Search This Blog

Sunday, July 10, 2022

MOYO WANGU UNAVUJA DAMU - 5

 





    Simulizi : Moyo Wangu Unavuja Damu

    Sehemu Ya Tano (5)





    ****



    “My God! She is my beloved Mum…”

    Alikuwa ni mama yake, Bi Miriam!



    Muda mfupi tangu Khaleed aondoke na kumuacha Girbons juu ya mti, Alibanwa na haja hivyo kulazimika kushuka chini. Aliamini hakuna ambaye angemuona kwani giza lilikuwa limetanda kila mahali. Alishuka taratibu mpaka chini na kuelekea kwenye kichaka kilichokuwa pembeni ya ule mti. Akiwa kwenye kile kichaka, alishtushwa kuona watu watatu wakiwa na tochi kubwa mikononi mwao, wakija usawa wa ule mti aliokuwepo. Walianza kumulika juu ya mti, wakimulika zaidi katika lile tawi walilokuwa wamejificha Girbons na Khaleed mchana kutwa tangu walipowasili asubuhi iliyopita.



    Wale watu waliendelea kumulika juu huku wakiulizana maswali ambayo Girbons akiwa pale kwenye kichaka aliweza kuyasikia vizuri.

    “Una uhakika ni huu mti kweli?”

    “Ni huu huu, nina uhakika kabisa kwani niliwaona mwenyewe kwa macho yangu. Walikuwa wawili na huyo mmoja ndio zeruzeru”



    Alikuwa akiongea mmoja wa wale watu kwa msisitizo mkubwa. Girbons alielewa moja kwa moja kuwa aliyekuwa akitafutwa ni yeye. Alijikuta akitetemeka mwili mzima na kukumbwa na hofu ya ajabu. Akiwa bado palepale kichakani alipojificha, wazo pekee lililomjia kichwani mwake ilikuwa ni kutimua mbio kwa kadri ya uwezo wake wote ili kuinusuru nafsi yake. Wale watu walikuwa wakizidi kuulizana maswali kwa sauti ya chini pale chini ya mti.



    “Hata kama watakuwa wameshuka basi hawajafika mbali, tukiwawahi tutawakuta tu! Tusiachie mamilioni ya yule zeruzeru yatupotee kirahisi namna hii. Tukipata hata kiganja kimoja kinatosha sana na tutakuwa tumeuaga umaskini!”

    Wale watu wenye roho za kishetani walikuwa wakizidi kujadiliana na sasa Girbons aligundua kuwa kumbe walikuwa na shida na viungo vya mwili wake.



    “Why me Albino! Oooh My God, save me” (Kwa nini niumbwe nikiwa Albino? Eeh Mungu niokoe) Aliongea Girbons na kwa kasi ya ajabu akaanza kutimua mbio kuondoka pale alipokuwa amejificha. Hakufika mbali akashtukia anamulikwa na tochi kubwa, kisha wale watu wakaanza kumfukuza. Sekunde chache baadae walikuwa wameshamkamata na wakamrudisha pale chini ya mti huku wakimtishia kuwa akipiga kelele basi ule ndio ungekuwa mwisho wake.



    Watu watatu waliokuwa wamevalia kofia maalum (Mask ) zilizoziba sura zao walikuwa wamemzunguka huku kila mmoja akiwa na kisu kikubwa mkononi. Girbons alijikuta akiishiwa na nguvu, akajua huo ndio mwisho wake. Alipiga yowe kubwa lakini wakamuwahi na kumziba mdomo asizidi kupiga kelele.



    Walimlaza chini na mmoja akamkandamiza mgongoni kwa nguvu. Yule mwingine alimkamata mkono kwa nguvu na kuuweka vizuri. Akainua kisu kikubwa alichokuwa amekishika na kukishusha kwa nguvu kwenye mkono wa Girbons.

    Kufumba na kufumbua, kiganja cha mkono kilikuwa kimetenganishwa kabisa na mkono.



    Girbons alishuhudia yule mtu akikiokota kile kipande cha mkono wake na kukiweka kwenye mfuko mweusi wa plastiki wakiacha damu nyingi zikimwagika kutoka kwenye jeraha kubwa mkononi.



    Yale maumivu aliyoyahisi yaliamsha nguvu za ziada za Girbons. Aliwarusha wale watu waliokuwa bado wamemkandamiza chini wakijiandaa kumkata mkono mwingine. Kwa nguvu za ajabu aliinuka na kutimua mbio kali akiwaacha wale watu wakipongezana kwa kufanikisha japo kidogo zoezi lao. Mkono wake ulikuwa umebakia kipisi ukivuja damu nyingi kuliko kawaida. Hakujali maumivu aliyokuwa akiyahisi, akazidi kutimua mbio akiwa hajui anakoelekea.

    ********

    Mvua kubwa ilikuwa ikinyesha ikiambatana na radi zilizokuwa zinapiga kwa nguvu, hali iliyowafanya watu waote wajifungie majumbani mwao. Mitaro ya kando ya barabara ilikuwa ikifurika maji yaliyokuwa yanaenda kwa kasi. Usafi wote uliozoeleka katika mitaa iliyopangwa vizuri, ulitoweka na barabara zote zikawa zimejaa takataka zilizosombwa na maji ya mvua.



    Mitaro yote ya maji ilikuwa ikienda kumwaga maji baharini, kwenye bahari ya Hindi. Upande wa pili wa mji, kulikokuwa na bandari kubwa iliyotmika kama kitovu cha mawasiliano kati ya nchi ya Blaziniar na majirani zake, ikiwemo nchi ya Tanzania, shughuli za kupakia na kupakua mizigo zilikuwa zikiendelea kama kawaida.



    Meli kadhaa zlikuwa zikiendelea kupakia mazao ya biashara na chakula kama karafuu, nazi, ndizi na mchele kupeleka nchi jirani. Blazinia ilikuwa ikitegemewa na majirani zake kwa kuzalisha mazao mengi ya chakula yaliyokuwa yakisafirishwa kwa meli na kwenda kuuzwa nchi jirani.



    Meli kubwa iliyokuwa na maandishi makubwa ubavuni yaliyosomeka MV PAINA ilikuwa ikijiandaa kung’oa nanga kuelekea nchini Tanzania, ikiwa na shehena kubwa ya mizigo. Manahodha na mafundi walikuwa kwenye vyumba vya chini vya meli (Main Deck) wakikagua injini na mitambo mingine kwa mara ya mwisho kabla hawajairuhusu meli ianze safari.



    Nahodha mkuu, Weston Maseleka ndio alikuwa akiwaongoza mafundi wengine na kuwaelekeza sehemu za kuzifanyia uchunguzi. Yeye aliingia kwenye chumba cha ndani kabisa nilichokuwa na injini kubwa. Akiwa anaendelea na kazi yake, kwa msaada wa mwanga wa tochi kubwa aliyokuwa ameishika, aliona kitu ambacho kilimshtua mno. Ilikuwa ni michirizi mikubwa ya damu ambayo ilikuwa imetapakaa chini. Hakufahamu mara moja damu ile imetoka wapi na imekuwaje, akajikuta akipatwa na hofu. Kwa tahadhari kubwa akaanza kuifuata kuelekea kule ilikokuwa inatokea. Kwa kadri alivyokuwa anzidi kusogea, michirizi ilizidi kuongezeka, akazidi kuifuata kwa msaada wa tochi kubwa aliyokuwa ameishika.



    Gkafla aliona kitu ambacho kilimshtua mno moyo wake, akajikuta aktetemeka mwili mzima. Ulikuwa ni mwili wa kijana mdogo wa kiume mwenye ulemavu wa ngozi. Alikuwa amelala chini huku mkono mmoja ukionekana kuvuja damu nyingi. Alizidi kumsogelea akiwa amemmulika na tochi kubwa pale chini alipolala. Hakuonekana kutingishika wala kugeuka, aliendelea kubaki vilevile. Aliinama na kumgusa mapigo ya moyo.

    “Ooh My God! Whats this?”

    *******

    Khaleed alikuwa amekaa juu ya mchanga wa baharini akiwa analia kwa uchungu baada ya kuamini hatamuona tena ndugu yake wa pekee aliyekuwa amesalia duniani, girbons. Japokuwa mvua kubwa ilikuwa inanyesha, hakuonekana kujali kuloana. Akawa amekaa chini huku mvua kubwa ikiendelea kumnyeshea. Alijikuta akiichukia nchi yake kuliko kitu chochote. Akili yake ilikua ikiwaza jambo moja tu, kutoroka na kwenda nchi jirani kwani alishakosa uhakika wa usalama wake ndani ya nchi aliyozaliwa. Hakuwa na ndugu tena, alishawapoteza mama na baba, kaka na dada na mwisho alikuwa amesalia peke yake.



    Mvua iliendelea kunyesha kwa muda mrefu na hatimaye ikaanza kupungua. Japokuwa alikuwa akiwaza kutorokea nchi ya jirani, hakujua angewezaje kuondoka kwani hakuwa na pesa hata kidogo. Aliendelea kukaa pale chini mchangani akizitazama meli zilizokuwa zikiingia na kutoka bandarini. Wazo pekee aliloliona linafaa kwa wakati ule ilikuwa ni kuzamia meli ya mizigo. Mvua ilipungua kabisa na sasa hali ya hewa ikaanza kuwa ya kawaida.



    Khaleed aliinuka kutoka pale alipokuwa amekaa na taratibu akaanza kutembea kuelekea bandarini. Alipanga kutumia mbinu zake zote, ilimradi ahakikishe anandoka siku ileile. Alitembea taratibu ufukweni huku mawazo yakipishana kichwani mwake. Roho ya kisasi ilikuwa ikiwaka ndani yake mithili ya moto wa Jehanum. Aliamini hakustahili kuishi maisha kama yale, maisha ya upweke,maisha ya uyatima kwa sababu tu ya tamaa za watu wachache.

    “I must revenge! Damn ‘em to hell! (Lazima nilipe kisasi, wote wakatupwe kuzimu)

    Alikuwa akijisemea Khaleed huku akijifuta machozi. Macho yake yalikuwa yamebadilika na kuwa mekundu sana baada ya kulia kwa muda mrefu. Aliendelea kutembea taratibu akielekea bandarini huku kichwani akiendelea kupanga mbinu za namna atakavyofanikisha zoezi la kuzamia meli.

    *****



    Baada ya kuwasili mjini Tanga nchini Tanzania, Khaleed anajichanganya pamoja na watoto wanaoshinda bandarini wakifanya kazi ya kubeba mizigo na kuambulia ujira mdogo. Kwa kuwa alikuwa akiijua vizuri lugha ya Kiswahili, hakupata taabu kuchanganyikana na watoto wa mitaani. Ndani ya siku mbili tu akawa tayari ameshaanza kuyazoea mazingira ya mji mkongwe wa Tanga. Alikuwa akibeba mizigo kama wenzie na ujira mdogo alioupata ulimfanya awe na uhakika wa kula, wakati usiku alikuwa akijichanganya na wenzake na kulala kwenye meli mbovu zilizokuwa pale bandarini. Akawa ameyaanza maisha mapya ugenini, akiapa kuwa lazima atarudi kwao kwa lengo moja tu, kulipa kisasi kwa wote waliohusika kuisambaratisha familia yao.



    Siku zikawa zinasonga mbele na akawa anazidi kuwa mwenyeji wa mazingira mapya. Pesa aliyokuwa anaipata kutokana na kazi yake ya kubeba mizigo aliweza kuitumia vizuri kwa uangalifu na akiba ndogo iliyokuwa inasalia, alikuwa akiihifadhi ili apate mtaji wa kufanya biashara ndogo ndogo. Baada ya siku chache, aliamua kuachana na kazi ya kubeba mizigo kwani alishapata akiba iliyomuwezesha kuanzisha biashara ndogo ya kuuza pipi barabarani. Aliendelea kuhangaika na maisha, na baada ya kuzunguka siku nzima akiuza pipi zake barabarani na kwenye stendi za daladala, usiku alikuwa akirejea kwenye meli mbovu na kulala na watoto wa mitaani.



    Alijitahidi kufanya biashara kwa umakini mkubwa na taratibu mtaji wake ukawa unakua. Aliacha kuuza pipi na sasa akafanikiwa kupata meza ya kuuzia machungwa karibu na kituo kikuu cha mabasi. Baada ya miezi miwili kupita alishakuwa mwenyeji kabisa wa mji wa Tanga na usingeweza kumdhania kuwa ni mhamiaji. Alifanikiwa kupata chumba cha kujisitiri kwenye banda la uani la mama mmoja na pesa kidogo alizokuwa anazipata kwenye biashara yake akawa analipia kodi ya pango pamoja na kujikimu mahitaji madogo madogo kama chakula na mengineyo. Hakutaka mtu yeyote afahamu historia halisi ya maisha yake, hiyo ikabaki kuwa siri ndani ya moyo wake.



    Heshima, upole, ukarimu na nidhamu ya hali ya juu aliyokuwa nayo vilimfanya apate wateja wengi kwenye biashara yake ya machungwa. Taratibu akaanza kuwa na jina. Mbali na kufanya biashara yake, Khaleed alikuwa na kipaji cha kuimba muziki ambao kwa Tanzania walikuwa wakiuita wa kizazi kipya. Kila siku jioni baada ya kumaliza biashara yake, alikuwa akiimba mashairi aliyoyatunga akiwa palepale kwenye biashara yake na watu wengi walionekana kuvutiwa na kipaji chake.



    “Jamani huyu kaka anaimba vizuri! Mi nampenda”

    Alisikika binti mmoja akiwaambia wenzake wakati wakitoka shule jioni moja. Khaleed alizidi kujijengea umaarufu mkubwa na akafanikiwa kupata marafiki wengi. Pamoja na kubadili kabisa mazingira ya kuishi, bado jinamizi la vifo vya ndugu zake lilikuwa likimwandama mara kwa mara. Alikuwa akijiwa na kumbukumbu mbaya za mambo aliyoyashuhudia akiwa na umri mdogo tu. Kumbukumbu ya vifo vya wazazi wake, wadogo zake na tukio la kaka yake mwenye ulemavu wa ngozi kufanyiwa ukatili wa kutisha vilikuwa vikimfanya alie sana usiku akiwa peke yake.



    Roho ya kisasi ilikuwa ikiongezeka siku baada ya siku na kadri alivyokuwa akizidi kukumbuka, hamu ya kisasi nayo ikawa inazidi kuongezeka. Hakupenda kujihusisha na mambo ya ujana kama wenzake aliokuwa anafanya nao biashara ambao pesa kidogo walizokuwa wakizipata kama faida walikuwa wakizimalizia kwenye pombe na kustarehe na wanawake. Kwake ilikuwa tofauti na siku zote alikuwa akifahamu kuwa kuna jukumu zito mbele yake lililokuwa linamngoja, jukumu la kulipa kisasi cha damu.



    Pamoja na kujitahidi kwa kadri ya uwezo wake kuwaepuka mabinti kabla hajafikia umri wa kuoa kama alivyokuwa akiaswa na marehemu baba yake enzi za uhai wake, alijikuta katika wakati mgumu mbele ya mabinti wa kitanga ambao kila siku walikuwa wakienda kujaa kwenye meza yake anayofanyia biashara wengi wakionekana kuvutiwa naye kimapenzi. Kihaiba, mchanganyiko safi kati ya baba yake na mama yake aliyekuwa na asili ya visiwa vya Shelisheli ulimfanya Khaleed kuwa na haiba yenye mvuto. Ukiongeza na kipaji chake cha kuimba, alijikuta akiwa katika wakati mgumu zaidi wa kukwepa kujitumbukiza katika janga la ngono katika umri mdogo kwani miongoni mwa mambo aliyokuwa akitahadharishwa sana na wazazi wake ni hilo.



    Baada ya kupata pesa ya kutosha, Khaleed alipata wazo jipya akilini mwake, la kwenda kujaribu bahati yake kwenye machimbo ya madini ya Tanzanite, huko Mererani mkoani Arusha, kaskazini mwa nchi ya Tanzania. Aliamini kuwa akifika huko maisha yanaweza kumnyookea kwani wengi wa vijana waliokuwa wakizamia machimboni, walikuwa wakirudi na utajiri. Akaanza kuandaa safari ya kuelekea Mererani kwa msaada wa pesa za akiba alizokuwa anajiwekea. Hakutaka kupoteza muda tena pale mjini Tanga, akafungasha kila kilichokuwa chake , akaaga kwa mwenye nyumba wake kisha akaenda stend ya mabasi ya Arusha alikokata tiketi tayari kwa safari.



    Baada ya safari ndefu, hatimaye alikuwa ndani ya jiji la Arusha na hakutaka kupoteza muda jijini Arusha, alitafuta usafiri wa kumfikisha machimboni Mererani. Alifika salama na akajichanganya na vijana wengine waliokuwa wamezamia machimboni kutafuta maisha. Akiba ndogo aliyokuwa nayo aliitumia kwa ajili ya chakula na muda wa kulala alikuwa akilala kwenye makambi wanayolala wachimbaji wadogowadogo. Kwa kuwa alishapitia maisha ya mtaani akiwa mjini Tanga, haikumuwia vigumu sana kuyazoea mazingira.



    Pesa ya akiba aliyokuwa nayo ilianza kupukutika kwa kasi kwani bado hakujua nini cha kufanya awapo machimboni pale, hali iliyomfanya awe anatumia pesa bila kuingiza chochote. Alianza kuchakarika kutafuta kazi ya kufanya kabla hajaishiwa kabisa pesa. Akafanikiwa kupata kibarua cha kutoa mchanga wenye madini kutoka kwenye mgodi uliokuwa unamilikiwa na kampuni moja ya kigeni. Aliungana na vijana wengine wengi waliokuwa wakifahamika kwa jina la utani la “Nyoka” kwani walilazimika kutambaa kama nyoka wanapokuwa chini kabisa ya mgodi kutafuta mchanga wenye madini.



    Kazi ile ilikuwa ngumu sana na ya hatari, lakini kwa kuwa hakuwa na jinsi nyingine ya kufanya, aliona ni bora aendelee kuvumilia mpaka atakapofanikiwa. Siku ya kwanza kuingia mgodini, alihisi kama anaingia kuzimu kwani njia ya kuingilia chini uliko mchanga wenye madini ya Tanzanite, ilikuwa ni ndogo sana na walilazimika kutambaa kama nyoka huku kukiwa hakuna hewa ya kutosha wala mwanga na walilazimika kufanya kazi kwa muda wa masaa mengi. Ni siku hiyo hiyo ya kwanza kuingia mgodini, alishuhudia jinsi vijana wenzake walivyokuwa wakipoteza maisha wakiwa mgodi kutokana na kuangukiwa na vifusi vikubwa vya udongo na wengine kwa kukosa hewa.



    “Chalii ‘angu huku chini bila kupata imani ya kazi bado hujaweza kufanya kazi, kunatisha mno! Ukiwa na roho nyepesi utakimbia mwenyewe, ukilemaa imekula kwako”

    Aliongea kijana mmoja ambaye baadae alikuja kuwa rafiki yake, kwa lafudhi ambayo Khaleed hakuitambua kuwa ni ya kabila gani. Alikuwa akimwelekeza namna ya kufanya kazi kwenye mazingira magumu kama yale na akamsisitiza kuwa asiogope kukutana na maiti kila baada ya hatua chache kwani hiyo ni hali ya kawaida pale mgodini. Khaleed alijikuta akiingiwa na woga kuliko kawaida kwai aliamini akikimbilia Tanzania angekuwa na amani, sasa hali aliyokuwa akiiona kule chini ilimfanya asijue nini cha kufanya.



    Muda wa kazi uliisha na wakaamriwa kutoka kuwapisha watu wa zamu nyingine waingie. Ujira waliopewa kwa kazi ile ulikuwa mdogo sana usifanana na ugumu wa kazi waliyoifanya. Khaleed alijilaumu kwa nini alifikia uamuzi wa kwenda Mererani bila ya kufahamu vizuri kilichokuwa kule. Aliona ni bora angeendelea kuuza machungwa mjini Tanga kuliko kuenda kuhatarisha maisha yake namna ile. Lakini kwa kuwa alikuwa ameshayavulia maji nguo, hakuwa na jinsi zaidi ya kuyaoga. Aliona bora aendelee kujikaza mpaka kieleweke.

    Wiki ya kwanza ndani ya machimbo ya Mererani, Khaleed anashuhudia mambo ambayo yanamuogopesha kupita kawaida. Anajuta zaidi kwa kuamua kwenda Mererani kwani kila siku anashuhudia jinsi vijana wenzake wanavyopoteza maisha huku kukiwa hakuna mtu anayemjali mwenzake.



    Wanatumikishwa kwa masaa mengi ndani ya mazingira yanayotisha mno, wakilazimika kukaa ndani ya mashimo kwa masaa zaidi ya kumi na mbili kila siku. Anakutana na kijana mmoja wa kimasai anayegeuka na kuwa rafiki yake mkubwa, akimuelekeza namna ya kuishi napo Mererani.



    Siku moja wakiwa ndni ya mgodi, zamu ya usiku, kunatokea ajali mbaya sana. Ilikuwa ni majira ya saa kumi na mbili za jioni, Khaleed na wenzake wakiwa wamepangwa zamu ya usiku. Kama kawaida kila mmoja alikuwa na zana zote za kufanyia kazi, tochi kubwa iliyofungwa kichwani huku mkononi kilammoja akiwa na sululu na koleo.



    Baada ya watu waliokuwa zamu ya mchana kutoka wote mgodini, watu wa zamu ya usiku walianza kuingia, Khaleed akiwa miongoni mwao. Wakati wanaingia, kulikuwa na dalili ya mawingu mazito kuashiria kuwa muda mfupi baadae mvua kubwa ingenyesha.



    “Chalii angu unaona hili wingu! Mvua itanyesha kinyama leo, huko chini inabidi kuwa makini maana mvua ikinyesha hali huwa inakuwa mbaya.”

    Rafiki yake Khaleed mwenye asili ya kimasai, aliyeitwa Ololosokwan alikuwa akimtahadharisha baada ya kuona dalili zote za mvua kubwa kunyesha. Walianza kuingia mgodini kwa kupitia njia mbili tofauti.



    Ilibidi Khaleed aongozane na rafiki yake Ololosokwan kwa sababu za kiusalama zaidi. Waliendelea kushuka kuelekea chini kabisa ya mgodi (Mantle). Wakati wakizidi kuteremka, walianza kusikia hali isiyokuwa ya kawaida. Hewa ilipungua sana na wakawa wanahangaika kupumua. Mara walishtukia kuona maji mengi yakiporomoka kutoka juu kuwafuata kule chini.



    “Si nilikuambia chalii ‘angu! Kazi imeanza. Nishike mgongoni na usiniachie”

    Khaleed alitii alichoambiwa na akamshikilia Ololosokwan kweye vazi lake la kimasai. Maji yakawa yanazidi kuporomoka kwa kasi huku wenzao waliokuwa nao kwenye msafara mmoja wakianza kupiga kelele za kuomba msaada.



    Muda mfupi baadae mgodi ulikuwa unatiririka maji yaliyokuwa yanaenda kwa kasi kubwa, na kwa macho yake, Khaleed alishuhudia wenzake wakisombwa na maji kuelekezwa chini kabisa. Yule rafiki yake wa kimasai alikuwa akihangaika kutoboa ukuta wa mgodi kwa kutumia sululu yake. Aliendelea kuchimba kwa nguvu huku Khaleed akiwa amemshikilia kwa nguvu mgongoni kuzuia asije kusombwa na maji.



    Baada ya kuhangaika kwa muda, hatimaye walifanikiwa kutoboa ukuta wa udongo na kuibukia kwenye njia ya pili iliyokuwa kavu. Ololosokwan alimvuta Khaleed kwa nguvu na wakawa wako eneo salama. Waliendelea kusikia vilio vya wenzao wakilia kwa sauti kubwa kuomba msaada lakini hakuna aliyewasikia. Bila kupoteza muda, walianza kupanda juu kutafuta njia ya kutokea. Walizidi kusikia maji yakipororomoka na kuwasomba wenzao wengi, wakazidi kuongeza kasi ya kupanda juu.



    Ile njia waliyokuwa wameingia Kheleed na yule rafiki yake wa kimasai ilikuwa haitumiki kwa muda mrefu kutokana na ubovu uliokuwa umetokea kwenye mlango wa kuingilia. Pamoja na ubovu ule, haikuwa na maji kama zilivyokuwa njia nyingine. Walizidi kutambaa wakipanda juu kuelekea nje. Wakiwa wanakaribia kufika nje, Khaleed aliona kitu kilichomfanya aishiwe nguvu.



    Alikuwa ni nyoka mkubwa sana akitambaa kuwafuata kule walikokuwa. Alimvuta miguu Ololosokwan na kumuonyesha yule nyoka na kwa haraka Ololosokwan alitoa sime kiunoni mwake na kumuwahi kabla hajaleta madhara. Alirusha sime yake na kumtenganisha kichwa na kiwiliwili. Khaleed hakuamini alichokiona. Ololosokwan aliokota sime, akaifuta damu na kuiweka tena kiunoni na safari ya kupanda juu ikaendelea.



    Wakati wanaendelea kupanda, Ololosokwan alimwambia Khaleed kuwa kwenye hiyo njia wanayopita, alikuwa ameficha jiwe kubwa la Tanzanite siku nyingi zilizopita, lakini alikuwa akishindwa kulitoa nje kwa kuhofia kukamatwa nalo, kwani walinzi wangeweza kumuua. Akamwambia kuwa kwa kuwa yeye bado hafahamiki vizuri na kumetokea ajali ile ya mgodi kujaa maji, watumie nafasi hiyo kulitoa mpaka nje na kama wangefanikiwa basi wangekuwa wameuaga umaskini.



    Khaleed alisita kidogo kukubali lakini alipofikiria kuwa kilichompeleka Mererani ni kutafuta pesa, ilibidi akubali. Walienda mpaka pale alipomuelekeza kuwa alilificha jiwe lile, ambalo kwa haraka lilikuwa na uzito ulio karibia gramu 900 (karibu kilo moja). Kaleed hakuwahi kuyaona madini ya Tanzanite kwa macho, akajikuta mwili mzima ukitetemeka kwa hofu kwani hakuamini kuwa masaa machache yajayo angekuwa ameuaga umaskini kabisa.



    Wazo pekee lililokuwa akilini mwake ilikuwa ni namna ambavyo angerudi upya kwao kulipa kisasi. Alilificha ndani ya kaptura yake ya Jeans aliyokuwa ameivaa kwa ndani na akahakikisha haliwezi kudondoka. Waliendelea na safari ya kutoka nje na baada ya muda wakawa wamefika sehemu ya kutokea nje. Walipochungulia nje, waliona vikosi vya uokoaji vikijitahidi kuzuia maji yasizidi kuingia mgodini huku wengine wakiitoa miili ya watu ambao walikuwa wameshapoteza maisha kutokana na maji yale. Miili ya vijana wengi ilikuwa imelazwa ardhini na kufunikwa kwa mashuka meupe na bado miili mingine ilikuwa ikizidi kutolewa. Ilikuwa ni ajali mbaya kuliko zote zilizowahi kutokea kwenye machimbo yale.



    Khaleed na Ololosokwan walikubaliana kuwa watumie mbinu ya kujifanya mmoja anamuokoa mwenzake ili wasije kushtukiwa na kupekuliwa kwani walitokea kwenye mgodi ambao ulikuwa umepigwa marufuku kwa mtu yeyote kuutumia. Wakakubaliana kuwa Khaleed ajifanye amepoteza fahamu na masai Ololosokwan ambebe mpaka kule waliko waokoaji kisha atajifanya amerudiwa na fahamu ndipo waondoke eneo lile. Khaleed alikubali na akalihamisha lile jiwe la Tanzanite na kulifunga vizuri kwenye sehemu zake za siri.



    Khaleed alifanya kama walivyokubaliana, na yule masai akambeba kama mtu aliyepoteza fahamu. “Saidia mimi yeyoo!”. Aliongea kwa sauti Ololosokwan na waokoaji wakamkimbilia na kumpokea Khaleed aliyekuwa amembeba mikononi. Akaenda kulazwa kwenye sehemu waliyolazwa maiti wengine. Alijikuta mwili mzima ukimsisimka kwani alilazwa katikati ya maiti za vijana wenzake waliokuwa nao kule ndani ya mgodi. Ololosokwan akawawahi na kuwaambia kuwa ndugu yake alikuwa bado hajafa na anaomba aendelee kumpatia huduma ya kwanza.



    Walimkubalia bila kujua kuwa walikuwa wamepanga mbinu kali ya kutorosha mali yenye thamani kubwa. Ololosokwan alimbeba tena Khaleed na akamsogeza pembeni ambako hakukuwa na watu wengi. “Sasa chalii ‘angu hapa tunaelekea kulamba dume, tukifanikiwa mi n’tanunua ng’ombe wengi sana na kurudi nao kwetu Kibororony. We utajua cha kufanya mwenyewe.” Ololosokwan alikuwa akimnong’oneza khaleed sikioni kwa lafudhi ya kimasai wakati akijifanya kama anamsaidia kupumua.



    Wakati wakiendelea kutafuta mbinu ya namna ya kutoka, kuna walinzi ambao walikuwa wamewashtukia na wakawa wanawafuatilia kwa karibu. Walihisi lazima kuna mzigo waliouficha kwani walikuwa wakimfahamu vizuri yule Masai kwani mara kwa mara alikuwa akijaribu kutoroka na mzigo lakini alikuwa akishindwa kutokana na kubanwa na walinzi.



    Khaleed aliinuka na kujifanya amepata nafuu na wakawa wanatembea huku Masai akiwa amemshikilia begani.



    Walielekea kwenye kichaka kilichokuwa karibu na mgodi na walipofika nyuma ya kichaka, mahali ambapo waliamini hakuna anayewaona, walianza kutimua mbio kali kuzidi kutokomea porini. Mi si nilikuambia, yule Masai mjanja sana. Hebu waone wanavyokimbia! Lazima watakuwa wametoka na mzigo. Njoo tuwawahi inaweza kuwa ni bahati yetu leo. Tukikuta wana mzigo wa maana, bora kuwapiga risasi halafu sisi tutambae na mzigo.



    Walinzi watatu wa mgodi walikuwa wakijadiliana baada ya kuwaona Masai na Khaleed wakitimua mbio kuzamia vichakani. Wakaweka silaha zao mikononi na kwa kasi ya ajabu wakaanza kukimbia kuelekea kule Khaleed na Masai walikokimbilia.

    *****



    Khaleed na rafiki yake wa kimasai, Ololosokwan walifanikiwa kutoroka na jiwe kubwa la madini ya Tanzanite kutoka kwenye mgodi wa Mererani baada ya ajali mbaya kutokea katika mgodi huo kufuatia ya maji kujaa kwenye mashimo yaliyokuwa na watu ndani yake.



    Wakati wanatoroka walinzi watatu waliwashtukia na wakawa wanawafuatilia kwa makini. Baada ya kuwaona wakitimua mbio kuzama vichakani, wale walinzi nao waliweka silaha zao tayari na kuanza kuwakimbiza. Khaleed na rafiki yake mmasai hawakujua kama wanafuatiliwa kwa nyuma, wakawa wanakimbia wakiamini hakuna aliyewaona. Mbele kidogo, masai anachezwa na machale na anamwambia Khaleed anahisi kuna hatari iliyokuwa inawakaribia. Ilibidi apande juu ya mwamba mkubwa wa mawe na kutazama kule walikokuwa wametokea.



    Hakuamini macho yake alipowaona walinzi watatu wenye silaha wakija kwa kasi kule walikokuwa. Alishuka haraka kutoka kwenye ule mwamba na kumwambia Khaleed alichokiona.

    Kwa kasi ya ajabu walitimua mbio wakibadili uelekeo ili kuwachanganya wale walinzi. Baada ya kukimbia kwa muda, wakatafuta pango lililokuwa chini ya miamba mikubwa ya mawe, wakaingia ndani na kujificha. Khaleed alikuwa akihema kwa kasi kufuatia uchovu mkubwa aliokuwa nao kutokana na ile ajali ya kule mgodini.



    Giza lilianza kuingia wakiwa bado ndani ya lile pango. Waliona ni bora waendelee kujificha mpaka kutakapokuwa shwari ndio waendelee na safari yao ya kutoroka na mzigo wa Tanzanite. Walipanga kwenda mpaka Arusha ambako ndiko kulikokuwa na soko la uhakika.



    Walipohakikisha kumetulia kabisa, walitoka na kuendelea na safari yao wakikatiza maporini kuitafuta barabara kuu ya kuelekea Arusha. Baada ya kitambo kirefu wakawa wametokea barabarani. Kila mmoja alikuwa na matumaini ya kufika mjini salama na wakawa wanawaza watakavyogawana mamilioni ya pesa baada ya kuuza madini yale.



    Khaleed alishaanza kupanga mipango ya namna atakavyorudi kwao kuanza kulipa kisasi. Kilometa chache mbele waliona mwanga wa taa za gari likija kutokea mbele yao. Kwa haraka walikimbilia kwenye vichaka vilivyokuwa pembezoni mwa barabara na kujificha kwani hawakutaka kuonekana na mtu yeyote.



    Katika hali ya kushangaza, walishtukia kuona lile gari likipunguza mwendo na kusimama jirani kabisa na pale walipokuwa wamejificha. Wakawaona askari zaidi ya sita wakiwa na silaha wakishuka na kuanza kuelekea upande ule waliokuwa wamejificha. Walipowatazama vizuri waliwatambua kuwa ni wale walinzi watatu ambao walikuwa wakiwafuatilia tangu kule mgodini wakiwa na askari polisi.



    Walijikuta wakitetemeka kwa hofu na kwa haraka wakaanza kukimbia upya kuzama porini. Japokuwa ilikuwa ni usiku na giza likiwa limwtanda kila mahali, walitimua mbhio kwa kadri ya uwezo wao wote wakikwepa kuonekana.

    Wale askari walianza kumulika huku na kule vichakani na kwa mbali wakawaona Khaleed na Ololosokwan wakitimua mbio.



    “Wale kule! Lazima watakuwa na mzigo mkubwa sana, si unaona wanavyojihami. Lazima tuwatie nguvuni” Aliongea mlinzi mmoja akiwaonyesha wenzake. Wakaanza kuwafukuza huku wakiwamulika na tochi kubwa.

    Khaleed na masai walizidi kutimua mbio kwa uwezo wao wote lakini wakajikuta wakimulikwa na tochi kubwa.



    “Simameni wenyewe kwa usalama wenu kabla hatujawafyatulia risasi”

    Askari mmoja alitoa amri akiwataka Khaleed na masai wasimame lakini hawakutii, wakawa wanazidi kuchanja mbuga. Mbele kidogo wakajikuta wamefika juu ya mwamba mkubwa wa mawe ambao mbele yake kulikuwa na korongo kubwa lenye maji kwa upande wa chini. Walijikuta wakisita kusonga mbele kwani hawakuwa na uwezo wa kuruka korongo lile hasa ukizingatia kuwa ilikuwa ni usiku sana.



    “Tujisalimishe tu chalii ‘angu, imekula kwetu leo! Hatuna tena ujanja”

    Aliongea Masai akimwambia Khaleed kuwa ni bora wasalimu tu amri. Wazo hilo halikumuingia Khaleed akilini kwani kama angekubali kutiwa mikononi mwa askari wale, tena akiwa ugenini hiyo ingemaanisha kuwa hataweza kamwe kutimiza kazi nzito ya kulipa kisasi.



    Alipokumbuka mikasa aliyokwisha kuipitia maishani mwake, aliona ni bora kufa kuliko kukubali kukamatwa kikondoo. Wakiwa bado wanajadiliana nini cha kufanya, wale walinzi na askari polisi walikuwa wameshafika na wakawa wanawamulika kwa tochi zao kubwa. Mmoja alifyatua risasi hewani kisha akatoa amri kali ya kuwataka wainue mikono juu kusalimu amri.



    Khaleed aligeuka na kulitazama tena lile korongo, urefu wake ulitisha. Rohoya ujasiri wa ajabu ikamuingia na akajikuta akiamini kuwa anaweza kiokoa nafsi yake kwa kuruka lile korongo. Aligeuka mzima mzima akawa anajianza kuruka. Yule rafiki yake mmasai alimkataza kwani alijua hatari ambayo angekumbana nayo kwa kuruka korongo refu namna ile. Khaleed hakutaka kumsikiliza tena... akahesabu moja... mbili... tatu! Akajirusha kama mwanasarakasi na kuanza kuporomoka kuelekea chini. Ololosokwan alipiga kelele kubwa kumzuia lakini alikuwa amechelewa.



    Hakuamini amepata wapiujasiri wa namna ile kwani licha ya yeye Ololosokwan kuwa mzawa wa maeneo Yale hakuwahi kumuona au kusikia mtu akiruka kwenye korongo refu namna ile. Alibaki amejishika kichwani akiwa haamini alichokiona. Sekunde chache baadae wale askari na walinzi walikuwa wameshamzunguka Ololosokwan. Nao hawakuamini kuwa ni kweli mhalifu wao amejitosa na kuruka kwenye korongo lile.



    “Huyo aliyeruka hakuna hata haja ya kumfuatilia, hili ndio jeneza na kaburi lake kwani hawezi kusalimika” Wale askari walikuwa wakielezana wakati wakimfunga pingu Ololosokwan. Walimulika chini ya lile korongo lakini hawakuona kitu. Wakambeba Ololosokwan juu juu na kuanza kurudi naye kule barabarani walikoliacha gari lao.



    Walimfunga Masai nyuma ya gari wakaanza kurudi mgodini huku wakimtolea maneno ya vitisho kuwa hatimaye mwisho wake ulikuwa umefika baada ya kuwasumbua kwa muda mrefu na asingeweza kukwepa adhabu kali ambayo angepewa na wamiliki wa mgodi baada ya kufanya hujuma kubwa.



    *****

    Baada ya kujirusha kwenye korongo lile, alikuwa akimuomba Mungu wake kimoyomoyo amnusuru kwani hakuna baya lolote alilokuwa amelifanya. Alizidi kumuomba Mungu wake afanye muujiza wowote ili asalimike. Aliamini hawezi kudhurika kwa kuwa Mungu alikuwa pamoja naye.



    Alipokuwa akiendelea kuruka, alijikuta akinasa juu ya tawi la mti kabla hajafika chini. Kwa haraka na kwa kutumia nguvu zake zote, alijishikilia kwenye lile tawi na akawa anabembea. Alipoinua macho na kutazama juu na chini, aligundua kuwa yuko katikati ya korongo, chini mbali na juu mbali.



    Aliendelea kuning’inia kwenye lile tawi la mti akiwa hajui angewezaje kutoka pale. Alijishikilia kwa mkono mmoja, na mkono mwingine akaupeleka kwenye ikulu yake alikoficha lile jiwe la Tanzanite. Alijikuta akitabasamu mwenyewe baada ya kuona kuwa liko salama. Kwa kuwa ilikuwa tayari ni usiku sana, aliona bora aendelee kujishikilia palepale mpaka kutakapopambazuka ndio atafute namna ya kujiokoa.



    Alijishikilia kwa nguvu zake zote na akawa anaomba kupambazuke haraka. Moyoni aliendelea kumuomba Mungu wake atende miujiza ili hatimaye afanikiwe kurudi salama nyumbani kwao kwa ajili ya kazi moja tu, kulipa kisasi cha damu ya ndugu zake iliyomwagika bila ya hatia.



    Masaa yalizidi kuyoyoma na taratibu kukaanza kupambazuka. Khaleed alikuwa bado amenin’gia kwenye tawi la mti katikati ya korongo refu. Alianza kuhisi mikono yake ikikosa nguvu na kuanza kutetemeka. Alizidi kujikaza kiume kwani kama angejiachia na kuporomoka mpaka chini, hakika huo ndio ungekuwa mwisho wake.



    Kulizidi kupambazuka na kijua cha alfajiri kikaanza kuchomoza kuashiria mwanzo wa siku mpya. Sasa Khaleed aliweza kuona vizuri mahali aliokuwa. Ilikuwa ni katikati kabisa ya korongo. Alijishangaa ujasiri wa kuruka korongo refu namna ile aliupata wapi. Alipotazama kule chini tena, alijikuta mwili wote ukimsisimka kwani kama isingetokea muujiza wa kunasa juu ya lile tawi basi ule ndio ungekuwa mwisho wake.



    Alianza kutafuta mbinu za kujikwamua kutoka pale alipokuwa amening’inia. Alianza kujivuta kwenye matawi ya ule mti akawa anapanda kuelekea juu. Alihangaika kwa muda mrefu sana lakini Mungu wake alimpigania kwani mwisho wa siku alifanikiwa kufika juu kabisa ya lile korongo. Alijitupa juu ya udongo akiwa haamini kama ni kweli amesalimika. Aligeuka na kutazama tena kule alikotaka kudondokea. Alijikuta akishusha pumzi ndefu na kumshukuru Mungu wake kwa kumnusuru na kifo kama kile.



    Aliendelea kulala pale chini kwani mikono yake ilikuwa imekufa ganzi kutokana na kuninginia juu ya mti kwa siku nzima. Akiwa amelala pale chini, aliskia vishindo vya mtu akija kwa kasi. Hakutaka hata kugeuka na kumtazama. Yule mtu akamsogelea jirani na kwa sauti ya ajabu akamuuliza…

    “Wewe ni nani na unafanya nini hapa!”



    Khaleed alishtushwa na ile sauti, akageuka na kumtazama. Alijikuta akipiga kelele

    “Mungu wangu!”



    Khaleed akiwa amelala pale chini yule mtu alimuuliza tena, safari hii kwa sauti ya ukali.

    “Nakuuliza wewe ni nani na unafanya nini hapa?” Kwa tabu Khaleed alijigeuza na kumtazama yule mtu aliyekuwa akimsemesha. Alikuwa ni mwanaume mwenye mwili mkubwa huku usoni akiwa na ndevu nyingi mithili ya gaidi la kiarabu.



    Khaleed alijikuta akitetemeka mno kutokana na hofu. Hakuwahi kumuona mtu kama yule maishani mwake. Akashindwa kuelewa nini cha kufanya. Lile jitu lilimuamuru kusimama juu na kwa haraka Khaleed alitii amri ile. Akainuka huku mikono yake akiwa ameiinua juu.



    Yule mtu hakuonyesha masihara hata kidogo, akamsogelea jirani kabisa na pale alipokuwa amesimama na kuanza kumhoji maswali. Ilibidi Khaleed aanze kujitetea na kumueleza yule mtu kuwa alikuwa amepatwa na matatizo makubwa. Hakusita kuongea uongo ilimradi tu aachiwe huru.



    Baada ya kuongea uongo mwingi, yule mtu wa ajabu alimuelewa na akaahidi kumsaidia usafiri wa kufika mpaka Arusha mjini. Alimchukua Khaleed na kwenda naye yalipo makazi yake, chini kabisa ya bonde ambalo Khaleed alinusurika kupoteza maisha usiku uliopita.



    Ilikuwa ni ndani ya kijumba ambacho kilikuwa kama pango na usingeweza kugundua kwa haraka kuwa kuna mtu anaishi ndani yake. Baada ya kufika, yule mtu alianza kumueleza Khaleed kuwa yeye ni jambazi na hufanya kazi ya kuteka magari yanayosafirisha madini kutoka machimboni Mererani.



    Khaleed alishindwa kuelewa yule mtu amemuamini vipi mpaka amfichulie siri nzito kama zile. Alizidi kumueleza jinsi ambavyo hufanya kazi yake na akawa anamuonyesha baadhi ya vifaa ambavyo huvitumia kwa ajili ya kazi yake.



    Khaleed hakuamini macho yake wakati akionyeshwa bunduki nyingi za kisasa zilizokuwa zimepangwa ndani ya sanduku kubwa la chuma. Alionyeshwa pia mabomu ya kurusha kwa mkono na silaha nyingine nyingi ambazo zilimfanya Khaleed awe anatetemeka kwa hofu.

    Baada ya kumueleza kwa kirefu, alianza kumshawishi Khaleed aungane naye kwenye kazi ile na akamhakikishia kuwa hakuna hatari yoyote kwani silaha ambazo wangekuwa wanazitumia zilikuwa ni za kisasa na hata Polisi walikuwa wakiziogopa.



    Khaleed alibaki kuduwaa akiwa hajui akubali au akatae kuungana na yule mtu kwenye kazi hatari ya ujambazi. Kwa kuwa alikuwa na shida, ilibidi ajifanye kukubali ili asije akadhuriwa na yule mtu. Alimkubalia kila kitu na akamdanganya kuwa alikuwa tayari kuungana naye kwani hata yeye alikuwa akitafuta pesa. Yule mtu alifurahia mno kupata kijana wa kusaidiana naye kazi.



    Khaleed mawazoni mwake alikuwa akiwaza namna ambavyo angemtoroka yule mtu. Akiwa kwao alizoea kusikia nchi ya Tanzania ikisifiwa kuwa na amani na utulivu wa hali ya juu. Alishangaa kwanini vitendo hatari kama vile vya ujambazi vilikuwa vikifanyika kwenye nchi inayosifika dunia nzima kwa amani na utulivu.



    Khaleed aliendelea kukaa na yule mtu kwa muda mrefu akimdadisi mambo mengi. Ndani ya masaa machache waliyokaa pamoja walizoeana kama watu waliofahamiana miaka mingi nyuma. Jioni ilipoingia, walitoka kule mafichoni na wakaenda mpaka barabarani wakitumia njia za mkato.

    Katika muda wote huo, Khaleed alikuwa makini sana kuhakikisha lille jiwe la Tanzanite liko salama ndani ya bukta yake. Baada ya kufika barabarani, walisimamisha gari lillilowapeleka mpaka Arusha mjini. Waliingia majira ya saa tano za usiku na wakafikia kwenye hoteli moja iliyokuwa uchochoroni. Yule mtu alimwambia Khaleed kuwa watakaa hapo mpaka saa nane za usiku ambapo wangetoka na kwenda kufanya tukio moja la ujambazi huko Kijenge Juu.



    Khaleed hakuwa tayari kuungana na yule mtu kufanya ujambazi, akili yake ikaanza kucheza kwa haraka akitafuta njia ya kumtoroka. Alimkabidhi kabisa Bastola na akawa anamuelekeza namna ya kuitumia. Hakutaka kuonyesha dalili zozote ambazo zingemfanya amshitukie kuwa anataka kumtoroka.



    Ilipotimu saa saba za usiku, likiwa limebakia saa moja kabla hawajaenda Kijenge kufanya Uhalifu wa kutumia silaha, Khaleed alipata upenyo na akafanikiwa kutoroka na bastola aliyopewa. Alikimbia mpaka alipohakikisha amefika mbali kabisa, akatafuta sehemu ya kujificha na kulala mpaka asubuhi.



    Kulipopambazuka tu, aliamka haraka na akahakikisha kuwa jiwe lake liko mahali pake. Alianza kutafuta sehemu ambako kuna wanunuzi wa madini ya Tanzanite na baada ya muda akawa ameshaoneshwa. Alisubiri mpaka maduka yote yalipofunguliwa, akaingia kwenye mojawapo ya maduka yanayonunua madini.



    Hakuamini macho yake pale alipokuwa akikabidhiwa kitita chake cha pesa. Zilikuwa ni takribani Shilingi za Kitanzania milioni kumi na moja, ambazo alizibadilisha palepale na kupewa dola za kimarekani. Alishangaa sana kwani hakudhania kuwa jiwe dogo kama lile lingeweza kufikia kiwango kikubwa cha pesa kama kile. Bila hata kuaga alitoka na kuanza kutafuta njia ya kuondoka haraka jijini Arusha.



    Kwa kuwa alikuwa na pesa za kutosha, aliona ni bora asafiri mpaka kisiwani Zanzibar ambako alipanga kwenda kuweka ngome yake wakati anafikiria na kupanga mipango ya kurudi nchini kwao Blazinia, kwa ajili ya kazi moja tu! Kulipa kisasi kwa wote waliohusika kuiangamiza família yao bila ya hatia.



    Baada ya siku mbili, tayari alikuwa ametua kisiwani Zanzibar, akatafuta hoteli moja yenye hadhi ya juu iliyokuwa ufukweni mwa bahari ya Hindi. Akaweka kambi na kuanza kupanga oparesheni maalum, oparesheni aliyoipa jina la Blood Revenge( Kisasi cha damu).



    MWISHO

0 comments:

Post a Comment

Blog