Search This Blog

Sunday, July 10, 2022

NDOA YANGU INANITESA - 1

 





    IMEANDIKWA NA : ADINANI K. KWANGAYA



    *********************************************************************************



    Simulizi : Ndoa Yangu Inanitesa

    Sehemu Ya Kwanza (1)







    Nilikuwa nikifanya kazi katika kampuni moja ya usafirishaji wa madini kutoka Tanzania kupeleka Bang kok nchini Thailand. Kampuni yetu ikiwa ya mtu binafsi na ilikuwa Mkoani Arusha. Mimi Sweedy Kachenje ndiye niliyekuwa idara ya usafirishaji, nikiwa afisa mauzo.

    Katika maisha yangu yote nilitegemea sana na nilihitaji kuwa na mwenzi wa kuishi naye, kama vile familia nyingine bora ambazo kila siku zina furaha na ridhaa. Kwa kila mmoja kuwa mwanandani wa mwenzake. Pia nilimuomba mungu kwa kila hali si kanisani na hata nikiwa katika mapumziko yangu, anipatie mwanamke ambaye angenifaa katika maisha yangu.Kila siku palipokucha,niliamka nikiwa na wazo la kumpata nimpendaye na anipendaye.Niliamini hivyo japo sikuwa na uhakika kama kweli ningepata mtu kama huyo maishani mwangu.

    Siku zote nilijibidisha kuwa mfano bora ili niweze kupata mchumba, nilikuwa mtiifu, nikiwa heshimu wenzangu na kushirikiana nao vema kujenga Taifa.Kujaribu kuwa na marafiki wengi wa jinsia tofauti. Nilijitahidi nikihisi pengine wale marafiki wangenifaa kumbahatisha wa ubani wangu. Pamoja na yote hayo sikuweza kubahatika kupata niliyempenda kutoka moyoni, na aliyenipenda. Nilizidi kumuomba Mungu anishushie neema ya kumpata wa ubani wangu. Ikafikia wakati nikaomba ushauri, lakini wale niliowaomba ushauri walionekana kuwa fukara wa mawazo.Walinishauri wakisema kuoa ni kuoa.Eti mwanamke ningemfunza kama angekuwa na tabia mbaya.Nikafikiri mara mia mia ushauri wao nikaona haukuwa na maana zaidi ya upofu.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Bw. Kachenje inamaana uwingi wa wanawake ulimwenguni umekosa umpendaye?”Lilikuwa swali nililoulizwa na rafiki yangu.Hatahivyo nilishinda kumjibu na hatimaye nikamdharau.

    “Inamaana kuchagua mke wa kuishinae ni sawa na kuokota fungu la samaki sokoni ama vipi?”Nilijiuliza bila kujijibu kwa wakati huo.

    Nilishindwa kuokota mke ilimradi mke kama vile mtu anavyookota nyanya sokoni na kulipa pesa, nafikiri hata anayeokota nyanya nae huchagua. Japo kuna usemi usemao mchagua nazi hupata koroma usemi huo niliupinga na kuutupilia mbali. Niliamini usemi wa kuoa ni kuoa pengine ningefanya hivyo basi ndoa yangu isinge kuwa na ladha ya unyumba na isingedumu maishani.

    Nilijawa na imani kuwa mke mwema hupewa na Mungu, niliishi kwa matumaini ya Mungu na nilitegemea msaada mkubwa kutoka kwake. Wazazi wangu Mungu aliwapa baraka walikuwa hai wakinisubiri nioe wamuone mkwe na wajukuu wao kabla ya kufa. Kwa bahati mbaya sikuweza kupewa upeo wa kuona mchumba mwema ambaye angekuwa mke wangu, japo nilikuwa na kazi nzuri na nafasi yangu kazini ilinifanya nionekane maridadi saa zote.

    Watu wengi walioniona walinishangaa sana, kwani sikuwahi kuonekana na mwanamke yoyote niliyeongozana naye katika maisha yangu. Si kwamba nilikuwa na hitilafu yoyote mwilini!. Hapana nilikuwa mwanaume rijali, na sikupenda kujihusisha na ngono,kwani magonjwa yamezagaa kama inzi kwenye mzoga.Licha ya magonjwa, ni dhambi kubwa kuzini nje ya ndoa.Nilitambua kwamba jambo hilo halimfurahishi muumba hata kidogo.Siku zote nilikuwa nikijilaumu,ikafikia wakati nikitaka kuokota mwanamke hata baa, moyo ukasita ukinitaka niwe na subira zaidi.Lakini subira gani huumiza matumbo. Je subira hii itazaa matunda ama nikunizidishia bala uzeeni?.Nikayatupilia mbali mawazo potofu. Nilihitaji kuwa na subira nikihisi pengine ningempata atakaye nipenda na mimi kumpenda.

    Umri wangu ulisogea kufikia miaka arobaini. Hali ambayo iliwaogopesha sana wazazi wangu, waliokuwa wazee wa kujikongoja. Nilizaliwa mtoto pekee wa kiume na dada zangu watatu.

    Wazazi wangu walichoka na maneno yangu. “Bado umri wa kuona. Nitaoa Mungu akipenda, mke mwema hupewa na Mungu” Miaka yote huwa nilikuwa najitetea hivyo .

    Ulifika wakati baba na mama walitaka kuniachia laana baada ya kuwadanganya zaidi ya miaka kumi toka nipate pesa na kuwajengea nyumba. Walitaka wawaone wajukuu wao kabla ya kufariki, walijua umri walio kuwa nao,wasingeishi miaka mitano ama saba mbeleni wangepoteza maisha.

    Kwa kuwaridhisha na kukwepa radhi za wazazi niliwaomba wanitafutie Mke. Niliamini mke ambaye ningepewa na wazazi angenifaa maishani. “Baba akimpenda binti, hata mimi sina budi kumpenda” nilijisemea mwenyewe baada ya kuwapa kazi ya kunichagulia msichana mwenye sifa zote zile mwanamke anatakiwa kuwa nazo. Ni miongoni mwa nidhamu kwa mume. Nilikuwa na furaha kidogo, kwani nilijiona niliyejaa Ukungu wa kutopendwa na kutopenda.

    Kwa ujumla sikujua ilikuwa ni mitihani ya Mungu kwani mimi ni miongoni mwa vijana waliokuwa wakicheka vijana waliochaguliwa wachumba na wazazi wao, hakuna kitendo nilichokichukia kama kuchaguliwa msichana na wazazi. Nilikuwa na imani ya kijana akichaguliwa mke basi hata ndoa ingejaa migogoro isiyoisha na pengine ikavunjika.

    **********



    Kampuni yetu iliitwa JOPHU MINING TRANSPORT CO LTD, mwenye Kampuni yetu, alijulikana kwa jina la Mzee Jophu Kundy . Ndiye alikuwa Mkurugenzi na mmiliki wa Kampuni.

    Kipindi cha miaka ya sabini kulikuwa hakuna gonjwa la Ukimwi, kama lilikuwepo basi ilikuwa halijajulikana kama sasa. Nilikuwa nikienda Nchi Thailand kila wiki kuuza madini aina ya Tanzanite. Siku zote nilikuwa na urafiki wa karibu na mmiliki wetu Mzee Jophu. Hakuna hata mtu mmoja aliyethubutu kuongea na mzee Jophu aliyeonekana mwenye uso wa ukali saa zote. Haikuwahi kupita siku bila mzee Jophu kuita “Sweedy njoo” nk.Alikuwa kazoea jina langu , pia alinipenda kama mwanae.

    Siku moja niliondoka katika uwanja wa Kia (Kilimanjaro International Airport) nikielekea Nchini Thailand, Bang kok.Vaaa yangu toshani kielelezo kwa mtu asiyenifahamu,kusema mimi ni mtu mwenye pesa za kunifanya niitwe tajiri. Nilivaa suti ya kijivu,chini nilivalia viatu vya mchongoko,vijana wa sasa huviita ‘Mkuki moyoni’,mkono wa kushoto nilishikilia ‘breefcase’lililojaa madini ya Tanzanite.Pia nilivalia miwani ya jua,iliyosababisha vigumu kuona macho yangu.

    Nilikuwa nimebeba madini gram 5000gm. Sawa sawa na kilo tano Kg 5. Kilo mbili ilikuwa ni rangi ya blue colour A na kilo tatu (3kg) yalikuwa ni rangi ya mkojo, kwa wale wakazi wa Mererani wanajua vizuri wakiona na rangi ya coke ile maji ya kunywa ilikuwa (gm 50).

    Ndege iliacha aridhi ya Tanzania mnamo saa nne unusu asubuhi, ambako ilichanja mawimbi angani saa mbili na sekunde ya kumi iltua uwanja wa kimataifa Bang kok.Nilifanikiwa kushuka salama nikiwa mtu wa tano. Sikuweza kwenda kwenye soko siku hiyo, nilielekea kwenye maegesho ya gari za kukodi amabako nilikodi gari.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Halo.kutoka hapa hadi Care lodge ni kiasi gani cha pesa?”

    “Dola tano.Karibu”

    “Sikuweza kubishana sana kwani niliamini kauli ya ‘nipunguzie bwana’ ni huku kwetu.Alinifungulia mlango wa mbele, nilivuta mguu wangu wa kulia na kuingia ndani mlango wa mbele kulia mwa dereva.Gari hilo lilikuwa ‘Left hand’.Nilienda moja kwa moja kwenye hoteli iliyoitwa CARE LODRGE .Dereva alitumia kama dakika nne kuingia lango la hoteli hiyo.Nilipofika, nilimlipa ujira wake, nikaelekea ofisi za kupokelea wageni(Mapokezi). Sikutaka kwenda kufanya biashara kwa wakati huo. Niliamua kujipumzisha kutokana na uchovu wa safari, jambo la kushangaza nilichokiona mbele ya macho yangu sikuweza kuamini macho yangu kama yalikuwa sawa sawa ama vipi, nilijaribu kupikicha macho pengine ni ule ukungu wa kutokuwahi kupenda. Lakini cha ajabu moyo wangu ulisimama kama sekunde kadhaa, kisha ukaendelea mapigo yake yakawa ya taratibu mno, ambayo sikuweza hata kuyasikia. Nilihisi jasho jepesi likitiririka, kwanza nilijitazama kisha nikamtazama mtu huyo, hata hivyo sikuamini kwamba kwa uzuri wake kamwe ningependwa mtu mweusi tena Mtanzania?.

    Niliona mwanadada mmoja aliyekuwa amekaa karibu na muhudumu wa mapokezi katika hoteli hiyo, msichana huyo alikuwa Mzungu si mzungu, muhindi si muhindi, mwarabu si mwarabu hata kwenye weusi hakuwepo. Baada ya dakika tano, nikiwa nimemtumbulia jicho la matamanio, alinisalimia .

    “Kaka habari yako”

    “Nzuri, sijui nyie”nilijibu salamu kwa wote,nikiwa bado sijabandua jicho usoni mwake.Sikushughulika na huyu mwingine,macho yangu tayari yalishapata chakula.Nilimtizama hamu haikuniisha nikatabani abaki pale pale macho yangu ya shibe.

    “Mimi mzima”aliitikia msichana huyo na aliyefuata ni wamapokezi.

    “Hata mimi mzima pia” walinisalimia.

    Sikupenda kukaa na ule mzigo wenye thamani kubwa niliandikisha jina langu na kuchukua chumba namba kumi.Kila nilipotaka kuondoka kuelekea chumba nilicholipia ,nilisita na kubakia mdomo wazi,mwili ulibweteka nikitamani kufahamiana zaidi na mwanadada yule.Niliamua kujilazimiza kuondoka ingawa nafisi ilitukutika,nilipofungua mlango wangu,niligeuka kumtizama yule mlimbwendekama vile nikihakikisha kama atakuwa pale.Nilimuona nae akinitizama.

    “Mtoto mtoto,Duu!.Tembea uone mengi”Niliongea akilini nikiwa nafungua mlango,katika kuzungusha funguo mlango ukatii sheria ,ukanipa nafasi ya kuingia.Nilihifadhi Breefcase yangu haraka na kufungua mlango kutoka nje.Nilikuwa nimeshikilia funguo,nikajikuta nikiziachia bila kujijua.Yote ni baada ya kumwona yule binti akiwa ametoka chumba kilichokuwa mkabala na changu.

    “Kumbe chumba nilichochukua kilikuwa karibu na chumba cha Binti yule niliyesalimiana nae muda mfupi tangu nifike pale.”Nilijisemea moyoni kiwa nimeacha mdomo wazi ,nikimtizama ,alikuwa kajifunga taulo nyepesi kabisa.Tayari kwa sasa alikuwa kanipa mgongo,kila alipovuta hatua , makalio yake yalitikisikia kama mawimbi ya maji baharini.Miguu yake minene iliyobeba umbile la wastani lilijivuta kwa madaha.Nilijikuta nikimtizama hadi alipoishia.

    Kwa kweli nilimpenda na niliamini angenifaa kuwa mwezi wangu na pambo la ndani. Hata hivyo niliumia moyoni je kama akinikubali nitafanya nini kama baba na mama watakuwa wamenipatia mchumba wa kumuoa?.Wazo hilo lilinijia na nikaamua kulitupilia mbali. Lakini ngoja nisiumize kichwa sijui nitakubaliwa au laa! Kwani nitese nafsi yangu? Nilizidi kuwaza wakati namalizia kufunga chumba. Pasipo kutegemea mara nambona tena akiwa kashikilia mafuta ya lotion. Safari hii alikuwa anakuja kwa mbele,niliweza kufaidi kuisawiri sura yake vema, ilioonyesha umahiri wa muumba.Tembe yake ungeweza kudhania kachoka vile,lakini hapana ukweli halisi.Ule ndio mwendo wake halisi,ikafikia hatua nikadhani hakanyagi chini, kwa jinsi alivyotembea utafikiri anaionea aridhi huruma. Nikajikuta moyo ukinipasuka “paaa” nikiwa na mshangaa nae alinitolea tabasamu nono! lililoshamiri usoni mwake.Tena likiwa limeambatana na mwanya mzuri.Nilishikwa na butwaa kama dakika kadhaa, nikajikuta ubongo ukifa ganzi. Tulibaki macho pima, hapo nilijua dhahiri kama kunapimana hivi.Nikajitizama na kumtizama kwa mara ya pili. Mapigo y a moyo yakaanza kupungua.Hata hivyo nilishindwa kuvumilia yote niliyoyaona kwa safari hii.

    “Samahani dada naweza kujua jina lako”alikuwa kesha nikaribia.

    “Yaa!. Jina langu ni Jeniffer John”

    “Sawa . Ahsante unajina zuri. Naitwa Sweedy Kachenje” nilijitambulisha nikilamba midomo yangu kuua aibu flani iliyochomoza kama mshale wa sekunde na kupotea.

    Tuliongea mengi na Jeniffer nae hakuwa mvivu wa kujibu maswali na chochote nilichomuelezea, niliamini ndoto yangu ilitimia, yule mwanamke niliyempata angeweza kufunika pengo kubwa maishani mwangu. Hata hivyo katika mazungumzo yetu alinitamkia kwa kinywa chake kuwa nae ananipenda sana, kuliko hata mimi ninavyompenda. Ni binti aliyeukonga moyo wangu na kuuteka kila sehemu ya viungo vya mwili wangu, “Kweli subira huvuta heri” niliongea kimya kimya kwenye mtiririko wa mawazo.

    Jennifer alikuwa ni mchanganyiko wa Mzungu na mwafrika (chotara) na ni msichana aliyetoka Bara la Africa kama mimi, tofauti ni kwamba yeye alitokea Africa ya kusini, na mimi nilitokea Tanzania. Wala hakujali Nchi niliyotoka kuwa ilikuwa ya kimaskini, inamaana alinipenda na umasikini wangu. Tuliongea na kujikuta mawazo yetu yakiwa sawa, kwa kutaka kunionyesha upendo alikubali ombi langu la kutaka anisindikize kuupitisha usiku uliojaa raha za kila aina. Alidiriki kuacha chumba chake na kuja kulala na mimi, nilimgusia suala la ndoa nalo alilikubali alikuwa tayari kubadili uraia kuwa Mtanzania. Lakini kama angekuwa Mtanzania aliyekuwa Afrika ya Kusini umwambie arudi aolewe Tanzania, angeruka hata futi mia.

    Kwa upande wa mapenzi nilikoga na penzi motomoto, hakuwa mvivu wa kujishughulisha, tulisaidiana kupitisha usiku huo mwanana uliojaa mahaba ya kila aina, si mlimani tulipanda vichochoroni tulipita kwa nia imara ya kumridhisha Jeniffer aliyeonekana mgeni kwenye ulimwengu huo. Asubuhi kulipopambazuka nilimuaga Jennifer na kuelekea soko la madini ya Tanzanite, lililoitwa King Life. Kabla ya kuondoka nilimuachia namba ya simu email address yangu kwa mawasiliano. Na niliamua kufanya hivyo ili kuwahi na kuwaeleza wazazi habari mpya, wasihangaike kunitafutia mchumba kwani nilishampata mrembo. Nilifanikiwa kuuza madini yote kwa bei nzuri na kurudi Tanzania.

    ************

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nilipofika kazini, nilikabidhi pesa kwa Tajiri yangu Mzee Jophu tukiwa katika maongezi ya mabadiliko ya kibiashara. Tulisikia mlango ukigongwa kwa nje, bila kujali wala kujua ni nani mtu huyo, Mzee Jophu aliamuru aingie, Aliingia na alikuwa sekretari wa Mzee Jophu.

    “Boss, samahani kuna wageni wa Sweedy wanamuhitaji” sekretari aliongea akijikanyaga kanyaga na kuuma vidole.Alionekana kumuogopa sana bosi wake.

    “Sawa waambie wasubiri kidogo” Mzee Jophu alijibu kwa kifupi na kuendelea na mazungumzo nami.

    Tuliongea na kumaliza, Mzee Jophu alikuwa wa kwanza kutoka kinyume na mashariti yake, tuliongozana kujua nani alikuwa ananiita. Kwenye viti vya mapokezi ya wageni, nilimuona baba na mama, mama mwingine wa makamo ambaye simfahamu, pembeni ya yule mama nisiye mfahamu nilimuona binti mwingine mrembo. Kwa haraka ubongo ulifanya kazi yake kwa bidii na kukumbuka kuwa niliwapa kazi wazazi wangu kunitafutia mchumba baada ya kuzunguka kila kona ya dunia bila mafanikio. Kumbukumbu hiyo iliutesa moyo wangu kwani nilishapata mchumba mwingine, tena mzuri kuliko yule niliyeletewa na wazazi, japo nae alikuwa mzuri lakini kamwe asingefurukuta kwa Jennifer.Ndivyo nilivyo hisi moyoni na wasiwasi ukawa umejidhatiti akilini.

    “Baba shikamoo, mama shikamoo!, Mama shikamoo!, Dada habari yako! Niliwasalimia wote nikipita kwa mstari huku nikiwashika mikono. Pia mzee Jophu naye alifanya hivyo hivyo nilivyofanya mimi. Lakini cha ajabu aliposhikana mkono na binti yule akabaki amemshika muda mrefu, macho ya upendo yakiwa yanatambaa usoni mwake. Nilishtuka pale yule binti alipovuta kujinasua mikononi mwa Mzee Jophu.

    Baba hakupenda kufanya mambo kwa siri, alizungumza yote mbele ya mzee Jophu mama na yule mama mwingine na binti yule.

    “Mwanangu unayemuona pembeni ya mama yako ni mama mkweo na msichana unae muona hapo ni mkeo kazi uliyotutuma tumeikamilisha. Sidhani kuna la ziada zaidi ya kuhitimisha ndoa kanisani” Baba alizungumza na alitegemea kuona furaha, lakini furaha yangu ilifunikwa na uzuri wa Jennifer niliyeonja penzi lake Nchini Thailand.

    “Mbona huongei wala huonyeshi furaha” Baba aliniuliza kwa mshangao.

    “Baba ningeomba tuzungumze faragha kidogo. Kuna mambo mengine hayafai kuzungumza mbele ya mama na watu wengine, nilipoongea hivyo baba alikiri na kujikuta akitikisa kichwa kuafiki yale niliyoyasema.

    Tuliondoka eneo lile na kulizunguka nyuma ya jengo la kazini. “Baba nimekuita mazungumzo ya pembeni nina jipya lililojitokeza”

    “Jipya lipi zaidi ya hili nililo kuletea? Baba alizidi kunikazia macho ya ukali.                            

    “Ndio hilo ni jipya ulilolileta wewe nashukuru. Lakini hata mimi nina jipya nililopata nikiwa Nchini Thailand kikazi”Baba alionekana mwenye furaha iliyotoka moyoni, alihisi pengine nimemletea zawadi, kumbe asijue ni ujumbe wa kumkataa binti walionitafutia.

    “Umeniletea suti nini mwanangu Sweedy?” Baba aliuliza huku akiwa ametoa tabasamu zito la kupokea zawadi.

    “Hapana baba, ila ninaomba radhi kwa usumbufu.”

    “Usumbufu gani?. Sema”

    “Nimewasumbua kunitafuti mchumba. Baba nikiwa Bangkok Nchini Thailand nimebahatika kupata mchumba ninayetegemea kufunga naye ndoa.”

    “Eti nini”? usinichezee naona unataka radhi ya wazazi, hatuelewi kila kitu tumemaliza. Mahari tumeshalipa tunachosubiri ni ndoa tu. Halina mjadala” Baba aliongea kwa ukali, mishipa ya shingoni ilimtoka, ghafla macho yake yalibadilika rangi na kuwa mekundu.

    “Naomba uniambie sasa hivi. Unamuoa yule binti au laa! Sitaki uniambie nikupe muda” Baba alizidi kufoka kwa sauti. Sauti yake ilienda mpaka alipokuwa mama na mama wa yule binti na binti. “Baba nisamehe sauti hiyo inasafiri naomba yaishe”Mara anakuja mama akikimbia huku kanga zikimdondoka alikwapua kanga na kufika pale nilipokuwa na baba.

    “Baba Sweedy kuna nini? Mama aliuliza kwa kudadisi .

    “Mwanao anataka kututia aibu.”Baba alisema akinikazia jicho la ghadhabu.

    “Aibu gani tena?”Mama akauliza akiwa anamtumbulia macho Baba.

    “Mwanao hataki tena kuoa.Anasema binti tuliyemtafutia hajampenda.Na ameshapata mchumba huko alikotoka” Baba aliongea kwa sauti ya taratibu iliyojaa uchungu.

    “Hakuna pingamizi lazima aoe la sivyo atazunguka hii dunia wakumwoa hatamuona. Hata huyo anayesema amempata pia atamkataa. Kama sisi sio…… nilimkatisha mama aliyekuwa anaongea kama kuniachia radhi.

    “Mama sasa naona mnaniachia laana, basi nitamuoa binti huyo.” Muda mfupi niliona maneno hayo yalirudisha furaha zao. Hawakupenda nichelewe kuoa, mipango ya harusi ilifanyika na tarehe ya harusi ilipangwa.

    Wiki tatu kabla ya kusafiri kwenda nchini Thailand. Nilipokubali wazazi wote walirudi kule tulipowaacha mama wa binti, binti mwenyewe ambaye ndiye mke wangu mtarajiwa na mzee Jophu. Lakini tukiwa katika mazungumzo mimi na wazazi wangu, huku nyuma Mzee Jophu alikuwa akiongea na mama wa binti aliongea kuwa anamuhitaji yule binti amuoe yeye na sio mimi tena mambo hayo yalifanyika haraka na kwa siri, si tu kwa maneno bali Mzee Jophu alimpatia hela nyingi kuliko zile za wazazi wangu walizolipa.

    “Mama kamata laki tano hizi ni zako bado nitakuongeza” kwa shida ya mwanamama yule alizipokea na kuziweka kibindoni kwa haraka huku akimuahidi kuvunja ndoa isifungwe, aliniamini angetumia njia yoyote ya kukwamisha ndoa. Ni mambo ya kusikitisha, mzee Jophu pamoja na kuwa baba wa familia ya watoto watatu, bado alihitaji mke wa pembeni aliamini kwa pesa zake nisingeweza kufurukuta “Pesa inazungumza. Pesa ni kila kitu.Haki pasipo haki kwa tajiri ni haki” mzee Jophu alizidi kuzungumza.

    Tuliporudi pale nilishangaa kumuona Mzee Jophu akiwa na hasira alikunja ndita aliponiona tofauti na mwanzoni. Nilijiuliza nina kosa gani, kama ni mazungumzo yetu yalikuwa mazuri nimemfanya nini boss mbona ananitupia jicho la ukali, nilishindwa kujua kilichoendelea kwa wakati huo.Mama mkwe mtarajiwa nae alipindua midomo yake na kuibetua kama iliyoteguka jicho la dharau lilinitizama kuanzia chini ya unyayo hadi juu ya nywele, kisha kabla ya yote nilisikia akisema “Kijana wenu hana hadhi ya kumuoa mwanangu. Kwa jinsi ninavyomuona” nilistaajabu kusikia sauti iliyoambatana na kusonywa.

    “Kwa nini mama Getu?. Amefanya nini mwanangu?” Mama alimuliza kwa sauti ya chini.

    “Mwanao hana nidhamu. Uso wake umetawaliwa na dharau. Hawezi kumuoa mwanngu” aliongea kama kawaida alinitupia macho ya kunitazama kama mtu aliyejinyea japo maneno yake niliona na niliyasikia yakinichoma moyoni mwangu. Nilikabwa na fundo kali la ghadhabu nikaamua kumuheshimu tu, kama si heshima basi ningeropoka neno lolote baya nae limkere moyoni. Mzee Jophu alikuwa kimya pembeni , macho yakipepesa kwa kuibia na furaha iliyojificha ilionekana usoni mwake, lakini sikuweza kugundua kwanini mama yule alibadilika yeye na Mzee Jophu.

    Mama na baba walimuomba radhi awasamehe kuzaa mtoto asiye na nidhamu na anisamehe, walijua pengine hasira ile ni kile kitendo cha mimi kumuambia baba siko tayari kumuoa mwanae kwani nilipata mchumba Thailand. Lakini mama mkwe mtarajiwa msimamo wake ulikuwa pale pale, hakutaka nimuoe mwanae, na alitaka arudishe mahari, kwa kile kitendo cha kusema

    “Mtoto wenu hana nidhamu” hata alipoulizwa nidhamu gani alishindwa na kubaki akisema.

    “Sitaki nasema basi. Chukueni hela zenu na ng’ombe zenu nne, sikotayari kumuozesha mwanangu” Aliendelea kuwa na msimamo wake. Kwa maneno ya mama yule yalikuwa ni furaha kwangu, kwani ningemkosa basi ningeenda kumuoa Jennifer na kwa upande mwingine yalinikera sana, hasa alipozidi kusema sina hadhi ya kumuoa mwanae. Eti nina dharau, nilishindwa kumuelewa alikuwa na maana gani?.

    Baba na mama yangu walinivuta pembeni na kuzungumza kama dakika takribani tatu, kisha wakarudi na kuomba waondoke wakayazungumze nyumbani. Waliondoka wote, baba, mama, mama Getruda na Getruda. Hawakutaka kuyazungumza pale kwani ilikuwa sio sehemu yake. Tulibaki mimi na mzee Jophu, lakini sikumuona akiwa na furaha kama nilivyomzoea, hakutaka kuongea na mimi.

    “Boss mbona unaonekana una hasira nini hasa nilichokukosea. Nimeona umebadilika” kimya kilitanda sikupata jibu lolote zaidi ya kunitazama na kuondoka zake.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kesho asubuhi nilipowasili kazini, nilifanya kazi vizuri kama kawaida nikiwa naongea na baba na mama kwenye simu. Mara Boss Mzee Jophu anaingia na wakati huo nilimaliza maongezi na kukata simu, nilipomsalimia hakuitikia salamu yangu, bali alinitupia barua mezani, na kusema “Sina shida na salamu yako. Barua hiyo na unijibu haraka iwezekanavyo.Nakupa nusu saa” aliondoka na kufunga mlango kwa kishindo kikubwa.

    Nilishindwa kumuelewa, lakini kwa matendo yake nilihisi na kuamini barua ile ilikuwa ya kufukuzwa kazi, lakini nilishindwa kuelewa kosa hasa lilikuwa lipi?. Homa ya kufukuzwa kazi ikaniingia, nilishindwa kuisoma ile barua, niliinamisha kichwa nikiwaza.

    “Hivi kama nitakuwa nimefukuzwa kazi nitaenda wapi? Nitamuonaje Jennifer tena? Nauli sina ya kwenda Bangkok” Ghafla mawazo yakanijia nilikumbuka kuwa boss alinipa muda wa nusu saa kuijibu barua yake. Ndipo nilipoanza kuifungua barua huku mikono na vidole vyote kwa pamoja vikitetemeka kama mgonjwa wa degedege. Nilifanikiwa kufungua Barua. Kitu cha kwanza kukutana nacho ni maneno yaliyoandikwa kwa herufi kubwa.

    YAH: UPIMAJI WA AFYA KWA AFISA MAUZO, JOPHU MINING TRANSPORT CO.LTD.

    Moyo wangu ulipasuka kwa furaha “nilihisi ni ridandasi kumbe ni kupima afya hilo halina shida. Ngoja niendelee kusoma” nilijisemea kimoyomoyo.

    HUSIKA NA KICHWA CHA HABARI HAPO JUU, TUMEPATA BARUA KUWA WAFANYAKAZI WA KAMPUNI YETU WANAHITAJIKA KUPIMA AFYA ZAO, HASA UKIMWI NA AFISA MAUZO AWE WA KWANZA . BODI ILIPANGA KIKAO CHA SIRI.

    MKURUGENZI WA KAMPUNI

    JOPHU KUNDY.

    Nilimaliza kusoma barua, lakini hata hivyo moyoni nilijiuliza “Kwanini Mzee Jophu na msalimia haniitikii, halafu akanipa barua ya kwenda kupima afya yangu, au anahisi nina virusi nini?. Ama anataka kunitafutia kosa ili anifukuze kazi nini?. Kwanini ananikasirikia, ni kwa vile wazazi wangu wamekuja kuongelea maswala ya kuoa hapa kazini au ni nini?.” Nilizidi kutumbukia kwenye kisima cha mawazo kem kem, bila kupata jibu muafaka. Kwa ujumla nilishindwa kuelewa wazo halisi la Boss kunitaka nikapime afya yangu, na nikiwa mtu wa kwanza kazini kupima virusi na kwa nini alinikasirikia. Muda niliopewa na Mzee Jophu ulitimia, hakupenda kupoteza muda, aliingia ofisini kwangu na kuniuliza,

    “Sweedy umeisoma barua niliyokupatia?. Naomba majibu. Utaenda kupima au hutakwenda?”

    “Nitakwenda boss, lakini kwani ni lazima kupima?”

    “Ndio, ni lazima hasa wewe” Mzee Jophu alinijibu kwa uhakika.

    “Kwa nini mimi iwe lazima, asiwe mfanyakazi mwingine. Boss unanitisha sana hasa unaposema ni lazima mimi, na cha kushangaza boss hutaki kuitikia salamu zangu. Nimekukosea nini, naomba uniambie, ndipo nami nikujibu kuhusu jibu la kupima” Niliongea nikilalamika kidhaifu kwa boss, niliogopa mabadiliko ya boss.

    “Ok, usihofu kuhusu kutoitikia salamu yako. Nilijaribu kukutingisha tu unajua Sweedy mimi na wewe dam dam. Pia watu wanatufananisha kama mtu na mdogo wake, wengine wanajua dhahiri kuwa wewe ni mdogo wangu wa toka nitoke. Nilikuwa nakupima imani yako, hivi wewe hushangai toka nikuajiri kazi hatujawahi kukasirikiana iwe sasa? Wewe ndiye ninaye kuamini katika kampuni yangu, hata nikifa leo, wewe ndiye utakaye shikilia mali mpaka watoto wangu watakapokomaa kiakili. Umenielewa Sweedy? Ondoa shaka yale yote ni matani.” Mzee Jophu aliamua kuficha ukweli uliopo moyoni mwake, alinichukia mno! kwa muda mfupi tu toka amuone Getruda, binti mrembo, hakutaka nijue nini kilichotaka kuendelea, alizidi kunifumba kwa maneno ya uwongo na kunifanya nimuamini kuliko siku za nyuma.

    Nilipandisha pumzi na kushusha kwa nguvu “oophhhh!” “Ni kweli boss lakini ilinifanya niwe na alama ya kuuliza ndani ya ubongo wangu, hata hivyo sikuamini kuwa ni wewe ulinibadilikia kiasi hicho. Kuhusu kupima nani kakupa wazo hili?”.

    “Ok, swali zuri, nilipata barua kutoka mamlaka ya Uhamiaji, kwamba si ruhusa mtu kutoka nje ya Nchi bila kupima afya, hivyo wewe kama Afisa mauzo bila kupima hutaenda Nchini Thailand lakini utakapopima utaendelea na kazi yako kama kawaida.”

    “Hakuna shida boss mimi nitapima virusi najiamini sina kitu, mimi sio mkware” Nilimjibu. Furaha yangu nikutaka kwenda nchini Thailand nikaonane na Jennifer .

    “Kesho asubuhi watakuja Daktari kukutoa damu. Hutaenda huko hospitalini, cheo chako kinakulinda na sitaki uhangaike. Watakuja na kukupima na wiki ya tatu utaenda Nchini Thailand kama hutakuwa na virusi. Sio sheria yangu hapana ni serikali”Akasema Boss akizunguka zunguka pale ofisini.Alionekana mwenye furahabaada yakukubali kuopimwa.

    “Nitakuongezea mshaharaasilimia hamsini wa mwanzoni”Alizidi kunipa motisha.

    “Nitafurahi Bossi” .

    Tukiwa kwenye maongezi nilisikia simu ikiita. Nilipoitoa mfukoni niliona namba za baba juu ya kio cha simu. Niliipokea na kuanza kuongea .

    “Shikamoo baba.Mama hajambo?”

    “Marahaba!. Wote wazima wanakusalimu. Jiandae kwa harusi yule mama amekubali umuoe mwanae. Ni baada ya kwenda kwenye mila na desturi, amepewa faini ya kutaka kurudisha mahari. Umenielewa mwanangu?”

    “Ndio baba. Kweli amekubali nimuoe mwanae?. Hata siamini nitajitahidi kukusanya mchango wa harusi”

    “Sawa jitahidi mwanangu” Tulimaliza maongezi na kukata simu.

    Nilipomtizama Mzee Jophu alinitupia macho ya lawama, lakini hata hivyo nilichukulia usemi wa kupima imani kumbe yeye maneno ya yule mama kukubali nimuoe mwanae yalimuumiza roho sana, na alikiri kumuua mama Getruda kwa kumsaliti na kumchukulia laki zake tano, lakini kwa upande wa mama Getruda hakula wala hakuzitumia hata senti tano yoyote, alipanga kumrudishia baada ya kushindwa kuzuia ndoa isifanyike.

    *************CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog