ooh.! uuh.! uuh!”
Ghafla ukafuatia mshindo kuashiria kile kitu kimeanguka chini baada ya kuachia mshale wangu wenye sumu kali. Bila kuwa na woga kwa kunyemelea nikaanza kufuata lile eneo kumtambua yule mtu. Nikiwa nikikaribia pale nimeshika panga langu mara akatokea fisi maeneo ya karibu nikamfyeka akawa amekufa. Nikaendelea na zoezi langu la kutambua ni kitu gani kitakuwa mbele yangu. Sikuwa na tochi,ila nilipoukaribia ule mwili niliupapasa lakini bado haikusaidia kumjua ni nani japokuwa ulikuwa ni mwili wa mtu pale chini ambao kwa namna moja au nyingine sikuweza kuutambua mara moja Kwa ushupavu wa halmashauri ya kichwa changu ikanituma nichukuwe panga na kuchana kipande cha nguo yake. Nikafanya hivyo kisha kile kitambaa nikakificha katika pindo la nguo yangu ya ndani halafu safari ikaendelea. Nilikatiza msituni bila kuogopa kitu chochote na wala kumuogopa yeyote. Hatimaye baada ya kukimbia muda refu nikahisi kama kitu kigumu nakanyaga chini. Furaha na amani vikaanza kutawala ndani ya moyo wangu kwani nilikuwa tayari nipo katika barabara ya lami. Akili ikawa katika kukisia ni upande gani ndo utakuwa unaelekea Dar na upande gani utakuwa unarudi Mbeya. Nikiwa bado natafakari likapita basi la kwanza. Nikashindwa kulisimamisha nikaamua kusubiri gari nyingine,kwani sikuwa hata na nauli hivyo nikaamua nijifiche niweze kudandia gari lolote litakalopita kwa mwendo mdogo.
Baada ya kukaa pale takribani lisaa moja na nusu bila ya kuona gari lolote hatimaye nikaliona gari kubwa likiwa linakuja kwa kujikongoja.
“kama kufa wacha nife tu,lakini hili gari siliachi”
nilijisemea kimoyomoyo huku nikijiweka tayari kwa kurukia lile gari aina ya roli,huku mikuki na mishale pamoja na lile panga nikilitupia msituni,kitendo cha lile gari kufika karibu yangu kikawa kosa kubwa sana kwangu kwani ndani ya mda mchache nikawa tayari nipo nyuma ya lile lori lililokuwa limebeba mbao,
Kwa ujasiri niliokuwa nao nikaingia mpaka mule ndani ya lile lori kwa nyuma ambapo sikumuona mtu yeyote kisha nikarudishia mlango na kujilaza kwenye zile mbao huku nikiwa sina uhakika na ninapoenda,
“Sijui ndo litaishia morogoro au ndo la Iringa hili gari?”
Hayo ni kati ya maswali yaliyokuwa yameniandama ndani ya kichwa changu,huku safari ikiendelea taratibu baada ya mwendo mrefu kidogo, ghafla gari likasimama kwa mbali nikahisi sauti ya watu wanajibizana kwa nje.
“Hapana mkubwa mzigo wetu hauwezi kuzidi kiasi hicho”
hapohapo jibu likanijia kuwa tutakuwa tumefika maeneo ya mizani,
“Embu fungua nyuma tuhakikishe maana tani zimezidi na kama hutaki paki pale gari yako uandikiwe faini”"
Wakiwa bado wanabishana pale tayari kwenye gari nikawa natetemeka mwili mzima huku nywele zikinisimama na akili ikinituma nifungue mlango.
Nikisema nijifiche nyuma ya mbao siwezi kwani ni kweli kulikuwa na mbao nyingi kiasi kwamba nilipata kanafasi kadogo sana ka kujificha.
“Mungu saidia! Mungu saidia! saidia jamani!”
ndio maneno niliyokuwa naomba nisiweze kukamatwa kwani nia yangu nikufika Dar.
muda si mrefu nikasikia muungurumo wa gari kuwashwa kuashiria safari inaendelea moyo wangu ukawa na furaha upya nikajihisi ni mtu tofauti sana duniani tena aliye na bahati mbaya kupelekwa gerezani lakini aliyejawa na bahati nzuri uraiani.
Nilikuwa sina hata lepe la usingizi huku safari ikiendelea niliweza kushuhudia tena kwa mara nyingine kuki kuchwa kwani mwanga ulikuwa umeshatoka kuashiria kuwa ni alfajiri. Gari nalo likatembea ka mwendo kidogo kisha likasimama. Sauti na makelele ya watu ndio yalichochea hisia zangu. Niliweza kutoa jicho langu kupenyeza kwenye kauwazi ka mlango nikaweza kushuhudia watu mbali mbali. Moja kwa moja nikapata wazo la kuangalia kile kipande cha nguo nilichokikata kule kwa yule mtu msituni alikuwa ni nani.
Taaratibu mkono wangu ukaanza kupenyeza mpaka kwenye upindo wa nguo yangu ya ndani nikakichukuwa kile kitambaa cha nguo na kukiangalia.
“Mamaa..! Mamaa..! nimeuwa tena mungu wangu!
nisamehe Pendo..! sijakusudia mimi..! Maaaaa aaaaaaah!”
kumbe kile kilikuwa nikipande cha nguo cha rafiki yangu niliotokanaye gerezani Pendo.
Wakati nikiendelea kutoa sauti kali nikahisi kunawatu wamezisikia kelele zangu hivyo nikasikia mlango unafungulia eneo nililokuwa.
“Sauti inatokea humu ndani bwana, tena ni sauti ya kike”
Aliongea mmoja ya watu waliokuwa wanazungumza nje ya lile lori nililokuamo ndani.
“mtoeni.!, mtoeni.! tena anasema ameua, embu mkamateni tumpeleke polisi”
Nilibaki nimezubaa huku nikiwa sijitambui kipi cha kufanya. Nikawa natetemeka sana huku nikiishiwa na pumzi. Nikahisi mapigo yangu ya moyo yakizidiwa kasi kwani nilijihisi napata joto ghafla huku kijasho chembamba kikiambatana na mchozi uliokuwa unanitoka mithili ya maji yakifuata mkondo wake. Sikuwa na jinsi tena kwani niliamini ndoto zangu za kuwa uraiani zimekwisha na sijui ntawaambia nini Gervas na mama yangu endapo watasikia nipo tena gerezani.
Huku kojo likiwa linanimwagika, ukakamavu na ujasiri wote ulinitoka. Nilijikuta natoa tena sauti ya ukali.
“sio mimi..! sio mimi..! jamani msinikamate”
Nilinyosha mikono yangu miwili kuelekea ile sehemu niliyoamini ni mlango,taratibu nikaanza kufungua ili nijisalimishe ile namalizia kufungua tu nikawa tayari nipo mikononi mwa raia nisiowafahamu lakini walikuwa ni wanaume wamevalia sare ambazo sikuweza kuzitambua mara moja huku juu wakiwa na mashati meupe na wengine masweta mekundu kutokana na hali ya baridi kali lililokuwa limezunguka.
Wale watu wenye hasira wakaanza kunishambulia kwa kunipiga makofi huku wengine wakinishambulia kwa matusi makubwa ya nguoni huku wakiniburuza mithili ya mzoga aliyeoza anayeenda kutupwa. Nilipiga kelele lakini haikusaidia nilivutwa sana na wale vijana.
“wauaji kama nyinyi ndo tunaowatafuta”
Aliongea mmoja wa wale watu huku wakiwa tayari wamenichania vipande vya nguo yangu mithili ya Yesu alivyokuwa akichaniwa vipande vya nguo zake na kugawana. Nilikuwa sina tena ujanja na pia kulikuwa hakuna tena muujiza utakaotendeka kwangu ili niweze kujikomboa katika mikono ya wale watu nisiowafahamu walioonekana makatili wasio na huruma hata kidogo.
***************
Waliniburuta kwa mwendo mrefu sana. Umati wa watu ukifurika kunishuhudia. Walipokezana kunishika na kunivuta kwa kuniburuta kwenye ardhi,huku nikiwa bado nalia na kung'ang'ania nisiweze kupelekwa kituoni.
Nilikuwa bado naendelea kulia. Nguvu ziliniishia na kuacha wafanye wanachokitaka.Damu damu zangu ziliendelea kunimwagika pembezoni mwa mdomo wangu. Maji machafu pamoja na matope vilitawala mwilini mwangu huku sura ikiwa imenivimba sana. Niliamini hata nikiendelea kulia haitasaidia chochote. Nilihisi sasa malengo yangu yote baada yakuwa huru yalikuwa yamefikia tamati kwani sasa nilikuwa nikipelekwa polisi.
Tukiwa njiani mwa safari huku kipigo kikinizidia katika mwili wangu na macho yangu yakiangaza huku na kule kupata japo msaada wowote ndipo yakakutana uso kwa uso na kibao kilichoandikwa.
'TOSAMAGANGA HIGH SCHOOL'
Halmashauri ya kichwa changu ikafanya kazi fasta hapo hapo nakugundua kuwa wale si raia wakawaida kama nilivyodhani bali walikuwa ni wanafunzi katika kile kijiji tena katika shule anayosoma Gervas japokuwa sikumuona katika wale watu waliokuwa wakinipiga lakini niliamini lazima alikuwa akisoma katika shule ile kama alivyonielezea hapo awali kwamba anasoma shule ya wavulana tupu iliopo Iringa na inaitwa 'Tosamaganga' hayo yote aliniambia kipindi kile nipo gerezani.
“Kabla hamjanifikisha huko kituoni naomba mniitie Gervas Phota nimuage”
Niliposema hivyo tu wale jamaa waliokuwa wamenishikilia wakaniacha ghafla kwa mshangao huku wengine wakiamini huenda nilikuwa nimejifanyisha nimeua ili niweze kuonana na Gervas na wengine wakijiuliza nimemjuaje Gervas? Wakanikazia macho.
“Gervas.? Mbona sisi hatumjui”
walinijibu huku wengine wakinicheka na kunisonya kwa dharau.
“We Dada una mashetani au kichaa enhh, unamuhitaji nani?”
Jibu alilonipa mmoja wa wale watu lilinifanya niingiwe na woga huku meno yakiumana nakuhisi labda Gervas alinidanganya anasoma shule hii. Lakini haiwezekani!
hasira zilizidi kunipanda kwani kipigo kiliongezeka mara mbili ya pale huku damu nyingi zikiendelea kunimwagika Ghafla nikasikia kama mlio wakengele ukipigwa pembeni ya shule huku watu waliokuwa wamevalia kofia wakiwa wako na virungu mikononi wakinifuata pale nilipokuwa nimeburuzwa na wale wanafunzi. Hofu ilizidi kunitanda kwenye ubongo wangu Mwili ulininyong'onyea kuona wale watu wamevalia sare kama polisi. Kila waliponikaribia lile eneo ndipo nilitamani nife hapohapo. Nikiwa bado nagala gala pale chini huku wale wanafunzi wakianza kutawanyika kwa kuwaogopa wale watu huku wakiniacha peke yangu nilianza kujisogeza kwa mwendo wa taratibu huku nikitumia magoti na makalio yangu kujisogeza mpaka nikaona chupa ya soda,nikaivunja ili niweze kujiua kabla ya wale askari hawajanifikia, nikiwa nataka kuanza zoezi la kujiua mara yule askari akawa ameshanikaribia na kunipokonya ile chupa,
"niache nife.., niacheni jamani!”
Nilikuwa nimeshakata tamaa tena ya kuishi. Kwa haraka niliweza kuyakodoa macho yangu na kumuangalia mtu aliyenipora ile chupa niliyokuwa nimeivunja vunja na kuacha ncha kali nikitaka kujiua. Nikaangalia mara mbili mbili nikagundua kuwa yule hakuwa askari polisi kama nilivyodhani bali alikuwa ni mmoja kati ya wale walinzi wa ile shule waliokuja kutawanya na kuwakamata wanafunzi sugu waliokuwa nje ya shule muda wa masomo.
“pole sana binti angalia sana siku nyingine watakuja kukubaka wale wanafunzi wavuta bangi wale!”
nilishangaa sana yule mlinzi kunipora kisha akaniacha na kuendelea kuwafukuza wanafunzi wengine. Nilijawa na nguvu na furaha ya ajabu nakujiona ni mtu wa bahati tena ya mtende. Watu wengi walinishangaa sana hilo sikujali kwani maisha ya kupigwa kama yale nilishayazoea tangu kipindi kile nipo gerezani.
Huku nikiwa nimelowa damu na kuchanika karibu nguo yote nliokuwa nimeivaa. Niliweza kujikokota chini chini mpaka eneo la nyuma na ile shule kisha nikaegemea chini ya mti mkubwa. Kwa uchovu na maumivu niliyoyapata yalinifanya nianze kunyemelewa na kausingizi japokuwa kulikuwa na baridi kali sikuwa na jinsi yoyote yakukabiliana nalo.
“Twende bwana au unapenda kubaki hapa porini? mimi nakuacha...hapana.
Pendo usiniache..! Pendo usiniache...! usiniache..! usiniache...! usiniache..!
Peeeendooooooooo.......!”
Ghafla nikashtuka nakuanza kuhema kwa kasi huku nikitetemeka Levina mimi kumbe ilikuwa ni ndoto tena nilikuwa nikiota nipo na marehemu Pendo kule msituni. Usingizi ulinikata nakuanza kuangaza kila upande nikaona giza limeanza kutanda lakini upande wa mbele yangu kulikuwa na taa kali zilizomulika ile shule. Nilianza kusogelea taratibu kwa kuzunguka yale majengo yaliokuwa yamewekewa uzio huku nikitafuta lango la kuingilia, Hatimaye niligundua geti lilipo. Walinzi takribani watatu walikuwa wametanda pale lango la kuingilia hivyo nikatafuta eneo la choo kwani niliamini kukijua choo itakuwa ni njia nyepesi ya kuingia ndani ya ile shule. Haraka haraka macho yangu yaliweza kuona wanafunzi wakiongozana wakiingia kwenye jengo lingine lililoonekana si kubwa sana kama majengo mengine huku wakiingia na kutoka. Kwa ujasiri na kwa shauku niliokuwa nayo ya kutaka kupambana mpaka nimuone Gervas nikawa na nguvu ya ajabu yakuweza kuruka ukuta japokuwa haukuwa mrefu sana . Ndani ya dakika chache nilikuwa tayari nipo kwenye kale kajengo kalichokuwa na vyoo vingi vyote vikiwa na milango nikaingia choo kimojawapo na kujifungia huku nikishuhudia hamna mtu ndani. Harufu kali ya kinyesi na mikojo katika vile vyoo nilipokuwamo ndani havikunizuia hata kidogo kuondoka mule ndani. Niliweza kutulia kimya huku nikiombea aje kati ya Gervas au mwanafunzi yeyote nimuulizie Gervas. Mpaka nilijishangaa kwa jinsi nilivyokuwa sina woga wowote.
Ghafla nikasikia sauti ya kama mtu anakuja. Nikazidi kukaa kimya ndani ya choo huku nikijiuliza ntaanzaje mara ile sauti ya mtu akiingia na kuanza kukojoa mlango wa pembeni yangu, nikafungua mlango wangu taratibu na kuanza kunyata kuelekea mlango aliokuwepo huku akili ikinituma nimuwahi na kumnyamazisha kabla hajashtuka na kuanza kupiga kelele.
“Shhh.....!!! usiniogope wala usikimbie,naitwa Levina natokea...”
Kabla sijamaliza kujitambulisha yule mwanafunzi akawa ameshanitambua.
” We si yule dada ambaye nimetoka kuskia stori yako sasa hivi kwa wenzangu kuwa umepigwa na kukuburuzwa mchana kutwa pale nje na umeokolewa na walinzi.?”
“Ndio mimi ila nipo hapa kwa msaada mmoja tu, unamfahamu Gervas Phota?”
“namfahamu na ninasoma naye lakini yupo Chumbani anaumwa leo siku ya pili yupo kitandani”
“tafadhali nisaidie kwa hili nenda kaniitie mwambie Levina, nipo hapa hapa chooni kwenye mlango huu nawasubiria mtanikuta.”
Ndani ya muda mfupi nikawa tayari nimeshayazoea mazingira ya kile choo ikiwa ni pamoja na harufu kali ya mule ndani, niliweza kujifungia mlango mmojawapo kwa mda mrefu tangu nimefika bila ya hata mtu yoyote kujua, mara nikasikia sauti ya watu wanaongea kwa nje huku sauti kama niliyokuwa naifahamu nilianza kuingiwa na furaha na amani isiyokuwa na kifani kwani niliamini Gervas ndiye mkombozi wangu na anayepajua mpaka nyumbani kwetu kwani nilikuwa nimeshapasahau hadi jina la mtaa,sikutaka kujitokeza hvyo nikavuta subira huku nikiisikia ile sauti kwa umakini taaratibu nikaweza kuitambua kuwa haikuwa sauti ninayoifahamu hata kidogo na hata maongezi waliokuwa wanaongelea hayakuwa yakiunafunzi hivyo halmashauri ya kichwa changu ikapambanua fasta na kujua kuwa wale watakuwa ni walinzi kwani walikuwa wanaongelea mambo ya kifamilia na kikazi tena kazi ya ulinzi, moyo ulianza kuniripuka kwani walikaa muda mrefu huku wakipiga stori na hata wanafunzi walipokuja nilisikia wakiwaamkia na kujisaidia na kuondoka zao,kwa ujumla nililegea sana na akili ilishaanza kuchoka,nikiwa bado nipo nao wale walinzi chooni huku wakinogewa na stori ila mlango nilikuwa nao tofauti bila ya wao kujua ghafla nikasikia sauti kali iliyotokea upande wa nje huku ikilitaja jina langu.
“LEVINAAAA...! LEVINAAA...! LEVINAAA...!”
“YUPO MLANGU UPI UMESEMA.?”
Nilitamani niweze kutoka lakini haikuwezekana kutokana na wale walinzi kukaa muda mrefu wakipiga stori, hakika ile sauti ilikuwa ni ya Gervas akiongea na mwenzake huku nikihisi ameshakaribia kuingia mule chooni, ghafla nikasikia ukimya umetanda halafu yakafuatia maswali kutoka kwa wale walinzi wakimuuliza Gervas,
"Levina..! Levina ndio nani? Na mbona mwenzako amenyoosha kidole mlango huo ambao umefungwa..?
Kuna nani...?"
wakiwa wanajibizana na walinzi mara umeme ukakatika na giza nene likatanda woga ukawa umenitawala huku nisijue nini kinaendelea mara nikaanza kuisikia sauti ya Gervas na walinzi kwa mbali huku ikitokomea nisijue wanaelekea wapi,ndani ya muda mfupi,mara umeme ukakatika
“Levina wangu bado upo?”
“nipo Gervas wangu.”
Nilitoka kwa shangwe zote huku nikiamini kuwa atakuwa Gervas tena kwa mara hii ya pili atakuwa kaja peke yake hayupo tena na wale walinzi. Gervas bado alikuwa hajiamini amini kama kweli ni Levina mimi kutokana nakuwa na giza maeneo yale lakini sauti yangu ilikuwa jibu tosha kwa yeye kuniamini.
“Twende mpaka hostel kwetu kulee”
“Gervas mimi naogopaa hatuwezi kushikwa,na je wenzako wakiniona?”
“uko na mimi wala usiwe na wasiwasi Levina wangu.”
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment