Search This Blog

Friday, July 15, 2022

NILIVYOMLIZA MKE WANGU KWA SIKU 366 - 2

 







    Simulizi : Nilivyomliza Mke Wangu Kwa Siku 366

    Sehemu Ya Pili (2)



    Sikuwa sawa, nilikuwa na mawazo mno, yaani hata ile nguvu ya kuvunja amri ya sita sikuwa nayo kabisa. Hakuacha, aliendelea huku akinifuata kwa juu, akaning’ata sikio, akanipuliza kidogo, akaupeleka mkono wake mbavuni mwangu, chini ya kiuno, alijitahidi kunichaji lakini sikupatwa na chaji kabisa, niliendelea kubaki vilevile kama roboti.

    Isabela: Jamani.....nataka haki yangu, baridi linaniua.... (aliniambia kwa sauti ya chini kabisa)

    Mimi: Isabela mpenzi, naomba nipumzike, kiukweli sipo sawa....

    Isabela: Kwani tatizo nini?

    Mimi: La kifamilia zaidi, ila utalijua.

    Nilipomwambia hivyo, akageuka upande wa pili na kutulia. Niliamini kwamba alikuwa amekasirika, alitaka nimwambie kile kilichotokea huko lakini sikutaka kufanya hivyo. Alikuwa msichana niliyempenda sana, naweza kusema zaidi ya msichana yeyote niliyebahatika kuwa naye katika maisha yangu.

    Usiku huo ulikuwa mkavu, hakupata kitu. Tulipoamka asubuhi, hakuonekana kuwa sawa, kwa kumwangalia tu niligundua kwamba alikuwa na hasira, nikajaribu kumbeleza na kumuelezea kwamba hali niliyokuwa nayo jana ilikuwa ngumu kufanya kile alichotaka nifanye.

    Isabela: Nimekuelewa mpenzi...CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Safari ya kurudi Dar ikaendelea. Tulikuwa tukizungumza mambo yetu, nilikuwa na mawazo mengi lakini wakati mwingine nilitakiwa kuachana nayo na kuconcetrate na mpenzi wangu, tulipofika Dar, akaenda kwao na mimi kutulia nyumbani nikijiandaa na kazi zangu hiyo kesho.

    Asubuhi niliamka na kujianda kisha kuelekea kazini. Sikuonekana kuwa mchangamfu na hata wafanyakazi wenzangu waliponiona waliligundua hilo hivyo kunihoji, jibu nililowapa ni kwamba nilikuwa naumwa kichwa.

    Ilipofika saa saba, nikapigiwa simu ya mezani na kuambiwa kwamba nilikuwa na ugeni mapokezi. Kwanza nilishtuka, tangu nianze kazi hakukuwa na siku ambayo nilikuwa na ugeni, nikahoji ulikuwa ugeni wa nani lakini nikaambiwa niende huko na ningejionea mwenyewe.



    Nilipofika huko, macho yangu yakatua kwa wazazi wangu, walikuwa wamefika ofisini kwangu huku wakiwa na msichana Salama ambaye ndiye walitaka nimuoe. Waliponiona, wote wakaonyesha tabasamu pana, sikuwaonyeshea tabasamu kwani walinichanganya, walikuja kufanya nini na kwa nini ofisini badala ya nyumbani?

    Sikutaka wakae hapo, nikawachukua na kuwapeleka ndani ya gari na safari ya kuelekea nyumbani kuanza. Sikufumbua mdomo wangu na hata wao hawakufumbua midogo yao, yaani kila kitu kilichokuwa kikifanyika, kilifanyika kwa vitendo tu. Tulipofika nyumbani, nikawakaribisa.

    Baba: Sisi hatukai sana, tumekuletea mkeo...

    Mimi: Mke wangu...!!

    Mama: Ndiyo! Tena tumeshakuolea kabisa, kazi kwako kuishi naye

    Mimi: Hivi mna akili kweli?

    Baba: Ndiyo! Tuna akili na ndiyo maana tukakuzaa, tukakusomesha mpaka kuwa hapo.

    Hawakutaka kubaki mahali hapo, walihisi kama ningewafukuza, walichokifanya, wakafungua mlango na kuondoka zao. Sikuwa nimewapa nauli, sikutaka kujua kama walikuwa na fedha au la.

    Nikabaki na Salama pale sebuleni, sikujua ni kitu gani nilitakiwa kufanya. Alionekana kuwa msichana mpole, anayetia huruma ambaye alipigwa sana na maisha ya kijijini. Nikaanza kujiuliza, hivi kweli niwaambie marafiki zangu kwamba Salama alikuwa mke wangu? Watanichukuliaje? Najua kitu cha kwanza kabisa wangeanza kumlinganisha Salama na Isabela, kiukweli, kama ni magari basi unafananisha Vitz na Lamborghini, ni vitu viwili tofauti.

    Isabela: Shikamoo mume wangu (alinisalimia huku akipiga magoti, mfuko wa Rambo wenye nguo ulikuwa mikononi mwake)

    Sikuitikia....nilishikwa na hasira ile mbaya......nikawa najiuliza nini nilitakiwa kufanya, kumpa taarifa Isabela au kumfukuza Salama nyumbani hapo, kiukweli NILICHANGANYIKIWA.



    Nilikuwa kwenye wakati mgumu mno, sikujua kitu gani nilitakiwa kufanya, kuna kipindi nilihisi kama nilikuwa ndotoni nikiota moja ya ndoto mbaya ambapo baada ya dakika kadhaa ningejikuta nikiamka kutoka usingizini.

    Moyo wangu ulinyong’onyea kabisa, sikuwa nikimpenda hata kidogo huyu Salama aliyeletwa nyumbani kwangu na kuambiwa kwamba tayari baba alishaniolea. Nilibaki nikimwangalia pale sebuleni, kiukweli, sikuwa nikimpenda, alionekana mchafu, asiyekuwa na uzuri hata kidogo, na kwa mbali niliweza kusikia harufu mbaya ya nguo zake.

    Nilishindwa kukaa hapo nyumbani kwani kwa jinsi hali ilivyokuwa, niliona kabisa kwamba ningemfukuza, hivyo nikaondoka na kuelekea katika baa iliyokuwa jirani na nyumba yetu. Nilipofika huko, nikaagizia pombe na kuanza kunywa mdogo-mdogo huku nikionekana kuwa kwenye lindi la mawazo.

    Mimi: Yaani baba amenifanyia ujinga sana, ananiolea mke, haya mambo mbona ya kitambo sana... (nilijisemea kwa hasira huku pombe ya siku hiyo ikionekana kuwa chungu sana kuliko zote nilizowahi kunywa, haikuwa tamu hata kidogo)

    Kitu kingine ambacho kilinipa maswali na hofu kubwa ni namna ya kumwambia Isabela kile kilichokuwa kimetokea, nilijuta, niliona ni bora hata ningemwambia jambo lile kulekule kijijini tulipokwenda, ila mpaka muda huo, tayari nilikuwa nimechelewa sana.

    Basi nikavuta muda mpaka ilipofika saa kumi na moja, nikachukua gari langu na kumfuata Isabela katika sehemu aliyokuwa akifanyia biashara. Nilipofika hapo, akanifuata na kunikumbatia, siku hiyo alionekana kuwa na furaha tele.

    Isabela: Mbona upo hivyo mpenzi?CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mimi: Nipo vipi?

    Isabela: Huna furaha, kuna tatizo gani?

    Mimi: Hakuna tatizo.

    Isabela: Una uhakika?

    Mimi: Ndiyo kipenzi.... (nilimwambia, nikamvuta na kisha kumbusu mdomoni)

    Japokuwa nilimuonyeshea manjonjo hayo lakini bado hakuonekana kukubali, alijua kwamba kulikuwa na tatizo na ndiyo maana nilionekana kama mnyonge japokuwa uso wangu ulitawaliwa na tabasamu pana.



    Nilikaa naye hapo kwa muda kama dakika arobaini na tano, nikaamua kuondoka naye hapo na kuelekea Mlimani City. Nilikuwa namuandaa kwa ajili ya kumwambia kile nilichotaka kumwambia. Sikutakiwa kukurupuka, nilitakiwa kumuandaa kukubaliana na kile nilichotaka kumwambia.

    Baadaye, nahisi akili yake ilikaa sawa kwani alionekana kuwa mwingi wa furaha na hata hakuwa na shaka yoyote ile juu ya muonekano wangu. Niliamini kwamba ningeshinda lakini swali lililonisumbua kichwani mwangu ni kwa namna gani angelipokea lile nililotaka kumwambia.

    Mimi: Isabela mpenzi!

    Isabela: Abee laaziz...

    Mimi: Nimekuwa nikikupenda sana, na milele nitakupenda mpenzi....

    Isabela: Hata mimi pia, ninakupenda mpenzi...uliwasiliana na wazazi wako baada ya juzi?

    Mimi: Hapana! Niliamua kukaa kimya kwani najua walikuwa wakinizingua tu.

    Isabela: Ilitakiwa uwasiliane nao, wale ni wazazi wako kumbuka, wakati mwingine wanaweza kuonekana kuwa hawapo sawa, unatakiwa kuwaambia walipokosea, lakini mara nyingi nawaamini wazazi hawakosei.

    Mimi: Unaamini wazazi hawakosei?

    Isabela: Ndiyo! Na mara nyingi hawapendi kumuona mtoto wao akipotea, wanapokwambia fanya hili, wewe fanya hata kama unahisi halipo sawa....

    Wakati akizungumza maneno hayo, nilikuwa nikijiuliza kuhusu Salama. Sikuwa nimemwambia kuhusu msichana huyo ambaye nilimwacha nyumbani kwangu. Kama anasema nilitakuwa kukubaliana na wazazi wangu, hii inamaanisha kwamba nikubaliane na suala lao la kunichagulia mke? Hakika ilikuwa ngumu.

    Mimi: Isabela....hebu twende sehemu tukatembee kwanza....

    Isabela: Sawa...

    Tukaondoka na kuelekea ufukweni. Huko kote tulikuwa tukihangaika kwa kuwa bado nilikuwa natafuta pozi la kumwambia kile nilichokuwa nacho moyoni mwangu. Nilitaka kumwambia tulipokuwa Mlimani City lakini nikaona kama ningeharibu mambo, inawezekana angelia sana, hata kumbembeleza ingekuwa ngumu na kwa sababu kulikuwa na watu wengi, hivyo ingekuwa ndivyo sivyo.



    Tulipofika ufukweni, nilitafuta sehemu nzuri na kutulia, muda wote moyo wangu ulikuwa ukijiuliza kama ulikuwa muda sahihi wa kumwambia kile kilichokuwa kikiendelea au nilitakiwa kusubiri. Nilipomwangalia usoni mwake, alionyesha tabasamu pana lakini nikawa nikijisemea kwamba tabasamu hilo lingeweza kupotea ndani ya dakika moja tu kama ningemwambia kilichokuwa kikiendelea nyumbani.

    Isabela: Nikwambie kitu mpenzi?

    Mimi: Niambie...

    Isabela: Kiukweli sina amani kabisa...

    Mimi: Kwa nini?

    Isabela: Ni kwa sababu haupo kawaida, unanionyeshea tabasamu pana, lakini kila nikikuangalia, bado naona una kitu, hebu niambie tatizo nini.

    Mimi: Sina tatizo lolote lile.

    Isabela: Kweli?

    Mimi: Ndiyo!

    Tulizungumza mengi, kama alivyosema kwamba hakuwa na amani, kweli mnilivyomwangalia alionekana kabisa kutokuwa na amani, nikajitahidi kumfurahisha lakini bado hali iliendelea kuwa vilevile. Kumwambia sikutaka kabisa japokuwa nilijua kwamba kuna siku angekuja kujua ukweli na mambo kuharibika zaidi.

    Isabela: Leo nataka nikashinde kwako, nilale hukohuko, sirudi nyumbani (Aliniambia maneno yaliyonishtua mno)

    Mimi: Unasemaje?

    Isabela: Nataka nikalale na wewe leo.

    Mimi: Leo?

    Isabela: Jamani! Mbona upo hivyo, una nini?

    Kiukweli nilichanganyikiwa, kumbuka kwamba Isabela alikuwa mpenzi wangu, niliyemuahidi mambo mengi kitendo cha kumkataza eti kulala kwangu yalikuwa makosa makubwa kwani sikuwahi kufanya kitu kama hicho.

    Nilichokifanya ni kumkubalia tu, sikuwa na jinsi, kama kumuona Salama, basi akamuone hukohuko nyumbani lakini si kumkatalia kwenda nyumbani kwangu. Ndani ya gari, nilionekana mpweke, tena uliongezeka zaidi ya mara ya kwanza, nilijitahidi kupiga naye stori lakini wapi, amani haikurudi kabisa moyoni mwangu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hatukuchukua muda mrefu, tukafika nyumbani huku ikiwa ni saa kumi na mbili jioni. Kuingia sebuleni tu, siku hiyo nyumba ilionekana kuwa tofauti kabisa, ilikuwa safi sana na kila kitu kiliwekwa katika mpangilio maalumu, hata Isabela mwenyewe alibaki akishangaa kwani hakuwahi kuiona nyumba ikiwa kwenye usafi wa namna hiyo japokuwa naye alikuwa akijitahidi kufanya usafi.

    Isabela: Nyumba yako imekuwa safi sana, umeajiri mfanyakazi?

    Mimi: Hapana! Nilisafisha mimi peke yangu... (nilisema huku nikionekana kuwa na wasiwasi)

    Isabela: Siamini kama kuna mwanaume anaweza kusafisha nyumba na kuwa safi namna hii.

    Ile nyumba ilikuwa ni kama ya Isabela kwani yeye alikuwa mpenzi wangu niliyeishi naye kama mke wangu. Wakati anasifia yote hayo kichwa changu kilikuwa kikifikiria huyo Salama alikuwa wapi, nilikuwa na mchecheto kupita kawaida.

    Basi baada ya kukaa dakika chache, akaniambia twende chumbani kupumzika, nikasema sawa huku nikiwa na uhakika kwamba inawezekana Salama amepumzika katika chumba cha wageni. Nikamshika mkono na kwenda naye chumbani, nilipofungua mlango na kuingia ndani, macho yetu yakatua kwa Salama ambaye alikuwa amelala, nguo pembeni, yaani pale kitandani alikuwa na nguo ya ndani tu. Nikausikia moyo wangu ukipiga paaaaaa....!

    Mwili ukaninyong’onyea.



    Nilitamani nifumbe macho ili nisione kile kilichokuwa kikiendelea, moyo wangu ulinyong’onyea mno na nilitamani kile kilichokuwa kikiendelea kiwe ndoto au kama si ndoto basi ardhi ipasuke na kunimeza.

    Moyo wangu ulichanganyikiwa, nilibaki nikimwangalia Salama pale kitandani alipokuwa, mapaja yake yalijaajaa japokuwa hakuwa msafi sana, yaani mafuta ya mjini, maji ya mjini hayakuwa yamemzoea kabisa.

    Masikio yangu yalikuwa yakimsikiliza Isabela angesema nini baada ya kuona kitu kama kile, nilishtukia tu akigeuka na kuondoka huku akionekana kukasirika. Sikuwa tayari kumpoteza Isabela wangu, hapohapo na mimi nikamfuata, alipofika sebuleni, nikamshika mkono.

    Mimi: Isabela mpenzi subiri.... (nilimwambia)

    Isabela: Niache, nimesema niache Denis.... (alisema huku akionekana kuwa na hasira)

    Mimi: Let me explain...(Acha nikuelezee)

    Isabela: Let me go Denis, let me goooo....(niache niondoke, niache niondokeeee) aliniambia huku akianza kutokwa na machozi.

    Halikuwa jambo jepesi, kumuacha Isabela aondoke ilikuwa ni sawa na kushindwa kabisa kumtuliza, nikamvuta kwangu, nikamshika kwa mikono miwili na kumwangalia usoni, alikuwa akilia, moyo wangu uliuma sana, sikuamini kama kuna siku ningekuja kumliza Isabela kiasi kile, sikuamini kama kuna siku angekuwa analia kwa ajili yangu.

    Niliyaona maumivu yake makali kupitia macho yake, niliumia pia ila sikuwa na jinsi, nilitakiwa kumwambia kilichokuwa kikiendelea na ajue kabisa kwamba kilichokuwa kimetokea, hakikuwa lengo lake.

    Isabela: Yaani unanifanyia hivi Denis, nimekufanya nini mpaka kuamua kuniumiza namna hii? Kwa nini Denis, au kwa sababu ninakupenda, au kwa sababu nilimwambia hakuna mwanaume yeyote zaidi yako...yaani yote hayo niliyokwambia, ahadi zote nilizokuahidi kama kukupenda maisha yangu yote umeona si kitu, unamuingiza mwanamke chumbani kwako, alalie kitanda tunacholalia, Denis, kwa nini? Kwa nini? Kwa nini Denis umeamua kunifanyia hivi? Kwa nini Denis umeamua kuniumiza hivi? (aliniuliza maswali matatu mfululizo)



    Sikumjibu kitu, niliendelea kumshika tu, nilijua hakuwa ametulia, kichwa chake kilichanganyikiwa na muda wote alikuwa akilia kwa uchungu. Niliumia zaidi, maneno yake yalinichoma, nikahisi kitu chenye ncha kali kikiuchoma moyo wangu.

    Nilishindwa kujitetea, niligundua kwamba huo haukuwa muda mzuri kwangu kumwambia Isabela ukweli kutokana na kile kilichokuwa kikiendelea. Alilia sana, nilibaki kimya, nikamsogeza na kumkumbatia, hakukuwa na kitu kingine cha kufanya zaidi ya hicho.

    Mimi: Naomba unisamehe Isabela mpenzi.....(nilimwambia kwa sauti ndogo karibu na sikio lake)

    Isabela: Kwa nini umenifanyia hivi Denis, kwa nini umeniumiza hivi?

    Mimi: Si lengo langu kukuumiza, naomba futa machozi mpenzi, nitakuelezea kila kitu, naomba tuondoke kwanza.....

    Nikamtoa hapo ndani na kuelekea naye nje, huko, nikamuingiza ndani ya gari na kuanza safari ya kuelekea katika lodge moja iliyokuwa maeneo ya Kinondoni. Ndani ya gari, muda wote alikuwa mwenye huzuni tele, bado alikuwa akilia kwa kilio cha kwikwi, macho yake yalivimba mno.

    Nilichanganyikiwa mno, kuna kipindi nilishika usukani, nikajisahau kutokana na mawazo mengi niliyokuwa nayo, ghafla, nikaliona gari letu likihama njia na kuelekea mtaroni, nilishtuka, kwa juhudi, nikalidhibiti, likarudi barabarani.

    Hatukuchukua muda mrefu, tukafika katika lodge hiyo ambapo nikasimamisha gari na kuingia ndani huku tayari ikiwa ni saa moja usiku. Nikalipia chumba na kuingia, siku hiyo hatukuja humo kufanya ufuska, tulikwenda kwa kuwa nilitaka kuzungumza naye.

    Mimi: Kwanza naomba unisamehe mpenzi... (nilimwambia mara baada ya kuingia ndani)

    Isabela: Yule ni nani? (aliniuliza huku akiniangalia usoni)

    Mimi: Anaitwa Salama.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Isabela: Ni nani yako? (aliniuliza swali jepesi ila lenye ugumu kujibika, nikashusha pumzi nzito)

    Isabela: Ni nani yako? (alirudia swali kwa sauti kubwa)

    Mimi: Baba aliniambia ni mke wangu.

    Isabela: Mke wako?

    Mimi: Isabela, nimechanganyikiwa, sijui nifanyeje.

    Isabela: Imekuwaje? Mke wako kivipi?

    Mimi: Leo wazazi walikuja kutoka kijijini, wamemleta yule mwanamke, wameniambia ni mke wangu, niishi naye kwani baba aliniolea kijijini.

    Isabela: Uongo, Denis unanidanganya.



    Mimi: Isabela, nikudanganye ili iweje? Unajua ni jinsi gani tumekuwa katika mapenzi haya kwa kipindi kirefu, nilikuahidi mengi, ya nini nikudanganye? Unakumbuka tulipokuwa kijijini, kila mtu alikuangalia kwa macho ya hasira, ukauliza tatizo nini, sikujua, nilipotoka pale nilimfuata rafiki yangu ambaye akaniambia kwamba wazazi wanataka nimuoe yule msichana.

    Isabela: Kwa nini hukuniambia?

    Mimi: Ningeanzaje mpenzi? Niliogopa, sikutaka kukuona ukilia, nilifikiri wazazi wangeniambia nimuoe, ningewakatalia, ila walichokifanya, wakaniolea kabisaaaaa.

    Isabela: Kwa hiyo wewe ni mume wa mtu?

    Mimi: Isabela mpenzi nimechanganyikiwa.

    Isabela: Hilo si jibu! Wewe ni mume wa mtu?

    Sikujua nijibu nini, sikujua ni kitu gani nilitakiwa nimwambie, nakumbuka kabisa siku hiyo ndiyo ilikuwa mwisho wa mwaka wa 2013, ilikuwa kama disemba 24, siku moja kabla ya sikukuu ya Krismasi.

    Isabela: Naomba nikuache na mkeo Denis.

    Mimi: Uniache na mke wangu?

    Isabela: Ndiyo! Siwezi kutembea na mume wa mtu, naomba nikuache na wewe uniache, nakuomba Denis. Moyo unaniuma sana lakini sina jinsi, naomba tu uendelee na maisha yako.

    Sikuamini kile nilichokisikia, eti nimuache Isabela na niendelee na maisha yangu, mbona kilikuwa kitu kisichowezekana, nilimzoea na kumuacha ilikuwa ngumu sana. Nilimwangalia machoni mwake, alionekana kumaanisha alichokisema kwamba mimi na yeye ilikuwa mwisho na hivyo tuachane.

    Mimi: Haiwezekani....

    Isabela: Niache tu Denis, siwezi kutembea na mume wa mtu (aliposema hayo, akaufungua mlango na kutoka)

    Mimi: Isabela...Isabelaaaa....Isabelaaa mpenziiiii.... (niliita lakini hakugeuka)

    Alipofika nje akachukua bajaji na kisha kuondoka zake. Hakukuwa na siku ambayo niliumia kama siku hiyo. Kwa mara ya kwanza tangu nifikishe miaka kumi na nane, machozi yakaanza kunibubujika machoni mwangu. Niliumia mno.

    Lawama zangu zilikuwa kwa wazazi wangu, ilikuwaje wakubali kuniolea msichana nisiyempenda na wakati huku nyumbani nilikuwa na msichana wangu.



    Niliondoka na kuelekea nyumbani, nilikuwa na mawazo mengi mno, nilipofika, nikashuka garini na kuelekea ndani. Nilikuta chakula kikiwa tayari mezani. Nilitulia kochini huku nikiwa na mawazo lukuki, mara Salama huyo akatokea sebuleni pale, akanisogelea na kuvichukua viatu.

    Salama: Pole kwa chovu mume wangu! (aliniambia, nikamkata mjicho huo, nahisi yeye mwenyewe alijishtukia)

    Akavichukua na kuvipeleka chumbani, alipoviweka akarudi sebuleni, akaelekea mezani, akachukua sahani na kuweka chakula, akakiweka mboga na kunisogezea meza ya kioo pale sebuleni na kunikaribisha kula.

    Hata hamu ya kula sikuwa nayo, nilichokifanya, hapohapo mbele ya macho yake, nikasimama na kuelekea chumbani. Nilipoingia, nikafunga mlango na kujiandaa kulala.

    Baada ya dakika kadhaa nikasikia mlango ukianza kugongwa, uligongwa na kugongwa, nikajua yeye tu, nikachuna ndani, sikuufungua, nikajilalia zangu.

    Asubuhi ilipofika, nikatoka chumbani, ile kufika sebuleni, tayari nilikuta kila kitu kipo mezani.

    Salama: Maji ya moto ya kuoga yapo tayari, pia nimeshakuandalia chai, karibu mume wangu....(aliniambia kwa upole sana)

    Nikamshangaa...!! *

    *

    Kwa wiki ya kwanza sikutaka kula chakula chake chochote kile kwa kuogopa kulishwa limbwata, bado nililifikiria penzi la msichana aliyeniacha kwenye mataa, Isabela ambaye hakutaka hata kupokea simu zangu na hata nilipokuwa nikimtumia meseji, hakujibu hata moja.

    Moyoni niliumia na ndivyo nikaongeza chuki kwa huyu mke wangu Salama. Sikumpenda kabisa, nilichoamua ni kumtesa, kumfanya akose raha ili aondoke kurudi kijijini lakini pamoja na kufanya hivyo kwa wiki nzima, bado siku iliyofuata alinionyeshea mapenzi utadhani jana nilimnunulia gari.

    Siku ambayo ndiyo ilikuwa ya mwisho katika mwaka huo, nilitulia sebuleni, sikutaka kuzungumza kitu chochote kile, macho yangu yalikuwa kwenye simu, nilikuwa namtafuta Isabela kwenye simu ili usiku wa siku hiyo tuwe wote na mwaka 2014 ukiingia basi uingie tuwe wote.

    Salama alikuwa kimya akiangalia televisheni, tayari alishachukua shuka lake na akawa ameifunika miguu yake pale kochini ambapo kila siku ndipo alipokuwa akilala, sikutaka alale chumbani kwangu kwani kila siku kazi yangu ilikuwa ni kumfungia mlango, asiingie, abaki palepale sebuleni, na alale hapohapo.

    Salama: Usiku mwema mume wangu...( aliniambia huku akilivuta shuka pale kochini, wala sikumjibu, mimi nilikuwa bize kumtafuta Isabela kwenye simu)CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mpaka saa sita kamili inaingia, mafataki kuanza kusikika nje, bado Isabela hakutaka kupokea simu yangu, niliumia mno, maumivu niliyokuwa nayo kipindi hicho hayakuweza kuelezeka.

    Ilipofika saa 6:30 usiku, simu yake haikuwa ikipatikana tena, ilikuwa imezimwa kitu kilichonifanya niwe na maumivu makali hata zaidi ya kipindi cha nyuma. Kinyonge sana nikasimama na kuanza kuelekea chumbani, nilipofika huko, nikajilaza kitandani huku nikiwa na mawazo lukuki.

    Siku hiyo nilipitiwa na usingizi ilipofika saa tisa usiku wa manane kwani muda wote nyuma nilikuwa kwenye mawazo lukuki. Asubuhi ilipofika, niliamka na kitu nilichokikumbuka ni Isabela tu, nikanyong’onyea mno kwani kitu kilichotokea usiku uliopita kiliniumiza mno.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog