Simulizi : Usilie Nadia
Sehemu Ya Tano (5)
Kila mmoja alikuwa na njaa na hakika tulikisosoa chakula kwa wingi, hata Nadia ambaye hawezi kula chakula kingi alijitahidi sana siku hiyo katika kiwango cha kuridhisha. Kama kawaida hakuna aliyesema na mwenzake hadi tuliporidhika, kijana muhudumu akaleta bili nikalipia.
Hapo sasa hapakuwa mahali sahihi pa kuendelea kukaa, nilimwonyesha ishara Nadia nasi tukasimama na kuondoka tukiwa na chupa za maji yetu. Hatukuelekea chumbani, bali siku hii nilimwongoza Nadia hadi katika fukwe za Ziwa Viktoria, jirani na lile jiwe maarufu ama tuseme mwamba maarufu wa Bismark….
Bismark rock!!
Hapakuwa na jua kali hivyo tukaamua kutembea kwa miguu tukapita kona kadha wa kadha hadi tukafika mahali tulipohitaji. Haikuwa mara ya kwanza kwa Nadia kufika eneo lile, lakini wakati wa mwisho kufika hapo labda alikuwa alikuwa katika kipindi kigumu, sasa mimi nilimpeleka pale kwa dhumuni la kupunga upepo na kuendelea kubadilishana mawazo mawili matatu kama yangetokea.
Hapakuwa na watu wengi sana eneo lile hivyo tulipata nafasi ya kujivinjari tuwezavyo kona kadha wa kadha.
“Mwenzako nayaogopa maji balaa.” Nilimweleza Nadia baada ya kuwaona vijana kadhaa wakiogelea kwa raha kabisa katika maji yale. Nadia alitabasamu kisha akanieleza kuwa yeye ni rafiki wa maji. Nilikumbuka katika mazungumzo alinieleza juu ya namna alivyoweza nkuogelea na kuwakimbia maadui wale waliokuwa wamemteka na kisha kumtumia katika kusafirisha madawa ya kulevya.
“Yaani hapa ningekuwa na nguo za ziada ungeshtukia tu nipo ndani ya maji.” Aliniambia huku akionekana dhahiri kuwa anayatamani yale maji.
“Wewe jifanye kuyazoea maji, maji ni rafiki na ni adui pia…”
“Unajuaje wakati maji ni rafiki na unajuaje kuwa wakati huu ni adui yakiwa yametulia katika namna ile.” Aliniuliza swali ambalo sikulichukulia uzito hata kidogo.
Lakini nilipotaka kulijibu ndipo nikagundua kuwa swali lile ni gumu.
“Kwa kuyatazama huwezi kujua, lakini ukipatwa na kiu na ukayanywa utautambua uzuri wake na ukukizama humo yakakuua utatuachia nafasi tulio hai kuutambua uadui wa maji.” Nilijaribu kumjibu.
“Kwa hiyo huwezi kutambua kwa kuona sivyo.”
“Naam!!” nilimwambia.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hapa akafanya tabasamu kidogo.
“Maji ni kama mwanadamu tu, huwezi kuyatambua madhaifu yake mpaka akufanyie jambo fulani.” Akasita kisha akaendelea huku akiyatazama maji. “Wasichana sisi huwa ni wapumbavu sana, yaani wapumbavu wa mwisho kabisa. Si wote lakini hao wapumbavu wanasababisha wote tuonekane sawa. Lakini ‘ishu’ ipo katika kumjua nani mpumbavu na nani si mpumbavu!! Upumbavu huu kwa silimia kubwa huja tukiwa katika mapenzi yaani kama mazezeta vile, basi wanaume wanatufanya watakavyo. Mwandishi unajua Jesca naweza kumuita mjinga ama mpuuzi wa mwisho. Yaani tumehangaika weee tumeshakaa kwenye mstari tunataka kusonga mbele na maisha yetu yeye anafanya mambo ya kijinga na kusababisha turejee tulipotoka.
Mwandishi, tumesafiri vizuri sana yaani wote tukiwa na lengo moja tu kuanza safari yetu ya kimaisha tukitambua kuwa mtoto anatutegemea sisi hivyo kwa ile pesa iliyokuwepo tulitakiwa kufika na kutulia tujue nini tunafanya. Hakika wote tukaunganisha mikono yetu na kuwa kitu kimojha na wazo moja.
Saa saba za usiku tukaingia Mwanza. Nikasimamia jukumu la kutafuta chumba yeye Jesca na mtoto wakabaki stendi wakiningoja. Baada ya dakika kumi na tano nilikuwa nimelipia chumba tayari.
Safari yetu ya kufika Mwanza ikawa imetimia haswa!! Na palipokucha maisha yetu jijini hapo yakaanza rasmi.
Nilikuwa namuamini samba Jesca na nilimwona ni mwanamke wa shoka lakini kilichokuwa kinanikosesha amani ni hali yake ya kulialia mara kwa mara na kukosa amani.
Moyo wa mtu ni kiza kinene huwezi kujua nini kinajiri humo ndani. Nami sikujua mwenzangu alikuwa anawaza nini, mimi nilijisikia ama kuishi katika nyumba ya kupanga jijini Mwanza hata kama haikuwa na umeme lakini tulikuwa na uhuru lakini mwenzangu alionekana kama maisha yale haridhiki nayo. Nilijiuliza kama alipenda kulawitiwa ili aendelee kuishi maisha bora nyumbani kwa Bryan ama ni kipi kilikuwa kinamnyima amani. Nilitambua kuwa labda kukatisha chuo ghafla nd’o jambo lililoiathiri akili yake nikajipa moyo kuwa labda atakuja kubadilika.,
Kweli ikawa kama nilivyotaraji!! Lakini ilikuwa ghafla sana
Jesca akaanza kupata furaha tena kama kawaida!! Lakini hii furaha ilikuja ghafla sana mwandishi hadi ikanitia mashaka, inakuwaje furaha kama hiyo upesi kiasi hicho? Sikutaka kumuuliza maana swali langu lingemaanisha kuwa mimi nataka awe mpweke kila siku. Wakati huo tulikuwa hatujaanzisha rasmi kitu cha kutuingizia pesa lakini nilikuwa katika michakato ya kufanya biashara ya ushirikiano na mwanamama jirani aliyekuwa anatengeneza supu ya makongoro.
Furaha ya Jesca ikanifanya nikumbuke kila mtu ambaye nimewahi kumuamini na mwisho kunifanya nijute kumuamini. Nikaamua kuchukua tahadhari, na nilijua kama hiyo furaha ina sababu basi sababu ile haitakuwa mbali sana, yaani ikiwa moyoni basi kuiona ni kazi ngumu sana lakini moyo mwingine usiokuwa na siri ni simu ya mkononi. Siku hiyo nikamtegea Jesca alivyoenda kuoga nikaikwapua simu yake bahati nzuri hakuwa ameifunga kwa namba za siri.
Nikakimbilia katika jumbe alizopokea na kutuma, nikakutana na jina baba watoto!!
Ina maana amepata kimwanaume hapa mtaani ama?? Nilijiuliza.
Lakini nikaamua kuzisoma meseji zile ili niweze kupata jibu.
Walikuwa wanajadiliana juu ya safari ya huyo baba watoto kuja jijini Mwanza. Nikaichukua nama upesi nikahifadhi katika simu yangu ambayo nilikuwa nimeinunua siku chache zilizopita.
Meseji nyingine zilitaja jina langu!! Mariam! Nikashangaa ni nani huyo anayenijua mimi.
Meseji ya muhimu kwangu ikawa kwamba yule mtu hakutaka mimi niambiwe kama anakuja eti kisa anataka kunishtua tu!!
“Mimi nilishasamehe mpenzi wangu na ninawapenda sana, kama Mary lazima nimpe zawadi baada ya kumwomba msamaha.” Aliandika huyo baba watoto.
Nikairejesha simu baada ya kumsikia Jesca anafunga bafu.
Mwandishi, hakuna kitu kibaya katika haya maisha kama kusalitiwa na yule unayempenda, tena ni heri afanye usaliti na uhadithiwe tu lakini sio kushuhudia. Yaani nilihisi kuwa yuyle anayewasiliana na Jesca atakuwa ni Bryan tu, lakini niliamua kuthibitisha nikatafuta simu nyingine nikampigia ili tu kuhakikisha.
Hakika alikuwa ni Bryan yule mwanaharamu aliyetaka kumlawiti Jesca. Yaani leo hii huyu Jesca ambaye niliumia moyo na kuamua kumwepusha na balaa lile kisha tukatoroka na kujiwekea ahadi kuwa hatutakaa tuwasiliane na Br4yan ama familia yake iwapo atakuwa amekufa!
Sasa Jesca anawasiliana na mwanaharamu……
Si nilisema wasichana sisi ni wapumbavu, wapumbavu wa kutupa mwandishi, hivi unamwamini vipi mtu aliyetaka kukulawiti bila huruma, unaanza vipi kumwamini mtu ambaye tulitaka kuupoteza uhai wake?? Kibaya zaidi sasa tulikubaliana kwa pamoja kuwa hatutawasiliana na Bryan lakini katika kuwasiliana naye akaamua kufanya mwenyewe, kwa hiyo mimi sikuwa na maana tena baada ya hayo yote tuliyopanga.
Nililia sana mwandishi. Nililia sana kwa sababu nilikuwa nimesalitiwa, tena nimesalitiwa na mtu ambaye ninamuamini.
Niliamua kujifanya naumwa ilimradi tu Jesca asijue ni kiasi gani amenikwaza na kunitia jeraha!!
Wanawake!! Dhaifu sana sisi, yaani dhaifu hadi kero.
Yaani mapenzi huwa yanakuwa mzigo sana kwetu, nd’o maana wasichana hujikuta wakiwaamini wapenzi wao kuliko wazazi wao wa kuwazaa. Eti kisa tu mpenzi amemuahidi kumuoa. Nayasema haya kwa sababu hata mimi niliwahi kuwa mpumbavu!!
Sikutaka Jesca naye awe mpumbavu, lakini ni kama alikuwa mpumbavu tayari. Ningeanza vipi kumwambia kuwa nilichukua simu yake na kusoma meseji zake. Angenionaje??
“Mariam…kesho nitatoka kidogo mwenzako yaani kuna rafiki yangu nilisoma naye jana kama mchezo nimejaribu anapatikana kwenye simu anakaa huko Airport. Ngoja nikaonane naye dada yangu, maana haya maisha hatutaweza na pesa hiyoo inaisha” Jesca aliniambia wakati tunapata chakula. Nilijisikia hasira sana kwa sababu alikuwa ananidanganya. Kwa nini Jesca ananidanganya wakati mimi nilikuwa muaminifu kwake nikamwokoa asikamatwe na majibu ya mtihani ilhali simjui?? Mbona niliendelea kuwa muaminifu kwake na nikaiweka roho yangu rehani ilimradi nimwokoe asilawitiwe?
Yaani ameshindwa kulipa uaminifu kidogo tu!! Jesca Jesca!!
Sikuweza kuendelea kula tena, nikasingizia kichwa kinaniuma. Nikajitupa katika godoro nikalala.
Nilisinzia nikiwaza jambo moja tu, kama Jesca ameamua kujipeleka katika domo la mamba basi mimi sitakubali hata kidogo Jonas naye atumbukie humo. Alikuwa mtoto mdogo sana kuingia katika kashkash.
Kesho yake majira ya saa nne asubuhi nikamwona Jesca akimwandaa Jonas, nikamsubiri niisikie kauli yake, majira ya saa tano akataka kutoka na Jonas. Nikamzuia, hakuna kwenda na mtoto huko kwa rafiki.
“Jesca jicho linanichezacheza hautaenda na mtoto kwa kweli kama jicho linanicheza kwa mabaya basi yakusibu wewe mtu mzima utajua kujiokoa lakini Jonas tutakuwa tunamwonea” niliunda uongo.
Alidhani natania lakini kwa mara ya kwanza nikamkunjia sura. Akaogopa akaniaga akiahidi kuwa akirejea nitatabasamu na jicho litaacha kucheza.
“Nakupenda Jesca.” Hilo lilikuwa neno la mwisho kumwambia, akaondoka na sikuwahi kumwambia neno jingine tena.
Alipoondoka na mimi nikaondoka nikiwa na Jonas na akiba ya pesa yote iliyokuwa imebaki. Nikaufunga mlango vyema, nikaweka funguo mahali anapopafahamu Jesca kisha nikaondoka. Nikampeleka Jonas kwa mama ambaye nilikubaliana naye kuungana katika biashara ya makongoro. Uzuri wa Jonas hakuwa akichagua mtu, hakuwa mtoto wa kulialia hovyo labda awe anaumwa.
Nikamwomba mama yule amuhifadhi pale hadi nitakaporejea, akakubali nikamwachia shilingi kadhaa kwa ajili ya dharula kama tu itajitokeza.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Sasa nikarejea kuwa shuhuda wa kitu ambacho kitaenda kutokea, imani yangu ilikuwa ndogo sana kumwamini Bryan niliyempasua na chupa kichwani, lakini ningemsaidia nini Jesca wakati wahenga walisema mkataa pema pabaya panamuita!!
Nilijiweka mahali pazuri nikawa natazama ugeni huo kama utakuja kwa amani.
Muda ulizidi kwenda bila matokeo yoyote.
Saa tisa za alasiri ndipo nikapokea simu kutoka katika namba ya Jesca.
“Mambo dada Mariam, nitachelewa kurudi, si Jonas yupo, niwaletee nini nikija.?” Alijiumauma Jesca, nikajikuta natabasamu kwani nilijua kuwa tayari hakuwa huru tena Jesca. Kitu nilichokuwa nawaza.
Majira ya saa kumi na mbili akanipigia simu akaniuliza kama nipo nyumbani. Kitu ambacho hakikuwa cha kawaida kabisa kwa Jesca, nami nikaendelea kutulia tu. Majira ya saa mbili usiku gari mbili zikafunga breki katika nyumba tuliyokuwa tumepanga. Wakaruka wanaume kwa fujo!! Jicho langu likamuona Jesca, alikuwa amelowa damu, na kisha nikamuona Bryan alikuwa ameiva kwa hasira kali. Nikajilazimisha kutabasamu maana sikuweza na nafsi iliniambia kuwa nitakuwa mjinga kumsaidia mpumbavu!!
Nikatoweka kimyakimya huku nikiwaachja wajinga hao wakitangaza kuwa ‘Mariam popote pale ulipo jitokeze’
Nikaondoka huku nikiumia sana hakika kwa hali aliyokuwanayo Jesca, usiri wake na kuamini mapenzi ya kijinga kulimponza.
Nilifika nyumbani kwa yule mama majira ya saa nne usiku, nikamchukua Jonas na kuondoka naye.
Hapo nikakumbuka kuwa nilikuwa nimelaaniwa na huenda ile laana ya mama ilisema kuwa nitaishi kama kivuli sitatulia wala kupata amani, hakuna atakayenipenda hata kidogo licha ya kujipendekeza kwake.
Naam!! Nilikuwa mkimbizi tena.
Nikalala nyumba ya kulala wageni pamoja na Jonas!!
“Jonas, sijui kama utamuona mama yako tena. Nasema sijui kwa sababu anajua mwenyewe ni wapi alipo. Hautakaa utulie tena maana utaandamana na mwenye laana Nadia, hautatabasamu tena kwasababu upo na nyumba ya kilio Nadia, hautakuwa na uhuru kwa sababu upo na mfungwa Nadia. Lakini kikubwa amini kuwa huyu mfungwa atakufa naye atakuacha, lakini hatakufa kizembe kama mmama yako, hatashikika kipuuzi kwa mapenzi na kubwa zaidi akifa atakuacha ukiwa katika mikono ya yeyote yule ambaye hajalaaniwa. Utamuita mama naye atakuita wewe mtoto wake. Sitakuacha Jonas hadi roho yangu itakapouacha mwili!!!” nilizungumza na kitoto kile kilichokuwa kinanitazama tu bila kusema chochote!!
Asubuhi nilikuwa mkiimbizi kuelekea mahali pengine!! Mwanza haikunifaa tena, mropokaji aitwaye Jesca angeweza kunichoma.
Nikazima simu yangu na kusahau kabisa kama niliwahi kuwa na simu!!!”…akasita Nadia akatazama kushoto na kulia.
“Wee G hapa huwa pabaya usiku wanakaba sana mwenzangu na hii afya yangu mgogoro wasije wakaniua bure….” Kauli hii ikanishtua, kweli palikuwa na giza na tulikuwa tumebaki watu wachache sana, tukasimama na kujikongoja tukapata teksi kwa ajili ya kuturudisha hotelini.
Kila mmoja alikuwa kimya!!
Nilikuwa na swali moja kubwa. Nadia alisema kuwa hatamwacha Jonas hadi yeye afe kwanza, sasa mbona Jonas hayupo na yeye yupo hai??
Nini kilitokea na kusababisha haya!!!
Na nini hatima ya Jesca…….
Tulifika hotelini, nikatarajia Nadia atakuwa amechoka na atahitaji kulala moja kwa moja. Lakini haikuwa kama nilivyotarajia, badala yake akaungana nami katika chumba changu kwa mara ya kwanza tangu tuwe katika hoteli ile ya G G jijini Mwanza.
“Nikajua unaenda kulala.” Nikamwambia, hapo akanitazama kisha akanieleza kuwa hakuwa na usingizi wa kulala mapema kiasi kile.
“Usingizi nilikuwa nao enzi zile lakini sasa hapana, yaani usingizi kitu cha ajabu mfano unakuwa unahitaji kulala lakini hauupati, na ukiwa na mambo ya msingi ya kufanya nd’o unakuandama. Leo nilitaka kulala mapema lakini ndo basi tena.”
“Au kibaridi hiki kinakusumbua?” nilimuuliza huku akiwa amekaa kitandani nami nikiwa katika kiti.
“Hii nayo utaiita baridi, achana na Mbeya na Iringa. Kuna baridi kali sana kule, hili linaweza kuitwa joto na mtu anayetoka huko. Mara yangu ya kwanza kwenda niliteseka sana, na hata nilipokuja kuzoea nilikuwa nimesota haswa. Halafu bora basi ningeteseka peke yangu, mbaya zaidi nilikuwa na mtoto, mtoto asiyejua kusema badala yake analia tu. Unashindwa kuelewa kuwa huyu anahisi baridi ama ana njaa ama anaumwa, yaani nilikuwa najikuta nalia wakati mwingine, mbaya zaidi ya yote Nadia mimi sikuwahi hata kulea mtoto asiyekuwa wangu. Na kubwa zaidi sijawahi kuwa mama. Labda nililaaniwa hivyo ili laana ya mama iishie kwangu tu isimwandame na mtoto ambaye nitamzaa. Sasa nilikuwa na mtoto mdogo.
Mama Aswile hakujali kama nilikuwa nina mtoto, alinilaza katika chumba kisichokuwa na chandarua na mbaya zaidi hata chakula kilikuwa kidogo sana na kisichostahili kuliwa na mtoto mdogo. Sikuweza kujilaumu kwa kuwa katika mkoa wa Mbeya bali nilijilaani tu kwa nini nilizaliwa.
Lakini zaidi nilimlaumu Jesca ambaye sikujua kama yu hai ama ni marehemu tayari, bila Jesca kunisaliti wala tusingekuwa hapo lakini Jesca akaendekeza mapenzi na hatimaye kilio kinakuwa cha mtoto, unadhani ghafla kiasi kile ningewezaje kupata akili ya ghafla ya kujua nini natakiwa kufanya?, mjini Musoma nilijua hapanifai ikiwa sijajipanga, Mwanza ndo hivyo Bryan atakuwa ananisaka, Dar es salaam napo hapakunifaa maana ndo yalikuwa makazi ya Bryan, hivyo nikajikuta katika sintofahamu. Nikaendelea kuishi na Bryan pale nyumba ya kulala wageni kwa siku zaidi ya tatu na hapo nikawa nimeamua kwenda katika wilaya ya Magu nje kidogo ya jiji la Mwanza. Na hapa nikaendelea kuitwa Maria mama mama Jonas.
Huku nilifikia nyumba ya kulala wageni na kisha nikawa nazurura na Bryan nikitafuta walau kazi za ndani ilimradi nipate sehemu ya kulala bure huku nikitafakari nini cha kufanya na pesa yangu ambayo ilikuwa inayoyoma.
Labda ningekuwa peke yangu ningeweza kwenda Musoma ama popote na kujificha nikifanya lolote niweze kula, lakini sasa nilikuwa na mtoto. Mtoto ambaye nilimuapia kuwa sitamwacha pekee hadi nife. Kiapo changu kikawa kinaniandama na kunifanya nijilazimishe kuizoea hali.
Nikabahatika kupata kazi katika banda la mama ntilie maarufu wilayani Magu, Mama Ntuzu. Nilimweleza shida yangu akanielewa na hapo nikaanza rasmi kushughulika katika banda lake, uzuri wa Jonas kama nilivyokwambia awali hana tabia ya kuchagua nani ambebe na nani asimbebe, yaani halii hovyo. Akilia ujue kuna jambo linamkabili. Hivyo nilikuwa namkabidhi kwa mtu ananisaidia kumbeba iwapo anataka kulala, na wakati mwingine anajumuika na watoto wenzake katikia kucheza, hapo akiwa na miaka takribani miwili.
Tatizo lilikuwa moja tu, kwa siku nilikuwa nalipwa shilingi elfu tatu na bado nilikuwa naishi nyumba ya kulala wageni, hapo nilikuwa nalipia chumba shilingi elfu tatu pia. Hivyo pesa yangu yote ilikuwa inaishia katika nyumba za kulala wageni.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Muda si mrefu nikapata rafiki akanieleza kuwa anaishi peke yake, akanizoea nikamzoea na mwisho akanikaribisha kwake. Kilikuwa chumba kimoja, nikajitoa mhanga nikamnunulia Jona kigodoro chake halafu mimi nikawa nalala na Hamida katika godoro moja. Hamida hakuwa mtu wa makuu, aliniheshimu nami nikamuheshimu na ni huyu aliyeniunganisha na mzee Aswile ambaye alinichukua hadi jijini Mbeya kwa ajili ya kufanya kazi za ndani. Nilimweleza kuwa nina mtoto lakini hakujali kuhusu hilo alionekana kumwamini sana Hamida ambaye alikuwa amempa sifa kemkem kuhusu mimi.
Nikaagana rasmi na Hamida nikatoweka nikiambatana na mzee Aswile kuelekea Mbeya. Tulisafiri kwa kutumia gari lake binafsi, nilikuwa najiuliza maswali kwanini mzee yule atoke mbali kote huko na mwisho kunichukua mimi kwa ajili ya kumfanyia kazi za ndani lakini sikupata majibu. Nafsi yangu ilikuwa na amani zaidi kuishi mbali na sehemu zote ambazo nilikuwa na mikasa, na Mbeya ilikuwa sehemu nzuri zaidi.
Nilipokelewa kwa furaha na familia nzima, wakazoea kuniita dada, mama mwenye nyumba alikuwa kama mama yangu nilimweshimu na yeye akanionyesha heshima waziwazi.
Mtoto wa Jesca ambaye alihesabiwa na kutambulika kama mtoto wangu alikuwa na furaha kama amezaliwa katika familia hiyo.
Tukuyu ikanizoea na mimi nikaizoea. Nikanawiri na kujiona mwanadamu mwenye baba na mama pamoja na wadogo na dada zangu. Familia ya mzee Aswile ikawa kama nyumbani nilipozaliwa.
Raha zile zikanifanya nisahau tetesi ambazo aliwahi kuniagusia mvulana wa kazi kuwa mzee Aswile na mkewe hawana maelewano mazuri sana baada ya mimi kufika pale, mkewe alikuwa akimtuhumu kuwa yule Jonas anayeaminika kuwa ni mtoto wangu, basi nilizaa na mzee Aswile tuhuma ambazo mzee Aswile alizikataa na kisha kumkanya mkewe asije akanibughuzi. Aliniambia pia kitu ambacho nilikuwa sikijui, kumbe wale watoto wote pale nyumbani si wa mama yule, bali mama wa wale watoto alikufa katika mazingira ya kutatanisha na mama huyu wa sasa hakubahatika kupata mtoto.
Niliyapuuzia na kuyasaha maneno yale hasahasa baada ya kijana yule kunitaka kimapenzi, hivyo nikagundua kuwa kumbe ile ilikuwa janja yake tu ya kunishawishi.
Maisha yakaendelea na yakasahaulika aliyonambia kijana yule, sikuona chuki yoyote kutoka kwa yule mama na familia nzima ilinipenda.
Jonas akamzoea sana mzee Aswile naye mzee akawa anamfanyia mambo ambayo hata watoto wake baadhi hakuwa akiwafanyia. Niliifurahia sana familia ile, lakini sikujua kama itafika siku ya mimi kuanza kulia tena na kuishi kama mkimbizi.
Usiku huu Jonas alikuwa mtu wa kulialia na kukosa raha, nilishangazwa sana na hali hiyo, si mimi hata mtoto mmoja wa mzee Aswile aliyekuwa anapenda sana kunitembelea chumbani kwangbu alishangaa, hatimaye akasinzia. Lakini saa tisa usiku akaamka tena na kuanza kulia huku akijinyonganyonga huku na kule, nikastaajabu, haikuwa kawaida hata kidogo kwa Jonas. Nikamuuliza alichokuwa anataka, sasa aliweza kusema neno moja tu ‘babuuu’ alikuwa akimtaka babu yake, nikajua ni mambo ya watoto haya kulilia hata visivyowezekana, nikambembeleza sana mwisho akalala, lakini hakudumu sana akaamka tena na kuendelea kunisumbua. Sasa nikaamini Jonas atakuwa anaumwa, nikafikiria kuwa pakikucha niangalie utaratibu wa kumpeleka hospitalini.
Kilio cha Jonas cha saa kumi na moja mara kikaambatana na kilio kingine kutoka kwa mtu nisiyemfahamu, mara mwingine na mwingine na hatimaye mimi naye nikaungana nao.
Tuliongana kumlilia mzee Aswile, kwani hakuweza kuamka tena tangu alivyolala usiku.
Mzee Aswile alikuwa amekufa!!
Mwandishi, nililia sana lakini sikumfikia Jonas ambaye ni kama alijua jambo lililotaka kutokea tangu usiku wa manane.
Mzee Aswile akazikwa huku tukisema kuwa sisi ni mavumbi na mavumbini tutarudi.
Na hapo ukaanza ule wakati wa kujuta na kishga kukumbuka kuwa umelaaniwa, wakati wa kuyakumbuka maneno ya ‘;shamba boy’ juu ya yule mama.
Ulianza ugeni, wakaja ndugu wa yule mama. Nikatolewa katika chumba nilichokuwa na lala na kisha kuhamishiwa chumba cha nje. Mara kila mara kugombezwa hata ninapofanya jema, baadaye inavyoonekana watoto walihoji kulikoni.
Naam!! Yule mam akawaambia kuwa baba yao alikufa kwa kulishwa sumu, na chakula hicho nilikipika mimi, nilimlisha sumu ili Jonas aweze kurithi mali. Kwa kuwa wote walikuwa wasichana basi Jonas ambaye ni mtoto haramu ninayemsingizia kuwa wa marehemu angeweza kurithi mali zote.
Maneno hayo aliniambia mtoto mkubwa wa marehemu siku moja baada ya kukasilishwa na uwepo wangu sebuleni, alisema kwa uchungu na kisha akaniita shetani.
Mama mwenye nyumba alikuwa amewajaza sumu watoto wale.
Hapo sasa nikaanza kuchukiwa!!
Nikabaini kuwa nilibweteka na sikuwa na utaratibu wa kujitunzia pesa, nilijiona kama nipo nyumbani kwetu. Pesa ya nini??
Chumba nilichohamishiwa hakikuwa na kitanda na enzi za uhai wa Aswile katika chumba kile bata na kuku wagonjwa walitengwa na wengine kwa kuhifadhiwa ndani ya chumba kile.
Niatakiwa kuishi mule, ni hapo nikagundua kuwa sikuwa na ile thgamani tena iliyokuwepo awali. Maneno ya shamba boi yakaendelea kujirudia kichwani mwangu, nikajua moja kwa moja kuwa mama yule alikuwa amemuua mumewe kutokana na wivu mzito wa kimapenzi. Lakini nani angeniamini iwapo nilikuwa nimerushiwa kesi ile.
Ugumu wa maisha ukaanzia hapo, nikahesabiwa siku niwe nimeondoka pale. Nikaomba nipewe mwezi mmoja.
Hakika ulikuwa mwezi mmoja lakini ni kama mwaka mzima kwa tabu nilizopitia. Nilitukanwa mimi na Jonas, tulilishwa makapi, sikuruhusiwa kuingia sebuleni na mbaya zaidi sikutakiwa hata kupika chakula. Watoto wakadai nitawaua wao pia.
Wakavuka mipaka wakaanza kumuita Jonas mwanaharamu. Hapo sasa wakaitibua hasira yangu na kunirudisha miezi kadhaa nyuma miezi ambayo hasira ilikuwa kando nami na iliweza kufanya kazi muda wowote.
Jonas mwanaharamu!!!
Monica, mtoto mkubwa wa marehemu mzee Aswile alikuwa wa kwanza kutambua upande wa pili wa Nadia. Siku hiyo Jonas akiwa mtoto hajui kama tumekatazwa kuingia sebuleni aliingia na kujibweteka katika kochi akawa anaangalia luninga, mimi nilikuwa nafua nguo zake na zangu.
“Mwanaharamu mkubwa wewe unakanyaga hayo makochi unasaidia kufua??” nilisikia sauti ya Monica akigomba. Nikasita kufua nikatazama huku na huko, Jonas hayupo. Kule ndani nikazidi kusikia Monica akigomba. Masikio yangu mara yakasikia Jonas akitoa kilio kikali.
Mbiombio nikakimbilia ndani, Jonas alikuwa analia kwa uchungu huku akiwa amejishika shavu. Aliponiona akanikimbili na kunikumbatia huku akiwa analia, aliponikumbatia akawa ameachia lile shavu.
Macho yangu yakaona alama za vidole vya mtu mzima.
Monica alikuwa amemnasa kibao Jonas.
Na hapo nikaisikia sauti ya Jonas akilaumu kitoto toto.
“Mama huyu pigaaaa….” Ilikuwa ni sauti ya kitoto lakini iliyotangaza uchungu. Nikanyanyua macho yangu na kumtazama Monica, nikamkuta akiwa ametingwa katika kufanya lolote alilokuwa akifanya katika luninga.
Mbiombio nikamvamia, yeye na luninga wakaenda chini, nikamweka vyema uso wake, na hapo nikamgeuza kitoweo changu. Nilimpiga haswa!!CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Akaja na mdogo wake nikawachanganya wote, nilikuwa na hasira kali kupita nyingine zilizopita.
Nilijua kuwa sihitajiki tena katikia mji ule, nami niliomba mwezi mmoja niweze kuondoka wakanikubalia. Sasa wanamuita Jonas mwanaharamu!!
Gusa pengine usimguse mtoto huyu, nililaaniwa mimi na si Jonas!!
Wakati natoka mlangoni nikakutana na mama Aswile. Sikujali lolote nikaelekea katika chumba changu, nikakusanya nguo zangu huku nikiwa natetemeka, Jonas akiwa mgongoni. Nikasikia chumba kikivamiwa, ni jambo nililolitarajia. Haraka nikageuka nikakutana na mama Aswile. Alikuwa amevimba huku akiwa ameshika mwiko. Taratibu nikamshusha Jonas. Halafu nikahamishia balaa kwa mama mAswile, nilimpiga huku nikimtuhumu kuwa amelaaniwa kwa kuwafanya watoto wake wanichukie bila sababu. Nilihakikisha amenyooka.
Baada ya hapo nikabeba kilicho changu na kuingia katika mitaa ya Tukuyu nikiwa na shilingi elfu tano tu!!
Pesa niliyoipata baada ya mama Aswile kuiangusha akijaribu kukabiliana na mimi!!
Jonas mgongoni, kibegi kidogo mkononi!!
Nikaingia katika mitaa yenye baridi kali. Sina ndugu wala rafiki!!.........
Sikuwa nafahamu ni wapi natakiwa kwenda muda huo, na hapo nikaanza kuona muda ukienda kwa kasi sana. Ilikuwa asubuhi mara ikawa mchana, bado nilikuwa katika kiza kinene bila jibu sahihi.
Mida ya saa nane mchana Jonas akaanza kulia huku akiwa mgongoni.
Njaa!! Nikawaza. Nikamgeuzia kifuani na kuanza kumbembeleza lakini hakubembelezeka, nikatamani angeweza kusema nini kinamtokea nitafute njia ya kumtibia lakini hakuweza kusema na badala yake alikuwa analia tu. Nikalazimika kuingia katika banda la mama lishe, nikaomba huduma ya chakula, nikapatiwa wali na maharage. Jonas akakataa kula badala yake akaendelea kulia kwa fujo na kuwa kero kwa wateja wengine. Hapa nikalazimika kutoka naye nje huku ule wali nikiulipia bila kuula hata kidogo, ningeanza vipi kula wakati Jonas alikuwa analia? Yule mama alinifuata nje na kuniuliza nini kimemsibu mtoto, nikamweleza kuwa nilihisi ni njaa lakini ajabu hataki kula hata hicho chakula. Yule mama akampima joto kwa kutumia mikono yake na kisha akanieleza kuwa mtoto alikuwa amechemka sana nijaribu kumpeleka hospitali ama la nimpatie dawa za kutuliza maumivu.
Hilo la hospitali lilikuwa zito sana kwa sababu nilikuwa na shilingi 5000 tu, sasa ingetosha vipi gharama za hospitali tena kwa mgonjwa asiyefahamika magonjwa yake. Nikaamua kushika la pili, nikanunua dawa za kutuliza maumivu, nikazikoroga katika maji kishas tukasaidiana na yule mama kumywesha Jonas, alisumbua sana lakini alimeza.
Baada ya saa zima Jonas hakuwa akilia tena na alikuwa amejilaza katika mikono yangu. Mama wa kufikia ambaye hajui hata kesho yake na sasa ana mtoto mikononi mwake.
Ngoja ngoja, tafakari tafakari hatimaye usiku ukafika akili ikiwa imeganda tu nikishindwa kufikiri hata kidogo ni kitu gani natakiwa kufanya.
Si kwamba hawakuwepo watu ambao ningeweza kuwakabili na kunipa hifadhi ya siku mbili tatu, hofu yangu ilikuwa usalama wangu katika wilaya hiyo. Hao watu niliokuwa nafahamiana nao walikuwa wakimfahamu mzee Aswile na familia yake, hivyo ilikuwa kazi nyepesi sana kuweza kuzisikia tetesi za shambulio langu dhidi ya familia ile. Na ningejuaje huenda nilikuwa natafutwa??
Ningekuwa mimi kama mimi ningejitoa muhanga lakini Jonas!! Jonas aliniumiza sana kichwa. Laiti kama ningeamua kujisalimisha huko kisha nikakamatwa, bila shaka Jonas angebaki katika familia ya mama Aswile! Familia ambayo inamuita yeye mwanaharamu. Angeishi vipi, kama wakati mtetezi wake nilipokuwa naye waliweza kumuita mwanaharamu na kumzaba vibao, je wakati ambao sipo kabisa nini kingejiri kama sio kumuua kabisa.
Hapana!! Siwezi kurudi nyuma. Nikafikia uamuzi huo. Nikasimama na kuelekea stendi ya mabasi ya pale Tukuyu, nikatafuta kona moja nikajiegesha huku Jonas akiwa salama kifuani kwangu.
Sijui hata nilikuwa nawaza nini hadi kufika pale stendi. Lakini ni sehemu pekee ambayo niliamini kuwa hapatakuwa na bughuza za hapa na pale, maana nikiwa na begi langu ningeweza kusingizia kuwa mimi ni abiria.
Baridi ilikuwa kali sana majira ya saa tatu usiku, meno ya Jonas yakawa yanagongana mdomoni, matumbo yake yakawa yanaunguruma. Nikajisemea nafsini kuwa yule mtoto yupo katika mateso makuu, alinikumbatia kwa nguvu sana lakini sijui kama alipata alichokuwa akikitafuta.
Joto!! Hakulipata joto kwani mwili wangu wote ulikuwa wa baridi pia. Nilimsikitikia sana, nikajaribu kujiuliza tena na tena ni kitu gani naweza kufanya kupambana na hali hii. Nilitazama huku na kule, kisha nikavamiwa na wazo moja kuwa iwapo nitaleta lelemama Jonas atanifia kifuani.
Wazxo la kifo likanigutusha kutoka pale chini, nikasimama wima, nikampigapiga Jonas mgongoni, akakohoa kisha akasema neno moja likaniumiza.
“Ataaka babuuu!!”
Chozi likanidondoka, nikaujua uchungu anaopitia Jonas kwa kumkosa mzee Aswile lakini nami pia nilikuwa katika uchungu mkubwa kwani laiti kama mzee Aswile angekuwepo ningekuwa natabasamu tena. Na ningekuwa nimemkumbatia Jonas huku tukiwa tumejifunika blangeti zito.
Lakini sasa nilikuwa stendi na mawazo yangu yakiwa yameganda.
Suala la kifo cha Jonas likanichangamsha na kunitia hofu kwa wakati mmoja. Na hapa nikakumbuka sehemu moja ambapo naweza kujaribu kukimbilia. Nikamkumbuka Stephano.” Nadia akasita kuzungumza kisha akanitazama na kuniuliza swali.
“Stephano…jina zuri eeeh!!” nikatikisa kichwa kukubaliana naye.
“….ni heri uwe na jina baya lakini matendo yako yawe mazuri kuliko kuwa na jina baya linaloficha matendo yako….alikuwa anaitwa Mchungaji Stephano na wengi walimuita mtu wa Mungu. Alikuwa anajitolea sana kwakweli, alikuwa akihubiri basi watu wote kimya na alikuwa anagusa samba nafsi. Mara yangu ya kwanza kumfahamu nilienda na akina Monica watoto wa mzee Aswile, ujue pale nyumbani ni mimi peke yangu nilikuwa muislamu, tena muislamu jina tu maana sikuwa nakumbuka hata mwezi mtukufu ni upi, sikumbuki mara ya mwisho kukanyaga msikiti ni lini. Kwa kifupi nilikuwa muislamu wa kale, hivyo ilipotokea familia ile inaenda katika ibada nami nilijumuika nao mara moja moja ninapokuwa najisikia, sikuwahi kulazimishwa kubadili dini hata siku moja. Na pia hakuna aliyewahi kuniuliza kwanini siendi msikitini. Nilipohudhuria kongamano hili ndipo nilimfahamu mchungaji Stephano, alikuja kuisalimia familia nzima ya mzee Aswile na hapo akatambulishwa kwangu. Alikuwa mchangamfu tena mwenye utani sana, haukuwa utani wa kukera, nilipomwambia mimi ni muislam akaniambia tushindane kuomba dua, aisee yule ni zaidi ya muislamu yaani kila aya ninayoifahamu mimi na yeye anaijua. Lakini mbaya zaidi alikuwa anazijua hata nisizozifahamu mimi. Ukaribu wetu ukaanzia hapa.
“Mariam wakristo na waislamu ni watoto wa baba mmoja, usisite kuhudhuria ibada kisa wewe ni muislamu, hakuna anayeutukana uislamu katika ibada na vilevile hakuna mwenye haki ya kuutukana ukristu misikitini sisi ni watoto wa baba mmoja Mariam, usibaki nyumbani mpweke.” Mchungaji aliniambia maneo yale yakaniingia na tangu wakati ule nikawa nikipata hamu ya kusikiliza kwaya nahudhuria kanisani, na kila nilipohudhuria mchungaji Stephano alikuwa akizungumza nami.
Sikuwahi kujutia hata siku moja kuhudhuria katika ibada zao.
Kanisa lao lilikuwa maeneo ya Uyole! Na siku ya kutimiza miaka miwili tangu awe mchungaji tulipata nafasi ya kwenda kwake kusheherekea na familia yake nyumba yake ilikuwa jirani na maeneo ya Uyole. Nilipakumbuka vyema.
Jina la mchungaji huyu likawa jina sahihi kabisa kwa wakati ule, kama aliweza kunielewa vyema tangu nikiwa kwa mzee Aswile na kwa kuwa alikuwa mtu wa kujitolea basi huyu alikuwa mtu sahihi kabisa wa kumweleza matatizo yangu.
Nikaingia stendi, sasa nilikuwqa abiria kweli.
“Mbeya mjini ya mwisho, Uyole Sai, Ilomba, Mama John, Soweto……mbeya mjini ya mwisho gariii..” nilisikia sauti ya mpiga debe akiinadi gari aliyokuwa anasimamia.
Nikaingia garini nikiwa nimembeba Jonas aliyekuwa usingizini nusu na nusu macho!!
Gari likapakia kwa takribani nusu saa, na hapo likaondoka kwa mwendo wa kusuasua likiokota abiria hapa na pale.
Saa tano usiku tulikuwa Uyole, nikashuka baada ya kulipa nauli.
Sasa nikabakiwa na shilingi elfu mbili tu!
Giza lilikuwa limetanda na bado baridi iliendelea kupiga, mji ulikuwa umetulia sana. Lakini niliendelea kusonga mbele hadi nikaifikia nyumba niliyoamini kuwa aliishi mchungaji Stephano. Niligonga geti mara nyingi sana, na hatimaye nikamsikia mtu akiligusagusa.
“We nani?” sauti inayounguruma kutoka usingizini ilisema nami. Nikajitambulisha lakini hakunielewa, nikasema mimi ni muumini wa kanisa la mchungaji Stephano, hapo sasa aliweza kufungua geti.
“Unamtakia nini usiku huu.”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Mtoto amezidiwa nahitaji huduma yake…” nilidanganya, hapa mlinzi akatilia maanani na kunikaribisha ndani. Kwa jinsi tulivyokuwa tunatetemeka hata angekuwa nani lazima angeamini nilichokuwa nasema. Mlizi akaelekea mlangoni, akanyanyua mkonga wa simu akaanza kusikiliza nikaisikia ikiita kwa ndani maana ulikuwa ni usiku ilisikika vyema. Simu ikapokelewa wakazungumza kwa dakika kadhaa kisha akaushusha mkonga chini na kungojea.
Baada ya kama robo saa akatoka mchungaji kijana, Stephano. Nikamkimbilia na kumwangukia kifuani mimi na Jonas, akaizungusha mikono yake nikalipata lile joto la upendo.
Akanikaribisha ndani sebuleni, nikaingia huku nikiwa nalia kilio cha kwikwi, akaniuliza kulikoni. Huku akiwa ananitazama katika hali ya kutia matumaini na upendo mkuu.
Ningeweza kusita kumweleza mtu yeyote yule juu ya maisha yangu lakini si mtu ambaye anaaminiwa na maelfu kama mtu wa Mungu, na alishiriki katika kuijenga imani yangu. Na alinifanya kila jumapili niione kuwa ya thamani kwa sababu tu alikuwa akiniambia maneno mazuri, Stephano alichangia kwa kiasi kikubwa kurejesha ushirikiano kati yangu na Mungu ambaye niliwahi kusema kuwa amenisahau ama anashiriki katika kunisulubu.
Nikamweleza historia yangu ngumu kwa ufupi sana, nikamweleza jinsi nilivyofika nyumbani kwa mzee Aswile na kisha nikagusia kiundani juu ya taarifa ya tetesi aliyonipa shamba boi juu ya hisia za mama Aswile kwangu mimi kuwa nina mahusiano na mumewe. Mchungaji akaduwaa, lakini nikafikia hadi hatua ya kumweleza kuwa nahisi mama Aswile anahusika katika kumuua mumewe. Hapa akaungana nami kwa hisia hiyo, akatazama juu akawa kama anayenena kwa lugha nisizozijua. Bila shaka alikuwa kiroho zaidi. Pia nikamgusia juu ya Jonas ambaye mama Aswile alidhani ni mtoto wa mume wake, hapa nikamtaja Jesca kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu na nikamweleza mchungaji nkuwa nina tatizo la uzazi na sijawahi kuwa na mtoto. Akanipa pole!!
“Mchungaji! Mimi nimeondoka katika familia ile kwa sababu nachukiwa, na mbaya zaidi nimefanya fujo pale nyumbani. Nipo hapa kwa kitu kimoja tu…uwezo wangu kiakili umefika mwisho, sijui nini cha kufanya na nimechanganyikiwa kabisa. Naomba unisaidie kutatua jambo hili, ni wewe pekee uliyebaki katika maisha yangu, ni wewe waweza kusema neno nami nikajiona ni mwanadamu tena. Tafadhali baba mchungaji!!” nilimsihi kwa sauti ya chini. Na hapo nikayangoja majibu yake.
“Mariam!! Bwana ni mwema na humulika taa kwa watu wake na kamwe hawatajikwaa, malaika wamewazunguka na kuwalinda kwa mabawa yao. Mungu yu pamoja nawe, haujayapita hayo yote kwa uweza wako. Sijisikii vyema sana usiku huu baada ya taarifa hii, sasa nakuomba ulale, mimi ninaingia katika maombi, na nitakesha kukuombea usiku mzima na asubuhi bwana ninayemuamini atatoa majibu.” Aliniambia huku kama kawaida akirusha mikono huku na kule kisha kunena kwa lugha za kigeni.
Mwisho akanipeleka katika chumba maalumu kwa ajili ya wageni.
“Watoto na mama yao wamesafiri nimekuwa mpweke sana, angekuwepo Suzan ungelala naye humo. Lakini hayupo sasa.” Aliniambia kwa kusihi, sikujali., nikaingia chumbani, nilitamani kuoga lakini ile baridi ikanisaliti nikaghairisha na kujitupa kitandani.
Blangeti zito likamfunika Jonas, sasa alitabasamu kidogo, kisha akapotea usingizini. Nami nikawa katika kusinzia. Lakini si hoi kama Jonas, baada ya muda kidogo nikiwa sijasinzia bado nikasikia sauti ikiniita, alikuwa ni mchungaji. Nikajifanya sisikii vyema, akaita tena bado sikuitika. Sijui kwanini sikutaka kuitika, labda ni msongamano wa mawazo kuwa mchungaji ameingiwa tamaa za kimwili ama vipi. Hatimaye akaondoka. Nami nikasinzia kweli.
Nilikuja kushtuka usingizini Jonas alikuwa analia, kilio chake kilitaka kufanana na kile cha usiku ule kisha asubuhi mzee Aswile akafariki. Nilitaka kupuuzia baada ya Jonas kusinzia tena kwani kilio kile hakikudumu. Lakini nikakumbuka kuwa mimi ni Nadia niliyelaaniwa, Nadia mwenye mwonekano wa mwanadamu lakini nikiishi kama kivuli, Nadia mwenye hofu wakati wote. Nadia asiyeaminika, Nadia asiyetakiwa kumwamini mtu.
Nikasimama na kuufungua mlango kisha nikajongea katika sebule, nikijifanya naenda kutafuta maji ya kunywa katika friji. Nikaisikia sauti ikiunguruma kwa chini chini, bila shaka katika simu. Nikaganda katika friji na sasa nikaweza kusikia maneno baadhi, lakini muongeaji akaendelea kujisahau na mwisho akawa anazungumza kwa sauti ya juu.
“Ameshasinzia nimeenda chumbani alipo nimemuita haitiki, amechoka kwakweli. Sasa sika wewe kitu cha msingi kama unafahamiana na bodaboda yeyote yule akupeleke kituoni asubuhi, si umeshachukua RB….wewe wape hela ya mafuta mje na difenda yao mtamkuta hapa…..
….wewe usijali kuhusu hilo, nitakifunga kile chumba mtamkuta kama alivyo. Tena jitahidi sana maana mambo aliyoniambia ni balaa, wewe naye ujifunze kuwa na siri mbona anajua mambo mengi hivyo, je angeenda kwa mtumishi mwingine unadhani tungeonekanaje mpenzi wangu.
……sio kama nakulaumu mamangu, mi nakwambia ukweli mpenzi. Haya hayo yaishe maana hukawii kukasirika. Wewe asubuhi sana uje umchukue halafu mimi nitamalizana na mkuu wa upelelezi afanye tunayotaka. Mbaya sana huyu binti, na niliwahi kukwambia kabisa haya mambo ya kufuga viumbe usiowafahamu ipo siku utafuga majini………(kimya akisikiliza upande wa pili)
…..kuhusu mtoto usijali hata cha msingi huyu paka kwanza. Alfajiri nakifunga chumba mtawakuta wote. Alijifanya mjuaji sana kukupigeni na kukimbia hii Mbeya yetu asingeweza, wewe nilikwambia ukajifanya kukata tamaa…..wewe saa kumi na mbili fika hapa…”
Nilibaki kama sanamu nimeganda pale katika friji. Alikuwa ni mchungaji Stephano, mtu pekee niliyekuwa namwamini kuwa atanisaidia katika tatizo hili linalonikabili, sasa anazungumza na mama Aswile, yaani mama Aswile na mchungaji kumbe ni wapenzi. Mungu wangu!! Nilipagawa, mbaya zaidi alikuwa amesisitiza kuwa asubuhi polisi wanakuja kunishika, na kuhusu Jonas watajua cha kumfanya. Nilitetemeka sana, nikaondoka kwa kunyata nikaelekea chumbani, Jonas alikuwa anapepesa macho huku na kule, na yeye alikuwa ametoka usingizini tena. Ukutani kulikuwa na saa, ilikuwa ni saa nane na dakika hamsini hivi. Sikutakiwa kulala tena, lakini ningetoka vipi katika nyumba ile.
Nadia mimi nilikuwa nimetupiwa pepo la kusalitiwa na kukataliwa, hata kiongozi wa kiroho alikuwa amenisaliti!!!! Hakika niliumia sana, na hapa nikajiona nisiyekuwa na ujanja tena.
Majira ya saa kumi na moja chumba kile kilifungwa kwa nje.
Saa kumi na mbili kama nilivyoyasikia mazungumzo kwenye simu ndo muda ambao askari walitakiwa kufika pale kunikamata. Jonas abaki na kufanywa wanavyotaka.
Milango ya jela nikaiona ikifunguka na Nadia mimi nikitakiwa kuingia. Nikaona akina Desmund wakitabasamu huku mzee Matata na wenzake wakinicheka, Bryan alikuwa akinizomea na familia yangu nzima ikipiga makofi, hata mama yangu akiwa mmoja wao katika orodha.
Nitafanya nini nikwepe mtego huu, kumwamini mtumishi wa kiroho kumeniponza. Muda nao ukazidi kusogea dakika kwa dakika………..mwandishi umewahi kuusikia moyo wako ukiwa wa moto huku ukidunda pigo moja baada ya jingine kwa kasi isiyohesabika. Basi nilikuwa namna ile. Sikuona dalili yoyote ya kujiokoa kutoka pale. Mlango mkuu wa kutokea nje ulikuwa umefungwa na mbaya zaidi mlinzi atakuwa amezuiwa asiniruhusu kutoka nje……..nilimwomba Mungu ile laana iishie kwangu lakini sasa alikuwa kwa mara nyingine amenihukumu na kunipa kisogo, Jonas alikuwa anaishi katika laana yangu, Jonas alsiyejua hili wala lile anahangaika nami..Jonas…Jonaa….asiyeweza hata kusema neno lolote la ubaya kwa mtu anahukumiwa na wanaojitambua, walimuita mwanaharamu sasa watamuua.” akasita kuzungumza, kilio cha kwikwi kilikuwa kimelikamata koo lake. Akalia kwa kujibana bana lakini hakuweza. Alikuwa anatetemeka sana.
Nikamchukua shingo yake na kumlaza begani mwangu, akaendelea kulia.
“USILIE NADIA….machozi yako bado yana thamani sana usiyaruhusu yamwagike zaidi ya hapa Nadia, nilikuahidi tangu siku ya kwanza kuwa sitakusaliti kamwe na nitakupigania upate unachokitafuta. Niamini, na nilikwambia tukifika Dar utajua nini namaanisha….” Nilimsisitiza lakini bado alilia kwa uchungu sana.
Nikamlaza kitandanbi kwangu, nikamfunika na shuka langu, mimi nikakaa katika kochi, Nadia akiwa analia pekee katika shuka.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Katika makochi mimi nikazidi kuchanganyikiwa.
Nadia alikamatwa ama alifanikiwa kuwashawishi wakamwachia?
Kama alikamatwa ilikuwaje akaachiwa huru wakati alikuwa na siri nzito kifuani mwake?
Na Jonas mwisho wake ulikuwa upi?
Vipi kuhusu Desmund?
Vipi mkewe Desmund?? Vipi mama mzazi wa Desmund na yule mzee Matata naye vipi?
Jesca hajulikanai alipo, na yeye hatima yake vipi?
Hakika maswali yalikuwa mengi kuliko majibu…nikatamani Nadia ajue jinsi gani maswali yale yananiumiza kichwa anyanyuke na kuendelea kunijibu. Lakini Nadia hakuwa anajua hilo….akasinzia pale kitandani.
*****
Nilisinzia katika yale makochi pale bila kujitambua kama nilisinzia, nilikuja kushtuka baada ya kusikia napapaswa. Nilipofumbua macho alikuwa ni Nadia, alikuwa anatabasamu pana usoni.
“Utaibiwa wewe!!” aliniambia huku akirejea kukaa kitandani.
“Mh!! Hivi saa ngapi sasa hivi?” nilimuuliza, akanieleza kuwa tayari ilikuwa saa kumi na mbili asubuhi. Nililala kwenye kochi na yeye alilala kitandani.
“Duh mgongo unauma kweli…umenilazaa kwenye kochi we mtoto.” Nilimtania Nadia wakati huo nikijinyoosha.
Nadia alinitazama kisha akajiweka katika namna ya kuchukua egemeo ukutani. Na hapo akaanza kuzungumza.
“Walaah!! Ungekuwa wewe usingeweza kudumu hata saa zima kumbe, yaani hadi Jonas anakuzidi kumbe, yule mtoto alikuwa jasiri sana, niliamini kabisa kuwa lazima ataniumbua tu usiku ule, lakini ya Mungu mengi kwakweli Jonas alivumilia. Nilimbeba akiwa katika usingizi nikamuhamishia nyuma ya kochi kubwa katika sebule ya kifahari ya mchungaji Stephano, nikamtandikia kitambaa chepesi tu nikamlaza katika vigaye vile, bila shaka unajua jinsi gani vigaye vinakuwa na baridi kali, pale kitandani nikaacha mashuka yakiwa katika namna ya kufunika viumbe hai. Ni hilo lilikuwa jaribio langu la mwisho kabla mchungaji hajachukua uamuzi wa kukifunga kile chumba kama alivyokuwa amesema katika simu.
Hakika baada ya kutoka mle chumbani na kujificha nyuma ya kochi lile mimi na Jonas wangu nilimsikia mchungaji akinyata hadi akaufikia mlango ule wa kitasa, akaingiza funguo kwa tahadhari bila hata kujihakikishia kama bado nilikuwa ndani ya chumba kile. Akaufunga mlango!! Baada ya hapo akampigia simu mama Aswile na kumweleza kuwa amekifunga chumba tayari.
Niliendelea kubaki nyuma ya kochi kubwa pale sebuleni huku nikiomba dua zote Jonas asije kushtuka na kuanza kulia. Jambo ambalo kwangu mimi lilikuwa hatari sana, na jinsi mchungaji yule alivyokuwa anazungumza kwa hasira na chuki basi angeweza kunitoa roho kama angegundua nimemchezea shere katika jambo hilo.
Niliendelea kuwa pale, Jonas alikuwa amelala lakini mimi nilikuwa nimejikunja katika namna ambayo mwanadamu wa kawaida katika mazingira ya kawaida asingeweza kudumu walau kwa nusu saa, lakini Nadia mimi kwa wakati ule sikuwa mwanadamu wa kawaida na kubwa zaidi sikuwa katika mazingira ya kawaida. Nilikuwa katika hatari na nilitakiwa kuchukua maamuzi ya haraka, maamuzi ambayo yangeniamulia kuwa aidha naendelea katika harakati zangu za kulipiza kisasi na kukomboa mali zangu kutoka kwa Desmund huku nikimfanya aione dunia chungu, ama kuzembea kidogo na kujikuta nikiishia jela ambapo nitakuwa katika machungu, labda kupita haya ya awali.
Hali hiyo ilinipa ujasiri na kuendelea kujikunja pale, sio siri mgongo ulikuwa unaniuma sana, ulichemka na kuwa wa moto, lakini kipi kingekuwa bora kwangu, aidha kuuumia kwa muda ama kuja kuteseka maisha yangu yote. Hali ilikuwa tete.
Majira ya saa kumi na mbili kwa mujibu wa saa iliyokuwa ukutani nilisikia kile ambacho Stephano alikuwa ameahidi, niliisikia gari ikisimama nje na geti likafunguliwa. Baada ya hapo chumba cha Stephano kilifunguliwa alipofika sebuleni, nikasikia vishindo vingine.
“Mh…..nikumbatie kwanza la sivyo simtoi..” nilimsikia mchungaji akisema, kimya kikatanda, na mara wawili hao ambao niliisikia miguno ya kimahaba ikiwatoka wakaangukia katika lile kochi ambalo mimi nilikuwa nimejificha nyuma yake, kishindo cha kuliangukia lile kochi mara Jonas naye akafumbua macho, Mungu wangu!! Nikajua kifuatacho ni kutokwa na kilio, nikaundaa mkono wangu iwapo Jonas atathubutu kutoa kilio niweze kumziba mdomo, hekaheka ziliendelea katika lile kochi bila shaka walikuwa wakibusiana, na walikuwa wamenogewa hadi pale honi ilipopigwa.
“Ndo hao uliokuja nao.” Stephano aliuliza.
“Nimekuja naye mmoja tu mbona, tumechukua teksi tu walishauri hivyo.” Alijibu mama Aswile sasa niliweza kuisikia sauti yake vizuri.
“Mpenzi yaani nd’o alikukwangua hivi?” mchungaji aliuliza.
“Mwendawazimu sana yule mtoto, namfunga maisha haki ya Mungu!!” aliapa kwa hasira, nami nikazidi kutetemeka lakini sikuhamisha macho kutoka machoni mwa Jonas.
“Kitu cha msingi wewe muuzie kesi kuwa alimuua mzee wako, hapo tu utamaliza. Ushahidi wa kutosha nitautoa mimi na Monica mtoto wako. Anafia jela huyu, na hapa ujue kitu kimoja yaani akibaki tu ujue muda wowote ule tunaumbuka.” Mchungaji alimsisitiza mama Aswile, na hapo wakasimama kisha wakatoka nje, kimya kikatanda kidogo, nikatega sikio langu kwa makini kabisa na hapo nikasikia vishindo kwa mbali. Wakaingia hadi sebuleni. Nikahesabu miguu iliyokuwa inakatiza pale kupitia upenyo uliopoa chini ya kochi. Walikuwa watu wanne, wote watu wazima.
“Kwa hiyo yupo na mtoto sivyo.” Aliuliza mwanaume ambaye sauti yake niliitambua kuwa ipo kiaskari.
“Yupo na mtoto ndio, lakini mkorofi na ana nguvu ndo maana nataka tumshike wote yule…” mama Aswile alisema kwa sauti ya uoga. Nikajisikia fahari kuwa kipigo nilichokitoa kule nyumbani kiliacha heshima ya kutosha.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Siwezi kubabaishwa na msichana hata wakiwa kumi mimi.” Mchungaji Stephano alijitamba, kisha akamalizia “Ila twende tu wote kama unavyosema.”
Wakatoweka pale sebuleni, nami hapo nikafanya tukio la kutumia sekunde chache sana kuokoa uhai na kuendelea na maisha yangu. Nikamkwapua Jonas, kisha nikanyata upesi na kutokea mlango wa sebuleni, huko nikatimua mbio zaidi. Nikaikuta ile gari pale nje, nikajifikiria kuingia ndani ya gari kisha niondoke nayo kwa sababu nilijua kuendesha vyema lakini nikahofia kuzidisha kuyafanya mambo kuwa magumu zaidi.
Nikaamua kupita kona kadhaa hadi nikafika stendi, nikasimamisha gari, lilikuwa lkimejaza sana na watu walinionea huruma sana kuwa nina mtoto sitaweza kupanda lakini ni gari hilo nilikuwa nalihitaji.
Nikapanda mwanaume mmoja akanisaidia kumbeba mtoto, gari likaondoka nikiwa nimebanwa mlangoni.
Gari lilikuwa linaelekea Mbalizi Mbeya, hapo mfukoni nikiwa na shilingi elfu mbili tu za kitanzania. Sikuwahi kufika Mbalizi hapo kabla na wala hilo halikuwa lengo langu. Kila kituo watu walikuwa wanashuka na hatimaye nikapata nafasi ya kukaa, nikajipekua katika nguo zangu.
Alhamdulilah!! Pesa haikuwepo, nikajipekua huku na kule, hakika pesa haikuwepo. Na katika kipindi hicho yule kondakta alianza kudai nauli kwa watu wote ambao walikuwa wamepandia njiani. Akili ilizunguka upesi sana nikijiuliza nafanya nini iliaweze kunielewa kijana yule ambaye hakuwa na dalili zozote za huruma.
Hatimaye akanifikia nikiwa nimempakata Jonas. Akanidai nauli yake. Nilimtazama kama sijamsikia, na yeye akanidai tena nauli.
“Nimeibiwa kaka yangu!!” hatimaye niliamua kuusema ukweli. Kondakta akaanza kucheka kwa fedheha, ni kama hakuwa tayari kuniamini hata kwa mbali.
“Hadi kina mama mnaanza kuwa wasanii siku hizi.” Akasema kauli hiyo, mimi sikusema lolote lile.
“Haya bwana sadaka yangu hiyo siku nyingi sijatoa sadaka wala sijaenda katika nyumba za ibada.” Alisema kama anayetania kisha kweli akaniacha hadi niliposhuka Mbeya mjini.
Nilijikuta tu nikiona Mbalizi si mahali stahiki kwangu, hivyo nikaamua kuimalizia safari yangu Mbeya mjini, walau hapo ningeweza kuwa karibu na huduma zozote za dharula.
Ilikuwa ni saa tano asubuhi wakati Jonas alipoanza kulia huku akilalamika njaa. Nilijaribu kuitafuta tena na tena ile pesa ambayo awali niliikosa katika gari lakini sikufanikiwa kuiona, nilitafuta kila mahali, nikajaribu kumbembeleza Jonas lakini bado hakuonyesha dalili ya kunyamaza na alikuwa akihitaji chakula. Ukimya wangu usingeweza kunisaidia kitu, nikatembea huku na kule hadi katika mgahawa mmoja wa watu duni. Nikamkuta mwanaume akiwa ameketi na ni kama alikuwa msimamizi wa mgahawa ule. Nikamwendea kwa heshima ya uoga.
Nikamsalimia na kumweleza shida yangu.
“Baba mimi nakuomba unisaidie, nioshe vyombo ama chochote ambacho naweza kusaidia hapa na umpatie mwanangu chakula, mwanangu tu!! Mimi hakuna haja nitahimili lakini huyu mtoto tangu asubuhi ya jana amekula wali kidogo tu!!” nilimsihi. Maneno yakamgusa na bila shaka kilio cha Jonas kutoka mgongoni kiliam,sha hisia zake, wanawake waliokuwa wafanyakazi pale wakawa wanamtazama ni maamuzi gani atachukua, nadhani hili nalo lilimtia aibu zaidi.
Akafikia hatua ya kunipa chakula bila kunifanyisha kazi yoyote, Jonas akala kwa fujo kabisa kuonyesha kuwa alikuwa na njaa kali. Na mimi nikapewa sahani yangu nikala. Hakika utu aliouonyesha yule baba ulikuwa wa aina yake. Nikamshukuru kwa utu wake kisha nikamfunga mwanangu mgongoni tukaondoka nikiwa bado sijajua baada ya kupata chakula mkile nini kinafuata?
Wazo kuu nilitaka kujua nafika vipi katika mji wa Musoma tena kwa ajili ya kudai haki yangu. Muda nao ulizidi kusogea kuikimbilia jioni nikiwa sina maamuzi thabiti, majira ya jioni ya saa kumi na mbili na dakika kadhaa nilianza kuona hekaheka huku na kule na baada ya dakika kadhaa nikaisikia adhana, hapa nikawaona watu wengi wakiwa wamejikita katika kula na kunywa katika namna ya kuharakisha.
“Kuna nini kwani?” nilimuuliza kijana mmoja muuza karanga aliyekuwa jirani nami.
“Mambo ya kufuturu hayo.” Alijibu kwa ufupi. Ile kusikia neno futuru akili yangu nayo ikapata uhai, si kwamba naweza kupata chakula cha bwelele jioni ile bali naweza kupata na kitu kingine cha ziada cha kuniwezesha kufika ninapotaka. Sikuonyesha mshtuko wowote na badala yake nilitabasamu tu lakini nilikuwa nimepata nguvu mpya kabisa. Na hapo nikajihakikishia kuwa nitalala Mbeya kwa tabu usiku huo tu lakini baada ya hapo nitaondoka na kufikia azma yangu vyema.
Nilikuwa nimemuhoji maswali mengi sana yule kijana na alikuwa ameyajibu vyema, sasa niliweza kuondoka na kutafuta mahali pa kufuturu. Kwa sababu nilikuwa muislamu na niliijua miiko ya dini hiyo hata sikuhangaika sana, mwisho nikapata mahali nikafuturu. Na kama bahati nyumba mbili baada ya mji ule kulikuwa na msiba, nami nikajumuika katika msiba ule. Huko nikajishughulisha na shughuli mbili tatu, lengo langu kuu likiwa ni kupata sehemu ya kulala, Jonas alipata fursa nnyingine ya kucheza na watoto wenzake. Kweli nikalala na asubuhi kulipokucha tu, nikaondoka na kuwa wa kwanza katika ofisi ya mabasi yaendayo jijini Dar es salaam, nikavizia hadi nilipomuona mmiliki wa basi nililokuwa nalihitaji.
Alipoingia tu na mimi nikaingia, nikazuiliwa mlangoni lakini nikajifanya kuwa ni abiria na nina shida na bosi yule. Nikakubaliwa kuonana naye.
Nikaingia ana kwa ana na mkurugenzi.
“Asalaamaleykum Shehe…” nilimsalimia. Akanijibu na kunikaribisha.
Nikachukua nafasi na moja kwa moja nikaingia katika mada iliyonileta.
“Mkuu, mimi si ombaomba lakini nina shida. Nimelitafuta kimbilio sahihi katika jiji hili nisilolijua na nimeona waweza kuwa mtatuzi sahihi. Shida yangu ni moja tu nisikupotezee wakati wao kaka yangu. Nahitaji kufika jijini Dar es saam, nahitaji kufika aidha kwa kusimama katika gari lako na kama ingekuwa inafaa hata kunihifadhi katika sehemu ya kuhifadhia mizigo kwangu ni sawa. Nimetelekezwa jijini hapa, naishi kwa kutangatanga, ukinisaidia tu kufika nyumbani sihitaji jambo lolote lile jingine. Nahitaji tu kufika nyumbani, nikishushwa pale Ubungo tu mimi nitakuwa nimefika, nitazame kwa jicho la huruma, kukataa kwako tu kunifikisha huko basi kiumbe hiki mikononi mwangu kitalala nje tena kikipigwa baridi. Usinionee huruma mimi na wala usitoe maamuzi yako kwa kunitazama mimi bali kitazame kiumbe hiki mikononi mwangu. Sina hata senti tano ya kukinunulia chakula, nisaidie ewe mkuu.” Nilimaliza kuzungumza nilichopanga kusema naye. Maneno yale yakamgusa haswa. Akawa kama anayekosa kauli.
“Kama haitawezekana nielekeze kwa wenzangu walio katika mfungo niwaeleze kama watanisikiliza.” Nikauvunja ukimya. Kauli hiyo ikawa shabaha maana nilijua kuwa amefunga mwezi mtukufu wa Ramadhani, kukataa kwake jambo ambalo lipo ndani ya uwezo wake ni kuiharibu funga yake, na kunielekeza kwenda kwa waislamu wengine basi angekuwa anaikaribisha dhambi waziwazi na pia kuwa katika hatia kubwa.
“Sasa unajua kusimamisha watu siku hizi hawaruhusu na basi langu haliruhusu kabisa…unaitwa nani?” aliniuliza.
“Naitwa Mariam bosi.” Nilimjibu kwa unyenyekevu mkuu.
“Mariam!! Mariam…haya basi kesho njoo asubuhi tuangalie itakavyokuwa.” Aliniambia hatimaye, nikajua kuwa tayari amenikubalia.
“Sijui nikushukuru vipi kwa kunipa nafasi hii hadimu ya kunisikiliza, nitafika hapa asubuhi sana” tuliagana akanipatia shilingi elfu tano.
Siku hiyo sikucheza mbali na stendi kuu!! Na nililala msibani tena hadi alfajiri.
Yule mkurugenzi akakutana nami asubuhi akampa maelekezo kondakta wake, kisha akanieleza kuwa yule atanisimamia hadi nafika jijini.
“Funga yako ni funga ya kweli!! Ubarikiwe sana” nilimweleza wakati naondoka kuingia ndani ya gari na yeye akajibu ‘inshalah’ Wakati nilitegemea kuwa yule bwana ameelekezwa kuwa nisimame ama nikae katika injini haikuwa hivyo, nilipatiwa siti mbele kabisa. Nikakaa!!
Nikajishukuru mwenyewe kwa ujasiri wangu kwani kama si hivyo aibu ingenikutia Mbeya.”
Kondakta alikuwa karibu yangu na mara kwa mara alikuwa akinijulia hali, yeye pia alikuwa mkarimu sana. Tuliingia Dar es salaam majira ya saa mbili usiku baada ya kuharibikiwa gari maeneo ya Iringa.
“Njoo huku dada.” Aliniongoza yule kondakta.
“Itabidi ukae hapa mpaka nitakapokupa maelekezo zaidi aliyonipa.” Alimalizia nami nikamsikiliza kwa makini na kumuelewa huku nikizidi kukumbuka ukarimu wa mmiliki wa magari hayo.” Hapa Nadia akasita na kisha akapiga mwayo mrefu kabla hajaketi vyema na kisha kuendelea.
“Mwandishi si kila mtu anayekwambia amefunga ujue amefunga kweli kuna watu ni majambazi na wenyewe unakuta wanajiita waumini safi kabisa mida ya mchana na wengine mchana wananyenyekea lakini usiku ni wazinzi. Mtu unapoamua kufunga basi usifunge ili fulani ajue wewe umefunga, maana utakuwa unajidanganya wewe mwenyewe, angalia huyu Rama yaani tangu Mbeya hakutia kitu mfukoni na kila mara alidai kuwa ameizoea swaumu tayari alizihesabu tasbihi mikononi na kila alipopata nafasi alionekana kuwa katika tafakari nzito, hali iliyonipelekea kuamini kuwa bosi wa kampuni ile alikuwa ameajiri watu makini na wacha Mungu sana, hata tulipofika Ubungo bado niliendelea kuwa na imani juu ya kampuni hilo la usafirishaji.
Lakini usilolijua ni sawa na usiku wa giza, kama Rama alikuwa vile kwangu bila shaka kwa mtu yeyote yule angeweza kuwa vile na bado akaonekana mtiifu.
Rama aliniweka pale hadi majira ya saa nne na nusu usiku, nilikula chakula kizuri na Jonas alifurahia chakula alichokuwa anakitaka, mwisho Rama alifika na kunitaka radhi kuwa alikuwa anafunga mahesabu kwa magari yote ya kampuni hiyo hapo ndipo nikatambua kuwa yeye ni kondakta mkuu ama la alikuwa ndiye anayeaminiwa zaidi na alipewa cheo fulani.
“Ujue muheshimiwa akisikia upo hapa hadi muda huu atachachamaa sana.” Alisema tena katika namna ya hofu kiasi, na hapo akanichukua na kuniongoza katika taksi. Mimi nikiwa kama kondoo nafuata kile ninachoambiwa, taksi ilienda kwa mwendo mfupi tukashuka na kuingia katika katika hoteli jirani tu na stendi ya Ubungo. Hapo tukaingia katika hoteli hiyo ambayo nilihisi kuwa amelipia chumba tayari, akanipeleka moja kwa moja hadi katika chumba hicho.
“Hii ndiyo hoteli ya bosi, akiwa na wageni wake huwa wanafikia hapa na gharama zote juu yake.” Alisema kauli ambayo ilinitoa hofu kabisa na kurejesha tumaini tena. Ukarimu wa mkurugenzi ule ulikuwa wa aina yake.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Chumba kilikuwa kikubwa!! Ramadhani akanielekeza kila kitu mle ndani na kisha yeye akatoka na kuahidi kurejea baadaye iwapo itabidi.
Kauli yake ikanitia utata, tayari ametukabidhi chumba sasa kwa namna gani tena anasema atarejea wakati ni usiku mnene ule?
Nikaipuuza kauli ile nikiamini ameitoa kimakosa, kwanza likuwa katika mfungo wa Ramadhani kama lilivyo jina lake sikutegemea kama atataka kuwa karibu na msichana yeyote yule kwani kwa kufanya hivyo ni kujikaribishia majaribu.
Kukumbuka kuwa huo ulikuwa mwezi wa toba kukanitia nguvu!! Nikapanda kitandani na kulala, niliangaza funguo niweze kufunga chumba sikuziona, nikajisahihisha kuwa huenda ni ushamba wangu labda mlango ule haufungwi kwa funguo.
Baada ya hapo nikajitupa kitandani na kujaribu kuutafuta usingizi huku nikiwa na maswali kuwa kesho yangu itakuwa vipi………hapo nikamsahau Ramadhani..” Nadia akapiga tena mwayo mrefu.
“Vipi ni njaa ama!!!”
:Yaani kama vile upo katika akili yangu, nina njaa kali kwakweli. Leo waambie walete chai ya maziwa na chapatti maana siku nyingi sana sijala halafu nd’o zitatibu njaa yangu.” Akanielekeza, nikanyanyua simu na kupiga kwa wahudumu. Nikasikilizwa, kisha nikaambiwa muda si mrefu tutakidhiwa haja zetu.
Hapo sasa maongezi yakawa juu ya vyakula mara Nadia aseme anapenda hiki nami namwambia napenda kile, mara aseme hiki anajua kukipika mimi nijigambe najua kupika zaidi yake. Mambo yalienda hivyo hadi muhudumu mnene alipokigonga chumba. Nikaenda kukifungua nikampokea alichokuwa amebeba. Alikuwa anathema juu juu. Nadia akauliza kulikoni.
“Nimepanda ngazi aisee leo lifti mbovu.” Alilalamika huku akitweta. Mimi nikampa pole, Nadia akaguna huku akibetua midomo.
Muhudumu alipoondoka nikamuuliza Nadia kulikoni mbona anaguna.
“Si namshangaa huyo kaka, yaani hivi vingazi sijui vingapi vinamtoa jasho hivyo, dah kuna watu wamezoea raha duniani jamani. Hivi mwandishi hizo chai na mtoto wa miaka miwili kipi kizito.’ Aliniuliza.
“Mtoto hata kama ni wa mwaka mmoja atakuwa mzito kupita chai.” Nilimjibu.
“Na ghorofa mbili na kumi na moja wapi kuna ngazi nyingi?” akauliza tena.
“We Nadia nawe, ghorofa kumi na moja kuna ngazi nyingi mbona..”
“Sasa huyu mkaka anavyolalamika hizi ngazi ngapi sijui je ingekuwa ngazi mia angeweza huyu kweli ama ndo angefia njiani!!!”
“Sio yeye tu hata mimi na wewe hakuna wa kupenya pale kirahisi bila kukomea njiani ama kuchoka sana.” Nilimpinga Nadia. Hapa sasa badala ya kukaa vyema kunywa chai akakaa vyema kusimulia ilimradi tu anithibitishie jambo analotaka kuniambia.
“G nitake radhi, yaani hizo ngazi zinishinde…labda kama hujafikwa na matatizo wewe na unaenda tu kwa starehe, lakini mimi niliziona chache sana siku hiyo. Tena ni siku ile ambayo Rama alitupeleka katika kile chumba akidai kuwa ni bosi wake amemwambia atuchukulie, mimi nikalala nimebweteka mara nasikia mpapaso, nakuja kustuka nakutana na Rama. Akanifanyia ishara ya kukaa kimya. Nikaamka na kuketi. Rama akataka kuendelea kunipapasa nikamzuia, hapo usingizi wote ukaisha.
“Rama wewe si umefunga wewe!!” nilimuhoji.
“Kufunga mchana bwana muda huu nimefungua lakini.” Lijibu kwa kujiamini, nikamlaani yeye na wengine wote ambao wanajifanya watakatifu mbele za watu wakati wakiwa mafichoni wanafanya mambo yao ya hovyo kwa sababu tu hakuna awaonaye.
“Rama hapana….” Nilikataa. Akaendelea kunipapasa.
“Sikia Mariam, mimi ni kondakta mkuu hapo, na hiki chumba wala si bosi nimekuchukulia mimi hapa upumzike mtoto mzuri, sasa wewe kigumu kwako nini eeh!! Wewe tufanye kisha nitaongeza pesa utaishi hapa na mtoto wako mambo mengine tutaangalia yanakuwaje.” Aliniongelesha katika maudhui ya kihuni, jambo ambalo sikupenda kabisa. Rama alionekana kuzichukulia shida zangu kama mtaji, hivyo kwa kuniambia tambo zile alijua kuwa lazima nitaingia mtegoni. Hakujua mimi ni wa aina gani, hakujua kuwa kama isingekuwa kudhulumiwa ningekuwa na pesa na mali nyingi tu na huenda tusingeweza kukutana katika mazingira yale katika namna yoyote ile.
“Rama naomba mimi nilale na kesho uniache tu nitaenda ninapojua kaka yangu.” Nikamsihi tena lakini Rama hakuonekana kuwa tayari kuniacha wakati amegharamia chumba.
“Mariam eeh acha utoto basi, kwani wewe bikra hadi ujifanye kubana, wamekuzalisha huko wamekukimbia watu tunataka kukuweka mjini wewe unaleta pozi za kishamba hapa??” sasa aliongea kama anayegombeza na wakati huohuo analazimisha.
“Rama nakuomba ujiheshimu basi….ona aibu mwanangu huyu hapa unataka kunifanyia mambo ya dharau kiasi hicho, acha Rama naomba utoke humu chumbani ama mimi na mwanangu tutoke twende tunapojua.” Nilimsihi huku nikihisi jazba ikianza kunipanda, Rama alikuwa ananikera na hapo hapo nikamkumbuka Ramso yule mwanaume aliyenilawiti jijini Mwanza. Nikawachukia Rama wote, hakika nilijiaminisha kuwa akina Rama wote ni walewale. Hasira ikanipanda maradufu, sasa nikawa najisikia kutetemeka. Sikutaka aniguse tena, lakini alionekana kutojali.
“Kwani bila haya mambo huyu mtoto ungempata mbona unaleta mambo ya kitoto kama umezaliwa jana.” Aliniambia kwa jazba. Sasa alikuwa akinizongazonga kama anayelazimisha.
“Sikia Mariam, kwani wewe unataka shilingi ngapi? Sema nikupe!!!”
“Rama sihitaji chochote kutoka kwako, mimi sio changudoa, sijiuzi Rama.” Nilijitahidi kuwa mstaarabu lakini bado haikuwezekana
Mara Rama akaniachia, akaenda katika kiti kilichokuwa wazi pale chumbani, chini ya kiti akatoka na kibegi kidogo, akakifungua. Akatoka na mabulungutu ya pesa.
“Tatizo unanichukulia poa sana Mariam, haya sema unataka shilingi ngapi unipe.” Aliniambia huku akitoa noti nyingi na kunirushia pale kitandani.
Ni kweli nilikuwa nahitaji sana pesa lakini sikuwa tayari kuwa mwepesi kiasi nkile, Rama alitaka kunidhalilisha na alikuwa anataka kuyafanya hayo katika mwezi mtukufu. Hakika nilikuwa na dhambi nyingi lakini sikutaka kumwingiza Rama katika dhambi ile ya kuzini katika mwezi mtukufu.
“Rama ….SITAKI!!” sasa nilimwambia kwa ukali.
“UTATAKA!!” alinikaripia na sasa alinikamata kwa nguvu. Rama alikuwa na nia ya kuniingilia kwa nguvu. Sikuwa na msaada zaidi ya mwanangu pale kitandani. Rama alikuwa na nguvu sana lakini nilijilazimisha nikafurukuta huku na kule kumwepuka, mbaya zaidi nilikuwa nimelala na nguo ya ndani pekee.
Mara Rama akaruka chini na kutua katika kibegi kile akakipapasa huku na kule, akachomoka na bisibisi.
“Ukijifanya mjanja Mariam nakuchomachoma tumboni.” Alinitisha na hakuonekana kutania, karipio lake likamshtua Jonas, akagutuka kutoka usingizini, akabaki kushangashangaa. Rama hakuonyesha kushtuka wala, akaendelea kunisogelea. Hakika alikuwa amenuia kunifanyia kitu kibaya.
“Haya Rama nimekubali.” Nilisalimu amri, nikanyanyua mikono juu. Na hapa Rama akafanya kosa ambalo wanaume wewngi hulifanya na kisha kuukosa hata muda wa kujuta.
Kosa la kumwamini msichana upesiupesi!! Rama akaweka bisibisi chini kisha akatoa nguo zake, akabaki kama alivyozaliwa, akanisogelea na mimi ili aweze kunitoa nguo yangu iliyobakia, nikamruhusu akanisogelea. Lakini akili ikiwa haijakubali kudhalilishwa mbele ya mtoto wangu JONAS……
Rama akawa ananivua huku akininong’oneza maneno ya kimapenzi. Alipopanda kitandani nikapata fursa ya kufanya nilichokiota. Kabla ya kukifanya nikamshukuru Mungu kwa sababu ananipa akili mara kwa mara na huku akinipa nafasi moja tu ya kufanya maajabu.
Upesi nikamkumbatia Rama kimahaba, akajua nimekolea halafu sekunde hizohizo nikamgeuza yeye chini mimi juu. Halafu mwisho nikamrusha kwenda sakafuni nikiwa juu yake. Kichwa chake kilitua katika marumaru ya pale chumbani. Rama hakupiga kelele na ule ulikuwa mwisho wa ile jeuri yake, na hapo nikashuhudia damu zikimchuruzika kutoka katika kichwa chake na kutapaka kwa haraka sana.
Nikamnyakua mwanangu na kuanza kushuka ngazi kuelekea chini. Nilishuka kwa mwendo wa kasi na sikukumbuka kama ile ilikuwa ghorofa ya kumi juu, ajabu sasa sikuchoka wala kupata dalili ya kuchoka.
Nilipofiuka ghorofa ya pili kwenda chini nikakumbuka jambo la msingi zaidi.
Pesa!! Yule mtu niliyemuacha anavuja damu pale chini alikuwa na pesa. Hapo hapo nikageuza na kupanda kazi, Jonas alikuwa analalamika lakini sikujali. Nikarejea kule chumba kwa tahadhari kubwa, nikaingia na kuchukua lile begi. Kwa mwendo wa haraka tena nikaanza kushuka zile ngazi, G nikikwambia kuwa huyu muhudumu aliyekuja kutuhudumia ni mzembe naomba uniamini, sawa baadaye niligundua kuwa nilichoka sana lakini cha muhimu ni kwamba nilishusha nikapandisha na nikashusha tena.
Mapokezi nilimkuta yule msichana wa mapokezi amelala, mlango ulikuwa umefungwa.
Nikamwamsha akaamka na kuniuliza kulikoni saa tisa usiku nahitaji kutoka.
“Nimegomaba na mpenzi wangu…hivyo tu..sitaki kuwa hapa tena.” Nilijibu kiujasiri. Akajizoazoa taratibu, nilitamani kumtusi lakini ningezua mengine na kumjengea wasiwasi, mwisho akanifungulia mlango nikatoka nikiwa na Jonas wangu mikononi. Na begi la pesa likiwa pamoja nasi.
Nikachukua taksi na kumuamuru dereva atupeleke Mbezi ya Kimara. Nikapekua lile begi nikavuta noti ya shilingi elfu kumi.
Nikampa dereva akakanyaga mafuta gari ikatoweka. Barabara ilikuwa tupu hadi tunafika Mbezi mwisho. Nikashuka bila kuonyesha wasiwasi wowote, na hapo nikaangaza huku na kule nikaona kibao kinachoonyesha nyumba ya kulala wageni, nikajongea huku nikitembea kijasiri sana.
Bahati ikawa upande wetu tena tukapata chumba, nikawalipa tukakabidhiwa chumba chetu. Humo ndani hata Jonas naye hakutaka kulala alikuwa na furaha sana na alikuwa akichekacheka, amakweli pesa sabuni ya roho.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nikahesabu mafungumafungu yote ya pesa na kufanikiwa kiwepesi kugundua kuwa jumla ilikuwa takribani milioni moja na laki tano.
Katika mahesabu hayo juu palikuwa na kikaratasi, kilikuwa na namba ya akaunti.
Jina lilikuwa la kampuni ya yule mfadhili wangu wa kutoka Mbeya!! Nilijisikia vibaya sana kwa kuwa zile pesa zilikuwa mikononi mwangu na ikiwa ni hasara kwa mtu aliyenifadhili, hapohapo nikajisafisha na kudai kuwa mimi si mkosefu wa kulaumiwa ni Rama.
Nililala nikiwa nimelikumbatia lile begi imara kabisa mikononi mwangu.
Asubuhi saa kumi na mbili nilimchukua Jonas mgongoni mwangu na kuondoka kuelekea barabarani ambapo tulisubiri mabasi yaendayo Mwanza yenye utaratibu wa kuchukua abiria barabarani.
Naam! Nikapata basi mimi na Jonas tukaingia humo na bahati nzuri zaidi tukapata nafasi ya kuketi. Nilikuwa nimeandaa pesa ya nauli tayari tayari hivyo sikulifungua tena lile begi.
Safari ikaendelea ya kuliacha jiji la Dar es salaam. Nilifumba macho yangu na kuduwaa ni kwa namna gani maisha yanaenda kasi namna ile, ndani ya juma moja tu yalikuwa yametokea mambo mengi sana katika maisha yangu. Nilikuwa nimepigana na familia ya mzee Aswile, nilikuwa nimekutana na mchungaji mnafiki Stephano, nilikuwa nimeponea tundu la sindano kukamatwana polisi, nililala nje jijini Mbeya, nilikutana na mkurugenzi wa mabasi na nilisafirishwa kuja Dar, nimekutana na Rama na tumefarakana nikamsukuma chini, sasa nina pesa nyingi na nipo safarini kuelekea jijini Mwanza. Safari ambayo sijui kwa nini naenda huko lakini ndo mji pekee ambao ulikuja ghafla katika kichwa changu. Wewe G wewe hivi unataka shida yako nisile chapatti zangu ama, mwee!! Nina njaa mwenzio tena nina njaa kweli.” Nadia alisema haya huku akifungua chupa ya chai, kisha akamimina katika vikombe vyote viwili, na hapo tukaanza kushughulika na mambo ya chai. Simulizi ile ikakaa kando.
****
“Kuna wanadamu wenyewe wameumbwa wakiwa na huruma tu, wameumbwa wakiwa na mioyo ya kujitolea tu, wana maisha magumu lakini wanapoweza kujitolea wanajitolea. Wanadamu kama hawa ni wachache sana, yaani wenyewe hali haziwabadili maana walipewa mioyo ya uaminifu, hakika uaminifu unaweza kumponza na kumpoteza kabisa mtu lakini hawa hawataki kujua kuhusu hayo kabisa.” Nadia alianza tena kusimulia baada ya kumaliza kunywa chai.
“Nilipofika Mwanza niliuhesabu kuwa mkoa ambao ulikuwa mbaya sana kwangu na mkoa ulionipa machungu mengi, lakini bado ilikuwa lazima nipite hapo ili niweze kufika mkoani Mara, wilaya ya Musoma. Kama kawaida tena nililala nyumba ya wageni, asubuni sana nilikuwa macho, kutazama saa ukutani ilikuwa ni saa kumi na moja na nusu.
Kuna mtu nilimuwaza kabla sijalal usiku uliopita hivyo nikaamua kwenda kumtafuta. Nilipenya huku na kule hadi nikaifikia nyumba aliyokuwa amepanga wakati ule. Nilikuwa na mashaka sana kuwa huenda aliwahi kuhama hivyo nilifanya kama kubahatisha.
Ajabu nilimkuta akiwa anaishi pale pale, niligonga mlango wake akaufungua, mwanzoni hakunitambua lakini baada ya sekunde kadhaa akanitambua. Akanirukia kwa nguvu na kunikumbatia, hakuamini hata kidogo kama ni mimi nilikuwa mbele yake. Huyu alikuwa ni yule dada ambaye wakati nikiwa baamedi niliwahi kuishi kwake, na ni huyu aliyekuwa wa mwisho kuniona jijini Mwanza wakati ule nikikabiliwa na kesi ya kumuua bosi wangu. Hata nilipoishi na Jesca kwa wiki kadhaa kabla hajanisaliti na kujikuta akiingia safari nyingine nami nyingine sikupata nafasi ya kwenda kuonana na dada yule. Lakini sasa alikuwa mtu wa muhimu sana kwangu.
Akanisikiliza vyema nikamueleza juu juu shida zangu, kubwa zaidi ilikuwa juu ya Jonas, nikamweleza kuwa nahitaji kuwa huru kiasi fulani katika kuzikabili changamoto kadhaa za maisha yangu kwa takribani siku kumi tu hivyo nilihitaji sana Jonas abaki naye pale halafu nikirejea nitamchukua. Yule dada hakupinga japo alijaribu kunieleza ugumu wa maisha alionao kwa kipindi kile, alikuwa hana kazi na aliishi kwa kubangaiza bangaiza hivyo hofu yake kuu ilikuwa ni kwa namna gani ataishi na Jonas. Nikakumbuka ile siku ananipatia shilingi elfu ishirini nikiwa naenda Musoma, alikuwa mpole na mwenye huruma na hata sasa alikuwa katika hali hiyo, huu ukawa wakati wangu wa kumwachia chochote kitu, nikajipekua katika ule mkoba nikatoa shilingi laki tatu na kumpatia kama matumizi, hakuamini kabisa akakodoa macho lakini nikamwondoa mashaka, nikamweleza kuwa naenda kufuatilia mali zangu nilizodhulumiwa Musoma.
Baada ya makubaliano nikambusu Jonas shavuni, na kumpa yule dada mkono wa heri tukaagana.
Majira ya saa kumi na mbili asubuhi hiyohiyo nilikuwa katika basi kuelekea Musoma. Sasa sikuwa na uoga tena moyoni, nilikuwa na kiasi cha pesa ambacho niliamini sitapata shida Musoma kwa namna yoyote, safari nzima niliwaza ni adhabu gani ambayo Desmund anayejiita muheshimiwa diwani anastahili, nikamuwazia pia mzee Matata ambaye alikuwa mtuhumiwa wangu wa kwanza kumuhisi kuwa alinbitupa katika domo la mamba na nikaokolewa kimiujiza. Huyu kama angekiri ni yeye ni hapo ningejua nini cha kumfanya.
Nilipofika Musoma nilinunua wigi jeusi na miwani nyeusi vilevile, nikaliweka kichwani, kisha nikaanza kutembea kwa kujiamini kabisa, sikutaka kulala kabisa, nikazunguka huku na kule hatimaye nikapata magari ya kukodisha. Tatizo lilikuwa moja sikuwa na mdhamini wa kuniwezesha kupewa gari lile mimi kama mimi, hivyo nilitakiwa kuwa na dereva wao ambaye atakuwa nami kila kona. Jambo hilo sikulitaka hata kidogo, nilihitaji kuwa peke yangu.
Nikaamua kuachana na magari ya kukodi, nikaamua kwenda moja kwa moja jirani na duka kubwa la mke wa Desmund, pale dukani hakuwepo yeye, nikaenda pale kama mnunuzi wa kawaida tu nikamkuta kijana wa kichaga, nikamchangamkia mara ninunue hiki mara kile ilimradi tu niweze kujua mambo kadhaa ambayo yangeweza kuja kunisaidia baada ya siku chache. Mara akaja mtoto mdogo pale, nikajifanya kustuka.
“Mh!! Mtoto wa muheshimiwa huyu ama…” nilijisemesha kama nisiyekuwa na athari.
“Mtoto wa mheshimiwa shangazi yangu.” Alinijibu bila kutilia maanani anachokijibu. Sikuendelea kuhoji juu ya jibu hilo badala yake nikahamia kwa yule mtoto.
Nikamsemesha semesha huku nikiwa mchangamfu sana na moyoni nikiwa na hasira kali, mtoto akawa ananijibu maswali yangu yote vizuri, akaniambia shule anayosoma akaniambia umri wake na mengine mengi.
Moyo uliniuma sana nikajisikia aibu kuu, kumbe Desmund alikuwa ana mtoto wakati nipo naye katika mahusiano, Desmund hakujali hata kidogo kilio changu juu ya lini tutapata mtoto wetu, kumbe nd’o maana alikuwa mwepesi kunibadilikia, kunipiga na kunisulubu awezavyo! Kumbe tayari ana mtoto wake wa kumzaa, hakika niliumia sana. Lakini mbele ya yule mtoto sikuacha kulitoa tabasamu langu.
Baada ya kulipia vikorokoro nilivyovinunua niliondoka pale.
Nikatafuta chumba nikajipumzisha huku nikiufikiria unyama wa Desmund ambaye anaheshimika kabisa kama diwani wa kata yake. Diwani mwongo, mtesaji na muuaji kabisa.
Desmund asiyejua uchungu wa mwenzake bali kujali masilahi yake, mwanaharamu kabisa asiyekuwa na chembe ya huruma wananchi wakamchagua aiongoze kata yao tena baada ya kumuua aliyekuwa diwani mtiifu.
Siku nzima sikutia chochote mdomoni, hivyo usiku huo nilijilazimisha kuonja chakula, kisha nikalala, kama kawaida begi langu likiwa kitu cha muhimu zaidi.
Siku iliyofuata majira ya saa nne nilikuwa nimechanganyikana na watoto wadogo wa shule fulani hivi ya mtu binafsi. Nilikuwa nawauliza maswali kadha wa kadha na kisha huku nikitazama huku na huko kama nitaweza kuiona damu ya Desmund.
Naam! Nikafanikiwa kumuona yule mtoto, uzuri wa watoto akishakuamini mara moja basi yatosha. Aliponiona akanikumbuka na kunikimbilia akiwa na wenzake, nikawapa senti kidogo kisha nikabaki na yule mtoto peke yake. Ili kuondoa utata nikaenda katika uongozi nikajitambulisha kama shangazi yake na yule mtoto ambaye aliniambia kuwa alikuwa anaitwa Desmund Juniour. Jina baya kupita yote katika akili yangu.
Walimu hawakuwa na shaka nilipowaeleza naenda kumnunulia chai mara moja, kwa sababu mtoto mwenyewe alionyesha kunijua basi hawakuwa na swali.
“Mama yake leo amechelewa kweli huwa hakosi kupita au ndo amekuagiza.” Mwalimu mmoja aliniambia.
“Hapana nadhani ametingwa tu maana yule dah simuwezi.” Nilidanganya na upesi nikaondoka na yule mtoto, nikiwa katika tahadhari kubwa maana kauli ya kuwa mama mtoto huwa anakuja mida kama hiyo ilinishtua.
“Gari ya mama ileee.” Tukiwa nje yule mtoto alinionyesha kwa kidole gari iliyokuwa inaingia pale shuleni. Akimaanisha ni ya mama yake, nikazidisha mwendo na kukata kona mbili tatu. Sikutaka kupoteza muda zaidi, nikafanya nilichopanga, nikampa yule mtoto pipi, akaidaka na kuitupia mdomoni, baada ya dakika ishirini nilikuwa nimetoa kanga na alikuwa mgongoni kwangu kama mwanangu wa kumzaa vile amelala hoi. Hatua ya kwanza ilikuwa imefanikiwa kwa kiasi kikubwa
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alipokuja kustuka alikuwa kitandani, nikamchukua na kumwogesha aliniuliza maswali nikamjibu vyema na kumtaka awe mtulivu kabisa.Alilala Musoma na sasa ameamka akiwa jijini Mwanza. Harakati zangu zilienda kwa usahihi sana.
Nia yangu ya kumnyanyasa Desmund na mkewe kimawazo ilikuwa inatimia sasa, nilijua watahangaika sana na mwisho watajiona hawana thamani yoyote katika maisha yao.
Namba ya Desmund ilikuwa kichwani mwangu na bado sikutaka kuwasiliana naye. Cha muhimu zaidi nilitaka ateseke hadi nafsi yangu iridhike.” Nadia akakomea hapa, uchovu ulikuwa umemshika akaaga na kwenda chumbani mwake. Mimi nilipojilaza kidogo nikapitiwa na usingizi kwa sababu usiku kucha nililala kwa kujibana sana katika kochi.
Nilikuwa naamini sasa mwisho wa simulizi unakaribia kwa sababu tayari Desmund alishaanza kuguswa pabaya.
Nikasubiri kwa hamu kabisa siku ambayo Nadia ataendelea kusimulia ili nijue aliishia wapi katika harakati zake hizo.
Nilikuja kushtuka mchana jua likiwa kali kabisa, nilitaka kwenda chumbani mwa Nadia lakini nikasita na kuamua kupiga simu ya chumbani mwake, iliita bila kupokelewa. Nikajua na yeye atakuwa katika dimbwi la usingizi mzito kabisa kama mimi nikapuuzia na kuendelea kulala.
Majira ya jioni nikapata cha kuingia chumbani mwa Nadia. Ni kumchukua twende kupata chakula na pia kujiandaa kwa safari ya kwenda jijini Dar es salaam kwa ajili ya kumtimizia ndoto zake za kuwa huru tena na mwenye furaha.
Nilifika nikakigonga chumba chake lakini hakujibu kitu, hii haikuwa kawaida ya Nadia hata kidogo, nikaamua kufungua, kitasa kikafunguka vizuri tu!! Kuingia chumbani hapakuwa na mtu. Lakini kitandani palikuwa na ujumbe mfupi.
“Nimetoka kidogo!!” ujumbe huu ulinishangaza, yawezekana vipi Nadia kutoka peke yake katika jiji hilo la Mwanza tangu nifike naye pale, hapa nikapata walakini. Nikajiuliza nichukue hatua gani lakini sikupata namna ya kufanya. Mara macho yangu yakakutana na rekoda yangu!!
Nikaduwaa imefika vipi pale ndani, wasiwasi ukaniingia maana hadi ninaposinzia ilikuwa katika chumba changu.
Nikaichukua na kutazama, nikakuta kuna kitu kimeongezeka katika ile reekoda, mara ya mwisho nilikuwa nimerekoda kwa masaa nane, lakini sasa yalikuwa masaa tisa. Hivyo kuna jambo la ziada.
HAKIKA katika maisha unatakiwa kujifunza na kukubaliana na ukweli kuwa moyo wa mtu ni fumbo gumu kabisa, fumbo lisilofumbuliwa kirahisi. Kuna jambo Nadia alikuwa amelihifadhi katika moyo wake ambalo sikulijua na mbaya zaidi ulikuwa mpango wake wa siku nyingi.
Nikaiwasha ile rekoda kuanzia pale nilipoishia yaani saa moja nyuma.
Nikakutana na sauti ileile ya Nadia.
“Gerlad Iron! Mwandishi mpole, msikivu muelewa mnyeyekevu na mwenye huruma, natamani sana moyo wako ungeukata kidogo na kuwagawia akina Desmund maana wapo wengi duniani. Naamini unahitaji sana kunisaidia huku ukihitaji pia kujua kila kitu kuhusu mimi. Lakini sina maana hata ukinisaidia mimi.
Mara ya mwisho kuzungumza nawe nilichoka ghafla kwa sababu tu sipendi kabisa kukumbuka kilichokuja kutokea katika maisha yangu! Sitaki kukumbuka machungu na maasi yangu.
Ni kweli nilifanikiwa kumteka mtoto wa Desmund na kumuhifadhi jijini Mwanza, hiyo kwangu ilikuwa hatua kubwa Desmund alitetemeka kama mtoto mdogo na bado hakujua kama ni mimi nahusika, baada ya kumweka mtoto Mwanza nyumbani kwa dada yangu aliyekuwa akiishi na Jonas niliamua kurejea Musoma tenma kwenda kukabiliana na Desmund, hakika walikuwa wamefadhaika sana na duka lilifunguliwa na yule kijana wa kichaga, mkewe Desmund hakugusa kabisa pale, nilipoonana na yule mchaga alinieleza kuwa kale katoto kamepotea katika njia za kishirikina, nilitabasamu huku nikiyasikitikia mawazo yao. Nikiwa Musoma nilikutana na kundi moja la wahuni likijiita WEST LAWAMA, nilizungumza nao vyema, hawa nikawaagiza kijijini kwao Desmund kule alipokuwa anaishi mama yake, huku nilihitaji jambo moja tu la kuiteketeza akili ya Desmund zaid, nilihitaji waichome ile nyumba. Hilo halikuwa na shida hata kidogo biashara ilienda vizuri sana, Desmund akazidi kupagawa. Bado nilienda mbele zaidi kutuliza kidonda changu moyoni, nikawaagiza wapeleleze ni wapi nyumbani kwa mke wa Desmund, upesi wakapapata, nikawalipa na huku wakateketeza, bahati mbaya kwake na bahati nzuri kwangu, wadogo zake mke wa Desmund wawili waliteketea katika moto. Sikuwa na huruma hata kidogo maana nimelaniwa, nisingeweza kukusimulia haya nikiwa nakutazama maana mimi ni zaidi ya shetani kwa malipo haya, malipo yaliyokuwa yakinifariji moyo wangu.
Baada ya hapo nikaenda nyumbani kwa Desmund mida ambayo nilijua kabisa kuwa hayuipo nyumbani, nikaacha ujumbe kwa mlinzi kuwa ‘AKIJA MWAMBIE MWENYE NYUMA ALIKUJA’, nadhani aliupata ujumbe ule na bado akaupuuzia ni hapo nikampa tena pigo jingine, pesa niliyokuwanayo zaidi ya kula na kulala haikuwa na kazi nyingine ile, hivyo nikaendelea kuitumia vilivyo. Mdogo wake Desmund wa kiume aliyekuwa akiishi naye akacharangwa mapanga vibaya sana lakini hawakumuua, nami nilitaka iwe hivyo. Wakamuachia ujumbe kuwa mwenye mali anataka mali zake. Ujumbe alioufikisha kwa kaka yake bila shaka.
Diwani akazidi kukonda, diwani akapagawa. Nikaifurahia hali hiyo.
Mwandishi, ujue sikupanga kabisa kumdhuru Desmund wala mkewe baada ya adhabu hiyo, badala yake nilitaka anipe mali zangu hata nusu nijiondokee kwenda ninapojua lakini si kumdhuru, nilikuwa nina tatizo la kuwa na huruma sana. Hiyo ilikuwa mbaya sana kwangu.
Lakini mawazo yalibadilika ghafla na kujikuta nikifanya kitu nisichokitarajia hata kidogo.
Siku hiyo niliamua kwenda nyumbani kwa Desmund siku niliyoamini kuwa alikuwepo nyumbani yeye na mkewe.
Niliingia hadi ndani baada ya mlinzi kuambniwa aniruhusu. Nikaingia katika nyumba ya Desmund na mkewe, walikuwa wameketi wakiwa wanatazama luninga lakini hawakuwa wameitilia maanani sana.
Desmund alishtuka sana kuniona nikiwa pale, alitaka kupiga mayowe lakini nikawahi kumwambia akae kimya.
“Maonyo yangu unayapata ama huyapati.” Nilimweleza na kisha kabla hajafanya lolote nikamuonya, “Ukithubutu kuleta ujuaji wako, nyumba hii itachomwa moto dakika hii na utafia humu ndani wewe na hiki kikaragosi chako.” Niliongea kwa ujasiri sana na wote walitetemeka.
“Nadia tafadhali nakuomba sema chochote nitakupa, lakini unipe mwanangu Nadia.” Alinisihi kwa sauti ya huruma sana.
“Mali zangu unanipa ama hunipi wakati huu, ama ndo hunijui tena mimi ni nani.’ Nilimuuliza bado nikiwa nimesimama.
“Nadia nakupa kila kitu utakachotaka.” Aliendelea kunisihi kwa huruma.
“Desmund naondoka muda huu nitarejea baada ya siku tatu, nahitaji nikute nyumba hii ipo mnadani, uiuze, vitu vya dukani uviuze, gari uliuze na bila shaka haitakuwa chini ya miloni miambili mezani. Nitaichukua hiyo na utampata mtoto wako, lakini vinginevyo, nitaanza na kile kiuchafu chako nitanyonga, halafu wewe na huyu mjinga mwenzio nita..” kabla sijamaliza kuongea yule mwanamke akaja kunikabili kwa jazba akilalamika eti nimemtusi sana. Pole yake hakujua mimi ni wa aina gani kwa wakati huo, alikutana na teke moja maridhawa akaangukia kwenye viti huko akatokwa na yowe la hofu, Desmund akamkanya asiniguse. Nikaondoka na kuahidi kurejea baada ya siku hizo tatu.
Niliondoka pale na kuchukua mabasi kwa safari ya Mwanza, kila abiria alikuwa akizungumzia habari ambayo nilikuwa siijui lakini nilipolikanyaga jiji ndipo nikaamini laana yangu inashambulia hadi watu wasiohusika.
Jiji la Mwanza lilikuwa limekumbwa na mafuriko, nyumba ziliezuliwqa na nyingine kusombwa na maji, hali ilikuwa mbaya. Sikuishughulisha akili yangu kuwaza juu ya familia yangu kwa wakati huo, yaani Jonas na Desmund Jr. lakini akili ilichanganyikiwa baada ya kukuta eneo alilokuwa akiishi yule dada na wale watoto nyumba zikiwa zimemezwa na maji. Nilifanikiwa kuonana na jamaa yake yule dada.
“Mvua imeondoka na dada yangu jamaniii…” aliugulia, nikakosa la kusema.
“Na vile vitoto masikini vimekufa vikiwa vimekumbatiana naye, jamani aah!! Dada weee!!” alianza kulia, nikaungana naye kwa uchungu mkubwa, nikiwa nimepagawa kabisa nakujiuliza kama ni kweli nayasikia maneno yale ama la!! Nilikuwa naota….hapakuwa na ndoto pale hali ilikuwa halisi kabisa. Nikaongozana na yule kijana hadi Bugando mochwari tukajieleza na kisha tukaonyeshwa maiti zile. Hakika alikuwa ni Jonas na yule mwingine alikuwa ni Desmund jr.
Mwandishi sikuwahi kushikwa na uchungu wa moja kwa moja moyoni namna ile katika misiba lakini msiba huu ulinichanganya na kujina mimi sina haki ya kuishi kabisa, nilijiona niliyelaaniwa na laana yangu inaishi nami. Nikaamua kurejea Musoma baada ya kuwazika watoto wale, nikamkabili Desmund, alikuwa ndani ya nyumba ileile lakini milioni mia mbili zilikuwepo mezani.
Nikahitaji kujua ni kipi chanzo zcha yeye kunitenda vile hadi kunisababishia laana.
Desmund alinisimulia mkasa juu ya baba yake mzazi alivyodhulumiwa mali na mzee wa kiarabu, akaelezea juu ya mzee huyo kumuua baba yake mzazi mbele ya macho yake yeye akiwa bado mdogo, hali hiyo ikamfanya awe na chuki na ngozi hii, baada ya kuamua kuendelea na maisha akaajiliwa na mwarabu huku napo akajikuta anateswa sana huku akizidi kupoteza uelekeao wa maisha, hiyo haikuwa simulizi pekee bali akaenda mbali zaidi na kunieleza juu ya kifo cha dada yake ambaye aliolewa na mwarabu licha ya yeye kumzuia, dada akayavumilia mengi ya ndoa lakini siku ya kukata roho akamweleza Desmund kuwa yule mwarabu alikuwa anamlawiti mara kwa mara, hivyo anakufa kwa sababu alikuwa anatendwa vibaya. Nilijisikia vibaya kumwona Desmund akliwa analia kwa uchungu huku akiikumbatia picha ya dada yake lakini nilijikaza nisidondoshe machozi kwani ungekuwa udhaifu wa hali ya juu.
Desmund akakiri kuwa alivurugwa akili kabisa na ngozi hiyo na hata ndugu zake na marafiki wa karibu walijikuta wakiichukia ngozi ile. Naam!! Desmund akanichukia na mimi na kuamua kutulizia maumivu yake huku. Nilimwelewa Desmund na sikutaka kumweleza zaidi juu ya upendo wangu kwake katika kipindi hicho. Sasa alikuwa amechelewa sana kunitaka radhi, nikambana na maswali juu ya nani alimuua Danny yule askari, akajibaraguza lakini baadaye akakiri kuwa angeweza kumdhuru mtu yeyote ambaye angeweza kunitetea, hivyo Danny alikosea kunitetea. Desmund alimuua Danny. Hasira zikanichemka nilipokikumbuka kifo cha Danny mtetezi wangu.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hapa sasa nikaamua kufanya nililotaka kufanya, nikamkabili Desmund aliyekonda klidhaifu kabisa nikachomoa kisu changu na kukisukumiza katika mbavu zake, aliga kelele nikawa kumziba mdomo. Niliona mwanaume huyu hakufaa kuishi hata kidogo na sikutaka kuwa na udhaifu kama ule wa Jesca wa kumchekea adui. Aliyefuata baada ya pale ni mkewe, huyu alipoingia ndani tu nikamkaba, hata sikutumia kisu, nilimnyonga hadi akapoteza uhai. Nafsi yangu ikapata ahueni. Wataishi vipi watu hawa wabaya wakati kitoto kisichojua lolote kimekufa huko Mwanza kwa makosa ya wazazi wao.
Nikaunganisha safari yangu moja kwa moja hadi nyumbani kwa Mzee Matata, nikamuulizia hakuwa anapatikana tena hapo, lakini si hapo tu hata ulimwenguni hakuwa anapatikana, mzee Matata alikuwa marehemu, alikufa kwa kupigwa risasi. Waliompiga hawakujulikana.
Wamenisaidia hao!! Nilijisemea na kujiaminisha kuwa ni mzee huyu aliyeniteka na kunitupa katika dimbwi la kuwa msafirishaji wa madawa ya kulevya .
Nilipomaliza hapo, nilikuwa nimechakaa nafsi na sikujua kabisa kama nilikuwa nina chochote cha kufanya duniani, milioni mia mbili hazikuwa na maana yoyote kwangu nikaziacha nyumbani kwa Desmund.
Nikaondoka kwa nia moja tu ya kujiua, na hapo ndipo nikakutana nawe kichakani usiku ule mkiwa mmeharibikiwa damu, ukanisihi sana hadi nikaamua kufuatana nanyi, hakika unayo lugha ya ushawishi sana, uliweza kunibadili mawazo yangu, umeweza kunifanya mtu mwingine tena na kujikuta natabasamu mara kwa mara. Uliponichukua sikuamini kama nitakuamini hata kidogo, lakini umekuwa wa pekee sana kwangu, lakini kitu kimoja tu, sihitaji twende wote Dar es salaam mimi nina mikosi sitaki kukuambukiza mikosi yangu, sitaki maafa yaliyolikumba jiji la Mwanza yahamie pia Dar es salaam, hii yatosha.
Wewe ni mshauri mzuri sana tena mwenye ushawishi sasa nahofia kuwa katika maamuzi haya ningekushirikisha lazima ungeyabadili mawazo yangu tu hiyo lazima ingetokea.
Ni kweli labda kuna maswali yako mengi sijayajibu, hii yote labda ni kwa sababu ya uchovu wa akili na msongo wa mawazo vilevile, kama utabaki na maswali naamini hautapata nafasi ya kuyasikia nikiyajibu, si kwamba hatutaonana tena ama labda niseme si kwamba hautaniona tena bali utaniona lakini hakika sitakuwa tayari kusema lolote lile. Najua wewe ni bingwa wa kusihi na kubembeleza lakini sitabembelezeka katika hilo niliyokueleza yanatosha sana, yasambaze katika dunia, mimi Nadia nimekubali kuwa mfano kwa wasichana na wanadamu wenzangu usiogope kusema ukweli kama nililawitiwa, usifiche juu ya shughuli za usafirishaji madawa kuwa muwazi kama nilivyokuwa muwazi kwako. Gerlad Iron baki na sauti hii milele, iishi sauti hii kizazi hadi kizazi, tone la chozi langu wasimulie wahangaikaji wa dunia, kwikwi yangu iwe funzo kwao na amani ya bwana iwe nawe G katika lolote lile utakalofanya na limpendeze Mungu!!! Uwe na amani. Tutaonana inshalah!!”
Sauti ya Nadia ilimaliza na ule ukawa mwisho wa kurekodi, nilivaa viatu vyangu upesi upesi huku nikiamini kuwa natakiwa kwenda mahali lakini ni wapi ningeenda, nikawa mnyonge na kukaa chini tena. Nikajipa moyo kuwa huenda Nadia atarudi jioni. Hadi kufikia saa kumi na mbili bado mambo yalikuwa yaleyale. Lakini saa moja Nadia alirejea!!
Hakika alirejea chumbani lakini katika namna ambayo alikuwa ameahidi, hakuwa Nadia ninayeweza kumshika na kumliwaza bali alikuwa Nadia katika luninga akiwa ametulia tuli waandishi wa habari wakimpiga picha.
Nadia alikuwa amejinyonga!!!
Niliishiwa nguvu nikabaki kukodoa macho tu..mwandishi yule aliyeisoma habari hiyo kwa majonzi alipiga nyundo ya mwisho kwa kusema kuwa, marehemu aliacha ujumbe mfupi sana wenye majina mawili.
“Nadia Gerlad”, hapo nikazidi kusisimka na kupagawa zaidi. Lakini sikuwa na ujanja kifo hakina mbadala, alikufa na inabaki hivyo kuwa alikufa.
Kumbe Nadia alipanga kujiua!! Nilijiuliza lakini nani angenijibu!! Hakuna wa kunijibu!!
Nikapitiwa na usingizi, kesho yake nikaamkia kituo cha polisi kutoa taarifa kuwa Nadia ni dada yangu!! Wakanielewa na nikapewa ruhusa ya kuuchukua mwili.
Nilifanikiwa kuuchukua na kufuata hatua zote, Nadia akasafirishwa kuelekea jijini Dar es salaam, familia yangu ambayo ilikuwa na taarifa tayari iliupokea mwili wa Nadia, kisha mimi nilifika siku moja baadaye. Nadia akazikwa kwa heshima zote kama ndugu katika familia yetu.
Kampuni iliyoniajiri ilijumuika nasi katika msiba huu huku kila mmoja akingojea kusikia ni kitu gani nilivuna kwa miezi yote hiyo tangu nikutane na Nadia.
Baada ya siku arobaini, niliibuka hadharani nikiwa na kila kitu kuhusiana na Nadia, sauti na baadhi ya picha.
Kila mwenye moyo wa nyama aliposikia juu ya Nadia alitokwa na machozi. Wengi walijifunza kutokana na simulizi ya Nadia
Kuna kipindi nilikuwa najiuliza hivi ni kweli nilikutana na Nadia, na hapo nikajikuta naisikiliza sauti yake tena na tena huku nikizitazama picha zake nilizowahi kumpiga.
Mwisho nikaibuka na kitabu kikubwa cha simulizi nilichokipa jina la USILIE NADIA…kitabu kilichokuwa maalumu kwa msichana aliyesota ulimwenguni kupigania haki yake na mwisho akatoweka akiwa amelipiza kisasi!!!
NADIA BARGHASH!!! Aliyeishi pia kwa jina la MARIAM na baadaye MAMA JONAS huku akiamua kufa kwa jina la NADIA GERLAD!!!!
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
MWISHOOO!!!
0 comments:
Post a Comment